Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Rashid Abdallah Shangazi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlalo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mchango wangu katika Wizara ya TAMISEMI kuhusu elimu. Katika halmashauri ya Lushoto na Bumbuli kuna takribani shule za msingi 168 ambazo ni kiasi kikubwa sana. Tunao uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa vipatavyo 228 kwa Halmashauri ya Lushoto, lakini pia kuna uhaba mkubwa wa Walimu wapatao 836. Hivyo kukosa ikama bora kwa mujibu wa taratibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Lushoto na Tanga kwa jumla kuna shule nyingi sana kulinganisha na mikoa mingine. Wakati Mkoa mzima wa Tanga una shule za msingi 1,032 mikoa kama Simiyu zipo 571, Katavi 177 ambao ni zaidi ya Wilaya ya Lushoto kwa shule tisa tu, Songwe 406, Njombe 499, Lindi 502 utaona uwiano huu hauwezi kuleta tija na ulinganishi kwa sababu mamlaka za usimamizi zinapata mzigo mkubwa kusimamia, itapendeza kama Mkoa wa Tanga utapewa uangalizi maalum ili kusimamia elimu kutokana na ukubwa huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, utawala; lengo la ugatuzi wa Serikali za Mitaa ni kuboresha utawala bora na kupeleka madaraka karibu na watu. Mkoa wa Tanga ni mkoa pekee wenye halmashauri nyingi ambazo ni 11. Hivyo kuhitaji muda, rasilimali fedha na watu ili kusukuma maendeleo. Halmashauri 11 wilaya nane (8) na majimbo 12 ni mzigo mkubwa hivyo kuhitaji kutazamwa kwa jicho la kipekee ili kuboresha maeneo ya utawala na kuleta utawala bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa kama ya Geita ina halmashauri sita (6), Katavi tano ()5, Iringa tano (5), Lindi sita (6), Rukwa sita (6) utaona kwamba Mkoa wa Tanga sasa unahitaji angalau kugawanywa na kupata mkoa wa zaidi. Wilaya ya Muheza, Kilindi na Korogwe ni kubwa mno kuweza kuzalisha wilaya ya ziada. Hali kadhalika Wilaya ya Lushoto inaweza kupatiwa halmashauri tatu yaani Mlalo, Lushoto na Bumbuli kwa sababu takribani robo ya wakazi wa Mkoa wa Tanga wanaishi Lushoto, idadi kubwa ya watu huhitaji usimamizi wa huduma za kijamii ni suala linalohitaji jicho la karibu kutafakari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, performance based audit, napendekeza ufanyike ukaguzi mahsusi juu ya utendaji wa Maafisa Ugani (Extension Officers) katika halmashauri zetu nchini. Watumishi hawa wanaonekana wenye kuzurura hawajulikani wanafanya kazi gani, hivyo kuwa mzigo kwa Taifa kuwalipa mishahara wakati hakuna tija yoyote inayopatikana kutokana na uwepo wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TARURA; Mamlaka hii mpya iishie pale ambapo halmashauri zimeishia, hata hivyo shughuli zao ziendane na mpango wa Taifa wa mwaka mmoja na miaka mitano ili kuleta uwiano wa usawa kuweza kwenda pamoja na sekta nyingine (mfano lengo la usambazaji umeme kijijini (REA) ni ifikapo 2020/2021 ifike mwisho. Je, kwa vijiji visivyokuwa na barabara TARURA wanahusianishaje zoezi hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika halmashauri ya Lushoto hakuna hata gulio moja ambalo lina miundombinu ya vyoo wala vizimba vya kuhifadhia bidhaa, hivyo kuleta kero kwa wananchi na kusababisha magonjwa ya milipuko kwa nyakati tofauti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.