Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Conchesta Leonce Rwamlaza (35 total)

MHE. CONCHESTER L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Msingi wa swali langu ni malalamiko ya wastaafu wanaopokea pensheni kwamba hawajawahi kuongezewa fedha hizi. Kwa kuwa kuna malalamiko hayo na kwa kuwa Serikali sasa imetoa tangazo hili kupitia swali langu, je, inasema nini kuhusu wale wastaafu ambao hawajalipwa kiwango hicho kipya na wanaelekezwa vipi namna ya kudai fedha zao hizo pamoja na arrears? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa swali zuri la Mheshimiwa Rwamlaza. Alichokisema na Serikali inafahamu kipo, lakini naomba niseme yafuatayo:-
Katika ongezeko hili ni Mfuko wa PSPF pekee ambao umeweza kulipa sh. 100,000 kwa mwezi mpaka leo. Mifuko mingine iliyobaki kwa mujibu wa vifungu vya 25 na 36 vya Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya mwaka 2008 kama ilivyorekebishwa na Sheria Na. 5 ya mwaka 2012, kima cha chini cha pensheni kwa mifuko yote inatakiwa kupandishwa na Mamlaka hii ya SSRA. Kwa sasa Mamlaka hii inamalizia kufanya actuarial valuation kwa Mifuko yote hii na Bodi za Mifuko hii pia zipo katika mchakato baada ya actuarial valuation kukamilika ili waweze kuanza kulipa rasmi.
Mheshimiwa Spika, kuhusu kulipa arrears zao, wastaafu wote watalipwa arrears zao baada ya actuarial valuation kukamilika na Bodi za Mifuko hii kukamilisha mchakato huu kuanzia Julai 2015. Kwa hiyo, wasiwe na wasiwasi watalipwa arrears zao zote.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Napenda niulize maswali mawili tu ya nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo alioyasema Waziri nakubaliana nayo, lakini bado katika nchi yetu watoto wanaendelea kuteseka na wengine wanarandaranda mitaani. Je, Serikali haioni kwamba, imeshindwa kuweka maandalizi kwa ajili ya kutoa huduma sahihi kwa watoto? (Makofi)
Swali la pili, moja ya kazi za Serikali ni kuandaa kizazi chake kutoka kizazi kimoja hadi kingine na ndiyo maana nchi nyingine wanatenga mifuko kama hiyo na wanadiriki hata kulipa wanawake wanapokuwa wajawazito pesa kidogo kidogo ambazo baadaye umsaidia mzazi pale mambo yanapokuwa magumu kule mbele.
Je, sasa Serikali haioni ni wakti muafaka wa kufikiria kuanzisha mfuko huo ili kuweza kulinda watoto wetu wakue vizuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, kuhusu mfuko, naomba arejee majibu yangu kwenye jibu la msingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la kwanza, napenda tu kusema kwamba jukumu la malezi ni jukumu letu sote kama wazazi na linaanzia moja kwa moja kwenye familia. Sisi wanaume na wake zetu, tuchukue jukumu la kulea watoto tuliowazaa wenyewe. Kwa tamaduni za Kiafrika, extended family ina wajibu kwenye kulinda ustawi na kutoa ulinzi kwa watoto wote ambao wanaachwa na ndugu zetu, ambao pengine wametangulia mbele ya za haki ama wamepoteza uwezo wa kutoa malezi kwa mtoto.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia Mamlaka za Serikali za Mitaa ambazo Wabunge ni Wajumbe, zina majukumu ya msingi ya kuhakikisha ulinzi na ustawi wa watoto kwenye maeneo yao. Hivyo, ninatoa wito kwa Wabunge wote na jamii kwa ujumla tuweke mikakati madhubuti katika Mamlaka za Serikali za Mitaa tunakoishi kwa ajili ya kutoa ulinzi na ustawi kwa watoto.
NAIBU SPIKA: Waheshimiwa muda wetu umeenda sana. Tunaenda kwenye swali la mwisho, Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mheshimiwa Peter Joseph Serukamba, Mbunge wa Kigoma Kaskazini, sasa aulize swali lake.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna umuhimu wa kuwa na sheria hii na pia imesema imetunga sheria kwa ajili ya mazao yale yanayosimamiwa na bodi ya mazao: Je, Serikali haioni sasa ni wakati muafaka wa kuweza kufanya marekebisho katika sheria hiyo ili hata mazao mengine mchanganyiko yaweze kulindwa ili wakulima waweze kufanikiwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; ni wazi kwamba bado ulanguzi wa mazao unaendelea, walanguzi wanafuata wakulima mashambani na siyo sahihi kusema kwamba magulio ni sehemu ya ushindani wa bei na Halmashauri zenyewe hazijawa na mkakati maalum wa kuweza kuunda sehemu za kuuzia mazao na kuweza kuzisimamia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali inachukua hatua zipi kuhakikisha kwamba vituo hivi vinakuwepo na vinakuwa na usimamizi ili wakulima waweze kunufaika kwa kupata bei nzuri kuweza kubadilisha maisha yao?
Mwenyekiti, ni kama ambavyo nimeeeleza katika jibu la swali la msingi kwamba Serikali inaona umuhimu wa kuanzisha sheria.
Kwa hiyo, ombi lake tumelipokea na Serikali imeshaonesha nia kwamba hilo inalishughulikia na imeshaanza kufanya kwa mazao hayo mengine. Kwa maana nyingine tutaendelea kushughulikia na mazao mengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kule kwetu Namtumbo magulio kwa kweli huwa yanaleta ushindani. Kwa hiyo, naungana kabisa na jibu la msingi kwamba Halmashauri waimarishe magulio na sehemu za minada kwa kweli maeneo hayo yanaleta ushindani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna njia nyingine kutokana na mazao mbalimbali mengine, tuwasiliane na Halmashauri hizo na sisi ni wajumbe wa Halmashauri, tuweze kuboresha kanuni zetu, bylaws zetu, ili tuhakikishe mkulima anapata haki yake kwa jasho analolitoa.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona.
Sehemu ya swali langu imeshajibiwa lakini naomba niulize. Kwa kuwa sasa hizi
pombe zinatumiwa sana na watu wengi, ni kwa nini Serikali sasa isifikirie kujenga
kiwanda cha kuzisafisha na kuziwekea viwango kama Uganda wanavyofanya
na kile kinywaji cha „Uganda Waragi‟?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi ya
Serikali ni kuweka mazingira ya uwezeshaji, wanaowekeza ni Sekta Binafsi.
Nichukue fursa hii shangazi, tujasirie kusudi tuweze kukusanya ile konyagi ya
nyumbani, tuiweke kwenye ubora tuweze kuuza. Kila mtu atafute fursa kwake
kusudi aweze kuboresha vile vinywaji ambavyo havina viwango viingie kwenye
viwango, tupate pesa, tutengeneze ajira lakini mwisho wa siku tulipe kodi.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, Bukoba Vijijini ni Wilaya ambayo
ina jiografia kubwa na magari ya Bukoba Vijijini yote hasa ya hospitali ni mabovu. Juzi imetolewa ambulance, badala ya kupelekwa kwenye Hospitali ya Wilaya ya Izimbya ikapelekwa kwenye Zahanati ya Kishanji. Naomba kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri ndivyo mlivyopanga au ni mipango ya Halmashauri?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, tumelisikia hili. Kama alivyosema Mheshimiwa Waziri wa Afya, lengo letu kubwa ni kwamba haya magari ya chanjo yakienda katika maeneo yafanye kazi inayokusudiwa. Sasa kwako wewe kuna scenario tofauti kwamba gari lilitakiwa liende katika hospitali lakini limeenda katika zahanati, lakini ninachoamini ni kwamba kule kuna DMO, viongozi na Mkurugenzi pale, inawezekana kuna jambo ambalo tutaenda kulifanyia kazi tujue nini kilichoendelea.
Mheshimiwa Spika, letu kubwa ni kuhakikisha tunazozipeleka resources na hasa katika sekta ya afya, lazima watu wasimamie mwongozo huu. Gari kama ni la afya litumike kwa ajili ya afya. Ndiyo maana sasa hivi mikoa mingine hata kiwango cha chanjo wanashuka kumbe ni kwa sababu hawazingatii miongozo maalum ya Serikali ambayo tunaelekeza kila siku.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
Mheshimiwa Spika, ni jambo la kushangaza na
kusikitisha kwa sababu wafanyakazi mimi nina malalamiko yao, nina document nitaweza kumletea Mheshimiwa Waziri hawajalipwa wale wafanyakazi na wengine wamefikia mahali pa kustaafu hawajapata hata pesa zao. Kile kiwanda
kimebaki kubadilishwa na wasimamizi mara kwa mara kwa ajili ya kutaka kuwadhulumu wafanyakazi pamoja na wakulima. Ni lini Waziri utakwenda pale kuhakikisha wewe mwenyewe kwamba wafanyakazi wameshalipwa? Mheshimiwa Spika, nina uhakika hawajalipwa hata senti tano.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwishasema kwa
Mheshimiwa Rweikiza, niko tayari kukutana na Waheshimiwa Wabunge ili tufananishe taarifa tulizonazo. Taarifa sisi tuliyonayo ni kwamba tayari kuna malipo ambayo yamefanyika siyo yote sawa, lakini niko tayari kama nilivyosema kukutana nae ili tuangalie kwamba nani ana taarifa sahihi na vilevile Wizarani au Serikalini kama kuna Afisa
ambaye ameniletea mimi taarifa za uongo atachukuliwa hatua.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu uhuru barabara hii ni ya vumbi, lakini pia wananchi hawa ni wakulima wakubwa wa kahawa ambao wamekuwa wakichangia katika uchumi katika nchi yetu, lakini pia inashangaza ni namna gani Serikali inawaza zaidi nchi jirani kuliko watu wake ambao wanaendelea kupita katika barabara mbovu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize Serikali kwa sababu miaka ya uhuru ni zaidi ya miaka 50 wananchi wa eneo hili wasubiri sasa miaka mingapi ili barabara hii iweze kutengenezwa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili nimeuliza swali langu kuhusu daraja la Kalebe lakini Serikali imekwepa kabisa kugusia daraja hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, daraja hili linasaidia sana wanafanyabiashara na linabeba mizigo ya tani na linapitisha mizigo ya tani 10 badala ya 40 na kuna biashara kubwa ya mbao ambayo wananchi wanahangaika kupitia kutoka Bukoba Vijijini kwenda Kyaka na baadae kurudi Bukoba Mjini na hatimaye sasa kwenda Mwanza, kwa hiyo wanachukua muda mrefu.
Je, kwa sababu mmenionyesha dhamira ya kutokuweza kujenga barabara hii na ndio maana mmepuuza Daraja la Kalebe, sasa naomba nimuulize Waziri daraja hili sasa lina muda upi wa maisha kwa maana ya life span linaweza kudumu kwa muda gani ili kabla ya kufanyiwa matengenezo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ENG. ATASHASTA J. NDITIYE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jibu langu la msingi nimeeleza vipaumbele vya Serikali ambavyo nina hakika hata Mheshimiwa Mbunge naye anakubaliana navyo. Tumejipanga kuunganisha mikoa pamoja na nchi jirani, kisha baada ya hapo tutaenda kwenye barabara za mikoa kuunganisha sehemu mbalimbali na barabara yake hiyo ya Kyaka ikiwemo. Hatuna nia ya kuipuuza barabara hiyo na ndio maana kupitia bajeti ya mwaka huu ambayo bahati nzuri kabisa mwenzangu yule hakuiunga mkono tumetenga shilingi milioni 411 kwa ajili ya ukarabati ili njia hiyo iendelee kupitika mwaka mzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili la Daraja la Kalebe ninaomba tuwasiliane naye twende tukaangalie status kwa sababu siwezi kumpa majibu ambayo ni nusu nusu ambayo sina uhakika nayo. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, Mhandisi aliyekuwa anasimamia kujenga Soko la Nkwenda alikuja na Fuso mbili akahamisha nondo, mabati na saruji akidai anapeleka vifaa hivyo vya ujenzi katika Soko la Sirari katika Mkoa wa Mara na Serikali ina taarifa ya tuhuma za huyu Mhandishi. Je, ni hatua zipi zilichukuliwa dhidi ya Mhandisi huyu ambaye kwa kweli alikuwa kikwazo katika ukamilishaji wa soko hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwa kuwa katika majibu ya Serikali imesemwa kwamba masoko haya yalijengwa kimkakati ili kuweza kusaidia wananchi kufanya biashara na nchi zilizo jirani na maeneo ambayo yamejengwa masoko hayo. Je, sasa ni lini Serikali itayakamilisha?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la kwanza anasema kwamba huyu Mhandisi alipeleka magari kuhamisha vitu hivyo na kwamba Serikali tunayo taarifa na anataka kujua kwamba tumechukua hatua gani. Mpaka sasa tulishavielekeza vyombo vyetu vya ulinzi na kiuchunguzi kuendelea kuchunguza tuhuma na jinai hiyo ili ikithibitika amefanya jambo hili hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali lake la pili ni lini masoko hayo yatakamilika, kama nilivyojibu kwenye swali lake la msingi, kwenye bajeti hii tumetenga zaidi ya shilingi bilioni 2.9, Waheshimiwa Wabunge mkitupitishia haraka iwezekanavyo kuanzia Julai 1, tutaanza kutekeleza ujenzi wa masoko hayo yote.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali moja tu la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wako maredeva ambao waliondolewa katika mfumo wa Serikali kwamba wamemaliza Darasa la Saba, kwa hiyo hawastahili kuwa madereva. Naomba kuiuliza Serikali, ni kigezo kipi ambacho kilitumika kuona kwamba dereva wa Darasa la Saba anaweza kuendesha gari vibaya kuliko yule wa Darasa la 12?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba Serikali pia inawajali hata hao madereva wa Darasa la Saba. Naomba niliambie Bunge lako Tukufu kwamba madereva wote wale wa Darasa la Saba ambao walikuwa wamebainika kwamba vyeti vyao viko safi na taarifa zao ziko safi na waliandika ukweli, wapo kazini na wanaendelea na kazi kama kawaida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwa kuwa, sasa Serikali imetenga pesa kama ilivyo katika majibu ya msingi. Na kwa kuwa, tatizo la maji katika Kata zilizotajwa katika swali hilo ni ya muda mrefu. Je, Serikali inaji-commit vipi kwamba, huu mradi wa kuweka maji katika kata hizo utakamilika wakati gani?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili ni kwamba, kumekuwa na matatizo makubwa sana katika miradi ya maji katika nchi yetu na Serikali inaahidi kutoa pesa kwenye bajeti, lakini fedha haziendi kama inavyotarajiwa, lakini pia hata fedha zinazoenda zinatumika vibaya na kuifanya miradi hii isikamilike. Je, Serikali sasa inachukua hatua zipi kuhakikisha kwamba, hii miradi ya maji ambayo inapata fedha za Serikali inakamilika na fedha zinatumika ipasavyo?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, nataka nimfahamishe Mheshimiwa Mbunge kwanza sisi kama Serikali tumefanya jitihada kubwa sana pale Mikumi Mjini. Zaidi ya mradi wa milioni 974 tumeweza kutekeleza kupitia chanzo cha Madibira katika kuhakikisha wananchi wale wanapata huduma ya maji, lakini katika kuhakikisha tunatumia chanzo hiki cha Sigaleti sisi tunapitia usanifu kwa mara ya mwisho kabisa. Na ninataka nimhakikishie sisi kama Wizara ya Maji tutafanya jitihada kuhakikisha mradi huu tunauanza na kutekeleza katika kuhakikisha azma ya Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kumtua mwanamama ndoo kichwani inatimilika.

Mheshimiwa Spika, kuhusu swali la pili; utekelezaji wa miradi ya maji unategemeana na fedha. Na sisi kama Serikali, Serikali inatupa fedha moja ya changamoto kubwa ilikuwa ni muundo, lakini kupitia Bunge lako Tukufu umetunga sheria katika kuhakikisha kwamba, tuna sheria Namba 5 ya Huduma ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira na Uanzishwaji wa Wakala wa Maji RUWASA. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge huu utakuwa muarobaini katika kuhakikisha usimamizi wa miradi ya maji na fedha, kwa maana ya wakandarasi katika kuhakikisha wanatekeleza miradi ya viwango na katika kuhakikisha tunatatua matatizo ya maji, ahsante sana.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri maswali mawili ya nyongeza. Pamoja na majibu yake, anasema kwamba watumishi wanaweza kulipwa na Halmashauri lakini Halmashauri hizi hazina fedha. Kwa hiyo, nataka kujua kwa sababu Halmashauri hazina fedha Kifungu cha kuwalipa kitatoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na matatizo ya Bima ya Afya kwa sababu kuna wakati mwingine Halmashauri zinashindwa kurejesha fedha katika Mfuko wa Bima, kwa hiyo, kunakuwa na matatizo ya upatikanaji wa dawa. Je, tatizo hili mtalimaliza namna gani? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Mheshimiwa Mbunge anaulizia uwezekano uliopo wa Halmashauri kulipa. Kwanza utaratibu uliopo kama nilivyosema, ni kwamba manunuzi mengi ya dawa yanafanyika na wale Phamasists katika maeneo yetu ya wilaya. Ila kama Halmashauri ina uhitaji, huwa inaangalia pia na uwezo wake wa fedha; na kwa kawaida wanaomba kibali hapa TAMISEMI, tunawaruhusu wanaendelea kuwaajiri watu kwa mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejibu kwenye swali langu la msingi kwamba kama Serikali itapata uwezo itawajiri wawe wa kudumu panapokuwa na mahitaji, kwa kuwa tayari shughuli kubwa ya manunuzi inafanywa na wataalam wenyewe kuangalia vizuri viwango na tunawasiliana na wenzetu wa MSD moja kwa moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mheshimiwa Mbunge alitaka kujua namna ambavyo kunakuwa na changamoto ya dawa katika maeneo haya. Hatujapata sehemu ambayo wameshindwa kununua madawa haya. Naomba tupokee hoja ya Mheshimiwa Mbunge tuifanyie kazi. Kama kuna Halmashauri imepata changamoto hii, basi tuwasiliane ili tupate namna ya kuitatua ili mradi wananchi wetu waendelee kupata huduma kama ambavyo Serikali imekusudia kuwapa huduma bora katika maeneo yao ya karibu. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba sasa niulize maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, katika Mkoa wa Kagera, Halmashauri ya Bukoba na hasa Jimbo la Bukoba Vijijini ni mahali ambapo hawafanyi vizuri kielimu katika matokeo na hasa darasa la saba lakini pamoja mambo mengine ni ukosefu wa walimu na ni tatizo la muda mrefu. Kutokana na jibu la msingi bado kuna mahitaji ya walimu zaidi ya 500. Je, Serikali inalichukuliaje jambo hili na kuhakikisha walimu wanapatikana ili Bukoba Vijijini na yenyewe iweze kwenda mbele kielimu?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, yapo maeneo mengine katika Halmashauri mbalimbali za Tanzania ambapo yako mbali kabisa yaani tuseme ni remote areas ambapo walimu wakipelekwa hawaendi. Je, Serikali ina mpango gani kufanya uwiano kwa kuhakikisha walimu wanaenda katika maeneo hayo ili Watanzania wote waweze kufaidika na mfumo wa elimu uliopo katika nchi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la mama yangu Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema ni kwamba tutaendelea kufanya kila liwezekanalo na hasa katika mpango wa kuajiri walimu. Naomba nimhakikishie kwamba tutaweka kipaumbele katika Mkoa wetu wa Kagera tukijua kwamba mkoa huu ni miongoni mwa mikoa ya pembezoni na tunajua kwamba lazima tufanye juhudi ya kutosha. Kwa hiyo, katika mipango ya baadaye suala la walimu katika Halmashauri ya Bukoba tutalifanyia kazi.

Mheshimiwa Spika, lakini suala la nini Serikali inafanya kuhakikisha usambazaji wa walimu unafanyika, kutokana na changamoto hiyo, tulichokifanya kupitia mpango wa PforR tumehakikisha tunafanya msawazo wa walimu. Tulipeleka fedha katika maeneo mbalimbali kuhakikisha walimu wanatawanya na tuliwaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe wale walimu waliojazana mijini wanahamishwa kwenda maeneo ya pembezoni kwa kupewa posho maalumu za kuwahamisha walimu ili hata watu wa pembezoni wafaidike na programu hii ya elimu bila malipo ambapo ni jambo jema kwa ajili ya vijana wetu. Kwa hiyo, suala hili tunalifanyia kazi kwa nguvu zote Mheshimiwa.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali yangu mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, watoto hawa wanapopelekwa kwenye shule wazazi wao wanawatelekeza, hawafuati watoto wao kuhakikisha kwamba wanapata mahitaji maalum hasa mavazi. Siyo hiyo tu, shule hizo zinakosa pesa za kulipia walinzi, kulipa, maji, kulipa mapato na Matron na wengine wanahitaji misaada maalum na hasa wale wenye uoni hafifu au wasiyoona.

Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu sasa kuwepo na mpango maalum wa kuhakikisha kwamba watoto hawa fedha hizo zinapelekwa kwa kuzingatia kwamba Halmashauri hazina mapato, zimezinyang’anywa mapato yote, haziwezi kuhimili kumudu kusaidia shule hizo; Kuwepo na mkakati maalum wa kuhakikisha kwamba huduma kama hizo zinapatikana kwa watoto hawa.

Mheshimiwa Spika, shule ambazo mimi nimeuliza swali ni za Serikali, sikutegemea kwamba Serikali inaweza ikakosa takwimu maalum kwa ajili ya kuweza kutoa huduma.(Makofi)

Je, Serikali inataka kutuambia kwamba inafanya kazi bila kuwa na takwimu sahihi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Swali lake la kwanza Mheshimiwa Conchesta amezungumza hoja ambayo kimsingi inatakiwa Watanzania wote tuichukue na kuifanyia kazi. Ni kweli kwamba wako wazazi ambao wametelekeza watoto wao, hata akimpeleka shuleni, anamwacha pale moja kwa moja, hawezi kumfuatilia.

Mheshimiwa Spika, kwa kweli ni jambo hili ni jukumu la kijamii, haliwezi kuwa la Serikali peke yake, tulichukue na tuwashauri kwamba hawa ni watoto wenye haki sawa na watoto wengine, tuwapokee, tuwakubali, na tuwasaidie. Tukishikamana sisi Watanzania na jamii kwa ujumla na Serikali, jambo hili litakuwa jepesi sana.

Mheshimiwa Spika, vile vile Mheshimiwa Conchesta anapendekeza kwamba kama kuna uwezekano wa kupeleka fedha zaidi, tufanye hivyo. Ninachokizungumza hapa, tunapeleka huduma kwenye shule kulingana na idadi ya wanafunzi kulingana na taarifa tuliyopokea hapa. Hili swali nalijibu kwa pamoja na swali lake la pili. Tunapozungumza kwamba taarifa hazipatikani, kama alivyosema mwenyewe ni kwamba kuna watoto wengine wanafichwa katika jamii, kuna wengine kweli hawako kwenye mfumo rasmi, kuna wengine wapo mashuleni, lakini taarifa ya Serikali Kuu hapa TAMISEMI pamoja na Hazina ambao wanatuma fedha moja kwa moja kwenye mashule, tunapata taarifa kutoka kwenye Halmashauri.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika jambo hili natoa wito kwa Waheshimiwa Wabunge, Madiwani, Viongozi wa Vijiji na Mitaa, tupatieni taarifa sahihi. Tukipata taarifa sahihi, tutapeleka fedha kwa kiwango kinachotosha katika eneo lile; na hiyo ndiyo ambayo inakosekana hapa. Kwa hiyo, jambo hili ni la kwetu wote, tunaendelea kufanya kazi. Inawezekana kuna upungufu katika maeneo mbalimbali, tumetembea katika shule mbalimbali, lakini kuna upungufu, lakini kadri Serikali inavyopata uwezo imekuwa ikiimarisha huduma hizi.

Mheshimiwa Spika, tumesema hakuna mtoto ambaye atakufa katika shule hii au kupata shida kubwa bila kupata huduma. Cha muhimu tusaidiane, Mheshimiwa Mbunge kule wa Kagera ameona taarifa ipo, tuwasiliane, tutaipokea, tutalifanyia kazi. Lengo ni kuhakikisha kwamba watoto hawa wanapata elimu na ushahidi upo kwamba huko watoto waliachwa, walitelekezwa, wamechukuliwa na Serikali na wasamaria wema, wameingia kwenye mfumo rasmi, sasa hiivi ni viongozi wakubwa katika nchi hii, wamejiajiri na wanasaidia wenzao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kitu cha kwanza, majibu niliyopewa ni tofauti kabisa na majibu ambayo nimesomewa na Waziri, lakini naomba niulize maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sheria inasema, wakithamini wanapaswa walipe wale wathaminiwa ndani ya miezi sita; na kwa kuwa watu wengine wameshalipwa: Je, wale ambao hawajalipwa, kuna nyongeza yoyote ambayo itawekwa kwa ajili ya fidia kwa sababu Serikali imechelewa kulipa na hawajaweza kuendeleza maeneo yao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: mwananchi yeyote anapochukua kiwanja cha Serikali ambacho kimepimwa anakuwa amejihakikishia makazi yake kwa sababu atajiandaa katika maisha yake; kuchukua viwanja vyao, ukachelewa kulipa ni kuwadumaza: Pamoja na majibu aliyotoa, wale watu waliobaki watalipwa lini kwa commitment ya Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Conchesta kama alivyouliza. Kwanza nimpongeze Mheshimiwa Dugange kwa majibu yake mazuri.

Mheshimiwa Spika, swali lake la kwanza ana hofu ya kujua kwamba wale ambao hawajalipwa, watalipwaje pesa zao? Je, kutakuwa na nyongeza? Sheria iko wazi na tuliipitisha hapa 2019 tukafanya marekebisho kwamba inapofika miezi sita kama hajalipwa, tunaanza ku-calculate interest kwa bei ya soko iliyopo wakati huo. Hii inakwenda ndani ya miaka miwili, ikifika miaka miwili hawajalipwa maana yake lile zoezi inabidi lianze tena uthamini upya. Sheria tuliipitisha hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimtoe hofu tu kwamba watu hawa watalipwa kwa bei ya soko wakiwa wamewekewa na riba yao katika pesa walizochukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza, ni lini pengine wataacha kuchukua maeneo ya watu halafu wanakuwa hawana uhakika wa malipo yao? Naomba niseme tu kwamba katika maeneo ambayo Serikali inakuwa na interest nayo, lazima itaongea na washirika waliopo pale, wenye ardhi zao, kuwaambia dhamira na nia njema ya Serikali; na kabla ya kutwaa kunakuwa na makubaliano ambayo ni lini maeneo haya yatatwaliwa na kwa kazi ipi? Inapokuwa na public interest, huwa haina majadiliano zaidi ya kukaa nao na kukubaliana nini kifanyike?

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa hili ambalo tayari tunaona ni miradi mikubwa ya Kiserikali ambayo inapita, hatutakuwa na mjadala mwingine isipokuwa ni kuzungumza nao. Tayari Tume ya Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi katika maeneo yote inayopita miradi mikubwa, wameshaandaa mpango wa matumizi ya ardhi. Kwa hiyo, wale watakaobaki pale, watapimiwa maeneo yao, wale watakaotakiwa kuondoka kwa ajili ya kupisha pengine labda ni zile stations zinazojengwa, basi watapewa fidia yao kwa mujibu wa soko la wakati huo. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza; kwa kuwa sasa Serikali inasema inatumia mfumo wa online katika kupokea maombi ya Walimu; na kwa kuwa malalamiko ni mengi ambayo yalikuwa yanahusu Walimu kutoajiriwa kutokana na mwaka waliohitimu. Sasa napenda kuiuliza Serikali; haioni sasa kuna haja pale nafasi zinapopatikana za kuajiri waweke ukomo kwa wale wanaoomba kwamba mwaka huu tutapokea maombi ya wahitimu wa vyuo vya Walimu wa mwaka fulani hadi mwaka fulani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu la pili; Walimu kutoajiriwa muda mrefu kunawafanya wakae mitaani, lakini pia miaka inapita wengine wanaweza kutoajiriwa kwa sababu ya umri walionao. Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuwapatia refresher courses kwa sababu wale Walimu waliokaa muda mrefu wanapokuwa hawakuajiriwa wanasahau baadhi ya mafunzo yao na hata zile methodologies za kufundisha. Je, Serikali haioni kwamba wanastahili kupewa refresher courses na wako tayari kuzitoa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfumo huu wa Online Teachers’ Employment System ni mfumo ambao kwanza umeleta uwazi, lakini pia umeleta haki kwa wale Walimu wenye sifa kuajiriwa bila kuwa na upendeleo wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuwa na ukomo wa ajira, tumesema vigezo vyetu vilikuwa vitatu; kigezo cha kwanza kilikuwa ni wale waliohitimu muda mrefu zaidi. Ndiyo maana zaidi ya asilimia 75 ni wale waliohitimu mwaka 2014 hadi 2017. Hiyo consideration iliwekwa ili wale wenye umri mkubwa wapate nafasi ya kuajiriwa kabla ya umri wao wa miaka 45 kufikiwa na kukosa fursa ya kuajiriwa Serikalini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, wale walioajiriwa mwaka 2018 hadi 2019, wahitimu wa miaka hiyo walikuwa wana mahitaji maalum na walio wengi walikuwa wenye ulemavu. Kwa hiyo bado itakuwa siyo sahihi sana kuweka kigezo cha kwamba tuajiri miaka miwili au mitatu; kwanza hatujui ni Walimu wangapi watajitokeza katika miaka hiyo kulingana na mahitaji yetu na ni wangapi watachujwa na kuwa na sifa husika. Tunaweza tukasema kati ya 2018 na 2019 lakini wakatokea wachache wenye sifa na tukakuta tumeweza kuathiri zoezi hilo. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawapa fursa wote kuajiriwa, lakini tunatumia vigezo vyetu kuona nani kwa sasa apate ajira na nani anaweza akapata ajira awamu inayofuata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Walimu kukaa muda mrefu zaidi bila ajira, ni kwa sababu tumekuwa na baraka nzuri kwamba Walimu wengi wanazalishwa kwenye vyuo vyetu kila mwaka ikilinganishwa na kasi ya ajira ambayo ipo Serikalini lakini pia kwenye taasisi binafsi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la msingi ni kwamba mara baada ya kuajiriwa katika shule zetu kuna taratibu za refresher courses na on-job training na mentorship ambazo watazipata. Kwa hiyo automatically ukishaingia kwenye shughuli zao za kazi watapata mafunzo kazini na kuwawezesha kuwa competent zaidi. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Licha ya kupewa vibali na sheria ilivyo lakini hawa askari, wakiwakamata watu hasa wenye baiskeli wanaobeba mkaa wanaharibu hata vyombo vyao vya usafiri. Je, Serikali inataka kutuambia kwamba sheria inaelekeza hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Askari wa Mazao ya Misitu wanapokuwa wanasimamia kwenye mageti, tuna changamoto kubwa sana ya usimamizi wa mazao haya. Ndani yake tuna askari wanaotoka kwenye halmashauri na kuna askari wanaotoka kwenye Wizara yetu ya Maliasili na Utalii. Kwa hiyo, kuna mkanganyiko hapa katikati ambao unajitokeza wakitaja maliasili, hata kama angekuwa ni Mgambo basi lawama inarudi Wizara ya Maliasili.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, niendelee kuwaomba wananchi, kwa kuwa tuna vyombo vya dola; pale ambapo unatendewa vivyo sivyo ripoti na taratibu za kisheria ziweze kuchukuliwa haraka.
CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Wananchi 71 wa Kata ya Busindi, Kijiji cha Businde na Kitongoji cha Nyakabumbwe, pia katika Kijiji cha Nyakashenye, waliambiwa wapishe eneo lao kwa sababu ni ushoroba wa kupita tembo na waliahidiwa kupewa maeneo mengine, lakini hadi sasa pamoja na kupita katika mamlaka mbalimbali hawajapewa mahali popote. Je, ni lini Serikali itawapatia eneo la kuishi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kuna maeneo ambayo yamevamiwa na shughuli za kibinadamu ikiwemo hata ujenzi wa nyumba. Eneo la Kitengule ni eneo ambalo ni ranch ambapo sasa wananchi walipoyavamia yale maeneo tembo wakawa kama wako kwenye kisiwa. Moja ya tiba ambayo tulitaka kuifanya ni kufungua ule ushoroba ili tembo waweze kuruhusiwa ku-move kwenda kwenye Hifadhi ya Burigi Chato. Tulielimisha wananchi katika eneo hilo na utaratibu sasa wa kufungua hizi shoroba ni pamoja na wananchi kukubali kupisha zile shoroba.

Mheshimiwa Spika, tunafanya tathmini na tukishafikia muda ambao ni muafaka fedha na namna ya kuwahamisha wale tembo basi tutarudi kwa wananchi kuwafahamisha zoezi hili. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Pamoja na majibu aliyoyatoa Naibu Waziri, ukitazama Viti Maalum vina utaratibu maalum ambao umeshushwa na Tume mpaka kwenye vyama vya siasa. Je, haiwezekani sasa kuhakikisha kwamba utaratibu huu unashushwa ndani ya vyama vya siasa ili vyama hivi viwajibike kuwateua wazee ili na wenyewe waweze kupata nafasi ndani ya Bunge?

SPIKA: Mheshimiwa Conchester Rwamlaza hebu tusaidie, hilo kundi la wazee, unataka kundi la wazee kwa ujumla au kundi la wazee wanawake?

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, kundi la wazee kwa ujumla wao bila kujali wanawake au wanaume.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PATROBAS P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli Katiba yetu imeainisha vizuri katika vifungu hivyo, lakini pia ipo katika kifungu cha 36, 37 na 61 ambavyo vinatoa haki ya uwakilishi, lakini pia Ibara ya 21 ya Katiba, nayo pia inatoa haki ya kushiriki kwenye majukumu moja kwa moja ama kupitia uwakilishi. Zaidi kwenye Ibara ya 3 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inaeleza Tanzania ni Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi ya kidemokrasia, kijamaa isiyofungamana na dini au isiyofuata misingi ya dini na ina mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Mheshimiwa Spika, sasa katika vyama vingi vya siasa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1992, vyama vya siasa vinapewa haki ya kupata wawakilishi kwenye vyombo mbalimbali vya maamuzi, ikiwemo vyama hivi vya upinzani. Kwa mfano mzuri tu ambapo moja ya chama ambacho kinafanya hapa nchini vizuri kuna jumuiya ya vyama ambazo zinakuwa na wawakilishi wake, kuna moja ya chama kina umoja wa vijana UVCCM, lakini pili chama hicho kinao umoja wa wanawake, lakini pia kuna umoja wa wazazi na wawakilishi hao wote wameendelea kuwemo humo.

Mheshimiwa Spika, pengine hata Mheshimiwa naye atanikubalia, naye ni mmoja wa wawakilishi katika chama chake kwa sababu ni bibi yangu na ni mama, Mheshimiwa Conchester, kwa hiyo, nafasi hiyo inatolewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona.

Mheshimiwa Spika, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera haina Mtaalam wa Mifupa na wagonjwa wanalazimika kupewa rufaa kwenda Bugando na hivyo kuwa na gharama kubwa.

Je, ni lini Serikali itapeleka Mtaalam huyo kuwasaidia wananchi?(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hospitali zetu zote za Rufaa za Mikoa zimewekea mpango mkakati kwanza kwa kuhakikisha Wataalamu na Madaktari Bingwa wa yale magonjwa ambayo ni kipaumbele sana ikiwemo matatizo ya mifupa wanakuwepo. Kwa hivyo, tunapokea hoja ya Mheshimiwa Mbunge ili tuifanyie kazi kama Serikali tupate Daktari kwa ajili ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Naibu Waziri, lakini mimi nina swali moja tu la nyongeza, linaweza kuchukua muda kidogo, naomba unilinde.

Mheshimiwa Spika, mgogoro huu upo kati ya mwanakijiji na wanakijiji na umechukua muda mrefu zaidi ya miaka 15 na mgogoro huu unafahamika katika Serikali ya Kata, Serikali ya Wilaya, Serikali ya Mkoa na wameshindwa kufanya suluhu yeyote.

Kwa hiyo, sasa nomba Serikali sasa ione muda muafaka kwa Wizara ambayo wanaona inahusika na swali hili, wafike katika kijiji hicho, wafanye suluhu ili huyu mwanakijiji apate haki yake na wanakijiji wapate haki yao, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mhesimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Conchesta, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niziombe tu Serikali zilizoko kwenye Mamlaka ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa wakishirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi washughulikie mgogoro huu ili sasa wananchi waweze kupata haki yao na huyo mwekezaji aliyeko katika maeneo hayo pia aweze kufanyiwa haki yake, ahsante. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, transformer zinapoharibika na hasa vijijini huchukua muda mrefu bila kurejeshwa au kufanyiwa matengenezo na wakati mwingine inapita hata miezi sita.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba hizi transforme zinapoharibika zinarejeshwa kwa wakati ambao haumizi wananchi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Conchesta Rwamlaza kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli siku za nyuma manunuzi yalikuwa yanafanyika centrally na hivyo procedure zilikuwa zinachelewa kutoka kwenye Wilaya, Mikoa, Kanda mpaka kuja Taifa lakini kwa sasa TANESCO imeboresha utaratibu wake na kushusha manunuzi haya kwenye ngazi za Kanda mpaka kwenye ngazi za Mikoa na hivyo kurahisisha manunuzi kwa wakati.

Mheshimiwa Spika, kwenye bajeti inayokuja ambayo tutakuja kuiwasilisha hapa imetengwa fungu la ziada la kufanya matengenezo kwenye maeneo haya, kwa hiyo pesa itapatikana kwa haraka na kuweza kurekibisha maeneo ambayo yatakuwa yanapata matatizo ili kuwapa huduma wananchi.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi niweze kuuliza maswali madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; daraja hili ni la muda mrefu sana mimi napenda Serikali itueleze uhimilivu wa daraja hili ni wa kiwango kipi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Serikali kutojenga daraja hili ni kuendelea kuwapa adha wasafirishaji wanaosafirisha mizigo zaidi ya tani 10 ambao wanalazimisha kufanya mzunguko kupitia barabara ya Kyaka kwenda mpaka Bukoba Manispaa.

Je, hawaoni kwamba wanaendelea kuwapa adha wasafirishaji hawa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza kwa pamoja ya Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, daraja alilolitaja la Kalebe tunavyoongea sasa hivi mkandarasi yupo anafanya kazi na tunategemea akamilishe mwezi Oktoba japo kwa jinsi anavyokwenda anaweza akamaliza hata kabla. Lengo kuu la kufanya usanifu huu upya ni ili daraja hili liweze kubeba mizigo zaidi ya tani 10 kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera na yapo madaraja mengine pia tunafanya usanifu ili kuyapa uwezo zaidi wa kubeba mizigo tofauti na ilivyo sasa. Ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi niweze kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kuna matatizo makubwa na ya muda mrefu ya mawasiliano katika Mapori ya Kasindaga na Kimisi Mkoa wa Kagera: -

Je, ni lini Serikali itamaliza matatizo hayo?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Conchesta kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nipokee changamoto hii ili tukaifanyie kazi.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Pamoja na majibu ya Serikali ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza, napenda kujua sasa kwa miradi ambayo inaendelea itakamilikalini?

Swali langu la pili, Bukoba Manispaa mradi wake una chanzo cha uhakika ambacho ni Ziwa Victoria. Je, Serikali haioni kwamba kwa kushirikiana na BUWASA wanaweza kutazama uwezekano wa kutumia mradi huu ambao una maji mengi, ambao unaweza kupeleka maji katika Kata za Bujugo na Maruku? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI K.n.y. WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ambayo imeanza kama ambavyo tumeainisha hapa, mingine ipo asilimia 88 maana yake iko katika hatua za mwisho za utekelezaji wake, kwa hiyo kikubwa tu nimhakikishie kwa niaba ya Waziri wa Maji kwamba Wizara itaendelea kufuatilia kwa karibu ili miradi yote itekelezeka kama ambavyo tumesainiana katika mikataba kati ya Wizara na Mkandarasi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu chanzo cha uhakika cha Ziwa Victoria na maoni ambayo umeyatoa Wizara imeyapokea na itayafanyia kazi ili kuhakikisha tutumie hicho chanzo kuwaletea huduma wananchi wa Bukoba Manispaa. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONCHESTA LEONCE RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kunipa nafasi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sera ya Nchi yetu ni kutoa Huduma ya Afya bure kwa wazee lakini sera hii imekuwa haitekelezeki kwasababu hakuna sheria. Je, ni lini Serikali itatunga sheria ili kumbana mpeleka huduma na mtoa huduma ili sera hii iweze kutekelezwa sawasawa kwa wazee? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anachokisema Mbunge kipo sidhani kama tatizo ni sheria tatizo ni kwamba wazee kweli wamewekewa dirisha lao lakini wanapoandikiwa prescription na madaktari na baadhi ya vipimo wanapofika kwenye kufanya vipimo au kuchukua dawa wanakosa dawa husika na hilo ndiyo maana tunazungumzia suala la usimamizi wa dawa kwenye vituo vyetu na kuhakikisha dawa zipo kwenye vituo vyetu ambalo kwaweli kama Wizara ya Afya na TAMISEMI sisi wenyewe huku juu hatutaweza tunawaomba Waheshimiwa Wabunge, Baraza la Madiwani na Wakuu wa Wilaya wasimamie kwasababu kuna fedha nyingi zinakuja za Basket Fund na mambo mengine ambayo usimamizi ukifanyika tutapunguza tatizo kwa zaidi ya asilimia 80 lakini Mheshimiwa Mbunge tukishapitisha Muswada wa Bima ya Afya kwa watu wote maana yake kimsingi suala hilo tena alihitaji sheria suala hilo ni kwamba tutakuwa tumelitatua moja kwa moja, ahsante sana.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kazi ambayo imetajwa kufanyika lakini katika mvua za masika ambazo zimenyesha na kumalizika juzi hili eneo lilibomoka maji yakafurika na magari yakashindwa kupita.

Sasa swali langu liko hivi bila shaka huyu mkandarasi aliyefanya kazi hiyo alilipwa; je, Serikali ilijiridhisha kabla ya kumlipa mkandarasi kwa kazi aliyofanya?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili; eneo hili ni eneo la Tingatinga na ni la miaka mingi, je, Serikali haioni haja kwamba panastahili kufanyika upembuzi yakinifu makini na kwa kutumia wataalamu makini ili eneo hili liweze kutengenezwa kwa ufanisi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Rwamlaza, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla ya kufanya malipo yoyote lazima Serikali ijiridhishe kwamba kazi iliyofanyika inahitaji malipo. Lakini nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kipindi cha mvua hata nyumba kama hii inaweza ikaondolewa na mvua. Kwa hiyo, suala la mvua ni suala lingine, lakini nachotaka kumwakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tathmini ilifanyika na kazi ilikuwa imefanyika lakini mvua inaponyesha haiwezi ikaondoa kitu chochote.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili kwa kuwa tathmini ilifanyika na eneo tunalojenga tuta walishafanya tathmini. Kwa hiyo tuna uhakika kwamba tutaendelea kuliinua hilo tuta na ndio maana tunaongeza madaraja na kuinua tuta ili eneo hilo ambalo Mheshimiwa Mbunge anafahamu ni swamp area tuta lazima liinuliwe na ndio maana tumeongeza madaraja ili yaweze kupitisha maji yasiweze kukwama, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu ya Waziri, jengo hili limeanza kujengwa tangu mwaka 2010 ni miaka 13 sasa.

Kwanza, niulize Serikali kwa nini imetelekeza jengo hili mpaka limekuwa gofu?

Mheshimiwa Spika, sasa kwa sababu Serikali imesema itatoa bilioni moja, mtupe commitment Serikali ili azma ya kujenga jengo hili iweze kutimia. Ni lini Serikali inakwenda kukamilisha jengo hili?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ni lini Serikali itakamilisha jengo hili? Nimeeleza kwenye jibu la msingi kwamba ni pale tutakapopata fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya mwaka huu kwa ajili ya ukamilishaji.

Mheshimiwa Spika, nikuhakikishie tu Mheshimiwa siyo dhamira ya Serikali kuacha majengo kuwa magofu, majengo mengine yalitegemea uwepo wa fedha pale ambapo tulikwama na umesema ni miaka 10 iliyopita, ndiyo maana majengo mengi sasa hivi tunayakamilisha. Ukienda maeneo mbalimbali Geita Jengo la Polisi la Mkoa linakaribia kukamilika, Mara linakaribia, Njombe limekaribia kukamilika. Kwa hiyo, tuna imani Wizara ya Fedha itakapotoa fedha hizi ili jengo la Kagera pia tutalikamilisha. ahsante sana. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru; ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo TBC Radio ambacho ni chombo kikuu cha habari cha Tanzania, walikuwa wanaendesha mjadala kuhusu jambo hili. Wao wamesema ni asilimia 19, ninyi mnasema ni asilimia kumi. Naona mkasawazishe hapo kwa sababu nyote mnatoa taarifa kwa jamii.

Je, Serikali imejipangaje kupunguza hii asilimia kumi ya vifo vitokanavyo na kutoa mimba kusiko salama?

Swali la pili; Serikali iliridhia na kusaini Mkataba wa Maputo wa Nyongeza ambao mkataba huu ulikuwa unatetea haki za wanawake na afya pamoja na uzazi salama. Makubaliano hayo yalilenga kwamba mimba zitolewe zile ambazo zinapatikana kwa kubakwa, mimba ambazo zinatokana na mashambulio ya ngono na zile mimba maharimu yaani zile mimba ambazo zinatokana na ndugu. Je, Serikali sasa haioni ni wakati muafaka wakuweka makubaliano hayo katika sheria za nchi yetu ili kuwasaidia wamama ambao wanapata mimba za aina hii waweze kuzitoa kwa usalama bila kuhatarisha maisha yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Mbunge, kwamba eneo hilo ni muhimu lizungumziwe ili kuendelea kutoa hamasa kwamba kuna tatizo na kuna watu wanapoteza maisha kwa sababu ya mimba zisizo salama. Mheshimiwa Mbunge umesema hili la TBC inategemeana ni nani alikuwa anaongea na source yake ya data ni wapi, lakini sisi tuna source ambayo inakubalika kwa sababu tunajua duniani kwa mwaka wanawake milioni 42, mimba zisizo salama ni milioni 20 na kidunia ni asilimia 13 ambayo wanapata haya matatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tutafuatilia TBC wametoa source wapi lakini data ambazo tunazo kwa kupitia mifumo ya hospitali zetu za Serikali na private inaonyesha hili ambalo tumelisema hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu tunashushaje sasa hiyo, tutaendelea kutoa hamasa kuhakikisha kwamba tunashirikiana na Wizara ya Elimu, tunashirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii na nyinyi wenyewe Wabunge kila mmoja awe balozi wa kuonyesha kwamba watoto wetu kuna wakati muafaka wa kupata mimba, kuna wakati muafaka wa kuanza hayo mambo ambayo yanasababisha hayo matokeo. Wote tukiboresha na tukahamasisha maadili katika jamii yetu ni mojawapo ya sehemu yakushusha mimba kama hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili unazungumzia kwamba mikataba ya kidunia lakini pia kuruhusu sasa ili watu waweze kwenda kutoa mimba, sheria zetu ziruhusu. Hii inahitaji mchakato mkubwa kwa sababu inagusa Wizara mbalimbali lakini inagusa imani mbalimbali za watu na mambo mengine. Ninakuomba tupeni muda tuendelee kuchakata ili tusije tukajaribu kuzuia tatizo kwa namna nyingine tukazalisha tatizo lingine. Mimi ninachokuomba Serikali ipo committed na elimu itaendelea kutolewa na wewe uwe balozi wetu kwenye eneo lako. (Makofi)
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro huu ni wa muda mrefu na Serikali ya Mkoa na Wilaya ina taarifa ya mgogoro huu na walishindwa kuukamilisha mpaka wakafika hatua hii. Mimi nasema kwamba kwa hatua ambayo Serikali inapanga kwamba sasa wamalize huu mgogoro ambao ni wa kijamii, mtu hawezi akawa na eka 240 akidai ni chifu na huku wanakijiji wanadai ni mali ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naitaka sasa Wizara yenyewe kwa sababu mmekuwa mnaonesha kumaliza migogoro hii, sasa mwende ninyi wenyewe mkasaidie hawa watu wa Mkoa na Wilaya ambao walishindwa kwa muda mrefu. Mwende mkahakikishe mnamaliza mgogoro huu ili mwekezaji apate eneo lake na wanakijiji wapate eneo lao waweze kukaa kwa amani, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ushauri uliotolewa na Mheshimiwa Mbunge tunauchukua na tunakwenda kuufanyia kazi. Nimwahidi tu Mheshimiwa Mbunge tutakwenda huko kwenye eneo la tukio ili tuone kwa kushirikiana na Mkoa tunamalizaje jambo hilo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kuniona, wananchi wa Kata ya Kasharunga katika Kijiji cha Kasharunga katika Wilaya ya Muleba wamejenga Kituo Kidogo cha Polisi na kimekamilika. Ni lini Serikali itafungua kituo hicho kwa kupeleka askari ili wananchi waweze kupata huduma waliyoihitaji?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nijibu swali la Mheshimiwa Rwamlaza, kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika eneo hilo na nimhakikishie kwamba tuko tayari kwenda kufungua wakati wowote hata baada ya Bunge la Bajeti na tutaleta askari tayari kwa kutoa huduma katika eneo hilo.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, ahsante ninayo maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza; ni kwa nini Serikali haitoi elimu na elimu ikawa endelevu kwa wanawake wanapokuwa wajawazito na pale wanapojifungua ili wapate uelewa kuhusu madhira haya uliyoyataja yanayotokana na watoto kutolia wanapozaliwa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; watoto wanaoathiriwa na jambo hili huwa wanatibiwa kwa gharama kubwa na kwa muda mrefu, je, ni kwa nini Serikali sasa haioni haja ya kupunguza au kuweka ruzuku katika dawa wanazotumia watoto ili waweze kutibiwa kwa gharama nafuu?
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kweli amekuwa akifuatilia kwa karibu sana masuala haya hasa kwenye Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Spika, moja kwanza nimtoe wasiwasi, kwa sababu ukiona Serikali imeboresha miundombinu unaweza ukaona jinsi teknolojia imepelekwa mpaka kule chini, miundombinu imeboreshwa na hiyo matokeo yake ndio maana WHO walitegemea kwamba Tanzania ishushe vifo vya akina mama toka vifo 556 mpaka 225 ifikapo mwaka 2025, lakini kwa kazi kubwa iliyofanyika maana yake toka mwaka jana hata kabla ya muda ulitegemewa vimeshuka mpaka vikafika 104. Maana yake kuna juhudi kubwa sana ya kuhamasisha, lakini kufanya kwa vitendo kuhakikisha zile huduma zinafika chini na akinamama wengi wana-enroll clinic ndio maana vifo vimepungua.

Kwa hiyo, nikuhakikishie kwamba tutaendelea kufanya hiyo juhudi na kuongeza nguvu kwenye eneo hilo la elimu, lakini pia Wabunge tushirikiane kwenye mikutano yenu kuhamasisha.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili, wanapopata matatizo umemsikia Waziri wa Afya alipokuwa anafanya presentation ya bajeti yake hapa, moja ya maeneo ya kipaumbele katika yale maeneo kumi mojawapo ni eneo la utengamao tiba utengamao tunataka sasa hivi kuwekeza nguvu nyingi katika eneo hilo na kuwatambua hawa watoto mapema na kama ikiwezekana kuwapeleka kwenye vituo maalum vya mazoezi na mambo mengine ambavyo wataweza kufanya shughuli zao kama kawaida.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Ni mara ya tatu nauliza swali hili na Askari Magereza wamekuwa na kilio cha muda mrefu, kwa sababu wapo chini ya utumishi, wanapenda kulipwa kupitia Mfuko wa consolidated. Ni kwa nini Serikali imechelewesha jambo hili na hapa wanasema kuwa wanatafuta wadau, ni wadau gani ambao Serikali wenyewe wanashindwa kuhakikisha kwamba hao watu wanapata haki kupitia Mfuko huo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuwepo chini ya Utumishi, Askari Magereza wamekuwa hawapandi vyeo kwa wakati na wakati mwingine hata madaraja yao hayapandi kwa sababu wao wanahudumiwa na Tume ya Utumishi. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba jambo hili sasa linakamalika na wao wanapata haki yao kama Askari wengine? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Naibu Spika, najua mama Conchesta na baadhi ya wabunge wamekuwa wakizungumzia suala hili na hisia hizi ni za msingi kwamba wangependa walipwe kutoka consolidated fund. Kimsingi nasema linatekelezwa kwa mujibu wa sheria kama nilivyojibu katika jibu la msingi. Ili sheria iweze kufanyiwa marekebisho huhusisha uhusikaji wa wadau mbalimbali wakiwemo Wabunge, Jeshi la Magereza, wadau wengine ni muhimu ili kuwezesha jambo hilo kufanyika. Kwa hiyo ndiyo maana tunasema mjadala unaenda kwa kuwashirikisha wadau ili muafaka utakapofikiwa waweze pia kuwa elevated kutoka huku ili waweze kulipwa consolidated fund.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda pia niseme the way anavyoiongea Mheshimiwa Mbunge ni kama vile wanaolipwa kupitia Utumishi wanaonewa, si kweli. Kwa mfano, amezungumzia kupanda vyeo, Magereza kama vilivyo vyombo vingine vya Wizara ya Mambo ya Ndani, hawapandishwi vyeo na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, badala yake ipo Tume ya Utumishi wa Magereza, Fire, Uhamiaji, pamoja na Polisi wenyewe ambapo Tume hukaa kila mwaka kwa ajili ya kuwaona waliokuwa due kupanda wanapandishwa. Kwa hivyo, si kwamba kwa sababu hawapo chini ya consolidated fund basi kule Utumishi wanaonewa. Nashukuru.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Mkoa wa Kagera umewahi kuwa na maabara kubwa na nzuri chini ya Mradi wa KALIDEP na baadaye KADADET. Miradi hii ilipokufa na maabara hiyo ikafa. Ni kwa nini Serikali haikuendeleza maabara hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Mkoa wa kagera licha ya ukubwa wake lakini kuna mifugo mingi na kuna ugumu katika kupeleka sampuli kwa sababu ya umbali pia ukosefu wa wataalam, wakati mwingine wa dharura hulazimika madkatari kutoka Mwanza kuja kuchukua sampuli kutoka Mkoa wa Kagera. Je, ni lini Serikali itakuwa na mpango wa kuhakikisha kwamba hii Wizara ya Mifugo inakuwa na wataalam wa kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la kwanza ambalo Mheshimiwa Mbunge anataka kujua kwa nini Serikali haikuendeleza hizi maabara? Ni kweli maabara hizi zilikuwepo katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu, hususan Mkoa wa kagera kulikuwa na maabara, na hii ni kwa sababu ya wingi wa mifugo iliyoko katika Mkoa wetu wa Kagera. Tunatambua na kuwapongeza sana wananchi wa Mkoa wa Kagera kuwa wafugaji wazuri na maabara ilikuwepo na kama nilivyosema katika jibu la msingi kwamba, Serikali inayo mkakati wa kufufua maabara zote zilizokuwa zimekufa katika maeneo yetu mbalimbali ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa, kwa sababu maabara hizo zimekufa, wananchi na wafugaji wanashauriwa kupeleka sampuli zao katika Mkoa wa Mwanza ambako ndiyo kuna maabara kubwa katika kanda ya ziwa. Maabara hiyo imekuwa ikifanya vizuri na ina wataalam wa kutosha na kwa bahati nzuri sana wataalam wetu wako tayari kusafiri kuwafuata wafugaji kokote wanakopatikana, lakini hii haiondoi mpango wa Serikali wa kufufua maabara zetu zilizokuwepo katika mikoa yetu ikiwemo pamoja na Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, mpango wa kuwa na wataalam wengi ni mpango madhubuti wa Serikali chini ya Mheshimiwa Rais, na ameshatoa maelekezo tuendelee kutengeneza wataalam wa mifugo ambao watatusaidia kutoa elimu kwa wafugaji wetu katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali kupitia vyuo mbalimbali ambavyo viko ndani ya nchi yetu ikiwemo Chuo Kikuu cha Sokoine na vyuo vingine vidogo vidogo ambavyo vinatoa kwa level ya certificate, diploma na advance diploma tunaendelea kutengeneza wataalam wa mifugo ambao watasaidia kutoa elimu kwa wafugaji wetu ili mfugaji anapofanya shughuli za ufugaji aweze kupata tija katika shughuli hiyo aliyoifanya, ahsante.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Naibu Spika, swali la kwanza; Meli ya MV Victoria husafirisha abiria kwa madaraja matatu, daraja la tatu, daraja la pili na daraja la kwanza. Mimi nilisafiri na meli hiyo kupitia daraja la kwanza, nikalala usingizi nilipoamka saa saba badala ya watu wawili nilikuta tupo watu sita. Sasa napenda kujua ni taratibu gani zinatumika ili hao watu wa TASAC au kama ni Marine Service wanahakikisha usalama wa abiria kwa kufuata taratibu zilizowekwa?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; huko nyuma Afisa Kazi wa Mkoa alikuwa katika daraja la kwanza kwenye meli, alifuatwa ndani ya meli, akachukuliwa na akatupwa ndani ya maji akafariki. Je, Marine Service au kama ni TASAC sasa wako tayari kuweka ulinzi thabiti ndani ya meli kuhakikisha kwamba kunakuwa na usalama wa kutosha hasa ule usiku mkuu maana hii meli inasafiri usiku ndani ya maji? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpe pole Mheshimiwa Mbunge kama alivyoeleza kwa aliyoyasema Bungeni, lakini nimhakikishie na nitumie nafasi hii kutoa maelekezo maalum kwa Wakala wa Meli pamoja na TASAC kuhakikisha kwamba wanadumisha ulinzi na usalama kwa abiria kwa vyombo vyote majini siyo tu Ziwa Victoria na maeneo mengine yote ikiwemo Ziwa Tanganyika, Ziwa Nyasa na kwingineko kote.
MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kijiji cha Kasharunga, Kata ya Kasharunga katika Wilaya ya Muleba walijenga Kituo chao cha Polisi kwa nguvu za wananchi. Ni kwa nini Serikali haitaki kufungua kituo hiki? Watoe sababu wananchi waelewe. Ahsante sana. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Conchesta kama ifuayavyo:-

Mheshimiwa Spika, ninawapongeza sana wananchi wa Kijiji cha Kasharunga kwa kujenga Kituo cha Polisi. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, baada ya Bunge hili tutaenda kufungua kituo hicho kilichojengwa ili kuhudumia wananchi wa maeneo haya. Ahsante sana. (Makofi)