Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

Hon. Abdallah Majurah Bulembo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Madini

MHE. ABDALLAH M. BULEMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote, nianze kuwapongeza shemeji yangu, Waziri wangu Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa kazi anazozifanya, Naibu Waziri Mheshimiwa Stanslaus Nyongo, Naibu Waziri Mheshimiwa Doto Biteko, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Msanjila na Watendaji wote waliopo ndani ya Wizara hii mpya, nawapongeza sana kwa kazi mnazozifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kuona na kuweza kutenganisha Wizara ya Nishati na Madini. Wizara ya Madini ni Wizara nyeti sana katika nchi nyingi, hapa kwetu sasa imeonesha kwamba tunayataka madini yetu yaweze kuleta faida katika nchi yetu. Pia nizipongeze Tume zote zilizoundwa, Profesa Abdulkarim Mruma, siwezi kumsahau kwa kazi kubwa aliyoifanya, Profesa Nehemia Osoro simjui sana lakini Profesa Mruma tunatakiwa tukupongeze na tukupe hati ya shukrani kwa jinsi ulivyojitolea Utanzania wako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madini katika nchi yetu tulivyoambiwa mara ya kwanza kwamba pato linalopatikana na madini ilikuwa haifikii hata shilingi bilioni moja lakini ukienda kwenye sekta ya madini watu hawa ndiyo wanaosamehewa kodi sana, watu hawa yaani wao ndiyo wao, wale wanaochenjua kidogo ni matajiri, lakini Serikali haipati pesa. Nalipongeza na Bunge kwa kupitisha sheria nzuri sana ambazo zitaongeza mapato kwenye Serikali angalau sekta hii iweze kuchangia uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu rasilimali za nchi yetu zimepotea sana lakini leo mwarobaini umepatikana. Nichukue fursa hii zaidi kuipongeza Serikali yangu ya Chama cha Mapinduzi chini ya Rais Mheshimiwa Magufuli kwa jinsi alivyoweza kuwajali wachimbaji wadogo wadogo. Wachimbaji wadogo wamekuwa wakinyanyasika sana katika nchi yao, wakifukuzwa huku na huku, wakipata taabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna watu katika nchi hii kwa sababu natoka Kanda ya Ziwa kule, hawajui kazi zaidi ya madini. Wakimwambia yako Singida anaenda, Chunya anaenda, wapi anaenda lakini anafukuzwa kila siku. Ombi langu kwa Serikali yangu, hebu hawa wachimbaji wadogo, wapate haki ya kuwa na leseni kwamba kuna mahali wanachimba, wako 500 wako 1,000 wapewe uhalali wa kumiliki eneo lile, liwe la kwao. Hawa wachimbaji wadogo, wanachimba kwenye sehemu unaweza kukuta leseni ya Bulembo mchimbaji mdogo yupo, inaleta tabu kidogo. Kwa sababu ni wenzetu, ni vijana wetu, ni watoto wetu, hebu basi tuwawekee utaratibu mzuri angalau wawe na amani, wakijua tunachimba hapa, magaragaja yako hapa, kila kitu kipo hapa, maisha yao yanajulikana yanavyopatikana lakini sasa wamekuwa ni watu wa kubahatisha. Mmewaruhusu wachimbe lakini kila wanapochimba mishale iko pembeni, bunduki ziko pembeni, hebu wapeni nafasi nzuri ili tuonekane thamani tunayowapa na kuna maeneo wanaenda kufanya hiyo kazi yao ili maisha yao waweze kubadilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni mpya lakini kuna changamoto naomba niwape. Siku za nyuma kuna watu watendaji walikuwa wanakata leseni kama kule kwa Mama Mheshimiwa Wambura au Mheshimiwa Lukuvi, mtu anaweza kutoa hati kwa Bulembo, kesho akatoa kwa Musa kiwanja hicho hicho, ndani ya madini pia neno hilo lipo. Unakuta mtu ana ‘pele’ namba fulani na amemwekea ‘pele’ pale pale mgongoni na hawa watumishi mmewarithi, tunawaomba sana, hatuna mengi ya kusema kwenu zaidi ya kuwashauri, hebu watafuteni hawa watendaji waliofanya makosa yale wawajibike kwa sababu walikuwa na dhamana ya Serikali. Unawezaje ukagawa kitalu mara tatu kwa watu watatu tofauti kitalu kimoja? Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha atuambie na watendaji wale atawafanyaje kwa sababu wataipa Tume hii shida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine naipongeza Tume iliyoundwa chini ya Profesa na wanakamati wake. Nampongeza Rais na Waziri, Tume ile ni muhimu sana kwa sababu sasa mwarobaini umepatikana lakini Tume ile nina uhakika itapata changamoto nyingi sana kwa sababu ni kitu kipya kimekuja kuna eneo lenye matajiri wengi, wachimbaji wa dhahabu ni matajiri. Tungekuwa kule Congo, kuanzia Waziri wa Madini na wenzake wote wangekuwa wamevaa cheni za dhahabu tu, mikono imejaa dhahabu si ndiyo? Eneo hili lina mambo makubwa sana. Sasa mnapoenda ku-deal na wale watu ambao ni matajiri, lazima Tume hii tuiombee wawe serious sana kwa sababu hawa watu kwenye sekta hii ni matajiri sana ingawa Serikali siyo tajiri. Kwa hiyo, walioteuliwa tunawaamini sana, wanaweze kufanya kazi vizuri sana lakini wawape ushirikiano kuwaonesha kwamba suala hili kwa kazi waliyopewa waitendee haki sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kwenye Tume, nawapongeza juzi kuna hati kama 9/10 mmefuta, kwa sababu watu walihodhi ardhi, wakaenda kwenye masoko ya ulimwengu, wakatajirika lakini sisi hatupati kitu. Hata hivyo, kuwanyang’anya isitoshe, waambieni kesho wachimbaji wadogo wadogo waanze kuchimba mpate chochote kama hamjapata watu wa kuwaweka katika maeneo yale. Kwa sababu kunyang’anya ni kitu kingine na kutekeleza ni kitu kingine. Bajeti ijayo kama mtakuwa hamjafanya chochote pale, nikiwa hai siwezi kuongea hivi nitakuwa naongea kwa sura tofauti, lakini leo sina uwezo wa kusema sana kwa sababu ni kitu kipya, mmekifanya kwa nia njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yale kwa sababu yanayo rasilimali, kama hamjajipanga wachimbaji wadogo waingie. Unajua hawa wachimbaji wadogo wako wengi katika nchi hii katika sekta hii, ukiwaambia leo kesho watakuwepo 10,000 hata 100,000 wanachimba mnapata pato kidogo, mmeshaweka sheria, kuliko tunawanyang’anya watu halafu tunakaa nayo tunaanza kutengeneza akili ya kufikirika, unajua bado, aah, tumeondoa kwa sababu hapatumiki, ni vizuri mkaandaa mazingira ya kuweza kupatumia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipongeze Jeshi la JKT kwa kutengeneza ule ukuta, watu walisema haiwezekani imewezekana. Wizara ya Madini nawapongeza sana kwa ushirikiano wenu, watu kitu walichokuwa wanafikiri kiko mbinguni sasa kiko tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Jenerali Venance Mabeyo na Meja Jenerali wa JKT, vijana wamefanya kazi nzuri sana na ya kupongezwa kwa sababu wametia moyo wanalinda nchi yao. Ombi langu kwenu Wizara na Jeshi, pale Mererani hamjafunga security. Mmemaliza kujenga ukuta, watu wako kwenye ukuta, haionyeshi faida ya ukuta ule, kama hatujazichunga rasilimali tulizotakiwa kujengea ukuta ule. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwenu, zile security mnatakiwa kujenga, inawezekana mmechelewa mnajipanga vizuri, jipangeni vizuri sana, wachimbaji wa madini mimi sijui tanzanite, lakini sehemu zingine nina uzoefu, wanaweza kutembea kilometa saba chini, wakatokea mle ndani ya tanzanite wakafanya kazi. Ni vizuri ile security mnayotaka kuiweka i-sense kwenda chini kama ni kilometa 10, 12 ili chochote kinachotokea kiweze kujulikana mapema lakini tukiutengeneza ule ukuta, halafu mkauacha muda mrefu, aah, si vizuri kusema sana. Nachoshauri, nguvu tuliyotumia, pesa, muda ni vizuri mkauweka ule ukuta security ili watu waone faida ya tanzania ya Tanzania sasa inapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini, sitaki kutoa ushuhuda tangu mmejenga ule ukuta bado ule mchezo wa Nairobi unaendelea tu, hamna jinsi ya kuuzuia, kwa sababu hamna scanner ya kumwangalia mtu, tukiingia pale Airport unaangaliwa mpaka sindano. Pale kwenye tanzanite inatakiwa mtu anatoka nayo kwenye gari, chombo kinalia, anaambiwa simamisha hilo gari, mtu anakuja nayo kwenye viatu, anaambiwa simama pale, ndiyo tutaweza kuona faida ya hilo ambalo Mheshimiwa Rais na Wizara wamedhamiria kulifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine, mimi ni mjasiriamali kidogo wa madini ya copper…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.