Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe (23 total)

MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, iliagiza Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kuanzisha maduka ya dawa kwenye hospitali kubwa nchini.
(a) Je, ni lini Serikali itaagiza MSD kufungua duka la dawa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida ili kuwasaidia wananchi kununua dawa kwa bei nafuu tofauti na zile zinazouzwa kwenye maduka ya mitaani?
(b) Je, lini Serikali itasambaza vifaa tiba vya kutosha kama vitanda vya wajawazito katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa na Hospitali za Wilaya za Mkoa wa Singida?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba katika hospitali zetu, Serikali iliangiza maduka ya dawa yafunguliwe kwenye Hospitali za Kanda na Taifa nchini. Aidha, ikumbukwe kwamba siyo jukumu la Bohari ya Dawa kuuza dawa kwa rejareja moja kwa moja kwa wateja, kuruhusu hili litokee ni kujaribu kunyakuwa fursa ya hospitali husika kupata mapato kwa kuuza dawa kwa wateja hivyo kuzichelewesha kuanza kujitegemea. Ili kutekeleza agizo hilo kwa Tanzania nzima ilionekana itahitajika rasilimali watu na fedha nyingi sana ambapo Bohari ya Dawa peke yake isingeweza kumudu. Kwa hiyo basi, Bohari ya Dawa ilikubaliana na TAMISEMI kuwa hospitali zilizo chini yake basi zifungue maduka yao wenyewe na MSD itakuwa tayari kutoa ushauri wa kitaalam pamoja na kuziuzia dawa na vifaa tiba.
(b) Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Rufaa ya Singida inashauriwa kutenga fedha kwenye mgao unaoletwa na Wizara kila robo mwaka pamoja na makusanyo kutoka vyanzo vingine kama Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ili iweze kununua vifaa, vitendea kazi pamoja na vitanda vya wajawazito.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Mkoa wa Singida ni miongoni mwa mikoa yenye ukame hapa nchini; ukame huo unasababisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa maeneo mengi Mkoani Singida:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Singida inapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kuwasaidia wananchi hususan wanawake kushiriki kwenye shughuli nyingine za uzalishaji mali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Singida, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa iliyo chini ya wastani wa kitaifa wa utoaji huduma ya maji. Hadi kufikia mwezi Juni, 2016 wananchi waliokuwa wanapata huduma ya maji katika mkoa huo ni asilimia 51.2 kwa maeneo ya vijijini na asilimia 71.3 kwa maeneo ya mijini. Katika Mkoa huo hakuna mito inayotiririsha maji kwa mwaka mzima. Vyanzo vingine vya maji juu ya ardhi kama maziwa na mabwawa ya asili maji yake yana chumvi nyingi isiyofaa kwa matumizi ya binadamu. Kwa msingi huo, vyanzo vinavyotegemewa kwa huduma ya maji safi ni maji ya ardhini kupitia visima virefu na visima vifupi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuhakikisha changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa Mkoa wa Singida inapatiwa ufumbuzi, Serikali imekamilisha kujenga mradi wa maji safi katika Manispaa ya Singida ambapo kwa sasa huduma ya upatikanaji wa maji safi na salama imeongezeka. Aidha, mkakati wa Serikali ni kuendelea kupanua mtandao wa maji na kufunga pampu katika visima vya ziada ambavyo vilichimbwa kwenye mradi huo uliokamilika.
Vilevile kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji katika Mji wa Manyoni na Kiomboi ambapo hadi sasa zabuni za ujenzi zimetangazwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa maji vijijini, Serikali inatekeleza miradi ya maji katika vijiji 66. Kati ya hivyo, vijiji 47 vimekamilika na vijiji vingine vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji kwa Mkoa wa Singida.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka wa fedha wa 2016/2017, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 6,750 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji katika Halmashauri zote za Mkoa wa Singida zikiwemo Halmashauri za Manyoni na Singida Vijijini. Aidha, katika juhudi za kukabiliana na hali ya ukame, Wizara imetoa agizo katika Ofisi ya Mkoa kuhakikisha kila Halmashauri inaainisha maeneo yanayofaa kwa ujenzi wa mabwawa madogo na kutenga fedha katika bajeti zao za ndani kwa ajili ya ujenzi wa mabwawa hayo.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Alizeti ndiyo zao kubwa la biashara na limekuwa kimbilio kubwa kwa maisha ya wananchi wa Mkoa wa Singida. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Singida ilipatiwa mashine ndogo tisa za kukamulia alizeti ambazo hazikidhi matarajio ya wakulima katika kujikwamua kiuchumi na alizeti inayozalishwa mkoani humo ambayo ni bora Afrika ya Mashariki na Kati haijapatiwa soko la uhakika kwa maana ya kuwa na viwanda vya kutosha ili wakulima waweze kuuza zao hilo kwa urahisi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuanzisha viwanda vya kisasa vya kukamulia mafuta ya alizeti Mkoani Singida?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Mkakati wa Fungamanisho la Maendeleo ya Viwanda la mpaka mwaka 2025, mkakati uliozinduliwa Desemba, 2011 na Mkakati Maalum wa Kuendeleza Sekta ya Alizeti, 2016 mpaka 2020 uliozinduliwa mwaka 2016, tunaendelea na uhamasishaji wa zao la alizeti nchini. Moja ya mpango wa kuendeleza sekta hii ni kuhamasisha uongezaji wa thamani hapa nchini kwa kutumia viwanda vya aina zote. Kwa Mkoa wa Singida, mpaka Desemba, 2016 tulikuwa na viwanda vidogo 126, viwanda vya kati viwili na kiwanda kimoja kikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jitihada nyingine za Serikali ni kuuweka Mkoa wa Singida katika kundi la mikoa inayonufaika na Mfuko wa SME Credit Guarantee Scheme unaoendeshwa kwa ubia kati ya SIDO na Benki ya CRDB. Pia ubunifu wa Shirika la TEMDO wa kuchonga vipuri vya mashine za kukamua alizeti na business-re-engineering ya mashine za alizeti unalenga kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya viwanda vya alizeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue fursa hii ya swali hili kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya kukamua na kuchuja alizeti. Kiwanda kidogo sana kinakadiriwa kuwa na gharama kati ya shilingi milioni 10 mpaka shilingi milioni 15; kiwanda kidogo kati ya shilingi milioni 16 mpaka 200 ambacho kina uwezo wa kukamua na kuchuja kwa kiwango kidogo. Kiwanda cha kati kinachoweza kukamua na kuchuja mara mbili (double refinery) kinagharimu kati ya shilingi milioni 200 mpaka milioni 500.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:- Wakati akiwa kwenye Kampeni ya Uchaguzi wa Mwaka 2010 Wilayani Singida Vijijini, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa. Dkt. Jakaya Kikwete aliahidi kuwa Serikali itajenga kwa kiwango cha lami barabara ya Njuki –Ilongero – Hydom lakini ni miaka saba imepita bila utekelezaji wa ahadi hiyo; na Mji wa Ilongero ambao ni Makao Makuu ya Wilaya ya Singida Vijijini unakua kwa kasi sana na suala la ujenzi na uboreshaji wa miundombinu yake ni suala la msingi sana kwa sasa:-
Je, ni lini Serikali itatekeleza ahadi hiyo iliyotolewa kwa wananchi wa Singida Vijijini ambao wanatarajia barabara hiyo kuwa mkombozi mkubwa wa maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe ,Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara ya Singida kutoka Njuki kuelekea Ilongero hadi Haydom yenye urefu wa kilometa 96.4 ni barabara ya Mkoa inayohudumiwa na Wizara yangu kupitia TANROADS. Barabara hii inaunganisha Mkoa wa Singida na Mkoa wa Manyara. Serikali inaendelea kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais ya ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2013/2014, Sh.2,851,585,000 zilitumika kujenga kwa kiwango cha lami, jumla ya kilometa 5.6 kuanzia Singida Mjini kuelekea Ilongero. Aidha, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Sh.1,297.377 zimetumika kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami wa jumla ya kilomita 2.1.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hii ili iweze kupitika katika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali imetenga fedha kwa ajili yakuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya Njuki – Ilongero hadi Ngamu tumetenga shilingi milioni 2,043.53 na hizo utazikuta katika ukurasa wa kitabu cha bajeti wa 326 na 345, 365 na 376 Kitabu cha Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Sehemu ya Ilongero kupitia Mtinko hadi Nduguti, shilingi milioni 169.76 zimetengwa, rejea ukurasa wa 345 na 376 wa kitabu cha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Mwaka 2007 Serikali ilianzisha rasmi Benki ya Wanawake Tanzania (TWB) kwa lengo la kuwawezesha wanawake wajasiriamali kupata huduma za kibenki ikiwemo mikopo yenye riba nafuu, lakini mpaka sasa benki hiyo ina matawi manne tu, mawili yakiwa Dar es Salaam na mengine Mikoa ya Mwanza na Dodoma wakati wanawake wenye uhitaji wa huduma hiyo wako nchi nzima.
Je, Serikali, ambayo inamiliki TWB kwa zaidi ya asilimia 90 inakwama wapi kuiwezesha benki hii ili kufungua matawi kote nchini ili wanawake waweze kunufaika na huduma hizo na hatimaye kujikwamua kiuchumi?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Benki ya Wanawake Tanzania ilianzishwa mwaka 2009. Tangu kuanzishwa kwake benki imefanikiwa kuwa na matawi mawili katika Mkoa wa Dar es Salaam na mpango wa Serikali ni kuhakikisha kuwa huduma za Benki ya Wanawake Tanzania zinawafikia wanawake waliopo katika mikoa yote hapa nchini. Utekelezaji wa mpango huo unakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa mtaji wa benki. Hivyo, katika kuhakikisha azma hii inafanikiwa, benki imekuwa ikipanua huduma zake katika Mikoa mbalimbali ya Tanzania kwa awamu kwa kufungua vituo vya kutolea mafunzo na mikopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, hadi sasa benki imeanzisha jumla ya vituo 252 katika Mikoa saba ya Dar es Salaam, Mbeya, Njombe, Iringa, Mwanza, Ruvuma na Dodoma. Kwa mwaka 2017/2018, benki inatarajia kufungua vituo vipya vya kutolea mafunzo na mikopo katika Mikoa ya Singida, Arusha na Zanzibar. Aidha, katika kipindi husika, kituo cha Dodoma kitaboreshwa na kupandishwa hadhi na kuwa tawi.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali itaendelea na jitihada za kuhakikisha kuwa mtaji wa benki hii unaimarika ili huduma za Benki ya Wanawake Tanzania ziweze kupatikana katika mikoa yote ya Tanzania. Jitihada hizo ni pamoja na:-
Kuimarisha mfumo wa ukusanyaji wa madeni kutoka kwa wakopaji; kuongeza amana kutoka kwa wateja na wawekezaji binafsi; kuimarisha ubia wa kimkakati na wadau, mfano African Development Bank pamoja na kuendelea kuajiri wafanyakazi wenye weledi na walio waadilifu.
MHE. MUSSA R. SIMA (K.n.y. MHE. AISHAROSE N. MATEMBE) aliuliza:-
Watumishi wa sekta ya afya hususani madaktari wanatakiwa kuishi kwenye maeneo ya kazi ili inapotokea akahitajika inakuwa rahisi kuwahi kwenda kutoa huduma kwa wagonjwa. Hata hivyo, katika Mkoa wa Singida watumishi wengi wa sekta ya afya wanaishi mbali na eneo la kazi hivyo kuwa na changamoto kubwa na wakati mwingine kusababisha vifo vya wagonjwa wakiwemo wajawazito.
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuhakikisha watumishi wa sekta ya afya wanakuwa na makazi kwenye maeneo jirani ikiwa ni pamoja na kuboresha nyumba chache zilizopo pamoja na kujenga zingine mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Singida una jumla ya nyumba za watumishi wa sekta ya afya 345 kati ya nyumba 1,072 zinazohitajika. Hivyo, kuna upungufu wa nyumba za watumishi wa afya 737. Serikali inaendelea na ujenzi wa nyumba za watumishi 21 katika vituo vya afya na zahanati. Aidha, shilingi milioni 280.8 zimetengwa katika mwaka 2017/2018 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa nyumba za watumishi wa afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeanza kutoa ruzuku ya maendeleo (Local Government Development Grant) ambayo inatumika kumalizia maboma yaliyoanza kwa nguvu za wananchi katika sekta za afya, elimu na sekta nyingine. Kipaumbele cha matumizi ya fedha hizo kinapangwa na Halmashauri zenyewe kupitia Mpango wa Fursa na Vikwazo kwa Maendeleo (O&OD).
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:-
Vijana wengi wa Mkoa wa Singida wamejikita katika shughuli za ujasiriamali ili kuondokana na umaskini, lakini wanakosa mbinu za kitaalam za kuwawezesha kupiga hatua kubwa kimaendeleo kupitia kazi wanazofanya.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia mbinu endelevu, zana za kisasa pamoja na mitaji ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA NA WATU WENYE ULEMAVU alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuwapatia vijana wa Singida mbinu endelevu na zana za kisasa pamoja na mitaji ya kufanyia kazi kwa ufanisi, Serikali inaendelea kutekeleza Programu ya Kitaifa ya Kukuza Ujuzi Nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujasiriamali. Hadi kufikia mwezi Oktoba jumla ya vijana 11,340 wamepatiwa mafunzo ya ujuzi wa fani mbalimbali na wengine wanaendelea na mafunzo ya kujenga ujuzi kutoka katika mikoayote nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano dhahiri wa mafunzo ya kukuza ujuzi ni pamoja na utumiaji wa teknolojia ya kitalu nyumba (green house) ili kuwawezesha vijana wetu kufanya kilimo kwa kutumia teknolojia za kisasa na kuongeza tija ya kazi zao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa wito kwa mikoa yote kushiriki katika program hii, mikoa ilielekezwa kutenga eneo la kujenga green house ya kufundishia; kutenga maeneo ya kilimo kwa vijana pamoja na kuweka miundombinu muhimu na upatikanaji wa maji; kuandaa vijana wenye nia ya kujifunza kilimo kwa kutumia teknolojia ya green house.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo yote Wizara yangu imeendelea kusimamia Mifuko ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ili kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa vijana wote wa Tanzania.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2015/2016 wanawake 85 Mkoani Singida walipoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi. Aidha, inaelezwa kitaalam asilimia 35 ya vifo hivyo vinaweza kuzuiliwa iwapo huduma za uzazi wa mpango zitazingatiwa na kuimarishwa.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuimarisha elimu na huduma za afya ya uzazi wa mpango kwani utumiaji wa huduma hizo kwa sasa unatekelezwa kwa asilimia 19 wakati wastani wa kitaifa ni asilimia 27?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu rasmi za sensa mwaka 2012 zinaonesha vifo vitokanavyo na uzazi katika Mkoa wa Singida ni 468 kwa kila wanawake 100,000. Kwa mujibu wa utafiti wa viashiria vya afya na Malaria Tanzania za mwaka 2015/2016 (Tanzania Demographic Health Surveys 2015/2016) matumizi ya uzazi wa mpango katika Mkoa wa Singida yalikuwa asilimia 38.4 wakati wastani wa Kitaifa ni asilimia 32.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ya afya katika Mkoa wa Singida wameweza kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma 77 katika kipindi cha mwaka 2015 na idadi watoa huduma ilikuwa 121 kwa mwaka 2016 ili waweze kutoa huduma sahihi za uzazi wa mpango kwa kuzingatia miongozo ya utoaji huduma za uzazi wa mpango zilizopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu juu ya uzazi wa mpango kwa kutumia simu za viganjani, huduma hiyo hujulikana kama m4RH na ili kupata elimu hiyo, mhusika anatakiwa kutuma ujumbe wa m4RH kwenye namba 15014 na hapo mtu yeyote ambaye ana umri wa miaka 15 hadi 49 wanaweza kupata ujumbe wenye elimu ya uzazi wa mpango. Katika Mkoa wa Singida wateja waliopatiwa huduma ya uzazi wa mpango kwa mwaka 2015 walikuwa 198,822, mwaka 2016 walikuwa wateja 209,511 na
mwaka 2017 walikuwa wateja 173,587.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile Serikali imeendelea kuboresha huduma za dharura za uzazi ikiwemo upasuaji wa kutoa mtoto tumboni katika Mkoa wa Singida ambapo vituo vya afya vinne vya Ndago katika Halmashauri ya Iramba, Ihanja katika Halmashauri ya Ikungi, Itigi katika Halmashauri ya Itigi na Kinyambuli katika Halmashauri ya Mkalama vimeweza kupata kila kimoja kimepata fedha zaidi ya milioni 500 kwa ajili ya ukarabati wa vituo hivyo.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Hospitali ya Mtakatifu Gaspar imekuwa Hospitali ya Rufaa tangu mwaka 2011 na inahudumia wananchi wa Mikoa ya Tabora, Singida na Mbeya. Wakati wa kampeni mwaka 2015, Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kuipatia vifaa tiba, dawa na watumishi wa kutosha ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo wagonjwa:-
Je, ni lini ahadi ya Mheshimiwa Rais itatekelezwa ili kusaidia hospitali hiyo kutoa huduma za afya kwa ufanisi na kuokoa maisha ya wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kuboresha ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) katika utoaji wa huduma za afya, Serikali inatoa ruzuku ya fedha kwa ajili ya kulipia mishahara ya watumishi pamoja na ruzuku ya dawa na vifaa tiba. Jumla ya watumishi 50 wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar wanalipwa mishahara na Serikali ambapo ni Daktari Bingwa mmoja (Bingwa wa Upasuaji), Daktari mmoja, Daktari Wasaidizi (AMO) wawili, Tabibu wawili, Wauguzi 43 na Mteknolojia wa Maabara mmoja.
Mheshimiwa Spika, mgao wa dawa na vifaa tiba kutoka Bohari ya Dawa (MSD) unaendelea kutolewa na Serikali katika Hospitali ya Mtakatifu Gaspar ambapo katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali ilitoa dawa zenye thamani ya shilingi milioni 105.67 na mwaka wa fedha wa 2017/2018 dawa zenye thamani ya shilingi milioni 114.67 zimetolewa katika hospitali hiyo. Aidha, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaandaa mwongozo wa gharama za matibabu katika hospitali ambazo siyo za Serikali ili kuzifanya hospitali hizo kutoa huduma zenye gharama nafuu.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Mkoa wa Singida unakua kwa kasi sana na ujenzi wa majengo makubwa ya kisasa umeongezeka, lakini kwa muda mrefu sasa hakuna gari la zimamoto linaloweza kuhudumia mkoa; gari lililopo kwa sasa ni bovu na lina ujazo wa lita 1,500 tu na lenye ujazo wa lita 7,000 lilipata ajali miaka iliyopita na Serikali iliahidi kulifanyia matengenezo lakini mpaka sasa haijafanya hivyo:-
Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kisasa la zimamoto Mkoani Singida ili kukabiliana na majanga ya moto yanayoweza kutokea?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kuwa Mkoa wa Singida unakua kwa kasi ingawa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji lina gari moja lenye ujazo wa lita 1,500 ambalo linafanya kazi zake na gari la pili ni bovu. Hata hivyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji linatarajia kulifanyia matengenezo gari la pili ambalo ujazo wake ni lita 7,000 na pindi fedha zitakapopatikana gari zote mbili zitaweza kufanya kazi kwa pamoja.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha shughuli za zimamoto na uokoaji, Serikali kwa kupitia bajeti ya mwaka 2018/2019, imepanga kununua gari tano za zimamoto ambazo zitagawiwa katika maeneo mbalimbali nchini yenye uhitaji mkubwa. Aidha, Wizara inaandaa marekebisho ya Sheria ya Zimamoto na Uokoaji Namba 14 ya Mwaka 2017 ili kuzitaka halmashauri za manispaa, miji na wilaya kununua magari ya kuzimia moto ili kuondokana na upungufu mkubwa wa magari uliopo hivi sasa.
MHE. MARTHA M. MLATA (K.n.y. MHE. AISHAROSE N. MATEMBE) aliuliza:-
Sanaa ya Maigizo na muziki ni miongoni mwa Sekta zinazochangia asilimia kubwa ya vijana kujiajiri lakini kuna Vyuo vichache nchini vinavyotoa elimu hiyo ya sanaa ya muziki na maigizo ambavyo ni Chuo cha Sanaa Bagamoyo na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam huku masharti yake yakiwa ni changamoto kwa vijana wa mikoani:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha matawi ya Vyuo hivyo kwenye Kanda ama Mikoa ili kuongeza fursa zaidi kwa vijana?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mafunzo ya Elimu ya Sanaa ya Maigizo na Muziki au kwa ujumla Sanaa, yanatolewa kwa ngazi ya Shahada na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Dodoma na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam kwa upande wa Serikali na Chuo Kikuu cha Tumaini Arusha kwa upande sekta binafsi. Aidha, mafunzo kwa ngazi ya Stashahada na Cheti kwa Vyuo vya Serikali hutolewa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) yenye matawi takribani nchi nzima. Vipo vilevile vyuo binafsi ambavyo hutoa mafunzo ngazi ya Stashahada pamoja na Cheti.
Mheshimiwa Spika, nitoe rai kwa vijana na wadau wengine wanaotaka kubobea kwenye sanaa wajiunge na vyuo hivi ambavyo vimetawanyika nchi nzima. Aidha, nawapongeza wadau wote walioanzisha vyuo hivyo ili kuunga mkono jitihada za Serikali.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-
Uhaba wa maji safi na salama imekuwa ni kero kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Manyoni na Mkoa wa Singida:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha miradi mikubwa ya maji ambayo itahudumia wananchi wa maeneo hayo muda wote?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maji kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji na katika awamu ya kwanza ya utekelezaji wa Programu jumla ya miradi minne ya Solya, Kilimatinde, Londoni na Majiri imekamilika na wananchi wanapata huduma ya maji. Katika awamu ya pili ya utekelezaji wa Programu, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni inatekeleza miradi ya Mangoli, Itetema, Kasanii, Kintinku, Maweni, Makuru, Nyaranga, Makutupora, Sanza/Ntope, Makanda, Igwamadete, Heka, Chikombo na Mazuchi ambayo ipo katika hatua za utafutaji wa vyanzo na kufanya usanifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mradi mkubwa wa Mbwasa ambao umeshafanyiwa usanifu na utaanza kutekelezwa katika mwaka 2018/2019 kwa ajili ya kuhudumia vijiji vya Mbwasa, Mwiboo, Chikuyu, Mtiwe, Chilejeho, Mvumi, Ngaiti, Kintinku na Lusilile.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mwaka wa fedha 2018/2019, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetengewa jumla ya shilingi bilioni 1.3 na Serikali itahakikisha miradi hiyo inatekelezwa na inakamilika mapema na kutoa huduma ya maji safi na salama kwa wananchi wa maeneo hayo.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Tatizo la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi linazidi kuwa janga la Kitaifa nchini huku jitihada za kulikabili zikionekana kutopewa kipaumbele; hali ni mbaya katika majiji makubwa kama Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya ambapo idadi kubwa ya watoto hao hujihusisha na kuomba pamoja na matukio ya uhalifu ikiwemo wizi wa vifaa vya magari kwenye maegesho.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha kampeni ya Kitaifa ya kukabiliana na tatizo hili kwa nchi nzima ikiwemo kuwaweka kwenye vituo maalum na kuwapatia huduma za msingi?

(b) Je, Serikali inatambua idadi kamili ya watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi kwa nchi nzima?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeandaa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto wa mwaka 2017/2018 ambao utaisha 2021/2022 ambapo miongoni mwa shabaha zake ni kuhakiksha watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi wakiwemo watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani wanapata huduma stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kuwaunganisha watoto hawa na familia zao na pale itakapobainika kuwa wazazi hawapatikani, watoto hawa wataunganishwa na familia za kuaminika wakati taratibu nyingine za kudumu zikiendelea kufanyiwa kazi na mamlaka husika ikiwemo utaratibu wa malezo ya kambo, kuasili au kuwapeleka katika makao ya watoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau imefanya utafiti ili kubaini idadi ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika mikoa sita nchini, kwa maana ya Mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma, Arusha na Iringa ambapo jumla ya watoto 6,393; wanaume wakiwa 4,865 na wanawake 1,528, wametambuliwa. Watoto waliotambuliwa walipewa huduma za chakula, malazi, mavazi na matibabu na kati ya hao ambao walitambuliwa, watoto 930 waliunganishwa na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau imeandaa mwongozo wa utambuzi wa watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuwaunganisha na huduma. Katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Juni, 2018, jumla ya waoto 864,496 walitambuliwa kuwa wanaishi katika mazingira hatarishi katika mikoa yote nchini kasoro Mikoa ya Lindi na Ruvuma.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inakabiliwa na uhaba mkubwa wa Watumishi, uchakavu wa majengo, mifumo mibovu ya maji safi na maji taka ikiwemo na ukosefu wa gari la wagonjwa:-

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia hospitali hiyo watumishi wa kutosha hasa ikizingatiwa kuwa hospitali hii ni tegemeo la watu wengi hasa akinamama wajawazito?

(b) Je, Serikali ina mikakati gani ya kuipatia hospitali hiyo vifaa tiba na vitendea kazi vingine ikiwemo CT Scan na MRI?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa mwaka wa fedha 2018/2019, imeajiri watumishi wa kada mbalimbali za afya 52, katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida hivyo kupunguza tatizo la upungufu wa watumishi na kufikia asilimia 45. Aidha, kwa mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara inategemea kuomba kibali cha kuajiri watumishi 197 wa kada mbalimbali za afya kwa ajili ya hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikiendelea kuboresha huduma za uchunguzi katika hospitali zote za Rufaa za Mikoa ikiwemo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida. Mpaka sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida imeshapelekewa mashine mpya ya kisasa ya X-ray (digital x-ray) na imeanza kufanya kazi. Sanjari na hilo, hospitali mpya, itakapokamilika itasimikwa vifaa vya kisasa ikiwemo CT Scan ili kuiwezesha kufanya kazi kwa hadhi iliyokusudiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa magodoro, vitanda na vifaa tiba Wizara itaendelea kuhakikisha Hospitali inatenga bajeti kupitia mpango kabambe wa Hospitali Comprehensive Hospital Operational Plan (CHOP) kwa ajili ya ununuzi wa vitanda, magodoro na vifaa tiba ambapo kwa mwaka huu wa fedha 2018/2019, tayari imetumia kiasi cha Sh.673,575,168.58/= kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na vitendea kazi kama magodoro, mashuka, vitanda, mashine ya kufulia, ultra sound pamoja na vifaa kwa ajili ya chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).
MHE. AYSHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Mradi wa maji wa Kitinku/Lusilile ndiyo uliotarajiwa kuwa mkombozi wa Wananchi wa Manyoni katika kupata huduma ya maji safi na salama, lakini mradi huo kwa muda mrefu umekwama kutokana na fedha kutopelekwa:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya kukamilisha mradi huo muhimu kwa wakati ili kumtua ndoo kichwani Mwanamke wa Manyoni?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Kintinku Lusilile ulibuniwa kwa lengo la kuhudumia vijiji 11 vyenye wakazi wapatao 55,485 kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012. Vijiji hivyo ni Kintinku, Lusilile, Maweni, Mvumi, Ngaiti, Chikuyu, Mwiboo, Mbwasa, Mtiwe, Makutupora na Chilejoho. Kwa mujibu wa usanifu uliofanyika mradi huu unakadiriwa kugharimu bilioni 10.

Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa mradi huu umepangwa skutekelezwa katika awamu nne ambapo awamu ya kwanza ilihusisha utafiti na uchimbaji wa visima vinne na utekelezaji wake ulikamilika. Hivi sasa utekelezaji wa awamu ya pili unaendelea ambapo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni tarehe 23 Mei, 2018 iliingia mkataba na Mkandarasi CMG Construction Company Limited kutekeleza awamu ya pili ya mradi huo ambao ulitarajiwa kukamilika mwezi Novemba, 2018. Hata hivyo kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha awamu hiyo haukuweza kukamilika kama ilivyopangwa na kwa sasa utekelezaji wa awamu ya pili umepangwa kukamilika mwezi Septemba 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mikakati ya kuhakikisha tunaongeza kiwango cha upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Manyoni, Wizara imetenga kiasi cha shilingi bilioni 2.4 kwenye mwaka wa fedha 2019/2020 kutekeleza miradi mbalimbali ya maji wilayani humo. Tayari RUWASA wamewasilisha maombi ya kuanza kutekeleza awamu ya tatu ya Mradi wa Maji wa Kintinku/Lusilile.
MHE. AISHAROSE N. MATEMBE aliuliza:-

Ukosefu wa gari la kubebea wagonjwa Wilaya ya Manyoni umekuwa na madhara makubwa ikiwemo kusababisha vifo vya akinamama na watoto pindi wanapotakiwa kukimbizwa kwenye hospitali za Rufani.

Je, Serikali ina mpango gani wa kuipatia Manyoni gari la Wagonjwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI WA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aisharose Ndogholi Matembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni ina magari mawili ya wagonjwa, gari moja lipo kwenye Kituo cha Afya cha Nkonko na jingine katika Kituo cha Afya cha Kintinku. Hospitali ya Wilaya inatumia pickup na gari aina ya land cruiser hardtop. Serikali itatoa kipaumbele kwa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni pindi itakapopata magari ya wagonjwa kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itakamilisha Mradi wa Maji Kintiku -Lusilile?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Kintinku -Lusilile ni mradi mkubwa ambao unatekelezwa kwa awamu nne na hadi mwezi Mei, 2021 utekelezaji wa awamu ya kwanza imekamilika ambayo ilihusisha ujenzi wa tenki la kukusanya maji la lita 300,000, ujenzi wa nyumba ya mtambo wa kusukuma maji na kufunga mitambo ya kusukuma maji, ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji lita milioni mbili na ulazaji wa bomba kuu umbali wa kilometa 1.2. Aidha, utekelezaji wa awamu ya pili unaohusisha ulazaji wa mabomba ya usambazaji umbali wa kilometa 1.3 unaendelea na unatarajiwa vijiji vitatu vya Chikuyu, Mwiboo na Mbwasa ambavyo vina jumla ya wakazi wapatao 6,020 vitaanza kunufaika na huduma ya maji kabla ya mwezi Julai, 2021.

Mheshimiwa Naibu Spika, utekelezaji wa mradi huu unatarajia kukamilika katika mwaka wa fedha 2021/2022 na utahudumia wakazi zaidi ya 55,000 wa vijiji 11.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kupeleka umeme katika vijiji 14 vya Jimbo la Manyoni Magharibi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kazi ya kupeleka umeme katika vijiji 14 pamoja na vijiji vingine vilivyobaki katika Jimbo la Manyoni Magharibi itaanza mwezi Julai, 2021 kupitia utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Disemba, 2022.

Mheshimiwa Spika, kazi ya utekelezaji wa mradi huu katika Wilaya ya Manyoni kwa ujumla inahusisha ujenzi wa njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 urefu wa kilometa 383.1, njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 0.4 urefu kilometa 31, ufungaji wa transfoma 31 zenye uwezo wa KVA 50 pamoja na kuunganisha huduma ya umeme kwa wateja wa awali 682. Gharama ya mradi ni shilingi bilioni 15.45.
MHE. DKT. PIUS S. CHAYA K.n.y. MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka Watumishi pamoja na vitendea kazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi, mwezi Julai, 2021, Serikali ilipeleka watumishi 28 wakiwemo watumishi 19 wa Sekta ya Afya na watumishi tisa wa Sekta ya Elimu. Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022, imepanga kuajiri jumla ya watumishi 477 ili kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi. Pamoja na jitihada hizo, Serikali itaendelea kufanya msawazo wa watumishi katika Halmashauri zote ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwa kadri ya mahitaji.

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa vitendea kazi, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imetenga na kuidhinishiwa bajeti ya shilingi milioni 705.85 kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi ikiwemo samani za ofisi pamoja na magari manne kwa gharama ya shilingi milioni 430.00. Mpaka sasa, Halmashauri ipo katika hatua za mwisho za ununuzi wa magari mawili ya awali kwa gharama ya shilingi milioni 220.00 yatakayosaidia kupunguza changamoto ya upungufu wa magari. Kwa ujumla, Serikali itaendelea kununua vitendea kazi kwa ajili ya halmashauri hiyo kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante sana.
MHE. DKT. RITTA E. KABATI K.n.y. MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kubebea Wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/ 2022 Serikali kupitia Mpango wa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatagawiwa kwa Halmashauri zote 184. Kupitia utaratibu huu kila Halmashauri itapatiwa gari moja la kubebea wagonjwa, ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.

Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa magari ya kubebea Wagonjwa ili kuboresha na kuimarisha hali ya utoaji huduma za afya nchini kote.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kubebea Wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ina gari moja la kubebea wagonjwa ambalo lipo katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama na linahudumia Vituo vingine vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. Ahsante.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka gari la kubebea Wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ina gari moja la kubebea wagonjwa ambalo lipo katika Hospitali ya Wilaya ya Mkalama na linahudumia Vituo vingine vya kutolea huduma za afya.

Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali kupitia Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano Dhidi ya UVIKO-19 itanunua magari 195 ya kubebea wagonjwa ambayo yatapelekwa kwenye Halmashauri zote nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama. Ahsante.
MHE. AYSHAROSE N. MATTEMBE aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kukarabati Hospitali ya Wilaya ya Manyoni?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Aysharose Ndogholi Mattembe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imetoa shilingi millioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wodi mbili za wanawake na wanaume pamoja na jengo la kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Wilaya ya Manyoni. Aidha, majengo haya yamekamilika na yataanza kutoa huduma mwishoni mwa Novemba, 2023.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imepeleka shilingi billioni 1.4 Oktoba, 2023 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

Mheshimiwa Naibu Spika, halmashauri inaendelea na taratibu za kupata mzabuni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la wodi ya wazazi lenye chumba cha upasuaji wa dharura, jengo la X-ray, stoo ya kuhifadhia dawa, jengo la kliniki ya Mama na Mtoto, jengo la kufulia, njia za kutembelea wagonjwa pamoja na kufanya ukarabati wa majengo mengine ya Hospitali ya Wilaya ya Manyoni, ahsante.