Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Martha Moses Mlata

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama unavyoniona haya ndiyo madini yetu tunayoenda kuyajadili leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipatia nafasi hii ili na mimi niweze kutoa mchango katika Wizara hii ya Madini ambayo ni muhimu sana kwa Taifa letu na wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwanza kabisa kwa kuona umuhimu wa Wizara hii na kuitenganisha kutoka kwenye nishati ikabaki kama Wizara ya Madini. Aliona umuhimu na kweli Wizara hii ina mambo mengi makubwa ambayo yanastahili kuwa na Wizara peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze kwa kuweza kumteuwa Waziri, mdogo wangu Mheshimiwa Angellah Kairuki kwa sababu nina imani naye. Kwanza ni mwanasheria, lakini ni mzalendo. Wizara hii inatakiwa mtu mzalendo kama alivyo Waziri, Naibu Mawaziri Mheshimiwa Doto Biteko shemeji yangu na mwanangu Mheshimiwa Stanslaus Nyongo. Naamini kabisa mtaitendea haki Wizara hii ili tuweze kunufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa kuonesha uzalendo namba moja. Mheshimiwa Rais kabla hajawa Rais alionesha uchungu wa namna gani nchi yetu ilivyokuwa inafilisiwa, madini yalikuwa yanapelekwa nje kwa kisingizio cha mchanga, sijui makinikia, akajitoa mhanga ili kuweza kulinusuru Taifa letu kwenye sekta hii ya madini. Nampongeza sana. Najua aligusa mahali ambapo watu hawakutegemea kuguswa. Ndiyo maana bado kuna vibaraka wanazungumza kutetea yale yaliyokuwa yakinyonya Taifa letu, namtia Mheshimiwa Rais moyo, songa mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Nabu Spika, niliwahi kusema humu ndani, ndiyo maana Mungu aliamua ajitenge mbali na sisi asionekane kwa sababu angeonekana hakika tungemsumbua. Ikiwa ni jua tutamwambia jua linawaka, ikiwa ni mvua tutasema hii mvua ya nini, ikiwa ni kimbunga tutasema kimbunga cha nini, ikiwa ni utulivu tutasema hewa hamna. Ndiyo mwanadamu alivyo, hasa wengine ambao wanaonesha tabia zao hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza kwa kujenga ukuta kwa sababu amelinda mali ambayo tumeona hata kwenye vyombo vya habari watu wanajimilikisha tanzanite ambayo siyo ya kwao. Nampongeza Mheshimiwa Rais kwa hatua ya kujenga ukuta pale Mererani. Hata kama tungejenga kama Mnara wa Babeli ili mradi tunalinda mali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nipongeze pia Tume ambayo ameiunda sasa hivi. Naomba Tume hii iliyoundwa inisikilize kwa makini, kwanza ikafanye kazi, lakini kuna sheria ambayo inasema first come first served. Naomba sheria hii ikaangaliwe tena kwa sababu haiwezekani
tukatumia online tukawa tunauza madini yetu online, unamuuzia mtu ambaye humjui. Mheshimiwa Waziri naomba ulisimamie jambo hili ili GST, kwanza nawapongeza kwa vitabu hivi ambavyo wamevitoa, wameonesha kila mkoa na madini yake kila mahali, japokuwa naamini hawajamaliza kwa sababu madini bado ni mengi. Wawezeshwe waende wakafanye utafiti ndipo tuweze kuuza vitalu hivyo baada ya kujua ardhi hii ina mali gani. Tusiwe tunauza tu unampa mtu yeye eti ndiyo aje akwambie hapa kuna madini kiasi fulani, ndiyo maana tunaibiwa. Tuhakikishe kwamba kwanza hiki kitalu kina madini kiasi gani halafu tuweke mnada. Kwa sababu nchi nyingine wanafanya hata mnada, kwa nini tusifanye mnada wa vitalu vyetu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nashauri badala ya kumpa mtu akatafiti mwenyewe, tutafiti wenyewe halafu ndiyo tufanye mnada. Tuende tukaone nchi nyingine walivyofanya ili tuweze kupata mapato yatakayokidhi kile kilichopo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia wananchi wanaoishi kwenye eneo lile jamani, pamoja na kwamba ni mali ya Serikali, lakini wananchi wa eneo lile wafanane basi na madini hayo yaliyopo pale. Kuwe na utaratibu wa kuweza kuwasaidia waondokane na ule umaskini wafanane na madini yanayopatikana pale na huduma ziwekwe pale. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri suala la One Stop Centre, kwani suala la Madini House limeishia wapi? Madini House siyo ofisi ya kukaa watu, ni wachimbaji wadogo wapate mahali pa kwenda kuuza madini yao na Serikali mnaweza mkanunua, mkaweka mashine ambazo zitatambua madini yaliyo halali na halisi, inaweza ikasaidia kukuza pato au shilingi yetu ikapanda. Kwa hiyo, naomba tuwe na sehemu moja ya wachimbaji wetu ili waondokane na kulaghaiwa na wale wanunuzi wadogowadogo na pia Tume iweke bei elekezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho kwenye shamba kuna mabwana shamba, kuna mabwana nyuki, sijui bwana kilimo, sijui bwana samaki, kwa nini kwenye madini kusiwe na mabwana madini? Hawa wawe washauri wa wachimbaji wetu wadogo ili wao wawe ni washauri tu na watoa leseni wawe watoa leseni. Tumeshuhudia wachimbaji wadogo wanapogundua madini anamuendea mtoa leseni, badala ya kumsaidia anauza kwa mtu mwingine eneo lile lakini kukiwa na bwana madini, bwana madini atatoa ushauri tu ili afuate taratibu za kuweza kupata leseni. Mheshimiwa Waziri naomba sana mabwana madini, kama ilivyo bwana nyama, bwana shamba, bwana kilimo, bwana nyuki na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kuwe na bei elekezi. Mbona kwenye kahawa kuna bei elekezi, kwenye korosho kuna bei elekezi na mazao mengine kwa nini hakuna bei elekezi kwenye madini? Kwa hiyo, naomba sana suala hili la bei elekezi nalo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Singida tuna madini yanaitwa zircon , Iramba, niliwahi kuuliza ile zircon imeambatana na almasi lakini wanunuzi wananunua kama zircon, wanawadhulumu wale wachimbaji. Bado naitaka GST wafanye utafiti watuambie hiyo ni zircon peke yake au ni pamoja na almasi na wafanyeje? Maana hata Tume ya makinikia iliwahi kuzungumza jambo hilo. Kwa hiyo, naomba sana Mheshimiwa Waziri jambo hilo liweze kushughulikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, wachimbaji wadogo hebu na wao wawe wanaangaliwa kwa sababu wao ndiyo wanakuwa wamegundua lile eneo, lakini anakuja mtu mwingine mnawaambia kwamba hili eneo lilikuwa la utafiti, lakini aliyegundua ni mtu mwingine, matokeo yake mnakuja kutoa leseni kwa watu wengine. Naomba Waziri kwa sababu namwamini sana, naamini atasimamia jambo hilo ili wachimbaji wetu waweze kupata haki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja, ahsante sana.