Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Magdalena Hamis Sakaya

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na wataalam wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri na kuandaa hotuba hii na kuleta hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bunge limekuwa linatenga fedha nyingi sana kwa ajili ya NIDA kuendesha zoezi la kuandikisha raia ili kupatiwa vitambulisho vya uraia. Zoezi hili lilianza mwaka 2011 na lilitegemewa kukamilika ndani ya miaka miwili. Leo ni zaidi ya miaka nane (2011-2018), naomba Serikali ieleze Bunge zoezi hili limefikia hatua gani? Watanzania wangapi wamepatiwa vitambulisho mpaka sasa na ni lini zoezi hili litakamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari polisi wamekuwa wanapanda madaraja wanakaa miaka mingi bila kupandishwa mishahara yao na maslahi mengine. Wapo askari waliopanda madaraja tangu 2010, 2015 mpaka leo hawajaboreshewa mishahara yao. Jambo hili linawanyima haki zao lakini pia linakatisha tamaa ya kiutendaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo kubwa sana la watuhumiwa kuwekwa lock-up za polisi/mahabusu kwa zaidi ya saa 48 kinyume na sheria. Polisi wanawaweka watuhumiwa mahabusu siku 7 - 14 bila kuwapeleka mahakamani. Serikali ilieleze Bunge na kutoa kauli kuhusu tatizo hili ambalo tunalisemea kila leo lakini bado linaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Zimamoto halitengewi fedha za kutosha kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Jeshi hili halina ofisi/vituo wilayani bado wamo kwenye ofisi za mikoa kwa maeneo mengi. Hakuna vitendea kazi vya kuokoa na kupambana na majanga ya moto, magari ni machache na hata pale wanapoitwa wanafika hawana maji. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Jeshi la Zimamoto linakuwa na vituo katika wilaya zote hapa nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kaliua hatuna nyumba za kutosha za askari polisi. Askari wengi wanakaa mitaani jambo ambalo ni hatari sana kwa usalama wao na familia zao. Serikali haijawahi kujenga nyumba za polisi Wilaya ya Kaliua kwani chache zilizopo ni juhudi za viongozi wa Kaliua na wananchi. Serikali sasa itenge fedha za kujenga nyumba za askari pale Kaliua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kituo cha Polisi Kaliua hakina vitendea kazi vya kutosha. Gari ni moja, pikipiki ni mbili tena mbovu, hakuna komputa hata moja na mafuta yanayotengwa kwa ajili ya gari hilo ni kidogo mno. Wilaya ya Kaliua ni kubwa sana hivyo matukio ya uhalifu ni mengi sana. Serikali itoe kipaumbele kwa Wilaya ya Kaliua kupatiwa vitendea kazi ili wafanye kazi kwa ufanisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jeshi la Polisi hutumia nguvu kubwa sana hasa wakati wa kukamata wahalifu wasiokuwa na silaha. Wanaumizwa kwa vipigo wakati hawajathibitishwa kama wamekosea. Wapo raia wengi wameumia na wengi wamepoteza maisha kwa sababu ya matumizi ya nguvu kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Kaliua, Kata ya Ushokora tuelekezwe kutenga eneo kwa ajili ya kujenga gereza. Tangu 2014 mpaka leo hakuna lolote linaloendelea pale. Wananchi waliokuwa wanatumia eneo hilo walinyimwa kutoliendeleza hata kwa kilimo. Serikali itueleze nini hatma ya eneo lile na nini mkakati wa Serikali kuhakikisha Kaliua panajengwa gereza?