Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza (22 total)

MHE. CONCHESTER L. RWAMLAZA aliuliza:-
Katika bajeti ya mwaka 2015/2016 Serikali kupitia Waziri wa Fedha iliahidi kupandisha pensheni kwa wastaafu wanaolipwa Sh.50,000 ili walipwe Sh. 100,000/=.
Je, Serikali imetekeleza ahadi hiyo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchester L. Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua nafasi hii kumfahamisha Mheshimiwa Rwamlaza na Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali ilitekeleza ahadi yake ya kuongeza kima cha chini cha pensheni kutoka Sh.50,114.43 kwa mwezi hadi kufika Sh.100,125.85 kwa mwezi, kuanzia Julai 2015 ikiwa ni ongezeko la asilimia 100.
Mheshimiwa Spika, nashukuru.
Kuanzisha Mfuko wa Kulinda Ustawi wa Watoto Nchini

Ni wajibu wa Serikali kulinda na kuhakikisha ustawi wa watoto katika nchi;
Je, ni lini Serikali itatenga asilimia ya mapato yake katika bajeti ili kuwepo na Mfuko wa Kulinda Ustawi wa Watoto wa nchi hii?
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ina wajibu kulinda na kuhakikisha ustawi na maendeleo ya watoto nchini, wajibu huu umeainishwa katika Katiba, Sera na Sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali kuhakikisha kuwa watoto wote nchini wanapata haki zao za msingi. Baadhi ya jitihada hizo ni pamoja na kutoa msamaha wa huduma za afya kwa wototo wenye umri chini ya miaka mitano na akina mama wajawazito, kutoa elimu bure kwa watoto kuanzia shule ya awali hadi kidato cha nne.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, Serikali kupitia Wizara yangu na wadau mbalimbali wa watoto imekuwa ikitoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa wazazi, walezi, familia na jamii kwa ujumla kuhusu umuhimu wa matunzo na ulinzi wa watoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa sasa haijaona umuhimu wa kuanzisha Mfuko Malaam wa Watoto kwa kuwa, afua zilizopo zinakidhi mahitaji. Hata hivyo, nachukua fursa hii kutoa wito kwa wazazi, walezi, familia na jamii kwa ujumla kutekeleza wajibu wao katika makuzi na maendeleo ya watoto kwa kutumia rasilimali walizonazo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, ni wajibu wa Serikali ambazo ziko katika mamlaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha kuwa mamlaka zenyewe zinaweka mipango madhubuti ya kulinda ustawi na maendeleo ya watoto katika maeneo yao. Wakati huo Serikali itaendelea kusimamia na kuratibu huduma zinazotolewa kwa watoto ili kuhakikisha kuwa haki na ustawi wao unazingatiwa ipasavyo kama ilivyoainishwa katika Katiba, Sheria na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa iliyoridhiwa na nchi yetu.
Mheshimiwa Niabu Spika, suala la ulinzi, ustawi na maendeleo ya watoto ni mtambuka, hivyo, naomba kutoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge kuhakikisha kuwa Halmashauri zetu zinatenga bajeti katika maeneo haya yanayohusu ustawi wa watoto.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-
Serikali inatakiwa kuweka mkakati wa kuhakikisha mazao yanauzwa katika vituo maalum vinavyotambuliwa ili kuzuia walanguzi kufuata mazao shambani na kununua kwa bei ndogo:-
Je, Serikali haioni kuwa kuna umuhimu wa kutunga sheria kuzuia walanguzi kwenda kununua mazao shambani?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (K.n.y. WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa kuna umuhimu wa kutungwa Sheria ya Kuzuia Walanguzi kwenda kununua mazao ya wakulima mashambani. Aidha, kutokana na umuhimu huo, Serikali imeweka sheria ya kuzuia kununua mazao yakiwa mashambani kwa mazao yote yanayosimamiwa na Bodi za Mazao. Mazao hayo ni kahawa, chai, pareto, pamba, korosho, mkonge na tumbaku.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri za Wilaya zimepewa mamlaka kamili ya kutunga sheria ndogo (bylaws) au kuweka kanuni na taratibu zinazofaa za kuuza mazao ya wakulima katika vituo vilivyowekwa na Halmashauri hizo. Vituo hivyo ni pamoja na magulio na minada, ambapo mazao mbalimbali ya wakulima na wafugaji huuzwa kwa ushindani na kwa kutumia vipimo rasmi. Vituo Maalum vya kununua mazao vinawezesha kusimamia ubora na kurahisisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imefanya marekebisho ya Sheria ya Vipimo kupitia Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na. 3) wa mwaka 2016 (The Written Laws Miscellaneous Amendments)(No. 3) uliopitishwa na Bunge hili mwezi Novemba, 2016. Sheria hiyo pamoja na mambo mengine, itawezesha Halmashauri kutunga sheria ndogo za usimamizi wa vipimo kwa kuhakikisha kila kijiji kinaaanzisha vituo vya kuuza mazao na kusimamia matumizi ya vipimo rasmi.
CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itajenga barabara ya Kanazi - Kyaka kwa lami na kuimarisha Daraja la Kalebe linalopitisha magari yenye mizigo tani kumi ili iweze kupitisha mizigo hadi tani 40?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE) alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Kanazi hadi Kyaka yenye kilometa 55.86 ni sehemu ya barabara ya Mkoa ya Kietama - Kanazi hadi Kyaka yenye urefu wa kilometa 60.65.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipaumbele cha Serikali kwa sasa ni kukamilisha utekelezaji wa sera yake ya kuunganisha makao makuu ya mikoa na nchi jirani kwa barabara za lami. Baada ya hapo ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara nyingine za mikoa ikiwemo ya Kanazi hadi Kyaka utafuata kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia umuhimu wa barabara hiyo Wizara ya Ujenzi na uchukuzi na Mawasiliano kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hiyo ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka ambapo mwaka 2018/2019 jumla ya shilingi milioni 411.688 zimetengwa kwa ajili ya barabara hiyo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Serikali ilikuwa na mradi wa kujenga masoko katika eneo la Nkwenda na Murongo katika Wilaya ya Kyerwa lakini masoko hayo hayajakamilika na yametelekezwa. Je, Serikali ilikuwa na malengo gani kujenga masoko hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, masoko ya Nkwenda na Murongo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa ni kati ya masoko matano ya kimkakati yaliyopangwa kujengwa kupitia Mradi wa Uwekezaji katika Sekta ya Kilimo Wilayani (District Agricultural Sector Investment Project – DASIP) na ujenzi ulianza kutekelezwa mwaka 2006/2007 hadi mwaka Desemba, 2013. Masoko mengine yapo katika Halmashauri za Busoka (Kahama), Kabanga (Ngara) na Sirari (Tarime). Mradi huo uligharamiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika na Serikali ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lengo la ujenzi wa masoko hayo ya kimkakati ilikuwa ni kuanzisha mfumo thabiti wa masoko utakaoongeza tija na pato kwa wakulima ndani ya Wilaya husika. Mfumo huu ulijenga mazingira wezeshi kibiashara katika maeneo ya mpakani ili kurahisisha biashara na majirani zetu na kuinua hali za kiuchumi za wananchi wa maeneo hayo na uchumi wa taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mradi wa DASIP unafungwa Desemba 2013/2014, kazi ya ujenzi wa masoko hayo ilikuwa haijakamilika na yalikuwa katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa kuzingatia umuhimu wa masoko hayo ya kimkakati katika Halmashauri husika, Serikali imepanga kukamilisha ujenzi wa masoko hayo na mengine nchini kupitia Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II). Katika bajeti ya mwaka 2019/2020 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.9 kuendelea na ujenzi wa masoko hayo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Kuna upungufu mkubwa wa Walimu katika Shule za Msingi Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba:-

Je, ni lini Serikali itapeleka walimu wa kutosha katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ina jumla ya shule za msingi za Serikali 141 zenye jumla ya wanafunzi 80,224. Halmashauri ina walimu 1,172 wa shule za msingi kati ya walimu 1,783 wanaohitajika hivyo kuwa na upungufu wa walimu 611.

Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kutatua changamoto ya upungufu wa walimu nchini kuanzia Mei, 2017 hadi Oktoba 2019, Serikali imeajiri walimu 15,480 wa shule za msingi, walimu 7,218 wa shule za sekondari na fundi sanifu wa maabara 297 ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba imepatiwa walimu 66 wa shule za msingi yaani 37 ajira mpya na 29 walihamishiwa kutoka sekondari kwenda shule za msingi. Serikali itaendelea kuajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kwa kadri fedha na vibali vitakavyopatikana?
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Shule za watoto wenye mahitaji maalum hupokea wanafunzi wenye matatizo mbalimbali kama vile ulemavu wa viungo, viziwi, uoni hafifu na wenye ualbino; baadhi ya wazazi wamekuwa wakiwatekeleza wototo wao wakishawapeleka kwenye shule hizo:-

(a) Je, ni kwa nini Serikali haitoi fedha kwa shule hizo iliziweze kuhimili mahitaji ya watoto hao?

(b) Je, ni kwa nini Serikali inaziachia majukumu Halmashauri kuendesha shule hizo wakati zinapokea wanafunzi kutoka nje ya mkoa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, wanafunzi wenye mahitaji maalum wana haki sawa ya kupata elimu kama wanafunzi wengine wasio na mahitaji maalum. Kwa kutambua changamoto wanazokutana nazo wanafunzi hawa, Serikali kupitia mpango wake wa elimu bila malipo, imekuwa ikigharimia huduma za chakula kwa wanafunzi wote wenye mahitaji maalum wanaosoma katika shule za bweni na za kutwa. Vilevile Serikali imekuwa ikinunua vifaa na visaidizi kwa kadri ya upatikanaji wa fedha kisha kuvigawa kwa wanafunzi husika.

Mheshimiwa Spika, kwa kipindi cha mwaka 2015/2016 hadi 2018/2019, Serikali imetumia jumla ya shilingi bilioni 3.87 kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu shuleni. Changamoto kubwa kwenye utaratibu huu ni upatikanaji wa takwimu sahihi za wanafunzi wenye mahitaji maalum kutoka kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa na Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa upatikanaji na utoaji wa takwimu sahihi za wanafunzi wenye mahitaji maalum. Serikali itaendelea kusimamia utoaji bora wa elimu kwa wanafunzi wote wakiwemo wenye mahitaji maalum bila kujali mkoa au eneo ambalo anatoka.

Mhehimiwa Spika, ahsante.
MHE. CECILIA D. PARESSO (K.n.y. MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA) Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itatengeneza eneo la Katokoro linalounganisha Kata za Katoro na Kyamulaile katika Jimbo la Bukoba Vijijini ili kuondoa adha ya usafiri inayowakabili wananchi wa maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu:-

MheshimiwaSpika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo korofi la Katokoro ambalo limejaa maji lina urefu wa kilomita 5 ambayo ni sehemu ya barabara ya Katoro – Kyamulaile – Kashaba yenye jumla yakilomita 15.7 inayounganisha Kata za Katoro, Kyamulaile na Ruhunga. Aidha, barabara hiyo pia inaunganisha maeneo mbalimbali ya Halmashauriya Wilaya ya Bukoba na Halmashauri ya Wilaya ya Misenyi.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imefanya usanifu kwa ajili ya kuboresha eneo hilo korofi ambapo kiasi cha fedha shilingi milioni 572 kinahitajika kunyanyua tuta la barabara na kujenga makalvati.

Mheshimiwa Spika, ili kupata ufumbuzi kwa sasa katika mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali ilitenga fedha kiasi cha shilingi milioni 87 kwa ajili ya kurekebisha eneo korofi katika barabara hiyo. Hata hivyo, kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha mkandarasi aliyekuwa anafanya kazi hiyo alisimamishwa kutokana na eneo hilo kujaa maji.

Mheshimiwa Spika, wakati jitihada za kutafuta fedha kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu wa barabara hiyo zikiendelea, mara maji yatakapopungua, mara moja Serikali itamrejesha kazini mkandarasi huyo ili kurejesha mawasiliano katika eneo hilo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA Aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itawalipa fidia Wananchi wenye Viwanja eneo la Miganga West na East, Kata ya Mkonze katika Manispaa ya Jiji la Dodoma kwa kuwa uthamini ulishafanywa na baadhi ya Wananchi bado hawajalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifauatavyo:-

Mheshimiwa Spika, eneo la Miganga West na East katika Kata ya Mkonze ni miongoni mwa maeneo ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma ambayo yamepangwa, kupimwa viwanja na kumilikishwa kwa wananchi ili waviendeleze kwa mujibu wa Mpango Kabambe wa Mji Mkuu (Master Plan).

Mheshimiwa Spika, kufuatia uwepo wa miradi ya kimkakati wa ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) na ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa 400KV kutoka Chalinze hadi Zuzu inayotekelezwa na Serikali kupita katika eneo hili na kuathiri viwanja vilivyomilikishwa, imelazimu eneo hilo kutwaliwa chini ya Sheria ya Utwaaji Ardhi Na. 47 ya Mwaka 1967, Sheria ya Ardhi Na. 4 ya Mwaka 1999, Kanuni za Ardhi za Mwaka 2001, Miongozo ya Uthamini na Sheria ya Uthamini na Usajili wa Wathamini Na. 7 ya Mwaka 2016.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilifanya uthamini kwenye jumla ya viwanja 309 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.77 vilivyoathiriwa na mradi wa reli ya kisasa ambapo kiasi cha shilingi milioni 576.5 imeshalipwa kwa wananchi ikiwa ni fidia ya viwanja 231. Viwaja 78 vyenye thamani ya shilingi bilioni 1.2 vinaendelea kuhakikiwa na Ofisi ya Mthamini Mkuu ili kukamilisha taratibu za fidia zao kwa mujibu wa sheria. Aidha, Serikali imeshafanya uthamini kwenye viwanja 123 na makaburi manne vyenye jumla ya thamani ya shilingi bilioni 1.1 vilivyoathiriwa na mradi wa ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa 400KV.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao viwanja vyao vimeathirika na mradi huo, watalipwa fidia mara baada ya Mthamini Mkuu kukamilisha taratibu za kisheria. Ahsante sana.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, Serikali haioni kuwa kuajiri Walimu bila kujali muda wa kuhitimu, baadaye baadhi yao watashindwa kuajiriwa kutokana na umri wao kuwa mkubwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali katika mwaka wa fedha 2020/2021 iliajiri Walimu wa shule za msingi na sekondari wapatao 6,949.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuhakikisha haki inatendeka katika ajira hizo, Serikali ilitumia mfumo wa kielektroniki (Online Teachers’ Employment Application System – OTEAS) kwa ajili ya kupokea, kuchakata na kuwapangia vituo kwa mujibu wa vigezo vilivyowekwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya vipaumbele vya ajira hizo ni cha wahitimu waliohitimu miaka ya nyuma zaidi. Katika ajira hizo takribani asilimia 75.6 ni wahitimu kati ya mwaka 2014 hadi 2017 na wachache, takribani asilimia 24.4, ni wahitimu waliohitimu kati ya mwaka 2018 hadi 2019 ambao wengi walikuwa na mahitaji maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuajiri Walimu kwa kuzingatia mwaka wa kuhitimu ambapo waliohitimu muda mrefu watapewa kipaumbele. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, ni lini Wazee watapata nafasi ya uwakilishi Bungeni kama ilivyo kwa Vijana na Wanawake ili waweze kusikilizwa na kutoa ushauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P KATAMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu Swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Ibara ya 66(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, imeweka sharti la aina sita za Wabunge ambao ni Wabunge wa kuchaguliwa kuwakilisha Majimbo ya Uchaguzi, Wabunge Wanawake wasiopungua asilimia thelathini ya Wabunge wote, Wabunge watano kutoka Baraza la Wawakilishi, Mwanasheria Mkuu pamoja na Wabunge wasiozidi 10 wa kuteuliwa na Rais na Spika iwapo hatakuwa amechaguliwa kutoka miongoni mwa Wabunge.

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa Ibara ya 67(1)(b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeainisha moja ya sifa ya mtu kuwa Mbunge ni lazima awe mwanachama na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa. Hivyo tunatoa wito kwa Vyama vya Siasa nchini kutenga nafasi za uwakilishi wa wazee kama ilivyo kwa watu wenye ulemavu na vijana ili waweze kupata nafasi ya uwakilishi Bungeni.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, Serikali imechukua hatua gani ili kumaliza mgogoro uliopo kati ya Mbuga ya Rwanyabara na Kijiji cha Bushasha kata ya Kishanje Wilayani Bukoba ambao umedumu kwa muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kijiji cha Bushasha kipo Kata ya Kishanje katika Wilaya ya Bukoba. Kijiji husika hakipakani na hifadhi yoyote ya wanyamapori katika Mkoa wa Kagera. Aidha, hakuna mgogoro wowote kati ya Kijiji cha Bushasha na hifadhi yoyote ya wanyamapori zilizopo katika Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, mgogoro uliokuwepo katika Wilaya ya Bukoba ulikuwa kati ya Kijiji cha Kangabusharo katika Vitongoji vya Nshisha, Kangabusharo na Kayaga na Hifadhi ya Msitu wa Ruasina ambao tayari umefanyiwa kazi na timu ya wataalam.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itajenga Daraja la Kalebe – Bukoba Vijijini ili kuwezesha magari yenye uzito zaidi ya tani kumi kupita kwenye daraja hilo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza maandalizi ya kujenga Daraja la Kalebe ambapo kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa daraja hili inaendelea chini ya Mkataba wa Usanifu wa Barabara ya Kyaka II – Kanazi – Kyetema. Kazi ya usanifu imepangwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu wa 2022.

Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Maruku, Karabagaine, Nyakato, Kunazi, Katoma, Kemondo na Bujugo Jirani na Bukoba Manispaa?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha utekelezaji wa mradi wa maji Kata ya Katoma na wananchi wanapata huduma ya maji. Vilevile, utekelezaji wa miradi ya maji unaendelea kwenye Kata za karabagaine na Nyakato ambapo miradi imekamilika katika vijiji vya Itahwa, Kabale na Burugo. Maeneo ya Kemondo na Kunazi utekelezaji wa mradi unaendelea na umefikia asilimia 88. Kwa Kata za Maruku na Bujugo, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kumuajiri Mkandarasi na ujenzi utaanza mwezi Juni, 2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2023/2024, Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi kwenye vijiji vilivyobaki katika Kata za Karabagaine na Nyakato.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, kuna juhudi gani za kufanya matengenezo ya kudumu katika eneo la Kyabalamba lililopo kati ya Kata za Rubale na Izimbya – Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeendelea kuinua tuta la barabara eneo la Kyabalamba kwa kifusi cha mawe na kujenga madaraja madogo manne. Hadi sasa tuta la mita 400 na madaraja mawili yamekamilika na kazi itaendelea mwaka wa fedha wa 2022/2023. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha jengo la Makazi ya Askari Polisi lililopo Kata ya Buyekera Bukoba?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni moja kutoka kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2023/2024 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa jengo la makazi ya Askari Polisi lililopo Buyekera - Bukoba Mjini. Ujenzi huo unatarajiwa kuanza mara baada ya Wizara ya Fedha kuhamishia fedha hizo Jeshi la Polisi.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza: -

Je, suala la vifo vitokanavyo na utoaji mimba usio salama lina ukubwa na madhara gani nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa, matatizo yatokanayo na utoaji mimba ni moja ya sababu inayochangia vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara yanayotokana na utoaji wa mimba usio salama ni pamoja na maambukizo makali kwa mfumo wa uzazi ambao unaweza kupelekea mgonjwa kutolewa mfuko wa uzazi na wakati mwingine kupoteza maisha kabisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itamaliza mgogoro wa ardhi wa Rwanyabara baina ya mwekezaji na wananchi wa Kijiji cha Bushasha Bukoba Vijijini?
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2008, uongozi wa Kijiji cha Bushasha kilichopo katika Wilaya ya Bukoba uligawa ardhi yenye ukubwa wa ekari 242 kwa wawekezaji ambao ni Ndugu Deusdelt Rwehabura na Kampuni ya Kagera Tea Company Limited.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hatua hiyo, familia ya Ndugu Sosthenes Ntagalinda Kajwahula ilifungua Shauri Na. 104/2008 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya Bukoba dhidi ya Halmashauri ya Kijiji cha Bushasha ikidai ardhi iliyogawiwa kwa wawekezaji hao ni yao. Tarehe 20 Desemba, 2015, shauri hilo liliamuliwa ambapo familia ya Ndugu Ntagalinda ilipata tuzo ya kuwa wamiliki halali wa ardhi hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia uamuzi huo wa Baraza, wananchi waliokuwemo ndani ya eneo hilo wameendelea kulalamika kwenye ngazi mbalimbali za Serikali, hivyo uongozi wa ngazi ya Mkoa na Wilaya umeanza taratibu za kuzikutanisha pande husika kwa ajili ya suluhisho la ardhi hiyo nje ya mfumo wa Mahakama. Natoa rai kwa wananchi waliopo katika eneo hilo kuwa na subira wakati Serikali ikitafuta njia nyingine ya kumaliza mgogoro uliopo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, ni madhara gani humpata mtoto anapozaliwa na kuchelewa kulia au kutolia kabisa?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, madhara yanayoweza kumpata mtoto anapozaliwa na kuchelewa kulia ni kuathirika kwa ubongo ambapo hupelekea:-

(i) Kupata utindio wa ubongo;

(ii) Kuchelewa kwa hatua za makuzi na maendeleo ya mtoto kama vile kuchelewa kukaa, kutembea na kuongea; na

(iii) Kutochangamana na wenzake au kutokucheza na wenzake na kadhalika, madhara ni mengi.

Mheshimiwa Spika, natoa wito kwa kila mjamzito kuanza kliniki mapema mara tu anapogundulika kuwa na ujauzito sambamba na kuhakikisha wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma ili ikiwa kuna tatizo la uzazi pingamizi watoa huduma waweze kuwasaidia mapema kabla mtoto hajaathirika.

Mheshimiwa Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, kwa nini Askari wa Jeshi la Magereza wasihudumiwe na Mfuko Maalum kama Majeshi mengine?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA K.n.y WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Watumishi wa Jeshi la Magereza wanachangia na kupata huduma za mafao kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa mujibu wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma Na. 2 ya 2018 (The Public Service Social Security Fund Act No. 2 of 2018). Kwa kuzingatia utofauti uliopo kati ya Watumishi wa Jeshi la Magereza na Watumishi wengine wa Umma hususan umri wanaoutumia kazini, kwenye utumishi kwa kuzingatia umri wa ajira na kustaafu kwa vyeo, muda wa kazi (masaa 24), asili ya kazi (mazingira hatarishi), Serikali imeanza kuchukua hatua kwa kuwashirikisha wadau mbalimbali ili kupata maoni na mapendekezo ya namna bora ya kushughulikia uchangiaji na ulipwaji wa mafao ya wastaafu wa vyombo vya usalama walio chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wakiwemo wa Jeshi la Magereza. Nashukuru.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itaanzisha Maabara ya kupima Sampuli za Magonjwa ya Mifugo Mkoani Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, uanzishwaji wa Maabara ya Kupima Sampuli za Magonjwa ya Mifugo Mkoani Kagera lipo kwenye mpango wa muda mrefu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) kama ilivyo pia katika Mikoa mingine. Aidha, utambuzi wa sampuli za magonjwa ya mifugo kwa Mkoa wa Kagera kwa sasa unafanyika kupitia maabara ya Kanda iliyopo Mkoani Mwanza ambayo ni miongoni mwa maabara 11 zilizopo nchini na zinamilikiwa na Serikali, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA aliuliza:-

Je, lini Serikali itahakikisha usalama wa abiria na mali zao kwa wasafiri wanaotumia Meli ya MV Victoria ndani ya Ziwa Victoria?
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, usalama wa abiria na mali zao kwa wasafiri wanaotumia meli ya MV Victoria ndani ya Ziwa Victoria ni suala la muda wote na ni kipaumbele namba moja kwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) inahakikisha usalama wa abiria na mali zao kwa wasafiri wanaotumia vyombo vyote vya majini, ikiwemo meli ya MV Victoria ndani ya Ziwa Victoria kwa kukagua meli hizo mara kwa mara na kuzipatia vyeti vya ubora, ambapo kwa cheti hicho inamaanisha meli imekidhi vigezo vya usalama kwa abiria na mali zao, ulinzi na utunzaji wa mazingira majini. Aidha, meli zote ikiwemo MV Victoria zinasisitizwa kuwa na vifaa vya uokozi ambapo abiria melini hutangaziwa uwepo wa vifaa hivyo na jinsi ya kuvitumia.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, TASAC inaendelea na mikutano ya uelewa na kufanya kaguzi za kushtukiza kwa meli na kuhakikisha manahodha na wafanyakazi wengine wote wamepata mafunzo ya umahiri na kuwa na vyeti hai vinavyotolewa na TASAC.