Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Tanga Mjini
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kumshukuru Mungu kunijalia afya njema na kuweza kuchangia katika Wizara ya Madini. Niwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga kwa kunituma kuja kuwasemea katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nitoe pole kwa Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kuondokewa na Mbunge mwenzetu marehemu Mwalimu Kasuku Samson Bilago, Mbunge wa Jimbo la Buyungu Kigoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe masikitiko yangu kidogo kwa kuwa leo ni siku ya Bajeti ya Wizara ya Madini lakini sijawaona wawakilishi wa wachimbaji wadogo wadogo wa Tanzania, hususani Chama cha Wachimbaji Wadogo wa Madini Wanawake na Chama cha Wachimbaji Wadogowadogo wa Madini Tanzania. Ushauri wangu kwa Serikali, katika bajeti ya mwakani, Wizara itoe mwaliko kwa wadau wa madini, wachimbaji wadogo, vyama vyao na kampuni.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgogoro wa wachimbaji wadogo na Serikali. Wachimbaji wadogo duniani kote ndiyo wagunduzi wa kwanza wa madini na baadaye ndipo hupatikana wachimbaji wakubwa (wawekezaji) na kuingia mikataba na Serikali na kulipa kodi za Serikali zinazojulikana kama mrabaha. Niwape pole kwa kuwa wanagundua madini kisha Serikali wanakuja kuwafukuza na kuwaweka wawekezaji wageni (matajiri). Jambo hili si sawa kwa kuwa wachimbaji ndiyo wagunduzi wa kwanza, Serikali ingewathamini na wageni wangewathamini, ikibidi wenye migodi waingie ubia na wenyeji.
Mheshimiwa Naibu Spika, naishauri Serikali badala ya kuwapelekea FFU (Field Force Unit) na kuwafukuza kwa mabomu ya machozi (tear gas), iwawekee utaratibu wa kuwaelimisha na waweze kuona madini ni mali ya Taifa. Vilevile wachimbaji wadogo wapewe ajira katika kampuni za uwekezaji kutoka nje na wachimbaji wapewe mikopo na benki. Watanzania wazawa wakiajiriwa wanaweza kuwa ni askari kanzu (inteligency unit) kujua wawekezaji wabaya (bad investors) ambao wanatorosha madini yetu na kuweza kutoa taarifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya tanzanite na madini ya vito. Tanzania tumejaliwa madini ya thamani ya aina nyingi mno kama vile tanzanite yanayopatikana Tanzania tu, ruby, sapphire (pink, white and red), rhodolite, alexandrite, rose, change colour, green garnet, red garnet, green tourmaline, ammolite, moonstones. Madini yote haya yana thamani na ni ajira kwa vijana wa Kitanzania, endapo patafanyika mipango ya makusudi ya kuanzisha viwanda vya kuchakata madini (mines cater center). Pia madini haya tungepata taarifa zake kwamba kila aina imeingiza/ inaingiza kiasi gani kwa mwaka na iwepo data base ya precious stone.
Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya tanzanite yanapatika nchini mwetu tu, duniani kote hakuna. Hivyo ni vyema yakafanyiwa matangazo ya kutosha kwani itakuwa ndiyo symbol ya nchi yetu kama ilivyo Mount Kilimanjaro kwa kuwa dunia nzima ipo Kilimanjaro moja tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, majanga katika uchimbaji madini. Katika migodi mikubwa na midogo duniani kuna changamoto kubwa ya ajali za moto, kufukiwa na vifusi, kuishiwa hewa ya oxygen, tetemeko la ardhi na mafuriko. Katika nchi za wenzetu kwa kuwa madini ni uchumi wamewekeza fedha nyingi lakini zipo rescue teams za uhakika ili kuweza kuokoa wachimbaji pale inapotokea dharura za ajali kama nilivyozitaja. Nashauri Serikali iweke utaratibu wa kuwa na rescue teams katika migodi yote mikubwa na midogo nchini Tanzania. Serikali inunue ambulance/helcopter ambayo itasaidia kuokoa maisha ya wachimbaji kwa kuwawahisha watakaokutwa na ajali katika hospital zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini madini yanatoroshwa? Madini yanatoroshwa kwa sababu mbalimbali kama: Foleni zinazosababishwa na uchache/ muda/teknolojia ndogo zinazosababisha wafanyabiashara wa madini kuyatorosha nje kwa kuwa ukataji unatumia muda mwingi kukata madini machache; technology iliyopo Tanzania ni ya kizamani na pia imepitwa na wakati; na mashine (mineral cutters machines) zipo chache mno.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nashauri Serikali yafuatayo:-
(i) Iwekeze katika vyuo vya madini ili vyuo vizalishe wataalam watakaosaidia wachimbaji wadogo.
(ii) Ianzishe course za masomo ya ukataji wa madini na aina za madini katika vyuo vyetu vya VETA. Kwa mfano, katika ziara ya Kamati ya PAC Shinyanga tulikuta course ya ukataji madini katika Chuo cha VETA Shinyanga. Ada ya course hizi ziwe kiwango cha chini kuwavutia wanafunzi.
(iii) Mashine za ukataji madini ziwekewe kodi ndogo ili kufanya bei ya ukataji iwe ndogo na kuweza kuongeza thamani ya madini yetu baada ya kukatwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, benki kutowaamini wachimbaji. Benki na taasisi za fedha haziwaamini wachimbaji wadogo kwa kuwa haziwakopeshi na ama kuna masharti magumu mno. Nashauri Serikali kama ifuatavyo:-
(i) Iweke mpango wa kuwakopesha vifaa (mitambo) wachimbaji wadogo kwa ajili ya uchimbaji badala ya fedha.
(ii) Mpango wa kuwawezesha wachimbaji wadogo US$50,000 (Sh.100,000,000) hadi US$100 (Sh.200,000,000) uwekwe wazi na vigezo vinavyotumika, wachimbaji waelimishwe ili wajue na kuweza kufaidika na mpango huu.
(iii) Benki zote zipewe maelekezo na namna ya kuwakopesha wachimbaji wadogo mitambo/fedha na uwepo uwazi.
(iv) Wizara itoe takwimu za wachimbaji wadogo wote waliowezeshwa na maeneo walipo.
Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya ujenzi/viwandani. Wizara katika taarifa yake haijatoa takwimu za madini ya uranium yanayotumika katika utengenezaji wa silaha za nuclear. Naomba tupatiwe taarifa kwa hapa nchini yapo maeneo gani na yapo kwa ujazo wa kiasi gani?
Mheshimiwa Naibu Spika, madini ya bati, ni madini ambayo Serikali kama ingetilia maanani kwa kununua mtambo wa kuchakata bati, wananchi wetu wasingekuwa na sababu ya kuishi katika nyumba za nyasi, tembe na bei isingekuwa kubwa. Naiomba Serikali inunue mtambo wa kuchakata bati kwa manufaa ya Watanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri afanye ziara katika maeneo yenye madini katika Jiji na Mkoa wa Tanga katika maeneo yafuatayo ili kutambua kero za wachimbaji.
Na. Eneo la Mgodi Sehemu Ulipo Aina ya Madini
1 Kalalani / Kigwase Tarafa Daluni - Korogwe Madini ya Vito
2 Ng’ombeni, Umba “
3 Amboni Kata ya Mzizima - Tanga Kokoto/ Mawe/ Chokaa
4 Maweni Kata ya Maweni Jiji la Tanga Kokoto na Mawe ya ujenzi