Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Anastazia James Wambura

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuchangia kwa maandishi. Hongera sana Mheshimiwa Waziri Mwigulu na Naibu Waziri, Mheshimiwa Engineer Masauni kwa kuliongoza vizuri Jeshi la Polisi, Magereza, Uhamiaji na taasisi zote za Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kazi nzuri inayofanywa na watumishi wazalendo wa Wizara, lakini wapo wachache ambao wanaharibu taswira ya Wizara. Viongozi wa juu wa Wizara wapite katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu, wasikilizeni kero za wananchi kuhusu utendaji wa baadhi ya Maafisa wa Polisi, Magereza na Uhamiaji ili waweze kuzitafutia ufumbuzi na nyingi zimesemwa humu ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna moja ambalo limenitokea jana shambani kwangu; Askari walivamia wakampiga mke wa mlinzi ambaye ni mjamzito, wakavunja mlango kwa madai kwamba wanakagua mali ya wizi na hawakukuta chochote. Walitaka kuchukua dawa za mazao ambazo bado hatujazilipia na yule mama akawaambia kwamba watafungwa kwani dawa zina deni, ndipo wakaziacha. Kwa bahati nzuri, mume wangu aliweza kwenda kuripoti kwa mkuu wa kazi wa Askari hao, wakaitwa na kuomba radhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafadhali naomba sana Mawaziri wetu wakemee mmomonyoko wa maadili unaoendelea miongoni mwa Askari wachache kwani jambo baya husambaa na kusikika kwa haraka kuliko jema lililo kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza taarifa za kupungua kwa uhalifu ikiwemo makosa ya usalama barabarani. Naamini chanzo kikuu cha mapato kwa Jeshi la Polisi ni faini na kwa uchache stika. Kwa mwaka wa fedha 2017/2018, lengo la kukusanya shilingi bilioni 73 halikutimia na badala yake zimekusanywa shilingi bilioni 43. Sasa kama makosa yamepungua ina maana faini pia zitapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nipate maelezo ya kuridhisha ni kwa nini Wizara kwa mwaka 2018/2019 imeongeza makadirio ya mapato kufikia shilingi bilioni 84? Je, kuna chanzo gani kipya cha mapato? Vinginevyo wananchi watalazimishwa kulipa faini isivyo halali. Leo nitashika shilingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.