Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CHADEMA
Constituent
Katavi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RHODA E. KUNCHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba hii ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi inabeba usalama wa Taifa. Kwa maana hiyo, kama Wizara hii ikiendelea kufanya vibaya kama ilivyo sasa, usalama wa Taifa utazidi kuwa hatarini. Ukizingatia kuwa usalama wa Taifa tunahitaji Serikali iangalie changamoto zifuatazo ili kunusuru Taifa; udhibiti wa uhalifu, mauaji, kubambikiziwa kesi, usalama mipakani, usalama wa wafungwa Magerezani, dawa za kulevya na matumizi ya nguvu kwa wananchi kupitia Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji katika Taifa letu imekuwa ni changamoto kubwa ambayo kimsingi mpaka sasa wananchi wamebaki hawana majibu ya mauaji ambayo yameshatokea, lakini taarifa za matukio haya haya na ripoti inayoeleweka; tukio la Mheshimiwa Tundu Lissu kupigwa risasi mpaka sasa Serikali imeshindwa kutoa majibu ya tukio hili na kuwataja wahusika hasa wa shambulio hili. Je, ni lini Serikali itatoa taarifa ya jambo hili ili wananchi waondokane na hofu iliyopo kwamba Serikali inaficha wauaji hawa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni kuhusu kupotea kwa Ben Saanane, kupotea kwa mwandishi wa habari Azory, maiti zinazookotwa bila taarifa kamili, kubambikiziwa kesi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri kupitia bajeti atuambie ana mkakati gani wa kuhakikisha Vituo vya Polisi na baadhi ya Polisi wanachukuliwa hatua kwa makosa ya kubambikizia kesi wananchi na wananchi wakitoa taarifa za matukio haya hawapati msaada kutoka Vituo vya Polisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Tanganyika ina malalamiko na kesi nyingi za wananchi kubambikiziwa kesi na badala yake watuhumiwa wanaombwa pesa na Askari ili wamalize kesi hizi. Je, Wizara ya Mambo ya Ndani hamwoni kwamba baadhi ya Polisi wasio waaminifu wanachafua Jeshi la Polisi? Mr. Said Anganisye ana kesi katika Kituo cha Polisi Kata ya Kabungu, Tanganyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mauaji ya bodaboda Mwakagana (Wilaya ya Mpanda) Polisi anashutumiwa kumpiga bodaboda mpaka kumuua na Polisi anajulikana kwa jina la Deus lakini mpaka sasa tunavyoongea wananchi hawana majibu ya vifo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira ya magereza yetu bado yana changamoto kubwa kwa maana ya kukosa vyumba vya kutosha pamoja na usafi; vyumba havina hewa na uchakavu wa magodoro yenye magonjwa. Wafungwa hawa pamoja na kwamba wanapewa adhabu, basi zisihusiane na kimazingira bali pia Wizara iangalie haki za binadamu. Kwa kuangalia utesaji na kazi ngumu sana wanazofanya wakiwa Gerezani, badala yake Serikali itumie wafungwa kufanya kazi za kimaendeleo zaidi na siyo mateso wanayopata ambayo hayana tija kwa Magereza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uchache wa vitendea kazi na sare za wafungwa ni aibu kwa Serikali kwa kushindwa kuwapa sare wafungwa na kupelekea Askari Magereza kuwapa nguo zao binafsi kama makoti na nguo za ndani. Mjitahidi kutatua jambo hili. Ni udhalilishaji kwa wafungwa kukosa hata nguo za ndani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iongeze ulinzi mipakani na mikoa inayopakana na nchi jirani kama Katavi, hali ni mbaya.