Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Mariamu Nassoro Kisangi (109 total)

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kabisa naomba nipongeze juhudi za Mheshimiwa Waziri Jenista Mhagama kwa kutembelea vituo vyote vya utoaji wa madawa ya kulevya katika Mkoa wetu wa Dar es Salaam. Pia nipongeze juhudi za Madaktari na Wauguzi wa vituo hivi ambao wanafanya kazi kila siku bila kujali Jumapili, sikukuu, kila siku ya Mungu wanafanya kazi ya kuwasaidia vijana wetu. Sasa naomba niulize maswali mawili:-
Kwa kuwa, matumizi ya madawa ya kulevya yanazidi kuongeza katika Jiji la Dar es Salaam siku hadi siku, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza vituo vya utoaji wa madawa hayo katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuwa sasa hivi vituo vinavyotoa hayo madawa ni vitatu, Mwananyamala, Temeke na Muhimbili. Serikali ina utaratibu gani wa kuongeza vituo hivyo katika Jiji la Dar es Salaam?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana wengi wameingia katika makundi ya madawa ya kulevya kwa sababu ya ukosefu wa kazi au shughuli mbalimbali za kujiajiri au ujasiriamali, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kituo kikubwa cha walioathirika na madawa ya kulevya ambacho kitawasaidia hawa waathirika wapate mafunzo ya ujasiriamali?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU (MHE. DKT. ABDALLAH S. POSSI): Mheshimiwa Naibu Spika, moja, kuhusiana na mpango wa kuongeza vituo vingine. Serikali inatambua wingi wa wahitaji wa huduma ya kuondokana na urahibu wa madawa ya kulevya. Wazo la kujenga vituo hivyo ni zuri na pale uwezo utakaporuhusu, basi jambo hilo litafanyika.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusiana na uwezekano wa kujenga kituo ambacho kitawapa mafunzo. Katika swali la msingi nilishajibu kwamba tayari Serikali imeandaa mwongozo maalum utakaotumika na vituo mbalimbali vinavyowasaidia watu kuondokana na urahibu na mengineyo, mwongozo ambao bado utapitiwa na wadau, naamini kabisa hilo ni moja ya suala ambalo limezingatiwa.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwanza kabisa nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ya nyongeza kutoka katika swali la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu hayo mazuri ambayo yametolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri, tatizo hili la dawa za kulevya katika nchi yetu ya Tanzania, pamoja na kwamba siyo linaweza kujionyesha waziwazi lakini linaendelea kukua na tafiti zinatuambia mikoa ambayo iko katika maeneo ya mwambao mwa Bahari ya Hindi, Tanga, Mtwara, unakwenda mpaka Mwanza, yanaonekana kwamba ni maeneo ambayo tatizo la dawa za kulevya linaendelea kuwa kubwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pamoja na kuona umuhimu wa kuanza kutumia dawa ya methadone kuhakikisha inawatibu warahibu wa dawa hizi za kulevya, inaendelea kutoa wito kwa mashirika mbalimbali ili tuweze kuendelea kushirikiana na Watanzania wote kuhakikisha tunafanya kazi ya pamoja kuwaondoa watoto wetu katika tatizo hili la dawa za kulevya.
Mheshimiwa Naibu Spika, nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge, tatizo la dawa za kulevya bado linapambana na hali ya unyanyapaa kama tatizo la ugonjwa wa UKIMWI lililotangulia. Sasa ni wajibu wa kila Mtanzania tuanze kuondoa unyanyapaa, vijana wetu waweze kujitokeza kwa wingi, wapelekwe katika maeneo hayo yaliyopangwa kuwasaidia ili kwa pamoja tuweze kupambana na tatizo hili kwa vijana wetu na tusiendelee kuwaficha katika nyumba zetu, wale walioko mitaani, Serikali za Mitaa tushirikiane pamoja tuwalete ili waweze kupatiwa huduma hii na tuwarudishe katika hali yao ya kawaida.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na mimi kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo haya ya wafanyakazi wa migodini yamekuwa yakijirudia mara kwa mara katika Bunge hili, tumekuwa tukiyasikia, nataka kujua.
Je, ni lini sasa Serikali tafanya ukaguzi huo wa makampuni makubwa ya madini na kuwabaini wadanganyifu ambao wanakwepa kuwalipa wafanyakazi mafao yao ya NSSF na kodi nyingine?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tumegundua kuna udanganyifu mkubwa sana katika migodi na makampuni makubwa ambayo yamekuwa yakihudumu katika nchi yetu ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, makampuni hayo wakati mwingine yamekuwa yakitoa salary slip mbili, moja ikionesha kiwango cha chini cha malipo ya mshahara na hicho ndicho kinachofanya contribution kwenye Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, lakini wana salary slip nyingine ambazo kodi za nchi hazikatwi inavyotakiwa wala mafao ya wafanyakazi hayapelekwi inavyotakiwa.
Naomba nilihakikishie Bunge lako Tukufu, tumegundua tatizo hilo na baada ya muda si mrefu mtasikia kikosi kazi kimeshaundwa kikiwa na wajumbe kutoka Wizara ya Fedha, TRA, Mwanasheria Mkuu, Ofisi ya kwangu - Ofisi ya Kazi, Kamishna Mkuu na watu wengine. Watafanya ukaguzi na kuwabaini hao wote na hatua kali zitachukuliwa na makato hayo yataanza kupelekwa kwa kuzingatia mshahara halisi wa mfanyakazi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa wananchi wa Kipunguni Serikali inakiri kabisa kwamba haijawalipa fidia na kwa kuwa Serikali imeonyesha kabisa nia ya wazi kwamba wanalihitaji eneo la Kipunguni kwa upanuzi wa Uwanja wa Ndege, je, Serikali ina mkakati gani sasa wa muda mfupi kuwasaidia wananchi wale wa Kipunguni kwa kuwa hawana maendeleo na wala hawakopesheki?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mariam Kisangi ameuliza Serikali ina mkakati gani wa kuweza kuwawezesha wananchi hao ili waweze kuondokana na adha waliyonayo? Naomba nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kama tulivyoeleza wakati wa bajeti kwamba tunakwenda kupitia taasisi zote ambazo zinadaiwa na wananchi kwa maana wametwaa maeneo yao lakini hawajalipa fidia ili tuweze kuwasisitiza waweze kulipa fidia hizo mapema. Kwa sababu ni kweli imekuwa ni muda mrefu, hata kama utapiga hesabu kwa kuweka 6% bado inakuwa ni ngumu kwa sababu kadri wanavyochelewesha kulipa ndivyo jinsi mwananchi anavyozidi kuumia. Kwa hiyo, Wizara inachukua hatua kwanza kuwabaini wale wote ambao wanadaiwa kwa maana kwamba wametwaa maeneo ya wananchi ili waweze kuwalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia kama hiyo haitoshi, Wizara imetoa Waraka Na. 1 wa mwaka 2015 wa Uthamini na Ulipaji wa Fidia ambao unataka kwa siku za baadaye, iwe taasisi au mtu binafsi akitaka kuchukua eneo la mtu ni lazima alipe kwanza fidia na Wizara lazima ijiridhishe kwamba kuna pesa ambayo ipo itakwenda kulipa watu hao kabla ya maeneo hayo kuchukua ili kuepuka hii migogoro ambayo imekuwa mingi. Kwa hiyo, Waraka Na.1 wa mwaka 2015 sasa hivi tunausimamia na wakati huo huo tunawafuatilia wale ambao wanadaiwa kuweza kuwa-push ili waweze kulipa fidia za watu ambao wanawadai.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa majibu ya Serikali yanaeleza wazi kuwa kufaulu kwa mtoto kunategemea mwanafunzi mwenyewe, Mwalimu, mazingira ya kufundishia pamoja na wazazi. Sasa, je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba mazingira ya kufundisha na kufundishia yanakuwa bora na pia kutoa elimu bora kwa wazazi kwamba wao ni wajibu wao pia kuwasimamia watoto wao?
Swali la pili, kwa kuwa hakuna Mwalimu anayefanya kazi kubwa kama Mwalimu ya KKK wa darasa la kwanza na la pili kwani yeye ndiye anayetoa msingi wa elimu au mwelekeo wa mtoto wa maendeleo yake ya baadaye. Je, Serikali imejipanga vipi kuwapa motisha Walimu wa KKK kutokana na kazi kubwa wanayoifanya?
WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi kwa ufuatiliaji mzuri. Anawajali sana Walimu na ndiyo maana maswali yake kila siku yanalenga katika kuangalia Walimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na ndiyo maana katika majibu yangu ya msingi nimeeleza kabisa kwamba, Serikali imekuwa inatoa mafunzo kwa walimu kazini na tumetoa mafunzo kwa walimu 22,697 kwa stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu, hii yote ni katika kujenga mazingira mazuri na kumwezesha mwalimu. Vilevile Serikali imeandaa vitabu na iko inasambaza vitabu katika kuimarisha stadi za kusoma, kuandika na kuhesabu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la kwamba Serikali inafanya nini ili wazazi waweze kutambua wajibu wao. Serikali imekuwa ikihamasisha wazazi na ndiyo maana hata kupitia Bunge lako naomba pia Waheshimiwa Wabunge mtuunge mkono katika maeneo yenu tuhamasishe wazazi ili watambue kwamba elimu ndiyo kila kitu katika maisha ya watoto wao na hivyo Serikali itaendelea kutoa uhamasishaji kwa wazazi ili waendelee kutambua wajibu wao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la mwisho la nyongeza anauliza kwamba, Serikali imejipanga vipi kutoa motisha kwa walimu wa darasa la kwanza na la pili ambao wanakuwa na mzigo mkubwa wa kufundisha watoto. Serikali inatambua mchango wa walimu na ndiyo maana nasema ukiangalia vipaumbele vyetu katika mafunzo kwa Walimu kazini tumejikita zaidi kwa Walimu hao kwa sababu tunatambua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile nitumie nafasi hii kusema kwamba tunakusudia na kesho nitasimama hapa mbele yenu kueleza mipango yetu ijayo lakini tunakusudia kuweka utaratibu wa kuweza pia kuwatambua Walimu wa darasa la kwanza na la pili wanaofanya vizuri kwa sababu tumekuwa na utamaduni wa kuwatambua kwenye darasa la saba, kidato cha nne, lakini tunaweka utaratibu mahsusi wa kuweza pia kuwatambua kwa sababu nayo pia ni motisha.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Spika kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.
Pamoja na juhudi za Serikali za kuboresha Soko la Samaki la Feri, naipongeza sana Serikali kwa kuwapa hata majiko ya gesi pale katika Soko la Samaki la Feri, mimi kama Mbunge wa Dar es Salaam napongeza.
Kwa kuwa utoaji wa leseni za uvuvi imekuwa ni kero kubwa sana kwa wavuvi kwani wanatakiwa kulipia leseni za uvivi kila wanapotoka sehemu moja kwenda nyingine.
Je, Serikali ina utaratibu gani wa kuwaondoshea wananchi kero hiyo ya kulipia leseni za uvuvi kwa kila wanapoenda kuvua?
Swali la pili, kwa kuwa Jimbo la Kigamboni na Mkoa wa Dar es Salaam kwa ujumla umezungukwa na Babari Kuu, na kwa kuwa wavuvi wa Mkoa wa Dar es Salaam, hawana mipango yoyote ya kuboreshewa mazingira ya kazi yao ya uvuvi na Serikali.
Je, Serikali imejipanga vipi kuwasaidia wavuvi wa Kigamboni na Dar es Salaam kwa ujumla katika kuboresha kazi yao ya uvuvi?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Kisangi kwa maswali mazuri, kuhusu swali la leseni kutozwa kila wanapovuka mpaka mmoja kwenda mwingine, jambo hili linahusisha Wizara zaidi ya moja, Wizara ya Kilimo tumeandaa waraka ambao tunategemea tutakaa pamoja na wenzetu wa TAMISEMI na wa Wizara ya Fedha, tunategemea jambo hili lipate ratiba hapa kabla ya Wizara ya Fedha ku-table Finance Bill, ili kuweza kukubaliana kuhusu mambo haya ya leseni ambazo zinatozwa kwa wingi, hili jambo linaendana sambamba na makato yanayotozwa kwa wazalishaji wetu wa sekta hizi. Hili ni agizo la Mheshimiwa Rais la kuhakikisha kwamba Watanzania wanaofanya kazi zao wanapata tija kutokana na shughuli hizo wanazozifanya kwa kuwaondolea makato mengi wanayoyapata kutokana na vyanzo mbalimbali kukata kutoka kwenye shughuli zao.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kuwaboreshea mazingira, moja ya mazingira linahusiana na hili alilolisemea la makato, Wizara tumepanga baada ya Bunge hili kukutana na Wavuvi wanaovua katika Jimbo lake na Waheshimiwa Wabunge, tutawakaribisha ili tuweze kupokea mapendekezo yao kuhusu mazingira ambayo tutayaboresha.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali langu la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninalo swali la nyongeza.
Kwa kuwa wananchi wengi wa Mkoa wa Dar es salaam na hasa katika maeneo ya Kitunda, Mvuti, Chanika, Mbande, Pugu, Somangila, Kisarawe II, Kibada, Vijibweni, Yombo, Kunduchi, Mabwepande na Kibamba wote wanategemea kupata vipato vyao na hasa akina mama kwa kwa kazi ya kufuga kuku wa nyama na kuku wa mayai, lakini bei ya dawa zimekuwa kubwa sana kiasi kwamba akina mama hawa wanashindwa kuuza bidhaa zao, wanashindwa kuuza kuku wa mayai na kuku wa nyama kwa gharama ambayo ingeweza kuwapa faida.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga maduka au kuweka dawa katika vituo vya mifugo vya Serikali ambavyo viko katika Wilaya zote Tanzania nzima ili wafugaji hawa waweze kupata nafuu ya bei za dawa kuliko vile wanavyolanguliwa na wafanyabiashara mbaimbali ambao wao hawana uchungu sana na wananchi, wao wanatafuta kipato?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali imeonyesha wazi lengo lake kwamba kuna Kituo cha Tiba cha Kibaha kinaweza kuzalisha chanjo mbalimbali; je, Serikali ina mkakati gani wa kukiongezea nguvu kituo hiki ili iweze kuzalisha chanjo kwa wingi, wananchi waweze kupata chanjo hizo kwa bei nafuu na wao waweze kuboresha vipato vyao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kama alivyosema kwamba kuna changamoto kubwa sana ya upatikanaji wa dawa za mifugo, vilevile kwamba bei imekuwa ni bei ambayo wakulima wengi, wafugaji wengi hawawezi kustahimili. Mkakati wa Serikali kwa sasa ni kujaribu kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili iweze kutoa huduma hizo, huo ndiyo mwelekeo wa sera tuliyonayo ya mwaka 2006.
Hata hivyo, Serikali kwa kutambua kwamba tayari utaratibu huo una changamoto Serikali inafikiria zaidi kuangalia ni namna gani tunaweza tukawezesha na tukahamasisha ujenzi wa viwanda dawa hizo ziweze kuzalishwa nchini ili bei ipungue. Kwa sababu kinachofanya dawa kwa kiasi kikubwa ziwe ghali ni kwa sababu nyingi tunazitoa nje ya nchi, kwa hiyo kuna utaratibu ndiyo maana tunahamasisha sana kuhusu ujenzi wa viwanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ili kuteremsha na kufanya bei ya dawa hizo kuwa nafuu Serikali imeendelea kupitia wigo wa kodi na tozo mbalimbali ambazo ziko kwenye dawa ili hatimaye dawa hizo ziweze kupatikana kwa urahisi zaidi. Serikali inaendelea kutumia Maafisa Ugani kufanya uhamasishaji na kutoa elimu ili wananchi wenyewe waweze kuona umuhimu wa kutumia dawa ili kuweza kunusuru mifugo yao isife.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili kwamba Serikali ina mpango gani wa kuongezea kiwanda kilichopo Kibaha nguvu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaweka mazingira wezeshi ili sekta binafsi waweze kujenga viwanda zaidi. Kwa hiyo, tuko tayari kushirikiana na viwanda hivyo kwa sababu kuna viwanda vya Farmers Center, vilevile kuna kiwanda cha Multivet Services kwa hiyo zote hizi tutaendelea kufanya nao kazi na kutoa msaada ambao watahitaji ikiwa ni pamoja na msaada ambao watauhitaji ikiwa na nafuu za kodi ili waweze kuzalisha zaidi ili wakulima wetu na wafugaji wetu waweze kupata dawa kwa haraka lakini na kwa bei ambayo ni nzuri. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Katika Mkoa wa Dar es Salaam bado kuna maeneo mbalimbali katika Kata ya Mianzini maeneo ya Mponda Wilaya ya Temeke, Chamanzi, Tuangoma, Somangila, Kimbiji, Pemba Mnazi, Vijibweni, Chanika, Majohe na Pugu, vyote hivyo bado havijapata miradi ya umeme kusambazwa katika vijiji mbalimbali.
Je, Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itasambaza umeme pembezoni mwa vijiji hivi vya Mkoa wa Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa maeneo ya Dar es Salaam maeneo mengi hatujapeleka umeme na hasa Kigamboni. Awamu ya kwanza tunayofanya tunapanga kujenga sub-station Kigamboni kwa sababu population ya sasa ni kubwa. Kwa hiyo, vitongoji vyote vya Kigamboni vitapelekewa umeme kupitia Awamu ya II. Pia maeneo ya Chanika, maeneo ya Gongo la Mboto, maeneo ya Kinyamwezi, maeneo ya Buyuni na yenyewe yanapelekewa kwenye mpango huu wa REA unaoanza mwezi Desemba.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na juhudi za Serikali ambazo nazipongeza sana lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Serikali ina mfuko ambao unawapa watumishi wa Serikali mikopo ya muda mrefu ya nyumba, watumishi hao ni pamoja na walimu. Lakini naweza kusema kwamba mfuko huo haupo wazi kwa walimu wote Tanzania na wala kwa watumishi wengine. Je, Serikali imejipanga vipi sasa katika kutoa elimu juu ya mfuko huu ambao unatolewa mikopo yaani mikopo inayotolewa kwa Serikali imejipanga vipi kutoa elimu kwa walimu na watumishi wengine wa Serikali ili waweze kufaidika na mkopo huo wa nyumba wenye gharama nafuu? (Makofi)
Swali la pili; Kwa kuwa Serikali imeonyesha wazi dhamira ya kutaka kuwasaidia walimu na watumishi wengine kupitia Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii lakini mifuko hii inajenga nyumba zenye gharama kubwa sana kuanzia milioni 50 kwenda juu mpaka milioni 75 gharama ambazo mwalimu wa kawaida hawezi kuzimudu.
Je, kwa nini Serikali sasa isiwashawishi Mifuko hiyo ya Jamii ikatoa mikopo ya fedha taslimu kwa walimu waweze kujijengea nyumba zao wenyewe kwa gharama nafuu? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza alitaka tu tutoe elimu kwa ajili ya walimu kufahamu kwamba kuna mfuko ambao unawawezesha wao kuweza kupata mkopo kwa ajili ya nyumba.
Naomba niseme kwamba mfuko huu tulionao Serikalini siyo kwa ajili ya walimu tu, ni mfuko kwa ajili ya watumishi ambao wanaweza kukopeshwa kupitia mfuko wa Serikali.
Kwa hiyo, elimu ambayo tunaweza kuitoa ni pamoja na sisi wenyewe Wabunge kuweza kutoa elimu hii katika Halmashauri zetu kupitia vikao vyetu vya Mabaraza ya Madiwani ili waweze kuwafahamisha pia walimu huko waliko pamoja na watumishi wengine wa kawaida kwamba wanaweza wakapata fursa hiyo kupitia Serikalini. Kwa hiyo, hili ni la kwetu tumelichukua pamoja lakini tushirikiane wote ili kuweza kufikisha ujumbe huu.
La pili, dhamira ya hizi Hifadhi za Jamii katika ujenzi wa nyumba anasema zina gharama kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba nimezungumzia suala la Watumishi Housing ambalo ni Shirika ambalo limeanzishwa na Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii na Shirika hili linatoa nyumba zake kwa gharama nafuu wala hazina gharama kubwa sana isipokuwa masharti yake yalipo ni lazima kwanza uwe na dhamana ambayo inaweza ikakusaidia katika kuweza kurudisha mkopo ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia mabenki yale ambayo yanatoa mkopo huu once ukishakubaliana na benki kwamba sasa unataka kuchukua mkopo, Shirika ndiyo linawasiliana na wewe katika hali halisi ya kutaka kujenga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba nyumba zinazojengwa ziko katika size mbalimbali, kwa hiyo bei ya nyumba na gharama yake itategemea pia na ukubwa wa nyumba. Kwa hiyo, tunapokuwa na mashirika mengi yanayofanya shughuli za ujenzi, ushindani utakuwepo lakini na ubora wa nyumba utakuwepo. Kwa hiyo, itakuwa ni juhudi ya mtu mwenyewe na kuweza kuchagua ni shirika lipi unataka wewe likujengee nyumba katika gharama ile ambayo unaweza, lakini nyumba ziko za gharama nafuu kulingana na vipato vya wananchi wetu.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na juhudi za Serikali na Wabunge wote tuliokuwepo katika Bunge lililopita katika kuhakikisha mradi huu wa Kurasini unatekelezeka; na kwa kuwa Serikali imetumia gharama kubwa katika kuwekeza mradi wa Kurasini Logistic Center; na kwa kuwa wananchi wa Temeke na Dar es Salaam kwa ujumla hususan wanawake na vijana tunatarajia kupata fursa kubwa sana za ajira katika eneo hilo la Kurasini Logistic Center; na kwa kuwa mimi kama Mjumbe wa PIC …
Je, ni lini sasa Serikali itaanza kutekeleza mradi ule? Nataka commitment ya Serikali.
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, ni bora nilieleze, mimi katika ofisi yangu katika Wizara ninayoiongoza, nimeanzisha mkakati unaoitwa fast-tracking of industrialization in Tanzania. Kuna mambo yanaendelea mimi sifurahishwi nayo, ukifuata sheria za manunuzi na mchakato wake ambazo Bunge tulipitisha shughuli hizi haziwezi kuanza. Mimi ningependa kuanza leo, wawekezaji ninao, nawajua lakini lazima nifuate sheria. Kwa hiyo, nitafuata fast-tracking na nimeamua sasa kwenda kwenye Baraza la Mawaziri, wakiniruhusu nianze kesho, nawahakikishia kabla ya mwezi wa tano nitakuwa nimeanza. Kwa hiyo, ni fast-tracking, mimi nakwenda kwa wakubwa zangu, Mawaziri wako hapa, waniruhusu naanza.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri.
Mheshimiwa Spika, kwanza, kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna ujenzi mkubwa unaoendelea katika barabara za Morogoro, Kilwa, Bagamoyo na Pungu, lakini Serikali inatoa hati pamoja na vibali vya ujenzi kwa wananchi hawa wanaojenga pembezoni mwa barabara. Inapotokea wakati wa upanuzi wa barabara wananchi hawa wanaambiwa kwamba wamefuata barabara na hawastahili kulipwa fidia.
Je, kwa nini sasa Serikali wanatoa vibali kwa wananchi wanajenga mpaka wanamaliza nyumba hasa nyumba ya ghorofa mpaka inaisha pasipo kutoa ushauri wa kitaalam kwa wananchi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wananchi wanapenda maendeleo, wanajenga majumba makubwa ya ghorofa na nyumba za kawaida pembezoni mwa barabara lakini wanakosa kuelewa matumizi sahihi ya ardhi iliyopo. Je, Serikali wako tayari kutoa elimu kwenye kata, vijiji na mitaa ili kuwaeleza wananchi wetu waelewe matumizi bora ya ardhi kuingana na mipango ya maendeleo iliyopangwa na Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, la kwanza ameuliza juu ya utolewaji wa vibali katika maeneo ambayo pengine hayakustahili kupewa vibali hivyo na baadaye yanabomolewa. Naomba kupitia Bunge lako hili Tukufu nitoe wito kwa halmashauri zote; kwa sababu tuna imani kila halmashauri inazo ramani za mipango miji katika maeneo yao; na ujenzi wowote unaoendelea unaangalia ile Mipango miji yao au Master Plan ambazo zinakuwepo zinasema nini katika maeneo hayo. Hili limekuwa likifanyika maeneo mengi na Mwanza ikiwemo.
Mheshimiwa Spika, sasa niseme kwamba, katika hili na ambalo tumekuwa tukilitolea maelekezo mara kwa mara. Pale ambapo uongozi wa Halmashauri husika utatoa kibali tofauti na matumizi ya eneo ambalo limetajwa au ambapo mtu kapewa kibali kwenda kujenga, halmashauri hiyo ijue itakuwa tayari kulipa fidia hasa kwa wale ambao waliohusika katika kupeleka vibali ambavyo vinakwenda kinyume na utaratibu kwa sababu tunazo ramani na master plan zetu. Kwa hiyo, niseme hili ni jukumu la kila Halmashauri kujiridhisha kwanza kabla ya kutoa vibali vya ujenzi kwenye maeneo. Tusingependa wananchi wapate hasara kwa kujenga halafu baadaye anabomolewa.
Mheshimiwa Spika, swali la pili amezungumzia kuhusu kutoa elimu sahihi kwa wananchi ili watambue. Niseme tu kwamba, sasa hivi tuna miji zaidi ya 13 ambayo inaandaa mipango miji yake, I mean kwa maana ya kuwa na master plan. Kabla ya master plan ile kutekelezwa lazima kunakuwa na ushirikishwaji wa jamii, ukiangalia sasa hivi katika Miji ya Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na maeneo mengine ambayo master plan zinaendelea ikiwemo na Musoma lazima kunakuwa na ushirikishwaji wa wananchi. Unapowashirikisha pale ndipo wanatakiwa na wao pia watoe mawazo yao ili kuweza kuona na watambue master plan ile inakwenda kujengeka namna gani.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi niseme elimu itaendelea kutolewa. Wizara tunavyo vipindi maalum ambavyo mara kwa mara Maafisa wetu huwa wanakwenda wanatoa na hata tunapofanya ziara tunatoa, kwa hiyo hili litaendelea kufanyika. Vile vile tuziombe, halmashauri kwa sababu unapokwenda ku- implement master plan utekelezaji wake lazima jamii iliyopo pale itambue. Pale mtu anapojenga nyumba ya kawaida wakati kwenye master plan yako inaonesha ni ghorofa, gharama ile utaibeba wewe ambaye unatoa kibali kujenga eneo ambalo tayari una Master Plan na bado unakiuka taratibu.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya Mang’ula yanafanana kabisa na yale ya Mbagala: Je, Serikali ina mpango gani wa kutaifisha Kiwanda cha Karosho (TANITA) Mbagala ili kiweze kuendelea na kazi na wananchi wa Mbagala, vijana na akina mama waweze kupata ajira kutokana na kiwanda hicho? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI): Mheshimiwa Naibu Spika, ili nisichukue muda wako mwingi sana wa Bunge hili, nirudie majibu ambayo nimeyatoa pale awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais tarehe 22 Juni, 2017 alipokuwa katika ziara Mkoa wa Pwani ameshatoa maelekezo kwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji kuhakikisha viwanda vyote ambavyo havifanyi kazi vifufuliwe na apelekewe taarifa mapema.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyozungumza hivi sasa, tayari Mheshimiwa Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango na Waziri wa Kilimo na Makatibu Wakuu wote, baada ya Bunge hili watakaa katika kikao maalum cha kuona namna gani sasa kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina kazi hii ya kuvifuatilia viwanda hivi na kuanza kuvitwaa ifanyike ili lile agizo la Mheshimiwa Rais liwe limetekelezwa.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ahsante pia Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri uliyonipa. Kwanza naipongeza Serikali kwa ujenzi wa daraja la Kigamboni ambalo litatusaidia sana wananchi wa Kigamboni kiuchumi, kiutamaduni na kijamii vilevile. Naipongeza sana Serikali kwa uamuzi wake huo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize swali langu la nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya Jimbo la Kigamboni kuhusiana na Mahakama ya Mwanzo yanafanana na yale ya Jimbo la Temeke na Mbagala. Mahakama ya Mwanzo ya Temeke ina hali mbaya sana, ni ya muda ina miaka zaidi ya 50 hakuna matengenezo yoyote. Pia Mahakama ya Mwanzo ya Mbagala, Magomeni na ile ya Buguruni zina hali mbaya sana. Lini sasa Serikali italeta mpango wa muda mfupi wa kuziboresha Mahakama zote ambazo nimezitaja hapa kwa sasa Mahakama hizi ziko katikati ya mji na hali ya majengo yale yanatia aibu, hayafanani na hadhi ya Jiji la Dar es Salaam?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, napenda kumthibitishia Mheshimiwa Mbunge kwamba wasubiri wiki mbili zinazokuja Wizara ya Katiba na Sheria itawasilisha mbele ya Bunge lako Tukufu bajeti ya mwaka 2016/2017 ambapo itaainisha ujenzi wa Mahakama za Mwanzo zitakazojengwa katika Kata mbalimbali na Mahakama za Wilaya katika Wilaya mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, niseme jambo moja, katika upande wa Mahakama za Mwanzo tunao upungufu wa asilimia 52 maana yake kuna Kata ambazo ni sawa na asilimia 52 hazina Mahakama za Mwanzo na kwa upande wa Mahakama za Wilaya ni karibia asilimia 81. Hata hivyo, nyie ni mashahidi, Mheshimiwa Rais ametoa shilingi bilioni 12.3 kwa Mahakama kwa ajili ya kujenga miundombinu ya Mahakama. Ukiangalia trend ya fedha, kwa mara ya kwanza Mahakama imepokea fedha za maendeleo kwa asilimia mia moja kwa mwaka huu wa 2015/2016. Kwa hiyo, tutajenga Mahakama zote kadri ya mpango wa ujenzi wa Mahakama utakavyoainishwa katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa posho ya shilingi 5,000 kwa kila shauri ni ndogo sana ukilinganisha na wakati uliopo kuwalipa hawa wazee. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea posho hawa wazee wa Mahakama za Mwanzo shilingi 5,000 ni ndogo sana? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wazee wanakuwa kwenye Mahakama kwa muda mrefu sana kusikiliza mashauri hayo. Je, Serikali haioni haja sasa kubadili mfumo wa malipo, badala ya kuwalipa kwa miezi mitatu au minne kwa mkupuo, wawalipe kwa mwezi hadi mwezi yaani kwa mwezi mmoja mmoja? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y. WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la kwanza la ongezeko la posho kutoka shilingi 5,000 kwanza kabisa nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba wazee hawa wanafanya kazi kubwa kuisaidia Mahakama katika kufikia maamuzi na sisi kama Serikali tunatambua mchango wao mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba siwezi kutoa commitment ya Serikali hapa kuhusiana na ongezeko la hii fedha lakini pindi bajeti itakaporuhusu basi tunaweza tukaona namna ya kuweza kusaidia katika kuboresha eneo hili la kipato kwa wazee hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo la pili la malipo ya mwezi kwa mwezi badala ya mkupuo. Kama nilivyosema katika majibu yangu ya msingi ni kwamba inafanyika hivi pia kwa ajili ya kupata kumbukumbu sahihi. Lakini vilevile pia inatokana sana na upatikanaji wa fedha kwa wakati kulingana na bajeti, tunalipokea wazo la Mheshimiwa Mbunge na Serikali tutaona namna ya kuweza kulifanyia kazi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ambayo yamenitosheleza, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza, kwa kuwa Serikali imekiri wazi kuwa kuna baadhi ya viwanda viliuzwa na kubadilishwa matumizi; na kwa kuwa sera ya Tanzania ni kutaka tupate Tanzania ya viwanda; je, Serikali inatoa tamko gani sasa kwa hao wanunuzi na wafilisi wa hivyo viwanda wasibadilishe matumizi na badala yake waendeleze viwanda kama Serikali yetu inavyotaka?
Swali la pili, kwa kuwa wanawake wa Dar es Salaam, Lindi na Mtwara walikuwa wanapata ajira kubwa sana katika viwanda vya kubangua korosho vya TANITA, leo hii viwanda hivyo vimewekwa kuwa maghala na maeneo ya kuweka matakataka tu mengine; hususan wanawake wa Mbagala, Kongowe, Temeke, Kurasini, Tandika, wote walio wengi walikuwa wanapata ajira katika kiwanda cha TANITA cha Mbagala; je, Serikali ina mpango gani wa kuvifufua viwanda vya TANITA vya kubangua korosho ili wanawake walio wengi waweze kupata ajira katika viwanda hivyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI:
Mheshimiwa Spika, kwanza kuhusiana na viwanda ambayo vimebadilisha matumizi, niseme tu kama ambavyo nimesema awali. Lengo la Taifa ni kuhakikisha kwamba viwanda vinatoa ajira. Kwa hiyo, tusingependa kusema moja kwa moja kwamba ni marufuku kubadilisha matumizi kwa sababu inawezekana biashara iliyokuwepo wakati huo, kulingana na mtaji na mashine zilizopo yawezekana haiendani na wakati wa sasa. Tunachotaka ni kwamba viwanda hivyo viendelee kufanya kazi hata kwa kuangalia bidhaa nyingine ambazo zinaweza zikazalishwa hapo na kuendelea kutoa ajira.
Mheshimiwa Spika, lakini kuna wale ambao wakati viwanda vinabinafsishwa, waliandika maandika na wakapewa masharti maalum ya kuendeleza viwanda hivyo. Wengine hawajatekeleza kabisa masharti hayo na matokeo yake, viwanda hivyo vimehujumiwa na vingine vimekuwa hata mashine zake hazipo. Tunawaambia ole wao, tutapitia kimoja hadi kimoja na wale ambao wataonekana kwamba hawajakidhi matakwa ya mikataba, naamini Serikali itachukua hatua kali inayostahili.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kiwanda ambacho ni cha TANITA, niseme tu kwamba sambamba na maelezo uliyoeleza Mheshimiwa Mbunge pia sisi tutatembelea lakini la msingi kama ambavyo nimesema awali tungehitaji kuona kwamba viwanda vyetu vinafanya kazi yenye tija na kuweza kutoa ajira kwa watu wengi zaidi ikiwemo akina mama.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo ya Geita yanafanana kabisa na yale ya Wilaya ya Kigamboni na Mbagala katika Wilaya ya Temeke, pamoja na juhudi za Serikali za kuchimba visima virefu katika Kata ya Kisarawe II Wilaya ya Kigamboni, lakini wananchi wale hawana kabisa mtandao wa maji safi na salama.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuweka mtandao wa maji safi na salama katika Wilaya ya Kigamboni na maeneo ya Mbagala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kumpongeza sana mama yangu, Mheshimiwa Mariam kwa namna ya kipekee anavyowapigania wananchi wake, lakini kubwa mimi kama Naibu Waziri nilipata kibali cha kufanya ziara katika Mkoa wa Dar es Salaam na moja ya maeneo ambayo nilifanya ziara ni eneo la Kigamboni, Temeke na maeneo mengine. Ni kweli zipo changamoto katika suala zima la maji, hususan pembezoni mwa Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara ya Maji tumechimba visima 20 pale Mpera na Kimbiji katika kuhakikisha tunatatua tatizo hili la maji, lakini visima vile bado havijafanyiwa utandazaji. Sisi kama Wizara tumeona haja sasa ya kufanya phase one ili kuhakikisha wananchi wale wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
Kwa hiyo, Mheshimiwa mama yangu Mheshimiwa Mariam, sisi kama Wizara ya Maji na kwa kuwa siyo Wizara ya ukame, tupo tayari kuhakikisha wananchi wa Kigamboni wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Mbinga Vijijini yanafanana kabisa na matatizo ya Jimbo la Mbagala katika Mkoa wa Dar es Salaam. Jimbo la Mbagala sasa hivi lina watu takribani watu 1,100,000. Idadi hii ya watu ni kubwa sana kiasi kwamba utoaji wa huduma katika jimbo hili unakuwa mgumu na miundombinu inaharibika mara kwa mara kutokana na wingi wa watu waliopo katika eneo hilo. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuligawanya Jimbo hili la Mbagala ili liweze kufikika na hata Mbunge aweze kutoa huduma zake kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza huyu ni ndugu yangu kabisa katika ukoo. Ni kweli Jimbo la Mbagala kwa idadi ya watu ni miongoni mwa majimbo yenye watu wengi ikiwemo Temeke na majimbo mengine hasa ya Dar es Salaam, lakini hivi karibu tumegawa majimbo ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, nashauri kwa vigezo vile ambavyo nimevizungumza kwenye jibu la msingi, naomba sasa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke wakae ili waweze kupendekeza, lakini wapeleke mapendekezo yao moja kwa moja Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutoa elimu bure, lakini kwa kuwa Serikali imesema wazi na inaonesha wazi kwamba mjadala na watu wenye shule binafsi kwa ajili ya kupunguza hizi ada bado haujafanyika; na kwa kuwa baadhi ya shule za msingi za binafsi zimekuwa na mtindo wa kuwalundikia watoto wadogo maswali kutoka 100 mpaka 1,200 kuja kufanya nyumbani, hali ambayo inawafanya watoto wengine waogope kwenda shule kwa kuwa hajamaliza homework na watoto wengine kufanyiwa kazi hizo na wadada wasaidizi wa nyumbani. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa walimu ambao hawatumii njia za ufundishaji zinazofuata misingi ya kazi ya ualimu na matokeo yake watoto wanafundishwa na watu wasiokuwa na taaluma ya ualimu? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa wazazi wengi wamepeleka watoto katika shule binafsi kwa malengo mbalimbali. Lengo kubwa lingine lilikuwa ni kuwaanda watoto wao kuweza kufanya vizuri katika masomo ya sekondari na chuo kikuu, lakini wazazi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamepata sintofahamu juu ya hatma ya watoto wao kukosa mikopo ya kusomea vyuo vikuu wakati maisha yana kupanda na kushuka. Je, Serikali inawaambia nini wazazi wanaosomesha watoto wao katika shule binafsi?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mariam Kisangi ambaye ni mwalimu mbobezi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali lake la kwanza kuhusu kutoridhika kwake na namna baadhi ya walimu wa shule za binafsi wanavyoendesha mambo yao, naomba tu nisisitize pamoja na kwamba shule ni za binafsi, mitaala, sheria, kanuni na miongozo ni ya umma. Kwa hiyo, hata kama tukitoa ruhusa wamiliki wa shule binafsi waweze kuendesha shule lakini ni lazima wafuate taratibu, sheria na sera iliyopo. Kwa hiyo, tunategemea kwamba kwa kutumia mfumo mpya ambao tumeuleta wa udhibiti ubora ambao kimsingi kila mtu sasa ni mdhibiti ubora kuanzia Kamati au Bodi za Shule vilevile shule zenyewe, tunategemea kwamba upungufu wowote ambao utatokea, utashughulikiwa na wadhibiti ubora ili kanuni zilizopo ziweze kufuatwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile lengo la Serikali la kuingia kwenye mchakato wa kuja na Bodi ya Kitaaluma ya Walimu ni kuhakikisha kwamba walimu wanaofundisha kwenye shule zote ikiwa ni pamoja na shule binafsi ni wale tu ambao watakuwa wana viwango vinavyohitajika lakini ni walimu ambao watakuwa wameandikishwa. Kwa hiyo, tunategemea katika mwaka huu tutakuja na Muswada ili kuhakikisha kwamba mwalimu yeyote ambaye atafundisha ni yule tu ambaye amethibitika kwamba amehitimu na ana ubora unaohitajika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili kuhusu wasiwasi wa wazazi wa wanafunzi ambao wamesoma katika shule za binafsi kupata mikopo ya kwenda katika elimu ya juu, naomba niendelee kuweka wazi jambo ambalo tumekuwa tukizungumza. Bajeti ya mikopo kwa ajili ya wanafunzi wanaoenda vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka ni shilingi bilioni 427 wakati wanafunzi ambao tunategemea kuomba mikopo kwa mwaka ni kama 70,000. Mwaka huu wa fedha unaoisha tuliweza kuchukua wanafunzi 30,000 na kwa mwaka unaokuja tunategemea kuongeza idadi hiyo kufikia wanafunzi 40,000. Katika hali ambayo fedha iliyopo inaweza kuwachukua wanafunzi kiasi fulani, ni lazima tufanye uchaguzi. Uchaguzi wetu utaangalia uwezo wa wazazi kulipa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mwanafunzi aliyesoma katika shule binafsi inachukuliwa moja kwa moja kwamba ana uwezo wa kulipa chuo kikuu. Mfano mzuri tu ni kwamba shule nyingi za binafsi nyingine ada zinafika hata shilingi milioni 30 na nyingine unakuta ada ya chini kabisa ni Sh.1,500,000 lakini University of Dar es Salaam kwenye baadhi ya masomo ni mpaka Sh.1,000,000 na Chuo Kikuu Mzumbe ni Sh.1,300,000.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachoomba ni kwamba wale watoto ambao hawana uwezo kabisa tuwape nafasi kwanza kabla hatujawachukua wale ambao historia yao inaonesha kwamba wana uwezo wa kulipa. Hata hivyo, kama itadhihirika kwamba kuna mwanafunzi ambaye alipata msaada wa kulipiwa shule za binafsi katika ngazi ya primary na secondary, tutahitaji tu ushahidi, vinginevyo naye atapata ufadhili.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Kwa kuwa Jiji la Dar es Salaam lina vivutio vingi vya utalii kama vile Daraja la Kigamboni, Hospitali ya Ocean Road, Uwanja wa Uhuru, Magomeni pale kuna Nyumba ya Mwalimu Nyerere, Karimjee Hall na Makumbusho ya Taifa. (Makofi)
Je, Serikali imejipanga vipi katika kulisaidia Jiji la Dar es Salaam ambao wameanza zoezi hilo la kutangaza vivutio vya utalii kulipa nguvu ili waweze kufanya vizuri zaidi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa Dar es Salaam nayo ni miongoni mwa mikoa ambayo ina vivutio vingi vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua hilo, ndiyo maana tulianza na mkakati wa kuhakikisha kwamba Dar es Salaam inatangazwa na tunaanzisha vituo vya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshirikiana na Mkoa kuhakikisha kwamba tunaanzisha basi maalum ambalo litakuwa linatembelea vituo vyote, kuanzia pale Makumbusho, Magomeni na maeneo mengine yote aliyoyataja kwamba yanatangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, tutaendeleza hizi jitihada ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba lile daraja letu la Kigamboni sasa linatumika kama mojawapo ya kivutio cha utalii. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, katika maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam na hasa katika Bonde la Mzinga Mbagala, maeneo ya Chanika, Msongola, Kitunda, Mwanagati, Boko, Kibamba, Bunju, Yombo, Kimbiji, Pembamnazi, na Kisarawe II; akinamama na vijana wa maeneo haya wanashughulika sana na biashara ya mbogamboga na matunda. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia akinamama wajasiriamali wa Mkoa wa Dar es Salaam waweze kupeleka bidhaa zao za mboga na matunda nje ya nchi ukizingatia tuna fursa kubwa ya uwanja wa ndege mpya mkubwa wa Kimataifa katika Mkoa wa Dar es Salaam.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kutoa mafunzo ya namna bora ya kusindika matunda hayo kwa kupitia SIDO vilevile kuona kwamba hata uuzaji wa mboga hizo unakaa katika viwango na tija. Jambo ambalo linahuzunisha kidogo ni kwamba katika Halmashauri zetu au Serikali za Vijiji tumekuwa hatutengi maeneo mazuri mahsusi kwa ajili ya hawa wakulima ili sasa hizo bidhaa zao za mashambani ziweze kukaa vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa rai kwamba, mkulima aweze kusaidiwa kuanzia shambani mpaka sokoni na pia kupewa mafunzo ya aina hiyo na hivyo kuweza kufanikisha hata inapokuja fursa ya kuweza kuuza nje ya nchi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa napenda kuipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa maboresho makubwa ya miradi ya maji katika Jiji la Dar es Salam. Kwa kweli katika maeneo ya Masaki, Oysterbey, Tabata, Segerea, masuala la maji yalikuwa magumu mno, sasa hivi Oysterbey, Masaki wanapata maji hawanunui kwenye maboza, ni jambo kubwa naipongeza sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nakiri kwamba bado kuna maeneo yana changamoto ya maji ikiwemo hilo Jimbo la Ukonga pamoja na maeneo ya Mbande, Chamanzi, Majimatitu, Mianzini, Kiburugwa, Mbagala Kuu, Kibondemaji na Kilungule, huko bado kuna matatizo ya maji.
Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi wa kuyasaidia maeneo hayo wakati tukisubiri visima vya Mpera?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe taarifa na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwamba tumepata fedha shilingi bilioni hamsini na saba kutoka Benki ya Dunia na tumeshatangaza tender tayari kwa ajili ya kuendelea kusambaza maji katika Jiji la Dar es Salaam. Kwa hiyo niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge wote kwamba Jiji la Dar es Salaam tutahakikisha tunakamilisha maji yanapatikana katika maeneo yote.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya Kilindi yanafanana kabisa na yale matatizo ya shule za Mbagala. Niishukuru Serikali kwa kujenga madarasa mengi katika shule ya Msingi Majimatitu na Mbande. Shule hizi zilikuwa zinaandikisha wanafunzi 6,000 kila mwaka, kwa kweli watoto hawa ni wengi. Je, Serikali haioni haja ya kuandaa shule ya sekondari za high school katika maeneo ya Chamazi, Mbande, Nzasa na Charambe katika Jimbo la Mbagala ili watoto wanaomaliza sekondari waende kwenye high school maeneo hayo hayo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, kwa halmashauri ambazo zinahitaji kuanzisha Shule za Kitado cha Tano na Sita, utaratibu ni kwamba wao wenyewe wajipange na wajenge miundombinu husika baadaye waombe kibali kutoka Wizara ya Elimu na sisi tutaangalia na tukijiridhisha kwamba inafaa hatutakataa kuzisajili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niendelee kusema kwamba kwa sasa kama kuna changamoto ya wanafunzi wa kutoka Mbagala kuweza kupata elimu ya kidato cha tano na sita karibu bado fursa zipo katika shule nyingine za kitaifa kwa sababu kimsingi kidato cha tano na sita zote ni shule za Kitaifa.
MHE. MARIAM KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na juhudi za Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza Irani ya Chama cha Mapinduzi, kujenga reli ya kisasa ya Standard Gauge ambayo naipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi; matatizo ya vituo vidogo vidogo pia yanawapata wakazi wa Dar es Salaam katika Treni yao ya station kwenda Pugu. Hakuna vituo vidogo vya kushushia abiria katika treni hiyo inayotoka station pale mjini kwenda Pugu. Treni inasimama tu na watu wanashuka shuka tu. Je Serikali ina mpango gani wa kuboresha vituo vya treni hiyo ambayo ni muhimu sana kwa wakazi wa Pugu, Ukonga, Kiwalani, Kipawa, Yombo na Vituka?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO – (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana na nimpongeze Mheshimiwa Mariam Kisangi kwa jinsi anavyofuatilia sana ile reli ambayo imebatizwa jina la Reli ya Mwakyembe. Ni reli muhimu sana kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na imekuwa ikitoa huduma mbalimbali za kusaidia usafiri katika Jiji la Dar es Salaam.
Mheshimiwa Naibu Spika, vituo vilivyopangwa kwa ajili ya kuhudumia reli hiyo ambayo inaitwa kwa jina la Mwakyembe ni vile ambavyo vilikuwa vinatumika kwenye reli ile ya toka mwanzo; na hatuna mpango mpaka sasa hivi wa kubadilisha. Nawaomba Watanzania na wakazi hasa wa Dar es Salaam wasishuke kama treni haijasimama, ni lazima waendelee kuheshimu kwamba treni ina vituo vyake maalum na ikisimama ndio mtu ashuke au kupanda, wasipandie njiani kwa sababu wanaweza kupata ajali.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Pamoja na juhudi za Serikali za kuweka barabara nyingi za kupunguza msongamano katika Jiji la Dar es Salaam hatua ambayo naipongeza, lakini ninalo swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Nzasa - Kilungule kuungana na Buza ni muhimu sana kwa wakazi wa Mbagala katika kuondoa msongamano. Je, Serikali lini itaanza ujenzi wa barabara hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa amekuwa akifuatilia barabara nyingi lakini nimhakikishie kwamba katika harakati za kukwamua msongamano katika Jiji la Dar es Salaam barabara 12 zimekamilika. Ziko barabara 10 ambazo mpaka kufikia mwezi Aprili tunaendelea nazo lakini ziko barabara nyingine ambazo tutazishughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba Serikali iko committed kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linafunguka. Nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge hii barabara anayoizungumza kutoka Nzasa – Kilungule - Jeti Kona itashughulikiwa na mradi wa DMDP. Nitajaribu kufuatilia baada ya mkutano wa leo ili nione hatua ilivyo na nitampa mrejesho lakini niombe tu tuendelee kushirikiana na kupeana taarifa kwa sababu lengo la Serikali ni kurekebisha maeneo mbalimbali ili yaweze kupitika vizuri.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na juhudi za Serikali ya Chama cha Mapinduzi katika kufanya maboresho ya barabara mbalimbali katika Jiji la Dar es Salaam jambo ambalo tunaipongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi, kwa kuwa barabara ya Kilwa maeneo ya Mbagala Rangi Tatu - Kokoto kuelekea Kongowe Mwisho kumekuwa na ufinyu wa barabara na kusababisha foleni kubwa ya magari muda wa asubuhi na jioni. Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza upana wa barabara na kuweka vituo vya mabasi maeneo ya Mzinga na Kongowe mwisho ili kuondoa kero kwa wananchi wanaokwenda Kongowe, Tuwangoma, Kigamboni na wale waendao Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza pongezi nyingi alizozitoa nazipokea lakini niseme tu kwamba nampongeza kwa kufuatilia barabara hii na barabara zingine katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu mwanzo kwamba tunao mpango wa kuitazama kwa upana barabara hii na mmeshuhudia tunaendelea kuweka maboresho mbalimbali ili kuweza kumudu foleni katika Jiji la Dar es Salaam, kwa hiyo, uvute subira tunalifanyia kazi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya ukosefu wa Maafisa Ugani inawakumba wananchi wa Jimbo la Ukonga katika Wilaya ya Ilala katika kata za Kitunda, Vigewe, Majowe na Mzinga. Wananchi wa eneo hilo ni wakulima wa mbogamboga na matunda lakini kuna Afisa Ugani mmoja anahudumia kata tatu, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza Maafisa Ugani katika Jimbo la Ukonga na Wilaya ya Ilala kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kuna upungufu wa Maafisa Ugani nchini, na kama nilivyojibu kwenye swali la msingi ni kwamba kwa maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi tunahitaji kuongeza Maafisa Ugani ambapo tukiwafikia hawa ambao tumepanga kuwaongeza kupitia maelekezo ya Ilani tunaamini tutakuwa na Maafisa Ugani wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi sasa Serikali ina kibali cha kuajiri watumishi takribani 52,000 na mpaka sasa hivi hatujafikia hata 20,000 katika kuajiri, kibali ambacho kitatoka hivi karibuni labda mwezi wa pili au wa tatu, tutaajiri Maafisa Ugani wa kutosha kupunguza tatizo lililopo. Naamini tutakapoajiri hao kabla ya mwezi wa sita na kata hizo ambazo umezitaja tutazipatia Maafisa Ugani. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi ili nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo kubwa la barabara hiyo ambayo inatoka Vianzi kwenda Marogoro mpaka Tundisongani ni daraja lililopo pale Tundisongani. Daraja hilo imekuwa ni shida mvua zinaponyesha wananchi wa Tundisongani na Wilaya ya Mkuranga wanakosa mawasiliano kabisa, hali ambayo imefanya Wabunge wa sehemu zote mbili Mkuranga na Kigamboni wamekaa pamoja lakini mpaka leo hakuna matunda yoyote juu ya barabara hii.

Je, Serikali sasa ina mpango gani wa kuboresha angalau lile daraja ili mvua zitakaponyesha wananchi wa Kigamboni na Mkuranga waweze kuwa na mawasiliano?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, naomba nimjibu Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wangu wa Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ambavyo ameuliza swali hili kwa uchungu na maeneo haya yote muhimu, kule Mkuranga kuna Naibu Waziri mwenzangu na kule Kigamboni Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, naomba niwaelekeze TARURA, Mkoa wa Dar es Salaam walifanyie tathmini eneo hili na leo kabla ya saa saba nipate majibu nini kinaweza kufanyika ili kuondoa kero hii ya wananchi katika eneo hili. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Mbagala limekuwa na ongezeko kubwa la watu hali ambayo inachangia sana kuwa na ongezeko kubwa la uhalifu lakini mazingira ya Kituo cha Polisi Mbagala Kizuiani ni mabaya sana pamoja na makazi ya polisi. Pamoja na hayo, Serikali imeeleza wazi kwamba utaratibu wa kujenga kituo hiki kwa sasa haupo. Je, Serikali ina mkakati gani basi wa kuwaboreshea angalau makazi ya askari wale jamani, hali mbaya, nyumba zile haziendani na eneo lile? Mbagala sasa imekua, mabasi ya mwendokasi yanakuja, zile nyumba za Polisi pale zinatisha. Je, Serikali mna mkakati gani wa kufanya angalau maboresho ya eneo lile?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Dar es Salaam, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya uchakavu wa nyumba za askari katika eneo la Mbagala Kizuiani tunaifahamu. Nichukue fursa hii kumpongeza kwa mara nyingine tena Mheshimiwa Rais kwa kuliona hilo na kutupatia fedha ambazo tunatarajia kujenga takriban nyumba 400 nchi nzima. Katika maeneo ambayo nyumba hizo zitajengwa ni Kanda Maalum ya Dar es Salaam ikiwemo Mkoa wa Kipolisi wa Temeke. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge na nimpongeze kwa concern na huruma aliyokuwa nayo kwa askari wetu, Serikali inalitambua na tunaendelea kulitatua hatua kwa hatua.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na niweze kuuliza wali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo yanayowapata watu Kibaha yanafanana na watu wa kigamboni

Je Serikali ina mpango gani wa kukamilisha mradi wa visima vya Kimbiji na Mpera ili wananchi wa Kigamboni, Tuangoma, Chamazi na Mbagala waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya lakini kikubwa katika kuhakisha tunatatua tatizo la maji katika Mkoa wa Dar es Salaam. Wizara yetu ya maji kupitia Wizara ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira DAWASA imechimba visima zaidi ya 20 Mpera na Kimbiji. Sasa agizo la Mheshimiwa Waziri nikuhakisha visima vitano wanatangaza tenda mkandarasi ampatikane ili wananchi wa maeneo ya Kigamboni na Mbagala waweze kupata maji safi, salama na ya kutosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tupo katika hatua hiyo tunataka mkandarasi akapopatikana kazi ianze mara moja na wananchi hawa waweze kupata maji.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo nimeridhika nayo na napenda nitoe pongezi kwa Mkuu wa Gereza la Segerea kwa kutekeleza hayo yote ambayo Mheshimiwa Naibu Waziri ameyasema kupeleka watoto kwenye Nursery na kuwarudisha gerezani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo yanayowapata watoto magerezani yanatokana na makosa ya mama zao; na kwa kuwa zipo adhabu nyingi wanazoweza kupewa mahabusu au wafungwa wenye makosa yasiyo ya kijinai; kwa nini Serikali isitoe adhabu ya kifungo cha nje kwa akina mama wenye watoto wadogo ili waweze kuwalea watoto wao vizuri uraiani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa tatizo kubwa la akina mama waliopo katika gereza la Segerea na magereza mengine yote ni kutokana na kesi zao kutokupelekwa mahakamani kwa wakati, jambo ambalo linawafanya akina mama wale wakae muda mrefu mahabusu bila ya kutambua hatima yao: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa wanapeleka kesi mahakamani kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI (K.n.y WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO): Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, naomba kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mariam Kisangi kwa kujali akina mama na watoto hawa. Nachukua fursa hii kumhakikishia Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba huu uchungu ambao aliokuwa nao yeye ni sawa sawa na uchungu ambao Serikali tunao. Ndiyo maana katika kushughulika na kesi hizi za hao akina mama wenye watoto, huwa Serikali inatoa kipaumbele maalum, hata mahakama hufanya hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo basi, nimhakikishie kwamba hata inapokuja katika ule utaratibu ambao tunautumia kwa ajili ya kutoa kifungo cha nje na mipango mingine mbalimbali ya kupunguza mahabusu na kusamehe wafungwa, akina mama wenye watoto huwa wanapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili; vilevile katika suala la kuhakikisha kwamba tunaharakisha upelelezi na kesi hizi zinamalizika, tuna utaratibu wa kuharakisha kesi ziweze kwenda kwa haraka. Tunaweza kutumia njia mbalimbali kufanya hivyo, tunafanya ziara kwenye magereza kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, lakini tunapobaini kwamba kuna kesi ambazo hazihitaji kukaa muda mrefu bila kuchunguzwa, hasa hizi zinazohusu akina mama na watoto tunakuwa tunazipa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimalizie kwa kumhakikishia Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba Serikali inaliangalia sana kwa karibu suala hili na haipendelei kuona watoto wadogo wakikaa magerezani kwa muda mrefu.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa matatizo ya daraja la Segerea ni ya muda mrefu sana na kila wakati liko katika upembuzi yakinifu; na kwa kuwa Serikali sasa inataka kufanya tena usanifu kupitia TARURA; mimi nauliza swali: Je, kwa nini TARURA sasa wasianze kujenga hilo daraja la Segerea badala ya kuanza tena upembuzi yakinifu ili kuwasaidia wananchi wa Segerea ambao wanapata shida sana kutokana na ukosefu wa daraja lile?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa matatizo wanayopata wananchi wa Segerea yanafanana kabisa na yale wanayowapata watu wa Jangwani pale maeneo ya Magomeni: Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha daraja la Jangwani ili kuondoa matatizo ya kufunga barabara ile wakati wa mvua nyingi kila wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi maswali yote mawili yanafanana. Adha ambayo tunaipata kutokana na lile daraja ambalo mto unahama, lakini na swali lake la pili kuhusiana na daraja la Jangwani ambalo linajaa maji kila muda, naomba Mheshimiwa Mbunge arejee katika siku moja ambayo nilijibu hapa, kwamba jumla ya shilingi bilioni 260 zimetengwa kwa ajili ya kuanza usanifu na kuhakikisha kwamba tunapata suluhu ya kudumu kuhusiana na Mto Msimbazi. Pia akubaliane name, kama ambavyo tunaweza tukafanya makosa tukajenga hilo daraja, baada ya muda likawa linaendelea kujaa, ndiyo maana tumemwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira kama ambavyo nimetoa majibu katika jibu langu la msingi, kwamba ni vizuri tukafanya usanifu wa kina kujua hasa tatizo ili ujenzi ukikamilika tuwe tumepata suluhu ya kudumu.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matatizo wanayoyapata wananchi wa Nkenge pia yanawapata wananchi wa Kigamboni. Je, Serikali ina mkakati gani mahususi wa kuhakikisha chanzo cha maji cha visima vya Kimbiji na Mpera kinakamilika ili wananchi wa Kigamboni, Mbagala, Chamazi, Temeke na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwa ufupi, hii ni Serikali ya Awamu ya Tano ikiahidi inatekeleza. Tumeshachimba visima zaidi ya 20 katika Kimbiji na Mpera na mpaka sasa tumeshamkabishi Mkandarasi kwa ajili ya uanzaji wa mradi wa Kigamboni ili wananchi wa Kigamboni waweze kupata huduma ya haraka. Kikubwa ambacho tunachotaka kumsisitiza Mkandarasi wa mradi ule aweze kufanyakazi kwa mujibu wa mkataba ili uweze kukamilika kwa wakati na wananchi wa Kigamboni na maeneo mengine waweze kupata huduma ya maji. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana Naibu Waziri kwa majibu mazuri, kwa kuwa Wilaya ya Mbinga ni Walaya ambao iko pembezoni sana na wananchi wake wnachangamoto nyingi sana pamoja na majibu mazuri bado kuna tatizo kubwa la kuwa gari la wagonjwa katika hospitali hiyo.

Je, Serikali ina mkakati saa wa kuhakikisha wanawapelekea gari la wagonjwa katika hospitali ya Wilaya ya Mbinga?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa matatizo ya hospitali haya yanaendana kabisa na hali ya hospitali Zakiemu Mbagala.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongezea hospitali ya Zakiem Mbagala ambayo imezidiwa wagonjwa ni wengi lakini majengo ni machache na wahudumu ni wachache, nakushukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kusimamia Mkoa wa Dar es Salama, pia ni Tanzania kwa ujumla wake hususan jambo la afya ya akinamama na watoto na wazee.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba unapokua unajenga kuboresha huduma za afya ni muhimu kuwa na gari la wagonjwa ili inapokea dharura iwe ni rahisi kumuwaisha katika huduma nyingine ya ziara ya pale alipokuwa, lakini naomba nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri kwa uwezo wa Serikali uwezo ukipatikana basi eneo hilo la Mheshimiwa Raphaeri Mapunda litapata gari la wagonjwa kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameulizia hapa.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme tu kwamba mpango wa Serikali ni kuboresha huduma zaafya na kupeleka hufuma karibu na wananchi, tumepokea hoja Mheshimiwa Mbunge bahati nzuri tunaenda kwenye mwaka wa bajeti 2020/2021 basi tuangalie uwezekano wa kupatikana ili tuweze kupeleka fedha katika eneo hili kuboresha huduma ya pale Mbagala pia Mkoa wa Dar es Salam kwa ujumla wake. Na natambua kwamba wnanchi wangu wa Jimbo la Ukonga pia wanaweza wakapata huduma pale Mbagala Zakiemu, ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwanza kwa ridhaa yako naomba niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa utekelezaji wake wa Ilani wa ujenzi wa Mahakama za Wilaya nchini Tanzania. Tunashuhudia Mahakama mbalimbali za Wilaya zikizinduliwa zikiwemo za Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niulize swali la nyongeza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuboresha Mahakama za Mwanzo za Kariakoo, Magomeni, Ilala, Temeke na Mbagala?
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam ni mahali pa watu wengi, mashauri ni mengi na kioo cha Taifa na cha Wizara yangu. Ni wajibu wetu kuhakikisha kwamba Mahakama hizi zinakuwa na sura nzuri na zinafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha ina maana tatu. Kwanza ni kufanya ukarabati wa kuhakikisha kwamba Mahakama hizi ziko katika hali nzuri. Kuboresha pia kunamaanisha kwamba, Mahakama hizi zipewe teknolojia ya kisasa hasa katika uwezo wa kuandikisha Mahakama na kuweza kusikiliza kesi hizi. Tunaingiza utaratibu wa teknolojia ya kuweza kusikilizwa kesi hizi na kuandikisha na Mahakama za Dar es Salaam zinapewa kipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika mkakati wetu wa kutumia magari ya kusikiliza kesi, tumeanza utaratibu huo na kufanya majaribio katika Mkoa wa Dar es Salaam. Katika uboreshaji wa aina hii mwanzo itakuwa ni Dar es Salaam kabla hatujapeleka sehemu nyingine zaidi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali la kwanza napenda niipongeze Serikali kwa kusikia kilio chetu Wabunge na kilio cha wananchi sasa wameanza kufanya tathmini ya barabara ya Kirwa Road kutoka eneo la Mbagala Kokoto kwenda Kongowe, eneo ambalo lilikuwa na msongamano mkubwa wa magari naiopongeza sana Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kusikia kilio chetu Wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa eneo la Mbagala Kokoto mpaka Kongowe wameanza sasa kufanyiwa tathmini ya maeneo yao na kuwekewa alama ya X. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba wananchi hawa watalipwa kwa wakati ili kupisha zoezi hilo la upanuzi wa barabara ya Kirwa Road. Ahsante sana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mbunge najua tumezungumza miradi mingi sana na anafahamu juhudi ambazo zinafanyika ndiyo maana anatoa pongezi, kwa niaba ya Serikali nazipokea pongezi hizo.

Mhehimiwa Mwenyekiti, nikuhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tumejipanga kuboresha barabara hii ili kuweza kupunguza pia msongamano ambao unajitokeza na usumbufu ambao unajitokeza, nami eneo hili nimelitembelea. Vile vile niwahakikishie tu wananchi hawa kwamba tumejipanga vizuri kwa sababu hata kwenye bajeti tuna fedha kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya maeneo haya na kulipa fidia, tutawalipa mara moja wakati tukiendelea kuboresha mradi huu. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika ahsante sana kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa takwimu zinaonyesha wazi kwamba matatizo ya magonjwa ya akili yanaongezeka yanayotokana na msongo wa mawazo pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya lakini hospitali maalum ya magonjwa hayo ni Milembe pakee. Je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga hospitali kubwa ya magonjwa ya akili katika eneo hilo la Chamazi ili kusaidia wananchi wa Kanda ya Pwani waweze kupata matibabu lakini pia waweze kupata eneo ambalo wataendelea kufanya kazi mbalimbali pale za mifugo ili kujikimu kuliko vile walivyo watoto wetu walioharibiwa na madawa ya kulevya, kwamba hawana ajira na wanahangaika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa Halmashauri ya Temeke imekuwa na tatizo kubwa la ardhi, na kwa kuwa idadi ya wagonjwa inaongezeka siku hadi siku katika Hospitali ya Zakiemu. Je, Serikali haioni haja sasa ya kushirikiana na Halmashauri ya Temeke ili kujenga hospitali pale katika eneo la Chamanzi Muhimbili ili iweze kuwasaidia wananchi wanaotoka Mbande, Chamazi, Mbagala, Maji Matitu pia na hata wale wa Wilaya ya Mkuranga?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YAJAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Kisangi Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli sasa hivi dunia imeweka msisitizo katika afya ya akili, na kwa sababu na sisi kama Serikali na dunia kwa ujumla inaona kwamba tatizo la afya ya akili linazidi kuongezeka kwa kasi sana na linahitaji msukumo na mtazamo wa aina ya pekee kabisa katika kutatua changamoto hizi.

Mheshimiwa Spika, ni kweli tuna hospitali moja kubwa ya Mirembe; na sisi kama Serikali mtazamo wetu wa mbele ni kuhakikisha kwamba, especially katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili badala ya kuwa na vitengo vidogo vidogo lengo letu sisi ni kwamba kila kitengo kuwa ni taasisi. Tumeanza na taasisi ya magonjwa ya moyo tumekwenda taasisi ya masuala ya mifupa; na lengo letu ni kwamba hata baadaye tuwe na taasisi ya magonjwa ya afya ya akili.

Mheshimiwa Spika, katika kujibu swali lake la pili; ameongelea kwa nini Serikali isione umuhimu wa kujenga hospitali ya ziada katika eneo hili la Chamanzi. Halmashauri ya Manispaa ya Temeke na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zote ni taasisi za umma. Sisi kama Wizara hatujapokea ombi lolote kutoka halmashauri ya Manispaa ya Temeke. Pindi tutakapopokea ombi hilo tutalijadili na kulifanyia uamuzi kwa sababu tunaamini eneo lote hili ni kwa ajili ya utoaji huduma ya afya, na kwa sababu tuna eneo kubwa hatuoni sababu kwa nini tusiongeze wigo wa utoaji huduma, especially katika eneo la Temeke ambapo kuna changamoto ya ardhi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kuuliza swali langu kwanza kwa ruhusa yako napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali yake kwa kutuletea ndege mpya aina ya Dreamliner Na.787 ambayo imefanya ndege zetu sasa kuwa saba (7). Sambamba na hilo, pia uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja katika Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema maneno hayo, sasa naomba niulize swali langu la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali imejipanga vipi katika kuhakikisha inaleta wawekezaji wengi na kuendeleza miradi mingi ya uwekezaji kwenye Jiji la Dar es Salaam katika maeneo ya Kigamboni ambayo yana ardhi ya kutosha, Ilala maeneo ya Chanika lakini pia Kinondoni katika maeneo ya Mabwepande? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa niseme kwamba tunashukuru kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya Mheshimiwa Rais kwa pongezi alizozitoa kwa jitihada ambazo Mheshimiwa Rais amezifanya mpaka sasa katika kuhakikisha kwamba tunaongeza miundombinu ya usafirishaji lakini vilevile miundombinu mingine kama vile ya mawasiliano pamoja na ya ujenzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa maeneo ya uwekezaji nipende tu kumhakikishia Mheshimiwa Mariam Kisangi kwamba kupitia Wizara Ardhi tayari maeneo ya uwekezaji yameshatengwa kwa Dar es Salaam Kigamboni na tutaendelea kufanya hivyo katika maeneo mengine ya Mkoa wa Dar es Salaam na tutaona ni kwa namna gani tunaendelea kuhakikisha kwamba tunapeleka Wawekezaji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano kwa Kigamboni tulishapata Wawekezaji hao wanaojenga Mradi huu wa Nyerere Hydro, wamekuwa wana nia ya kujenga Industrial packs pamoja na vyuo vya kiufundi na tayari tumeshawapeleka Kigamboni waweze kuangalia na endapo wataridhika na maeneo hayo, basi kwa hakika wataweza kuwekeza kwa upande wa Kigamboni.

Pia niendelee kumuhakikishia pia Mheshimiwa Mbunge wapo Wawekezaji wengine katika viwanda vya nguo kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara watakuja tarehe 8 Novemba, kutoka Italy na kwenyewe pia tutafanya hivyo kuona ni kwa namna gani tunawapeleka wakaangalie na kuendelea kuwashawishi ili waweze kuwekeza katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee niendee kutoa rai kwa Wizara ya Ardhi pamoja na Mamlaka zetu za Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya uwekezaji ambayo yana miundombinu wezeshi ili na sisi iwe kazi rahisi kuvutia uwekezaji, lakini wanapokuja basi wapate maeneo ambayo ni tayari ambayo watatumia muda mfupi katika kuanzisha uwekezaji wao, nakushukuru.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa matumizi ya gesi asilia siyo kwa viwandani tu, bali hata majumbani:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba unapeleka gesi asilia kwenye majumba katika maeneo ya Ubungo, Manzese, Vingunguti, Mbagala, Gongolamboto, Tandika, Mwananyamala na Tandale; maeneo ambayo yana wakazi wengi ili kuwasaidia akina mama kupata nishati ya gesi kwa bei nafuu; pia katika kupunguza gharama za mkaa na uhifadhi wa mazingira?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Mheshimiwa Mariam Kisangi anapozungumzia masuala ya usambazaji wa gesi majumbani, anamzungumzia mwanamke ambaye ndio mtumiaji mkubwa wa rasilimali ya gesi majumbani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimtaarifu kwamba ni mkakati wa Serikali kwamba kwanza mpaka sasa zaidi ya kaya 500 zimeshasambaziwa gesi asilia katika Mikoa ya Dar es Salaam na Mtwara. Kazi inayoendelea sasa kwa mwaka 2019/2020 tuna matarajio ya kaya zaidi ya 1,000 kuzifikia na kazi inaendelea na mpaka sasa vifaa vyote vya kuunganishia yakiwemo mabomba, mita za matumizi ya gesi vimeshafika na vimeshafungwa na vipo katika nyakati za majaribio.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, maeneo aliyoyataja ikiwemo Tandale, Mwananyamala, Mbagala na maeneo ambayo Mbunge anawakilisha, nataka nimthibitishie kwamba Serikali imedhamiria na ndiyo maana imetenga katika mpango mzima matumizi ya gesi, kiasi cha futi za ujazo trilioni 0.7 kwa ajili ya matumizi ya majumbani ili kuokoa mazingira pia. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tatizo la daraja linawakumba pia wananchi wa Mbagala – Nzasa – Kilungule
- Mwanagati - Buza. Eneo hilo maji yanapojaa katika Mto Mzinga wananchi wanashindwa kuvuka na hata watoto wanashindwa kwenda shuleni mpaka wananchi wamejijengea daraja lao la miti. Je, Serikali lini itajenga daraja hilo ili kuwasaidia wananchi hao?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Kisangi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli, ukiangalia maeneo ya Mbagala yote yalikuwa na changamoto kubwa sana na ndiyo maana Serikali tumeanza awamu kwa awamu. Mheshimiwa Kisangi unakumbuka kulikuwa na changamoto kubwa kati watu wa Mbagala Kuu na Kibada kupitia Twangoma. Serikali imekalisha ujenzi wa daraja kubwa maeneo yale kwa mabilioni ya fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, nafahamu changamoto iliyopo katika Mto Mzinga na mimi mwenyewe nimeshatumia barabara ile kwa kutumia pikipiki mara kadhaa, nalifahamu eneo hilo. Nimhakikishie kwamba ni jukumu la Serikali eneo lote la Jiji la Dar es Salam miundombinu ambayo ilikuwa ina changamoto kubwa kupitia mpango wa awamu kwa awamu maeneo yote tutaweza kuyaunganisha ili wananchi waweze kusafiri kutoka eneo moja mpaka eneo lingine.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuja na majibu mazuri sana yenye faraja kwa wakazi wa Dar es Salaam waliokuwa wakilazwa katika Hospitali za Amana, Temeke na Mwananyamala sasa mashine za kufulia zinapatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nampongeza sana kwa majibu hayo mazuri, ninayo maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mashine za kufulia katika hospitali hizo zinakosa pia mashine nyinginezo za vipimo zikiwemo mashine za MRI, mashine za kupima ubongo na mashine nyingine hali ambayo inawalazimu wagonjwa kufuata huduma hiyo ya vipimo katika Hospitali ya Muhimbili. Wanapofika katika Hospitali ya Muhimbili, vipimo hivyo hupewa kwa gharama mara mbili ya ile bei ya kawaida ya Hospitali ya wagonjwa waliopo Muhimbili. Je, Serikali kwa nini inatoa gharama tofauti wakati hospitali hizi zote ni za Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwanza naipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza Ilani yake ya Chama kwa kujenga Hospitali za Wilaya 67 na zimepewa fedha karibia bilioni 1.5 na milioni 500 wameongezewa ikiwemo Kigamboni katika Jiji la Dar es salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuhakikisha hizo hospitali 67 ambazo zitajengwa kuwa na mashine na vipimo vyote vinavyostahili katika kila hospitali.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es salaam amekuwa ni Mbunge wa mfano katika Wabunge wa Viti Maalum katika ufuatiliaji wa mambo mbalimbali yanayotokea katika Mkoa wa Dar es salaam na sisi kama mmoja wa Wabunge wa Mkoa wa Dar es Salaam nampongeza sana Mheshimiwa Mariam Kisangi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba sasa hivi Serikali inafanya maboresho makubwa katika Sekta ya Afya na tumeona kwamba kuna uhitaji wa kuboresha na kupanua wigo wa utoaji wa huduma za afya hususan vile vipimo mahsusi kama uwepo wa MRI, CT Scan na vipimo vingine mahsusi ambavyo hapo awali vilikuwa vinapatikana katika Hospitali za Rufaa za Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hivyo, kupitia mpango wetu wa sasa hivi wa kuboresha huduma na kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za uchunguzi wa magonjwa Serikali imedhamiria kupanua wigo kuhakikisha kwamba vipimo kama CT Scan na MRI zitaanza kupatikana katika baadhi ya Hospitali za Rufaa za Mikoa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ameuliza kwa nini baadhi ya vipimo vinachajiwa mara mbili zaidi ya zile gharama halisi ambazo zipo pale. katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tumeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba rufaa inazingatiwa na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ni Hospitali ya Taifa, maana yake ni kwamba unapokwenda pale unahakikisha kwamba umetoka katika ngazi ya zahanati, kituo cha afya, Hospitali ya Wilaya, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, umekwenda Hospitali ya Kanda Mloganzila wameshindwa pale sasa unakwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kumekuwa na baadhi ya watu ambao katika magonjwa ya kawaida ambayo yangeweza kutibiwa katika maeneo mengine wanakwenda moja kwa moja katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili. Ili sasa kuweka mfumo wa rufaa ukae vizuri, mtu ambaye amekwenda kwa mfumo wa rufaa gharama zake zinakuwa chini, yule ambaye amekwenda kwa mfumo nje ya rufaa, yule anahesabika kwamba ni mgonjwa amekwenda kama mgonjwa binafsi na gharama zake mara nyingi zinakuwa zipo juu. Lengo ni kuhakikisha kwamba mfumo wa rufaa umezingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ameuliza ni nini mkakati wa Serikali kuelekea katika ujenzi huu ambao tumejenga hospitali za Rufaa za Wilaya 67 tuna mpango gani wa kuhakikisha kwamba inakuwa na vifaa vya kutosha. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kusudio la Serikali ni kwamba pale miundombinu ya hospitali hizi za Wilaya zitakapokuwa zinakamilika na sisi kama Wizara pamoja na kushirikiana na Ofisi ya Rais – TAMISEMI tumeshaanza maandalizi ya kuhakikisha kwamba hospitali hizi zitakapokamilika vifaa vitapatikana ikiwa ni pamoja na rasilimali watu. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza; pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri kwamba sasa Serikali iko tayari kutuletea mashine za CT-SCAN na MRI katika Hospitali za Mikoa, ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini bado tuna changamoto kubwa, katika Hospitali zetu za Mkoa wa Dar es Salaam hatuna mashine za kufulia nguo, hali ambayo inasababisha tuishiwe mashuka mara kwa mara, kwa sababu mashuka yanafuliwa katika Hospitali ya Muhimbili ndiyo yaletwe Temeke, Je, Serikali ina Mpango gani sasa wa kutuletea mashine za kufulia nguo katika Hospitali zetu za Temeke, Mwananyamala na Amana. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Mariam Kisangi hasa kwa jinsi anavyofuatilia huduma za afya hasa, afya ya mama ya mtoto kwa Wanawake wa Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mashine za kufua nguo kama nilivyoeleza wakati tunawasilisha Bajeti yetu, tumezipokea Hospitali za Rufaa za Mikoa kuanzia tarehe 1 Julai, 2018 na tumejipanga kama Wizara kuhakikisha tunaboresha huduma zote ikiwemo miundombinu pamoja na kufunga na kununua mashine za kufulia katika Hospitali zetu zote za Rufaa za Mikoa sambasamba na kuweka Madaktari bingwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo lini, naomba nilichukue halafu tutatoa majibu ndani ya Bunge hili, lini tutaanza kuweka vifaa hivyo lakini kama nilivyoeleza tumeshaanza kuondoa vifaa vya kuweka kwa ajili ya Hospitali zetu za Rufaa za Mikoa.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kumekuwa na ongezeko la watoto wenye mahitaji maalum; na kwa kuwa shule ambazo zinapokea watoto wenye mahitaji maalum kama Majimatitu Maalum, Mtoni Maalum, Salvation Army, Wailesi Maalum, Uhuru Mchanganyiko, Mgulani Inclusive na Sinza Maalum zinakuwa hazitoshelezi mahitaji, watoto wale bado wanabaki majumbani:-

Je, Serikali haioni haja sasa ya kuongeza katika shule zote za msingi vitengo vya watoto wenye mahitaji maalum ili nao waweze kupata elimu katika maeneo yao wanayotoka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mariam Kisangi kwa mawazo haya mazuri ya kuunga mkono Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Naomba nitoe taarifa kwamba sasa hivi baada ya kuona kwamba unapotenga shule maalum ni kama wale watoto unawatenga, wanakuwa isolated sana katika mazingira yao. Kwa hiyo, sasa hivi tumekuja na kitu kinaitwa Elimu Jumuishi. Ndiyo maana tumetoa maelekezo nchi nzima, tunapojenga miundombinu mipya, hata kama ni Kituo cha Afya izingatie mahitaji maalum, kama ni shule zetu za msingi na sekondari ziwe na mahitaji maalum.

Mheshimiwa Spika, ukienda kule Buhangizo utawakuta, Chaibushi utakuwata, Kilosa Sekondari utawakuta. Kwa hiyo, hiyo imeshaanza. Cha muhimu, ametoa warning, tuendelee kuzingatia. Tumeendelea kuwaeleza wanafunzi wa kawaida kwamba hawa watoto wenye mahitaji maalum ni wenzao, wawapokee, wawakubali, wawasaidie na wasome kwa pamoja pale inapowezekana. Hilo kwa kweli linafanyika. Cha muhimu hapa tutaongeza nguvu zaidi na kwa maoni ya Mheshimiwa Mbunge tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Kwa kuwa wananchi wa Rufiji wamekuwa na shida kubwa kupata Chuo cha VETA rufiji, pamoja na juhudu za Mbunge wao kupambana kutafuta jinsi gani ya kupata Chuo cha VETA ndio sababu akaona hata kuna haja kubadilisha vyuo vya FDC labda wanafunzi wa Rufiji waweze kupata elimu hiyo ya VETA, na Kwa kuwa Serikali sasa imeshatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa VETA - Rufiji ni jambo la shukrani na pongezi sana kwa Serikali, je, Serikali sasa ni lini ujenzi huo utaanza rasmi.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna Chuo kikubwa sana cha VETA Kipawa, chuo hiki ni kikubwa mno, lakini hatujawahi kuona matangazo mbalimbali juu ya elimu inayotelewa hapo au ni mwaka gani wa mafunzo ambao unaanza lini na lini wanafunzi waweze kuhamasika kujiunga na Chuo cha VETA Kipawa?

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kukitangaza hiki Chuo cha VETA Kipawa ambacho Serikali imewekeza fedha nyingi sana na chuo ni kizuri mno, ili wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali waweze kujiunga na chuo hiko?
NAIBU WAZIRI ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na lini ujenzi wa Chuo cha VETA cha Rufiji kitaanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fedha zimetengwa katika mwaka wa fedha unaokuja na fedha hizo zipo, kwa hiyo, siyo za kutafuta. Kwa hiyo, ujenzi utaanza mara moja, Rai yetu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji ni kwamba watupatie eneo lenye hati ili ujenzi uanze bila kuchelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini pia swali lake la pili kuhusiana na Chuo cha VETA Kipawa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba VETA nchi nzima kawaida inakuwa na utaratibu wa kutangaza nafasi za masomo katika vyuo vyake vyote lakini kama Mheshimiwa Mbunge anaona haitoshi katika Chuo cha Kipawa naomba nitumie fursa hii kumuagiza Mkurugenzi Mkuu wa VETA ahakikishe kwamba matangazo yale yanatolewa na aongeze kasi na wigo wa kutangaza nafasi mbalimbali za VETA zote nchini.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ambayo ninaridhika nayo na ninaipongeza Serikali kwa kupandisha hadhi Hospitali hizo za Ilala, Amana, Mwananyamala na Temeke, kwa kweli hosptali hizo zimekuwa msahada mkubwa na tumepunguza sana route za kwenda Muhimbili na Mloganzila.

Swali langu sasa kwa kuwa katika hospitali hizo za Mkoa hazina hizo mashine za MRI jambo ambalo linasababisha msongamano mkubwa wa kupata huduma hiyo katika Hospitali ya Muhimbili. Je, Serikali inautaratibu gani wa kupunguza foleni ya kupata kipimo hicho katika Hospitali ya Muhimbili? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam una Wilaya mpya za Kigamboni na Ubungo ambazo Wilaya ya Kigamboni wanatumia Hospitali ya Vijibweni kama Hospitali ya Wilaya na Wilaya ya Ubungo wanatumia Hospitali ya Sinza Palestina kama Hospitali ya Wilaya.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo hizo za mashine za x-ray na mashine nyingine katika hospitali hizo ambazo zinawasaidia wananchi wa Kigamboni na wananchi wa Wilaya ya Ubungo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza sana Mhemiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, amekuwa ni chachu ya kufuatilia mambo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam ni mfano wa kuigwa Wabunge wa Viti Maalum kwa sababu amekuwa ametupa ushirikiano mkubwa sana sisi Wabunge wa Majimbo ya Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu langu la msingi tuliona mahitaji ya huduma ya CT-Scan na MRI yanazidi kukua kutokana na hali ya mabadiliko ya wagonjwa na nitoe tu historia kwa sababu miaka ya nyuma tulikuwa na changamoto ya magonjwa ya kuambiza, sasa hivi tuna matatizo ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo huduma hizi za CT-Scan na MRI zinahitajika sana. Na kwa mwanzo tulikuwa tumeanza katika Hosptali za Rufaa za Taifa na Kanda, lakini kutokana umuhimu wa huduma hizi za CT- Scan na MRI ndiyo maana sisi kama Serikali tumesema sasa tunataka tuziweke katika ngazi ya Rufaa ya Mkoa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili tuweze kupunguza tatizo la foleni la huduma ya CT-Scan pale Muhimbili ndiyo maana sasa sisi tumekusudia kuhakikisha kwamba huduma hizi zinapatikana katika Hospitali za Rufaa za Amana, Mwananyamala pamoja na Temeke na hilo ndilo kusudio letu na mchakato tumeshaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swala lake la pili ameuliza jinsi gani tunaweza tukapanua wigo wa huduma hizi katika hospitali nyingine hususani katika zile za Wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, na hii naomba niliseme kwamba tunajenga Hospitali hizi za Wilaya moja pale Kigamboni, vilevile kule katika Wilaya ya Ilala. Lakini na mimi niombe niseme kwa sababu moja ya hoja ambayo umeigusia hapa ni katika Jimbo langu ambalo na mimi ni mwakilishi wa wananchi na niseme hivi tunavyoongea leo tunazindua huduma za x-ray katika Hospitali ya Vijibweni na nitoe rai kwa wananchi wa Kigamboni kwenda katika Hospitali ya Vijibweni huduma ya x-ray sasa inaanza kupatikana kuanzia leo.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo yanayowapata wananchi wa Tunduru yanafanana kabisa na matatizo ambayo yanawapata wananchi wa Kigamboni katika Mkoa wa Dar es Salaam. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga barabara ya Kibada - Kisarawe Two - Mwasonga - Tumbi Msongani ili kuwasaidia wananchi Wilaya ya Kigamboni waweze kupata unafuu wa usafiri?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam kuhusu barabara za Kigamboni. Hiki ni kipindi cha bajeti na kama tulivyoahidi barabara hizi zitajengwa ndani ya miaka mitano, kwa hiyo kwenye bajeti pengine suala la kuanza usanifu wa awali na wa kina litajitokeza. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hizi kama tulivyoahidi zitajengwa. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kuandikisha watoto kuingia darasa la kwanza kunakuwa na sharti la Watoto kwamba ni lazima waje na certificate ya kumaliza elimu ya awali; na changamoto hii imekuwa ni kubwa sana katika maeneo ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam katika shule kama za Mbande, Majimatitu, Charambe, Nzasa na maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam:-


Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kuondoa changamoto hii kwa wananchi au wazazi ambao wanapeleka watoto wao kuwaandikisha darasa la kwanza? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa uwiano wa darasa la kwanza utakuta kuna mikondo minne au mitano ya lakini darasa la awali linakuwa moja tu, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa watoto wote ambao wanaanza darasa la kwanza kwenda kujiunga na elimu ya awali katika shule husika:-

Je, Serikali imejipangaje sasa kuweka bajeti ya kutosha katika kuimarisha elimu ya awali katika shule zote za msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali hapa kwamba kumekuwa na sharti la certificate ya Elimu ya Awali; na anataka kufahamu Serikali inatoa kauli gani? Kwanza nieleze tu kabisa kwamba katika ngazi ya awali, Serikali haina utaratibu wa certificate. Hizo ni taratibu ambazo watu wamejitungia huko chini. Mara nyingi sana ni hizo shule za private zaidi ndiyo wamefanya hivyo, lakini huo utaratibu haupo.

Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali ni moja tu; certificates zilizopo ni za darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita na kuendelea, lakini kwa shule za awali certificate hakuna. Huo ni utaratibu ambao Serikali haiutambui. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali.

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, uwiano wa wanafunzi, hususan darasa la kwanza na shule ya awali; na kwa sababu hiyo niseme tu kwamba kutokana na umuhimu wa kuongeza wanafunzi katika shule za awali, ndiyo maana sasa hivi katika mipango yote ya Serikali ambayo tunayo, ikiwemo EP4R, Boost, Lens, RISE, miradi yote, tumehakikisha kabisa kwenye kila mradi tunaweka na component ya kujenga madarasa ya shule za awali ili kuhakikisha watoto wetu wanapata madarasa bora na tunaongeza madarasa ili watoto hao waweze kupata mazingira bora ya kujifunzia.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na vile vile nampongeza Mheshimiwa Mariam Kisangi. Nataka tu kuendelea kutoa tamko la kisera; ni marufuku shule kudai certificate ya awali kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza.

Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba bado hatujafanya vizuri katika kuongeza access ya watoto kuanza elimu ya awali. Kwa hiyo, haileti mantiki kusema kila mtoto ili aanze Darasa la Kwanza awe na certificate ya awali. Tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwenda kuweka nguvu za kuboresha watoto wetu hususan wa masikini kupata elimu ya awali, hususan katika maeneo ya vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona niweke hiyo; na wote ambao wanadai certificate ya elimu ya awali wajue kwamba wanatenda kinyume na maelekezo na miongozo ya Serikali.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, bandari hiyo sasa imesharasimisha na ninaipongeza sana Serikali: Je, Serikali sasa ina mpango gani wa muda mfupi kuboresha eneo hilo ili liweze kufikika?

Swali la pili; kwa kuwa wanawake wa Kata ya Mbweni ni wadau wakuu katika eneo hilo la bandari: Je, Serikali ina mpango gani ya kuwatengea eneo mahususi kabisa ya kufanya shughuli za ujasiliamali ili nao waweze kufahidika na fursa hiyo ya bandari? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya muda siyo mrefu sana tutatembelea eneo hilo. Anasema kuna shida ya barabara kwamba eneo halifikiki; tutarekebisha miundombinu ili waweze kupata huduma nzuri pale.

Mheshimiwa Spika, swali la pili amewasemea akina mama wa nchi hii na hasa Mkoa wa Dar es Salaam maeneo ya Mbweni; naomba niseme tumepokea wazo hili nzuri na jema, tutalifanyia kazi akina mama wapate sehemu maalum ya kufanya shughuli zao katika Bandari ya Mbweni. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali lini itakamilisha mradi wa maji wa visima vya Kimbiji na Mpera kuwasaidia wananchi wa Halmashauri ya Kigamboni waweze kupata maji safi na salama; na pia katika Kata za Tuangoma, Chamazi, Mbande, Mianzini, Kibondemaji na Charambe wote hawa waweze kunufaika na mradi huo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Visima hivi vya maji vya maeneo ya Kimbiji, Kigamboni na maeneo haya yote ya ukanda ule vinatarajiwa kuhakikishwa vinakamilika mwaka ujao wa fedha, kadiri fedha ambavyo tutakuwa tukiendelea kuzipokea ndani ya Wizara yetu. Maeneo ya Tuangoma, Majimatitu, kote huko Wizara inatupia jicho la kipekee kabisa. Tunafahamu ongezeko la wakazi ni kubwa, hivyo na sisi tutahakikisha tunafanya kazi usiku na mchana ili maji yaweze kuwafikia wananchi wa maeneo haya.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa mchakato wa kuanzisha Wilaya ya Ukonga ulifanywa mwaka 2015 sambamba na uazishwaji wa Wilaya ya Kigamboni na Ubungo katika halmashauri mbili ambazo wakati huo Mkoa wa Dar es Salaam ulikuwa na Halmshauri ya Temeke, Ilala na Kinondoni. Kwa hiyo, Wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam zilifanya mchakato wa kutaka kuongeza halmashauri ikiwemo Halmashauri ya Wilaya Ukonga. Je, Serikali haioni haja sasa ya kurudia kwenye kumbukumbu zake kuangalia jambo hilo ili lifanyiwe utaratibu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwanza, niipongeze Serikali kwa kuanzisha Jiji la Dar es Salaam lakini kwa kuwa Ofisi za Halmashauri ya Jiji ziko katika Mtaa wa Morogoro Road na Drive In kwa kifupi mjini Posta na kwa mkazi wa Chanika, Msongora, Mzinga, Kitunda, Zingiziwa, wana changamoto kubwa ya kufika kwenye Halmashauri hizo za Wilaya ili kuweza kupata huduma za kijamii. Je, Serikali haioni haja ya kusisitiza jambo hili la kupata Wilaya mpya ya Ukonga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza Mheshimiwa Mbunge anasema mchakato ulifanyika mwaka 2015, wakati wa mchakato ule Halmashauri za Ubungo na Kinondoni ndizo zilizokuwa na sifa za kupata Halmashauri za Wilaya na anasema twende tuka-review mchakato wa mwaka 2015. Nafikiri jibu la Serikali ni la msingi, kama kuna maombi mapya ni lazima muanze upya mchakato na kila kipindi kinapopita kinakuwa na sababu zake. Kwa hiyo, maombi yote ya nyuma kwa sasa hivi tunasema ni maombi ambayo hayatambuliki kwa sababu zoezi lile lilifanyika kwa wakati mmoja na halmashauri ambazo zilikidhi vigezo zilipewa hiyo hadhi za kuwa wilaya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ushauri wangu utabaki palepale kwamba kama kuna nia hiyo anzeni upya watu wa Ukonga mfuate taratibu zote za kisheria, mlete maombi na sisi tutayapeleka kwa Mheshimiwa Rais. Rais ndiye atakayekuwa na maamuzi ya mwisho ya kuanzishwa either kwa Wilaya ya Ukonga ama kusitisha kwa kadri atakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo la pili amerudia jambo lilelile kwa sababu Makao Makuu ya Ofisi za Jiji yapo mjini sana na anaona kwamba kuna haja ya kuwa na wilaya mpya ili kusogeza huduma. Kikubwa ni kwamba Serikali tutaendelea kupeleka huduma kwa wananchi, lakini hayo maombi yenu kama yatakidhi basi Serikali itaendelea kuangalia. Hilo nafikiri ndiyo jibu sahihi kwa wakati huu. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kwa sasa wagonjwa wote wa akili katika Hospitali za Temeke, Mwananyamala na Amana, wanapelekwa katika Hospitali ya Muhimbili, lakini jengo hilo la wagonjwa wa akili la Hospitali ya Muhimbili halijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu kiasi kwamba, mwananchi wa kawaida kuingia kwenye ile wodi unaogopa. Sasa napenda niiulize Serikali.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati jengo la wagonjwa wa akili katika Hospitali ya Muhimbili, ili Madaktari wetu waweze kufanya kazi zao katika mazingira mazuri na wagonjwa waishi katika mazingira mazuri? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha kwamba, kuanzia mwaka 2020 kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa akili duniani na hasa vijana kuanzia miaka 15 mpaka miaka 35 na hiyo inatokana na matatizo na changamoto mbalimbali za kimaisha. Haya yameanza kujitokeza katika nchi yetu ya Tanzania, watu wameanza kuuana ovyo na matendo ambayo sio ya kibinadamu yanatendeka sana, tunapata hizo taarifa. Je, Serikali haioni haja sasa ya kujenga hospitali maalum ya wagonjwa wa akili badala ya kuwa Mirembe, Dodoma peke yake? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mbunge kwa ufuatiliaji mzuri sana anaoufanya kwa kufuatilia masuala ya afya ya watu wanaoishi kwenye Mkoa wa Dar-es-Salaam, tunampongeza sana Mheshimiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kama Mheshimiwa Mbunge anavyosema kwamba, kweli jengo lile liko chakavu pale Muhimbili, lakini kwa mwaka huu tu, hii miezi miwili iliyopita, hospitali ya Muhimbili Rais wetu amepeleka bilioni 16 pale, lakini ilitengwa zaidi zaidi ya milioni 400 kwa ajili ya kukarabati jengo lile, lakini kwa sababu ya matatizo ya corona na kulikuwa na umuhimu wa kuhakikisha baadhi ya expenses zilizoongezeka wangebeba wananchi wenyewe ingeleta shida, fedha zile zilielekezwa upande huu, lakini ameshatoa maelekezo Waziri wa Afya juzi alivyotembelea Muhimbili na sasa hiyo kazi inaenda kuanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, samahani. Swali lake la pili amezungumzia kwamba, kuna matatizo ya akili yameongezeka duniani, lakini vilevile hapa nchini kwetu Tanzania. Ni kweli, yameongezeka, suala sio kuongeza idadi ya hospitali, lakini ni kuangalia visababishi ambavyo vinasababisha watu kupata matatizo hayo viweze kutatuliwa. Vilevile sio tu kujenga hospitali maalum kwa ajili ya hiyo, lakini ni ku-integrate hizi huduma kwenye huduma nyingine mpaka kushuka chini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu ameshaelekeza kwamba, hospitali zote zianze na nilianza na Kigoma kama uliangalia kwenye vyombo vya habari, kulikuwa na wataalam wa afya ya akili na wale wataalam wa afya ya akili tukaanza kuelekeza kwamba, waanze sasa kutengewa bajeti na zile ofisi zao zipewe bajeti ya kutosha ili waweze kufanya kazi zao na kushuka chini mpaka kwenye vituo vya afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata unapoona CT-Scan zimesambazwa kwenye hospitali zote za mkoa, wakati mwingine wagonjwa wa akili wamekuwa wakitibiwa kwa kuangalia dalili zao tu, lakini sasa tunataka kwenda kuwaangalia kabisa, kwa sababu wanaweza wote kuonesha dalili zinazofanana, lakini visababishi vikawa tofauti. Kwa hiyo, sasa tunaenda kwenye level ya kupiga CT scan za ubongo ili kila mmoja aweze kutibiwa kwa namna ambavyo ana tatizo lake. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza, lakini pia niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kuweka jiwe la msingi barabara ya mwendokasi ya Mbagala, kutoka Bendera Tatu kwenda Mbagala mambo ni mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza; ni lini sasa Serikali itakamilisha barabara ya kutoka Mbagala Kokoto mpaka kwenda Kongowe kupunguza msongamano wa magari na kero kubwa ya kupoteza muda katika eneo la Mbagala Rangi Tatu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja ni muhimu sana na imeainishwa kukamilishwa kwa kiwango cha lami, lakini itajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha na kwa kuwa tuko kwenye kipindi cha bajeti basi tutaangalia ili iweze kupangiwa bajeti kwa mwaka ujao wa fedha. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati makazi ya askari polisi Wilaya ya Mbagala ambayo yana hali mbaya sana, sana, sana pamoja na kituo cha polisi cha Wilaya ya Mbagala? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niliahidi tarehe 22 Februari nitakuwa Dar es Salaam naomba Mbunge awe tayari tuzunguke naye kwenye maeneo ya Mbagala, kuona kiwango cha uchakavu ili kwa pamoja tutafakari namna ya kuboresha majengo hayo kupitia bajeti yetu tunayotoa kila mwaka. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya ulipaji wa fidia inawakumba pia wakazi wa Mbagala, maeneo ya Kokoto mpaka Kongowe na Tuangoma, bado wanadai fidia kwa ajili ya upanuzi wa barabara ya Kilwa Road; na kwa kuwa toka imefanyiwa tathmini mwaka 2019 mpaka leo hii hakuna malipo yoyote yanayofanyika kwao: Je, Serikali ina mpango gani wa kulipa fidia hiyo kwa wananchi wa Mbagala – Kokoto mpaka Kongowe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wote ambao wamefanyiwa tathmini yao watalipwa haki zao kwa sababu Serikali haina muda wa kutaka kwenda kumtapeli mwananchi yeyote. Kwa hiyo, nimwondoe wasiwasi huo. Kwa sababu Serikali ni moja, barabara ile najua iko upande wa TANROADS, basi tutafanya kazi hiyo kwa pamoja kuhakikisha jambo hili linawafikia. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa madereva wengi wamekuwa wakifanya kazi na kupata ajali lakini na matatizo mengine ya kiafya hali ambayo wanakuwa mzigo kwa familia. Je, Serikali ina mpango gani wa kuwasaidia hawa madereva waweze kupata haki zao za msingi kuepukana na vifo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, tamko limetolewa muda mrefu na mpaka sasa kuna baadhi ya wamiliki wa magari hayo hawajatoa mikataba hiyo. Je, nini tamko la Serikali kuhusiana na hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza Mheshimiwa Kisangi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, madereva ambao wanaopata ajali au maafa kutokana na kazi ambazo wanazifanya, Serikali imeweka utaratibu mzuri wa kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao unawajibika na kuhakikisha kwanza maeneo yote rasmi ya waajiri yanasajiliwa na kutoa michango kwa ajili ya fidia pale mfanyakazi anapopata madhila.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo Sheria ya Workers Compensation ambayo nayo pia inahusika na masuala ya ulipaji fidia. Sambamba na hilo Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko na maboresho kwenye sheria za bima ambapo vyombo hivi vinakatiwa bima na zipo bima ambazo zinawa-cover pia wale ambao watapata madhila kutokana na ajali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili la nyongeza la Mheshimiwa Kisangi ameuliza kuhusu waajiri ambao hawajatoa mikataba. Naomba nitoe tamko rasmi la Serikali kama jinsi alivyonitaka nifanye, tamko rasmi ni kwamba, ni kosa kisheria kama umeajiri mfanyakazi na haumpatii mkataba, kwa sababu sheria zinatoa maelekezo, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, inatoa haki za mfanyakazi, lakini pia wajibu wa mwajiri. Wajibu wa mwajiri unaelezwa katika sheria hiyo zikiwa ndiyo haki za mfanyakazi. Kwa hiyo, ina reciprocate kwamba haki za mwajiri, ndio wajibu wa mfanyakazi na wajibu wa mfanyakazi ndio haki za mwajiri. Kwa hiyo, mtu yoyote ambaye hatatoa mkataba wa kazi na maeneo hayo tumekuwa tukiyabaini, tumekuwa tukiwachukulia hatua na ikibidi kuwapeleka mahakamani ili waweze kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe rai kwa maeneo yote Watanzania wanaonisikiliza lakini pia Waheshimiwa Wabunge, kama kuna maeneo ambayo tuna uhakika kwamba hawatoi mikataba ya kazi pamoja na kaguzi zetu mtupe taarifa ili tukachukue hatua stahiki kwa wakati unaostahili. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali lini itakamilisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Ubungo iliyopo Kata ya Kimara ili iweze kupokea wagonjwa wa aina zote badala ya kupokea wagonjwa wa OPD ilivyo sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali ilipeleka fedha takribani shilingi bilioni moja na milioni mia tano kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo na kazi ile inaendelea, nimefanya ziara pale zaidi ya mara tatu na huduma za awali zimeanza kutolewa.

Mheshimiwa Spika, hospitali ile itakamilishwa kwa fedha za awamu ya pili ambazo zitakwenda kukamilisha miundombinu ambayo imebaki.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza naipongeza Serikali kwa kutenga hiyo shilingi bilioni 2.04 kwa bajeti ijayo kujenga maeneo ya kusubiria wagonjwa, lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza, changamoto ya watu kukosa sehemu za kusubiria wagonjwa inaikumba hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam za Temeke, Amana na Mwananyamala. Maeneo ambayo yametengwa ni madogo sana kiasi kwamba idadi ya watu ni wengi.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua maeneo ya watu kukaa wanaosubiria wagonjwa katika hospital hizo za Mkoa wa Dar es Salaam?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa changamoto ya watu kukosa sehemu za kusubiria wagonjwa inaikumba hospitali ya Taifa ya Muhimbili, hali ambayo imesababisha taharuki, wananchi wanaokuwa kule ndani ni wengi lakini hawana sehemu maalum za kukaa, kusubiria kupata huduma na kusubiria kuona wagonjwa.

Je, Serikali inatoa kauli gani kwa wananchi wake ili waondokane na kadhia hiyo ya kufukuzwa hovyo hovyo na Askari Mgambo kule ndani ya hospitali ya Taifa ya Muhimbili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa hospitali ya Mwananyamala na hospitali ya Temeke wametenga kwenye bajeti ya mwaka huu kabla ya Juni watakuwa wamejenga maeneo hayo, lakini hospitali ya Muhimbili hiyo kadhia inatokana na kazi hiyo anayoisema Mheshimiwa Mbunge kwamba wamefunga pale OPD wanafanya renovation kujenga vizuri, lakini kujenga hiyo sehemu ya kungojea na kuna maeneo mengine ambayo yamefungwa kazi hiyo anayoisema Mbunge ikifanyika, kwa hiyo ndani ya miezi mitatu hiyo kadhia itakuwa imeondoka. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Mahakama ya Mwanzo ya Mbagala ambayo ina hali ngumu sana, mazingira yake na idadi ya watu wanaopata huduma pale ni wengi sana?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi tumelichukua ombi lake na tutakwenda kulifanyia kazi ili tuweze kuiweka katika mazingira mazuri ya matumizi, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninalo swali la nyongeza.

Kwa kuwa mgonjwa anapofika hospitalini hawezi kupata matibabu sahihi bila kupata vipimo; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha zahanati zote nchini zinapata maabara ili kutoa huduma sahihi kwa wagonjwa wetu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba ili upate huduma bora za afya lazima vipimo vya maabara vifanyike na Serikali kwanza imechukua hatua ya kuboresha ramani za majengo ya zahanati kwa kuongeza vyumba kutoka sita hadi vyumba 15, ambavyo vitawezesha kuwa na jengo zuri ambalo linakidhi huduma za maabara katika zahanati zetu.

Mheshimiwa Naibu Sspika, pili, zahanati zetu ambazo zilijengwa miaka ya nyuma ambazo hazikuwa na nafasi nzuri kwa ajili ya huduma za maabara, tumetenga maeneo ambayo huduma za maabara za msingi, kwa mfano vipimo vya malaria, vipimo vya wingi wa damu vinafanyika katika vyumba ambavyo vimekuwa improvised na huduma hizi zinaendelea kutolewa katika maeneo haya. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Naomba kuuliza kwa kuwa akinamama wa Mkoa wa Dar es Salaam wengi ni akinamama lishe na wanafanya shughuli ndogondogo, lakini katika eneo hilo hilo la stendi ya Mbezi bado kuna eneo kubwa ambalo Serikali inaweza ikawajengea vibanda vidogo vidogo. Je, Serikali haioni haja hata kwa kutumia Mfuko wa Akinamama ile asilimia yao kuwajengea mabanda rahisi ya kuweza kufanya kazi zao, akinamama wote wa Mkoa wa Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tunahitaji kuboresha maeneo ya wafanyabiashara wadogowadogo na ndio maana Mheshimiwa Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuboresha maeneo ya wafanyabiashara wadogo wadogo wakiwemo akinamama ntilie lakini pia machinga na wafanyabiashara wengine. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba eneo la Mbezi ambalo anasema lina nafasi ya kujenga tutakwenda kulitazama ili tuone uwezekano wa kuwekeza hapo. Wazo lake la kutumia asilimia 10 pia tutalifanyia tathmini kuona au kutafuta chanzo kingine kwa ajili ya ujenzi huo. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga au kuboresha barabara inayotoka Chuo cha Diplomasia Kurasini kupitia Tom Estate kupitia Msikitini ka Mzuzuri mpaka kuunganisha na barabara ya Mandela? Kipande hicho ni korofi, makontena yanapita kwa shida sana ukiwa na gari ndogo unaweza ukafikiria sasa kontena linaniangukia, nashukuru.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kisangi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiri tu kwamba sijaielewa vizuri hiyo barabara aliyoitaja lakini nimuombe pia Mheshimiwa Mbunge, kama ataridhia basi niweze kukutana naye ili niweze kuielewa hiyo barabara ili niweze kumpa hasa majibu sahihi badala ya kujibu tu. Sijaielewa vizuri hiyo barabara, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Taasisi ya Kansa ya Ocean Road Dar es Salaam imekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa siku hadi siku na idadi kubwa ya wagonjwa ambayo inaongezeka hapo ni akina mama wenye matatizo ya kansa ya kizazi: Je, Serikali haioni haja sasa kuwasaidia akina mama hawa kufungua vituo vya kansa katika hospitali za kanda na mikoa ili kupunguza gharama za usafiri kwa akina mama hao na mahitaji muhimu? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeonesha kwamba kuna huduma za awali za uchunguzi wa kansa katika hospitali mbalimbali: Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuziunganisha huduma za uchunguzi wa awali za kansa katika kliniki zetu za mama na mtoto ili mama apate huduma hiyo kabla na baada ya uzazi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri anayoifanya ya kufuatilia eneo hili la afya ya akina mama. Nimwondoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwa swali lake la kwanza kwamba Serikali yetu imejipanga, ndiyo maana mmetusikia hapa tukisema Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa kwa mwaka huu tu shilingi bilioni 290.9 kwa ajili ya kuleta vifaa tiba. Kwa hiyo, kwenye hospitali zetu za kanda na mikoa, vifaa vile vitasaidia kuchunguza, lakini kwenye kanda wanatibiwa kabisa. Kwa hiyo, hiyo huduma imepelekwa, kanda watatoa, mikoa watatoa. Tuliona juzi madaktari waliokuwepo hapa, kazi yao mojawapo ni kwenda kuhakikisha wanatambua mambo hayo.

Mheshimiwa Spika, kwenye maana ya kufika kule wilayani, labda nikwambie tu, tunalichukua, tunaliongezea nguvu lakini wenzetu waliokuja hapa pia mojawapo ya kazi yao ni kukutana na akina mama mpaka kwenye vituo vyetu na zahanati, wakiendelea kuhakikisha kwamba mojawapo ya jambo la kuzingatia ni kuangalia hiyo saratani ya kizazi, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi. Kwa kuwa changamoto za hospitali za kidini inaikumba pia hospitali ya Mbagala Mission kwa jina jingine kwa Buluda, ni hospitali ya muda mrefu, na wananchi wote wa Mbagala na maeneo mengine ya Dar es Salaam wanaitegemea sana hospitali hiyo;

Je, Serikali haioni haja kuwaongezea nguvu kituo kile cha Consolata Sisters Mbagala Mission ili waweze kusaidia vizuri zaidi wananchi?
NAIBU WAZIRI, 0FISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nirejee tena majibu yangu ya msingi, kwamba Serikali inao utaratibu wa kukaa na hospitali hizi teule katika maeneo mbalimbali hapa nchini na kama nilivyokwisha toa maelekezo kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI kwa waganga wakuu wote wa mikoa kuhakikisha wanakaa kuangalia uendeshaji wa hospitali hizi teule na kuona ni namna gani ambavyo zinaweza zikaboreshewa huduma zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongezee tu kwa faida ya Bunge lako Tukufu, kwamba Serikali hupeleka watumishi katika hospitali hizi teule lakini vile vile inapeleka mgao wa fedha katika hospitali hizi teule kuweza kusaidia ili wananchi wa maeneo hayo waweze kupata huduma ambayo wanastahili.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante sana. Kwa kuwa huduma ya ultrasound imekuwa na umuhimu wa kipekee kwa wakinamama wajawazito.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka huduma hiyo ya ultrasound katika vituo vya kliniki ya mama na mtoto? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni adhma ya Serikali hii ya awamu ya sita kuhakikisha kwamba inakuwa ina vifaatiba vya kisasa katika vituo vyetu vyote vya afya hapa nchini. Tutahakikisha kwamba kadri miaka inavyokwenda na bajeti inatakavyoruhusu tunatenga fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya ultrasound kwenye maeneo yenye wodi za mama na mtoto kama ambavyo Mheshimiwa Kisangi amezungumza.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa wako watumishi wa Serikali wakiwemo walimu ambao walikumbwa na mfumo huo wa kikokotoo wa muda katika kile kipindi ambacho kilianza kutumika, lakini mpaka sasa walimu hao mfumo wao wa pensheni haueleweki na hauko sawa: Nini kauli ya Serikali kuhusiana na walimu hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama alivyouliza kwamba mifumo ya ulipaji wa mafao ya walimu haueleweki.

Mheshimiwa Spika, huu utaratibu uliofanyika wa kuunganisha mifuko na kutengeneza uwiano sawa wa malipo haukuacha kundi lolote nje likiwemo kundi la walimu. Kwa hiyo, kama kuna sehemu ambayo anadhani kwamba kuna walimu wana changamoto hiyo, mimi nilipokee tu jambo hili kutoka kwake na nikalifanyie kazi, kwa sababu mfuko huu haujabagua kundi lolote katika kutengeneza maslahi ya wafanyakazi wetu, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali ya nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya mikopo ya vikundi imekuwa kubwa sana katika maeneo ya Jiji la Dar es salaam na hususani katika Jimbo la Kinondoni, kutokana na masharti mbalimbali wanayopewa wakopaji wanashindwa kukopa. Je, Serikali haioni haja katika hiyo mikakati yake sasa kuangalia sehemu ya mtu kukopa mmoja mmoja?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wakinamama wengi wajasiliamali wa mitaani wanashindwa kuungana kwenye vikundi na wanahitaji kupata mikopo mmoja mmoja mwenye kuuza mandazi, vitumbua na nini. Je, Serikali imejipanga vipi sasa katika hiyo mikakati yake kuhakikisha kwamba, sasa wanaruhusiwa kukopa mtu mmoja mmoja ili aendeleze biashara yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ifahamike kwamba vikundi katika mikopo ya asilimia 10 vinatumika kama dhamana, kwa sababu wajasiliamali wanaokopeshwa kwa mikopo ya asilimia 10 ni wale ambao hawana uwezo wa kutosha kuwa na dhamana ya kupewa mkopo. Kwa hiyo, concept ilikuwa kwamba kikundi ni dhamana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tumechukua hoja hii na chini ya Mheshimiwa Waziri wetu wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutaifanyia tathimini kwenye tathimini inayoendelea nakuona uwezekano wakuiboresha kama itakuwa inatija, ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa, Sheria ya Utumishi inaelekeza pia likizo ni haki ya mtumishi lakini likizo ile inatakiwa iambatane na stahiki zake za usafiri au nauli kwa mtumishi, lakini mpaka sasa kuna changamoto ya Walimu kupewa likizo lakini kutokupewa nauli ya kwenda makwao. Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inapokea malalamiko ya watumishi juu ya baadhi ya madai au malimbikizo ya madai kama ambavyo ameeleza Mheshimiwa Mbunge lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeendelea kufanya hatua za malipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nitoe taarifa mbele ya Bunge lako kwamba hadi sasa tunapozungumza Serikali imekwishalipa zaidi ya wafanyakazi 126,924 ambao kwa gharama ya kifedha ni sawasawa na bilioni 216 kwenda kulipa madeni yote ambayo yanaendelea, ninachoweza kusema katika Bunge lako wale wafanyakazi wote ambao wana madeni ya malimbikizo wawasiliane na Ofisi zetu kupitia Wakurugenzi wa Halmashauri pia kupitia Ofisi ya Rais ili madeni yao yote au madai yao yote ya malimbikizo tuweze kuyaangalia mara mara moja.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nampongeza sana; lakini ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali imeonesha wazi kwamba wameweka hiyo dawa. Hata hivyo, tatizo la popo katika maeneo ya Upanga, Sea View, Leaders Club, Kinondoni, Oysterbay, Masaki, Msasani Peninsula na maeneo mengine ya ukanda wa pwani linaongezeka siku hadi siku na kusababisha popo hao mpaka wanavunja vioo vya madirisha kwenye nyumbani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza hiyo dawa ili popo hawa waweze kuondoka na kuwaondolea adha wananchi wa maeneo hayo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa changamoto inayowapata wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam katika maeneo ya Upanga na mengineyo, pia inawakuta wananchi wa Dodoma kuvamiwa na nyuki katika maeneo mbalimbali hasa maeneo ya Area D katika majengo ya TBA, Makole yote pamoja na maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma nyuki wanavamia na kuhama hama hovyo hovyo;

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea wananchi wa Jiji la Dodoma adha ya kuvamiwa na nyuki?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye swali la msingi, hatua ya kwanza ya kukabiliana na popo hawa ilikuwa ni kufanya utafiti wa kujua kiwango cha ukubwa wa tatizo na aina ya dawa ambayo inaweza kutumika ili kukabiliana na changamoto hii.

Mheshimiwa Spika, utafiti huu umekamilika, sasa jukumu lililopo mbele yetu ni kuhakikisha kwamba wadau wote wanaohusika na kukabiliana na jambo hili, zikiwepo Halmashauri zetu zinachukuwa hatua ya kuhakikisha tunasambaza dawa hizi kwa wananchi ili tuweze kukabilianana tatizo hili. Niombe wadau wote wanaohusika tushirikiane ili tuweze kuondokana na tatizo hili.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili la tatizo la uvamizi wa nyuki kwenye Mkoa wa Dodoma. Nitumie fursa hii kuwaagiza wataalamu wetu wa idara ya nyuki kushirikiana na wenzetu wa jiji la Dodoma ili kufanya tathmini ya haraka na kuona ukubwa wa tatizo hili na kuchukua hatua za haraka za kuangamiza nyuki hawa, ahsante sana.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na kumpongeza, tunafanya kazi vizuri kwa pamoja na nimpongeza kwa majibu mazuri sana.

Mheshimiwa Spika, kwa kuongezea majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa upande wa popo, tayari tumeagiza dawa nyingine za majaribio ikiwemo Pepzol na Super Dichlorvos ambazo zinapatikana Marekani na Kenya. Imeonekana kwamba dawa hizo zikitumika ndani ya miezi miwili mpaka mitatu popo hao wanaweza wakatoweka.

Mheshimiwa Spika, pia nitoe rai kwa Halmashauri zetu za Jiji la Dar es Salaam na Halmashauri nyinginezo katika maeneo ya miti ya barabarani waweze kununua dawa hizo ili waweze kupiga kwa ajili ya kuweza kufukuza na kudhibiti popo hao.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa Jiji la Dodoma kuhusu suala la nyuki, kama ambavyo Naibu Waziri ameeleza, nako pia tutoe rai kwa Halmashauri ya jiji Dodoma nao watenge fedha ili waweze kununua dawa hizo ili pale tutakapokuwa tumepata tathmini ya kuweza kujua ni dawa gani zinaweza kufanya kazi vizuri katika kudhibiti basi waweze kununua dawa hizo na kuweza kutumia.

Mheshimiwa Spika, Wizara kupitia taasisi ya TAWIRI tutaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na taasisi katika kuhakikisha kwamba tunadhibiti tatizo hili. Tuombe ushirikiano kwa wale wenye makazi pia waweze kununua dawa hizi katika maduka mbalimbali yanayozalisha dawa hizi. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri, kwanza naipongeza Serikali kwa niaba ya Mheshimiwa Askofu Gwajima, kwa kweli alikuwa huko na amelishughulikia suala hili na Serikali imelipokea na imelifanyia kazi. Pongezi sana kwa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, je, Serikali imejipanga vipi sasa kuhakikisha inadhibiti migogoro yote iliyopo katika jimbo hilo ili isijirudie tena? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha Mgogoro wa Shamba la Malolo upande wa Jimbo la Kibamba Halmashauri ya Ubungo nao unaumaliza kama vile walivyomaliza kwenye Wilaya ya Kinondoni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza udhibiti wa migogoro isiweze kujitokeza, ni juhudi za Serikali na tumekuwa tukishirikiana na taasisi mbalimbali katika kuhamasisha migogoro hii isiendelee kujitokeza. Hata hivyo, suala la Malolo, Kibaha nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kwamba baada ya Bunge lako Tukufu kumalizika, tutaanza ziara za kutembelea maeneo haya na kukutana na wananchi na taasisi zile ambazo zinagongana kwenye migongano hii ili kuitafutia suluhisho la kudumu, ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza;

Je, lini Serikali itakamilisha barabara ya kutoka Mji Mwema mpaka Pemba Mnazi ni ya muda mrefu sana?

Je, lini sasa itakamilisha kipande cha kutoka Gomvu mpaka Pemba Mnazi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, nataka kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilishafanya taratibu na tuko kwenye hatua za manunuzi kwa maana ya kujenga barabara ya kilometa 41 kwa kiwango cha lami. Barabara ambayo ametaja kilometa 41.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa kipande hicho cha Mbagala Rangi Tatu hadi Kongowe kinakuwa na msongamano mkubwa wa magari kiasi kwamba ni foleni masaa yote: Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi kuhakikisha wanapanua ile barabara ili magari yaweze kupita na kuepukana na foleni?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema, tunatambua changamoto ambayo ipo kwenye hii barabara na ndiyo maana tumeiweka kwenye mpango. Serikali itakachofanya ni kuhakikisha kwamba inaanza haraka ujenzi wa kipande hiki ili kuondoa adha ambayo inawakuta wananchi ambao wanatumia hii barabara ikiwa ni pamoja na kupunguza msongamano kwa maana ya kupunguza muda mwingi ambao unatumika katika kipande hiki. Ndiyo maana tayari tumeshaingiza kwenye mpango. Kwa hiyo, cha msingi ni kuanza haraka ujenzi wa barabara hii kwa hizo njia nne, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Moja; kwa kuwa changamoto za barabara na za Mkoa wa Simiyu zimekuwa zikiongezeka siku hadi siku, barabara ni mbovu, wananchi wanashindwa kupita na kusafirisha mazao yao; je, Serikali ina mpango gani sasa wa muda mfupi kuhakikisha wanarekebisha barabara za Mkoa wa Simiyu zile ambazo zinachangamoto kubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa changamoto ya barabara za Mkoa wa Simiyu inafanana na zile za Mkoa wa Dar es Salaam. Mkoa wa Dar es Salaam umekuwa na changamoto kubwa ya barabara chakavu lakini na kukosa mitaro hali ambayo inasababisha wakati wa mvua shuhuli zote za kiuchumi kusimama katika Mkoa wa Dar es Salaam; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha wanajenga mitaro na kurekebisha ili sasa wakati wa nyakati za mvua magari yaweze kupita? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu maswali mawili ya nyongeza la kwanza hili la mpango wa barabara za Mkoa wa Simiyu kama ambavyo nimeisha kwenye majibu yangu ya msingi, ukiangalia mwaka 2021 Serikali ilikuwa imetenga shilingi bilioni tano kwa Mkoa wa mzima wa Simiyu kwa ajili ya ukarabati wa barabara lakini kuonyesha ni namna gani Serikali inajali wananchi wa Mkoa wa Simiyu, inajali wananchi wake wa Tanzania iliiongezea fedha TARURA kutoka shilingi bilioni 226 na kwenda shilingi bilioni 776 zaidi ya mara tatu ya ile bajeti ya mwanzo.

Mheshimiwa Naibu Spika, na ukiangalia Mkoa wa Simiyu peke yake kutoka shilingi bilioni tano kwenda shilingi bilioni 17 ambayo imetengwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2023/2024. Hivyo Serikali itaendelea kuweka kipaumbele cha kuhakikisha kwamba barabara zinatengenezwa kwa wakati ili ziweze kupitika na kuendelea kupunguza asilimia ya barabara mbovu kwa kuhakikisha TARURA inaendelea kuwekewa fedha kwa ajili ya matengenezo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la pili kuhusu Mkoa wa Dar es Salaam; wewe pia ni shahidi kwa sababu ni Mbunge wa Mkoa wa Dar es Salaam tayari hivi karibuni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Angellah Kairuki alikaa na Wabunge wote wa Mkoa wa Dar es Salaam na vilevile aliita Kamati ya Bunge ya TAMISEMI na kusaini mikataba kwa ajili ya kuanza Mradi wa DMDP II ambayo itakwenda barabara zote ambazo zinachangamoto, zilizosalia ambazo hazikuwepo kwenye DMDP I katika Mkoa wa Dar es Salaam ni zaidi ya shilingi bilioni 800 ambayo Serikali hii ya Mama Samia Suluhu Hassan imetenga kwa ajili ya kuhakikisha Mkoa wa Dar es Salaam unaboreka. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa, barabara hiyo ya Kibada hadi Tundwi - Songani inakwenda mpaka Pemba Mnazi ambapo kuna viwanja vingi vimetengwa na Serikali, lakini kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa Barabara. Ukosefu wa kujengwa barabara hiyo unasababisha kuongezeka kwa nauli kwa wananchi wa Kisarawe II, Mwasongwa na Tundwi - Songani.

Je, nataka commitment ya Serikali, ni lini? Je, ni kweli itaanza kujengwa barabara hiyo mwezi Juni, maana imekuwa ni ahadi ya muda mrefu.

Swali la pili, changamoto ya ukosefu wa barabara inaikumba pia Halmashauri ya Ubungo. Barabara ya Victoria – Mbezi – kwa Yusufu hadi Mpiji Magohe. Ni lini barabara hiyo nayo itajengwa?(Makofi)
NAIBU WAZIRI UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na swali la kwanza la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba, barabara hii niliyoitaja tunakwenda kuijenga, ndiyo maana bila kusita tunategemea mwezi kabla haujaisha huu wa Juni tuwe tumeisaini kwani Mkandarasi alishapatikana tuanze ujenzi wa barabara hii. Tunatambua umuhimu wa barabara hii kwani sasa limekuwa ni eneo muhimu sana kwa shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa Dar-es-Salaam na hasa Jimbo la Kigamboni. Pia ni kwamba, tunajua alikuwa amepata changamoto ya kuharibika, Mkandarasi tayari yupo site kuanzia Mji Mwema, Kimbiji lakini Mji Mwema - Mwasonga hadi Kimbiji kuhakikisha kwamba, anarudisha barabara kwenye hali yake nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu barabara alizozitaja hizi tayari, kama ataangalia kwenye bajeti za Jimbo la Ubungo, barabara hizi tumeziingiza kwenye mpango. Kulikuwa na barabara moja ilikuwa haijafanyiwa usanifu hasa ile ya Kwa Yusufu - Makabe, lakini barabara nyingine hizi tumeziweka kwenye mpango wa kuanza kuzijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mvua kunyesha pasipo utaratibu na mafuriko pia. Je, Serikali imejipanga vipi katika kukabiliana na hali hiyo ya njaa pamoja na mfumuko wa bei katika nchi yetu? (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Mariam Kisangi hilo swali lako hapo mwishoni hebu litengeneze lirudi kwenye hoja yako kwa sababu mfumuko wa bei sasa utaelekea Wizara nyingine.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri sana wakulima pamoja na makazi ya watu. Je, Serikali imejipanga vipi kukabiliana na hali hiyo? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri yote yaliyopita, lakini swali la Mama Mariam Kisangi ni swali la msingi sana.

Mheshimiwa Spika, Wataalam wa Idara ya Hali ya Hewa wanatuambia hivi sasa kiwango cha mvua maeneo mengine kimeshuka. Inaonesha wastani wa mita 1,500 sasa imefika mpaka mita 750, lakini tunakumbuka hivi karibuni tumekumbana na changamoto kubwa sana ya ukame katika Mikoa mbalimbali hasa Mkoa wa Arusha na Mkoa wa Manyara. Katika hili ndiyo maana Serikali tumejielekeza kuelekeza suala zima la utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi, Ibara ya 238(L) kinachosema kwamba kila Halmashauri ipande miti milioni 1.5.

Mheshimiwa Spika, ninawashukuru Wabunge hawa na Watanzania na wadau wengine hatuna jinsi yoyote ya kupambana na hali hii, ni lazima tupande miti kwa kiwango kikubwa sana. Ninawaomba Watanzania wote tushirikiane na Serikali katika kulinda mazingira kupambana na mabadiliko ya tabianchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza.

Kwa kuwa wapo walimu ambao michango yao ilikuwa haikupelekwa na watumishi, lakini wakaambiwa wajilipie wenyewe, wamejilipia wenyewe, wana risiti mkononi, lakini marekebisho ya mafao yao hayakufanyika.

Je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na walimu hao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kwa Mwanachama ambaye alikuwa amesajiliwa kihalali na sahihi kabisa, lakini pia kuna mwajiri ambaye alikuwa na wajibu wa kulipa michango hajatekeleza wajibu wake na badala yake mwanachama akalazimika kujichangia mwenyewe, hilo kwanza siyo sahihi na linahitaji ufuatiliaji.

Kwa hiyo, niombe nipate takwimu sahihi za wanachama hao ambao walifanya hivyo na bado pia hawajaweza kutendewa haki, tulichukue kama ofisi na kwenda kulifanyia kazi, kwa sababu sina takwimu sahihi nitaomba nipate majina lakini pia na takwimu zao ili niende nikafanye ushughulikiaji wa jambo hili, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa gesi asilia ina gharama ndogo sana kuliko ile gesi ya mitungi, na kwa kuwa Serikali imeshawekeza katika Mkoa wa Dar es Salaam, maeneo ya Mikocheni na Msasani: -

Je, Serikali ina mpango gani sasa kuhakikisha gesi hiyo asilia inapelekwa katika wilaya zote za Mkoa wa Dar es Salaam?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inayo azma ya dhati kabisa, na katika bajeti ya mwaka huu imetenga pesa kwa ajili ya kuendelea kupanua miundombinu ya upelekaji wa gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uunganishaji wa gesi asilia kwa mteja mmoja nyumbani kwake kwa miundombinu tuliyokuwa nayo sisi ina-range kutoka milioni mbili mpaka sita kwa mteja mmoja. Kwa hiyo, Serikali inaendelea kutafuta uwezeshaji wa kuweza kutambaza mabomba mengi zaidi katika maeneo yetu na kufikisha miundombinu hii ya gesi ili wananchi walio wengi zaidi waweze kupata nishati hii na kuitumia kwenye maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hili tumefungua milango kwa wawekezaji wengi zaidi ili waje washirikiane pamoja na Serikali kuweza kuendelea kusambaza gesi asilia katika Mkoa wa Dar es Salaam. Lakini tunao mpango wa kuleta mpaka Mkoa wa Dodoma na maeneo mengine ambayo wanaendelea kutumia na kuhitaji nishati ya gesi.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua Kituo cha Afya Tandale katika Wilaya ya Kinondoni ili kipate Jengo la Mama na Mtoto na hasa ukiangalia idadi ya watu wanaoishi katika Kata ya Tandale ni wengi sana? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MIKOA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, tutatuma timu katika kituo hiki cha afya ambacho amekitaja Mheshimiwa Kisangi kufanya tathmini na kuona ukubwa wa eneo uliopo na kama linaweza likahimili kupata majengo mengine. Baada ya tathmini hiyo kufanyika itawasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI ili tuweze kutafuta fedha kwa ajili ya kukipanua kituo hiki cha afya.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Je, Serikali lini itakamilisha kujenga barabara ya Kibamba - Kibwegere mpaka Mabwepande kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara aliyoitaja ipo kwenye mpango wetu kati ya barabara ambazo zipo Dar es Salaam kwa ajili ya kupunguza misongamano ya Dar es Salaam. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami ikiwa pia ni mkakati wa kupunguza foleni kubwa zinazotokea katika Jiji la Dar es Salaam. Ahsante.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali lini itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Kibada, Kisarawe II mpaka Tundi- Songani?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY KASEKENYA MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge Mariam Kisangi Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti iliyopitisha jana barabara hiyo inajengwa kwa kiwango cha lami na iko kwenye manunuzi na tutajenga kilomita 41 kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na juhudi kubwa za Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutujengea barabara ya mwendokasi kutoka Bendera Tatu mpaka Mbagala Rangitatu, lakini bado kuna changamoto kubwa katika maeneo ya Rangitatu.

Je, Serikali lini itakamilisha kujenga tena upya na vizuri kwa kiwango cha lami barabara kutoka Mbagala Kokoto - Rangitatu kwenda Kongowe - Mwandege? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli barabara hii imekuwa na changamoto kubwa hasa ya foleni na Serikali sasa imeiweka kwenye mpango barabara hii ili iweze kujengwa upya na kupunguza foleni kubwa ambayo ni adha kubwa sana kwa wakazi wa Mbagala kwenda Kongowe, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwanza; kwa kuwa changamoto ya miundombinu katika Chuo cha VETA cha Kitangali ni kubwa sana; na kwa kuwa wanafunzi wanaotoka sehemu hiyo wanatoka katika maeneo mbalimbali vijijini. Je, ni lini sasa Serikali itakamilisha mradi huo na kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi wanaotoka sehemu mbalimbali ikiwepo wanaotoka kwenye Jimbo la Mheshimiwa Maimuma Mtanda?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa changamoto ya vijana wanaomaliza Sekondari na Shule za Msingi imekuwa ni kubwa, vijana wengi wanamaliza shule na wengi wanatarajia sasa kwenda kwenye vyuo hivi vya VETA kupata elimu. Je, Serikali ina mkakati gani sasa wa kuhakikisha kwenye hivi Vyuo vya VETA vyote nchi nzima wanaweka miundombinu na mabweni ili watoto mbalimbali wanaomaliza shule kutoka vijijini waweze kwenda kwenye Vyuo vya VETA na kupata mafunzo na ujuzi wa mbalimbali? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI YA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali iliweza kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa baadhi ya mbiundombinu katika chuo hiki; na naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mwaka wa fedha ujao, tutahakikisha kwamba maeneo haya ambayo ameyataja hasahasa katika hiki Chuo cha Kitangali kupitia mapato ya ndani ya VETA tutakwenda kuongeza miundombinu katika eneo hili ikiwemo pamoja na mabweni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali lake la pili, ni kweli tukiri kwamba tunajenga VETA katika wilaya zote Tanzania, lakini focus yetu kwanza ilikuwa ni ujenzi wa miundombinu ya vyuo hivi na tumeweza sasa kukamilisha karibu katika Wilaya 77 nchini. Kuna wilaya chache ambazo bado hatujazifikia, tunaamini katika kipindi kijacho kwanza tutakwenda kukamilisha kwenye wilaya hizi ambazo hazina Vyuo vya VETA, lakini vilevile kuhakikisha kwamba haya maeneo ambayo yana upungufu wa mabweni nao vilevile tunaweza kuwafikia kwa ajili ya kukamilisha miundombinu hii ili wanafunzi wetu, vijana wetu, waweze kupata mafunzo katika maeneo hayo.

Mheshimwa Naibu Spika, nakushukuru sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Mheshimiwa Ikupa, napenda kuuliza swali la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sheria hiyo Na. 9 ya mwaka 2010 ndiyo sheria pekee ambayo inaonesha haki zote za watu wenye ulemavu; na kwa kuwa marekebisho ya sheria hiyo yanategemea marekebisho ya sera: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha inaharakisha mchakato huo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa watu wenye ulemavu wana haki nyingi sana za kimsingi na wapo wengi ambao hawaelewi haki zao za kimsingi ikiwepo upatikanaji wa ajira, elimu na mambo mengine: Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutoa elimu kwa watu wenye ulemavu ili waweze kutambua haki zao na pia kutoa nyongeza katika marekebisho ya sheria hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza, tumeshaanza kufanya kazi ya kufanya mapitio ya Sera ya Watu Wenye Ulemavu kwa sababu sera hiyo ni ya mwaka 2004 na sheria ni ya mwaka 2010. Kwa hiyo, katika kufanya hivyo, sera ndiyo inayotangulia ili iweze kutengeneza mazingira mazuri zaidi na kufanya tathmini na kuwashirikisha wadau wote ili kuweza kujua changamoto za sasa zinazowakumba watu wenye ulemavu ili kuweza kuwahudumia vizuri zaidi na kutunga sheria ambayo itakuwa inaendana na mahitaji halisia katika mazingira yetu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tayari tumeanza kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024. Matarajio yetu, tutakuwa tumemaliza kwenye hatua ya sera, na 2024/2025 tutakuwa tunaenda sasa kwenye kutunga sheria ambapo tayari hatua ya awali tumeshaanza na procedure ya kufanya mabadiliko kwenye sera, kukutanisha wadau, kufanya situational analysis kwenye mikoa na maeneo mbalimbali, na pia kukutanisha mashirikisho ikiwemo Shirikisho la Chama cha Watu Wenye Ulemavu na Shirikisho la Wanawake Wenye Ulemavu na taasisi nyingine zote ambazo zinahusika na haki za watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kama nilivyoeleza, ndani ya mwaka huu wa fedha tutakuwa tumejitahidi kwenye upande wa sera na mwaka wa fedha unaofuata tutakuwa tumeumaliza katika upande wa kutunga sheria ambapo itakuwa muafaka wa kutibu changamoto ambazo zinawakumba watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ameniuliza kuhusiana na haki za msingi za watu wenye ulemavu kwamba wapo wengi ambao hawazifahamu. Tumeendelea kufanya hivyo, mbali na kuwa na sera na sheria ya watu wenye ulemavu, tumekuwa tunasajili pia taasisi mbalimbali ambazo zinaendelea kutoa elimu na kusimamia haki za watu wenye ulemavu.

Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo, upande wa Serikali pia tumeendelea kutoa elimu kupitia vyombo vya habari lakini pia kuyafikia makundi mbalimbali ikiwemo kuunda mabaraza ya kuanzia ngazi ya kata mpaka Taifa ya watu wenye ulemavu ikiwa ni pamoja na kushirikiana na mashirikisho ya watu wenye ulemavu ili kuendelea kutoa elimu.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kufanya hivyo pia, alitoa fedha zaidi ya shilingi bilioni tatu kufufua vyuo zaidi ya saba vya watu wenye ulemavu ambapo tumeshafanya kazi hiyo. Lengo ni kuwapa fursa zaidi watu wenye ulemavu na kuwaingiza waweze kujitegemea. Zaidi tumeboresha hata mwongozo unaotoa haki kwa watu wenye ulemavu kupata mikopo ya asilimia mbili kutoka kundi la watu wenye ulemavu watano na sasa mkopo anaweza kupata mtu mwenye ulemavu mmoja na tunaweza kumpa mkopo wa kuanzia shilingi milioni moja hadi milioni hamsini.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jitihada za Serikali zinazofanyika ni kubwa, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Je, Serikali ina mpango gani wa kupanua au kurekebisha barabara ya Kilwa kipande cha Mbagala Zakheim kutoka Zakheim mpaka Mzinga, kwa sababu kipande hicho kimekuwa na changamoto, unatoka huko lakini unafika pale magari hayaendi, kunakuwa na msongamano mkubwa sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, nimshukuru Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, barabara zote za Dar es Salaam kulingana na ukuaji wa mji zinafanyiwa study kuona barabara zote ambazo zina changamoto zinafanyiwa marekebisho, ikiwa ni pamoja na kuongeza upana wa barabara hizo, na siyo za Dar es Salaam tu hata barabara za Mikoani ambazo zilijengwa zamani nyingi zilikuwa na upana mdogo.

Kwa hiyo, sasa hivi hizo barabara zinapitiwa upya ikiwa ni pamoja na barabara aliyoitaja ili kuhakikisha kwamba sasa tunakwenda kwa kipindi cha sasa kuzipanua hizo barabara, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Mbande ya Chamazi katika Mkoa wa Dar es Salaam ni kata ambayo ina idadi kubwa ya watu, lakini wana Zahanati ya Mbande: Ni lini sasa Serikali itaipandisha Zahanati ya Mbande kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mama Mariam Kisangi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba idadi ya wananchi katika Kata ya Mbande kule Chamazi ni kubwa na Zahanati ile ya Mbande kwa kweli inazidiwa na idadi ya wananchi na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeshaainisha kwamba eneo la Zahanati ya Mbande ni sehemu ya eneo la kimkakati kuona uwezekano wa kujenga Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tunalifanyia kazi na tutahakikisha kwamba tunatafuta eneo linalotosheleza kama lile la Zahanati linatosha ama tunahitaji kupata eneo lingine kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kwa manufaa ya wananchi walio wengi katika eneo lile, ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Kwa kuwa matatizo ya moto yamekuwa mengi sana katika nchi yetu na hasa katika maeneo ya shule na masoko, lakini kumekuwa na changamoto kubwa ya magari ya zimamoto kufika maeneo ya tukio bila ya kuwa na maji. Tatizo hili limekuwa ni kubwa kiasi kwamba watu wanakata tamaa na Jeshi lao la Zimamoto. Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na changamoto hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa katika nchi yetu kumekuwa na miradi mingi ya kimkakati ya Serikali kama vile standard gauge, Bwawa la Mwalimu Nyerere pamoja na bomba lile la mafuta la Chongoleani Hoima, je, Serikali imejipanga vipi katika kuweka tahadhari ya moto katika maeneo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la mwanzo la kwamba magari yanafika yakiwa hayana maji, naomba leo nisaidie kuweka sawa hisia hizo kwa kusema yafuatayo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kawaida gari lenye uwezo wa kubeba lita 5,000 litakapofika kwenye eneo lenye athari ya moto, kwa pressure yake linaweza likazima moto kwa dakika mbili maji yale huwa yamekwisha. Sasa wananchi wana-tend kuamini kwamba halina maji linaenda kutafuta maji mengine. Ila ni kwa sababu dakika mbili tu lita 5,000 zinakuwa zimemalizika. Haiwezekani gari yetu iende kwenye tukio la kuzima moto halafu haina maji na kiuzoefu gari linapokuwa lime-park, always linakuwa na maji. Kwa hiyo, wananchi waondoe dhana hiyo potofu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juu ya kuchelewa kufika ni changamoto ya miundombinu yetu, lakini na shughuli za kibinadamu zinazofanyika kwenye maeneo ambayo gari hilo linapita. Kama kila mwananchi ataelewa na akasaidia kufungua njia wakati wa dhararu kama hizo, tatizo kama hili litapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali kuzingatia miradi ya kimkakati ikiwemo Bwawa la Mwalimu Nyerere, SGR, bomba la Chongoleani, napenda nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote kwamba maeneo yenye uwekezaji wa kimkakati kama hizi kwa maana ya vital installation kuweka tahadhari ya kudhibiti matukio ya kuzima moto ni kipaumbele cha juu cha Serikali. Kwa hiyo, namhakikishia Bwawa la Mwalimu Nyerere na miradi mingine kama hiyo itazingatiwa katika kuwekewa magari na vifaa vya kuzima moto na uokoaji, ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Kata ya Mbande ya Chamazi katika Mkoa wa Dar es Salaam ni kata ambayo ina idadi kubwa ya watu, lakini wana Zahanati ya Mbande: Ni lini sasa Serikali itaipandisha Zahanati ya Mbande kuwa Kituo cha Afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mama Mariam Kisangi, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba idadi ya wananchi katika Kata ya Mbande kule Chamazi ni kubwa na Zahanati ile ya Mbande kwa kweli inazidiwa na idadi ya wananchi na sisi Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumeshaainisha kwamba eneo la Zahanati ya Mbande ni sehemu ya eneo la kimkakati kuona uwezekano wa kujenga Kituo cha Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba jambo hilo tunalifanyia kazi na tutahakikisha kwamba tunatafuta eneo linalotosheleza kama lile la Zahanati linatosha ama tunahitaji kupata eneo lingine kwa ajili ya kujenga Kituo cha Afya kwa manufaa ya wananchi walio wengi katika eneo lile, ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Nataka kuuliza Je, Serikali katika hivyo vyuo 36 itakavyojenga na Wilaya ya Ubungo nayo imo katika orodha hiyo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ambazo hazina vyuo hadi hivi sasa ni Wilaya 62 na katika bajeti yetu ijayo Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi katika Wilaya 36, ni ukweli usiokuwa na shaka kwamba siyo wilaya zote zitakazoweza kupata kwa hiyo tunaweka vigezo na vielelezo vya demand analysis ili kuhakikisha yale maeneo yenye uhitaji mkubwa ndio tunaweza kujenga kwanza halafu vingine tutakwenda kujenga katika mwaka ujao wa fedha, nakushukuru sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza; kwa kuwa Fungu la CSR linaikumba pia Halmshauri yetu ya Ilala kwenye kupitisha bomba la gesi.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha na sisi kwenye Halmashauri ya Jiji la Ilala kupewa ile mrabaha wa kupitisha lile bomba la gesi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwamba maeneo yote ambayo kuna miradi ya makampuni sheria ifuatwe ili waweze kupata ile huduma ya jamii kwa maana CSR. Kwa hiyo, ninamhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba sheria zipo kanuni zipo. Tutahakikisha kwamba Halmashauri ya Ilala pia inapata haki yake kutokana na ujenzi wa bomba hili la gesi, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, niipongeze Serikali kwa ujenzi wa visima vya Kimbiji na Mpera. Mradi ule ni wa muda mrefu lakini umekamilika tunaipongeza sana Serikali. Mradi huo kukamilika kwake kumepelekea kupatikana kwa maji ya bomba safi na salama katika Kijiji cha Tungi Songani, Kata ya Pembamnazi, Wilaya ya Kigamboni, lakini kumekuwa na changamoto ya kutopatikana maji hayo sasa pamoja na kujengwa kwa mradi ule katika eneo hilo na wananchi walipata maji haya kwa muda na sasa hawapati tena.

Je, Serikali ina kauli gani kuhusiana na changamoto hiyo inayowakuta akina mama wa Pembamnazi Kijiji cha Tundu Songani, kukosa huduma hiyo ya maji safi?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge, Mama yangu Mariam. Ni kweli katika Eneo la Kigamboni tumejenga mradi mkubwa takribani wa tanki la lita milioni 15 kwa ajili ya kuhakikisha wana-Kigamboni wanapata huduma ya maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepata hii taarifa, kwa kuwa ni mpya naomba niipokee na niweze kuifanyia ufuatiliaji kwa haraka ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo ya Kigamboni wanaenda kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa mkakati wake wa kuhakikisha kwamba sasa tunakwenda kupata nishati safi na salama ya kupikia. Ni jambo kubwa, tunampongeza sana na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamelipokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam wamehamasika na wako tayari katika matumizi ya nishati safi ya gesi ya kupikia, lakini kwa kuwa changamoto kubwa ni gharama ya hiyo gesi na Serikali imeonesha mipango ya kusambaza gesi hiyo ambayo ina gharama nafuu kwa wananchi, je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuelekeza nishati hiyo au mabomba hayo kwenye maeneo yenye wananchi wengi kama Kawe, Mwenge, Mbagala, Manzese na maeneo mengine, badala ya ku-base kwenye eneo hilo hilo la Mbezi Beach na Mikocheni peke yake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tunao mpango wa kuhamasisha matumizi ya gesi asilia nchini, na kwa sasa hivi tunao mkakati wa kupeleka gesi kwenye nyumba takribani 10,000. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba maeneo hayo ambayo ameyataja yenye watu wengi yatafikiwa na huduma hii ili waweze kutumia gesi kwa gharama nafuu zaidi kwa sababu gesi hii inayounganishwa majumbani ina unafuu zaidi kuliko gesi ile ya LPG ya mitungi. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza wauguzi na waganga katika Zahanati ya Makuburi na Mavurunza katika Halmashauri ya Ubungo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge Mariam kwamba tunatambua kwamba vituo hivyo vinahudumia wananchi wengi sana na vinahitaji kuongezewa watumishi. Tayari Serikali imeshatambua pengo la watumishi katika vituo hivyo na katika ajira hizi tutapeleka watumishi. Pia tutaendelea kupeleka watumishi kwa awamu kadri ya vibali vya ajira vinavyojitokeza. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuboresha treni inayotoka stesheni kwenda Pugu inayojulikana kwa jina la treni ya Mwakyembe kwa kuweka miundombinu ya vituo ili kuepusha ajali zinazojitokeza baina ya treni na magari?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli treni hizi ambazo zinatusaidia sana Mji wa Dar es Salaam, hususan kipindi cha asubuhi na jioni ambacho kunakuwa na foleni kubwa kuna changamoto baadhi ya maeneo. Sisi upande wa Shirika, kupitia Shirika letu la reli nchini tumejipanga kuboresha maeneo yote hususan maeneo yale ya makutano kati ya barabara na treni ili kuweka alama. Na alama hizi zitaenda na elimu pia kwa jamii katika mazingira hayo kwa sababu wakati mwingine treni inapopita kunakuwa na changamoto pia ya watu kupita na huwa zinatokea hizo ajali. Kwa hiyo tumejipanga kutoa hiyo elimu, lakini tutaendelea kushirikiana na vyombo vingine vya Dola hususan Polisi kwa ajili ya kuelimisha jamii katika maeneo hayo ambapo kuna makutano kati ya barabara na reli. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mito ya Nyakasangwe, Mbezi, Mpiji na Tegeta hiyo mito ni mito mikubwa na imeathiri sana familia zilizopo kule, nyumba zote zimebomoka, kwa mfano Mto Tegeta majumba yanaondoka, maji yamejaa kwenye maeneo ya wazi, watu wanashindwa kuishi vizuri na wanashambuliwa na magojwa kutokana na kujaa kwa maji hayo.

Je, Serikali sasa haioni kuna hatua gani za muda mfupi za kuliangali suala hili badala ya kusubiri hiyo bajeti ambayo inajumuisha maeneo kadhaa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa utaongozana na Mbunge wa Kawe Mheshimiwa Askofu Gwajima uende ukaone hali halisi ya Jimbo la Kawe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumeeleza kwenye jibu letu la msingi, moja ni kwamba tumetenga fedha hizo na bahati nzuri tayari bajeti hii ndiyo inaendelea kumalizika, maana yake once tutakapopata fedha hizo tunakwenda kuanza huo upembuzi yakinifu, lakini kama nilivyoeleza tena kwenye jibu la msingi kwamba tayari tumeshaingia makubaliano na makubaliano haya yanakwenda kuanza haraka sana iwezekanavyo hapo mbele, ndani ya mwaka huu yanaanza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe tu Mheshimiwa Mbunge aendelee kuwa na subira, Serikali inatambua changamoto iliyokuwepo, inatambua wananchi wanapata shida lakini na sisi tupo mbioni kufanya hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, aidha nimwambie Mheshimiwa Mbunge, nipo tayari kuhakikisha kwamba tunakwenda na tunafuatana pamoja tunakwenda Jimboni Kawe kwenda kuona hali ilivyo na kuona namna ya kuweza kuwasaidia wananchi, nakushukuru. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuliboresha Soko la Stereo Temeke liendane na ukuaji wa Mji wa Temeke?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumekwishafanya tathmini ya masoko makubwa ya kimkakati katika halmashauri zetu zote ikiwemo Halmashauri ya Temeke katika Soko lile la Stereo. Tayari Serikali imeshaweka mpango kwanza kupitia mapato ya ndani ili ianze kutengwa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wakati Serikali Kuu inatafuta fedha kwa ajili ya kuunga mkono juhudi hizo. Kwa hiyo, naomba nitumie fursa hii kumwelekeza kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke kuweka kipaumbele katika bajeti zake ili tuanze kuboresha Soko la Stereo. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na juhudi kubwa za Serikali, lakini bado kuna changamoto. Kwa kuwa, zao la nazi ni zao la kiuchumi katika ukanda wa Pwani na Zanzibar, minazi mingi imekuwa ikifa kwa kushambuliwa na magonjwa na hakuna juhudi mbadala. Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuinusuru minazi inayokufa na inayoshambuliwa na magonjwa katika ukanda wa Pwani na Zanzibar?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa minazi mingi ni ya muda mrefu na hasa katika Mikoa ya Dar es Salaam, Lindi, Pwani, Mtwara, Tanga na Zanzibar na inakufa na hakuna juhudi yoyote ya kuimarisha zao la minazi: Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu katika mashule pamoja na vyombo mbalimbali vya habari ili kuimarisha zao hilo la mnazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe shaka Mheshimiwa Mbunge kwamba Wizara ya Kilimo moja ya kazi kubwa tunayoifanya ni kwamba tumeandaa mipango wa muda mfupi, mpango wa kati na mpango wa muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mipango ambayo tunaendelea nayo sasa hivi ni kuendelea kufanya tafiti ili kukabiliana na magonjwa. Ndiyo maana ukiona katika jibu la msingi tumepata mbegu mpya ambayo inaweza kukabiliana na magonjwa ya nazi, kwa hiyo, tutaendelea kufanya hivyo kwa wakulima wote wa Kanda za Pwani na tutaendelea kutuma wataalamu wetu waendelee kufanya tafiti kukabiliana na hayo magonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu elimu, tutaendelea kutoa elimu mashuleni na huo ndiyo mpango tuliokuwanao sasa hivi, isipokuwa tu tutaongeza kasi ili uweze kuanzia level ya shule kwa maana ya wanafunzi mpaka kufika kwa wanakijiji ambao ni wakulima, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza; kwa kuwa matibabu ya kusafisha figo ni gharama kubwa ni kuanzia shilingi 145,000 mpaka 350,000 na gharama hiyo ni kubwa sana kwa Mtanzania wa kawaida, kwa kuwa Serikali mnaelekeza kwamba, mpaka Muswada utakapokuja wa Bima ya Afya kwa wote ndiyo tuangalie punguzo la hilo.

Je, Serikali kwa nini sasa kwa wale ambao wameingia mpango wa Bima ya Afya kujipimia tena wana vifurushi vikubwa, wasipewe huduma hiyo mpaka tusubiri huo Muswada wa Bima ya Afya kwa wote jambo ambalo ni gumu kama mmeshindwa kwa wachache mtaweza kwa wengi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa matatizo haya ya figo yanakua kwa kasi, na tafiti zinaonesha kwamba zilizofanyika katika Mikoa ya Kaskazini asilimia 6.8 ya Watanzania wana magonjwa ya figo pasipo kujitambua.

Je, Serikali imejipanga vipi sasa katika kutoa elimu kwa wananchi wake kujua dalili na matatizo hayo yanatokana na nini, kwa sababu yanakuja ghafla? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge.

Kwanza, kwamba kuna watu wanaolipa kifurushi kikubwa cha Bima ya Afya na kwa nini wanashindwa kupata hiyo huduma. Mheshimiwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ameshaelekeza kwamba watu wanaokata vifurushi vyao wapate hiyo huduma. Kwa sababu tujiulize maswali, ukienda kwenye private sector utakuta bei ni ileile na ukirudi kwenye Serikali bei ni ileile, lakini wakati huo private sector wao wenyewe ndiyo wananunua vifaa, wanajenga na wanafanya mambo mengine na kulipa mishahara. Serikalini, kujenga na kununua vifaa vinafanyika na Serikali, kwa maana hiyo ndiyo maana Waziri wa Afya ameita timu ya kukaa chini ili kujadili ni namna gani tuweze siyo tu kuwasaidia wale wenye vifurushi vikubwa vya bima lakini hata wagonjwa wengine wasio na bima, ishuke kabisa hata ikiwezekana kuwa Shilingi 50,000 kwa mtu mmoja badala ya bei ya Shilingi 900,000 kwa wiki ambayo ipo sasa. Kwa hiyo, Waziri analifanyia hilo kazi na siyo muda mrefu tutapata majibu kuanzia tarehe Mosi Julai, 2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli hata kwa dunia, sisi kwetu ni asilimia Sita ya watu wanaonesha kuna hilo tatizo lakini kwa dunia ni asilimia 10, ni tatizo la kidunia siyo la Tanzania peke yake. Kwa hiyo, kimsingi Serikali inajipanga moja kuhakikisha kwamba tunatoa elimu kama unavyosema na wewe ni mmojawapo wa mdau ambaye wa kutusaidia kwa sababu kuna masuala mazuri kwamba sisi wenyewe tujipange namna tunavyokula, kufanya mazoezi na mambo mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa Serikali ndiyo maana unaona kuna mjadala mkubwa wa usalama wa chakula na usalama wa madawa. Tunakwenda kuboresha eneo la usalama wa chakula ili kuhakikisha kwamba tunapunguza matukio kama haya, lakini utaona hamasa kubwa iliyokuwa inafanyika hasa wakati wa Corona tufanye mazoezi, tule vizuri, tuhakikishe kwamba tunakula vyakula ambavyo siyo vya protini za wanyama tule zaidi protini za mimea na vitu vingine kama hivyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukifanya hivyo nasi Wabunge tunapofanya mikutano yetu tuendelee kuhamasisha zile tabia nzuri za afya, mimi naamini tutapunguza haya matatizo ambayo yanatokea. Pia wote tuwe wadau hasa kwenye suala zima la usalama wa chakula na masuala ya chakula kuingia na kufikiriwa katika angle ya kibiashara zaidi badala ya kufikiriwa kwenye angel ya usalama wa nchi hatutaweza kutoka, ndiyo maana nasema tushirikiane pamoja kuhakikisha wafanyabiashara hawatusukumi hasa kwenye eneo la chakula, vyakula vyote vinavyozalishwa na wadau ni kusimamia usalama, tuungeni mkono.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Je, Serikali ina mpango gani wa kuiongeza na kuipandisha hadhi Zahanati ya Ununio ambayo itawasaidia sana wananchi wa Tegeta, Boko, Ununio, Mtongani na Kunduchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipandisha hadhi baadhi ya zahanati kuwa kituo cha afya. Moja ya vigezo ambavyo vinatumika ni ukubwa wa eneo ambapo zahanati ipo, kama linatosha kujenga miundombinu ya kituo cha afya, pia idadi ya wananchi wanaohudumiwa katika eneo hilo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kulifanyia kazi suala la Zahanati ya Ununio.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina uhakika sana na ukubwa wa eneo lake kwa sababu napafahamu. Kama eneo litakuwa linatosheleza lakini pia kama litakidhi vigezo vingine basi Serikali italifanyia kazi ili kuweza kuipandisha hadhi na kama haikidhi tutaona namna nzuri zaidi ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata huduma bora za afya. Ahsante sana.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Mkoa wa Tanga umezungukwa na bahari, pamoja na mipango mizuri ya Serikali; je, Serikali haioni haja sasa ya kutoa mafunzo kwa wavuvi wa Mkoa wa Tanga kupitia Chuo cha VETA cha Tanga Mjini na Mkinga kama vile walivyofanya wenzao wa Chato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa Mkoa wa Dar es Salaam umezungukwa na Bahari ya Hindi sehemu za kuanzia Jimbo la Kawe mpaka kule Jimbo la Kigamboni limezungukwa na Bahari ya Hindi lakini sioni kama kuna mpango wowote wa kujenga kiwanda cha kuchakata mazao ya samaki. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kujenga Kiwanda cha Kuchakata Samaki katika Mkoa wa Dar es Salaam? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la kwanza kwamba kutoa mafunzo kwa wavuvi katika Mkoa wa Tanga. Kwanza Wizara tayari imeshaanza kutoa mafunzo kwa wavuvi katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa hivyo tuko tayari pia kuendelea kutoa mafunzo katika Mkoa wa Tanga na kama specific Mheshimiwa Mbunge anajua kuna wavuvi wanahitaji mafunzo pia tuko tayari kuwapa elimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari tumeshaendelea kutoa mafunzo katika Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika na maeneo mbalimbali na sasa tuko tayari kutoa mafunzo katika Mkoa wa Tanga kwa wavuvi wanaozunguka kwenye Bahari ya Hindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mpango wa kujenga viwanda pembezoni. Kama nilivyosema kwenye jibu la msingi kwamba mwambao wa Bahari ya Hindi Serikali tayari ina mpango wa kujenga kiwanda kule Tanga kupitia wawekezaji. Pia, wale maeneo ya Dar es Salaam tuko tayari kujenga viwanda vya kuchakata mazao ya bahari. Kwa mfano kule TAFICO tunafufua hilo Shirika letu la TAFICO ambalo litakuwa na uwezo wa kuchakata mazao yetu ya baharini kwa ajili ya kuyaongeza uthamani, kuongeza ubora na kuyafanya kuwa na thamani katika mazao yetu yote ya baharini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nimhakikishe Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inaendelea kujipanga kuhakikisha kwamba tunaongeza viwanda lakini pia tunahamasisha wawekezaji mbalimbali kupitia maeneo mbalimbali ambao wako tayari kuwekeza katika eneo hilo pia tunahamasisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata Mheshimiwa Mbunge kama ana nafasi hiyo tunamwomba pia na yeye tushirikiane kwa pamoja kuhamasisha wawekezaji wa mazao hayo ili tuweze kuongeza viwanda vya samaki. Ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto zinazolikuta Jimbo la Kawe zinafanana kabisa na zile za Jimbo la Kigamboni, maeneo ya Kisarawe II, maeneo ya Kigogo ya Viwandani, Mwasonga, Tundwi Songani, Kimbiji na Mkundi katika Kata ya Pemba Mnazi, maeneo haya barabara zimeharibika kabisa na mvua.

Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kurekebisha barabara hizo ili zikae vizuri na wananchi wa maeneo hayo waweze kupita vizuri? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa kupaza sauti yake ili kuhakikisha wananchi wanaweza kutengenezewa barabara hizi ambazo ni muhimu sana kiuchumi, lakini kijamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba niendelee kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kila mwaka wa bajeti inatenga fedha kwa ajili ya kuhudumia barabara hizi za TARURA ikiwemo katika Jimbo la Kigamboni.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuna nafasi ya Mkurugenzi kutumia mapato ya ndani kwa ajili ya kuhakikisha na yeye anaweza kusimamia katika kurekebisha barabara hizi. Mheshimiwa Mbunge ule Mradi wa DMDP II ambao ni mradi wa jumla ya USD milioni 438 na wenyewe unaenda kunufaisha Manispaa ya Kigamboni.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hatua hii tayari kazi zilishatangazwa na tayari wakandarasi wameshapatikana, ipo katika hatua za mwisho kabisa za ununuzi na mikataba itasainiwa ili wakandarasi waingie site waanze sasa kurekebisha barabara. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa, barabara hiyo ni ya muda mrefu sana na ukarabati unaofanyika wa vipande vipande umesababisha barabara hiyo kuwa mbovu zaidi, je, Serikali haioni haja sasa ya kuijenga upya barabara hiyo, kipande cha kutoka Kongowe – Mjimwema?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Changamoto ya barabara pia, inaikumba Ilala kipande cha kutoka Mvuti – Dondwe – Magereza – Kiwamwi, Mkoa wa Pwani. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuikamilisha barabara hiyo ili kuwasaidia wananchi wa Jimbo la Ukonga wanaotoka Mvuti waweze kufika Dondwe pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara ya Kongowe – Mjimwema ni barabara ya muda mrefu na imechoka, lakini kwa sasa wakati tunatafuta fedha, moja ni kuifanyia usanifu na kuipanua kwa sababu sasa imekuwa ni barabara ambayo imekuwa na traffic kubwa kwa maana ya magari mengi. Kwa hiyo, tunafanya usanifu ili kuipanua, lakini wakati tunatafuta fedha hiyo, ni lazima sasa hivi tuhakikishe kwamba magari yanapita kwa kuifanyia hayo matengenezo ya kawaida ambayo ni ya lami.

Mheshimiwa Spika, kuhusu Barabara ya Mvuti – Dondwe, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa sisi Wizara ya ujenzi na hasa TANROADS, tukitoka Chanika – Mvuti barabara yetu hasa tunayoihudumia ni ile inayoenda Mbagala. Kuanzia Mvuti – Dondwe – Magereza inahudumiwa na wenzetu wa TAMISEMI. Kwa hiyo, nina uhakika tutawasiliana ili waweze kuona namna ya kuiboresha na pengine kuiweka katika mipango ya kuijenga kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, changamoto ya ongezeko la viwanda na watu liko katika Mkoa wa Dar es Salaam, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza dampo katika Mkoa wa Dar es Salaam kwa sababu dampo kuu ni lile la Kinyamwezi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ni kweli kwamba Jiji la Dar es Salaam lina idadi kubwa ya wananchi na viwanda, kwa hiyo, uzalishaji wa taka ngumu nao umeendelea kuongezeka.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali pia imeendelea kuweka mipango katika kila Manispaa ya Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Dar es Salaam, kutenga maeneo kwa ajili ya kujenga madampo. Pia tutaendelea kufanya tathmini kuona namna ambavyo tutaongeza madampo makubwa zaidi ili kuendana na kasi ya uzalishaji wa taka katika Mkoa wa Dar es Salaam.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa changamoto ya ukosefu wa hati miliki na uzio katika maeneo haya ya wazee imekumba Makazi ya Wazee Nunge, Vijibweni, Kigamboni, hali ambayo imeleta mgogoro mkubwa baina ya wananchi wa maeneo yale. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kufuatana na mimi kwenda kuona changamoto iliyopo katika Makazi ya Wazee ya Nunge, Kigamboni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMIII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Naibu Spika, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Kisangi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nipo tayari kufuatana na Mheshimiwa Mbunge nitakapomaliza Bunge hili kuona utaratibu mzuri wa Nunge ili tuweze kuukamilisha vizuri kwa kutenga fedha kwa ajili ya wananchi wetu. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, lini Serikali itarekebisha majengo na kuweka vitendea kazi katika Kituo cha Polisi cha Wilaya Mbagala?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Kisangi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, tunatambua Mbagala ni eneo ambalo lina wakazi wengi, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutatenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Kituo cha Polisi cha Mbagala pia kinapata fedha kwa ajili ya kukarabatiwa ili waweze kutoa huduma kwa wananchi wetu.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa lishe katika nchi yetu imekuwa na changamoto kubwa sana, tunashuhudia watu wakiwa na uzito wa kuzidi, lakini wengine wakiwa na upungufu kabisa wa uzito wa chini hali ambayo inasababishwa na ukosefu wa lishe bora, je, Serikali haioni haja ya kuhakikisha au kupanga mpango wa haraka ili kuhuisha taasisi hii ili iweze kufanya kazi kwa wananchi wetu waweze kupata lishe bora au elimu bora zaidi kwa kutumia taasisi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa sababu siku zote amekuwa ni Mbunge anayefatilia masuala ya afya kwenye mkoa wake na hasa zaidi anavyofuatilia wagonjwa mbalimbali kwenye makundi mbalimbali waweze kusaidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza amesema tumetoka kwenye eneo ambalo tulikuwa tunapambana na ukondevu. Nchi yetu kwa sababu ya kupiga stage ya kimaendeleo na kazi kubwa ambayo imefanywa na Rais wetu na Serikali yetu ya Chama Cha Mapinduzi, leo tunapambana na watu kula vyakula kwa maana ya kuongezeka uzito mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimwambie Mheshimiwa Mbunge, ndiyo maana tunakwenda kuanzisha hii programu ya lishe. Nataka kuwahakikishia kuwa elimu itaenda kutolewa kwa kasi kubwa sana na ndiyo maana wakati wote nimekuwa nikiwasisitiza Wabunge na Watanzania kwamba elimu mbalimbali zinazotolewa na wataalamu wa afya, lakini elimu anayoitoa Mheshimiwa Prof. Janabi na Madaktari wengine wote, tuhakikishe tunasikiliza na kufuatilia ili tuweze kuishi maisha ya afya.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa changamoto ya ukosefu wa umeme wa Gridi ya Taifa, lakini pia mitambo mizuri ya umeme inawakumba wananchi wa Kigamboni katika Kata za Kigamboni, Vijibweni, Mji Mwema, Gezaulole, Somangira, Kibada, Kisarawe II na Mwasonga kukosa umeme wa uhakika kwamba ikifika saa 12.00 jioni kunakuwa na low voltage kiasi kwamba maeneo hayo huwezi kupika, huwezi kuwasha microwave, huwezi kuwasha chombo chochote na umeme unakuwa kama wa kibatari.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni kweli kwa yale maeneo ya Kigamboni ikifika jioni umeme unakuwa na low voltage. Serikali tayari imekwishaanza kulifanyia kazi jambo hilo. Kupitia Kituo cha Kupooza Umeme cha Mbagala tumeongeza transfoma nyingine ili kuhakikisha kwamba tunaongeza nguvu ya umeme kwa ukanda wote ule kuanzia Kigamboni, Mbagala mpaka kwenda Pwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, transfoma ile imekwishafika na mkandarasi yuko site. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inafanya kila jitihada ili kuhakikisha kwamba wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam hususan maeneo ya Mbagala, Kigamboni na Pwani wanaendelea kupata umeme wa uhakika na hivi karibuni mradi utakamilika na umeme utakuwa wa uhakika, ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa kwa ruhusa yako naomba nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuboresha vyuo vyote vya wenye ulemavu ikiwemo kile cha Yombo, Ilala - Dar es Salaam, Masiwani – Tanga na Luwanzari - Mwanza vyuo hivi vilikuwa katika hali mbaya na sasa vina mazingira mazuri sana pongezi kwake Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kulijali kundi hili muhimu la watu wenye ulemavu. Sasa naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwenye vyuo hivi vya wenye ulemavu ambavyo nimevitaja hapo mwanzo vina wanafunzi ambao wana ulemavu wa aina mbalimbali na kuna wenye ulemavu wa viungo ambao wana changamoto kubwa ya kufanya zile kazi za kiufundi, lakini pia idadi ya walimu kwenye vyuo hivyo hailingani na idadi ya wanafunzi kwa sababu wanafunzi wale wanatakiwa sasa idadi yao iwe mwanafunzi mmoja kwa mwalimu mmoja au wanafunzi wawili kwa mwalimu mmoja.

Je, Serikali haioni haja sasa yakuvifanya hivi vyuo viwe inclusive ili wanafunzi wale waweze kusaidiana wenyewe kwa wenyewe? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa kwenye Shule ya Msingi Wailesi iliyopo katika Wilaya ya Temeke kuna kitengo cha watoto wenye ulemavu wa ubongo ambao wao wanasoma pale kwenye elimu jumuishi na wanapofikia hatua fulani wanapelekwa kwenye kujifunza mafunzo ya ufundi na chuo hicho hakina mapato yoyote wala hakipewi ruzuku yoyote kutoka Serikalini.

Je, Mheshimiwa Waziri muhusika yupo tayari kufuatana na mimi kwenda kwenye hiyo Shule ya Msingi Wailesi iliyopo katika Wilaya ya Temeke? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM K.n.y. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumpongeza Mheshimiwa Mariam kwa kufuatilia watu wenye ulemavu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan inawajali sana watu wenye ulemavu na ndiyo maana imejenga shule ambazo mchanganyiko na watu ambao wasio walemavu ili waweze kuwasaidia katika kazi wanazozifanya na kuwapa vifaa vya kuwasaidia ili waweze kuwa na uelewa rahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, Serikali ipo tayari na Wizara husika kwenda kwenye chuo hicho kuangalia mazingira yaliyopo ili kuweza kuwasaidia kwa umakini, ahsante. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri mimi kwanza naipongeza Mamlaka ya Hali ya Hewa inafanya kazi nzuri sana ya kutoa tahadhari ya hali ya hewa ya nchi yetu na tahadhari ambazo ni za ukweli kwa asilimia kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa taarifa za hali ya hewa zinatolewa mapema sana, lakini Serikali haichukui hatua za mapema matokeo yake kunatokea madhara makubwa sana kama vile inaponyesha mvua kubwa katika maeneo mbalimbali. Je, mamlaka zinazohusika zina mpango gani sasa wa kuhakikisha wanafanyia kazi taarifa za hali ya hewa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa tumeshuhudia kunyesha kwa mvua kubwa katika maeneo na kusababisha mafuriko kama vile ya Rufiji, Kibiti, Kilwa, Lindi na Arusha - King’ori kulitokea mvua kubwa, madaraja yakavunjika mpaka gari la wanafunzi likaingia kwenye daraja.

Je, Serikali imejipanga vipi sasa kutoa taarifa pale inapotokea mvua inanyesha angalau kusimamisha masomo kwa wanafunzi wa shule za msingi na nursery school? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ninamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutoa pongezi kwa Mamlaka yetu ya Hali ya Hewa kwa kazi kubwa ambayo wanafanya na hii ni kutokana na uwekezaji mkubwa sana ambao Serikali imefanya katika kuiwezesha mamlaka hii itoe taarifa sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili, amezungumza kuhusu kufanyia kazi, Mamlaka ya Hali ya Hewa ina jukumu kubwa la kuangaza, kukusanya, kuchakata pamoja na kuhifadhi na kusambaza taarifa za hali ya hewa na mara baada ya kukamilisha jukumu hilo la kwanza, jukumu la pili ambalo linafanyika sasa ni namna gani taarifa hizo zinakwenda kuwafikia wananchi mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri tunayo sheria ya mwaka 2006 ambayo ni Sheria yetu ya TMA inaipa mamlaka kufanya kazi hiyo, lakini pia tuna Sheria ya Maafa Namba 6 ya mwaka 2022 ambayo kimsingi inatoa nafasi kwa Kamati zetu za Maafa mbalimbali nchi nzima. Mara baada ya kupokea taarifa za TMA, kuhakikisha kwamba zinasambazwa na kufikishwa katika maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo Serikali kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali imeendelea kutoa elimu mbalimbali kwa wananchi kupitia vyombo vya habari, kuimarisha mifumo yetu ya tahadhari pamoja na kujenga uwezo wa watendaji ili kuhakikisha kwamba taarifa zinakuwa sahihi, lakini pia zinafika kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamshukuru pia kwa swali lake la pili juu ya ushauri alioutoa kwamba pengine inapotolewa taarifa hizo za hali ya hewa pengine kutakuwa labda na kimbunga na kadhalika, ni vyema shule zikafungwa. Ushauri huu ni mzuri na sisi kama Serikali tumeupokea, tutaenda kuuchakata na kuufanyia kazi hatua kwa hatua. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Je, Serikali ina mapango gani wa kuipandisha hadhi zahanati ya Toangoma kuwa Kituo cha Afya kwa kuwa Kata ya Toangoma ina idadi kubwa ya watu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Tulikwishatoa maelekezo na mwongozo unaelekeza hatua za kufuata kwa zahanati ambazo zina sifa ya kupandishwa hadhi kuwa vituo vya afya. Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigamboni, kufanya tathmini kwa kushirikiana na Mganga Mkuu wa Halmashauri na Mganga Mkuu wa Mkoa, kuona kama vigezo vyote kwa maana ya eneo na idadi ya wananchi vinakidhi kuwa na zahanati na kupandishwa hadhi kuwa kituo cha afya ili tuweze kuanza hatua za upandishaji wa kituo cha afya. (Makofi)
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati na kuweka jengo la upasuaji katika Kituo cha Afya cha Round Table Mbagala Kizuiani? Kituo hicho ni cha muda mrefu, mama anapozidiwa inabidi atafutiwe gari kupelekwa Temeke au Zakiem, Serikali ina mpango gani sasa wa kuweka jengo la upasuaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Afya cha Round Table kule Mbagala ni kituo cha muda mrefu na ni kituo ambacho kinahudumia wananchi wengi. Serikali tulishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa Halmashauri kuweka kipaumbele kwenye vituo vya afya ambavyo vina uhitaji mkubwa wa majengo, kama Kituo cha Round Table kule Mbagala.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ninaomba nitumie nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inalichukua jambo hili kwa uzito unaostahili, lakini nimuagize Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kwenda kufanya tathmini ya mahitaji ya fedha ambazo zinatakiwa kuboresha kituo hicho cha afya, kuwasilisha Ofisi ya Rais, TAMISEMI, lakini pia kufanya tathmini ya uwezo wa mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuanza ukarabati wa kituo hicho cha afya mapema iwezekanavyo. Ahsante.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa majibu mazuri. Pamoja na majibu mazuri ninayo maswali miwili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Kwa kuwa, hali ya Barabara za Kigamboni ni mbaya sana, watu wanashindwa kwenda kufanya kazi. Barabara ya kutoka Mji Mwema kwenda Kimbiji Pemba Mnazi haipitiki kabisa. Barabara ya Kibada – Pemba Mnazi mpaka Tundwi Songani haipitiki kabisa, hali ambayo inafanya wananchi wa Kigamboni sasa washindwe kufanya kazi na pia, kupandishiwa nauli za daladala. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mfupi kuhakikisha barabara hizo zinakwenda kupitika na watu wanaendelea na shughuli zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa, mzunguko wa lami wa barabara za Kigamboni ni mdogo sana ukizingatia sasa Kigamboni ni eneo ambalo lina viwanda na ni eneo ambalo linakua kiuchumi, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wanajenga barabara mpaka kufika kwenye viwanda hivyo, ili wawekezaji wetu waweze kufanya kazi zao vizuri sana? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kuuliza maswali yenye tija sana. Naomba nimhakikishie kwamba, Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa miundombinu ya barabara hizi za TARURA. Natumia nafasi hii kumwagiza Meneja wa TARURA wa Wilaya aweze kwenda kufanya tathmini kuona anachosema Mheshimiwa Mbunge kwa sababu, kama barabara hizi hazipitiki, kipaumbele cha Serikali ni kuhakikisha inarudisha mawasiliano sehemu ambazo hamna mawasiliano.

Kwa hiyo, naomba nitumie nafasi hii kumwagiza Meneja aweze kwenda kufanya tathmini ya barabara alizozitaja Mheshimiwa Mbunge kwenye eneo la Mji Mwema, Kibada na Pemba Mnazi ili kuona hali ilivyo na hatua za dharura ziweze kuchukuliwa kuleta mawasiliano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge ukiacha kwamba, Serikali inatenga fedha katika bajeti ya TARURA, lakini nakuhakikishia kwamba, kupitia Mradi wa DMDP ambao ni mradi utakaojenga barabara zenye urefu wa kilometa 250 Jimbo la Kigamboni na lenyewe litakuwa ni mnufaika mkubwa sana wa mradi huu. Kwa hiyo, ukiacha tu ujenzi ambao utafanyika kupitia TARURA, pia huu Mradi wa DMDP ambao unagharimu US Dollar milioni 438 utaleta tija kubwa sana katika miundombinu ya Jimbo la Kigamboni.
MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza. Je, Serikali ni lini itakamilisha ujenzi wa Barabara ya Lami ya Kibada – Kisarawe II – Mwasonga mpaka Tundwi, Songani katika Halmashauri ya Kigamboni? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, mkandarasi alishasaini kilomita zote 41 na tunategemea muda wowote ataanza kufanya kazi. Ahsante. (Makofi)