Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Tauhida Cassian Gallos Nyimbo (8 total)

MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS NYIMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa, toka tumalize Uchaguzi Mkuu Zanzibar imekuwa na baadhi ya watu wakitoa kauli za vitisho, hususan wakati huu wa sikukuu wanatoa kauli za vitisho kupitia mitandao ya kijamii;
Je, Serikali inawaambia nini wananchi wa Zanzibar, hususan vijana na watoto ambao wanatarajia kusherehekea sikukuu ya Eid al-Fitr.(
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inachoweza kuwaeleza wananchi wa Zanzibar na Watanzania kwa ujumla ni kwamba wasiwe na wasiwasi wowote, nchi yetu iko salama na itaendelea kuwa salama. Ninyi ni mashahidi kwa kazi nzuri ambayo imekuwa ikifanywa na Jeshi la Polisi. Kwa matukio ya hivi karibuni jana na juzi mmejionea. Pia kwa upande wa Zanzibar juu ya hawa watu ambao wanajaribu kutaka kutuletea mrafaruku katika nchi yetu, tumewadhibiti. Nataka nitoe tu wito kwa wananchi kuacha kukubali kuchochewa na baadhi ya wanasiasa, wahakikishe kwamba wanaendelea kufuata sheria za nchi yetu, yeyote ambaye atakiuka sheria hiyo kama ambavyo tumekuwa tukizungumza kila siku, kwamba ikiwa ni mwanachama wa chama cha siasa, ikiwa ni kiongozi basi hatua kali za kisheria zitachukuliwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nisisitize tu kwamba wananchi wasiwe na wasiwasi, waendelee kusherehekea siku ya Eid-al-Fitr bila wasiwasi wowote. Serikali yao ipo itaendelea kuwalinda wao pamoja na mali zao.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALOSS: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa suala la elimu ya juu ni suala la Muungano, je, wanafunzi wangapi katika idadi ya hao aliowataja wametokea Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili, je, wanafunzi hawa wanaporudi masomoni hukuta ajira tayari au wanaachwa wanazurura mitaani?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kimsingi nafasi hizi za kusoma nje mara nyingi zinapotolewa zinatangazwa kupitia Balozi husika ambazo zimepanga kutoa masomo hayo, lakini wakati mwingine pia kupitia vyuo vyetu vikuu. Wakati wa uombaji suala linalozingatiwa zaidi ni sifa ikizingatiwa kwamba masuala ya elimu ya juu ni masuala ya Muungano.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia wakati mwingine inawezekana kabisa Ubalozi ukaamua kama umependa watu wa Zanzibar, basi utaelekeza moja kwa moja kupitia masuala ya kimahusiano kwa upande wa Zanzibar.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kimsingi kwa sasa sitaweza kukupa taarifa kamili na ikizingatiwa kwamba linahitaji data. Kwa upande wa ajira, hawa wanafunzi wakirudi, kwa sababu wengi wanakuwa wamepelekwa kwa ajili ya jambo mahsusi, kwa mfano, upande wa gesi, kwa hiyo wanapofika yale maeneo ambayo yanawahitaji ndiyo ambayo yanakuwa yametangaza kazi na wakati huo huo wenye sifa wanakuwa wanachukuliwa kupitia taratibu zetu za kiutumishi.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia fursa hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza pamoja na majibu aliyonipa Mheshimiwa Waziri lakini sikuridhika na majibu haya.
Mheshimiwa Waziri katika majibu yake ya msingi anasema kwamba kati ya bidhaa ambazo hazitozwi kodi pamoja na vinyago, lakini katika swali hilo hilo la msingi anabainisha kwamba kati ya vitu vinavyokamatwa na kupigwa mnada ni pamoja na vinyago. Mheshimiwa Waziri katika suala hili ulivyolijibu huoni kwamba umejichanganya? Kama vinakamatwa na kupigwa moto, vinakamatwa kwa kosa lipi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kuuliza swali la pili, je, Serikali imetoa elimu yoyote kuhusiana na suala zima la uuzaji wa vinyago kwa wajasiriamali wadogo wadogo ukizingatia Mheshimiwa Rais ameondosha kodi ndogo ndogo kwa wajasiriamali?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, naomba nikiri kwamba sijamchanganya, vinyago tunafahamu ni bidhaa zinazotokana na maliasili za nchi yetu hivyo inawezekana watu wa Wizara ya Maliasili wanatozo zao ambazo wanazitoza. Mimi nimekanusha utozaji wa kodi ambao tunatoza sisi kama Wizara ya Fedha kwamba hizi hazipo katika orodha ya bidhaa tunazozitoza kodi (extport duty). Kwa hiyo, ndiyo maana katika jibu langu la sehemu ya pili nilisema yawezekana zilikuwa zinatakiwa kulipiwa tozo mbalimbali kutoka katika Wizara ya Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili, elimu ya ujasiriamali tunaendelea kuitoa, kuna kitengo ndani ya Wizara yangu ya Fedha na tunaendela kuifanyia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wajasirimali wote nchini wakiwepo wafanyabiashara wa vinyago.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili madogo ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Waziri kwa kunijibu swali langu kiufasaha kabisa, lakini vilevile nina maswali mawili madogo.
Je, Serikali inaweza kutuambia nini uchorongaji utafanyika wa kazi hiyo?
Swali langu la pili, je, nje ya Mkoa wa Rukwa kuna Mkoa mwingine wowote umeweza kugundulika kwa gesi hii?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi ya uchorongaji itaanza pale taarifa za kijiolojia zikishakamilika na kwa mujibu wa taratibu zilivyokuwa zimepangwa katika Kampuni hii ya Hellium One Tanzania Ltd. wamepanga kuanza shughuli ya uchorongaji kuanzia mwaka 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile swali la pili, ni sehemu gani ambapo hii hellium inapatikana. Kwa kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge ni kwamba gesi ya hellium vilevile inapatikana katika Ziwa Eyasi lililoko Mkoa wa Manyara na sehemu nyongine ni sehemu ya Singida ambapo na penyewe inapatikana hii gesi ya hellium. Ahsante sana.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii ya kuuliza maswali mawili. Ningependa kufahamu njia gani zinazotumika katika kutoa elimu hiyo hususan vijijini?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kwa kuwa Mkuu wa Mkoa amekuwa mdau mkubwa wa kuwapigania watoto wanaoachwa na wazazi wao wa kiume, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuja na sheria za kuwabana wanaoacha watoto hususan wakiwemo na raia wa kigeni.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Tauhida kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tunayo sheria ambayo inaharamisha matukio ambayo yanahusisha mtu yeyote kutelekeza mtoto ama kutotoa matunzo na sheria hiyo si nyingine ni Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 kifungu cha 166, kwa hiyo sheria tunayo tayari. Niwaombe akinamama wote ambao wameathirika na jambo hili kwa kuwa ni la jinai, waende kwenye vituo vya polisi vilivyo karibu wafungue kesi hizi ili Serikali tutumie sheria nyingine zozote tulizonazo za kuwarejesha nchini wajibu mashtaka.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo zoezi alilolifanya Mheshimiwa Makonda Mkuu wa Mkoa ambalo Mheshimiwa Mbunge ame-refer ni zoezi ambalo lilionyesha dhahiri kwamba sio wageni tu wanaotelekeza watoto isipokuwa hata Watanzania wanatelekeza watoto na tulishuhudia wengine humu ndani sura za watoto zikiwa zinawafanana.

Mheshimiwa Spika, nitoe wito kwa akinamama wa Tanzania, nawaomba mtumie kilicho ndani ya nchi, kilicho chenu kuliko kuanza kukimbilia kutumia raia wa kigeni ilhali hata humu ndani, rudini humu ndani kumenoga.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS NYIMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza kabisa pia nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais wetu kuweza kuirudisha ndege yetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la nyongeza litakuwa moja; je, Waziri anaweza kutuambia ni njia gani zinazotumika kwa viongozi wa Wilaya na Mikoa kufuatilia ahadi zinazotolewa na viongozi hawa wanapokuja nchini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Tauhida kwa kazi nzuri ambayo anaifanya kule Zanzibar akiwakilisha wananchi. Amefanya mambo mengi, ametoa kompyuta na kujenga madarasa ya kompyuta na amekuwa akijulikana kama ni rafiki wa wanawake na watoto. Swali lake ni ushahidi tosha kwamba anafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kupitia Idara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Zanzibar inashirikiana kwa karibu kabisa na viongozi wa Wilaya na Mkoa pamoja na Ofisi ya Rais kule Zanzibar, katika kufanya vikao vya mashauriano ili kuona kwamba ahadi ambazo zimetolewa na hazijatekelezwa zinatekelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, niwashauri Mheshimiwa Tauhida tuendelee kushirikiana kupitia viongozi wa Wilaya, Mkoa, Wizara za Kisekta, Ofisi ya Rais Zanzibar pamoja na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki katika kuhakikisha kwamba ahadi zote zinatekelezwa. Kama kuna ahadi sugu ambayo haijatekelezwa nitamuomba tuonane ili tuweze kuitekeleza haraka iwezekanavyo.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa fursa hii kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa kumejitokeza suala la uhalifu ambao unafahamika kwa jina la panya road, je, Serikali ina mikakati ipi ya kuweza kuwaelimisha wananchi ili kuendelea kujikinga na suala hili la panya road?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, kwa kuwa uhalifu huu unafanyika Zaidi kwa silaha za jadi pamoja na silaha nzito. Serikali ina mkakati gani juu ya udhibiti wa silaha hizi?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Tauhida, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na utaratibu wa elimu kwa jamii kuhusu kukabiliana na uhalifu wa aina mbalimbali ikiwemo uhalifu ambao ameuzungumza Mheshimiwa Mbunge. Kwanza hivi karibuni tumeweka utaratibu wa kupeleka askari katika kila kata, kuna askari ambao walihitimu mafunzo ya kuupandishwa vyeo na hawa tumewatawanya katika kata zote nchi nzima kwa ajili ya kwenda kusaidia utaratibu na mifumo ya ulinzi shirikishi katika maeneo husika pamoja na utoaji elimu kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, kama hilo halitoshi hivi karibuni tumepata maelekezo kutoka kwa Amiri Jeshi Mkuu kwamba tuhakikishe tunakamilisha ununuzi wa magari ambayo yatakwenda moja katika wilaya na utaratibu wa kupeleka mafuta uende moja kwa moja wilayani kusaidia kuimarisha vitendea kazi kwa askari wetu walio karibu na wilaya na kata zetu kwa lengo la kuandaa mipango thabiti ya elimu kwa umma kuhusiana na ulinzi shirikishi pamoja na jitihada nzima za kushirikisha wananchi katika kusaidia vyombo vyetu vya usalama hususan Jeshi la Polisi katika kudhibiti uhalifu, si katika elimu tu hata kujipanga katika kudhibiti matukio ya kiuhalifu yasijitokeze.

Mheshimiwa Spika, nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba, baadaye Jeshi la Polisi watafanya mazungumzo na vyombo vya habari, watazungumza kutoa na kuainisha mkakati kabambe wa kupambana na waharifu ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam, hatua zilizofikia, mafanikio, changamoto, sababu na mipango ya kudhibiti jambo hilo lisiendelee kutokea zaidi. Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine, wananchi wanaweza kupata ufafanuzi zaidi wa kina juu ya jambo hili hapo baadaye.
MHE. TAUHIDA CASSIAN GALLOS: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza swali moja la nyongeza. Ninamshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri ambayo yanaendelea kutia matumaini ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, pamekuwepo na baadhi ya wasanii ambao wanawakilisha ndani ya mataifa mengine ya nje, lakini wasanii hao ni wazuri, hawana scandal ya aina yoyote. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri anaonaje kwa wakati huu achukue fursa ya kuwezesha wasanii hawa kupatiwa hata Passport za kihuduma ambazo zitawafanya wao waendelee kuitunza sana aa kuiwakilisha vizuri Tanzania?
NAIBU WAZIRI WA UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Serikali inatambua umuhimu wa wasanii katika kuitangaza nchi yetu, lakini pia katika kuchangia uchumi wetu. Ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, upo umuhimu wa kuendelea kuwarahisishia wakati wanavyofanya safari za kwenda kufanya kazi zao nje ya mipaka ya Tanzania ambako wanakwenda kuitangaza nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, nchini mamlaka ambayo ina jukumu la kutoa Passport na hati nyingine za kusafiria ni Idara ya Uhamiaji ambayo iko chini ya Wizara ya Mambo ya Nchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Passport na Hati Nyingine za Kusafiria ya Mwaka 2002, wasanii si miongoni mwa wanufaika wa Hati za Kidiplomasia ama Hati za Kihuduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninamhaidi Mheshimiwa Mbunge, swali lake hili ambalo limekuja kama maoni na ushauri, tutakaa na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Ndani kuona namna ambavyo tunaweza kuendelea kuwarahisishia wasanii wetu wanaofanya kazi kubwa ya kuitangaza nchi yetu nje ya mipaka yetu namna ya kusafiri ili waendelee kuifanya kazi hiyo kwa moyo mmoja. Ahsante.