Bunge la Tanzania
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania
Sex
Female
Party
CCM
Constituent
Special Seats
Contributions
nil
Answers
nil
Commettees
0
Ministries
nil
MHE. ZAYNAB M. VULU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nianze kwanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kufika hapa na kuipongeza Serikali yangu kwa kutimiza miaka mitatu katika utekelezaji wa shughuli zake. Pongezi nyingi kwa Mheshimiwa Rais, pongezi nyingi kwa Baraza la Mawaziri, pongezi nyingi kwa viongozi wote waliokuwa maeneo mbalimbali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumzia Mpango wa Maendeleo. Naomba kwanza nianze kupongeza kwa yale ambayo yemetekelezwa kwa wakati na yakakamilika. Hapo hapo, naipongeza Serikali kwa kuthubutu kutengeneza reli ya Standard Gauge kwa kutumia fedha za ndani kitu ambacho siyo cha kawaida. Kwa kutumia fedha za ndani, Mheshimiwa Rais amethubutu na ameweza kuanza kuijenga reli hiyo. Ujenzi wa reli hiyo utatusaidia kukuza uchumi wetu kwa sababu itarahisisha suala la usafiri iwe wa abiria, iwe wa mizigo kwa Tanzania na hata kwa nchi jirani na kwa muda mfupi sana. Ujenzi wa reli unakwenda sambamba na ujenzi wa barabara ambazo zinaunganisha Mikoa yote nchini Tanzania hata zile za kwenye Halmashauri zetu tunakotoka. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni ufufuaji wa reli ya kutoka Ruvu – Tanga – Moshi. Hili ni jambo jema. Reli hii ilisahaulika kwa muda mrefu sana. Ukichukulia hii awamu ya uchumi wa viwanda, reli hii itakuwa kiunganishi cha usafiri hasa kwa wale ambao mikoa yao imepakana na reli hii, wanaofanya biashara ikiwemo Mkoa wetu wa Pwani, ambako kuna viwanda vingi, imevunja record, viwanda vingi vinazalisha na malighafi zinatoka ndani na nje ya nchi yetu. Kwa hiyo, hili litakuwa litasaidia sana na sisi wote hapa ni mashuhuda. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, napongeza Serikali kwa juhudi ambazo zimeanza upya za ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo. Hii ni bandari ambayo inatakiwa ijengwe kwa wakati kwani itasaidia katika kukuza uchumi wetu na wa nchi nyingine. Kuna kikwazo kidogo, sina mashaka, nina uhakika Serikali italifanyia kazi kwa maana ya kulipa fidia wale wananchi waliokaa katika maeneo yale ili ujenzi uanze na uende kwa wakati na watu wa kujenga hiyo bandari tunawajua ni watu wa kutoka Oman na Wachina wako pale wanasubiri. Kwa hiyo, ulipaji wa fidia ni jambo la msingi na juhudi tunaziona. Juzi tulikuwa na Makamu wa Rais katika Mkoa wetu wa Pwani, aliweka juhudi ya kwenda kuona jinsi bandari ile ilivyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya kama tutaweka utaratibu wa ujenzi wa Bandari ya Uvuvi. Nchi yetu ina eneo kubwa sana la ukanda wa bahari lakini hatuna bandari mahsusi kwa ajili ya uvuvi. Ni wakati muafaka sasa tukaweka Bandari ya Uvuvi ikaweza kuwasaidia wavuvi wakubwa na hata wadogo wadogo. Bandari zetu za uvuvi ziwepo lakini yale maeneo ya fukwe (beach) ambapo wanachi wanaweza kwenda wakapumzika, ijulikane hili ni eneo la kupumzika na hili ni eneo la biashara ya uvuvi kuliko sasa hivi maeneo mengi ya ufukwe yamechanganyika kati ya wavuvi na watu wanaotaka kwenda kupumzika jioni. Mfano mzuri, miaka ya nyuma, pale Posta ya zamani ule ufukwe ulitengenezwa vizuri na wananchi wengi jioni walikuwa wanakwenda kupumzika, wanapata upepo wa bahari na kupata afya nzuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tupo kwenye awamu ya uchumi wa viwanda ambao unakwenda sambamba na nguvu kazi ya wananchi ambayo inatokana na afya bora, naipongeza Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na Hospitali za Wilaya. Kwenye maeneo ambayo majengo hayajakamilika, yalijengwa kwa nguvu za wananchi, ni vyema sasa Serikali ikaongeza juhudi zake, ikatenga fedha, ikashirikiana na wale wananchi kwenye yale maboma, wakajenga na kuhakikisha majengo yale yanakamilika ili wananchi wetu waweze kupata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, huduma ya ujenzi ndiyo hiyo tunaiona na magari ya wagonjwa tumeona yamepelekwa, tunaomba maeneo mengine ambako hamna magari ya wagonjwa yapelekwe. Kwenye maeneo ambayo majengo yamejengwa na vyumba vya upasuaji vimeshajengwa, nashauri na kuiomba Serikali iangalie uwezekano wa kupeleka vifaa tiba na miundombinu ya kuweza kufanya kazi vizuri katika hayo maeneo, kwa maana ya Madaktari wa Upasuaji, Madaktari wa Macho na wa magonjwa mbalimbali ili iweze kukidhi standard ya kile kituo ambacho kimejengwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, utakuta maeneo mengi hawana hata vifaa vya kupimia sukari kwa wagonjwa wasukari na vya kupimia pressure. Ni vizuri sasa tukapeleka zaidi hivyo vifaa kule chini vitasidia wananchi wasiweze kuhamishwa kutoka hospitali hiyo kwenda kwenye ngazi ya Hospitali ya Wilaya au ya Mkoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika naipongeza Serikali yangu kupitia Wizara ya Afya kwa hatua ilizofikia kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaimarika. Inahakikisha idadi ya vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua inapungua, hali kadhalika na matatizo mengine yanayomkuta mwana mama. Hili ni jambo jema lakini bado kampeni hii naomba iendelee. Pia naomba ikiwezekana vile vifaa vya kujifungulia mama kwa sababu mama naye ana haki ya kuzaa salama na mtoto hana kosa lolote, anahitajika azaliwe, aishi maisha salama, ni vyema basi vile vifaa tiba ikaangaliwa uwezekano, bei iliyokuwepo siyo kubwa sana, lakini bado siyo vibaya kama itapungua zaidi ya hapo, ikibidi hata wakipewa bure nao ni haki yao ya msingi. Kwa hiyo, ni vizuri tukaliangalia hilo ili kuweza kumlinda mama mjamzito, mama anayejifungua halikadhalika na yule mtoto anayezaliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali yangu inavyosaidia watoto wanaozaliwa na vichwa vikubwa. Mungu azidi kuwasaidia hao watoto lakini juhudi tumeziona. Maagizo na maelekezo kwenye Halmashauri zetu tunayasikia yakitolewa. Haya ni mambo mazuri sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nigusie suala la maji. Maji ni muhimu sana. Tunalenga kumtua mama ndoo kichwani lakini pia tunalenga kumtua na baba ndoo kichwani kwa sababu naye kama hajaoa lazima akajitafutie mwenyewe maji. Juhudi ya Serikali iliyofanyika kusogeza huduma ya maji tunaipongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miradi mikubwa ya maji tuliyoiona, tumeona Mradi wa Maji wa Kisarawe, nashukuru Serikali na imefanya vizuri lakini naomba speed isilegee, iendelee, speed iwe nzuri, watu waweze kupata maji, hasa wale ambao hawajapata maji ya bomba kwa muda mrefu hasa Wilaya ya Kisarawe. Vilevile kuna Mradi wa Maji Mkuranga na Chalinze na naipongeza Serikali kwa Mradi wa Maji wa Mafia Jibondo. Hicho kisiwa kilikuwa hakijawahi kusikia hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.