Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niungane na wenzangu kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia kuwa na afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara hii muhimu. Vilevile pia nami nawapongeza Waheshimiwa Mawaziri ambao wapo sasa hivi katika Wizara hii, lakini tutashauri na kueleza upungufu uliopo, wauchukue na kuweza kufanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya pongezi hizo nawatakia ndugu zangu Waislamu wote Tanzania na duniani kwa ujumla mfungo mwema wa mwezi wa Ramadhani. Pia natoa pole kwa Bunge letu kwa kuondokewa na Mbunge mwenzetu Mwalimu Bilago, Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema. Amina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, nitoe tu nami shukurani zangu vilevile kwa Wizara, lakini naona kuna upungufu kidogo, kwa sababu najua vipo vyama vya wachimbaji wadogo hususan wachimbaji wanawake, lakini sikuona au hawapo kama ilivyozoeleka kwa Wizara nyingine ambapo wahusika wanakuja kama tulivyoona katika uvuvi na kilimo. Kwa hiyo, nieleze kwanza upungufu au changamoto zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tatizo kubwa la mashine za kukata madini katika nchi yetu au hizi wanazoziita mineral cutters, zipo chache. Sasa nazungumzia hili kwa sababu hili tatizo la utoroshwaji wa madini kwa uchunguzi ambao kwa maoni yangu nimeufanya unasababishwa na foleni kubwa ambapo unapokata madini, madini labda ya gram moja yanaweza yakatumia kukata kareti kwa muda wa saa nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa madini yanayochimbwa Tanzania ni mengi, matokeo yake sasa kunakuwa na foleni kubwa katika utakataji madini kama vile ilivyo kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwenye Wizara ya Afya ambapo specimen moja inaweza ikachukua miaka miwili. Sasa inawezekana hii nayo ikawa ni sababu mojawapo ya kutoroshwa kwa madini yetu kwa sababu teknolojia tuliyonayo Tanzania ni ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naishauri Wizara na Serikali kwamba tuondoe au tupunguze kodi kwenye mashine za kukata madini ili ziwepo kwa wingi ili Watanzania sasa waweze kukata madini kwa muda mfupi baada ya kuwapeleka nchi jirani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naliona, ni ushauri wangu kwa Serikali kwamba Chuo cha Madini kinafanya kazi vizuri, lakini ama kipo kimoja au vipo vichache.

Sasa tulipofanya ziara na Kamati yetu ya PIC, tulipofika Shinyanga VETA tulikuta nao wana kozi ya ukataji wa madini. Naishauri Serikali, kwa kuwa Shinyanga VETA imewezekana, basi naamini katika VETA nyingine napo kozi zile zinaweza kuendeshwa. Kwa hiyo, naishauri Serikali iweke kozi za kukata madini katika Vyuo vya VETA. Kwanza, tuzalishe wataalam wengi wa madini ambao watakwenda kuwasaidia wachimbaji wadogo ili wawe wachimbaji bora, waepuke uchimbaji wa kubahatisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, itakuwa ni ajira kwa watu wetu ambao baada ya mafunzo yale naamini Wizara itaweza kuwaajiri na kuwapa shughuli ya kwenda kuwatembelea au kwenda katika maeneo ambayo yanachimbwa madini na kuweza kuwafanya wachimbaji wetu wawe wa kisasa kuepuka kufukiwa na vifusi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo naishauri Serikali, Wizara haina rescue team. Tumeshuhudia mafuriko yaliyoporomoka ndani ya machimbo ya Mererani, mwaka 2016 kama sikosei, walikufa watu wengi tu. Ni kwa sababu kama pangekuwa pana zana za kisasa za uokoaji na kungekuwa na rescue team ambayo ina vifaa vya kisasa, tungeweza kuokoa maisha ya watu wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia hata katika upasuaji wa mawe, kwa mfano, katika kware zilizopo Tanga ilitokea ajali pale, kuna mtu mmoja alilaliwa na jiwe. Kama kungekuwa na Helcopter Ambulance naamini angeweza kuchukuliwa akafikishwa Muhimbili Dar es Salaam angeweza kuokolewa maisha yake. Kwa hiyo, Wizara pia ijitahidi basi iwe na japo Ambulance Helcopter ambayo itaweza kuokoa maisha ya watu wetu pale itakapotokea ajali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulizungumzia ni mabenki kutokuwaamini au kutokuwathamini wachimbaji wadogo. Imezungumzwa hapa kwamba Serikali imeanzisha uwezeshaji wa wachimbaji wadogo na kama sikosei katika kitabu cha Kamati imeeleza kwamba kuna wachimbaji ambao walikuwa wanawezeshwa U$ Dollar 50,000 ambayo ni sawasawa na milioni 100 hadi U$ Dollar 100,000 ambayo ni sawasawa na milioni 200.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika Mkoa wangu wa Tanga napo kuna madini kule ya aina nyingi tu ya vito ambayo nitayataja baadaye. Ningetaka kujua, vigezo vinavyotumika kuwawezesha wachimbaji wadogo hawa kupata Dollar 50,000 na Dollar 100,000 ili na wale wachimbaji walioko Tanga waweze kupatiwa msaada huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo nataka kulijua pia ni idadi ya wale wachimbaji wadogo ambao wamewezeshwa hasa ile Dollar 50,000 na 100,000 ni wangapi; na ni maeneo gani ya machimbo katika Tanzania yetu? Ili tuweze kujua na tunapoulizwa na baadhi ya wachimbaji tuweze kuwapa elimu, wafuate vigezo waweze kupatiwa msaada huo wa Dollar 50,000 na Dollar 100,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yametajwa madini mengi sana hapa, kwa mfano madini ya jasi, yametajwa almasi, dhahabu, tanzanite lakini kuna madini mengine ya thamani ya vito. Kwa mfano, kama vile uranium pia hapa sikusikia ikitajwa taarifa yake, lakini kuna rubby kuna rhodolite, kuna green-garnet kuna green tourmaline na kadhalika. Yangechambuliwa katika takwimu ya mapato tujue kwamba green garnet kwa mwaka huu imeiingizia Serikali kiasi gani? Green tourmaline imeingiza kiasi gani? Rhodolite imeingiza kiasi gani? Rose imeingiza kiasi gani? Sapphire imeingiza kiasi gani? Ingekuwa ni takwimu bora zaidi kwa faida ya vizazi vijavyo na pia kwa faida ya Taifa kujua kwamba, kumbe madini tuna faida nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine nasikitishwa kidogo na hii taarifa ya madini ya bati. Tanzania tulikuwa hatuna sababu ya kuwa na nyumba zilizoezekwa kwa majani, matembe, lakini pia kununua mabati kwa bei ghali. Sasa pana taarifa hapa imeeleza kwenye ukurasa wa 18 kwamba kuna masikitiko yaliyoelezwa na Kamati nami nayaunga mkono kwamba imekosekana fedha za kununua mtambo wa kuchakata bati na vilevile kukosa hati ya uasilia (ICGLR) yaani Certificate of Origin.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza, Wizara inakuwaje ishindwe kupata fedha za kununua mtambo wa kuchakata bati wakati bati ni bidhaa ambayo kwanza ina soko wakati wote? Mabati yanatumika katika ujenzi wa nyumba, lakini pia kwa sasa hivi kwa sheria za ujenzi, kabla ya kujenga lazima uzungushe mabati; na yana soko kubwa ambapo Serikali kama ingekuwa na mtambo huo ingeweza kukusanya fedha nyingi tu ambazo zingesaidia katika matumizi ya masuala mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kujua, je, ni lini Wizara sasa itanunua mtambo wa kuchakata bati? Vilevile, huu mpango mpaka tukashindwa kununua huu mtambo wa kuchakata bati, siyo hujuma za wenye viwanda vya mabati kwamba wanatufanyia hujuma kusudi waendelee kuuza mabati kwa bei ghali? Hilo nalo nitataka jibu lake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, niliona katika taarifa hapa, kuna wanafunzi wa Chuo cha Madini Dodoma. Nafikiri vikwazo vingi na changamoto nyingi katika vyuo ni bajeti kuwa ndogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iongeze bajeti ya fedha katika Chuo cha Madini Dodoma ili wanafunzi wale waweze kujifunza kwa nafasi, lakini pia wasiwe na upungufu na usumbufu katika mafunzo yao. Watakapoingiziwa fedha kwa wakati, naamini wataweza kusoma vizuri na tutazalisha wartaalam bora zaidi.