Supplementary Questions from Hon. Anastazia James Wambura (19 total)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri nina maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza; kama tulivyosikia majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri ni kwamba ni hekta 10 tu ndizo zimeendelezwa kwa asilimia 100 na wakati hekta zilizotengwa zaidi ya miaka 10 ni hekta 110. Kwa hiyo inashangaza sana kuona kwamba uendelezaji unasuasua sana. Napenda kujua, ni lini sasa hekta zote 110 zitaendelezwa ili kusudi wapatikane wawekezaji wengi Zaidi kwa sababu mpaka sasa ni wawekezaji watatu tu ndiyo wamepatikana? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; nataka kujua kama Serikali sasa itakuwa tayari kutoa sehemu ya eneo kwa ajili ya wajasiriamali wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kufuga kuku katika large scale kwa ajili ya ku-export nchi Jirani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Wambura.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza dhamira ya Serikali bado haijabadilika kwa hiyo ku-off load hilo eneo kwa ajili ya matumizi mengine, mahitaji ya namna hiyo yakitokea na ikionekana malengo ya awali yaliyokuwa yametengwa eneo hilo lote kwa ajili ya uwekezaji wa Oil and gas yamekuwa absolute kwamba haliwezi kufanyika then Serikali inaweza kutazama. Mpaka sasa Serikali bado inaamini kwamba kuna umuhimu wa kulihifadhi eneo hilo, kwaajili ya kuendelea kufanya expansion kwa awamu kutokana na mahitaji kama ilivyo sasa hivi. Kwa hiyo suala la kuligawa hilo eneo kwa matumizi mengine hilo bado halina nafasi kwa kipindi hiki.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu lini litaendelezwa lote; kama sote tunavyofahamu kwamba kuna wakati wa biashara ya gas na oil duniani ina-boom na kuna wakati imeshuka. Sasa hivi kama mtaona kwamba malengo yalikuwa ni kufanya uwekezaji kwa ajili ya kuhudumia uwekezaji wa oil and gas katika nchi yetu ya Tanzania, lakini kwa ajili ya nchi ya Msumbiji.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunafahamu kwenye ulimwengu namna gani ambavyo explorations ya gas ilivyoshuka na namna ambavyo uwekezaji uliokuwa ufanyike Msumbiji na wenyewe ume-delay sasa hivi. Kwa hiyo naamini kwamba Waheshimiwa Wabunge wa Mkoa wa Mtwara, mahitaji ya eneo hilo kwa ajili ya uwekezaji mkubwa kwa ajili ya gas na mafuta bado unahitajika duniani. Kwa hiyo tuta- expand matumizi ya eneo hilo kutokana na demand na kama kuna wawekezaji wako tayari maeneo ya Mtwara na wameshawa-approach Wabunge ama wananchi wa Mkoa wa Mtwara wanakaribishwa Wizara ya Viwanda na Biashara ili tuweze kujadili pamoja namna ya kulitanua hilo eneo.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake ambayo yanaonesha kwamba kazi inaendelea. Lakini niiombe Serikali, pamoja na kazi, kasi iendelee. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mkoa wa Mtwara una Kata 191 na kati ya Kata hizo, 137 zina shule za sekondari na Kata 57 hazina shule za sekondari. Na jambo hili linasababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu sana kufuata shule za sekondari, na matokeo yake ni upungufu mkubwa wa vyumba vya madarasa katika Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, katika shule hizi 310 Mkoa wa Mtwara umetengewa shule ngapi katika kipindi hiki? Hilo ni swali la kwanza.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili ni kwamba shule ni walimu pamoja na mambo mengine yote. Sasa Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu wa sayansi wa asilimia 41. Sasa nina wasiwasi kwamba kama hakutakuwa na maandalizi ya kutosha, kukamilika kwa madarasa au kwa shule hizi zitakazojengwa kutaongeza tena upungufu wa walimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba baada tu ya kukamilika kwa shule kunakuwepo na walimu wa sayansi wa kutosha ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu wa sayansi? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali madogo ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, tayari umeshanipa mwongozo kuhusu takwimu sahihi na mimi nitampatia takwimu sahihi katika mwaka huu wa fedha tutajenga shule ngapi. Lakini niwahakikishie wananchi wa Mtwara kwamba Kata zote zilizobaki 57 zitajengwa sekondari za Kata kwa sababu zipo katika mpango wetu kwa sababu idadi ya shule tulizonazo zinatosheleza Kata zote nchini ambazo hazina shule hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, anasema Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu, hususan wa sayansi, na alitaka kujua mpango wa Serikali ni upi kuongeza. Ni kwamba Serikali itaendelea kuajiri kama ambavyo tulitangaza hizi ajira ambazo muda mfupi, ndani ya wiki mbili hizi tutakuwa tumeshatoa hayo majina. Lakini vilevile Serikali itaendelea kuajiri walimu wengi zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie tu kwamba tutaendelea kuangalia hivyo vigezo ambavyo amevitaja, wakiwemo walimu wa sayansi, na masomo mengine hatutayaacha kwa sababu yote yanahitajika katika elimu yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)
NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, wakati unajibu hapo umesema fedha zinatosheleza kwenda kwenye kata zote ambazo hazina shule, na Mtwara wanazo 57. Hizo sule zote zitajengwa mwaka huu wa fedha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ambacho nilikuwa nakieleza kwa kifupi ni kwamba Mradi wetu wa Uboreshaji wa Elimu ya Sekondari Nchini ni ujenzi wa shule za sekondari 1,000. Na awamu ya kwanza Mwaka huu wa Fedha ambao tunakwenda, 2021/ 22, tunaanza kujenga shule 310.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo katika hizi 310 ni kwa mwaka huu. Halafu mwakani tutakuwa na idadi nyingine ya shule kwa Mwaka mwingine wa Fedha kwa maana ya 2022/2023, tutaleta fedha nyingine. Lakini mradi wetu unatosheleza kujenga shule zote kwa sababu tuna upungufu katika Kata kama 780 ambazo hazina sekondari za Kata hapa nchini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo bado tutajenga na bado zile kata ambazo zina idadi kubwa ya wanafunzi tutapeleka vilevile sekondari nyingine, yaani kutakuwa na sekondari mbili katika Kata moja ili tuweze ku-accommodate idadi kubwa ya wanafunzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilichomwambia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba awe na uhakika kwamba Kata zote za Mtwara zitafikiwa. Lakini kwa mwaka huu nitampa idadi kamili ya shule ngapi tunajenga na mwakani tutajenga shule ngapi na mara ya mwisho tutamaliza kwa ngapi. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa majibu yake mazuri na kutokana na hayo basi swali langu la kwanza litakuwa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa takwimu zake na kwa jinsi hali halisi ilivyo, zipo Halmashauri ambazo hazijakamilisha zoezi hili na ni kwa madai kwamba hazina mapato ya kutosha. Sasa je, Serikali inatoa tamko gani kwa zile Halmashauri ambazo hazina fedha za kutosha kukamilisha zoezi la utambuzi na la utoaji vitambulisho? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni kwamba lipo tatizo wazee wanapofika hospitalini wanaandikiwa dawa na kuambiwa waende kununua katika maduka ya dawa kwa madai kwamba katika kituo husika hakuna dawa: Je, Serikali inatoa maelezo gani pale ambapo wazee wanakuwa wakiambiwa wakanunue dawa ilhali wanastahili kupata matibabu ya bure? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge Anastazia kwa kuendelea kuwatetea na kuwapambania wazee. Naomba kujibu maswali yake mawili ya nyongeza kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kweli zipo Halmashauri ambazo zinashindwa kutimiza hili, kati yake zipo ambazo hawatimizi tu mpaka uwafuatilie sana na wapo wengine ambao kwa kweli uwezo wao unakuwa mdogo sana. Niseme kwenye bajeti yetu hii iliyopita, nilishukuru sana Bunge lako Tukufu kwa kupitisha ile bajeti yetu ya shilingi bilioni 149 ambazo tunatarajia kwenye muswada huu wa sheria zitakwenda kuhudumia zile nyumba zote wakiwemo wazee ambao watakuwa wamebainika kwamba hawana uwezo kabisa. Kwa hiyo, tunatarajia kumaliza kabisa hili suala la wazee hawa wasio na uwezo kabisa ili wawe covered kupitia Mpango wetu wa Bima ya Afya Kwa Wote tunaotarajia kwenda kuuchukua.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hivi tumekuwa na vikao vya kwenye mtandao pamoja na Mtandao wa Wazee nchi nzima, kila Jumamosi; tumeanza hiyo sera, “Jumamosi Zungumza na Wazee.” Tunafanya hivi vikao kujadili hizi changamoto. Wiki iliyopita tumekubaliana kwamba; awali iliagizwa asilimia sita ya bajeti tunayopanga lazima dawa zake ziende kwa wazee. Kwa hiyo, hata sasa hivi Serikali imefanya uamuzi wa kurudisha kupitia Hazina ile fedha ya Hospitali kwa mfano za Mikoa iliyokuwa inaenda moja kwa moja MSD, ili dawa zinapokosekana, zinunuliwe huko kwenye hospitali. Asilimia sita ya ile fedha ndiyo itumike kununua hizo dawa za wazee. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, katika Kamati za Maamuzi kwenye Vikao vya Bodi za hizi hospitali zetu, tumeona kwamba tuweke hata mwakilishi wa wazee awe anahakikisha kwamba anatetea ile hoja yake pale. Hii ni mikakati ya kufanya kwamba wazee wawe na sauti katika vikao vya maamuzi vya management za hospitali zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, vilevile tumeanza mkakati wa kila hospitali; mnawaona wale wamevaa nguo za “Mpishe Mzee Apate Huduma Kwanza.” Hawa nao wanachukua takwimu za kujua mzee gani amekwenda kituoni, ameondoka bila dawa ili Medical Officer in Charge ahusike kuhakikisha mzee huyu anapata dawa kwa taratibu hizi za kuweka bajeti ya dawa pembeni yao. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri na nampongeza sana kwa sababu aliweza hata kutembelea maeneo ya kiwanja hiki pamoja na mambo mengine aliyoweza kuyafanya. Nina maswali mawili ya nyongeza la kwanza kumekuwa na ongezeko la gharama za mradi awamu ya kwanza kwa kiasi cha takriban shilingi bilioni tano na ni kutokana na sababu mbalimbali na moja ya sababu ni kuchelewa kukamilika kwa mradi huu awamu ya kwanza.
Mheshimiwa Spika, lakini kwa hesabu za haraka haraka hizi bilioni tano zingeweza hata kujenga vituo takriban 10 vya afya. Swali langu je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na ongezeko hili la shilingi bilioni tano?
Mheshimiwa Spika, Swali la pili kama alivyoeleza Mheshimiwa Waziri, ni kwamba maboresho ya uwanja huu yamelenga kukidhi ongezeko kubwa la shughuli za kiuchumi na kijamii katika mikoa ya Kusini. Na ili kupandisha daraja kutoka Code 3c hadi 4e ni lazima ujenzi wa awamu ya pili ukamilike. Swali langu ni kwamba je ni lini awamu ya pili ya mradi huu itaanza? Ahsante.
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali ya nyongeza mawili ya Mheshimiwa Wambura kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na ongezeko la shilingi bilioni tano kwenye ujenzi huu na sababu kubwa iliyosababisha kuongezeka kwa bei hiyo, ni kutokana na makisio halisi hasa ya kufunga taa mwanzo ilikisiwa ni shilingi bilioni 2.2 lakini baada ya kupata mkandarasi gharama ikaenda mpaka bilioni 6 pia na kwenye fire equipment (gari la kuzimia moto) makisio yalikuwa milioni 800 na ilikwenda mpaka bilioni 1.5 kwa vile hii ndiyo iliyosababisha ongezeko liongezeke mpaka kwa shilingi bilioni tano.
Mheshimiwa Spika, swali la pili ni lini uwanja huu tutaweza kufungwa hizo taa. Awamu ya pili ambayo ni kufunga taa pamoja na kujenga jengo la control tower pamoja na jengo la abiria utaanza mara moja tu mara itapomalizika awamu ya kwanza ambayo itakuwa kunako mwezi Julai mwaka huu.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kuna zile fedha za marejesho za miaka iliyopita ambazo huwa zinajeshwa ambazo inaonekana kwamba kila halmashauri inakuwa na utaratibu wake.
Mheshimiwa Spika, nini kauli ya Serikali kuhusiana na hizi fedha zinazorejeshwa ambazo zingeweza kuongeza kiasi cha wanaokopa wakapata fedha nyingi zaidi? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la Mheshimia Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, maelekezo ya fedha za marejesho ya asilimia 10 zimefunguliwa akaunti zake mahsusi, kwa hiyo wajasiriamali wanaporejesha fedha zile zinatakiwa kuingizwa kwenye akaunti mahsusi ya marejesho ya mikopo ya asilimia 10. Akaunti ile ni revolving fund, maana yake baada ya kurejeshwa zinatakiwa kuendelea kuwakopesha vikundi vya wajasiriamali. Kwa hiyo, matarajio ya Serikali ni kwamba akaunti zile kila baada ya mwaka wa fedha zitakuwa zinaendelea kuongezeka na kutakuwa na fedha za kutosha zaidi.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kumhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali ilitoa maelekezo, na hakuna halmashauri inayotakiwa kwenda kinyume na maelekezo haya. Nitoe wito kwamba halmashauri zote ni lazima zihakikishe kwamba akaunti za marejesho zinafanya kazi, na fedha zile zikirejeshwa ziendelee kukopesha wajasiriamali wengine.
Mheshimiwa Spika, ahsante sana.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri, swali langu la kwanza, je, nini kauli ya Serikali kuhusiana na wale wastaafu ambao wanapigwa danadana wakati wakifuatilia mafao yao ambayo ni difference au utofauti ya kile kipindi ambacho makato yamepelekwa kwenye mifuko na kile kipindi ambacho hayajapelekwa kwenye mifuko na madai ni kwamba Maafisa Masuuli wamehama au hawakupata uteuzi?
Swali la pili, ningependa kujua kama Serikali itakuwa tayari sasa kuwataka waajiri au kuwahimiza watekeleze masharti ya mifuko haraka iwezekanavyo ili wale wastaafu waweze kulipwa haki zao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwa kipindi cha nyuma kulikuwa na changamoto ya wazee wetu waliotumikia Taifa kwa nguvu zao lakini pia kwa uadilifu na utumishi uliotukuka, walikuwa wakipata usumbufu katika kupata mafao yao aidha kwa kuambiwa kuleta barua na changamoto nyingine nyingi ambazo zilikuwepo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Profesa Joyce Ndalichako pamoja na mimi na wasaidizi wengine kulikuwa na mpango kabambe wa kuweza kupita katika mikoa yote, kukutana na wastaafu na kutatua changamoto hizo na zoezi hili lilifanikiwa na kwa hatua ya sasa tayari tumekwisha kuanza kutatua changamoto hizo na kama kuna specific case ambayo bado haijafanyiwa kazi, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aweze kutufikishia ili tuchukue hatua haraka sana iwezekanavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la pili pia kwamba kutokana na waajiri sasa kutokutekeleza wajibu; ni tamko la Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba waajiri wote nchini wanao wajibu wa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini lakini sambamba na hilo Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii yaani National Social Security Fund Act ambayo inamtaka mwajiri kuwasilisha michango ya mwajiriwa wake bila usumbufu wowote na wajibu huu upo kwa mwajiri kwa mujibu wa sheria na kama atakiuka, kama jinsi ambavyo tumefanya kwa hawa 123 kuwapeleka mahakamani.
Mheshimiwa Spika, sambamba na hilo hata mahakama kwa mujibu wa Bunge lako tukufu lilitunga sheria ambayo mwajiri ambaye atakuwa amekiuka kupeleka michango ya mwajiriwa wake akienda mahakamani anatumia procedure ya summary suit, kwa hiyo hana hata wajibu wa kuweza kujitetea na hatua tunachukua.
Kw ahiyo, niwaombe na kuwataka waajiri wote nchini kutimiza takwa hilo la kisheria ili tusije tukafikishana mahakamani na kuchukuliwa hatua kali zinavyostahili kwa mujibu wa sheria, ahsante.
SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri, malalamiko haya ni mengi, hebu tusaidie, ni kazi ya nani kuhakikisha mwajiri anapeleka makato anayoyatoa kwenye mshahara wa mfanyakazi na ile anayotakiwa kulipa yeye kuhakikisha inaifikia Mifuko ya HIfadhi ya Jamii; ni kazi ya nani?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante kwa swali zuri; kwa mujibu wa sheria ambayo ilipitishwa na Bunge lako tukufu Sheria ya National Social Security Fund inasema wajibu ni wa mwajiri kufikisha, lakini sambamba na hilo ni wajibu wa mfuko pia kuweza kufanya ufuatiliaji wa michango hiyo kuhakikisha inafikishwa. Kwa hiyo ni pande zote mbili; mwajiri anao huo wajibu kwa mujibu wa sheria lakini mchango wanao ma-compliance officer kwa mujibu wa sehria katika utekelezaji nao NSSF au PSSF au mifuko hii ya hifadhi inapaswa kuendelea kumkumbusha mwajiri na kumpa notice. Na kwa sasa tayari kumekwishachukuliwa utaratibu wa kufungua akaunti ya kimtandao ya moja kwa moja, kila mwanachama sasa anapewa taarifa yake kupitia simu ya kiganjani. Kwa hiyo, kama michango haiendi kwa sasa tunawakamata.
Mheshimiwa Spika, kwa hili kwa kweli tunaendelea na operation kali kuweza kufanya ukaguzi ili kuweza kuhakikisha takwa hili la kisheria linatimia na wastaafu wetu wasisumbuliwe. Ahsante.
SPIKA: Nawaona Waheshimiwa nataka kwenda nalo vizuri, kwa sababu Ofisi za Wabunge zina malalamiko mengi sana ya wastaafu wa nchi hii na tukisema kwamba tutaliacha liendelee mtu anafuatilia mafao miaka miwili anaambiwa michango yako haikuja, kama ni kazi ya mwajiri kupeleka na mfuko unajua mwajiri hajapeleka, ni kazi yao, mfuko umlipe huyu mafao yake wao wakatafute fedha zilipo kwa sababu sio kazi yangu mimi kama mwajiriwa kuanza kusema fedha kama zilikuja ama hazikuja sio kazi yangu halafu huyu mwajiri mimi naweza kumuadhibu asipopeleka? Siwezi. Kwa hiyo, ni kazi ya mifuko kufuatilia fedha ambazo hazijalipwa na ndio maana sheria imeweka isipolipwa kuna riba inayotakiwa kulipwa.
Kwa hiyo, sidhani kama wananchi wanatakiwa kuteseka baada ya kuwa wamelipa kwenye mifuko na mwajiri ameshakata fedha. Ninyi Serikali mtengeneze utaratibu mzuri wa kuisimamia mifuko izitafute hizo fedha iwalipe wastaafu, wasataafu wasiwe wanaseka. (Makofi)
Waziri nakuona umesimama, nadhani tutapata tamko zuri hapo ili wastaafu wetu wawe na utulivu. Ahsante sana karibu Mheshimiwa Waziri wa Nchi.
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwanza nimshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri kuhusiana na hatua ambazo Serikali inafanya kuhakikisha kwamba wastaafu ambao wamelitumikia Taifa letu kwa uadilifu mkubwa hawapati usumbufu wa kupata mafao.
Mheshimiwa Spika, ni kweli kumekuwa na changamoto ya baadhi ya waajiri kutopeleka michango yao katika mifuko na hivyo kusababisha wasataafu ambao michango haikupelekwa ama kutopata mafao yao kwa wakati au kupata mafao ambayo yana mapunjo.
Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba Serikali imeliona suala hili na tunalifanyia kazi ili kuweza kupata ufumbuzi kwa wale waajiri ambao madeni yao yameshakuwa ya muda mrefu yako ambayo yanafika miaka kumi, bado hajaleta hizo fedha. Kwa hiyo, nilihakikishie Bunge lako kwamba tayari Serikali inafanyia kazi, na niahidi kwamba ndani ya miezi miwili mitatu, tutakuja na muafaka wa kutatua tatizo hili ambalo limekuwa la muda mrefu.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kuniona. Je, ni lini Serikali italeta mashine ya ultra sound kwa ajili ya wanawake wajawazito katika Hospitali ya Rufaa ya Ligula? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mtwara, maarufu kwa jina la Ligula, iko chini ya Wizara ya Afya nasi kama Serikali tunachukua hoja hiyo kuona uwezekano wa kupeleka mashine ya ultra sound mapema iwezekanavyo. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali madogo mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, hii dust suppression system inapunguza vumbi kwa kiasu kidogo sana, lakini pia ukienda bandarini pale utakuta maji yameshakuwa meusi kutokana na hili vumbi. Swali langu la kwanza: Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inatunza au inalinda vyanzo vya maji ili kusudi visiweze kuathirika kutokana na yale maji ya mvua yanayotiririka ambayo tayari yameshakuwa na vumbi? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali langu la pili: Je, Serikali itakuwa tayari kupokea ushauri kwamba haya makaa ya mawe kutoka kwenye migodi yawe yakisafirishwa yakiwa yamefungwa kwenye vifungashio, kwa mfano, labda viroba au maboksi ili kusudi kuzuia lile vumbi lisitimke wakati wa usafirishaji, wakati wa kushusha mzigo na vile vile wakati wa kupakia mzigo katika meli? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Spika, naomba swali la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Mkoa wa Mtwara, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Sheria ya Usimamizi na Utunzaji wa Vyanzo vya Maji imewaelekeza watu wote, makampuni, taasisi zote zinazofanya shughuli zote ambazo zitakuwa zinagusia sehemu zenye maji au vyanzo vya maji; tumeshawaelekeza pamoja na hawa wa Mtwara wanaofanya biashara hiyo. Kwanza tumewaelekeza kwa kuwapa taaluma, lengo na madhumuni, watunze vyanzo vya maji. Pia tumekuwa tunasimamia sheria kwa kushirikiana na wenzetu wa NEMC, watu wa Halmashauri na wengine. Lengo na madhumuni ni watu watunze vyanzo vya maji.
Mheshimiwa Spika, pia tumeshakaa nao kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunachukua hatua mbalimbali, na tayari zipo hatua ambazo NEMC wamezichukua kwa baadhi ya watu hawa. Hapa nataka nitoe wito kwa Watanzania wote wanaofanya shughuli za kibinadamu karibu na vyanzo vya maji, wahakikishe kwamba wanatunza vyanzo vya maji. Kinyume na hapo, sheria na taratibu zitakuwa zinachukuliwa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, suala la pili, tupo tayari, tumepokea huo ushauri. Ingawa makaa ya mawe haya yanakuwa ni mawe makubwa, lakini tutajua namna ya kuwashauri wafanyabiashara wawe wanaweka katika package maalum ili yaweze kupunguza hilo vumbi ambalo linaweza kuathiri afya za wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na tatizo la wakulima kugaiwa kiasi kidogo sana cha viuatilifu ukilinganisha na kile kiasi ambacho kimefika katika maeneo husika.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba wakulima wanapata kile kiasi ambacho wanastahili?
Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, hivi tunavyoongea sasa hivi tumeiagiza Bodi yetu ya Korosho, lakini vilevile kwa ajili ya kuweza kupata the light data base ya wakulima na ukubwa wa mashamba yao, tunashirikiana na Halmashauri za Wilaya na Serikali za Mkoa kupitia vyama vyao vya ushirika. Cha kwanza, tunachukua takwimu za uuzaji kupitia vyama vya ushirika ili kumjua mkulima na idadi ya uzalishaji wake.
Mheshimiwa Spika, cha pili, kuanzia msimu wa mwaka 2022/2023 Serikali itatenga fedha kwenye bajeti yetu ya kuzipatia Sekretarieti za Mikoa pamoja na Vyama Vikuu vya Ushirika ili zoezi la usajili wa mashamba ya wakulima na utambuzi wa wakulima liweze kufanyika vizuri ili kujua mahitaji halisi ya pembejeo ambazo wakulima wataigawa.
Kwa hiyo, kuna uwezekano kukaendelea kuwepo kwa changamoto kwa muda, lakini ni jambo ambalo tunalolifanyia kazi. Naamini kwamba ndani ya kipindi cha mwaka mmoja au miwili zoezi la usajili wa utambuzi wa wakulima litakuwa limekamilika na tutaondokana na hili tatizo.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza. Kwanza nishukuru sana majibu ya Mheshimiwa Waziri, na nimpongeze, huwa anatembelea sana Mkoa wa Mtwara.
Mheshimiwa Spika, ninakiri hizo fedha milioni 250 kwa ajili ya Kituo cha Afya cha Mkunwa, zimefika na zinaendelea kufanya kazi.
Mheshimiwa Spika, nimpe taarifa Mheshimiwa Waziri kwamba wananchi wa Mangopacha Nne, tayari walishaandaa eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya muda mrefu tu, zaidi ya miaka mitano. Kwa hiyo, niombe sasa Serikali itoe kipaumbele fedha zitakapopatikana.
Mheshimiwa Spika, hii Kata ya Mangopacha Nne ni moja ya kata katika Tarafa ya Dihimba, ambapo tarafa hii haina hata kituo kimoja cha afya lakini kuna zahanati katika baadhi ya vijiji. Kuna tatizo kubwa sana la wanawake…
SPIKA: Swali lako Mheshimiwa.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nauliza swali, katika kutatua tatizo la wanawake kujifungua hasa nyakati za usiku. Je, Serikali itakuwa tayari kuboresha huduma katika hizi zahanati ili kusudi akina mama waweze kupata huduma bora?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia James Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ninatambua kwamba anafanya kazi nzuri kwa Mkoa wa Mtwara na ndiyo maana amekuwa akitetea sana katika huduma za afya, hususan wanawake katika mkoa wake. Nimhakikishie tu kwamba Serikali ipo tayari kuboresha huduma katika tarafa hiyo, na tutalifanyia kazi, ahsante sana.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ninapenda kujua sasa ni lini Serikali itaanza kuimarisha miundombinu ya shule hizo 56 lakini niombe na miundombinu ya Shule ya Mkalapa pia iboreshwe?
Swali la pili, ninapenda pia nijue Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba shule zote zinapata walimu wa michezo ili kusudi vijana wetu waweze kushiriki katika michezo kikamilifu? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, Serikali itaboresha miundombinu ya shule hizi 56 ikiwemo kama nilivyosema tathmini inafanyika katika Shule ya Sekondari Mkalapa ambayo imefanya vizuri sana katika michezo ya UMISETA lakini vile vile michezo ya Afrika Mashariki. Kwa hiyo Serikali inafanya tathmini na itaijumlisha na yenyewe Shule ya Mkalapa na tutatafuta fedha na kwenda kujenga miundombinu kwa awamu.
Mheshimiwa Spika, nikienda kwenye swali lake la pili la walimu wa michezo. Katika ajira ambazo Serikali imetangaza hizi 21,000 ambapo 13,390 hizi ni ajira za walimu. Tutaangalia ni namna gani nayo tuna-accommodate walimu wa michezo, walimu wa kilimo, walimu wa ufundi ili kuweza kuboresha elimu yetu hapa nchini.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante, je, ni lini sasa Serikali itaanzisha revolving fund ikiwa na maana kwamba zile fedha zinazokusanywa ziwekwe kwenye mfuko ambao ni fedha lindwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Wambura amezungumzia swala la revolving fund kama nilivyoeleza kwenye swali la nyongeza la Mheshimiwa Tweve nadhani kwamba hivi sasa tunafanya mapitio ya sheria ile. Katika mapitio yale tutakwenda kuangalia hayo mambo yote pamoja na kuangalia kama mfuko unaweza kujiendesha lakini vilevile katika kujiendesha katika taratibu za kibenki ikiwemo na hii revolving fund. Kwa hiyo, nimuondoe wasi wasi jambo hili linafanyiwa kazi.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi; moja ya changamoto ambayo inayopelekea kuchelewa kuwapa vitambulisho vya NIDA wananchi wa Mkoa wa Mtwara ni pamoja na uhaba wa watumishi; je, Serikali imejipanga vipi kuondoa changamoto hii? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia Wambura kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema kwenye majibu ya maswali yaliyopita, kwa kweli changamoto sio idadi ya watumishi changamoto ilikuwa ni kukosa vitendea kazi vilivyokuwa vimesababishwa na kukwama kwa mkataba, sasa baada ya suala la mkataba tumeshalitatua bila shaka ataona kasi ya utoaji wa vitambulisho kule Mtwara inatatuliwa, lakini pale itakapoonekana kwamba shida ni watumishi Serikali itaendelea kuajiri watumishi wanaohitajika ili kutekeleza majukumu yako ya utoaji wa vitambulisho itasavyo.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Kwanza nishukuru majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri ambayo yanaonesha hali halisi.
Mheshimiwa Spika, Halmashauri 24 kati ya 184 ni chache sana na ni dhahiri kwamba kasi ni ndogo sana ya utekelezaji wa kifungu hiki cha sheria. Je, Serikali sasa imejipanga vipi kuhakikisha kwamba inaondoa vikwazo vyote ambavyo vinazuia utekelezaji mzuri wa sheria hii?
Mheshimiwa Spika, swali la pili; suala la elimu ni muhimu sana katika kuhakikisha kwamba sheria hii inatekelezwa vizuri, lakini elimu hii inaonekana haijawafikia walengwa.
Je, Serikali ina mpango gani sasa wa kuhakikisha kwamba inatoa elimu kwa wale maafisa wanaohusika na manunuzi ya umma, lakini vilevile wale walengwa wa makundi maalum lakini hata zile taasisi ambazo zinahusika...
SPIKA: Mheshimiwa Anastazia Wambura umeshauliza mawili au hilo la mwisho lile lina vipengele?
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, sijauliza mimi natoa tu, ni swali la pili hili, la kwanza nimeuliza.
SPIKA: La kwanza nimekusikia.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ndiyo.
SPIKA: Ndiyo hilo la pili naona kama lina vipengele hivi?
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, hapana ni kwamba elimu itolewe kwa yale makundi yanayohusika na utekelezaji wa hii sheria na makundi yenyewe ni yale makundi maalum, lakini pia wale maafisa wanaohusika na manunuzi, lakini pia taasisi zinazosimamia yale makundi maalum. Ndiyo nataka sheria hii itolewe elimu yake kwa makundi haya matatu, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia Wambura, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kasi ya vikundi hivi kunufaika na mpango huu wa asilimia 30 bado ni ndogo. Halmashauri 24 kati ya 184 bado kasi ni ndogo na ndiyo maana Serikali imeweka utaratibu wa kuonesha kwamba tunahamasisha vikundi kuhakikisha wananufaika na asilimia 30 kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhamasisha vikundi hivyo, lakini pia kuto elimu ili waweze kujisajili PPRA.
Mheshimiwa Spika, nani kuhusiana na mpango huo tutaendelea kuhakikisha kwamba tunawaelekeza Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa zote kote nchini kuhakikisha kigezo hicho kinazingatiwa kwenye bajeti. Kwanza kutenga asilimia 30 ya fedha zote za ununuzi pili kuhamasisha vikundi vyenye sifa hiyo na kuviwezesha kusajiliwa PPRA. Ahsante. (Makofi)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Mkoa wa Mtwara una zahanati sita ambazo hazijaanza kutoa huduma kutokana na kutokupata mgao wa watumishi katika ajira mpya: Je, ni lini Serikali itapeleka watumishi ili kusudi zahanati hizi ziweze kuanza kufanya kazi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, tulishatoa maelekezo kwa Wakurugenzi na Makatibu Tawala wa Mikoa kwamba pale zahanati zinapokamilika, hatuna sababu ya kuziacha zisianze kutoa huduma za awali. Natumia fursa hii kwanza kumkumbusha Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo na Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara kwamba watumie utaratibu wa kuwa-reallocate watumishi ndani ya halmashauri ili angalau huduma za OPD zianze kwenye zahanati hizi.
Mheshimiwa Spika, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tutatoa kipaumbele kwenye ajira zinazofuata ili watumishi wafike katika zahanati hizi. Ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, wakati wa Bunge la Bajeti, Serikali iliahidi kupeleka turbine ya megawati 20 kule Mtwara kama hatua za dharura za kupunguza tatizo la upungufu wa umeme ambalo linasababisha kukatikakatika kwa umeme; je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Anastazia Wambura kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, ni kweli tuliaahidi kupeleka hii taibai kutoka Ubungo kwenda Mtwara. Baada ya tathmini ya kina tulijirididha mtambo huu hautafanya kazi vizuri pale Mtwara. Tumeshaongea na Kampuni ya CSI juu ya kuzalisha umeme hapo na tumeshakamilisha, na tuna kituo cha kupoza umeme tunakijenga hiyari ambacho tunategemea kitakamilika ndani ya mwezi huu. Kikikamilika basi, umeme ambao utatolewa na Kampuni ya CSI utaweza kwenda kwenye Mkoa mzima wa Mtwara na Lindi na hivyo tutakuwa tumeondoa kabisa changamoto ya umeme kwa Mikoa miwili.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tunawaomba Waheshimiwa Wabunge na wananchi wa Mtwara na Lindi watuvumilie kidogo mpaka mwishoni mwa mwezi huu tutakuwa tumekamilisha na kuwapatia umeme wa uhakika, ahsante.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika kufuatilia kwangu hali ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, nimekuta kwamba Mradi huu wa Makonde ulikuwa ukamilike mwaka 2024, lakini mkandarasi ameongezewa muda na ni kutokana na hali ya ucheleweshaji wa malipo.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba sasa mradi huu unatekelezwa na unakamilika Disemba, 2025 kama alivyosema Mheshimiwa Naibu Waziri? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ningependa nifahamu kwamba je, Serikali imeweka utaratibu gani kuhakikisha kwamba miradi mingine ikiwa ni pamoja na ule wa Mto Ruvuma yote inakamilika kwa wakati? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Anastazia, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuendelea kufuatilia kwa ukaribu sana utekelezaji wa miradi hii kwa faida ya wananchi wa eneo lake. Ni kweli kabisa mradi huu unaenda kukamilika Disemba, 2025 na Mheshimiwa Mbunge amegusia namna ambavyo ulitakiwa kukamilika mwaka 2024.
Mheshimiwa Naibu Spika, mradi huu nature yake ni design and build. Maana yake kwamba tunakuwa tunafanya design na ndiyo tunaendelea kujenga, kwa hiyo, muda ambao ulikuwa umetolewa wa kwanza wa kufanya feasibility study na kuja kufanyia mapitio ulisababisha tufanye extension ambapo mradi huu tunauhakika utaenda kukamilika mwaka 2025...
Kwa upande wa swali la pili ni kwamba miradi yote nchini tumeweka mkakati wa kuhakikisha kwamba fedha zinapelekwa katika miradi mbalimbali ili iweze kukamilika kwa wakati, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Spika, namshukuru Naibu Waziri kwa majibu yake mazuri. Mkoa wa Mtwara una upungufu wa walimu wa shule za sekondari zaidi ya 11,300 ikiwa ni pamoja na walimu 205 ambao walihama, lakini nafasi zao bado hazijajazwa. Je, Serikali itajaza lini nafasi za walimu hawa ambao walihama kwa muda mrefu? (Makofi)
Mheshimiwa Spika, swali la pili. Ukiangalia idadi ya walimu wa shule za msingi na sekondari ambao tutaletewa bado haitatosha ukizingatia upungufu ambao upo na kikubwa ambacho sisi tunahitaji ni kwamba, pale walimu wanapokuwa wamehama, basi angalau Serikali ijitahidi kujaza zile nafasi kwa wakati. Swali langu ni kwamba, je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kwamba inakuwa ikijaza nafasi hizi za walimu wanaohama kwa wakati? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, kwanza nampongeza Mheshimiwa Mbunge kwa maswali mazuri sana. Kuhusu swali lake la kwanza, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kama nilivyojibu kwenye swali la msingi, katika ajira mpya zilizotangazwa za walimu Mkoa wa Mtwara atapata walimu 502.
Mheshimiwa Spika, kuhusu swali lake la pili, Ofisi ya Rais, TAMISEMI tayari ilishatoa mwongozo wa utaratibu wa uhamisho wa walimu kwamba, uhamisho wa walimu unafanywa kwa kuzingatia kubadilishana, kwa hiyo, sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutaendelea kusimamia utaratibu huo ili kuondoa upungufu wa walimu kwenye eneo moja kutokana na uhamisho.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tutazingatia ili wale walimu wanapohama kwenye kituo kimoja, basi apatikane mwalimu mwingine wa kuja kuziba ile nafasi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge tumezingatia sana ombi na mwongozo wako na sisi kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI, tutazingatia utaratibu huo.
MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, wataalamu ambao wamehitimu degree ya lishe katika nchi yetu ni wengi na wapo mitaani. Je, Mheshimiwa Waziri atakubali sasa kwamba wawaajiri wale ambao wamemaliza waliohitimu degree ya lishe? Ahsante.
WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Anastazia Wambura kwa swali lake zuri kuhusu wataalamu. Kama nilivyosema ni kweli tunao wataalamu katika ngazi ya degree ambapo tumejitahidi katika halmashauri nyingi sasa hivi angalau tuna Afisa Lishe, lakini tumeona ili tufanye vizuri zaidi tunahitaji Maafisa Lishe katika ngazi ya chini na tunaamini tukiwapata pia wa ngazi ya diploma wataweza pia kufika rahisi zaidi kwa jamii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nataka kukuhaidi katika nafasi za ajira tutaongeza ajira kwa maafisa lishe lakini nitawaomba sana basi wasitake kubaki mjini wawe tayari kufanya kazi katika halmashauri zote ikiwemo halmashauri za pembezoni ambazo ndizo zina changamoto kubwa ya lishe. (Makofi)