Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Hon. Susanne Peter Maselle

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

MHE. SUSANNE P. MASELLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na miradi ya maji ambayo imeshindwa kukamilika katika Mkoa wangu wa Mwanza, nitazungumzia mradi ulioko katika Halmashauri ya Buchosa Jimbo la Buchosa Wilaya ya Sengerema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Lumeya-Kalebezo Nyehunge wenye thamani ya shilingi bilioni 1.69; mradi huu ulianza Desemba, 2012 na ulitarajiwa kumalizika ndani ya miezi sita hadi leo ni miaka sita, mradi huo haujakamilika na mkandarasi alishalipwa bilioni 1.3 ambayo ni asilimia 90 ya fedha ya mradi mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ungekamilika kwa wakati ungesaidia kuondokana na matatizo ya maji kwa wakazi zaidi ya 16,000 katika halmashauri hiyo. Pamoja na mradi huo kutokamilika kwa wakati Serikali imekuwa ikitoa matamko ambayo mpaka sasa hayajasaidia mradi huo kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, terehe 30 Aprili, 2016, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema alisema Serikali imeunda Tume ya kuchunguza uzembe na madudu yaliyosababisha mradi huo kutokamilika huku mkandarasi akiwa ameshalipwa pesa karibu zote na maji hayatoki. Mwezi Juni, 2016, Mkuu huyo wa Wilaya akasema kuwa ripoti ya timu aliyoiunda imebaini u badhirifu mkubwa kwenye mradi huo na kuziomba mamlaka za juu kumchukulia hatua aliyekuwa handisi na Mkurugenzi wa Wilaya ya Sengerema kwa kumlipa mkandarasi pesa nyingi wakati kazi hajamaliza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, terehe 5 Aprili, 2017 aliyekuwa Naibu Waziri wa TAMISEMI akijua kabisa muda wa kukamilika mradi huo umepita na pesa nyingi zimelipwa, akasema kuwa utakamilika na maji yatatoka ifikapo Juni, 2017, lakini mpaka sasa maji hakuna na watu wanahangaika.

Tarehe 15 Februari, 2018 Waziri wa Maji alitoa agizo akiwa hapa Dodoma akiwaagiza TAKUKURU kuchunguza mradi huo wa maji baada ya kuona Waziri Mkuu ambaye ni bosi wake akiwa Mwanza. Tarehe 15 Februari, 2018 Waziri Mkuu naye akaagiza TAKUKURU na Serikali ya Mkoa wa Mwanza walichunguze suala hilo na kuchukua hatua lakini mpaka leo hakuna majibu yaliyotolewa na maji hayatoki na wananchi wanazidi kuteseka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe wahusika wanapokuja kuhitimisha wawaeleze wananchi wa Buchosa ni lini mradi huo utakamilika na ni hatua gani zitachukuliwa kwa watu waliochelewesha mradi huo mpaka sasa wananchi wanateseka huku watu wengine wakitafuna kodi zao. Ni aibu kubwa kwa Halmashauri ya Buchosa iliyoko Nyehunge kilometa chache kutoka ziwani kukosa maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie miundombinu ya barabara ya Halmashauri ya Buchosa, wananchi wa maeneo haya walitaja mojawapo ya neema ambayo wangeipata kwa kuwa na halmashauri ni kuboreshwa kwa miundombinu ya barabara. Barabara ya kutoka Nyamadoke ulipo mpaka wa Mwanza na Geita kuelekea Nyehunge Kalebezo, Bukokwa, Nyamazugo hadi Sengerema ni mbovu kwelikweli miaka yote na hata inapofanyiwa matengenezo au marekebisho yamekuwa yakifanyika kwa kiwango cha chini na kuifanya kutodumu kwa muda mrefu na kuwekewa molamu ngumu inayoweza kudumu hata zaidi ya mwaka haina mitaro ya kupitisha maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii imekuwa ikileta usumbufu kwa wafanyabiashara wa magari( vyombo vya usafiri) kwa magari kuharibika sana na hivyo kuongeza adha na shida ya usafiri hasa wagonjwa wanaokwenda kutafuta matibabu hospitali za Sengerema wakiwemo akinamama wajawazito. Pia wafanyabiashara na wakulima wa mananasi wanaotokea Nyamadoke, wavuvi wa kutoka Kahunda, Kafunzo, Kanyara, wasafishaji wa mazao ya misitu kutoka Bihindi, Bupandwa wanapata shida sana kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wahusika wanapokuja kuhitimisha wawaeleze wananchi wa Buchosa na Sengerema ni lini barabara hiyo itawekewa lami na kuwa barabara bora, pia wanataka kusikia ni lini barabara hiyo itaboreshwa kuanzia njia panda ya Nyamazugo- Sengerema ili wapite Katunguru wanapoelekea hadi Kamanga. Aidha, wananchi waelezwe ni kitu gani hasa kinasababisha barabara ya kuanzia Sengerema kuelekea Manga pamoja na umuhimu wake haijawahi kuwa katika hali inayostahili kwa shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nata kujua je, ni kwa sababu gani Serikali inagombania mapato ya vivuko na wale wawekezaji kule Kamanga kwa sababu Serikali nayo inamiliki vivuko Busisi, hivyo haitaki wananchi wavuke Kamanga hali inayowaathiri wananchi wa maeneo ya kuanzia Sengerema kuja Kasunganile, Lubondo hadi Kamanga kwa sababu hawawezi kwa vyovyote kwenda kurukia Busisi. Wanataka kusikia Serikali ina mipango thabiti kwa barabara hii badala ya kufanya ukarabati wa kuweka mchanga wa mfinyanzi, lini itaweka lami au molamu iliyo imara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali sasa ituambie lini itaipandisha hadhi barabara hizi za Buchosa hadi Sengerema kutokana na matumizi muhimu na unyeti wake wa shughuli za kiuchumi na kijamiii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha