Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Answers to supplementary Questions by Hon. Zainab Athuman Katimba (62 total)

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Kwanza nashukuru Serikali kwa kutenga fedha hizi kwa ajili ya kumalizia bwalo hili la Shule ya Malagarasi, hata hivyo, nina maswali ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; shule hii imeanza mwaka 1995 baada ya wananchi kujenga madarasa sita, madarasa haya hayajawahi kufanyiwa ukarabati. Je, ni lini Serikali itatenga fedha ili kukarabati madarasa ya shule hiyo?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; shule hii ina zaidi ya wanafunzi 1,240 ikiwa ni kuanzia kidato cha kwanza mpaka cha sita na wanafunzi takribani 418 wa kidato cha sita hawana mabweni. Je, ni lini Serikali itajenga mabweni angalau mawili kwa ajili ya mabinti wetu katika shule hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa jinsi anavyowapambania wananchi wake. Swali lake la kwanza, kuhusu ukarabati wa madarasa chakavu, napenda Mheshimiwa Mbunge afahamu kwamba Serikali inatambua uwepo wa shule chakavu za msingi na sekondari na ndio maana Serikali tayari imeshaanza ukarabati wa shule hizo kupitia miradi ya EP4R, SEQUIP na BOOST. Serikali kwa kutambua uhitaji na kwa kadri fedha zitakapokuwa zikipatikana, Serikali inakusudia kuja kufanya marekebisho katika shule yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili, ambapo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kuhusu ujenzi wa mabweni na hasa kwa wasichana. Mheshimiwa Mbunge naomba ufahamu Serikali inatambua kwamba kuna umuhimu wa kupata mabweni na hasa kwa watoto wa kike na ndio maana Serikali ilianza ujenzi wa shule za sekondari za bweni za wasichana katika kila mkoa kupitia Mradi wa SEQUIP. Kwa hiyo, kwa kuzingatia umuhimu wa kuwa na mabweni na hasa kwa watoto wa kike Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni hayo. Ahsante. (Makofi)
MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja fupi. Shule ya Msingi Igumila madarasa yake mawili yamebomoka na Naibu Waziri Utumishi alipopita pale alituahidi kutupa madarasa mawili. Je, ni lini fedha hizo zitapelekwa ili turejeshe hayo madarasa mawili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge kutambua uhitaji wa madarasa katika Shule ya Msingi Igumila, Serikali inaendelea kuangalia vipaumbele na kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itafanya jitahada kwa kadri fedha zinavyopatikana iweze kujenga madarasa haya. Ahsante
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na nashukuru kwa majibu, lakini nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; shule hii ilitembelewa na Mheshimiwa Rais wakati akiwa Makamu wa Rais na kuahidi kuipandisha hadhi mbele ya wadau na wadau hao tayari wameshakamilisha ujenzi wa madarasa. Je, Serikali wakati inaendelea kutafuta fedha haioni sababu ya kuwaomba wadau hao hao kukamilisha ujenzi wa mabweni ili shule hiyo iweze kuanza kwa sababu wako wadau ambao tayari wamejenga madarasa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Shule ya Sekondari Ilula iliyotajwa kama yenye kidato cha tano na sita, mabweni yake yametitia kutokana na mvua na kuwa hatarishi kwa watoto wanaosoma pale. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kuongozana na mimi kwenda kujionea hali hiyo na kuchukua hatua za dharura?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa natambua jitihada anazozifanya Mheshimiwa Mbunge kuwapigania wananchi wake. Kuhusu swali lake la kwanza ambapo anasema Mheshimiwa Rais alitoa ahadi ya ujenzi wa mabweni basi na yeye ameweza kutoa maoni kwamba Serikali itazame namna ya kushirikiana na wadau katika kukamilisha mabweni hayo. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge mawazo yake ni mazuri na Serikali imeyapokea na tutayachakata na kufanya mawasiliano na wadau ili tuone kwamba kwa pamoja Serikali na wadau tunaweza kujenga mabweni hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kuhusu bweni kuzama na nipo tayari kuambatana naye kwenda kuona hali halisi na kuchukua hatua za dharura. Nakubali Mheshimiwa Mbunge kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, ahsante
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Je, ni lini Serikali itaipandisha hadhi Shule ya Sekondari ya Lukoto iliyoko katika Wilaya ya Rungwe ukizingatia sekondari hiyo imezungukwa na kata ambazo na zenyewe zina uhitaji wa shule hiyo na kata zenyewe ni Kata ya Ikuti, Kimo, Masukuru, Bagamoyo, Suma na Sheli ya Masukuru?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rungwe aweze kwenda kufanya tathmini katika shule aliyoitaja Mbunge ili kutazama miundombinu na kuweza kuona kama miundombinu inakidhi vigezo vya kupata usajili wa kidato cha tano na sita. Baada ya kukamilisha tathmini hiyo waweze kuwasilisha maombi katika Wizara ya Elimu kwa ajili ya taratibu za kupata usajili wa kidato cha tano na sita. Ahsante.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naomba kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwanza kabisa nipongeze majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri kuhusiana na taulo za kike. Pamoja na kwamba Serikali zinatenga hizo fedha halmashauri, lakini bado kuna malalamiko makubwa sana katika shule zetu. Je, utaratibu gani unatumika kuhakikisha kwamba hizi fedha zinatengwa na hizi taulo zinawafikia wadau wanaotakiwa kupatiwa fedha hizi kwa sababu siku zote ukienda katika shule zote huoni kabisa taulo za kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuhusiana na swali la Mheshimiwa Mbunge, nataka kumhakikishia kwamba, fedha hizi zinatoka. Nachukua nafasi hii kuwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri kusimamia kwa umakini zoezi hili, ili fedha hizi zinazotengwa kwa ajili ya kupata taulo za kike ziweze kusimamiwa kwa ufanisi na kuleta tija. (Makofi)
MHE. FATMA H. TOUFIQ: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuuliza swali la nyongeza. Ni nini mkakati wa Serikali wa kupunguza kodi kwa malighafi ambazo zinatumika kutengeneza taulo za kike, ili taulo hizi sasa ziweze kutengenezwa shuleni kwa kupitia somo la maarifa ya jamii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea mawazo mazuri ya Mheshimiwa Mbunge na tutawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Fedha ili kuangalia masuala haya ya kikodi na kuona kinachoweza kufanyika. (Makofi)
MHE. NICODEMAS H. MAGANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Swali la kwanza; kwenye Wilaya ya Mbogwe kuna hizo barabara alizozitaja Mheshimiwa Naibu Waziri, kuna madaraja ambayo hayapitiki kabisa sasa hivi pamoja na kwamba nashukuru kwa majibu ya Serikali. Je, Serikali ina mpango gani wa kulitengeneza na Daraja la Ikalanga – Ilangale kwa sababu sasa hivi haipitiki na wakulima wamelima mazao mengi ambayo yanatarajiwa kutoka huko?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; mpango wa Serikali wa kuunganisha kwa kiwango cha lami wilaya na mkoa. Je, ni lini sasa Serikali itaitimiza ahadi hii ili kuunganisha Wilaya ya Mbogwe na Geita kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza Mheshimiwa Mbunge, naomba nitumie nafasi hii kumwagiza Meneja wa TARURA katika Wilaya ya Mbogwe ili aweze kwenda kufanya tathmini na kubaini kwamba barabara hiyo inahitaji kupatiwa fedha za dharura kwa ajili ya kuirekebisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kuunganisha wilaya na mkoa, tutaendelea kufanya tathmini na kuzingatia uhitaji na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi.
MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Mwakibete, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; tunaishukuru Serikali kwa kutenga fedha hizo kwa ajili ya kujenga daraja hili, lakini kutenga ni jambo lingine, kuanza ujenzi ni jambo lingine. Je, lini ujenzi utaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa katika Halmashauri ya Mji wa Mafinga kuna daraja kama hilo kutoka upande wa Isupilo kwenda Itimbo kufupisha njia ya watu wanaokwenda Iringa na kusafirisha mazao ya misitu. Je, Serikali iko tayari wakati ujao kututengea fedha ili na sisi tujenge daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu maswali ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na swali lake la kwanza ni kwamba, fedha imetengwa na dhamira ya Serikali ni kutekeleza miradi kwa kadiri bajeti inavyokuwa imetengwa. Kwa hiyo kwa kadiri fedha itakapokuwa inapatikana daraja hili litajengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili la kuhusiana na daraja katika jimbo lake. Nimwambie pia kazi kubwa ya TARURA ni kufuatilia na kuangalia sehemu zenye mahitaji na kupanga vipaumbele. Kwa hiyo kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na kwa kuzingatia vipaumbele daraja hilo litajengwa.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa kuwa daraja linalounganisha Kata ya Nkilizya na Kata ya Bukongo Jimboni Ukerewe limekuwa ni kilio cha muda mrefu na limekuwa linaathiri sana uchumi wa wananchi wa maeneo haya. Je, ni lini sasa daraja hili litajengwa kupitia Kijiji cha Msozi na Nkilizya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua umuhimu wa miundombinu hii na kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha Serikali itajenga miundombinu hii kwenye jimbo la Mheshimiwa Mbunge. Nashukuru.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri Daraja hili la Kiteputepu ni daraja ambalo linatumia mbao, linacheza na maji ni mengi sana. Wamesema kwamba wametenga na wataweka bajeti ili waweze kulifanyia kazi. Tunaomba Serikali ifanyie kazi haraka kwa maana wanawake wengi wanazama katika daraja hili pale Ntaba.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, napokea maombi ya Mheshimiwa Mbunge, tutayachakata na nitarudisha mrejesho kwake Mheshimiwa Mbunge.
MHE. DKT. ALICE K. KAIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, je, Serikali sasa haioni kuwa kuna haja ya kutumia wahitimu waliohitimu ufundi katika Miradi ya Force Account?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali haioni kuwa, kuna haja ya kushirikiana na taasisi za ufundi ili kusimamia miradi ya force account badala ya kutumia watumishi ambao hawana fani hizo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokea mawazo ya Mheshimiwa Mbunge, tutachakata maoni yake na tuone tunaweza vipi kuboresha ufanisi katika utekelezaji wa miradi hii.
MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Mji wa Tarime ina upungufu wa walimu wa sayansi na hesabu wapatao 83,000 lakini pia ina walimu wa sayansi na hesabu ambao wanajitolea 44 ambao ni takribani 53% ambao wamehakikiwa. Kwa sababu Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 na ukichukua sample ya Tarime Mji ina maana Tanzania nzima wana average zaidi ya walimu hao wanaojitolea ni zaidi ya 50%, sasa kwa nini Serikali katika hizo ajira 12,000 isitenge 50% kwa ajili ya walimu hao wanaojitolea ili kuendelea kutoa motisha zaidi kwa walimu wengi kuweza kujitolea na kupunguza uhaba wa walimu wa sayansi na hesabu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Shule ya Msingi Magufuli yenye wanafunzi wenye uhitaji maalum iliyopo Halmashauri ya Mji wa Tarime ambayo ni kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wa akili, ulemavu wa kuona na kusikia, ina upungufu wa walimu 13 ambao ni takribani 53%. Kwa nini Serikali isitoe kipaumbele kwa shule zote maalumu nchini kwa kuwa wote tunatambua ugumu uliopo wa kufundisha wanafunzi wenye ulemavu wa kusikia, kuona na akili? Serikali iweze kutoa kipaumbele na kupeleka walimu toshelezi katika shule hizi (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la walimu wanaojitolea kupewa kipaumbele katika ajira zilizotangazwa za walimu, maoni haya ya Mheshimiwa Mbunge tunayachukua na tutaona namna ya kuyachakata tulishirikiana na wenzetu wa Utumishi ili tuweze kuona ni namna gani nzuri tunazingatia miongozo na taratibu za kiutumishi katika kuajiri walimu hao.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo amezungumzia uhitaji wa kuajiri walimu wenye uhitaji maalumu, kwa mujibu wa taratibu katika kila ajira zinazokuwa zimetangazwa za walimu angalau asilimia tatu, ni lazima wawe ni walimu wanaofundisha wanafunzi wenye uhitaji maalumu. Mwaka 2023 Mei, ajira za mwisho za walimu tayari waliajiriwa walimu kwa 2.7% kwa sababu kwa kawaida wanaojitokeza huwa hata asilimia tatu hawafiki.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, watakaojitokeza, walimu watakaoomba nafasi hizo ambao wanakidhi vigezo vya kuwa walimu kwa ajili ya wanafunzi wenye uhitaji maalumu kwa mujibu wa taratibu watachukuliwa. (Makofi)
MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo kubwa la walimu, takwimu zilizopo, walimu wa sayansi ni walimu wa somo la physics. Je, Serikali ina mkakati gani wa makusudi kuhakikisha inaajiri walimu wa somo hilo ukizingatia tunaenda kwenye mafunzo ya amali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua umuhimu wa kuwa na walimu na hasa wanaofundisha masomo ya sayansi na kwa kila ajira zinapotangazwa, Serikali inajitahidi kuhakikisha kwamba inaajiri walimu wa sayansi. Kama tunavyofahamu, tayari zimetangazwa ajira za walimu 12,000. Kwa hiyo, Serikali itazingatia katika kuajiri walimu hao 12,000 wapatikane walimu wa sayansi na hasa wa somo la fizikia kama aliyotaja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza. Mkoa wa Simiyu kuna upungufu wa walimu zaidi ya 6,000 katika shule za sekondari na za msingi: Je, ni lini Serikali italeta walimu wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kutetea wananchi wake na kutetea na wanafunzi waliopo katika eneo lake la utawala. Aidha, Serikali tayari imeshatangaza ajira 12,000 kwa sababu inatambua upungufu wa walimu. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika ajira hizi za walimu 12,000 jimbo lake la lenyewe litatizamwa kwa kipaumbele. (Makofi)
MHE. MOHAMED SAID ISSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ipo tayari kuainisha aina ya michango hiyo ambayo imeruhusiwa kuombewa kibali?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, je, Serikali ipo tayari kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Shule kuwaruhusu wanafunzi ambao hawana uwezo wa kuchangia michango hiyo kwa wakati? Nakushukuru. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kama nilivyojibu kwenye majibu yangu ya msingi, Waraka wa Elimu Na. 3 wa mwaka 2016 umeeleza na umeweka utaratibu wa kuzingatiwa ili kuweza kupata kibali kwa ajili ya kuwepo kwa michango katika shule za msingi lakini katika shule za sekondari iwapo kuna uhitaji na katika waraka huo ni lazima kupata kibali cha Mkuu wa Wilaya, lakini michango hii ambayo tunaizungumzia hapa inaweza ikawa ni ile michango ambayo wazazi wenyewe kupitia mikutano ya wazazi na kamati za shule wanakubaliana, kwa mfano wanaweza wakasema wanataka wanafunzi wawe wanavipindi vya ziada, kwa hiyo wanakubaliana kutoa michango ya aina fulani, lakini michango mingine ni hii ambayo inafahamika ambayo ni michango ya uendeshaji wa shule ambayo kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi ukomo umewekwa kwa shule za bweni kidato cha tano ni shilingi 80,000 na kwa shule za kutwa ni shilingi 50,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba niendelee kusisitiza maagizo ambayo yametolewa huko awali kwamba Maafisa Elimu wa Mikoa, wa Wilaya, wa Kata, Wakuu wa Shule hawaruhusiwi kukataa kuwapokea wanafunzi kwa sababu tu wamekosa pesa za michango.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nisisitize hilo kwa sababu ni maelekezo ambayo tayari yalishatolewa, mwanafunzi asikataliwe kupokelewa shuleni kwa sababu amekosa pesa ya michango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba nichukue nafasi hii kutoa wito kwa wazazi wa wanafunzi wa kidato cha tano wale waliyochaguliwa kuingia kidato cha tano waweze kuhakikisha kwamba wanawapeleka watoto wao shule hata kama hawajakamilisha michango au kuwa na sare, ni muhimu sana watoto wanapochaguliwa kwenda kidato cha tano waweze kwenda shuleni kuripoti. (Makofi)
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, nina maswali mawili.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa madarasa mengi na nyumba za walimu nyingi zilizopo sasa hivi zilijengwa wakati wa mpango huu mkubwa wa Maendeleo ya Elimu ya Msingi (MMEM) na kwa kuwa kiasi kinachotengwa sasa hivi kwenye halmashauri zetu kwa ajili ya ukarabati na ukamilishaji wa maboma ni kidogo; je, Serikali haioni haja ya kutafuta fedha nyingi ili madarasa haya ambayo yamechakaa yaweze kukarabatiwa kwa kiasi kikubwa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili mpango huu wa MMEM ulihusisha na uboreshaji na uendeshaji wa vituo vya walimu (TRCs). Je, Serikali inampango gani wa kuendeleza vituo hivi ili walimu waweze kupata mafunzo kazini wakiwa katika maeneo yao ya kazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifanya kazi kubwa sana ya kufuatilia maslahi ya wananchi wake na hususani kwenye masuala pia ya elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza kama nilivyojibu kwenye majibu ya msingi, Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya ukarabati wa madarasa ambayo katika mwaka wa fedha 2022/2023 – 2023/2024 Serikali imetoa jumla ya shilingi bilioni 70.39 kwa ajili ya ukarabati wa shule 793 lakini kupitia miradi ya elimu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI miradi kutoka Wizarani, Serikali inatenga na imekuwa ikitoa fedha nyingi sana kwa ajili ya ukarabati wa shule zetu hizi kongwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, marekebisho ya shule hizi au ujenzi wa madarasa mapya unalenga kupunguza umbali wa wanafunzi kusafiri ili kufika mashuleni, lakini pia unalenga kupunguza msongamano.

Kwa hiyo, Serikali inaendelea kupitia mradi wa BOOST kutenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaendelea kukarabati shule kongwe, lakini kujenga madarasa mapya.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge kuhusu vituo vya walimu naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kupitia mradi wa GPETSP, mradi huu ambao upo kwenye awamu ya tatu umepanga kujenga vituo vya walimu 300 lakini mpaka hivi tunavyozungumza tayari kuna vituo vya walimu 252. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kutekeleza mradi huu na kuendelea kujenga vituo hivi muhimu vya walimu. (Makofi)
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Naibu Spika, Shule ya Sekondari Ngonga iliyopo Wilayani Kyela imejengwa tangu mwaka 2007 mpaka sasa haina nyumba hata moja ya walimu; sasa je, Serikali ni lini itajenga nyumba za walimu kwenye shule hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, kupitia Mradi wa GPETSP nilioutaja hivi punde, mradi huu pia unalenga katika kujenga nyumba za walimu, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ina mkakati na imetengeneza mipango ya kuhakikisha inaendelea kujenga nyumba za walimu katika maeneo mbalimbali nchini. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, Serikali itakuja kufika ijenge nyumba za walimu katika shule aliyoitaja ya Ngonga. (Makofi)
MHE. DKT. CHARLES S. KIMEI: Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali ipo tayari kuweka wazi mpango mkakati wa ukarabati shule kongwe zilizochakaa sana kwenye Wilaya ya Moshi Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imepanga kufanya ukarabati wa shule kongwe 50, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaweka katika kipaumbele ombi lake la kurekebishiwa au kufanyiwa marekebisho katika shule kongwe aliyoitaja katika jimbo lake.
MHE. JOSEPH M. MKUNDI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; kwa kutambua changamoto za kijiografia ambazo zimekuwa zinaathiri utendaji na kupata wakandarasi bora kwenye maeneo ya pembezoni kama Ukerewe, mwaka jana Serikali iliniahidi kutupatia vifaa vya ujenzi kama magreda na kadhalika kwa ajili ya kuondoa changamoto hiyo. Nataka kujua na Wakerewe wanataka kujua hatua ipi imefikiwa?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa pesa za mafuta kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji kwa TARURA zinapelekwa mkoani jambo ambalo limekuwa linaathiri wahandisi wilayani kufuatilia hasa inapotokea dharura. Ni upi sasa mkakati wa Serikali kufanya marekebisho ya utaratibu huu? Nashukuru sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, ni kweli Serikali ilitoa ahadi ya kupeleka magreda na vifaa mbalimbali vya ujenzi wa miundombinu ya barabara na ahadi hii mpaka sasa bado haijatekelezwa. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inatambua umuhimu wa upatikanaji wa vifaa hivi katika jimbo lake na inafanya taratibu za upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kununua vifaa hivyo ili viweze kupelekwa. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itatekeleza ahadi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili, Serikali inatambua changamoto aliyoiainisha Mheshimiwa Mbunge kuhusiana na upatikanaji wa fedha kwa wakati kwa ajili ya TARURA kuweza kutoa huduma zake kwa dharura. Kwa muktadha wa suala hili analozungumza Mheshimiwa Mbunge, Serikali itaendelea kuhakikisha inasimamia upatikanaji wa fedha za TARURA kutoka Serikali Kuu lakini kutoka katika Serikali ya Mkoa zinapatikana kwa wakati ili kuweza kutimiza mahitaji ya ujenzi wa barabara kwa dharura. Ahsante. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa ahadi ya Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni kuongeza milioni 500 kuwa bilioni moja katika Barabara za TARURA, je, ni lini fedha hizo zitatoka?

Mheshimiwa Spika, pili, kwa kuwa barabara nyingi zimekatika kutokana na athari za mvua ikiwemo Chiwale, Masasi Mkoani Mtwara. Je, Serikali ina mpango gani kupitia TARURA wa kuhakikisha barabara hizo zinapitika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali iliahidi kweli kuongeza bajeti kutoka shilingi milioni 500 mpaka shilingi bilioni 1.5 na Serikali ina nia ya kutekeleza ahadi hiyo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri ya upatikanaji wa fedha, Serikali itaweza kutimiza ahadi hii na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitalifuatilia suala hili. Tukitoka hapa tunaweza tukakutana tukazungumza ili kujua mustakabali wa masuala ya wananchi wa Geita Mjini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, Serikali imeendelea kutenga bajeti ya kutosha na hivi sasa bajeti ya TARURA imetoka shilingi bilioni 272 na imeongezwa mpaka shilingi bilioni 710. Ni ongezeko kubwa, lakini tunatambua kwamba bado kuna mahitaji zaidi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri pesa zinavyopatikana Serikali inatambua umuhimu wa barabara hizi za TARURA na hasa kwa sababu zinagusa ustawi wa wananchi lakini pia zinagusa ustawi wa uchumi. Kwa hiyo, kwa kadri fedha zitakavyokuwa zinapatikana Serikali ina nia ya kuhakikisha barabara hizi zinajengwa na zinafanyiwa ukarabati. Ahsante. (Makofi)
MHE. BENAYA L. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante na nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, hata hivyo, nina maswali madogo mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; hii Kata ya Ngima wananchi kwa kushirikiana na mimi Mbunge tumejenga tayari madarasa manne. Je, Serikali iko tayari kutenga fedha japo kidogo kukamilisha madarasa haya ili yaweze kutumika mwakani Januari?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; wananchi wa Kata ya Matiri pamoja na Kata ya Nguzo nao wamejenga Shule ya Sekondari Nguzo pamoja na Benaya Sekondari hazina miundombinu ya kutosha. Je, Serikali iko tayari kupeleka fedha kukamilisha miundombinu ya shule hizi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali ina nia ya kuendelea kuboresha miundombinu ya shule na hivyo kwa kadri ya upatikanaji wa fedha Serikali itaweza kujenga madarasa hayo aliyoyataja Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili, Serikali inatambua jitihada ambazo zimefanywa na wananchi wa Mbinga DC za kujenga Shule ya Sekondari ya Benaya na Nguzo na shule hizo tayari zimeshasajiliwa na zina wanafunzi mpaka kidato cha pili. Kwa kuzingatia miundombinu ambayo bado haijakamilika katika shule hizo, Serikali kupitia bajeti ya halmashauri ya 2024/2025 imepanga kutumia shilingi milioni 62.5 kwa ajili ya shule hizo. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kufanya tathmini ya ukamilishwaji wa miundombinu ya shule hizo ili kuongeza fedha kulingana na upatikanaji wake kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ujenzi wa shule hizo unakamilishwa na kuunga mkono jitihada za wananchi. Ahsante. (Makofi)
MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri sana ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, je, ni lini Serikali itapeleka gari la usimamizi wa huduma katika Halmashauri ya Uyui ambayo ina majimbo mawili Tabora Kaskazini na Igalula?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na jiografia kati ya vituo hivi vya afya, mfumo wa kutumia gari moja la Kaskedi hautofanya kazi vizuri, je, ni lini Serikali itapanga kupeleka magari mawili katika Kituo cha Afya cha Upuge na Kituo cha Afya cha Mabamba?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, magari 70 yaliyokuwa yamebaki ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za afya tayari yameingia nchini na Serikali inaendelea na utaratibu wa kuyatoa magari haya bandarini na hatua nyingine za usajili wa haya magari. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba magari haya yakitoka, Halmashauri ya Uyui na yenyewe itapata gari moja.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge nimhakikishie kwamba kama Serikali ilivyotenga pesa kununua magari ya kusafirishia wagonjwa na kuweza kuyaleta katika jimbo lake. Nimhakikishie kwamba Serikali itaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza magari ya wagonjwa kwa ajili ya kuhudumia katika Vituo vya Afya vya Upuge na Mabamba kama alivyoomba. (Makofi)
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana, Serikali tayari imejenga vituo vitatu vya afya katika Tarafa zilizopo Mbulu Mjini. Je, Serikali ina mpango gani wa kuvipatia gari la wagonjwa vituo hivi vyote vitatu vya Jimbo la Mbulu Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu awali kwamba Serikali itahakikisha inatafuta pesa ili iweze kupata magari ya kuhudumia wagonjwa na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kwa kadiri fedha itakavyokuwa inapatika na magari haya kununuliwa, basi yanaweza yakaja kuletwa kwenye vituo vya afya ulivyoomba.
MHE. SUMA I. FYANDOMO: Mheshimiwa Spika, suala la magari linaendana na watumishi wanaohusika kwenye hospitali. Sasa je, ni lini Serikali itapeleka madaktari kwenye Hospitali ya Wilaya ya Chunya maana hospitali nzima ina madakari wawili na mahitaji ni madkatari nane? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imekuwa ikitoa vibali vya ajira kwa ajili ya ya kuajiri watumishi katika kada ya afya na kila mwaka imekuwa ikiajiri watumishi hawa.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa katika mwaka huu wataajiriwa na katika mwaka ujao wa fedha wataendelea kuajiriwa ili waweze kuhudumia katika vituo vyetu vya kutoa huduma ya afya ya msingi.
MHE. HASSAN Z. KUNGU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, tunaishukuru Serikali kwa kuipatia Hospitali ya Wilaya ya Tunduru gari la utawala, je, ni lini Serikali itaipatia gari la wagonjwa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutafuta fedha za kuhakikisha inanunua magari ya kuwahudumia wagonjwa na kuyapeleka katika maeneo mbalimbali ya kutolea huduma ya afya msingi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba magari haya yakipatikana na yeye ataangaliwa kwa jicho la kipaumbele kwenye jimbo lake.
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, Kitomanga ni miongoni mwa kituo cha afya ambacho hakina magari. Je, kati ya magari hayo 70 Kitomanga itakuwa ni miongoni mwake?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu la msingi kwamba magari 70 ndiyo yaliyokuwa yamebaki na tayari mpaka muda huu yamefika na yapo bandarini yanaendelea na taratibu za kutolewa na kufanyiwa usajili. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba na wao watapata gari hili la usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za afya. (Makofi)
MHE. EDWIN E. SWALLE: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Mtwango ni kituo cha afya kikubwa sana ambacho kinahudumia Kata ya Kichiwa, Igongolo, Ikuna na Mpakaninga lakini hawana gari la ambulance kwa ajili ya wagonjwa. Ni upi mpango wa Serikali wa kupeleka ambulance Mtwango?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuhakikisha inatafuta fedha kwa ajili ya kununua ambulance. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadri fedha zitakavyopatikana na magari haya ya kuhudumia wagonjwa yatakaponunuliwa nimhakikishie kwamba Kituo cha Afya cha Mtwango na chenyewe kitapewa mgao wa magari haya.
MHE. HASSAN S. MTENGA: Mheshimiwa Spika, kwanza niishukuru Serikali kwa majibu mazuri ya ujenzi huo wa ofisi.

Swali la nyongeza, kwa kuwa Serikali ilitoa fedha nyingi sana kwenye ujenzi huo na majibu ambayo nimeyapata ni mazuri, lakini niiombe Serikali kwa sasa bado hali haijawa nzuri kwenye miundombinu ambayo imebakia.

Je, ni lini Serikali mtaikamilisha ile miundombinu kwa sababu kituo kile tayari kimekwishaanza kutumika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa Serikali imeamua kuleta huduma kule chini kwa wananchi, tunayo Kata moja ya Chikongola ambayo ina Kata moja ya Magomeni katika Jimbo la Mtwara mjini ina watu zaidi 29000.

Ni lini Serikali itatuletea kituo cha afya ili kuboresha huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali imefanya tathmini na kubaini kwamba zinahitajika shilingi milioni 883.7 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la utawala, lakini inahitaji milioni 176 kwa ajili ya ukamilishaji wa jengo la hospitali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imetengeneza mikakati na ukamilishaji wa majengo hayo yapo katika mpango wa Serikali na Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha inakamilisha majengo haya muhimu.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili Mheshimiwa Mbunge linahusu uhitaji wa kituo cha afya kuhudumia idadi kubwa ya wananchi 29,000 nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake hili la Mtwara Mjini tayari Serikali imepokea maombi ya ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati na Mheshimiwa Mbunge na yeye ameleta eneo lake mahsusi ambalo anaona kwamba linahitaji ujenzi wa kituo cha afya na bila shaka eneo hilo kwa kauli ya Mheshimiwa Mbunge ndio hili aliloliombea hapa fedha.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika mipango ya upatikanaji wa fedha wa kujenga vituo vya afya vya kimkakati tutazingatia maombi yake ili kituo cha afya kiweze kujengwa.
MHE. ESTHER L. MIDIMU: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Bariadi Somanda ni ya kwanza kabisa kujengwa katika Mkoa wa Simiyu lakini haina jengo la ICU, ni lini Serikali itatuletea fedha tujenge jengo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama vile Serikali ilivyoanza kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa majengo mengine katika hospitali hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imetenga fedha katika mwaka wa bajeti 2024/2025 kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi viporo ya hospitali za halmashauri. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge fedha itakuja kwa ajili ya kuendelea kukamilisha na ujenzi wa jengo hilo la ICU.
MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ya Tanganyika haina fence kwenye majengo yake. Ni lini Serikali itapeleka fedha kukamilisha ujenzi wa fence ya hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia umuhimu mkubwa sana wa miundombinu aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia Serikali Kuu, lakini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kunajengwa uzio huo katika hospitali aliyoitaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. ABDALLAH D. CHIKOTA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwa kuwa Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Nanyamba ina nyumba moja tu ya daktari, je, Serikali ina mpango gani wa kuongeza nyumba za madaktari ili watumishi hawa wakae karibu na hospitali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu mkubwa sana wa nyumba za watumishi na hasa katika kada ya afya, Serikali itaendelea kutenga fedha kupitia Serikali Kuu, lakini kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa maana ya mapato ya ndani ya halmashauri kuhakikisha kwamba inajenga nyumba za watumishi ili waweze kuwa karibu na vituo vya kutolea huduma ya afya ya msingi na kuweza kuwahudumia wananchi kwa ukaribu.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Spika, nashukuru, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Myula, Wilaya ya Nkasi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, Serikali inaendelea kutafuta fedha kuhakikisha vituo vya afya vyote ambavyo Waheshimiwa Wabunge waliorodhesha kwamba ni vituo vya kimkakati vinaweza kujengwa.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha na kama kituo alichokitaja ni kituo cha kimkakati katika eneo analotoka nimhakikishie Serikali itahakikisha inapata fedha kwa ajili ya kujenga kituo hicho cha afya.
MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, ahsante ninayo maswali madogo mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Vituo vya Afya vya Kharumwa na Nyang’hwale vina uhitaji mkubwa, je, uko tayari kumwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ili atenge fedha kupitia mapato ya ndani kuweza kujega majengo ya x-ray machine hizo?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, lini Serikali itapeleka mashine ya x-ray katika Manispaa ya Mpanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kama tunavyofahamu D by D yaani ugatuzi wa madaraka kutoka Serikali Kuu kwenda kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa inazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa na zenyewe kutafuta mapato na kuweza kuweka katika mipango na bajeti zake kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali na ujenzi wa miundombinu muhimu. Kama alivyotaja Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna umuhimu mkubwa sana wa kuwa na chumba au jengo mahsusi kwa ajili ya matumizi ya mashine hizi za x-ray.

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kumwagiza Mkurugenzi kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mkurugenzi aweze kuweka katika mipango ya kibajeti na waweze kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kujenga majengo haya ili mashine hizi za x-ray ziweze kuanza kuwanufaisha wananchi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, nimhakikishie kwamba katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 66.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaweka ombi lako katika kipaumbele ili na wewe kituo chako kiweze kupata mashine ya x-ray.
MHE. ASIA A. HALAMGA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi, je, ni lini Serikali itapeleka mashine ya x-ray katika Vituo vya Afya vya Hirbadau, Mogitu pamoja na Bassotu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 66.7 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wewe vituo vyako hivi vya afya vitakuwa katika mgao wa manunuzi ya vifaa tiba. Kwa hiyo, utapata mashine hii ya x-ray.
MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Halmashauri ya Arusha DC katika Jimbo la Arumeru Magharibi tumeomba x-ray kwa maandishi kupitia Wizara. Je, ni lini sasa Serikali itapeleka x-ray kwenye hospitali hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa sababu Serikali imeshatenga bajeti ya vifaa tiba shilingi bilioni 66.7 katika mwaka wa fedha 2024/2025 nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge maombi yake yamepokelewa na yatachakatwa, na yeye atakuwa kwenye mgao wa manunuzi ya vifaa tiba hivi ikiwemo hiyo x-ray machine.
MHE. FRANCIS K. NDULANE: Mheshimiwa Spika, vituo vyote sita vya afya katika Wilaya ya Kilwa havina mashine za x-ray. Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka mashine za x-ray katika vituo hivyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kadiri ya fedha itakapokuwa imepatikana na kwa kuzingatia bajeti iliyopangwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali itaanza kununua vifaa tiba mbalimbali ikiwemo mashine za x-ray. Kwa hiyo, wakati wa ugawaji wa vifaa hivyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaangalia na itaona vipaumbele, lakini itaweza kununua vifaa tiba na yeye atakuwa kwenye mgao.
MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, je, ni lini Serikali itapeleka x-ray machine katika Kituo cha Afya cha Mabamba kilichopo katika Jimbo la Muhambwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA, RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali tayari imeshatenga bajeti kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na kwa kuwa Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025 itanunua vifaa tiba, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumepokea maombi yake kwa ajili ya kuona ni namna gani tunaweza tukanunua vifaa tiba ikiwemo hiyo x-ray machine aliyoiomba.
MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali nina maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wana utaalamu wa kuanzisha vikundi na kuvisimamia kwa nini wasibaki huko kwenye kusimamia vikundi tu?

Mheshimiwa Spika, lakini pia tuna Maafisa Masoko na Biashara ambao wako kwenye halmashauri na wana utaalamu wa mikopo kwa nini hawa wasisimamie mikopo na kutoa mikopo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, vikundi vyetu hivi vinavyoundwa katika halmashauri vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu havijishughulishi na biashara peke yake, lakini vinajishughulisha na shughuli nyingine za miradi kama ya kilimo, ufugaji, utoaji wa huduma za afya, habari na teknolojia. Kwa hiyo hawa maafisa maendeleo ya jamii kazi yao kimsingi ni uratibu na wanashirikiana na wataalamu katika kila sekta wakiwemo hao maafisa biashara, wakiwemo maafisa kilimo, maafisa mifugo, wataalamu wa afya na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii ni maafisa mahususi kabisa kwa ajili ya kufanya hii kazi, lakini zaidi ya hapo pia umuhimu wa kuwatumia hawa maafisa maendeleo ya jamii ni kwa sababu wapo pia katika kila kata yaani muundo wao wapo katika kila kata na hivi vikundi vinavyoundwa vipo katika ngazi ya kata na vijiji, lakini ukiangalia maafisa biashara wenyewe muundo wao unaanzia katika ngazi ya halmashauri. Kwa hiyo, tafsiri yake hawa Maafisa Maendeleo ya Jamii wanakuwa ni maafisa bora zaidi na mahsusi kwa ajili ya kufanya uratibu kwa kushirikiana na wataalamu kwa ajili ya kufanya kazi ya vikundi hivi.
MHE. JONAS V. ZEELAND: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.
Swali la kwanza, kwa kuwa tuna upungufu mkubwa sana wa watumishi hasa kwenye vituo vya afya na zahanati zilizopo pembezoni, je, lini Serikali itatuongeza watumishi ili kuweza kupunguza kero hii ya watumishi iliyopo sasa hivi katika vituo vyetu na zahanati?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, sera ya afya imeweka wazi kwamba kila kijiji lazima kiwe na zahanati na kila kata lazima kuwe na kituo cha afya. Mimi pamoja na wananchi wangu wa Mvomero tumeshajenga maboma zaidi ya kumi, je, lini Serikali itatupatia fedha kwa ajili ya kumalizia haya maboma ambayo tumejenga wenyewe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu mkubwa sana wa watumishi wa kada ya afya katika kuhakikisha huduma bora inawafikia wananchi katika vituo vya kutoa huduma ya afya msingi, tayari Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuajiri watumishi wa kada ya afya na katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali iliajiri watumishi wa kada ya afya 33, mwaka 2022/2023 Serikali iliajiri watumishi wa kada ya afya 36 na mwaka 2023/2024 Serikali imeajiri watumishi wa kada ya afya 48 katika Jimbo la Mvomero.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha inaajiri na kunakuwa na watumishi wa kada ya afya ili waweze kutoa huduma zilizo bora katika vituo vyetu vya kutolea afya msingi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili ambalo anaeleza kwamba ameweza kuwashirikisha wanchi wake katika kujenga maboma ya zahanati, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali inatambua jitihada kubwa ambayo imefanyika katika ujenzi wa maboma haya na tayari Serikali imefanya tathmini na kubaini kwamba kuna maboma ya zahanati 1,265 ambayo yatahitaji jumla ya shilingi bilioni 75.9 kuyakamilisha.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali imeweka mikakati ya kutafuta na kupata fedha kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za wananchi. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali ipo kazini na itahakikisha inatafute fedha ili kujenga maboma hayo uliyoyataja ambayo yako katika jimbo lako.
MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, Kata ya Ilangu ni kata ya kimkakati, je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya katika Kata ya Ilangu Wilayani Tanganyika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kutumia mwongozo na maoni ya Waheshimiwa Wabunge Serikali tayari ilishaainisha vituo vya afya vya kimkakati vya kujenga katika kila jimbo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kama kituo hiki alichokitaja katika Kata ya Ilangu ni miongoni mwa vile vituo vya afya vilivyoainishwa vya kimkakati nimhakikishie Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha inaenga vituo vya afya hivyo vya kimkakati.
MHE. JUSTIN L. NYAMOGA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, ni lini Serikali itamalizia majengo ya zahanati katika Kijiji cha Iyayi, Uhominyi Nyawegete, Kitoho na Winome ambayo tayari yameshapauliwa na yako katika hatua za umaliziaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali inatambua umuhimu sana wa huduma ya afya msingi na imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha inajenga miundombinu kwa ajili ya kutoa huduma hii ya afya msingi, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutafuta fedha ili iweze kukamilisha miradi ambayo tayari imeanza ikiwemo mradi alioutaja Mheshimiwa Mbunge.
MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi hii niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kabwe kimekuwa kinatolewa kauli tofautitofauti juu ya umaliziaji wake, leo nataka kusikia kwa mara ya mwisho, ni lini mtakamilisha kituo hiki ili kianze kufanya kazi?

SPIKA: Mheshimiwa Aida Khenani kinaitwa nini ili siku nyingine ukiuliza tukukumbushe ulisema leo ni mara ya mwisho.

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Kabwe, leo ni mara ya kumi nauliza.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ilishakusanya vituo vya afya vya kimkakati vya kujengwa katika mwaka wa fedha 2024/2025 bila shaka Mheshimiwa Mbunge ulileta kituo hiki kukiombea fedha kujengwa katika mwaka wa fedha huu. Nikuhakikishie Serikali inatafuta fedha kuhakikisha kwamba vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo yote vinajengwa na kama hiki kituo ni kituo ambacho wewe ulikileta kwamba ni kituo cha kimkakati nikuhakikishie Serikali inatafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho
MHE. MASACHE N. KASAKA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kuniona, Kituo cha Afya cha Mji Mdogo wa Makongolosi kimekamilika na kimeanza kutoa huduma, lakini hakina nyumba za madaktari. Chama Cha Mapinduzi Kata ya Bwawani Makongolosi wameanzisha ujenzi wa nyumba za madaktari.
Je, ni lini sasa Serikali itatoa fedha ili nyumba hizi za madaktari ziweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kuwapongeza wananchi kwa kushirikiana pamoja kuhakikisha kwamba wanaunga mkono jitihada za maendeleo na kwa kuanza ujenzi wa miundombinu hii muhimu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama vile ambavyo Serikali imekuwa ikiunga mkono jitihada mbalimbali za kuboresha miundombinu na hasa katika sekta ya afya na kuunga mkono tafsiri yake ni kupitia miradi kutoka Serikali Kuu, lakini pia kupitia Mamlaka za Serikali za Mitaa. Kwa hiyo, nikuhakikishie Serikali kwa utaratibu huo huo itaendelea kuhakikisha kwamba fedha zinapatikana kwa ajili ya kuunga mkono miradi ambayo inaenda kugusa miundombinu muhimu ya afya.
MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Halmashauri hii ya Manispaa ya Mtwara Mikindani kwa kweli ina changamoto kubwa sana. Mfano, hapa ninapozungumza kuna baadhi ya shule ina mwalimu mmoja tu wa chemistry, kuna baadhi ya shule ina mwalimu mmoja tu wa physics...

MWENYEKITI: Uliza swali.

MHE. YAHYA A. MHATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haioni kwamba wakati umefika, katika huu mgao wa walimu, Halmashauri hii ya Mtwara Mikindani ikapewa kipaumbele zaidi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, nakwenda kwenye Halmashauri yangu ya Nanyumbu. Katika halmashauri hii, hali ndiyo mbaya zaidi ya huko. Hapa ninapozungumza, hata ufaulu wa wanafunzi ni mbaya. Mfano katika mitihani iliyopita kati ya wanafunzi 998 ni wanafunzi 19% tu ndiyo waliofaulu masomo ya sayansi. Je, Serikali haioni haja sasa kwa hii Mikoa ya Kusini ikapewa kipaumbele kupatiwa walimu wa sayansi ili vijana nao wapate haki ya kusoma masomo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu mkubwa wa walimu katika Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, mwaka huu Serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000. Sasa katika mgao huo, Serikali itaweka jicho la kipekee katika jimbo hili kwa ajili ya kuhakikisha kwamba walimu hao wanaweza kupatikana ili kupunguza upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili, naomba nimjibu Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inafahamu umuhimu wa kuwa na walimu na hasa walimu wa masomo ya sayansi na kwa sababu Serikali tayari inaajiri walimu 12,000, kwa hiyo, itaangalia jimbo lako kwa jicho la pekee ili kuona kwamba walimu wanapatikana ili kupunguza ukali wa upungufu kwenye jimbo lako. (Makofi)
MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Zipo halmashauri ambazo zina uwezo wa mapato na zina uwezo wa kuajiri walimu. Je, Serikali ina mpango gani wa kugatua suala la ajira ya walimu liende kwenye halmashauri ambazo wanaweza wakaajiri na wakaweza kuwalipa walimu badala ya kusubiri mgao wa kitaifa? Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Rais, TAMISEMI pamoja na mambo mengine inasimamia suala la ugatuzi kwa maana ya D by D na inapenda sana kuona halmashauri zinaweza kuwa na uwezo na ubunifu wa kutengeneza mapato makubwa ya ndani na kuweza kujiendesha zenyewe. Kwa hiyo, mawazo ya Mheshimiwa Mbunge ni mawazo mazuri, tunayachukua sisi kama Serikali, tutayachakata na tunaamini kwamba yataweza kutekelezeka.
MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Jina langu ni Kikoyo siyo Chikoyo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kikoyo.

MHE. DKT. OSCAR I. KIKOYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la nyongeza. Wilaya ya Muleba tumejenga zaidi ya shule 30 mpya, lakini walimu wamebaki wale wale. Serikali ina mpango gani mahususi kwa Wilaya ya Muleba kutupatia walimu wa ziada?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua kwamba kumekuwa na shule nyingi mpya ambazo zimejengwa ambazo zina uhitaji mkubwa wa walimu. Tayari Serikali imeanza mikakati mbalimbali ikiwemo kufanya msawazo wa walimu kutoka kwenye shule zile za zamani kuwahamishia kwenye shule hizi mpya. Pia Serikali inatumia njia ya kuajiri walimu ili kufidia upungufu katika maeneo ya shule hizi mpya na hata zile shule za zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Serikali itaendelea na mikakati hii ili kuhakikisha shule zote zinazojengwa zinaweza kupata walimu ili wanafunzi waweze kupata elimu iliyo bora.
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa hii fursa. Shule ya Sekondari Indoombo ina walimu watano tu. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha ili kukidhi uwiano unaokubalika kitaifa na kimataifa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu mwaka huu tuna ajira mpya za walimu, kwa hiyo, katika mgao ule tutaangalia kipekee pia kwenye jimbo lake naye aweze kupata mgao wa walimu hao.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali imeanza kupeleka maabara za kompyuta kwenye shule zetu za sekondari nchini: Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa wale walimu wanajengewa uwezo ili kompyuta hizi ziweze kufanya vizuri zaidi na wanafunzi waweze kupata uelewa wa kutosha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba pamoja na ujenzi wa miundombinu na kupatikana kwa vifaa mbalimbali muhimu katika elimu, pia itawajengea uwezo walimu wake ambao wote wanatoa huduma kwa wanafunzi. Kwa hiyo, Serikali itaendelea kuhakikisha hilo.
MHE. BUPE N. MWAKANG’ATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa masomo ya sayansi katika Mkoa wa Rukwa hususan Shule ya Sekondari ya Mazwi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Serikali katika mwaka huu wa fedha itaajiri walimu 12,000, kwa hiyo katika mgao wa walimu hawa Serikali itaweka jicho la kipaumbele na la kipekee kwenye maeneo yenye upungufu mkubwa ikiwemo katika shule zilizopo katika Mkoa wa Rukwa.
MHE. DKT. DAVID M. DAVID: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naishukuru Serikali kwa kuanzisha mpango huo wa kuweka zege kwenye barabara za milimani kwa sababu wanapoweka vifusi pindi mvua inaponyesha barabara zile zinazolewa na tunatia hasara Serikali na wananchi wanashindwa kupita, hata hivyo na maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Barabara za Msanga – Chome – Ikokoa – Makanya – Tae – Suji na Barabara ya Kisiwani hadi Msindo zina maeneo makorofi mengi sana, je, Serikali haioni kwamba umefika wakati wa kutenga bajeti ya kutosha kusudi barabara hizi zitengenezwe kwa kiwango cha zege ili tuweze ku-save hela za Serikali zinazotokana kumwaga vifusi ambavyo vinazolewa na mvua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, ningependa kumuuliza Mheshimiwa Waziri ni lini yuko tayari kutembelea Jimbo hili na kuziona hizi Barabara za Chome, Barabara za Makanya – Tae pamoja na Kisiwani – Msindo ili aweze kuona umuhimu wa kutenga fedha za kutosha haraka iwezekanavyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana na nianze kwanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kutetea wananchi wake. Kuhusiana na swali lake la kwanza ambalo ameuliza baadhi ya barabara Serikali ina mkakati gani wa kuzijenga kwa tabaka la zege na hasa kwenye maeneo korofi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Barabara ya Msanga – Chome – Ikokoa katika mwaka wa fedha huu wa 2023/2024 zimetengwa shilingi milioni 267.15 kwa ajili ya kujenga meta 100 kwa kiwango cha zege kwenye eneo korofi, lakini pia kwenye eneo hatarishi la Mlima wa Chome imejengwa strip concrete ya meta 350, lakini katika mwaka wa fedha ujao 2024/2025 Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 74.9 kwa ajili ya kujenga kwa kiwango cha zege meta 180 kwenye eneo hatarishi la Mlima Ikokoa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu Barabara ya Makanya – Tae – Suji Serikali imetenga katika mwaka wa fedha 2024/2025 milioni 161.18 kwa ajili ya kujenga kwa tabaka la zege urefu wa meta 100 kwenye eneo la Mgwasi – Tae, lakini pia ujenzi wa driffs nne za meta 32 na kwenye Barabara ya Kisiwani – Msindo, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali ilitumia shilingi milioni 250 kwa ajili ya kujenga meta 500 za strip concrete. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendelea kujenga kwa kiwango cha zege kwenye maeneo hatarishi, kwenye barabara zake hizi ili ziweze kupitika kipindi chote cha mwaka mzima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakaa mimi na yeye tutazungumza, tutapanga ratiba vizuri nipo tayari kutembelea Jimboni kwake kuangalia miundombinu hii ya barabara ili tuweze kuona umuhimu wa kuendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuzikarabati na kuzijenga vizuri. (Makofi)
MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali inaendelea kufungua barabara za mitaa kwenye Makao Makuu ya Wilaya ya Nyang’hwale pale Kharumwa kwa kiwango cha udongo. Je, Serikali ina mpango gani kuziwekea mpango wa kuweka changarawe na baadaye lami hizo barabara za mitaa Kharumwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba inaweza kuzihudumia barabara za wilaya kwa kiwango cha lami, lakini kama wote tunavyofahamu tunaanza. Kwa hiyo, tayari Serikali imeanza kuhudumia barabara hizi kwa viwango tofauti ikiwemo viwango vya changarawe, lakini mwisho wa siku hatimaye tunataka barabara zetu zote hizi za wilaya ziwe kwa kiwango cha lami ambacho kitafanya barabara ziweze kudumu kwa muda mrefu na ziweze kupitika mwaka mzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itaendelea kutenga fedha kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara zetu hizi za wilaya na hususan pia kwenye Jimbo lako Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)
MHE. DKT. JOHN D. PALLANGYO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali la nyongeza.

Mheshimiwa mwenyekiti, changamoto za barabara za Mlimani kule Same Magharibi zinafanana sana na hali ilivyo kule kwetu Meru na nimeishalisema hapa mara nyingi. Kwa hiyo, sasa niulize Serikali inatoa tamko gani kuhusu barabara za milimani kule Arumeru Mashariki? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akipambania sana suala la Ujenzi wa barabara kwa viwango vitakavyodumu hasa katika Jimbo lake ambalo lina milima. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa sababu tayari tumeshazungumza na suala tayari lipo kwenye michakato na fedha tayari zimeshatengwa, nikuhakikishie Serikali itakuja kujenga barabara, itatenga fedha kila mwaka kuhakikisha kwamba inaboresha miundombinu ya barabara hizi na hasa katika jimbo lako ambalo ni la milima. (Makofi)
MHE. KATANI A. KATANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Luagara kwenda Liponde kilometa 1.5 ilishafanyiwa feasibility study na watu wa TARURA na walishaweka kwenye bajeti miaka miwili nyuma, ni lini sasa Serikali itakwenda kuweka lami kipande kile?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu barabara hii tayari imeshafanyiwa usanifu na tayari ipo kwenye bajeti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, tutafuatilia kwa karibu hata baada ya kutoka kwenye maswali hapa tutakaa tutafuatilia kwa karibu ili tuhakikishe kwamba mwaka huu kwa sababu fedha tayari imeishatengwa ili iweze kujengwa barabara hii.
MHE. EMMANUEL L. SHANGAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali nina swali moja la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, okay kwa kuwa sasa ujenzi wa shule umefikia 85%, ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi huo pamoja na nyumba za watumishi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mbunge kwa swali hili zuri sana kwa maslahi ya watoto wote wa kike ambao watasoma kwenye shule hizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha mwaka 2023/2024 Serikali itapeleka shilingi bilioni 1.1 katika shule zote zile 16 za wasichana ambazo zilipelekewa shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa kumi, lakini chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu na mabweni manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itapeleka fedha hii kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza kuzitumia.
MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana naomba unipe fursa nimpongeze sana Rais wa Nchi Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuliona hili kwa ajili ya wasichana. (Makofi)

Naomba kuuliza swali je, katika shule hizo zinazoenda kujengwa ambazo ni za sayansi, wamezingatia kutupatia lab technicians? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika ujenzi wa hizi shule kama nilivyotangulia kusema awali ukiacha majengo tu ya madarasa, lakini kutakuwa kuna chumba cha TEHAMA, kutakuwa na maktaba, nyumba za walimu na mabweni. Kwa hiyo, chumba cha TEHAMA kitakuwepo na kwa sababu msingi ni kuhakikisha kwamba shule hizi zinatoa elimu iliyobora kwa watoto wa kike, wakati wa kutoa watumishi yaani wakati wa kuajiri na kupanga watumishi kwa ajili ya kuhudumia shule hizi lazima Serikali tutazingatia ili hiki chumba cha TEHAMA kipate matumizi kiwe kina lab technicians.
MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Rungwe tuna shule nzuri sana ya wavulana. Tunashukuru Serikali kwa kuikarabati ni lini mtatujengea shule ya wasichana katika wilaya hiyo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi shule hizi zipo 26 ziko kwenye Mradi wa SEQUIP na kila mkoa inapata shule moja ya wasichana, ya bweni na ni ya sayansi. Kwa hiyo, Mkoa wa Mbeya tayari una shule moja kwa hiyo hatutojenga katika kila kata, ni shule maalum Mheshimiwa Rais amehakikisha ametenga fedha kwa ajili ya kuhakikisha kila mkoa unapata shule hii ya bweni ya wasichana ya sayansi. (Makofi)
MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuliona hili na kujenga na kutupatia hizo shule 26 katika nchi yetu ya Tanzania na mkoani kwetu Lindi hasa kwenye Jimbo langu kuwa ni miongoni mwa zile shule za kwanza ambazo zimejengwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watoto wa kike wanahitaji ulinzi, je, ni lini mtatupatia pesa kwa ajili ya uzio kwa ajili kuwalinda watoto hawa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa sababu amekuwa akitetea sana, sana, sana maslahi ya watoto wa kike kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake kama nilivyotangulia kujibu katika swali la nyongeza hapo awali Serikali italeta na itapeleka shilingi bilioni 1.1 kabla ya mwisho wa mwaka huu wa fedha kuisha, mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili ya kukamilisha miundombinu yote ya msingi katika shule hizo ambazo zilipewa fedha katika awamu ya kwanza, kwa sasbabu shule hizi 16 ikiwemo shule ambayo imejengwa Mkoa wa Lindi zilipokea shilingi bilioni tatu awamu ya kwanza na sasa zitapokea mwaka huu shilingi bilioni 1.1 awamu ya pili kwa ajili ya ukamilishaji wa miundombinu yote ya msingi.
MHE. ISSA J. MTEMVU: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, naomba niulize maswali mawili yenye kifungu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2021/2022 ilishawahi kutengwa shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa daraja hili la kivuko hiki, lakini haijatekelezwa. Leo majibu ya msingi yanaonesha kwamba wanaendelea au wamekamilisha tathmini na gharama wamezipata upya, sasa wanatafuta fedha. Nini commitment ya Serikali kujenga daraja hili ili kuokoa vifo vya watoto ambapo hata jana tu mtoto mmoja amekufa kwenye kivuko hiki?

(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya Jimbo la Kibamba kuna Mto Mpiji wenyewe na Mto Mbezi ambapo kuna vivuko vingi sana hatarishi kwa watoto wetu na watu wanaotumia. Je, ni ipi ahadi ya Serikali kuleta fedha maalum kujenga vivuko hivi ili tuokoe maisha ya watu wetu? Nashukuru.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyotangulia kujibu kwenye majibu yangu ya msingi, tayari Serikali imefanya tathmini na imebaini kwamba zinahitajika shilingi bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hiyo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ya Mama, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kazini na ndiyo maana kuna ongezeko kubwa la bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka muda huu Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia imeridhia kuongeza bajeti maalum ya shilingi bilioni 350 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu hii. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Rais, TAMISEMI imepokea na itaweka kipaumbele kikubwa sana kuhakikisha kwamba inaanza ujenzi wa miundombinu hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, vivyo hivyo nirejee maelezo yangu ya awali kwamba Serikali inaona umuhimu mkubwa sana wa miundombinu hii muhimu kwa maslahi ya wananchi, na tayari bajeti ya dharura ya TARURA imeongezeka. Vile vile kuna bajeti maalum kwa ajili ya ukarabati na marekebisho na ujenzi wa miundombinu hii muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalichukulia suala hili la ujenzi wa miundombinu hii kwa umakini mkubwa na itakuja kujenga miundombinu hii.
MHE. OMAR M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwulize Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba kwenye Wilaya ya Kilindi kipo Kijiji cha Mgera ambacho kina daraja limekatika takribani miaka mitatu sasa na Serikali haijarekebisha hali hiyo na upande wa pili ndipo ambapo taasisi zote za Serikali zipo huko. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri yuko tayari kutoa maelekezo kwa TARURA kwenda kurekebisha daraja hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika vipaumbele vya TARURA ni pamoja na kuhakikisha kwamba inahakikisha miundombinu ya barabara hizi haikatiki kimawasiliano. Kwa hoja ya Mheshimiwa Mbunge naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu tukutane, tukae, tuweze kufanya mawasiliano na kama ni kweli eneo hili limekata mawasiliano, kuna umuhimu na kipaumbele kikubwa sana ambacho inabidi kitolewe kwa ajili ya kuhakikisha tunarudisha mawasiliano katika eneo hili.
MHE. MOHAMED L. MONNI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Mpendo na Kijiji cha Amia kinatenganishwa na mto mkubwa ambao unaitwa Mto Bubu. Ni lini sasa Serikali itajenga daraja ili kuunganisha vijiji hivi viwili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kama nilivyotangulia kusema kwamba ni muhimu sana kuwe kuna mawasiliano na ndiyo kipaumbele katika mipango kazi au utekelezaji wa majukumu ya TARURA kuhakikisha kwamba mawasiliano hayakatiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kadiri alivyoleta maombi yake na kwa kuzingatia vipaumbele na upatikanaji wa fedha, Serikali itamsaidia kwenda kurekebisha miundombinu hii.
MHE. DKT. ALFRED J. KIMEA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye Jimbo langu la Korogwe Mjini kuna madaraja mawili ambayo yana changamoto kubwa. Moja lipo katikati ya mji ambalo vivuko vyake vimekatika pembeni, watoto wanapata ajali ya kuanguka; daraja lingine la Kitifu, limekatika kabisa, hakuna mawasiliano kati ya kata mbili; Kata ya Mgombezi pamoja na Mtonga: Je, Waziri haoni sababu ya kuwaelekeza TARURA kurekebisha madaraja hayo mawili muhimu kwenye Jimbo la Korogwe Mjini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nitafanya mawasiliano na Meneja wa TARURA ili kufahamu changamoto iliyopo katika eneo hilo na kama ni dhahiri kwamba mawasiliano yamekatika, basi kama ulivyo utaratibu wa TARURA ni kuweka kipaumbele katika kuhakikisha inaunganisha na kuna mawasiliano katika barabara zetu hizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili tumelipokea na tutalifanyia kazi.
MHE. JONAS W. MBUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwanza naishukuru Serikali kwa kutenga shilingi milioni 947.2 kujenga kilometa 31. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza. Katika majibu ya Serikali ni kwamba, kilometa mbili zitajengwa kwa kiwango cha lami kupitia Mradi wa TACTIC. Nataka nifahamu, ni lini mradi huo utaanza kutekelezwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Ni lini Serikali itajenga Barabara ya Mbinga – Kikolo – Kihungu na barabara ya Mbinga – Kitanda hadi Miembeni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tayari hatua zote za muhimu zimekamilika kwa kadiri ya upatikanaji wa fedha, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, mradi huu sasa utaanza kutekeleza ujenzi wa barabara hiyo ya lami ya kilomita mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili ambalo ameuliza juu ya ujenzi wa Barabara ya Mbinga Mjini – Kikolo mpaka Kihungu yenye urefu wa kilometa 30, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika mwaka wa fedha 2024/2025 zimetengwa shilingi milioni 60 kwa ajili ya kufanya marekebisho ya barabara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kitanda ambayo yenyewe ina kilometa 28, kwenye mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali ilitenga kwenye bajeti shilingi milioni 80, lakini katika mwaka wa fedha 2024/2025 Serikali imetenga shilingi milioni 47.18 kwa ajili ya marekebisho. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali imelichukua suala hili la ujenzi wa barabara hizi kwa umakini mkubwa na itaendelea kutekeleza ujenzi huo.