Primary Questions from Hon. Subira Khamis Mgalu (18 total)
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, ni lini Ujenzi wa barabara ya Kibaha - Mapinga, km 23 kwa kiwango cha lami utaanza na kukamilika kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya CCM ya mwaka 2015?
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kibaha (TAMCO) - Mapinga yenye urefu wa kilometa 23 ni barabara ya mkoa inayohudumiwa na Wakala wa Barabara kupitia Ofisi ya Meneja wa Mkoa wa Pwani. Ili barabara hii iweze kujengwa kwa kiwango cha lami, Serikali imefanya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ambao umekamilika. Pamoja na juhudi hizo hadi sasa tayari ujenzi kwa kiwango cha lami wa kilometa moja kuanzia njia panda ya TAMCO umekamilika kwa kuwa eneo hilo halikuwa na tatizo la ulipaji wa fidia.
Eneo lote lililobaki katika barabara hii linahitaji kulipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi wa barabara hiyo. Kwa sasa Serikali inatafuta fedha za kulipa fidia kabla ya kuendelea na ujenzi wa sehemu iliyobaki.
MHE. SUBIRA K. MGALU Aliuliza:-
Je, ni lini ujenzi wa barabara ya kutoka Kisarawe - Mwanerumango kilometa 64 itajengwa kwa lami na kukamilika kama ilivyoahidiwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Kisarawe - Mpuyani - Maneromango yenye urefu wa kilometa 54 ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Pugu - Kisarawe - Maneromango - Vikumburu ambayo jumla yake ni kilometa 97.7 inayohudumiwa na Wakala ya Barabara wa Mkoa wa Pwani. Upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami wa barabara hii umekamilika. Aidha, mpaka sasa kilometa 7.67 zimeshajengwa kwa kiwango cha lami. Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa kipande kingine cha mita 800.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu iliyobaki ya barabara hii ni ya changarawe na hufanyiwa matengenezo ya kawaida na ya muda maalum kila mwaka ili ipitike muda wote. Ujenzi kwa kiwango cha lami utaendelea hatua kwa hatua kulingana na upatikanaji wa fedha.
Aidha, katika mwaka wa fedha 2017/2018 jumla ya shilingi bilioni 3,157 zimependekezwa kwa ajili ya kuendelea kuijenga kwa kiwango cha lami barabara hii.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, ni lini ukarabati wa barabara ya Mlandizi – Chalinze utaanza kama ilivyoahidiwa katika Ilani ya CCM ya mwaka 2015?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, barabara ya Mlandizi – Chalinze yenye urefu wa kilometa 44 ni sehemu ya barabara kuu itokayo Dar es Salaam kwenda Tunduma kupitia Morogoro. Kwa mara ya mwisho sehemu hii ya barabara ilifanyiwa ukarabati mkubwa kati ya mwaka 1990 hadi 1992. Kulingana na umri huo barabara hii inatakiwa ijengwe upya hata hivyo kutokana na uhaba wa fedha Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbli za kuwezesha barabara hii kupitika wakati inatafuta fedha za kuijenga upya.
Mheshimiwa Spika, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Marabara Mkoa wa Pwani pamoja na maabara kuu ya vifaa vya ujenzi yaani Central Materials Laboratory, imefanya utafiti wa kina ili kutathimini uwezo wa barabara ya Mlandizi – Chalinze kuhimili ongezeko kubwa la magari na uzito. Matokeo ya utafiti huo yalipendekeza zichukuliwe hatua za muda mfupi ambazo zinahusisha kuondoa tabaka la lami ya sasa katika maeneo yenye mawimbi na yaliyodidimia na kuweka tabaka ya lami nzito iliyoimarishwa. Kazi hii ya ukarabati itaanza mara tu msimu wa mvua utakapoisha.
Mheshimiwa Spika, aidha, hatua za muda mrefu zitahusisha kuijenga upya barabara hii mara fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2014/2015 na 2015/2016 jumla ya kilometa 15 zilifanyiwa ukarabati kwa gharama ya shilingi bilioni 9.072. Aidha, katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017 shilingi 3,000,000,000 zilitengwa kwa ajili ya ukarabati na mkandarasi ataanza ukarabati mara tu msimu wa mvua utakapoisha ambapo jumla ya kilometa 12.55 zitafanyiwa ukarabati. Vilevile Serikali imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.175 kwa ajili ya kuendelea na ukarabati wa barabara hii katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, ni lini Hospitali ya Rufaa Tumbi na Hospitali za Wilaya za Mkoa wa Pwani zitapokea vifaa tiba ikiwa ni sehemu ya fedha za kupambana na UVIKO-19?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani - Tumbi imeshapokea vifaa tiba 74 kati ya 77 vilivyoagizwa kwa fedha za kupambana na UVIKO-19, hii ni sawa na asilimia 94 ya vifaa vyote vilivyoagizwa ikiwemo mashine ya CT Scan. Kazi ya kusimika vifaa hivi inaendelea na inatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba, 2022.
Mheshimiwa Spika, aidha, kwa upande wa Hospitali za Wilaya, ujenzi wa majengo ya huduma za dharura yaani EMD na majengo ya huduma za wagonjwa waliopo kwenye uangalizi maalum yaani ICU unaendelea. Hivyo vifaa tiba kwa ajili ya hospitali hizi vitafikishwa mara baada ya ujenzi kukamilika.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, kuna mpango gani wa kugawa mashine za kutolea risiti EFD kwa Wafanyabiashara ili kuongeza wigo wa walipa kodi?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha kuwa kila mfanyabiashara anapata mashine za EFD kwa njia rahisi na isiyo na gharama, Serikali kupitia TRA ilianzisha mfumo rahisi wa utoaji wa risiti ujulikanao kama Visual Fiscal Devices (VFD). Mfumo huu wa kisasa wa utoaji wa risiti pasipo kuhitaji kutumia mashine kama ilivyo sasa badala yake mtumiaji anaweza kutumia vifaa vingine vya kieletroniki kama vile simu janja, kompyuta na vishikwambi kutoa risiti zilizounganishwa na mfumo wa TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo unaendelea kutumika na kusambaa nchi nzima na hauna gharama badala yake mtumiaji ataingia gharama ndogo ya bando ili kupata mtandao wakati wa matumizi. Aidha, wafanyabiashara wanaruhusiwa kisheria kujirejeshea gharama ya ununuzi wa mashine za EFD wakati wa uandaaji wa hesabu zao za kodi wanazopaswa kulipa. Ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za ujenzi wa kiwango cha lami kwa barabara ya Mziha – Kibindu – Mbwewe?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, kunahitajika kufanyika upembuzi yakinifu na usanifu wa kina. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kwa barabara ya Mziha – Kibindu – Mbwewe yenye urefu wa kilometa 68.63. Baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na gharama za ujenzi kujulikana Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi huu, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya uendeshaji wa Mabaraza ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, nakushukuru na kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikiendesha Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi tangu mwaka 2017. Lengo kuu la majukwaa hayo ni kuwakutanisha wanawake ili waweze kujadili fursa za kiuchumi na changamoto mbalimbali wanazokutana nazo wakati wa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi nchini.
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwaka 2021/2022, mikoa yote 26 imezindua majukwaa ya wanawake katika halmashauri 140 kati ya halmashuri 184 na kata 1,149 kati ya kata 2,404. Lakini pia mitaa na vijiji 1,776 kati ya mitaa na vijiji 7,613.
Mheshimiwa Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali ilitenga fedha zaidi ya milioni 72 na katika mwaka wa fedha unaokuja 2023/2024, Serikali imetenga shilingi milioni 200 kwa ajili ya uendeshaji wa majukwaa hayo.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, lini Serikali itatekeleza mradi wa kusambaza maji kutoka Mlandizi hadi Mzenga – Kisarawe?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea na usanifu wa kina wa mradi wa maji kutoka bomba kuu la DAWASA Mlandizi kupeleka kwenye vijiji 19 vya Wilaya ya Kisarawe vikiwemo vijiji vya Kata ya Mzenga. Usanifu huo unatarajia kukamilika mwezi Agosti, 2023 na ujenzi kufanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE K.n.y. MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, lini Serikali itatangaza Mamlaka ya Mji Mdogo Bagamoyo kuwa Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri Wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI ilipokea mapendekezo ya kupandishwa hadhi ya Mamlaka ya Mji Mdogo wa Bagamoyo kuwa Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo.
Mheshimiwa Spika, baada ya kufanya tathmini ya kina imebainika kuwa, Halmashauri hii bado ina upungufu wa miundombinu mbalimbali yakiwemo majengo ya utawala na huduma za kijamii na mapato yasiyotosheleza kuipandisha hadhi Mamlaka ya Mji Mdogo kuwa Halmashauri ya Mji.
Mheshimiwa Spika, dhamira ya Serikali kwa sasa ni kuboresha miundombinu katika maeneo ya utawala yaliyopo na siyo kuanzisha maeneo mapya.
MHE. TWAHA A. MPEMBENWE K.n.y. MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, Serikali ina mkakati gani wa kukarabati na kuongeza uwezo wa Gereza la Dimani Wilayani Kibiti?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Twaha Ally Mpembenwe, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali itatenga fedha shilingi milioni 350 kwa ajili ya ukarabati na upanuzi wa baadhi ya Magereza nchini. Gereza la Dimani Wilaya ya Kibiti ni moja ya magereza yatakayokarabatiwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali, kupitia mpango na bajeti wa kila mwaka itaendelea kutenga fedha za ukarabati na upanuzi wa Magereza yenye uhitaji huo, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Vijiji vya Msata, Kihangaiko na Pongwe Msungura kutokana na maeneo yao kuchukuliwa na Jeshi la Wananchi?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa vile na mimi ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu tangu niteuliwe tena kuwa Waziri wa Ulinzi na na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa baraka zake, lakini nitoe shukrani zangu za dhati kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuniamini kuendelea kumsaidia katika nafasi hii. Niahidi kwamba nitaendelea kufanya kazi zangu kwa uwezo wangu wote, kwa uaminifu, kwa uadilifu na kwa kujituma.
Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, maeneo ya Vijiji vilivyotajwa yaani Msata, Kihangaiko, na Pongwe Msungura yapo katika Makambi mawili ya Jeshi ambayo ni RTS Kihangaiko na Msata Military Training Base katika Wilaya ya Chalinze. Serikali imeendelea na kutatua migogoro hii ya ardhi katika maeneo haya na katika mwaka 2021 ulifanyika uthamini wa awamu ya kwanza uliojumuisha Vijiji vya Msata, Pongwe Msungura na baadhi vitongoji katika Kijiji cha Kihangaiko. Uthamini awamu ya pili ulifanyika mwaka 2022 ukijumuisha vitongoji viiyosalia katika Kijiji cha Kihangaiko.
Mheshimiwa Spika, Taarifa ya Uthamini uliofanyika mwaka 2021 iliwasilishwa katika Ofisi ya Ardhi Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ili kukamilisha taratibu. Taratibu zitakapokamilishwa na Halmashauri ya Wilaya hii itawasilisha jedwali la malipo kwa Mthamini Mkuu wa Serikali kwa kuidhinishwa na hatimaye kufanyiwa uhakiki na malipo na Wizara ya Fedha.
Mheshimiwa Spika, katika uthamini uliofanywa na Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 2022, Wizara ya Fedha imekwishafanya uhakiki kwa Vitongoji vya Funta, Chokozeni na Kudikongo, vilivyopo katika Kijiji cha Kihangaiko kwa ajili ya kulipa fidia na malipo ya shilingi 330,788,467 yameshafanyika kwa wananchi katika Kitongoji cha Funta.
Mheshimiwa Spika, Wizara inaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha, lakini pia na Halmashauri ya Chalinze ili kuhakikisha ulipaji wa fidia unakamilika.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, kuna mpango gani wa kujenga nyumba za walimu Shule za Msingi katika Kata za Salale, Kiongoroni, Mbuchi na Maparoni Kibiti?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uhitaji wa nyumba za walimu hususan katika maeneo ya visiwani na imeendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali ilitenga shilingi bilioni 55.57 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 809 zenye uwezo wa kuchukua kaya 1,916.
Mheshimiwa Spika, kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Kata za Maparoni na Kiongoroni ambazo zipo visiwani, Serikali imepeleka shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za walimu (2 in 1) katika Shule za Msingi Maparoni na Jaja na taratibu za ujenzi wa nyumba hiyo zinaendelea.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu hususan katika maeneo ya pembezoni ikiwemo katika Visiwa vya Kata za Salale, Kiongoroni, Mbuchi na Maparoni Kibiti.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza: -
Je, upi mpango wa kuwapa mafunzo Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ngazi za Vitongoji, Vijiji, Kata na Wilaya – Pwani?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa Mikoa iliyofanya vizuri katika kuanzisha majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ambapo Jukwaa la Mkoa limeanzishwa kwa mafanikio makubwa hadi kufikia wazo la kuanzisha kiwanda cha vifungashio. Wizara katika bajeti yake ya mwaka 2023/2024 imetenga kiasi cha shilingi milioni 161 kwa ajili ya kujenga uwezo wa majukwaa, ambapo Mkoa wa Pwani utakuwa miongoni mwa Mikoa iliyopo.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha Mradi wa Building a Better Tomorrow katika Bonde la Mto Rufiji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi kufikia Machi, 2024, jumla ya ekari 340,245.3 zimebainishwa na kupimwa afya ya udongo kwa ajili ya Programu ya BBT katika Mikoa ya Dodoma, Kigoma, Mbeya, Singida, Tanga, Njombe na Kagera. Kwa sasa maandalizi ya mashamba yameanza katika Mkoa wa Dodoma.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2024/2025, Wizara imepanga kuanza Mradi wa BBT kwa halmashauri 100 zitakazotenga maeneo yenye hekta 200 kwa kujenga miundombinu ya umwagiliaji na kutoa utaalam. Aidha, halmashauri zitakuwa na jukumu la kudahili vijana kutoka katika halmashauri husika ili waweze kunufaika na programu hiyo. Hivyo, namshauri Mheshimiwa Mbunge ahimize halmashauri yake itenge eneo litakalohitajika ili iwe miongoni mwa halmashauri 100 zitakazonufaika na mpango huo.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Mingoi - Kiembeni Kata ya Mapinga iliyoharibiwa na Mvua za El-nino?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka 2023/2024, Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini ilijenga mfereji wa mita 500 kwa gharama ya shilingi milioni 62 kwa eneo lililoharibiwa na mvua. Katika bajeti ya mwaka 2024/2025, itajengwa mifereji mita 400 kwa gharama ya shilingi milioni 44.62 ili barabara hii iweze kupitika wakati wote wa mwaka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kutambua umuhimu wa barabara hii, serikali imeweka kwenye mpango wa Climate Response Window (CRW) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kujenga miudombinu ya kutolea maji katika Barabara ya Mingoi – Kiembei.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini itaendelea kuhudumia na kuboresha miundombinu ya barabara za Wilaya ya Bagamoyo kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, lini Serikali itaweka taa Uwanja wa Ndege wa Mafia ili kuwezesha ndege kubwa kupeleka watalii kutembelea Kisiwa cha Mafia?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka ujao wa fedha 2024/2025, Serikali ina mpango wa kufunga taa za kuongozea ndege katika Kiwanja cha Ndege cha Mafia kwa ajili ya kuwezesha kutolewa kwa huduma za masaa 24 ambapo kutachangamsha uchumi wa Mafia na kukuza utalii nchini.
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, Serikali imejipangaje kuanzisha mpango wa M-Mama katika maeneo ya Kibiti, Mafia na Mkuranga, ili kuzuia vifo vya akinamama wajawazito?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Pwani ulianza kutumia mfumo wa M-Mama tarehe 15 Septemba, 2023. Mkoa huu umeingia mkataba na madereva ngazi ya jamii 112 ikihusisha madereva 14 toka Halmashauri ya Kibiti na Mafia wanaotumia boti. Hadi sasa jumla ya dharura 2,816 kutoka katika Halmashauri zote za Mkoa wa pwani zimesafirishwa kwa kutumia mfumo wa M-Mama.
Mheshimiwa Spika, naomba kusema kuwa mfumo huu unafanya kazi katika maeneo yote nchini. Hivyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge wote kwanza kuhamasisha wananchi juu ya matumizi ya namba 115 wawapo na dharura itokanayo na uzazi wakati wa ujauzito. Naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU aliuliza:-
Je, lini Serikali itatenga fedha za Ujenzi wa Barabara ya Makofia - Mlandizi - Mzenga hadi Maneromango kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa Barabara ya Makofia – Mlandizi - Mzenga hadi Maneromango yenye urefu wa kilometa 100 umefanyika na kukamilika. Katika Mwaka wa Fedha 2023/2024, shilingi bilioni 2.5 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa Barabara ya Mlandizi – Ruvu SGR kilometa 23 ikihusisha kilometa 15 za Barabara ya Makofia – Mlandizi – Mzenga - Maneromango kipande cha kutoka Mlandizi hadi Ruvu Junction na Roundabout ya Makutano ya Mlandizi. Kwa sasa taratibu za manunuzi ya kumpata Mkandarasi wa ujenzi wa Mlandizi – Ruvu SGR kilometa 23 zinaendelea na zinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2024. Kwa sehemu iliyobaki Serikali inaendelea kutafuata fedha za kuendelea na ujenzi.