Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nashukuru sana kupata nafasi hii kuchangia hoja hii muhimu sana. Ni hoja muhimu kwa sababu ni madini ambayo yanaongeza pato la Taifa. Kwanza napenda kumshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa hatua mbalimbali ambazo amezichukua kuweza kuboresha sekta hii ya madini na mpaka sasa hivi tunaanza kuona faida yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi kifupi sana utaona Wizara hii kazi ambayo imefanya ni kubwa sana kwa sababu imeweza kuongeza pato la Taifa kwa asilimia 4.8. Hii ni kutokana na uimarishaji wa mifumo mbalimbali ya madini ambayo imefanyika kwa haraka sana, uangaliaji wa mikataba mbalimbali ambao umefanyika pia kwa haraka sana na utungaji wa sheria mbalimbali ili kuweza kuendana na hali ambayo inaweza kurahisisha kufanya mchango huu wa madini uweze kuongeza pato la Taifa na uboreshaji wa biashara hii ya madini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais ameunda Tume mbalimbali kwa lengo la kuweza kusaidia uimarishaji huu ambapo kwa kweli manufaa yake yanaanza kuonekana sasa hivi. Utoroshaji ulikuwa ni mkubwa sana na sasa hivi udhibiti ambao umefanyika ni mzuri sana. Nashauri Wizara na Mheshimiwa Waziri muendelee na kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo napenda kushauri ni kuhusu tanzanite kule Mererani. Nafahamu kwamba ukuta umejengwa, ni kazi nzuri sana ambayo imefanyika. Kwa kipindi kifupi tu cha miezi mitatu ukuta ule umeweza kujengwa ambao ni mkubwa sana na umeweza kuzaa matunda kwa sababu sasa udhibiti wa tanzanite umeanza kuonekana. Tanzanite ilikuwa unatoroshwa sana na kama unaona takwimu ambazo zimetokea kwenye mitandao mbalimbali India imeonekana kuna tanzanite nyingi sana, ikifuatiwa na Kenya na sisi ambao ndiyo wazalishaji hatuna tanzanite au kiwango chake ni kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningeshauri kama nilivyoshauri Kamati kwamba camera’s ziwekwe na ziwekwe kuanzia kwenye ulipuaji kule chini ili kila kitu kiweze kuonekana. Hivi ni viboresho ambavyo vitaongeza udhibiti pale pamoja na ule ukuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, kuna suala la kujenga kituo ambacho kinakuwa one stop pale pale kwenye mlango pale kwamba baada ya kutoka waingie kwenye kile kituo waweze kukaguliwa au kukabidhi kama ni leseni au ni export license, kama ni masuala ya benki yaweze kufanyika pale pale. Kwa hiyo, hicho kituo ni muhimu sana vinginevyo wanaweza wakatoka pale halafu ikaingia mjini. Kwa hiyo, tunataka ikitoka tanzanite pale Mererani basi moja kwa moja inakwenda airport kwa ajili ya usafirishaji. Hilo ni suala muhimu sana ambalo ningeomba Waziri aliangalie na liko kwenye mapendekezo ya Kamati.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kulizungumzia ni ujenzi wa kiwanda cha ku-add value kwenye madini yetu ambayo yanapatikana, si tanzanite tu bali hata dhahabu na almasi. Nimeona kwenye hotuba ya Waziri na hotuba ya Waziri wa Viwanda, lakini ni muhimu suala hili likajengwa haraka ili liende sambamba na hizi juhudi ambazo zinafanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo napenda kuliongelea ni kwenye Jimbo langu Amani. Kule tuna aidha dhahabu, kwa sababu watu wengi sana wanakwenda kuchimba na imekuwa ni tabu sana kwa sababu wananchi wa Amani, Muheza wanasumbuliwa mara kwa mara kukamatwa na kufukuzwa. Kule kuna safu za milima ya Sakale, tunaamini kabisa kwamba kwenye hiyo milima ya dhahabu, ndio maana wananchi wanakwenda wanafukuzwa na wanayapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kuongea na Naibu Waziri, Mheshimiwa Doto, nafikiri analifanyia kazi. Ni muhimu tupate wataalam waende wakakague ili waweze kuwashauri wananchi wa Muheza waweze kujua kwamba tunachimba dhahabu na iko kiasi gani na waweze kupata leseni kihalali kabisa badala ya kukamatwa kamatwa na kusumbuliwa kama inavyofanyika sasa hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, kuna maeneo ambayo watu wameyahodhi, mengi tu na wengine wana leseni na wanalipia lakini hawayafanyii kazi. Wengine wanayaweka kwa lengo ya kuyauza, sasa wanapokuja wawekezaji wanataka kuwekeza inakuwa ni tabu kwa sababu wanakosa ardhi, wanakosa sehemu ya kuwekeza na inaleta matatizo sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakumbuka niliwahi kuleta wawekezaji na wakaambiwa hakuna sehemu yenye madini, sasa inakuwa ni tabu, ukitaka muone mtu fulani. Sasa ni suala ambalo linatakiwa kuangaliwa. Hili shirika letu la STAMICO lipewe huo uwezo, wawe na maeneo ambayo ni maalum kabisa mtu ambaye anataka kuwekeza anakwenda STAMICO anaambiwa nenda mahali fulani utalikuta hilo eneo, kaangalie, kapime endelea na hiyo kazi. Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na maeneo maalum ambayo yataweza kuwasaidia wawekezaji whether ni wa hapa nchini au wa nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana.