Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Manonga
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
1
Ministries
nil
MHE. SEIF K. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami kuchangia Wizara hii ya Madini. Kwanza kabisa napenda tu kupongeza sana Wizara hii ya Madini ambayo inaongozwa na Mheshimiwa Angellah Kairuki. Pongezi nyingi sana kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia pongezi nyingi sana kwa Naibu Waziri ambaye ni Mheshimiwa Doto Biteko pamoja na Mheshimiwa Stanslaus Nyongo. Kwa kweli Waheshimiwa hawa wanafanya kazi nzuri kwa sababu tunawaona; siyo kama tukiwaona kwenye vyombo vya habari, lakini pia tunawaona wakiwa field wanakuja katika Majimbo yetu, wanatembea usiku na mchana kuhakikisha kwamba Wizara hii inakwenda mbele. Hongereni sana Mawaziri na timu zenu zote kwa pamoja. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi nataka kuzungumza machache tu, lakini katika mchango wangu nataka nijielekeze kama mchangiaji hapa aliyekuwa akizungumzia kuhusu STAMICO katika usimamizi mzima wa miradi yote ambayo inasimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, STAMICO kwa kweli kama ilivyokuwa na wachangiaji wengine, inafeli katika usimamizi wa miradi na rasilImali hizi za Taifa la nchi hii. Hiyo inadhihirisha wazi, kwa mfano, katika migodi kama STAMIGOLD na hii tunaita Buhemba. Sisi kama Kamati tulienda pale Buhemba tukajionea ule mgodi ulioko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Buhemba ilikabidhiwa na Mwekezaji mwaka 2008 na ikarudishwa Serikalini kwenye hiki chombo chetu ambacho ni STAMICO. Wakati huo walikabidhi vikiwepo na vifaa; magreda, magari na kila kitu kilichoko mle ndani yakiwemo majumba. Yaani kiasi ambacho unaweza kuanza kesho kuendeleza ule mradi ukasonga mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichotokea, tumekwenda juzi, kabla ya pale kulikuwa kuna kampuni inaitwa G4ST Limited, ni Kampuni ya Ulinzi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba rasilimali zilizokabidhiwa na mwekezaji zinabaki kuwa salama. Hii kampuni ya Ulinzi binafsi iliyokuwa inalinda baadaye ikabidi i-handle kwenye Serikali kwa maana ya Jeshi la Polisi. Ule mgodi sasa ukabaki kama hauna mwenyewe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilichokuja kutokea, pale kuna watu walienda mpaka kung’oa madirisha ya nyumba za watumishi, watu wameng’oa madirisha ya milango ya magari na vifaa vyote vilivyomo mle ndani kwenye mgodi. Yaani sasa imetoka kwenye kampuni binafsi, tumeikabidhi Serikali, Serikalini huko sasa ambako tumekabidhi Jeshi la Polisi wamengo’oa kila kitu, yaani vitu vimeibiwa vyote. Hapo hapo maana yake tayari mgodi umerudishwa STAMICO.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa utaratibu huu ambao migodi yetu inakuwa ipo chini ya usimamizi wa STAMICO na STAMICO imeendelea kuomba fedha kwa ajili ya kuendesha migodi iliyopo ndani ya nchi yetu. STAMICO imefeli. Binafsi kabisa nasema STAMICO imefeli na tumeipa fedha kwa ajili ya kujaribu. Iendelee kujaribu hivyo hivyo huku ikiendelea kutupa hasara juu ya hasara. Hapa tumeona tuna deni zaidi ya shilingi bilioni 60. Tumezalishiwa na hawa ambao walikuwa wanatusimamia na hatupati faida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani sekta binafsi ikisimamia kwenye madini inaleta faida na kampuni inanawiri, mpaka wakati mwingine tunasema kampuni inaiibia nchi yetu. Sasa kama tunaweza tukakabidhi shirika letu wenyewe lisimamie rasilimali lifanye uzalishaji, badala ya kuleta faida linaleta hasara, kwa hiyo hii STAMICO kwa kweli, kwa namna moja ama nyingine, sijui kwa sababu wamesema wamekuja watu wapya wanaanza tena mchakato upya kwenye kusimamia, lakini tunapata wasiwasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui kwamba hata hao wataalam ambao wako chini watabadilishwa mpaka huko chini! Maana yake Taifa hili limekosa watu waaminifu. Watu Wazalendo wamepungua, tunawakabidhi rasilimali kuhakikisha kwamba tunapata, nchi yetu tunafaidika kutokana na madini, lakini hao hao tunaowakabidhi na wenyewe imepelekea sasa tunapata hasara badala kupata faida. Mchango wangu kwenye STAMICO ni huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Madini napenda binafsi kuishukuru na kuipongeza kwa sababu katika kuzunguka kwao wamekuwa wanatatua migogoro mbalimbali. Hata walienda kwa Mheshimiwa Kiula pale Jimbo la Mkalama, Kijiji fulani cha Tumuli, wametatua tatizo pale. Mheshimiwa Nyongo nadhani ndio alifika pale, ametatua na sasa hivi tunaenda kupata suluhisho la mgogoro ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge yule alikuwa anakushukuru sana, lakini kwa sababu ni majirani, nami natambua tunahusiana kwa sababu migodi hii inatembea ikitoka pale Tumuli inakuja Shelui na Shelui iko Igunga pale Igurubi. Ametatua mgogoro mkubwa sana katika eneo hili, tunampongeza sana watu wa maeneo ya kule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuzungumzia kuna suala hili limeibuka. Tumeona tangazo limetolewa na Mkuu, nafikiri Serikali ya Mkoa wa Geita kwamba inazuia carbon zisisafirishwe kutoka Geita kwenda Mwanza. Sasa hii sijaelewa ni sheria inakuja ama inakuwaje? Ndani ya nchi yetu tunazuia usafiriishaji wa carbon kupeleka kwenye viwanda sehemu nyingine ambayo mtu anataka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mtu anaamua kupeleka kwenye kiwanda ambacho anaona kinafaa. Haiwezekani ulazimishe kwamba carbon niliyonayo ifanyiwe processing ndani ya mkoa wangu. Tunatafuta ubora wa kazi zinavyotakiwa kufanyika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unaniambia nibaki labda nifanyie hizi process zote katika Mkoa wangu wa Geita, lakini ni katika viwanda vilivyoko Geita labda havina ubora wa kuchenjua dhahabu ninavyotaka. Inawezekana nilikuwa na-expect kupata kilo moja au kilo tatu. Nikifanyia Geita ama nikifanyia ndani ya mkoa wangu wa Tabora sipati hizo kilo mbili au tatu, lakini nikipeleka labda mkoa jirani wa Shinyanga, Mwanza au Arusha nikapata kilo tatu, usinizuie mimi ambaye nawekeza, ninayefanya hii kazi kutoka mkoa mmoja kwenda mkoa mwingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo tangazo tumeliona, watu wenye sekta hii ya madini wanalalamika. Namwomba Mheshimiwa Waziri alichukue na atoe maelekezo kwamba hii amri ya kuzuia watu wasisafirishe carbon kupeleka mkoa wowote ule katika nchi yetu, iondolewe na isiwepo katika utaratibu ambao ni rasmi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba carbon mtu apeleke sehemu yoyote ili mradi afuate sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Madini, kwa maana ya vibali na vitu vinginevyo, lakini wasizuie watu wasiende katika mkoa mwingine kufanya kazi ambayo yeye anahitaji. Kazi hizi ni bora. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitu kingine nataka kuchangia suala zima la wawekezaji katika migodi. Wanatumia umeme mkubwa sana na pia gharama za uendeshaji wa migodi hii ni kubwa sana. Naomba Wizara ya Nishati isaidie, gharama za umeme ni kubwa sana katika viwanda hivi. Tuna-discourage uzalishaji kwa sababu gharama ya kulipia umeme ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri akae na Waziri wa Nishati ili waone namna gani watakavyoweza kusaidia wawekezaji katika Sekta ya Umeme kwa sababu hizi units ambazo wanalipa zinakuwa ni kubwa sana. Tunaomba Mheshimiwa Waziri alichukue hilo na walifanyie kazi ili wapunguze gharama za uzalishaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufanya hizi wata- encourage wawekezaji wengi zaidi wawezeke katika Sekta ya Madini. Nafiri hilo Mheshimiwa Waziri atakuwa amelichukua na wataenda kulifanyia kazi na watavutia zaidi wawekezaji kwa sababu mwekezaji anaweza kutumia generator akapata faida kuliko kutumia umeme wa Serikali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama mtu akiamua kutumia generator, hebu angalia na generator ni gharama kubwa sana. Pamoja na gharama kuwa kubwa mtu anaona ni bora kuliko kutumia TANESCO, namwomba Mheshimiwa Waziri wakae chini waone ni jinsi gani ambavyo wanaweza kuwasaidia hawa watu ili kuhakikisha kwamba nchi yetu haipotezi mapato ambayo inahitaji katika sekta hii kutokana na kodi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kingine ambacho nataka kuchangia ni kuhusu suala zima la ruzuku. Hapo siku za nyuma tulikuwa tunatoa ruzuku kwa wachimbaji wadogo wadogo katika kuwawezesha kufanya kazi zao na kuweza kufikia katika malengo. Mheshimiwa Waziri nasi kule kwetu kwa maana ya Jimbo la Manonga katika Kata zile za Mwashiku, Nguru na Ntobo tuna madini na wachimbaji wadogo wadogo wapo, waliwahi wakati fulani kupata ruzuku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba Mheshimiwa Waziri, hebu tutilie mkazo katika hili zoezi la kutoa support kwa wachimbaji wadogo wadogo, watu wa Jimboni kwangu waweze kupata lakini pia wa maeneo mengine katika nchi yetu wapate hizi ruzuku kutoka katika Wizara. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia kuhakikisha kwamba tunawanyanyua wachimbaji wadogo kwenda kuwa wachimbaji wa kati, lakini pia kesho na kesho kutwa watafikia katika level ambayo watakuwa walipaji wa kodi wakubwa sana katika nchi yetu. Lengo ni kuhakikisha kwamba tunajikwamua na umaskini tulionao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Taifa hatufurahii kuona kila siku tukiendelea kuwa walalamikaji ama tukiendelea kuwa katika hali ya ambayo kila siku ni maskini. Hili neno maskini inatakiwa lifike wakati tuliondoe katika nchi yetu ya Tanzania. Kuliondoa ni katika kuwawezesha hawa wachimbaji wadogo wadogo na wao wafikie katika level ambayo kila sehemu akienda anatambulika, huyu mtu anastahili kuwepo katika nchi yetu hii ya Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mchango wangu huu mdogo, napenda sasa kuishukuru Serikali, Wizara, lakini Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kweli siwezi kuacha kumshukuru kwa sababu anafanya kazi kubwa sana katika kuhakikisha kwamba rasilimali hii ya madini inalindwa na nchi inanufaika kutokana na rasilimali Mwenyezi Mungu amelijalia Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, nashukuru sana na naunga mkono hoja.