Primary Questions from Hon. Neema William Mgaya (34 total)
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Kumekuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa maji katika Mji wa Makambako:-
Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kupita awamu ya kwanza ya programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (Water Sector Development Program - WSDP) imekamilisha upembuzi yakinifu na usanifu wa mradi wa maji wa Makambako. Kazi zitakazotekelezwa katika mradi huu ni pamoja na ujenzi wa bwawa la Tagamenda, uchimbaji wa visima virefu vya Idofi na chemichemi ya Bwawani, ujenzi wa bomba kuu na mfumo wa usambazaji wa maji na matanki makubwa ya kuhifadhi maji. Mradi huu unakadiriwa kugharimu kiasi cha wastani wa shilingi za Kitanzania bilioni 70.3 sawa na dola za Marekani milioni 32.39 na unatarajiwa kunufaisha wananchi wapatao 155,233.
Mheshimiwa Naibu Spika, Ujenzi wa Mradi wa Maji Makambako utatekelezwa katika awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji (WSDP II) katika mwaka wa fedha 2016/2017. Hivi sasa Serikali inakamilisha taratibu za kupata mkopo wa gharama nafuu kutoka Serikali ya India kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo. Katika mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali ilitenga shilingi bilioni moja ili kuboresha hali ya huduma ya maji katika Mji wa Makambako. Wakati mradi mkubwa unasubiriwa na pindi fedha zikipatikana kabla ya mwaka kumalizika fedha hizo zitatumwa.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Hospitali ya Kibena inakabiliwa na uchakavu pamoja na upungufu wa madawa:-
Je, Serikali itakarabati hospitali hiyo pamaja na tatizo la upungufu wa dawa?
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Wiliam Mgaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ukarabati wa majengo yote ya Hospitali ya Kibena unakadiriwa kugharimu shilingi milioni 805.5 katika bajeti ya mwaka 2014/2015. Serikali imefanikiwa kupeleka shilingi milioni 22 ambazo zimetumika kukarabati chumba cha kuhifadhia maiti na kazi hiyo imekamilika.
Mheshimiwa Spika, ili kuendeleza ukarabati huo Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016 imepanga kutumia shilingi milioni 260, kwa ajili ya ujenzi wa uzio na ukarabati wa chumba cha X-Ray. Hospitali ya Kibena ina uwezo wa kuwahudumia wagonjwa 134,801 lakini idadi halisi ya wagonjwa wanaohudumiwa hospitalini hapo ni 471,613, wakiwemo wagonjwa kutoka Mikoa na Wilaya ya jirani. Serikali katika bajeti ya mwaka 2015/2016, imefanikiwa kupeleka shilingi milioni 77.78, kati ya shilingi milioni 106 zilizotengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa. Mpango wa Serikali uliopo ni kuipandisha Hospitali ya Kibena kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe ili dawa zitakazopatikana ziweze kuendana na mahitaji halisi.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itahakikisha wakulima wanapata pembejeo za kilimo kama mbolea kwa wakati kwa kuwa tatizo hilo limekuwa sugu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, baada ya kutoa maelezo kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa usambazaji wa pembejeo ni wa soko huria na kwamba, wakulima hujinunulia pembejeo wenyewe kutoka kwa Makampuni ya Pembejeo ambao wana Mawakala wao wanaosambaza na kuuza pembejeo Mikoani, Wilayani hadi Vijijini. Kwa upande mwingine Serikali hutoa pembejeo za ruzuku kwa ajili ya mbolea na mbegu kwa mazao ya mahindi na mpunga kwa wakulima wa badhi ya kaya maskini vijijini ili wajikwamue na kadhia ya upungufu wa chakula katika kaya zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, sasa napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaweka utaratibu kwamba maandalizi ya vocha kwa ajili ya ruzuku ya pembejeo zinakuwa tayari mapema ili ziendane na muda ambao wakulima wanauza mazao yao, ili iwe rahisi kwao kuchangia 50% ya gharama za pembejeo na kujipatia pembejeo mapema. Vilevile Serikali itawalipa makampuni shiriki katika mpango wa ruzuku ya pembejeo mapema iwezekanavyo ili pia watoe huduma bila vikwazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuwahimiza wafanyabisahara wa pembejeo za kilimo, hususan mbegu na mbolea, kuhakikisha kwamba wanapeleka pembejeo kwa wakati. Aidha, Serikali itafanya uchunguzi kubaini mawakala ambao wanachelewesha pembejeo ili kuona namna ya kuwanyima leseni. Tayari Serikali inapitia mfumo wa sasa wa upatikanaji wa pembejeo kwa lengo la kuja na mfumo mpya utakaoweza kuwapatia wakulima pembejeo kwa wakati na kwa bei nzuri. Ahsante sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Lini Serikali itatatua kero ya pembejeo za kilimo kutofika kwa wakati katika Kata za Kipengele, Wangama, Igima, Ulemwe na Makoga?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ucheleweshaji wa pembejeo kwa wakulima unasababishwa na baadhi ya mambo kama haya yafuatayo:-
La kwanza, ni mawakala kutokulipwa kwa wakati kutokana na uhaba wa fedha na hivyo kuwapunguzia uwezo wa kutoa huduma hiyo kwa wakati.
Pili, utaratibu au mchakato mzima unaofanya mpaka mkulima apate vocha au pembejeo ni mrefu na hivyo huchukua muda mwingi na kuchangia kuchelewa kwa pembejeo. Serikali inaangalia jinsi ya kurahisisha utaratibu huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali katika msimu wa mwaka 2015/2016 imetumia makampuni ya pembejeo za kilimo kuteua mawakala wa kusambaza pembejeo kwa wakulima. Kupitia utaratibu huu, mawakala waliteuliwa na makampuni badala ya Kamati za Pembejeo za Wilaya ili kuokoa muda wa pembejeo kuwafikia wakulima.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa wanufaika wa vocha za pembejeo, Wizara ilikabidhi vocha za pembejeo kwa Mkoa wa Njombe tarehe 4/11/2015 na kwamba Mkoa ulikabidhi Wilaya ya Wanging’ombe tarehe 6/11/2015 na Kata ya Igima ilipokea vocha tarehe 9/11/2015. Kata ya Kipengele, Wangama, Ulembwe, Kidugalo, Imalinyi, Igosi na Makoga zilipokea vocha za pembejeo tarehe 10/11/2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia tarehe 20/11/2015 huduma ya usambazaji wa pembejeo ilianza kutolewa na mawakala walioteuliwa na Makampuni ya Pembejeo ili kuwahi msimu wa kilimo ambao huanza kati ya mwezi Oktoba na Novemba.
Wizara ya Kilimo na Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Mikoa na Halmashauri za Wilaya tunaendelea kuhamasisha Makampuni na mawakala wa pembejeo kufikisha pembejeo kwa wakulima kwa wakati kabla ya msimu haujaanza.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya hifadhi ya Mpanga na wananchi wa Wilaya ya Wanging‟ombe?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa William Mgaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, uhifadhi katika hifadhi ya Mpanga Kipengele ulianzishwa za Tangazo la Serikali (GN) Na. 483 la tarehe 25 Oktoba, 2002 ambapo eneo lililoidhinishwa lilitangwazwa kuwa pori la akiba kwa maslahi mapana ya Kitaifa. Uhifadhi wa eneo hili unahusisha utunzaji wa rasilimali zinazotoa fursa ya utalii, matumizi ya kiikolojia na vyanzo vya maji kupitia mito ya Mbarali, Mlomboji, Kimani na Ipera ambayo kwa pamoja huchangia maji ya mtoa Ruaha Mkuu, ambao ni muhimu kwa shughuli za kilimo ikiwemo umwagiliaji wa mashamba, mahitaji ya watu na uzalishaji wa umeme katika mabwawa ya Mtera na Kidatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Wilaya za Makete na Mbarali, poli la akiba Mpanga na Kipengere limepatikana na takribani Vijiji kumi vya Wilaya ya Wanging‟ombe ambapo chanzo cha mgogoro ni wananchi wa Vijiji vinne ambavyo viko ndani ya mpaka wa hifadhi, na vingine vinne nje wa mpaka wa hifadhi kukataa kutambua mipaka iliyowekwa na Tangazo la Serikali na hivyo kugoma kuhama kupisha shughuli za uhifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika juhudi za kutafuta suluhu ya mgogoro huu na eneo lote linalozunguka pori hili, Wizara yangu ilifanya vikao vya majadiliano na Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya ya Makete tarehe 20 mpaka 21, Novemba, 2014; Wanging‟ombe tarehe 26 mpaka 27, Novemba 2014 na Wilaya Mbarali tarehe 26 mpaka 27, Februari, 2015 na hatimaye kufanyika kwa tathmini kutambua idadi ya wananchi na mali zao zisizohamishika na uthamini wa kiasi cha fedha kitakachohitajika kuwalipa fidia kwa mujibu wa sheria.
Mheshimiwa Naibu Spika, kufuatia uthamini uliofanyika mwaka 2007 na 2012 katika Wilaya ya Makete mwaka 2007, wananchi 325 wa Vijiji vya Ikovo, Usalimwani na Kigunga vya Wilaya ya Makete walilipwa fidia ya shilingi 190,067,151. Mwaka 2012 wananchi 161 wa Kijiji cha Ikovo walilalamikia kupunjwa, hivyo uthamini wa ardhi na gharama za kuhama ulifanyika tena ambapo walilipwa jumla ya shilingi 829,841,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika tathmini iliyofuata iliyofanyika na kukamilika mwaka 2015 Wilayani Mbarali, wananchi 308 katika Kitongoji cha Machimbo, Kijiji cha Mabadaga wanategemewa kulipwa jumla ya shilingi 717,650,000 katika mwaka wa fedha 2016/17. Tathmini na uthamini kwa Vijiji vya Wilaya ya Wanging‟ombe imepangwa kufanyika kupitia bajeti ya mwaka wa fedha ujao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwaomba wananchi kuendelea kuwa watulivu, wavumilivu na kuepukana na shughuli ambazo zinaweza kuleta athari katika maeneo hayo muhimu kwa Taifa letu, kwani Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutatua changamoto za migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na ya wananchi. Vilevile tunahimiza Mkoa, Halmashauri za Wilaya na Waheshimiwa Wabunge washirikiane na Wizara kuhamasisha elimu ya uhifadhi na pia kuwashawishi wananchi kukubali kuhama na kupisha uhifadhi mara baada ya taratibu kukamilika.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya wananchi wa Malangali ndani ya Wilaya ya Wanging‟ombe na wafanyakazi wa Hifadhi ya Mpanga?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali namba 422, la Mheshimiwa Neema William Mgaya kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Nabu Spika, Hifadhi Mpanga au Kipengere lenye ukubwa wa Kilomita za mraba 1,574 kwa mara ya kwanza ilitangazwa kuwa hifadhi mwaka 2002 kupitia Tangazo la Serikali (GN) Namba 483.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya Oktoba10, 2012 Serikali ilitangaza tena Hifadhi hii kuwa Aifadhi ya Akiba, tangazo ambalo lilioneshwa kuwa kijiji hiki kipo ndani ya hifadhi na hivyo kusababisha mgogoro kati ya wanakijiji, wafanyakazi wa hifadhi pamoja na hifadhi yenyewe kwa ujumla.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu, Serikali imekuwa ikifanya juhudi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Wanging‟ombe mwezi Februari, 2016, aliunda Tume ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huu. Pamoja na timu hiyo, Wizara yangu itakutana na Wizara ya TAMISEMI, Wizara ya Maliasili na Utalii na wadau wote kwa lengo la kufanya mapitio ya matangazo yote mawili ili kupata tafsiri sahihi ya mipaka ya Hifadhi na kijiji kisha kurekebisha kasoro zote zilizojitokeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa jambo hili ni nyeti, naomba kuahidi kulifanyia kazi mapema iwezekanavyo mara baada ya vikao vya Bunge lako Tukufu kumalizika.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Vijana wengi nchini wanakabiliwa na tatizo kubwa sana la ukosefu wa ajira.
Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: alijibu:-
Mheshiwa Spika, kwa niaba wa Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ni asilimia 11.7. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imejipanga kutekeleza yafuatayo:-
Mheshimiwa Spika, moja, ni kuendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi. Aidha, ili kuwapa vijana wengi fursa za mafunzo Serikali imeanzisha programu maalum ya kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti.
Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha hilo kwa sasa Serikali inaendelea kufundisha vijana 400 katika kiwanda cha Took Garment Company Ltd. lengo ni kufundisha vijana 1000. Mafunzo mengine yataanza mwezi Novemba, 2016 katika kiwanda cha Mazava Fabrics, Morogoro pamoja na DIT Mwanza ambayo ni kwa ajili ya kutengeneza viatu na bidhaa za Ngozi. VETA nchi nzima watafundishwa vijana 4000. Serikali inaendelea kujadiliana na taasisi nyingine zikiwemo kiwanda cha Karanga Moshi na nyinginezo.
Mheshimiwa Spika, pili, ni kuwezesha vijana kuwa wajasiriamali kwa kuwatambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimbali na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya vijana.
Mheshimiwa Spika, tatu, ni kuhamasisha vijana wenye utaalamu mbalimbali kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususani kilimo na biashara.
Aidha, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha vijana na kuwawezesha kuwekeza kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikisha lengo la asilimia 40 ya nguvu za kazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.
Mheshimiwa Spika, nne ni kuendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao kupitia mfuko huo vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 vimepata mikopo yenye masharti nafuu ya kiasi cha shilingi takribani bilioni moja na milioni mia sita kupitia kwenye SACCOS zao za Halmashauri za Wilaya ili ziweze kuwakopesha vijana mikopo ya masharti nafuu na hivyo vijana waweze kujiajiri.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga Hospitali katika Wilaya mpya ya Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe imeanza maandalizi ya awali ya kuanza ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kwa kutenga eneo la ekari 60 katika kijiji cha Igwachanya ambalo limetolewa na wananchi bila kuhitaji fidia. Katika mwaka wa fedha 2016/2017 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 35 kwa ajili ya kupima eneo hilo na kuliweka mipaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 zimetengwa shilingi milioni 24 kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya maandalizi ya awali ili kuanza ujenzi. Serikali itaendelea kushirikiana na Halmashauri katika kusukuma vipaumbele vilivyoainishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe sambamba na kutafuta fedha ili kufanikisha huduma ya afya kwa wananchi wa Wanging’ombe.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaboresha MSD ili dawa zifike kwa wakati?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imefanya mabadiliko makubwa katika utendaji wa MSD. Kutokana na malalamiko mengi juu ya utendaji wa MSD siku za nyuma, katika mwaka wa fedha 2015/2016 Serikali iliajiri Kampuni ya Ushauri wa Kitaalam ya Deloitte ili kupitia mfumo wa utendaji kazi wa MSD kwa minajili ya kuuboresha. Deloitte walitengeneza ripoti ya utendaji wa MSD na kuleta mapendekezo ya maboresho ambayo iliwasilishwa Wizarani mnamo mwezi Januari, 2016. Taarifa hiyo ilikuwa na mapendekezo 21 ya utekelezaji ili kuiboresha MSD na kuhakikisha dawa zinafika vituo vya afya kwa wakati kulingana na mahitaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, mapendekezo hayo yalikuwa pamoja na kuimarisha mifumo ya uwajibikaji ya MSD, kuongeza mtaji wa usambazaji dawa, kulipwa kwa deni la MSD, kuboresha mifumo ya kusimamia rasilimali watu, kuupitia mnyororo wa ugavi wa dawa nchi nzima na kuondoa kero ya uhaba wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kupokea ripoti hiyo, Wizara iliunda timu maalum ya kusimamia utekelezaji wa mapendekezo ya Deloitte kuhusu uboreshaji wa MSD ikiongozwa na Mganga Mkuu wa Serikali. Napenda kukujulisha kuwa hadi kufikia tarehe 31/7/2017 MSD ilikuwa imetekeleza mapendekezo 19 kati ya 21 ya Deloitte. Mapendekezo mawili yaliyosalia ya kuongeza upatikanaji wa dawa na kufuta deni la MSD yanaendeea kufanyiwa kazi na yanatarajiwa kukamilika kabla ya Juni, 2019.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na maboresho hayo ndani ya MSD, kwa sasa hali ya upatikanaji wa dawa muhimu imeendelea kuimarika hadi kufikia wastani wa asilimia 80. Aidha, ununuaji wa dawa kutoka moja kwa moja kwa wazalishaji kumepunguza gharama za ununuzi wa dawa kwa wastani wa asilimia 40 na hivyo kuwawezesha wananchi wengi kupata dawa nyingi zaidi kwa wakati.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia kukujulisha kuwa ili kuhakikisha dawa zinafika kwa wakati, Wizara kupitia msaada wa Mfuko wa Dunia (Global Fund to Fights Aids, Malaria and Tuberculosis) inatarajia kuipatia MSD magari ya usambazaji 181 kwa ajili ya usambazaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba ili ufanyike kila baada ya miezi miwili badala ya miezi mitatu ya sasa. Utaratibu huu utaongeza upatikanaji wa dawa kuanzia mwezi Januari, 2018.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Ni muda mrefu tangu transfomer katika Kijiji cha Itengelo, Kata ya Saja imefungwa lakini umeme haujawashwa. Je, ni lini Serikali itawasha umeme katika kijiji hicho?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Itengelo ni miongoni mwa vijiji vilivyonufaika na mradi wa REA Awamu ya Pili uliotelekezwa na Mkandarasi Kampuni ya M/S Sengerema Engineering Group Limited ambaye alipewa kazi ya mradi kwa Mkoa wa Njombe. Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa kilometa 8.5 za njia za umeme msongo wa kilovoti 33 na kilometa sita za njia za umeme msongo kilovoti kwa gharama ya shilingi milioni 564. Maradi ulikamilika mwezi Desemba, 2016.
Mheshimiwa Naibu Spika, Kijiji cha Itengelo kiliwashiwa umeme tarehe 22/08/2017 kwa kufungiwa transfomer mbili pamoja na kuwaunganisha umeme wateja 56 waliolipia.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Tatizo la maji katika Jimbo la Wanging’ombe limekuwa sugu kwa sasa:-
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kubabiliana na tatizo la maji katika Jimbo la Wanging’ombe ambapo katika mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Wanging’ombe imetengewa jumla ya shilingi bilioni 4.7 na mpaka Machi, 2018, Serikali imepeleka jumla ya shilingi bilioni Kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na Usafi wa Mazingira, Halmashauri ya Wanging’ombe imekamilisha miradi katika Vijiji vya Wangama, Mtama, Masaulwa, Isimike, Igenge na Idenyimembe na wananchi wanapata huduma ya maji. Miradi mingine katika vijiji tisa ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Exim ya India itatekeleza mradi wa kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yanayopata huduma ya maji kutoka mradi wa kitaifa wa Wanging’ombe pamoja na Mji wa Igwachanya. Kazi zinazotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na ukarabati wa chanzo cha Mbukwa na Mtitafu; ulazaji wa bomba kuu katika chanzo cha Mbukwa umbali wa kilomita 112; ukarabati wa matanki 59; kulaza bomba kuu kutoka chanzo cha Mtitafu umbali wa kilimita 15; ujenzi wa tanki la ujazo wa lita 200,000 katika eneo la Igwachanya; na ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji. Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2018/2019.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Halmashauri ya Makete ni miongoni mwa Halmashauri zinazozalisha maziwa ya ng’ombe kwa wingi:-
Je, ni lini Serikali itajenga Kiwanda cha Kusindika Maziwa katika shamba la Ng’ombe la Kitulo Makete - Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Shamba la Mifugo la Kitulo linalomilikiwa na Serikali lipo Wilaya ya Makete, Mkoa wa Njombe na lina mifugo kwa maana ya ng’ombe wa kisasa wapatao 799. Ng’ombe walioko Kitulo utumika kuzalisha mitamba pamoja na maziwa.
Mheshimiwa Spika, Wizara ina mpango wa kuboresha Shamba la Mifugo la Kitulo kwa kuboresha kosaafu za ng’ombe kwa kununua ng’ombe bora wa maziwa aina ya Holstein Friesian majike 400; kuongeza ng’ombe bora wa maziwa kutoka 450 waliopo hadi kufikia ng’ombe bora wa maziwa 1,200; kuongeza uzalishaji mitamba ya kuuza kutoka mitamba 80 kwa mwaka hadi mitamba 213 kwa mwaka; na kuongeza uzalishaji wa maziwa kutoka lita 400,000 kwa mwaka hadi lita 3,350,816 kwa mwaka ifikapo mwaka 2023.
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Njombe una Kiwanda cha Kusindika Maziwa cha Njombe Milk Factory, wakati Mkoa wa jirani wa Iringa una viwanda vya ASAS Dairy na Mafinga Milk Group ambapo kwa pamoja viwanda hivi vina uwezo wa kusindika lita 56,600 za maziwa kwa siku lakini vinasindika lita 18,300 tu kwa siku. Hivyo, wananchi wa mikoa hii wanayo fursa kubwa ya kuongeza uzalishaji wa maziwa ili kuwezesha viwanda hivyo kusindika kulingana na uwezo wa viwanda hivi.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri ya uanzishwaji wa viwanda ikiwemo kuboresha miundombinu ya barabara; kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika; kuondoa kodi kwenye mitambo na vifaa vya kupoozesha na kusafirishia maziwa; pamoja na kuhamasisha viwanda hivi kununua magari maalum ya kusafirisha maziwa ili viweze kufikia wafugaji katika maeneo yao.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatatua tatizo la maji katika Jimbo la Njombe Kusini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Awamu ya Pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji inaendelea kutekeleza miradi ya maji katika Halmashauri zote nchini, ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018, Halmashauri ya Njombe imetengewa kiasi cha shilingi bilioni 1.55 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na ukarabati wa miradi ya maji. Mpaka sasa Serikali imekamilisha Miradi ya Maji katika Vijiji vya Peruhanda, Limage, Igominyi, Igoma na Iwongilo. Miradi mingine ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuboresha huduma ya maji Njombe Mjini ambapo ni Makao Makuu ya Mkoa mpya wa Njombe, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali inatekeleza mradi kutoka Chemchem ya Kibena kwa gharama ya shilingi bilioni 1.1. Hadi kufikia Mei, 2018, kazi zilizokamilika ni ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilomita 2.2; ujenzi wa kidakio cha maji; ununuzi wa dira za maji na ufungaji wa pampu mbili za kusukuma maji zenye uwezo wa kuzalisha maji mita za ujazo 72 kwa saa. Kwa ujumla utekelezaji wa mradi umefikia asilimai 90 na unatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali itatekeleza mradi wa maji kutoka Mto wa Hagafilo kwa ajili ya kutoa huduma ya maji kwa wakazi wa Njombe Mjini na maeneo ya pembezoni mwa mji huo. Usanifu wa mradi huo umekamilika na kazi zitakazotekelezwa ni ukarabati wa chanzo cha Magoda; ujenzi wa chanzo cha Mto Hagafilo; ulazaji wa bomba kuu; ulazaji wa mabomba ya usambazaji; ujenzi wa matanki na ufungaji wa dira za maji. Mradi huo utagharimu Dola za Marekani milioni 13.5 ikiwa ni mkopo nafuu kutoka Serikali ya India. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
MSD kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa dawa za kuongeza damu kwa mama mjamzito na dawa za usingizi:-
Je, ni lini changamoto hiyo itatatuliwa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kupitia Bohari ya Dawa (MSD) imeboresha upatikanaji wa dawa muhimu hadi kufikia wastani wa asilimia 90 katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Upatikanaji wa dawa hizi kwa kiasi kikubwa umetokana na ongezeko la bajeti ya dawa hadi kufikia bilioni 269 katika mwaka wa fedha 2018/2019 toka bilioni 31 kwa mwaka wa fedha 2015/2016, pia kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa dawa hizo katika mnyoroo wa ugavi.
Mheshimiwa Spika, dawa za kuongeza uwingi wa damu (Ferous sulphate/fumerate + Folic acid) na dawa za usingizi (Anaesthesia drugs) ni kati ya dawa zilizo katika orodha ya dawa muhimu zaidi ambazo upatikanaji wake umeimarika hadi kufikia asilimia 90. Kwa sasa dawa hizi zote mbili zinapatikana kwa kiasi kikubwa katika Bohari ya Dawa. Kutokana na umuhimu wa dawa hizi kwa mama wajawazito na katika kuhakikisha tunapambana na vifo vya mama wajawazito, Wizara inawaagiza Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha dawa hizi zinapatikana katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali italeta fedha za on call allowance kwa madaktari wanaofanya zamu hasa katika hospitali za Wilaya na vituo vya afya ambavyo mapato yake ni madogo kwani sasa ni zaidi ya miaka miwili fedha hiyo haijaletwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, hapo awali Serikali iliweka utaratibu wa kulipa fedha za on call allowance kupitia Hazina, ambapo halmashauri ziliwasilisha orodha za madaktari na wataalamu wote wanaostahili kulipwa fedha za on call allowance. Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo hupeleka madai hayo Wizara ya Fedha na Mpipango. Hata hivyo utaratibu huo ulipelekea baadhi ya wataalam wasiyo waaminifu kutoa taarifa ambazo siyo sahihi na hivyo kusababisha madeni makubwa kwa Serikali.
Mheshimiwa Spika, ili kuondokana na hali ya kuwa na madeni makubwa yasiyo na uhalisia, halmashauri zilielekezwa utaratibu wa kuweka fedha za on call allowance kwenye mipango na bajeti zao ili kuweza kulipa stahiki hizi. Pamoja na kuweka fedha za on call allowance kwenye mipango na bajeti, ilibainika kuwa zipo halmashauri zenye uwezo mdogo wa kimapato hivyo maelekezo yaliyotolewa hospitali na vituo vya afya kutenga asilimia 15 kutoka kwenye mapato yatokanayo na uchangiaji wa huduma za afya kwa ajili ya kulipa motisha kwa wataalam ikiwa ni pamoja na on call allowance.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Makambako ili kupisha ujenzi wa soko la Kimataifa?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mradi wa ujenzi wa soko la Makambako ulianza baada ya Serikali kuona umuhimu wa kujenga masoko ya kimkakati (Strategic Markets) kwa lengo la kuwezesha upatikanaji wa masoko ya uhakika kwa mazao ya Wakulima. Soko hilo lilibuniwa, ili kufanikisha upatikanaji wa soko la uhakika kwa mazao ya kilimo hususan nafaka za mahindi na mchele ambazo huzalishwa kwa wingi katika Mikoa ya Njombe, Ruvuma na Mbeya.
Mheshimiwa Spika, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba, mwaka 2018 Serikali ililipa kiasi cha shilingi 3,026,341,089.58 ikiwa ni fidia kwa wananchi 209 wa Makambako ili kupisha ujenzi wa soko hilo. Aidha, wakati wa ulipaji fidia, walijitokeza wananchi 15 ambao wakati wa uhakiki wa mwisho hawakupatikana na wananchi 20 ambao hawakuwepo kwenye daftari wala taarifa ya uhakiki. Kwa muktadha huo, Serikali imeamua kufanya tathmini tena kwa wananchi ambao hawajalipwa fidia zao ili waweze kulipwa kama wanastahili.
Mheshimiwa Spika, ninaupongeza uongozi wa Mkoa wa Njombe na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka Mkoa huo kwa ushirikiano walioutoa katika zoezi zima la ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha mradi wa ujenzi wa soko la Kimataifa la Makambako. Zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wote litakapokamilika litawezesha mradi husika kutekelezwa bila kuwa na vikwazo.
MHE. PROF. NORMAN A. S. KING (K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga kiwanda cha maziwa Wilayani Makete?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe una ng‟ombe wa maziwa 19,759 na idadi kubwa ya ng‟ombe hawa wapo katika Wilaya ya Makete ambapo wanakadiriwa kufikia 8,310.
Katika mwaka 2018/2019 uzalishaji wa maziwa kwa Mkoa wa Njombe ulifikia lita 8,846,496 zinazokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi 6,596,925,230/= na wastani wa bei ya maziwa ulikuwa kati ya shilingi 670/= hadi 1,000/= kwa lita moja. Mwaka 2018/2019 Wilaya ya Makete ilizalisha maziwa lita 1,241,550 zinazokadiriwa kuwa na thamani ya shilingi 1,241,550,000/= na kuifanya Wilaya hii kuwa ya tatu kwa uzalishaji wa maziwa katika Wilaya za Mkoa wa Njombe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla Wilaya ya Mekete inazalisha lita 103,462.5 kwa siku moja. Kwa takwimu hizi ni wazi kwamba maziwa ni bidhaa muhimu kwa kuongeza kipato cha wananchi wa Wilaya ya Makete na Mkoa wa Njombe kiujumla .
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe una kiwanda kimoja cha Maziwa cha Njolifa kilichopo Njombe Mjini chenye uwezo wa kusindika maziwa lita 20,000 kwa siku na mwaka 2018/2019 kilisindika lita 1,620,000. Ni wazi kwamba kiwanda hiki kina uwezo mdogo wa kusindika maziwa ukilinganisha na ma ziwa yanayozalishwa na wafugaji kwa Mkoa wote.
Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kutambua umuhimu wa tasnia ya maziwa kwa wananchi wa Wilaya ya Makete na nchi kwa ujumla, Serikali ya Awamu ya Tano imeendelea kuhamasisha wawekezaji katika Wilaya ya Makete na eneo nzima la Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini. Kwa sasa kiwanda cha ASAS kipo katika hatua za mwisho za upanuzi wa kiwanda chake kipya Wilayani Rungwe.
Mheshimiwa Mwen yekiti, Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara na Kituo cha Uwekezaji tunaendelea na kampeni ya kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya maziwa kwa eneo la ukanda huu ili kuweza kutumia maziwa yote yanayozalishwa Mkoani Njombe ikiwemo Wilaya ya Makete. Hivyo, Wizara inaendelea na jitihada za kuhakikisha mwekezaji mahiri anapatikana ili kuhakikisha maziwa yote yanayozalishwa na Mkoa wa Njombe ikiwemo Wilaya ya Makete na maeneo yanayouzunguka Mkoa huu yanapata soko la uhakika kupitia kiwanda au viwanda vitakavyojengwa.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuliingiza zao la parachichi katika mazao ya kimkakati kutokana na zao hilo kuiingizia nchi fedha za kigeni?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, parachichi ni miongoni mwa mazao ya bustani ambayo yanapewa kipaumbele katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kutokana na umuhimu wake katika kuongeza kipato na lishe kwa wakulima na jamii kwa ujumla. Zao hilo ni miongoni mwa mazao yanayokua kwa kasi na limeonesha mafanikio makubwa.
Mheshimiwa Spika, aidha, mauzo ya parachichi nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 3,279 mwaka 2015 hadi tani 9,000 mwaka 2018. Mauzo hayo yameliingizia Taifa kiasi cha Dola za Marekani milioni 8.5 kutokana na masoko ya nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza na Kenya.
Mheshimiwa Spika, zao la parachichi limeingizwa tayari kuwa miongoni mwa mazao ya kimkakati na wizara ipo katika hatua za awali za mapendekezo ya kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mazao ya Bustani (Hotculture Development Authority) ambayo itakuwa na jukumu la kusimamia mazao ya bustani likiwemo zao la parachichi ili kuongeza tija na kukidhi mahitaji ya soko la ndani, kikanda na Kimataifa.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali inaendelea kukamilisha mkakati wa kuendeleza tasnia ya mazao ya bustani ya mwaka 2021 – 2030 utakaotumika kama dira ya kuwekeza katika Sekta ya Horticulture itakayojumuisha zao la parachichi. Mkakati huo umehusisha wadau wote muhimu kwenye mnyororo wa thamani wa mazao ya horticulture.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha gharama za usafirishaji wa mazao ya horticulture ikiwemo parachichi zinapungua, Serikali ipo katika hatua za awali kuanzisha Kituo cha Huduma za Biashara ya Mazao ya Kilimo (Agricultural Logistics Hub) kwenye eneo la ekari 20 katika ukanda maalum wa uwekezaji (Export Processing Zone – EPZ) Kurasini, Dar es Salaam.
Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na sekta binafsi, TAHA kwa maana ya TPSF, TAHA na Wizara ya Viwanda na Biashara, kituo hicho kitakuwa ni kituo cha huduma ya pamoja (One Stop Centre) chenye wataalam na miundombinu ya mnyororo wa baridi (cold chain) wa kuhifadhi mazao kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa bei nafuu tofauti na hali ilivyo sasa ambapo baadhi ya mazao hulazimika kusafirishwa kupitia Uwanja wa Ndege wa Nairobi ama Bandari ya Mombasa kwa kuwa na mindombinu thabiti.
Mheshimiwa Spika, kutekelezwa kwa mkakati wa kuendeleza mazao ya bustani na kuanzishwa kwa mamlaka ya kusimamia mazao hayo likiwemo zao la parachichi kutaongeza tija na mchango mkubwa katika pato la mkulima na Taifa.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza Mradi wa Liganga na Mchuchuma ili uweze kuchangia katika kukuza Uchumi wa Taifa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi unganishi wa madini ya chuma na makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma uliopo katika Wilaya ya Ludewa, Mkoani Njombe ni mradi wa kimkakati na upo katika hatua za awali za utekelezaji.
Aidha, mradi huo unategemea kutekelezwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambalo litakuwa na 20% na Kampuni ya Sichuan Hongda Group Company Limited ambayo itakuwa na 80% ambayo ni kampuni ya China baada ya majadiliano kuhusiana na baadhi ya vipengele katika mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika utekelezaji wa mradi huo, utafiti wa kina umeshakamilika na kubaini kuwepo kwa tani milioni 428 za makaa ya mawe katika eneo la Mchuchuma na tani milioni 126 za chuma katika eneo la Liganga. Aidha, uwekezaji katika mradi huo utagharimu kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kazi za awali ambazo zimeshafanyika ni pamoja na utafiti wa athari za mazingira zitakazotokana na utekelezaji wa mradi huo pamoja na njia ya kupunguza athari hizo. Uthamini wa mali na fidia kwa wananchi watakaopisha mradi umeshafanyika, lakini pia, tumeshatoa elimu ya kujenga uwezo wa wananchi kuweza kutumia kiuchumi katika eneo la mradi (Local Content) pale ambapo mradi huu utaanza kutekelezwa. Pia, uboreshaji wa kilometa 221 za barabara kutoka Itoni, Njombe, hadi maeneo ya mradi na ukamilishaji wa utafiti wa reli ya kisasa kutoka Mtwara hadi Mbamba Bay na matawi yake kwenda hadi Mchuchuma na Liganga.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuendelea na utekelezaji wa mradi huu, mwekezaji aliomba vivutio (incentives) ambavyo vilishindwa kutolewa na Serikali kwa sababu vinakinzana na baadhi ya sheria za nchi. Kwa sasa, Serikali ipo katika hatua za uchambuzi wa mradi na kujiridhisha zaidi kuhusu namna bora ya kutekeleza mradi huo ili kukidhi matakwa ya Sheria mpya Namba 5 na 6 za mwaka 2017 zinazolinda rasilimali za nchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuzingatia uchambuzi huo, Timu ya Serikali ya Majadiliano (Government Negotiation Team) ilishaundwa na inaendelea kujadiliana na mwekezaji. Hivyo, utekelezaji wa mradi huo utaendelea mara baada ya kukamilika kwa majadiliano baina ya Serikali na Mwekezaji.
MHE. MASACHE N. KASAKA K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa barabara ya Njombe – Mdandu – Iyayi kuelekea Mbeya?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Njombe (Ramadhani) – Mdandu – Iyayi yenye urefu wa kilometa 74 ilikamilika tangu mwaka 2015. Kwa sasa ujenzi unaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ambapo jumla ya kilometa 14.11 kati ya kilometa 74 tayari zimejengwa kwa kiwango cha lami ikiwemo sehemu ya Mji wa kihistoria ya Mdandu.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2020/2021 kipande cha kilometa 1.5 kinaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami kwa gharama ya shilingi milioni 929.288 na katika mwaka wa fedha 2021/2022 kipande kingine cha barabara chenye urefu wa kilometa 1.5 kinatarajiwa kuanza kujengwa na inakisiwa kugharimu shilingi milioni 929.288. Ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Serikali imewekeza kiasi cha Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya kutengeneza miundombinu ya ukaguzi wa magari nchini (Destination Inspection).
Je, ni sababu zipi zilisababisha Serikali kubadilisha mfumo huo?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilianza kukagua magari yaliyotumika yanayoingia nchini kuanzia tarehe 01 Machi, 2021 katika Bandari ya Dar-Es-Salaam. Sababu za kusitisha utaratibu uliokuwepo awali (Pre-Shipment Verification of Conformity to Standards – PVOC) ni pamoja na changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mfumo huo na pia, faida tarajiwa baada ya kutekeleza mfumo wa Destination Inspection (DI).
Mheshimiwa Spika, changamoto za PVOC ni pamoja na Mosi; ukosefu wa ufanisi, gharama kubwa za ukaguzi na upimaji. Mawakala kutokutokuwa na ofisi za ukaguzi katika maeneo yote, mawakala kushindwa kufanya ukaguzi inavyostahili, nchi kupoteza fedha za kigeni, upotevu wa ajira kwa Watanzania, nchi kushindwa kujenga uwezo wa miundombinu ya ukaguzi na wataalam wa ukaguzi na ugumu wa kuhudumia Wajasiriamali Wadogo wanaonunua bidhaa nyingi za aina mbalimbali zenye thamani ndogo.
Mheshimiwa Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, tangu ukaguzi huu uanze hapa nchini mwezi Machi hadi tarehe 25 Agosti, 2021 jumla ya magari 13,968 yamekaguliwa na TBS na kuliingizia Taifa jumla ya Shilingi 4,888,800,000 ikiwa ni tozo za ukaguzi. Aidha, wateja wengi wameridhika na kufurahia utaratibu huu wa DI. Nashukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
(a) Je, ni kwa nini Serikali iliifuta iliyokuwa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)?
(b) Je, Serikali haioni kwa kuifuta TFDA itashindwa kudhibiti ubora wa vyakula ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo: -
(a) Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilifutwa kwa kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Fedha Na. 8 ya mwaka, 2019 iliyohamishia majukumu ya udhibiti wa chakula na vipodozi kutoka TFDA kwenda Mamlaka ya Udhibiti wa Viwango (TBS). Lengo la kuhamisha majukumu haya ilikuwa ni kuondoa mwingiliano wa majukumu, kati ya TFDA na TBS na kuweka mazingira wezeshi ya uendeshaji wa biashara nchini.
(b) Serikali imeendelea kudhibiti ubora wa chakula kupitia Taasisi ya Viwango Nchini (TBS). Aidha, wataalam wa chakula waliokuwa TFDA pamoja na vifaa vya maabara vya uchunguzi wa ubora wa chakula vilivyokuwa vinatumika TFDA vilihamishiwa TBS ikiwa ni pamoja na shughuli zote zinazohusiana na udhibiti wa ubora wa chakula. Hivyo, kufutwa kwa TFDA hakuwezi kuathiri usimamizi wa ubora wa chakula nchini. Ahsnate. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, ni lini Mradi wa Maji wa Halmashauri 28 ambapo Njombe ni mojawapo utaanza kutekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifauatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imeanza kutekeleza mradi wa maji wa Miji 28 ambapo Wakandarasi wote walisharipoti site mwezi Julai, 2022. Kwa sasa, Wakandarasi wanaendelea na usanifu wa kina na ujenzi wa miradi kwa Miji 28 ikiwemo Njombe utaanza mwezi Novemba, 2022.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji Igando - Kijombe ili kupunguza changamoto ya maji Jimbo la Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, hali ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe ni wastani wa asilimia 76. Katika kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Wanging’ombe, Serikali inatekeleza Mradi wa Maji ya Mtiririko wa Igando – Kijombe ambao utahudumia wakazi wapatao 14,377 katika vijiji 10 vya Malangali, Igando, Mpanga, Luduga, Mayale, Kijombe, Wangamiko, Hanjawanu, Iyayi na Lyadebwe.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huo unahusisha ujenzi wa chanzo cha maji, chujio, ulazaji wa bomba kuu lenye urefu wa kilometa 28.9 na mabomba ya usambazaji yenye urefu wa kilometa 18.2; ujenzi wa matenki mawili ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa lita 150,000 na lita 100,000, vituo vya kuchotea maji 22 na mabirika mawili ya kunyweshea mifugo (cattle trough). Utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022 na kuboresha huduma ya maji kutoka asilimia 76 ya sasa na kufikia asilimia 80.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi iliyoainishwa katika mpango wa kuhakikisha lengo la kufikisha huduma ya maji vijijini ni asilimia 85 na asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imedhamiria kuona mradi unganishi wa Linganga na Mchuchuma unatekelezwa mapema iwezekanavyo. Serikali imefanya uthaminishaji mpya katika eneo la mradi baada ya ule wa kwanza kwisha muda wake kwa mujibu wa sheria na zoezi la kuhuisha tathmini ya taarifa za wananchi lilikamilika mwezi Disemba, 2022. Pia tumehuisha majadiliano na mwekezaji wa mradi ili kuhakikisha majadiliano yanakamilika kwa wakati pasipo kuleta hasara kwa Taifa na kutoa fedha za kutengeneza miundombinu kwa maana sehemu korofi za barabara katika eneo la Milima ya Kemilembe Mchuchuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa wa Mradi huo kwa Taifa letu, napenda kuwahakikishia kuwa juhudi zinazofanyika hivi sasa zitawezesha utekelezaji wa mradi huo haraka.
Mheshimiwa naibu Spika, nakushukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itakamilisha Ujenzi wa Barabara ya Njombe – Ludewa – Itoni hadi Manda kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na ujenzi kwa kiwango cha zege wa Barabara ya Itoni - Ludewa hadi Manda yenye urefu wa kilomita 211.42. Ujenzi kwa kiwango cha zege wa sehemu ya Lusitu – Mawengi kilomita 50 umekamilika na ujenzi wa sehemu ya Itoni – Lusitu kilomita 50 unaendelea.
Mheshimiwa Spika, ujenzi wa sehemu zilizobaki utaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, lini Serikali itaboresha miundombinu ya Shule za Mtapa, Kanani na Wangutwa Wilayani Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021, kupitia mapato ya ndani, Halmashauri ya Wilaya ya Wanging`ombe ilipeleka shilingi milioni mbili kwa Shule ya Msingi Kanani kwa ajili ya ujenzi wa vyoo. Katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vya madarasa. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 75 kwa ajili ya ukarabati katika shule hiyo.
Mheshimiwa Spika, Shule ya Msingi Wangutwa inaendelea kufanyiwa ukarabati kwa kushirikiana na wananchi. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 Serikali ilipeleka shilingi milioni 61.6 kwa ajili ya ukarabati na ujenzi wa matundu ya vyoo. Vilevile, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, shule hiyo imetengewa shilingi milioni 75 kwa ajili ya kuongeza madarasa matatu.
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika mwaka wa fedha wa 2019/2020, Serikali ilitoa shilingi milioni 12.5 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba vinne vya madarasa katika Shule ya Msingi Mtapa. Aidha, katika mwaka wa fedha wa 2020/2021 shule hiyo ilipelekewa shilingi milioni 40 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa.
MHE. MARIAM N. KISANGI K.n.y. MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaondoa popo waliopo maeneo ya Upanga ili kulinda afya za wakazi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara imeendelea kudhibiti popo katika Jiji la Dar es Salaam kwa kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kufanya soroveya (survey) ya kuangalia ukubwa wa tatizo, maeneo yaliyoathirika, mbinu gani ambazo ni rafiki kwa mazingira zitumike kudhibiti na pia kubaini aina ya popo wanaosumbua. Imebainika kuwa kuna aina mbili ya popo wanaosumbua, ambao ni popo wanaokula matunda (hawa wanaotumia miti kama maeneo yao ya makazi) na popo wanaotumia mapango au magofu ya nyumba kama makazi yao.
Mheshimiwa Spika, katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo, majaribio ya dawa tano za kunyunyizia yalifanyika ili kufukuza popo katika makazi hayo. Kati ya dawa hizo; dawa mbili (Napthalene na Bat CRP) zimeonekana kuwa na uwezo wa kuwafukuza popo hao. Juhudi zaidi zinaendelea kwa kushirikiana na wadau kwenye maeneo husika.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Bwalo la Shule ya Sekondari Igwachanya Njombe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ikiwemo ujenzi wa Mabwalo katika Shule za Sekondari nchini. Hata hivyo, natoa rai kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kuanza kutenga fedha kupitia Mapato ya Ndani kwa ajili ya ujenzi wa bwalo katika Shule ya Sekondari Igwachanya.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, lini mkataba na mwekezaji utakamilika ili Mradi wa Liganga na Mchuchuma uweze kufanya kazi na kuchangia pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imedhamiria kuona mradi unganishi wa Liganga na Mchuchuma unatekelezwa, kwa kuzingatia dhamira hiyo, hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuanza utekelezaji wa mradi huo muhimu. Hatua hizo ni pamoja na kulipa fidia ya kiasi cha shilingi za Kitanzania 15,424,364,900 kwa wananchi 1,142 na kuanza upya majadiliano na mwekezaji wa mradi ili kuhakikisha kuwa mradi unatekelezwa pasipo kuleta hasara kwa Taifa, nakushukuru. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, lini Mradi wa Maji wa Igongwi utakamilika katika Tarafa ya Igominyi Wilayani Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji nijibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na Utekelezaji wa Mradi wa Maji wa Igongwi katika Halmashauri ya Mji wa Njombe unaolenga kutatua tatizo la maji kwa wakazi 9,717 waishio katika Vijiji vya Kitulila, Madobole, Luponde na Njoomlole. Hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 78.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika mradi huo imekamilisha ujenzi wa vyanzo vinne vya maji, uchimbaji wa mtaro na ulazaji wa bomba kuu kilometa 49.7, ulazaji wa mabomba ya usambazaji maji umbali wa kilometa 26 kati ya 35, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 32 kati ya 55, ujenzi wa matenki mawili yenye jumla ya ujazo wa lita 100,000 kati ya matenki manne pamoja na ujenzi wa miundombinu sita ya mfano ya kuvuna maji ya mvua iliyojengwa katika Shule za Msingi Madobole na Kitulila, Ofisi ya Serikali ya Kijiji Madobole na Zahanati ya Kijiji cha Kitulila. Kazi zote zilizosalia zinatarajiwa kukamilika kabla au ifikapo mwezi Juni, 2024.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, lini Serikali itapeleka fedha na wataalam katika eneo la Mbongo, Kata ya Manda ambalo linafaa kwa ufugaji wa samaki kwenye vizimba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba katika ziwa ni lazima kuzingatia vigezo vya kisheria na kitaalam, ikiwemo kufanya tathmini ya kimkakati ya mazingira (Strategic Environmental Assessment). Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024, kupitia Progaramu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDP II), Serikali imetenga kiasi cha shilingi 233,500,000 kwa ajili ya kuiwezesha Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi (TAFIRI) kufanya tathmini ya kimkakati ya mazingira, ambayo ni takwa la kisheria katika Ziwa Tanganyika na Ziwa Nyasa yakiwemo maeneo ya Manda ili kutambua maeneo yanayofaa kwa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba.
Mheshimiwa Spika, baada ya tathmini kukamilika, maeneo yatakayobainika kuwa yanafaa kwa ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba yataingizwa kwenye Bajeti na Mpango wa Wizara wa mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuwezesha upatikanaji wa fedha na wataalam katika eneo hilo, ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mpanga Kipengele na Vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mpanga Kipengele na Vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko vilivyopo katika Wilaya ya Wanging’ombe umetatuliwa baada ya kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kupitia Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta. Maelekezo ya Serikali ilikuwa ni kutoa sehemu ya ardhi ya hifadhi kwa vijiji, kufyeka na kuweka alama za mpaka.
Mheshimiwa Spika, kupitia maelekezo haya, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi, Mikoa ya Njombe na Mbeya ilifanya mapitio ya mpaka wa Hifadhi ya Mpanga Kipengere na kumega eneo lenye ukubwa wa ekari 18,221.43 na eneo hilo kutolewa kwa wananchi wa vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko. Aidha, Hifadhi ya Mpanga Kipengere kwa ujumla imemega ardhi yenye ukubwa wa ekari 52,877.602 na kutolewa kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo na hivyo kumaliza migogoro iliyokewepo kati ya hifadhi na vijiji hivyo.
MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:-
Je, lini Serikali itamaliza kulipa madeni ya muda mrefu ya watumishi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kudhibiti uzalishaji wa madeni ya watumishi ikiwemo malimbikizo ya mishahara kwa kujenga Mfumo Mpya wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) ulioanza kutumika mwezi Mei, 2021 ambao umeweza kudhibiti uzalishaji wa malimbikizo mapya ya mishahara.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hatua hiyo, kuanzia Mwezi Mei, 2021 hadi sasa Serikali imelipa madai ya malimbikizo ya mishahara kwa watumishi 132,611 yenye thamani ya shilingi bilioni 219.7. Aidha, Serikali inatoa wito kwa waajiri wote nchini kuhakiki na kuwasilisha taarifa za madeni ya watumishi kwa ajili ya taratibu za uhakiki na malipo.