Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Flatei Gregory Massay (156 total)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa miradi hii haijakamilika na wananchi sasa hivi wanapata adha ya kutopata maji hasa katika miji niliyoisema na vijiji vyake, je, Serikali itahakikisha vipi leo hii itapeleka pesa kule ili wananchi wapate maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kutokana na adha ya maji katika maeneo yetu, yuko mwananchi mmoja amechimba maji na kuyapata katika Mji wa Hydom. Je, kwa nini Serikali isiweze kupata maji katika maeneo yale na kuweka hela nyingi namna hii? Waziri yuko tayari kufuatana na mimi akaone jinsi ambavyo wananchi wanapata adha katika mji wa Hydom na maeneo mengine ya Mbulu Vijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Massay yeye mwenyewe tayari anafahamu kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inafanya juhudi kubwa sana kukusanya pesa. Sasa hivi pesa zimeanza kupatikana kwa hiyo wakati wowote ule fedha zitaanza kutumwa kwenda kukamilisha miradi ambayo haijakamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyozungumza katika maswali yaliyopita kwamba tumekuwa na miradi ya maji 1,855, miradi 1,143 tayari imeshakamilika na iliyobaki ni 454 ambayo tunatarajia tuipatie pesa ili iweze kukamilika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, muuliza swali amedai kwamba kuna mwananchi ambaye amepata maji lakini haku-specify kwamba huyo mtu aliyapata hayo maji kwa shilingi ngapi? Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna miradi inayoendelea katika wilaya yake. Kuna Mradi wa Tumati, Hasha, Mungay, Hydom, Moringa na Dongobesh. Miradi hii ikikamilika, naimani kabisa kwamba matatizo ya maji katika eneo lake yatakuwa yamekwisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kwa kibali cha Mheshimiwa Spika, nitakuwa tayari kufuatana naye ili kwenda kuona tatizo lilivyo kwenye Jimbo lake.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, ninaomba kumuuliza Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa uhalifu umeongezeka katika bonde la Yayeda Chini, hasa ubakaji na mengineyo mengi; gari lililosemwa hapo kwanza ni bovu au chakavu katika eneo hilo la polisi au kituo cha polisi, Hydom. Lakini hiyo haitoshi hapo, mvua ikinyesha kidogo bonde la Yayeda Chini halipitiki kutoka Haidom kwa gari lolote.
Je, Serikali haioni kwamba bado wananchi wa Yayeda Chini wana haki ya kulindwa wao na mali zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa wananchi wa Yayeda Chini wanahitaji kulindwa: Je, tukiwahamasisha, Serikali iko tayari ku- chip in ili kujenga kituo hicho pamoja na wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu katika jibu langu la msingi, ni kwamba hatua zilizochukuliwa kwa kiasi fulani zimesaidia sana kupunguza tatizo la uhalifu, hasa wizi wa mifugo katika Bonde la Yayeda Chini. Nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba jitihada hizo zinahitaji kuongezwa ili kuondosha kabisa masuala ya uhalifu, hasa wizi wa mifugo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, hii inadhihirisha kutokana na ukweli kwamba kwa mfano kwa takwimu za mwaka 2014/2015 katika Wilaya ya Mbulu ambayo imeonesha kwamba kuna matukio karibu 21 ya wizi wa mifugo, eneo la Yayeda Chini lilikuwa na takwimu ya matukio matano ambayo ni makubwa zaidi ukilinganisha na maeneo mengine katika Wilaya hiyo. Hata hivyo, kwa mfano, katika Mkoa mzima wa Manyara, Wilaya ya Mbulu ndiyo iko chini ukilinganisha na Wilaya nyingine kama Kiteto ambayo inaongoza kwa matukio 71, ikifuatiwa na Babati yenye matukio 41 pamoja na Simanjiro 27 na Hanang 26. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kutokana na hayo basi, naomba nichukue fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge akubaliane nami kwamba baada ya Bunge hili tukae pamoja ili kujiridhisha kwamba kama kuna haja ya kuchukua hatua zaidi. Hatua zaidi zitategemea mambo makubwa matatu; kwanza, siyo tu kwamba kutokana na wingi wa matukio ya uhalifu, lakini inategemea vilevile na idadi ya watu, inategemea hali ya kijiografia ya sehemu husika pamoja na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, tutakapokuwa tunafanya ziara pamoja na Mheshimiwa Mbunge, tutajua jinsi ya kufanya kulingana na upatikanaji wa fedha kadri utakavyoruhusu.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na swali lake la pili kwamba wananchi wa Jimbo lake na yeye mwenyewe wakishirikiana Serikali itachukua hatua gani? Mimi nataka nimpongeze sana kwa hatua zake hizo nzuri kwamba tunaamini kabisa kwamba Serikali ina ufinyu wa bajeti na hivi sasa vituo karibu kumi ambavyo viko katika hatua za ujenzi vimekwama kutokana na upungufu wa fedha. Sasa ikiwa Mheshimiwa Mbunge atashirikiana na wananchi wake katika kuwahamasisha ili kuisaidia nguvu Serikali, basi tutamuunga mkono.

Mheshimiwa Spika, nataka niahidi tu kwamba Serikali itakuwa pamoja kushirikiana naye pamoja na wananchi wake kuhakikisha kwamba inasaidia kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa Mbulu walishapewa ahadi ya kujengewa uwanja na Olympic na sasa wale wameondoka na eneo hilo lipo mpaka sasa na wananchi wa Mbulu wamekubali kutoa eneo hilo. Je, Serikali haioni ndiyo sasa wakati wa kuja kuwekeza au kujenga kituo hicho Mbulu?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa wanariadha wazuri ambao wamevunja rekodi ya dunia mpaka leo na haijawahi kuvunjwa mfano Philbert Bai ambao wamekuwa msaada mkubwa kwa Tanzania, je, Serikali haioni sasa ndiyo muda muafaka wa kujenga kituo hicho Mbulu kwa sababu uwezo wa Mbulu na uoto wa asili na hali ya hewa inawaruhusu wanariadha kuweza kufanya mazoezi na kushinda Olympic?
WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza Serikali inatambua kazi nzuri iliyofanywa na wanariadha wanaotoka Mbulu wakiwemo akina Philbert Bai na wenzake. Tunakubaliana na hoja kwamba kama eneo lipo ambalo kwa kweli halitahitaji fidia na litaondoa hii haja ya mazungumzo ya kupata eneo, tutashauriana na Serikali ya Mkoa wa Manyara kuona namna ambavyo tunaweza kulitumia eneo hilo kwa ajili ya kujenga kituo hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana naye kwamba kwa kutambua mchango wa wanariadha kutoka Mbulu na namna nzuri ya kuwaenzi nadhani ni vizuri tukaangalia namna ya kujenga kituo hiki Mbulu kwa kuzingatia mazingira hayo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri je, ni lini sasa Serikali itaanza kutoa mikopo hiyo?
Swali la pili, kwa kuwa wananchi wa Mkoa wa Manyara hasa Mbulu Vijijini wako tayari kabisa kwa elimu hiyo ya ujasiriamali, je, Mheshimiwa Waziri anaweza kusema anaweza kuanza na Mkoa huo kwa kuwa uko tayari?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, kuhusu suala la lini fedha hizo zitaanza kugawanywa lazima tuangalie practical realities. Kwa sababu elimu inahitajika na ahadi haikuwa imewekewa time frame ni vizuri tuelewe kwamba fedha hiyo itatolewa ndani ya kipindi hiki, na mapema iwezekanavyo, mara baada ya taratibu zote za kuhakikisha matumizi salama na yenye tija ya kifedha yanakamilika. Kwa hiyo siwezi nikasema exactly ni lini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu whether kuanza na Mkoa upi, Manyara au mwingine na hili pia litategemea sana na hali halisi, lakini ninampongeza na ninawashukuru wananchi wa Manyara, kwa kuonesha utayari katika suala hilo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana.
Kwa kuwa, ni makosa ya uchapaji nashukuru amekiri kuwa Kata hii ya Qurus ipo na kwamba Kijiji hiki cha Gongali ndiko ofisi ya TANESCO ilipo. Sasa
kuna Vijiji ambavyo amevitaja hapa katika swali la msingi ambavyo vinaitwa Gendaa na Bashay;
Je, ni lini vitapata umeme?
Pia, kwa kuwa Wilaya hii ya Karatu ni pacha kabisa na jimbo la Mbulu Vijijini; Je, Vijiji vya Mbulu Vijiji ambavyo vinafanana kabisa kwa majina haya ya Gendaa ambavyo viko Mbulu Vijijini na Bashay ambavyo viko Mbulu Vijijini na Vijiji vingine vya Endara Gadati na Vijiji na Haidereri, Kantananati, Bashay, Yaeda Ampa lini vitapatiwa umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa katika Jimbo la Karatu ni vijiji vichache vimepata umeme. Lakini nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge anayeuliza swali kwa niaba ya Mheshimiwa Mbunge ambaye hayupo ni kwamba, vijiji vingi sana mbali na alivyovijata vya Qorong‟aida na vingine, ikiwemo na kijiji cha Changarawe kitapata umeme kule kwa Mheshimiwa wa Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mambo mengine kijiji cha Kambi ya Faru kitapata umeme kijiji cha Udongo Mwekundu kitapata umeme, pamoja na Vijiji vingine vya Rositeti vitapata umeme, hilo ni katika Jimbo la Karatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Jimbo lake Mheshimiwa Mbunge alivyouliza vijiji vya Mbulu ametaja Qorong‟aida, ametaja na vingine. Lakini kuna vijiji vingi ambavyo hajavitaja ni jumla ya vijiji 73 kwenye Jimbo la Mheshimiwa Mbunge havijapata umeme. Ninamshukuru sana anavyoendelea kuwahangaikia wananchi wa Mbulu, nimhakikishie tu ametaja vijiji vinne lakini bado kuna vijiji vingi ambavyo bado havijapata umeme kwenye Jimbo lako. Nikivitaja vitano tu kati ya vile 78 ambavyo havijapata ni pamoja na Masiedo haina umeme, Labei haina umeme, Mangandi haina umeme, vijiji vyote hivi vitapata umeme kwenye REA awamu ya tatu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niulize swali la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo hili la Same Mashariki linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kwa mahitaji. Same Mashariki wanalima kitu kinachoitwa tangawizi, Mbulu Vijijini tunalima vitunguu na tuna tatizo hili la soko. Je, Serikali ina mpango gani kusaidia wananchi wa Mbulu Vijijini kwa zao hili la vitunguu swaumu maana yake ni maarufu sana pale Bashineti Mbulu ili kuhakikisha kwamba maisha haya yanakwenda vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa tunatambua kwamba wananchi wa Mbulu wako makini na ni kati ya wazalishaji wakubwa sana wa vitunguu nchini. Serikali iko tayari kukaa na Mheshimiwa Mbunge kuangalia changamoto ambazo zipo katika soko la vitunguu ili wananchi waweze kupata soko la uhakika. Kwa sababu ni jirani yangu yeye anatoka Mbulu na mimi Ngorongoro namkaribisha vilevile tutumie ujirani huo kuongea ili niweze kuwakaribia zaidi wananchi wake na kutoa msaada ambao anauhitaji.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipatia muda wa kuweza kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amesema amefika mikoa hii 23, kwanza nimshukuru sana kwa kuweka plan ya kujenga barabara ya Mbulu - Karatu, Mbulu - Haydom - Singida kwa kiwango cha lami. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni lini sasa Serikali itaanza kujenga barabara hii kwa kuanzia na upembuzi yakinifu? Ahsante sana.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwenye mpango wetu tumeweka barabara hii na hatua inayofuata sasa hivi ni kufanya feasibility study na detail engineering design tutafanya tu pale tutakapopata hela sasa hivi tupo katika mchakato wa kutafuta hela mara hela hizo zitakapopatikana nataka kuhakikishia Mheshimiwa Mbunge tutakuja kuifanya kazi hiyo ili hatimaye tuijenge kwa kiwango cha lami.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mbulu ni Wilaya kongwe, imeanza 1905, sawa na Nairobi. Pamoja na ahadi zilizotolewa kwa muda mrefu na Marais waliyotangulia. Je, kwa kuchelewa kutengeneza barabara hii, huoni kwamba ni kuwadanganya wananchi wa Mbulu na kuwakatisha tamaa?
Swali la pili, kwa kuwa barabara hii ya kwenda Hydom, ipo Hospitali kubwa ya Rufaa ya Hydom ambayo ni Hospitali ya Kanda; na sasa hivi daraja la Enagao limevunjika na wananchi hawezi kwenda kwenye Hospitali hiyo: Je, Serikali haioni kwamba kwa kuendelea kutopitika barabara hii kunaweza kuendelea kupoteza maisha ya watu na wasipate huduma katika hospitali hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba kumhakikishia kwamba dhamira ya Serikali kujenga barabara ni kubwa na Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi. Tuna barabara nyingi ambazo kutokana na ufinyu wa fedha, hazijaisha. Namwomba awe na Subira na ninamhakikishia, katika kipindi hiki cha miaka mitano ahadi hii iliyotolewa itatekelezwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa upande wa matatizo yanayotokea ambayo yanatokana na hali ya hewa, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba TANROADS wataendelea kutumia fedha za dharura kuhakikisha barabara hizo zinapitika na zinaendelea kuwahudumia wananchi wa maeneo hayo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa umeme umefika Dongobesh miaka 11 iliyopita na haujawahi kwenda kijiji hata kimoja na pia miaka ya tisini umefika Haydom. Je, Serikali iko tayari sasa kusogeza umeme huo kutoka Kata hizo ambazo nimezisema kuelekea kwenye Kata ambazo amezitaja? (Makofi)
Swali la pili, kwa kuwa tuna miradi ambayo ni ya maji, na inahitaji umeme na kwenye REA phase two, hatujawahi kupata mradi huo: Je, Serikali iko tayari kukubali sasa kuanza na Vijiji hivi vya Kata ya Hayderer, Getanyamba, Dinamu, Maretadu, Masieda, Laba na Dinamu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, Serikali iko tayari kusogeza umeme kwenye Vijiji alivyotaja Mheshimiwa Mbunge. Nikiri kwanza Vijiji ambavyo amevitaja kwa lugha yangu, naweza nisivitamke kwa usahihi, lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hata Vijiji mbavyo amevitaja ambavyo havikuwa kwenye REA Awamu ya Pili, tunaviingiza kwenye REA Awamu ya Tatu.
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, pamoja na REA, Awamu ya Pili inayokamilika na REA, Awamu ya Tatu inayoanza, tutampelekea pia mradi mwingine wa kusambaza ma-transformer ili kuhakikisha Vijiji ambavyo viko karibu na Vijiji vilivyopewa umeme na vyenyewe vitapata umeme. Lengo ni kuvipatia Vijiji vyako vyote umeme kwenye REA, Awamu ya Tatu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kunipatia muda wa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwa kuwa Hospitali ya Haydom inahudumia Mikoa ambayo umeitaja ya Singida, Simiyu, Arusha, Dodoma na Mara; na nashukuru Serikali kwa kutoa fedha na kupanga kiwango hiki cha shilingi milioni 570.
Je, kwa kuwa Serikali sasa imesema haya na hela iliyopelekwa ni kidogo, haioni sasa ni muda wa kuongeza ruzuku hii ili hospitali hii ikaweza kutoa huduma nzuri kwa watu wanaozunguka?
Swali la pili, kwa kuwa tumeleta maombi ya hospitali hii kupandishwa hadhi kuwa hospitali ya Kikanda na kwa kuwa Wabunge wanaozunguka hospitali hii na Mikoa niliyoitaja tumeomba namna hiyo.
Je, ni lini sasa Serikali itajibu maombi haya ya kuipandisha Hospitali ya Haydom kuwa Hospitali ya Kanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto ya Mheshimiwa Mbunge anasema kwamba hospitali hiyo ikiwezeana iongezewe ruzuku; kwanza naomba niwapongeze watu wote wa Mkoa wa Manyara kuanzia wewe, Mheshimiwa Jitu Soni, Kaka yangu pale, wote mnafanya juhudi kubwa kwa ajili ya Mkoa wenu wa Manyara, lazima niwapongeze. Mara nyingi mmefika katika ofisi yangu suala la kutaka madaktari, kutaka nini, inaonekana mnajali shida za wananchi wenu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na hilo ndiyo maana nimesema Serikali iko katika mchakato wa kuweka mkataba vizuri, kwa sababu hospitali hii sasa hivi huduma kubwa ilikuwa inatokea Kiwilaya, lakini sasa hivi ruzuku ya mishahara zaidi ya shilingi milioni 500 kwa sasa, na zile za madawa zaidi ya shilingi milioni 134, na kwa mwaka huu wa fedha ambao tunaendelea nao, tutawapatia ruzuku ya shilingi milioni 714 mishahara peke yake, vivyo hivyo katika dawa kutoka shilingi milioni 130 tunakwenda mpaka zaidi ya shilingi milioni 300, maana yake tunazungumza suala la shilingi bilioni moja. Hivyo, Serikali imeshaona jinsi gani sasa Hospitali hii ya Haydom inatakiwa ipewe kipaumbele, kwa hiyo tumeshaiweka katika mikakati. Tunachokifanya sasa hivi ni kusubiri suala ule mkataba ufanyiwe vetting utaratibu ukishakamilika basi nadhani suala zima la ruzuku litakwenda vizuri kama linavyokusudiwa Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la kupandisha hadhi, naamini kwa sababu suala la kupandisha hadhi ni mchakato mzuri na naamini katika kikao cha RCC nitamaliza hilo lipo katika Ofisi ya Waziri wa Afya, litapitiwa. Mwisho wa siku suala la Hospitali ya Haydom kuwa Hospitali ya Kanda itafanyiwa hivyo. Serikali lengo lake kubwa ni kuboresha maisha ya wananchi wake na hususan kuboresha sekta ya afya. Kwa hiyo, kwa sababu mchakato huu wote ulishakamilika na Wizara ya Afya, mwisho wa siku tutapata majibu halisia kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wa Manyara wanapata huduma bora.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa majibu mazuri sana, kwanza nampongeza. Pili kwa kuwa kundi la walemavu limekuwa likisahaulika sana hasa katika suala hili la mikopo, ukizingatia wapo vijana wa kike na wa kiume, lakini je, kwenye mpango huu wa milioni 500, kundi la walemavu limekuwa considered namna gani. Je, Mheshimiwa Waziri anaweza kunithibitishia hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WALEMAVU): Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii pia kumpongeza sana Mheshimiwa Massay kwa kazi nzuri anayoifanya Bungeni ya kuwawakilisha wananchi wake wa Jimbo la Mbulu na hata walemavu pia.
Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria Namba Tisa ya mwaka 2010 ambayo inaongoza na kuratibu shughuli zote za watu wenye ulemavu nchini, zinatutaka na kutukumbusha kwamba, katika kila suala tunalolifanya kwenye nchi yetu ya Tanzania, lizingatie pia kwamba walemavu wanatakiwa wapewe haki sawa katika nchi yetu ya Tanzania. Kwa hiyo, tunapoandaa taratibu na miongozo kwa ajili ya fedha hizi, Sheria Namba Tisa ya mwaka 2010 itachukua nafasi yake, kuhakikisha pia walemavu wanakumbukwa katika mpango huu mzima.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Mheshimiwa Profesa Maji Marefu la Korogwe Vijijini ni pacha kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kutokana na hali ya kukosa mawasiliano. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka mawasiliano kwenye Kata ya Ari, Tumati, Mung’ahai, Ng’orati, Masieda, Endagi, Chani kule Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Massay alileta hiyo orodha na tuliongea na tena siyo na mimi tu, nilimpeleka na kwa Mheshimiwa Waziri. Naomba kumhakikishia tena, siyo pale ofisini tu, hata na hapa. Sina tatizo, yeye aendelee tu kufuatilia, maana amefuatilia mara nne kuhusu suala hilo hilo, nami nampongeza sana kwenye hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba tutatekeleza na tutafuatilia utekelezaji wa mawasiliano katika eneo hili la Mbulu Vijijini kama ambavyo tunafanya katika maeneo mengine na kwako nilikuahidi nitakuja. Siyo kwa
sababu hii tu, ni pamoja na ile barabara inayopitia Mbuyu wa Mjerumani mpaka lile eneo lako. Nilikuahidi na ninahakikisha nitalitekeleza.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa Jimbo la Morogoro Mjini linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini juu ya tatizo hili la ukosefu wa maji. Kwa kuwa Waziri alishaniahidi kwamba tukipeleka certificate atawasaidia wakandarasi kuwalipa fedha waendelee na mradi. Je, ni lini sasa watapatiwa fedha, miradi ya Mbulu iliyopo Haidom na Dongobeshi ili wakandarasi waweze kumalizia na wananchi wapate maji? Ahsante
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru. Tumekuwa na matatizo huko nyuma kwamba, tunapeleka fedha katika Halmashauri wanachelewa kutekeleza miradi. Sasa hivi tumeweka utaratibu kwamba tukishatenga bajeti, basi Halmashauri zitangaze tenda zianze kutekeleza miradi. Certificate ikipatikana watuletee tutaipeleka Hazina, halafu wakitupatia pesa ndiyo tuweze kupeleka.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama tulivyoongea kama ulivyosema Mheshimiwa Massay naendelea kusisitiza kwamba walete certificate halafu pesa tutalipa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Jimbo la Mpwapwa linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini kwa ukosefu wa maji kwa eneo kubwa mno, je, ni lini Serikali itakuwa tayari kuja kuviangalia hivi vijiji na kata za Labay, Bisigeta, Maretadu, Endamilay, Endahagichan, Bashnet na Dinamu, ili kuzipatia visima virefu na wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kupata maji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme wazi, nilifika kwa Mheshimiwa Mbunge takribani wiki nne zilizopita kutembelea katika jimbo lake. Nipende kumpongeza kwa harakati kubwa sana anazozifanya na mwezake Mbunge wa Mbulu Mjini. Naomba nikiri wazi kwamba kweli kuna changamoto ya maji na kwa sababu mpango wetu wa Serikali sasa hivi ndani ya miaka mitano kujielekeza tunahakikisha kwamba Mpango wa Maji katika Awamu ya Pili unafanyika vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili naomba niseme kwamba tutafanya kila liwezekanalo kutumia wadau mbalimbali kupitia bajeti hizi tulizokuwa nazo lakini kutumia fursa nyingine mbalimbali tunazozipata, lengo kubwa na ushahidi niliyouona nilivyofika site nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutashirikiana kwa pamoja kwa kadri iwezekanavyo kwa ajili ya wananchi wa Mbulu Vijijini.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri amefika katika hospitali ya Hydom, lakini nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa Naibu Waziri amekiri kwamba hospitali hii imepandishwa hadhi miaka sita toka 2010 hadi leo ya kuwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na haijapata hata siku moja ile haki ya kibajeti ya hospitali ya Mkoa. Je, sasa ni lini hospitali hii itatengewa bajeti ili ifanane na hospitali zote za Rufaa za Mikoa ya Tanzania?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwa kuwa kwenye majibu ya msingi amesema hospitali hii ina tatizo la miundombinu na watumishi. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuijengea uwezo na kuipatia watumishi ili hospitali ya Haydom iweze kutoa huduma kwa sababu na yeye amekiri kwamba inafikika na maeneo ya jirani na mikoa hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Flatei Massay kwa ufuatiliaji anaoufanya kiasi kwamba amenilazimisha kufika kwenye hospitali hii katika ziara zangu mara mbili toka nimeteuliwa katika nafasi hii. Katika mara zote nimefika na kutatua changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikiikabili hospitali hii.
Mheshimiwa Naibu Spika, ukweli ni kwamba, pamoja na kwamba hospitali hii ingependa iwe Hospitali ya Rufaa ya Kanda bado haijakidhi vigezo. Pili, kuteuliwa kuwa hospitali ya ngazi ya Kanda hakuifanyi hospitali kudai haki ya kupewa fedha kibajeti wakati haimilikiwi na Serikali. Serikali inashirikiana na mashirika ya hiyari kama KKKT kutoa huduma kwa wananchi kwa kuwawezesha kupata michango ya health basket fund pamoja na watumishi ambao wanapelekwa by secondment na Serikali kwenye hospitali husika. Kwa sasa, Mkoa wa Manyara una hospitali yake ya rufaa ya mkoa na Serikali inaijengea uwezo hospitali hii ili iweze kutoa huduma ambazo zinaendana na hadhi ya hospitali ya rufaa ya mkoa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa hali ya barabara za Lulindi ni nafuu kuliko Mbulu Vijijini; na kuna barabara imeahidiwa ya Karatu - Mbulu; Mbulu – Hydom; Hydom – Sibiti na Mheshimiwa Rais, kwa kujengwa kwa lami; na majibu ya MheshimiwaWaziri yalikuwa yanasema mwanzoni uchambuzi yakinifu umeshaanza. Je, barabara hii inajengwa lini sasa ili wananchi wa Mbulu na maeneo mengine wapate nafuu ya kiuchumi na kupita hasa kuelekea kwenye Hospitali ya Hydom?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano inapoahidi ina dhamira ya dhati ya kutekeleza ahadi zake zote ikiwa ni pamoja na barabara hii. Tumeongea mara nyingi ofisini kuhusu hili suala na tumemwambia mara nyingi kwamba tuna dhamira ya dhati, tunatafuta fedha. Hatuwezi kuanza ujenzi kabla hatujapata fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juhudi za kutafuta fedha zinaendelea kwa kasi na mara zitakapokamilika tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa maeneo ya Mbulu mpaka wanavyoungana na Hanang wajue kwamba lini barabara yao sasa itakuwa vizuri na sasa wataenda kwenye ile hospitali wakiwa na barabara nzuri.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa sasa wanafunzi wa vyuo vikuu wamekuwa wengi ukizingatia Chuo hiki cha Maendeleo ya Jamii Tengeru kimeanza kujaa. Je, Serikali ina mpango gani wa kupandisha vyuo vidogo vya diploma kama vile vya Monduli CDTI ili kuwa university kuweza kuwa-accommodate vijana waweze kusoma kwa wingi maana elimu inayotolewa na vyuo hivi ni nzuri sana kwa ajili ya Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Serikali haina utaratibu wa kuendelea kuvipandisha vyuo vya taaluma za kati kuwa vyuo vya kutoa degree kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano haiamini kwamba inahitaji watu wengi zaidi wenye degree kwenye soko la ajira, hapana! Serikali ya Awamu ya Tano inahitaji watu wengi zaidi wenye ujuzi kwa ajili ya ku-support uchumi wa viwanda na maendeleo ya kilimo na maendeleo ya biashara na ujasiriamali vijijini. Kwa hivyo, tutaendelea kuvijengea uwezo vyuo vyetu vya CDTI nchi nzima ili viendelee kutoa kozi kwenye ngazi hii ya wanataaluma na watu wenye ujuzi wa kati ili ku-support uchumi wa viwanda ambao tunaujenga kwa sasa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii adimu. Mbulu Vijijini tuna tatizo linalofanana na Ngara.
Mheshimiwa Spika, tuna Bwawa la Dongobesh ambalo limejengwa zaidi ya shilingi bilioni mbili; na kwa kuwa limekaribia kukamilika na Naibu Waziri ameshafika; kilichobaki ni njia tu ya maji ya kwenda kuwafikia watumiaji. Je, Mheshimiwa Waziri atuambie lini anapeleka fedha kwa ajili ya kumalizia tu hilo bwawa ambalo kimsingi limekamilika bado tu njia ya kwenda kupeleka maji kwa watumiaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli kwamba Mheshimiwa Flatei Massay Jimbo lake nimelitembelea, Bwawa la Dongobesh nimeliona na limekamilika kwa zaidi ya asilimia 90. Kilichobaki ni spillway ambayo itakuwa inatoa maji yale yanayozidi ili yasije yakabomoa ule ukuta mkubwa uliojengwa kwa gharama kubwa.
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwamba fedha imeanza kutoka. Mwezi uliopita tumepata shilingi bilioni moja na fedha zitakazotoka mwezi huu nitahakikisha napanga kwa sababu hela iliyobaki ni ndogo sana ili tulikamilishe hilo Bwawa la Dongobesh liweze kufanya kazi iliyotarajiwa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti nikushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina swali moja la nyongeza.
Kwa kuwa Daraja la Magala na barabara yetu ya Karatu - Mbulu - Haydom - Sibiti Mheshimiwa Waziri aliahidi kwamba itaanza upembuzi yakinifu, sasa swali, je, barabara hii iko kwenye hatua gani, upembuzi yakinifu na lini anafikiri kwamba itaanza ujenzi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimuombe Mheshimiwa Massay, tulikubaliana kwamba twende site kwa sababu kuna mambo kama matatu ya msingi katika eneo lake. Mimi nimuombe, tutakapofika site tukaifanya kazi inayokusudiwa kuifanya baada ya hapo kama kutakuwa na maswali zaidi ndipo aulize, lakini kwa sasa nimhakikishie kwamba ahadi yangu ya kwenda site iko pale pale na tumekubaliana kipindi gani twende. Mimi naomba tuitumie fursa hiyo kushughulikia mambo makubwa yote matatu ikiwa ni pamoja na Daraja la Mto Ugala, barabara hiyo aliyoitaja Karatu - Mbulu - Haydom vilevile pamoja na wale watu wa Yaeda Chini ambao hawana mawasiliano ya simu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, ninayo maswali
mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa tumeleta maombi haya muda mrefu; na vikao hivi vimekaa muda mrefu; na tuna miji miwili ya Dongobesh na Haydom; na kwa kuwa muda umepita, je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa
kutuma wataalamu wake kutoka TAMISEMI ili kushirikiana na wataalamu walioko Wilayani kusaidia vigezo hivi kutimia?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Waziri yuko tayari, je, ni lini sasa atawatuma wataalamu hawa ili
kiu ya wananchi wa Mbulu Vijijini itimie?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kama
nilivyosema pale, kwanza elekezo langu ni kwamba naomba niwasihi ndugu zetu wa Mbulu kwamba kwa sababu kazi kubwa na Mbunge umekuwa ukipigania jambo hili sana kwa wakati wote kwamba zile taarifa zipite katika vikao vile vya kisheria sasa zije huku kwetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuwatuma hili jambo, siyo tatizo kubwa sana, kwa sababu hata Mheshimiwa
Flatei kama atakumbuka, kuna team mara ya kwanza ilikuja kule kwa maombi yake vilevile na taarifa tunazo kuhusu Mji huu wa Haydom.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Mheshimiwa Mbunge amesema na suala zima la Mji wa Dogobesh. Kama
nilivyosema mwanzo ni kwamba hata Mji wa Dogobesh wakati unataka upandishwe, lazima taratibu hizi za kisheria ziweze kufuatwa ambapo mamlaka haya kuanzishwa kwake, yanatuletea utaratibu wa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mheshimiwa Flatei naomba nikutoe hofu kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI, cha kufanya ni kwamba tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kukupa ushirikiano wote. Ninachokiomba ni kwamba vile vikao vya kisheria viweze kutimiza wajibu wake, tukipata taarifa hizo katika ofisi yetu, nitakupa ushirikiano wote
kuhakikisha Halmashauri yako katika maeneo yako ya Mamlaka Mji Mdogo, basi yaweze kupitiwa na kuweza
kupewa hadhi kama tulivyozungumza.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Kwa kuwa Mbulu Vijijini katika REA Awamu ya Pili tumepata vijiji viwili tu na sasa Mbulu Vijijini hatuna sub-station tunapata umeme kutoka Katesh na Mheshimiwa Waziri anafahamu, amekuja, tunapata kutoka Babati na Mbulu Mjini. Je, mtatuhakikishiaje sasa katika awamu hii REA itafika maeneo yote ya kata na hasa katika vijiji vya mwanzo vya Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa Mheshimiwa Flatei nakupongeza, mwaka jana mwezi Novemba tulitembea na wewe kwenye jimbo lako lote na ukanionesha vijiji vyako vyote 78 ambavyo havijapata umeme pamoja na vijiji vya karibu kabisa na Wilaya za jirani. Hata hivyo, natambua katika utekelezaji wa REA Awamu ya Tatu kazi zinazofanyika ni pamoja na kufunga transfoma. Kinachokosekana katika Jimbo lako Mheshimiwa Flatei ni ufungaji wa transfoma katika vijiji ambavyo umevitaja ikiwa ni pamoja na Katesh.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kazi ambayo itafanyika sasa ni kukupelekea umeme katika vijiji vyako 78 vilivyobaki pamoja na vitongoji 120 kama ambavyo umeomba. Kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Mbulu Vijijini kwamba wote watafikiwa na umeme vijijini, vitongojini pamoja na kwenye taasisi zako za umma.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nataka nimpe taarifa kwamba katika Kata ya Hayderer kuna mnara wa Airtel umeanzishwa, una miaka miwili, haujamalizika kabisa, uko kwenye foundation. Sasa kwa kuwa Kata za Yaeda Ampa na Tumati zinakaribiana. Je, Wizara iko tayari sasa kujenga mnara katikati ya kata hizi ili angalau katika mnara huu uliotangazwa tender, kata hizi mbili zikapata mawasiliano?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa kuwa maeneo mengi mitandao haifiki, maeneo ya Endagichan, Endamasak, Enargatag, Runguamono, Munguhai, Gembak na Gidamba. Serikali sasa ituambie, ina mpango gani tena wa kuingiza vijiji hivi na kata hizi ili angalau basi Jimbo langu lipate mawasiliano? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutafuatilia mnara wa Airtel ambao amesema umekaa kwa muda mrefu katika kiwango cha msingi. Tutafuatilia tuone tatizo ni nini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kuhusu ombi la kujenga katikati ya zile kata mbili; tumelipokea na tutalifuatilia na vilevile vijiji vyote ambavyo amevitaja tumepokea ombi hili, tutaangalia namna ya kuyashughulikia ili hatimaye vijiji hivyo vyote vipate mawasiliano. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri alifika Jimboni kwangu na amekiona Kituo cha Dongobesh na tukaleta ombi la kujengewa theater, je, Mheshimiwa lini sasa theater ile inajengwa ili wananchi wangu wapate matibabu hayo ya upasuaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tuliweza kufika Dongobesh na kuweza kufanya tathmini ya changamoto kubwa inayokabili huduma ya afya katika eneo lile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mpango wa Serikali ndiyo nimezungumza katika vituo 142 kwamba na Dongobesh ni miongoni mwa kituo ambacho tunaenda kukijengea theater; lakini siyo theater peke yake; tutajenga pale theater tutaweka na vifaa lakini halikadhalika tutaweka uboreshaji wa miundombinu kwa bajeti iliyotengwa pale Dongobesh. Kwa hiyo, naomba niwatoe hofu wananchi wa Dongobesh kwamba jambo hili kwa sababu manunuzi yake tumepeleka kwa ujumla, tufanye subira, ni commitment ya Serikali kwamba siyo muda mrefu sana kazi hii itaanza mara moja.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa pembejeo nyingi mwaka huu mawakala wengi walipewa muda wa kupeleka kwa wakulima na hazikufika kwa wakulima mwaka huu, mawakala wameshapewa na Kamati ile ya pembejeo za Wilaya na sasa pembejeo hazijafika.
Je, Serikali inatuambia nini kwa pembejeo hizi ambazo hazijafika wakulima bado wanasubiri na msimu umeshapita?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Flatei kwa sababu suala alilolileta kwenye swali la nyongeza limekuwa ni suala ambalo amelifuatilia mara nyingi sana Wizarani. Kimsingi amekuwa ni Mbunge mzalendo kama mlivyo wengi humu ndani. Ameniletea orodha ya Mawakala ambao walichelewa kuleta pembejeo Jimboni kwake lakini bado wanataka kulipwa. Nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba Wakala ambaye hakuweza kuleta pembejeo kwa wakati hatalipwa. Kimsingi Wizara na Serikali haiwezi kulipa kwa huduma ambayo haijatolewa.(Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza, Kwa kuwa, Serengeti Boys vijana wale walionesha umahiri mkubwa wa kiwango kile cha soka kinachotakiwa na wakatutangaza sana kule nje na sasa wamerudi. Je, Wizara ina mpango gani sasa kuwaendeleza vijana hawa ili kutokuwa na ile kazi ya zimamoto, wachezaji hawa wakaendelea kufanya vizuri wakati mwingine wa ligi za kimataifa. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serengeti Boys imefanya vizuri na imetoa mfano mzuri katika timu za Taifa under seventeen, lakini nadhani sote tunakumbuka kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu hapa alipokuwa akifunga Bunge tarehe tano mwezi wa saba alitoa maagizo kwa TFF kwamba wawatunze vijana hawa wasiwaache wakapotea. Kwa hiyo, sisi kama Serikali/Wizara tulichokifanya ni kuwachukua vijana hawa na kuwaunganisha na majeshi. Kwa hiyo, mpaka sasa wanatunzwa katika kituo cha JKT na pale wanafanya mazoezi ya kila siku na baadae tunaweza kuwatumia katika timu za wakubwa za Taifa. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mradi wa Maji wa Haydom unafanana kabisa na jinsi ambavyo matatizo ya Ngara yalivyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi huu wa Haydom umekaa miaka saba, mkandarasi amechukua pesa na muda wa kukabidhi mradi umeshafika. Mkurugenzi kafanya jitihada mpaka leo mradi haujaisha.
Je, Mheshimiwa Waziri atanisaidiaje sasa kuisaidia Halmashauri yangu ule mradi wa Haydom ukaisha na wananchi wakapata maji?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa
Naibu Spika, ni kweli, ipo miradi mingi ambayo ukamilishaji wake umechukua muda mrefu na sababu mojawapo ni ama kulikuwa na matatizo ya mkandarasi au kulikuwa na matatizo ya vyanzo au kulikuwa na matatizo ya kutokulipwa. Sasa tulipoingia awamu hii, maana hii ni miaka saba, sisi tuna miaka miwili, tumeanza kwanza kufuatilia miradi mmoja baada ya mwingine na kuhakikisha kwanza Wakandarasi wanarudi. Miradi mingi wakandarasi walikuwa wameondoka kwenye utekelezaji ikiwa ni pamoja na huo mradi wake ambao umechukua miaka saba.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mkandarasi amerudi na sasa hivi tunawapa fedha kwa kazi ambazo wamefanya. Kwa hiyo, nitafuatilia huu mradi anaousema ili niweze kuona nini kinachoendelea na tuweze kumwambia Mheshimiwa Mbunge ni lini kazi ile ingeweza kukamilika? (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Kwa kuwa Serikali ilitoa ahadi ya kujenga Kituo cha Polisi katika bonde la Yaeda Chini na muda umepita sasa na wananchi wanaibiwa mifugo na kutokea mauaji katika lile bonde.
Je, ni lini sasa Serikali itatekeleza ahadi ya kutengeneza Kituo cha Polisi ya Yaeda Chini? (Makofi)
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Flatei jambo hili amelileta mara nyingi sana nami nampongeza kwa hamasa ambayo ameifanya Jimboni kwake kuhusu masuala haya ya ulinzi na usalama. Nilimhakikishia kwamba baada ya Bunge hili la Bajeti kuisha nitazungukia maeneo hayo ambayo kuna uhalifu umekuwa ukijitokeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, namuahidi kwamba punde tutakapoanza utaratibu wa ujenzi wa vituo hivyo, eneo lake ni moja ya eneo la kipaumbele kufuatana na uhalifu ambao umekuwa ukijitokeza katika eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata kwenye jibu nililojibu la masuala ya magari, Mheshimiwa Flatei pamoja na ndugu yake (pacha yake) Mheshimiwa Issaay, Mbunge wa Mbulu Mjini, alikuja jana tu kusemea mambo ya aina hiyo yakihusisha pia na mambo ya magari.
Kwa hiyo, Mheshimiwa Flatei pamoja na Mheshimiwa Issaay, niwahakikishie kwamba tutawapa kipaumbele kwenye vituo pamoja na upatikanaji wa magari kufuatana na jiografia ya Majimbo yao na Wilaya yao.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri na kutaja vizuri vijiji hivi, nina swali la nyongeza. Mwaka jana bajeti yetu ilikuwa shilingi bilioni 2.4 ikarudi na sasa hivi Mheshimiwa Waziri amesema tumetengewa shilingi bilioni, tatizo lililoko pale ni kwamba wakandarasi wanaojenga miradi hiyo baadhi yao hawako site ndiyo maana bajeti mwaka jana imerudi na kadri inavyoendelea hivi bajeti ya mwaka huu kuna wasiwasi wa kurudi. Je, atanisaidiaje kusukuma sasa bajeti hii iishe kwa kuwa wakandarasi wengi hawako site?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mradi wa Haydom mpaka sasa una tatizo la kwisha pamoja miradi hii ambayo ameitaja mwenyewe ya Arri-Harsha, Barshai, Quantananat na mradi wa Mongahay kuja Tumati. Je, atakuja lini kule na kuwaahidi wananchi wangu ili aweze kuona jinsi ambavyo wakandarasi wanawadanganya kutomaliza miradi na pesa za maendeleo kurudi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda nimpongeze sana Mheshimiwa Mbunge kwa namna ya pekee anavyowapigania wananchi wake wa Mbulu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ieleweke kabisa nia ya Serikali ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji, si maji tu bali ni maji safi na yenye kutosheleza. Hata hivyo, imeonekana baadhi ya wakandarasi wamekuwa wakikwamisha jitihada za Serikali. Labda niziagize tu Halmashauri kwa wakandarasi ambao wanakwamisha miradi ya Halmashauri waondolewe mara moja kwa mujibu wa mikataba yao waliyoingia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine niwaombe sana Wakurugenzi wasiwape kazi wakandarasi kishemejishemeji au kiujombaujomba, wananchi wanapata tabu wakati Serikali inatoa fedha. Kikubwa naomba wale wakandarasi wanaokwamisha miradi waondolewe mara moja wapatikane wapya ili wananchi waweze kupata maji. (Makofi)
Mheshimiwa mwenyekiti, kuhusu suala la mimi kufanya ziara katika Jimbo la Mbulu, nipo tayari baada ya Bunge tunaweza tukaongozana pamoja kwenda kuzungumza na wananchi wa Mbulu. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa Mheshimiwa Rais aliahidi maeneo mengi hasa wakati wa kampeni katika Jimbo la Mbulu Vijijini aliahidi ujenzi wa barabara kilometa tano katika Mji wa Haydom na Dongobesh kilometa mbili. Je, ni lini sasa ahadi hizi za Mheshimiwa Rais zitatekelezwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilizungumza hapa siku za nyuma zilizopita kwamba kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba uratibu wa ahadi zote za Mheshimiwa Rais umefanyiwa kazi na nikuhakikishie Mheshimiwa Flatei kwamba commitment yetu ni kwamba, tutakapofika mwaka 2020 tuhakikishe kwamba, zile ahadi zote za barabara hizi ambazo zimelengwa ziweze kukamilika. Na kupitia Wakala wetu wa TARURA tumewapa hayo maelekezo kwamba, wahakikishe kwanza jambo la kwanza wana-identify ahadi za Mheshimiwa Rais na ahadi za viongozi wakuu katika maeneo hayo lengo kubwa kwamba waweke mpango kazi jinsi gani tutafanya tukifika mwaka 2020 maeneo hayo yote tuwe tumeweza kukamilisha jambo hili.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii. Kwa kuwa, Mheshimiwa Naibu Waziri ametoa majibu mazuri ya kueleweka katika maswali haya na katika majibu yake ya msingi. Je, yupo tayari sasa kuandika maelekezo haya yaende kwenye Halmashauri yetu ili hizi Community Centers zifanye kazi yake iliyokusudiwa? (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze ndugu yangu Mheshimiwa Dkt. Faustine Ndugulile kwa umahiri wake wa kwenda vizuri katika eneo hilo la afya na maendeleo ya jamii. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwa muda mrefu sana Maafisa Maendeleo ya Jamii walikuwa wanatumika kama spare tyre. Matumizi yao mara nyingi sana katika Halmashauri zetu walikuwa hawatumiki vizuri, lakini kuanzia sasa ndiyo maana last week tulikuwa na training kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii yaliyodumu kwa siku tano mfululizo. Licha kutoa mafunzo hayo tuliwapa terms of reference nini wanatakiwa kufanya katika kazi zao. Namshukuru sana Mheshimiwa Jenista Mhagama, Waziri wa Afya na Waziri wa Viwanda, tuliwapa mwongozo maalum kwa ajili ya kwenda kusimamia katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi sasa nimewaagiza Wakurugenzi wote kwa sababu Maafisa Maendeleo ya Jamii ndio agent of change katika maendeleo ya Halmashauri zetu. Sasa wawatumie na wawawezeshe kwa rasilimali fedha hali kadhalika kuwafanya kwamba kazi zao zifanyike vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge naomba niwahakikishie kuanzia sasa mtaona mwenendo tofauti wa Maafisa Maendeleo ya Jamii chini ya Wizara ya Afya na chini ya TAMISEMI ambao ndio tunawasimamia kwa karibu zaidi kama waajiri wao. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza naipongeza Serikali kwa kuandaa mpango huu wa kunusuru kaya maskini. Katika jimbo langu Mheshimiwa Waziri alishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya. Je, Mheshimiwa Waziri, kwa sababu anajua Bonde la Yaeda Chini kwa Hadzabe kule wana tatizo hili la umaskini. Je, ataweza kutuongezea angalau Vijiji vile Mungwamono, Eshkeshi na Endagechani tukapata zaidi msaada huu wa TASAF?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS UTUMISHI NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli nakubali kwamba nilikuwa DC wa Mbulu 1983 mpaka 1988 na maeneo anayoyataja ya Yaeda Chini nimefika, wanakaa Wahadzabe, wanaishi kwa kuwinda tu badala ya kulima. Nataka nimwahidi kwamba kwa kushirikiana na Mheshimiwa Mbunge, wanachotakiwa wao ni kuzitambua zile kaya maskini, wakituletea sisi tutachukua hatua. Nilipita siku nyingi kule Yaeda Chini, Mheshimiwa Mbunge akinialika kwenda kuwahamasisha, nitashirikiana naye.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hospitali hii ya Haydom kwenye swali la msingi iko katika jimbo langu na inaihudumia Mikoa ya Arusha, Manyara, Mara, Singida na Shinyanga. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri Mkuu alishafika na kutuahidi kwamba atatupatia watumishi zaidi na Mheshimiwa Ummy amefika kwenye hospitali hiyo. Je, lini sasa Serikali inatimiza ile ahadi yake ya kutupatia watumishi katika hospitali hii ambayo inahudumia mikoa mingi niliyoisema?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Serikali ilishatoa ahadi kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tatizo la watumishi linaweza kutatuliwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mbunge ni shahidi, jana alikuwepo, Mheshimiwa Waziri wa Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora alitoa majibu kwamba kwa zile Halmashauri na maeneo ambayo tunahitaji kuweza kuziba pengo hilo kwa haraka ni vizuri barua zikaandikwa. Pia tunakiri kabisa juu ya kujengea uwezo Hospitali ya Haydom kwa sababu inahudumia wagonjwa wengi, naomba tufuate procedures za kawaida ili jambo hili liweze kutatuliwa kwa wakati.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa ahadi za Rais, zimekuwa zikitolewa na moja ya Mji wetu wa Haydom, Mbulu na Dongobesh tumeahidiwa kujengwa barabara ya lami kwa kilometa tano. Je, lini Serikali inatekeleza ahadi hii ya Mheshimiwa Rais?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu na nimeshajibu hoja hiyo huko nyuma kama mara mbili hivi. Najua kwa nini anarudia, ni kutokana na umuhimu wa barabara hiyo, lile eneo halina lami kabisa kama ilivyo kwa Mbunge wa Loliondo. Niliwaambia kwamba ahadi ya Rais wa Awamu ya Tano na Awamu ya Nne, ni lazima tutazitekeleza kwa sababu ndiyo wajibu tuliopewa katika Wizara yetu. Lini hasa? Naomba atuachie kwani siyo rahisi kutoa tarehe hapa Bungeni.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imefanya feasibility study (upembuzi yakinifu) kwenye malambo mengi na kwa kuwa swali la msingi la Bunda linafanana na Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini, je, Serikali ina mpango gani kuyajenga malambo hayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli huwezi kufanya jambo lolote katika mradi mkubwa bila kufanya upembuzi kwanza kuangalia jinsi utakavyotekeleza mradi huo. Kama alivyosema katika eneo lake kuna maeneo ambayo wamefanya feasibility study kujua gharama ya ujenzi itakuwaje na anataka kujua ni lini sasa kazi hii itafanyika. Naomba niseme wazi kwamba katika mchakato huu wa bajeti kila Halmashauri imetengewa bajeti yake kutokana na vipaumbele vilivyowekwa na bahati mbaya tulikuwa na ukomo wa bajeti.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, inawezekana feasibility study imeshafanyika lakini mradi haujionyeshi katika mwaka huu wa fedha. Lengo kubwa ni ndani ya kipindi cha miaka mitano mradi ule uweze kutekelezwa. Imani yangu kubwa ni kwamba kama feasibility study imefanyika, kama fedha hiyo haijatengwa specific katika Jimbo lake katika mwaka huu wa fedha, basi katika mchakato wa bajeti ya mwaka unaokuja itakuwepo ili malambo yajengwe wananchi wapate huduma ya maji.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda kueleza masikitiko yangu kuhusiana na mradi huu, mwaka 2014 alikuja Katibu Mkuu wa Chama akadanganywa kuhusu mradi huu. Akaja Waziri Kamwelwe Januari mwaka jana akadanganywa kuhusu mradi huu, mimi nimekuja Ofisi na hao uliowasema mwaka jana Desemba mradi ulikuwa uishe tukadanganywa tena.
Mheshimiwa Naibu Spika, nahitaji muda gani na mara ngapi kuja hapa kuuliza maswali haya na uwongo wa kudanganywa namna hii, wananchi kule umetaja 17,000 hawana maji?
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa miradi ya maji katika Jimbo la Mbulu Vijijini iko mingi, nayo hakuna muda ambao umetajwa wa kumalizika na mikataba imeisha, na mimi kule sina fundi kabisa au Mhandisi wa Maji ndani ya Halmashauri yangu.
Je, unanisaidia pamoja na kwamba tutakaa baadae kuhusu ya watumishi katika Wizara hii au katika sekta ya maji?
MHE. JOSEPH J. KAKUNDA - NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI):
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema wakati ninajibu swali la msingi kwamba mradi huu kimsingi umeshatekelezwa kwa asilimia 90 bado asilimia 10 tu, zikazuka changamoto ambazo zilizungumzwa kwenye kikao, zikaonekana kwamba zinatatulika, lakini usiku wa leo nimepata mwendelezo unaohusu changamoto za ziada ambazo tunahitaji kuzitatua baada tu ya kikao hiki.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote wa Haydom na Jimbo la Mbulu Vijijini kwamba mradi huu kama tutatatua hizi changamoto ambazo amekumbana nazo mkandarasi ninaamini ndani ya wiki mbili hadi tatu hii asilimia 10 itakuwa imekamilishwa, ndiyo maana tumesema ifikapo mwezi Aprili, tutakuwa tumekamilisha mradi huu.
Swali la pili, kuhusu watumishi, napenda nimwakikishie ndugu yangu Mheshimiwa Flatei kwamba tunaiangalia Wilaya ya Mbulu kwa ujumla na Halmashauri yake ya Mbulu Vijijini kwa uangalifu mkubwa kutokana na mazingira ya eneo lenyewe na physiology ya eneo lenyewe la Wilaya ambalo nimefika ni juu na tambarare zimechanganyika na kwa hiyo tutampatia Mhandisi wa Maji hivi karibuni.(Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji wanafanya kazi nzuri na imekuwa ikiwategemea kwenye kazi zote na hata kualika mikutano yote ya Wabunge, Madiwani na kufanya kazi kubwa, asilimia 20 ambayo Mheshimiwa Waziri ameitaja katika majibu yake ya msingi haijawahi kupelekwa hata siku moja.
Je, kwa nini sasa Serikali isilete namna nzuri ya kuwalipa moja kwa moja hawa Wenyeviti kwa sababu, ni viongozi ili pasiwe na utaratibu huu wa asilimia ambayo haijawahi kupelekwa tangu wameanza kazi hizi mpaka sasa? (Makofi)
Swali la pili, kwenye swali langu la msingi nilieleza habari ya Madiwani. Madiwani kimsingi wanapata posho ndogo ya shilingi 300,000 na kitu kama sikosei. Je, ni lini sasa mnaongeza posho hizi ili walau basi wafanye kazi nzuri katika chini ya Halmashauri zetu huko Wilayani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nafahamu concern ya Mheshimiwa Flatei, lakini jambo hili sio la Mheshimiwa Massay peke yake, naamini Wabunge wengi sana wanaguswa na jambo hili. Na ndio maana unaona Mheshimiwa Massay alivyosimama hapa watu wengi sana, kila mtu alismama kutaka kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu zangu naomba niseme ni kweli, kuna baadhi ya Halmashauri hizi posho hazirudi, lakini Halmashauri nyingine zinafanya vizuri katika urejeshaji wa posho hii ya asilimia 20. Ndiyo maana sasa tumesema katika mpango wetu wa kufanya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa, Sura Namba 290, tumeweka kifungu maalum ambacho kinampa Waziri mwenye dhamana na jambo hilo kuweka suala zima la regulation maalum ya kulilazimisha suala hili sasa liwe suala la kisheria sio suala la kihiyari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge ni kwamba utaratibu wetu katika jambo hili mimi ninaamini si muda mrefu sheria hiyo ya fedha itakuja hapa, tutaifanyia marekebisho, sasa itakuwa ni muarobaini na katika hili naomba niwasihi kwa hali ya sasa hasa Wakurugenzi wetu wote kwamba asilimia 20 kupeleka kila kijiji sio jambo la hiyari ni jambo la lazima sasa tulipeleke ili wananchi wetu kule chini waweze kufanya kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika ajenda ya posho ya Madiwani, ninakumbuka kwamba tulikuwa na Tume Maalum hapa ilikuwa maarufu kama Tume ya Lubeleje ambayo ilipitia maeneo mbalimbali na bahati nzuri Mheshimiwa Mzee Lubeleje amerudi tena Bungeni kama Senior MP, ilipendekeza mapendekezo mbalimbali, ndio maana tumesema kwa nyakati mbalimbali kwamba, Serikali inaangalia jambo hili na jinsi gani utaratibu wetu wa mapato utakuwa vizuri basi tutafanya marekebisho kwa kadri itakavyowezekana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa swali la msingi linahusiana na usalama wa wasafiri, na kwa kuwa Mheshimiwa Waziri aliahidi kuja maeneo ya Mbulu na kwa kuwa ile barabara ya lami ya kilometa tano ya Hydom na Dongobesh bado. Je, Mheshimiwa Waziri lini sasa atakuja Hydom kuangalia barabara ile ambayo haina usalama kwa wasafiri? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli anavyosema Mheshimiwa Mbunge na niko tayari wakati wowote kwenda kutembelea eneo hilo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, kwa kuwa sasa kutokana na vyeti feki vimeondoa kabisa watumishi wa afya katika zahanati zetu. Je, ni lini hasa hawa watumishi wataenda kuajiriwa yaani wanayo time frame kwa sababu sasa hivi zahanati zina shida katika huduma hii ya afya? Ahsante sana. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kutokana na vyeti fake, watumishi takribani 12,000 wameondolewa katika utumishi wa umma.
Hata hivyo, kibali kilichotolewa na Mheshimiwa Rais ni cha watumishi 15,000 na tunaamini kabisa kwamba hawa watakwenda kuziba. Mchakato wake ilibidi kwanza tufanye uhakiki mzuri kwamba waliotoka ni wa idara zipi na zipi, walimu ni wangapi, manesi wangapi na madaktari wangapi. Kazi hiyo tumeimaliza na tumeshakabidhi Wizara ya Utumishi na mchakato unaendelea. Bila shaka wakati wowote tunaweza tukawaingiza katika ajira watumishi hawa wapya.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante. Mheshimiwa Waziri alifika Hydom akaona matatizo ya maji yaliyoko pale na Dongobesh na certificate ziko Ofisini kwake, je atatusaidiaje sasa Certificates zilipwe kwa haraka ili miradi hii ikamalizika kwa wakati na kama alivyoahidi siku ile ulivyofika Hydom? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze sana ndugu yangu Mheshimiwa Flatei anafuatilia. Certificate kila zikifika hazichukui muda tunalipa, kuna moja iliyokuja tumeshalipa tayari, kwa hiyo, kama kuna nyingine imekuja asiwe na wasiwasi Wizara ya Fedha kupitia kwenye Mfuko wa Maji ambao Waheshimiwa Wabunge mnatusaidia sana kuutetea uongezeke fedha zake zinakuja bila wasiwasi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei tutalipa. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kuniruhusu niulize swali la nyongeza. Kwa kuwa swali hili la Ndanda la Bwawa la Lukuledi linafanana kabisa na bwawa lililopo Mbulu Vijijini, Bwawa la Mangisa ambalo linahudumia Kata ya Yaeda Ampa, Bashay na Gidihim na hali yake kwa kweli inaelekea kuisha kabisa kwa sababu linakauka.
Je, Serikali itatusaidiaje ili hili Bwawa la Mangisa liweze kupatiwa ufumbuzi ili vijiji nilivyovitaja viendelee kupata huduma ya maji?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kufanya clarification vizuri katika maswali yote.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la Mbulu kweli kuna changamoto kubwa ya hili bwawa ambalo Mheshimiwa Flatei analizungumzia, lakini naomba nikiri wazi kwamba miundombinu ya mabwawa katika maeneo mbalimbali imeendelea kuathirika siku hadi siku na kushindwa kuhakikisha uwezo wake unapotea.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika hali hiyo changamoto kubwa ni suala zima ambalo hata Naibu Waziri hapa amezungumza, uharibifu mkubwa wa mazingira katika vyanzo vya maji, watu wanapenda katika maeneo ya mabwawa kuweka mashamba, kinachotokea ni kwamba mvua inavyonyesha udongo unatiririka kutoka mashambani unaenda kujaza katika mabwawa na mabwawa haya yanakufa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Flatei tumeisikia hoja yako tutawatuma wataalam kwenda kufanya uhakiki kuangalia nini kinachotakiwa kufanyika pale. Hata hivyo, naomba niwasihi viongozi wote katika maeneo mbalimbali hasa katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, wahakikishe kwamba katika suala la vyanzo vya maji hasa mabwawa kuzuia vitendo vya shughuli za kibinadamu hasa kilimo, kwa sababu jambo hilo linaharibu miundombinu ya mabwawa katika nchi yetu. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Jimbo la Liwale linafanana kabisa na Jimbo Mbulu Vijijini; katika Mji wa Haydom hakuna Mahakama ila kuna kituo kikubwa cha polisi, kwa hiyo, mahubusu inabidi wapelekwe kilometa 86 kutoka Haydom mpaka Mbulu. Je, ni lini sasa pamoja na maombi niliyoleta watajenga Mahakama katika Mji wa Haydom?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (K.n.y WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nisiweke commitment ya ni lini lakini nimwambie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba ni mpango wa Serikali kuhakikisha tunaendelea kujenga Mahakama nyingi za Mwanzo katika nchi yetu. Kwa hiyo, pindi pale fedha zitakapopatikana pia Mahakama ya Mwanzo Haydom itaingizwa kwenye mpango ili wananchi waweze kupata huduma ya mahakama.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ametoa majibu yake kuhusiana na swali la msingi, je, ahadi hizi zinazotolewa kuhusu barabara hizi hasa ya Mbulu by-pass ambayo inakwenda mpaka Maswa, ni lini sasa Serikali itakuja na mpango wa kuzijenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye bajeti tumeonesha na Mheshimiwa Mbunge anajua na namshukuru kwa kufuatilia kwa sababu anajua ziko barabara mbili, hii by-pass ya kupita Eyasi na hiyo inayopita kwenye Jimbo lako Katesh, Haydom kwenda Mbulu Mjini na unafahamu tuko kwenye hatua nzuri tunaendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutaendelea kupeana taarifa na Mheshimiwa Mbunge ili kuona hatua nzuri zinavyokwenda ili naye aendelee kuwapa taarifa wananchi katika Jimbo lake la Mbulu. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa muda wa kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, tatizo sugu linaloonekana kwenye swali la msingi la Wanging’ombe linafanana kabisa na tatizo sugu la kukosekana maji Mbulu Vijijini. Kwa kuwa Mheshimiwa Waziri amefika katika Jimbo langu, kwanza namshukuru, lakini sasa tumesaini Mkataba na DDCA wa kuchimba visima sita (6), tangu Januari mpaka leo hawaonekani na hawakuchimba visima vile. Waziri atatusaidiaje sasa DDCA waje kuchimba visima ambavyo tumeingia nao mkataba na Halmashauri yangu Jimbo la Mbulu Vijijini? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Massay kwa jinsi anavyoshughulikia Jimbo lake. Nilishawahi kufika kule na ni kweli kwamba DDCA wamesaini mkataba wa visima sita. Kwa sababu hili suala ni la kiutendaji, mimi na yeye baada ya Bunge leo tuwasiliane ili tuweze kuwauliza DDCA kwa nini hawajapeleka mitambo kwenda kuchimba.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-
Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa katika majibu yake Mheshimiwa Naibu Waziri amesema mkataba ukisainiwa utachukua miezi sita mpaka mnara ujengwe. Nina minara mitatu ambayo kimsingi imejengwa miaka miwili mpaka sasa haijamalizika, kwa mfano; mnara wa Airtel ambao uko Maga, mnara wa Halotel ambao upo Gidilim na mnara wa Halotel mwingine ambao upo Tumati haujakamilika. Je, Mheshimiwa Waziri atasaidiaje minara hii ikamilike kwa sababu Serikali imeweka fedha nyingi ili wananchi wa Mbulu vijijini wapate mawasiliano?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa vijiji ni vingi ambavyo havina mawasiliano, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja kuonja taste ya kukaa nje ya mawasiliano? Kwa mfano; Getereri, Mewadan, Migo, Harbaghe, Endadug, Eshkesh, Endamasaak, Gorad na Endamilai, yuko tayari sasa kuja ili uone hali ya mawasiliano ilivyo vibaya Mbulu Vijijini ili akatupangia vijiji hivi kupata minara?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. Eng. ATASHASTA J. NDITIYE): Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna minara mitatu ambayo imefungwa muda mrefu na mpaka sasa haifanyi kazi ipasavyo. Kuna mnara wa Maga ambao ulijengwa na Airtel, kuna matatizo yaliyotokea kati ya wakandarasi na jamii inayozunguka eneo hilo iliyosababisha mpaka sasa hivi mgogoro ambao unaendelea kutatuliwa kwa ngazi ya kata.
Mheshimiwa Spika, nahakikisha kwamba naendelea kuwafuatilia hawa watu wa Airtel kwa sababu wao waliingia mkataba na UCSAF kwa ajili ya kupeleka mawasiliano. Masuala ya mgogoro kati ya Airtel na Kata yanatakiwa yatatuliwe miongoni mwao lakini mawasiliano ya wananchi wa maeneo ya Maga yapatikane.
Mheshimiwa Spika, vilevile eneo la Gidilim ambako Halotel wamejenga mnara kuna kama miaka miwili haujaanza kufanya kazi kutoka na Mkandarasi kutopata vifaa vya kutosha kupeleka maeneo hayo. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tunafuatilia yote hayo pamoja na Yaeda, Ampa ambako Halotel vile vile wamefunga ili kuhakikisha kwamba hiyo minara inaanza kufanyakazi kwa haraka sana.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, ni kuhusu kuambatana na yeye kuona maeneo hayo aliyoyataja. Kwanza nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Massay, kwa kweli anafanya kazi kwa bidii sana. Muda mwingi sana huwa tunawasiliana kuhusu masuala ya mawasiliano; na mimi kama mwenye dhamana ya mawasiliano namhakikishia kwamba Serikali tunajua umuhimu wa kuwa na mawasiliano kwa wote kwa sababu mpaka sasa hivi tuna asilimia 94 ya Watanzania wanawasiliana. Hatutaki wabaki hata kidogo inapofika mwisho wa mwaka huu, tunataka Watanzania wote wawe wanawasiliana. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana pamoja na majibu haya ya Serikali Jimbo la Mbulu Vijijini lina Kata 18 na tuna kituo kimoja tu cha afya na kama alivyosema kwamba tumetenga maeneo na wananchi wameshakusanya material yaani mchanga, simenti na wengine tumeanza kujenga, je, Serikali itaongeza nini katika jitihada hizi za wananchi ambao wenyewe wameamua kujenga vituo vya afya? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili kwa kuwa wamekiri kwamba Zahanati ya Hayderer miundombinu yake haifai ili zahanati ile ikahuishwe ikawa kituo cha afya, je, uko tayari sasa kuja pale ili kuangalia namna gani na kutusaidia ili tukapata walau kituo cha pili katika Jimbo la Mbulu Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimejibu katika majibu yangu ya msingi tunakubaliana kabisa na jithada zinazofanywa na wananchi katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya kama kazi nzuri ambayo imeanzishwa na wananchi wa Jimbo la Mheshimiwa Flatei.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekee naomba nichukue fursa hii kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Flatei Massay jinsi ambavyo amekuwa akipigania wananchi wake kuhusiana na suala zima la afya, na sisi Serikali kwa kuunga mkono ndio maana katika hospitali 67 za Wilaya ambazo zinajengwa na wao ni wanufaika. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa kadri bajeti itakavyokuwa inaruhusu na hasa kwa wananchi ambao tayari wameonesha jitihada zao katika kujenga vituo vya afya na zahanati sisi kama Serikali tutakuwa tayari kwenda kushirikiana na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini juu ya utayari wangu hata kabla yeye hajasema anajua kwamba mimi niko tayari kwenda kule kwake ili tuende tukaone kitu gani kiko site tuweze kushauri namna bora ya kuweza kupeleka huduma kwa wananchi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nitoe ombi, Hospitali ya Haydom umeme unakatika mara nyingi sana. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri atafute namna mbadala ya kusaidia umeme wa Haydom.
Swali sasa kwanza, nimshukuru Mheshimiwa Waziri alifika katika Jimbo la Mbulu Vijijini na kuahidi kwamba umeme utafika Endagichan Masieda, Endagichan Endamila, Yaeda Chini na Eshkeshi; je, ahadi hiyo bado ipo na umeme utafika vijiji hivyo?
Swali la pili; kwa kuwa Hospitali ya Haydom inatumia shilingi milioni 12 kwa ajili ya jenereta za dizeli kwenye vyanzo vya maji, je, Serikali ina mpango gani wa haraka ili kuisaidia hospitali ile kujihudumia vizuri kwa umeme kufika pale katika vyanzo vya maji?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa ya kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini.
Kwa kweli nampongeza kufuatia ziara aliyofanya Mheshimiwa Waziri katika Jimbo lake tarehe 9 Mei, 2018 na kama mwenyewe alivyosema Mheshimiwa Waziri alipofika katika Jimbo lake alitoa ahadi ya kuongezeka kwa vijiji 22 kwa kuwa Jimbo hili lina vijiji vingi. Kwa hiyo, namthibitishia Mheshimiwa Mbunge, vijiji alivyovitaja ni miongoni mwa vijiji ambayo Mheshimiwa Waziri aliahidi na tumeshaviwasilisha REA kwa ajili ya taratibu za awali za upembuzi yakinifu.
Swali lake la pili kuhusu Hospitali ya Haydom, Mheshimiwa Waziri kupitia ziara yake ya tarehe 9 Mei, 2018 alitoa maelekezo kwa TANESCO kukamilisha ukarabati wa miundombinu ili wananchi wa Mkoa wa Manyara wapate umeme wa uhakika kwa wakati wote. Kwa hiyo, naomba niwahimize TANESCO wakamilishe hiyo kazi mwisho wa mwezi huu. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Babati - Basodesh kuna korongo kubwa sana ambalo linawazuia watoto kwenda shule na kutokana na mvua hizi, ndiyo kabisa hali imekuwa mbaya. Je, Serikali ina mpango gani kuwasaidia watu hawa wa Hanang ili daraja au korongo hili likaweza kujengwa kwa sababu bajeti ya Halmashauri ya Hanang ni ndogo haiwezi kujenga barabara?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wilaya ya Hanang na Jimbo la Mbulu Vijijini lilikuwa pacha. Kuna barabara nyingine inayotoka Dongobesh kupitia Maretadu kwenda Haydom hapitiki kabisa kwa sababu ya mvua hizi ambazo zimekuwa nyingi maeneo ya kule Mbulu. Je, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ina mpango gani wa kusaidia kukarabati barabara hizi ambazo mvua nyingi zimeharibu kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti na Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami kwamba mvua zilizonyesha ni nyingi, mvua ni neema lakini wakati mwingine zikizidi pia zinaleta uharibifu mkubwa sana wa miundombinu. Kwa hiyo, kwa ujumla wake, naomba niwaagize Mameneja wa TARURA wa Wilaya zote mbili wakatazame uharibifu ulivyo, halafu waweze kushauri Serikali nini tuweze kufanya katika kusaidia ili wananchi waendelee kupata huduma.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Jimbo la Mbulu Vijijini na Halmashauri ya Mbulu tumejenga Shule ya Kidato cha Tano na kila kitu tayari na Mheshimiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI amekuja kuigagua. Tumetuma maombi na Naibu Waziri anafahamu tunahitaji kuianzisha mwaka huu na kila kitu tayari. Je, kibali hicho kinatoka lini ili mwaka huu watoto hawa waingie shuleni na kusaidia Tanzania ya elimu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia sana kuhusu shule anayosema na ombi lao liko mezani kwenye Wizara yetu. Naomba tu nimhakikishie kwamba tutalishughulikia mapema iwezekanavyo ili ikiwezekana katika mwaka wa masomo unaofuata wanafunzi wa kidato cha tano waweze kuingia katika shule anayosema.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyopo Ubungo inafanana kabisa na changamoto iliyopo Jimbo la Mbulu Vijijini. Tuna kituo kimoja tu cha afya Jimbo zima; je, Serikali ina mpango gani sasa wa kutuongezea angalau kituo kimoja ili katika huduma za afya jimboni, pakawa na hali ya kuwasaidia wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto iliyopo kwenye Kituo cha Afya katika swali la msingi, ni suala la eneo, lakini kwake yeye eneo siyo tatizo kama ambavyo iko Sinza, Palestina pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia naomba kwa dhati kabisa ya moyo wangu nimpongeze Mheshimiwa Flatei Massay kwa jinsi ambavyo amekuwa akilipigania Jimbo lake, amehakikisha kwamba Halmashauri inajengwa lakini pia ni miongoni mwa maeneo ambayo yanakwenda kujengewa Hospitali za Wilaya. Naomba nimhakikishie kwa dhati hiyo hiyo ambayo Serikali imeonesha kuhakikisha kwamba tunajenga Hospitali za Wilaya, ni azma yetu pia kuhakikisha kwamba tunajenga Vituo vya Afya vya kutosha na kwa kadri bajeti itakavyokuwa imeruhusu hakika hatutasahau eneo la kwake. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa, Mheshimiwa Waziri amesema fedha za TARURA ni kidogo na yeye amepita barabara za Mbulu, hasa Tumati kwenda Martado ni mbaya sana. Je, atatusaidiaje kwenye kipindi hiki ili barabara zile ziweze kutengenezwa na wananchi wakaondoa ile adha ya kupita kwenye barabara ambayo haipitiki kwa sasa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tulivyoeleza katika jibu la msingi na kama ambavyo amejibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa muuliza swali la msingi, Mheshimiwa Kwandikwa Naibu Waziri wa Ujenzi; taarifa ya tathmini ile ya kina ambayo tutaipata kuanzia kesho, hiyo ndiyo itakayotupatia taarifa sahihi ya barabara zote ikiwemo barabara ile ya kwenda Tumati ambayo tulipita na Mheshimiwa Mbunge kuanzia Yaeda Chini mpaka Tumati kule barabara si nzuri sana. Kwa hiyo, tutaiwekea utaratibu mzuri sana wa kipaumbele baada ya kuwa tumekubaliana vizuri zaidi na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Mbulu Vijijini lina uhaba sana wa umeme na Mheshimiwa Waziri amefika. Sasa lini atakuja kuwasha umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini na anafahamu kwa sababu amefika na vijiji vingi havina umeme. Atutajie tu lini atafika Jimbo la Mbulu Vijijini kuwasha umeme? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Mbunge, vijiji vya Mheshimiwa Mbunge vya Mbulu Vijijini na Mbulu Mjini vyote vipo kwenye mpango wa REA mwaka huu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika swali la msingi la Korogwe Vijijini na hali ya pale inafanana kabisa na Mbulu Vijijini. Barabara ya kutoka Sibiti-Hyadom-Mbulu kuelekea Karatu imeahidiwa kwenye Ilani. Je, ni lini sasa barabara ile itawekewa fedha hasa ukizingatia kwamba huu mwaka unaelekea kuwa wa mwisho?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Flatei kwa sababu ameifuatilia sana barabara hii lakini anafahamu pia kwamba barabara hii muhimu ziko hatua muhimu sana ambazo zinaendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kuanza kukamilika kwa ujenzi wa daraja katika Mto Sibiti. Ziko hatua nzuri zinaendelea ili kuweza kujenga kwa kiwango cha lami sehemu ambayo ilikuwa korofi katika eneo hili. Mheshimiwa Mbunge anafahamu pia harakati za usanifu kutambua gharama za barabara hii ambayo anaizungumzia kwamba tunaendelea kukamilisha zoezi la usanifu ili tuweze kujua gharama za ujenzi wa barabara hii. Baada ya kupatikana kwa gharama za ujenzi wa barabara hii, Serikali itaendelea kutenga fedha kuweza kuiboresha.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nitakuwa mchoyo wa fadhila kama nisiposhukuru kwa kweli kwa utayari wa Serikali kuanzisha Baraza la Ardhi la Wilaya ya Mbulu.

Mheshimiwa Spika, lakini bado, kwa kuwa Mheshimiwa Waziri ameonesha katika majibu yake ya msingi kwamba kuna changamoto hizi za watumishi na kwa kuwa wananchi wa Mbulu bado watakuwa wanakwenda Babati ambaki ni mbali kwa kutafuta hiyo huduma. Je, ni lini sasa ataanzisha Baraza hili ili wananchi hao wasisafiri umbali mrefu?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa wataalam walishakuja kuangalia maeneo ya kuanzisha Baraza hilo na tumeshawapa na jengo na kwa kuwa Wilaya ya Mbulu ni kubwa. Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kuja kuangalia na kuona eneo gani sahihi la kuanzisha barabara hilo?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza ni lini Baraza hili litaanzishwa. Katika majibu yangu ya msingi nimesema tayari Serikali imeshatupa Wizara Wenyeviti 20 ambao watapunguza kero katika baadhi ya Mabaraza ambayo hayakuwa na Wenyeviti wa kutosha, lakini pia kuna wale ambao hawakuwa na Wenyeviti kabisa watapelekwa. Kwa hiyo, mimi nimesema kwamba tayari Wenyeviti wapo, wanachosubiri kufanya sasa ni kupata tu maelekezo ya awali (induction course) kidogo ili waweze kwenda kufanya kazi zao, wakati wowote Baraza litaanza.

Mheshimiwa Spika, swali la pili ameuliza kwamba Baraza hilo litawekwa wapi. Naomba tu nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda katika eneo husika kwanza kujiridhisha na jengo lililoandaliwa, lakini pia na eneo lililopo. Kwa hiyo nitafika Mbulu ili kuweza kuona eneo sahihi ni lipi ambalo tutaweka baraza na wananchi hawatapata usumbufu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza nafasi kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa tatizo la umeme limekuwa na kasi na hali ni mbaya katika Jimbo la Mbulu Vijijini na Mheshimiwa Naibu Waziri amefika na vile vijiji alivyoahidi mpaka sasa umeme haujapatikana: Je, atatusaidiaje angalau umeme uweze kupatikana kwenye vijiji alivyoahidi Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nilitaarifu Bunge lako, kwamba miradi inayoendelea ya kupeleka umeme vijijini, miradi hii inachukua miezi 24. Kwa mujibu wa taratibu na kwa kuwa hizi LC (Letter of Credit) zilifunguliwa mwezi wa Saba mwaka 2018, naomba niwatie moyo Waheshimiwa Wabunge kwamba tunao muda wa kutekeleza huu mradi na kasi inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Mheshimiwa Flatei amekuwa mfuatiliaji mzuri, msimamizi mzuri, nimeshafanya ziara kwenye Jimbo lake, Mheshimiwa Waziri ameshaenda, tutamsimamia karibu Mkandarasi ambaye anafanya mradi katika maeneo hayo na miradi itakamilika kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mbulu Vijijini lina kituo kimoja tu cha afya, je wananchi wa Maretadu wamejenga sana kituo cha afya cha Maretadu, je, Mheshimiwa Waziriy uko tayari kutusaidia fedha ya kumalizia kituo cha afya Maretadu?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri yote ya kwanza. Namfahamu Mheshimiwa Flatei Massay na katika Jimbo lake kulikuwa na changamoto kubwa sana ya afya na ndio maana katika kelele zake nyingi sana kwa kuwaombea wananchi wake tulimpelekea hospitali ya Wilaya na kituo cha afya cha Dongobeshi. Hata hivyo, tunalichukua ombi hilo tutalifanyia kazi kwa sababu lengo letu na mkakati wetu wananchi wote wapate huduma ya afya, kwa hiyo jambo hili tutalichukua, tutaangalia jinsi gani ya kulifanyia kazi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza, kwa kuwa Halmashauri hazina uwezo wa kuwalipa Madiwani na mpaka sasa Madiwani wengi wamekopa posho zao; na kwa kuwa mapato madogo na hali hii inapelekea Madiwani kutolipwa stahiki zao: Je, Serikali ina mpango gani kubadilisha namna hii ili Serikali ilipe toka Hazina kama walivyo Watumishi wengine sasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Wenyeviti wa Vitongoji na Wenyeviti wa Vijiji nao wanafanya kazi sawasawa na Madiwani na Watendaji, hao Ma-VEOs na WEOs wanalipwa mishahara: Je ni lini sasa Serikali itawaona Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji ili kuwalipa posho au mshahara?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru. Swali lake la kwanza anapendekeza kwamba Waheshimiwa Madiwani walipwe posho kutokea Hazina na kwa maelezo yake anasema kwamba kuna Halmashauri ambazo hazina uwezo. Ukweli ni kwamba Halmashauri ambayo haina uwezo wa kujiendesha inapaswa kufutwa kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, lazima vyanzo viwe vimeainishwa na vinasimamiwa na hii hatujapata malalamiko rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachoelezea ni kwamba Halmashauri kwa mapato yake ya ndani wanajipangia namna ya kuweza kulipa Waheshimiwa Madiwani. Kama Serikali itapata uwezo mkubwa zaidi ya huu uliopo sasa, hili jambo litafanyiwa kazi. Kwa sasa Halmashauri zote zinapaswa kulipa na tunajua kuna Halmashauri ambazo Waheshimiwa Madiwani wanazidai fedha mpaka sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshaelekeza kila Mkurugenzi ahakikishe kwamba Madiwani wanalipwa stahiki zao kwa sababu wanafanya kazi kubwa. Swali lake la pili, anapendekeza pia kwamba kuwe na mpango wa kulipa Wenyeviti wa Mitaa. Ni kweli, nami ni Mwenyekiti wa Mtaa Mstaafu kule Kivule Dar es Salaam Ukonga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maelekezo ya Serikali kwamba kila makusanyo yote ya Halmashauri asilimia 20 inabidi irudi katika Mitaa yetu na Vijiji, inawezekana jambo hili halitekelezwi vizuri. Naomba niwaelekeze Wakurugenzi, Wenyeviti wa Vijiji kwa sasa, ile asilimia ambayo inapaswa kurejeshwa baada ya kodi kukusanywa katika eneo lao, ipelekwe na waweze kulipa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea kuwalipa asilimia nyingine zaidi hii au Serikali Kuu ichukue jukumu hili, kwa kweli itategemea uwezo wa Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyikiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri amefika Jimbo la Mbuli Vijijini na ameona changamoto iliyopo hapo inayofanana na Jimbo la Mlimba. Mheshimiwa Naibu Waziri aliahidi kisima kichimbwe Hyadom na tumeomba shilingi milioni 80 na akaahidi itatumwa. Je, ni lini sasa atatupatia fedha za kuchimba kisima pale Hyadom?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri sana anayofanya katika jimbo lake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilifika pale Hyadom tumeona kuna mradi mkubwa lakini katika kuhakikisha tunawaongezea chanzo kwa maana ya uzalishaji tukaona kuna haja ya uchimbaji wa kisima. Sisi tuna Wakala wa Uchimbaji Visima (DDCA), kwa hiyo, niwaagize wachimbe kisima kile haraka ili wananchi wa Hyadom waweze kupata ongezeko la maji na waweze kupata huduma hii muhimu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Zao hili la tumbaku ina changamoto zinazofanana na zao la vitunguu swaumu. Je, mna mpango gani sasa wa kusaidia zao la vitunguu swaumu kama zao la biashara kama ilivyo tumbaku?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbogo Flatei kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitunguu swaumu pia ni zao muhimu ambalo linaweza kuwapatia wakulima wetu kipato na liko kwenye fungu la spices, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwa sababu Serikali tuna mkakati wa pamoja wa kuhakikisha tunasaidia wakulima kupata masoko ya spices, basi na suala la vitunguu swaumu tutaliweka katika hilo fungu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri amefika na Serikali imetupa fedha ya kujenga hospitali ya wilaya, lakini Mheshimiwa Waziri atakumbuka tulimsimika kama Mzee wa Mbulu Vijijini na akatuahidi atatupatia Kituo cha Afya kile cha Maretadu na maombi yako kwake. Ndugu yangu awaambie watu wa Maretadu je, kituo cha afya kitaletewa fedha lini? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muungwana ahadi ni deni. Naomba Mheshimiwa Mbunge aendelee kuiamini Serikali kama ambavyo tumepeleka fedha katika Kituo cha kwanza cha Dongobesh, tukapeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, halikadhalika tutahakikisha kwamba, pale nafasi inapopatikana hatutasahau kwa sababu tumeahidi.
MHE. FLATEY G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa majibu ya Mheshimiwa Waziri yanasema fedha hazipatikani na zitengwe kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri ya Karatu; na kwa sababu ukiangalia mapato ya Halmashauri hayana uwezo wa kujenga hata bwawa: Je, Serikali haioni sasa itumie namna mbadala kutokana na hali hii ili kusaidia watu wa Bonde la Eyasi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kwa kuwa Wilaya ya Karatu na Wilaya ya Mbulu zilikuwa Wilaya moja na Bonde la Eyasi ni sawasawa na Bonde la Bashai: Je, kuna mpango gani pia wa kusaidia Bonde la Bashai kulipatia fedha ili skimu hii ipate kuendelea?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Swali la kwanza la Mheshimiwa Flatey Massay anasema kwamba Serikali ya Halmashauri ya Wilaya haina fedha ya kuweza kujenga hili bwawa wala miundombinu mingine mbadala wa vyanzo vya maji.

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, lakini kama nilivyosema katika jibu langu la msingi, Serikali tutaendelea kutenga bajeti ile ya kiserikali kutoka Serikali Kuu kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, lakini kama tulivyoelekeza, naye mwenyewe anajua. Hili Bonde la Eyasi kwenye kilimo tu cha vitunguu ndiyo linachangia mapato zaidi ya asilimia 33 ya Halmashauri hiyo ya Karatu, lakini haipeleki Halmashauri hiyo ya Karatu hata senti tano kuendeleza kilimo cha umwagiliaji na kilimo cha vitunguu katika bonde hilo.

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana kama Serikali tumeelekeza watenge kwenye mapato yao ya ndani asilimia 20 ili kwenda kunenepesha ng’ombe yule wanayemkamua kwenye vitunguu ili waweze kukamua zaidi siku zijazo. Hatujasema kwanza hicho ni chanzo pekee cha kuendeleza huko, hapana. Hicho ni kimojawapo, ndio maana nimesema kwenye ile programu ya Jenga, Endesha na Kabidhi kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Benki ya Rasilimali pia wanaruhusiwa kwenda kuchukua mkopo. Tutaenda kujenga hiyo miundombinu baada ya kuiendesha halafu baadaye tutakabidhi baada ya mapato hayo kuisha. Pia tutaendelea kutenga kwenye bajeti kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, skimu hii iliyokuwa katika Wilaya ya Jimbo la Mbulu pia utaratibu utakuwa ni huo huo na ombi lake nimelipokea, ni vizuri alete sasa hilo andiko na tutatuma Tume ya Taifa ya Umwagiliaji waende huko wakafanye tathmini na kuangalia mahitaji, baadaye tutaingiza kwenye bajeti kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa skimu hiyo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mbulu Vijijini, Mji wa Haydom hauna Mahakama na kutoka Haydom mpaka Mahakama ya Wilaya ni kilomita 86 na tunayo ahadi ya kujengewa Mahakama ya Mwanzo pale. Kutokana na Mbulu tumeshawapa eneo:-

Je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari sasa kutenga bajeti ya kujengewa Mahakama ya Mwanzo katika Mji mdogo wa Haydom? (Makofi)
WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, nasema Wilaya ya Mbulu ina mahitaji mengi ya huduma, mojawapo ni Mahakama. Kwa mpango nilionyesha hapa, nitafanya ushauriano na Mahakama Kuu na Msajili wa Mahakama tuone kwamba pale Haydom tutachukua hatua gani. Ila kama iko kwenye mpango; na nadhani iko kwenye mpango, nitathibitisha, tutajitahidi kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Spika, nataka pia nichukue nafasi kusema, kuna Mbunge alisema juzi kwamba kuna mahabusu ambao wanachukuliwa na bodaboda kutoka Magereza kwenda Mahakamani katika Gereza la Ulanga. Nimezungumza na DPP ambaye alikuwa kule Ulanga hivi karibuni, anasema hakuna haja ya kutumia pikipiki wala gari kupeleja mahabusu katika Mahakama ya Ulanga kwa sababu watu wanaweza kutembea siyo zaidi ya mita 500 kutoka kwenye Gereza lile mpaka kwenye Mahakama.

Mheshimiwa Spika, kama Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani alivyosema, taarifa ile ilikuwa imetiwa chumvi. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza Kijiji cha Yaeda Chini, Masieda, Endamilay na Mbullu Vijijini wamesaini mikataba ya kujenga minara TTCL na Holotel wameondoka. Je, ni lini Mheshimiwa Waziri watarudi hawa TTCL kujenga minara Mbullu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu TTCL wamepewa kandarasi ya kujenga minara maeneo mbalimbali. Tatizo au changamoto ambayo ilikuwepo kidogo ni kwamba TTCL wanavyopewa kazi sambamba na wakandarasi wengine kwa maana hawa Tigo, Airtel, Vodacom kidogo tumekwenda kusuasua, siyo kusuasua kwa sababu wenyewe sasa kama taasisi ya Serikali lazima wafuate Sheria ya Manunuzi ambayo imetuchelewesha kwenda kusimika minara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, hatua za manunuzi ziko vizuri kwa maana TTCL watakuja katika eneo lake na kusimika ile minara ambayo wamepewa fedha na Mfuko wa Mawasiliano. Kwa hiyo, avute tu subira wanakuja na tutaweka hiyo minara kuongeza mawasiliano katika eneo lake.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa masoko haya ya vitunguu yamekuwa tatizo karibu maeneo mengi, je, kuna mpango gani sasa kama Serikali kusaidia eneo hilo la msitu wa tembo na maeneo hayo ili wachuuzi wanapokuja basi waweze kuuza vitunguu vyao katika hali ya biashara.

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa eneo la Simanjiro ni kubwa sana na walima vitunguu kwa maeneo hayo. Je, unaonaje, uko tayari kushirikiana na Mbunge wa Simanjiro ili kusaidia ujenzi wa soko la vitunguu katika Jimbo la Simanjiro? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, kwanza niseme tu kwamba katika mikakati ya Tanzania kwa ujumla wake na hasa katika kuwezesha biashara kufanyika katika mazingira mazuri, suala la ujenzi wa masoko pamoja na kuweka muunganiko kati ya wafanyabiashara na wazalishaji ni jambo muhimu sana. Kwa hiyo, kwa ujumla wake niseme tu kwamba kwa kushirikiana na ofisi ya Rais TAMISEMI Wizara ya Viwanda na Biashara lakini pia pamoja na uwekezaji kwa pamoja tunaangalia kwanza kusaidia katika suala la kuongeza thamani mazao hayo kwa kuwezesha kuwepo kwa viwanda vidogo vidogo na viwanda vikubwa. Vilevile kuhakikisha kwamba bei zinazotumika zinakuwa ni nzuri na sio zile za kuwanyonya wakulima ikizingatiwa pia suala la vipimo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Hali ya ukosefu wa maji iliyopo Simanjiro inafanana kabisa na Mbulu Vijijini, Mheshimiwa Naibu Waziri umefika Mbulu Vijijini. Je, miradi hii ya maji na kisima cha Hyadom ulichotoa ahadi nini unatimiza, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ninachotaka kumhakikishia Mbunge maji hayana mbadala na nilikwishafika katika Jimbo lake na kuna fedha ambayo tuliikuta, nawaagiza sasa DDCA wafike haraka katika kuhakikisha wanakichimba kisima kile ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante pamoja na mazuri ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Bashay tunazalisha vitunguu na tunasindika pale pale kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri tunasindika kwa kutumia mashine ile na kwakuwa tuna rojo na oil na tuna powder; je, Mheshimiwa Naibu Waziri haoni kwamba sasa umefika wakati wewe mwenyewe kuja Bashay kuwasaidia wakulima kwa changamoto hii ya uuzwaji wa vitunguu saumu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili kwa kuwa kuna wanunuzi na walanguzi ambao hawafuati taratibu kama alivyosema kwenye jibu la msingi; je, aoni yeye mwenyewe hataisaidiaje AMCOS ya Bashay kuondokana na uchuuzi huo ambao haufuati vigezo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anataka kwamba Serikali tufike pale ili kuona changamoto hii na kuona namna ya kuwasaidia wakulima hawa, kwamba nikimaliza ziara ya Mikoa ya Katavi na Rukwa basi mkoa utakaofuata ni Mkoa wa Manyara pamoja na kufika Mbulu Vijijini kuangalia hali halisi ya wakulima wetu wa vitunguu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili anataka kujua kwa sababu sasa hivi ni chama kimoja tu cha msingi kinanunua mazao haya ya vitunguu kutoka kwa wakulima na wanapitia watu mbalimbali kwa ajili ya ununuzi huo, nitafika wakati huo huko kwa ajili ya kuona utaratibu huo wa ununuzi unaofanyika, hasa hawa waliosema kwamba ni madalali ambao sisi tunawaita kwamba ni wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo. Lengo kwamba tutaweza kuunganisha na kuweka mfumo rasmi kwamba kila kijiji wafungue vyama vya msingi vya ushirika ili viweze kukusanya mazao kutoka kwa wanachama wao na wakulima, baadae hawa wanunuzi wadogo wa kutoka ndani na nje ya nchi wakija watumie vyama hivi vya msingi kununua mazao kutoka kwa wakulima.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la msingi lipo kwenye Jimbo la Mbulu Mjini na mimi nipo Jimbo la Mbulu Vijijini. Jimbo la Mbulu Vijijini kuna kata 18, Mheshimiwa Waziri umefika umekuta kituo kimoja cha afya kama mke wa Mkristo; unaonaje ndugu yangu? Maretadu wamejenga kituo cha afya wamefika lenta; utatupatia fedha ili walau tuwe na kituo cha pili cha afya?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kweli nimefika Mbulu na ni kweli ni changamoto kubwa ndiyo maana Serikali katika eneo lile kutokana na shida kubwa tulianza na ujenzi wa Kituo cha Afya cha Dongobesh. Lakini hata hivyo tuliamua kutoa fedha zaidi ya shilingi 1.5 billion kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbulu Vijijini.

Mheshimiwa Spika, nafahamu Mbulu jinsi ilivyo kuna maeneo wengine wako katika Bonde la Ufa na wengine wako juu. Tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo kama maombi Mheshimiwa Mbunge alivyoyaacha mara kadhaa ofisini kwetu tutajitahidi kwa kadri iwezekanavyo wale watu wa kata zingine kule za mbali tuangalie jinsi gani tutafanya tupate fedha kuwasaidia ujenzi wa kituo cha afya.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza pamoja na majibu aliyonipa Mheshimiwa Naibu Waziri umeme mahali ambako umekwenda kama alivyosema kwenye majibu ya swali maeneo ya taasisi na visima vya maji vimerukwa. Swali la kwanza kata za Mahitadu, Masieda, Endage Chan, Heda Chini, Getiree, Bashai, Endamillai, Rolward, Endargati, Esheshi, lini zinapata umeme?

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru pia umefika kwenye jimbo langu na Mheshimiwa Waziri amefika na iko ahadi ya vijiji 22 kupatiwa umeme mwaka huu. Na leo ni bajeti ya wizara yako je, Mheshimiwa Waziri vijiji hivi na ahadi hii vipo katika bajeti hii au nitegemee nini niwaambie wananchi wa Mbulu Vijijini?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze sana Mheshimiwa Naibu Waziri katika maswali ya msingi ya Mheshimiwa Mbunge. Nimpongeze sana Mheshimiwa Flatei Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini alivyofuatilia masuala ya umeme vijijini.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli zipo kata sita ikiwemo Masieda, Yaendachini pia Endagi chan pamoja na Gorand, na Esheteshi pamoja na Bashi. Zipo umbali wa takribani kilometa 15 kutoka Ngoradi na kilometa 14 kutoka Mbulu Mjini. Lakini utaratibu tunaofanya sasa wananchi wa kata hizo TANESCO pamoja na REA wameshaanza kushirikiana na utekelezaji wa kupeleka umeme katika vijiji hivyo unaanza mwezi Julai mwaka huu na utakamilika Desemba mwaka huu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge wafikishie taarifa wananchi wa Mbulu Vijijini kwamba utekelezaji wa miradi hiyo katika kata hizo utafanyika kama kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika swali lake la pili ahadi ni lini, taasisi pamoja na maeneo mengine tuwape uhakika. Mheshimiwa Mbunge anavyofuatilia masuala ya Mbulu Vijijini anavyo vijiji 76 na kati ya hivyo tayari vijiji 32 tumevipatia umeme, vijiji vinavyobaki nikupe taarifa na tathmini ya Serikali imekamilika vyote vitapelekewa umeme ifikapo mwezi Juni, 2021.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, umepita Barabara ya Mbulu kwa upande wa Mashariki na Mheshimiwa Naibu Waziri amepita barabara hiyo ya Mbulu kwa upande wa Magharibi. Je, Mheshimiwa Naibu Waziri utuambie sasa na uwaambie wananchi wa Mbulu, barabara ile ya Mbulu – Haydom – Mbulu inajengwa lini kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli ziko changamoto katika huu ushoroba kwa maana ya hii barabara kuu ambayo anaizungumza Mheshimiwa Mbunge kwa maana itatuunganisha kutoka Karatu, tutakuja Mbulu, tunakwenda Dongobesh, tunakwenda Haydom, tunapita kule Sibiti ambako daraja kubwa limekamilika halafu tutakwenda kwenye Mikoa ile ya Shinyanga, Mkoa wa Simiyu, Mwanza, hii barabara muhimu na niseme tu na kuwahakikshia wananchi wa Mbulu na majirani zao ni kwamba, tunaanza sasa ujenzi kwa sababu ule usanifu ulishakamilika na katika bajeti hi mliyotupitishia tumetenga kuanza ujenzi wa kiwango cha lami wa kilometa 50 kutoka Mbulu kuja Dongobesh na tutaendelea hivyo hivyo kadri tutapopata fedha mpaka barabara hii muhimu iweze kujengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Yaeda Chini kimejengwa na wananchi mpaka kufikia mwisho, kilichobaki ni nyumba za askari. Je, Serikali ipo tayari kuleta fedha za kujenga nyumba za askari ili kituo hicho kifunguliwe?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, Mbunge wa Mbulu Vijiji, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nichukue fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Flatei kwa jitihada zake kubwa sana. Niliwahi kwenda huko tukashirikiana naye katika kuhakikisha kwamba tunatatua changamoto hii na ameichukua kwa haraka sana na kuifanyia kazi, amejenga kituo kizuri tu.

Mheshimiwa Spika, kwa maana hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwamba Serikali inazithamini sana jitihada zake na za wananchi wa jimbo hilo na hivyo basi katika mkakati wetu wa nyumba za askari nchi zima, tutakapokuwa tumefanikiwa kupata uwezo basi tutashirikina naye vilevile kutatua tatizo hilo la makazi ya askari ili kituo hicho kiwezi kufanya kazi vizuri zaidi. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY:Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali hili muhimu sana la nyongeza. Kwa kuwa amesema katika majibu yake ya msingi kwamba ametenga milioni 401 na ni wazi haiwezi kujenga barabara na Rais ameahidi mara mbili kwenye vipindi vyake viwili, je, haoni sasa aje na mpango mzuri wa kujenga barabara hii kwa kuitengea fedha?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, naomba nimalize tu mwenyewe kwa vile nimeanza. Nimshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na anafahamu na niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge kama walivyosimama, nilipokuwa Naibu Waziriwa Ujenzi nilitembelea sana maeneo haya kwa sababu ya upendo mkubwa sana wa Waheshimiwa Wabunge, lakini pia kwa shida ambazo niliziona katika maeneo haya. Jiografia ya maeneo haya siyo nzuri Mheshimiwa Spika ndiyo maana kama nilivyosema awali kwamba Serikali imetenga fedha kuweza kuwakwamua wananchi wa maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anafahamu hata ile barabara kuja Babati imeendelea kutengenezwa naamekuwa na mradi wa kilomita mbili za lami pale kwake ni kwasababu Serikali ina upendo mkubwa.

Mheshimiwa Spika, nimpongeze sana na kumshukuru Mheshimiwa Rais sana kwasababu katika juhudi za kutengeneza barabara za nchi hii tumeshuhudia kipindi kilichopita madeni ya wazabuni kiasi kikubwa sana yamelipwa na hii inaashiria kwamba tutaenda kutengeneza barabara kwa kasi kubwa zaidi, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, kwa kuwa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri mwenyewe kwamba barabara hii ina umuhimu na sasa kwa miaka miwili imekuwa ikiwekwa kwenye bajeti na haikujengwa na amesema imetegwa shilingi bilioni 5, je, atuambie ni lini atatangaza tenda ili barabara hii ianze kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa anajua wazi kwamba bilioni 5 haiwezi kujenga barabara na barabara hii iko kwenye Ilani ya uchaguzi mwaka 2015-2020 na 2020-2025 na Mheshimiwa Rais ameahidi kwenye kampeni juzi hapa, je, yupo tayari kuweka fedha kwenye bajeti ya mwaka 2021/2022 ili kumaliza kilomita zingine 20 kufika 70 kufikia eneo la Haydom?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini jana pia aliuliza swali la nyongeza lakini leo pia ameleta swali la msingi, kwa hivyo, natambua jinsi anavyofuatilia barabara hii kwa ajili ya wananchi wa Wilaya ya Mbulu. Nimhakikishie kwamba kwa kuwa tayari fedha za awali zimeshatengwa hizo shilingi bilioni 5, kwa hiyo, taratibu za awali zitaanza ikiwa ni pamoja na kutangaza tenda na kufanya shughuli za awali za kuanza ujenzi wa barabara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye jibu langu swali namba 28 kwamba Serikali imeahidi barabara zote ambazo imezitolea ahadi katika Ilani lakini pia ni ahadi za Rais katika kipindi cha miaka hii mitano zitatekelezwa ikiwa ni pamoja na barabara hii ya Karatu – Dongobesh - Haydom ambayo Mheshimiwa Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini anaiulizia. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza, Mbulu Vijijini tumepata minara sita ambayo imejengwa. Mwingine umejengwa 2017, mingine inayofuata imejengwa mpaka juzi hapa lakini sasa minara hii sita haifanyi kazi.

Je, Mheshimiwa Waziri ana mpango kuwafuata au kuwaona wakandarasi ili wawashe minara hii sita ambayo sasa wananchi wanaisubiri mpaka leo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa amesema kata hizi atazipelekea mawasiliano na kujenga minara; je, kata zilizobaki lini zinakwenda kupata hiyo minara ambayo amekwishaisema?
NAIBU WAZIRI WA MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kulingana na changamoto ambayo ilikuwepo ya masuala ya ujenzi, kata hizo zilikuwa zimechelewa kukamilishiwa miradi hiyo. Hata hivyo, hivi navyoongea wataalam wetu tayari wameshaanza kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia naomba kutumia fursa hii kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna hatua mbili katika ujenzi wa minara; kuna hatua ambayo inatokana na ujenzi wa mnara wenyewe ambao tunaita passive equipment na hatua ya pili ambayo sasa ni kuweka vile vifaa ambavyo tunaita kwamba ndiyo active equipment.

Mheshimiwa Naibu Spika, vifaa hivi tumekutana na changamoto ya wakandarasi wetu ambao walikuwa wamepewa majukumu ya kukamilisha miradi hii kwa sababu wanatumia sana vifaa kutoka nje na mwaka jana tulikumbana na changamoto ya Corona, hivyo tukaona kwamba tuwaongezee muda ili waweze kukamilisha ujenzi wa minara hii. Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, suala hili tayari tunalifanyia kazi na hizi kata ambazo amezisema tayari wataalam wetu wameshafika site kwa ajili ya kujua nini kinafanyika ndani ya muda ambao unatakiwa. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninalo swali la nyongeza.

Kwa kuwa asilimia hizi zipo kisheria na bado kuna ukakasi katika mgawanyo huu; je, yupo tayari sasa kuja kuona uhalisia wa suala lenyewe katika Jimbo la Mbulu Mji na Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Naibu Spika, niko tayari kushirikiana naye na Halmashauri ya Mbulu kuweza kuona namna gani tunatatua huo ukakasi ambao Mheshimiwa Mbunge ameuripoti uliotokana na mgawanyo wa mali kati ya Halmashauri ya Mbulu Vijijini na Halmashauri ya Mbulu Mjini.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba baada ya Mkutano huu wa Bunge tutapanga tuone utaratibu mzuri wa kuwaza kutatua changamoto hiyo. (Makofi)
MHE. FLATEI I. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Butiama ni majimbo ya zamani kama ilivyo Mbulu Vijijini na changamoto ya umeme karibu zinafanana. Zipo Kata za Masieda, Eda Chini, Eshkesh ambazo Mheshimiwa Waziri naye alikuja akaziona. Je, ni lini sasa maeneo hayo niliyoyataja yatapata umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa REA, unapeleka umeme katika vijiji vyote vilivyokuwa vimebakia katika awamu zilizotangulia bila kupelekewa umeme.

Kwa hiyo, nimhakikishie Mbunge kwamba katika awamu hii inayoanza ambayo pengine imeshaanza kwenye maeneo mengine na kufikia Disemba, 2022 vijiji vyote vilivyo katika eneo lake vitapata umeme na vitongoji vitapata umeme kupitia utaratibu huo huo kwa sababu mkandarasi anapopeleka umeme kwenye Kijiji kimsingi anaunganisha wateja kwenye vitongoji na kuunganisha wateja kwenye kaya na mteja mmoja mmoja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu kwa ujumla kwamba vijiji vyote Tanzania Bara vilivyokuwa havina umeme, vitapelekewa umeme katika awamu ya tatu, mzunguko wa pili wa REA bila kukosa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Mbulu Vijijini liko juu ya Bonde la Ufa na vijiji vingi sana havina maji, ni kwasababu ya Bonde la Ufa. Na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, alifika wakati wa kampeni na kuahidi vijiji vile vitapata maji kutoka kwenye Ziwa la Madunga, Je. Mheshimiwa Waziri, lini ahadi ya Mheshimiwa Rais itatimizwa kwa wananchi hawa kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge suala hili kama tulivyokubaliana, tunaliingiza kwenye mpango mkakati wetu wa mwaka wa fedha 2021/2022 na mradi huu utaaanza utekelezaji wake mara moja mara baada ya Mwaka wa Fedha mpya kuanza.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa vijiji vya Aicho vina vijiji pacha vya Gembak, Kamtananat, Maretadu-Chini, Khaloda, Umburu, je, ni lini vijiji hivi vitachimbiwa visima vya maji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwakuwa Wakala wa Maji alishachimba visima sita Jimbo la Mbulu Vijijini katika Kijiji cha Khababi, Labai, Endagichani, N’ghorati, Gendaa Madadu-Juu, je, lini sasa watamalizia kazi ya usambazaji kwa sababu walishamaliza kazi ya uchimbaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Zacharia, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, lini vijiji pacha ambavyo amevitaja Mheshimiwa Mbunge vitapata visima vya maji. Wizara tumeendelea kujipanga kwa dhati kabisa kuona kwamba kwa miezi hii miwili iliyobaki katika mwaka huu wa fedha kuna maeneo ambayo visima vitaendelea kuchimbwa na kwa mwaka ujao wa fedha tumetenga visima vingi vya kutosha karibia majimbo yote. Kwa hiyo na vijiji hivi tutaendelea pia kuvipa mgao kadri fedha tutakavyoendelea kuzipata.

Mheshimiwa Spika, kuhusu visima sita vilivyochimbwa usambazaji wa maji utaanza lini, tayari tumeendelea kujipanga, maeneo ya aina hii tunahitaji kuona wananchi wanapata maji kutoka kwenye mabomba. Kwa hiyo, usambazaji utaendelea kuwa wa haraka. Kwa eneo hili la visima sita naagiza watu wa Babati (BAWASA) wajipange vizuri kwa sababu ipo ndani ya uwezo wao waweze kukamilisha kazi hii.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Elimu, kutoka Mbulu Vijijini sehemu ya Haydom kwenye Mbulu Mjini ni kilometa 90 na kwenda Babati ni zaidi ya kilometa 130. Kwa majibu yake haoni kwamba atakuwa amewaondolea fursa vijana wa Mbulu Vijijini kupata uzoefu na ufundi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kwa kuwa Mbulu Vijijini hatuna kabisa chuo, je, yuko tayari kutenga fedha sasa ili bajeti ijayo tuweze kupata chuo katika Jimbo la Mbulu Vijijini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kutoka Mbulu Mjini mpaka Mbulu Vijijini ni kilometa 90 lakini kama nilivyojibu katika swali langu la msingi kwamba Serikali inafanya juhudi mbalimbali za kutafuta fedha ili kuendelea na mpango wake wa ujenzi wa vyuo hivi vya VETA katika kila wilaya na mkoa. Kwa hiyo, nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali itakapopata tu fedha tutahakikisha kwamba maeneo yote ikiwemo na Mbulu Vijijini yatajengewa vyuo hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hivi sasa naomba kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa tuna vyuo vingi ambavyo viko katika Wilaya ile ya Mbulu kiujumla. Tuna Vyuo vya Ufundi Stadi Mbulu, Haydom, Masieda, Jiendeleze, Integrity na St. Jude Yuda Thadei. Vyuo hivi vyote vinaweza kutumika kwa ajili ya vijana wetu kupata uzoefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hilo, vyuo nilivyovitaja mwanzo vile vya Manyara vina nafasi ya wanafunzi kulala pale pale chuoni. Kwa hiyo, wanafunzi wetu hawa wanaotoka mbali wanaweza kupata fursa ya kupata ujuzi wao pale na kuondoa usumbufu huu wa kutembea au kwenda umbali mrefu.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Swali la msingi linafanana kabisa na Jimbo la Mbulu Vijijini na changamoto iliyopo Hanang’ inafanana kwa sababu ilikuwa ni wilaya moja. Barabara ya kutoka Mugitu kuja Hydom iliahidiwa na ipo kwenye Ilani ya Uchaguzi na Mheshimiwa Naibu Waziri aliipita. Je, ni lini tunajengewa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatel Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Barabara ya Mugitu - Hydom imeshakamilishwa kufanyiwa usanifu wa kina na sasa hivi kinachosubiriwa ni upatikanaji wa fedha ili ianzwe kujengwa kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Mbulu kwamba kadri fedha zitakapopatikana barabara hii itajengwa pia na ndio maana tayari usanifu wa kina umeshafanyika ikiwa ni maandalizi ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwanza nionyeshe furaha yangu kwa Serikali kwa kukubali kujenga hii Mahakama ya Mwanzo ya Hydom. Swali, Mahakama ya Wilaya bahati mbaya eneo lake limepitiwa na barabara, je, Wizara ina mpango gani wa kuingiza kwenye bajeti zao ili Mahakama ile ipate kujengwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; Waziri amesema Mahakama imeanza kujengwa, je, yupo tayari sasa kwenda Hydom kuona ule ujenzi unaendeleaje ndani ya Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimtoe wasiwasi kwenye mfumo huu wa Mahakama asicheze ile sarakasi aliyokuwa ameiahidi kwenye Wizara ya Kilimo. Kwa hiyo nipende tu kumuhakikishia kwamba kwenye swali lake la kwanza la nyongeza kuhusu ile Mahakama ya Wilaya kupitiwa na barabara hilo tutalifanyia kazi na kwa kushirikiana naye tutajua namna ya kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la kutembelea Mahakama inayoendelea kwenye ujenzi, nipo kwenye ratiba leo ninapomaliza kujibu swali hili nakwenda huko Hydom. Kwa hiyo nimualike tu Mheshimiwa Mbunge tufuatane naye kwa sababu tunahakiki yale majengo yanayoendelea kujengwa. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, nikisikia barabara inayotoka Simiyu kuja Kolandoto ni kama inanitonesha vile kidonda. Mheshimiwa Naibu Waziri ulisema tender itatangazwa; je, lini mnatangaza tender kwa barabara hii?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, barabara anayoisema ya Mbulu na hasa Mbulu Hydom yenye kilometa 50 ipo kwenye mpango wa kutangazwa kabla ya mwisho wa bajeti ya mwaka huu. Kwa hiyo, taratibu zote za manunuzi zote zinakamilisha, muda wowote barabara hii itatangazwa kabla ya kuanza bajeti ya mwakani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara hii ambayo pia Mheshimiwa aliombea kupiga sarakati itatangazwa kabla ya mwisho wa mwaka huu, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hospitali nyingi za Halmashauri zimebaki bila kumalizika na kwa bahati mbaya Serikali imekuwa na tabia ya kupeleka fedha na mwisho wa bajeti inazichukua. Jimbo la Mbulu Vijijini hospitali imefikia asilimia 95 kumalizika.

Je, ni lini Serikali itarudisha shilingi milioni 300 ilizozichukua ili hospitali ile iweze kumalizika?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tatizo ambalo amelizungumzia Mheshimiwa Mbunge Massay limetokea kwenye Wilaya nyingi hapa nchini, hata ikiweko Wilaya yetu ya Siha.

Mimi ninachoweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge tukimaliza hapa, hebu tutoke mimi na wewe twende Hazina tuangalie ni nini kimetokea na waweze kusuluhisha hilo tatizo liweze kufanyiwa kazi na fedha hizo zipatikane kazi hiyo imalizike ambayo ni asilimia tano imebaki ili hiyo hospitali ianze.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiii ndiyo ile barabara ambayo nilitaka kuruka somersault humu ndani. Kwanza niishukuru Serikali kwa kutangaza hizi kilometa 25.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa kwenye bajeti ya Serikali ziko kilometa 50;

Je, ni lini unatangaza tena slot iliyobaki ya kilometa 25?

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwa kuwa amesema barabara hii ina kilometa 70,

Je, kilometa 20 zinazobaki point tano atatangaza lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Grerory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini, kwa pamoja kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru kwanza leo hajataka kuruka sarakasi. Na kama alivyoahidi Mheshimiwa Waziri wakati wa bajeti kwamba barabara hizi zitatangazwa ni kweli zimetangazwa, na hizo kilomita 25 zinaanza kujengwa kwa bajeti ya mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika bajeti ya mwaka tutakayoanza Julai pia kuna fedha imetengwa. Kwa hiyo tutaendelea na ujenzi kadri fedha itakapopatikana, lakini kwenye bajeti pia tumetenga. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri fedha itakapopatikana kilomita zote na barabara yote hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa
kuwa mgawanyo wa Halmashauri hizi mbili ulitangazwa kwenye GN ya mwaka 2015, kwa nini sasa ichukuwe miezi mitatu wakati tangazo liko wazi na sheria hii iko wazi sana?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Flatei Massay ameeleza kwamba GN ni kweli ilitoka mwaka 2015 lakini bahati mbaya sana tamko la wazi lilicheleweshwa kuwasilishwa. Kwa hiyo, nikiri kabisa kwamba nafikiri kulikuwa na kupitiwa kwenye utekelezaji wa jambo hili na ndiyo maana, kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita tuko hapa, tumeahidi kulitekeleza ndani ya miezi mitatu ili kuhakikisha jambo hili limeisha kabisa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, nimpongeze Naibu Waziri kwa kazi anayofanya na Waziri mwenyewe kwenye Wizara hii. Lakini tatizo lililoko sasa REA inapokwenda kwenye kupeleka umeme vijijini zinapelekwa nguzo 20 tu na kwa sababu ni vijijini, nyumba ziko mbalimbali inatokea nyumba 10 tu zinapata umeme vijijini. Je, REA mnaonaje kwa nini msiongeze nguzo ili nyumba nyingi zikapata nguzo kuliko kupata nguzo hizo 20? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Waziri amekuwa akitoa taarifa ya wateja wanaotumia unit chini ya 70 kuuziwa unit kwa shilingi 100. Lakini sasa wateja hawa wanauziwa unit kwa shilingi 300. Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa taarifa humu ili wananchi hawa wakajua nini hasa, umeme unatakiwa kulipiwa kwa hawa wateja wanaofikisha unit chini ya 70? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya ngongeza ya Mheshimiwa Flatei kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kumshukuru kwa pongezi alizozitoa kwa Wizara na kweli tunaendelea kujitahidi kwa maelekezo ya Serikali kuhakikisha tunatimiza maelekezo tunayopewa. Lakini nimpongeze kwa kufuatilia maeneo kwenye Jimbo lake na mimi nilienda kuzindua umeme na mambo yanakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na nimuhakikishie kwamba nguzo 20 ni kwa wateja wa awali. Naomba uniruhusu nichukue nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa Wabunge wote kwamba, tunapoendelea na mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili karibia kila eneo tumetoa kwa kuanzia nguzo 20. Lakini ni wateja tunawaita wateja wa awali sio kwamba ndio tumemaliza zoezi, kadri muda unavyozidi kuendelea TANESCO wataendelea kupeleka umeme katika maeneo hayo. Lakini pia REA wenyewe wataendelea kuongeza wigo wa kazi wanayoifanya kuhakikisha kwamba sasa watu wengi zaidi wanapata umeme katika maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika eneo la pili kuhusiana na gharama za umeme. Kabla sijajibu kwanza nipende kutoa shukurani zetu kubwa sana kwa Mheshimiwa Rais wa Awamu ya Sita, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuamua kuwapenda watanzania na kuwafikishia huduma ya umeme kwa gharama nafuu. Kwanza nguzo haziuzwi, mita haziuzwi, nyaya haziuzwi na connection ya umeme ni shilingi 27,000/= tu na hayo ndio maelekezo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo la umeme mwaka 2016 zilitengenezwa Kanuni kulingana na mazingira tuliyokuwa nayo, ambazo zilikuwa zinasema waunganishiwaji wote wa umeme na watumiaji wa umeme wa maeneo ya vijijini watauziwa unit 1 kwa shilingi 100 endapo matumizi hayazidi unit 75 kwa mwezi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini maeneo ya Mijini hayakuwa yanahusika na utaratibu huu. Lakini baada ya kufikisha miundombinu mingi zaidi kwenye maeneo hata ya mjini tangu Disemba mwaka jana, Serikali imeelekeza popote pale ulipo ili mradi unatumia unit zisizozidi 75 gharama ya unit 1 itakuwa ni shilingi 100/=. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba unipe nafasi ya kuwaelekeza Mameneja wote wa TANESCO nchi nzima, kukamilisha utaratibu ambao Serikali imeelekeza kupitia Wizara ya Nishati. Kuhakikisha watu wote wanaotumia umeme chini ya unit 75 kwa mwezi, kupata gharama kwa shilingi 9,150 ambayo ni unit moja ni shilingi 100. Na zoezi hili lilianza tangu mwezi wa saba. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri swali lake ni kwamba, Serikali haioni namna ambavyo wale wanatakiwa kuendelea kuuziwa? Maana yake umeme umepanda bei kwa swali la Mheshimiwa Mbunge ni kwamba umeme sasa hauuzwi unit shilingi 100 umepanda. Sasa unampa maelekezo nani wewe ndio tunakusikiliza hapa, kwa nini umepanda yaani ndio swali lake. Kwa nini wasiendelee kuuziwa vile vile ile bei iliyokuwepo? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa ufafanuzi. Umeme haujapanda bei, kwa siku za hivi karibuni kumekuwa kuna utaratibu mpya wa kukusanya kodi ya majengo kupitia kwenye LUKU. Tunaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuwaelimisha kwamba hizo sio gharama za umeme bali ni conduit tu ya kupitisha hizi gharama za upande wa pili.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kwenye eneo la umeme, kilichotokea ni kwamba, utaratibu wa kuwaweka watu kwenye gharama ndogo ulikuwa haujafanyika. Kwa hiyo, watu waliwekwa kwenye gharama kubwa kwa maana ya kwamba waliwekwa kwenye viwango sahihi kwa mujibu wa Kanuni zilizokuwepo mwaka 2016. Sasa kuanzia Disemba mwaka jana Kanuni zilirekebishwa na utekelezaji unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, maelekezo ya Serikali ni kwamba, wale wote ambao walikuwa wamepelekwa kwenye tunazoziita Tariff 1, Tariff 2 na Tariff 3, lakini gharama zao hazizidi unit 75 kwa mwezi warudishwe kwenye tunayoita D1 ambayo ni domestic one ambayo unit ni shilingi 100.

NAIBU SPIKA: Sasa ngoja, sasa hapo umeshajibu. Wewe kaa. Maana yake ni kwamba bei inatakiwa kuwa ni ile ile sasa wewe wasiliana na watu wako wa TANESCO huko, wasiwauzie bei zaidi ya ile iliyokuwepo mwanzo ndio jibu lako hapo. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa kama utaendelea kupata changamoto huko Mbulu Vijijini bila shaka utampigia simu Mheshimiwa Naibu Waziri, ili awaeleze hao wa huko Mbulu Vijijini waliopandisha hiyo bei. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo. Jimbo la Mji Korongo hili la Gunyoda linalosemwa lipo kwenye barabara moja hiyo hiyo kuja Jimbo la Mbulu Vijijini, lipo korongo la Hudaya ambalo lina thamani kubwa ya 1,200,000,000.

Je, Serikali ipo tayari sasa na hii ya Hudaya kuweka kwenye mpango kwa sababu ukiweka hili la Gonyoda la Hudaya utakuwa hujaweka kwenye mpango wa kujengwa barabara hiyo itakuwa haitumiki kabisa.
Je, Waziri yupo tayari na hili ili barabara itumike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba kwa sababu na hili ni ombi jipya na bahati nzuri lilishafanyiwa tathmini na gharama ya fedha na jukumu letu sisi kama Serikali ni kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa hayo madaraja. Kwa hiyo na lenyewe nilipokee tutaenda kushauriana na wataalam ili na lenyewe tuliingize katika mpango wa awamu inayofuatia. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Serikali imetangaza kilometa 25 nashukuru. Je, bajeti ya sasa ina kilometa 50 ni lini sasa utatangaza kilometa 50 ili kufikia Hospitali ya Hydom barabara ile kujengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay Mbunge wa Mbulu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimhakikishie kwamba kipande cha kilomita 50 kati ya Hydom na Mbulu tumetangaza kilomita 25 na Wizara tayari imepeleka maombi maalum ili kipande chote kile kiweze kutangazwa na loti nzima ikamilike kwa hiyo tuko kenye hatua nzuri, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia shilingi 1,500,000,000 tukajenga Hospitali ya Halmashauri. Sasa hospitali hii inafanya clinic ya watoto pake yake, haina vifaa tiba na hasa madaktari bingwa.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuleta vifaa tiba ili hospitali ile ifanye kazi kama ilivyokusudiwa na Serikali?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa ufuatiliaji wake mzuri wa masuala ya wilaya yake. Labda nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala siyo fedha za kununua bidhaa hizo, tayari Rais wetu ametoa fedha na sasa ni mchakato wa manunuzi unaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge, nikimaliza muda wa maswali njoo tukae pamoja ili ueleze specifically na tuwasiliane na DMO wako ili aweze kutuletea list specifically kinachotakiwa ili kiweze kwenda kununuliwa na kufanyika haraka ili upate huduma hiyo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri, amekuja kuzindua umeme katika Jimbo la Mbulu Vijijini. Lakini nataka nimtaarifu kwamba pamoja na kuja kuzindua ule umeme baada ya kuondoka hakuna kilichoendelea, maana yake mkandarasi hayuko site.

Je, atafanya nini ili walau mkandarasi yule arudi site aweze kuendelea kuunganisha vile vijiji ambavyo mkandarasi amesaini kama mkataba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ziko kata ambazo kwa kweli zina hali mbaya na uliahidi kwamba umeme utafika; ni lini hasa zile kata ambazo wewe mwenyewe alitamka wakati anazindua umeme Mbulu Vijijini zitapata umeme? Maana sasa hivi kama nilivyosema, wakandarasi hawako site. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nimpongeze Mheshimiwa Massay kwa sababu kweli tulikwenda kuzindua umeme katika jimbo lake na tulizindua umeme katika Kijiji kinachoitwa Munguhai, ni eneo zuri sana, na uwepo wa Mungu ulionekana kweli katika kijiji hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kwamba mkandarasi anapopewa kazi ya REA kuna awamu kama nne za kufanya. Baada ya kusaini mkataba mkandarasi anakwenda site kufanya survey ili kubaini kama ile kazi iliyoandikwa kwenye karatasi ndiyo hasa ile ya kufanyika kazini. Na hiyo mara nyingi inachukua miezi mitatu mpaka mitano kulingana na hali ya hewa, eneo linavyofanana na wigo wa upana wa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linafanyika baada ya hapo, wanakwenda kufanya uhakiki watu wa TANESCO, REA pamoja na mkandarasi mwenyewe, wanashirikiana kuona kama kilichoonekana site ndicho hicho hasa ambacho kinatakiwa kifanyike na wanakubaliana. Baada ya hatua hiyo, inakwenda sasa kwenye ununuzi wa vifaa. Baada ya vifaa kupatikana ndiyo sasa tunakwenda kwenye utekelezaji wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi hatua tatu nilizozitaja za kwanza za survey, kwenda kwenye kufanya uhakiki na ununuzi wa vifaa unachukua miezi nane mpaka kumi kukamilika. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge, najua kwenye maeneo mengi hatua hizi ndiyo sasa zinaelekea kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna maeneo mengi sana ambapo wakandarasi watakuwa hawaonekani site, siyo kwamba wame-abandon site, hapana, watakuwa kwenye moja wapo ya hizo hatua ambapo pengine hawaonekani kuwepo sana katika maeneo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niwahakikishie kwa maelekezo yaliyokuwepo mikataba yote inatakiwa ikamilike Desemba mwaka huu na tunatarajia kuanzia mwezi Machi mwanzoni wakandarasi wengi watakuwa wamemaliza zile hatua za manunuzi na survey na watakuwa wamefikisha vifaa site wataanza kuonekana wakifanya kazi kwa miezi nane mfululizo ili kazi hizo ziweze kukamilika kwa wakati. Kwa hiyo na ndugu yangu, Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini atakuwa kwenye category hiyohiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye eneo la pili kama nilivyosema tangu mwanzo, vijiji vyote ambavyo havina umeme vitapatiwa umeme kabla ya Desemba na vijiji vingine vilivyopo kwenye kata alizozitaja vikiwemo. Nashukuru.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza: -
Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru Naibu Waziri amefika na ametembelea Jimbo la Mbulu Vijijini. Wananchi, wameshajenga vitu vitatu vya afya ambavyo viko hatua mbalimbali; cha Maretadu, Getanyamba na Gembako. Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka fedha katika vituo hivi ili kuvimalizia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge w Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge na kuwapongeza wananchi wa Mbulu kwa kazi nzuri wanayoifanya. Na wiki moja iliyopita tukiwa ziara tuliona kazi nzuri sana ya ujenzi wa miundombinu ya huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, kazi hii ya ujenzi wa vituo vya afya inafanyika kwa nguvu za wananchi na Serikali kuchangia nguvu za wananchi kupitia aidha, mapato ya ndani ya halmashauri au fedha za Serikali Kuu. Kwa hivyo, naomba nitoe wito kwamba, Halmashauri ya Mbulu Vijijini katika bajeti zao, na bahati nzuri wana zaidi ya bilioni moja na milioni 300 kwa mwaka kwa hiyo, waanze kutenga kwa awamu fedha za kukamilisha baaadhi ya vituo vya afya ambavyo wananchi tayari wamejenga, lakini na sisi Serikali Kuu tutafanya tathmini kuona kiasi cha fedha ambacho kitapatikana kwa ajili ya kuchangia nguvu za wananchi kukamilisha vituo hivi.

Mheshimiwa Spika, kwa hivyo, vituo hivi vitaendelea kukamilishwa kwa awamu. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutashirikiana kwa karibu, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwa kuwa Mbulu Vijijini tumeshapata halmashauri na majengo yameshakamilika, na kwa kuwa Mbulu ina halmashauri mbili; je, lini mnatupatia mamlaka ya kuwa na wilaya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu ina Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Vijijini. Na halmashauri hizi zote zinaendelea kuwekewa miundombinu ya ujenzi ikiwepo Halmashauri ya Mbulu Vijijini ambako jengo la kisasa kabisa la utawala limejengwa, limekamilika na hatua hiyo itawezesha halmashauri hii kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwa halmashauri zile mbili na kwa ukubwa wa jiografia ile, tunafikiri bado tunastahili kuboresha kwanza halmashauri zilizopo na baadae kama kutakuwa na sababu ya kuanzisha halmashauri nyingine basi tathmini itafanyika na wananchi watapewa taarifa hiyo. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwa kuwa kwenye swali la msingi kulikuwa na hiyo barabara ya Kiberashi na imetengewa Kilometa 25 na tender imeshatangazwa; na Mbulu Vijijini, barabara ya Haydom – Mbulu kulikuwa na tender ya namna hiyo hiyo: -

Je, unataumbaje; tenda hiyo imetangazwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ziko nyingi, ikiwepo moja ya Mheshimiwa Flatei Massay ambayo iko kwenye hatua za mwisho za kusainiwa mikataba ili wakandarasi waanze kazi. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante nampongeza kwanza Mheshimiwa Waziri kwa kusoma vizuri vijiji hivyo, lakini kuna mnara ambao uko Masqaroda haujawaka mpaka leo na umejengwa kwa gharama kubwa.

Je, lini Mheshimiwa Waziri mnara huu utapata kuwaka ili mawasiliano yakapatikana Jimbo la Mbulu Vijijini?

Pamoja na majibu yako haya na kata ulizotaja na kwa kuwa hakuna uhalisia wa kutosha; je, uko tayari kufuatana na mimi kwenda Jimboni ukayaona haya yote uliyoyasema na majibu yako haya? (Makofi)
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Massay Mbunge wa Mbulu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba mnara alioutaja umejengwa na umekamilika kwa maana ya vifaa, lakini ulikuwa haujawashwa kwa sababu tulikuwa na changamoto ya vifaa vya mwisho vya kuwashia ule mnara kutokana na tatizo la covid uzalishaji wa baadhi ya vifaa ulichelewa, lakini sasa vifaa vipo tayari na mnara huu utakwenda kuwashwa.

Mheshimiwa Spika, pia niko tayari kuambatana naye tumekuwa tukishirikiana naye katika kutatua tatizo la mawasiliano katika eneo lake; na yeye anajua kwamba hata katika mradi wa kidijitali tumeweka zaidi ya minara saba kwenye Jimbo lake kwa ajili ya ku-facilitate mawasiliano. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara ya Dongobesh – Dareda, ni lini itajengwa kwa kwiango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K.
MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii imeshapata kibali kuanza kujengwa kwa awamu kwa kiwango cha lami kuanzia Dareda kwa kilometa zisizopungua nane. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Halmashauri ya Mbulu Vijijini haina vifaatiba. Je, Serikali ina mpango gani kuleta vifaatiba kwenye Halmashauri hii?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nilijibu kwa Wabunge wa awali kuhusu vifaatiba ni kwamba, sasa hivi moja ya jukumu kubwa ambalo tunalifanya sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, ni kupeleka fedha kwenye hospitali na vituo vya afya ambavyo vimekamilika kwa ajili ya kununua vifaatiba; na hilo limekuwa likifanyika. Kwa hiyo, hata yeye katika Halmashauri yake najua kwamba akiwasiliana nao kule kuna fedha nyingine tumepeleka Machi, mwaka huu kuhakikikisha wananchi wale wanapata vifaatiba. Kwa hiyo, hilo ndiyo jibu la Serikali kwa ujumla katika maeneo yote ambayo yanahitaji vifaatiba. Ahsante sana.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu haya ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, shilingi bilioni mbili aliyoisema kwenye majibu yake ya msingi, ni ndogo sana kutokana na swali lilivyoulizwa wa kila Kijiji kuchimbwa mabwawa.

Je, Serikali ina mpango gani sasa kuongeza bajeti ili maeneo haya anayoyasema yaweze kuchimbwa mabwawa? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; tumeleta maombi ya Mbulu Vijijini kuchimbiwa mabwana katika vijiji vya Gidihim, Eshkesh, Yaeda, Masieda na Endagichan na wewe Naibu Waziri unafahamu: Lini mtatuchimbia hayo mabwawa kama tulivyoomba?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Massay. La kwanza ni juu ya kuongezwa kwa bajeti. Nimelipokea jambo hili na kwa kuwa sasa ndo tuko kwenye Bunge la Bajeti, namwomba Mheshimiwa Flatei Massay na Waheshimiwa Wabunge wengine, tusiwahishe shughuli; tusubiri, nina imani mambo mazuri yanakuja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ni hivi vijiji vyake alivyovitaja. Naomba mimi na yeye tuzungumze mara baada ya hapa kuona namna ambavyo tunaweza kujipanga kwa ajili ya kutekeleza kile alichokiomba. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru Mheshimiwa Naibu Waziri alifika Mbulu Vijijini na Mheshimiwa Waziri kwenye Kata ya Maga. Je, ni lini watatuletea fedha kwa ajili ya kujenga kituo cha afya katika Kata ya Maga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tumefanya ziara zaidi ya mara katika Jimbo hili la Mbulu, lakini nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya, na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ambavyo havijakamilika.

Mheshimiwa Spika, lakini kwa vituo vya afya vipya tuangalie utaratibu baada ya kukamilisha ujenzi wa vituo vya afya vya zamani lakini pia kupeleka vifaa tiba katika vituo hivyo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ni nini kinakwamisha ujenzi wa barabara kipande cha Haydom mpaka Labay?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hakuna kinachokwamisha ujenzi wa barabara hii. Zabuni ya kwanza ilitangazwa kilometa 25 ambayo inatoka Mbulu Mjini hadi Galbad; na kuanzia Labay - Haydom, barabara hii zabuni za kuitangaza zinaendelea. Kwa hiyo, awe na Subira, zikikamilika taratibu za manunuzi, barabara hii itatangazwa kwa kilometa nyingine 25 lakini pia barabara hii imeingizwa kwenye EPC+F. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Jimbo la Mbulu Vijijini ziko sekondari 16 lakini sekondari 11 hatuna vifaa vya maabara ya sayansi.

Je, Mheshimiwa Waziri lini utapeleka vifaa hivyo ili wanafunzi waweze kujifunza vizuri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kwamba kama nilivyojibu katika swali la awali na swali la nyongeza la Mheshimiwa George Mwenisongole, ni kwamba katika maeneo yote ambayo wameshamaliza ujenzi wa maabara sisi tutapeleka vifaa ikiwemo katika Jimbolake la Mbulu Vijijini. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge aondoe wasiwasi katika hilo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, pamoja na majibu mazuri ya Serikali ya kutoa elimu ninalo swali hili: -

Mheshimiwa Spika, kwa sababu matukio haya ya uvunjifu wa sheria kwa vitendo hivi ambavyo nimevieleza katika swali la msingi vimeanza kuwa na matukio mengi, na sasa hivi yanapelekea matishio hata kwenye shule zetu za msingi na sekondari: Je, kwa nini Serikali isianzishe kampeni ya kutoa elimu ambayo itakwenda kila maeneo kunusuru Taifa hii na vitendo hivi vya uvunjifu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Massay, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli anachokisema tumepata malalamiko kwamba baadhi ya matendo yanayokiuka maadili ya Taifa na jamii zetu yameingia hadi kwenye shule, siyo msingi, sekondari na pengine hata vyuo. Wizara ya Mambo ya Nchi kama Wizara yenye dhamana ya kusimamia sheria, ulinzi wa mali, watu na mali zao, na kukabiliana na makosa ya kijinai yakiwemo haya, inaendelea kuhimiza jamii nzima, kama tulivyosema mara kwa mara, makosa mengi ni matokeo ya vitendo vilivyoko kwenye jamii zetu. Kwa hiyo, tunapaswa kuwa na ushirikiano kwa maana ya wazazi walezi jamii, shule, taasisi za dini na makundi mbalimbali kupigia kelele maeneo haya ili kuyatokomeza.

Mheshimiwa Spika, upande wa Jeshi la Polisi yeyote anayekiuka sheria ikiwemo kutenda makosa haya yanayobainika, uchunguzi unafanywa, tukithibitisha, wanapelekwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake. Kwa maana ya jamii nzima, nimeona juhudi zinafanywa na Wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Elimu hili liwe jukumu letu sote kukemea matendo kama haya.

Mheshimiwa Spika, naungana na Mheshimiwa Mbunge kuhusu kutoa elimu kwa ujumla kwa nchi nzima ili kukomesha vitendo hivi ambavyo vinakiuka kwa kiwango kikubwa maadili ya nchi yetu, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Serikali imeahidi kujenga Chuo cha VETA Jimbo la Mbulu Vijijini na tumeandaa ekari 50, na umetuma wawakilishi wako; je, lini mnaanza kujenga Chuo cha VETA Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Flatei, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyoeleza katika swali la mwanzo kwamba ujenzi wa vyuo 63 unatarajia kuanza hivi karibuni, kwa hivi sasa tunaandaa michoro pamoja na kufanya geotechnical survey, topographical survey, pamoja na kufanya estimate kwa ajili ya kuanza ujenzi kwenye maeneo mbalimbali, ikiwemo na Wilaya ya Mbulu. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi.

Kwanza niishukuru Serikali kwa kuchimba maji katika Mradi wa Dambia na yanapatikana kwa wingi.

Je, Mheshimiwa Waziri lini mnajenga Mradi ule wa Dambia ambao unaufahamu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tumeshachimba kinachofuata sasa ni hatua za usambazaji. Mradi huo ulioutaja ujenzi wake mara tukipata fedha tunakuja kuanza mara moja.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itajenga Skimu ya Mogahay, Dirimu na Yaeda Chini?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hivi sasa tupo katika taratibu za kupitia skimu zote hizo kwa maana ya kuangalia status zake na hatua za kuchukua. Nimuahidi Mheshimiwa Mbunge ya kwamba pindi wataalamu wetu watakapopita na kuona hali ambayo imefikia tutaweka katika bajeti yetu ili tuweze kutekeleza mradi huo.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mabwawa ambayo yanajengwa na tumeleta kwenye Wizara yako, Bwawa la Mungahai, Dirimu, Yaeda Chini, Masieda, Endagichani, Basodere, Eshdeshi, Getire na Haribapeti.

Je, ni lini unatujengea mabwawa haya ambayo tumeshayaleta kwenye Wizara yako?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa kuwa Waziri alikuja Haydom na akaahidi kwamba tusubiri wali wa kushiba unaonekana mezani, na akaahidi kisima cha Haydom.

Je, ni lini kinachimbwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Massay kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na mabwawa, mabwawa haya yapo katika ngazi mbalimbali za utekelezaji na maeneo mengi ya nchi tunafikiria kuchimba mabwawa kwa lengo la kuhifadhi maji ya mvua kutumika wakati wa kiangazi, hivyo mwaka ujao wa fedha naamini maeneo kadhaa yatapata huduma hii.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusiana na kisima alichokiahidi Mheshimiwa Waziri, ahadi ni deni lazima tutakuja kuchimba hiki kisima, tutaangalia bajeti hii kabla haijakamilika mwaka huu wa fedha na ikibidi basi mwaka ujao wa fedha kisima hiki kitapatikana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mbulu Vijijini liko ukanda wa juu wa Rift Valley visima vingi vilivyochimbwa na Serikali kwenye Shule na Taasisi nyingi vimekauka. Bahati nzuri tuna Ziwa Basutu tuna ziwa Madunga, je, ni nini mpango wa Serikali wa kupeleka maji kwenye Jimbo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbulu Vijijini tayari huduma ya maji inaendelea kupatikana kwa wananchi. Maeneo ambayo maji bado hayajafika tunaendelea na kazi. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge kuvuta subira, maeneo yake yote ya Jimbo yatafikiwa na huduma ya maji safi na salama.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Jimbo la Mbulu Vijijini lina uhaba mkubwa wa Afisa Maendeleo ya Jamii pamoja na Walimu wa Sayansi: -

Je, katika mgao huu ukoje? Mtaangalia majimbo haya ya vijijini ili kuweka mgao sawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kujibu kwenye jibu langu la msingi, kwamba katika ajira ambazo hivi sasa zinaendelea na utaratibu wa kuajiri, tumeshaainisha maeneo yenye upungufu mkubwa wa wataalamu; wataalamu wa maendeleo ya jamii na pia wataalamu kwa maana ya Walimu wa Sayansi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, kufuatia tathmini ile, tutahakikisha tunatoa kipaumbele katika maeneo yenye upungufu mkubwa zaidi ikiwemo katika Jimbo la Mbulu Vijijini. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Kwa kuwa barabara hii ina vipande vingi; je, kipande hiki cha Labay kwenda Hydom na cha Dongobesh kwenda Dareda mnakijenga lini?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kwa kuwa kipande hiki cha Mbulu kuja Garbabi mmeshamuweka mkandarasi pale na yuko site na hamjamlipa advance payment na hajengi tena barabara;

Je, ni lini mnamlipa advance payment ili ajenge barabara au mpaka turuke tena?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kipande cha Mbulu- Garbabi mkandarasi yuko site, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hajatoka site yupo; na mudo siyo mrefu fedha aliyokuwa anaidai, kwa sababu ilikuwa ni sanifu na jenga, italipwa muda siyo mrefu na kwa hiyo tunaamini kwamba kasi itazidi.
Mheshimiwa Spika, barabara ya Dareda – Dongobesh ipo kwenye hatua za manunuzi na sasa tuko kwenye hatua ya majadiliano na mkandarasi. Ahsante

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa majibu mazuri. Nilitaka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na wala asiruke sarakasi tena, fedha ile Wizara ya Ujenzi walishaleta maombi yale na tunakamilisha maandalizi tutatoa ile fedha ili mkandarasi asikwame. Na tumeongea na wenzetu wa Wizara ya Ujenzi tutapata majumuisho hata maeneo mengine ambayo yalikuwa na uhitaji wa aina hiyo ili tuweze kukamilisha na kazi zisikwame.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Pamoja na Mkandarasi anayetekeleza kazi kwa Jimbo la Mbulu Vijijini kusuasua, sasa ameanza kuweka nguzo katika kila Kijiji, vingine nguzo 12, 13 na 15.

Je, ni kiasi gani cha nguzo kinatakiwa kiwekwe kila Kijiji ili sisi tusimamie?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, pesa iliyokuwa imepatikana katika awamu ya kwanza ya REA III round II ilikuwa unawezesha nguzo takribani 20 kupelekwa katika kila Kijiji, lakini tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, alisikia kilio cha Watanzania na akatafuta pesa ya ziada na kuongeza, kwa hiyo kila Kijiji kitapata takribani kilomea Tatu ambazo ni 20 mara Tatu maana yake karibia nguzo 60 katika awamu hiyo inayokuja ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ninawaahidi Waheshimiwa Wabunge wote kwamba kutoka nguzo 20 sasa tutapata nguzo 60 katika kila Kijiji kwa ajili ya kuongeza wigo wa upelekaji wa umeme katika maeneo hayo. Tunakamilisha taratibu za kusaini mikataba kwa Wakandarasi ambao wanaonekana wanaweza wakaongezewa kazi katika maeneo yao ili waongezewe katika kilometa Mbili ambazo wanatakiwa kuzifanya katika vijiji vyote ambavyo tunavimalizia katika mradi huu wa mwisho wa REA III round II.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, Mbulu Vijijini tumeshaanzisha slogan ya kuhamasisha ujenzi wa vituo vya afya mimi na DC Kheri James. Tuna vituo vya afya vya Hayderer, Geterer, Masqaroda, Dinamu, Ladha, Endamilay na Maghang. Je, uko tayari sasa kupeleka fedha hizo ili kuzihamasisha juhudi za wananchi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa, Hospitali ya Halmashauri bado haijaisha na inahitaji Shilingi milioni 500 na Kituo cha Hydom hakina jengo la upasuaji: Je, ni lini utapeleka fedha hizo ambazo maombi yetu unayo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake la kwanza la nyongeza la lini Serikali itapeleka fedha kuunga mkono juhudi za wananchi za kujenga vituo vya afya; kwanza, nampongeza Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya, tumeona jitihada kubwa wanayoifanya katika kujenga vituo hivi vya afya. Serikali itajitahidi kadiri ya upatikanaji wa fedha kuweza kutenga bajeti kwa ajili ya kwenda kuongeza nguvu pale ambapo wananchi watakuwa wameishia.

Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili, tayari Hospitali ya Wilaya imeshawekwa kwenye bajeti hii tunayoenda kuitekeleza ya 2023/2024, shilingi milioni 500. Fedha hizi zitakwenda kwa ajili ya ukamilishaji wa hospitali hiyo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka jana tulipitisha bajeti hapa ya kujengwa kipande cha Haydom mpaka Labay kwa kiwango cha lami na bajeti ya Waziri bado hatujapitisha.

Je, ni lini atasaini mkataba ule ili barabara ile ijengwe kipande hiki nilichosema kwa kiwango cha lami au tuje na sarakasi kwa namna nyingine tena kwenye bajeti hii ya Jumatatu?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwenye mwaka huu wa fedha tunatakiwa tujenge barabara hii aliyoitamka Mheshimiwa Mbunge na nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kabla ya mwaka huu wa fedha kwisha kwa sababu mwaka wa fedha wa Serikali ni mpaka tarehe 30 Juni, nina hakika tutakuwa tumesaini barabara hii ili mkandarasi aanze kufanya kazi pale. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi. Barabara ya Mbulu – Karatu – Haydom – Sibiti mliahidi kujenga kwa kiwango cha lami na kipande hiki cha Mbulu – Haydom, Mheshimiwa Waziri uliahidi utasaini mkataba kabla ya bajeti yako Jumatatu. Hebu tuambie leo na uwambie wananchi wa Mbulu, mkataba huo utasaini lini?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Mheshimiwa Mbunge amekuwa akifuatilia sana suala la barabara hii na wewe ni shahidi kwamba Mheshimiwa Mbunge, katika Bunge lililopita alipiga sarakasi kuhusiana na suala hili la barabara.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi chini ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni Sikivu. Sasa, tunakwenda kusaini mkataba kesho na tutasaini pale Haydom. Kwa hiyo, niwatangazie wananchi wa jimbo hili kwamba kesho ni siku muhimu kwao katika kushuhudia kusainiwa mkataba wa ujenzi wa barabara hii. Hongera sana Mheshimiwa Mbunge, kwa kufuatilia barua hii.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Je, ni lini Serikali itajenga Soko la Haydom na stendi yake na bahati nzuri Mheshimiwa Naibu Waziri ulifika, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tulielekeza Halmashauri ya Mbulu Vijijini kufanya tathmini na kuanza kutenga fedha za mapato ya ndani kwa awamu kwa ajili ya ujenzi wa Soko la Haydom. Kwa hiyo, nitumie fursa hii kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kusisitiza maelekezo hayo yafanyiwe kazi na pale itakapohitajika nguvu ya Serikali Kuu basi tutakwenda kuunga mkono juhudi za ujenzi wa soko hilo, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tumejenga vituo vya afya viwili vya Hydom na Eshkesh, havina vifaa tiba na mmetuletea madaktari: Je, lini mnapeleka vifaa tiba ili wananchi wapate huduma ya utabibu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeshasema hapa, Rais wetu ameshatoa kwa ajili ya kununua vifaa tiba kwa vituo vyote ambavyo vimeisha. Namwomba Mheshimiwa Mbunge, nikitoka hapa, tutakaa pamoja naye tujue ni vifaa gani vinahitajika ili tuweze kuweka utaratibu wa kuvipeleka kwenye eneo lake. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza namshukuru Naibu Waziri amefika kwenye jimbo langu. Je, minara ya Kata za Eshkesh, Endahagichan, Geterer, Maretadu, Gidarudagaw na Endamiley lini inajengwa?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbulu Vijijini lipo katika minara 758 na tayari watoa huduma wapo katika hatua mbalimbali, hivyo nwmwomba Mheshimiwa Mbunge, wanapofika katika maeneo yake wananchi watoe ushirikiano kwa ajili ya kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa minara hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, akishirikiana na watoa huduma, basi ujenzi wa minara utaanza mara moja. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa mmepeleka fedha shilingi milioni 500 na mmechukua milioni 300. Je ni lini inapeleka fedha kwa ajili ya kumaliza kituo cha afya cha Maretadu?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu DC, ambako fedha ya Serikali shilingi milioni 500 ilipelekwa kwa ajili ya kujenga kituo cha afya lakini kwa maamuzi ya Mkurugenzi na Baraza la Madiwani walikiuka utaratibu wakahamisha shilingi milioni 300 kutoka kituo cha afya wakapeleka kwenye mradi mwingine wa hospitali ya wilaya.

Mheshimiwa Spika, naomba kutumia fursa hii kumuelekeza Mkurugenzi wa Mbulu Vijijini kuhakikisha shilingi milioni 300 waliyoihamisha bila kufuata utaratibu inarejeshwa kwenye kituo cha afya na kukamilisha kituo cha afya kwa haraka iwezekanavyo na sisi ofisi ya Rais, TAMISEMI tutafuatilia, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kwa nini Serikali isiweke mfumo kwa wastaafu na ukajulikana kabisa kulikoni kusumbuliwa kuleta barua kila wakati wanapodai madai yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imekwishakuweka utaratibu kupitia mifuko ya pensheni. Sasa hivi hakuna hitaji la kwamba apeleke taarifa zake, tayari tumeshaweka utaratibu ambao moja kwa moja mtumishi anapoelekea kwenye kustaafu miezi sita kabla taarifa zake zinaanza kuandaliwa na sasa tunatoa pensheni yake ndani ya siku 60 na kama hakuna dosari yoyote hata siku tatu anapata mafao yake. Kwa hiyo, changamoto hiyo tumekwishaitatua.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu mazuri naomba niweke kumbukumbu sawa ya majina haya. Miqaw, Aidurdagawa, Qamtananat, Endahagichan.

Swali langu la nyongeza, Je, ni lini sasa minara hii unakwenda kuijenga hasa vijiji nilivyotaja na Endahagichan?

Swali la pili, kwa kuwa umefika Jimbo la Mbulu Vijijini na wewe mwenyewe umeona kabisa. Ninaimani hakuna sababu ya kufanya tathmini kwa kuwa umefika mwenyewe na minara haipo katika vijiji nilivyovitaja na iko mbalimbali. Je, ni lini sasa unaweka kwenye mpango huu unaokuja ili vijiji hivi vikapata mawasiliano?

NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Gregory Massay Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na namna ambavyo amesahihisha majina namna anavyoyatamka lakini pia nakubaliana na hali halisi ya changamoto ya mawasiliano katika Jimbo la Mbulu Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilifanya ziara na Mheshimiwa Mbunge katika Jimbo lake na tulipita meneo mengi. Maeneo mengi yalikuwa na changamoto ya mawasiliano lakini ukubwa wa tatizo tumeupunguza. Mheshimiwa Rais amekubali kutoa fedha kwa ajili ya kupeleka huduma ya mawasiliano katika Kata zifuatazo:-

Kata ya Endahagichan yenyewe ambapo tumepata mtoa huduma wa Airtel pia kuna Kata ya Eshkesh ambayo pia tumepata Artel, kuna Kata ya Geterer ambayo imepata Tigo, kuna Kata ya Masqaroda wamepata TTCL, Kata za Yaeda Ampa na Yaeda Chini wote wamepata Halotel na TTCL. Kwa hiyo, tunaendelea kupunguza ukubwa wa tatizo la changamoto ya mawasiliano ndani ya Jimbo la Mbulu Vijijini. Hivyo tunaamini kwamba awamu ijayo vijiji ambavyo tumesema tutavifanyia tathmini vitakapokamilika tutafikisha huduma ya mawasiliano. Ahsante.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali. Mwaka jana Jimbo la Mbulu Vijijini na Jimbo la Babati na Mbulu Mji wakulima waliahidiwa kukopeshwa kulima vitunguu, mahindi katika eneo hilo. Kwa bahati mbaya hawakukopeshwa mpaka msimu umeanza mpka leo.

Je, ni nini kauli ya Serikali kuhusiana na jambo hili?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilichukue jambo hili la Mheshimiwa Mbunge niende kulifanyia kazi na kufahamu nini ilikuwa ni changamoto ili tuweze kulitatua na changamoto hiyo isijirudie tena.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, pamoja na mkakati uliosema wa kugeuza kilimo kama cha biashara.

Je, kuna mkakati gani kwenye eneo la Yaeda Chini na Eshkesh ambayo ni kame unavyojua kuyageuza maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, tunakwenda kuanzisha ukanda wa kilimo wa kikanda nchi nzima ili kuweza kuyafikia maeneo yote kutokana na ikolojia, kwa hiyo, na maeneo ambayo Mheshimiwa Mbunge ameyataja kupitia utaratibu huu tutaweza kuyafikia na kuwasaidia wakulima wetu kulima kwa tija.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Moja ya sababu za kushuka kwa ufaulu katika maeneo ya vijijini hasa Mbulu Vijijini ni kukosekana kwa nyumba za walimu na sisi tumejenga maboma yamefikia hatua mbalimbali.

Je, ni lini uko tayari kupeleka fedha katika majengo hayo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Naibu Spika, nikijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei la nyumba hizi za walimu zilizojengwa kwa nguvu za wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa Ofisi ya Rais, TAMISEMI, inafanya tathmini ya maboma yote ya nyumba za walimu ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi na pale tathmini hii itakapokamilika basi itawasilishwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI na tutaiwekea katika mipango yetu kwa ajili ya utafutaji wa fedha ya ukamilishaji wa nyumba hizi.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Jimbo la Mbulu vijijini tumepata vituo vya Afya vitatu na tuna upungufu wa watumishi. Je, ni lini mnatuletea watumishi hao?

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) Mheshimiwa Spika, nijibu swali la Mheshimiwa Massay, hivi sasa Serikali imetoka kuajiri watumishi 8070 wa kada ya afya nchini kote katika mwaka huu wa fedha 2022/2023. Pia tumeweka kipaumbele katika maeneo yenye upungufu ikiwemo kule Jimboni Mbulu Vijijini. Hivyo, basi ni wajibu wao na Mkurugenzi kuhakikisha kwamba hawa watumishi watakaopelekwa katika halmashauri yao wapangiwe kwenye maeneo ambayo yana upungufu zaidi.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi. Mbulu Vijijini wananchi wamechanga na wamejenga kwenye Kata ya Geterei OPD kama Kituo cha Afya, na Kata ya Maseda vilevile; je, lini mtapeleka fedha kuunga juhudi za wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niwapongeze Mheshimiwa Mbunge Flatei Massay vile vile na Mheshimiwa DC wake pale Ndugu Heri James kwa jitihada kubwa ambazo wanazifanya kwa ajili ya kusukuma gurudumu la maendeleo kwa kuhamasisha wananchi kujenga miundombinu ya afya. Nitakaa na Mheshimiwa Flatei kuona ni mipango gani ambayo imewekwa kwetu katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ajili ya kumalizia vituo vya afya ambavyo amevitaja.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri nina maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Kata za Eshkesh, Yaeda Chini na wakati unajibu swali mwaka jana ulisema mwezi wa saba ndiyo watapata umeme lakini sasa umepeleka mwezi wa 12. Je, huoni kwamba utakuwa unatucheleweshea kupata umeme katika Kata hizi?

Mheshimiwa Spika, swali la pili Waziri ametupa vijiji kadhaa ambavyo vitapa umeme kama underline. Kwa sisi wa vijijini, vijiji vyetu lazima umeme upelekwe ndio uweze kupatikana umeme na kama utapeleka umeme katika maeneo ya underline peke yake ni kwamba sisi wa vijijini hatutapata umeme.

Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari sasa kubadilisha kauli hii na mpango huu ili kuhakikisha sisi wa vijijini tupate umeme?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli tulikuwa tunatarajia kumaliza mradi wa REA III Round II kwa awamu tofauti tofauti katika maeneo mbalimbali na sasa kwa walio wengi imekwenda mpaka Desemba mwaka huu na sababu kubwa ni mbili ambazo nyingine tulishazieleza huko nyuma za UVIKO na kuongezeka kwa bei za vifaa. Sababu nyingine iliongeza mwezi wa kumi wa mbili kuwa ndio deadline sasa ni kuongezeka kwa zile kilometa mbili ambapo Wakandarasi takribani wote 31 tayari wameshasaini ile mikataba ya kuongeza hilo loti kilometa mbili ili tuweze kuwa sasa kuwa na kilometa tatu za kupeleka umeme. Yote hiyo inatakiwa ikamilike kufikia mwezi Desemba.

Kwa hiyo, nimwombe Mheshimiwa Flatei pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine wote tusaidiane katika hili tumalize kazi hii ya upelekaji wa umeme katika vijiji vyote ifikapo Desemba mwaka huu ikiwa na extention ya hizo kilometa mbili.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali la pili naamini alikuwa anazungumzia vitongozi japokuwa ametaja vijiji ambavyo viko underline, kwa sababu vijiji vyote vitakamilika Desenba mwaka huu. Tunafahamu kwamba tuna vitongoji 15 ambavyo tutapeleka kwa kila Jimbo. Kumekuwa kuna concern za Waheshimiwa Wabunge kwamba wapo ambao hawana vitongoji ambavyo viko chini ya line ambazo ni existing kwa sasa.

Mheshimiwa Spika, Serikali sikivu ya Daktari Samia Suluhu Hassan tumerudi tena mezani kutizama namna ambavyo tunaweza tukapanua wigo wa mradi na tunatafuta aidha tupate pesa ya nyongeza au tubadilishe procurement process ili tuweze kupata vifaa na kuwapa Wakandarasi kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote.

Mheshimiwa Spika, hili tunalifanyia kazi na ninaamini litakuja na majibu mazuri katika muda mfupi ujao.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mbulu Vijijini kuna vitongoji 400 na vijiji 76; ulifika Mheshimiwa Waziri ukatoa ahadi vijiji vyote vitapata umeme.

Je, ni lini ahadi yako inatekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay kama nilivyojibu swali la msingi kwamba kadri Serikali inavyoendelea kupata fedha itajitahidi kuhakikisha kwamba vitongoji vyote vinapatiwa umeme katika muda mfupi ujao.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Kwa kuwa, Serikali imekiri kwamba inatafuta fedha kulipa Madiwani na Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji na umeelekeza kwamba Halmashauri ifanye utaratibu huo. Je, uko tayari kuelekeza Halmashauri zote ili hela hizi zilipwe kwenye Mfuko Mkuu ili watu hawa wakapate kulipwa katika bajeti ya mwakani?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa sababu ameona na amesikia kilio cha wafanyakazi ameongeza asilimia 23 kwenye mshahara. Je, huoni kwamba sasa ndiyo muhimu kuona kwamba watumishi wengine na hasa hawa niliowataja kwenye asilimia hii wapo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Gregory Massay, Mbunge wa Jimbo la Mbulu Vijijini kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na hili ni agizo kwa Halmashauri zote kuhakikisha sehemu ya mapato ambayo yanashuka kwenda katika vijiji ni sehemu ya posho ambazo wenyeviti wa vijiji wanapaswa kulipwa. Kwa hiyo, tutakachokifanya tu ni kufuatilia kuona agizo hili ama utaratibu huu unatekelezeka.

Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la pili kuhusu asilimia 23 linahusu wale ambao ni Watumishi wa Umma ambao wako kwenye mishahara, kwa hiyo, kwa madiwani bado wako katika sehemu ya posho, ndiyo maana tumesema tunatafuta vyanzo vingine ili kuhakikisha kwamba tunawaongezea posho Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza nishukuru Serikali kwa kujenga Mahakama ya Hydom imekamilika kabisa. Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri mnafungua Mahakama ile ya Hydom ili ipate kutumika?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Hydom tayari jengo limeshakamilika na utaratibu wa matumizi unaweza ukaanza wakati wowote. Lini tutakwenda kuzindua rasmi ni mpango wa Mahakama ambao huwa wana utaratibu ambao wanautumia katika kwenda kuzindua na uanzishwaji wa matumizi ya Mahakama. Juzi Waziri wangu alikuwa pale Hydom kuangalia hilo jengo na nina uhakika kabisa Mheshimiwa Mbunge alikubaliana jambo na Mheshimiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mbulu Vijijini kuna kata tatu ambazo hazina umeme na vijiji 15. Nakubali majibu ya Mheshimiwa Waziri kwamba REA wameondoka site kutokana kupanda umeme na kupanda gharama za umeme: -

Je, ni lini mnamaliza huo utaratibu wa kukubaliana na hao wakandarasi ili warudi site wakakamilishe mradi huu wa REA?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi mwenyewe nilienda katika Jimbo lake kuzindua umeme katika REA III round II na kazi ilikuwa inaendelea. Kama alivyosema, ni kweli tulikuwa na changamoto hiyo, lakini tayari tumeshakamilisha taratibu za mazungumzo, na wakati wa maonesho hapa Mheshimiwa Waziri aliwaambia wakandarasi wote Serikali tayari imeshatoa fedha kwa ajili ya kuongeza ile nakisi iliyokuwepo. Kwa hiyo, wakandarasi wanarudi site kwa ajili ya kuendelea kufanya kazi wakiwa na uhakika kwamba Serikali ya Awamu ya Sita itatoa fedha ili kazi iweze kukamilika.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Kwanza nishukuru sana Mheshimiwa Rais kutupatia shilingi 711,000,000 kwa Skimu ya Magisa, lakini skimu ile sasa inakwenda kuharibika kwa sababu ya uchakavu na uliniahidi kwamba utakuja kufanya ukarabati.

Je, ni lini utatekeleza ahadi ya Serikali ya kufanya ukarabati kwenye Skimu ya Magisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli skimu hii inahitaji ukarabati hasa baada ya kuwa tulituma timu yetu ambayo imepitia miradi yote na katika bajeti inayokuja, tumepanga miradi ya ukarabati natumai pia mradi huu ambao Mheshimiwa Mbunge ameusema utakuwemo katika kazi hiyo. (Makofi)

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeahidi kujenga barabara kilometa tano kwenye Mji wa Hyadom; je, ni lini Serikali watatimiza ahadi ya kujenga kilometa hizi za lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, tunatambua ahadi ambazo viongozi wametoa ikiwemo katika eneo la Hyadom, katika Jimbo la Mbulu Vijijini ambako hadi sasa tunatafuta fedha na tumeendelea kutenga kila mwaka hizo fedha ambapo tutakuwa tunapeleka katika maeneo hayo ili kukamilisha ahadi hizo.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Kwanza nishukuru Serikali kwa kujenga Mahakama ya Hydom imekamilika kabisa. Je, ni lini sasa Mheshimiwa Waziri mnafungua Mahakama ile ya Hydom ili ipate kutumika?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Hydom tayari jengo limeshakamilika na utaratibu wa matumizi unaweza ukaanza wakati wowote. Lini tutakwenda kuzindua rasmi ni mpango wa Mahakama ambao huwa wana utaratibu ambao wanautumia katika kwenda kuzindua na uanzishwaji wa matumizi ya Mahakama. Juzi Waziri wangu alikuwa pale Hydom kuangalia hilo jengo na nina uhakika kabisa Mheshimiwa Mbunge alikubaliana jambo na Mheshimiwa Waziri. Ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa kuwa wananchi wa Haydom wameshawapa eneo la kujenga majengo ya mkandarasi ili aanze kazi na wewe ulikuja kusaini ule mkataba.

Je, ni lini anakuja kujenga yale majengo ili barabara ianze kujengwa ya Haydom – Labay?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, bahati nzuri hiyo barabara mkandarasi ambaye anajenga kipande cha kwanza ndiyo atakaejenga kipande cha pili. Kazi anayofanya sasa hivi ni kufanya usanifu, kwa sababu barabara hiyo inayojengwa ni sanifu inajengwa na atakapokuwa amekamilisha nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge ndipo atakapoanza sasa kujenga hiyo kambi yake eneo ambalo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Mbulu kwa kulitoa hilo eneo la ujenzi bure kabisa, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, Barabara ya Orbesh ambayo inatoka kwenye Kata yako kuja Bashneti na kwenda mpaka Haiderere iliahidiwa na Katibu Mkuu kujengwa na sasa hivi hali ni mbaya.

Je, ni lini TARURA itakwenda kujenga barabara ile ili wakulima wapate nafuu ya kuleta mazao yao?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikia Mheshimiwa Flatei akiuliza kwamba barabara hii inaanzia kwenye, Jimboni kwako Kata yako ya Orbesh na kuelekea Bashneti ambako anatoka yeye Mheshimiwa Flatei. Nitakaa na Mheshimiwa Flatei ili kuona ni namna gani TARURA, Eng. Bwaya, Meneja TARURA Mkoa wa Manyara pamoja na timu yake walivyojipanga katika kuanza utekelezaji wa matengenezo ya barabara hii mara moja. (Kicheko/Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Serikali, lakini nina maswali mawili. Swali la kwanza; je, Mheshimiwa Waziri yuko tayari kuweka fedha kwenye bajeti ijayo ili Barabara hii ya Ugalla - Kahama ikawa kwenye bajeti kwa uhakika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; Barabara ya Dareda - Dongobesh aliiweka kwenye mpango wa kujengwa kwa kilomita tisa na mpaka leo haijaanza kujengwa. Je, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara niliyoitaja kuna baadhi ya maeneo ambayo yalikuwa hayajafunguliwa, kwa hiyo kitu cha kwanza ni kuifungua yote na kuikamilisha. Pia tuliona kwanza tufanye usanifu uliokamilika kwenye Daraja kubwa la Mto Ugalla, lakini kabla ya kufika kwenye Daraja la Mto Ugalla kuna madaraja madogo sita ambayo tumeanza kuyajenga ili kulifikia hilo daraja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tutakapokamilisha ujenzi wa hayo ma-culvert, hatua ya pili itakuwa ni kujenga hilo daraja ili kuifungua barabara yote ambayo inaunganisha Mkoa wa Katavi – Tabora na Mkoa wa Shinyanga kwa upande wa Kahama. Kwa hiyo, tutakapokuwa tumekamilisha hii kazi sasa Serikali itaweka kwenye bajeti kuijenga barabara yote, lakini cha muhimu kwanza ni kukamilisha hayo madaraja ili kwanza tuifungue hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye swali lake la pili la Barabara ya Dareda – Dongobesh, ni kweli tulikuwa tumepata mkandarasi, lakini ikatokea tatizo la kimkataba ambalo sasa limeshatatuliwa na tunategemea kukamilisha manunuzi ya hiyo barabara. Baada ya hapo naamini barabara hiyo inaenda kujengwa kwa kiwango cha lami, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi.

Jimbo la Mbulu Vijijini Kata ya Yaeda Chini ulikuja Mheshimiwa Waziri ukatuhamasisha tukajenga Kituo cha Polisi, sasa nguvu za wananchi pamoja na mimi tumeshindwa kujenga nyumba za Polisi. Utatusaidiaje kwenye bajeti hii ili nyumba hizo zipate kujengwa?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli mimi na yeye wakati nikiwa Naibu Waziri wa Wizara hii miaka kadhaa iliyopita tulishirikiana kuanza ujenzi wa kituo hiki. Kwa hiyo nichukue fursa hii kumpongeza yeye na wananchi wa Jimbo hilo kwa kuweza kutumiza ile ndoto tuliyokuwa nayo wakati tunaanza ujenzi huo na sasa hivi kituo kimekamilika.

Kwa hiyo nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba nguvu hizo za wananchi na nguvu zake hatuwezi kuziacha hivi hivi. Tumechukua suala la ujenzi wa Nyumba za Askari katika eneo hilo kwa uzito unaostahili na mimi nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama tuliweza mimi na yeye kuanza jitihada za ujenzi wa kituo hicho, hatutashindwa mimi na yeye tukishirikiana kujenga Nyumba za Askari.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nina maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza; kwa kuwa sasa barabara hii ya Mbulu – Garbabi ni kweli Mkandarasi yupo site, lakini ana tatizo hilo la kutolipwa fedha baada ya yeye ku-raise certificate ambayo iko ofisini kwa Mheshimiwa Waziri. Je, lini atalipwa hiyo fedha ili aendelee kuweka au kumalizia barabara hii ya Garbabi kwenda Mbulu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine, nashukuru kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri alikuwepo katika kusaini Mkataba wa Barabara ya kutoka Haydom kuja Labay. Sasa ni miezi sita, tumesaini tarehe 25 Mei, 2023. Je, ni lini sasa barabara hii itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami ili wananchi waweze kupita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Flatei Massay, Mbunge wa Mbulu Vijijini, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkandarasi ambaye anafanya kazi kati ya Mbulu na Garbabi, nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba anaendelea na kazi kwa sasa. Hii ni baada ya Mkataba wake unamtaka asisimame kazi baada ya kuanza kazi. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, nimepata taarifa leo kwamba kazi zinaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande alichokisema cha Labay – Haydom, ni kweli kilisainiwa. Nataka kumkumbusha Mheshimiwa Mbunge kwamba utaratibu unaotumika katika kipande hiki ni sanifu na jenga. Wajibu wa Mkandarasi kwanza ni kufanya usanifu wa ile Barabara. Halafu ikishasanifiwa ipate kibali kwamba iko sawasawa na Mamlaka kwa maana ya TANROADS ndipo anatakiwa sasa aanze kujenga hiyo barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba kazi hizo zinaendelea na akishakamilisha, basi tutamwona site akiwa anaanza kuijenga hiyo barabara, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024 Mbungi Vijijini tulipangiwa kujengewa mabwawa mawili. Bwawa la Mungahai na Bwawa Diri; je, lini mnajenga mabwawa haya?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, mabwawa yaliyopo Mbulu Vijijini yapo katika mpango wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa ajili ya utekelezaji wake. Ambacho kinafanyika sasa hivi ni ule upembuzi na usanifu wa kina. Tukishamaliza hapo maana yake tutakwenda katika hatua ya pili ya kuanza ujenzi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa kuwa ajira wakati huu watu wengi wanahitaji na kumekuwa na tabia sasa ya wanafunzi waliomaliza 2015, 2016 kutoajiriwa na wanaajiriwa wa 2021.

Je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha kwamba wale wa miaka ya zamani wanaajiriwa kwa sababu muda wa umri wao unakwenda?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, jambo moja ambalo Mheshimiwa Mbunge ajue kwamba moja ya vigezo ambavyo Ofisi ya Rais TAMISEMI inatumia katika kuajiri walio mtaani ni pamoja na wale wa miaka ya nyuma. Kwa hiyo hilo limekua likitekelezeka na bahati nzuri hata mimi nilikuwa huko kwa hiyo nalifahamu. Tumejitahidi kuajiri walimu kuanzia 2010 mpaka 2016 na baadhi ya miaka hii ya mbele especially walimu wa sayansi, kwa hiyo hilo linazingatiwa katika ajira, ahsante.

MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, lakini kwanza, nishukuru kwa hatua na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuna vijiji vya Getesh, Qamtananat, Gidbiyo, Dotina, Qaloda, Geterer, Muslur, Endanyawish, Maretadu na Qatros. Je, lini unavipatia fedha ili kupata maji katika vijiji nilivyovitaja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa sasa vijiji nilivyotaja ni vingi na fedha umezitoa; je, ni lini sasa tunaambatana ili kufanya ziara katika maeneo haya uliyoyataja?
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa ambayo ameifanya hasa juu ya kupigania mradi huu wa Dambia, lakini kubwa katika vijiji ambavyo amevieleza nataka nimuhakikishie utekelezaji wa Miradi ya Maji unategemeana na fedha. Tutatoa fedha juu ya ujenzi wa miradi hiyo hasa katika vijiji vyake ili wananchi wake waweze kupata huduma ya maji safi na salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ameniomba kwenda, nipo tayari kuongozana na Mheshimiwa Mbunge hasa katika Jimbo lake la Mbulu Vijijini kwenda kutazama ufuatiliaji wa ujenzi wa mradi huu wa maji.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Barabara ya Dareda kule Dongobesh mlitangaza na mlituambia mnakwenda kusaini mkataba. Je, kwanini mkataba ule hausainiwi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Ni kweli barabara hii ilitakiwa isainiwe lakini kulitokea changamoto ambazo Mheshimiwa Mbunge na Mheshimiwa Mbunge wa Babati wanajua. Mara baada ya Bunge hili barabara hii inakwenda kusainiwa kwa sababu kila kitu kipo tayari. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, naleta swali hili kwa mara ya sita, lakini nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Naibu Waziri ajue Mbulu Vijijini, Wenyeviti wa Vitongoji hawajawahi kupata hizi posho. Je, lini wanapata posho hizi ili kukidhi na kuweza kufanya shughuli zao kama swali langu linavyosema?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili. Niliwauliza, lini mnawaongezea posho Waheshimiwa Madiwani? Sikuuliza kama mnaendelea kuwalipa, nimeuliza, “lini”? Naomba jibu, lini mnawaongezea posho Waheshimiwa Madiwani ili waweze kufanya kazi kama inavyostahili? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, nampongeza Mheshimiwa Flatei Massay, ni kweli ameuliza swali hili mara kadhaa kwa nia njema ya kutaka kuona Wenyeviti wa Vijiji, Vitongoji na Mitaa wanapata posho zao za kila mwezi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali hii ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inathamini sana kazi za viongozi hao. Ndiyo maana imeendelea kutenga fedha kupitia Serikali Kuu na mapato ya ndani ya halmashauri kwa ajili ya kulipa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa vitongoji vya halmashauri hiyo ambavyo havijalipwa, nimwelekeze Mkurugenzi wa Mbulu Vijijini kuanza kutenga fedha kwenye mapato ya ndani kwa ajili ya kuanza kulipa posho kwa kadri ya maelekezo ya Sheria na Miongozo iliyopo ili viongozi hao wapate posho zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, kuhusu hoja ya lini tunapandisha posho za Waheshimiwa Madiwani, Serikali inaendelea kufanya tathmini ya kuona uwezo wake wa kifedha na baadaye itatoa tamko kuhusu namna gani tunakwenda kulifanyia kazi suala hilo. Ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa vijiji alivyovitaja vyote vina shule mbili mbili za msingi, wamejenga ofisi katika vijiji, na karibu mambo mengi yamekuwa tayari; na kwa sababu idadi ya watu ni kubwa: Kwa nini usiruhusu sisi wenyewe wananchi tukaanzisha vijiji hivyo mpaka Serikali itakapopata uwezo wa kuvianzisha?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili. Kwa sababu kata anazotaja, kwa mfano Kata hii ya Hayderer inapakana na majimbo ya uchaguzi; Hanang, Babati na Singida na ni kubwa sana; kama Kata ya Haydom ina watu 30,000; na kwa kuwa hali imekuwa mbaya na haitawaliki: Kwa nini usiruhusu basi chini ya halmashauri tukawa na kata ndogo ili walau patawalike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, natambua kwamba Mheshimiwa Mbunge mara kwa mara ameleta hoja ya kuanzisha vijiji hivi kutokana na ukubwa wake, pia kuanzisha kata hizi kutokana na ukubwa wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua. Tumepanga kwanza kukamilisha maeneo ya utawala yaliyopo, na ninyi Waheshimiwa Wabunge ni mashuhuda kwamba tumekuwa kila siku tukiomba kujenga majengo ya utawala, ofisi za kata, majengo ya halmashauri, kwa Wakuu wa Wilaya, na Wakuu wa Mikoa. Bado tuna kazi ya kukamilisha miundombinu katika mamlaka zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba tunatambua kwamba vijiji hivi ni vikubwa, lakini kwa mujibu wa sheria, halmashauri haina mamlaka ya kuanzisha Kijiji. Kwa hiyo, hatuwezi tukasema halmashauri iende ikaanzishe vijiji yenyewe au ianzishe kata yenyewe, lazima tuzingatie sheria na ni suala tu la muda. Nimhakikishie Mheshimiwa Flatei kwamba muda ukifika, tutahakikisha kwamba tunafanyia kazi kata hizi pamoja na vijiji hivi, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, Hospitali ya Halmashauri ya Mbulu imeanza kujengwa na karibu inamalizika lakini haitoi huduma kwa sababu shilingi milioni 500 za mwisho ilikuwa zipelekwe na mpaka sasa hazijapelekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, lini mtapeleka ile fedha shilingi milioni 500 ili hospitali ile ikaisha na wananchi wakapewa huduma ambayo wanastahili?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha ujao Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi viporo ya hospitali za halmashauri. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba hospitali ya kwao ya Halmashauri ya Mbulu na yenyewe itakuwa miongoni mwa hospitali zitakazohudumiwa kwa maana ya kukamilisha miundombinu ya hospitali ile iliyokuwa imebakia kwa sababu fedha imetengwa katika mwaka ujao wa bajeti.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Mbulu na Wilaya ya Mbulu haina kabisa Chuo cha VETA na kwa kuwa maelekezo yako ilikuwa tukupe ekari 50 na tumeshatenga tayari.

Je, ni lini utatuletea fedha za kujenga Chuo cha VETA Mbulu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Flatei, Mbunge wa Mbulu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi kwamba sera ya Serikali ni kuhakikisha kwamba tunakwenda kujenga chuo katika kila Wilaya nchini. Nimuondoe wasiwasi Mheshimiwa Flatei, kwa vile katika mwaka wa fedha ujao tunatengeo la vyuo karibu 36 katika Wilaya 36 tutaangalia zile Wilaya ambazo zina mahitaji makubwa ikiwemo na Wilaya ya Mbulu.
MHE. ZACHARIA P. ISSAAY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Pamoja na kwamba Serikali tayari imepeleka fedha za awamu ya kwanza katika ujenzi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Mbulu, je, ni lini fedha za awamu ya pili zitapelekwa katika ujenzi wa Chuo cha Maendeleo TANGO FDC Mbulu? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Issaay kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Issaay nadhani mimi na wewe tunazungumza mara kwa mara kuhusiana na chuo hiki; na nilikuomba kaka yangu kwamba kwenye ujenzi wa vyuo hivi vya FDC vilikuwa vyuo 54, na maeneo mengi sana tumefanya ujenzi pamoja na ukarabati. Nikakueleza kwamba katika mwaka wa fedha ujao tuna awamu ya pili ya ujenzi wa vyuo hivi kikiwemo na chuo hiki ulichokitaja. Kwa hiyo, nikuondoe wasiwasi katika mwaka wa fedha ujao tutazingatia yale maelekezo ambayo tulikuwa tumepewa na Mheshimiwa Rais kuhakikisha tunakamilisha ujenzi kwenye eneo hili. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante. Barabara ya Haydom – Mbulu tumesaini mkataba mwaka jana mpaka leo haijajengwa. Je, lini wanawapa pesa wakandarasi ili wajenge barabara ile?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumeshasaini barabara na mkandarasi tayari amesha-raise certificate, lakini alikuwa na changamoto yeye mwenyewe katika kampuni yake ya kiuongozi ambayo tayari ameshaitatua. Tuna hakika baada ya kipindi hiki cha mvua kasi itaanza kwa ajili ya kujenga hiyo barabara, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Bajeti ya mwaka huu tulipangiwa kuchimbwa visima Mbulu Vijijini. Je, ni lini watachimba visima hivi ili wananchi wapate maji?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa kifupi.

NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sijasikia vizuri.

MWENYEKITI: Anasema hajasikia vizuri.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka huu ambayo inakwisha mwezi ujao kuna visima vitano tulikuwa tuchimbe Mbulu Vijijini. Je, ni lini tunachimba visima hivi ili wananchi wapate maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpomgeze Mheshimiwa Flatei Massay kwa kazi nzuri anayoifanya. Serikali na Sekta ya Maji tuna maelekezo mahsusi kutoka kwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupitia miradi yote ya 2021/2022, 2022/2023 na 2023/2024 ili kuhakikisha kwamba kule ambako tumeshafanya mkataba na wananchi kwamba tunawapelekea maji basi miradi hiyo tukaikamilishe kwa wakati ili Watanzania wapate maji safi na salama. Ahsante
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa katika Jimbo la Kisesa zipo zahanati na nguvu za wananchi zimetumika, je, lini mnamalizia zahanati zilizobaki katika Jimbo la Kisesa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la Jimbo la Mbulu Vijijini pia kuna zahanati 13 wananchi wameshajenga na ziko kwenye hatua mbalimbali. Je, ni lini mnapeleka fedha ili Jimbo la Mbulu Vijijini tukapate huduma hiyo ya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali tumeshafanya mapping ya zahanati zote ambazo zimejengwa kwa nguvu za wananchi katika halmashauri zote 184. Serikali imeendelea kutenga fedha na kupeleka fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma. Ndiyo maana katika mwaka huu wa fedha 2023/2024 mpaka Machi, tayari fedha zote 100%, shilingi bilioni 18.8 zimeshapelekwa na zahanati zinaendelea kujengwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie kwamba hizo zahanati za Jimbo la Kisesa na zahanati za Jimbo la Mbulu Vijijini ni sehemu ya kipaumbele na tutaendelea kupeleka fedha ili ziweze kukamilishwa, ahsante.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, kwa kuwa Barabara ya Haydom tumeshasaini mkataba na wewe ulikuwepo. Je, lini mnampelekea mkandarasi aliyeko site fedha ya kujenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, Wizara ilishapeleka maombi ya mkandarasi Wizara ya Fedha na wenzetu sasa hivi wako kwenye maandalizi ya kuandaa fedha hizo ili mkandarasi aweze kulipwa na aendelee na ujenzi.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, je, ni lini Serikali itapeleka fedha za kujenga kituo cha afya Masieda Jimbo la Mbulu Vijijini?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, maeneo yote ambayo yanahitaji ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati yalishaainishwa. Ikiwa eneo hilo la Masieda ni eneo la kimkakati katika Halmashauri ya Mbulu Vijijini, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutahakikisha kwa awamu tunapeleka fedha hizo ikiwa vigezo vya kujenga kituo hicho vinakidhi, lakini ikiwa imewasilishwa jina la Kata hiyo kama ni kipaumbele katika Jimbo lake, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nimshukuru Rais kwa kujenga minara Mbulu Vijijini. Je, Mheshimiwa Waziri lini tutaambatana kuizindua ile minara?
WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Naibu Spika, minara mingi kwa sasa imekamilika katika maeneo mengi na mpango ilikuwa minara zaidi ya 250 ingewashwa wakati wa Sherehe za Muungano. Kwa hiyo, tutaangalia ratiba na kwa sababu hapa siyo mbali, tutapanga mimi na yeye, tutakwenda kukagua na wataalamu wetu wakiridhika tutawasha hiyo minara ambayo imekuwa tayari. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa nafasi. Kwanza namshukuru Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupitishia bajeti ambayo inajenga mabwawa matatu; Bwawa la Ari, Bwawa la Dirim. Je, ni lini wametangaza mabwawa haya ili yaweze kujengwa na wananchi wa Mbulu Vijijini wapate kumwagilia mashamba yao? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Flatei, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, haya ni miongoni mwa mabwawa 100 ambayo yametangazwa katika Mkoa wa Manyara na nataka kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa usanifu ukikamilika tu, mabwawa haya 100 ambayo yametangazwa sasa yataingia kwenye ujenzi. Tunatarajia usanifu utachukua kipindi cha miezi sita ili uweze kukamilika and then tuanze kutangaza mabwawa hayo. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, Haydom ni Kijiji na Dongobesh ni Kijiji, lakini umeme wake unaingizwa kwa shilingi 320,000. Je, ni lini utatoa mwongozo katika vijiji hivyo ili walipe shilingi 27,000 kama vijiji vingine vyote?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema kwenye swali la msingi, maeneo yote ya vijiji gharama ya kuingiza umeme ni shilingi 27,000. Kama maeneo haya kulingana na miongozo ya TAMISEMI ni maeneo ya vijiji, tutafuatilia kuhakikisha gharama ya kuunganisha umeme ni shilingi 27,000, ahsante. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa majibu mazuri kutoka kwa Naibu Waziri. Nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya Mbulu Vijijini. Swali la kwanza; je, ni lini sasa mtatupatia umeme kwenye vitongoji vilivyobaki kwa sababu, kule ni sawasawa na vijiji?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tulikubaliana kwenda kufanya uzinduzi wa kuwasha vijiji hivyo sita, je, Mheshimiwa Naibu Waziri ni lini sasa tunakwenda kuwasha hivi vijiji, ili Jimbo la Mbulu Vijijini lipate umeme wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Namshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mawili ya nyongeza. Jimbo la Mbulu lina jumla ya vitongoji 361 ambapo kati ya hivyo, vitongoji 80 ndivyo ambavyo vina umeme. Tutaongeza upatikanaji wa umeme kwenye vitongoji kupitia mradi wa vitongoji 15 vilevile tuna mradi wa ujazilizi pale kwa vitongoji 16. Namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tutapunguza idadi ya vitongoji zaidi kupitia mradi wa REA ambao unatarajiwa kupeleka umeme kwenye vitongoji 20,000 kwa awamu.

Mheshimiwa Spika, ahsante. Samahani, kuna hili swali la pili la Mheshimiwa Mbunge, kuhusu kwenda kuwasha.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, nilimuahidi Mheshimiwa Mbunge, tutaenda kuwasha vijiji hivi sita. Kwa kuwa, natambua vijiji vitatu vitakuwa vimekamilika Tarehe 27, vijiji viwili vitakuwa vimekamilika Tarehe 28 na kimoja kitakuwa kimekamilika Tarehe 30 mwezi huu, basi tutapanga, ili kuona namna gani baada ya kukamilika Bunge hili tutaenda kuwasha vijijini kwako, Mheshimiwa Mbunge, ahsante sana. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Barabara ya Maretadu – Dongobesh – Haydom kwa kiwango cha zege kwa sababu barabara hii imekuwa ikichakaa kila mwaka na haipitiki?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba nianze kwa kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi nzuri ya uwakilishi anayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala lake la barabara zake kujengwa kwa kiwango cha zege hatua ya kwanza itakuwa ni kufanya usanifu na kubaini ni kiwango gani cha bajeti kinachohitajika kwa ajili ya kuziendeleza barabara hizi. Baada ya hatua hizo kukamilika, hatua zinazofuata zitachukuliwa ili hatimaye fedha ziweze kupatikana na kuhakikisha kwamba barabara zinaweza kuboreshwa.
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuuliza swali dogo la ngongeza. Barabara ya Haydom – Labay imesainiwa na Mheshimiwa Waziri alikuja. Tumesaini barabara ile na akatuahidi ujenzi utaanza. Je, ni lini pochi la Mama linafunguliwa ili fedha zianze kupelekwa kwa mkandarasi na amalize kazi ya kujenga barabara ile? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Flatei kwa namna ambavyo anafuatilia barabara hii na tumeshakaa naye pamoja na Hazina. Mkandarasi anasubiri advance payment. Kwa hiyo, nakuhakikishia yeye pamoja na wananchi wake kuwa barabara hii itaanza kujengwa tutakavyopata tu advance payment. (Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Spika, kwanza ninashukuru kwa barabara ya Haydom tumekwenda na Naibu Waziri tumesaini. Je, unawaambia nini wananchi wa Jimbo la Mbulu Vijijini kuhusiana na barabara hiyo kujengwa kutoka Haydom kwenda Labai?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, kwa kuwa tumeshasaini na mkandarasi ameshapatikana, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, tutaendelea kuijenga na mkandarasi hatatoka site kwa sababu tayari ameshasaini mkataba, ahsante.(Makofi)
MHE. FLATEI G. MASSAY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa nafasi, Scheme ya Mangisa imejengwa muda mrefu na imejaa udongo na tuliomba fedha kwa ajili ya kuondoa ule udongo. Je, ni lini Serikali italeta fedha ili scheme ile ikaweze kuwafaidisha na kuwasaidia wakulima wa Mangisa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwamba jambo hili na mimi nalifahamu na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji inalifanyia kazi. Sehemu ambayo ipo sasa hivi ni kwamba wanatafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunatoa ili iweze kuwasaidia wananchi ule mradi uweze kufanya kazi, ahsante. (Makofi)