Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Geita Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya njema na nimepata nafasi ya kuchangia hotuba hii ya Wizara ya Madini. Nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Manaibu wake na Watendaji wake wote kwa kazi nzuri ambayo wanaendelea kuifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza pia Serikali yangu kwa sheria ambayo tuliitengeneza mwaka 2017 ambayo imeenda kuboresha kabisa shughuli za madini na mpaka sasa tayari waombaji zaidi ya 5,000 kwa taarifa ambazo tunazo, waliyokuwa wamekaa zaidi ya mwaka mmoja kusubiri license wameshapata, nawapongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kama alivyosema Mheshimiwa Waziri kwenye hotuba yake kwenye suala la CSR, tulipitisha Sheria ya CSR hapa mwaka jana na tukaitengenezea utaratibu ambao utawahusisha Halmashauri ili ziweze kushiriki pamoja na migodi kwenye matumizi ya pesa hasa katika kuchambua miradi na kukubaliana na mgodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali, nadhani kuna maeneo ambayo hatukuyaona vizuri, sisi katika maeneo ya migodi tulikuwa na tatizo la migodi hii kuja na mahesabu makubwa sana yanayoonesha wametumia kwenye miradi, wakati miradi iliyofanyika ni midogo na tatizo hili linaonekana bado linaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Naibu Waziri alikuja Geita akaomba watu wa Mgodi wampe orodha ya pesa ambazo zimetumika na miradi, hawakumwambia mradi huu wametumia shilingi ngapi. Nadhani angeona suala hilo angeshangaa sana. Mwaka huu baada ya vikao na Halmashauri tumeona tatizo hili litakuja kuwa kubwa zaidi. Kwa mfano, katika hesabu ambayo Halmashauri ya Mji wa Geita wametuletea kwenye miradi ambayo tumependekeza, cement wao wanasema ni Sh.48,000/= mfuko, wakati pale mjini mfuko ni Sh.18,000/=. Bati la gauge 28 wanasema ni Sh.78,000/=, wakati bati pale mjini ni Sh.22,000/= bati moja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nondo ya milimita 16 wamewekwa Sh.52,000/= na kokoto trip moja wameweka Sh.80,000/=. Sasa unaona sheria hii imewapa loophole ya kuendelea kudanganya kama ilivyo kwenye transfer pricing, matokeo yake itakuwa ni Kampuni zao zile zile ambazo wanaziteua, zinawauzia material kwa bei kubwa mara nne zaidi. Mradi wa shilingi milioni 10 watajenga kwa shilingi milioni 80.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri na Waziri wa Sheria tutazame upya sheria hii ili ikiwezekana Halmashauri Kitengo chake cha Manunuzi kishiriki kwenye Procurement System nzima kwa bei ambazo ni shindani kwenye maeneo husika na kwa kutumia wazabuni na local contents. Bila kufanya hivyo tutarudi kule kule tulikotoka, takwimu zitaonesha mabilioni ya shilingi lakini miradi iliyofanyika ni midogo na pesa zote zinarudi kule zinakotoka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala langu la pili, ni suala ambalo Mheshimiwa Naibu Waziri pia alikuja Geita kulishughulikia. Pale Geita tunao mgogoro mkubwa wa Mgodi wa GGM pamoja na wananchi wa Geita pale, nyumba zaidi 800 zimepasuka kutokana na milipuko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna wananchi wengi ambao wanaishi kwenye vigingi vya migodi kwa zaidi ya miaka 18. Mheshimiwa Waziri alikuja akatoa maelekezo mazuri na kabla ya maelekezo yake Mgodi wenyewe ulifanya study kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Waziri aliyekuwepo, Waziri Kalemani alitoa maelekezo watu wa GST wakafanya study kuonyesha sababu za mipasuko kupitia GST, taarifa zipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti,Ametoa maelekezo lishughulikiwe tangu mwezi wa pili, mpaka leo ninavyozungumza, wananchi wa Geita hawajui hatma ya maagizo ya Mheshimiwa Waziri kwa sababu hawaoni kinachoendelea. Wenye nyumba zile, wengine wanakufa, nyumba zile zilizopasuka zinaanguka, ripoti zote mbili za Serikali zipo mezani, lakini mambo hayashughulikiwi na hayaendi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali, Mheshimiwa Waziri sehemu ambazo tuna migogoro ya muda mrefu kama Geita, kabla Mheshimiwa Waziri hajaja kwenye ziara ya Jimbo langu iwe ni vyema kupitia zile documents zilizopo mezani kwake na kujua wenzake walitoa maagizo gani; kuliko kuja kutoa maagizo yale yale yaliyotolewa na Waziri mwingine na yasitekelezwe, wananchi wanaona kama vile Mgodi huu unaidharau Serikali. Tunao wananchi katika maeneo ya Magema, tunao wananchi ambao wameteseka kwa muda mrefu sana na hawajapata haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala lingine la tatu. Katika eneo la Mgusu tunao wananchi watatu ambao wamekuwa na kesi na Mgodi tangu mwaka 1995. Majaji sita ambao wameshiriki kwenye kesi ambalo lilikuwa ni kosa la Serikali, Serikali ilikuwa imewapa license wananchi watatu; Felix Isidory Ngowi, Ezekiel Magese na Philipo Paskali na walikuwa wanaendesha leseni zao za utafiti na uchimbaji mdogo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa bahati mbaya, siyo kwa makusudi Kamishna akatoa leseni nyingine juu ya leseni zile zikiwa bado ziko hai, wananchi hawa wakakamatwa, wakapigwa, wakafungwa lakini wakaenda Mahakamani. Majaji sita wote wametoa hukumu iliyowapa haki wananchi kwa nyakati tofauti tangu mwaka 2005.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka leo Mgodi unaendelea kuonesha unakata rufaa. Jaji Matupa, Jaji Bukuku, Jaji Mero, Jaji Nyangarika, wote hawa wamewapa haki wale wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha sana ni kwamba hukumu nyingine ya mwisho ilitolewa mwaka 2016 na ikatoa permanent injunction ya kuzuia mgodi kuwaondoa wananchi hao kwenye eneo hilo. Kwa namna yoyote wanapokuwa wanaendelea na kesi nyingine, bado Mkurugenzi wa Mgodi na Polisi na wengine walioko pale wameendelea kuwakamata na kuwafukuza na eneo lile lina wachimbaji wadogo zaidi ya 5,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, kwanza ni aibu kwa Serikali. Majaji hawa wote wameonesha kwamba wachimbaji hawa wadogo wana haki na kosa ni la Kamishna, lakini bado wanaendelea kuonesha kwamba huyu mwenye Mgodi mtu mmoja ana haki ya kuwafukuza watu na kuwanyanyasa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri wananchi hawa wapewe haki yao, wamekamatwa zaidi ya mara 20, wanawekwa ndani miezi sita, Mgodi hauji kuendelea na kesi, wanatoka, wanapigwa, mali zao zinachukuliwa, wanafukiwa mashimo bila sababu yoyote ile ya msingi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa kwa kweli hawana sababu yoyote ile ya kuendelea kuteseka, kwa sababu vyombo vya Sheria; tuna mazoea wananchi wakifukuzwa huwa wanasalimu amri, wanaondoka. Hawa walikwenda Mahakamani wakafuata utaratibu kwa miaka 20 wameipigania haki yao na wameshinda na hukumu wanayo, lakini Mgodi unaendelea kuwafukuza. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri, suala hili lishughulikiwe vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine la nne, naomba kuishauri Serikali, tunao Mgodi wetu wa GGM pale awali ulikadiriwa kuchukua miaka 30 au 25, lakini baada ya sheria hizi mpya tulizozitengeneza, ule Mgodi unaanzisha pits nyingi na wanafanya kama lashing, matokeo yake ninayoyaona, baada ya miaka mitano watafunga Mgodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachoendelea sasa, wakiona tu gharama za kupata madini zimeongezeka, wanahama wanaanzisha pit mpya. Matokeo yake wanakwenda wana-lash badala ya kuchukua miaka 30, tutaachiwa mashimo na mashimo yale ni makubwa, wataondoka kabla sisi wenyewe tuliotarajia kwamba tutachimba madini haya kwa miaka 30 hatujafaidika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iangalie namna ya ku-control. Kuna maeneo migodi inachukua zaidi ya miaka 50 kwa sababu wanalazimishwa kufanya utafiti na kumaliza madini yaliyoko chini. Shimo lililokwenda milimita 200 ukiondoka leo anayekuja hawezi kuchimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho ni suala la GST. GST nawapongeza kwa kazi wanazozifanya, lakini nina tatizo moja na GST. Mwaka 2016 walikuwa kule Bukombe, nami nikaomba leseni kupitia wachimbaji wadogo wadogo wa Jimbo langu kama tulivyoshauriwa na Mheshimiwa Waziri, wakapewa leseni. Utafiti wa GST unaonyesha kuna dhahabu. Wamechimba wamekwenda mpaka mita 100 watu hawapati dhahabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba sana GST, kabla ya kuishauri Serikali iwape wananchi maeneo haya yenye dhahabu, kwa sababu wananchi wanakopa, wanajichanga na pesa zao ndogo, nawaomba GST wahakikishe wanatoa elimu ya kutosha kwamba dhahabu hii ipo umbali gani kwa miamba iliyolala vipi? Tunafika mahali sasa tunaacha kuwaamini, ni bora ukatafute private watu wengine huko waje wakufanyie utafiti kuliko GST kwa sababu wanafanya utafiti wa kijanja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, Mheshimiwa Waziri naomba sana wananchi wangu wa Geita Mjini na wananchi wa Mgusu waweze kupatiwa haki yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.