Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Sengerema
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. WILLIAM M. NGELEJA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii. Nami naanza kwa kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kumpongeza sana Waziri pamoja na Wizara kwa ujumla kwa hotuba yao nzuri, lakini pia na mipango ambayo wameonesha katika hotuba yao.
Mheshimiwa Spika, katika maisha ya mwanadamu hakuna jambo lisilokuwa na changamoto, lakini kiukweli kabisa ukifuatilia utendaji kazi wa Wizara kwa sasa pamoja na wasaidizi wao, unaungana tu na wanaosema usipokuwa muungwana hutakubali hata kidogo unachokipata, lakini ukiwa muungwana utasema ahsante. Tunazungumza hapa lakini kila mmoja anazungumzia eneo lake na ndilo lenye uzoefu kuonesha namna ambavyo mipango ya Serikali kupitia Wizara hii ilivyosimama vizuri ama kama ina kasoro zinazohitaji kufanyiwa maboresho. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mimi nampongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Profesa Kitila Mkumbo na Naibu Katibu Mkuu Injinia Kalobelo, nikitambua staff nzima ya Wizara ya Maji nimtaje Mkurugenzi wa Maji Vijijini, kaa sijakosea Engineer Mafuru. Kwa wale ambao tumepata nafasi ya kufanya nao kazi utakubali kwamba wanajitahidi kwa kadri inavyowezekana kuisukuma sekta hii kuisogeza mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa sababu mimi ni miongoni mwa watu wanaotoa ushahidi wa kuona kwa sababu nimekaa nao na nimeona reflection ya yale ambayo tumeyazungumza wakati tunafuatilia miradi kwenye hotuba hii. Hapa nazungumzia kuona utekelezaji wa visima vya Vijiji vya Nyamililo, Mlaga, Imalamawazo, Nyamatongo, Kinyenye, Ishishang’olo, kule Sengerema sasa, maana yake hapo nazungumza kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Sengerema. Hivi ni visima ambavyo nimeahidiwa baada ya kufuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lakini pia naona kuna miradi ambayo inatekelezwa kutokana na chanzo cha Ziwa Victoria. Hapa nauona Mradi wa Buyagu, Kalangalala hadi Bitoto nakotoka mimi.
Pia naona Mradi wa Chamabanda kwenda Nyandakubwa, ni mambo ambayo tumezungumza nao yameingizwa kwenye mpango na hatimaye tunaiona taswira ya hotuba ikiwa imezingatia haya ambayo tumezungumza nao. Ndiyo maana nasema wanachokistahili tuwape, lakini kwenye changamoto tuwasaidie kuboresha mazingira ya kazi yalivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kule Sengerema pia tumepata bahati, Sengerema tuna hadhi ya Mamlaka ya Mji na tuna mradi mkubwa wa maji ambao Mheshimiwa Rais mwaka jana aliuzindua tarehe 4 Julai. Ni mkubwa kiasi kwamba wana mitambo ambayo mpaka sasa hivi hatujaweza kuitumia kwa ukamilifu. Kwa kuzingatia hilo, tumekuwa na mipango ya kupanua miundombinu iwafikie wananchi wengi zaidi katika vijiji vingi zaidi. Hapa nauona mradi huo ukiwa umetengewa fedha kwa ajili ya kuuboresha kuwafikishia wananchi maji katika vijiji ambavyo mitambo ama miundombinu ya mradi huo inapita. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, hotuba ya Mheshimiwa Waziri nasema imeandaliwa kutokana na mambo mengi, moja ni Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Mpango wa Maendeleo Awamu ya Pili, pia umezingatia ahadi na maelekezo ya viongozi wetu wakuu na hapa nazungumzia kuanzia Mheshimiwa Rais, Makamu wa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Sengerema lilivyo tuna bahati ya aina yake, Rais wa Awamu ya Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, anapokwenda Chato kama anatokea Mwanza lazima atapita Jimbo la Sengerema. Kwa sababu ni Mheshimiwa Rais aliyechaguliwa kutokana na kura za wananchi ni utaratibu wa kawaida kila anapopita anazungumza na Wanasengerema. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, Jimbo la Sengerema tumebahatika kupata ugeni wa Mheshimiwa Rais mara mbili toka achaguliwe na amezungumza na wananchi pamoja na mambo mengine amezungumzia habari za maji, ameahidi kufikisha maji katika baadhi ya maeneo. Nawashukuru wataalam na Mheshimiwa Waziri kwa namna ambavyo wamekuwa wakifanyia kazi ahadi ambazo Mheshimiwa Rais ametoa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nazungumzia mpango wa kufikisha maji kwenye Kijiji cha Nyampande ambacho Mheshimiwa Rais aliahidi, lakini pia naona mipango ya kufikisha maji kwenye Vijiji vya Sima, Tunyenye, Nyamililo pamoja na Nyamahona ambako ndiyo chanzo cha maji kinaanzia. Naishukuru sana Serikali kupitia Wizara hii kwa namna ambavyo imezingatia ahadi ya Mheshimiwa Rais na inaonekana katika hotuba hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukipitia majedwali ya hotuba ya Mheshimiwa Waziri, katika ukurasa wa 124 unaelezea fedha ambazo zimegawiwa katika halmashauri mbalimbali kusaidia miradi ya maji vijijini. Naishukuru Serikali kwa sababu Sengerema tumepagiwa shilingi 1,700,000,000. Ahsanteni sana kwa kutusikiliza na kuzingatia hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, haya ni mambo ambayo yanakwenda kuongeza kiwango cha upatikanaji wa maji kwa Watanzania. Kwa sababu miradi hii itakapokamilika kwa hakika kwa vyovyote vile tutakuwa tumefaidika.
Mheshimiwa Spika, lakini nauona Mradi wa Nyasigu, Lubungo, Ngoma A ambao sasa hivi mchakato wake unaendelea, Serikali mlishatupa kibali, tenda ilishatangazwa, tunakamilisha taratibu za kupata mkandarasi. Nauona Mradi wa Chamabanda/Kasomeko; nauona Mradi wa Kamanga/ Chinfunfu na hapa ndipo napompongeza sana Mkurugenzi wa Maji Vijijini, Engineer Mafuru, ametusikiliza, ametuma wataalam wamekuja kufanya upembuzi wa awali na hatimaye wameonesha kwenye mipango yao ya utekelezaji. Kwa hiyo, sisi Sengerema tunasema ahsante sana, kwa hapa mtakuwa mmetusaidia kupunguza adha ya Watanzania kwenye kiwango cha maji wanachokipata. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, ombi langu kwa Serikali, ukisoma ukurasa wa 189 utakuta Miji ya Sengerema, Nansio na Geita tumetengewa shilingi bilioni 4.7 na huu ni mwendelezo wa miradi ambayo imekuwa ikitekelezwa katika miji ambayo inazunguka Ziwa Victoria. Ninachokiuliza na naomba Serikali mfafanue mtakapokuwa mnafanya majumuisho, katika utatu wetu huu, huu mgawanyo wa shilingi bilioni 4.7 umesimamaje, Sengerema sisi chetu ni kiasi gani?
Mheshimiwa Spika, kwa sababu kitabu hapa kinavyoonesha mmetufunga wote watatu, mnasema ni shilingi bilioni 4.7. Tunaomba Mheshimiwa Waziri atupe ufafanuzi ukurasa wa 189; Nansio wanapata kiasi gani huko Ukerewe, Geita wanapata kiasi gani na sisi Sengerema tunapata kiasi gani ili iwe rahisi kufuatilia kujua Wanasengerema wanastahili kiasi gani na tunachokistahili kuwafikishia wananchi kwa sababu hizi fedha zinakuja kuendelea kuboresha hudumaya maji katika Mji wa Sengerema na vijiji vyake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumezungumza kwa mtazamo tofauti hapa Bungeni. Tupo tunaoamini kwamba changamoto kubwa iliyopo katika Wizara hii siyo fedha isipokuwa ni utekelezaji na tupo tunaoamini kwamba fedha ni tatizo. Mimi naamini kwamba pamoja na yote yanayofanyika lakini bado kuna ufinyu wa bajeti.
Mheshimiwa Spika, tuna taarifa hapa ya Kamati inaonyesha kiwango cha fedha ambacho kimeshatoka kwenye miradi ya maendeleo kinatofautiana na ambacho kimesemwa na Mheshimiwa, tunaamini Mheshimiwa Waziri atakuja nalo. Taarifa hizi zinavyosema ni mpaka tarehe 31 Machi, lakini leo ni tarehe 8 Mei, inawezekana Serikali labda ina taarifa za hivi karibuni hatujui lakini watasema wao.
Mheshimiwa Spika, nachotaka kusema kwa vyovyote vile fedha hizi hazitoshi kutufika kwenye lengo letu la kufikisha maji mijini asilimia 95 na vijijini asilimia 85 mwaka 2020. Kwa hiyo, lazima tufanye yale ambayo tunaona yanaweza kutufikisha mbali.
Moja ni hilo ambalo tumekuwa tukisema, naungana na taarifa ya Kamati kwamba tuongeze shilingi 50 kwa mara nyingine kwenye mafuta ya dizeli na petroli. Tulifanya mwaka jana zimepatikana fedha kiasi fulani na zimetufikisha pazuri na sasa naomba tena tufanye hivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukisema hapa, tulivyoanzisha Wakala wa Umeme Vijijini tulifanikiwa sana na hivi karibuni kwenye barabara tumetengeneza TARURA na hapa tulisema tuanzishe Wakala wa Maji Vijijini, tunaomba hili jambo likamilike. Najua Serikali inasema kwamba mchakato wa kuanda wakala huo unaendelea, tunaomba basi ifanyike haraka ili tuone manufaa tuliyoyakusudia kwa sababu tunaamini tukiwa na wakala unaosimamia maji vijijini tutafika mbali zaidi kwa kasi kubwa kuliko ilivyo sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu skimu za umwagiliaji, narudia hoja yangu ya kila mwaka, ukisoma hata Hansard utaona, nadhani Wizara ya Maji mnanisikia vizuri, tumeongea na watendaji, sina hakika kama mnayo inventory ya miradi ambayo Serikali ilishaianzisha lakini ikakwama na haiendelei. Kwangu wamesema kuna huo Mradi wa Katunguru, kwa nini fedha mlizoziweka pale shilingi milioni 700 hamuongezi tuukamilishe kwa sababu ulikuwa unahitaji shilingi bilioni 2.5.
Mheshimiwa Spika, nimepata maelezo kwamba wanafanya uchambuzi kwanza waone hatua za kuchukua, nasema kwa niaba ya wananchi wa Sengerema tukamilishe uchambuzi huu haraka halafu mradi uendelee kwa sababu shilingi milioni 700 zilizowekwa pale ni kama zimetupwa na sisi hatuamini kama Serikali ilikuwa nia ya kutupa fedha hizo. Kwa hiyo, naomba sana huu Mradi wa Katunguru tuukamilishe.
Mheshimiwa Spika, mawili ya mwisho, moja, taarifa katika ukurasa wa 97 Serikali imetukumbusha Waheshimiwa Wabunge hapa madeni ambayo taasisi zake zinadaiwa na hasa hizi Mamlaka za Maji kwenye maeneo mbalimbali imewasilisha madeni hayo Wizara ya Fedha ili yalipwe juu kwa juu. Nazungumza hili nikikumbushia kilichotokea mwishoni mwa mwaka jana na mwazoni mwaka huu, Halmashauri nyingi ziliathirika ikiwemo Sengerema, wananchi waliadhibiwa na kama tunavyofamu hakuna fidia, wananchi wameumia kwa makosa ambayo hayakuwa ya kwao. Kwa yale madeni ya Serikali tunaomba jambo lile lisijirudie na niipongeze Serikali kwa kuonesha hapa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho kabisa siyo kwa umuhimu, miradi mingi hapa tunalalamika Waheshimiwa Wabunge siyo kwa sababu haina wakandarasi mingi ina wakandarasi lakini certificate walizonazo ambazo wamekuwa wakizileta kwa utaratibu wa kawaida wapate huduma waendeleze kazi zile hazijalipwa...
(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Mheshimiwa Spika, naomba certificates ambazo zimeshaletwa Wizara zilipwe ili miradi iendelee.
Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja.