Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nsimbo
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. RICHARD P. MBOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mungu mpo salama. Natoa pole kwa Wabunge wote kutokana na matukio na ajali ya power bank. Natoa pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Waziri Jafo, Mheshimiwa Waziri Mkuchika na Makatibu Wakuu wote na Watendaji kwa kazi nzuri ya kusimamia Halmashauri nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2017 Serikali ilifanya mabadiliko ya Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura 290 ambapo uzito ndani ya tani moja hakuna tozo unaposafirisha kutoka Halmashauri moja kwenda nyingine. Pia katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Rais waliweza kueleza nafuu hiyo, lakini mwongozo au sheria hiyo haikuzingatia mazao yanayodumu katika muda mfupi (perishable goods) ambayo mkulima hawezi kuhifadhi na inamlazimu kupeleka sokoni moja kwa moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali katika hitimisho la bajeti itoe tamko juu ya tozo kwenye mboga mboga (perishable goods) kwa kuwa wakulima wengi wa Jimbo la Nsimbo wanasafirisha kwa kiwango chini ya tani moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona maeneo mengine wanategemea perishable goods kama own source kubwa. Basi, nashauri mtu mwenye mzigo chini ya kilo 50 asilipe ushuru ili kutoa nafuu kwa wakulima wadogo wadogo. Pia produce cess 3% on value inavyotozwa na Halmashauri, ipo tofauti na sheria kwani Councils wanatoza fixed amount mfano shilingi 1,000/= kwa tenga, lakini ukitathimini kwa bei ya soko inakuwa chini ya shilingi 1,000/=. Serikali pia iangalie eneo hilo ingawa kwa kudhibiti fixed charge, itasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi wa Serikali hususan Walimu wanadai pesa nyingi ingawa Serikali hivi karibuni ililipa kiasi. Kwa mfano Walimu wa Mkoa wa Katavi kwa madeni yasiyo ya mshahara wanadai kiasi cha shilingi bilioni 1.3. Naomba Serikali ifanye tena malipo ya madeni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mkoa wa Katavi kuna madai ya kupanda madaraja mfano mwaka 2016, Februari Tume ya Utumishi ya Walimu ilitoa barua lakini kufikia Novemba, 2016 Walimu waliambiwa warejeshe barua hizo. Mpaka sasa hakuna waliopanda, lakini kwa wale wachache ambao hawakutii agizo hilo walipanda madaraja. Tunaomba Serikali iangalie Walimu hawa ili wapande madaraja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wapo Walimu ambao wanatakiwa kupanda mishahara, lakini bado Lawson haiwatambui ingawa Halmashauri zimeshawasilisha madai yote Utumishi, naomba Mheshimiwa Waziri ashughulikie maombi hayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA, wazo la kuanzisha TARURA ni jema, lakini mgao wa road fund kwa uwiano wa 3:7 na TANROADS bado hauna tija kwa kuanzishwa kwa TARURA. Kuna ongezeko la gharama za utawala ambazo zinapunguza fedha za maendeleo. Ukiangalia hiyo asilimia 30 itakuwa imepungua; fedha za maendeleo inaenda asilimia 20 na nyingine utawala. Hivyo mgao na uwe uwiano wa 4:6 TARURA Vs TANROADS ili fedha za maendeleo zibaki kama ilivyokuwa kabla ya kuanzisha TARURA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TAMISEMI ilifanya kikao na madeni, Afisa Mipango na Wenyeviti wa Halmashauri 2018, Februari mwishoni ikiwa ni mkakati wa kuhakikisha miradi inafanyika kwa ukamilifu na kutumia chini ya fedha za ruzuku. Tunaomba Serikali itoe fedha angalau asilimia 50 ili miradi iliyorekebishwa katika bajeti. Halmashauri zilifanya mawasilisho upya Machi, 2018. Kwa kutoa fedha kiasi itawezesha Halmashauri zianze kutekeleza miradi ya maendeleo iliyo chini ya LGCDG.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa Halmashauri nyingi nchini zina Wakuu wa Idara ambao wamekaimu kwa muda mrefu. Aidha, kutokana na kutotimiza masharti au uzembe katika mchakato wa kuthibitisha. Naomba Serikali iangalie upya vigezo vya Utumishi kama Wakuu wa Idara mfano kupunguza miaka saba mpaka mitano, ikiendana sambamba na kupandisha cheo. Hii itasaidia watumishi kufanya kazi kwa hali na mori.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Jimbo haina uwezo mkubwa na kati ya Kata 12 tuna Vituo vya Afya vitatu tu. Hivyo kwa kuwa mwaka 2018/2019 hatuna mgao wa Hospitali ya Wilaya, basi tunaomba msaada wa fedha kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya katika Kata ya Kapalala, chini ya Kijiji cha Songambele ambapo kituo hicho cha afya kitasaidia jumla ya Kata nne ambazo ni Kapalala, Nsimbo, Urwira na Mtapenda. Tunaomba sana Serikali itupatie msaada huo wakati tunasubiri bajeti ijayo kwa Hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaishukuru sana Serikali kwa kutupatia gari la wagonjwa (ambulance) Maruti Suzuki, itasaidia kwa kiasi changamoto ya usafiri. Hivyo basi, tunaomba tena gari la wagonjwa aina ya Land Cruiser Hardtop, ambalo linaendana na mazingira ya msingi kwani miundombinu bado mibovu sana na pia matukio ya vifo vya mama na mtoto bado yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Nsimbo bado ina uhaba mkubwa wa Walimu na Watumishi wa Idara ya Fedha. Tunaomba TAMISEMI katika ajira za Walimu zinazokuja mwangalie Halmashauri ya Nsimbo. Pia Wahasibu hawatoshi mpaka inapelekea kutofanya kazi kwa ufanisi katika kusimamia mapato ya Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, TEHAMA, Serikali imefanya kazi nzuri katika TEHAMA upande wa kukusanya mapato, lakini changamoto iliyopo ni kwenye POS, hakuna udhibiti wa kutosha kwa kuwa mtozaji ndiyo anachagua aina ya tozo na idadi za bidhaa. Hivyo, upotevu wa mapato bado upo. Nashauri Serikali ihimize Halmashauri ziwe na takwimu ili kulinganisha na makusanyo halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, napenda kutoa shukrani nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Jafo kwa kuweza kutoa kwa Nsimbo fedha za Kituo cha Afya na
ambulance, pia fedha za Equip, P4R, TEA, Shule za Msingi na nyingine nyingi.