Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa ambayo tumeipata kuja angalau kujibu hoja za baadhi ya Wajumbe kwa maana ya Wabunge ambao wamechangia. Mpaka sasa waliochangia kwa kuongea ni 15 na waliochangia kwa maandishi ni 13.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini, baada ya mabadiliko madogo ya Bazara la Mawaziri, basi aliendelea kuniacha katika Wizara hiyo ili niweze kuendelea kushirikiana na Mheshimiwa Lukuvi. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Waziri wangu ambaye siku zote amekuwa akinielekeza na kuniongoza vyema katika kutenda kazi na tunawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote ambao wametupongeza kwa sababu tunafanya kazi kama team work kwa maana ya Mheshimiwa Waziri, Katibu Mkuu pamoja na timu yake kule ndani. Pia kwa upande wa Waheshimiwa Wabunge tunashukuru Kamati ambayo imekuwa ikitusimamia na kutuelekeza vizuri. Napenda kuwashukuru pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitaishukuru familia yangu ambayo imenivumilia kwa muda wote pamoja na kufanya shughuli za Kitaifa lakini bado wameendelea kuniamini na kunivumilia. Nawashukuru wapiga kura wangu, muda wote tumekuwa nao na pale ambapo sipo nao basi wanaendelea kunivumilia kwa sababu walinipa dhamana na Mheshimiwa Rais akanipa dhamana nyingine ya Kitaifa, lakini wanalitambua hilo na nawashukuru sana na wengine wako hapa leo kushuhudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi zote zilizotolewa, nawashukuru sana Watendaji wetu wote katika Halmashauri, Manispaa, Majiji na Miji ambao wamebadilika sana katika utendaji kiasi kwamba wanafanya Wizara ionekane inafanya kazi vizuri, lakini ni kwa sababu ya uadilifu wao, wamekuwa wakizingatia yale ambayo tunaelekeza. Ni wachache tu ambao bado hawajakaa sawa, nasi tutaendelea kuwafuatilia ili tuweze kwenda nao sambamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais, kwa namna ambavyo anaendesha Serikali hii ya Awamu ya Tano katika maelekezo na mtazamo chanya wa kwenda kwenye uchumi wa kati, lakini pia tukiwa na kauli mbiu ya Tanzania ya Viwanda. Kwa kweli Mheshimiwa Rais, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri wote tumelibeba hili kwa pamoja na tunahakikisha kwamba uchumi wa kati tutakwenda kuufikia na hasa tutakapotumia rasilimali ardhi vizuri kama ambavyo tunatarajiwa na watu waliotupa dhamana hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na michango yote iliyotolewa, katika kujibu hoja hizi tutazijibu chache kulingana na muda lakini nyingine zote tutazijibu kwa maandishi na Waheshimiwa Wabunge wote watapata nakala zao. Kwa uelewa wangu na nilivyoangalia maeneo mengi ambayo yamezungumziwa, tatizo kubwa liko kwenye uelewa ambapo wananchi wetu wengi hawajaweza kuelewa na ndiyo maana changamoto zinakuwa nyingi. Hawajajua haki zao na hawajajua wafuate utaratibu gani pale ambapo wanatakiwa kudai haki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile uhaba wa vitendea kazi umezungumzwa. Haya yote yanachangia katika suala zima la kupunguza ufanisi katika maeneo yetu. Upungufu wa watumishi vile vile ni changamoto. Kwa hiyo, unapokuwa na mapengo kama hayo, lazima utendaji pia utakwenda kwa kusuasua kidogo kwa sababu ya uwezo mdogo katika Halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa ambazo zimetajwa na Wabunge na ambazo pia Kamati wamezungumzia, nitazijibu kama ifuatavyo kulingana na muda. Kamati yetu inayosimamia Wizara ya Ardhi, Maliasili na Utalii, wamezungumzia suala la pesa kutopelekwa katika Halmashauri zetu. Hili huchangia pia katika utendaji mdogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili tumelichukua na tunasema tutahakikisha kiasi kilichokuwa kimetengwa na wenzetu wa fedha hapa wanasikia, kitakwenda ili kurahisisha kazi za utendaji. Kwa sababu kama tuliwekea bajeti na pesa inakusanywa, basi kadri inavyoingia, ndivyo jinsi tunavyowapelekea ili waweze kufanya kazi zao. Kwa sababu wasipokuwa na rasilimali fedha hapo hapo na upungufu wa rasilimali watu lazima utendaji kidogo utayumba. Kwa hiyo, hili tumelichukua na tunatii maelekezo ya Kamati yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yamezungumziwa masuala mazima ya Shirika la Nyumba. Shirika la Nyumba limezungumziwa pia hata na wachangiaji waliochangia kwa kuongea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Shirika la Nyumba kama ambavyo sura ilikuwa inaonekana, sivyo ambavyo uhalisia wake ulivyo. Kamati inayosimamia imeshuhudia na imelizungumza pia katika taarifa zake. Napenda niwahakikishie tu Waheshimiwa Wabunge kwamba Shirika letu la nyumba pamoja na kelele zilizoko nje, lakini bado lina uwezo wa kufanya kazi zake vizuri. Ukiangalia zile mali walizonazo, thamani yake inazidi shilingi trilioni 2.8 kwa maana ya thamani tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madeni yaliyokuwa yanazungumziwa, shilingi bilioni 249, ukichukua thamani ya rasilimali ya majengo waliyonayo National Housing ukagawia kufanya hesabu ndogo tu, unakuta linaweza kuendesha au kulipa madeni yale mara ishirini zaidi kwa maana ya kwamba lina mtaji mkubwa hasa ukiangalia thamani ya majengo ukilinganisha na madeni ambayo wako nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapenda kuwahakikishia kwamba sura inayozungumzwa nje ni tofauti na uhalisia. Wajumbe wa Kamati wamefika na wameona. Kwa hiyo, napenda kuwahakikishia, changamoto nyingine zilizoko ndani, kwa mfano mmezungumzia suala la Menejimenti pengine, suala la bodi kutokuwepo, haya yote yanafanyiwa kazi na sasa hivi Wizara iko katika mchakato wa kuweza kuona kwamba ni jinsi gani tunaweza kupata bodi nyingine mpya baada ya Mheshimiwa Rais kuivunja ile nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunajua bila kuwa na bodi, kazi haziwezi kwenda vizuri. Kwa hiyo, hili kama Wizara linashughulikiwa kwa haraka na tutakwenda kupata taarifa siku siyo nyingi pale ambapo masuala ya vetting yatakuwa yamekamilika. Tukumbuke hili shirika ndiyo limebeba dhamana ya Wizara, ndiyo hasa ambalo tunatarajia liweze kumkomboa Mtanzania wa kawaida ukiacha haya mashirika mengine ambayo nayo yanafanya suala la uendelezaji miliki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, tunahitaji Watanzania wawe na makazi bora na makazi ambayo yamepangika. Kwa hiyo, hili tumelibeba na tunalifanyia kazi kama ambavyo inatakikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Lupembe amezungumzia suala la nyumba kuwepo na kwamba hazipati wanunuzi. Naomba niseme tu kwamba, katika suala zima la ujenzi wa nyumba, kuna Halmashauri ziliomba ikiwemo ile ya Mpanda kule Katavi, lakini kuna nyingine walijengewa baada ya National Housing kuweza kupata maeneo kule.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa zile Halmashauri ambazo ziliomba, basi zitekeleze malengo yake, kwa sababu, tumeshatoka kwenye kulazimisha kwamba watu lazima wanunue, suala la msingi sasa hivi, National Housing wana product tatu kwa maana ya kwamba unaweza ukawa mpangaji mnunuzi; unalipa kidogo kidogo baadaye nyumba inakuwa yako. Unaweza ukainunua moja kwa moja wewe mwenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, haya yote yanawezekana, lakini kikubwa tunachotakiwa, pale ambapo Halmashauri inahitaji, tunaomba sana mikataba iwe kamili na muweze kumaliza gharama hizo na kuweza kuchukua zile nyumba. Nawapongeza wenzetu wa Uyui, ndiyo Halmashauri pekee inayoongoza kwa kununua nyumba nyingi ukilinganisha na Halmashauri nyingine, ikifuatiwa na wenzetu wa Busekelo, Mvomero, Geita na Halmashauri nyingine ambazo zimeweza kuchukua nyumba hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumziwa suala la manunuzi kwamba pengine utaratibu siyo mzuri. Naomba niwaambie, suala zima la manunuzi katika Shirika la Nyumba, linazingatia sheria zilizowekwa katika kumpata mnunuzi. Tuzingatie kwamba Shirika hili pia mbali na kuwa Shirika, lakini bado lina Taasisi mle ndani ambazo zimeandikishwa kisheria na zinatambulika. Zinapoingia kwenye mchakato wa kutaka kujenga, basi na wao wanatathiminiwa kama wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, suala la kupata Wakandarasi linazingatia sheria na hakuna mahali ambapo panakiukwa. Kwa hiyo, hili tunalizingatia, tunalifuata na tunaheshimu ushauri wa Kamati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imezungumzia suala la ukusanyaji wa mapato kuonekana kwamba pengine linasuasua na mapato hayapatikani. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa sababu katika suala zima la ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi, aliweza kutoa fursa kwa wananchi ambao walikuwa wamelalamikia kwamba pengine wanapokwenda pamoja na tatizo la EFD Machines na mitandao katika Halmashauri zetu, walikuwa wanapanga foleni kubwa sana, wanashindwa kulipa kwa wakati. Akatoa miezi minne, lakini bado akaongeza mwezi huu wa Tano ambao unaokwenda kwisha kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba muda ulioongezwa unatosha sana kwa wenzetu kuweza kutimiza wajibu wao kulipa kodi. Nami niseme kwamba baada ya kesho tunaomba sana Halmashauri zichangamkie fursa hii ya kuhakikisha kwamba inawabana wale wote ambao hawajaweza kuzingatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna changamoto chache zinazoletwa na Wajumbe na Waheshimiwa Wabunge kwa kulalamika kwamba pengine gharama ni kubwa. Nadhani gharama siyo kubwa kiasi kile ambacho wanafikiria, lakini unapoona una changamoto kwenye invoice yako, tujue tatizo ni nini? Kwa sababu, suala la ardhi liko fixed, halipunguzwi wala halifanywi chochote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoweza kuangalia, ni lini wewe ulitakiwa kulipa na umelipa wakati gani? Kwa hiyo, interest inapigwa kila mwezi asilimia moja kulingana na wewe ulivyochelewa kulipa. Kwa hiyo, lazima tulione hili kwamba pia tunao wajibu wa kuzingatia muda wa kisheria ambao unatutaka kuweza kulipa madeni ambayo tunakuwa nayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala zima la Mabaraza ya Ardhi ambayo yamezungumzwa. Nasema Mabaraza ya Ardhi mpaka sasa tunayo 97, lakini yanayofanya kazi ni 53, kwa maana ya kwamba yapo na Watendaji. Mpaka sasa hivi tuna kibali cha kupata Wenyeviti wa
Mabaraza 20 na tuna imani wakija hao wataweze kutupunguzia ile adha iliyokuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilonalo, kila Mheshimiwa Mbunge akinyanyuka, akiongelea Baraza, kama haliko kwake, kama wana-share labda Wilaya mbili, anataka liende kwake. Naomba tutambue kwamba Baraza linakuwepo pale kulingana pia na idadi ya mashauri au kero zilizopo pale. Kwa sababu hata ukikuta kwamba Mwenyekiti anahudumia Mabaraza matatu au manne, kuna Baraza lingine unaweza kukuta kwa mwaka wana mashauri yasiyofika 200, lakini Mabaraza mengine unakuta kuna mashauri yanakwenda mpaka 1,000 na kitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ukikuta kwamba Mwenyekiti anakuja mara moja moja ni kutokana na wingi wa mashauri yaliyoko katika maeneo mengine ukilinganisha na ya kwako. Kwa hiyo, tunaomba tu tuvumiliane katika hili. Pia Wizara imetenga shilingi milioni 165 kwa ajili ya kufanya ukarabati katika maeneo mengine ambayo tunatarajia kuwa na Mabaraza. Kwa hiyo, nawaomba tu mvute subira kwa sababu tayari kama Wizara tumeshajipanga kuweza kuona ni jinsi gani tutaondoa hii adha ambayo imekuwepo katika suala zima la kuweza ku-solve matatizo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie mipaka ambayo imezungumzwa katika suala zima la kulinda mipaka yetu. Wamezungumzia suala la usalama, hakuna ile njia ya kupita pengine kuweza kujua ni jinsi gani ambavyo unaweza ukalinda usalama wa mipaka yako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kusema, kama tulivyojibu swali moja wakati limeulizwa hapa Bungeni, katika mkutano huu, tayari Wizara kwenye mradi pesa za maendeleo tulizokuwa tumeomba kwa mwaka huu wa fedha unaoisha, mlituidhinishia shilingi bilioni nne na tulizipata zote na kazi hiyo imeshaanza. Wanasafisha masuala ya mkuza ili ukae vizuri, kuweza kujua, mipaka ya nchi na nchi, lakini pia makubaliano ya kiasi gani kiachwe kutoka kwenye eneo la Nomad’s land kwenda kwenye eneo lingine, tayari wenzetu wa Uganda tulishaingia nao katika ile protocol kwamba ni mita 30. Zoezi la Kenya lilikuwa linaendelea. Upande ule wa Tunduma na Zambia kule tayari yalishazungumzwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa ambalo nataka kuwaambia ni kwamba, tunachohitaji kama Watanzania ni kuzingatia yale ambayo tumekubaliana kama nchi na nchi. Kwa upande wa Kenya na Tanzania bado kuna mazungumzo yanaendelea. Sasa suala la barabara ambayo itafanya kuwe na movement nzuri ya kuweza kukagua ule mpaka, hili linafanyiwa kazi. Tujue kwamba sekta ya barabara ni Wizara nyingine inayohusika lakini kwa sababu tunafanya kazi kama Serikali, tunalichukua na tunaenda kulifanyia kazi na tayari wenzetu ambao tulikwenda kukagua mipaka, tuliwaomba pia Halmashauri kwa sababu zile ni barabara za Halmashauri. Basi ihakikishwe angalau kunakuwa na upenyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inakosekana heshima ya nchi pale unapokwenda eneo, halafu ili uangalie mpaka wako lazima uingie nchi nyingine; na kama unapeperusha bendera, maana yake uishushe halafu uingie, ukitoka tena kule upandishe, inasumbua. Hilo tumeliona, tumepokea maoni ya Kamati linafanyiwa kazi na tunawaahidi litakwenda kufanyiwa kazi vizuri. Nawaomba tu wenzetu wa Halmashauri wajue yale pia ni maeneo ya usalama wao. Kwa hiyo, wanapochonga barabara zao, wazipe kipaumbele barabara za mipakani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala zima limeongolewa la ukamilishaji wa maandalizi ya Sera ya Nyumba ya Taifa. Sera hiyo imefikia katika hatua nzuri. Sasa hivi tuko kwenye kukusanya maoni ya wadau. Pale ambapo tutakuwa tumeshakusanya wadau kuona wanaiboreshaje ile sera, italetwa hapa mtaweza kuiona, tutaendelea katika utaratibu wake wa kuandaa. Kwa sababu itapelekwa Wizarani kwa ajili ya ukamilishaji ili tuweze kujua, kwa sababu huwezi kutunga sera ambayo haihusishi wadau. Kwa hiyo, kama Wizara mnakuwa na draft ambayo mnaona kwamba sera itapendeza kama ikiingiza vitu fulani. Ili iboreshwe vizuri, ni lazima maoni ya wadau yaheshimike. Kwa hiyo, Sera ya Taifa ya Nyumba imeshafikia hatua ya kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali na lengo likiwa ni kuiboresha. Itakapokuwa tayari, taarifa zitaletwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala limezungumzwa kuhusu tozo ya mwanzo kwa ajili ya kupata kiwanja (premium). Kweli watu wamepongeza na kusema ilitoka 15 ikaenda 7.5, ikaenda 2.5 na Kamati sasa imependekeza ishuke. Naomba kusema tu kwamba kama Wizara tulishaliona hilo na kadri unavyozidi kuwapa nafuu wananchi ndivyo jinsi kazi inavyozidi kuongezeka. Hata kazi ya urasimishaji iliyofanyika Mwanza mpaka kuongeza lengo, walipewa viwanja 35,000, lakini mpaka sasa wamevuka lengo wana 42,563 ni baada ya kupunguza kutoka 7.5 kwenda 2.5 ambapo Mheshimiwa Waziri ambaye ndio ana mamlaka hiyo aliweza kupunguza na kasi ikaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tumeipokea, kweli tumeona matokeo chanya pale ambapo unampa nafuu mlaji wa kawaida. Kwa hiyo, hili tumelichukua kama Wizara, tutaona namna bora ya kuweza kuhakikisha tunawapunguzia gharama wananchi wetu ili wengi waweze kumiliki maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe rai tu katika Halmashauri zetu, pale ambapo mnafanya zoezi la urasimishaji, zoezi hili siyo endelevu kama tunavyofikiri. Kwa ile miji ambayo imeshapanga mipango yake kabambe, pale ambapo mpango kabambe unaanza kutumika, unless uwe uliingiza wakati unapanga mpango wako kabambe, ukasema kutakuwa na sehemu kinaendelea na urasimishaji kama wenzetu wa Singida walivyofanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama haikuwa katika mpango huo, tunapoanza kutekeleza mpango kabambe maana yake zoezi la urasimishaji linakuwa halipo. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Halmashauri zote ambazo zina zoezi la urasimishaji na wakati huo huo bado kuna zoezi la master plan ambazo amekuwa anaziandaa, lazima kasi iongezeke na wananchi waelimishwe watambue kwamba unapokuwa unatekeleza mpango kabambe huwezi kuendelea kurasimisha kule ndani, utakuwa unagonganisha mambo ambayo siyo sahihi. Vinginevyo, vikiingiliana ina maana utakapokuja kupimiwa ni lazima uende sambamba na mpango kabambe ambao umeandaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitoe rai tu kwa Halmashauri zetu kuwaelewesha wananchi wetu waweze kujua. Maeneo yale lazima tuwaelimishe wananchi wetu waweze kupata namna bora ya kuwa uhakika wa milki zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, limeongelewa suala la migogoro katika vijiji vinavyopakana na hifadhi. Maeneo mengi yenye migogoro ya hifadhi, tunashukuru kwamba sasa kuna mradi ambao Idara yetu yetu ya Mpango wa Matumizi ya Ardhi inapofanya kazi pamoja na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa maana ya TANAPA wanakwenda kupima vijiji 392. Vijiji vyote vinavyozunguka maeneo hayo katika hizi mbuga ambazo ziko kama nane ambazo zinakwenda kufanyiwa kazi hiyo, jumla yake viko vijiji 427, lakini huu mpango ni wa kama miaka mitatu. Kwa hiyo, tunakwenda kupima maeneo hayo, yanapangiwa mpango wa matumizi bora ya ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani wakishafanya ile, hapatakuwa na kelele tena kwa sababu wananchi wenyewe wanashirikishwa. Hatua iliyoko sasa hivi ni kuelimisha wananchi namna ambavyo mpango huu utakwenda. Wameanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya na baadaye watashuka kwenye vijiji vyenyewe ili viweze kushiriki. Hati zinazotolewa kule zinatambulika na mabenki. Tunayo mabenki zaidi ya 13 mpaka sasa yanatoa pesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama mmesikiliza hotuba ya Mheshimiwa Waziri kipindi hiki, tayari zaidi ya shilingi bilioni moja zimetoka kwa kutumia hati miliki za kimila. Kwa mwaka wa fedha uliokwisha wa 2016/2017, mabenki yalishatoa pesa zaidi ya Sh.59,164,000,000/=. Kwa maana hiyo ni kwamba hati hizi zinatambulika na siyo kwamba hazitambuliki kama ambavyo wengine wanafikiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nililiruka suala la Mheshimiwa Mtuka, ambapo aliongelea kuhusu mpango kabambe. Naomba kusema, maandalizi yoyote au mamlaka ya upangaji miji ni Halmashauri zenyewe husika. Kwa hiyo, Halmashari yoyote ikishaona kwamba sasa inahitaji kupanga mji wake vizuri, kuwa na mpango kabambe wa miaka 15, 20, wanatakiwa wao kuanza kuja na hoja yao, halafu Wizara itawasaidia pale watakapoona kwamba pengine wamekwama wanahitaji utalaam. Kwa hiyo, mchakato lazima uanzie kwenye Halmashauri husika kwa sababu ndizo zenye mamlaka ya kupanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba tu kupitia hoja ya Mheshimiwa Mtuka, maeneo ambayo pengine walitajarajia kuwa na mpango kabambe wanafikiri ni Wizara inayoanzisha, mnatakiwa wenyewe muanze, Wizara tunakuja kusaidia pale ambapo pengine mtahitaji utaalam, kwa sababu lazima pia Wizara ipitishe, utafika kwenye Wizara, utashauriwa pale panapohitaji kushauriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza miji ambayo tayari mipango yake kabambe imeshazinduliwa na inafanya kazi. Miji ya Musoma, Singida, Mtwara ambao wote wameshamaliza na kazi inaendelea. Mwanza na Arusha nayo iko katika utaratibu, wenzetu wa Dar es Salaam nao bado, mchakato nadhani haujakaa vizuri sana lakini, wako hatua hiyo. Tukishakuwa na hilo itatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ILMIS ambalo mjumbe amepongeza, niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri wakati anawasilisha hotuba yake, ameongelea faida ya kuutumia mfumo huu na namna gani ambavyo tunaweza pia tukadhibiti wale watumishi ambao hawakuwa waadilifu sana, tukadhibiti masuala ya kuchakachua nyaraka kwa kumwagia chai, majani ya chai na nini. Ukishakuwa katika mfumo huu huwezi ku-temper nao hata mara moja. Kwa sababu kazi atakayeifanya mtu Wilayani, moja kwa moja Wizara inaona. Kwa hiyo, mpango huu umeanzia Kinondoni lakini utakwenda utasambaa kwa nchi nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hili tuelewe tu kwamba mfumo huu wa utunzaji wa kumbukumbu umeanza kwa majaribio, lakini utakwenda katika maeneo yote ili kuweza kuona ni jinsi gani ambavyo tunaweza kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la upungufu wa Watumishi katika maeneo yetu na vitendea kazi; naomba nimshukuru tena Mheshimiwa Rais kwa namna ambavyo amewarudisha Watendaji wa Halmashauri katika Wizara. Naomba niseme, kama Wizara tutakwenda kulisimamia hili, tutapitia watumishi wote wa sekta hii walioko kwa nchi nzima na kuweza kuwapanga katika utaratibu ambao uta-balance ili angalau kila Halmashauri iweze kuwa na uhakika wa kuwa na watumishi. Kwa sababu ni kweli kuna maeneo hawana Watumishi, kuna maeneo mengine hawana Watumishi wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili tutaangalia kwa upya tukishapata ikama yao wako kiasi gani na mahitaji ya kila Halmashauri then tuanze kuwapanga kwa uchache wao wakati huo tunaangalia namna bora ya kuweza kuongeza idadi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la vifaa vya upimaji kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameongea kwenye hotuba vitakuwepo by July. Nawapongeza sana, pamoja na kwamba na-declare interest kwamba mimi natoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, Ilemela wameweza kununua vifaa vyao wenyewe na vinawasaidia katika kasi ya upimaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tu Halmashauri nyingine, unapokuwa na vifaa vyako, unaepuka pia zile gharama ambazo zinakwenda kufanya gharama ya upimaji iwe kubwa. Kwa hiyo, pamoja na juhudi zinazofanywa na Wizara, pamoja na kuimarisha kanda zetu lakini bado pia kama Halmashauri tunahitaji kuona kipaumbele cha upimaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fidia katika malipo, naomba sana na tumekuwa tukilizungumzia hili kwamba hatutakiwi kuwapunja wananchi; na mwananchi yoyote hataruhusiwa kutoa ardhi yake bila fidia, unless kuna suala ambalo ni la Kitaifa sana na halina mjadala katika suala hilo, bado kama Serikali tutazungumza nao na kuweza kuonesha umuhimu wa ule mradi ili aweze kuridhia. Ila hakuna kuchukua ardhi ya mtu bila kulipa fidia yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kukushuru sana kwa kunipa fursa ya kujibu machache. Kama nilivyosema, mengine tutajibu kwa maandishi, nimalizie tu kwa kuwashukuru wote na kuwatakia kila lililo jema katika Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani, lakini pia tuombe ushirikiano wenu ambapo sifa zote mnazotupa hatuwezi kuzipata kama hatuna ushirikiano na ninyi. Nasi tunaahidi kuendelea kuwatumikia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.