Supplementary Questions from Hon. Subira Khamis Mgalu (37 total)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona. Kwa kuwa, Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2016/2017 mpaka 2020/2021 na katika mpango huo upo pia mpango wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo; na kwa kuwa katika ujenzi huo uliwekwa jiwe la msingi na kwa kuwa katika Mji wa Bagamoyo limetengwa eneo la viwanda ambapo kunahitaji uwepo wa bandari:-
Je, mpaka sasa Serikali imefikia hatua gani ya kuanza ujenzi huo ukuzingatia unategemea utaratibu wa Public Private Partnership? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, tulieleza kwa kirefu dhamira na mpango ambao tayari Serikali imeshauweka wa kujenga Bandari ya Bagamoyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie kwamba mpango huo tunautekeleza kwa kupitia PPP. Kama ambavyo tulieleza katika bajeti, ni nchi tatu zinashirikiana katika hili kwa mpango wa PPP.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi tunavyosema, kikao cha karibuni kitakachofuata cha kufanya maamuzi ya kuingia katika hatua ya pili, kwa sababu kwa sasa kuna Joint Technical Committee imeundwa na inafanya kazi kila wakati kujaribu kupangilia, hatimaye utaratibu wa ujenzi wa hiyo bandari utakuwaje na hizo kazi zinapelekwa kwa hizi nchi tatu ambazo wanashiriki katika PPP hiyo; namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa itakapofika mwezi wa Kumi tutakuwa na jibu la uhakika la nini kitaanza na kitaanzia wapi.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, ninayo maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwa kuwa Wanaochaguliwa kwenda JKT kwa sifa za chuo kikuu na form six ni wachache kwa baadhi ya maeneo hasa Mkoa wa Pwani; je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kwamba nafasi hizi zichukuliwe na vijana wanaomaliza kidato cha nne ili kuweza kukabili ongezeko la vijana hao? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa vijana hawa wanaokwenda JKT baada kuhitimu, wengi wao wakirejea katika maeneo wanakosa ajira wakati wanakuwa na ujuzi, lakini wanashindwa kujiajiri kutokana na kutokuwa na mitaji ya kutosha; je, Wizara ipo tayari kufanya tathmini ili kuweza kuwawezesha hasa vijana ambao wameonesha vipaji katika makambi hayo? Ahsante.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nataka nieleze tu kwamba wale vijana wanaokwenda kwa mujibu wa sheria ni wengi kuliko uwezo wa Serikali wa kuwachukua kwa sasa, yaani wanaomaliza form six kabla ya kwenda kujiunga na vyuo idadi yao ni kubwa mno kiasi cha kwamba kwa uwezo wa sasa hatuwezi kuwachukua wote, ndiyo maana baadhi tu wanachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, siyo sahihi kwamba wanaokwenda ni wachache.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili; na hii niseme kabla sijaingia kwenye swali la pili, kwamba Serikali inaendelea kujipanga kuongeza kambi, kuongeza majengo ndani ya makambi ili hatimaye tuweze kuchukua vijana wote wanaomaliza form six kabla ya kwenda kujiunga na vyuo waweze kupita katika Jeshi la Kujenga Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, ni kweli kwamba kwa wale wanaokwenda kwa kujitolea ambao idadi yao ni kubwa, ni zaidi ya vijana 5,000 kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi, siyo wote wanaopata nafasi ya kuajiriwa ndani ya vyombo vya ulinzi na usalama. Kwa kiwango kikubwa kama tulivyosema wakati wa bajeti yangu, takriban asilimia 71 ya vijana hao, wanapata ajira kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, lakini asilimia iliyobaki wanalazimika kurudi nyumbani kwa sababu hakuna uwezo wa kuwaajiri wote.
Kwa hiyo, nakubalina na wazo la Mheshimiwa Mbunge kwamba ni lazima sasa tufanye utaratibu wa kuwawezesha vijana hawa ili wanaporudi waweze kujitegemea, kujiajiri wao wenyewe. Utaratibu huu umeshaanza kupangwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ili vijana hawa waweze kupatiwa mitaji na kwa kuwa wana ujuzi fulani wanaotokanao JKT waweze kujiajiri wao wenyewe.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Kwa kuwa Mkoa wa Pwani ni Mkoa ambao umeelekezwa kupima maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda; na kwa kuwa Wilaya ya Kisarawe imetenga eneo la viwanda ambalo inapita barabara ya Kiluvya - Mpuyani.
Je, Naibu Waziri pamoja na jibu lake kwa swali la msingi, yupo tayari kutembelea barabara hiyo mara baada ya Bunge hili; ili kuona eneo la mkakati la ujenzi wa viwanda ambalo limetoa zaidi ya viwanja 111 na wawekezaji mbalimbali wameonesha fursa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba baada ya kumaliza Bunge hili, nitatembelea hii barabara inayoanzia Kiluvya, ili kuangalia changamoto zake
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la kutopeleka fedha kwenye miradi ya maji ambalo kwa mujibu wa swali la msingi liko pia katika miradi mbalimbali inayotekelezwa Mkoa wa Pwani. Mfano mradi wa Ujenzi wa Bwawa Kata ya Chole, Wilaya ya Kisarawe, lilitengewa kiasi cha shilingi 1,500,000,000 lakini zilipelekwa 500,000,000 na bwawa lilipojengwa pamoja na mvua bwawa lile limeharibika.
Je, Naibu Waziri yupo tayari kufanya ziara Wilaya ya Kisarawe kwa kuwa ipo karibu na Dar es salaam ili kuona namna gani watakavyofanya na Wizara ili bwawa lile likamilike kwa wakati na wakazi wa Chole wapate maji kama ilivyokusudiwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimwambie kwamba niko tayari kuongozana naye baada ya Bunge kwenda kuangalia hilo bwawa. Lakini pili nimuhakikishie kwamba tayari tunayo tume ambayo kazi yake itashughulikia masuala ya kujenga mabwawa kwa ajili ya umwagiliaji. Tume hiyo sasa hivi iko tayari na tutahakikisha kwamba tunapeleka fedha na tatizo hili kwamba ilipelekwa fedha lakini nyingine haijaenda nafikiri tatizo kubwa ni huu utaratibu tuliouweka kwamba kama ujaleta hati sasa na sisi tutashindwa kuomba fedha kutoka Hazina. Tunachataka kwanza utuletee hati ili ile hata tuipeleke Hazina na Hazina wapate ushahidi kwamba kazi imefanyika waweze kutupa fedha ili tuweze kuzileta.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na naishukuru Serikali kwa ujenzi wa kilometa moja lakini pamoja na majiibu hayo ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kwa mujibu wa jibu la msingi kwamba kiwango cha kilometa 24 zilizobaki zinahitaji malipo ya fidia na kwa kuwa tarehe 7 Septemba, 2016 tulifanya kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa na taarifa ilitolewa kwamba takribani shilingi bilioni nane zitatakiwa kwa ajili ya fidia. Je, Serikali haioni kwa kuwa kiwango ni kikubwa kuongeza kama kilometa tano za ujenzi wa barabara hii kwenye eneo la viwanda kwenye maeneo hayo Kibaha?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa ujenzi wa barabara hii ni ahadi ya Serikali ya Awamu ya Nne na kwa kuwa zipo ahadi mbalimbali za ujenzi wa miundombinu ambazo hazikukamilika kwa Awamu ya Nne, je, Wizara haioni imefika wakati sasa iunde timu ya tathmini ya ahadi zote ambazo hazikutekelezwa ili ziweze kutekelezwa awamu hii na hususani kuanzia mwaka ujao wa fedha na kuendelea? Ahsante.
NAIBU WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Subira Mgalu kwa kufuatilia mambo mbalimbali ya Mkoa mzima wa Pwani, hongera sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo hilo la viwanda la kilometa tano analoliongelea mimi namhakikishia ujenzi utaanza kama nilivyosema katika jibu langu la msingi mara tutakapopata zile fedha za fidia na kuwaondoa wale watu ambao wanatakiwa wafidiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la tathmini ya ahadi ambazo hazijatekelezwa na viongozi wakuu, kwanza naomba nimhakikishie ahadi zote za viongozi wetu wakuu wa Serikali ya Awamu ya Nne na Serikali ya Awamu ya Tano orodha tunayo. Namhakikishia Serikali hii ya Awamu ya Tano kazi yake kubwa ni kuhakikisha kwamba ahadi zote za viongozi wakuu wa kuanzia Serikali za nyuma zinatekelezwa kikamilifu. Nitamshirikisha kumuonesha orodha kamili ya ahadi ambao zilitolewa na Awamu ya Tatu, Nne na Tano katika Mkoa wa Pwani
ili aelewe ninachokisema kwamba tuna dhamira ya dhati kuhakikisha ahadi za viongozi wetu zinatekelezwa.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.
Kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jibu zuri lenye kuleta matumaini kidogo kwamba mwaka huu wa fedha wamependekeza kutenga kiasi cha shilingi bilioni tatu. Kwa kuwa kiwango hiki ni kidogo na kwa kuwa barabara hii imeahidiwa tangu Ilani ya 2005.
Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kutafuta chanzo kingine, mfano mikopo yenye masharti nafuu kutoka Benki ya Dunia, Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuweza kuikamilisha kwa kuwa eneo hili linataka kuwa la viwanda?
Swali la pili, kwa kuwa wakazi wa maeneo hayo yanayopita barabara hii ya Kisarawe - Mpuyani -
Manerumango, maeneo ya Kazimzumbwi, Masaki, Kibuta pamoja na Marumbo na Manerumango yenyewe, wakazi hawa walizuiwa maeneo yao wasiyaendeleze wala kukarabati nyumba zao lakini mpaka sasa wakazi hawa
hawajui fidia gani watakayolipwa. Kwa kuwa katika jibu la msingi amesema upembuzi yakinifu umekamilika.
Je, ni lini wakazi wa maeneo haya watalipwa fidia
yao wale wanaostahili? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA
MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, nimepokea ushauri wake wa kutafuta vyanzo vingine ili kuhakikisha barabara hii tunaikamilisha, tutakwenda kuufanyia kazi ushauri wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia kwa wananchi wa Kazimzumbwi, Mabuta na maeneo mengine, hadi Maneromango, kwanza ningeomba hii dhana ya fidia ieleweke wazi na Waheshimiwa Wabunge wote na mtusaidie kwa wananchi. Tukiwa na kauli moja wananchi hawatahangaika, kwa sababu kauli yetu kupitia sheria tuliyoipitisha ndiyo ilikuwa kwa umoja wetu, sasa ni vizuri
tunapolishughulikia hili suala la fidia katika maeneo ambayo barabara zinapita au miradi mingine ya miundombinu inapita, tuwe na kauli inayofanana na sheria tulizopitisha ili tusiwachanganye wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuwekewa alama ya ‘X’
iwe ya kijani au iwe nyekundu maana yake ni kwamba nyumba hiyo au jengo hilo au shamba hilo au miti hiyo iko ndani ya hifadhi ya barabara. Waliowekewa kijani maana yake ni kwamba watakuja kufidiwa, lakini haina maana kwamba wanafidiwa wakati huo huo au waendeleze nyumba zao, maana yake ukiendeleza unaongeza gharama tena za kufidia, unaipa gharama zaidi Serikali na lengo la Serikali ni kupeleka miundombinu katika maeneo hayo, prime objective siyo kufidia, prime objective ni kujenga
miundombinu, lakini ni lazima tuwafidie wale ambao wana haki ya kufidiwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe wananchi wote ambao wamewekewa ‘X’ wajue kwamba wako ndani ya eneo la mradi, watafute maeneo mengine, tena ni vizuri wakatafuta taratibu kwa muda wa kutosha badala ya kuja kuhangaika dakika za mwisho, mara nyingi kwa mfano wale ambao wana ‘X’ nyekundu watakuja kubomolewa bila fidia na wale wa kijani kwa vyovyote kabla barabara haijajengwa au kupanuliwa tutawafidia mara tunapopata fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba sana Mheshimiwa Subira Mgalu, kupitia kwako natambua mchango mkubwa unaotolewa na pacha wako, Mheshimiwa Selemani Jafo katika suala hili…
Ninawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya kwa pamoja…
Kwa ushirikiano huo tutahakikisha barabara hii inajengwa.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza na namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa suala la upembuzi yakinifu limekuwa likijibiwa hata Bunge la Kumi kwenye swali hili la msingi na kwa kuwa hata majibu ya msingi ya swali hili yameonesha hakuna hata kiwango cha fedha kilichotajwa waziwazi kutengwa kwa mwaka wa fedha 2017/2018, hali inayopelekea wasiwasi wa utekelezaji wa kazi hii. Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kuambatana na Mbunge Mheshimiwa Azza kutembelea eneo hili la Masengwa ili asikie kilio cha wananchi hawa na ikizingatiwa Mkoa huu wa Shinyanga umekuwa ukiendelea kunyemelewa na janga la ukame?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa matatizo ya maji ya Halmashauri ya Shinyanga yanafanana kabisa na matatizo ya maji ya Halmashauri ya Chalinze yanayotokana na kusuasua kwa mradi wa Chalinze Wami Awamu ya Tatu na kwa kuwa mradi huu pia ulitembelewa na Mheshimiwa Waziri Mkuu miezi miwili iliyopita na kutoa maelekezo kwa mkandarasi kukamilisha kazi hii kwa siku 100. Je, mpaka sasa Wizara imefikia hatua gani katika ufuatiliaji wa maelekezo ya Waziri Mkuu ili tatizo la maji linaloikumba Halmashauri ya Chalinze hususani Mji wa Chalinze, Ubena na maeneo mengine lipate majibu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimhakikishie Mheshimiwa Subira kwamba utaratibu wa utekelezaji wa miradi huwa unaanza na hatua ya awali ambao kwa lugha ya kigeni tunaita basic concept baada ya hapo tunakwenda kwenye feasibility study. Kumekuwa na lugha ya kiujumla ambayo inafahamika kwa wengi (usanifu wa awali). Kwa hiyo, hiyo iliyokuwa inatajwa mwanzoni ilikuwa ni kwa ajili ya basic concept sasa ni kweli tunaenda kwenye feasibility study ambao ni usanifu wa awali.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia amesema hajaona fedha iliyotengwa Mheshimiwa Mbunge leo ndiyo tunaanza kusoma bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa mwaka 2017/2018. Asingeweza kuiona kabla ya hapo lakini kwa leo baada ya kuanza kusoma bajeti nina uhakika ataona tunaelekea wapi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa ameomba pia tuambatane na Mheshimiwa Azza, ni kazi ya mimi Naibu Waziri kuhakikisha kwamba natembelea Majimbo na Halmashauri zote kujionea utekelezaji wa miradi ya maji safi na salama pamoja na miradi ya umwagiliaji. Kwa hiyo, asiwe na wasiwasi hata huko Shinyanga nitafika.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Mheshimiwa amezungumzia utekelezaji wa mradi wa Chalinze, kwanza nimwambie kwamba sasa hivi mkandarasi ana kasi kubwa ya utekelezaji wa mradi wa Chalinze. Mheshimiwa Waziri pamoja na mimi tunapata taarifa kila siku na taarifa ya jana ni kwamba mkandarasi amefikisha asilimia 44.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia ni kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu alitembelea pale na wakati ule tulitamka siku 100 za kumpima mkandarasi, tunakupa siku 100 ili tuone kama utaongeza speed basi tutaendelea na wewe. Sasa anaendelea kuthibitisha kabla ya hizo siku 100 kwamba ameongeza kasi. Kama ataendelea hivyo, tutaendelea naye kuhakikisha kwamba mradi ule unakamilika.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kulifanywa swali langu na mimi kuwa swali la Kibunge.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri naomba kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa kwa mujibu wa jibu lake la nmsingi ameeleza kwamba kwa mwaka huu 2016/2017 zimetengwa shilingi 3,000,000,000 kwa ajili ya ukarabati wa kipande hiki cha barabara ya Mlandizi – Chalinze kwa kuwa tupo mwezi huu wa sita umebaki wa mmoja tu, je mpaka sasa ni kiasi gani wamekipeleka kwenye mamlaka yetu ya barabara TANROADS Pwani?
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria za Fedha inapofika mwisho wa mwaka wa fedha 30 Juni, 2017 pesa zote zilizosalia zinarudishwa kwenye Mfuko Mkuu wa Hazina. Na kwa kuwa barabara hii haijakarabatiwa mpaka sasa, je, Mheshimiwa Waziri anatuthibitishiaje kwamba barabara hii itakarabatiwa kwa kuwa mwaka wa fedha umekaribia kukamilika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumhakikishia Mheshimiwa Subira Mgalu kwamba fedha hizi zilizotengwa ni za ukarabati, fedha zinazorudishwa ni zile za maendeleo, fedha za ukarabati huwa hazirudishwi. Kwa hiyo, nikuhakikishie fedha hizi zilizotengwa zipo na zitafanya hiyo kazi iliyokusudiwa mara taratibu za kusaini mikataba itakapokamilika. Nikuhakikishie Mheshimiwa Subira Mgalu huo ndio ukweli wenyewe, fedha hizi hazitarudishwa.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kwa mujibu wa jibu lake la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri, ameonesha kuna bakaa ya fedha ambazo zimebaki hazijawasilishwa kwenye Halmshauri ya Wilaya ya Msalala, kiasi kwamba itapelekea miradi kutokamilika kwa wakati. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, anaweza kulihakikishia Bunge hili kabla ya mwaka wa fedha mpya haujaanza miradi ile itakamilika na Serikali itapeleka fedha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa swali la msingi limeelekeza changamoto ya upelekaji wa fedha za maendeleo ambalo ni changamoto inayoikabili karibu nchi nzima kwa mwaka huu wa fedha, hususani, Halmashauri zetu za Mkoa wa Pwani. Je, Naibu Waziri yupo tayari kutoa maelekezo kwa Wakurugenzi kwa miradi ambayo ni viporo hasa ya Sekta ya Afya, wawasilishe taarifa haraka ili Serikali iweze kuikalimisha katika Halmashauri mbalimbali za Mkoa wa Pwani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli, bajeti pale mpaka mwezi Desemba, nimesema zilikuwa hazijafikia shilingi bilioni 3.1 zilizokuwa zimepelekwa, lakini mpaka mwezi Mei, hivi sasa fedha ambazo zimepelekwa katika ile bajeti imefika bilioni mbili (2), lakini fedha zingine za nje zimeongezeka na zimefikia karibu bilioni 1.9 mwezi uliopita. Kwa hiyo, jukumu kubwa ni nini? Tunaona kwamba kuanzia mwezi Desemba, mpaka hivi sasa kuna fedha nyingine za Serikali zimezidi kupelekwa na hapa maana yake Serikali itajitahidi kwa kadiri iwezekanavyo ili miradi iliyokusudiwa iweze kukamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, isipokuwa katika hili, ni lazima wataalam wetu, wakati mwingine ule uwezo wa utumiaji wa fedha za miradi kwa watendaji wetu umekuwa ni udhaifu zaidi. Kwa mfano, hapa tunapozungumza fedha nyingi zimeshapelekwa kule Msalala, basi nawaomba watendaji wetu waweze kuhakikisha kwamba, fedha zilizofika za maendeleo zitumike ilimradi wananchi waweze kupata huduma.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ni jinsi gani tutafanya kwa Mkoa wa Pwani. Kikubwa zaidi naomba niwaagize kama nilivyosema, ni kwamba Wakurugenzi wote wa Mkoa wa Pwani na mikoa mingine yote katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wahakikishe kwambam kwanza wanaandaa zile changamoto zilizokuwepo katika Sekta ya Afya na miradi mingine, lakini tubainishe kwamba hata hizo fedha zilizofika ziweze kutumika kwa ajili ya maslahi ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili, naomba nitoe onyo kwa Wakurugenzi mbalimbali, kipindi cha mwaka unapofika siku hizi za mwisho, watu wamekuwa wakifanya mambo ya ajabu sana katika matumizi ya fedha za Serikali, wakijua kwamba mwaka unakwisha. Wakati mwingine fedha zinapelekwa sehemu ambazo hata zisizohusika, ambazo haziendi kuwagusa wananchi. Kwa mwaka huu naomba nikiri wazi kwamba, Mkurugenzi yeyote ambaye atacheza na fedha za Serikali, naamini Waziri wangu ataamua kuchukua fimbo kubwa sana kuhakikisha kwamba watu hawa wanawajibishwa. Lengo kubwa kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma kutokana na kazi kubwa inayofanywa na Serikali yao ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. STANSLAUS S. MABULA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa matatizo ya bei za dawa yanaonekana yako maeneo ya mengi na kwa sababu tayari Serikali kupitia Wizara ya Afya imeanzisha maduka ya madawa MSD kwenye Hospitali zetu za Mkoa. Je, Serikali ina mpango gani sasa kupeleka maduka haya kwenye hospitali za Wilaya, kwa sababu ndiko kwenye watu wengi zaidi, lakini pia inaonekana ndiyo maduka yanayosaidia zaidi kwa dawa za gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, majibu ya swali la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba, sisi kama Wizara ya Afya na Taasisi yetu ya Bohari ya Taifa ya Dawa, hatuna jukumu la kuuza dawa moja kwa moja kwa wateja kwa mujibu wa sheria iliyopo na kwa maana hiyo tumefuata maelekezo ya Kiongozi Mkuu wa nchi yetu kufungua maduka ya mfano katika Hospitali ya Taifa na Hospitali za Kanda na tutaishia hapo, naomba hili kwanza lieleweke.
Mheshimiwa Naibu Spika, tuna mkakati wa kuyawezesha maduka ya Mikoa na Wilaya, ambayo yatatamani kuwa na maduka yanayofanana na yale ya MSD Community Outlets, kwenye maeneo yao, lakini yale maduka watayamiliki wao, watayaendesha wao. Sisi tutawasaidia ufundi (technical expertise), tutawasaidia namna ya kuyajenga, kuyakarabati kwamba yanatakiwa yakae vipi, tutawasaidia mifumo ya computer kwa ajili ya kuendeshea biashara hiyo ya kuuza dawa; na tutawasaidia expertise kwamba wafanyeje customer care yao ili yafanane kutoa huduma katika mfumo ule ambao tunatoa kwenye maduka ya MSD Community Outlets. Hata hivyo, chanzo hiki cha mapato kizuri na cha uhakika kwenye hospitali za Wilaya, hatuwezi kukiondoa kwenye hospitali za Wilaya tukakileta Serikali Kuu.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri yenye kuleta matumaini ya ujenzi wa Vituo vya Polisi na Magereza, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Gereza hili la Kigongoni lina changamoto kubwa ya tatizo la mgogoro wa mpaka wa ardhi kati yake na wananchi wa Sanzare na Matibwa, mgogoro huu umepelekea uvunjifu wa amani mara kadhaa. Je, ni lini Serikali itashirikiana na uongozi wa Wilaya ya Bagamoyo katika utatuzi wa mgogoro huu?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Mkoa wa Pwani ukiachia Wilaya ya Mafia una tatizo kubwa la kutokuwepo kwa Vituo vya Polisi na kwa kuwa kuna hali tete ya usalama katika maeneo hayo ya Wilaya za Mkoa wa Pwani ukiacha Mkuranga, Kibiti na Rufiji. Pia kwa kuwa Wilaya ya Mkuranga imeanza ujenzi wa Kituo cha Polisi kwa ushirikiano wa Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo na wananchi wa Wilaya ile ya Mkuranga. Je, ni lini Serikali itakubali kuisaidia Wilaya hii ya Mkuranga kukamilisha kituo hicho cha Polisi ili kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Mbunge na wananchi wake? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri. Nikianza na la kwanza la mgogoro uliopo kati ya Gereza pamoja na wananchi wa kule Bagamoyo, nikiri ni kweli mgogoro huo upo na Mheshimiwa Mbunge Dkt. Shukuru Kawambwa amekuja mara kadhaa Ofisini na mara nyingine aliongozana na baadhi ya viongozi.
Mheshimiwa Spika, kitu tulichomuahidi ni kwamba baada ya Bunge, ama tukipata fursa baada ya kupigia kura bajeti, tutatembelea eneo husika tukiwa na Timu ya Mkoa ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ili tuweze kujionea wapi na nini chanzo cha mgogoro huo na njia nzuri ya kulimaliza tatizo hilo ili wananchi wake wasipate shida na uwepo wa Gereza hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kuhusu kuunga mkono jitihada za Mbunge wa Mkuranga, ni kweli na Mbunge anafanya kazi nzuri sana na sisi kama Serikali ukanda ule tumeupa Mkoa Maalum wa Kipolisi, kwa hiyo Wilaya zote ambazo zinakaa ukanda ule ikiwemo Mkuranga tutazipa umuhimu na upendeleo unaostahili ili tuweze kupata makazi ya Askari, Ofisi za Polisi pamoja na Ofisi za Kanda na kwa pamoja na wingi wa Askari ili kuweza kusaidia shughuli za usalama katika eneo hilo ili wananchi waweze kufanya kazi bila kuwa na hofu yoyote. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali kwa majibu mazuri yenye kutia matumaini ya wakazi wa Jimbo la Kibiti. Hususani walio jirani na barabara ya Bungu Nyamisati kwa kuwa Serikali imetenga fedha, ya kuanza upembuzi yakinifu na hizi milioni 700 kwa ajili ya matengenezo ili ipitike muda wote.
Mheshimiwa Spika naomba sasa niulize swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa katika hilo Jimbo la Kibiti kuna barabara muhimu ya Kibiti Dimani Mloka ambapo pia, magari yanayoelekea kwenye mradi muhimu wa kimkakati wa ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere wanaitumia.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanza upembuzi yakinifu kwa kuwa barabara hii pia ipo kwenye ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025, kwa ajili ya ujenzi wa kiwango cha lami? Ili kuwezesha ipitike muda wote kuelekea kwenye Mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Subira Mgalu Mbunge wa Viti Maalum Pwani kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara aliyotaja ni kati ya barabara ambazo zinafika kwenye mradi wetu wa kimkakati na imeainishwa kwenye ilani ya Chama cha Mapinduzi kama alivyosema ambayo ni ya 2020 – 2025. Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara zote ambazo zimeainishwa katika ilani haziwezi zote zikatekelezwa kwa mwaka mmoja. Lakini nimuhakikishie kwamba zipo kwenye mpango na zitafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina, kama ilivyoainishwa kwenye ilani katika kipindi hiki cha miaka mitano. Ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza naishukuru sana Serikali kwa kazi nzuri iliyofanya kupitia fedha hizi za UVIKO na naishukuru sana Wizara ya Afya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa kwenye jibu la msingi ameeleza vifaa hivi vimefika zaidi ya asilimia 94 katika Hospitali ya Tumbi; je, Mheshimiwa Waziri anatuahidi ndani ya mwezi Oktoba kwamba CT Scan itafanya kazi, yupo tayari kuwaelekeza wataalam wake kuhakikisha kweli mwezi Oktoba vifaa hivi vitafanya kazi kwa kuwa ni jambo la kihistoria na halijawahi kutokea kuwa na CT Scan ngazi ya hospitali za rufaa za mkoa?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa kazi kubwa imefanywa ya ujenzi ya miundombinu ya afya ikiwemo vituo vya afya Mkwakwani tuna vituo vya afya 10 kutokana na tozo na hospitali za wilaya na zahanati.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kupunguza ujenzi wa miundombinu mipya ili ijielekeze kuhakikisha miundombinu hii ambayo imejengwa kwa kasi inapata vifaa tiba kwa kuwa pia inakuja na mpango wa bima ya afya ili mpango huu ukianza kutekelezeka hospitali zote na vituo vya afya viweze kuwa na vifaa tiba? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Subira Mgalu kwa maswali yake mazuri na hususan kusema kwamba suala la ununuzi wa vifaa tiba ni jambo la kihistoria ambalo limefanywa na Rais Samia Suluhu Hassan haijapata kutokea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa CT Scan kama nilivyosema itafungwa by October, 2022 lakini kabla ya kuanza kufanya kazi lazima pia tufanye testing (tufanye majaribio) na watu wa Tume ya Atomic Energy lazima pia watoe kibali cha kuanza kutumika. Kwa hiyo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Subira Mgalu kwamba suala hili kwetu ni la kipaumbele.
Mheshimiwa Spika, suala la pili kuhusu je, kwa nini sasa Serikali isijielekeze katika kuimarisha huduma za afya? Nakubaliana nawe Mheshimiwa Subira na mimi nilishatoa maelekezo kwa wenzangu Wizara ya Afya, lakini kwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Tumejenga zahanati nyingi, tumejenga vituo vya afya vingi, tumejenga hospitali za wilaya nyingi. Sasa hivi tujikite kuhakikisha kwamba huduma zinatolewa zenye ubora katika hospitali tulizojenga.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kipaumbele cha Wizara ya Afya au kwa sekta ya afya sasa hivi ni mambo mawili; ubora wa huduma, kuhakikisha huduma zinapatikana, dawa zinapatikana, tunao watumishi wa kutosha lakini pamoja na lugha ambazo wataalam wetu wa afya wanawahudumia wananchi. Kwa hiyo, hiki ndiyo kipaumbele cha sekta ya afya katika kipindi hiki.
Mheshimiwa Spika, sisemi kwamba hatutajenga zahanati na vituo vya afya kwa sababu Waheshimiwa Wabunge wengi mnataka, lakini tutajikita katika maeneo ya kipaumbele ambayo tunadhani labda kuna umbali mrefu, kuna idadi kubwa ya wananchi, lakini pia mzigo wa magonjwa bado ni mkubwa katika eneo hilo husika. Nakushukuru sana.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naishukuru sana Serikali kwa majibu mazuri na naipongeza TRA na wadau mbalimbali kwa ubunifu huo wa mashine ambayo inarahisisha, sasa maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa bado yapo matukio ambayo baadhi ya wafanya biashara ya kutotoa risiti hasa katika maeneo yenye biashara mfano Kariakoo. Je, Serikali kupitia TRA kwa kuwa imepewa kibali kwa mara ya kwanza kaujiri watumishi wengi kwa wakati mmoja, inawatumiaje watumishi wale katika mapambano dhidi ya vitendo hivi vya kutotoa risiti? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, kwa kuwa katika jibu lake la msingi ameeleza kwamba, wafanyabiashara wanaruhusiwa kusheria kurejesha gharama za mashine za EFD wanazozinunua wakati wanakokotoa mapato ya kutoza kodi. Je, Serikali inajipangaje kutoa elimu hii kwa wafanyabiashara wengi ili kuondoa dhana ya kwamba mashine za EFD ni gharama zaidi? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote kabla ya kujibu maswali haya, kwa idhini yako, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyofuatilia na pia ni Balozi wa TRA.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza, Serikali iliwapatia mafunzo yale ambayo ni muhimu kabisa, awali kabla ya kuanza kufanya kazi, lakini kama hilo halitoshi, Serikali imeandaa Mkakati wa kutoa mafunzo ya watumishi hawa, mafunzo maalum kwa watumishi hawa wapya kila baada ya miezi minne.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili, Serikali kupitia TRA ina program ya kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, tv pamoja na redio. Nichukue fursa hii kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, kuwaelekeza TRA kuendelea kutoa mafunzo hayo kimkakati. Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, asante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Je, ni lini Serikali itakamilisha taratibu za manunuzi ya mashine ya CT-Scan ambapo na tunategemea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Pwani Tumbi itapata mojawapo?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, ni kweli anachosema Mheshimiwa Mbunge na tayari CT-Scan yao iko kwenye manunuzi kabla ya mwezi Juni itakuwa imefika ST-Scan ya hospitali ambayo Mheshimiwa Mbunge anaisema.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nashukuru pamoja na majibu ya Serikali ambayo pamoja na kwamba hayatoi matumaini ya karibuni, lakini napenda nitumie fursa hii kuishukuru sana Serikali kwamba barabara hii iko chini ya TANROADS kwa matengenezo ambayo yanaendelea inawezesha walau kupitika na barabara hii ni shortcut kwa ajili ya kutoka Magila – Turiani – Mziha - Handeni - Mziha, Kibindu -Mbwewe kwenda Mikoa ya Kaskazini.
Mheshimiwa Spika, sasa naomba niulize maswali yangu kama yafuatavyo; je, Serikali ipo tayari kuielekeza TANROADS katika matengenezo yanayoendelea kutenga pesa kwa ajili ya matengenezo ya mifereji, kwa sababu eneo hili lina mvua nyingi ili barabara hii iendelee kupitika na kwa kuwa kuna vyakula vingi katika eneo hilo ili uweze kufika sokoni?
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa Serikali imepanga mpango mzuri wa kuendelea na upanuzi wa ujenzi wa njia sita kutoka Kibaha mpaka Chalinze na ilishafanya tathmini; je, Serikali inasemaje ina mpango gani juu ya fidia kwa maeneo ambayo barabara hiyo itapita? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli barabara hii kwanza ina umuhimu mkubwa sana kwa mikoa hii yote miwili ya Morogoro pamoja na Pwani, na katika mwaka huu wa fedha ili iweze kupitika tumetenga fedha takribani kiasi cha shilingi milioni 346.981 na wakandarasi wawili wapo site.
Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba suala la ujenzi wa mifereji pia tutajenga kwa kuwa tayari wakandarasi wako site ni sehemu ya scope ya kazi tuliyompatia mkandarasi.
Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa ajili ya barabara kutoka Kibaha – Chalinze kuja Morogoro kwa ajili ya fidia, tayari barabara hii wizara imekusudia tutafanya kwa mfumo wa EPC+Finance, lakini sasa tumebadilisha kwa tutafanya kwa njia ya Public Private Partnership (PPP). Tayari mtaalam mwelekezi Kampuni kutoka Korea ya Kusini yupo site na tunategemea tutakabidhi kazi hii kati ya mwezi wa tatu ama wa nne na kupitia ripoti atakayoleta kwa ajili ya fidia na gharama zote, Serikali itatumia hiyo ripoti kwa ajili ya kulipa wale wote watakaokuwa wameathirika na barabara hii, ahsante.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imeleta milioni 500 kumalizia ujenzi wa Hospitali za Halmashauri ya Kibiti, Kibaha Mjini, Kibaha Vijjini na bilioni moja Halmashauri ya Chalinze. Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wananchi wa maeneo hayo juu ya kuleta vifaa tiba kwa wakati ili iendane na jitihada hizi za uwekezaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Subira Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali kwa kutambua umuhimu wa huduma za afya kwa wananchi wa Kibiti na wananchi wa Chalinze imepelekwa jumla ya shilingi bilioni moja na milioni mia tano kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na hospitali. Hata hivyo, nimhakikishie mara baada ya kukamilika kwa vituo hivi Serikali itapeleka vifaa tiba kwa sababu katika bajeti ya mwaka ujao shilingi bilioni 69.95 imetengwa kwa ajili hiyo.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa majibu mazuri ambayo imeonesha kwa mara ya kwanza Serikali yetu imetenga pesa kwa ajili ya kuwezesha majukwaa haya.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Mkoa wa Pwani unaongoza nchi nzima wa kusajili majukwaa 1,723 na kuyasajili 945 ambayo yamepelekea kuanzisha kampuni ya Go Mama Public Company Limited. Je, Serikali ipo tayari kutumia Milioni 200 zinazotengwa mwaka huu wa Fedha kwa ajili ya kuwezesha Mkoa wa Pwani kwa kuwa umeonesha dira umeanzisha kampuni ambayo inayo matarajio ya kujenga kiwanda cha vifungashio?
Swali la pili, kwa kuwa Serikali ina Mifuko mingi ya Uwezeshaji zaidi ya 72 ambayo ipo katika Wizara tofauti tofauti. Je, Serikali haioni ipo haja ya Mifuko hii kuwa chini ya chombo kimoja ili iwe fursa kwa majukwaa haya ya uwezeshaji badala ya majukwaa haya kutegemea asilimia 10 ya mikopo ya mapato ya ndani ya Halmashauri. Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, nashukuru na naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu, Mbunge kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Subira kwa kazi kubwa anayoifanya katika Mkoa wa Pwani kama ambavyo wamesema wameanzisha hiyo kampuni ya Go Mama ambayo wanasema ina nia ya kuanzisha kiwanda cha vifungashio ambayo italeta pato kubwa sana katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema Serikali imeendelea na itaendelea kusaidia na kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia fursa mbalimbali ikiwemo Mifuko hii ya kuwezesha wananchi kiuchumi. Kwa hiyo, kwa kazi hiyo wanayoifanya naamini tutaangalia katika bajeti hii ili tuone namna gani mahsusi kusaidia kampuni hii ambayo inaenda kusaidia kujenga viwanda katika nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili tayari Serikali tumeshaanza utaratibu wa kuunganisha Mifuko hii ambayo mingi ipo ndani ya Serikali katika Wizara mbalimbali, pia mingine kutoka sekta binafsi, kwa hiyo tunaifanyia kazi, naamini katika mwaka wa fedha ujao tutafanya hivyo ili kuhakikisha Mifuko hii inakuwa na tija kwa ajili ya kuwasaidia wanawake kiuchumi. Nashukuru. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza niishukuru Serikali kupitia Mheshimiwa Waziri hapo, nimefuatilia leo na kupata uhakika kwamba mafundi sanifu wako site kwa ajili ya mradi huu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Tarafa hii ya Mzenga, na hususan Kata hii ya Mzenga, zikiwemo Kata za Vihingo, Kurui na Mafizi, zina shida kubwa ya maji, licha ya kwamba Serikali mmetoa commitment.
Je, ni namna gani Serikali inaweza kutusaidia kwa dharura ikizingatia tumeshapata lile gari la kuchimba visima? Na tunaishukuru sana Serikali.
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imefanya miradi mingi ya maji Mkoa wetu wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Je, Serikali haioni ipo haja sasa ya kuweza kupunguza gharama za kuunganisha maji, hasa vijijini, ili wanawake watumie maji majumbani ili iweze kuleta tija ya miradi mikubwa iliyofanyika? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna anavyowapigania wananchi katika Mkoa wa Pwani. Kubwa ambalo nataka nisisitize ni kwamba Mheshimiwa Rais ametupatia fedha juu ya ununuzi wa mitambo na mitambo tumekwisha inunua, niwaelekeze watu wa DDCA wafike katika haya maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyaomba ili tuweze kufanya tafiti za haraka na kuhakikisha visima hivi vinachimbwa wananchi hawa waweze kupata huduma ya maji.
Mheshimiwa Spika, swali la pili, amezungumza juu ya gharama za maunganisho, hasa kwa wananchi kupata maji majumbani. Tumekwishatoa maelekezo katika Wizara ya Maji na watendaji wanalifanyia kazi. Tunataka tuwe na bei elekezi, hasa juu ya maunganisho ya maji majumbani. Kwa hiyo tunalifanyia kazi na tumelipokea kuhakikisha kwamba gharama zake zinakuwa reasonable na wananchi waweze kupata huduma ya maji safi na salama.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Pamoja na majibu yenye kuleta matumaini ya Serikali nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa, Serikali imesema imetenga fedha milioni 350; na kwa kuwa, Gereza la Dimani ni miongoni mwa magereza ambayo yatafanyiwa ukarabati. Je, Serikali inasema nini juu ya nyumba chakavu zilizopo kwenye Gereza hili la Dimani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa, changamoto ya uchakavu wa miundombinu inafanana na Gereza la Kigongoni, Bagamoyo na binafsi niliwahi kulitembelea na nikaona jitihada zao wenyewe askari magereza kwa kujenga nyumba na nikawachangia mifuko 50 ya simenti, lakini bado nyumba nyingine ni chakavu. Je, Serikali ina mpango gani wa muda mrefu wa kuwajengea nyumba askari magereza kwenye magereza mbalimbali kama inavyofanya kwenye majeshi mengine likiwemo Jeshi la JKT na Jeshi la Wananchi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uchakavu wa nyumba kama pia zitahusika katika ukarabati huu, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, fedha za ukarabati zinapelekwa kwenye gereza. Mkuu wa gereza pamoja na menejimenti yake wataangalia wapi pana tatizo kubwa zaidi na wanalipa kipaumbele katika ukarabati. Hatuta-prescribe, hatutaagiza kwamba, karabati gereza acha nyumba kwa hiyo, kama nyumba zina hali mbaya zaidi wataanza kukarabati nyumba, kama gereza lina hli mbaya zaidi wataanza na gereza. Kwa hiyo, uhuru tunawaachia wao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukarabati wa Gereza la Bagamoyo ambalo pia, Mheshimiwa Mbunge amesema limechakaa sana. Nimhakikishie tu mpango wetu wa ukarabati na ujenzi wa magereza unaenda sambamba kama tulivyokwishasema. Tumeanza mwaka jana, mwaka huu tunaendelea na mwaka ujao pia tutaendelea. Kwa hiyo, gereza la Bagamoyo kulingana na hali ya upatikanaji wa fedha litakuwa moja ya magereza yatakayoingizwa kwenye mpango wa ukarabati. Ahsante sana.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza mawali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza niishukuru sana Serikali yetu ya Awamu ya Sita kwa kuonesha dhamira ya kushughulikia mgogoro huu ambao ulikuwa wa muda mrefu. Sasa kwa kuwa hatua ya kwanza ya kuanza kulipa malipo haya kwa Kitongoji cha Funta zaidi ya milioni 330 imeleta kama sintofahamu kwa wananchi wa Vitongoji vya Chokozeni na Kudikongo katika Kijiji cha Kihangaiko hicho hicho. Je, Serikali haioni ipo haja kwa vitongoji hivi viwili vya Kijiji kimoja cha Kihangaiko walipwe fidia yao kwa mwaka huu wa fedha unaoendelea?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa wapo baadhi ya wananchi waliotoa maeneo wa Vijiji vya Msata, Kihangaiko na Pongwe Msungura hawakupimiwa na kwa kuwa imeanza kulipa fidia. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wale wananchi ambao bado hawajapimiwa ili waweze kupata matumaini na waweze kuyaachia yale maeneo kuliko wanavyokwenda kufanya shughuli na wanakumbwa na matatizo makubwa? Ahsante sana.
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa swali la kwanza ambalo ni kwamba kuna hawa ambao hawajalipwa, napenda tu kutoa rai kwa wenzetu ambao ni Halmashauri ya Chalinze kukamilisha taratibu na kuwasilisha jedwali ili taratibu ziendelee na ziweze kukamilika. Kama alivyosema ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kwamba migogoro hii inakamilishwa na kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wataona tulikuwa na migogoro 87 katika mpango wetu wa mwaka 2020 - 2023 na kati ya migogoro hiyo 87 migogoro 74 imekwishatatuliwa. Kwa hiyo hii 13 iliyosalia ni dhamira yetu kuhakikisha kwamba tunaikamilisha mwaka huu wa fedha kwani hata mpango tuliokuwa tumejiwekea kukamilisha mwaka 2023 umeshapita, tumeongeza mwaka mmoja.
Mheshimiwa Spika, kwa hao wengine ambao wamejitokeza, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutaangalia kama hii migogoro mipya iko sehemu ya mpango wetu na kama haiko sehemu ya mpango wetu tutaona tunaiingiza namna gani. Jambo la kwanza ni muhimu tuende tukajiridhishe kwamba haya maeneo anayoyataja ni maeneo ambayo yapo katika maeneo ya vikosi vya Jeshi. Tutafanya hivyo Mheshimiwa Mbunge kwa kushirikiana na wewe.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa hizi shilingi milioni 470 kuna baadhi ya maeneo sekondari hizi hazikukamilika bado maabara nyingine hazikukamilika, je, Serikali ina mpango gani wa kufanya tathmini ya kina na kuweza kuongeza ili miundombinu ya shule hizi mpya ikamilike? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Subira Mgalu. Hizi shilingi milioni 470 ambazo zilikwenda kwenye ujenzi wa shule za Kata kwenye kata ambazo hazikuwa na shule zilienda na maelekezo maalum na zilitakiwa kutosha. Kuna Halmashauri kwa mfano pale Kongwa Mkoani Dodoma na Bahi Mkoani Dodoma walimaliza kwa shilingi milioni 470. Ni wao kule chini ambao hawakutekeleza maelekezo yaliyopelekwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI na wakategemea kuna fedha nyingine ya kuja kumalizia.
Mheshimiwa Spika, Serikali ilishafanya tahmini na baada ya tathmini hiyo ikaongeza fedha kwenye awamu hii ya pili kutoka shilingi milioni 470 mpaka kwenye minimum ya shilingi milioni 560 katika halmashauri zote hapa nchini. Tutaendelea na tathmini kuona ni namna gani tunaweza tukatafuta fedha kwa ajili ya kumalizia kule ambapo hawakumalizia lakini wengine ilikuwa ni uzembe wao wenyewe.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika,pamoja na jibu zuri la Serikali lenye kuleta matumaini lakini kwa kuwa hii Tarafa ya Mbwera ipo visiwani na changamoto kubwa ya upungufu wa nyumba za walimu zaidi ya 35, hasa katika maeneo ya Twasalie, Kiongoroni, Mbuchi na Saninga. Je, Serikali inatupa matumaini gani kwa mwaka wa fedha wa 2024/2025?
Swali la pili kwa kuwa Tarafa hii ya Mbwera siku za nyuma huko ilijengewa sekondari moja tu kwa ajili ya Kata zote tano lakini kwa sasa Mheshimiwa Mbunge Twaha Mpembenwe na wananchi wa Tarafa hizi hasa Kata ya Mbuchi na Msala wamejenga sekondari imefikia ngazi ya lenta. Je, Serikali ina mpango gani wa kuchangia jitihada hizi za Mheshimiwa Mbunge na Madiwani na wananchi wa maeneo haya ili kukamilisha hizi sekondari? ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Khamis Mgalu Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la kwanza nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba upatikanaji wa bajeti ndiyo kigezo kikubwa kinachoweza kusaidia shule hizo kujengwa. Hivyo nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi wa Kata hizo za pembezoni hatutowaacha isipokuwa Serikali yao inaendelea kutafuta fedha na itaendelea kuweka fedha ili kujenga shule hizo.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kwanza nataka nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi ambavyo anashirikiana na Mbunge wa Jimbo Mheshimiwa Mpembenwe kwa jinsi anavyofuatilia maendeleo ya wananchi wetu. Nataka nimhakikishie kwamba pamoja na kujengwa kwa shule ambapo kumekwama katika Kata hizo za Mbuchi na kule alikosema nataka nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kutenga bajeti katika mwaka ujao wa bajeti kama ilivyofanya katika mwaka huu kwa kutenga bilioni 55.75 ili kuendelea kusaidiana na wananchi kuweza kufikia malengo makubwa ya kuwapelekea elimu wananchi wetu.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imefanya mapinduzi makubwa ya kutumia utaratibu wa EPC + Financing na kesho inasainisha mikataba saba hiyo; je, ipo tayari kuifikiria barabara ya Makofia – Mlandizi – Mzenga – Mwanarumango kwenye utaratibu huo siku za usoni? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ni wazi kwamba hii barabara aliyoitaja tumekuwa tunaitengea bajeti na bado hatujakamilisha kulipa fidia hasa kwa kipande cha Makofia hadi Mlandizi, lakini mpango ni kuijenga hii barabara yote kwa kiwango cha lami. Sasa kama itaingia kwenye utaratibu wa kawaida ama utaratibu wa EPC + F itategemea na kipindi hicho ambapo sasa tutaanza kuijenga hiyo barabara.
Mheshimiwa Spika, wakati najibu barabara za EPC nilisahau pia kuwakumbusha watu wa kuanzia Handeni – Kiberashi – Kibaya – Kwamtoro hadi Singida, pia hiyo barabara itakuwepo kesho, ahsante. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza naishukuru sana Serikali kutupongeza Mkoa wa Pwani kwa kufanya vizuri, lakini pia kwa kutenga kiasi cha shilingi milioni 161 kwa kuanza hayo mafunzo. Maswali yangu mawili ya nyongeza ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, je, ni lini hasa mafunzo hayo yataanza kwa kuwa majukwaa yale yameundwa muda mrefu na tumefanya jitihada mpaka Kitongoji, Vijiji, Wilaya mpaka na Mkoa?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa katika jibu lake la msingi amesema zimetengwa hizo fedha shilingi milioni 161 na ndani yake kutakuwa na za Mkoa wa Pwani, lakini nataka niulize, je, Serikali inaipa wajibu gani Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kupitia Katibu Tawala wa Mkoa na Halmashauri zetu za Mkoa wa Pwani katika kulea majukwaa haya ili yalete tija iliyokusudiwa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, swali lake la kwanza kama nilivyoeleza kwenye jibu la msingi, Serikali imetenga shilingi milioni 161 kwa ajili ya kuwajengea uwezo na kuwajengea uwezo wanawake ili kuinuka kiuchumi ambapo Mkoa wa Pwani umetengewa shilingi milioni 58.5 kwa ajili ya kuendesha mafunzo hayo.
Niwaombe tu Maafisa Tawala wa Mikoa wote nchini waanze kuandaa programu hizo za mafunzo na mwaka wa fedha ukiingia mafunzo hayo yaanze. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, zipo taasisi mbalimbali za binafsi ambazo zinawezesha wananchi kutoa mikopo mmoja-mmoja na vikundi. Kwa hiyo, niwaombe wananchi waendelee kutumia fursa hizo kuhakikisha uchumi wao unakua, ahsante. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, kwa kunipa fursa ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Wizara ya Maji kupitia DAWASA inaendelea na kazi nzuri ya upanuzi wa miundombinu ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, lakini yapo maeneo jirani na mitambo hiyo hayana maji kwa mfano; Kata ya Mzenga, Vihingo, Kisarawe.
Je, ni lini Serikali itasambaza maji kwenye kata hizo ambapo ni jirani kama kilometa 20 kutoka Mji wa Mlandizi? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Subira Mgalu kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, nipokee kwanza pongezi na kutambua kazi kubwa inayofanywa na DAWASA; maeneo haya uliyoyataja Mheshimiwa Mbunge yanaelekea kufikiwa baada ya miradi mikubwa sana ambayo inaendelea kufanyika pale DAWASA na maeneo yote ya huko ulikotaja Mzinga, Kisarawe kote yanatarajiwa kupata maji ifikapo mwaka ujao wa fedha. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, Serikali imeongeza kwa kiwango kikubwa bajeti ya umwagiliaji kutoka Shilingi Bilioni 46 mpaka Bilioni 361 na kwakuwa Wilaya yetu ya Bagamoyo tunayo skimu ya umwagiliaji - Ruvu inaitwa Chauru yenye wanachama zaidi ya 900 lakini inayo changamoto kubwa ya uchakavu wa miundombinu.
Je, Serikali inatoa ahadi gani kwa wanachama wa skimu hii ya umwagiliaji Chauru katika ukarabati wa miundombinu? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Subira Mgalu Mbunge, kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Spika, mradi huo tunaufahamu na changamoto iliyopo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge kwamba katika miradi ambayo Tume imepanga kuifanyika kazi katika bajeti inayokuja mradi huo pia umeainishwa, kwa hiyo wakulima wa eneo hilo watapata nafasi ya kuweza kufaidika na uboreshaji wa miundombinu hasa baada ya kuanza utekelezaji kupitia bajeti inayokuja.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, Serikali imejenga majengo mazuri sana ya Makao Makuu ya Polisi katika Mkoa wa Kusini Unguja, Tunguu na Mkoa wa Kaskazini Unguja na yamezinduliwa, tuliyashuhudia katika ziara ya Mheshimiwa Mwenyekiti wa UWT Taifa. Je, ni lini sasa majengo haya yatapatiwa samani ili yaanze kutumika kutokana na uwekezaji mkubwa mliofanya Serikali wa zaidi ya shilingi bilioni tatu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa Mbunge kutambua juhudi ambazo zimefanywa na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kutengeneza mazingira ya kutolea huduma za kiusalama yakiwemo majengo ya Polisi ngazi ya Mkoa na Wilaya.
Mheshimiwa Spika, ni kweli ujenzi ni hatua, kukamilisha majengo ni jambo moja na uwekaji wa samani ni jambo la pili. Hatua itakayofuata ni kuruhusu majengo yaanze kutumika na Jeshi la Polisi limejipanga vema katika bajeti yake ya mwaka huu kuyapatia samani majengo hayo, yakiwemo hayo ya Tunguu na Kusini Unguja. Nashukuru.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.
Kwanza naishukuru Serikali kwa ukarabati wa ofisi ya kituo kidogo cha Polisi Jimbo la Chalinze.
Kwa kuwa, Wilaya yetu ya Bagamoyo ofisi ya Polisi majengo yake ni ya muda mrefu na yamechakaa na kwa kuwa tunatarajia watalii wengi kutokana na Royal Tour ambapo Mheshimiwa Rais alifika Bagamoyo.
Je, Serikali inatuahidi vipi katika kukarabati ofisi ya Polisi Wilaya ya Bagamoyo? Ahsante sana.
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Kwanza ninapokea pongezi kwa niaba ya Serikali juu ya kazi ambayo tayari imeshaanza kufanyika kama alivyoeleza Mheshimiwa Mbunge. Vilevile nichukue nafasi hii kutoa maelekezo kuwa tathmini ya ukarabati huo ufanyike ili tuweze kuangalia utaratibu wa kupata fedha kwa ajili ya kukarabati kituo hicho.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa ujenzi wa chuo cha VETA Wilaya ya Rufiji na Wilaya ya Mafia.
Kwa kuwa, Serikali imetenga Bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa vyuo vya VETA kwa Wilaya 36; na kwa kuwa ndani ya Mkoa wetu wa Pwani Wilaya ya Bagamoyo na Wilaya ya Mkuranga hakuna chuo cha VETA.
Je, Serikali inatuambiaje kama kuna uwezekano wa kupata chuo kutoka na vyuo 36 vitakavyojengwa?
Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Subira Mgalu, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Pwani, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli anachozungumza Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mgao uliopita miongoni mwa wilaya za Mkoa wa Pwani, Wilaya ya Mafia pamoja na Rufiji vilipata vyuo hivi lakini wilaya nyingine kama Mkuranga, Kisarawe pamoja na Bagamoyo bado havijapata vyuo hivyo.
Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kama Wilaya hizi zitakuwa tayari zimetenga maeneo yaliyopimwa tayari yana Hati kama nilivyozungumza wakati najibu swali la Mheshimiwa Mulugo vitapata kipaumbele. Kwa hiyo, jukumu kubwa hapa ambalo ninakupa Mheshimiwa Mbunge ni kuhakikisha mnaweza kutenga maeneo kwa haraka ili kwamba wakati tunajaribu kutenga zile fedha maeneo haya yaweze kufikiwa kirahisi.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nampa pole Mheshimiwa Mbunge Twaha na wananchi wa Kibiti kwa mafuriko makubwa yanayoendelea kule, lakini pamoja na hayo, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa, jibu la msingi limeonyesha utayari wa Serikali kufungua Ofisi ya Forodha katika Bandari ya Nyamisati; na kwa kuwa, Bandari ya Nyamisati imeonesha ofisi katika Mamlaka ya Mapato (TRA). Naomba kujua, je, Serikali ipo tayari mpaka Desemba, 2024 ofisi hiyo iwe imefunguliwa kwa umuhimu wake wa kuongeza mapato? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa, wafanyabiashara wa vyombo vya mashua kutoka Zanzibar wapo tayari kusafirisha bidhaa kwa kutumia Bandari ya Nyamisati kwa sababu ina miundombinu iliyo kamili. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kushirikiana na Mbunge Twaha pamoja na mimi Mbunge wa Mkoa kukutana na wafanyabiashara hao ili kuzungumza na kuwatia moyo katika maandalizi ya kutumia Bandari ya Nyamisati? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Subira, Balozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali iko tayari na ndiyo maana katika jibu la msingi tumesema Mwaka huu wa Fedha 2024/2025 forodha hiyo itafunguliwa. Kwa hiyo, Serikali iko tayari haitafika Disemba tutakuwa tumeanza zoezi hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, Naibu Waziri yuko tayari kuambatana na Mheshimiwa Mbunge Twaha na Mheshimiwa Balozi wetu Bi. Subira kwenda kukaa na wafanyabiashara hao. Ahsante sana.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, natoa pole kwa wananchi wenzangu wa Rufiji wakiwemo wanawake na watoto kwa janga kubwa la mafuriko linaloendelea kutokana na mvua nyingi. Pia nampa pole Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mheshimiwa Mchengerwa, lakini niishukuru sana Serikali kwa kutukimbilia kwa haraka kupitia Kitengo cha Maafa kwa Wilaya za Rufiji na Kibiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya salamu hizo za pole, naomba sasa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kupitia ukurasa rasmi wa Mheshimiwa Waziri Bashe amefahamisha kwamba tarehe 20 Serikali itatangaza kazi ya ujenzi wa mabwawa ya umwagiliaji ya Ngorongo na Umwe; na kwa kuwa, mabwawa haya yanatarajia pia kushughulikia changamoto ya mafuriko; je, Serikali haioni sasa ipo haja ya Mradi huu wa BBT kwa Bonde la Rufiji hususan Wilaya ya Rufiji kwenda sambamba na ujenzi wa mabwawa haya ambayo yanatarajiwa kujengwa na Serikali? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa inapotokea mafuriko mashamba ya umwagiliaji yanapata changamoto kubwa ya kuharibiwa kwa mazao, kwa mfano Skimu ya Umwagiliaji ya Bagamoyo, inapotokea tatizo hilo wananchi hao wanaendelea kulipa tozo na ada mbalimbali kwenye Mfuko wa Umwagiliaji wa Taifa. Je, Serikali haioni ipo haja ya kuja na mwongozo kwamba, endapo kunatokea mafuriko na yanaharibu mashamba ya umwagiliaji na wananchi hawapati mazao, waweze kupewa nafuu katika tozo inayotakiwa kulipwa kwenye Mfuko wa Umwagiliaji wa Taifa kwa kuwa wamepata matatizo? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Wizara ya Kilimo kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji mwezi huu tutatangaza tender ya kujenga mabwawa makubwa mawili katika ile downstream ya Mwalimu Nyerere Hydropower hususan katika eneo la Ngorongo pamoja na Mbatia Mtuli eneo la Umbwe kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri, huo ndiyo msimamo na haya ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais ambayo aliyatoa wakati ametembelea katika Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, hilo ni kweli na linakwenda kutekelezeka kuhakikisha kwamba tunapunguza athari za mafuriko katika eneo la Bonde la Mto Rufiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kuhusu mwongozo, nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, ushauri wake tumeupokea na tutaufanyia kazi kwa sababu jukumu la Serikali ni kusikiliza wananchi wake. Ahsante.(Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nampongeza sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kutujibu vizuri na naishukuru Serikali kwa kutupa matumaini kupitia majibu ya swali hili. Maswali yangu ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; kwa kuwa, barabara hii ya Mingoi – Kiembeni ya kilometa sita inatumika na wakazi wengi takribani 17,000 wa mitaa kwa mfano Kiharaka, Kiembeni yenyewe, Mingoi, Tungutungu na kadhalika; na kwa kuwa wananchi wa maeneo haya wameunda mpaka Kamati ya Barabara chini ya uongozi wa Ndugu Mapunda ambayo imekuwa ikijichangisha mara kwa mara kutengeneza barabara hii. Sasa, ninamuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri, je, yupo tayari kutembelea maeneo haya ili aone athari za mvua hizo za El-Nino na aone kama kiwango hiki kilichotengwa kwenye bajeti hii kama kitatosha?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; kwa kuwa barabara hii linajengwa daraja kubwa la Mpiji Chini, chini ya TANROADS na Waziri wa Ujenzi Mheshimiwa Bashungwa alitembelea pale na kutoa ahadi kwamba kuna uwezekano wa kuipandisha hadhi barabara hii kwa kuwa ni kiungo kati ya Bagamoyo na Kinondoni. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri, yupo tayari kuisimamia TARURA ili ikamilishe mchakato wa vigezo ili barabara hii iende TANROADS na ile ahadi ya kujengwa kwa kiwango cha lami iweze kutimia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, hakika Mheshimiwa Mbunge amekuwa akisemea sana Barabara hii ya Mingoi – Kiembeni na hasa kwa sababu ina wakazi wengi, kwa maana wakazi zaidi ya 17,000. Wengi ni wanawake na watoto wapo humo kwa hiyo amekuwa akisemea sana barabara hii ili kulinda maslahi ya makundi hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza kama nipo tayari kuambatana na yeye kwenda kujionea hali halisi katika eneo hili ili kuona kama bajeti inatosheleza kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mara baada ya kutoka katika kujibu maswali haya, tutakaa, tutazungumza na tutapanga ratiba ili niweze kufika. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge hata kwenye swali lake la pili, nikija kwenye ziara hiyo, nina imani hata suala hili la kuharakisha mchakato wa kuitoa barabara hii ya eneo la Mpiji Chini kwenye daraja hili linalojengwa na TANROADS kupandisha hadhi barabara hizi ili ziweze kutoka TARURA zihamie TANROADS, ninaamini tunaweza kulisimamia nikiwa nimefika kwenye eneo husika. Kwa hiyo, ninaomba nimhakikishie kwamba nipo tayari na tutafanya kazi bega kwa bega kwa maslahi mapana ya watu wa Bagamoyo. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Serikali ya kutia matumaini, naomba kuuliza. Swali la kwanza; je, Serikali au Mheshimiwa Naibu Waziri yupo tayari kutaja kiwango kilichotengwa kwa ajili ya kuanza kazi hii ya kufunga taa katika Kiwanja cha Ndege cha Mafia? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa Uwanja wa Ndege wa Mafia licha ya kwamba hauna taa lakini una uwezo wa kuruhusu ndege kubwa kutua na kwa kuwa Serikali imefanya uwekezaji mkubwa kwenye Shirika letu la Ndege ATCL. Je, ni lini Shirika la ATCL litaanza safari ya kwenda Mafia ili kuwawezesha watalii hasa kipindi cha Mwezi wa Kumi mpaka wa Tatu ambapo utalii wa samaki mkubwa anayepatikana kwenye nchi sita tu hapa duniani aina ya samaki potwe?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyojenga hoja kuhusiana na Uwanja wa Ndege wa Mafia na nimhakikishie swali lake la pili kwamba tumeshaanza tathmini ya kina kufahamu mahitaji na habari za kutosha kuhusiana na Uwanja wa Mafia na tukikamilisha tutapeleka Ndege ya ATCL.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la kwanza kuhusiana na habari aliyozungumza, kwanza nimkumbushe Serikali inafahamu umuhimu mkubwa sana wa Kiwanja cha Ndege cha Mafia kilichojengwa miaka mingi iliyopita kuanzia wakati wa mkoloni na tumefanya kazi kubwa pale. Tulirekebisha runway tukajenga ambayo ina urefu wa mita 1,500 na upana wa mita 30, tukaongeza eneo la kuegesha ndege kiasi kwamba ndege sita ndogo Caravan C208 zinaweza kutua pale. Kama hiyo haitoshi, tunapozungumza hapa tunafanya usanifu kwa ajili ya kuongeza jengo la abiria ili liwe na uwezo wa kubeba abiria zaidi kwa sababu jengo lililopo linabeba abiria 50.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, katika mwaka huu wa fedha nimeshamtamkia, Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia inao mpango na inakwenda kuweka taa za kuongozea ndege katika kiwanja hicho. Atupe muda tu tutakwenda kukamilisha.
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri kwa sababu, nimefuatilia, hasa maeneo ya visiwani, kama mpango huu kweli unaendelea. Maswali yangu mawili ni kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; licha ya mpango huu wa M-Mama kufanya vizuri. Je, kuna sababu gani nyingine ambazo zimechangia kupunguza vifo vya akinamama wajawazito kutoka 556 kwa vizazi hai 100,000 hadi 104 kwa vizazi hai 100,000 kulinganisha na baadhi ya nchi ambazo zimeripoti vifo vya akinamama zaidi ya 386? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; kwa kuwa, mpango huu wa M-Mama pia, una malengo ya kushughulikia changamoto za watoto wachanga wakiwemo watoto wanaozaliwa kabla ya muda, watoto njiti. Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga vituo, kwa ajili ya watoto njiti kwa kuwa, vifo vya watoto njiti vinachangia 48% vya vifo vya watoto wote chini ya umri wa miaka mitano? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, yes. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, lakini niseme tu kwamba, kama mnakumbuka Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alipohutubia kwa mara ya kwanza Bunge hili, akiwa amesimama hapo ulipo Mheshimiwa Spika, alipofika eneo la mama na mtoto alilisisitiza sana na kurudia mara mbili.
Mheshimiwa Spika, lakini hakuishia kwenye kusisitiza, ameleta shilingi trilioni 6.7 ambazo zimeenda kwenye maeneo ya miundombinu, teknolojia na pia, kufunza wataalamu na hizo fedha zote zimekwenda zikabadilisha, zikatutoa kwenye vifo 556 mpaka sasa tumefika vifo 104 na ni mfano wa kuigwa duniani. Kwa sababu tulikuwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwenye Mkutano wa Umoja wa Mataifa ni Marais wawili tu walikuwa wanapewa, kwenye eneo la afya nishani, kwa ajili ya kufanya vizuri. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu alikuwa anapewa nishani kwenye eneo hili na walipoona Rais wetu hakuwepo akasema wenyewe watakuja Tanzania, kwa ajili ya kumshukuru. Wanataka waonane naye physically na kumpongeza na kumpa hiyo nishani yeye mwenyewe kwa hiyo, ni kazi kubwa imefanyika. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pili, Mbunge amezungumzia eneo la watoto njiti. Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatutafutia shilingi bilioni 190. Siyo muda mrefu Waziri wetu tunaendelea na mchakato ndani ya Wizara ya Afya namna ya kujenga hivyo vituo vya watoto njiti na siyo muda mrefu Waziri wa Afya, Mheshimiwa Jenista Mhagama atakuja kutoa maelezo ni namna gani tunaweza kwenda mbele kwa kutumia hizo shilingi bilioni 190. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa kuwa Serikali imekwishaanza kutangaza kazi za ujenzi wa kilometa tano kwa ajili ya wakandarasi wanawake na kazi imefanyika Mkoa wa Songwe. Je, anatupa matumaini gani, kwamba jambo hili litakuwa endelevu? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Subira Mgalu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza niendelee kumpongeza kwa namna ambavyo anawapambania wakandarasi wanawake. Nimwondoe wasiwasi, kwenye bajeti ya Wizara ya Ujenzi ambayo nitakayowasilisha kesho kutwa tunayo mikakati kabambe kwa ajili ya wakandarasi wanawake. Si hizi kilometa tano tu, tunazo kilometa nyingi ambazo tumezi-earmark kwa ajili ya kutekelezwa na wakandarasi wanawake. (Makofi)
MHE. SUBIRA K. MGALU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa, ni mara ya kwanza kwa Barabara hii ya Makofia – Mlandizi – Maneromango kupata jibu la matumaini kwamba, awamu hii ya sita imeanza kutekeleza ujenzi wake kwa kipande cha kilomita 23.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza; ninataka niulize kwa kuwa, katika barabara hii vipo vijiji kwa mfano, Kijiji cha Matimbwa na Yombo, wananchi walifanyiwa tathmini, kwa ajili ya kulipwa fidia. Je, Serikali haioni haja sasa ya wananchi walio kando ya barabara hii, wakiwemo wa Vijiji vya Matimbwa na Yombo, kulipwa fidia wakati Serikali ikitafuta fedha za ujenzi wa kipande kilichobaki? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Kwa kuwa, wakati wanawasilisha bajeti ya Wizara ya Ujenzi walitupa matumaini Wakazi wa Bagamoyo juu ya ujenzi wa Daraja la Mpiji Chini na kwamba, watamsimamia mkandarasi, ili aendelee na kazi. Je, Serikali ipo tayari kutimiza ile ahadi yao ya kupandisha hadhi kipande cha Barabara ya Mingoyi – Kiembeni inayounganishwa na Daraja hili la Mpiji Chini ili kuwarahisishia Wakazi wa Bagamoyo na Kinondoni, kwa ajili ya mawasiliano? Naomba kuwasilisha na ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutambua jitihada za Serikali. Namhakikishia kwamba, suala hili tunalifanya haraka sana kwa sababu ni barabara ambayo inaenda kuunganisha Mji wa Mlandizi pamoja na Kituo cha SGR na tayari tupo kwenye hatua za mwisho kabisa za manunuzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fidia ya vijiji alivyovitaja Mheshimiwa Mbunge, tayari tulishawasilisha jedwali ambalo limehahakikiwa na lipo Hazina likisubiri tu fedha itoke tuweze kuwalipa wananchi hawa ambao watapisha ujenzi wa barabara hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Daraja la Mpiji Chini; ni kweli kwamba, daraja hili lilishapata mkandarasi. Mimi binafsi nimeenda, lakini pia, Waziri ameenda pale na kutoa maelekezo ni nini mkandarasi aweze kufanya. Katika mito ambayo ilipanuka sana ni pamoja na eneo hili ambalo mkandarasi alikuwa analijenga kwa hiyo, kuna haja ya kufanya mapitio upya ya usanifu uliokuwa umefanyika kwa sababu, daraja hili limeongezeka sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kupandisha hadhi barabara aliyoitaja; namwomba tu Mheshimiwa Mbunge kwamba, taratibu zipo, tunasubiri maombi kutoka Mkoa ambayo tathmini itafanyika na wataalam wetu mara tutakapopata maombi rasmi ya kupata Mkoa kama taratibu zilivyo. Ahsante. (Makofi)