Supplementary Questions from Hon. Juliana Daniel Shonza (49 total)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo la Maswa linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo la Wilaya ya Momba, kwa sababu Wilaya ya Momba haina hospitali ya Wilaya. Kipindi cha kampeni Mheshimiwa Rais alituahidi kutupatia majengo ya pale Chipaka yatumike kama hospitali ya Wilaya. Nataka kujua, je, Serikali ina mpango gani wa kutupatia majengo yale ili yatumike kama Hospitali ya Wilaya ya Momba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Momba hatuna hospitali ya wilaya pale na siyo hospitali ya wilaya hata zile infrastructure za wilaya yenyewe, halmashauri hatujakaa vizuri. Momba kwa sababu ni eneo jipya, mkakati wetu ni kuweza kuimarisha, lakini kwa sababu kuna majengo tayari, kikubwa zaidi ni kwamba wataalam watatakiwa kufika pale kufanya assessment ya hayo majengo.
Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri katika ziara yangu ambayo nitaanzia Mkoa wa Iringa kuanzia tarehe 17 vilevile nitafika na maeneo ya Momba. Nikifika Momba, nitaomba wanifikishe katika yale majengo. Lengo letu ni nini? Tubainishe jinsi gani wananchi wataweza kupata huduma hizi. Kwa hiyo, namshukuru sana Mheshimiwa Juliana Shonza kwa juhudi kubwa anayofanya kwa ajili ya wananchi wa Momba.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika jibu la msingi Mheshimiwa Waziri amesema kwamba usanifu umekamilika katika Miji ya Isongole, Vwawa pamoja na Tunduma, lakini nisikitike kusema kwamba neno usanifu umekamilika bado haliwezi kuleta matumaini kwa akina mama wa Mkoa wa Songwe ambao wanapata shida kubwa sana ya maji. Kwa hiyo, napenda kuomba Mheshimiwa Waziri aniambie kwamba ni lini mradi huo utaanza katika maeneo hayo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili la nyongeza kama tunavyojua Mkoa wetu wa Songwe ni mkoa mpya na lengo la kuleta Mkoa mpya ni kusogeza huduma karibu na wananchi. Huduma mojawapo ni huduma ya maji ili akinamama wale wa Mkoa wa Songwe waweze kupata huduma kama inavyostahili. Hata hivyo, nioneshe masikitiko yangu makubwa kwamba mpaka sasa, hasa…
MWENYEKITI: Naomba uulize swali tafadhali!
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nauliza. Kwa maeneo ambayo ni ya pembezoni, mfano kule Ibaba, Ileje, ukienda Mkwajuni Wilaya ya Songwe, ukienda Iwula, ukienda Kamsamba bado miundombinu ya maji haijakaa vizuri. Naomba kupata jibu la Mheshimiwa Waziri kwamba ni lini Serikali itajenga miundombinu mizuri ya maji, hasa kwa maeneo ambayo ni ya pembezoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyofuatilia upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi wake na kwa sababu ni Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum nafikiri wananchi hawakupoteza kura zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ameniuliza maswali mawili ya nyongeza, ni lini miradi hii iliyofanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina itaanza. Kama nilivyojibu katika swali la msingi kwamba, tayari sasa hivi Serikali inafanya majadiliano na wafadhili kwa ajili ya kupata mikopo ya masharti nafuu. Hii miradi ni mikubwa, uwezo wa Serikali tunaendelea lakini bado siyo mkubwa sana kiasi cha kuweza kutekeleza miradi mikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba kuna Miji ya Mkoa wa Songwe, Mkoa ni mpya, kuna maeneo mengi bado hayajapata huduma ya maji. Serikali inaendelea, tumeanza programu ya kwanza ya maendeleo ya maji mwaka 2006/2007, programu ya kwanza ya miaka mitano imekwisha mwaka 2015 Disemba. Sasa hivi tumeanza programu ya pili, kwa hiyo ile miradi ambayo haikukamilika, miradi ambayo haikuanza katika awamu ya kwanza, basi tutaianza na kuikamilisha katika awamu ya pili.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Katika majibu ya msingi ya Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba benki hii kwa sasa inajikita katika kutoa huduma kwa kutumia vituo vya mikopo. Sasa nataka nijue kwamba ni lini wanawake wa Mkoa wa Songwe watapata kituo angalau kimoja ili waweze kujiinua kiuchumi?
Swali la pili, kwa kuzingatia kwamba madhumuni ya uanzishwaji wa benki hii ni kuwainua wanawake wanyonge, hususan wanaoishi vijijini, ambao hawana uwezo wa kumiliki ardhi wala nyumba kama ilivyo kwa wanawake wangu wengi wa Mkoa wa Songwe, lakini masharti ya mikopo ya benki hii kimsingi hayatofautiani sana na masharti ya benki nyingine. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kurekebisha masharti haya ya mikopo ya benki ili basi wanawake wa Mkoa wa Songwe waweze kunufaika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Napenda nimpongeze kwa kuwajali wanawake wa Mkoa wa Songwe, yeye akiwa kama Mbunge wa eneo hilo na mimi nikiwa kama Balozi wa Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza ni lini tutafungua angalau kituo kimoja cha mkopo kwenye Mkoa huo. Naomba nimpe taarifa kwamba tayari tuna kituo kimoja Songwe, maeneo ya Tunduma na kwamba tayari tumemwambia kwenye jibu letu la msingi kwamba tunauweka Mkoa wa Songwe katika mpango wetu wa kufanya kazi wa mwaka 2017/2018. Hivyo mtaji utakaporuhusu basi tutaufikiria mkoa huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, naomba na yeye atuhurumie kwa kutambua kwamba tayari benki yetu inajitanua kidogo kidogo na kwa sababu Songwe imemeguka kutoka Mkoa wa Mbeya, ambao tayari una vituo 11 vya kutolea mikopo, atuhurumie twende na maeneo mengine, kama kumwongezea basi tutamwongezea kidogo sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, kuhusu masharti ya mikopo kwenye Benki ya Wanawake; tayari Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto alikwishatoa maelekezo Siku ya Wanawake Duniani mwezi wa Machi mwaka huu, kwamba Benki ya Wanawake iweke utaratibu mpya wa kushusha masharti na gharama za kutoa mikopo kwa wanawake ili wanawake wenye kipato cha chini waweze kumudu gharama za kurejesha mikopo hiyo bila usumbufu wowote. Tayari maelekezo haya ya Mheshimiwa Waziri yanafanyiwa kazi na Benki yetu ya Wanawake.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye bajeti ya mwaka huu tayari tumeweka provision, ambapo kutakuwa kuna fungu maalum la pesa litakalokwenda moja kwa moja kwa wanawake wenyewe, badala ya kutumika katika administrative activities za benki.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na ni mkoa ambao uko mpakani, lakini kiongozi ambaye anahusika na mambo ya ulinzi na usalama wa Mkoa wetu wa Songwe ambaye ni RPC anaishi kwenye nyumba ambayo ni sawa na gofu. Nilitaka kupata kauli ya Serikali kwamba ni lini RPC wa Songwe atapatiwa nyumba nzuri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua changamoto ambayo inakabili makazi ya RPC kule Songwe hasa ukitilia maanani kwamba mkoa huu ni mpya, kwa hiyo utakumbana na changamoto mbalimbali na unahitaji muda mpaka kuweza kukaa sawa. Kwa kulitambua hilo basi, nikiamini kabisa kwamba tuna programu kabambe ya ujenzi wa nyumba za makazi kwa askari ambazo tumekuwa tukizizungumza hapa kila siku, tutaangalia huo uwezekano kufikia utaratibu huo ama utaratibu mwingine wowote ili tuweze kurekebisha hilo jambo, tunalifahamu na tutalifanyia kazi.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona, kwa kuwa tatizo la maji lililopo Urambo linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo la maji lililopo katika mji wangu mdogo wa Mlowo, na kwa vile katika Mji huo kuna mto uitwao Mto Mlowo.
Je, Serikali haioni umuhimu wa kuchimba mabwawa katika mto huo ili kuhakikisha kwamba wananchi wa mji mdogo wa Mlowo, hususani wanawake ambao Mheshimiwa Waziri amekiri kwamba ndio wachotamaji wakubwa wanaondokana na adha hiyo ya mji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ametuomba kwamba tuna Mto Mlowo na akinamama wanakwenda kuchota maji Mto Mlowo, sasa haoni kwamba kuna umuhimu wa kuchimba mabwawa?
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeshaagiza tayari kwamba Halmashauri zote zifanye utafiti na zilete mapendekezo ili Serikali iweze kutenga fedha kuhakikisha kwamba kila Halmashauri na tumeomba kwamba kila Halmashauri kila mwaka ihakikishe inachimba bwawa moja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Shonza naomba na wewe ni Diwani, tusaidiane kwenye vikao vyetu tuelekeze kwamba Wakurugenzi na wahandisi wa maji wa Halmashauri zetu wafanye utafiti ili tuweze kupata maeneo ya kuchimba mabwawa tuweze kuondoa hii kero ya maji.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri, lakini ni wazi kwamba kwa miaka mingi sana Serikali haijatoa kipaumbele kwa suala la nyumba za walimu. Kwa mfano, kwenye majibu ya Mheshimiwa Waziri amesema kwamba kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imepanga kujenga nyumba 1,818, ukiangalia nikitumia Mbozi kama case study ya Mkoa wa Songwe, kuna uhaba wa nyumba za walimu 1,432. Je, ni lini sasa Serikali italeta mpango kabambe wa kumaliza tatizo la nyumba za walimu hasa wa vijijini ili iwe kama motisha?
Swali la pili, Mheshimiwa Waziri ambacho nilitaka kufahamu kwamba je, ni lini madeni hayo ya walimu yataanza kulipwa kwa sababu ukisema kwamba yamepelekwa tu Hazina bado haileti tija kwa walimu wa Tanzania. Ninataka kujua kwamba ni lini rasmi madeni hayo yataanza kulipwa?
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, najua Mbunge anaguswa sana na sekta ya elimu na nikupongeze sana kwa sababu ukiwa kijana lazima uguswe na elimu.
Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi na mkakati wa Serikali nimezungumza pale awali. Kwa vile tumebaini changamoto ya nyumba za walimu ndiyo maana Serikali katika bajeti ya mwaka huu tunaoenda nao imetenga takribani shilingi bilioni 13, hii ni kwa ajili ya nyumba za walimu wa shule za msingi peke yake, lakini shilingi bilioni 11 kwa ajili ya shule za sekondari. Hata hivyo, commitment katika mpango mwingine wa MMES II, nimezungumza hapa karibuni nyumba zipatazo140 tumeshazikamilisha.
Mheshimiwa Spika, naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge katika ziara zangu katika Mikoa mbalimbali, miongoni mwa mambo ninayoyatilia kipaumbele sana ni kukagua ujenzi wa nyumba za walimu. Naomba niwapongeze Wabunge wote kwa ujumla wetu katika maeneo yetu nilipopita nimekuta ujenzi wa nyumba za walimu kwa kweli unaenda kwa kasi sana. Kwa vile katika commitment ya Serikali imeshatenga hizi fedha, naomba niwaambie fedha tunaendelea kuzipeleka katika Halmashauri zetu, lengo kubwa walimu waweze kupata mazingira salama ya kuweza kuishi.
Mheshimiwa Spika, katika suala zima la madai ya walimu, nimesema kwamba sasa hivi tumeshahakiki deni la shilingi bilioni 26.04 na haya ni madeni yasiyo ya mshahara. Maana yake Serikali haiwezi kulipa madeni lazima kwanza kuweza kuhakiki, ndiyo maana nimesema zoezi la uhakiki limeisha Oktoba, 2016. Sasa hivi ni mchakato ambao upo katika Wizara ya Fedha kwa utaratibu wa mwisho wa kuweza kulipa. Kwa hiyo, naomba tuwe na subira tu kwa sababu kigezo kikubwa ni kwamba ni lazima deni lihakikiwe na madeni haya yameshahakikiwa na naomba niwaambie walimu wa Tanzania kwamba wawe na subira kipindi siyo kirefu, Hazina kwa kadri inavyojipanga, madeni haya yanaweza kulipwa walimu mbalimbali ili mradi wapate haki zao.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuzingatia umuhimu wa magari ya zimamoto katika Mikoa yetu, lakini mikoa mingi mipya hususan Mkoa wa Songwe unakabiliwa na ukosefu wa magari ya zimamoto.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kupata kauli ya Serikali kwamba je, Serikali ina mpango gani wa kutuletea
magari ya zimamoto katika Mkoa mpya wa Songwe? Ahsante.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa
ufuatiliaji wake na siyo tu jambo la zimamoto, bali masuala mazima yanayohusu idara zilizopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ikiwemo Makao Makuu ya Polisi katika Mkoa mpya wa Songwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu Songwe ni moja ya mikoa mipya, lakini una bahati ya kuwa karibu na uwanja
wa ndege. Tutaupa kipaumbele kama Mkoa mpya lakini pia kama mahitaji ya Mji ambao upo karibu na Mji wa Tunduma ambao unakua kwa kasi, ambao mara nyingi sana Mheshimiwa Juliana Shonza amekuwa akitetea masuala ya maendeleo ya mkoa huo na miji hiyo.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniona. Kwa kuwa tatizo lililopo Manonga linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo lililopo katika Mkoa wa Songwe na kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya, lakini mpaka sasa Wilaya za Mbozi, Ileje, Momba pamoja na Songwe hazina vyuo vya ufundi. Je, ni lini Serikali itajenga vyuo vya ufundi katika wilaya hizo ili kuwasaidia vijana wa Mkoa wa Songwe kuweza kuondokana na tatizo la ukosefu wa ajira? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Ninavyofahamu ni kwamba Wilaya ya Songwe ni miongoni mwa maeneo ambayo yamo kwenye mpango, nafahamu kuna kiwanja kilishatengwa eneo la Makutano, kwa hiyo, muda ukifika tutafanya hiyo shughuli ya ujenzi.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu ya Waziri japokuwa niseme kwamba majibu haya hayaridhishi na wala hayajatosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la msingi nilitaka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi mpya ya akinamama katika Hospitali hii ya Wilaya ya Mbozi ukizingatia kwamba hospitali hii inahudumia wilaya mbili mpaka sasa. Hali halisi ilivyo pale kuna vitanda 25 tu vya akinamama vya kulala baada ya kujifungua lakini kwa siku wanawake wanaozalishwa katika hospitali hiyo ni wanawake 42 mpaka 50. Kwa hiyo, kukarabati hili jengo hakuwezi kusaidia. Kwa hiyo, swali langu la msingi nataka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya akinamama mpya na kubwa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, katika
swali langu la msingi pia nataka kujua kwamba Serikali ina mpango gani wa kujenga Hospitali ya Wilaya ya Momba?Hili jambo nimekuwa nikilipigia kelele sana katika Bunge hili kwamba mpaka sasa Wilaya ya Momba hawana Hospitali ya Wilaya. Hali hiyo inapelekea usumbufu sana kwa sababu mara nyingi wanalazimika kuja kutibiwa katika hospitali ya Mbozi ambayo pia nayo jengo lake ni dogo. Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Naibu Waziri aniambie ni lini sasa Serikali itajenga Hospitali ya Wilaya ya Momba? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba niwaambie Waheshimiwa Wabunge, haya yote yanatokana na needs za Wabunge wenyewe tunavyokaa katika vikao vyetu. Kwenye vikao vyetu ndipo ambapo tunaweka priority nini kifanyike. Eneo hili priority ya kwanza imeonekana ni lazima tutenge shilingi milioni 180 kwa ajili ya kufanya ukarabati huo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niseme mipango hii yote inaanzia kwetu sisi Wabunge katika maeneo yetu tunapofanya needs assessment au tunapopanga mipango yetu. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Juliana kwa jinsi anavyopigania haki za akinamama na watoto Serikali tutafanya kila liwezekanalo kuona jinsi gani tutafanya kwa sababu pale Vwawa sasa hivi ndiyo kama Makao Makuu. Licha ya ukarabati huu, lakini tutaangalia nini kingine kifanyike lengo kubwa ni akinamama na watoto hasa wanaozaliwa waweze kuwa katika mazingira salama.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Hospitali ya Momba, niliongea na Mkuu wa Mkoa wetu wa Songwe, Mama Chiku Gallawa wakati tunafanya mikakati ya ukarabati wa vituo vya afya 100, hili jambo aliweka kama priority na aka-identify kwamba Momba haina Hospitali ya Wilaya. Tulibadilishana mawazo tukaona lile eneo la awali ambalo limepangwa kuwa Makao Makuu ya Halmashauri ya Momba kile kituo cha afya cha pale tukiwekee miundombinu ya kutosha ili wananchi wa eneo lile waweze kupata huduma ya kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Juliana kwamba tutafanya kila liwezekanalo kuhusiana na hoja hii na kwamba katika Makao Makuu ya Momba tunaenda kufanya uwekezaji mkubwa sana ndani ya kipindi hiki hiki kabla ya mwezi wa saba. Kilio cha wananchi wa pale ni kwamba wanapata shida na Serikali tumesikia kilio hiki, tutaenda kufanya kazi kubwa na ya kutosha kuwasaidia akinamama na watoto wa maeneo yale. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kuniona. Tatizo lililopo Mfenesini linafanana kwa ukaribu kabisa na tatizo ambalo lipo katika Mkoa wa Songe na ukizingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na umekuwa na changamoto kubwa sana za kiuhalifu. Changamoto kubwa iliyopo ni suala la usafiri kwa Jeshi la Polisi hususan katika Wilaya mpya ya Songwe. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka magari katika Mkoa wa Songwe hususan katika Wilaya mpya ya Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, tunatambua Mikoa na Wilaya mpya nyingi zina changamoto sio tu za magari pamoja hata na vitendea kazi, ofisi na nyumba. Kwa hiyo, ni kipaumbele cha Wizara yetu kuona kwamba tunapopata vifaa na uwezo wa kuweza kuimarisha vitendea kazi katika maeneo hayo, tunaangalia mikoa hii ambayo ni mipya ukiwemo Mkoa wa Songwe.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Kampasi ya DIT iliyoko Myunga anayoizungumzia Mheshimiwa Naibu Waziri yalikuwa ni majengo ya TANROADS ambayo kwa sasa ni takribani mwaka mmoja umepita tangu Serikali ipeleke Walimu wanne, lakini hakuna maandalizi mengine yoyote yanayoendelea pale kuonyesha kwamba hicho chuo kitafunguliwa hivi karibuni. Kwenye jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri amesema kwamba hicho chuo kitafunguliwa hivi karibuni.
Mheshimiwa Naibu Waziri anatuhakikishia vipi wananchi wa Wilaya ya Momba pamoja na Mkoa wa Songwe kwa ujumla kwamba hicho chuo kitakuwa bora kwa sababu mpaka sasa maandalizi yake ya ufunguzi ni hafifu sana?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; katika Wilaya ya Ileje kuna chuo cha VETA ambacho kimejengwa kwa jitihada kubwa za Halmashauri pamoja na JICA, mpaka sasa chuo hicho hakijafunguliwa kwa sababu ya ukosefu wa vifaa. Je, Serikali sasa haioni kwamba kuna umuhimu wa kukiongezea nguvu chuo hicho ili kiweze kufunguliwa na hatimaye kiweze kutumika kama chuo cha VETA kwa Mkoa wa Songwe ukizingatia kwamba mpaka sasa Mkoa wa Songwe hakuna chuo cha VETA? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Chuo cha Myunga, kwanza nichukue nafasi hii kuwashukuru sana wenzetu TANRODS kwa kukubali kambi hiyo itumike kwa ajili ya kutoa mafunzo kupitia Chuo cha DIT. Kimsingi ni kweli kwamba ile kambi haikuandaliwa kama Chuo cha Ufundi, kwa hali hiyo ilibidi kuanza kufanya taratibu zinazostahili ikiwa ni pamoja na kuangalia ni course zipi zinaweza zikafanyika kwa kuanzia katika eneo lile. Vvilevile kupata mahitaji muhimu kama umeme, pamoja na miundombinu ambayo itakuwa sahihi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shughuli hiyo imekamilika lakini tumekwama hasa katika suala la umeme na tumeona tutaanza na umeme wa Solar mna generator lakini baadaye tunategemea kupitia umeme vijiji mahali hapa patakuwa pameshapata umeme na kuweza sasa kutoa mafunzo makubwa zaidi kwa mujibu wa fursa zinazotolewa katika kampasi za vyuo vyenye uwezo wa kutoa mafunzo kuanzia ya ufundi wa sanifu mpaka degree.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika swali la pili kuhusiana na Chuo cha Ileje. Suala hili limekuwa pia likifuatiliwa na Mheshimiwa Janeth Mbene na tulikuwa tumetoa maelekezo baada ya Mkuu wa Wilaya kuja ofisini kwetu. Tulilokuwa tunaliomba kwao ni wao kuongeza eneo lile ukubwa kidogo lakini wakati huo kutupa sisi hati baada ya kupitia mikutano yao ya Halmashauri za Wilaya na RCC ili sasa kuhamisha ile ardhi kuwa katika mikono ya VETA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo sisi tutaendelea na hayo tumeshayafanya maeneo mengi ikiwemo Busekelo. Kwa hiyo, ninachoomba tu kwamba wao wenyewe wajitahidi katika kuongeza jitihada katika hilo. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na jitihada kubwa za Serikali za kumaliza tatizo la maji katika Mji wa Tunduma, bado changamoto kubwa imebaki kuwa kukosekana kwa chanzo cha uhakika katika Mji wa Tunduma. Je, nini mkakati wa Serikali wa kutekeleza ahadi aliyotoa Mheshimiwa Rais wakati wa uchaguzi ya kuvuta maji kutoka chanzo cha uhakika kilichopo katika Mji wa Ileje? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, chanzo cha uhakika cha maji kwa Mji wa Tunduma kama alivyoongelea chanzo cha maji kutoka Ileje, feasibility study inaendelea kufanyika na mara itakapokamilika basi mradi ule utatengewa fedha kwa awamu na utekelezaji utaanza mara moja. Vile vile kwa nyongeza pale Tunduma nimeshafika na kuona namna gani bora ya kuweza kupatikana kwa maji kwa sababu miundombinu ya awali tayari ilikamilika Mheshimiwa Mbunge niseme tulishaweza kumpa maelekezo Meneja wa Maji Mkoa, RUWASA na yule Engineer ni Engineer ambaye tunamtegemea katika Wizara na anafanya kazi vizuri sana. Hivyo, nikuhakikishie shida ya maji katika Mji wa Tunduma inakwenda kuwa historia. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Kata 29 za Wilaya ya Mbozi, Kata tatu za Bara, Kilimpindi na Nyimbili bado hazijapelekewa umeme. Naomba kufahamu ni lini Serikali itapeleka umeme katika kata hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shonza kuhusu kupeleka umeme katika kata alizozitaja katika Jimbo la Mbozi. Katika Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Pili wa REA iliyoanza Machi tutahakikisha tunapeleka umeme maeneo yote ambayo yalikuwa hayajapata umeme. Hivyo na yeye atakuwa mmojawapo kati ya wale watakaopata umeme katika awamu hii.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kufahamu kwamba, ni lini barabara ya kutoka Mlowo kwenda Kamsamba ujenzi wake utaanza, ikizingatiwa kwamba, suala zima la upembuzi pamoja na usanifu limeshakamilika, lakini pia ni barabara ambayo ipo kwenye Ilani ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi na ni ahadi ya Mheshimiwa Rais ya Awamu ya Tano pamoja na Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipokuja kwenye kampeni. Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA – MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Spika, barabara hii naifahamu vizuri ni barabara ambayo inasimamiwa na TANROADS. Ni kutoka Mloo mpaka Kamsamba ambapo ni nyumbani kwetu kabisa ni kilometa 166.6 na miaka yote imekuwa ikihudumiwa na TANROADS. Bahati nzuri kwasababu Serikali ni moja na ndio maana iko katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ninaamini mimi na yeye tukishirikiana kwa pamoja ile barabara itajengwa kwa kiwango cha lami na ninajua Serikali imeipangia fedha kwa ajili ya ujenzi utakaoanza hivi karibuni. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Mamlaka ya Mji Mdogo wa Mloo wenye wakazi zaidi ya 70,000 unakabiliwa na changamoto kubwa sana ya maji. Naomba kufahamu nini mpango wa Serikali katika kuwatua ndoo wanawake wa Mji Mdogo wa Mloo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tayari imeendelea kutoa maelekezo na kutekeleza miradi maeneo ya Mloo mpaka Tunduma. Kote huko tunaendelea kuhakikisha maji yanakwenda kupatikana. Katika maeneo ambayo nimefanya ziara yangu ya awali kabisa ni Mloo pamoja na Tunduma. Tayari tumemsimamisha yule mtumishi ambaye hakuwa tayari kuendana na kasi ya sasa na tukamweka pale Meneja wa Mkoa wa RUWASA kwa sababu ni mtendaji mzuri. Pia tayari mkeka tumeshauandaa tunaenda kuongeza timu maeneo yale ya Mloo na Tunduma ili kuhakikisha maji yanakwenda kutoka.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, lakini vilevile kwa commitment ambayo ameitoa kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe. Nataka nitoe tu ushauri kwamba katika kutekeleza mkakati huo, wasisahau taasisi muhimu, hususan shule za boarding, kwa sababu katika Mkoa wa Songwe, shule nyingi sana za boarding zinakabiliwa na changamoto ya kutokuwepo kwa umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba niulize swali langu moja la nyongeza. Utakubaliana nami kwamba upatikanaji wa umeme wa uhakika ni aspect muhimu sana katika kukuza uchumi wa eneo husika; nasi wananchi wa Mkoa wa Songwe tunakabiliwa na changamoto kubwa sana ya kukatika katika kwa umeme mara kwa mara; na hii imekuwa ni changamoto kubwa hususan katika ile miji mikubwa ya kibiashara kwa maana ya Miji ya Mlowo, Tunduma kule kwa Mheshimiwa David Silinde na Vwawa:- (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nataka kujua kwamba je, Mheshimiwa Waziri atakuwa tayari kwenda ama kutuma wataalam wake katika Mkoa wa Songwe ili kuweza kubaini changamoto hiyo na kuipatia ufumbuzi? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi la Mheshimiwa Shonza. Kwanza, ni kweli zipo taasisi nyingi ambazo kimsingi zinahitaji kupatiwa umeme, hasa huu wa Programu ya REA; na tumeainisha taasisi zote zikiwemo shule za msingi, sekondari na vituo vya afya, na tumetoa maelekezo kwa wakandarasi kuzingatia kipaumbele cha kupeleka umeme kwenye taasisi za Umma kama kipaumbele. Kwa hiyo, naomba nitoe msisitizo kwa wakandarasi kuzingatia hilo. Pili, nawaomba Wakurugenzi na Wenyeviti wa Halmashauri kutenga fedha kidogo angalau kulipia kupelekea taasisi za Umma umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika swali la pili ambalo ni la uimara wa umeme katika Mkoa wa Songwe. Nampongeza sana Mheshimiwa Shonza na Wabunge wa Songwe kwa ujumla kwa kufuatilia masuala ya umeme katika mkoa wao. Ni kweli Mkoa wa Songwe unapata umeme kutoka Iyunga iliyoko Mbeya, na ni takribani kilometa 70 kutoka kwenye kituo cha kupoozea umeme.
Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua mbili madhubuti, na niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Songwe kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hatua ya kwanza, tumejenga njia ya kusafirisha umeme kwa dharura kwa kuepusha kukatika kwa umeme katika Mkoa mzima wa Songwe kwa kujenga laini ya kilometa 70 kutoka Iyunga mpaka Mlowo; na tumeanza hivyo toka Januari na mradi unakamilika Mei mwaka 2021. Tumetenga shilingi bilioni 2.4 ambazo ni fedha za ndani.
Mheshimiwa Spika, maeneo yatakayopelekewa umeme ni Mlowo, Tunduma, Vwawa yenyewe pamoja na Momba; na tutagawa laini specific kwa kazi hiyo. Kwa hiyo, kuazia mwezi Mei mwaka huu, maeneo ya Songwe yatapata umeme wa uhakika. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, maeneo mengi ya Mkoani Songwe ikiwepo Kata Maalum ya Mbangala ambayo ni Kata maalum kwa ajili ya uchimbaji wa madini ya dhahabu yanakabiriwa na changamoto kubwa sana ya mawasiliano. Nataka kufahamu nini mkakati wa Serikali katika kupeleka mawasiliano katika maeneo haya ya Wilaya nzima ya Songwe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote iko kwenye mchakato na katika hatua za awali kabisa katika kuhakikisha inafanyia tathmini Vijiji na Kata zote nchini ili kujiridhisha wapi tuna tatizo la mawasiliano ili tuhakikishe kwamba katika mwaka wa fedha ujao tuweze kuviingiza na kuhakikisha kwamba wananchi wote wanapata mawasiliano.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kituo cha polisi cha Itaka ambacho kinahudumia kata zaidi ya tano ikiwepo kata ya Nambizo pamoja na Halungu kinakabiliwa na changamoto kubwa sana kwanza jengo lake limechakaa, lakini pili hakuna pia vitendea kazi lakini kama haitoshi kituo kile cha polisi kina polisi wanne tu. Naomba kufahamu Serikali imejipanga vipi katika kukabiliana na hiyo changamoto? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Shonza kama ifuatavyo; Serikali tunafahamu na tunatambua changamoto iliyoko katika Jeshi la Polisi na tunafahamu kwamba bado kuna vituo vimechakaa, tunafahamu kwamba tuna changamoto ya vitendea kazi, lakini pia tunafahamu kwamba tuna baadhi ya upungufu wa watumishi katika Jeshi. Kikubwa nimwambie Mheshimiwa aendelee kutustahimilia kwa sababu hatua za kuhakikisha kwamba tunachanganua ama tunatatua hii changamoto ama hizi changamoto tumeshazianza zikiwemo za uajiri, za upatikanaji wa vitendea kazi na za kurekebisha majengo yaliyochakaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kubwa nimuombe tu Mheshimiwa aendelee kustahimili sisi kama Serikali kama Wizara tupo mbioni kuhakikisha kwamba watengenezea mazingira mazuri wananchi kwa ajili ya kupata huduma nzuri za ulinzi na usalama.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa nafasi. Sote tunafahamu kwamba ni adhma kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita kumaliza changamoto ya vifo vitokanavyo na uzazi. Pia tunafahamu kwamba kwenye mwaka huu wa fedha Serikali imetenga zaidi ya bilioni 1.5. Lengo ni kuhakikisha kwamba baadhi ya majengo katika Hospitali hii ya Tunduma yanakamilika. Hata hivyo changamoto kubwa ni kwamba mpaka sasa hivi hakuna jengo la wazazi. Kwa hiyo mimi nilitaka nitoe ombi kwa Serikali, kwamba iangalie sasa namna, kwamba kwenye mwaka huu wa fedha iharakishe kupeleka fedha hizo kwa haraka ili majengo hayo yatakapokamilika yasaidie pia kutoa huduma za uzazi kwa wanawake wa Mji wa Tunduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu; kwa kutambua jitihada kubwa ambazo zinafanywa na Mbunge wa Jimbo la Tunduma na Naibu Waziri Mheshimiwa David Silinde katika kuhakikisha kwamba hospitali hii inakamilika kwa wakati; nilitaka tu niweze kufahamu na wananchi wa Tunduma, Maporomoko, wa Muungano wa Kaloleni wanataka kumsikia Mbunge wao kwamba anasemaje, kwamba ni lini sasa Serikali itakamilisha ujenzi wa hii hospitali kwa maana ya majengo, vifaa Pamoja na watumishi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza kwa kazi nzuri sana anayoifanya kwa wanawake wa Mkoa wa Mkoa wa Songwe, hususan kwenye kupigania masuala yao ya afya, anafanya kazi nzuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hili swali nasema nina interest nalo kidogo kwa sababu ni jimbo langu, na bahati nzuri leo nalijibu mimi mwenyewe. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya mama yetu Samia Hassan Suluhu ina dhamira ya dhati kabisa ya kusaidia sekta ya afya nchini. Ndiyo maana katika bajeti ya mwaka wa fedha huu 2021/2022 katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma imetengewa bilioni 1.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nimhakikishie tu kama Mbunge wa Jimbo husika fedha hiyo itafika na tutahakikisha kwamba inajenga kama amabvyo imekusudiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili ni kwamba anauliza ni lini hospitali ile itakamilika. Ni kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais imeshatoa fedha awamu ya kwanza imepeleka bilioni nne ambazo zimeshajenga jengo la kwanza na ambalo linatumika sasa hivi. Awamu ya pili tunapeleka bilioni 1.5, kwa hiyo itakuwa imebaki bilioni kama nne ya mwisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaamini Serikali ya Awamu ya Sita ina dhamira ya dhati kwenye hilo na ile hospitali itapelekewa fedha zote, kwa sababu muda bado upo na itajengwa na itakamilika kama ambavyo imekusudiwa. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, jengo la Kituo cha Polisi katika Mji Mdogo wa Mlowo ambapo mpaka sasa hivi tayari kimeishawekewa alama ya X kwa sababu kimejengwa kwenye hifadhi ya barabara.
Nilikuwa naomba kufahamu nini mkakati wa Serikali wa kutujengea Kituo kipya cha Polisi pale Mlowo na ikizingatiwa kwamba tayari tunalo eneo ambalo limetengwa pale Forest maalum kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Polisi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shonza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli moja miongoni mwa changamoto ambazo tuko nazo ni kwamba vituo vingi vipo maeneo ya barabara na wakati Serikali inataka kutanua ama kupanua miundombinu ya barabara inabidi lazima kuna vituo vipitishwe doza kwa ajili ya kuvunjwa ili sasa barabara itengenezwe. Sasa nimwambie tu Mheshimiwa kwamba kwa kuwa eneo lipo, basi tutajitahidi tutenge fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma za ulinzi na usalama.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru pia.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kuwa kuna uhaba mkubwa sana wa Walimu wa Elimu Maalum nchini Tanzania na hasa katika Mkoa wangu wa Songwe; na sasa hivi Serikali ina-practice inclusive education kwa maana ya elimu jumuishi: -
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka iwe ni compulsory kwa kila Mwalimu ambaye anasomea masuala ya elimu, kusomea elimu maalum kwa ajili ya watoto wetu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Shonza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu katika majibu yangu ya msingi, amezungumzia suala la inclusive education na nimeeleza, katika kipindi kilichopita tumeweza kutoa mafunzo kwa Walimu wote wa Shule za Sekondari katika shule zile ambazo zinachukua wanafunzi hawa wenye uziwi. Katika mwaka huu tunatarajia mwezi Machi tutafanya mafunzo kwa Walimu wote wa shule za msingi zile ambazo zinachukua wanafunzi hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa vile lengo lake ni kuhakikisha kwamba mitaala yetu inakwenda kuboreshwa ili somo hili liwe compulsory, hili ni eneo ambalo tutakwenda kulifanyia kazi katika uboreshaji wa mitaala hii ili wakati tunapoandaa mitaala, masomo ya lugha ya alama na mbinu za kufundishia wanafunzi wenye uziwi yaweze kuingia kwenye mitaala yetu. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru. Kwa kuwa bado changamoto ni kubwa sana katika hospitali ya Wilaya ya Mbozi, na fedha ambazo tayari zimepelekwa hazijatosha kumaliza changamoto katika wodi ya wazazi. Nilikuwa nataka kufahamu, kwa nini sasa Serikali isifikirie kutuongezea fedha katika mwaka ujao wa fedha ili kuweza kumaliza changamoto zilizopo katika wodi ya wazazi likiwemo suala la upanuzi pamoja na ukarabati?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, wanawake wa Mkoa wa Songwe katika Wilaya za Mbozi, Ileje, Songwe pamoja na Momba tuko vizuri sana katika suala la kuijaza dunia. Kitakwimu, katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi wastani wa watoto 450 huzaliwa kwa mwezi. Kutokana na changamoto hiyo Hospitali hii ya Wilaya ya Mbozi iko katika Kata ya Vwawa, na kata hiyo mpaka sasa hivi ninapoongea hakuna kituo cha afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, kwa nini sasa Serikali isifikirie kutujengea kituo cha afya katika Kata ya Vwawa ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitambue mchango wa Mheshimiwa Mbunge kwa wanawake wa Mkoa wa Songwe; amekuwa akifanya kazi. Ndiyo maana kama unavyoona, katika swali lake la kwanza ambalo ameliuliza hapa, anasema Serikali ifikirie kuongeza fedha kwa ajili ya kusaidia ile wodi ya akina mama na watoto ya Hospitali ya Mbozi ambako yeye mwenyewe safari iliyopita kabla ya Bunge hili alikuwa hapo na ameahidi kulikarabati jengo hilo. Kwa hiyo nimpongeze kwa hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ambacho ninaweza nikakisema ni kwamba Serikali imepokea maoni ya Mheshimiwa Mbunge ambapo katika swali letu la msingi tumejibu kuwa katika mwaka unaofuata tutaweka milioni 50, lakini pia tutazingatia kwa kuangalia vyanzo vingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, kuhusu kujenga kituo cha afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi Kata ya Vwawa, na hili tumelipokea. Kwa sababu moja ya malengo la Mheshimiwa Rais ni kuhakikisha kwamba tunasogeza huduma kwa wananchi. Kwa hiyo, ombi lake nalo tumelipokea ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wanawake wa Mkoa wa Songwe na kazi nzuri ambayo wanaifanya ili kuhakikisha tunakisaidia Chama chetu Cha Mapinduzi pamoja na kuwasaidia wananchi ambao wana imani na Serikali yao. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kata ya Kalembo, Isongole pamoja na Malangali katika Wilaya ya Ileje ni miongoni mwa Kata ambazo hazina kituo cha afya. Naomba kufahamu, ni lini Serikali itajenga vituo vya afya katika Kata hizo? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Shonza, amekuwa mara kwa mara akiulizia kuhusiana na Kata hizi na amekuwa akiwasemea kwa dhati wananchi wa Mkoa wa Songwe. Nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha inakwenda kwa awamu na kimkakati kujenga vituo vya afya katika Kata ambazo amezitaja. Ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, kwa kuwa barabara ya Mlowo Kamsamba, ina umuhimu mkubwa sana wa kiuchumi kwa wananchi wa Wilaya ya Mbozi pamoja na Momba. Naomba kufahamu sasa, ni lini ujenzi wa kiwango cha lami utaanza katika barabara hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mlowo Kamsamba, imeshafanyiwa usanifu wa kina na Serikali inatafuta fedha ili barabara hiyo iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya na upo mpakani na kwenye jibu la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba magari yatapelekwa kwenye maeneo ambayo yanauhitaji mkubwa, Mkoa wa Songwe una uhitaji mkubwa wa magari ya Polisi.
Mheshimiwa Spika, naomba kufahamu nini ahadi ya Serikali katika kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto ya magari katika Mkoa wa Songwe? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimejibu katika swali la msingi kwamba magari yale yatakapokuja tutayapeleka katika Mikoa ambayo ina uhitaji zaidi na Mheshimiwa Mbunge amethibitisha kwamba Mkoa wa Songwe ni moja kati ya Mikoa ambayo ina mahitaji basi tutalizingatia hilo.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa na changamoto kubwa sana ya foleni pamoja na msongamano wa magari kuanzia eneo la Mpemba, Sogea mpaka unafika Custom Tunduma. Naomba kufahamu Serikali imejipangaje kutuondolea adha hiyo wananchi wa Mkoa wa Songwe kwa kutujengea barabara kutoka Mbozi, kwa maana ya pale Mlowo mpaka kufika Tunduma?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Songwe, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara aliyoitaja ni sehemu tu ya barabara ya Igawa, Mbeya hadi Tunduma, maeneo yote haya yameshafanyiwa usanifu na yale maeneo ya Miji, barabara hizi zitajengwa njia nne ili kupunguza msongamano wa katika maeneo ya Miji ikiwemo na hilo eneo la kuanzia Vwawa kwenda sehemu ambapo tutajenga mizani.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Nimekuwa nikiuliza swali hili mara kwa mara na nishukuru sana Serikali kwa sababu imetupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa chumba cha upasuaji kwa ajili ya wanawake. Swali la kwanza; kwa kuwa Kituo hiki cha Afya cha Itaka kinatumika kama Kituo cha Afya cha Tarafa, kutokana na kwamba kata zote zinaunda Tarafa ya Itaka hazina vituo vya afya. Naomba kufahamu sasa ni lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya ujenzi wa wodi za kawaida za watoto, wanaume pamoja na wanawake?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, mama yetu Mama Samia Suluhu Hassan alipokuja kwenye kampeni mwaka 2020 katika Kata ya Mlowo…
NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Shonza.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, sawa. Naomba kufahamu sasa, ni lini Serikali itatekeleza ahadi yake aliyoahidi Mheshimiwa Rais wa Awamu ya kutujengea kituo cha afya katika Kata ya Mlowo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba Mheshimiwa Shonza amekuwa akiulizia sana suala la Kituo cha Afya cha Itaka akishirikiana na Mheshimiwa Mbunge Mwenesongole, lakini nimhakikishie Serikali sikivu ya Awamu ya Sita, chini ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, imepeleka fedha hizo na kazi ya ujenzi wa jengo la upasuaji inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba Serikali inajenga vituo vya afya hivi kwa awamu, tumeanza majengo hayo ya awali, lakini fedha itatafutwa kwenda kujenga wodi ya wanawake, watoto na wanaume.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na ahadi ya Mheshimiwa Rais, kujenga Kituo cha Afya katika Kata ambayo Mheshimiwa Mbunge ameitaja, nimhakikisie kwamba ahadi za viongozi wetu ni kipaumbele. Kwa hiyo, Serikali tayari imeshaanza kufanya michakato ya kuhakikisha kwamba tunapata fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya. Ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, kwanza nishukuru sana kwa majibu ya Serikali; lakini naomba nitoe ombi moja, kwamba niombe waharikishe sana kuweza kupatikana kwa huyo mkandarasi ili kuweza kuwapunguzia adha ya maji wanawake wenzangu wa Mji wa Tunduma, Mji wa Vwawa pamoja na Mji wa Mlowo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nitakuwa na swali moja la nyongeza. Hali ya upatikanaji maji katika Wilaya ya Songwe ambayo ina kata 18 ikiwepo Kata ya Mkwajuni, Kata ya Saza pamoja na Galula sio ya kuridhisha, naomba nipate kauli ya Serikali kwamba ina mpango gani wa kuboresha hali ya upatikanaji maji katika Wilaya ya Songwe, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Shonza, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nipende kupokea pongezi zake, nawe nakupongeza kwa kuwa mfuatiliaji mzuri wa masuala ya maji ili kuhakikisha mwanamke anatuliwa ndoo kichwani.
Mheshimiwa Spika, kuharakisha kupata mkandarasi, hii ni moja ya jitihada tunayoifanya Wizara. Nikuombe Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana kuhakikisha tunakwenda sambamba na lengo la kumtoa mama ndoo kichwani linakamilika kwa wakati. Maeneo ya Wilaya ya Songwe, Mkwajuni na Kisasa, tayari Serikali inaendelea na jitihada mbali mbali kuhakikisha matatizo ya maji katika maeneo haya tunakwenda kuyafanyia kazi.
Mheshimiwa Spika, miezi michache iliyopita gari la uchimbaji visima lilikuwa kule Wilayani Songwe na liliweza kufanya kazi ya uchimbaji visima katika maeneo kadhaa. Kazi hii itaendelea, lengo ni kuona visima vile tunavipata, tupate vyanzo vya maji ili tuweze kusambaza maeneo yote ambayo bado yanaathirika na tatizo la maji. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Kwanza nianze kwa kuishukuru Serikali kwa sababu imetupatia fedha zaidi ya Shilingi Milioni 300 kwa ajili ya ujenzi wa wodi za upasuaji pamoja na wodi za akina mama katika kituo cha afya cha Itaka.
Je, Serikali sasa inatuhakikishieje kwamba ujenzi huu utakapokamilika watatupatia Daktari wa upasuaji ikizingatiwa kwamba mpaka sasa hatuna Daktari wa upasuaji lakini kituo kile cha afya cha Itaga kinahudumia Kata takribani Tano kwa maana ya Kata ya Harungu pamoja na Nambizo. Kwa hiyo nilitaka kufahamu commitment ya Serikali kwamba itatuletea lini Daktari wa upasuaji?
Mheshimiwa Spika, swali la pili mamlaka ya Mji mdogo wa Mlowo una wakazi takribani 100,000 lakini katika hali ya kusikitisha mpaka sasa hivi hatuna Kituo cha Afya pale na sasa hivi ninavyoongea tayari wananchi wamefyatua tofali zaidi ya 150,000 vilevile mamlaka ya Mji imetoa eneo heka kumi…
SPIKA: Mheshimiwa Juliana Shonza uliza swali.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, naomba kufahamu sasa ni lini Serikali itatuletea fedha kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya cha Mlowo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Daniel Sh onza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Shonza kwa namna ambavyo anawasemea wananchi wa Mkoa wa Songwe pia kwa namna ambavyo anaendelea kuwapa ushirikiano Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Songwe akiwepo Mheshimiwa Mwenisongole Mbunge wa Jimbo la Mbozi.
Mheshimiwa Spika, Serikali imepeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Itaka na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge baada ya jengo lile kukamilika tutapeleka Daktari ambaye atatoa huduma za upasuaji. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili kuhusiana na Kata ya Mlowo kuwa na wananchi wengi na haina kituo cha afya nina imani kwamba Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo aliwasilisha vipaumbele vya Kata Tatu za kimkakati nasi tutakwenda kufanya tathmini na kuona kama Mlowo iko katika orodha hiyo basi tutatafuta fedha ili tuweze kujenga kituo cha afya. Ahsante. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Barabara za Wilaya ya Ileje zinakabiliwa na changamoto kubwa sana ya kutopitika hasa wakati wa masika. Naomba kufahamu ni lini Serikali itaipatia fedha TARURA Wilaya ya Ileje ili kuwaondolea adha wananchi wa Wilaya ya Ileje? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, moja ya halmashauri ambazo zimeongezewa bajeti ili kuweza kukidhi matengenezo ya barabara za vijijini na mijini ni Halmashauri ya Wilaya ya Ileje. Hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, hiyo barabara ambayo ameitaja ni sehemu ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha na tutahakikisha kwamba tunaendelea kuitengeneza kwa awamu ili iweze kupitika vizuri. Ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi. Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa mipya na mpaka sasa hatuna stendi ya mkoa, tayari fedha zilishatengwa. Naomba kufahamu nini mkakati wa Serikali katika kutupatia hizo fedha bilioni 29 ili tuweze kujenga stendi ya mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Mkoa wa Songwe kwa sababu ni mpya hauna stendi ya mabasi ya mkoa na kama alivyosema Mbunge Serikali tayari imeshaweka mpango wa kujenga stendi ya mabasi ya Mkoa wa Songwe na imeshatenga fedha. Kwa hiyo nimhakikishie kwamba kazi iliyopo sasa tunatafuta fedha ili twende kujenga stendi ya kisasa ya Mkoa wa Songwe.
MHE. JULIANA D SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru; wananchi wa Kata ya Sanga katika Wilaya ya Mbozi wamejenga boma la kituo cha afya; je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo hicho? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Kata ya Sanga ambayo wananchi wamejenga boma kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya ni sehemu ya Kata nyingi kote nchini ambazo wananchi wamejenga, Serikali imeweka mpango mkakati, kwanza kukamilisha vituo vya afya ambavyo ujenzi wake umeanza lakini baada ya kukamilisha vituo hivyo tutakwenda awamu ya pili ya kuainisha maboma na kuanza kuyakamilisha na wakati huo tunatoa kipaumbele pia katika jengo hili la kituo cha afya cha Sanga, ahsante. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nishukuru majibu mazuri ya Serikali, lakini kwa kuwa kukosekana kwa hicho kivuko kumekuwa kunatokea ajali za mara kwa mara. Kwanza kwa wananchi vilevile kwa bajaji pamoja na magari. Sasa nilitaka nifahamu kwamba kwa nini Serikali isione kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuharakisha upatikanaji wa hizo fedha ili hicho kivuko kiweze kujengwa ili kuwapunguzia adha kubwa wanayopata wananchi wa Mji wa Tunduma; vilevile ikizingatiwa kwamba ilikuwa ni ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo analolisema na changamoto anayoisema mimi binafsi ninaifahamu na ni sehemu ambayo na mimi barabara hii naitumia sana. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwamba jitihada zimeshaanza kuchukuliwa kuweka hizo alama za kusaidia kupunguza ajali.
Mpango wa Serikali kwa sasa tayari wanafanya usanifu kuangalia namna ya kuweka kivuko cha chini badala ya kivuko cha juu kwa sababu tumekuja kuona kwamba mara nyingi vivuko vya juu havitumiki sana kuliko vivuko vya chini.
Kwa hiyo nimwakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali inatambua na iko tayari kuwalinda wananchi na kivuko hicho kitajengwa kama kilivyoahidiwa na Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Tano, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya kutujengea barabara ya Mlowo – Kamsamba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, babrabara ya Mlowo - Kamsamba naomba Mheshimiwa Mbunge avute subira ni barabara ambayo imepigiwa sana kelele katika Bunge hili, kwa hiyo tunategemea kwamba itakuwa kwenye mapendekezo kwa ajili ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Kata ya Kapele pamoja na Kata ya Mkomba katika Jimbo la Momba ni miongoni mwa kata ambazo zenye shida kubwa sana ya mawasiliano. Naomba kufahamu ni lini Serikali itapeleka mawasilino katika kata hizo? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, kata ambazo amezitaja Mheshimiwa Mbunge zipo katika vijiji 2,116 ambavyo tunasubiri Serikali ipate fedha ili tuweze kufikisha huduma ya mawasiliano katika maeneo hayo. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itatujengea soko pamoja na Stendi ya Mkoa wa Songwe? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, tunatambua kwamba Mkoa wa Songwe ni miongoni mwa mikoa mipya, hauna stendi lakini na soko na suala hili limekuwa likiulizwa mara kwa mara na Serikali imeendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi na soko katika Mkoa wa Songwe. Kwa hiyo, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ipo kazini na itatekeleza suala hilo, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa kuzingatia kwamba Mkoa wa Songwe ni mpya naomba kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kutujengea angalau kampasi moja tu ya chuo kikuu cha umma, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shonza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza katika majibu ya swali la msingi kwamba tunakwenda kujenga kampasi 14 katika mikoa kumi na nne nchini. Moja ya Mikoa ambayo tunaweza kujenga ni katika Mkoa wa Songwe ambapo Chuo chetu cha DIT ndicho ambacho kitakwenda kujengwa katika eneo hili la Songwe.
Mheshimiwa Spika, kwa ruhusa yako labda ningeweza kusema na mikoa mingine ambayo inaweza kujengewa ili Waheshimiwa Wabunge waweze kujua. Naanza na Mkoa wa Manyara Chuo chetu cha TIA kitakwenda kujenga tawi pale. Singida ni TIA, Kagera University of Dar es Salaam, Lindi University of Dar es Salaam, Ruvuma ni TIA, Shinyanga ni MAMCU, Simiyu ni IFM, Rukwa ni MUST, Tabora ni Julius Nyerere, Kigoma ni MUHAS, Zanzibar ni University of Dar es Salaam, Mwanza ni ARU, Tanga ni Mzumbe na Songwe ni DIT, nakushukuru.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Makao Makuu ya Mikoa mingi yamepewa Manispaa. Nataka kufahamu ni lini Serikali itatupatia Manispaa katika Mkoa wa Songwe kwa maana ya Vwawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Songwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali kama hili nililijibu siku ya jana, ambako nilisema Mbunge wa Jimbo la Vwawa, Mheshimiwa Japhet Hasunga. Nimhakikishie tu kwamba Mkoa wa Songwe ni moja kati ya Mikoa ambayo imeiomba kupewa hadhi ya kuwa na Manispaa, kinachofanyika sasa hivi ni kuhakikisha kwamba vile vigezo ambavyo vimewekwa vinapitiwa na wakishakidhi vile vigezo maana yake tutaishauri mamlaka iweze kama kuipatia ama yenyewe itaona vingenevyo. Kwa hiyo, huo ndiyo msimamo mpaka sasa wa Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.(Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itatujengea kituo cha afya katika Kata ya Vwawa ili kupunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mbozi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Mwenyekiti, Ahsante sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Songwe, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, awamu ya kwanza ilikuwa ni kuhakikisha kwamba Tarafa zote zinapata vituo vya afya, hilo eneo ambalo analianisha ndiyo Makao Makuu ya Mkoa ambako tunayo hospitali ya Mkoa ambayo tumeipandisha hadhi kutoka hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, baada ya kumaliza hizo process zote ambazo tunazo sasa hivi, maana yake ndiyo tutafuatia hiyo hatua ambayo Mheshimiwa Mbunge anaainisha, ahsante. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itatujengea Kituo cha Afya, katika Kata ya Bara ili kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto katika Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa mkakati, kwanza wa kukamilisha vituo vyote zahanati na hospitali za Halmashauri ambazo zimekamilika lakini hazijaanza kutoa huduma. Baada ya hapo tutakwenda sasa kujenga vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati likiwemo eneo hili ambalo Mheshimiwa Juliana Shonza amelisema.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tutakwenda kuhakikisha kwamba tunajenga pia kituo cha afya baada ya kukamilisha vituo vingine.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, kwa kuwa nimekuwa nikifuatilia mradi huu kwa muda mrefu sana na majibu ya Serikali yamebaki kuwa haya haya.
Sasa naomba kupata commitment ya Serikali inawahakikishiaje wanawake wa Mlowo, wanawake wa Vwawa na Tunduma kwamba ni kweli kwa mwaka wa fedha ujao watatuletea mradi huu wa kutoa maji Ileje na kuweza kuyasambaza kwenye maeneo hayo?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa Serikali imekiri kwamba hatuwezi kumaliza tatizo la maji kwa kujenga miradi midogo midogo; sasa naomba kufahamu tunaye mkandarasi ambaye anatatujengea miradi ya maji katika Kata ya Mkwajuni pamoja na Galula kule Songwe, lakini mpaka sasa hivi hajamaliziwa fedha na huo mradi umeanza mwaka 2019.
Je, ni lini sasa Serikali itammalizia fedha mkandarasi huyo ili kuweza kuwapunguzia adha ya maji wanawake wa Wilaya ya Songwe? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Shonza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, commitment ya Serikali ni kuhakikisha maji yanapatikana maeneo yote nchini na hili tumeona jitihada za dhati kabisa Mheshimiwa Rais ametoa fedha nyingi zaidi ya asilimia 95 mpaka sasa, mpaka tumalize mwaka huu wa fedha itakuwa zaidi ya hapo. Hivyo, Serikali tutafika maeneo yote na kuhakikisha miradi ambayo haikutekelezeka inakwenda kutekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na mkandarasi kulipwa Mkwajuni – Songwe wakandarasi wanaendelea kulipwa kulingana na walivyofanyakazi walivyo raise certificates na kuna sababu mbalimbali zinazopelekea hawa baadhi ya wakandarasi malipo yao kuchelewa hivyo niwatake wakandarasi wote wafanyekazi kadri ya mikataba nakwa ambaye hajalipwa basi aweze kufuata taratibu ili malipo yake yaweze kufanyika mara moja.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itatujengea Kituo cha Afya, katika Kata ya Bara ili kupunguza idadi ya vifo vya mama na mtoto katika Wilaya ya Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imeandaa mkakati, kwanza wa kukamilisha vituo vyote zahanati na hospitali za Halmashauri ambazo zimekamilika lakini hazijaanza kutoa huduma. Baada ya hapo tutakwenda sasa kujenga vituo vya afya kwenye maeneo ya kimkakati likiwemo eneo hili ambalo Mheshimiwa Juliana Shonza amelisema.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tutakwenda kuhakikisha kwamba tunajenga pia kituo cha afya baada ya kukamilisha vituo vingine.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; kwa kuwa Songwe ni Wilaya naomba kufahamu ni lini sasa Serikali itatujengea Kituo cha Polisi katika Kata ya Mkwajuni chenye hadhi ya Kiwilaya? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Songwe kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi kusema kwenye majibu yetu ya msingi ujenzi wa vituo vya polisi vya wilaya na mikoa utaendelea kadri tutakavyopata fedha, kipaumbele kwa mwaka ujao ni kujenga Makao Makuu ya Mikoa na baada ya hapo tutaingia kwenye wilaya zetu. Kwa hiyo, tutakapopata fedha tutajenga ndani ya Wilaya ya Songwe. Nashukuru. (Makofi)
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, naomba kufahamu ni lini Serikali itatuboreshea Kituo cha Afya cha Isasa kwa maana ya kutujengea wodi ya akina mama pamoja na wodi ya akina baba? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuainisha vituo vyote ambavyo vina majengo pungufu ili kuyajenga kwa awamu. Kwa hiyo, naomba nichukue hoja ya Mheshimiwa Juliana Shonza ili tuweze kuona majengo yapi yanapungua, gharama kiasi gani inahitajika ili tuanze kujenga majengo yanayopungua, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Naomba kufahamu ni lini Serikali itaanza Upembuzi yakinifu katika mradi wa maji katika Kijiji cha Lukululu uliopo katika Jimbo la Vwawa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Juliana Shonza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, upembezi yakinifu tunatarajia kuanza mwaka ujao wa fedha na kadri fedha itakapopatikana kasi itakuwa ni kubwa, lengo ni kuwafikia wananchi wote ili waweze kupata maji safi na salama bombani.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kuwa Hospitali yetu ya Wilaya ya Mbozi ni chakavu sana kama ambavyo Mheshimiwa Waziri alivyosema na hizi fedha ambazo zimetengwa kwa kweli ni kidogo. Sasa nataka nifahamu kwamba Serikali ina mpango gani au mkakati gani wa kudumu kuhakikisha kwamba majengo yote ya Hospitali ya Wilaya ya Mbozi yanakarabatiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama alivyosema Mheshimiwa Juliana Daniel Shonza kwamba Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi ni hospitali kongwe ni hospitali chakavu. Ndiyo maana kwa utashi na mapenzi mema ya Mheshimiwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameainisha hospitali hiyo miongoni mwa hospitali 19 nchini kote za kipaumbele kwa ajili ya kutenga fedha kuhakikisha majengo yanakarabatiwa na kuwa na hadhi ya hospitali ya halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Rais tayari ameshatenga shilingi milioni 900 katika bajeti ya mwaka huu na itapelekwa kwa ajili ya ukarabati. Tutaendelea kutenga fedha kwa awamu kuhakikisha majengo yote ya Hospitali ya Halmashauri ya Mbozi inakarabatiwa na kutoa huduma nzuri kwa wananchi wa Mbozi, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa tuko katika hatua za mwisho za kupata eneo jipya katika Kitongoji cha Ipanga, naomba kupata commitment ya Serikali endapo process hizo zitakamilika. Je, Serikali itakamilisha huo mchakato haraka kwa sababu wananchi wa Mbebe wanapata changamoto sana hasa kwenye masuala ya afya?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, tunacho Kituo cha Afya katika Kata ya Isansa lakini kwa muda mrefu sana hakina wodi za kulaza wagonjwa hususan wodi ya akina mama. Naomba kujua lini Serikali itatupatia wodi za akina mama katika Kituo cha Afya cha Kata ya Isansa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Kata ya Mbebe kwa kuanza kutafuta eneo lingine ambalo litatosheleza ujenzi wa kituo cha afya. Nimhakikishie Mheshimiwa Juliana Shonza kwamba Serikali hii sikivu ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan itatafuta fedha na kupeleka kwenye Kata ya Mbebe kwa ajili ya kuwaunga mkono wananchi kwenye ujenzi wa hicho kituo cha afya.
Mheshimiwa Spika, pili, kuhusiana na upungufu wa majengo katika Kituo cha Afya cha Isansa, naomba nimhakikishie kwamba Serikali ilishafanya tathmini kwa vituo vyote vya afya vyenye majengo pungufu ya yale yanayohitajika kwa ajili ya kutoa huduma za afya. Hivyo, tutahakikisha pia tunapeleka fedha katika Kituo cha Afya Isansa kujenga hilo jengo la wazazi na majengo mengine ili tuweze kutoa huduma nzuri zaidi kwa wananchi, ahsante.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba kufahamu, je, ni lini mradi wa kutoa maji katika Mto Momba na kuyasambaza katika Miji ya Tunduma, Vwawa pamoja na Mji wa Mlowo utaanza kutekelezwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, mradi wa kutoa maji kutoka Mto Momba tayari Serikali imeshaanza kuufanyia kazi. Namwomba tu Mheshimiwa Mbunge aendelee kushirikiana nasi ili tukamilishe hatua ambazo tuko nazo na baada ya hapo tutakwenda kuukamilisha mradi huo. Ahsante sana.
MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Spika, naomba kufahamu ni lini Serikali itajenga Kituo cha Afya kwenye Kata ya Mkomba katika Tarafa ya Kamsamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Juliana Shonza, amefuatilia sana kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hilo kuhusiana na kituo hiki cha afya. Tumemwahidi na tumekiingiza kwenye orodha ya vituo vya afya vya kimkakati. Kwa hiyo, naomba tu nimhakikishie kwamba tayari Serikali inatambua na inaweka mipango yake kwa ajili ya kwenda kutekeleza ujenzi wa kituo hicho cha afya, ahsante.