Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Mariamu Nassoro Kisangi (34 total)

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Tatizo la matumizi ya dawa za kulevya linazidi kuongezeka siku hadi siku:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwasaidia vijana wetu walioathirika na dawa za kulevya?
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inalitambua tatizo la matumizi ya dawa za kulevya hapa nchini na athari wanazozipata watumiaji, hasa vijana ambao ni nguvu kazi muhimu, ambao huathirika kiafya, kiuchumi na kijamii. Ili kuwasaidia vijana walioathirika kwa kutumia dawa za kulevya, Serikali imekuwa ikitekeleza mikakati ifuatayo:-
(i) Serikali kupitia hospitali na vituo vya afya imekuwa ikitoa huduma mbalimbali ya kuwaondoa katika urahibu watumiaji wa dawa za kulevya. Baadhi ya hospitali ambazo zimekuwa zikitoa huduma hizo ni pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Magonjwa ya Akili Mirembe - Dodoma, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Hospitali za Temeke na Mwananyamala za Mkoa wa Dar es Salaam na Hospitali ya Afya ya Akili Lulindi - Korogwe. Huduma zinazotolewa katika hospitali hizo ni pamoja na ushauri nasaha, kuondoa sumu mwilini na matibabu ya methadone.
(ii) Serikali kwa kushirikiana na Asasi za Kiraia inaendelea na programu maalum ya kutoa huduma za upataji nafuu katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali imetoa mwongozo wa uendeshaji wa huduma hizo na inaendelea na ujenzi wa kituo kikubwa cha huduma za matibabu ya utengemao katika eneo la Itega mjini Dodoma na inaratibu ujenzi wa kituo kama hicho mjini Tanga.
MHE. STANSLAUS S. MABULA (K.n.y. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Wajasiriamali katika Mkoa wa Dar es Salaam hususan Machinga na Mama Lishe wamekuwa wakisumbuliwa sana na Mgambo wa Jiji hali inayowafanya kushindwa kujitafutia riziki ya kila siku:-
Je, Serikali inawasaidiaje Wajasiriamali hao wadogo wodogo ambao hujipatia riziki zao kupitia biashara ndogo ndogo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inathamini sana mchango wa wafanyabiashara wadogo katika kukuza ajira na kipato. Hata hivyo, wafanyabiashara wadogo wote wanatakiwa kuendesha biashara zao katika maeneo yaliotengwa rasmi kwa ajili hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wale wanaokiuka utaratibu huu, Halmashauri hulazimika kuwatumia Mgambo kwa ajili ya kuwaondoa wafanyabiashara hao na kuwaelekeza kwenda katika maeneo yaliotengwa rasmi. Aidha, katika kutekeleza wajibu huo, mgambo wanatakiwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kuwatengea maeneo ya kufanyia biashara, Serikali inatekeleza mpango wa kurasimisha biashara katika mfumo usiokuwa rasmi ili kuzitambua, kuzisajili na kuongeza mchango wake katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutumia fursa hii kuzikumbusha Halmashauri zote kutenga maeneo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili biashara hizo zifanyike katika maeneo rasmi ambayo itakuwa rahisi kuwatambua na kuwahudumia.
Aidha, wafanyabiashara wadogo wanashauriwa kuunganisha mitaji yao midogo na kuunda kampuni ndogo za biashara ili waweze kukopesheka katika Taasisi za fedha na hivyo kuongeza tija katika biashara hizo.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Matatizo ya wanafunzi kutojua kusoma na kuandika pamoja na kutofanya vizuri katika mitihani yao mara zote lawama zinakwenda kwa Walimu.
Je, Serikali imefanya utafiti wa kina na kuona kama Mwalimu peke yake ndiye anayeweza kumfanya mwanafuzi aweze kufanikiwa katika masomo yake?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassor Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na ufuatiliaji unaofanyika kupitia Wadhibiti wa Ubora wa Shule na wataalam mbalimbali wa elimu, imethibitika kwamba Mwalimu ana nafasi kubwa katika kumwezesha mwanafunzi kumudu stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu ili aweze kufanya vizuri zaidi katika masomo yake ya baadaye. Hata hivyo, ili Mwalimu aweze kufanya kazi yake kwa ufanisi na kumsaidia mwanafunzi ipasavyo, masuala mengine yanayopaswa kuzingatiwa ni pamoja na:-
Uwiano wa Mwalimu kwa wanafunzi katika darasa, upatikanaji wa vitabu, vifaa na zana stahiki, ushirikiano wa wazazi na jamii pamoja na mazingira rafiki ya kujifunzia na kufundishia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia hayo, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuimarisha ufundishaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ikiwa ni pamoja na yafuatayo:-
Kwanza, kutoa mafunzo kazini kwa Walimu, Wadhibiti Ubora wa Shule na Wakuu wa Shule; kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara; kuhakikisha upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia na kufundishia kwa wakati; na kuweka mazingira mazuri ya shuleni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa wito kwa wazazi na jamii kwa ujumla kuwapa ushirikiano wa kutosha Walimu ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Aidha, napenda kutumia nafasi hii kuwahimiza Waheshimiwa Wabunge ambao ni wawakilishi wa wananchi kuweza kuwahamasisha wazazi/walezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanafuatilia maendeleo ya watoto wao mara kwa mara ili waweze kumudu stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu na kufanya vizuri zaidi katika masomo yao.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Bei za dawa za mifugo na kilimo zinaongezeka siku hadi siku na kufanya mfugaji mdogo ashindwe kupata maendeleo:-
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kudhibiti hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kulijulisha Bunge Tukufu kuwa asilimia 99 ya dawa zote za tiba na kinga kwa mifugo zinazotumika nchini huagizwa kutoka nje. Jukumu la uagizaji na usambazaji wa dawa na chanjo hufanywa na sekta binafsi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Mifugo ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa bei za dawa za mifugo katika baadhi ya maeneo zinaongezeka siku hadi siku. Miongoni mwa sababu zinazochangia kupanda kwa bei hizo ni pamoja na:-
Mheshimiwa Naibu Spika, moja, uhaba wa Sekta Binafsi katika baadhi ya maeneo kwa ajili ya kusambaza dawa husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pili, baadhi ya wafugaji kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu namna ya kupata pembejezo za mifugo kutoka kwa mawakala halisi au wasambazaji na hivyo kununua pembejeo hizo kupitia kwa watu ambao huuza kwa bei ya juu wenye malengo ya kupata faida kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuongeza upatikanaji wa chanjo na dawa za mifugo na zenye bei nafuu, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Chanjo Tanzania, (Tanzania Vaccine Institute) iliyoko Kibaha chini ya Wakala wa Maabara ya Vetenari (veterinary) Tanzania inazalisha chanjo dhidi ya magonjwa ya mdondo kwa kuku pamoja na chambavu na kimeta kwa ng’ombe.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa 2015/2016 taasisi imezalisha dozi 30,396,100 za mdondo, dozi ya chambavu 136,800 na dozi 304,300 za kimeta. Aidha, Baraza la Vetenari Tanzania limeendelea kuchukua hatua stahiki za kuhamasisha Sekta Binafsi kuwekeza katika kuanzisha vituo vya kutolea huduma za mifugo nchini hususan katika maeneo ya wafugaji ili kupanua wigo wa upatikanji wa huduma hizi pamoja na dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hatua zingine zinazochukuliwa na Serikali ni pamoja na kuondoa ushuru wa kuingiza dawa zote za mifugo zinazoingia nchini na kodi ya ongezeko la thamani VAT.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuwapunguzia wakulima makali ya bei za dawa Serikali kila mwaka imekuwa ikitoa ruzuku ya dawa kwa ajili ya mazao ya korosho na pamba. Pia Serikali imekuwa ikitoa ruzuku kwa ajili ya miche bora inayostahimili magonjwa kwa ajili ya mazoa ya kahawa na chai. Pamoja na ruzuku hizo Serikali imekuwa ikitoa bure dawa za kudhibiti panya, viwavijeshi, kweleakwelea na nzige. Vilevile Serikali imekuwa ikigharamia ndege ya kunyunyizia dawa hizo ili kudhibiti visumbufu hivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni tano kwa ajili ya kununua dawa za kilimo na shilingi bilioni moja kwa ajili ya kununua dawa za majosho.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia walimu kupata mikopo ya muda mrefu na yenye riba nafuu ili waweze kujenga nyumba bora za kuishi?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo:-
Serikali inao Mfuko wa mikopo ya nyumba kwa watumishi wa Serikali inaowezesha watumishi kupata mikopo ya nyumba wakiwemo walimu. Mikopo hiyo inaweza kurejeshwa ndani ya miaka 30 lakini kabla ya mtumishi kustaafu. Masharti makuu ya kupata mkopo huo ni mhusika kuwa na hati ya kumiliki ardhi pamoja na uwezo wa kurejesha mkopo anaohitaji na kubakia na angalau theluthi moja ya mshahara wake kwa matumizi mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 1995 mpaka 2016 jumla ya walimu 95 walipata mikopo yenye jumla ya shilingi 892,254,796.50. Walimu hao ni kutoka Mikoa ya Dodoma, Tabora, Mwanza, Morogoro, Pwani, Bukoba, Musoma na Dar es Salaam.
Aidha, Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, Bima ya Afya pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa imeanzisha Watumishi Housing Company mwaka 2013. Lengo kuu la kuanzisha kwa Kampuni ya Watumishi Housing ni kujenga nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya kuuzia watumishi wa umma na mashirika yake. Kampuni hii tayari imefanya makubaliano na Benki tano za biashara ili zitoe mikopo ya kununua nyumba kwa watumishi kwa masharti nafuu. Benki hizo ni Azania, CRDB, NMB, BOA na Exim.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Watumishi Housing Company imeingia pia makubaliano na Mamlaka ya Elimu ya Sekondari kujenga nyumba zipatazo 240 katika mikoa 23 ya Tanzania Bara. Hivi sasa ujenzi wa nyumba 90 kwa ajili ya walimu unaendelea katika Mkoa ya Mtwara - Nanyumbu, Tandahimba na Liwale, Mkoa wa Morogoro - Kilosa, Jiji la Tanga - Mkinga, Pwani - Msata na Rufiji pamoja na Jiji la Dar es Salaam - Wilaya ya Ilala eneo la Mvuti na Singida eneo la Mkalama na pia katika Mikoa ya Simiyu na Shinyanga.
Aidha Wizara yangu kupitia mortigage financing chini ya TMRC na BOT imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 374,515,110,203 kwa wananchi 4,065 wakiwemo walimu kupitia mabenki 54 yaliyopo nchini.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Kumekuwa na ujenzi wa nyumba za ghorofa kando kando ya barabara kuu na Serikali ndiyo inatoa vibali vya ujenzi huu ambapo baada ya muda maghorofa hayo yanaweza kubomolewa na mwenye jengo kulipwa fidia.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuainisha maeneo yenye mipango ya maendeleo ili kuepuka gharama kubwa ya kulipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MANDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na ujenzi wa nyumba za ghorofa na za kawaida kando kando ya barabara kuu na barabara nyingine. Kasi ya ujenzi wa nyumba hizo huchochewa na kuimarika kwa miundombinu hususan barabara za kiwango cha lami. Uimarishaji wa barabara za lami huvutia wawekezaji kujenga nyumba za biashara, vituo vya mafuta, mahoteli pamoja na makazi. Hali hii ni ya kawaida katika uendelezaji miji kwa kuwa uboreshaji miundombinu hususan barabara hupandisha thamani ya ardhi katika eneo husika na kuvutia ujenzi wa majengo ya ghorofa.
Mheshimiwa Spika, ili kupunguza uwezekano wa kubomoa au kulipa fidia maeneo yaliyoendelezwa kwa ujenzi wa nyumba za ghorofa, Serikali imejiwekea mikakati ifuatayo:-
(i) Kuanisha meneo yote ambayo yameiva kiundelezaji upya (areas ripe for redevelopment) ili kuoanisha matumizi ya sasa na ya baadaye.
(ii) Kupanga maeneo hayo ili uendelezaji wake uendane na thamani ya ardhi na kuboresha sura ya miji. Mipango kina ya uendelezaji maeneo haya ni kama vile Kariakoo, Kurasini, Temeke, Msasani, Oysterbay, Magomeni na Ilala.
(iii) Kwa upande wa miji mingine, upangaji wa maeneo haya unazingatiwa katika utayarishaji wa mipngo kabambe (master plan) ya miji husika.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa nyumba za ghorofa kando ya barabara kuu hauna budi kufuata taratibu za mipango miji, uhandisi, mazingira na masharti ambayo muendelezaji hupewa katika kibali chake cha ujenzi. Natoa rai kwa taasisi zenye mamlaka ya kutoa vibali vya ujenzi ambazo ni Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa pamoja na Majiji kuzingatia masharti ya uendelezaji wa miji ili kuzuia uwezekano wa kubomoa maghorofa na kulipa fidia.
MHE. ZAYNAB M. VULLU (K.n.y MHE. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Ongezeko la watoto wenye matatizo ya afya ya akili na ubongo limekuwa kubwa kwa sasa katika nchi yetu:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha vitengo vya elimu kwa watoto wenye mahitaji maalum (walemavu) wa viungo na ubongo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua uwepo wa watoto wenye ulemavu wa akili na wenye usonji na jitihada mbalimbali zinafanyika ili kuhakikisha kuwa watoto hao wanapata fursa ya elimu kama watoto wengine. Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha kuwa kuna jumla ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji 11,386 katika ngazi ya elimu ya awali na msingi na wanafunzi wenye ulemavu wa viungo 8,115 wanaosoma ngazi ya elimu ya awali, msingi na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kupanua fursa za upatikanaji wa elimu na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia kwa wanafunzi wenye ulemavu nchini. Hatua hizo ni pamoja na:-
Wizara ilitoa mafunzo kazini kwa Walimu wapatao 699 wanaofundisha wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji kwa lengo la kuwajengea uwezo ili kuinua ubora wa elimu itolewayo; kuboresha miundombinu ya shule ili kukidhi mahitaji ya ujifunzaji kwa wanafunzi wenye ulemavu wa viungo; kuanzisha na kuimarisha vitengo 349 vinavyopokea wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji nchini; na kufanya mapitio ya mwongozo wa ujenzi wa majengo ya shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu. Mwongozo huu utazingatia mahitaji maalum ya wanafunzi wenye ulemavu wa viungo ili kuwawezesha kusoma bila vikwazo wawapo shuleni.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara inakamilisha uandaaji wa mwongozo wa kufundishia wanafunzi wenye ulemavu wa akili na wenye usonji ambao utasambazwa katika vitengo vyote 349 vinavyopokea wanafunzi hao. Mwongozo huo una lengo la kupanua uelewa wa Walimu juu ya mbinu za kufundishia, matumizi ya vifaa pamoja na saikolojia ya kufundishia wanafunzi hao kwa ubora zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Wizara imetenga jumla shilingi bilioni 3.5 katika mwaka wa fedha 2017/2018 kwa ajili ya ununuzi na usambazaji wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia pamoja na visaidizi kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum wakiwemo wanafunzi wenye ulemavu wa viungo, akili na wenye usonji.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Kumekuwa na mlundikano wa viwanda vingi vya aina moja katika kanda moja, kwa mfano kumekuwa na viwanda vingi vya saruji (cement) katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi na Mtwara.
Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na tatizo hilo ili kuondoa changamoto za madhara ya athari kwa binadamu wanaoishi maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uamuzi wa wapi kiwanda kijengwe kwa kiasi kikubwa hutegemea uwepo wa soko la bidhaa itakayozalishwa na/au upatikanaji wa malighafi na/ au teknolojia.
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Ukanda wa Pwani kuanzia Tanga mpaka Mtwara wanayo faida ya kuwa na malighafi nyingi na yenye ubora wa hali ya juu wa utengenezaji wa saruji. Lakini pia inapotokea malighafi hiyo inaagizwa kutoka nje ya nchi, viwanda vilivyoko Pwani vinakuwa na faida katika unafuu wa gharama za usafirishaji. Vile vile kihistoria soko kubwa la saruji na hata bidhaa nyingine ni Ukanda wa Pwani na hasa Dar es Salaam, si kwa nia mbaya viwanda kulundikana katika eneo hilo.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuondoa changamoto za madhara ya shughuli za viwanda kuwa ndani ya makazi ya watu wanaoishi maeneo ya karibu kupitia Sera ya Mazingira, ambapo kwanza kabla ya kiwanda kujengwa katika eneo husika, Tathmini ya Athari za Mazingira (Environmental Impact Assessment) hufanywa. Zoezi hili hufanywa na Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara inayosimamia.
Mheshimiwa Spika, pili, baada ya kiwanda kuanza kufanya kazi Ukaguzi wa Athari za Mazingira (Environmental Auditing) hufanyika kila baada ya mwaka mmoja. Tatu, Serikali huhamasisha matumizi ya teknolojia rafiki kwa mazingira. Kwa mfano matumizi ya Electrostatic precipitator, west scraper ili kuzuia vumbi kusambaa hewani na kwenye makazi ya watu. Wizara yangu kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira inaendelea kutoa mafunzo na kusimamia Sheria ya Mazingira ili kuepusha madhara yatokanayo na shughuli za viwanda nchini.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Katika Jiji la Dar es Salaam kuna Viwanda vingi ambavyo vimebadilishwa matumizi yake na kugeuzwa kuwa maghala ya kuhifadhia vifaa mbalimbali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvirejesha viwanda hivyo kwenye matumizi yake ya awali?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kati ya Mashirika ya Umma 341 yaliyobinafsishwa hadi mwaka 2007 viwanda vilikuwa 156. Madhumuni ya ubinafsishaji wa viwanda yalikuwa ni pamoja na kutoa ajira, kuzalisha bidhaa zinazokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa na kuongeza mchango wa viwanda katika uchumi wa Taifa. Ufufuaji wowote wa viwanda ambao unaleta matokeo hayo ni sahihi kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, katika Jiji la Dar es Salaam, ni kweli kuna baadhi ya viwanda vilivyobadili matumizi ya awali na kuanza shughuli nyingine za kiuchumi. Baadhi yake ni vile vilivyouzwa kwa utaratibu wa ufilisi na mali moja moja na hivyo kutokuwa na mikataba ya mauzo inavyowalazimisha wamiliki kuendeleza shughuli za viwanda za awali.
Mheshimiwa Spika, Viwanda hivyo ni pamoja na TANITA One ambacho kwa sasa kinatumika kama maghala; Tanzania Publishing House Limited Investment ambacho kwa sasa ni duka la vitabu, Tractors Manufacturing Company Limited ambapo kwa sasa kuna jengo la biashara la Quality Centre, Light Source Manufacturing ambapo TATA Holding) pamoja na Tanganyika Packers Ltd ya Kawe (Kawe Meat Plant) ambapo eneo lilinunuliwa na National Housing kwa ajili ya ujenzi wa makazi.
Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuhamasisha na kuwezesha viwanda visivyofanya kazi, vifanye kazi. Mpaka sasa uhamasishaji huu umewezesha viwanda 18 vikiwemo vya Dar es Salaam kama vile kiwanda cha UFI kilichokuwa kinatengeneza zana za kilimo, kilibadilishwa na kuwa Tanzania Steel Pipe Limited na kuanza kutengeza mabomba ya maji na vingine vinaendelea kufanyiwa ukarabati na vingine tayari vinafanya kazi.
Hivyo, chini ya Kamati Maalum yenye wataalam toka sekta mbalimbali, tunafuatilia utendaji wa kiwanda kimoja hadi kingine mpaka vyote viweze kufanya kazi kwa tija.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-
Tatizo la ada kwa wanafunzi katika shule binafsi nchini linazidi kuongezeka siku hadi siku. Mwanafunzi wa darasa la kawaida katika baadhi ya shule analipa mpaka shilingi milioni tatu hali inayosababisha wazazi wengine kuwapeleka watoto wao katika nchi jirani za Kenya na Uganda ili kutafuta nafuu ya ada:-
Je, kwa nini Serikali isikae na wadau husika ili kupanga ada elekezi kwa wenye shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua na kuthamini mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya elimu nchini ambapo hadi sasa jumla ya shule za msingi 1,432 kati ya shule 17,583 zinamilikiwa na sekta binafsi. Aidha, jumla ya shule za sekondari 1,250 kati ya shule 4,885 zinamilikiwa na sekta binafsi. Serikali inatambua utofauti wa viwango vya ada kati ya shule za umma na shule binafsi. Vilevile Serikali inatambua utofauti wa viwango hivyo kati ya shule moja na nyingine za binafsi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haitajihusisha na upangaji wa ada kwa shule binafsi bali itaendelea kusimamia viwango vya ubora, taratibu, kanuni na sheria za uendeshaji wa shule zote nchini. Lengo la Serikali ni kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanapata elimu bora kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na tofauti ya viwango vya ada na huduma zitolewazo kwenye shule binafsi, nitoe ushauri kwa wazazi kuchagua shule kulingana na uwezo wao wa kulipa ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kwa watoto na hata kwa wamiliki wa shule hizo.
MHE. ZAYNABU M. VULU (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) aliuliza:-
Serikali imekuwa ikitoa ahadi ya ujenzi wa Barabara ya Nzasa – Kilungule – Buza – Temeke:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga barabara hiyo muhimu kwa wakazi wa Mbagala, Mwanagati na Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nzasa – Kilungule – Buza – Temeke ina urefu wa kilomita 7.6. Barabara hii imeongezwa kwenye mpango wa maboresho ya Jiji ya Dar es Salam kupitia mradi wa DMDP na katika awamu inayofuata itajengwa kwa kiwango cha lami. Serikali imekwishalipa fidia ya jumla ya shilingi bilioni 3.25 kwa wananchi 310 ambao wanatakiwa kupisha mradi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya usanifu imeshakamilika na kazi zinazotekelezwa ni ujenzi wa barabara ya lami kilomita 7.6, ujenzi, wa madaraja mawili yenye urefu wa mita 60 na makalvati makubwa matano kwenye bonde la Mto Mzinga, uwekaji wa taa barabarani jumla ya taa 324 ambazo zinatumia mwanga wa jua; pia kujenga vituo tisa vya mabasi ya daladala. Gharama ya kutengeneza shughuli hii inakadiriwa kuwa shilingi bilioni 22.6.
MHE. MARIAM NASORO KISANGI aliuliza:-

Wapo watoto wanaoishi Gerezani na huenda shule na kurudi Gerezani kulala na mama zao. Hali hiyo siyo nzuri kwa malezi ya mtoto hasa mambo wanayoyaona na kusikia wakiwa Gerezani:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia watoto hao waondokane na hali hiyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu maswali ya Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto kuwepo magerezani inatokana na mama zao kuhukumiwa kutumikia adhabu ya kifungo wakiwa katika hali ya ujauzito au kuwa na mtoto aliye chini ya umri wa miaka miwili ambaye anapaswa kupata haki ya kunyonya maziwa ya mama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kutoa maelezo ya ufafanuzi kama ifuatavyo: hakuna watoto wanaokwenda shule wakiwa magerezani isipokuwa kuna watoto walio chini ya miaka miwili wanaolazimika kubaki gerezani na mama zao ili kupata haki yao ya kunyonya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile yapo mazingira yakiwemo kukosekana kwa malezi mbadala kwa watoto zaidi ya miaka miwili na wasiozidi miaka mitano kubaki na mama zao gerezani, hivyo kulazimika kuhudhuria katika vituo vya kulelea watoto wadogo mchana (Day Care Centres) kwa madhumuni ya kupata huduma ya malezi changamshi ya awali ili kuchochea ukuaji na maendeleo ya kiakili, kimwili, kihisia, kijamii na kimaadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka 2015 kulikuwa na watoto 150, mwaka 2016 tulikuwa na watoto 85 na mwaka 2017 kulikuwa na watoto 108. Watoto hawa ni kwa mgawanyiko wa akina mama walioko mahabusu na wafungwa katika magereza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009 Kifungu cha 114, Kanuni za Ulinzi na Usalama wa Mtoto Mwaka 2015 na Sera na Uratibu wa Ulinzi na Mtoto katika Magereza ya Mwaka 2018, imeweka utaratibu wa kuhakikisha kuwa mtoto anapata malezi yanayohitajika ikiwemo mlo kamili, virutubisho, huduma za afya pamoja na chanjo kwa watoto wa chini ya miaka miwili. Utaratibu wa watoto chini ya miaka mitano kuhudhuria kwenye vituo vya kulelea watoto wadogo mchana, unalenga kupunguza muda watoto kukaa gerezani na kutumia muda wa zaidi ya masaa sita katika vituo hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chini ya Sheria ya Mtoto Na. 21 ya Mwaka 2009, Serikali imeanzisha program ya malezi mbadala kama vile walezi wa kuaminika, malezi ya kambo na kuasili. Lengo ni kuhakikisha watoto wote wanaolelewa katika taasisi wanapata malezi ya kifamilia. Pia watoto walio na mama zao gerezani ambao wamekosa malezi mbadala, wanapata fursa ya kupokelewa katika makao ya watoto kwa muda wakati jitihada nyingine zikiendea. Program hizo zinahakikisha watoto wa zaidi miaka mitano wanaondolewa gerezani na kuunganishwa na watoa huduma wa malezi.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Eneo la Chamazi Mbagala katika Kitengo cha Afya ya Akili limetelekezwa na hakuna ukarabati wa majengo yaliyopo wala uendelezwaji wa eneo hilo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuliendeleza eneo hilo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo na Chamazi lina ukubwa wa ekari 165 na linaendelea kutumika kwa shughuli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na ufugaji wa ngo‟mbe, kuku wa mayai na nyama. Shamba hili pia linatumika kwa kilimo ambapo zaidi ni mazao ya mboga za majani, mahindi na nazi yanazalishwa. Pia kazi mbalimbali za mikono zinafanywa katika eneo hili zikiwemo kazi za ususi wa vikapu, mifuko, mikufu, bangili na mapambo mbalimbali kwa kutumia malighafi za asili. Kazi nyingine ni pamoja na ufumaji wa vitambaa, kofia na utengenezaji wa nguo za batiki.

Mheshimiwa Spika, shughuli hizi ni sehemu ya tiba kwa wagonjwa wa akili waliopata nafuu ili waweze kurudi katika hali ya kawaida na kushiriki katika shughuli za kiuchumi wanaporudi katika jamii. Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imeajiri Watalaamu wa Mifugo na Kilimo ili kuweza kusimimia shughuli za ufugaji na kilimo. Aidha Hospitali imekuwa ikisafisha shamba hilo kila mwaka kwa kuondoa vichaka na kukata majani.

Mheshimiwa Spika, mipango inaendelea katika mwaka wa Fedha 2019/2020. Hospitali ya Taifa Muhimbili imepanga kuanza ujenzi wa uzio kwa kuanzia eneo linapaka na maeneo yanamilikiwa na wananchi wanaoishi karibu na shamba hili. Sanjari na hilo Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kushirikiana na Kituo cha Afya cha Uwekezaji inaendelea kufanya mazungumzo na wabia kwa ajili ya kutumia sehemu ya shamba hili kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vya kuzalisha vifaa tiba na dawa. Hospitali imeshafanya mazungumzo na wadau kutoka China, Hong kong, Uturuki, Tunisia na Jamhuri ya Czech.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Hospitali za Amana, Mwananyamala na Temeke hazina mashine za kufulia nguo:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mashine za kufulia katika Hospitali hizo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana imeshatenga eneo kwa ajili ya kujenga chumba cha utakasaji. Hospitali ipo kwenye mchakato wa ununuzi wa mashine kubwa ya kufulia kupitia mkopo kutoka NHIF wenye thamani ya shilingi 80,000,000. Kwa sasa hospitali imenunua mashine ndogo mbili kwa ajili ya kufulia nguo zinazotumika katika chumba cha upasuaji zenye thamani ya shilingi 300,000,000.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke imeagiza mashine ya kufulia automatic washing machine yenye uwezo wa kufua kilo 70 kwa awamu moja na pasi yake kwa jumla ya shilingi milioni 83,348,950. Na Hospitali ya Mwananyamala imeagiza mashine mbili za kufua kupitia MSD zenye thamani ya shilingi 71,000,000 na tayari mashine moja imewasilishwa katika Hospitali ya Mwananyamala na ipo katika utaratibu wa usimikwaji. Aidha, kwa sasa huduma za ufuaji katika Hospitali ya Temeke na Mwananyamala zinafanywa kupitia Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa mkataba wa ufuaji mpaka pale watakapokamilisha taratibu zote.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka kipimo cha MRI katika Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mwongozo uliokuwepo huduma za CT-Scan na MRI hazikuwepo katika Hospitali za Rufaa za Mikoa. Hata hivyo, kufuatia mabadiliko ya kiuchumi na uhitaji wa huduma hizi kwa wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilifanya mabadiliko ya mwongozo kwa kutengeneza mwongozo mpya wa vifaa vya Radiolojia nchini wa mwaka 2018 (Standard Medical Radiology and Imaging Equipment Guidelines) ambapo pamoja na mambo mengineyo huduma za CT-Scan na MRI zitapatikana katika ngazi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa na huduma za MRI zitapatikana katika ngazi ya Hospitali za Rufaa za Kanda na Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na mabadiliko hayo Serikali inakusudia kufunga CT-Scans katika Hospitali za Rufaa za Mikoa ikiwa ni Mwananyamala, Temeke na Amana.
MHE. LUCY T. MAYENGA (K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI) Aliuliza: -

Nchi yetu imekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa Afya ya Akili: -

(a) Je, nini chanzo cha ugonjwa huo?

(b) Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwasaidia wagonjwa hao?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO Alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, afya ya akili ni ile hali ya mtu kuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwemo utambuzi, uzalishaji wa mali, kutunza familia na kumudu shughuli za kijamii. Magonjwa ya akili ni pale mtu anaposhindwa kukabiliana na changamoto za kimaisha ikiwa ni pamoja na kushindwa kumudu shughuli za kijamii, kujitunza, hisia na utambuzi ambapo sababu za magonjwa haya ni mchanganyiko wa sababu za kibaiolojia, kisaikolojia na kimazingira.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kukabiliana na ongezeko la magonjwa haya, Serikali imefanya yafuatayo: -

(1) Kuandaa Sheria ya Afya ya Akili ya Mwaka 2008 ambapo sheria hii inatoa mwongozo na utaratibu wa namna ya kuwapokea na kuwahudumia watu wenye ugonjwa wa akili.

(2) Kuandaa Sera na miongozo ambapo wagonjwa wa afya ya akili ni miongoni mwa makundi maalum ambayo huduma zake zinaweza kutolewa kwa msamaha kwa watu ambao hawana uwezo.

(3) Serikali inahakikisha kuwa huduma hizi zinatolewa katika ngazi zote za huduma za afya kuanzia kwenye jamii, ngazi ya afya ya msingi, mkoa, kanda, mpaka hospitali maalum ya Taifa ya afya ya akili.

(4) Kuhakikisha upatikanaji wa dawa muhimu za afya ya akili kwenye vituo vyote vya huduma za afya.

(5) Kuongeza udahili wa wanafunzi wa uzamivu (Masters) katika masomo ya wagonjwa wa akili.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Utaratibu wa watoto kuingia darasa la kwanza ni lazima awe amepitia shule za awali.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha madarasa ya elimu ya awali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, elimu ya awali ni muhimu katika kumwandaa na kumjengea msingi mwanafunzi wakati wote atakapokuwa anaendelea na masomo katika ngazi zote. Kwa kuzingatia suala hili, Serikali ilitoa maagizo kuwa kila shule ya msingi nchini iwe na darasa la awali ili kuwapokea wanafunzi walio na umri kati ya miaka minne hadi mitano ikiwa ni maandalizi ya kujiunga na darasa la kwanza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanda Mtaala wa Elimu ya Awali unaoendana na aina ya ujifunzaji unaotakiwa kwa watoto wa elimu ya awali. Mtaala huo umezingatia ujifunzaji kwa kutumia michezo. Hadi Februari 2021, walimu 70,712 wanaofundisha darasa la awali, la Kwanza na la Pili wamepatiwa mafunzo ya namna ya utumiaji wa mbinu sahihi za ufundishaji, ufaraguzi na utumiaji wa zana za kufundishia. Hatua hii imeimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika madarasa ya awali nchini.

Mheshimiwa, Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa watoto wa Darasa la Awali, la Kwanza na la Pili wanapatiwa vyumba vya bora vya madarasa vinavyowawezesha kutengeneza mazingira bora ya kujifunzia kwa rika lao na kuhakikisha kuwa mtoto wa Darasa la Awali analindwa na kupata eneo zuri la kujifunzia kwa kucheza ndani na nje ya darasa. Hatua hii pia imehusisha kubadilisha madarasa haya kwa kuweka zana za ujifunzaji.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha Elimu ya Awali katika shule zote nchini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurasimisha Bandari ya Mbweni kuwa Bandari ndogo?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbuge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekamilisha kazi ya kutambua Bandari bubu zote zilizo katika mwambao wa Bahari ya Hindi ikiwemo bandari ndogo ya Mbweni kwa ajili ya kurasimishwa kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania kwa kushirikaina na Manispaa ya Kinondoni, zipo katika hatua ya kutambua mipaka ya eneo la bandari hiyo kwa upande wa bahari na nchi kavu ili kuweka miundombinu rafiki kama vile maegesho ya majahazi, barabara, ofisi, choo, maji, umeme na ghala la kuhifadhia mizigo.

Mheshimiwa Spika, tangu mwezi Februari, 2020, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania imepeleka wafanyakazi na mashine za POS katika bandari ndogo ya Mbweni ili kusimamia shughuli za kibandari na kukusanya mapato. Katika miezi tisa ya mwaka wa fedha 2020/2021 (Julai 2020 hadi Machi 2021), TPA imeweza kukusanya kiasi cha shilingi milioni 117. Mapato hayo yanatarajiwa kuongezeka baada ya kuirasimisha bandari hiyo na kuiwekea miundombinu muhimu.

Mheshimiwa Spika, kwa hivi sasa ipo katika hatua za mwisho za kumpata Mkandarasi Mshauri ambaye pamoja na mambo mengine, atafanya usanifu katika Bandari za Mbweni na Kunduchi na kushauri aina ya uwekezaji wa miundombinu itakayofaa katika bandari hiyo. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Wilaya mpya ya Ukonga katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la Ukonga liko katika Wilaya ya Ilala ambayo ni moja kati ya Wilaya tano zinazounda Mkoa wa Dar es Salaam. Utaratibu wa kuanzisha Mkoa na Wilaya mpya umebainishwa kupitia Sheria ya Uanzishwaji wa Mikoa na Wilaya Na. 397 ya mwaka 2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kuanzisha Wilaya mpya huanzia kwenye Serikali za Vijiji/Mitaa ili kupata ridhaa ya wananchi kisha hupelekwa kwenye Mabaraza ya Madiwani ya Halmashauri, Kamati ya Ushauri ya Wilaya (DCC) na Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC). Baada ya hatua hiyo, maombi hayo huwasilishwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI kwa ajili ya uhakiki na kujiridhisha na baadaye kuwasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maamuzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Ilala bado haijawasilisha maombi hayo kadri ya matakwa ya sheria.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Wodi za Wagonjwa wenye matatizo ya Ubongo na Akili katika Hospitali za Temeke, Amana na Mwananyamala?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, lakini vilevile kumshukuru Rais wetu kwa kuendelea kutuamini mimi na Mheshimiwa Ummy Ali Mwalimu kusimamia Wizara ya Afya kwa niaba yake Rais.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali ya Rufaa ya Temeke ipo katika mchakato wa kukarabati jengo lililokuwa likitumika kwa wagonjwa wa kisukari ili liweze kutumika kwa ajili ya kulaza wagonjwa wa akili. Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala imetenga kiasi cha shilingi milioni mia mbili kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wagonjwa wa akili. Pia, Hospitali ya Rufaa ya Amana kwa kuwa ujenzi huo upo kwenye mpango mkakati wa miaka mitano wameelekezwa kutenga bajeti ya ujenzi wa jengo la afya ya akili katika bajeti ya mwaka 2022/2023. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kufanya utafiti wa chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano baada ya kuzaliwa na Mama kuishiwa nguvu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti nyingi zimefanyika Kitaifa na Kimataifa kujua chanzo cha watoto wachanga kugeuka njano mara baada ya kuzaliwa. Tafiti hizo zimeonyesha kuwa hali ya umanjano inayotokea ndani ya masaa 24 baada ya kuzaliwa inaonyesha tatizo la kiafya (Pathological) na linahitaji kutambua sababu na kutoa tiba stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo likitokea baada ya masaa 24, mara nyingi linatokana na sababu za kawaida za mwili wa mtoto kupunguza chembechembe nyekundu nyingi alizokuwa nazo tumboni kwa Mama, hata hivyo hili pia uchunguzi wa kina ni muhimu ili kujihakikishia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utafiti ni muhimu na ni suala endelevu katika afya. Ahsante.
MHE. ABDALLAH J. CHAUREMBO K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya kutoka Buza-Kilungule hadi Nzasa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Buza-Kilungule hadi Nzasa ina urefu wenye jumla ya kilomita tisa. Barabara hii imekasimiwa kwenye mtandao wa barabara zinazohudumiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa barabara TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua za utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami kuanzia Nzasa hadi Buza kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam yaani Dar es Salaam Metropolitan Development Project. Mradi huu wa DMDP unasimamiwa na Wizara ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI na kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA). Aidha, kwa sasa mkandarasi yupo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuongeza na kujenga maeneo ya kusubiri kuona wagonjwa katika Hospitali nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea na ujenzi wa Hospitali mpya kwenye Halmashauri ambazo hazikuwa na hospitali, ambapo mpaka sasa jumla ya hospitali mpya 127 zinaendelea na ujenzi. Aidha, kumekuwa na changamoto ya kukosekana kwa majengo ya Ndugu wa Wagonjwa kusubiria kuona wagonjwa katika hospitali hizo.

Mheshimiwa Spika, ili kutatua changamoto hiyo, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/2024 itatenga bajeti ya shilingi bilioni 2.04 kwa ajili ya ujenzi wa sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye hospitali 102 ambazo zinakamilisha ujenzi wa wodi za kulaza wagonjwa. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuondoa kodi kwenye vifaa tiba?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, vifaa tiba, kinga, dawa na vitendanishi ni miongoni mwa bidhaa zenye sifa za kupata msamaha wa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kupitia Jedwali la II la Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani Sura 148. Jedwali hilo hufanyiwa maboresho mara kwa mara ili kuhakikisha huduma zitokanazo na bidhaa hizi zinapatikana kwa gharama nafuu, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali imejipangaje kukabiliana na ongezeko la Wagonjwa wa Kansa ya Kizazi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali katika kukabiliana na ongezeko la wagonjwa wa kansa ya kizazi, kwa kufanya yafuatayo: -

Moja, kutoa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa wa saratani kupitia vipindi vya redio, televisheni, machapisho na magazeti, mitandao ya jamii kama facebook, Instagram na pia televisheni za sehemu za kusubiria wagonjwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya.

Pili, Serikali inatoa chanjo kwa wasichana ili kuwakinga na kirusi kinachosababisha saratani ya mlango wa kizazi.

Tatu, kuanzisha huduma za awali za uchunguzi na matibabu ya saratani ya mlango wa kizazi kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za Taifa.

Nne, Serikali imeimarisha huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu kwa kuhakikisha uwepo wa wataalamu na vifaa tiba kwa ajili ya kukabiliana na Saratani.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. STELLA I. ALEX K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Mkoa wa Dar es Salaam umefaidika vipi na uzalishaji wa madini ya ujenzi yaliyozalishwa katika Mkoa huo?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba Mkoa wa Dar es Salaam unazalisha na unanufaika na madini ujenzi, hata hivyo wastani wa asilimia 60 ya madini ujenzi yanayotumika kwenye ujenzi wa miradi ya kimkakati katika Mkoa huo yanazalishwa kutokea Mkoa wa Pwani katika Wilaya za Mkuranga, Bagamoyo, Kisarawe na Kibaha.

Mheshimiwa Naibu Spika, madini ujenzi yanayozalishwa katika Mkoa wa Dar es Salaam yanajumuisha mchanga, kifusi na limestone, ambayo yanazalishwa katika Wilaya za Kigamboni, Ilala na Kinondoni. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, makusanyo ya mrabaha na ada ya ukaguzi yatokanayo na madini hayo katika Mkoa wa Dar es Salaam yalifikia kiasi cha shilingi bilioni 1.9.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini itaendelea kuimarisha usimamizi katika uzalishaji wa madini ujenzi katika Mkoa wa Dar es Salaam na nchini kote kwa ujumla ili kuongeza manufaa ya madini hayo kwa mwananchi mmoja mmoja na Taifa.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa Barabara ya kutoka Kibada – Tundwi hadi Songani kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nipokee marekebisho ya Mheshimiwa Mbunge aliyoyasema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge Viti Maalum, Mkoa wa Dar-es-Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepanga kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara ya Kibada – Tundwi, Songani, Kimbiji yenye urefu wa kilometa 41 ambapo kwa sasa upo kwenye hatua za mwisho za manunuzi ya kumpata Makandarasi atakayetekeleza ujenzi wa mradi huu. Mkataba unatarajiwa kuwa umesainiwa kabla ya mwisho wa mwezi huu Juni, 2023. Ahsante.
MHE. ISSA J. MTEMVU K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza kilimo cha minazi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha minazi nchini ambapo imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika Kituo Kidogo cha Utafiti cha Chambezi, Wilaya ya Bagamoyo ili kuzalisha miche iliyo bora ya minazi. Kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepanga kuzalisha miche bora 750,000 na kuisambaza kwa wakulima wa zao la minazi ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo na kuanzisha mashamba makubwa ya pamoja.

Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali imeanza mazungumzo na Kampuni ya Deejay Coconut Farm Private Ltd. ya nchini India katika mashirikiano ya uzalishaji wa miche ya inayozalisha nazi 250 kwa mnazi mmoja kulinganisha na minazi ya kawaida inayozalisha nazi 80 kwa mti mmoja.
MHE. STELLA I. ALEX K.n.y. MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kurahisisha huduma ya upatikanaji wa bima ya afya kwa wananchi wake?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali ipo katika hatua ya ukamilishaji wa Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote ambao utawezesha kurahisisha huduma ya upatikanaji wa bima za afya kwa wananchi wote. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, kuna mpango gani wa kuimarisha kilimo cha Minazi katika Ukanda wa Pwani ya Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imefanya utafiti na kuanzisha aina mpya ya mbegu ya minazi iitwayo East African Tall (EAT) ambayo inastawi katika maeneo ya ukanda wa Pwani na kuvumilia magonjwa. Baada ya kupatikana kwa mbegu hiyo, Serikali katika msimu wa mwaka 2023/2024 imeiwezesha TARI kuzalisha miche 140,000 ambayo itasambazwa kwa wakulima katika Halmashauri za Wilaya za ukanda wa Pwani kuanzia mwezi Oktoba, 2024.

Aidha, jumla ya mbegu za nazi 18,000 zinatarajiwa kusambazwa kwenye vitalu vya Halmashauri za Ruangwa, Mtwara Vijijini, na Muheza. Katika msimu wa 2024/2025 TARI inatarajia kuzalisha miche 200,000 ya aina hiyo ya nazi na kusambaza kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile, Serikali kupitia taasisi zake itaendelea kutoa elimu ya kanuni bora za kilimo cha nazi na teknolojia za uthibiti wa visumbufu vya nazi kwa maafisa ugani na wakulima katika wilaya zote zitakazopatiwa miche mipya kwa ajili ya kufufua mashamba ya nazi.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia wagonjwa wa figo kupata matibabu ya kusafishwa figo kwa gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassor Kisangi, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali katika kupunguza gharama za kusafisha figo ni kununua vifaatiba na vitendanishi moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji. Pia Muswada wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote utakapokamilika utakuwa suluhisho la kudumu. Hata hivyo, sera ya afya ya nchi inaelekeza hakuna Mtanzania anayetakiwa kufa kwa sababu ya kukosa fedha, hivyo Serikali imekuwa ikitoa msamaha kwa wasio na uwezo na waliotimiza vigezo.
MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Barabara ya Kongowe hadi Mjimwema?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikifanya ukarabati wa maeneo korofi katika Barabara ya Kongowe – Mjimwema – Kivukoni yenye urefu wa kilometa 25.01, hasa yale yaliyoharibika sana katika kipindi cha mvua. Aidha, katika mwaka wa fedha 2024/2025, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi milioni 500, kwa ajili ya ukarabati wa maeneo yote yaliyoharibika, ahsante.

MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza watu wasio na ulemavu kujiunga na vyuo vya watu wenye ulemavu?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM K.n.y. WAZIRI MKUU alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Elimu Jumuishi wa miaka mitano 2021/2022 – 2025/2026. Pia Serikali imeandaa Mwongozo wa Utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Elimu Jumuishi 2022/2028 wa Oktoba, 2022. Aidha, Serikali inatekeleza Mpango Mkakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu 2023/2024 – 2025/2026 ambapo pamoja na mambo mengine unahusu suala la elimu na ujuzi kwa kuzingatia ujumuishaji wa watu wenye na wasio na ulemavu katika maeneo ya kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuwaandaa wanafunzi kuishi maisha jumuishi katika jamii imeandaa mikakati na miongozo kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wenye ulemavu wanajifunza na kuishi katika mazingira yanayowaunganisha na jamii nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mpango Mkakati wa Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu wa mwaka 2023/2024 – 2025/2026, Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 imepanga kudahili wanafunzi 2,000 kupitia vyuo vya watu wenye ulemavu, kati yao wasio na ulemavu ni 400 hii ni 20% ya wanafunzi wote. Aidha, mwaka 2024/2025 Serikali imepanga kupitia vyuo vyake vya watu wenye ulemavu kudahili wanafunzi 1,500 kati yao wasio na ulemavu ni 500 sawa na 30% ya wanafunzi wote, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutumia Taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa ili kupunguza vifo vinavyotokana na mabadiliko ya hali ya hewa?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imeendelea kuwezesha miundombinu ya ukusanyaji, uchakataji na ufungashaji wa taarifa za hali ya hewa hapa nchini. TMA imeendelea kufanya usambazaji wa taarifa hizo za hali ya hewa kwa umma kupitia vyombo vya habari mbalimbali na kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii.