Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CUF
Constituent
Wingwi
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. JUMA KOMBO HAMAD: Mheshimiwa Spika, nashukuru kuwa miongoni mwa wachangiaji wa Wizara hii kubwa, Wizara ya Fedha na Mipango.
Mheshimiwa Spika, kabisa niungane na waliopita kuzungumza japo kwa ufupi au hata kuitaja barabara ile inayokwenda Kigoma kutoka Nyakanazi kwamba ni barabara muhimu na ni barabara ambayo nilipata fursa na mimi kwenda kwenye msiba ule wa kumsitiri Mwalimu wetu, Mbunge mwenzetu Mwalimu Bilago, nikaona mazingira yalivyo, nikaona barabara ilivyo kwa kweli inahuzunisha na inatia huruma sana.
Mheshimiwa Spika, naamini kwamba ni miongoni mwa barabara zile ambazo siku za mvua magari yanazama kwenye mito ikisubiri siku mbili au tatu wananchi wapate kupita kwa ajili ya kufika Kigoma na maeneo mengine ya kule. Kwa hiyo, ni vyema Wizara ya Fedha barabara ile waingalie kwa jicho la huruma sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, la pili, ukiangalia kitabu cha Kamati ukurasa wa 26 kumezungumzwa hizi milioni 50 kila kijiji, lakini ikiwa Serikali ya Awamu ya Tano hii inakwenda ukingoni tena tunakwenda kwenye mwaka wa tatu sasa, Waziri wa Fedha anakuja hapa kutuaminisha kwamba sasa kumetengwa jumla ya bilioni 60 ambazo zinakwenda kufanya utafiti yaani pilot studies kwa ajili ya kuona kwamba vipi tutafanikisha mpango huu wa milioni 50 kila kijiji.
Mheshimiwa Spika, hii maana yake ni kwamba, kwa miaka mitatu sasa bado tunakwenda kwenye pilot studies, kwenye kufanya research kuona vipi tutafanikisha utoaji wa fedha hizi, lakini tukumbuke kwamba milioni 50 kila kijiji ni ahadi ya Rais na imo ndani ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi. Hii inamaanisha kwamba wananchi Watanzania tuliwadanganya. Tuliwadanganya kwa sababu kama hadi leo miaka mitatu fedha hii haijatoka ina maana hakuna dalili na bado tunakwenda kufanya study, bado hakuna dalili ya Watanzania kupata fedha hii na ni wazi kwamba huu ulikuwa ni usanii wa kisiasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la tatu ni kuhusu mfumo wa kodi ambao mara nyingi tumekuwa tukiuliza na umekuwa ni wenye utata kwa kiasi kikubwa sana. Naomba nitoe maelezo kwamba mifumo ya kodi kwenye bandari hizi za Afrika Mashariki inatofautiana sana kutokana na interest za nchi na tozo ambazo zimo katika kila nchi ambayo inahusika na Bandari hizo husika. Kwa mfano, container ambalo lina futi 20, ina uzito sawa, thamani sawa, bandari ya Dar es Salaam wanatoza dola 240 wakati bandari ya Mombasa wanatoza dola 70 tu, hii ni tofauti kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kontena ambayo urefu wa futi 40, bandari ya Dar es Salaam wanatoza dola 420, wakati bandari ya Mombasa wanatoza dola 105, hii ni tofauti. Gari ambayo ina thamani ya dola 10,000 bandari ya Dar es Salaam wanatoza 1.6% wakati Bandari ya Mombasa inatoa 0.8% hii ni tofauti kubwa. Kuonesha kwamba utofauti huu haupo tu baina ya Bandari ya Zanzibar ambayo kila siku inakandamizwa, inaonewa kwa sababu tu ya mfumo huo wa kodi lakini suala hili haligusi bandari nyingine za Mombasa na bandari nyingine ambayo ziko ndani ya Afrika Mashariki na Kati. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kusema nini, nitakachokizungumza hapa, tumekuwa tukiuliza mara nyingi kwamba, vipi mifumo hii ya kodi ambayo inaenda kuua uchumi wa Zanzibar, inaenda kuua bandari ya Zanzibar, lini itapatiwa ufumbuzi na lini Wanzanzibari wataachwa waendeleze masuala yao ya biashara bila kulazimishwa kwamba eti wafuate mfumo wa TANCIS,kwa sababu tofauti hii zipo kila mahali.
Mheshimiwa Spika, tumekuwa tukilalamikia suala hili sana, nataka nioneshe sisi kama Wabunge kutoka Zanzibar kwa sababu sisi Wabunge kutoka Zanzibar Jimbo letu ni kama Zanzibar. Kwa sababu kama Mbunge siwezi kuzungumzia suala la maji Jimboni kwangu, siwezi kuzungumzia suala la kilimo jimboni kwangu, kwa hiyo, jimbo langu ni Zanzibar sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumezungumzia masuala hapa, hata leo tumezungumzia masuala ya kodi ya umeme. Sisi tumeuziwa umeme na TANESCO lakini tumeuziwa kwa bei ambayo si sahihi. Tumekuwa tukilalamikia, Serikali kupitia Wizara ya Fedha inatuambia tunazungumza. Tumekuwa tukizungumzia tozo za bandari haziko katika mazingira sahihi kwa bandari ya Zanzibar. Kodi zile zinaua bandari ya Zanzibar, tumeambiwa suala hili tunazungumza. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tumezungumza masuala ya vyombo ya moto, tumelalamika sana, leo ni vitu vya ajabu sana, leo mtu kutoka Burundi, mtu kutoka Kongo, mtu kutoka Zambia anaingia Tanzania na gari lake, anatumia miezi miwili kwa kujaza tu fomu pale mpakani, halafu anaweza kuongeza tena miezi miwili lakini mtu kutoka Zanzibar huu ni uonevu, udugu uko wapi? Mtu kutoka Zanzibar hana uwezo wa kuleta gari Tanzania Bara akaweza kutumia. Huo udugu wa damu uko wapi?
Mheshimiwa Spika, kila siku tunasema udugu wa damu, tunadumisha, tunadumisha ndio ni sahihi, hakuna anayekataa umoja lakini umoja uwe na nia njema. Tukizungumza haya tunaambiwa tunazungumza, tutazungumza mpaka lini? Miaka 54 ya Muungano, kero hizi zimeanza muda mrefu zipo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kila siku akija Waziri wa Fedha tutazungumza, akija Waziri mwingine yoyote, tunazungumza, tunazungumza mpaka lini? Juzi hapa tumelalamikia masuala ya Akaunti ya Pamoja ya Fedha. Leo tumeona kwenye kitabu kwa ajili ya Tume ya Pamoja ya Fedha inafanya kazi gani? Mheshimiwa Mpango kwenye hotuba yake amesema kabisa kwamba, tayari tume ile imekamilisha kufanya utafiti. Sasa hii fedha iliyotengwa hapa ya nini? Maana amesema mshahara ni zero points.
Mheshimiwa Spika, sasa kama kuna mshahara zero points sasa ile bilioni ngapi uliyoitenga imo kwenye kitabu ni ya kazi gani kama watu wamekamilisha utafiti na hii akaunti itaanzishwa lini ili tuone sasa kuna equality kwenye masuala ya mgawanyo wa fedha za muungano. Kuna equality katika makusanyo ya fedha za muungano, tujue nani anahusika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, yote haya tunaambiwa tunazumgumza. Huu unaoendelea unaitwa ulaghai wa kisiasa ambao hakika kila siku unaendelea kudumaza na kuua maendeleo ya upande mmoja wa Muungano. Kwa sababu hizi zote ambazo nimezizungumza hapa hizi ndizo channel za maendeleo katika Taifa, katika nchi. Zanzibar ni nchi ya visiwa inajitegemea kimaendeleo ina Serikali yake. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tuendelee kuangalia, Mheshimiwa Mpango aje atujibu sasa haya masuala ya kodi bandari na tozo. Leo Zanzibar pale unasafirisha hata vitenge 10, kanga 10 au tano, TV moja ya kuja kuangalia mwenyewe ukija pale unapigwa difference. Leo wafanyabiashara wote soko lote, tulilokuwa pengine lingekuwa soko linaloenda kuchukua bidhaa Zanzibar kuleta maeneo ya Tazania Bara mikoa tofauti leo wamehamia Uganda.
Mheshimiwa Spika, tukitoka hapo nje tu hapo wajasiliamali wapo wanasema hili shati linatoka Uganda hili, shati hili linatoka Kongo, kitenge hiki kinatoka wapi, wale wote walikuwa wanakuja Zanzibar wanachukua bidhaa na kuleta Tanzania Bara kuuza, leo soko lile wafanyabiashara wa Zanzibar limekufa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, mwisho niseme mwisho leo tunaambiwa hapa bidhaa zinazotoka na inasikitisha sana maji, kama kuna maji Zanzibar yanayozalishwa na kiwanda kilichopo Zanzibar hayaruhusiwi kuuzwa Tanzania bara. Inaashiria nini? Tulipiga marufuku sukari wakasema Zanzibar haitoshi. Hivi vifaa vyote, bidhaa zote zinazouzwa Tanzania Bara, zinazozalishwa Tanzania Bara ndio zikavushwa Zanzibar?
Mheshimiwa Spika, sio kweli huu ni usanii wa kisiasa ambao kimsingi haukubaliki, lakini tukisema tunazungumza hivi tunazungumza na nani? Tunazungumza na mtu ambaye hana mamlaka, mtu ambaye hana uwezo wa kusema, mtu ambaye wanaenda kuzungumza naye asubuhi jioni wanamwona mpuuzi wanasema achana naye yule. Sisi tunaendelea na mambo yetu, hili haliwezekani.
Mheshimiwa Spika, naomba nizungumze hayo kwa masikitiko makubwa nikijua kwamba Wizara ya Fedha na Mipango itakuja na majibu ya haya sasa kuona kwamba vipi tunaenda kutatua hizi changamoto ambazo tumezizungumza hapa, kwa nia njema kabisa na kwa nia njema kwa nchi hizi. Hizi story za kwamba tunazungumza, tunazungumza at least zifikie mwisho sasa tuone kwamba maendeleo haya yanakuwa kwa Tanzania nzima na sio upande mmoja wa Muungano.
Mheshimiwa Spika, Zanzibar haina pa kwenda, Zanzibar hatulimi mahindi, Zanzibar hatulimi nyanya, Zanzibar hatulimi, yote tunatumia kutoka Tanzania Bara na yanaingia vizuri tu, lakini leo kinachozalishwa Zanzibar unaambiwa lazima tukifikie kiwango hiki, lazima tutoe hiki.