Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

Hon. Rose Cyprian Tweve

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Fedha na Mipango

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kutoa mchango wangu siku ya leo. Awali ya yote naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Watendaji wote wa Wizara kwa kazi kubwa ambayo wanaifanya. Ni matumaini yangu Watanzania wanatambua mchango mkubwa ambao wanautoa kwenye Wizara yao na kwa Taifa hili.

Mheshimiwa Spika, nina jambo moja tu ambalo nitapenda kuliongelea siku ya leo ambayo ni issue ya hawa ndugu zetu wa TIRA (Tanzania Insurance Regulatory Authority). Mwaka 2009 Bunge lako lilipitisha Sheria Ndogo, Sheria ya Bima Na. 10 na lengo lilikuwa ni kutatua changamoto kwa wananchi, hasa pale wanapopata ajali, kama mtu amepoteza maisha, basi ndugu zao waweze kupata fidia na kama kuna upotevu wa mali, basi waweze kupata stahiki zao.

Mheshimiwa Spika, kama Mheshimiwa Waziri alivyokiri kwenye hotuba yake ukurasa wa 60 kumekuwa na upungufu mkubwa kwenye chombo hiki ambacho kilipewa mamlaka ya kusimamia na kuratibu taratibu zote zinazohusu bima nchini. Kwenye ukurasa wa 60 Mheshimiwa Waziri anasema, Wizara imekuwa ikipokea malalamiko kutoka kwa wananchi hasa ya ucheleweshaji wa fidia pale wanapopatwa na majanga. Hiki kimekuwa ni kilio kwa nchi nzima hasa wananchi wangu wa Mkoa wa Iringa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chombo hiki kimekuwa na upungufu mkubwa, kwanza hakijulikani na hao wachache wanaokijua chombo hiki, notion iliyopo inakuwa ina-benefit sana makampuni ya Insurance badala ya wananchi wa kawaida. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, chombo hiki kiliundwa kuhakikisha kinaratibu shughuli zote za bima, lakini suala hili niliuliza ilikuwa tarehe 3 Aprili, nikataka kujua takwimu ni ajali ngapi zimetokea na watu wangapi walikuwa wamelipwa stahiki zao? Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo hapa kuanzia 2016 - 2018 ni majeruhi na vifo ilikuwa ni zaidi ya 14,000. Mpaka tarehe hiyo 3 Aprili, Mheshimiwa Waziri alipokuwa anatolea hapa ufafanuzi ni watu 1,500 tu ndio ambao walikuwa wamelipwa stahiki hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, hiki chombo kifanyiwe mapitio, kumekuwa na upungufu mkubwa sana. Kuna hata hili suala ambalo wameweka la Msuluhishi wa Bima. Chombo hiki hakitambuliki na ofisi yao ipo moja tu Dar es Salaam. Sasa kwa hali halisi Mheshimiwa Waziri mtu atoke sijui Makete, Njombe, Iringa aende kwa huyu Msuluhishi wa Bima inakuwa ni kazi kubwa. Kwanza umbali na pili ni gharama.

Mheshimiwa Spika, juu ya hilo, kuna upungufu, huyu Msuluhishi wa Bima anataka kuonana na mdai mwenyewe, hawaruhusu Mwanasheria au Mwakilishi yeyote kukutana na chombo hiki. Namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kwa sababu hawa TIRA wako chini ya Wizara yake, hebu tuangalie tena kwa namna ya utendaji wao kazi. Moja, watoke maofisini waweze kuwafikia wananchi.

Mheshimiwa Spika, elimu ya Bima bado ipo nyuma kwa wananchi wetu, wengi wanajua tu ni Bima pale ajali inapotokea. Kuna wananchi wengi mkoani kwetu Iringa pale wanajishughulisha na shughuli nyingi za kilimo, mashamba yanaungua pale lakini hawajui bidhaa ambazo zinapatikana kwenye hizi huduma za bima ili pale wanapopata majanga waweze kupata stahiki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu ni kwamba kwanza tupitie sheria, kama kuna upungufu wowote ziletwe hapa zipitiwe ili tuweze kufanya mabadiliko tuwasaidie Watanzania. Pia TIRA wapewe pesa za kutosha. Najua sasa hivi wameanzisha Website yao, nawapongeza kwa hilo, at least inafanya kazi, watu wanaweza ku-check wamelipwa premium zao wanaweza kufanya follow-up kujua kama zimelipwa na hayo makampuni. Kwa hiyo, wapewe pesa za kutosha, watoke maofisini wasiishie Dar es Salaam, waweze kufika sehemu mbalimbali hata zile za vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hizi dakika chache zilizobaki, naomba pia niwasemee Walimu. Kumekuwa na manunung’uniko makubwa juu ya kulipa malimbikizo yao. Tunajua wana mchango mkubwa sana kutuandaa na na kutulinda. Wengine tumefika hapa Bungeni ni mchango wa Walimu.

Mheshimiwa Spika, najua Mheshimiwa Naibu Waziri alitoa ufafanuzi mzuri asubuhi, tunaomba kuendelea ku-keep update kuhakikisha tunalipa hizi stahiki zao kwa wakati, wanafanya kazi kubwa kuhakikisha wanajenga Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, nashukuru kwa kunipa nafasi hii.