Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

Hon. Silafu Jumbe Maufi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 – Wizara ya Madini

MHE. SILAFU J. MAUFI: Mheshimiwa Naibu Spika, natoa shukurani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, kwa kukubaliana na ushauri wa kuzitenganisha Wizara ya Nishati na Madini kwa maslahi ya Taifa. Hii yote ni jitihada ya kupambana kwa kufahamu rasilimali za nchi zenye maslahi ya wananchi na kunufaika nazo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia napongeza kwa uteuzi wa Mheshimiwa Waziri, Naibu Mawaziri na Katibu Mkuu. Ni watu wenye mwitikio wa kujituma, kujitoa kwa uzalendo uliotukuka kwa maendeleo ya nchi na utendaji wao ambao unaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais.

Mheshimiwa Naibu Spika, STAMICO nimeisikia muda mrefu nchini ikiwa inahusika na madini, lakini matunda yake hayana afya kwa maendeleo ya nchi yetu. Ni vyema ikaangaliwa upya katika mfumo wake wa utendaji na usimamizi kwa maslahi ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu ina madini kadhaa na wananchi wengi wanajihusisha na uchimbaji mdogo mdogo wa kupata madini yanayofahamika na yasiyofahamika na hapa ndipo wananchi ambao ni wachimbaji wadogo wanadhulumiwa na watalaamu wachache tulionao. Mkoa wa Rukwa kuna wachimbaji wadogo kwenye milima ndani ya Kijiji cha Kastuka, hawayafahamu hayo madini lakini wachimbapo wanayaleta Dar es Salaam na bado wanaendelea na kazi hiyo, ndiyo kusema wataalaam wameyafahamu. Tunaomba Wizara iweke utaratibu wa kitengo maalum kuzungukia nchi nzima na kubaini madini yanayopatikana kila Mkoa na kuwekwa takwimu sahihi ya madini tuliyonayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashauri Wizara ijipange vyema na suala zima la uchenjuaji wa madini hayo kwa kuyaongeza thamani na kutambua kwa kuchanganua aina za madini moja moja. Kwa umakini huu, ukizingatiwa, tutafahamu thamani ya madini yetu na kuwa na mchango mkubwa kwa pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekuwa na njia nyingi za panya za kutorosha madini yetu katika kutafuta soko zuri kwa wachimaji wadogo. Tunaomba Serikali kurejesha utaratibu wa Soko la Dhahabu la Benki Kuu kwani wanatapeliwa na walanguzi na bei wanayoipata ni ndogo, huku kazi waifanyayo hadi kuipata mali hiyo ni ngumu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa 21 wa hotuba ya Wizara, pamezungumzia suala la usimamizi wa matumizi ya baruti na udhibiti wa matumizi ya baruti kwenye shughuli hizo mbalimbali kwa kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa usalama na kwa madhumuni yaliyokusudiwa. Sikuona ni namna gani wananchi wanaozunguka maeneo yanayotumia baruti na majengo yao kuathirika, wanalipwaje fidia na wahusika au wanahudumiwa vipi na wahusika?

Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Rukwa tuna hao wahusika wa matumizi ya baruti katika kupasua mawe na kutengeneza kokoto, changarawe na kadhalika. Wananchi wanaozunguka eneo hilo, nyumba zao zimepata nyufa kadhaa na kupunguza uimara. Ni vyema Serikali ikaona namna ya kuwaangalia wahanga hawa. Pia uwepo msukumo wa hao wahusika kwa mchango wao kwa maendeleo ya huduma za jamii kuwa ni lazima, siyo hiari au mahusiano ya viongozi kwa matakwa yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa madini yanaonekana kuwa na uwezo mkubwa wa kuchangia pato la Taifa, hivyo tunaomba Wizara ya Fedha kuweka jitihada ya makusanyo na kuwapelekea Wizara ya Madini bajeti ya Maendeleo ya shilingi 19,620,964,000 ambazo asilimia kubwa ni fedha za ndani. Ni matumaini yetu kwamba wachimbaji wadogo na wananchi wetu watanufaika na kupata maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba kujengewa ofisi ya madini kwenye mikoa yenye madini kuliko kuwa na Ofisi Dar es Salaam, ndipo Wizara itakuwa na shinikizo la kuandaa wataalam na kuwasambaza mikoani au kwenye kanda kwa kuanzia. Tutaimarisha wachimbaji wetu, tutawadhibiti walanguzi na matapeli na mapato yatafahamika na kuyasimamia kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.