Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Male
Party
CCM
Constituent
Nachingwea
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. HASSAN E. MASALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kunipa nafasi ya kuweza kuwa mchangiaji wa kwanza wa Mpango wa Serikali kwa mwaka 2019/2020. Naomba nijielekeze kwenye eneo moja baada ya kuwa nimeupitia mpango wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia, kabla sijasema nilichokusudia kusema naomba nitumie nafasi hii kwanza kupongeza jitihada kubwa ambazo zimekuwa zinafanywa na Serikali yetu katika kuhakikisha mipango tuliyoipanga mwaka 2018/2019 inakwenda, lakini wakati huo tuna-focus kuangalia namna ya kutekeleza mipango ya mwaka wa 2019/2020.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukamilisha mipango ambayo tunaipanga kwa sehemu kubwa lazima tuangalie mambo gani ambayo yanatuwezesha kuhakikisha mipango yetu tunayoipanga inakwenda sambamba. Leo naomba nijielekeze kwenye eneo moja tu la kilimo kwa sababu ya kazi kubwa au faida kubwa ambayo tunaipata kupitia kilimo ambacho tunakishiriki au tunakifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kilimo ndiko ambako tumekuwa tunaboresha huduma nyingine za kijamii. Kupitia mipango ambayo Mheshimiwa Waziri leo ameiwasilisha hapa kwa sehemu kubwa ndiko ambako tunapata fedha kwa ajili ya kuhakikisha mambo mengine yote yanakwenda ikiwemo maji, afya, barabara, lakini pia tunapozungumzia viwanda lazima tuzungumzie malighafi ambazo zinatokana na kilimo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya utangulizi huo naomba pia, nitumie nafasi hii kutoa pongezi kwa Mheshimiwa Rais pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu. Wamefanya kazi kubwa, lakini kwetu sisi wakulima ambao tunatokana na zao la korosho ambalo limetoa mchango mkubwa sana kwa mwaka wa fedha uliopita nimeona nilizungumzie hili kwa kina kwa sababu, kama sitafanya hivi hata wakulima ambao nawawakilisha hapa ndani nafikiri hawawezi kunielewa. Kwa hiyo, naomba nijielekeze zaidi kuzungumzia zao la korosho na namna ambavyo limeleta fedha nyingi kwa ajili ya kuimarisha uchumi wetu na hivyo kuhakikisha mipango tunayoipanga inakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu pamoja na Mheshimiwa Waziri Mkuu wamefanya kazi ya kukaa na wanunuzi wa korosho, lakini pia, wamefanya intervention kubwa sana kuhakikisha hali inayoendelea sasa hivi katika maeneo yanayolima korosho haiendelei kuwa mbaya. Katika hili naomba nitoe pongezi kwa niaba ya wale ambao tunawawakilisha kwa sababu, walichokifanya viongozi hawa ni sehemu ya kilio ambacho sisi wakulima tayari tulishakuwanacho. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua ambazo zimechukuliwa na viongozi wetu bado yako mambo ambayo niliona nitumie nafasi hii kuishauri Serikali. Vikao walivyovifanya pamoja na wafanyabiashara, pamoja na kwamba, matarajio yetu yalikuwa ni kuona korosho za wakulima zinaondolewa, lakini bado mpaka leo ninapozungumza kwa makadirio ya haraka haraka kuna jumla ya tani 34,000 kupitia vyama vikubwa vitano mpaka sasa hivi zimekusanywa. Katika hizi tani ambazo zimekusanywa jumla ya tani 2,500 plus kwenda 3,500 ndizo ambazo zimeuzwa mpaka leo ninapozungumza kwa mnada uliofanyika leo kwenye baadhi ya maeneo ya Tandahimba kule kupitia TANECU.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii na muda ambao tunao kwa kweli, kidogo inatupa mashaka sisi wakulima ambao tumewekeza sehemu kubwa ya fedha zetu kwenye eneo hili. Kwa hiyo, nataka tuone kupitia watu wa Wizara ya Fedha, lakini pia kupitia watu wa Wizara ya Kilimo na pia kupitia Mheshimiwa Rais mwenyewe kwa sababu, yeye ndio mtu wa mwisho ametoa kauli na tunaamini kiitifaki yeye ndiye pia, anapaswa kurudi na kwenda kulizungumzia jambo hili, basi apokee mapendekezo ambayo yanatoka kwa wakulima ili tuweze kuwasaidia kuondokana na hasara ambayo inaweza kwenda kujitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara ambao walikaa kwenye kile kikao ni kama wamesusia, naweza nikasema hivyo. Kwa sababu, ukiangalia trend ya tani wanazozichukua na makubaliano yaliyofanyika hayafanani na kiasi cha korosho ambacho wakulima tunategemea tukiuze. Misimu kwa kawaida huwa inaanza mwezi wa 10, leo tunapozungumza ni mwezi wa 11, nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wa Kilimo anazungumza kwamba, msimu wa korosho ni miezi mitatu, ni kweli, lakini kuna vitu ambavyo nafikiri bado hajaijua korosho na hajaiishi korosho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimueleze kwa sisi tunaotoka kwenye maeneo ya korosho, ikishaanza kunyesha mvua hiyo miezi mitatu ambayo anaihesabia ambayo mpaka sasa hivi hatujafanya biashara itakuwa tena hakuna biashara ambayo inaenda kufanyika kule mara mvua itakapokuwa imeanza kunyesha kutokana na Jiografia ya maeneo yetu, lakini pia kutokana na hali ya hewa ambayo inaathiri kwa kiasi kikubwa sana korosho za wakulima ambao wametumia gharama kubwa kuzihudumia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya juu katika minada hii ni Sh.3,016/= na bei ya chini imebaki Sh.3,000/= ileile, jambo ambalo sisi tunashukuru kwa sababu, Mheshimiwa Rais alizingatia gharama za uzalishaji ambazo wakulima wamezifanya katika kipindi chote cha kuandaa mashamba, kuvuna, kuokota pamoja na kupeleka kwenye maghala. Ushauri ambao nataka niutoe ni huu ufuatao; kwa sababu wanunuzi wameshindwa kununua hizi korosho kwa kadri ya makubaliano yalivyokuwa yamewekwa, pendekezo la kwanza ambalo nataka nitoe ni kwa Serikali kwa kadri ilivyokuwa imezungumzwa siku ile ya kikao ambacho Mheshimiwa Rais alifanya, Serikali ione uwezekano wa kuzinunua hizi korosho kama hiyo njia tumejipanga nayo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivi kwa sababu ambayo nimeshaitaja kwamba, tuliotegemea wanunuzi wazinunue wameshindwa kununua na sasa hivi muda unakwenda na tunategemea watarudi kwenye duru ya pili ambayo pia, haioneshi matumaini ya kwamba, bei itaenda kupanda zaidi ya bei ambayo Mheshimiwa Rais ameipendekeza. Kwa hiyo, Serikali yetu kama imejipanga na fedha ipo, basi tunaomba ichukue hatua za makusudi za haraka kunusuru hali inayoendelea kule sasa hivi, ili korosho za wakulima ziweze kuchukuliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pendekezo la pili, hebu twende tuangalie kwenye Bodi ya Korosho yenyewe. Bodi ya Korosho kuna tozo na kuna fedha ambazo kama Serikali itaenda kuzikata nina hakika zitaenda kumpunguzia mnunuzi mzigo na hivyo azma ya kununua korosho kwa Sh.3,000/= itabaki palepale na haitaathiri pendekezo ambalo Mheshimiwa Rais amelitoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tozo ya kwanza ambayo napendekeza ikatwe ni tozo ya service charge. Hawa wanakata Sh.10/=, badala ya Sh.10/=, nashauri Serikali ingewaagiza watu wa bodi wakate Sh.5/= ibaki kwa wanunuzi Sh.5/=, ibaki kwa watu wa bodi kwa ajili ya ku- service hizo huduma ambazo wanaendelea kuzifanya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la pili naomba nipendekeze kukata fedha ya kugunia; fedha ya gunia inakatwa Sh.52.5/= napendekeza ingekatwa Sh.42/= ili 10/= itakayokatwa iingie katika kuhakikisha mnunuzi habebi mzigo mzito kwa sababu wanazozitoa za kushuka kwa soko la dunia. Basi naamini kwa kufanya hivyo itaenda kupunguza uzito ule wanaoupata sasa hivi kwenda kununua korosho zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pendekezo la tatu tuiangalie pia, export levy ambayo kimsingi kuna 15% ambayo tayari hata Mheshimiwa Rais alishaizungumzia. Naomba nishauri hapa, badala ya 15%, Serikali ingebakiwa na 9% ili tuache 6% kwa wanunuzi, nayo pia itaenda kutusaidia. Ikiwezekana hii tutakwenda kusaidia kununua korosho kwa bei ambayo Mheshimiwa Rais ameipanga na hii nafikiri itaenda kutunufaisha sisi wakulima ambao tumeingia gharama kubwa kwa ajili ya kuhakikisha kilimo kinakwenda kutunufaisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo la mwisho katika eneo hili ni kupitia makato yale yote yaliyoko kwenye fedha ya mjengeko wa bei. Kuna makato ambayo kwa hali ilivyo na kwa sababu, hatukujipanga na hiki ambacho kinajitokeza, basi tungeangalia kwenye ile fedha ya mjengeko wa bei Sh.240/= kuna fedha kule za vyama, kuna fedha kule kwa ajili ya kuhudumia vyama vya ushirika, hizi zote tungeziangalia vizuri, lakini pia tungetoa maelekezo kwenye halmashauri zetu ziondoe zile fedha ambazo hazina ulazima kukaa kwenye fedha hii, ili mkulima aweze kunufaika, lakini pia, wafanyabiashara wasipate hasara ambayo wanafikiri wataipata kama watachukua korosho zetu.