Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Rose Cyprian Tweve (13 total)

MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Serikali imeweka utaratibu wa kuzitaka Halmashauri zote za Wilaya kutenga asilimia tano ya mapato ili kuwawezesha wanawake na vijana kupata mikopo:-
Je, ni akinamama wangapi au vikundi vya wanawake vingapi vimenufaika na mikopo hiyo katika Halmashauri za Wilaya ya Mufindi, Kilolo, Iringa Mjini na Iringa Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2015/2016, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na Wanawake, Halmashauri za Mkoa wa Iringa zimewezesha vikundi vya wanawake 430 na vikundi vya vijana 47 kupata mikopo.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi iliwezesha vikundi vya wanawake 331, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo vikundi vitatu, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vikundi 73 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa vikundi 23.
Kwa upande wa vikundi vya vijana; Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi vikundi 13, Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo vikundi sita, Halmashauri ya Wilaya ya Iringa vikundi 28 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa hakukuwa na kikundi hata kimoja.
Mheshimiwa Spika, Serikali inaimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kupitia mfumo wa electronic ili kuongeza mapato yanayokusudiwa kufanya mifuko hiyo kutengewa fedha zaidi. Aidha, katika bajeti ya mwaka 2016/2017 sharti la kupitisha makisio ya bajeti ya kila Halmashauri ilikuwa ni kuonesha kiwango kilichotengwa kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Napenda kulihakikishia Bunge lako kuwa tutaendelea kusimamia kwa karibu suala hili na kuchukua hatua yoyote itakayobainika kuhujumu mpango huu wa kuwawezesha wananchi.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Ni azma ya Serikali ya CCM kumuinua mwanamke kiuchumi na azma hiyo ilipelekea Serikali kuanzisha Benki ya Wanawake.
Je, Serikali haioni kuwa sasa ni wakati muafaka kufungua madirisha ya benki hiyo mikoani hasa Mkoa wa Iringa ambapo kuna Community Bank (MUCOB) iliyopo Wilayani Mufindi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia Desemba, 2016 Benki ya Wanawake imefanya kazi katika mikoa saba ambayo ni Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Iringa, Njombe, Mbeya na Ruvuma. Mwaka 2014 madirisha mawili yalifunguliwa Iringa Mjini na Makambako na hadi kufikia Desemba, 2016 jumla ya wajasiriamali 6,850; wanawake wakiwa 5,350 na wanaume wakiwa ni 1,500 walipata mikopo kupitia madirisha hayo ambayo wajasiriamali wa Mufindi nao wamefaidika. Aidha, benki imefungua vituo vya kutolea mikopo 252 kufikia Desemba, 2016 na Mufindi kuna kituo kimoja kilichopo Mafinga ambacho kimetoa mikopo ya jumla ya shilingi milioni 120 kwa wateja 146, wanawake wakiwa 117 na wanaume wakiwa 32.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Benki ya Wanawake Tanzania imeingiza suala la kufungua dirisha katika Benki ya Wananchi ya Mufindi (MUCOB) kwenye mpango mkakati wa mwaka 2012 mpaka 2017. Tunatarajia dirisha hili litafunguliwa mara tu tutakapopata fedha za kutekeleza mpango huu. Benki ya Wanawake ina mkakati wa kuenea nchi nzima, lakini kikwazo kikubwa ni ukosefu wa mtaji. Endapo benki itafanikiwa kupata mtaji wa kutosheleza itaweza kufungua ofisi zaidi mikoani ili kuwahudumia wananchi wengi zaidi na kwa ukaribu.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Pamoja na kwamba sekta ya kilimo ndiyo yenye kuajiri Watanzania walio wengi, lakini sekta hiyo imekuwa na maendeleo hafifu kutokana na watumishi wachache wenye ujuzi wa kutosha na ukosefu wa vitendea kazi kama vile pikipiki, zana za kufundishia na kadhalika.
Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi wa kufanya mapinduzi ya kilimo kwa kuwa na wataalam wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa Sekta ya Kilimo ni muhimu na ndiyo yenye kuajiri Watanzania wengi, hivyo mapinduzi ya kilimo pamoja na mambo mengine yatachangiwa uwepo na wataalam wa kutosha wenye taaluma na ujuzi stahiki ili waweze kushauri matumizi ya teknolojia na kanuni bora za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ili kuleta mapinduzi ya kilimo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya Maafisa Ugami wenye ujuzi ili kila Kata na kijiji kiwe na Afisa Ugani mmoja. Aidha, Serikali inaendelea kuboresha na kuwezesha Vituo vya Kilimo na Vituo vya Rasilimali za Kilimo za Kata kwa ajili ya kufundisha teknolojia mbalimbali za kilimo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia mwaka 2016/2017, Serikali imeajiri Maafisa Ugani 8,756 sawa na asilimia 43 ya mahitaji ya Maafisa Ugani 20,374 katika ngazi ya kijiji, Kata na Wilaya. Jumla ya wataalam wa kilimo 8,000 ngazi ya Astashahada na Stashahada waliohitimu mafunzo katika Vyuo vya Kilimo wameajiriwa katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, Serikali inaendelea kusomesha vijana tarajali na kuwaajiri kulingana na upatikanaji wa rasilimali fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mikakati mingine ni pamoja na kuboresha huduma za ugani kwa kusambaza teknolojia za kilimo bora kwa wakulima kwa kutumia njia mbalimbali hususan shamba darasa, vipindi vya redio na luninga, mchapisho na Maonesho ya Kilimo - Nane Nane.
Aidha, Serikali itaendelea kutoa ushauri wa kitaalam na kuandaa miongozo na mafunzo ya huduma za ugani, ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa kazi za ugani na kuboresha usambazaji wa teknolojia za kilimo bora kwa wakulima nchini.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-
Kumekuwa na idadi kubwa ya ajali nchini zinazosababisha vifo, majeruhi na upotevu wa mali:-
• Je, kwa kipindi cha miaka miwili kuanzia 2016
– 2018 ni ajali ngapi zimetokea na kusababisha vifo au majeruhi?
• Je, ni waathirika wangapi waliomba fidia na wangapi mpaka sasa wamelipwa fidia zao kutoka kampuni za bima?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani lilichukua hatua za makusudi kupunguza ajali ambapo mpaka kufikia Disemba, 2017 limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani kwa asilimia 43.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2016 kulitokea jumla ya ajali 9,856 ambazo zilisababisha vifo 3,256 na majeruhi 2,128. Mwaka 2017 kulitokea ajali 5,310 ambazo zilisababisha vifo 2,533 na majeruhi 5,355 wakati kwa kipindi cha Januari hadi Februari, 2018 zimetokea ajali 769 ambazo zimesababisha vifo 334 na majeruhi 698.
• Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 jumla ya waathirika wa ajali 1,583 walilipwa fidia yenye jumla ya thamani ya fedha za kitanzania bilioni 7.3 kutoka kampuni mbalimbali za bima.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Imekuwa ni kawaida sasa kwa Askari wa Usalama barabarani kusimamisha magari ya usafiri wa Umma kama vile daladala na mabasi na kadhalika:-

Je, ni lini Serikali itaandaa utaratibu wa kuwa na Vituo Maalum vya Ukaguzi huo ili kuokoa muda wa wasafiri?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usalama Barabani, Sura ya 168 iliyorejewa mwaka 2002 Kifungu cha 81, kinampa uwezo Askari Polisi wa kulisimamisha gari lolote barabarani au sehemu yoyote anapolitilia shaka na kulikagua au pindi linapokuwa limetenda kosa.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani limeshaandaa utaratibu wa kuwa na vituo maalum vya ukaguzi wa mabasi ya Umma katika vituo vikuu vya mabasi vyote katika kila Mkoa ambapo mabasi ya abiria hufanyiwa ukaguzi kabla ya kuanza safari na pale yanapofika mwishoni wa safari.

Mheshimiwa Spika, aidha, ukaguzi wa pembezoni mwa barabara (road side inspection) ambao huhusisha mabasi ya daladala na vyombo vingine vya moto hufanyika katika vituo vya ukaguzi maalum (check points) ambavyo vipo katika barabara kuu na katika barabara nyingine za Miji pamoja na Majiji.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Serikali imekuwa ikihimiza wananchi kuchangia damu na kuihifadhi katika benki za damu kwa ajili ya watu wenye uhitaji.

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo kama vile figo na moyo kutoka kwa watu waliopata ajali na wapo kwenye hali ya kupoteza maisha au kutoka kwa watu walioridhia kutolewa viungo hivyo na kuvihifadhi kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo?.
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ipo katika hatua za mwisho za kuandaa Muswada wa Sheria ya Uvunaji, Utunzaji, Usafirishaji na Upandikizaji wa viungo vya binadamu ikiwemo, Figo, Moyo, Maini, Mapafu, sclera ya macho, Uroto, IVF, pamoja na Stem cells itakayoweka utaratibu mzuri wa namna ya kufanya kazi hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria itaelekeza vitu vya kuzingatia kwa mpokeaji na mtoaji wa viungo. Sheria hii itaweka utaratibu kwa watu wanaoridhia kutolewa viungo vyao pindi wanapokaribia kupoteza maisha ikiwa mchangiaji (donor) huyo atakuwa ameridhia viungo vyake vitumike kwa ajili ya jamii inayohitaji viungo hivyo pindi akipoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi yetu inaheshimu haki za binadamu ikiwemo haki ya kuishi, mtu kupata ajali na kutolewa viungo vyake litafanywa pale ambapo mhusika atakuwa ameridhia akipata ajali na akawa hana uwezo wa kupona atolewe viungo, basi hatua za kisheria na kitabibu zitatumika ili kutoa viungo hivyo na kuvihifadhi kwa ajili ya matumizi ya mtu atakayehitaji.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha utaratibu maalum wa kuvuna viungo vya binadamu kama vile figo na moyo kwa ajili ya Watanzania wenye uhitaji wa viungo hivyo?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Hospitali ya Benjamin Mkapa zimeanza kutoa huduma ya uvunaji na upandikizwaji wa figo nchini tangu mwezi Novemba, 2017 kutoka kwa wachangiaji walioridhia. Hadi sasa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili imepandikiza figo 62 na Hospitali ya Benjamin Mkapa imepandikiza figo 18. Aidha, kwa upande wa upandikizaji wa moyo, Serikali inaendelea kujenga uwezo wa ndani wa kutoa huduma hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya upandikizaji wa viungo nchini kama ambavyo Mbunge ameainisha, Serikali imeandaa Muswada wa Kutunga Sheria itakayoongoza taratibu za uvunaji, utunzaji na upandikizaji wa viungo ambayo ipo kwenye hatua ya ukusanyaji wa maoni kutoka kwa wadau. Hata hivyo, kwa kuwa huduma zimeanza kutolewa, kwa sasa nchi inatumia miongozo ya kimataifa inayosimamia uvunaji na upandikizaji wa viungo.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Kumekuwepo na mkanganyiko wa tafsiri ya umri wa miaka 18 katika Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto na Sheria ya Kanuni za Adhabu na kupelekea kuvunja misingi ya Katiba: -

Je, Serikali haioni umuhimu wa kuzifanyia mapitio Sheria hizo hususan kifungu cha 131 (2) ya Sheria ya Kanuni za Adhabu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve Mbunge wa Viti Maalumu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, mtu aliye na umri chini ya miaka 18 anatambulika kuwa ni mtoto. Pamoja na kwamba kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mtoto kinabainisha kuwa mtoto ni mtu mwenye umri chini ya miaka 18, Kifungu cha 131(2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu hakitoi tafsiri ya mtoto bali kinatoa adhabu kwa mtu mwenye miaka 18 au chini ya hapo anayekuwa na hatia ya kosa la kubaka na kupewa adhabu mbalimbali ikiwemo kuchapwa viboko kwa mkosaji wa mara ya kwanza, kufungwa jela kwa miezi 12 pamoja na viboko kwa mkosaji wa mara ya pili, au kifungo cha maisha kwa mkosaji kwa mkosaji anayejirudia kwa mara ya tatu. Kitaalamu hawa wanaitwa young offenders’ au wakosefu wenye umri mdogo.

Mheshimiwa Spika, Sheria zetu mbalimbali nje ya sheria ya Mtoto, zinaweka umri wa mtoto kulingana na muktadha na mazingira ya jambo mahsusi kama vile mikataba, jinai, kupiga kura, leseni za udereva na kadhalika. Kufuatia kutungwa Sheria ya Mtoto mwaka 2009, iliyotokana na Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto wa 1989 pamoja na masharti ya Ibara za Haki za ujumla za Binadamu kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977, na kwa kuwa Kifungu cha 131(2) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kilifanyiwa marekebisho mwaka 2009 na baada ya kutungwa kwa Sheria ya Mtoto, ni dhahiri kuwa hakivunji misingi ya Katiba.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, Serikali sasa inapoendelea kuzipitia sheria mbalimbali, itakipitia pia kifungu hicho cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ili kufanya marekebisho kutokana na uhitaji uliopo kwa kuzingatia ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Mbunge, ahsante.
MHE. HAWA M. CHAKOMA K.n.y. MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Je, kwa nini Serikali isiwekeze fedha Kiwanda cha Viuadudu Kibaha ili kutokomeza malaria nchini?

NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali na Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mhemishimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha mwaka 2017 hadi 2023, Serikali imenunua viuadudu vyenye thamani ya shilingi bilioni 5.9 na kutumika katika ngazi ya halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuhakikisha uhakika wa upatikanaji wa viuadudu kutoka Kiwanda cha Kibaha, kwa kipindi cha mwaka 2024 - 2026, Wizara ya Afya imeomba kupatiwa jumla ya shilingi bilioni 129.1 kwa ajili ya utekelezaji wa afua ya unyunyiziaji wa viuadudu ili kuangamiza viluilui vya mbu kwenye mazalia ili kufikia lengo la kutokomeza malaria ifikapo mwaka 2030.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya inashirikiana na Shirika la Taifa la Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha kiwanda kinapata ithibati kutoka Shirika la Afya Duniani ili kuongeza wigo wa upatikanaji wa fedha za kutekeleza afua hii kutoka kwa wadau mbalimbali wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. HUSNA J. SEKIBOKO K.n.y. MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza:-

Je, lini Serikali itabadili Mitaala ya Elimu ili kwenda na wakati?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha uandaaji na uidhinishaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la mwaka 2023 na Mitaala katika ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Mafunzo ya Ualimu kwa lengo la kufanya elimu yetu iende na wakati. Mitaala iliyoboreshwa imezingatia mahitaji ya sasa ikiwa ni pamoja na kuweka msisitizo katika stadi za karne ya 21 ili kumjengea mhitimu stadi za Kuwasiliana, Kushirikiana, Ubunifu na fikra tunduizi. Aidha, ratiba ya utekelezaji wake inatarajiwa kuanza rasmi Mwezi Januari, 2024 na kukamilika mwaka 2027.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Elimu ya Kati na Elimu ya Juu, mapitio ya programu mbalimbali pia yanaendelea kwa lengo la kuifanya iende na wakati, vipaumbele vya nchi na mahitaji ya soko la ajira. Kwa mfano, kwa upande wa Elimu ya Juu kupitia Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET) programu zaidi ya 300 zitahuishwa au kuanzishwa, nakushukuru.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa zao la pareto?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Rose Cyprian Tweve, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mikakati mbalimbali ya kuongeza uzalishaji wa zao la pareto. Mikakati hiyo ni pamoja na kuimarisha utafiti wa zao hilo ili kubadili kilimo kuwa cha kibiashara, chenye tija, himilivu na kushirikisha sekta binafsi ili kuwa na kilimo endelevu.

Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia misingi hiyo ya kuleta mageuzi katika kilimo cha zao la pareto, katika mwaka 2021/2022 Serikali ilitoa fedha kiasi cha shilingi milioni 200 kwenda Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kwa ajili ya kuzalisha mbegu bora za pareto ambapo kiasi cha kilo 1,400 zimezalishwa na kusambazwa kwa wakulima katika msimu wa mwaka 2023/2024. Mbegu hizo zinatarajiwa kupandwa katika eneo la ekari 5,600 na kuzalisha wastani wa tani 2,240 za maua ya pareto.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Je, Halmashauri ngapi zimetekeleza agizo la Waziri Mkuu kununua dawa za viuadudu kutoka Kiwanda cha Kibaha ili kutokomeza mazalia ya mbu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa kudhibiti Malaria imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa afua ya unyunyuziaji wa viuadudu katika mazalia ya mbu yaliyotambuliwa katika halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeendelea kuzielekeza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kununua dawa za viuadudu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2023/2024 jumla ya halmashauri 126 zimetenga shilingi milioni 775.89 kwa ajili ya ununuzi wa dawa hizo.
MHE. ROSE C. TWEVE aliuliza: -

Je, kigezo cha mtihani wa kuandika kabla ya kujiunga na Vyuo vya Ufundi (VETA) ni cha lazima kwa wanafunzi wa mafunzo kwa vitendo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) inatoa mafunzo ya ufundi stadi kwa nadharia kwa 30% na vitendo kwa 70%.

Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa stadi za kuandika, kusoma na kuhesabu katika utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) hutoa mitihani ya majaribio (aptitude test) wa kujiunga kwenye vyuo vyake. Hii ni kwa sababu kuna umuhimu wa kubaini endapo wanaotaka kujiunga na vyuo vya VETA wanamudu stadi za KKK ikiwa ni kigezo cha kujiunga na vyuo vya ufundi stadi na pia kwa ajili ya muendelezo wa kielimu kwa hapo baadae pindi mwanafunzi akihitaji kujiendeleza zaidi. Ninakushukuru sana.