Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii nami kuchangia jioni hii ya leo. Kwanza nipongeze Wizara kwa juhudi mbalimbali ambazo inazifanya katika kuhakikisha kwamba inatatua changamoto za maji ambazo zipo katika maeneo yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, wengi wamezungumza juu ya tatizo la maji katika maeneo yetu na mimi nilipata bahati kuwa katika Kamati hii ya LAAC, tulibahatika kwenda kule Mbeya tukaenda kujionea hii miradi ya maji inavyotekelezwa. Tulienda pale maeneo fulani yanaitwa Kyela na sehemu moja panaitwa Tukuyu. Kuna fedha zilitengwa kule, katika usanifu zikahitajika kama shilingi bilioni moja mradi utekelezwe. Mradi ule umeenda ukakwama katikati, wakafanya tena wakataka kama shilingi bilioni nne hivi. Mradi ule wakagawa kwa wakandarasi wengi sana lakini at the end of the day hakuna ambacho kimefanyika mpaka siku tunakwenda kama Kamati kwenda kushuhudia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukatoka pale tukaenda Tukuyu, tulivyofika tukakuta story ni ile ile iliyoko Kyela iko Tukuyu, shilingi bilioni moja imeenda shilingi bilioni nne, shilingi bilioni nne ikaenda shilingi bilioni saba. Wamegawanyishwa wakandarasi; mkandarasi huyu kafanya kwa hatua fulani , mwingine ameingia mitini, yaani ni kama vile mchezo fulani ambao ndiyo yale yaliyokuwa yanazungumzwa hapa na waheshimiwa wenzangu hapa kwamba ni kama kuna ka-chain ambako kuna fedha zinatiririka zinaliwa na kama kuna- hang yaani hakuna ile kunakuwa kama sintofahamu na miradi hii imekuwepo ndani ya nchi yetu yote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yaani hata juzi walikuja Kamati ya LAAC pia kukagua mradi wa maji Wilaya ya Igunga. Walienda kijiji kimoja kinaitwa Blangamilwa tulipata fedha lakini ni zaidi ya shilingi milioni 700. Katika hii juzi iliyokuja shilingi milioni 900. Wameenda kuangalia utekelezaji mabomba yaliyowekwa ilitakiwa wajenge matenki ya kuhifadhia maji, wameenda kununua matenki ya shilingi laki tatu/tatu kaweka matenki mawili. Ni jambo la aibu kwenye miradi hii ya maji ni janga lingine la kitaifa kwenye hii miradi ya maji ni janga la kitaifa.
Mheshimiwa Spika, tumeona tunaunda tume mbalimbali kufuatilia, Tume ya Makinikia, sijui Tume ya Madini ya Almasi; hebu sasa nikuombe, na juzi tumemsikia Rais alipiga simu pale kila mmoja akamwagiza Katibu Mkuu aende kwenye kile kijiji kutatua tatizo la maji kwa mkandarasi yule. Nikuombe tuisaidie Serikali tuunde tume ifuatilie miradi ya maji nchi nzima ilete taarifa na tutoe way forward ambayo itaweza kusaidia hii Serikali wapi twende. Nimekusikia ulipokuwa unasema hawa watu ni wapya. Ni kweli Mheshimiwa Waziri ni mpya, Naibu Waziri mpya hata Katibu Mkuu ni mpya. Sasa kwa sababu ya upya wao tuwasaidie kuhakikisha kwamba wapi tulikosea, wapi tupo, wapi tunatakiwa twende kupitia miradi hii ya maji na itatatua tatizo ambalo tunalo katika miradi yetu ambayo tunayo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tunazungumza kwamba Wizara ya Maji haina fedha, lakini hata fedha zilizokuwepo zinazopelekwa ndivyo zinavyoliwa. Leo mimi binafsi naunga mkono tuongeze fedha shilingi 50 iwe shilingi 100 katika kodi ya mafuta, lakini kwa utaratibu huu ambao uliokuwa unaendelea na ukaendelea maana yake tutaweza kuongeza fedha nyingi zaidi.
Mheshimiwa Spika, kwa utaratibu huo huo ambao tunaushuhudia katika maeneo mbalimbali ya ubadhirifu wa fedha hizi za umma unavyojitokeza iko haja ya Bunge kuchukua hatua na kuisaidia Serikali katika utatuzi wa miradi hii ya maji ambayo…(Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilitaka kuchangia, Mheshimiwa Waziri alikuja jimboni kipindi ambacho akiwa Naibu Waziri wa Maji. Alikuja akatembelea Choma cha Nkola akaona mbuga kubwa ya ulimaji wa mpunga ambayo ilivyokuwa ikistawi mpunga na aliona maeneo ambako bwawa kubwa lilikuwa limekuwa designed kwa ajili ya kuchimbwa na akaahidi kulifuatilia. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwaka jana nilibeba documents zote za feasibility study ambazo zilifanyika kwa ajili ya uchimbaji ule wa bwawa. Bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja kama Naibu Waziri. Leo amekuwa Waziri kamili, kwenye kitabu hiki nilikuwa nataka kuangalia angalau nione labda ametenga sasa fedha za kuanzia uchimbaji wa bwawa lile, sijaona sehemu yoyote ambako ameweka na ukizingatia tunapata mvua na mvua ni nyingi. Sasa tunapoziacha zinapotea na mbuga tunayo kubwa maana yake uzalishaji unapungua badala ya kuongezeka na kama tuna mbuga tungeitumia vizuri tukazalisha mpunga kwa wingi tukaweza kuuza ndani na nje ya nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, nimuombe Waziri alichukulie hili suala la bwawa kwa uzito wake wa hali ya juu sana. Hili suala la bwawa, tuna maeneo mengi ya uchimbaji wa bwawa, tunaweza tukachimba bwawa kubwa pale Choma ambapo tayari documents zote anazo mpaka na Mwenyekiti wa Umwagiliaji Taifa alimwita hapa Dodoma kwa ajili ya kulifanyia uchambuzi wa kina tupate fedha, lakini sijaona. Hata ukienda Ziba pale tuna maeneo makubwa sana ya uchimbaji wa mabwawa na maji ni mengi yanapotea pale, tungechimba sisi bwawa lingine pale Ziba, lakini tungechimba bwawa lingine pale Simbo ambako lingeweza kusaidia kilimo cha umwagiliaji ambacho kingeondoa tatizo la njaa. Katika nchi yetu kuwa na njaa ni aibu.
Mheshimiwa Spika, sehemu nyingine ambayo nilitaka kuchangia ni kuhusu wakandarasi, sasa hivi wako site wanafanya kazi ya usambazaji maji katika miji midogo midogo. Kwa mfano kuna mkandarasi anafanya kazi ya usambazaji maji katika Kijiji cha Isenegeja Kata ya Mwisi amesha-raise zile certificate Wizarani shilingi milioni 180 haijatolewa leo ni muda mrefu. Sasa huyu mkandarasi atasimama na akisimama maana yake atachelewa ataacha kufanya kazi halafu vile vifaa vilivyopo vitaibiwa na vikiibiwa maana yake mradi utaanza kupoteza mwelekeo.
Mheshimiwa Spika, niombe sasa wizara zile certificate ambazo zimekuwa raised pale Kata ya Mwisi na katika Vijiji vile vya Mwamala, Mwakabuta na Mangungu certificate zake ambazo zipo wizarani nimuombe Waziri atoe go ahead ili hawa wakandarasi waendelee. Kwa sababu tunapochelewesha inaweza kusababisha upotevu wa vifaa ambavyo tayari viko katika maeneo yetu. Nimuombe Mheshimiwa Waziri alichukue hili na alifanyie kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, lingine ambalo nilikuwa napenda kuchangia kwa usiku wa leo, katika maeneo yetu yako maeneo ambayo visima vinachimbwa na maji tunapata kwa kiwango fulani. Tafiti zimefanyika katika baadhi ya maeneo imebahatika kuna sehemu kuna maji, tunaweza tukapata, na wao pia wame- raise certificate ambazo ziko wizarani. Nilikuwa nimuombe tu Waziri kwamba aweze kutoa go ahead ili hizi kazi ziweze kufanyika na wananchi waweze kupata maji katika yale maeneo ambako utafiti umefanyika na maji yamepatikana. Tunaishukuru Serikali mradi mkubwa wa maji ya Ziwa Victoria unatoka sasa Nzega unakwenda Igunga na baadhi ya vijiji vyetu vitapata maji.
Kwa hiyo ni shukrani pekee ziende kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli; lakini pili na watu ambao wako wizarani pale kwa maana ya Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Timu yao nzima kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa ukaribu mradi huu uweze kutekelezwa kwa umakini sana.
Napenda kuunga mkono hoja ahsante sana.