Primary Questions from Hon. Issaay Zacharia Paulo (35 total)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Ingawa kuna tatizo la ajira Serikalini, lakini inasemekana kuwa ziko nafasi nyingi zilizo wazi katika ngazi ya Wizara, Mikoa, Wilaya hata Vijiji:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali inalificha jambo hili na ni lini sasa itajaza nafasi za ajira zilizo wazi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Halmashauri ya Mji wa Mbulu katika sekta za Utawala kama vile VEO, WEO ambapo wananchi huwalipa watumishi wa kukaimu kwa fedha zao wenyewe kinyume na taratibu?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isipandishe mishahara ya kima cha chini kwa kuzingatia mahitaji ya maisha ya sasa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, UTUMISHI NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, maombi ya nafasi za ajira mpya Serikalini hufanyika kwa uwazi kupitia bajeti ya Serikali ambayo huidhinishwa na Bunge hili. Ajira hizi hufanyika baada ya waajiri kuwasilisha maombi yao Serikalini na kuidhinishwa kwa kuzingatia ukomo wa bajeti ya mishahara Serikalini.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka huu wa fedha 2015/2016, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilitengewa nafasi za kuajiri Watendaji wa Vijiji (VEO) kumi na Watendaji wa Kata (WEO) Sita.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na nafasi hizo Serikali itaendelea kujaza nafasi wazi kila mwaka kulingana na uwezo wa kibajeti na vipaumbele vilivyowekwa.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekuwa ikipandisha kima cha chini cha mshahara kulingana na uwezo wa bajeti au mapato ya ndani na kwa kuzingatia kupanda kwa gharama za maisha. Kutokana na hatua hii, Tanzania ni moja ya nchi za Afrika ambazo kwa sasa hulipa kima cha chini cha mshahara sawa na asilimia 80 ya kiwango cha gharama za chini za maisha (minimum living wage).
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali itaendelea kuboresha mishahara ya watumishi wake wa umma kulingana na uwezo wake wa kiuchumi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Serikali imekuwa na azma nzuri kujenga zahanati katika kila kijiji na kituo cha afya katika kila kata nchi nzima:-
(a) Je, ni lini Serikali itapanua Chuo cha MCH Mbulu kinachotoa cheti kuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Binadamu kwa kuwa tayari Baraza la Madiwani limekubali kutumia ardhi yake ya akiba?
(b) Je, kwa nini Serikali isitembelee chuo hicho ili kujionea fursa zilizopo?
(c) Je, ni kwa nini pia Chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Tango FDC kisitumike kama chuo cha VETA kwa sababu kwa sasa hakina taaluma nzuri katika fani mbalimbali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Uuguzi na Ukunga Mbulu kiliandaliwa kwa ajili ya kukidhi mafunzo kwa ngazi ya cheti kutokana na miundombinu iliyokuwa nayo pamoja na uwezo wa hospitali inayotumika kama sehemu ya mafunzo. Upanuzi wa vyuo kudahili wanafunzi wa kada za juu kwa kawaida huwa unaendeana sambamba na upanuzi wa miundombinu na upatikanaji wa wataalam kwenye hospitali iliyoridhiwa kuwa ni hospitali ya mafunzo. Wizara ya Afya inaishukuru Halmashauri ya Mbulu kwa kuanzisha mchakato wa kukitengea eneo zaidi chuo hiki ili kijipanue zaidi. Wizara itashirikiana na Ofisi ya Rais, TAMISEMI juu ya upatikanaji wa ardhi hiyo kabla ya kuingiza suala la upanuzi wa chuo hiki katika mipango yetu.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imekuwa ikitembelea Chuo cha Mbulu katika taratibu zake za kawaida za kiutendaji. Mwaka 2015/2016, timu za Wizara zimefanya ziara za ufuatiliaji kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya ukusanyaji taarifa na pia katika kukagua miradi ya maendeleo na ukaguzi wa hesabu za mapato na matumizi ya fedha. Kwa mwaka 2016/2017, Wizara itafanya ufuatiliaji kwenye chuo hiki na lengo kuu litakuwa ni kuona utekelezaji wa ahadi hii ya Halmashauri kuhusu upatikanaji wa ardhi.
(c) Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi – Tango kinatoa mafunzo ya maarifa na stadi katika fani za kilimo na mifugo, ushonaji, useremala, uashi na umeme wa majumbani. Aidha, hutoa pia mafunzo ya udereva kwa muda mfupi wa miezi mitatu. Chuo hiki kina watumishi wapatao 21 na wakufunzi 10. Kwa sasa chuo kina wanachuo 98 ambapo 59 wanachukua mafunzo ya ufundi stadi kwa kufuata mtaala wa Mamlaka ya Ufundi Stadi yaani VETA Level I - III na 39 wanachukua mafunzo ya muda mfupi ya udereva.
Mheshimiwa Naibu Spika, Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vina makubaliano maalum na VETA yaani MOU (Memorandum of Undestanding) ya kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na yale ya elimu ya wananchi ambayo yalikuwa yakitolewa tangu awali. Kufuatia makubaliano hayo, vyuo 25 viliboreshwa na kuanza kutoa mafunzo ya ufundi stadi sanjari na mafunzo ya elimu ya wananchi kuanzia mwezi Januari, 2013. Lengo likiwa ni kuhakikisha Vyuo vyote 55 vya Maendeleo ya Wananchi vinatoa mafunzo kwa mifumo yote miwili yaani mafunzo ya elimu ya wananchi na yale ya ufundi stadi (VETA).
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Tango kimewekwa katika awamu ya pili ya maboresho hayo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kumekuwa na ahadi za viongozi wa juu hususan Marais za kujenga daraja la Magara pamoja na barabara ya Mbuyu wa Mjerumani kwa kiwango cha lami na usanifu wa daraja na lami ya zege sehemu ya mlimani hasa ikizingatiwa kuwa ukosefu wa daraja na jiografia ya Mlima Magara kuwa hatarishi sana hasa kipindi cha mvua.
(a) Je, ni lini ahadi hiyo ya viongozi wetu wa Kitaifa itatekelezwa?
(b) Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kujenga barabara ya lami yenye urefu wa kilometa tano katika Mji wa Mbulu itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuunganisha Mji wa Mbulu na barabara Kuu ya Babati – Arusha katika eneo la Mbuyu wa Mjerumani. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja la Magara lenye urefu wa mita 84. Taratibu za kumpata mhandisi mshauri wa kusimamia ujenzi wa daraja hili zinaendelea. Aidha, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS), inafanya maandalizi ya kutangaza zabuni kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa ujenzi wa daraja la Magara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2016/2017, jumla ya shilingi milioni 300 zimetengwa kwa ajili ya kuanza ujenzi wa daraja la Magara na shilingi milioni 455 zimetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha zege (rigid pavement) kwenye Mlima Magara katika barabara ya Mbuyu wa Mjerumani hadi Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara itaendelea kutekeleza ahadi za viongozi wa Serikali kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha ikiwemo ahadi ya ujenzi wa barabara ya lami katika Mji wa Mbulu yenye urefu wa kilometa tano.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Aliuliza:-
Maziwa Madogo nchini kama vile Ziwa dogo la asili la Tlawi katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu yanaelekea kukauka kutokana na kuongezeka kwa magugu maji, kadhalika Ziwa Babati na Ziwa Manyara pia yana dalili ya kukauka na Mamlaka za Serikali za Mitaa hazina uwezo wa kuyaokoa:-
(a) Je, Serikali haioni umuhimu wa kuyaokoa maziwa hayo muhimu katika ustawi wa nchi yetu na kizazi kijacho?
(b) Je, kwa nini kusiwe na mpango kabambe wa Kitaifa kuyaokoa maziwa hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inaona umuhimu mkubwa wa kuokoa Ziwa dogo la Tlawi lililopo Halmashauri ya Mbulu na maziwa mengine kote nchini yanayokabiliwa na tishio la kukauka na magugu maji kutokana na kuongezeka kwa shughuli za binadamu hususan kilimo na ufugaji usio endelevu, uvuvi haramu na athari ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mheshimiwa Spika, kutokana na umuhimu huo, mwaka 2008 Serikali iliandaa Mkakati wa Taifa wa Hatua za Haraka za Kuhifadhi Mazingira ya Bahari Ukanda wa Pwani, Maziwa, Mito na Mabwawa. Mkakati huu unaelekeza Wizara na sekta na halmashauri zote nchini kuchukua hatua za haraka kuzuia shughuli zote za binadamu kufanyika kandokando ya maziwa, mito na mabwawa ili kuzuia uharibifu wa mazingira unaoweza kusababisha kukauka kwa maziwa hayo.
Mheshimiwa Spika, ili kunusuru Ziwa dogo la Tlawi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imechukua hatua zifuatazo:-
1. Mradi wa DADP’s Wilaya ya Mbulu umetenga Shilingi milioni 100 katika mwaka wa fedha wa 2016/2017 kwa ajili ya kuondoa magugu maji katika Ziwa Tlawi.
2. Katika Bajeti ya Mwaka 2017/2018, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu imepanga kutenga kiasi cha Shilingi 15,742,000 ili kutekeleza shughuli za kunusuru Ziwa Tlawi pamoja na kuainisha mipaka ya ziwa hilo, uvamizi wa watu katika shughuli za kilimo, kuhimiza
kilimo endelevu pamoja na miinuko inayozunguka ziwa hilo, kutoa elimu kwa wananchi ya kuhifadhi mazingira na vyanzo vya maji, kuimarisha Kamati za Mazingira na ulinzi shirikishi kwa ziwa katika ngazi za kata, vijiji na mitaa.
Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada zinazofanywa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Serikali itafanya tathmini ya kina kubaini chanzo cha ukubwa wa tatizo na kuchukua hatua stahiki za ziada kuhimili athari katika Maziwa ya Tlawi, Babati na Manyara ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja kuwa yako kwenye tishio la kukauka.
MHE. ZACHARIA P. ISSAY aliuliza:-
Katika mwaka wa fedha 2013/2014, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ilipeleka maombi maalum ya fedha za ujenzi wa daraja la Gunyoda na wakati huo kutokana na kugawanywa kwa Wilaya ya Mbulu kupata Wilaya mbili, daraja la Gunyoda limebaki kuwa kiungo muhimu kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mbulu vijijini.
Serikali Kuu ilitoa kiasi cha Sh.100,000,000/= ambazo Halmashauri ya Wilaya ya Mji wa Mbulu kwa maagizo ya aliyekuwa Rais wa Awamu ya Nne fedha hizo zilielekezwa kwenye ujenzi wa maabara za sayansi katika Halmashauri zote nchini na kuacha daraja hilo bila kujengwa kwa sababu Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu haina uwezo wa kulijenga kwa fedha za ndani:
(i) Je, Serikali ina mpango gani wa kusaidia ujenzi wa daraja hilo ambalo ni kikwazo kikubwa kwa huduma za kijamii katika Halmashauri zote mbili?
(ii) Kwa kuwa mabadiliko ya Tabianchi yamesababisha uwepo wa makorongo makubwa ambayo yako katika Kata za Gonyoda, Silaloda, Gedamara, Bargish, Dandi, Marangw’ na Ayamaami jambo linalosababisha jamii kukosa huduma za jamii, afya na utawala. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutafuta fedha za dharura ili kusaidia janga hilo katika Halmashauri mbalimbali ikiwemo Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(i) Mheshimiwa Naibu Spika, daraja la Mbulu linalopita kwenye Korongo la Gunyoda lenye urefu wa mita 70.4 na kina cha mita tano lilifanyiwa usanifu wa awali kwa mwaka wa fedha 2013/2014 na kubaini kwamba zinahitajika shilingi milioni mia nane na hamsini kulijenga. Hadi sasa ni muda mrefu umepita, hivyo Serikali kupitia Wataalam wa Halmashauri itafanya usanifu wa kina kujua gharama halisi za kuingiza katika mpango wa bajeti wa mwaka wa fedha 2018/2019 ili kuanza ujenzi.
(ii) Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwkaa wa fedha 2017/2018 Serikali inaanza utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ambao utatekelezwa kwenye halmashauri 15 ili kuandaa mpango wa kuzingatia athari za tabianchi. Serikali itashirikiana kikamilifu na halmashauri ili kuhakikisha fedha zilizotengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 kwa ajili ya matengenezo ya dharura. Natoa wito kwetu sote kwa pamoja tushirikiane kikamilifu katika kutunza mazingira.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kati ya mwezi Juni – Desemba, 2015 wananchi wapatao sita walishambuliwa na kuuawa na wanyamapori na Shirika la Hifadhi Tanzania (TANAPA) halikushiriki mazishi ya watu hawa, wala hakuna fidia yoyote waliyopata ndugu wa marehemu, hali inayoonesha mahusiano mabaya kati ya jamii na Mamlaka ya Hifadhi, zaidi ya hayo wanyama kama tembo, wamesababisha hasara kubwa sana kwa kuharibu mazao katika Tarafa ya Daudi, Kata za Marangwa, Daudi, Bargish na Gehandu.
• Je, ni lini Serikali itawalipa fidia ndugu wa hao watu sita waliouawa na wanyama wakali katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
• Je, ni lini Serikali kupitia TANAPA italipa fidia kwa wale wote walioharibiwa mazao shambani mwaka 2014/ 2015?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaya, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hailipi fidia kwa madhara yanayosababishwa na wanyamapori hatari au waharibifu, badala yake inatoa kifuta jasho au kifuta machozi, kwa mujibu wa kifungu cha 68(1) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Aidha, kifungu cha (3) cha Kanuni za Malipo ya Kifuta Jasho na Kifuta Machozi za mwaka 2001 kinaainisha masharti na viwango vya malipo ya kifuta jasho na kifuta machozi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imepokea madai ya wananchi watano waliouawa, wanne walijeruhiwa na 31 walioharibiwa mazao yao katika eneo ambalo Mheshimiwa Mbunge analizungumzia. Madai hayo yamefanyiwa kazi kwa mujibu wa kanuni na yatalipwa mara fedha zitakapopatikana.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Wilaya ya Mbulu haina barabara ya lami kutokana na kuzungukwa na Bonde la Ufa kuanzia Karatu, Mto wa Mbu, Babati – Hanang hivyo, kufanya magari makubwa kutoka Uganda, Kenya na Dar es Salaam kuzunguka umbali mkubwa ili kufika Mbulu Mjini.
Je, Serikali ina mpngo gani wa kutekeleza ahadi yake ya kuweka lami katika barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom - Mkalama – Lalago Shinyanga ili kurahisisha usafiri katika njia hiyo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Karatu – Mbulu - Hydom – Mkalama – Lalago – Kolandoto, yenye urefu wa kilometa 389 ni kiungo muhimu kwa Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Singida kwa kupitia Kusini mwa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kuwa barabara hii ina umuhimu mkubwa wa kiuchumi na kijamii na ni kiungo muhimu kati ya Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Shinyanga na Singida. Maandalizi ya ujenzi kiwango cha lami ya barabara hii yameanza kwa hatua za awali, ambapo Wizara yangu kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeingia mkataba na Mhandisi Mshauri aitwaye HP Gauff Ingenieure GmbH & Co. KG – JBG ya Ujerumani ili kufanya kazi ya upembuzi yakinifu ambayo inaendelea hadi sasa. Kazi hii inagharamiwa na Serikali ya Ujerumani kupitia Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika, Serikali itatafuta fedha na kuanza ujenzi wa barabara hii kwa kiwango cha lami.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Hospitali ya Wilaya ya Mbulu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa watumishi; upungufu huo wa watumishi umeathiri utoaji wa huduma wa Hospitali hiyo na Vituo vya Afya vya Tawi na Daudi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kuongeza watumishi katika Hospitali hiyo?
• Serikali inatekeleza mpango wa upanuzi wa Vituo vya Afya zaidi ya 200 nchini; je, Serikali inachukua hatua gani kukabiliana na changamoto za watumishi, fedha na vitendea kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya watumishi wa sekta ya afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ni 345, watumishi waliopo ni 206 na upungufu ni watumishi 139. Serikali imeendelea kuajiri watumishi wa afya kadri wanavyohitimu na kupangwa moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali iliajiri watumishi 2,058 wa kada za afya kwenye Mikoa na Halmashauri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya hao, Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipangiwa watumishi kumi wakiwemo Madaktari wawili, Matatibu wawili; Afisa Muuguzi mmoja; Afisa Afya Mazingira mmoja na Msaidizi wa Afya, Mazingira mmoja; Mteknolojia Msaidizi mmoja na Wauguzi daraja la pili wawili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile katika mwaka wa fedha 2018/2019 Halmashauri imeomba kibali cha kuwaajiri watumishi 91 ili kupunguza upungufu uliopo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali inaendelea na ujenzi wa Vituo vya Afya 208 nchi nzima ili kuboresha huduma ya dharura kwa mama wajawazito. Ujenzi wa vituo hivyo utagharimu shilingi bilioni 132.9 hadi kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na ujenzi huo, vituo hivyo vimetengewa shilingi bilioni 35.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa na vifaatiba ili kuviwezesha kutoa huduma kwa wagonjwa. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeomba kibali cha kuwaajiri watumishi wa kada ya afya wapatao 25,000 ili kuhakikisha kunakuwepo na watumishi wenye sifa stahiki kwenye hospitali, vituo vyote vya afya na zahanati.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Mwaka 2016 Serikali kupitia Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi aliahidi kuipatia Wilaya ya Mbulu Baraza la Ardhi la Wilaya:-
• Je, ni lini ahadi hiyo itatekelezwa na hatimaye Wilaya ya Mbulu kuwa na Baraza la Ardhi la Wilaya?
• Je, ni kwa nini Serikali isipime ardhi ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu na kuwapatia hati ili kuondoa migogoro ya ardhi?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, mwishoni mwa Julai, 2018 Wizara kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma imetangaza nafasi za ajira kwa ajili ya kupata Wenyeviti 20 wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya. Wenyeviti hawa ni kwa ajili ya Mabaraza 17 ambayo hayana Wenyeviti. Vilevile Wenyeviti wawili ni kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye Mabaraza katika Mikoa ambayo imeelemewa na mashauri mengi na ina Mwenyekiti mmoja kama Dar es Salaam na Mwenyekiti mmoja ni kwa ajili ya Baraza la Mbulu ambalo litafunguliwa na kuanza kufanya kazi punde taratibu za kupata watumishi wengine zitakapokamilika. Kwa ushauri wa Mkoa na Wilaya Baraza hili litakuwa Makao Makuu ya Wilaya ya Mbulu.
(b) Mheshimiwa Spika, azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila kipande cha ardhi nchini kinapimwa. Azma hii inatekelezwa kwa kupeleka huduma zote za sekta ya ardhi ikiwemo huduma za upimaji katika Ofisi za Ardhi za Kanda na Wapima wa Wilaya. Aidha, Wizara imekalimisha taratibu za kupeleka vifaa vya kisasa ambavyo vitasaidia zoezi hili la upimaji na TEHAMA katika ngazi za Kanda vyenye thamani ya shilingi bilioni 4.3 ambavyo zimekabidhiwa kwa viongozi wa Kanda wiki hii ambavyo vitasaidia sana katika kurahakisha zoezi hili la upimaji katika Wilaya zetu katika Kanda husika.
Mheshimiwa Spika, napenda kukumbusha kuwa jukumu la upimaji ni la Mamlaka ya Upangaji, hivyo, Halmashauri zote zinatakiwa kushirikiana na Wizara kupitia Afisa Ardhi, Ofisi za Ardhi za Kanda, kuhakikisha kuwa azma ya kupima kila kipande cha ardhi nchini inafikiwa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Hali ya barabara zinazosimamiwa na halmashauri ni mbaya sana kutokana na fedha zinazotolewa na Mfuko wa Barabara kukaa kwa muda mrefu na hali ya kuongezeka kwa magari binafsi na yale ya biashara ambapo kila tarafa ina zaidi ya magari 20 na hivyo, kufanya barabara hizo kuharibika na kuwa vigumu kupitika nyakati za masika:-
(a) Je, Serikali haioni haja ya kuleta mapendekezo mapya ya mgao wa fedha za barabara?
(b) Barabara nyingi za Halmashauri ya Mji wa Mbulu zimejifunga katika Tarafa za Nambis na Daudi. Je, kwa nini wataalam kutoka Wizarani wasifike kuzikagua na kutoa ushauri stahili?
(c) Je, kwa nini BQ za tenda za barabara ngazi ya mkoa zisiwekwe kwenye kitabu cha RRB, ili Waheshimiwa Wabunge na wananchi wafahamu shughuli zitakazofanywa na makandarasi waliopewa kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye Sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya mtandao wa barabara nchi nzima ili hatimaye utumike kuangalia kwa kina utaratibu mzuri zaidi wa mgawo wa fedha za barabara kati ya TANROADS inayoshughulikia barabara kuu na barabara za mikoa na TARURA inayoshughulikia barabara za Mamlaka za Serikali za Mitaa.
b) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Mwaka wa Fedha 2017/2018 Barabara za Mji wa Mbulu zilitengewa shilingi milioni 814.56. Kati ya hizo shilingi milioni 262.12 zilitengwa kwa ajili ya barabara kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum (Periodic Maintenance) Barabara za Ayamaame – Kainam – Hhasama – Mbulu – Endagikot – Tlawi, Tango FDC, Waama – Masieda, Ayayumba – Hhayloto zenye urefu wa kilometa 35.7 katika Tarafa za Daudi na Nambisi na kuweka changarawe katika Barabara za Ayamaami – Kainam – Hhasama, Mbulu – Kuta na Ayayumba - Hhayloto zenye urefu wa kilometa 8.13
Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile kuchonga barabara ya Uhama – Masieda – Hayayumba – Hailoto zenye urefu wa kilometa 31.5 na ujenzi wa kalavati za njia mbili zenye kipenyo cha milimita 900 katika Tarafa ya Daudi. Barabara zilizokuwa zimejifunga kwa kuharibika na mvua sasa zinapitika ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 95 na kazi inaendelea. Katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 Barabara za tarafa za Nambis na Daudi zimetengewa shilingi milioni 438.8 kwa ajili ya matengenezo.
c) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni haki ya wajumbe wa Bodi ya Barabara ya Mkoa na wananchi kupata taarifa za jumla za barabara zilizopangwa kujengwa katika mkoa, ikiwemo gharama za kazi ambazo wajumbe wanaweza kuzipata katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara ya Mkoa.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY atauliza:-
Serikali ina nia njema ya kuuweka Mji Mkongwe wa Mbulu kwenye mpango kabambe wa maboresho ya Miji na Majiji, Mikoa na Wilaya na kwenye Awamu ya Pili ya mpango huo kwa ajili ya miundombinu ya masoko, barabara, vituo vya mabasi na taa za barabarani:-
(a) Kwa kuwa Mji wa Mbulu ni mkongwe toka kuanzishwa kwake, je, ni lini sasa nia hiyo njema itatekelezwa?
(b) Je, mpango huo wa maboresho ya Mji utasaidiaje miundombinu ya barabara za mitaa ya Mji wa Mbulu ambazo ni zaidi ya kilomita 40 za changarawe kwa kuwa ni kilomita 1.8 za lami kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikalli kupitia Ofisi ya Rais - TAMISEMI inatekeleza miradi ya uboreshaji Miji Tanzania ambayo ni Urban Local Government Strengthening Programme (ULGSP) na Tanzania Strategic Cities Project (TSCP) na Dar es Salaam Metropolitan Development Project (DMDP) kwa fedha za mkopo nafuu toka Benki ya Dunia. Mpaka sasa miradi hii inatekelezwa katika Majiji 6, Manispaa 19 na Halmashaurui za Miji 6. Utekelezaji wa Programu ya Kuzijengea Uwezo Mamlaka za Miji (Urban Local Government Strengthening Programme-ULGSP) ulianza katika mwaka wa fedha 2013/2014 na unatarajiwa kukamilika mwaka wa fedha 2019/2020. Wakati wa maandalizi ya programu hii, Mji wa Mbulu ulikuwa haujapata hadhi ya kuwa Halmashauri ya Mji na hivyo kukosa vigezo vya kujumuishwa kwenye programu. Serikali itatoa kipaumbele kwa Mji wa Mbulu kwenye awamu nyingine za mradi huu.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Programu ya Kuzijengea Uwezo Mamlaka za Miji inajumuisha ujenzi wa miundombinu ya msingi katika miji, kujenga uwezo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani na kuwezesha uandaaji wa mipango kabambe ya uendelezaji wa miji na kuboresha uwajibikaji na utawala bora. Hivyo Mji wa Mbulu ukijumuishwa utanufaika na mradi huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inafahamu umuhimu wa kuboresha miundombinu ya barabara katika Mji wa Mbulu. Katika mwaka wa fedha 2018/2019 kupitia fedha za Mfuko wa Barabara, Serikali inajenga barabara yenye urefu wa kilomita 0.4 kwa kiwango cha lami nyepesi (double surface dressing) kwa gharama ya shilingi milioni 300 na kazi ya ujenzi inaendelea.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Sera ya Afya ni kuwa na Kituo cha Afya kwa kila Kata na Zahanati kwa kila Kijiji; Tarafa ya Nambis katika Jimbo la Mbulu Mjini haina Kituo cha Afya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Vituo vya Afya kwenye Kata za Kainem, Murray, Nambis na Nahasey?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay,Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli kuwa Tarafa ya Nambis haina Kituo cha Afya na wananchi wa Tarafa hiyo wanapata huduma kwenye Zahanati 4 za Serikali zilizoko katika Tarafa ya Nambis pamoja na Hospitali ya Wilaya ya Mbulu ambayo iko jirani na Kata ya Nambis.
Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Mji wa Mbulu, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Vituo vya Afya Daudi na Tlawi sambamba na vifaa tiba ambapo hadi Oktoba, 2019 Kituo cha Afya Daudi kimepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 203.8 na Kituo cha Afya Tlawi kimepokea vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi 203.8.
Vilevile Mkoa wa Manyara umepatiwa kiasi cha shilingi billioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Halmashauri za Wilaya za Mbulu na Simanjiro. Ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Mbulu utapunguza msongamano katika Hospitali ya Wilaya ya Mbulu iliyoko Mbulu Mjini.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kujenga na kukarabati Vituo vya Afya nchini kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha uliopo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY Aliuliza:-
Katika mradi wa REA I na II vijiji vingi vya Jimbo la Mbulu Mjini havikufikiwa na umeme na katika vijiji vilivyofikiwa ni kaya kati ya 20 mpaka 30 pekee ndizo zilizopata umeme:-
(a) Je, ni lini REA III itapeleka umeme katika Vijiji 26 vya Jimbo la Mbulu Mjini?
(b) Awamu ya I na II ziliruka shule nyingi, vituo vya afya na Makanisa. Je, ni lini sasa taasisi hizo zitapelekewa umeme?
(c) Je, ni lini Serikali itarudia usambazaji wa umeme katika vijiji vyote vilivyosambaziwa sehemu ndogo sana katika Jimbo la Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a), (b) na (c), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utekelezaji wa Mradi wa REA III, Mzunguko wa Kwanza katika Jimbo la Mbulu Mjini, jumla ya Vijiji vitatu vya Gwaami, Tsaayo na Banee vitapatiwa umeme na Mkandarasi Kampuni ya Angelique International Limited.
Aidha, vijiji vitatu vya Murray, Silaroda na Gunyoda vinaendelea kupelekewa umeme na Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kwa Mpango wa Umeme Vijijini. Vijiji 20 vilivyobaki vya Jimbo la Mbulu Mjini vya Hereabi, Maheri, Kuta, Qwam, Nahasey, Hayasali, Hasama, Hayloto, Kwermusi, Amowa, Gwandumehhi, Aicho, Gedamar, Qalieda, Laghanda mur, Gidamba, Qatesh, Landa, Tsawa na Jaranja vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III, Mzunguko wa Pili unatarajiwa kuanza Januari, 2020.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, shule, vituo vya afya na taasisi nyingine ambazo hazijaunganishwa umeme katika vijiji au maeneo ya karibu yaliyounganishwa umeme na miradi ya awali ikiwemo REA I na II yatapelekewa umeme katika kipindi hiki. Tumetoa wito kwa Halmashauri au taasisi husika zilipie gharama za kuunganisha umeme ili taasisi hizo ziunganishiwe umeme.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maeneo ya Mbulu Mjini yaliyosambaziwa umeme, tunawaomba wananchi wa maeneo ya karibu na maeneo yenye umeme kuendelea kulipia Sh.27,000 ili maeneo hayo nayo yatumie umeme huo uliopo katika maeneo hayo. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Kupitia Sera ya Serikali ya kila kata kuwa na kituo kimoja cha afya, ni kata mbili tu zimebahatika kuwa na vituo vya afya kati ya kata kumi na saba (17) za Halmashauri ya Mji wa Mbulu; vituo hivi viko kwenye Tarafa za Daudi na Endagikot:-
(a) Je, ni lini Serikali itajenga kituo kimoja cha afya Kata za Kainam au Muray kwa ajili ya kupeleka huduma ya afya katika Tarafa ya Nambis yenye kata nne na vijiji ishirini na mbili na wakazi 24,800 kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012?
(b) Serikali ina sera ya kutoa huduma za afya bila malipo kwa watoto walio chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito; je, Serikali inachukua hatua gani katika vituo ambavyo bado vimeendelea kuchangisha kundi hili muhimu katika jamii?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua changamoto ya uhaba wa vituo vya afya katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu. Kutokana na hali hiyo, Serikali iliamua kuanza na ujenzi wa Vituo vya Afya viwili na Daudi na Tlawi vilivyogharimu jumla ya shilingi bilioni moja kwa kila kituo kupata shilingi milioni 500. Hata hivyo, Serikali inatambua na imesikia kilio cha Mheshimiwa Mbunge, Serikali itafanya juhudi kwa kadri iwezekanavyo ili kuwasaidia wananchi wa kata hizo.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeongeza bajeti ya dawa kutoka shilingi bilioni 31 hadi bilioni 270 ili kuboresha huduma za afya kwa wananchi yakiwemo makundi yenye msamaha wa matibabu. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imeidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 104 kupitia Mfuko wa Afya wa Pamoja, ile basket fund, ambapo sehemu kubwa ya fedha hizo ni kwa ajili ya dawa na vifaatiba. Hivyo, Serikali haitarajii kuona akina mama wajawazito pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano wakichangishwa. Serikali haitasita kuchukua hatua kwa wote watakaobainika kuwatoza makundi hayo kwa kuwa ni kinyume na maelekezo ya Serikali. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAY aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Mbulu mpaka Haydom kilometa 50 kama ilivyopitishwa kwenye bajeti ya 2019/2020?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mbulu – Haydom kilometa 50 ni sehemu ya barabara ya Karatu, Mbulu, Haydom, Sibiti, Lalago – Maswa kilomita 389 ijulikanayo kama Serengeti Southern Bypass. Barabara hii inahudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kupitia Mikoa ya Arusha, Manyara, Singida na Simiyu. Kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali wa mradi wa Serengeti Southern Bypass iko katika hatua za mwisho. Mara baada ya upembuzi yakinifu na usanifu wa awali kukamilika hatua itakayofuata ni usanifu wa kina wa maandalizi ya nyaraka za zabuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mradi huu unahusisha barabara ndefu yenye urefu wa kilometa 389, ili kurahisisha utekelezaji wake wakati wa ujenzi, mradi huu umegawanywa katika sehemu saba ambazo ni Karatu – Mbulu kilometa 79; Mbulu - Haydom kilometa 70.5; Haydom - Chemichemi kilometa 67; Chemichemi - Mwanhuzi kilometa 80; Mwanhuzi – Lalago - Maswa kilometa 83; Haydom - Kadash kilometa 67 na Lalago - Kolandoto kilometa 62.
Mheshimiwa Spika, ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii utaanza baada ya kukamilisha usanifu wa kina.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa lami barabara yenye urefu wa Kilometa 50 toka Mbulu kwenda Haydom ambayo ipo kwenye mpango wa Bajeti tangu 2019/2020, 2020/2021?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) Alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kujibu swali na ni mara yangu ya kwanza, naomba kuchukua nafasi hii kumshukuru kwanza Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kuwa Mbunge. Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Joseph Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi.
Mheshimiwa Spika, pia nikishukuru sana chama changu Chama Cha Mapinduzi kwa kuniteua na hatimaye kunipitisha kuwa mgombea wa Jimbo la Ileje, lakini niwashukuru sana….
SPIKA: Sasa majibu Mheshimiwa Naibu Waziri.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika,kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba nijibu swali laMheshimiwa Zacharia Paul Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika,Barabara ya Mbulu - Haydom yenye urefu wa kilometa 70.5 ni sehemu ya barabara yaKaratu – Mbulu – Haydom– Sibiti – Lalago – Maswayenye urefu wa kilomita 398 inayohudumiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS). Kazi ya Upembuzi Yakinifu na Usanifu wa Awali (Preliminary Design) wa barabara hii (kupitia mradi wa Serengeti Southern Bypass) ili kuijenga kwa kiwango cha lami umekamilika. Kazi hii ilifanywa na Kampuni iitwayo H.P. Gauff Ingenieure GmbH & Co. KG – JBG mwaka 2016 kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Ujerumani (KfW).
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu wa wananchi wa Mbulu pamoja na Hospitali ya Haydom, Serikali ilianza kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi kwa sehemu ya Mbulu
– Haydom yenye urefu wa kilomita 50 kwa kiwango cha lami, ambapo katika mwaka wa fedha 2019/2020, ilitenga Shilingi milioni 1,450.00 na mwaka wa fedha 2020/2021, imetenga Shilingi milioni 5,000.00. Ujenzi wa barabara hii utatekelezwa kwa njia ya Kusanifu na Kujenga (Design and Build) na zabuni ya kazi hii itatangazwa wakati wowote katika mwaka wa fedha wa 2020/2021.
Katika mwaka wa fedha 2020/2021, zimetengwa shilingi milioni 401 kwa ajili ya kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY (K.n.y. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY) Aliuliza:-
Mwaka 2015 Serikali ilitangaza kugawa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri za Mbulu Wilaya na Mbulu Mji walipitisha rasmi mgawanyo wa rasilimali na madeni.
Je, ni lini Serikali itarejesha tamko la mapendekezo hayo ili kufanikisha maendeleo ya mambo yaliyopendekezwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kupitia vikao vya Mabaraza ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mji Mbulu waliridhia na kupitisha mgawanyo wa rasilimali na madeni na kuwasilisha mgawanyo huo Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Tarehe 9 Novemba, 2018 mgawanyo wa mali na madeni ya Halmashauri hizo ulitolewa na Waziri mwenye dhamana na kutangazwa kwenye Gazeti la Serikali Toleo Namba 45 la mwaka 2018 pamoja na mgawanyo wa mali na madeni wa Halmashauri nyingine 42 kupitia Tangazo la Serikali Namba 696 la mwaka 2018.
Mheshimiwa Naibu Spika, mgawanyo wa rasilimali watu, magari, pikipiki, rasilimali na madeni umefanyika kwa asilimia 100 kwa kuzingatia Mwongozo wa Ugawaji wa Mali na Madeni ulioandaliwa na Ofisi ya Rais, TAMISEMI wa mwaka 2014. Katika mgawanyo huo, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu (Halmashauri mama) ilipata asilimia 60 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipata asilimia 40.
MHE. FLATEI G. MASSAY K.n.y. MHE. ZAKARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Je, ni lini Wakala wa Maji Vijijini atachimba visima sita katika Vijiji vya Aicho, Gidamba, 7 Gunyoda, Silaloda, Boboa na Titiwi katika Jimbo la Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zakaria Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kazi ya kuchimba visima kwa ajili ya kutumika kama vyanzo vya maji inafanyika maeneo mengi hapa nchini hivyo ili kuepuka ucheleweshaji inabidi kushirikisha makampuni binafsi kuchimba visima baada ya Wataalam wa Mabonde kufanya utafiti na kuainisha maeneo yenye maji chini ya ardhi. Hivyo, kazi hii zabuni imetangazwa kupitia Bodi ya Zabuni ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira ya Mkoa - Babati (BAWASA) ambapo Visima virefu vitatu katika vijiji vya Aicho, Boboa na Titiwi vitachimbwa kuanzia mwezi Mei, 2021 na kukamilika mwezi Juni, 2021.
Mheshimiwa Spika, visima vilivyobaki katika vijiji vya Gidamba, Silaloda na Gunyoda vitachimbwa katika mwaka wa fedha 2021/22.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Je lini Serikali itaajiri walimu wa masomo ya sayansi katika Shule za Sekondari za Halmashauri ya Mji Mbulu ili wanafunzi wapate ujuzi wa masuala ya sayansi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paul Issaay , Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2016/2017 hadi 2019/2020 Serikali imeajiri na kuwapanga walimu 17 wa sayansi na hisabati na mafundi sanifu wa maabara wawili katika Halmashauri ya Mji Mbulu kati ya walimu 10,418 wa Sekondari na mafundi sanifu maabara 397 walioajriwa katika kipindi hicho.
Aidha, Serikali inaendelea kuratibu zoezi la kuajiri walimu 6,949 kwa nafasi za ajira zilizotangazwa mwezi Mei, 2021 ambao watapangwa kwenye shule mbalimbali zikiwemo na shule za Halmashauri ya Mji Mbulu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatoa uamuzi wa mwisho wa mapendekezo ya mgawanyo wa rasilimali, madeni, majengo, watumishi na mashamba kati ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Mji wa Mbulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyojibu katika swali Na. 116 tarehe 12 Januari, 2021 mgawanyo wa rasilimali watu, magari, pikipiki, rasilimali na madeni kati ya Halmashauri ya Mji Mbulu na Halmashauri ya Mbulu umefanyika kwa asilimia
100 kwa kuzingatia mwongozo wa ugawaji wa mali na madeni ulioandaliwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI wa Mwaka
2014. Katika mgawanyo huo Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu kwa maana ya Halmashauri mama, ilipata asilimia 60 na Halmashauri ya Mji wa Mbulu ilipata asilimia 40.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Daraja la Gunyoda ambalo linaunganisha Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu hususani Tarafa ya Mang’ola kwenye mashamba ya vitunguu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekwishachukua hatua za kufanya upembuzi wa awali kwenye Korongo la Gunyoda lililoko katika Barabara ya Waama-Masieda, Kata ya Gunyoda katika Halmashauri ya Mji wa Mbulu ambako ndiko daraja hilo litajengwa. Korongo hilo lina urefu wa mita 70.4 na kina cha mita 5.0. Kutokana na ukubwa wa korongo hilo, upembuzi ulibainisha kuwa, ili kujenga Daraja la Gunyoda zinahitajika shilingi bilioni 1.2. Fedha hizi ni zaidi ya ukomo wa bajeti ya Halmashauri katika Fedha za Mfuko wa Barabara.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, kwa kuona umuhimu wa daraja la Gunyoda ikizingatiwa daraja hilo linaunganisha Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha daraja hilo linajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je ni lini serikali itajenga madaraja ya Gunyoda na Baray ikizingatiwa kuwa madaraja haya ni muhimu sana katika kuunganisha Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Halmashauri ya wilaya ya Mbulu na Karatu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Korongo la Gunyoda lenye urefu wa mita 70.4 na kina cha mita tano lipo barabara ya Waama-Masieda katika ya kata ya Gunyoda, Halmashauri ya Mji wa Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kutokana na umuhimu wa daraja la Gunyoda ambalo linaunganisha Halmashauri za Wilaya ya Mbulu, Karatu na Halmashauri ya Mji wa Mbulu, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini imetetenga bajeti katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na usanifu ili kufahamu gharama halisi zinazohitajika katika ujenzi wa daraja hilo. Baada ya kukamilika kwa upembuzi na usanifu wa barabara hiyo, Serikali itatafuta fedha kutoka vyanzo mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali imekuwa ikifanya matengenezo ya barabara ya Waama – Masieda yenye urefu wa kilomita 19.98 lenye korongo la Gunyoda ambapo katika mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya kilometa 17.25 za barabara zilifanyiwa matengenezo kwa shilingi milioni 70.25. Kwa upande wa mwaka wa fedha 2021/ 2022 jumla ya kilometa 14.2 zitatengenezwa kwa shilingi milioni 34.22 na Mkandarasi ameanza kazi za matengenezo na zitakamilika mwezi Mei, 2022.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya barabara katika Jimbo la Mbulu kulingana na upatikanaji wa fedha, ili kuimarisha upatikanaji wa huduma muhimu za jamii na kiuchumi.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya zege ya kilometa tatu kwenye Mlima Magara katika Jimbo la Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, eneo korofi na hatarishi katika Mlima Magara lina urefu wa kilometa saba. Kati ya hizo kilometa saba, Serikali imekamisha ujenzi kwa kiwango cha zege kilometa nne. Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali itaendelea na ujenzi kwa kiwango cha zege kwa kiasi cha kilometa moja. Kilometa mbili zilizobaki zitaendelea kujengwa kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Soko, Stendi, Dampo na Machinjio na barabara kilomita 12 za lami kupitia TACTIC katika Mji wa Mbulu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Mbulu ipo kwenye kundi la tatu lenye miji 18 ambayo utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa stendi kuu ya mabasi, soko jipya na barabara kwa kiwango cha lami unatarajiwa kuanza mwaka huu wa fedha 2022/2023 kwa kuandaa mipango kabambe (master plans).
Mheshimiwa Spika, hivi sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeanza kupokea taarifa za hatua mbalimbali za utambuzi wa mipaka ya kila mji pamoja na taarifa nyingine kwa ajili ya kuandaa hadidu za rejea ili kuwapata Washauri waliobobea katika kuandaa mipango kabambe.
Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilisha maandalizi ya mipango kabambe, kazi ya usanifu kwa halmashauri za kundi hili utaanza mwaka ujao wa fedha 2023/2024 na kazi za ujenzi zinategemea kuanza katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi 40,000 katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kama ilivyopitishwa katika Bajeti wa mwaka 2021/2022?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 tayari Serikali imekwishatoa Ikama na Kibali cha ajira kwa halmashauri zote nchini ambapo jumla ya nafasi za ajira za watumishi 17,412 wa kada ya afya na elimu zimetangazwa. Taratibu za kuajiri watumishi hao zinaendelea kukamilishwa. Aidha, ajira za kada zingine zinaendelea kutolewa kupitia Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma na halmashauri husika, ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaajiri watumishi wa kada ya ulinzi, upishi na makatibu muhtasi katika shule za sekondari za kata nchini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, naomba kujibu swali namba 82 lilliloulizwa na Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikitoa ajira kila mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2022/2023, Serikali imetenga nafasi 201 za Makatibu Muhtasi na tano za Wapishi. Watumishi husika wataajiriwa kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha. Aidha, kwa katika Kifungu cha 6(1) cha Sura ya 298 cha Sheria ya Utumishi wa Umma, Toleo la 2019, Waajiri mbalimbali zikiwemo Mamlaka za Serikali za Mitaa hutenga bajeti kwa kuzingatia kada na maeneo yote ya vipaumbele ikiwemo Walinzi, Wapishi na Makatibu Muhtasi na kuwapanga katika maeneo yenye uhitaji ikiwemo shule za sekondari za kata nchini.
MHE. REGINA N. QWARAY K.n.y. MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini ujenzi wa maabara za sayansi katika shule za sekondari utakamilika kama ilivyokusudiwa katika bajeti ya 2022/2023?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali ilitoa kiasi cha shilingi milioni 180 kwa ajili ya ukamilishaji wa maabara Sita Halmashauri ya Mji wa Mbulu na tayari mabara hizo zinatumika.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Halmashauri ilitenga na kutoa shilingi milioni 30 kupitia mapato ya ndani ili kukamilisha ujenzi wa vyumba viwili vya maabara na ujenzi huo upo katika hatua ya umaliziaji.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga na kupeleka fedha kwa ajili ya umalizaji wa maabara 11 ambazo hazijakamilika kadri ya bajeti itakavyoruhusu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza ujenzi wa jengo la Mahakama Wilayani Mbulu?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Spika, ninakushukuru na pia ninamshukuru Mwenyezi Mungu, na naomba sasa kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria niweze kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mahakama ya Wilaya ya Mbulu kwa sasa inaendeshwa katika jengo ambalo ni chakavu na finyu sana kukidhi mahitaji. Aidha, jengo hilo pia lipo kwenye eneo la hifadhi ya barabara na hivyo linapaswa kuondolewa. Katika mpango wetu wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Mbulu itajengwa katika mwaka wa fedha 2023/2024 na tayari mshauri elekezi ameshakamilisha usanifu na maandalizi ya zabuni kwa ajili ya kupata mkandarasi wa ujenzi. Ujenzi unatarajia kuanzia mwezi Septemba, 2023 na kukamilika kabla ya Juni, 2024.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji, Mitaa na Vitongoji kupitia Bajeti ya Serikali Kuu?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua kazi kubwa inayofanywa na Wenyeviti wa Mitaa, Vijiji na Vitongoji katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi. Kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura Na. 290, kila Halmashauri inatakiwa kuweka utaratibu wa malipo ya posho kwa wenyeviti wa vijiji, mitaa na vitongoji kutoka katika vyanzo vya mapato vya ndani ya Halmashauri.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 Serikali imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 222 kwa ajili ya matumizi mengineyo kwa halmashauri zote nchini. Hivyo Ofisi ya Rais – TAMISEMI inahimiza halmashauri zote nchini kuimarisha vyanzo vya mapato pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa fedha kwa kutumia mifumo ya kieletroniki ya kukusanya na kutumia fedha katika kutekeleza miradi ya maendeleo pamoja na matumizi mengineyo.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikai itajenga kwa kiwango cha lami km 76 za barabara ya Karatu – Mbulu kwa kuwa usanifu wake ulifanyika 2021/2022?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Serikali ipo kwenye maandalizi ya kujenga kwa kiwango cha lami kwa utaratibu wa EPC+F (Engineering, Procurement, Construction plus Finance). Barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom – Sibiti – Lalago – Maswa (km 389) ambapo barabara ya Karatu – Mbulu (km 76) ni sehemu ya barabara hii. Hadi sasa Mkandarasi amepatikana na mkataba wa kuanza ujenzi umesainiwa tarehe 16 Juni, 2023.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa Vyumba vya kuhifadhi maiti nchini vinakuwa na majokofu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zakharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hospitali zote 28 za Rufaa za Mikoa zina majokofu ya kuhifadhia maiti. Pia hospitali 16 za Mikoa zimepewa majokofu mapya kati ya hospitali 28 za Rufaa za Mikoa. Aidha, Serikali inatambua kuwa tatizo kubwa la upungufu lipo kwenye hospitali za Wilaya na vituo vya Afya vipya. Hata hivyo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imepanga kununua majokofu 103 kwa ajili ya kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Ahsante.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga Bwawa la Umwagiliaji Bonde la Endayaya Tlawi ambapo usanifu wake ulifanyika mwaka 2007?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Zacharia Paulo Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha usanifu wa kina wa bwawa la kuvunia maji la Tlawi litakalotumika katika kilimo cha umwagiliaji na Skimu ya Tlawi yenye ukubwa wa hekta 650 zilizopo katika wilaya ya Mbulu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Tlawi na skimu ambapo taratibu za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo zinaendelea.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kufanya upya tathimini ya maeneo kwenye Jimbo la Mbulu Mjini ambayo yalirukwa na Mradi wa REA I na II?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbulu Mjini lina jumla ya vijiji 34, kati ya hivyo, vijiji 31 vimepatiwa umeme na vijiji vitatu vilivyosalia yaani Kwam, Aicho na Tsawa vitapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA III Mzunguko wa II ambapo kazi imeshaanza na inatarajia kukamilika tarehe 30 Juni, 2024. Aidha, Jimbo la Mbulu Mjini lina mitaa 58 ambapo mitaa 46 imepatiwa umeme na mitaa 12 haina umeme. Kutokana na tathmini iliyofanywa na REA, mitaa 12 iliyosalia itapatiwa umeme kupitia mradi mkubwa wa kupeleka umeme vitongojini ambapo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/2025 kulingana na upatikanaji wa fedha, ahsante. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupunguza gharama za kusafisha figo kupitia Bima ya Afya kwa Wote?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Bohari ya Dawa (MSD) inafanya jitihada za kununua vitendanishi na vifaa vinavyotumika kusafisha figo moja kwa moja kutoka viwandani ili kupunguza gharama za huduma hiyo.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa wananchi mara utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote utakapoanza waweze kujiunga kwani ni njia pekee ya kuweza kuwasaidia kuepuka gharama za matibabu.
Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY aliuliza:-
Je, lini Serikali itaanza Ujenzi wa Minara ya Simu katika Kata za Nahasey, Gunyoda, Silaloda na Marang - Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI K.n.y WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI alijibu:-
Mheshimiwa Spika, hadi kufikia mwezi Machi, 2024, Serikali kupitia UCSAF, imetekeleza miradi katika Kata Tano za Wilaya ya Mbulu Mjini, ya ujenzi wa minara ya simu, ambapo miradi ya ujenzi katika Kata hizo imekamilika na wananchi wananufaika na huduma za mawasiliano. Aidha, katika Kata ya Nahasey, Kampuni ya Airtel ilikamilisha ujenzi wa mnara katika Kijiji cha Banee mwezi Machi, 2024.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Serikali kupitia Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (Digital Tanzania Project) inaendelea na ujenzi wa minara katika Kata mbili za Gunyoda na Marang. Minara katika kata hizi inatarajiwa kukamilika kabla ya mwezi Mei, 2025 ambapo kukamilika kwa Kata hizi mbili kutaboresha huduma za mawasiliano ya simu katika Vijiji vya Banee, Hassama, Haysali, Nahasey, Gedamar, Gunyoda, Silaloda, Aicho na Gwandumehi na hivyo kuifanya Kata ya Silaloda kuwa na mawasiliano.