Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa fursa hii. Nianze kwa kumpongeza sana mtoa hoja Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa kutuletea mpango huu mzuri sana ambao kwa kiasi kikubwa sana unahitaji maoni yetu sisi Wabunge kuweza kuuboresha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mezani kwangu hapa nina nyaraka kama tatu hivi ambazo zote zinahitaji sisi Waheshimiwa Wabunge tuzipitie ili tutoe maoni ili na Mheshimiwa Dkt. Mpango ayazingatie atakapokuja mwezi Machi hapa kutuletea mpango wenyewe. Nitakuwa na maoni katika maeneo kadhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ni ugharamiaji wa mpango. Nitazungumzia namna gani mpango utagharamiwa kwa kupitia miradi ya PPP. Sijaona hasa, bahati nzuri tulirekebisha Sheria ya PPP Bunge lililopita ili tuone namna gani tunaweza tukavutia miradi mingi ya PPP ili kupunguza mzigo wa Serikali katika kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kiasi kikubwa sana, bado sijaona hasa namna gani miradi ya PPP inaweza ikatupunguzia mzigo. Kama tatizo ni sheria, basi hiyo sheria ileteni tena tuibadilishe ili tupate kuvutia wawekezaji wengi. Miradi niliyoiona humu ndani, kwa heshima sana, miradi sijui ya kujenga Hostel za CBE, miradi ya kujenga VETA na MSD, kwangu ni miradi mizuri, lakini naiona ni miradi midogo. Tunahitaji kuvutia miradi mikubwa zaidi ili miradi hii ya PPP ipunguze mzigo kwa Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, imezungumzwa sana hapa. Nami nilipata bahati wiki mbili zilizopita, tulikuwa na ziara ya Makamu wa Rais, tumeona pale hali inakwenda vizuri lakini tunaiihitaji bandari hii sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bandari ya Bagamoyo pamoja na mradi wa Standard Gauge ni miradi miwili pacha. Tunahitaji meli kubwa ziende pale. Bandari ya Dar es Salaam pamoja na kwamba tunaiboresha hivi sasa lakini hizi meli zinakwenda kwa generations. Bandari ya Dar es Salaam inaweza ika-host pale meli ambayo ni za third generation basi na sasa hivi dunia inakwenda mpaka kwenye tenth generation.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunahitaji tupate Bandari ya kisasa ya Bagamoyo ambayo itaweza kubeba mizigo mikubwa, meli kubwa zenye kubeba mpaka container 10,000 ndiyo SGR itakuwa na maana zaidi. Kwa sababu ile SGR inahitaji iwe feeded na mizigo mizito. Kama meli haziwezi kufunga katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na ufinyu wa magati pale, tutarajie kwamba Bandari ya Bagamoyo itakapokuwa kubwa ndiyo itaweza kuifanya SGR kuwa na manufaa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, limezungumzwa hapa suala la Bandari ya Uvuvi. Mheshimiwa Waziri atakubaliana nami, tulipokuja kwenye Kamati tulizungumza hili suala la Bandari ya Uvuvi, tunahitaji kuwa na bandari hii pengine sambamba na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo, pale pale tuweke na section ya Bandari ya Uvuvi ili tupate kuua ndege wawili kwa jiwe moja. Kwa sababu tunaona suala la ujenzi wa Bandari ya Uvuvi limekuwa likisuasua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mwenyewe ni shahidi, tulitenga pesa mwaka 2013/2014 shilingi milioni 500 kwa ajili ya feasibility study. Feasibility study imefanyika lakini hakuna kinachoendelea. Bajeti hii tuna shilingi milioni 300 kwa ajili ya feasibility study ya hiyo hiyo Bandari ya Uvuvi na bado hatujajua hata location Bandari ya Uvuvi itakuwa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, naomba sana Bandari ya Uvuvi iunganishwe na ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo ili tumalize hili tatizo. Hili suala ambalo amelizungumza ndugu yangu Mheshimiwa Rehani vizuri kabisa la kuwa na meli zetu wenyewe kwa ajili ya uvuvi katika Bahari Kuu ni muhimu sana pamoja na kufufua lile Shirika letu la Uvivu la TAFICO. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu leo yupo hapa. Kwenye masuala haya ya usafiri wa bahari, nilikwenda ofisini kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, tukakaa pale Speaker’s Lounge na Mheshimiwa Waziri Mbarawa kuhusiana na tatizo la usafiri katika Kisiwa cha Mafia na meli ile ambayo Bakhresa ameipa Serikali bure kabisa ili ije itusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba Waziri mwenye dhamana Mheshimiwa Isack Kamwele hataki kuipeleka meli ile Mafia. Ameniambia point-blank kwamba hatupeleki meli hii Mafia kwa sababu hakuna abiria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wananchi wa Mafia wako katika kadhia kubwa sana ya usafiri hivi sasa. Tunasafiri na magogo ambayo wakati wowote yanaweza yakapata madhila yakazama. Leo Serikali imepewa meli bure na Bakhresa, iko pale DMI, namshukuru sana Mheshimiwa Waziri Nditiye amenipa ushirikiano mkubwa sana kwenye hili, lakini Waziri Kamwele amenitamkia. Namwambia mbona kuna maagizo hapa tuliongea na Mheshimiwa Waziri Mkuu na wakati ule Waziri Mbarawa, tukakaa pale Speaker’s Lounge, Mheshimiwa Waziri Mkuu akatoa maagizo? Yeye anasema, hayo mambo ya siasa, achana nayo. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nashangaa, hivi maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ni mambo ya siasa? Mheshimiwa Waziri Kamwelwe anakataa kutekeleza maagizo ya Waziri Mkuu anayaita maagizo ya kisiasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubwa zaidi, nimeongea na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Mheshimiwa Hawa Mchafu anisaidie kufikisha huu ujumbe. Mheshimiwa Hawa Mchafu anakwenda kuongea na Mheshimiwa Waziri Kamwele anamwambia siwezi kupeleka meli Mafia itabidi nitoze nauli labda Sh.100,000, hailipi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka Mheshimiwa Waziri Mkuu anieleze, je, ile habari ya kupeleka meli Mafia ni habari ya kisiasa? Labda Waziri atakapokuja kujibu atuambie, kwa sababu meli tumepewa bure, haihitaji usanifu, haihitaji bajeti, haihitaji sijui upembuzi yakinifu, inatakiwa kauli tu kwamba meli peleka Mafia. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ninavyozungumza pale Nyamisati kuna watu 150 wanalala pale wamekosa boti na wanasafiria boti za mbao. Boti ya kisasa ipo lakini wakubwa hawataki kuipeleka Mafia kwa makusudi tu. Sasa mnaipeleka wapi basi? At least mtuambie mnaipeleka wapi kwa sababu kule Zanzibar boti za Bakhresa ziko nyingi tu. Huwezi kupeleka sehemu nyingine yoyote isipokuwa labda ni Mafia. Mheshimiwa Waziri anasema achana nayo hiyo. Kwenye bajeti hii tunashukuru sana…

K U H U S U U T A R A T I B U . . .

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ingekuwa taarifa, basi nasema nimeipokea na naomba iwe sehemu ya mchango wangu. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bado nasisitiza, sitaki niwe mbashiri mbaya, likitokea tatizo pale kwenye kivuko kile cha kutoka Nyamisati kwenda Mafia, halafu watu wakapoteza maisha, tunachokuomba Mheshimiwa Waziri Kamwelwe usije Mafia kuendesha zoezi la rambirambi pale. Maana yake inaonekana wewe ni fundi sana wa kukusanya rambirambi na masuala ya uokozi, sisi hatuko tayari kwa hilo. Kama unataka kutusaidia, utusaidie sasa hivi, usitusaidie wakati wa majanga kwa sababu meli ya kisasa kabisa ipo.