Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAINAB N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kuniwezesha na mimi kutoa mchango wangu kwa maandishi katika Wizara hii nyeti ya TAMISEMI. Nianze kwa kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. Nampongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kujitoa kwake mhanga kwa Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu kwa namna ambavyo amekuwa anafanya kazi usiku na mchana kumsaidia Mheshimiwa Rais. Nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mawaziri wote pamoja na watendaji wote kwa kazi nzuri wanazozifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee nampongeza sana Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo pamoja na Naibu Mawaziri, Mheshimiwa Josephat Kandege na Mheshimiwa Joseph Kakunda wanafanya kazi kweli bila kuwasahau watendaji wote wa Wizara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua na kuzithamini kazi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano kufika kuwaelekeza na kuwaongoza Watanzania katika uchumi utokanao na viwanda. Viwanda ni matokeo ya mambo mengi moja ya mambo yatakayowawezesha Watanzania kuumiliki na kuuendesha uchumi wa viwanda ni elimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira bora ya kufundishia na kujifunza ni suala lenye umuhimu wa kipekee kwa wakufunzi na wanafunzi. Nafahamu wakati mwingine rasilimali fedha huwa chache lakini niombe Wizara ya TAMISEMI iangalie kwa jicho la kipekee Shule ya Sekondari ya Kalanga. Shule hii ina uchakavu mkubwa mno wa majengo kiasi ambacho Walimu, wafanyakazi na wanafunzi wakiyaona mawingu yenye dalili ya mvua mawazo yao yote hujielekeza katika kufikaria usalama wao pindi mvua itakaponyesha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee niiombe Wizara iinusuru shule hii. Pili, naomba niishauri Serikali katika eneo hili la uimarishaji miundombinu ya shule, Serikali iangalie uwezekano wa kutenga na kutumia fedha nyingi katika mambo machache kwa mwaka husika na kisha kuhamia katika masuala mengine. Nionavyo mimi hali hii itaweza kutatua changamoto nyingi za jambo moja kwa kipindi kimoja cha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwombe Mheshimiwa Waziri Jafo apatapo nafasi aje atembelee Shule hii ya Sekondari ya Kalanga iliyopo katika Kijiji cha Kalanga ambayo iko umbali wa kilomita saba tu kutoka Iringa Mjini na itampa fursa pia ya kujifunza mengi ikiwemo utajiri uliolala wa historia ya Wahehe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.