Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Leah Jeremiah Komanya (37 total)

MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Ujenzi wa bwawa la Mwanjoro lililopo Wilaya ya Meatu ulianza mwaka 2009 lakini hadi sasa ujenzi wa bwawa hilo haujakamilika:-
(a) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa bwawa hilo ili liweze kutumika kwa ajili ya wananchi na mifugo katika Vijiji vya Jinamo, Mwanjoro, Itaba, Nkoma na Paji?
(b) Je, ni lini Serikali italeta fedha za miradi ya aina hii kwenye Halmashauri ili Halmashauri ziweze kutafuta Mkandarasi kufanya usimamizi na ufuatiliaji wa karibu na hatimaye kuondoa usumbufu kwa wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bwawa la Mwanjoro ulisimama baada ya Mkandarasi kuondoka eneo la mradi bila ridhaa ya mtaalam mshauri wala mwajiri. Hadi wakati shughuli za ujenzi zinasimama utekelezaji ulikuwa umefikia asilimia 78. Serikali itafanya tathmini ya bwawa hilo mwezi Mei, 2016, baada ya mvua zinazonyesha hivi sasa kupungua ili kujua ubora wa tuta lililojengwa, viwango vya kazi zilizobaki, kazi zinazohitajika kuboreshwa, kuandaa michoro ya kuendeleza ujenzi na kuandaa kabrasha la zabuni kwa ajili ya kutafuta Mkandarasi mwingine. Kazi ya ujenzi inatarajiwa kufanyika mwaka wa fedha 2016/2017
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuondoa usumbufu wa huduma ya maji kwa wananchi, Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuainisha maeneo ya kujenga mabwawa na kutenga bajeti ya ujenzi wa bwawa angalau moja kila mwaka. Aidha, Serikali itaendelea kutuma fedha kwenye Halmashauri kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. MASHIMBA M. NDAKI (K. n. y. MHE. LEAH J. KOMANYA) aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu hauna Chuo cha Ufundi (VETA) na kuwa vijana wengi waliohitimu elimu ya msingi na sekondari:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kujenga chuo cha ufundi ili vijana hao waweze kupata elimu ya ufundi na kuweza kujiajiri?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ya Mkoa wa Simiyu tayari imeshatenga eneo kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Simiyu, katika bajeti ambayo Waheshimiwa Wabunge waliipitisha ya Wizara yangu, kiasi cha fedha cha shilingi 4,045,000,000 kimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya ujenzi huo. Maandalizi ya awali ikiwemo kumpata mshauri elekezi, uandaaji wa michoro pamoja na makadirio ya ujenzi yaani Bills of Quantities (BOQ) na kumpata Mkandarasi yanatarajiwa kukamilika ifikapo Novemba, 2016 na ujenzi unatarajiwa kuanza rasmi mwezi Januari, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la ujenzi wa Chuo cha VETA cha Mkoa wa Simiyu ni kutoa mafunzo ya ufundi stadi na huduma kwa vijana wanaohitimu elimu ya msingi na sekondari katika Wilaya zote za Mkoa wa Simiyu ili waweze kupata elimu ya ufundi na hivyo kuwawezesha kujiajiri.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Jeshi la Polisi nchini linafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda usalama wa raia na mali zao, lakini linakabiliwa na upungufu mkubwa wa makazi kwa Askari wake:-
(a) Je, Serikali imepanga kujenga majengo mangapi katika Wilaya Mpya ya Itimila na Busega kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuyakamilisha makazi ya Askari Polisi yaliyomo Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa Mwaka huu wa Fedha 2016/2017, Wilaya Mpya za Itilima na Busega hazikutengewa fedha za ujenzi. Hata hivyo, kwa kuwa Wilaya ya Itilima na Busega ni mpya hivyo kuwa na mahitaji makubwa. Katika mradi wa nyumba 4,136 unaotarajiwa kuanza punde taratibu za mkopo wa ujenzi wa nyumba hizi utakapokamilika kipaumbele ni kwa mikoa mipya ukiwemo Mkoa wa Simiyu wenye Wilaya za Itilima na Busega.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni nia ya Serikali kukamilisha miradi yote ya Makazi ya Askari nchi nzima ambayo ujenzi wake umesimama kutokana na
ukosefu wa fedha. Azma hii nzuri itategemea upatikanaji wa Fedha za Maendeleo katika Bajeti ya Jeshi la Polisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Wizara itaendelea na juhudi mbadala zikiwemo kuhamasisha Waheshimiwa Wabunge, wananchi na wadau mbalimbali wa maendeleo kuchangia na kushiriki katika kusaidia juhudi za Serikali za kupunguza tatizo kubwa la makazi ya Askari nchini pamoja na ofisi.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Kumekuwa na mauaji ya Watanzania wenye ulemavu wa ngozi kwa muda mrefu sasa ambapo hali hiyo imesababisha wananchi wasamaria wema kuanzisha makazi maalum kwa ajili ya kuwahifadhi.
Je, Serikali inashiriki vipi katika kutoa huduma muhimu ikiwemo kuhakikisha wanapata elimu, matibabu pamoja na lotion?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha takriban miaka kumi, kumekuwa na matukio ya vitendo vya kikatili dhidi ya watu wenye ualbino ambavyo vimesababisha baadhi ya wasamaria wema kuanzisha makazi maalum ya kuwahifadhi watu wenye ualbino. Licha ya matukio hayo kupungua, bado kuna makazi yanayotumika kuwatunza watu wenye ualbino kwa sababu mbalimbali zikiwemo sababu za unyanyapaa na taarifa za baadhi ya matukio ya mashambulio japo si mara kwa mara kama ilivyokuwa katika miaka iliyopita. Makazi hayo yanajumuisha yale yaliyoanzishwa na Serikali na yale yaliyoanzishwa na wasamaria wema.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika makazi haya, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali inawajibika kuhakikisha kuwa watoto wenye ualbino wanapata elimu katika mazingira salama na kadri inavyowezekana kwa kuzingatia hali halisi Serikali itahakikisha watoto hawa wanapata elimu katika mazingira shirikishi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa matibabu na mafuta maalum ya ngozi, Serikali kwa kushirikiana na Taasisi za Tiba za Ocean Road, KCMC, Bugando na wadau wengine imekuwa ikitoa matibabu na mafuta maalum ya kuzuia athari za mionzi ya jua katika ngozi, yaani sun screen lotion, kwa watu wenye ualbino. Aidha, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Madawa (MSD) imeandaa mkakati wa kusambaza mafuta maalum katika hospitali zote za Wilaya ili kuwasaidia watu wenye ualbino ambapo mafuta hayo yameingizwa katika kundi la dawa kwa lengo la kurahisisha upatikanaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile Serikali ikishirikiana na wadau wengine imeandaa utaratibu wa kuwapima macho na ngozi watu wenye ualbino na kuwapatia tiba pamoja na ushauri ili wasiathirike.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaamini kuwa suluhisho la kudumu la kuondoa vitendo vya ukatili na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ualbino nchini ni kutoa elimu ili kubadili fikra potofu kwa jamiii kuliko kunzisha makazi na vituo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hii, Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana mamlaka ya Serikali za Mitaa na wadau wengine imeanzisha kampeni ya kupinga unyanyapaa na ukatili dhidi ya watu wenye ualbino kwa lengo la kutoa uelewa na kutokomeza imani potofu iliyojengeka miongoni mwa jamii kuhusu watu wenye ualbino.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali imeweka kipaumbele kwenye sekta ya kilimo na kuainisha kwamba mazao ya kilimo yatakuwa moja ya malighafi kwenye viwanda nchini:-
(a) Je, Serikali imeweka mkazo gani kwenye vyanzo vya kilimo ambavyo ndivyo vitakuwa malighafi na kusababisha uzalishaji ukue?
(b) Je, Serikali ina mkakati gani juu ya uhakika wa wakulima wengi zaidi kuingia kwenye kilimo cha umwagiliaji?
(c) Je, Serikali imewekeza kwa kiasi gani kwenye zana za kilimo za kisasa kwa wakulima wadogo na hasa wanawake waishio vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mchango wa Serikali kwenye sekta ya kilimo ni pamoja na:-
(i) Kutoa ruzuku ya pembejeo za kilimo kwa wakulima ili kuongeza uzalishaji na tija.
(ii) Kutoa elimu ya kilimo bora kwa kutumia mashamba darasa 16,786 na mashamba darasa 44 ya vijana yaliyoanzishwa.
(iii) Kutumia Vituo vya Rasilimali vya Kata 587.
(iv) Kuanzishwa kwa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ili kuimarisha soko la mazao ya kilimo.
(v) Kukarabati maghala ya kuhifadhia mazao katika Halmashauri ambapo hadi sasa maghala 33 yamekamilika na maghala haya yatanufaisha wakulima wadogo 13,800 kwa kuhifadhi mazao yao.
(b) Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ili wakulima wengi zaidi waingie kwenye kilimo cha umwagiliaji. Mikakati ya muda mfupi ni pamoja na:-
(i) Kukarabati na kuziboresha skimu za umwagiliaji 37 zenye ukubwa wa hekta 28,612.
(ii) Kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya umwagiliaji kwa njia ya matone.
(iii) Kuanzisha na kuimarisha vyama vya wamwagiliaji 442 katika skimu za wakulima wadogo.
(c) Mheshimiwa Spika, Serikali imetekeleza mikakati mbalimbali kwenye zana za kilimo kwa wakulima wadogo na hasa wanawake waishio vijijini ili kuwarahisishia kazi shambani. Kwa mfano, hadi sasa kuna matrekta makubwa 10,283 na matrekta madogo ya mkono 7,350.
Wizara kupitia Mradi wa Sera na Maendeleo ya Rasilimali Watu (Policy and Human Resource Development) imesambaza mashine za kuvuna mpunga 64, kukata mpunga 16 na mashine za kukoboa mpunga 14 katika skimu 14 za umwagiliaji. Mashine hizo zilizosambazwa zitasaidia kuongeza tija na kurahisisha kazi mashambani hususani kwa wanawake.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali hutumia gharama kubwa katika utafiti wa maji na ujenzi wa miundombinu ya maji, lakini baadhi ya miradi inayokabidhiwa kwa mamlaka za maji za mji na jumuiya ya watumia maji (COWUSA) zinasuasua na kutonufaisha jamii kama ilivyokusudiwa:-
Je Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha miradi ya maji inanufaisha jamii kama iliyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiaha Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji mijini na vijijini. Katika kuhakikisha miradi hiyo inanufaisha jamii kama ilivyokusudiwa Wizara imeandaa na inatekeleza uundaji, usajili wa vyombo vya watumia maji na kuvijengea uwezo kwa ajili ya uendeshaji na usimamizi. Katika kuhakikisha mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira zinatoa huduma endelevu mamlaka hizo zinasimamiwa na bodi ambazo zinajumuisha wadau mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na utekelezaji huo kumekuwa na changamoto mbalimbali katika miradi hiyo ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya maji, wizi wa vifaa vya maji pamoja na watumiaji maji kutolipia huduma hiyo zikiwemo taasisi za Serikali. Hali hiyo ya baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa madeni yao kumepelekea mamlaka nyingi kushindwa kugharamia matengenezo ya miundombinu ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na wizi wa maji pamoja na uchakavu wa miundombinu Wizara inaendelea kurekebisha Sheria za Maji ili ziweze kutoa adhabu kali kwa wezi wa maji na wahujumu wa miundombinu ya maji. Vilevile mamlaka za maji na usafi wa mazingira mijini zinaendelea kukarabati miundombinu ya maji iliyochakaa, kufunga dira za maji kwa wateja wote ili kubaini matumizi yao halisi na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji. Aidha, Wizara imeanza kuchukua hatua za kutumia nishati ya jua kwenye mitambo ya maji hususani vijijini kwa ajili ya kupunguza gharama za uendeshaji.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Kutokana na msongamano mkubwa wa wagonjwa wa saratani katika Hospitali ya Ocean Road pamoja na gharama kwa ndugu wa wagonjwa ya kuwaleta na kuwauguza ndugu zao.
Je, Serikali haioni haja ya kuanza kutoa huduma hiyo katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII (K.n.y WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza leo nasimama hapa toka niteuliwe na Mheshimiwa Rais, naomba na mimi nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuniamini na kunipa majukumu zaidi kwenye Serikali yake, pia niwashukuru wananchi wa Jimbo la Nzega Vijijini, Wilaya ya Nzega na Mkoa wetu wa Tabora kwa ujumla kwa ushirikiano ambao wameendelea kunipa. Napenda kusema tu kwa wote kwamba kwa hakika sitowaangusha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wagonjwa wenye Saratani ili kusogeza huduma hizi karibu zaidi na wananchi na kupunguza msongamano katika Hospitali ya Ocean Road, pia kupunguza gharama kwa wagonjwa na ndugu. Kwa sasa Serikali inakamilisha maandalizi ya kuanzisha matibabu ya saratani kwa mionzi katika Hospitali ya Bugando ambapo baadhi ya majengo kwa ajili ya huduma husika yamekamilika, yakiwemo jengo maalum ambalo ni kwa ajili ya kudhibiti mionzi, ambapo ukuta wake umejengwa kwa zege nene la mita moja (bunkers), jengo la kutolea huduma za mionzi, baadhi ya wataalam wapo na baadhi ya mashine za matibabu kwa mionzi zimeshanunuliwa zikiwemo Cobalt 60 na CT Simulator.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha brachytherapy na immobilization devices zinatarajiwa kuwasili mwezi Disemba, 2017. Kwa sasa huduma za tiba ya saratani zinazopatikana Bungando ni zile za matibabu yasiyo ya mionzi (chemotherapy) na zilianza mwezi Januari mwaka 2009, kufuatia sera ya Serikali ya kutoa huduma hizo kikanda. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa kipindi cha mwaka 2009 - 2017 hospitali imetoa matibabu kwa wagonjwa 39,300 kati yao 12,200 wakiwa ni wapya, sawa na wastani wa waginjwa 1,500 kwa mwaka.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Mkoa wa Simiyu ambao ni mkoa mpya hauna Hospitali ya Rufaa, hivyo wagonjwa wanalazimika kusafiri umbali wa zaidi ya kilometa 140 kufuata huduma hiyo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Shinyanga na Mwanza; mwaka 2015/2016 Mkoa wa Simiyu ulipokea fedha kidogo ya kuanzisha jengo la OPD.
• Je, Serikali itaendelea kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa?
• Je, ni lini Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kwa kukukaribisha tena katika Bunge letu tukufu. Tumefurahi sana kukuona. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, awali ya yote, Wizara inapenda kumshukuru sana Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kwa kutambua jitihada ambazo Serikali imefanya katika kuendeleza mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu, ukiwa ni mmoja wa mikoa mipya ulioanzishwa mwaka 2012. Kutokana na uhitaji wa huduma za afya ngazi ya rufaa katika ngazi ya mkoa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Simiyu iliandaa na kupeleka andiko Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Mkoa kwa kuzingatia mahitaji ya kitabibu kwa ajili ya kuingizwa kwenye bajeti.
Mheshimiwa Spika, niongeze hapa tu kwamba, pamoja na andiko hili hospitali hii sasa kwa agizo la Mheshimiwa Rais, zimeletwa tena katika Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa nyakati tofauti imekuwa ikitoa fedha na hadi sasa jumla ya shilingi 2,087,268,672 zimeshatolewa. Kati ya fedha hizo, shilingi 299,896,185 zilitumika kununua ardhi yenye ukubwa wa ekari
(a) Shilingi milioni 595,650,815 zilitumika katika ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na utawala katika awamu ya kwanza na shilingi 1,191,721,672 zilitumika kuendeleza ujenzi wa jengo la OPD katika awamu ya pili.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali imetenga fedha zaidi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za tiba katika Hospitali za Rufaa za mikoa ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Simiyu. Hii inaenda sambamba vilevile na kupatiwa ahadi ya fedha ya shilingi bilioni 10 ambayo zilitolewa na Mheshimiwa Rais alipotembelea Mkoa wa Simiyu tarehe 11 Januari, 2017.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali hupeleka katika Halmashauri zilizopo katika Hifadhi ya Wanyamapori asilimia 25 ya fedha zitokanazo na mapato ya uwindaji wa kitalii na upigaji picha pasipo Halmashauri husika kujua msingi wa tozo hizo.
• Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki zake?
• Je, ni kiasi gani cha mapato kimepatikana kutokana na Maswa Game Reserve na Hifadhi ya Makao na kiasi gani kilipelekwa katika Wilaya ya Meatu kila mwaka kuanzia mwaka 2015 hadi 2017?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa mgao wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada za wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya Wilaya husika. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 Wilaya ya Meatu ilipata mgao wa shilingi 40,017,158 na shilingi 41,696,616.43 sawia ikiwa ni asilimia 25 ya mapato yatokanayo na wanyamapori waliowindwa katika vitalu vya Mbono na Kimali katika Pori la Akiba la Maswa na Makao WMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha katika vitalu vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na kutolewa taarifa mbalimbali. Aidha, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama MNRT Portal ambapo taarifa zinazohusu Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana humo. Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 1 Julai, 2018. Aidha, nakala ngumu zitatumwa kwenda Wilaya husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa Halmashauri nchini zinazopata mgao huu kutumia asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali kama ilivyokubalika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Pamoja na nia nzuri ya Serikali kudhibiti ulimbikizaji wa madeni lakini kumekuwa na changamoto katika utekelezaji wa shughuli za kila siku katika Idara za Halmashauri za Wilaya zinazopokea ruzuku ya matumizi ya kawaida toka Serikalini:-
Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka fedha za ruzuku katika Halmashauri za Wilaya kama zilivyopitishwa na Bunge?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kulifahamisha Bunge lako Tukufu kwamba, bajeti ni makadirio ya mapato na matumizi. Kinachoidhinishwa na Bunge lako Tukufu ni makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka husika. Pili, utekelezaji wa bajeti ya Serikali kwa sasa unafanyika kwa mfumo wa cash budget. Hivyo basi, ruzuku kutoka Serikali Kuu hupelekwa kwenye Halmashauri za Wilaya kulingana na makusanyo halisi ya mapato ya mwezi husika. Serikali yetu kwa mtindo huo itaendelea kupeleka fedha za ruzuku kwenye Halmashauri zetu kutokana na makusanyo halisi kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Moja ya mkakati wa EQUIP – Tanzania ni kuinua ubora wa elimu inayotolewa kwa watoto wa kike ili waweze kuhitimu Shule ya Msingi na kuendelea na Sekondari, lakini mtoto wa kike ana vikwazo vinavyoweza kukatiza ndoto hii:-

(a) Je, mpango huu umejikita vipi katika kutokomeza mimba na ndoto za utotoni, udhalilishaji kingono, ukeketaji na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto?

(b) Je, ni upi usaidizi wa mpango wa wanafunzi walio katika hatari zaidi kwa makundi kama vile waliotelekezwa, walio katika umasikini wa kupindukia, yatima na walionusurika kutokana na unyanyasaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutokomeza mimba na ndoa za utotoni, udhalilishaji kongono na ukeketaji, Serikali kupitia programu ya EQIP Tanzania imeanzisha clubs za wanafunzi ziitwazo Jiamini Uwezo Unao (JUU) kwenye Shule za Msingi 4,476. Malengo ya clubs hizo ni kuwajengea wanafunzi hasa wa kike uwezo wa kujiamini, kujieleza na kujitambua. Kupitia clubs hizo, wanafunzi wanajifunza masuala mbalimbali ikiwemo hedhi salama na athari za kupata mimba katika umri mdogo.

Aidha, ili kuboresha mazingira ya watoto wa kike, mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kwa kupitia programu hii ilitoa ruzuku ya jumla ya shilingi bilioni 2.46 kwenye shule 4,476 ambazo kila shule ilipewa shilingi 550,000/=. Kupitia ruzuku hiyo, elimu ilitolewa kwa wanafunzi wa kike na wazazi kupitia ushirikiano wa Wazazi na Waalimu (UWAWA), kuhusu namna ya kutengeneza taulo salama za kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali kupitia programu ya EQUIP Tanzania imetenga jumla ya shilingi bilioni 2.3 kwa ajili ya kutoa elimu na kuhamasisha jamii wakiwemo wanafunzi, wazazi na Walimu kupiga vita vitendo vya ukatili kwa watoto na kujenga mazingira rafiki ya kujifunzia kwa makundi maalum wakiwemo watoto wa kike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia programu ya EQUIP Tanzania, Serikali imeongeza fursa ya kujifunza kwa watoto wa kike sawa na wa kiume na kuwakinga na masuala ya adhabu zenye kudhuru mwili na akili za watoto. Jumla ya shilingi bilioni 6.8 zimetumika kuwajengea uwezo Walimu 50,446 kuhusu mbinu bora za ufundishaji na ujifunzaji ikiwemo matumizi ya mbinu zinazojali jinsia na ujenzi wa mazingira rafiki na salama ya kujifunzia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati huo umeboresha mbinu rafiki na zinazozingatia jinsia katika ufundishaji na ujifunzaji kutoka asilimia 54 mwaka 2014 hadi aslimia 65 mwaka 2016 katika shule zilizo katika Mikoa iliyotekeleza programu hiyo ya EQUIP Tanzania. Tathimini inaonesha kuwa wasichana waliopata wastani wa juu katika kumudu stadi za kusoma na kuandika, walifikia asilimia 26.7 ikilinganishwa na wavulana asilimia 18 katika kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Moja kati ya vigezo vya “Capital Development Grant Assessment”ni namna Halmashauri inavyoweza kutoa taarifa kwa wananchi juu ya mtiririko wa fedha ambazo Serikali imepeleka katika Halmashauri na miradi iliyokusudiwa kutekelezwa:-

(a) Je, kwa nini mchakato huo ulisitishwa?

(b) Je, Serikali haioni umuhimu wa kurejesha mchakato huo ambao utakuwa ukiongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa mwenyekiti, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa wa viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upimaji wa Halmashauri ulikuwa ni kigezo cha kuziwezesha Halmashauri kupata ruzuku ya maendeleo isiyo na masharti (Local Government Development Grant) kuanzia mwaka 2005. Miongoni mwa vigezo vilivyozingatiwa ni kuwepo kwa uwazi katika mapokezi na matumizi ya fedha kwenye ngazi ya Vijiji, Kata na Mitaa kwa kuhakikisha mapato na matumizi yanabandikwa kwenye mbao za matangazo. Mradi huo ulitekelezwa kupitia fedha za wafadhili ambapo Serikali pia ilikuwa na mchango katika fedha hizo. Mradi huo ulifikia ukomo mwaka 2013, baada ya wafadhali kujitoa na Serikali kuendelea kutekeleza mradi huo kuanzia mwaka 2014/2015 na 2017/2018.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kutoa ruzuku ya maendeleo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuziwezesha kutekeleza miradi ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwemo afya na elimu. Wananchi wanachangia nguvu kazi na vifaa mbalimbali kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hiyo. Serikali inakubaliana na wazo la kuzipima Halmashauri katika matumizi ya ruzuku hiyo inayotolewa na Serikali kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hilo liko kwenye mjadala ndani ya Serikali ili kuona namna bora ya kulitekeleza katika kuhakikisha kunakuwa na uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha zinazotolewa na Serikali kwenye Halmashauri hadi ngazi ya vijiji.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni vigezo vipi vinatumika kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. HUSSEIN M. BASHE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kumjibu Mheshimiwa Leah Komanya swali lake, kama ifuatavyo:-

Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika anapaswa kuwa na sifa kuu mbili ambazo ni kuwa mwanachama wa Chama cha Ushirika; na awe na sifa ya kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushirika. Aidha, sifa nyingine ni sawa na zile za utaratibu wa uteuzi wa Wajumbe wa Bodi ya Ushirika ambazo zimeelezwa katika Kanuni za Maadili, kifungu 134(3) na Jedwali la Pili la Sheria ya Vyama vya Ushirika Na.6 ya mwaka 2013.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, pamoja na maelezo hayo, Wizara imebaini upo upungufu katika sheria kuhusu taratibu na sifa za kumpata Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika. Wizara inakamilisha mabadiliko ya Sheria ya Ushirika ili pamoja na mambo mengine kuiboresha na kupata viongozi bora. Mabadiliko hayo yatazingatia kuweka mfumo wa kupata viongozi wenye uaminifu na uadilifu, uwezo wa usimamizi, kiwango cha elimu na teknolojia. Aidha, sheria iliyopo ilikidhi mahitaji na mazingira ya wakati huo ambayo inafanyiwa maboresho ili kuendana na mazingira ya sasa. Mwanachama wa Chama cha Ushirika hatapaswa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushirika endapo atakuwa na mgongano wa maslahi na Chama cha Ushirika katika kufanya shughuli za biashara zinazofanywa na Chama cha Ushirika husika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 kinatekelezwa ipasavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WENYE ULEMAVU (MHE. STELLA A. IKUPA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremia Komanya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kifungu hiki kinahusu utoaji wa nafasi ya ajira kwa watu wenye ulemavu waliokidhi vigezo vya msingi vya nafasi zilizo wazi. Sharti hili la sheria ni kwa waajiri wote yaani Serikali na waajiri binafsi. Sharti hili la sheria ni kwa sababu Serikali inatambua kwamba kazi ni muhimu katika maendeleo ya watu wenye ulemavu inayowawezesha kujitegemea na kuondokana na hali ya kuombaomba. Pia inaleta heshima na hali ya kujiamini katika maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya Serikali ya kuhakikisha kifungu hiki kinatekelezwa ipasavyo ni kama ifuatvyo:-

i. Serikali imeanzisha kanzidata ya wahitimu wenye ulemavu wenye fani mbalimbali ambao wanazo sifa za kupatiwa ajira kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Ajira na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

ii. Lakini pia tumekuwa tukifanya kaguzi za kazi kupitia Sheria ya Taasisi za Kazi kifungu cha 45A kinachompa fursa Afisa Kazi kutoa adhabu za papo kwa papo.

iii. Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kufanya uhamasishaji wa ajira kwa watu wenye ulemavu kwa njia mbalimbali zikiwemo warsha, mikutano, makongamano, vipindi vya redio pamoja na runinga.

iv. Kwa kushirikiana na Chama cha Waajiri Tanzania tumekuwa tukitoa tuzo kwa mwajiri bora ambaye ameajiri watu wenye ulemavu na kuwawekea mazingira wezeshi ya kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.

v. Tumekuwa tukitumia programu ya ukuzaji ujuzi kwa kukuza ajira kwa kutoa mafunzo ya kitalu nyumba kwa vijana wakiwemo wenye ulemavu katika Halmashauri mbalimbali ili kuwajengea uwezo wa kujiajiri wao wenyewe lakini pia kuajiri wenzao na pia kuweza kuajiriwa.

vi. La mwisho tumekuwa tukitoa mafunzo kupitia vyuo vya ufundi kwa watu wenye ulemavu vya Yombo - Dar es Salaam na Sabasaba -Singida ambavyo mafunzo haya ambayo yamekuwa yanawawezesha kujiajiri na kuajiriwa.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Serikali ina Mkakati gani wa kuhakikisha kuwa watumishi hewa hawapo katika payroll ya Serikali:-

Je, Serikali inadhibiti vipi mishahara ya watumishi wasiostahili kulipwa kama wastaafu, waliofariki, walioacha kazi na waliofukuzwa kazi katika Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHESHIMIWA JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani mwishoni mwa mwaka 2015 kumekuwepo na mkakati madhubuti wa kudhibiti uwepo wa watumishi hewa katika Mfumo wa Malipo ya Mishahara kwa Watumishi wa Umma nchini. Utekelezaji wa mkakati huo ulifanyika kuanzia mwaka 2016 kwa kuendesha zoezi la uhakiki wa vyeti vya watumishi wote waliopo kwenye taasisi zote za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa. Katika uhakiki huo, watumishi wote ambao hawakuwa na sifa ya kulipwa mishahara waliondolewa mara moja katika Orodha ya Malipo ya Mishahara (Payroll).

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kudhibiti malipo ya mishahara kwa watumishi wasiostahili kulipwa kama vile wastaafu, waliofariki na waliofukuzwa kazi, Serikali imekuwa ikisitisha mara moja malipo ya mishahara ya watumishi wa aina hiyo kupitia Mfumo wa Taarifa za Kiutumishi (Human Capital Management Information System) na Mfumo wa Malipo ya Mishahara (Government Salary Payment Platform) pindi tu wanapokosa sifa ya kuendelea na Utumishi wa Umma. Mifumo hii inatumika katika Taasisi zote za Serikali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna udhibiti ulivyo hivi sasa na ufuatiliaji unavyofanyika, hakuna mtumishi anayeweza kulipwa mshahara bila kustahili. Aidha, naomba kutoa wito kwa Maafisa Masuuli katika Taasisi zote za Umma kuendelea kusimamia kikamilifu udhibiti wa malipo ya mishahara kupitia mifumo iliyopo.
MHE. LEAH J. KOMANYA Aliuliza: -

Mji wa Mwanhuzi unakabiliwa na tatizo kubwa sana la maji safi na salama kutokana na chanzo chake cha maji cha bwawa la Mwanyahina kujaa tope: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi wa Mji wa Mwanhuzi na vitongoji vyake wanapata maji safi na salama ya kutosha kwa mwaka mzima?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Mwanhuzi, Wilayani Meatu unategemea chanzo kimoja cha Maji ambacho ni Bwawa la Maji la Mwanyahina. Bwawa hilo lilijengwa mwaka 1999 lenye uwezo wa kuhifadhi maji mita za ujazo millioni 1.6. Bwawa hili kwa sasa limejaa tope jingi na kusababisha kupungua kina cha kuhifadhi maji kutoka kina cha mita 9 hadi mita 5 zinazohifadhi maji kwa matumizi ya wakazi wa Mji wa Mwanhuzi na vijiji jirani.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha huduma ya maji katika mji wa Mwanhuzi na vitongoji vyake, Serikali imekamilisha utafiti, usanifu na kuanza kutekeleza ujenzi wa chanzo mbadala cha ukusanyaji na usafirishaji wa maji kutoka bonde la Mto Semu hadi kwenye matanki yanayotumika kusambaza maji katika Mji wa Mwanhuzi. Gharama za mradi huo shilingi milioni 742. Tayari Serikali imetuma kiasi cha shilingi milioni 276.6 kwa ajili ya kazi hizo za ujenzi wa mradi mbadala wa kutoa maji katika bonde la Mto Semu na kuyapeleka mjini Mwanhuzi. Mradi huu unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa lengo la kutatua tatizo la muda mrefu katika mji wa Mwanhuzi na vitongoji vyake, Serikali ipo katika hatua za awali za kutekeleza mradi mkubwa wa kutoa maji kutoka Ziwa Victoria unaolenga kumaliza changamoto za huduma za maji katika mkoa wa Simiyu zikiwemo Wilaya za Busega, Bariadi, Maswa, Itilima na Meatu.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika Kata za Mwamalole, Mbushi, Mwamanongu, Imalaseko, Mwamanimba, Mwabuzo na Kimali ili wananchi waweze kufaidika na huduma hiyo na kuchochea maendeleo katika Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mradi Kabambe wa kupeleka umeme vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inaendelea kupeleka umeme katika kata na vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na umeme Tanzania Bara zikiwemo Kata za Mwamamole, Mwamanimba, Mwabuzo, Imalaseko, Mwamanongu, Mbushi na Kimali. Kata hizi pamoja na vijiji vyake vyote vya Meatu vinatarajiwa kufikishiwa umeme ifikapo mwezi Desemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, kazi za mradi katika Wilaya ya Meatu zinajumuisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 555.90, msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 48, ufungaji wa transfoma 48 za 50kVA, pamoja na kuwaunganishia umeme wateja wa awali 1,056. Gharama ya mradi huu ni takriban shilingi bilioni 22.6.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Halmashauri ya Wilaya ya Meatu imekumbwa na wimbi kubwa la uvamizi wa wanyamapori kwenye maeneo ya vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba la Maswa na Hifadhi ya Wanyamapori Makao na kusababisha uharibifu wa mazao na kutishia usalama wa watu.

(a) Je, ni lini Serikali itashughulikia tatizo la uhaba wa watumishi wa Idara ya Wanyamapori?

(b) Je, ni lini Serikali itatatua changamoto ya ukosefu wa vitendea kazi vikiwemo gari na silaha?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante na kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu Swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu lenye sehemu
(a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Pori la Akiba la Maswa lililopo Mkoani Simiyu katika Wilaya za Bariadi, Meatu na Itilima limepakana na vijiji 32 ambapo vijiji 18 vipo katika Wilaya ya Meatu. Pori hilo lina ukubwa wa kilometa za mraba 274 na lilianzishwa mwaka 1974 kwa Tangazo la Serikali Na. 275. Mwaka 2016 usimamizi wa pori hilo ulihamishwa kutoka Idara ya Wanyamapori kwenda Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) na wakati huo kulikuwa na watumishi 62.

Mheshimiwa Spika, kwa vipindi tofauti TAWA imechukua hatua za kuongeza watumishi kwa ajili ya kuimarisha usimamizi wa eneo hilo. Hadi kufikia Januari, 2021 pori hilo lina watumishi 87 sawa na ongezeko la asilimia 40 kutoka watumishi waliokuwepo mwaka 2016. Serikali inaendelea kuziba mapengo ya idadi ya watumishi kwa kadri ya upatikanaji wa vibali vya kuajiri watumishi. Vilevile Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, kujenga uwezo wa Halmashauri kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu.

Mheshimiwa Spika, kuhusu ukosefu wa vitendea kazi, Wizara itaendelea kutenga fedha za ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo magari na silaha ili kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya vijiji vinavyopakana na Pori la Akiba la Maswa.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, ni lini ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kolandoto – Oldean Junction utaanza kwa kuwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ulishafanyika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kolandoto –Lalago – Mwanhuzi – Sibiti – Qangded – Oldean Junction yenye urefu wa kilometa 328 ni barabara kuu inayounganisha Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Singida na Arusha.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga kiasi cha shilingi milioni 2,000 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa awamu kwa kiwango cha lami kwa sehemu ya barabara ya Kolandoto – Mwanhuzi yenye urefu wa kilometa 62.5 na shilingi milioni 3,000 kwa ajili ya barabara ya Lalago – Ngóboko – Mwanhuzi yenye urefu wa kilometa 74 ambayo ni sehemu ya barabara aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge. Ujenzi wa barabara hizi utaendelea kutekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati juhudi za kuanza ujenzi wa barabara hizo zikiendelea, Serikali itaendelea kutenga fedha za matengenezo ya barabara hii ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 shilingi milioni 849.97 zimetengwa kwa sehemu ya Kolandoto hadi Mwangongo mkoani Shinyanga, shilingi milioni 540.995 zimetengwa kwa sehemu ya Mwangongo hadi Sibiti mkoani Simiyu, shilingi milioni 579.118 zimetengwa kwa sehemu ya Sibiti hadi Matala mkoani Singida na shilingi milioni 1,507.352 zimetengwa kwa sehemu ya Matala hadi Oldean mkoani Arusha. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzipandisha hadhi barabara za TARURA zinazochochea ukuaji wa uchumi kwenda TANROADS ili zipatiwe fedha za kutosha za kufanya matengenezo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kabla ya kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, naomba kutoa maelezo mafupi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, suala la kupandisha hadhi barabara ni la kisheria kwa kuzingatia vigezo vilivyowekwa. Barabara ambayo inakidhi vigezo kutoka daraja la barabara ya wilaya kwenda daraja la barabara ya mkoa inatakiwa ijadiliwe kwenye kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa husika. Ikionekana inakidhi vigezo ndio Bodi hiyo kupitia Mwenyekiti wake itamshauri Waziri mwenye dhamana na barabara kuwa barabara husika imekidhi vigezo vya kuwa na hadhi ya Barabara ya Mkoa na hivyo ipandishwe daraja na kuwa Barabara ya Mkoa chini ya TANROADS.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la uwezo wa TARURA hususani uwezo wa rasilimali fedha, Serikali kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo, itaendelea kuiwezesha TARURA kwa kuiongezea fedha na kuijengea uwezo ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na weledi.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza azma hiyo, katika mwaka wa fedha 2021/2022 zimetengwa shilingi bilioni 966.90 ikilinganishwa na shilingi bilioni 275.03 zilizotengwa mwaka wa 2020/2021 kwa ajili ya ujenzi na matengenezo ya barabara na madaraja zinazosimamiwa na TARURA.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasambaza maji katika Vijiji vya Mwanjoro, Jinamo, Mbushi na Witamihya Wilayani Meatu baada ya ujenzi wa Bwawa la Mwanjoro kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vijiji vya Mwanjoro, Jinamo, Mbushi na Witamihya kwa sasa vinapata huduma ya maji kwa wastani wa asilimia 24 kupitia visima vifupi 13.

Mheshimiwa Spika, bwawa la Mwanjolo lilikamilika mwishoni mwa mwaka 2018 likiwa na lengo la kuhudumia vijiji vya Jinamo, Mbushi na Mwanjoro, lakini katika utafiti uliofanyika hivi karibuni bwawa hilo limeonekana kupungua kina kutokana na kujaa kwa mchanga unaosababishwa na kunyweshea mifugo na changamoto ya uharibifu wa mazingira iliyopelekea pia kuathiri ubora wa maji hayo.

Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha kuwa Bwawa la Mwanjolo linatumika kusambaza maji vijiji vya Mwanjoro, Jinamo, Mbushi. Serikali katika mwaka wa fedha 2022/2023 itatenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa Bwawa la Mwanjolo ambapo ukarabati huu utahusisha kuongeza kwa kina cha bwawa, kujenga kingo za bwawa ambazo kwa sasa zimechakaa. Kujenga miundombinu ya kuzuia mchanga kuingia katika Bwawa (sand trap) pamoja na upandaji wa miti na nyasi ili kuzuia mmomonyoko wa ukuta. Pia katika bajeti hiyo Serikali itatenga fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu ya kunyweshea maji mifugo ili wafugaji wasiweze kuingiza mifugo yao kwenye bwawa na mwisho wananchi wa maeneo haya watapewa elimu ya utunzaji wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, mpango wa muda mrefu vijiji hivi pia vitaweza kunufaika na mradi mkubwa unaotarajia kujengwa katika Mkoa wa Simiyu kupitia program ya mabadiliko ya tabia ya nchi maana vijiji hivi vya Mwanjoro vipo umbali wa kilomita 12 toka kwenye eneo la ujenzi wa bomba kuu.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, ni lini Maboma ya Zahanati Vijiji vya Lata, Ikigijo, Lukale, Malwilo, Bulyanaga, Shushuni, Nata, Usiulize na Igushilu yatakamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilipeleka Shilingi milioni 200 katika Wilaya ya Meatu kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati nne. Aidha, katika mwaka 2022/2023 Serikali imetenga Shilingi milioni 200 kutoka Serikali Kuu na Shilingi milioni 100 kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ukamilishaji wa Zahanati za Mwandukisesa, Masanga, Mwanyahina, Mwabagashi na Ikigijo.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2023/2024 kiasi cha Shilingi milioni 100 kitatengwa kutoka mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya ukamilishaji wa zahanati za Igushilu na Nata. Ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Nghoboko kuwa ya kidato cha tano na sita?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ili shule ya sekondari iwe na hadhi ya kidato cha tano na sita inatakiwa iwe na vyumba vya madarasa viwili kwa mkondo mmoja, matundu ya vyoo manne, bweni, maktaba, jiko na bwalo la chakula.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Shule ya Sekondari ya Nghoboko bado haijakidhi vigezo vya kuwa ya kidato cha tano na sita. Kwa kutambua umuhimu wa shule hiyo, Serikali kwa kushirikiana na Halmashauri inaendelea kutafuta fedha kwa ajili kukamilisha miundombinu ya shule hiyo ili iwe na vigezo vya kupandishwa hadhi na kuwa ya kidato cha tano na sita.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi wa daraja la juu Mto Semu katika Kijiji cha Mwamanongu Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana na kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa fedha 2005/ 2006, Serikali kupitia Mfuko wa Barabara ilijenga daraja la chini (drifting) lenye urefu wa mita 100 kwa gharama ya Shilingi Milioni 105 ili kurahisisha mawasiliano katika Kijiji cha Mwamanongu.

Mheshimiwa Spika, TARURA inaendelea na upembuzi yakinifu (Geotechnical Investigation) kwa ajili ya kuanza kazi ya usanifu ili kupata gharama za ujenzi wa daraja la juu katika Mto Semu lililopo katika Kijiji cha Mwamanongu.

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa usanifu wa Daraja hili, Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa hili daraja.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kukamilisha ujenzi wa maboma ya Ofisi Kata za Nkoma, Mwangudo, Mwamanimba na Imalaseko – Meatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa maboma manne ya Ofisi za Kata ya Nkoma, Mwangudo, Mwamanimba na Imalaseko katika Jimbo la Meatu ambayo yanahitaji kukamilishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Bajeti ya mwaka wa Fedha wa 2023/2024, Halmashauri ya Meatu imetenga fedha za mapato ya ndani kiasi cha shilingi milioni 60 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya Ofisi za Kata ya Imalaseko na Lingeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwenye vyanzo mbalimbali kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma ya ofisi za Kata nchini kote zikiwemo Kata za Nkoma, Mwangudo na Mwamanimba, ahsante.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, mashine ngapi za kukusanya mapato zilibainika kutokuwa hewani na hazikutambulika na Halmashauri mwaka 2018/2019, 2019/2020 na 2020/2021?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 kulikuwa na mashine 14 za kukusanyia mapato (POS) katika halmashauri mbili, mwaka 2019/2020 kulikuwa na mashine 1,469 za kukusanyia mapato (POS) katika halmashauri 54 na mwaka 2020/2021 kulikuwa na mashine 1,355 katika halmashauri 46 ambazo hazikuwa hewani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imefanya maboresho ambapo matumizi ya mashine za kukusanyia mapato kupitia mfumo wa LGRCIS yatakoma ifikapo tarehe 30Juni, 2023 hivyo kuanzia tarehe 1 Julai, 2023 hakutakuwa na POS zitakazokuwa offline zaidi ya saa 24.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itatekeleza ahadi ya ujenzi wa daraja la juu katika Mto Mwamanongu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 43 kwa ajili kufanya usanifu wa Daraja la Mto Mwamanongu. Usanifu huo umekamilika na jumla ya shilingi bilioni 7.5 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo. Serikali itajenga daraja hilo kadri ya upatikanaji wa fedha.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhudumia miundombinu ya Wilaya ya Meatu kwa kujenga, kukarabati na kufanya matengenezo ya barabara na madaraja kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali haioni haja ya kuigawa Shule ya Msingi Mwanhuzi kwa kuwa shule hiyo ina wanafunzi 1,400?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli Shule ya Msingi Mwanhuzi ina changamoto ya mlundikano wa wanafunzi. Katika kutatua changamoto hiyo katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali kupitia Mradi wa BOOST imepeleka shilingi milioni 348.5 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya katika Kata ya Mwanhuzi. Baada ya kukamilika kwa ujenzi wa shule hiyo, changamoto hii itakuwa imetatuliwa.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni nini mpango wa Serikali kufanya asilimia 50 ya wanafunzi wanaojiunga na Kidato cha Tano katika shule za Kata watoke ndani ya Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la Serikali kuchanganya wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali ili kujenga Utaifa, kuchanganya wanafunzi kunasaidia msawazo wa nafasi zilizopo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi ya kujiunga Kidato cha Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutumia wanafunzi asilimia 50 kujiunga na Shule za Sekondari kutasababisha baadhi yao kukosa nafasi kwa kuwa siyo kila mchepuo unapatikana kwenye shule zilizopo katika Halmashauri husika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, kwa nini ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Kijiji cha Mwagwila haukamiliki ingawa Serikali imetuma fedha nyingi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2013/2014 Serikali kupitia Mradi wa DASIP ilipeleka fedha za ujenzi wa Skimu ya Umwagiliaji Mwagwila yenye ukubwa wa hekta 250. Kazi iliyofanyika ni ujenzi wa banio na sehemu ya mfereji mkuu. Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha mradi huo haukuweza kukamilisha ujenzi wake.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha eneo lote linalofaa linamwagiliwa. Katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imetenga bajeti kwa ajili ya kufanya mapitio ya usanifu wa mradi huu ili kubaini gharama halisi ya kukamilisha ujenzi wa skimu hii. Aidha, ujenzi wa mradi huu utaanza mara baada ya kazi ya mapitio ya usanifu kukamilika.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itajenga Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, naomba sasa kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutekeleza Mpango wa Ujenzi wa Vyuo vya VETA kwa awamu katika mikoa na wilaya mbalimbali kulingana na upatikanaji wa fedha. Katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha VETA katika Wilaya ya Meatu, wananchi wa Meatu wanashauriwa kutumia Vyuo vingine vya VETA na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo kwa ajili ya kupata elimu ya mafunzo ya ufundi, nakushukuru sana.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza: -

Je, lini Bwawa la Mwanjoro litakarabatiwa ili kuwezesha usambazaji wa maji Vijiji vya Jinamo na Witamihya - Meatu?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Jimbo la Meatu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Jinamo na Witamihya kwa sasa vinapata huduma ya maji kupitia kisima chenye uwezo wa kuzalisha maji wastani wa lita 24,000 kwa siku. Katika muendelezo wa kuboresha huduma ya maji katika vijiji hivyo Serikali katika bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 itatenga fedha kwa ajili ya kukarabati Bwawa la Mwanjoro, ili kuwezesha ujenzi wa miundombinu ya usambazaji wa maji katika Vijiji vya Mwanjoro, Jinamo na Witamihya vyenye jumla ya wakazi 5,002. Kazi zinazotarajiwa kutekelezwa katika ukarabati wa bwawa hilo ni pamoja na ukarabati wa tuta umbali wa mita 100 (embankment), ukarabati wa utoro wa maji (spill way) na uimarishaji wa kingo za tuta la bwawa (side slopes).
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga Malambo ya kunyweshea mifugo katika Jimbo la Meatu?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa bwawa/lambo hufanyika kwa hatua tatu ambazo ni kutafuta chanzo cha maji (water source), kufanya usanifu (design) na kutekeleza kazi ya ujenzi. Wizara itawasiliana na Halmashauri ya Wilaya Meatu kwa ajili ya kupata mapendekezo ya eneo linalofaa kujenga lambo ambalo halina mgogoro wa umiliki, ili hatua za usanifu ziweze kufanyika na kuingiza gharama zake kwenye Mpango wa Bajeti ya Wizara kadiri ya upatikanaji wa fedha za miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia kutoa wito kwa wafugaji na wadau wengine hapa nchini kuwekeza kwenye ujenzi wa miundombinu ya maji ili kusaidia kupunguza changamoto ya maji kwa ajili ya mifugo. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga jengo la kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Meatu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania imeendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na ya kisasa na kukarabati majengo chakavu. Wilaya ya Meatu ni moja ya wilaya ambazo zina majengo ya Mahakama lakini jengo lake ni chakavu na siyo la kisasa. Kwa mujibu wa mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama, Wilaya ya Meatu itajengewa jengo la kisasa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga jengo la kisasa la Mahakama ya Wilaya ya Meatu?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania imeendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na ya kisasa na kukarabati majengo chakavu. Wilaya ya Meatu ni moja ya wilaya ambazo zina majengo ya Mahakama lakini jengo lake ni chakavu na siyo la kisasa. Kwa mujibu wa mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama, Wilaya ya Meatu itajengewa jengo la kisasa katika Mwaka wa Fedha 2025/2026.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza tatizo la kukatika kwa umeme Wilaya ya Meatu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Meatu inapata umeme kutokea Kituo cha Kupoza Umeme cha Ibadakuli kilichopo Mkoani Shinyanga umbali wa kilomita 135. Kukatika kwa umeme Wilayani Meatu kunatokana na umbali mrefu wa njia ya kusafirisha umeme pamoja na uchakavu wa miundombinu ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kukabiliana na tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kufungwa vidhibiti umeme katika njia ya awali, kujenga njia ya kusafirisha umeme kutoka Mkalama Mkoani Singida hadi Bukundi Wilayani Meatu na kuendelea na zoezi la kubadilisha nguzo zilizochakaa kwa kuweka nguzo za zege.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kwa mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imeanza kutekeleza ujenzi wa Kituo cha Kupoza Umeme katika eneo la Imalilo, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu ambapo itajengwa line ya umeme kutokea kwenye kituo hicho hadi Meatu. Jitihada hizi zimepunguza changamoto ya kukatika umeme kwa kiasi kikubwa sana.
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-

Je, lini Serikali itajenga uzio katika Shule ya Sekondari ya Nyalanja Meatu ili kurahisisha ulinzi wa mali na wanafunzi wa bweni wapatao 600?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwaka wa Fedha 2022/2023 na 2023/2024, Serikali ilipeleka shilingi milioni 916.2 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali yakiwemo madarasa 14, mabweni 4 na matundu ya vyoo 22 katika shule ya Sekondari Nyalanja kwa ajili ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa uzio kwa ajili ya ulinzi wa mali na wanafunzi wa bweni. Hata hivyo, kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni ujenzi wa miundombinu ya msingi inayowezesha kuongeza nafasi za udahili wa wanafunzi. Ahsante.