Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Mpanda Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
2
Ministries
nil
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Nami naomba nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na Watendaji wote katika Wizara hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vizuri nikaufahamisha umma kuwa mimi pia ni mmoja kati ya wachimbaji wadogo wa madini. Kwa sura hiyo, naona kabisa kwamba eneo hili likiendelea kutulea wachimbaji, mchango wetu kwa nchi hii utakuwa mkubwa. Mara ya mwisho niliwahi kuzungumza hapa, uzuri wa wachimbaji wadogo, fedha wanayopata hawaendi kuwekeza nje, wanakwenda kuwekeza ndani ya nchi hii. Kwa hiyo, tukiwaendeleza wachimbaji wadogo kwa ujumla wake, maana yake tunakwenda kuboresha maendeleo ya miji yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niliwahi kusema hapa Johannesburg imejengwa kwa fedha ya pale pale. Kwa hiyo, naamini iwe ni Mwanza, Shinyanya, Chunya na Mpanda nakotoka, wachimbaji hawa wadogo wana nafasi kubwa ya kuleta maendeleo katika maeneo hayo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naiona kazi nzuri ya GST kwa maana ya suala zima la utafiti. Nina eneo moja la Kapanda pale kwangu ambapo kwa maana ya kitabu hiki inaelezea wakia 47,605 ziliweza kubainika pale Kapanda. Rai yangu, pamoja na tafiti hizo nzuri zinazofanywa na ndugu zetu wa GST, eneo lile la Kapanda wameshaelekeza kwamba kitajengwa kituo kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia wachimbaji, siioni kasi ya kufanya zoezi hilo. Kwa hiyo, naomba pamoja na tafiti hizo nzuri ambazo amezifanya, basi ile kasi ya kwenda kujenga kituo pale isomeke.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, nami nizungumzie suala la leseni. Nafahamu utoaji wa leseni hapa katikati tulikuwa tunasubiria Tume. Nashukuru kwamba Tume imepatikana na kuna watendaji mahiri katika Tume hiyo basi nilichokuwa naomba tu-speed up suala la utoaji leseni. Niseme hivi, utoaji wa leseni ni chanzo kingine cha mapato. Kwa hiyo, tunapochelewa kutoa hizo leseni, pia tunachelewa katika suala la mapato. Tutakapokuwa tukitoa leseni hizo tusiwasahau wachimbaji wa eneo la Kapanda, Dilifu na kwa ujumla wake, maeneo yale ya Mpanda ambapo Serikali iliahidi kuwasaidia wachimbaji hawa wadogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona suala la migodi ya STAMICO pale ambapo inakuwa haifanyi vizuri, basi Serikali ione namna ya kuweza kuwapatia wachimbaji wa kati. Hilo nalo nami naendelea kuishauri Serikali, kama STAMICO itakuwa imeshindwa kufanya vizuri, basi mwone nafasi hiyo ya kuweza kuwapatia wachimbaji wa kati. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu ujenzi wa smelter, nafahamu na hapa katika ukurasa wa 38 na 39 inaelezea. Kwa mfano, ukija maeneo ya Mpanda kwa maana tu ya tailings, hapa Kiswahili cha tailings wanasema visusu, ukija katika suala la tailings tu pale maeneo ya Mpanda kuna visusu vya kutosha katika eneo lile, tatizo lake ni teknolojia sahihi ya jinsi ya kuitoa dhahabu katika maeneo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, najua jiolojia ya Mkoa wa Katavi ni tofauti na ilivyo Mwanza na Chunya, kwa hiyo, kila watu wachukuliwe kwa namna yake. Ndiyo maana leo unaweza ukakuta mchimbaji wa Mpanda pamoja na kuwa na visusu vya kutosha lakini hana uwezo wa kuipata ile dhahabu kwa sababu ya lack of technology. Kwa hiyo, naomba sana Wizara ituangalie kwa jicho hilo la huruma watu wa kanda ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta kwa maana ya mwamba wa eneo lile, kuna madini mengi tu. Kwa wakati mmoja anaweza akapata dhahabu, copper, fedha na mambo mengine mengi. Kwa hiyo, sasa namna ya ku-separate, it is an issue. Kwa hiyo, naomba sana hilo nalo liweze kuangaliwa kwa sura hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana naendelea kusisitiza, najua kwa maana ya thamani iongezewe hapa nchini, ujenzi wa smelter ni jambo la msingi, ingawa nafahamu uwezekano wa kujenga smelter inaweza isifanyike kwa usiku mmoja, ni suala la hatua. Kwa hiyo, wakati tukijipanga kwenda huko, tuendelee kuangalia tunafanyaje na wale ambao tayari wanaendelea na uchimbaji katika sura hiyo nyingine? Najua Mheshimiwa Waziri na Watendaji kwa ujumla wenu na Serikali yangu kwa ujumla wake kwa usikivu huu mtaliangalia suala hilo kwa jicho la pekee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la ruzuku pia, kwa maana ya wachimbaji hawa tunapozungumzia kuwawezesha ni pamoja na kuwapatia ruzuku. Kama kulikuwa na upungufu huko nyuma, naomba tuzitoe zile tofauti lakini tusiache kutoa ruzuku kwa watu hawa. Ni kwa kufanya hivyo tutaongeza mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nikitoka hapo, najua kuna suala la local content, kwa maana ya kuhakikisha wazawa wananufaika na suala zima la uchimbaji. Mimi naliangalia kwenye sura hii, tutakapojenga uwezo wa wachimbaji wadogo, fedha ambazo watapata watu hawa, mzunguko wake unarudi palepale. Mtu huyu kama akienda sokoni atanunua materials ambazo ni za hapa hapa nyumbani, atampeleka mtoto shule na maeneo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama unamzungumzia mama lishe, fedha ikitoka mgodini itakuja huku, itamkuta mama lishe, fedha ikitoka mgodini ikija huku itamkuta mchuuzi mwingine sokoni. Kwa hiyo, kwa sura hiyo tunauona mtiririko wote wa suala la fedha kwa watu wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na suala la ujenzi wa Ofisi ya Kanda ile ya kule kwetu Mpanda. Mpaka leo suala hili la ujenzi wa ofisi sioni dalili. Kwa hiyo, naomba sana na Mheshimiwa Waziri wangu anasikia pale, sisi ni Kanda ya Magharibi, utashangaa Makao Makuu ya Kanda hata ofisi haipo. Kwa hiyo, naomba sana lile zoezi la ujenzi wa ofisi liendelezwe. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona katika maeneo tofauti tofauti upelekaji wa fedha katika Wizara inarudishwa kwa kiwango kidogo. Tutaipataje tija kama watu hawa hawapewi fedha za maendeleo? Naomba sana kwa ujumla wake kama ni Wizara ya Fedha tuendelee kuwaangalia watu hawa. Watu ambao wanachangia kwenye pato la Taifa unaposhindwa kuwarudishia fedha maana yake unakuwa umewakata miguu, hawataweza tena kutoka hapo walipo ili kuongeza mafanikio.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nashukuru sana.