Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Neema William Mgaya (64 total)

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na naipongeza pia Serikali kwa kutambua umuhimu wa kuipandisha hadhi Hospitali ya Kibena kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Njombe.
Swali langu la nyongeza, Mheshimiwa Naibu Waziri, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kujenga Hospitali ya Wilaya mpya ndani ya Wilaya ya Wanging‟ombe, ukizingatia kwamba Wilaya hii ni mpya na iko ndani ya Mkoa mpya?
Vilevile swali la pili la nyongeza, Serikali haioni kwamba tatizo la ukosefu wa madawa na uchakavu wa majengo ya Hospitali lipo pia katika Wilaya ya Ludewa na lini Serikali itatafutia ufumbuzi suala hilo.
NAIBU WAZIRI WA TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, hoja ya Mheshimiwa Mbunge ni kwamba Hospitali ile ilikuwa ya Wilaya ya Njombe, sasa maana yake itaenda kupandishwa kuwa hospitali ya Mkoa, watakuwa hawana hospitali ya Wilaya, hiyo ndiyo hoja ya Mheshimiwa Mbunge. Naomba tulichukue hili, kwanza, kwa sababu matatizo makubwa ya hospitali hii hivi sasa ya Kibena imekuwa ni kwa sababu mwanzo ilikuwa ni hospitali ya Wilaya na kwa vile ni hospitali ya Wilaya hata ule mgao wake unaenda kiwilaya Wilaya, ndiyo maana Serikali imeona sasa ni vema hospitali hii kuipandisha daraja kuwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa.
Mheshimiwa Spika, kitendo cha kuifanya kuwa hospitali ya Mkoa, maana hata catchment area yake inakuwa tofauti na hivi sasa ilivyo. Maana yake ni nini, wananchi wa Mkoa wa Njombe watakuwa na fursa kubwa ya kupata matibabu mazuri zaidi kulinganisha na pale mwanzo.
Mheshimiwa Spika, kwa nini sasa tusihakikishe tunajenga hospitali ya Wilaya nyingine mpya, hili kama Ofisi ya TAMISEMI kwa kushirikiana na halmashauri husikia tutafanya hiyo kazi. Naomba niseme kwamba hapa sasa hivi ukiangalia hata kwa ndani kuna mgogoro, ukiangalia wale wanaosema kwamba hii hospitali yetu ikiwa ya Mkoa tutakuwa hatuna hospitali ya Wilaya. Nadhani sasa hivi tushikamane kwa pamoja tupate Hospitali ya Mkoa, mikakati mingine mipana iende katika suala zima la upataji wa hospitali ya Wilaya.
Mheshimiwa Spika, naomba nilichukue hili Suala la Ludewa kwa sababu yote ni maeneo ambayo yanatakiwa yatafanyiwa kazi na wewe najua ni Mbunge wa Viti maalum wa Mkoa wa Njombe tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo. Mkoa wa Njombe ni Mkoa mpya, wananchi wake waweze kunufaika na huduma za afya ya Serikali yao, asante sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Kwa kuwa hatuna muda nitauliza swali moja tu la nyongeza na swali langu liko hivi. Kwa kuwa, kumekuwa na mlolongo mrefu wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo kwa wakulima.
Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kutafuta njia mbadala ili kufupisha mlolongo huo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Serikali iko kwenye mpango tayari wa kupitia mfumo wa kutoa pembejeo ili kuleta mfumo ambao utaleta ufanisi zaidi katika ugawaji wa pembejeo ambao sisi tunaamini kwamba siyo tu kwamba, utarahisisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, lakini vilevile kwa bei nafuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni kama mnavyofahamu tumekutana na Wabunge wote wanaotoka maeneo wanayolima mazao muhimu ili kupata mawazo yao ya namna ya kuboresha mfumo huu. Nawaahidi kwamba, katika bajeti inayokuja, Serikali inakuja na mapendekezo ya mpango mpya kabisa ambao utaondoa hii kero na changamoto, ili isiwepo tena. Nashukuru sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya, lakini zile pembejeo hazifiki kwa wakati. Kwa hiyo, lengo lililokusudiwa haliwanufaishi wakulima. Nataka kujua, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba wakulima wananufaika na pembejeo hizo ikiwa ni kufika kwa wakati?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Neema Mgaya kwa swali lake zuri na kwa jinsi anavyofuatilia jambo hili la pembejeo ikizingatiwa kwamba Mkoa wa Njombe ni Mkoa wa kilimo na hivyo waliomchagua hawakufanya kosa kumrejesha Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu mfumo huu wa pembejeo umekuwa na upungufu mwingi na Serikali imejitahidi mara kwa mara kuangalia mifumo mipya ili kuhakikisha kwamba kusudi lililokusudiwa linakuwa na ufanisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge, nakiri kwamba pembejeo zinapochelewa kusudi la Serikali linakuwa halijafikiwa. Kwa hiyo, kwa sasa hivi tunachoangalia kwenye pembejeo, katika mfumo mpya tunalenga mambo mawili; kwanza ni kuhakikisha kwamba pembejeo zinafika kwa wakati; na pili, tunaangalia namna bora ambayo itafanya pembejeo ziwafikie wakulima wengi kuliko hivi sasa ambavyo tunachukua wachache.
Kwa hiyo, utaratibu ambao tunapanga kama Mheshimiwa Mbunge alivyopendekeza ni kuangalia mfumo ambao utawezesha pembejeo hizi zipatikane madukani kama zinavyopatikana nyingine zile ambazo hazitolewi kwa ruzuku ili wakulima wengi waweze kujinunulia pembejeo zikiwa madukani na zikiwa na bei nafuu. Tunaangalia pembejeo hizi ziweze kupatikana kama coca cola inavyopatikana dukani kwa maskini na tajiri na kila eneo anaipata kwa wakati pale pale anapotaka kuichukua.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Naibu Waziri. Nina swali moja tu la nyongeza, nataka kujua katika hifadhi ya Kitulo iliyokuwepo Makete kuna migogoro mikubwa sana pale kati ya hifadhi ya Kitulo na Vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. Je, Serikali imejipangaje kuhakikisha kwamba, matatizo ya mipaka kati ya wanavijiji wanaozunguka hifadhi ya Kitulo na hifadhi ya Kitulo ya Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la Kitulo na migogoro ya ardhi inayotokana na wananchi wanaoishi katika Vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, jana wakati tukiwa tunatoa ufafanuzi wa hoja nzima ya migogoro ya ardhi katika maeneo ya hifadhi na yanayopakana nayo, tulitoa ufafanuzi kama ifuatavyo na ambao unahusisha pia hifadhi ya Kitulo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imejipanga kwa ajili ya migogoro yote ya ardhi ikiwemo ile inayohusisha hifadhi. Kwa hiyo, kwa hifadhi ya Kitulo tunakwenda kuijumuisha hifadhi ya Kitulo kwenye orodha ya hifadhi zote ambazo zina migogoro kwenda kushughulikia migogoro hiyo kwa kuitazama inahusisha Wizara zipi kati ya zile Wizara sita zilizotajwa. Kwamba, tunakwenda kutazama migogoro hiyo chanzo chake ni nini, inahusu nini na suluhisho lake ni nini kwa kushirikisha Serikali katika Wizara zote zitakazohusika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema jana wakati tunapokwenda kupitia migogoro hiyo tunakwenda kuzingatia maslahi ya Taifa zaidi.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka kujua ni lini Serikali itasambaza mashine za EFD katika Mikoa yote ya Tanzania, ili mwananchi aweze kulipa kodi kihalali na kuweza kulipatia Taifa mapato? (Makofi)
Swali la pili; kuna changamoto katika mtandao, changamoto hii ya mtandao inapelekea kukatika kwa mawasiliano kati ya mashine hizi na TRA. Mfano mnunuzi yupo kituo cha mafuta X akiwa safarini kuelekea Mkoa Y na ikatokea kuna changamoto hiyo, je, mnunuzi anatakiwa afanyeje ikiwa juzi tu tumepitisha sheria kwamba lazima mtu achukue risiti?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nilithibitishie Bunge lako Tukufu kwamba nia ya Serikali yetu ni kusambaza mashine hizi nchi nzima. Kama tunavyofahamu jambo lolote lina gharama na mashine hizi pia zina gharama, kwa sasa Serikali imeanza kugawa mashine hizi za EFD katika Mkoa wa Dar es salaam kwa wafanyabiashara wadogo wenye mauzo ghafi kati ya shilingi milioni 14 hadi milioni 20. Katika awamu ya kwanza Wizara yangu imepanga kugawa mashine za EFD 5,703 na mpaka leo tayari wafanyabiashara 118 wameshachukua mashine zao. Naomba pia niwashajihishe wafanyabiashara wote wa Dar es salaam ambao waliainishwa kuchukua mashine hizi sasa waende wakachukue mashine, kama ambavyo tumesikia kwenye vyombo mbalimbali vya habari kwamba mashine hizi zipo lakini wafanyabiashara hawataki kujitokeza kwenda kuchukua mashine hizi. Nawaomba wafanyabiashara wafike na wachukue mashine hizi katika Mamlaka yetu ya Mapato. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili la Mheshimiwa Neema ameuliza changamoto katika mtandao. Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi kwamba Serikali yetu pia imefanya jitihada ya kusambaza mkongo wa Taifa nchi nzima. Kwa hiyo, changamoto hii ya mtandao naamini haina muda mrefu itafika mwisho na pia naomba niseme na niwaombe wafanyabiashara, wamekuwa wakisingizia changamoto ya mtandao kumbe hakuna tatizo la mtandao. Naomba niwaambie ni vizuri wakaweza kutumia sasa fursa hii ya kuenezwa kwa mkongo wa Taifa na kuweza kutumia mashine hizi katika kutoa risiti pale ambapo wanauza au wanatoa huduma yoyote kwa wananchi. Nimekuwa nikiongea na wafanyabiashara nikiwauliza swali na Waheshimiwa Wabunge naamini ninyi ni mashahidi nani amewahi kufika katika mabenki ya biashara akaambiwa mtandao upo chini, hakuna. Kwa hiyo, hii pia ni danganya toto ya wafanyabiashara, naomba niwaambie sasa Serikali tumeingia vizuri na tunaanza kazi kila mmoja aweze kutoa risiti hizi za mashine ya EFD.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi nami kuweza kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo la barabara katika Wilaya ya Kalambo linafanana na tatizo lililopo katika Wilaya ya Wanging‟ombe; naomba kujua ni lini Serikali itatengeneza barabara ya kutoka Njombe – Iyai inayopita Makao Makuu ya Igwachanya kutokea Mkoa wa Mbeya kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nina uhakika Mheshimiwa Mgaya anakumbuka, wakati mnaipitisha bajeti yetu; na kwa kweli tunashukuru sana mlipoipitisha; katika maeneo ambayo tumeyatengea fedha na tutahakikisha tunayasimamia katika mwaka huu wa fedha, ni pamoja na barabara hii ya Njombe – Iyai na kuendelea. Kuna kiwango cha fedha kimetengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mgaya, nafahamu kwamba unanikumbusha, pamoja na kwamba tuliahidi wakati wa bajeti lakini unaendelea tena kutukumbusha kila wakati ili kwa kutumia njia hiyo ya kurudia kutukumbusha kwamba tutatekeleza.
Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mgaya kwamba, sisi tuliopo Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasilaino tukiongozwa na Mheshimiwa Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, tukiahidi mara moja tunafuatilia utekelezaji. Nami namhakikishia kwamba ataona mwenyewe mwaka huu wa fedha utakapokwisha, ahadi hiyo ambayo ilishatolewa wakati wa kipindi cha bajeti itakuwa imetekelezwa.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yenye matumaini, hata hivyo, nina swali moja la nyongeza. Kwa kuwa, tatizo la maji ni sugu katika Kata ya Saja, Kijombe, Wanging‟ombe na Njombe Mjini, je, Serikali itatatua lini tatizo hili nimekuwa nikiulizia mara kwa mara swali hili katika Bunge lililopita? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, naomba niongezee kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya kama ifuatavyo:-
Kwanza tunakiri kweli kuna upungufu mkubwa wa maji maeneo hayo unayoyataja, Njombe Mjini kuna tatizo kubwa, Makambako kuna tatizo kubwa, hizo Kata za Saja, Kijombe na Wanging‟ombe zote zina matatizo makubwa. Ndiyo maana Serikali imeshafanya usanifu wa kukarabati miradi iliyopo na kuongeza miradi mipya.
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari Serikali imepata milioni 500 US dollar sawasawa na shilingi za Kitanzania trilioni moja kwa ajili ya kuweza kukarabati miradi pamoja na Miji mingine 17. Kwa hiyo, kazi hii tuko kwenye hatua ya mwisho ya kuanza kutekeleza na tutafanya hivyo kwa kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana wananchi wa huko wawe na imani na Serikali ya Awamu ya Tano kwamba tunakwenda kumaliza tatizo hili. Mheshimiwa Rais alipokuwa Makambako, nakumbuka kabisa alisema nipeni Urais, nitakwenda kumaliza tatizo la maji Makambako. Mheshimiwa Sanga alikuwepo nataka nikuhakikishie tatizo la maji Makambako tunakwenda kulimaliza. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la ajira ni kubwa na kwa kuwa tuna miradi mingi ya kilimo; kwa mfano kilimo cha chai kule Njombe, miwa Kilombero, kahawa, pamba kule Kanda ya Ziwa na katika miradi hii kuna fursa ya kuweka programu ya outgrowers.
Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua Serikali inatumia vipi hii fursa ya programu ya outgrowers kuwashirikisha vijana ili kuweza kutatua tatizo la ajira nchini?
Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tatizo hili la ajira nimekuwa nikilizungumzia mara kwa mara takribani miaka sita tangu nilipokuwa ndani ya Bunge hili, tangu nilipokuwa Mbunge wa Vijana. Nilitaka kujua, Serikali iniambie imeweza kutatua kwa kiasi gani tangu nianze kuzungumzia tatizo hili?
NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza namna gani Serikali tunaweza tukawashirikisha vijana kwenye fursa mbalimbali hasa za kwenye kilimo.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 mwezi uliopita kupitia Wizara ya Kilimo pamoja na sisi Wizara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tumezindua mpango maalum wa kilimo ambao utawashirikisha vijana. Lengo lake ni kuwaweka vijana hawa katika makundi mbalimbali kutokana na mikoa yao waweze kushiriki katika kilimo cha nchi hii.
Mheshimiwa Spika, katika mpango huu tunakwenda pia sambamba na mpango ambao upo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambao ni mpango wanaouita ODOP (One District One Product) na lengo lake ni kufanya kitu kinachoitwa District branding ya kila sehemu kwa nchini nzima ambako shughuli za kilimo pamoja na shughuli nyingine za ujasiriamali zinafanyika. Kuwepo na kitu cha utambulisho katika Wilaya husika.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inatambua kabisa kilimo biashara ni kati ya eneo ambalo linaweza likachukua vijana wengi kwa wakati mmoja, na tumeweka msisitizo mkubwa kuhakikisha kwamba makundi makubwa ya vijana yanapata fursa ya kuweza kushiriki katika uchumi wa nchi yao.
Mheshimiwa Spika, lakini pili, katika swali lake ameuliza ni kwa kiwango gani sasa tumetatua changamoto hii. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu zinasema ukosefu wa ajira hasa kwa vijana nchini Tanzania umepungua kutoka asilimia 13.7 ya mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7.
Mheshimiwa Spika, lakini ukilinganisha Tanzania na nchi nyingine za jirani kwa maana ya Kenya na Uganda; tatizo la ukosefu wa ajira kwa Kenya ni takribani asilimia 17.3, kwa Tanzania tumekwenda mpaka asilimia 11.7.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni dhahiri kwamba Serikali kupitia mipango yake mbalimbali imejaribu kutengeneza mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kutengeneza fursa mbalimbali na vijana wengi wameendelea kupata ajira.
Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu kwamba tunayo mipango madhubuti ya kuendelea kusaidia kundi kubwa hili la vijana waweze kupata ajira na kuondoka katika adha hii ya ukosefu wa ajira.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuulize Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Wanging’ombe wametumia nguvu kubwa sana kujenga zahanati na vituo vya afya vilivyopo kule Mdandu, Saja, Ilembula na maeneo mengine. Je, Serikali itapeleka lini pesa ili vituo hivyo vya afya na zahanati viweze kumalizika ujenzi?
Swali langu la pili, kule Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Jimbo la Lupembe wananchi wamejitolea ekari 52 za kuweza kujenga hospitali; je, Serikali pia inafikiria lini itaanza ujenzi wa hospitali ndani ya Halmashauri ya Njombe?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, kwanza naomba nimpongeze Mbunge kwa initiative kubwa sana ya Mkoa wake wa Njombe. Nafahamu kwamba Wanging’ombe tunatumia Hospitali ya Ilembura kama DDH kwa ajili ya Wananchi kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha mnafahamu kwamba zile fedha ambazo nyuma zilikuwa hazipatikani za Local Government Development Grants ambazo zilikuwa zinaenda kusaidia hii miradi ya mabomba na ujenzi ulioanza, mwaka huu sasa zimeweza kutoka. Ninashukuru sana Halmashauri mbalimbali wameelekeza fedha hizo hasa katika kumalizia viporo vya zahanati, vituo vya afya, sehemu zingine na madarasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo naomba nimuagize Mkurugenzi wa Wanging’ombe na Baraza la Madiwani kwamba mpaka mwezi wa sita tutaendelea kutoa fedha zingine mpaka ziweze kukamilika katika bajeti yetu ya mwaka huu, zikija kule lazima zingine wazielekeze katika kuhakikisha hizi zahanati na vituo vya afya katika eneo la Wanging’ombe zimefanyiwa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo katika Halmashauri ya Njombe kama ulivyosema ni kweli jambo hilo limejitokeza mara kadhaa hapa katika Bunge hili na eneo limeshatengwa. Naomba niwahakikishe kwamba Halmashauri kwa kadri itakavyoibua katika bajeti yake mpango wa bajeti wa Serikali katika Halmashauri husika na Ofisi ya TAMISEMI tutashirikiana nao.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo letu kubwa ni kwamba kila Halmashauri kuwe na hospitali ya Wilaya ili wananchi waweze kuhudumiwa katika eneo hilo. Kwa hiyo, Serikali iko tayari kushirikiana na wananchi wa Njombe kuhakikisha katika mipango yetu hii tunafanikisha ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Njombe ili wananchi waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, napenda kumuuliza kaka yangu Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla, deni la MSD lilikuwa ni kiasi gani na kiasi gani kimeshalipwa?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, nataka kujua MSD tayari wameshapewa pesa, ni maboresho gani waliofanya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata dawa kwa wakati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kumpongeza kwa jitihada anazofanya kuzungumzia masuala mbalimbali yanayohusu afya za wananchi wa Mkoa wa Njombe na ndiyo maana amenialika kwenye mkoa wake mara mbili ili kwenda kutatua changamoto zinazowakabili.
Mheshimiwa Naibu Spika, deni la MSD mpaka kufikia mwezi Juni, 2016 lilikuwa linafikia shilingi bilioni 143.4 na uhakiki ulikuwa bado unaendelea. Sehemu kubwa ya deni ilikuwa imehakikiwa na mpaka sasa bado uhakiki wa deni hilo unaendelea kufanywa na wenzetu wa Hazina. Tayari pia hatua mbalimbali za kuanza kulipa deni la MSD zilikwishaanza kuchukuliwa kwa wenzetu wa Wizara ya Fedha kutuletea pesa kwa ajili ya kulipa deni hilo kila baada ya muda wa miezi mitatu. Mpaka sasa tayari deni la MSD limeshapunguzwa kwa takribani shilingi bilioni 12 na linaendelea kuhakikiwa lakini pia kulipwa taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tuna changamoto moja kwamba kuanzia 2016 - 2017 Juni, kipindi hiki cha mwaka mmoja hapo, deni pia limeongezeka tena kwa shilingi bilioni 11 na ni kwa sababu ya miradi misonge ambapo kwa kiasi kikubwa inafadhiliwa na taasisi mbalimbali za kimataifa ikiwemo Global Fund to Fights Malaria, HIV/AIDS and Tuberculosis. Kwa msingi huo, wanatupa dawa na vifaa tiba lakini tunatakiwa sisi tuingie gharama za ku-clear. Sasa pesa hizi zimekuwa zikichelewa kuja kutoka kwa wenzetu wa Hazina. Kwa hiyo, deni limeendelea tena kuongezeka mpaka kufikia tena shilingi bilioni 144 kufikia Julai, 2017.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye majibu ya swali ya msingi niliyoyatoa hapa nilieleza maboresho mbalimbali ambayo tumeendelea kuyatekeleza kufuatana na ushauri wa kitaalam tuliopewa na taasisi ya kutoa ushauri ya kimataifa ya Deloitte and Touche na mpaka sasa tunaendelea kufanyia kazi mapendekezo yao 21 ambayo yalitolewa. Kutilia msisitizo tu ni kwamba changamoto kubwa ambazo zilijionesha katika ripoti ile, pamoja na kuwepo changamoto ya deni, magari machache ya kusambaza dawa na mtaji wa MSD kwisha kutokana na madeni kuwa makubwa lakini pia kulikuwa kuna changamoto nyingine ya kukosekana kwa maoteo (quantification) kutoka kwenye Halmashauri.
Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni mambo ambayo tumekuwa tukiyaboresha kwa ukaribu sana katika kipindi hiki na sasa upatikanaji wa dawa kwa kweli imekuwa ni suala la kihistoria. Mimi nazunguka sana kwenye vituo vya afya, Hospitali za Wilaya nakuta upatikanaji wa dawa upo kwa zaidi ya asilimia 90 na mpaka sasa wastani umefika asilimia 80. Hakuna mtu atasimama leo hii na kulalamika kwamba kuna upungufu wa dawa kwenye eneo lake. Ukiona imejitokeza hivyo basi ujue DMO ama Mkurugenzi hawafanyi kazi yao ipasavyo na wala siyo suala la MSD ama Serikali Kuu. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Waziri katika Jimbo la Njombe Mjini kuna vijiji ambavyo vimepitiwa na mradi wa Makambako - Songea na mradi huu haujaingia kwenye vitongoji, haujaingia kwenye zahanati, shule ikiwemo shule ya sekondari ya Anne Makinda; na kwa kuwa mradi huu ni wa muda mrefu sana na vijiji vinaendelea kupanuka.
Je, ni lini Serikali itapeleka umeme katika vijiji hivi vilivyopitiwa na mradi wa Makambako - Songea?
Swali langu la pili, Jimbo la Lupembe lina vijiji 45, kati ya vijiji 45, vijiji 34 havina umeme ikiwemo Kijiji cha Ninga na kwa kuwa wananchi wa Kijiji cha Ninga wameamua kuunga mkono sera ya viwanda kwa kununua mashine ya kusaga yenye uwezo wa kusaga sembe zaidi ya tani 12 kwa siku, kwa nia ya kuanzisha kiwanda.
Je, Serikali itapeleka lini umeme katika vijiji hivi hususani Kijiji cha Ninga ili ndoto yao ya kiwanda chao kiweze kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge Neema pamoja na Wabunge wa Viti Maalum kwa namna ambavyo wanauliza maswali katika sekta yetu ya nishati.
Swali lake la kwanza amerejea kwamba mradi unaoendelea wa ujenzi wa msongo wa KV 220 Makambo - Songea; kwanza awali ya yote nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kutuwekea jiwe la msingi katika mradi huu. Mradi huu unaendelea vizuri mpaka sasa umefikia asilimia 70, na utaunganisha vijiji 120 katika Mikoa ya Njombe na Ruvuma.
Mheshimiwa Naibu Spika, Katika maeneo ambayo ameyataja Mheshimiwa Mbunge Neema na naomba nimtaarifu mpaka sasa Vijiji vitano katika Mkoa wa Njombe vimeshawasha umeme kupitia mradi huu na kwamba katika maeneo ambayo ameyataja hayajafikiwa na mradi huu, nataka nimwambie tu pia Serikali inaendelea kutekeleza mradi wa densification na kwa mkoa wa Njombe peke yake mpaka sasa hivi vijiji 12 vimeshaunganishwa.
Kwa hiyo nataka nimwambie maeneo ambayo yatakakuwa mradi huo haukuyafikia yatafikiwa na miradi ambayo inaendelea REA Awamu ya Tatu pamoja na densification ambavyo kama nilivyosema na kama ambavyo Serikali imekuwa ikitoa maelekezo, taasisi za umma ikiwemo shule ya sekondari na hapa amerejea sekondari ya Mama Anne Makinda viunganishwe katika miradi hii inayoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili amekitaja Kijiji cha Ninga, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kama alivyosema Jimbo la Lupembe lina vijiji 34 kati ya vijiji hivyo, vijiji 24 vipo katika mradi wa REA Awamu ya Tatu pamoja na kijiji ambacho amekitaja, na naomba niwapongeze vijiji vyote ambavyo vinatekeleza sera ya viwanda na kwa kuwa Serikali yetu ya Awamu ya Tano imedhamiria kutekeleza mapinduzi ya viwanda, nishati ya umeme itafika katika Kijiji cha Ninga pamoja na vijiji vingine kwa Awamu ya Tatu ambayo inaendelea. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina maswali mawili ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Spika, Serikali imejenga Mradi wa Maji wa Kibena Howard lakini mpaka hivi sasa mradi ule bado haujaanza kutoa maji. Je, ni lini Serikali itahakikisha mradi huu unaanza kutoa maji ili wananchi wa Kibena na Hospitali ya Mkoa wa Kibena ili iweze kupata huduma hii ya maji?
Mheshimiwa Spika, lakini swali langu la pili, ni lini Serikali itaanza kutekeleza Mradi wa Maji Tarafa ya Matamba, Wilaya ya Makete?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kuhusu Mradi wa Kibena umekamilika tatizo ambalo lipo ni umeme na tulishaagiza walete quotation kutoka TANESCO tuwalipe ili waunge umeme na wananchi wa Kibena waendelee kupata maji safi na salama.
Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na suala la Matamba, nilitembelea Matamba na nikatoa maelekezo. Nishukuru kwamba Mheshimiwa Mbunge ameleta makadirio yale na katika mwaka ujao wa fedha tutatekeleza mradi mkubwa ili wananchi wa eneo la Matamba waweze kupata huduma ya maji safi na salama kwa kukarabati mradi uliokuwepo ambao ulikuwa na bomba dogo sasa tutaweka bomba kubwa ili maji yaweze kupatikana kwa wingi.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, nimekuwa nikihamasisha sana wananchi wa Mkoa wa Njombe hususani akina mama kufuga ng’ombe wa maziwa. Je, ni Serikali itawasaidia kina mama hawa wa Mkoa wa Njombe katika suala la kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika maziwa ili kuweza kuinua uchumi wa nchi yetu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Tanzania tumebarikiwa kuwa na ng’ombe wengi sana, je, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuweza kuanzisha mashamba ya ng’ombe wa maziwa katika Wilaya mbalimbali ikiwemo Wilaya ya Chato - Mkoani Geita, Wilaya ya Busega - Mkoani Simiyu na Kilolo - Mkoani Iringa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Neema Mgaya. Katika hili aliloliomba Serikali na kuiuliza nini mkakati wake juu ya kuanzisha viwanda vidogo vidogo, yeye amekuwa champion wa jambo hili. Katika mwaka huu tumemshuhudia akiwapa support akina mama wa Mkoa wa Njombe kwa kuwapa vyerehani ambavyo tunavitafsiri kuwa ni viwanda vidogo, kwa hivyo nampongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, nataka nimhakikishie tu kwamba Serikalini hasa Mkoa wa Njombe umekuwa ukipata faida kubwa sana ya ushirika wa vyama vidogo vidogo ambavyo vinafanya kazi ya usindikaji wa maziwa. Pale Mufindi viko vyama vidogo vidogo vingi sana. Naomba pia uniruhusu niwapongeze Wabunge wa Mufindi karibu watatu, Mheshimiwa Mahmoud Mgimwa, Mheshimiwa Mendrad Kigola na Mheshimiwa Cosato Chumi wa Mufindi. Nimekuta pale kuna vyama vingi vya ushirika na hivyo nataka nimuombe Mheshimiwa Neema Mgaya na yeye aweze kushirikiana na Wabunge hawa wa Majimbo waweze kuvisaidia vyama vile vya ushirika viweze kusindika maziwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni jambo linalohusu ni lini Serikali itakwenda kuanzisha mashamba katika Wilaya mbalimbali. Bahati njema sana katika wilaya hizi alizozitaja tayari tuna shamba kubwa katika Kanda ya Ziwa la Mabuki, ambalo lina ng’ombe wazuri na bora kabisa. Naomba nitangaze kwa Waheshimiwa Wabunge wote shamba letu la Mabuki sasa lina ng’ombe wa kuuza, wanyama na wa maziwa wazuri ambao kwa kusema ukweli hata wateja sasa wamepungua sana. Tunawahamasisheni karibuni mnunue ng’ombe pale kwenye shamba letu. Ng’ombe wazuri wanaanzia Sh.1,500,000 mpaka Sh.1,800,000 kwa ajili ya nyama na maziwa.
Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mgaya kwamba kwa upande wa eneo hilo tunalo shamba zuri na kwa Kilolo kule tuna shamba zuri lile la Sao Hill. Hapa Kongwa kwa Mheshimiwa Spika pia tunayo Ranchi yetu ya Kongwa ambayo ina ng’ombe wazuri na Spika na wananchi wa pale Kongwa ni miongoni mwa watu ambao wanaweza kufaidika kwa ng’ombe wale wazuri kwa ajili ya ufugaji bora. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji Jimbo la Kilolo ni sawasawa na tatizo la maji lililokuwepo katika Jimbo la Lupembe, Mkoani Njombe. Ni zaidi ya nusu ya vijiji ndani ya Jimbo la Lupembe havina maji, napenda kumuuliza Mheshimiwa Waziri, ni lini Serikali itaona umuhimu wa kupeleka maji katika vijiji hivyo vya Jimbo la Lupembe kikiwemo Kijiji cha Kanikelele?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Lupembe. Miongoni mwa Halmashauri ambazo zimekuwa zinatumia hela za maji vizuri ni pamoja na Halmashauri ya Lupembe, ndiyo maana kila bajeti tumekuwa tunaiongezea fedha. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hakuna wasiwasi, Halmashauri ya Lupembe imekaa vizuri itatekeleza miradi mingi na kazi ya Serikali na Wizara inayoongozwa na mimi ni kuhakikisha kwamba nawapa bajeti ya kutosha Halmashauri ya Wilaya ya Lupembe ili waweze kutekelezaji miradi kweye vijiji vyote ambavyo Mheshimiwa Mbunge amevitaja.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Wanging’ombe kuna Kituo cha Afya cha Makoga. Kituo hiki ni cha kimkakati, kinahudumia wananchi wa Tarafa ya Imalinyi na Mdandu. Tuseme ni theluthi mbili ya wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe wanapata huduma katika Kituo cha Afya hicho cha Makoga, lakini hali yake ya miundombinu ni mibaya sana. Je, ni lini Serikali itatoa pesa ili kuweza kukarabati Kituo kile cha Afya cha Makoga?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpongeza Mheshimiwa Neema Mgaya na Wabunge wa Njombe wote kwa ujumla wake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tulikuwepo kule tukifanya harambee na tulipata shilingi milioni mia moja na thelathini na saba. Namshukuru Mheshimiwa Neema, Mheshimiwa Lwenge na Waheshimiwa Wabunge wote. Hii tulifanyia pale Makoga na kweli changamoto yake ni kubwa. Hata hivyo tulitembelea Kituo kingine cha Afya cha Palangawano ambacho kinajengwa. Kwa hiyo, kama Serikali tumeweka kipaumbele katika maeneo haya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabla ya mwezi wa 12 kati ya vituo hivyo viwili tutaweza kukiboresha kituo kimojawapo. Hata hivyo priority ya Makoga na Palangawale lazima tuikamilishe kwa ajili ya wananchi wa Wanging’ombe waweze kupata huduma vizuri. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Njombe tunaishukuru sana Serikali ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imetupa pesa kwa miradi mikubwa ya maji ya Njombe Mjini, Wanging’ombe na Mji wa Makambako. Je, ni lini Serikali itaanza kutekeleza miradi mikubwa ya maji Wanging’ombe pamoja na Mji wa Makambako? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili, je, ni lini Serikali itaenda kutatua kero ya maji Wilaya ya Ludewa katika Kata za Milo, Mavanga na Mkomang’ombe? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum, Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeza kwamba swali lake ni zuri na swali hili linahusu pia maeneo mengine ambayo mkopo wa masharti nafuu kutoka Serikali ya India Dola milioni 500 utakwenda kutekeleza miradi ya maji katika miji 17. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 6 Juni, Katibu Mkuu ameunda kikundi cha Mainjinia nane ambao wanatengeneza terms of reference, watafanya kazi kwa muda wa siku 16, tarehe 20 tutakuwa tumeanza kuaandaa nyaraka kwa ajili ya kuanza kutangaza zabuni. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Neema Mgaya kwamba tayari tunalifanyia kazi pamoja na wote watakaofaidi mkopo huo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusiana na Ludewa Serikali ya Chama cha Mapinduzi inatekeleza miradi katika maeneo hayo. Kwa sasa tunaingia katika Programu ya Awamu ya Pili, tutahakikisha kwamba vijiji vyote alivyovitaja vinapata huduma ya maji safi na salama.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi kuuliza swali moja la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Njombe kuna wananchi wengi sana wameomba leseni kwa ajili ya utafiti na uchimbaji wa makaa ya mawe. Mheshimiwa Naibu Waziri, ni lini wananchi hawa mtawapa leseni hizo ili tuweze kuinua uchumi wa Mkoa wetu wa Njombe?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. DOTO M. BITEKO):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Neema William Mgaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Neema Mgaya yuko mstari wa mbele kuwapigania wananchi wa Mkoa wa Njombe na hususan wanawake. Naomba nichukue nafasi hii nimpongeze kwamba juhudi zake si bure, wananchi na wanawake wa Mkoa wa Njombe wanaziona na sisi kama Serikali tutamuunga mkono kwa hatua alizonazo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili jambo la lini tutaanza kuwapa leseni, naomba nimpe taarifa njema Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali kupitia Tume yetu ya Madini ambayo imeteuliwa hivi karibuni, tumeanza kutoa leseni kwa wachimbaji wadogo zote ambazo zilikuwa zimeombwa na tunapitia maombi mengi ambayo yapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa kwamba mpaka sasa kuna jumla ya zaidi ya leseni 5,000 tunazitoa nchini kote. Wananchi wa Mkoa wa Njombe ambao wapo kwenye maombi hayo na wao watahudumiwa kama wengine. Nashukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nikiri kwamba sisi watu wa Mkoa wa Njombe hospitali zetu na vituo vyetu vya afya tunapata pesa za dawa zaidi ya asilimia 90, lakini bado Mheshimiwa Naibu Waziri kuna changamoto. Tuna changamoto ya dawa za afya ya akili pamoja na chanjo ya kichaa cha mbwa ambazo inatulazimu vifaa vya afya kwenda kununua kwa wa zabuni kwa bei kubwa sana. Sasa je, ni lini MSD itatatua changamoto hii kuhakikisha kwamba, inapeleka dawa za afya ya akili na chanjo ya kichaa cha mbwa katika vituo vya afya na hospitali za Mkoa wa Njombe?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, pesa za Basket Fund zimekuwa zikichelewa sana katika vituo vyetu vya afya na hospitali zetu za Wilaya ndani ya Mkoa wa Njombe. Hivi sasa ninavyozungumza Hospitali ya Wilaya ya Ludewa, Hospitali ya Wilaya ya Makete, wamepata pesa za Basket Fund kwa quarter ya kwanza tu ilihali sasa hivi tuko quarter ya tatu. Je, ni lini Serikali itapeleka pesa hizi za Basket Fund kwa wakati ili hospitali hizi ziweze kununua dawa kwa sababu bila kuwa na pesa hata waki-place order kule MSD, MSD hawakubali kuwapatia dawa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Mgaya kwa kuwa mfuatiliaji wa masuala mbalimbali katika sekta ya afya na kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya kule Njombe katika kuwahudumia akinamama na watoto. Sasa naomba niseme kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utaratibu ambao tunautumia sasa hivi Serikali ni utaratibu unaitwa pull system, hapo awali tulikuwa tunapeleka dawa pasipo kuzingatia mahitaji na uhalisia ambao ulikuwepo katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya. Sasa hivi utaratibu ni kwamba hospitali zinaagiza kulingana na mahitaji yake na nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, chanjo tunazo zote asilimia mia moja na hizi tunazisambaza kulingana na mahitaji ya mikoa.

Mheshimiwa Spika, la pili, chanjo za kichaa cha mbwa na dawa za afya ya akili; dawa hizi tunazo katika bohari yetu ya madawa na katika stoo zetu za kanda pale Iringa. Niombe tu Mheshimiwa Mbunge atusaidie kuwaomba mamlaka kule kuagiza kwa sababu zile dawa zina mahitaji mahususi, huwezi ukazipeleka tu kwa sababu wagonjwa wa afya ya akili pamoja na wagonjwa ambao wameumwa na mbwa si wengi kiasi hicho. Hata hivyo, sisi kama Serikali kupitia bohari ya dawa, tunazo dawa hizo.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kweli tunakiri kwamba pesa za Basket Fund zinakuwa zinachelewa na hii kwa sababu fedha hizi nazo zina mkono wa wafadhili, wanapochelewa kutufikishia na sisi mchakato mzima unachelewa kuzifikisha kule. Hata hivyo, niseme tu kwamba fedha za Basket siyo chanzo pekee cha fedha ambazo zinatumika katika dawa, tuna fedha za ruzuku za dawa ambazo tunazipeleka, tuna fedha papo kwa papo na tuna fedha za bima ya afya ambazo zote kwa kiasi kikubwa nazo zinapelekwa katika manunuzi ya dawa. Kwa hiyo kutokuwepo kwa pesa ya Basket Fund, siyo kigezo na wala siyo sababu ya kukosekana dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza niipongeze Serikali kwa kuweza kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha ya Serikali. Lakini Mheshimiwa Waziri pamoja na kwamba mmeelekeza ile asilimia 15 ya mapato kutoka kwenye hospitali na vituo vya afya ziende kulipa on call allowance kwa madaktari hawa, lakini bado kuna changamoto kwa sababu kuna halmashauri ambazo ni nyingi zina mapato madogo sana.

Sasa je, nyie kama Wizara mmejipangaje kuhakikisha kwamba zile halmashauri ambazo mapato yake ni madogo mtumie njia gani nyingine ambayo itakuwa muafaka ili kuweza kuhakikisha kwamba madaktari hawa wanapata stahiki zao?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa bado kumekuwa na changamoto za kupandishwa vyeo kwa mfano kutoka clinical officer kwenda kuwa daktari lakini vile vile kutoka mkunga kwenda kuwa muuguzi na vile vile promotion zao bado tumeziona zikiwa zina suasua. Je, nyie kama Wizara mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba mnatatua changamoto hii pia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, kwanza naomba uniruhusu kipekee nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Neema, amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba wananchi wa Mkoa wa Njombe wanapata huduma nzuri ya afya. Binafsi ameonekana akichangia mifuko ya saruji lakini pia nikimuona amepeleka mashuka kwa ajili ya kusaidia wagonjwa wetu.

Mheshimiwa Spika, baada ya pongezi hizo, katika swali lake la kwanza anaongelea namna ambavyo uwezekano mdogo kwa baadhi ya halmashauri. Kwanza katika kuimarisha tumeajiri wahasibu zaidi ya 350 ambao katika vituo vya afya wameenda kusimamia na mapato yameongezeka. Hakika fedha hii ikiweza kusimamiwa vizuri hakuna uwezekano wa kwamba madaktari na wauguzi wanaweza wasilipwe on call allowance. Nilienda kituo cha afya Kisosora pale Tanga nimekuta katika fedha ambazo zinapatikana mpaka wanafanya na ukarabati katika vituo vya afya. Kwa hiyo, ni suala tu la kusimamia vizuri na hakika maeneo yote ambayo yanasimamiwa vizuri, fedha inatosha na hatujapata malalamiko hivi karibuni.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili anaongelea suala zima la kuwapandisha vyeo. Hizi n afasi zinategemeana na ujuzi kwa hiyo si rahisi kwamba mtu atapanda bila kwenda kuongeza ujuzi na ni matarajio ya Mheshimiwa Mbunge kwamba asingependa akapandishwa cheo mtu ambaye hana ujuzi mahsusi na ndiyo maana zimekuwa zikitolewa fursa za wao kujiendeleza na pale anapojiendeleza na kuhitimu akirudi huwa anapandishwa cheo.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sisi wananchi wa Mkoa wa Njombe tunaishukuru Serikali kwa hatua za awali ilizofanya katika barabara ya Kibena – Lupembe – Madeke, usanifu yakinifu umeshafanyika na vilevile barabara hii imewekwa kwenye bajeti ya mwaka huu. Nilitaka kujua lini Serikali itaanza kujenga barabara hii ya Kibena – Lupembe - Madeke?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa sababu siyo hapa tu Bungeni ameendelea kufuatilia sana barabara za Mkoa wa Njombe.

Naiseme kwamba katika mwaka wa fedha 2018/2019 tunayo bajeti, harakati za kuanza kujenga kilometa 50 kutoka Kibena kwenda Lupembe zinaendelea. Kama hiyo haitoshi tukifika Lupembe, katika mwaka wa fedha unaokuja iko bajeti ambayo tumepitishiwa tutatoka eneo la Lupembe kuelekea Madeke mpakani na Mkoa wa Morogoro.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kuna maboresho makubwa maeneo ambayo yana uzalishaji mkubwa wa matunda, miti, na kadhalika yale maeneo ambayo ni korofi tunaendelea kujenga kwa kiwango cha zege, yale maeneo ambayo yalikuwa na vilima. Harakati hizi zimetusaidia sana kwani sasa hivi wananchi wanaotoka Mlimba wanaweza sasa kuja Lupembe wanakwenda mpaka Makambako kupitia hiyo barabara ambapo awali ilikuwa haipitiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira, tumejipanga vizuri kwa sababu tunaitazama barabara hii kutoka Kibena ili tuweze kuwaunganisha wananchi wa Mikoa ya Njombe na Morogoro.

Ndugu yangu Mheshimiwa Mbunge wa Mlimba alitoa machozi hapa katika eneo lake lakini upo mpango unaoendelea wa kujenga kutoka Ifakara - Kihansi kwa maana ya kujenga kwa kiwango cha lami ili tuunganishe na kile kipande cha kilometa 28 kutoka Kihansi - Mlimba.

Vilevile ile sehemu ya kutoka Mlimba - Madeke nayo tumeiweka kwenye mpango ili mnyororo mzima usafiri ukitoka katika eneo hili la Ifakara tunaunganisha mpaka kwenda Njombe, tumejiwekea mipango mizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Mbunge avute subira na wakati nyingine tuonane ili aone mipango yote kwa maana ya barabara nzima ukitoka Njombe kwenda kwa wenzetu wa Morogoro na utusaidie pia kuzungumza na wananchi waone kwamba Serikali hii imejipanga kuwasaidia wananchi wa maeneo haya.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, sisi watu wa Mkoa wa Njombe ni wakulima wazuri wa kilimo cha chai tangu enzi ya ukoloni, nilitaka kujua.

Ni lini Serikali itawasaidia wakulima wadogo wadogo wa kilimo cha chai ndani ya Mkoa wa Njombe na Mikoa mingine kuanzishia viwanda vidogo vidogo vya kuchakata chai ili kukuza thamani ya chai ile na kuweza kuuliza kwa bei nzuri kwenye kiwanda vikubwa?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kwamba wakulima wa Njombe, kwanza nipongeze jitihada ambazo zimeshafanyika na vilevile nipongeze kiwanda cha Unilever ambacho tayari kimeshaanza kuchukua chai ya wakulima wanjombe pamoja na inayozalishwa na hao wenyewe. Lakini wakati huo nimepata barua kutoka kwa chama cha Ushirika cha Muvyulu cha Njombe kule Lumbembe ambao nao wanaona kuna changamoto ziko pale kuhusiana na kiwanda ambacho kilianzishwa toka mwaka 1969 na kimekuwa hakijaweza kuendelea na uzalishaji kama ilivyokusudiwa.

Kwa hiyo, tutakapotembelea maeneo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo naamini tutapata hatua nzuri zaidi za kuwasaidia wananchi wa Njombe.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ninampongeza Mheshimiwa Waziri kwa majibu mazuri lakini nina maswali mawili ya nyongeza:

Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua lini Serikali itamaliza kufanya tathmini hiyo ya pili na kuweza kulipa fidia kwa wananchi hawa wa Halmashauri ya Makambako ambao walikubali kabisa kupisha ujenzi wa soko la Kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, Wizara ya Viwanda na Biashara mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba ndani ya Mkoa wa Njombe na Tanzania kwa ujumla kunakuwa na viwanda vingi vidogo vidogo vya kuchakata na kuongeza thamani ya mazao ili wanapoenda kuuza kwenye viwanda vikubwa na kwenye soko la Kimataifa tarajiwa wananchi hawa waweze kupata mapato zaidi na kuinua hali zao za kiuchumi, vilevile ili tuweze kufikia azma ya uchumi wa kati. (Makofi)
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge Neema Mgaya kwa namna anavyofuatilia changamoto za wananchi wa Mkoa wa Njombe, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza la Mheshimiwa Mgaya ni kwamba lini tathimini itakamilika. Kwa kuzingatia azma ya Serikali ya kuhakikisha tunawasaidia wakulima wetu kupata masoko ya uhakika, jambo hili tunalichukulia kwa uzito na tathmini, tutahakikisha inafanyika haraka iwezekanavyoo na kwa vile kupitia Wabunge, wananchi watatupa ushirikiano katika kukamilisha suala la fidia, basi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tathmini itakamilika haraka iwezekanavyo, ili kupitia soko la kimataifa la Makambako, wakulima wanaotoka kwenye Nyanda za Juu Kusini waweze kuzalisha kwa wingi na kupata masoko ya uhakika kupitia soko la kimataifa la Makambako.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, Mheshimiwa Mgaya angependa kujua nini mkakati wa Wizara yetu katika kuhakikisha tunaongeza viwanda vidogovidogo ili kuchakata mazao ya wakulima. Nimhakikishi Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali tayari ina mikakati mizuri, bilaterally kwa kuandaa makongamano mbalimbali nchini, ambapo wafanyabiashara kutoka nchi za SADC, wafanyabishara kutoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, wanakuja hapa Tanzania kukutana na wafanyabiashara na wenye viwanda hapa nchini, lengo hilo na mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kupitia forum hizi tunavutia uwekezaji lakini tunasaidia wafanyabiashara na wenye viwanda nchini ku-network na wenzao ambao wanatafuta fursa za kuwekeza hapa nchini na kwa vile utekelezaji wa blue print unakwenda vizuri, basi nina imani kabisha mikakati hii itaweza kusaidia kuchochea ujenzi wa viwnada nchini.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza swali la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa jitihada kubwa walizozifanya katika Jimbo la Makambako, lakini vilevile eneo la Polisi la Makambako lilipimwa na kufanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipa fidia wananchi ambao walikuwepo ndani ya eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, nataka kujua, lini Serikali itawalipa wananchi hawa pesa zao kama fidia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wilaya ya Wanging’ombe tuna changamoto ya Kituo cha Polisi; nichukue nafasi hii kulipongeza Kanisa Katoliki kwa kuona umuhimu wa usalama wa raia na kujitolea baadhi ya majengo kutumika kama Kituo cha Polisi ndani ya Wilaya yetu ya Wanging’ombe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, vilevile Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe imeshatoa kiwanja, nilitaka kujua: Je, lini Serikali itajenga Kituo hiki cha Polisi ndani ya Wilaya yetu ya Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na fidia ya wananchi, nataka nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeamua kuwaachia hilo eneo wananchi, kwa hiyo, suala la fidia halipo tena.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la Kituo cha Polisi, niwapongeze Kanisa kwa kuanzisha hizo jitihada pamoja na wananchi wa eneo hilo; na niwahakikishie kwamba pale ambapo hali itaruhusu tutaongezea nguvu jitihada hizo ili Kituo hicho kiweze kukamilika. Tunatambua umuhimu wa Kituo hicho.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, ndani ya Mkoa wa Njombe Wilaya ya Wanging’ombe kuna mradi wa maji wa Igando - Kijombe wenye thamani ya bilioni 12. Lakini mpaka sasa hivi tunavyozungumza ni bilioni mbili tu ambazo zimekwenda kwenye mradi ule na mkandarasi yuko site lakini amesimamisha mradi hule hauendelei kwa sababu Serikali haijapeleka pesa.

Je, lini Serikali itapeleka hizo bilioni 10 ili mradi ule uweze kukamilika na Wananchi wa Wilaya ya Wanging’ombe waweze kupata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la
Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifutavyo: -

Mheshimiwa Spika, hili suala tumeshalifanyia kazi kama Wizara na kwa ushirikiano mkubwa ambao tumekuwa nae Mheshimiwa Neema pamoja na Mheshimiwa Dkt. Dugange, tumeweza kufatilia na fedha tutaleta mgao ujao tutaendelea kutoa fedha kidogo kidogo, tutaleta bilioni Moja ili kazi ziendelee na mgao unaofuata pia tutaendelea kuleta fedha kadri tunavyopata.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali. Nataka kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa kuna umuhimu na mmeshaanza kufanyia kazi suala la Kurasini Logistic Hub kwa ajili ya mazao ya horticulture ili kuweka mfumo huo wa cold chain; Serikali mmejipanga vipi kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kwa sababu, ndiko wakulima wakubwa wa zao hili la parachichi waliko? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba wanaweka mfumo wa ubaridi kwenye reli ya TAZARA ili kuendelea kuwasaidia wakulima hawa kusafirisha parachichi zao kwa bei nafuu kwenda kule Kurasini kwa ajili ya kupelekwa nje kwa kutumia Bandari ya Dar es Salaam; na vilevile kuhakikisha kwamba parachichi zao na mazao mengine ya mbogamboga yanafika yakiwa na ubora?

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kuna umbali wa kutoka Nyanda za Juu Kusini mpaka Kurasini kule Dar es Salaam kitu ambacho bado kinaweza kukasababisha mazao yale yakakosa ubora: Je, mmejipanga vipi kama Serikali kuhakikisha kwamba mnaweka mfumo wa ubaridi katika mabehewa haya ya TAZARA?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa zao hili limeonyesha linaingiza pato kubwa Tanzania; Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba wakulima wale wanaendelea kulima kwa ubora kwa kuwapelekea mbolea na kuwasimamia katika suala zima la uzalishaji wa zao la parachichi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba zao la parachichi na subsector ya horticulture ni moja kati ya sekta zinazokua kwa kiwango kikubwa na inaajri watu wengi sana hasa vijana, akina mama na middlemen wameanza kwenda katika maeneo haya. Tunafanya nini?

Mheshimiwa Spika, cha kwanza, hivi karibuni Wizara ya kilimo kupitia Waziri wetu, Profesa Mkenda amekutana na representative wa European Business Council kwa ajili ya ku-attract private sector kuja kuwekeza kwenye cold chain ikiwemo mabehewa yenye ma-fridge kwa ajili ya reli ya TAZARA na hata reli yetu kuelekea upande wa Kaskazini kwa sababu ni maeneo ya uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, vilevile pilot katika Wilaya ya Njombe, tumeanzisha centre ya kwanza ambayo imekuwa ni mradi uliofanywa na Wizara ya Kilimo, Tanzania Horticulture Association na Halmashauri ya Njombe kuweka park house ya kwanza ikiwa ya majaribio na imeonesha mafanikio.

Mheshimiwa Spika, kwa sasa kama Wizara tunaangalia uwezekano wa ku-attract sekta binafsi ili iweze kuwekeza katika maeneo haya ambayo yanakuwa kwa kiwango kikubwa na wengi wameonesha appetite na wamekuja kuongea nasi. Nasi tunatumia Bunge lako Tukufu kuwaomba na kuendelea kuwahamasisha wawekezaji wa Kitanzania waweze kuwekeza. Hata hivyo Kurasini itaunganishwa na Njombe ili tuweze ku-process katika primary level na tuweze kupeleka Kurasini kwa ajili ya kuingiza kwenye meli.

Mheshimiwa Spika, kuhusu tumejipanga vipi kwenye kuwasaidia wakulima; sasa hivi hatua ambayo tunachukua na lilitolewa agizo na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba katika maeneo yote ya uzalishaji hasa ya maeneo ya Nyanda za Juu Kusini, halmashauri zote zimeagizwa zitenge maeneo kwa ajili ya kuzalisha miche ambayo itatumika kuwagawia wakulima.

Mheshimiwa Spika, sasa hivi wakulima wananunua karibu na shilingi 5,000/= kwa mche mmoja, lakini hatua ya pili tuliyochukua kwenye eneo la miche ni kwamba, tumeanza kuwasajili wazalishaji wote wa miche ambao ni wazalishaji wadogo wadogo na kuwaunganisha na kituo chetu cha Uyole ili kuweza ku-protect mbegu ya hasi ambayo ndiyo mbegu yenye thamani kubwa katika soko la dunia.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Wizara sasa hivi tunavyomalizia huu mkakati wa kutokea 2021 mpaka 2030, itakuwa ni road map ambayo itaonesha ushiriki wa Serikali, ushiriki wa sekta binafsi na hatua tutakazochukua kwa ajili ya kuhakikisha kwamba sekta hii tunailinda na kuipatia vivutio vyote ili viweze kumsaidia mkulima na kuongeza pato la Taifa. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, asante kwa kunipa nafasi. Swali la kwanza; uthamini wa mali na fidia ulifanyika tangu mwaka 2015, takribani miaka sita sasa wananchi wa Kata ya Mkoma Ng’ombe, Lwilo, Iwela pamoja na Mundindi hawajalipwa fidia hii ya bilioni 11.

Je, Serikali haioni kwamba, kuchelewesha kulipa fidia kwa wananchi hawa kutaiingizia Serikali gharama kubwa kwa sababu, nina wasiwasi isije tathmini hii ikaja kushuka thamani kipindi hicho wao watakachokuwa wanataka kuwalipa wananchi hawa fidia hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa kumekuwa na uhitaji mkubwa sana wa makaa ya mawe na NDC wamechukua vitalu vyote vya makaa ya mawe. Je, Serikali haioni umuhimu wa kutoa baadhi ya vitalu kwa wananchi wachimbaji wadogowadogo wazawa ili waweze kuchimba na kuweza ku-stimulate uchumi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, uthamini wa mali kwa ajili ya kulipa fidia ili kupisha kuendelea kutekeleza mradi huo ulifanyika mwaka 2015 na kweli wakati ule thamani ya fidia iliyokuwa imeainishwa ni bilioni 11.03.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kwamba, utekelezaji wa mradi huu bado uko kwenye majadiliano. Moja ya vipengele ambavyo viko kwenye majadiliano ni kuona namna gani mwekezaji ambaye atapatikana ataweza kulipa fidia ambayo iliainishwa, lakini pia baada ya kupitiwa kutokana na hali halisi ya sasa itabainika. Kwa hiyo, ulipaji wa fidia huu nao ni sehemu ya majadiliano ambayo tunaona kwamba, mwekezaji ambaye atapata nafasi sasa kuwekeza katika eneo hili yeye pia atahusika katika kulipa fidia ambayo ilibainishwa kwa ajili ya wananchi kupisha mradi ule.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu vitalu vya makaa ya mawe ambavyo vinasimiwa na NDC; naomba niwahakikishie kuwa ni kweli vitalu hivi kwa ajili ya maendeleo ya nchi NDC ndio inasimamia uendelezwaji wa uchimbaji katika maeneo hayo, lakini kwa ajili ya maendeleo endelevu mambo haya au biashara hizi za uchimbaji zinakwenda kibiashara zaidi. Kwa hiyo, wananchi au ambao wana uwezo kama wafanyabiashara au wawekezaji ikiwemo wananchi wa maeneo hayo wanaweza kwenda kuomba nafasi ya kushiriki katika maendeleo au uendelezaji wa uchimbaji wa makaa ya mawe katika vitalu hivi kwa kushirikiana au kupata vibali kutoka Shirika letu la Maendeleo la Taifa (NDC).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tunawakaribisha na kama watakidhi vigezo na kuweza kuwa na mitaji stahiki ya kuwekeza katika maeneo haya, nadhani hakutakuwa na shida, tunawakaribisha na shirika letu liko kwa ajili ya kusaidia Watanzania.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa fursa hii. Naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza, moja hilo ambalo umelileta la TAKUKURU na hili la Mheshimiwa Kamonga ambalo ameliuliza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimepanga kutembelea mradi huu mara baada ya bajeti yetu, Ijumaa. Katika ratiba zangu moja ya weekend nitatembelea mradi huu na tutazungumza na wananchi kwa ajili ya kuwapa maendeleo. Kwa kweli, katika bajeti yetu ambayo tutaitoa wiki hii tutaeleza kwa kina zaidi hatua ambazo zimefikiwa katika utekelezaji wa mradi huu na lini hasa utaanza. Kwa hiyo, nitafurahi sana Mheshimiwa Mbunge tukifuatana tukaenda kuzungumza na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili la TAKUKURU. Naomba nilichukue hilo, tulifanyie kazi, tupate details hasa TAKUKURU wanafuatilia nini na katika mazingira yapi, ili tuweze kutoa jibu ambalo linaeleweka. Kwa sababu, kwa kweli, sina details za kutosha kuhusu TAKUKURU wanawakamata wananchi na kuwahoji katika masuala yapi hasa. Kwa hiyo, tunaomba tupate nafasi tulifuatilie tupate details, ili tukitoa jibu hapa tutoe jibu ambalo linaeleweka. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na nampongeza Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri. Nina maswali mawili tu ya nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ni lini Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Kibena Stop Lupembe kutokea Madeke ambayo inaunganisha Mkoa wa Njombe na Morogoro? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; ni lini Serikali itajenga kwa haraka barabara ya Makete ambayo inapita Hifadhi ya Kituro kutokea Mbeya. Sababu barabara zote hizi zina umuhimu kwa Mkoa wetu wa Njombe na zitaongeza uchumi wa Mkoa wa Njombe kwenye masuala ya utalii, lakini vilevile kwenye masuala ya biashara, naomba nipate majibu ya maswali haya. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili kwa pamoja ya Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Kibena - Kona kwenda Madeke ambayo inakuja kutokezea Mlimba, Ifakara ni barabara ambayo kwenye bajeti hii imetengewa fedha na itaanza kujengwa katika bajeti tunayoanza. Hali kadhalika, barabara aliyoitaja ya Makete - Isyonje kwenda Mbeya pia imepangiwa bajeti na itatangazwa katika mwaka wa fedha ujao. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge barabara zote barabara zote mbili alizozitaja zipo na zimepangiwa fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kwa mwaka ujao wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika ahsante kwa kunipa nafasi, Wilaya ya Wanging’ombe kuna Mradi wa Maji wa Igando - Kijombe wa shilingi bilioni 12 ulitakiwa uwe ushakamilika tangu mwaka 2019 lakini hadi sasa hakuna kitu kinachoendelea. Nilitaka kujua lini Serikali itakamilisha mradi huu?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge, sawa na nataka niseme tu unatosha mpaka chenji inabaki, lakini kubwa ambacho ninachotaka kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maji inategemeana na fedha, sasa sisi tumeshapatiwa fedha kuhakikisha kwamba tunakamilisha miradi mbali mbali, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaupa nguvu mradi wake, kuhakikisha tunapeleka fedha kwa wakati, ili mradi ukamilike na wananchi waweze kupata huduma maji safi na salama.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mheshimiwa Naibu Waziri, Tanzania Bureau of Standards na Bureau of Standards zote ulimwenguni kazi yake ni kulinda na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingia nchini na zinazozalishwa ndani ya nchi.

Je, utakubaliana nami kwamba, TBS haipimwi kwa kiasi cha pesa inazoingiza nchini, kutokana na jibu lako ulilonijibu katika swali langu la msingi?

Swali la pili; kuna wale ambao wanashindwa kulipia yale magari, kwa kushindwa huko kulipia yale magari inabidi yale magari mtueleze mnapeleka wapi yale magari? Hamuoni kwamba, Tanzania mnataka kuigeuza kuwa dumping area? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Neema kwa ufuatiliaji wa siku nyingi kuhusiana na ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini. Ni kweli, kazi ya msingi ya TBS ni kuhakikisha na kudhibiti ubora wa bidhaa zote zinazoingizwa nchini ndiyo maana tumeamua sasa ili kuwa na ufanisi katika hilo kukagua sisi wenyewe kwa sababu kama nilivyosema katika jibu la msingi, baadhi ya mawakala huko nje walikuwa hawafanyi kazi ipasavyo na malalamiko bado yalikuwa mengi sana kwamba kuna baadhi walikuwa wanaletewa bidhaa ambazo hazina ubora lakini kwa sababu tayari mawakala walikuwa wamethibitisha kwa hiyo maana yake TBS ilikuwa haina namna ya kufanya.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa sababu sasahivi tunathibitisha wenyewe, pia tumeshawaambia makampuni yanayoleta bidhaa nchini kuhakikisha wanaleta bidhaa ambazo zina ubora. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Neema kwamba kazi hiyo inafanyika na ndiyo maana tunaamua kujiimarisha sasa ili TBS waweze kufanya kazi hiyo kwa uthabiti.

Mheshimiwa Spika, pili, kuhusu ubovu wa bidhaa au magari yaliyotumika yanayoingizwa nchini, kama nilivyosema mpaka sasa zaidi ya wateja hao 13,968 ambao wameingiza magari nchini hakuna hata mteja mmoja ambaye amelalamika kuhusiana na ubovu wa magari au bidhaa zinazoingizwa. Kwa hiyo, tunaamini sasa mfumo huo utaenda kuboreshwa zaidi kwa maana ya kukagua kwa ubora zaidi na tunawaelekeza wateja wetu kuhakikisha wanaingiza bidhaa kupitia makampuni ambayo tumekubaliana ambayo yanatoa bidhaa hizo kutoka nje. Ninakushukuru.
NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Nimekuwa nikiuliza mara kwa mara Mradi wa Maji wa Igando Kijombe ndani ya Wilaya ya Wanging’mbe. Mradi huu sasa hivi ni muda wa miaka mitatu imepita, bajeti yake ya kwanza ni bilioni 12, lakini hadi sasa ni bilioni nne tu ambazo zimekwenda kwenye mradi hule, muda umekuwa mrefu na mradi huu ni muhimu kwa wananchi wa Wilaya Wanging’mbe. Je, ni lini mradi huu utaenda kukamilika ili uweze kuleta tija kwa wananchi wa Wanging’ombe?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akitoa ushirikiano sana katika mradi huu, lakini napenda kumwarifu Mheshimiwa Mbunge huu mradi tayari tumeutembelea hivi karibuni na nimpongeze kwa ushirikiano na Mheshimiwa Dkt. Dugange ameweza kufuatilia. Vile vile niseme tu kwamba tayari mkandarasi anaendelea na kazi na kwa sababu mradi huu ulikuwa ni mkubwa tunafikia phase za mwisho, maeneo ambayo tayari yalikamilika wananchi wameanza kupata huduma ya maji. Hivyo napenda kumtoa hofu Mbunge, mradi huu unakwenda kukamilika ndani ya sera ya kumtua ndoo mama kichwani, tumshukuru Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuisimamia vizuri. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba kumwuliza Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza, naipongeza Serikali kwa kutujengea daraja nzuri linalotuunganisha Wilaya ya Ludewa pamoja na Mkoa wa Ruvuma. Serikali imefanya kazi kubwa sana: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa barabara ya Njombe – Ludewa – Manda – Itoni?

Mheshimiwa Spika, barabara hii ikikamilika itakuwa na umuhimu mkubwa sana wa kuunganisha Ludewa pamoja na Ruvuma, lakini vile vile watu wa Ruvuma watapita shortcut baada ya kuzunguka...

SPIKA: Mheshimiwa, swali la nyongeza hilo.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, vile vile bararabara hii itawezesha mradi wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara ya Njombe – Ludewa – Manda ni barabara ambayo tayari Serikali imeanza kuijenga. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanzania tuna barabara hii tu kilometa 50 ambayo mkandarasi yuko site tunajenga kilometa 50 barabara nzima kwa kiwango cha zege ambayo inakwenda kuunganisha na hilo daraja, hatuna barabara nyingine Tanzania kama hiyo.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nataka nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba kuanzia junction pale inapotoka barabara kwenda Songea hapa Itoni kwenda Lusitu, hii barabara tayari tunatangaza zabuni kilometa 50 kwenda kuunganisha pale ambapo tumeanza kujenga barabara ya zege ili hatimaye tuweze kukamilisha barabara yote kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kutokana na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukizwa yanayosababishwa na ulaji wa vyakula, kwa mfano cancer na viriba tumbo: Je, Serikali haioni kwamba TBS imeshindwa kudhibiti ubora wa vyakula?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili. Kwa kuwa TBS inadhibiti ubora wa vitu vingi ikiwemo petroli, magari, matairi, chemicals na vitu vingine: Je, Serikali haioni kwa unyeti wa chakula ikaweza kutenganishwa na vitu hivi vingine? Ahsnate. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Neema Mgaya kwa sababu tu ushauri wake hauishii kwenye kutushauri kupitia maswali, lakini amekuwa ni mdau mzuri sana wa Wizara ya Afya katika kutoa ushauri hasa kwenye kuboresha afya za Watanzania. Swali lake la kwanza anadhani sisi hatuoni kwamba kutokana na matatizo ya cancer pamoja na viriba tumbo, inawezekana ikawa ni vigumu kusimamia eneo hilo kama haya mambo yataendelea kubaki TBS. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza moja, hili ni suala la kisheria. Lilikuja Bungeni na ikaonekana sababu za kuweza kuhamisha hizi shughuli ziweze kupelekwa TBS badala ya kubaki Wizara ya Afya. Sasa, wazo lake ni zuri kwa sababu kweli kama ambavyo hata wiki iliyopita na inaonekana masuala ya cancer yamekuwa yakisumbua watu, lakini kuna umuhimu wa masuala ya chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakwenda kujadiliana na Wizara ya Afya na tuko tayari kupokea maelezo na kujadiliana na Wizara ya Viwanda, ambayo ni Wizara husika. Tukiona kuna umuhimu wa kuhamisha, basi tutarudi Bungeni kwa ajili ya kufanya hilo ambalo amelisema. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kwamba anadhani vile vile kule TBS wanafanya mambo mengi mengine hayahusiani kabisa na afya. Hata hivyo, nimwambie tu, hata petroli yenyewe ina-impact vile vile kwenye afya. Kwa hiyo, usipoangalia vizuri unaweza ukahamisha kila kitu ukaleta afya. Kwa sababu, petroli ukienda kwa maana ya mazingira na mambo mengine bado yanarudi pale pale kumuumiza binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachoweza kusema, wazo lake ni zuri, lakini ni suala la kisheria na Bunge lilikaa likapitisha, tutaendelea kukusanya maoni ya wadau, tutashirikiana na Wizara ambayo inahusika na masuala hayo. Kukionekana kuna uhitaji wa kurudi Bungeni kubadilisha sheria na mambo hayo yaje Wizara ya Afya, tuko tayari kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kweli input ya Mheshimiwa Mbunge ni muhimu kwa sababu tuna changamoto kubwa sana sasa hivi kwenye masuala mazima ya afya. Mimi nalichukua kama wazo, tunakwenda kuanza kufanyia kazi. Nafikiri na mimi kuna umuhimu wa kuanza kutafakari kama anavyofikiri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mimi na Mheshimiwa Festo Sanga tunaishukuru Serikali kwa hatua za awali kuhusiana na bwawa hili, lakini tulikuwa tunataka Serikali ituhakikishie ni lini wananchi wetu watalipwa fidia?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa wananchi wa Jimbo la Makete wamekuwa na changamoto kubwa sana ya kukatika katika kwa umeme kwa muda mrefu kwa sababu umeme huo unatoka Mbeya.

Je, Serikali inawahakikishia nini wananachi wa Makete kwamba bwawa hili litakuja kuwa tija ya kutatua changamoto hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza yaliyoulizwa na Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la kwanza baada ya kukamilisha uthamini mwezi Oktoba ndiyo sasa taratibu za malipo zitaanza ikiwa ni kupelekea Mthamini Mkuu wa Serikali na fedha tayari imeshatengwa. Kwa hiyo, baada ya kukamilisha taratibu hizo fedha italipwa, tunaamini kabla ya kufikia mwanzoni mwa mwaka unaokuja wa fedha taratibu zikienda kama zilivyopanga fedha za fidia zitakuwa zinalipwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili ni kweli mradi huu ukikamilika utawafaa wananchi wa Mkoa wa Njombe, Wilaya ya Makete, lakini na Watanzania wengine wote kwa sababu ni mradi utakaopeleka umeme kwenye Gridi ya Taifa. Katika kipindi hiki ambacho umeme unakatika katika Serikali imeshafanya tathimini ya kujenga vituo vingine vya kupoza umeme kwenye maeneo mbalimbali na Makete ni eneo mojawapo ambalo limetizamwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya umeme.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwanza tunaishukuru Serikali kwa hatua hizo za awali. Ili mradi uweze kwenda na wakati ni lazima yale maeneo ambayo mabomba yanapita yawe wazi. Na ili yale maeneo ambayo mabomba yanapita yawe wazi, lazima wananchi walipwe fidia.

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi hao?

Swali langu la pili; je, ni lini mradi wa Igongwe wa Kata Nne za Jimbo la Njombe Mjini utapatiwa pesa ili Mkandarasi aendelee na kazi yake? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote ninampongeza Mheshimiwa Neema kwa ufuatiliaji. Suala la fidia tunaelekea kulipa kadri mradi unavyoendelea kujengwa na kila kitu kitakuwa kinakwenda kwa pamoja.

Mheshimiwa Spika, suala la mradi wa Igongwe kwenye Kata Nne, fedha zitaendelea kwenda kadiri tunavyozipata, na fedha ambazo zinafuata msimu ujao, huu mradi pia nao upo katika mpango.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri swali la nyongeza kwamba, hii barabara ambayo inazunguka fence ya kwa Waziri Mkuu; fence ile imepakwa rangi nyeupe, lakini ina vumbi na kipindi cha mvua ina tope. Ni lini mtajenga kwa kiwango cha lami ili kuweza kutunza ile fence nzuri inayozunguka kwa Waziri Mkuu yenye rangi nyeupe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Mheshimiwa Mbunge anachozungumza kwamba, hii barabara ya nyuma inayozunguka fence ya Waziri Mkuu ni ya vumbi na tumekuwa tukiitengeneza kwa kiwango cha changarawe. Kwa hiyo, sasa anahitaji commitment ya Serikali ya kujenga kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, niwaagize TARURA Mkoa waende wakafanye tathmini ya ujenzi wa kiwango cha lami. Wakishakamilisha hiyo tathmini, basi watuletee Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutajua wapi ambapo tutatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo. Ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante Mradi wa Maji Matamba - Kinyika wenye thamani ya bilioni mbili ndani ya miaka minne sasa Wilaya ya Makete bado haujakamilika. Naomba kujua, je, ni lini Serikali itasambaza mabomba pamoja na kujenga ofisi ili wananchi wa Wilaya ya Makete waweze kupata maji kwa uhakika?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nipende kumpongeza Mheshimiwa Neema kwa ufuatiliaji mzuri wa miradi mbalimbali katika Mkoa wa Njombe. Kwa upande wa Makete nilifika huko na Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo tulitembelea miradi hii yote na mradi huu ni kipaumbele cha Wizara kwa sababu unakwenda kuhudumia wananchi wengi na lengo la Serikali ya Awamu ya Sita ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona maji yanapatikana katika maeneo yote. Maeneo ambayo muda mrefu hayajapata nayo yanakwenda kupata, hivyo hivi karibuni tutaendelea na utekelezaji wa mradi huu ili kuona kwamba maji yanapatikana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa usemi wa majadiliano unaendelea na umekuwa wimbo wa muda mrefu; na kwa kuwa mradi huu nji muhimu sana kwa Taifa letu ikiwa ni sambamba na kupata ajira 5,000 zilizo rasmi na zisizo rasmi 25,000 na vile vile tunatambua kwamba, baada ya miaka 15 makaa ya mawe yatakuwa hayana soko tena duniani kutokana na teknolojia zinazoendelea.

Je, Serikali inaweza ikatupa muda specific time lini mtamaliza majadiliano na muwekezaji huyu ili tuende awamu nyingne na mradi huu, uweze kutekelezeka kwa maslahi ya wananchi wa Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Neema William Mgaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, mtakumbuka wakati tunawasilisha Taarifa ya Kamati kwenye Bunge lako tumeeleza kwa kirefu jinsi ambavyo Serikali imechukua jitihada za maksudi kuhakikisha tunakamilisha mapema majadiliano haya, lakini changamoto ilikuwa kwa upande wa wawekezaji hawa ambao tuliingia nao mkataba kabla. Hata hivyo tunaamini katika mwaka wa fedha ujao (2023/2024), In Shaa Allah, tutaweza kukamilisha kwa sababu tayari tuko kwenye hatua nzuri zaidi ili tuweze kufikia hatma ya majadiliano haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Naomba nimuulize swali la nyongeza Mheshimiwa Naibu Waziri, Shule ya Sekondari ya Kijombe ina shida sana ya maji ambayo iko ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe. Je, lini Serikali itahakikisha kwamba inapeleka maji katika shule ile kwa sababu ni shule ya bweni ili watoto wetu waweze kupata maji safi na salama?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Mbunge Neema kwa ufuatiliaji wa usalama wa watoto wetu na hili ni agizo ambalo tayari Wizara imelitoa katika mikoa yote. Naomba nitumie Bunge lako Tukufu niendelee kuwaagiza watendaji wetu wa Mkoa wa Njombe wahakikishe Sekondari ya Kijombe inapata maji safi na salama.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa biashara ya parachichi hivi sasa ni kubwa for export, na kwa kuwa biashara hii inafanywa zaidi na Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Mkoa wa Njombe pamoja na Mbeya.

Nataka kujua lini Serikali itaweka mfumo rafiki katika kuhakikisha kwamba wanaweka mfumo wa cold-room kwenye baadhi ya mabehewa ya TAZARA kama ilivyoainishwa kwenye blue print ili kuweza kuhakikisha kwamba parachichi zinafika Bandarini au Airport zikiwa na ubora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli moja ya changamoto kubwa katika mazao au biashara ya matunda na mbogamboga ni hii mifumo ya cold-rooms ambayo ni changamoto kubwa. Sasa hivi tayari tumeshaanza kwenye ngazi za maeneo ambayo wanalima parachichi ikiwemo Njombe na Iringa kuwa na viwanda lakini pia na cold-rooms ambazo zitasaidia kutunza matunda hayo.

Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa hoja yake kwamba tuone sasa kwenye vyombo vya usafirishaji kwa maana miundombinu hii ikiwemo kwenye reli nao wawe na mabehewa maalum ya kuwa na cold-rooms ambazo zitasaidia kusafirisha parachichi ili zifike Bandarini au Airport kwa wakati bila kuharibika.

Mheshimiwa Spika, tunalichukua hilo wazo na tunalifanyia kazi kuhakikisha kwamba biashara hii inakuwa endelevu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa ni muda mrefu Nyanda za Juu Kusini tumekuwa tukiainisha vivutio vipya mbalimbali vya utalii, lakini vile vile Nyanda za Juu Kusini tumebarikiwa kuwa na hifadhi ya kipekee ya Kituro ambayo hifadhi hii ulimwenguni ni aina ya kipekee, hakuna ambayo inafanana nayo.

Je, Serikali mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba mnakuza utalii wa nyanda za juu kusini?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nimpongeze sana Mheshimiwa Neema kwa kuendelea kuhamasisha utalii na hili ninalisema kwa dhati kabisa kwa sababu sasa hivi focus yetu ni kuelekea kwenye Nyanda za Juu Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mradi wa REGROW ambao ulishaanza tayari na tayari ni mradi ambao una madhumuni ya kuboresha maeneo ya Nyanda za Juu Kusini hususan miundombinu. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kuwa Kaskazini sasa hivi tunaelemewa watalii nikimaanisha kwamba ukipeleka watalii 1000 tayari kule kuna jam; focus ya Serikali ni kuelekeza hawa watalii sasa warudi nyanda za juu kusini na maeneo mengine na ndiyo mkakati wa Serikali. Nimhakikishie kwamba uhamasishaji unaoendelea sasa hivi ni kuwekeza lakini pia na kuhamasisha utalii katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini.

Kwa hiyo hili tumeliona na tunaendelea kulitengenezea mkakati madhubuti. Ahsante sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa wananchi wa Kata ya Saja, Kijombe, Uhenga ndani ya Wilaya ya Wanging’ombe wako mbali sana na huduma za kipolisi. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Kituo cha Polisi ndani ya Kata ya Saja ili kuwapa unafuu wananchi hawa?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Neema amekuwa mara kwa mara anaulizia masuala ya ulinzi, lakini jambo moja analonivutia ni kwamba kiwango cha uhalifu Njombe hakilingani na maeneo mengine hasa ile ya mipakani. Kwa hiyo niwapongeze wananchi kwa kuzingatia hilo. Kwa hivyo kadri hali ya fedha itakavyoruhusu tutaendelea kuimarisha kujenga vituo vya polisi katika maeneo yanayohitajika ikiwemo hii Kata aliyoitaja ya Saja kule Njombe.

Mheshimiwa Spika, nashukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kuweza kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Njombe – Itoni, watu bado hawajalipwa compensations nilipenda kujua lini watalipwa fidia wakazi hao? Lakini kibaya zaidi Mawengi – Mlangali tayari barabara imejengwa lakini kuna baadhi ya watu bado hawajalipwa fidia lini watalipwa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili naomba kujua barabara ya Makete – Mbeya mkandarasi ameisha saini mkataba lakini mpaka hivi sasa tunavyozungumza hajafika site lini atafika site na ujenzi wa barabara hii ukaendelea? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema William Mgaya Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi ambao ameuliza kwamba hawajalipwa fidia kwa eneo la Mawengi – Mlangali nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imeisha andaa na kukamilisha Jedwali la malipo ya hao watu wenye fidia wa Mawengi pamoja na hawa wa Itoni – Lusitu na zoezi la kuwalipa nataka nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge litafanyika muda si mrefu.

Mheshimiwa Spika, nakuhusu suala la barabara ya Makete – Isyonje mkandarasi alishapatikana ameisha onyeshwa site lakini kinachosumbua kwasasa kuanza yupo kwenye mobilizations ni hali halisi ya hewa kwa maana ya mvua nyingi inayoendelea lakini tayari mkandarasi ameishapatikana na ameisha kabidhiwa site, ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Gati la kushukia abiria jengo la mizigo ya wasafiri, jengo la abiria Bandari ya Manda Wilayani Ludewa utaanza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Gati la Manda upo kwenye mpango, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha kwamba tunajenga gati hili la Manda ili wananchi wasipate changamoto ambayo wanaipata sasa hivi, ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Moja kati ya sababu zinazowafanya vijana wa Nyanda za Juu Kusini, hususan Mkoa wa Njombe kutokupenda kulima zao hili la chai ni pamoja na bei ya chini ya zao la chai.

Je, ninyi kama Serikali mmejipanga vipi kuhakikisha kwamba mnawa-motivate vijana waweze kushiriki katika kilimo hiki cha chai ikiwa ni pamoja na kuanzisha program za out growers kwenye mashamba ya chai? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli zao la chai siyo vijana peke yake, baadhi ya maeneo wakulima wameanza kuling’oa. Tunapitia upya mfumo mzima wa chai. Ni sahihi kwamba, wakati bei ya chai inapanda ama pale ambapo tunakuwa tegemezi, mfumo wetu wa masoko kwa wenzetu walioko nje ya nchi, maana yake tunakuwa vulnerable siku zote. Kwa hiyo, kama Serikali kama hatua nilizozisema za mwanzo kuanzisha mnada, kuongeza value addition ndani ya nchi, kupunguza importation ya chai kutoka nje, automatically jambo hili litasaidia wakulima kuwa na uhakika wa soko na bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hii ni safari, nawaomba wakulima wa chai nchini, Serikali imeanza kuchukua hizi hatua. Nawaomba wasing’oe chai na wale wote waliouziwa viwanda, hasa nyanda za Kaskazini na baadhi ya maeneo ya Nyanda za Juu, tumewaandikia barua wafufue mashamba na kuviendesha vile viwanda. Kama hawawezi tutafute watu wengine watakaoweza kuwekeza katika maeneo hayo.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Shule ya Sekondari ya Igwachanya kuna boma la bwalo ambalo limejengwa kwa nguvu za wananchi takribani miaka kumi sasa. Waziri wa TAMISEMI, Mheshimiwa Jafo alipita akaahidi kupeleka pesa, na vilevile Mheshimiwa Bashungwa alipita tena akaahidi kupeleka pes: Je, lini mtapeleka pesa hizo zaidi ya Shilingi milioni 200 ili ziweze kukamilisha bwalo lile la Shule ya Sekondari ya Igwachanya?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili. Kuna Shule ya Msingi ya Saja, Usuka na Udonja, ziko kwenye hali mbaya sana, miundombinu yake ni chakavu sana: Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha kwamba shule zile zinakarabatiwa na kuwa bora kama shule nyingine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, nikijibu swali lake la kwanza la boma la bwalo katika shule hii ya sekondari ambayo ameitaja Mheshimiwa Neema, Serikali itaendelea kutafuta fedha na kuweka kipaumbele katika kumalizia bwalo hili. Kama alivyosema yeye, ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa. Hivyo tutakaa na wataalam wetu kuona tutapata wapi fedha kuweza kwenda kumalizia mabwalo haya.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, la shule hizi za msingi ambazo ni chakavu, Mheshimiwa Mbunge amezitaja; Serikali inaendelea kufanya ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi na ninyi Waheshimiwa Wabunge humu ndani mtakuwa ni mashahidi, kuna zaidi ya Shilingi bilioni 230 ya mradi wa boost ambayo tayari fedha zile zimeshakuwa disbursed katika shule hizi kwa ajili ya kuanza ukarabati na ujenzi wa miundombinu mipya katika shule hizi za msingi na ni nchi nzima.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya kutoka Njombe – Mdandu – Iyai kutokea Mbeya kwa kuwa barabara hii ni muhimu ndani ya Jimbo la Wanging’ombe na hatuna barabara ya lami yoyote zaidi ya hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara inayoanzia Njombe – Ramadhani – Iyai, Serikali imekuwa inajenga kwa awamu. Na katika mwaka huu wa fedha nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tumetenga fedha kwa ajili ya kuendelea kuijenga barabara hii kwa kiwango cha lami kuunganisha Makao Makuu ya Wanging’ombe na Makao Makuu ya Mkoa wa Njombe.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, ni lini Serikali itakarabati na kujenga upya majengo ya shule chakavu Wilaya ya Njombe, Ludewa, Wanging’ombe na Makete ndani ya Mkoa wa Njombe?

Swali la pili, ni lini Serikali itatua tatizo la upungufu wa Walimu wa Sayansi ndani ya Mkoa wa Njombe? ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nikijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Mgaya, swali lake la kwanza kuhusu ni lini Serikali itakarabati shule hizi kongwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Daktari Samia Suluhu Hassan ilikwisha karabati shule 89 hapa nchini, ambapo kule Mkoani Njombe kuna shule mbili ambazo zilipata fedha ya kukarabati ambayo ni shule ya Kivavi Sekondari iliyokuwepo Wilayani Makambako vilevile Njombe sekondari. Tunaendelea kuangalia ni namna gani tunaweza tukaendelea ukarabati wa shule kongwe ikiwemo zile zilizokuwepo Mkoani Njombe. Nimtoe mashaka Mheshimiwa Mbunge, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mheshimiwa Kairuki analishughulikia hili suala kuona ni namna gani atapata fedha ya ukarabati wa shule hizi kongwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikienda kwenye swali lake la pili la Walimu wa Sayansi. Hivi sasa Serikali ipo katika ukamilishaji wa mchakato wa kuajiri Walimu wa Sayansi na walimu kwa ujumla ambao ni 13,390 ambao wataanza kazi muda Serikali mrefu. Kwa hiyo, nikutoe shaka Mheshimiwa Neema Mgaya kwamba kule Mkoani Njombe nanyi mtapata mgao wa Walimu hawa ambao wanakuja. Mheshimiwa Neema amekuwa akilifatilia sana hili suala na nimwakikishie kwamba Serikali imekusikia na italifanyia kazi suala la upungufu wa walimu katika Mkoa wa Njombe. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Serikali imejenga madaraja mazuri kwenye barabara ya Lupila kwenda Ikonda: Je, lini mtajenga kwa kiwango cha lami ili kukamilisha kazi ile nzuri na wananchi wetu wakaweza kupita vizuri kwenye barabara ile? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, azma ya Serikali ni kujenga hizi barabara kwa kiwango cha lami. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kwa kuwa tumeshaanza kujenga hii barabara nzuri, tutahakikisha tunaifikisha mwisho ikiwa ni pamoja na barabara aliyoitaja kuijenga kwa kiwango cha lami kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Swali la kwanza; lini Serikali italipa fidia ya Mradi wa Makaa ya Magangamatitu na Katewaka, Wilaya ya Ludewa? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana ya kupitia upya Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma, amekwenda mpaka China sambamba na kulipa fidia. Sisi tunataka kujua, majadiliano na mwekezaji yamefikia hatua gani, lakini tunataka kujua vile vile mkataba utasainiwa lini ili mradi huu uanze kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kuhusu suala la fidia kwa Mradi wa Magangamatitu na Katewaka kwa sababu tumeshaanza kulipa fidia kwenye mradi mkubwa, tukikamilisha zoezi hili maana yake zoezi litakalofuata ni kuangalia tena miradi hii ya Magangamatitu na Katewaka ili kuona nako fidia zinalipwa kwa wananchi wanaopisha miradi hiyo.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua umuhimu wa Mradi huu mkubwa wa Liganga na Mchuchuma ambao kwa kweli utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa letu. Kama alivyosema Mbunge, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anafanya kazi kubwa sana, Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Diplomasia ya Kiuchumi tumeweza kufikia hatua nzuri sana kuweza kukamilisha majadiliano na hawa wawekezaji ambao mwanzoni walikuwa hawaji kwenye majadiliano.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie kwamba juhudi zinazochukuliwa na Rais wetu mpendwa, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ili kuhakikisha mradi huu unaanza mapema ziko kwenye hatua nzuri na tunaamini majadiliano haya sasa yatakamilika mapema kwa sababu nao wameanza kuonesha nia ya kutekeleza mradi bila kuleta vikwazo au vivutio vile ambavyo walikuwa wanadai mwanzo ambavyo vina hasara kwa Taifa letu, nakushukuru.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa barabara ya Makambako – Songea ni mbovu na nyembamba sana na hivi juzi imeleta ajali na watu tisa wamefariki.

Je, lini Serikali itatengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami yenye ubora kutoka Makambo mpaka Songea? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Njombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa kwamba barabara ya Makambako – Njombe hadi Songea ni barabara ambayo kwa kweli imechoka, ni barabara ya zamani sana, barabara ya tangu miaka ya 1984. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii tayari usanifu ulishakamilika na World Bank wameshaonesha nia ya kuijenga barabara hii upya ikiwa ni pamoja na kuipanua kwenye viwango vya sasa na mradi huu utahusisha pia na kujenga barabara ya bypass katika Mji wa Songea. Ahsante.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Njombe wengi wao ni wakulima wa zao la chai. Nataka kuuliza wizara mmejipanga vipi kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI kuhakikisha kwamba mnaboresha miundombinu katika mashamba ya chai ili tuweze kupata chai nyingi zaidi?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Njombe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuna changamoto katika baadhi ya maeneo ya uzalishaji kutokuwepo kwa miundombinu Rafiki lakini tunayo miradi ambayo tunaendelea kuitekeleza kupitia Agree connect ambayo pia imejihusisha na utengenezaji wa miundombinu. Nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba tutashirikiana na TAMISEMI kuhakikisha maeneo yote ya uzalishaji yanapitika kiurahisi ili tuweze kuimarisha na kukuza zao letu la chai katika Mkoa wa Njombe.

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; Serikali ina mpango gani wa kuimarisha Shamba la Mifugo la Kitulo wilaya ya Makete na shamba la mifugo la Sao Hill Iringa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 tumedhamiria kuhakikisha kwamba tunaimarisha mashamba yetu matano likiwemo hili la Kitulo na lile la Mabuki na Sao Hill ambayo tutayaongezea zana za kazi kama vile matrekta na zana zile za kuweza kuvunia majani kwa maana ya malisho, lakini pia vilevile kwa kuyaongezea ng’ombe wazazi bora ili tuweze kuzalisha zaidi ya ng’ombe 3,500 na kuwasambaza nchini kote, kwa hivyo, mpango huu tunao na tunaelekea katika kuutekeleza, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Waziri kumekuwa na mgogoro wa muda mrefu sana kati ya Hifadhi ya Kitulo na Vijiji vya Misilo, Lugoda, Igenge, Nkindo na Makwalanga. Je, lini Serikali itamaliza tatizo hili la mipaka kati ya Hifadhi na vijiji hivi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Neema, Mbuge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwape pole wananchi wa Makete hususan wanaozunguka eneo hili la Kitulo. Nilishawahi kuzungumza na Mheshimiwa Mbunge na nikatoa ahadi kwamba tungeenda kuutatua huu mgogoro, lakini kutokana na changamoto mbalimbali sikuweza kupata huo muda. Lakini ninamuahidi Mbunge na ananitazama hapa kwamba wananchi wa Makete wakae mkao wa kusubiri, tunaenda na Mheshimiwa Mbunge kutatua mgogoro huu. Na mgogoro huu tunaenda kuumaliza ili wananchi waweze kufanya kazi kwa uhuru na hifadhi tuweze kuisimamia vizuri. Ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Kutokana na mvua nyingi zilizonyesha mwaka jana kuna madaraja matatu ndani ya Wilaya ya Ludewa ambayo yapo chini ya TANROADS yaliharibika. Eneo la Muhoro, Nyapandi na Ludewa Vijijini, je, lini Serikali itajenga madaraja ya kudumu?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nataka nimuhakikishie Mbunge kwamba baada ya changamoto ya hayo madaraja bahati nzuri mimi nimekwenda na nimefika na tumefanya ukarabati na tunachokifanya sasa hivi katika bajeti hii ni kuagiza madaraja mengi ya vyuma ambayo yatatumika pale panapotekea changamoto ili kuweza kuokoa na kufanya matengenezo ya haraka ili kurudisha mawasiliano, ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Sisi watu wa Mkoa wa Njombe tunatambua kazi kubwa iliyofanywa na Serikali katika Mradi huu wa Maji wa Igongwi. Lakini vilevile tunatambua sababu mojawapo ya kusababisha mradi huu wa Igongwi kutokuendelea ni kutokana na kutopeleka fedha kwenye Mradi wa Maji wa Ruvuyo Wilaya ya Ludewa ambako ndiyo chanzo cha maji kinatokea. Je, lini Serikali itapeleka pesa kwenye Mradi wa Ruvuyo ili kuweza kuruhusu mradi huo wa Igongwi uendelee?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pil; Kuna baadhi ya Vijiji ambavyo viko ndani ya Jimbo la Njombe Mjini kikiwepo Kijiji cha Ihanga havikuwekwa kwenye mradi wa maji vijijini kimakosa. Je, lini Serikali itaweka vijiji hivi ambavyo viko kwenye Jimbo la Njombe Mjini havikuhesabika kama viko vijijini kuwekwa kwenye Mradi wa Maji Vijijini? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nimpongeze kwa ufuatiliaji. Mheshimiwa Neema hili umeishawahi kuniuliza mara kadhaa na nimeishalifanyia kazi kulingana na ufuatiliaji wako. Ili huu mradi upate kuendelea ni kweli fedha hapa katikati zilisimama lakini tumshukuru sana Mheshimiwa Rais tayari fedha Januari hii tumeanza kupokea ndani ya Wizara. Kwa hiyo, ni moja ya maeneo ambayo tutakwenda kupeleka fedha kwa awamu ili kazi ziweze kuendelea.

Mheshimiwa Spika, Eneo la Njombe mjini hivi vijiji ambavyo havikuhesabika katika miradi ya vijijini, ilifanyika hivyo kwa sababu ya jiografia yake. Lakini kwa ushirikiano wako wewe pamoja na Mbunge wa Jimbo wote mmeweza kufikisha suala na Viongozi wa Mkoa wa Njombe wameishapewa maelekezo kuona kwamba vijiji hivi navyo vinapelekewa huduma ya maji safi na salama. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, lini Serikali itatatua changamoto ya maji iliyopo ndani ya Wilaya ya Makete kule Mfumbi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Njombe, Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba baada ya kikao chako hiki cha Bunge, kwa sababu ni eneo specific ambalo amelitaja, tuweze kuonana ili niweze kujua na kuona kama limetengwa. Kama halijatengwa, basi tuone Serikali tunafanya nini ili kuhakikisha wananchi wa maeneo hayo wananufaika. Ahsante sana.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, naipongeza Taasisi ya Uvuvi na Utafiti kwa kuweza kuendelea na mchakato wa kubaini maeneo yanayofaa kwa ajili ya ufugaji wa samaki wa vizimba. Swali langu la kwanza; ni lini Serikali itamaliza mchakato huo ili wananchi wa Ludewa wapate fursa ya kuendelea na biashara hiyo?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Wizara ina mkakati gani wa kufanya utafiti katika maeneo ambayo ni mazalia ya samaki kwa lengo la kuhifadhi na kufanya samaki waendelee kuwa wengi katika Ziwa Nyasa? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba, tumepokea concern ya Mheshimiwa Mbunge, tutaiweka katika bajeti ya 2024/2025 ili kwenda kufanya tathmini katika eneo hilo analolizungumza Mheshimiwa Mbunge.

Mheshimiwa Spika, hili la pili, namna gani ya kuongeza uzalishaji wa samaki; kama nilivyosema katika majibu ya msingi kwamba, Serikali sasa imekuja na mpango wa vizimba na tunazidi kuhamasisha wavuvi wajikite zaidi katika vizimba kwa sababu, uvuvi huu wa sasa umebadilika duniani kote, kwamba sasa tunakwenda katika hali ya kutengeneza vizimba ili kuleta tija zaidi katika uzalishaji wa samaki.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu katika Maziwa yetu yote makubwa Nyasa, Victoria na Tanganyika, ukweli ni kwamba, mazalia ya samaki yanapotea kwa sababu ya wingi wa watu na uvuvi haramu. Kwa hiyo, ni lazima tuje na mkakati mpya ambao utawezesha watu wetu kuendelea na uvuvi wa kisasa zaidi, hasa kwenye vizimba, ahsante.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza baadhi ya mabehewa kuweka mfumo wa ubaridi (cold room) katika reli ya TAZARA ili tuweze kusafirisha parachichi zetu na mazao ya mboga mboga yamfikie mlaji wa mwisho yakiwa na ubora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Mgaya kwa sababu ni mdau mkubwa sana wa reli ya TAZARA na tukubali ukweli kwamba kwa sasa katika reli yetu na mabehewa yaliyopo hatuna cold rooms, lakini kila mtu anafahamu umuhimu wa ukuwaji wa sekta ya parachichi katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa Wizara tunapokea ushauri huu na tunapokwenda kwenye hatua ya pili ya maboresho makubwa ya reli yetu kutoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi tutaona namna ya kuweza kuweka hicho alichokizungumza cha cold room.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa maji wa kujenga mtambo wa kusafisha maji chanzo cha Mbukwa, Wilaya wa Wanging’ombe wenye thamani ya shilingi bilioni 3.5 mkandarasi alikabidhiwa tangu Oktoba, 2023. Wananchi wa Wanging’ombe wanataka kujua, ni lini mradi huu utaanza kufanya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, kwa niaba ya wananchi wa Mkoa wa Njombe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa mradi huu upo kwa ajili ya kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji. Serikali imetoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 154 kwa ajili ya kuhakikisha kwamba upatikanaji wa maji vijijini unaendelea kutekelezwa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeongea juzi hapa kwamba wakandarasi wamekuwa wakijifichia kwenye kivuli cha kwamba Serikali haijalipa. Serikali imetoa shilingi bilioni 154 kwa ajili ya maji vijijini na shilingi bilioni 69 kwa ajili ya Mamlaka ya Maji Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, namwomba tu Mheshimiwa Mbunge tuendelee kushirikiana na kupeana taarifa, nasi kama Serikali tuweze kuchukua hatua dhidi ya wakandarasi ambao wameonekana wanasuasua katika miradi ya Serikali, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, mgogoro wa Hifadhi ya Kituro na Vijiji vinavyozunguka Hifadhi ya Kituro ngazi ya Wilaya ya Makete, ngazi ya Mkoa wa Njombe ulishapeleka mapendekezo Wizarani. Kazi iliyobakia ni kwa Wizara tu kuthibitisha ili mapendekezo hayo yaweze kufanyiwa kazi.

Je, ni lini Wizara itafanyia kazi suala hilo ili tumalize ule mgogoro kule Makete? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge swali lake kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali inashughulikia migogoro hii kupata utatuzi wa migogoro ili kuondokana na changamoto hii. Katika kushughulikia migogoro hii umakini mkubwa unahitajika ili kuhakikisha kila mtu anapata haki stahiki, namuomba Mheshimiwa Mbunge awe na subira wakati tunalishughulikia jambo hili ili mwisho wa siku tukilimaliza lisiwe na changamoto nyingine yoyote.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ni lini Serikali itatatua shida ya maji Tarafa ya Wanging’ombe katika Jimbo la Wanging’ombe maeneo ya Saja, Kijombe na Kata ya Wanging’ombe? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana na pia nimshukuru sana Mheshimiwa Neema Mgaya, Mbunge wa Njombe Viti Maalum kwa kuendelea na kazi yake kubwa ya kuwasemea akina mama ambao ndio tunawapa kipaumbele katika kutatua changamoto za maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaaomba nilipokee suala hili twende tukalifanyie kazi kwa sababu bado tunaenda kwenye bajeti ijayo ili tuone kwamba ni namna gani tutaweza kuliweka kwenye mpango wa bajeti ili tuweze kwenda kuchukua hatua ya kuwafikishia huduma ya maji safi na salama kwa kujenga miradi ambayo itawasaidia kupata huduma ya maji safi na salama, ahsante. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Serikali imeshajenga kilometa 19.4 za barabara ya Njombe – Iyai yenye kilometa 74 ambayo inaunganisha Mkoa wa Njombe na Mbeya ndani ya Jimbo la Wanging’ombe kwa kiwango cha lami. Je, ni lini Serikali itamalizia ujenzi wa barabara hii kutokana na umuhimu na uzalishaji mkubwa unaofanywa na wananchi wa Jimbo la Wanging’ombe? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Mgaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua umuhimu wa barabara hii na namhakikishia Mheshimiwa Neema Mgaya kwamba tutaipa kipaumbele barabara hii kadiri fedha zitakavyokuwa zinapatikana, ahsante sana. (Makofi)
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haioni umuhimu wa kutengeneza baadhi ya mabehewa kuweka mfumo wa ubaridi (cold room) katika reli ya TAZARA ili tuweze kusafirisha parachichi zetu na mazao ya mboga mboga yamfikie mlaji wa mwisho yakiwa na ubora? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana dada yangu Mheshimiwa Mgaya kwa sababu ni mdau mkubwa sana wa reli ya TAZARA na tukubali ukweli kwamba kwa sasa katika reli yetu na mabehewa yaliyopo hatuna cold rooms, lakini kila mtu anafahamu umuhimu wa ukuwaji wa sekta ya parachichi katika mikoa ya Mbeya, Njombe, Iringa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa unyenyekevu mkubwa Wizara tunapokea ushauri huu na tunapokwenda kwenye hatua ya pili ya maboresho makubwa ya reli yetu kutoka Dar es Salaam mpaka Kapiri Mposhi tutaona namna ya kuweza kuweka hicho alichokizungumza cha cold room.
MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Igando – Kijombe ndani ya Jimbo la Wanging’ombe mkandarasi amepewa kazi tangu Septemba, 2023 wenye thamani ya shilingi bilioni 10.8. Tunataka kujua, ni lini mradi huu utaanza? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Mbunge. Nataka nimhakikishie kwamba, kwa kuwa mradi huo upo katika utaratibu, utaanza mara moja. Nami nipo tayari kwenda kufuatilia na kusimamia juu ya uanzaji wa mradi huo, ahsante sana.