Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Ester Amos Bulaya (123 total)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Ukarabati wa barabara pia unaendana na utanuzi wa barabara. Serikali ilikuwa inatanua barabara kuu ya kutoka Mwanza kwenda Musoma na ilifuata nyumba za wananchi na wakawafanyia tathmini, lakini kwa bahati mbaya mpaka leo hawajalipwa na kuna wazee wangu kule wanapata taabu sana, nyumba zao hazijalipwa na wanaishi kwa taabu. Miongoni mwa wazee wangu ni pamoja na baba yangu Mzee Wasira, naye nyumba yake imefanyiwa tathmini katika kijiji chetu cha Manyamanyama.
Je, ni lini mtawalipa wananchi wa Bunda kwa sababu mmeshawafanyia tathmini miaka mitatu iliyopita?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:-
MWENYEKITI: Lini mtawalipa.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Fedha zitakapopatikana tutawalipa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Serikali kuamua kufanya tathmini kwenye Mabaraza ya Watoto ni kwamba kuna changamoto ambazo zipo na kuyafanya Mabaraza hayo yasitetee haki za msingi za watoto hasa za watoto yatima.
Je, tunatambua kwamba kuna center za watu binafsi ambazo zinahudumia watoto yatima na zinafanya kazi kwenye mazingira magumu sana nchi nzima ikiwepo na Jimboni kwangu Bunda. Serikali ina mkakati gani wa kusaidia center hizi ili kusaidia watoto yatima waweze kulelewa vizuri na kupata huduma sahihi hasa za elimu kama wanavyopata wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, mmesema Rais aliweka sahihi tarehe 22 Mei, 2015 na kwamba mpaka sasa hivi hamjakamilisha taratibu za kanuni. Ni jambo gani linawakwamisha, hamuoni kwamba kuna haja ya kukamilisha hizi kanuni mapema na mwaka huu wa fedha tutenge bajeti ili Baraza ili lianze na vijana wawe na chombo chao cha kuibana Serikali na kutetea vijana wao katika nchi hii?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitumie nafasi hii kumpongeza muuliza swali Mheshimiwa Ester Amos Bulaya na aliyeuliza swali la msingi Mheshimiwa John John Mnyika kwa kuendelea kufuatilia haki na maslahi ya vijana wa nchi yetu. Pamoja na pongezi hizo naomba kujibu maswali yake ya nyongeza kama ifuatavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwamba kuna changamoto zinazowakabili watu wenye taasisi ama vituo binafsi vinavyolea watoto yatima na kwamba Serikali inawasaidiaje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina majukumu ya kutengeneza mfumo wa kisheria ambao utaziwezesha taasisi mbalimbali zikiwemo za Serikali na za watu binafsi kutekeleza majukumu yake ya kutoa huduma kwa wananchi kama ilivyopangwa kwa mujibu wa sheria hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana hiyo mfumo huo sasa upo na tunatengeneza Mabaraza haya kwa malengo ya kutoa ushauri kwa Serikali juu ya namna bora ya kuendesha taasisi mbalimbali za binafsi ama za Serikali zinazotoa huduma kwa watoto yatima ama watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kwamba tumechelewa kuunda kanuni. Ni miezi takriban sita tu toka sheria ile imesainiwa na Mheshimiwa Rais na sidhani kama tumechelewa. Imani yangu ni kwamba, kanuni zitatengenezwa haraka na zitaanza kufanya kazi kwa sababu mwaka 2015 ulikuwa ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu na watu wengi walikuwa busy na kwa kipindi kirefu, hivyo Mawaziri wasingeweza kufanya kazi ya kutunga kanuni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ipo kazini, naomba atuamini, tutatunga kanuni hizo haraka na tutawashirikisha wadau wote ili mawazo yao yaweze kuwemo humo ndani na mwisho wa siku tutunge kanuni zilizo bora ambazo zitaweza kuleta ustawi wa vijana wa nchi yetu.
MHE. ESTER N. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimemsikiliza Naibu Waziri wa Fedha kwa makini, kwa jinsi alivyojibu ametutajia figure kubwa sana ambazo zimeenda katika sekta ya kilimo, lakini ni wazi na Waheshimiwa Wabunge wanajua bado wakulima wetu kilimo chao ni cha kusuasua na wanalima katika mazingira magumu. Hata wale ambao wanajitokeza katika kilimo cha umwagiliaji wakiwemo watu wangu wa Tamau, Nyatwali na maeneo mengine wanakosa vifaa. Mna mkakati gani wa kuhakikisha hizi figure zinaendana na hali halisi ya mkulima mmoja mmoja?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba nimshukuru kwa kuelewa kwamba kiasi hiki nilichokitaja ndicho ambacho kimetoka Benki ya TIB (Tanzania Investment Bank) kwenda katika miradi ya kilimo na miradi mingine niliyoitaja. Mimi kama Naibu Waziri wa Fedha na Mipango jukumu langu ni kuhakikisha pesa hizi zinafika kwa wale wanaomba pesa hizi. Kwa hiyo, naamini tutafanya kazi kwa ushirikiano mzuri mimi na Waziri wa Kilimo, mtani wangu Mheshimiwa Mwigulu Nchemba ili tuhakikishe sasa pesa hizi zinawanufaisha walengwa na zinaweza kukidhi mahitaji yale waliyoomba.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, katika Jimbo la Bunda Mjini tangu nikiwa Mbunge wa Viti Maalum nilikuwa nazungumzia mradi wa maji wa kutoka Nyabeu kuja Bunda Mjini. Huo mradi una miaka nane, sasa niulize hivi ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa mradi ule, wananchi wa Bunda ambao hawajawahi kupata maji safi na salama tangu uhuru waone na wenyewe ni wananchi wa Tanzania na ndiyo liwe swali la mwisho kuuliza katika Bunge hili Tukufu.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, na mimi naomba nikiri wazi kwamba Mheshimiwa Ester toka tukiwa katika timu moja alikuwa akiuliza swali hili, naomba niseme.
Mheshimiwa Spika, lakini najua kabisa katika mpango wa maji ambao nadhani Wizara ya Maji watakapokuja ku-table bajeti yao hapa watazungumzia jinsi gani wana programu kuhakikisha maeneo haya miradi yote ya maji inaenda kukamilika. Ukiangalia jinsi gani watazungumza katika bajeti yao ya Wizara ya Maji, sitaki kuwazungumzia sasa. Lakini nikijua kwamba Wizara ya Maji na TAMISEMI ni Wizara pacha, tunahusiana Wizara ya Maji, TAMISEMI, Kilimo halikadhalika na Wizara ya Afya. Mambo yetu yanaingiliana yote kwa pamoja kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi. Ninajua kabisa katika mpango wa maji wa sekta ya maji namba mbili imeweka mipango ya kumalizia miradi yote ya muda mrefu. Mimi ninaamini wananchi wa Bunda kipindi hiki sasa ule mradi wa maji kama Serikali ilivyokusudia utaweza kukamilika katika kipindi hiki.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru, na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka mwezi Machi, REA walikuwa wamepata karibia asilimia 40 tu ya fedha za kwenda kumalizia katika REA ya Awamu ya Pili. Nilitaka kujua, mpaka sasa hivi Wizara yako imepokea kiasi gani ili vijiji vyangu ambavyo vilikuwa viporo kabla ya hii REA ya Awamu ya Tatu, kama Kunzugu, Mihale, Nyamatoke, Bukole, Kamkenga, Kangetutya, Rwagu na maeneo mengine yapate umeme katika ule ule mpango wa REA ya Pili na huu wa REA ya Tatu?
WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli ni kwamba tulikuwa asilimia 40, lakini kwa sasa hivi tuko zaidi ya asilimia 75, kwa hiyo jinsi ambavyo tunakusanya fedha na ndivyo jinsi ambavyo Hazina inatupatia fedha. Kwa hiyo, kwa mipangilio inavyokwenda na wakandarasi tumewaambia huu mwezi Mei tutafanya tena tathmini kwa kila mkandarasi amefanya kazi kiasi gani, nadhani hadi kufikia mwezi Mei tutakuwa tumefika karibu asilimia 80. Mheshimiwa Mbunge nataka kukuhakikishia na ndiyo maana tumekubaliana na ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge kama miradi yako ya REA Awamu ya Pili haikukamilika ni lazima itapewa kipaumbele kwenye REA Awamu ya Tatu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Tatizo la maji la Makambako kwa asilimia kubwa linafanana na Jimbo la Bunda Mjini. Natambua Serikali ya Awamu ya Nne ilianza mradi mkubwa wa maji tangu mwaka 2006 ni wa muda mrefu sana na ulikuwa ukamilike, lakini mpaka sasa hivi haujakamilika.
Mheshimiwa Naibu spika, mradi ule unaanzia Kata ya Guta lakini hauna vituo na kama mradi ule wa kupeleka maji katika Mji wa Bunda ukiwa na vituo, vile vijiji jirani Kinyambwiga, Tairo, Guta A, Guta B, Gwishugwamala, vyote vitanufaika na mradi wa maji. Sasa je, Mheshimiwa Waziri haoni kwamba kuna haja ya kuweka vituo ili vijiji hivyo vinavyopita mradi kwenda Mji wa Bunda vinufaike na mradi huo? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna mradi ambao tumetekeleza katika Mji wa Bunda tumeweza kujenga bomba kubwa kutoka Ziwa Victoria, tumeweza kujenga matanki, hiyo ni awamu ya kwanza. Sasa awamu ya pili tutakwenda kusambaza katika maeneo yale ambayo bomba hilo limepita. Kwa hiyo, naomba niseme tu kwamba, kazi hiyo tutakwenda kuifanya kwa manufaa ya wananchi wa Bunda. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Angellah, nilikuwa napenda niulize swali fupi la nyongeza.
Je, kumekuwa na malalamiko katika baadhi ya maeneo kwamba fedha hizi zinatumika vibaya na wahusika wanatoa majina hewa, na inasemekana Waziri aliyekuwa ana-deal na TASAF, alitumia fedha hizo vibaya kwa ajili ya kutafuta nafasi ya Urais. Uko tayari kuchunguza hilo?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS (UTUMISHI NA UTAWALA BORA): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme tu kwamba malalamiko yoyote tukatakayoyapokea, tutafanya uchunguzi. Nimekuwa nikisema suala hili kuna uwazi mkubwa katika vikao mbalimbali vya vijiji na wakati wowote mtakapoona kuna matatizo, basi msisite kututaarifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nami mwenyewe nimejipanga, kutokana na malalamiko mengi ambayo nimeyasikia, kwa kweli hayo majipu tutayatumbua. (Makofi)
MHE. ESHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, wananchi ambao wanazungukwa na hifadhi kwa Mkoa wa Mara, Tarime, Serengeti, Bunda Mjini na Bunda, wamekuwa wavumilivu sana. Hivi tunavyozungumza hakuna mwaka ambao tembo hawatoki kwenye hifadhi na kuja kwenye vijiji, nazungumzia kwenye Jimbo langu, Kijiji cha Serengeti, Tamau, Kunzugu, Bukole, Mihale, Nyamatoke na maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivi karibuni tulienda na Mheshimiwa Jenista, akajionea mwenyewe tembo wanavyoharibu mazao ya wananchi, lakini bado fidia ni ndogo, shilingi 100,000/= mtu anaandaa shamba kwa milioni 10. Hivi karibuni Mheshimiwa Waziri wa Utalii na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu…..

MHE. ESTER A. BULAYA: Komeni basi, kelele niongee!

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Jenista wamepeleka magari mawili na askari sita kuhakikisha yale mazao ya wananchi yanalimwa. Tunaposema ni lini Serikali mtatafuta ufumbuzi wa kudumu ili hao wananchi waepukane na njaa wakati wana uwezo wa kulima na lini ufumbuzi wa kudumu utapatikana badala ya kupeleka magari na askari kwa ajili tu ya kulinda mazao ambayo yako shambani?
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa fursa ya ziada ya kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu alikuwa kule na alitoa ahadi, alijionea mwenyewe na kutoa ahadi kwamba Serikali itafanya juhudi ya kupeleka magari na askari wa ziada ili kuhahakikisha kwamba tembo hawaharibu mazao ya wananchi. Ni wiki moja na nusu sasa magari yale yako kule yanafanya kazi na tunaamini kabisa kwamba hii ni hatua ya kwanza ya Serikali kulishughulikia jambo hili kwa hatua za kudumu.

Mheshimiwa Spika, tumeanza pia kutumia ndege ambazo hazina rubani, tumeanza majaribio katika Wilaya ya Serengeti na Wilaya ya Bunda ili kuzitumia ndege hizi kuwatisha tembo na kuwaondoa katika maeneo ambayo wako karibu na mashamba ya watu na tunategemea kwamba jambo hili litatatuliwa kwa kudumu kwa kutumia utaratibu huo wa teknolojia.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kwa baadhi ya majibu ya uongo ambao Mheshimiwa Naibu Waziri ameyajibu. Mimi ndio
Mbunge wa Jimbo husika na kuna mwananchi wangu nimemhudumia katika Hospitali ya DDH. Aliyekupa hizo taarifa kamwulize vizuri, amekuongopea.
Mheshimiwa Naibu Spika, naenda sasa kwenye swali. Sheria ya Kazi Na. 6, mtu anapokufa kazini, analipwa fidia shilingi milioni 10. Hawa wananchi wangu walikuwa kazini, mbali na kwamba wamejiajiri wenyewe, mwalipe fidia, siyo kifutajasho cha laki moja moja. (Makofi)
Swali la pili; Mheshimiwa Waziri, tatizo la mamba katika vijiji nilivyokwambia ni kubwa sana, hata kwa kaka yangu kule Mheshimiwa Kangi, wananchi wanavua kienyeji kwa kutumia kuku. Lini Wizara yako itapeleka wataalam mwavue? Wananchi wangu wanakufa kila siku wanakuwa vilema halafu unatoa majibu mepesi hapa!
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kwamba umesema swali la kwanza pengine lingejibiwa na Waziri wa Sheria lakini napenda kutoa sehemu ya majibu.
Mhehimiwa Naibu Spika, Serikali inafanya kazi zake kwa kutumia mfumo wake. Kwa hiyo, taarifa ambazo zimo katika majibu niliyoyatoa zimetoka kwenye Halmashauri ya Bunda na vyombo vya Serikali vilivyopo kule. Kwa hiyo, kwa kuwa Mheshimiwa Ester Bulaya ni Mjumbe wa Halmashauri ya Bunda, anaweza kwenda kuwahoji waliotoa taarifa hizi ambao ni Halmashauri inayohusika kwamba kwa nini wameleta majibu ya uongo?
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia kwamba Serikali inalipa kifuta jasho au kifuta machozi na siyo fidia; na Mheshimiwa Mbunge angependa badala yake tulipe fidia, kwa sababu kiwango cha shilingi laki moja ni kidogo; nchi hii inaendeshwa kwa mujibu wa sheria. Hakuna namna yoyote ambayo unaweza kuendesha nchi bila kufuata sheria, kanuni na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ulipaji wa kifuta jasho na kifuta machozi ni utaratibu uliopitishwa kwa mujibu wa sheria ambayo imepitishwa na Bunge hili. Iwapo itaonekana kwamba utaratibu huo haufai kwa namna yoyote ile, ni wajibu wa Waheshimiwa Wabunge kwa niaba ya wananchi, Mheshimiwa Ester Bulaya akiwa mmoja wao kuleta mapendekezo ya kufanya mapitio upya ya Sheria hii na kama itafaa, pengine Serikali inaweza ikaanzisha utaratibu mwingine badala ya huu.

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuongezea jibu zuri ambalo limetolewa na Mheshimiwa Naibu Waziri. Kwanza napenda niseme kwamba Wizara itafuatilia kuona kama kuna taarifa zaidi ya zile ambazo tunazo ili tuweze kuzishughulikia kama ambavyo tumeshughulikia sheria hizo nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, mimi sio Mwanasheria, lakini najua kwa sababu nilifanya kazi kwenye Wizara ya Kazi, kwamba hakuna Sheria ya Kazi ambayo inafidia raia wakati yuko kwenye shughuli zake. Sheria ile ya Kazi ni ya wafanyakazi kama ambavyo inajulikana kwenye sheria ile.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, najua moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi yetu ni migogoro ya ardhi na eneo ambalo inasemekana kumekuwa na migogoro ya ardhi ni pamoja na eneo la Kibada Kigamboni ambapo kuna viwanja vilipimwa na Serikali na wananchi wakapewa na Wizara husika. Sasa, nataka kujua nini status ya eneo hilo wakati Wizara imepima, imewapa wananchi lakini leo imetokea kwamba eneo ambalo amepewa mtu mmoja tayari amejitokeza mtu mwingine amesema hilo eneo ni la kwake wakati Wizara ndio wametoa hati; nini status ya eneo hilo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tutakumbuka sote hapa Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi akiwa hapa Bungeni alitamka kwamba migogoro yote ya ardhi ambayo Waheshimiwa Wabunge mliwasilisha humu Bungeni na migogoro mingine ambayo inahusisha taarifa mbalimbali ambazo zimeshafanyiwa uchunguzi, Mheshimiwa Waziri wa Ardhi aliunda Tume ya kupitia taarifa hizi za uchunguzi zilizofanyika, lakini na migogoro ambayo Waheshimiwa Wabunge tayari waliiwasilisha kipindi cha bajeti.
Mheshimiwa Mwenyekit, nataka kuwaambia kwamba, timu hiyo ya wataalam iko kazini na Mheshimiwa Bulaya avumilie, asubiri, taarifa hiyo ya wataalam itakapokamilika tutawaletea hapa Bungeni ili kila mmoja ajue status ya kila eneo la mgogoro ambavyo limeshughulikiwa na Serikali.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jinsi Mheshimiwa Waziri alivyojibu swali lake, kwamba bado hawajagundua nani ambaye amesababisha tatizo, lakini Serikali iliji-commit kulipa fidia. Sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa suala la pamba limekuwa ni issue kubwa sana.
Je, Mheshimiwa Waziri, tatizo la pamba likijitokeza tena, uko tayari kujiuzulu kwa sababu majibu yako tayari unajikanganya hapa?
WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri kama ofisi inawezekana anavyosema Mheshimiwa Mbunge alitoa majibu ya kusema Serikali italipa fidia. Lakini hizo fedha ni fedha ya umma ambayo haiwezi ikalipwa tu bila kujiridhisha kwa kweli kwamba anayelipwa anastahili na kwamba Serikali inayo liability katika hilo jambo. Kwa hiyo, ni lazima kuwa na uhakika kwamba kwanza kweli Serikali inayo liability katika hilo jambo, lakini pili anayelipwa anastahili kulipwa hizo fedha na ndiyo maana hatua hizi zinafanyika. Kama nilivyosema kwenye suala la viuatilifu, tumekwisha jiridhisha beyond doubt nani wamehusika na hilo kosa la kusababisha dawa zisiwe na effect katika kuua wadudu kama ilivyotarajiwa na kwa hiyo hawa watachukuliwa hatua kama sheria inavyotaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo hata kwenye mbegu, tutakapajiridhisha exactly ni nani muhusika kwanza hawa watachukuliwa hatua na kama ni Serikali, itakuwa na wajibu wa kulipa tutafanya namna hiyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona. Dhamira ya Benki ya Kilimo ni kuwasaidia wakulima wadogowadogo, lakini kwa muda mrefu wanaokopa katika benki hii wengi ni wakulima wakubwa ambao pia wanakopesheka katika mabenki mengine.
Swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, ni lini sasa Serikali itahakikisha benki hii inawanufaisha wakulima wadogowadogo ambao wengi wako vijijini na si wale wakulima wakubwa ambao wanaweza kukopesheka katika mabenki mengine?
ambao wanasemwa ni wakubwa ambao wanakopeshwa na Benki ya Kilimo, benki hii imewakopesha wakulima wadogowadogo katika mikoa ambayo nimeitaja katika vikundi. Mpaka sasa katika hiyo mikoa niliyotaja, vimekopeshwa vikundi 89 ambavyo vina wakulima wadogowadogo 21,526 na hawa wanaokopeshwa wanakopeshwa mikopo midogomidogo kutegemea, wengine wanapata mikopo miaka miwili, wengine miwili mpaka mitano na wengine mitano mpaka 15. Kwa hiyo, si kweli kwamba benki hii imekuwa inakopesha wakulima wakubwa tu. Tunawakopesha pia vikundi vya wakulima wadogowadogo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nasikitika kwamba Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara wamemuongopea kabisa. Kwa sababu suala la EPZ nilianza ku-deal nalo tangu nikiwa Mbunge wa Viti Malaam na mpaka Mbunge wa Jimbo, hiyo Kata ndiyo Kata yenye wapiga kura wengi na ndiyo waliyonipa kura nyingi kwa sababu ya hiki kitu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, pesa zilizotumika kulipa EPZ ni shilingi 1, 240, 000, 000, hakuna ukaguzi wowote ambao umefanyika, wala uchunguzi wowote mpaka hivi sasa tunavyoongea. Kilichotokea, Mkaguzi wa Ndani alitoa ripoti kwa Mkuu wa Mkoa ambaye naye katumbuliwa kuhusiana na hili na Mkuu wa Wilaya aliyeshiriki na ubadhirifu huu ametumbuliwa kwa ajili ya udanganyifu wa suala hili.
Swali la kwanza, je, uko tayari sasa kuagiza TAKUKURU na CAG kufanya uchunguzi ili watu waliokuwa wakilindwa na Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wiliya washughulikiwe?
Swali la pili, nini hatma ya wananchi wa eneo hili ambao waliahidiwa watapelekwa katika eneo mbadala ili kupisha mradi wa EPZ na wala hawana tatizo nalo?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kwa masikitiko makubwa naomba nijibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya.
Mheshimiwa Spika, taarifa nilizopewa na watendaji wangu wanasema wamelipa bilioni 2.3, yeye alizopata ni bilioni moja, hapa kuna tatizo na hili ni tatizo la kipolisi. Mimi pamoja na CAG pamoja na TAKUKURU, nitamuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi anisaidie. Hili siyo suala la TAKUKURU siyo suala la Polisi, tofauti ya bilioni moja ni pesa kubwa sana wala haihitaji uchuguzi, ni kupiga foleni watu, aliyelipwa akae huku, ambaye hakulipwa akae huku watu wanakwenda selo. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niko tayari na nitaomba Mheshimiwa Mwigulu anisaidie na Mheshimiwa Simbachawene, kwa sababu wanaotuhumiwa ni watu wa TAMISEMI. Hili siyo langu, hivi siyo viwanda hivi, hili siyo eneo langu ni la Mheshimiwa Simbachawene na Mheshimiwa Mwigulu. Wizi siyo viwanda.
Mheshimiwa Spika, swali la pili la Mheshimiwa Bulaya nashukuru, Serikali itakwenda kulishughulikia tunapokwenda Mawaziri watatu kukamata panya hao, tutahakikisha wananchi wanapewa maeneo mazuri. Zaidi niwaambie watu wa Mara, jambo la muhimu linaloniuma ni kuhakikisha watu Mara tunatafuta wawekezaji ili EPZA iweze kutengeneza sehemu ya uwekezaji kwa ajili ya maendeleo ya ukanda ule.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, nimesikia na tutalishughulikia!
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mbali na changamoto ambayo inakikabili Chuo cha Maendeleo ya Jamii - Kisangwa kuhusiana na kutopata fedha za uendeshaji, karakana na kadhalika lakini chuo hicho pia hakina gari. Hivi tunavyozungumza aliyekuwa Mkuu wa Chuo alijiuzia VX kwa Sh. 600,000/= na kufanya Mkuu wa Chuo wa sasa hivi asiwe na gari na kusababisha shughuli za chuo zisiende. Je, Serikali iko tayari kushughulikia ufisadi huu kwa sababu hakuna VX inayouzwa Sh. 600,000/= na kupeleka gari ili chuo hicho kiendeshe shughuli zake vizuri?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa swali kutoka kwa rafiki yangu Mheshimiwa Ester Amos Bulaya kuhusu kile anachopenda kukiita ufisadi. Majibu ya Serikali ni kwamba kwenye kuuza mali za umma ambazo zimemaliza muda wake na ama zimekuwa classified kama ni dilapidated ama mali zilizochoka unajulikana na umeandikwa. Kwa hivyo, kama Mheshimiwa Mbunge ana ushahidi kwamba utaratibu huu ambao umeandikwa kwenye sheria mbalimbali za kuuza mali za Serikali zilizochakaa haukufuatwa, naomba anikabidhi nyaraka alizonazo ili niweze kufuatilia na kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za nchi yetu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kuhusiana na wakandarasi kujenga barabara chini ya kiwango au kukarabati barabara
chini ya kiwango si jambo geni na Mheshimiwa Spika, na wewe ni shahidi barabara ya kutoka Morogoro kuja hapa
Dodoma sasa hivi tayari imeshavimba, Wabunge wote mnajua. Lakini hiyo barabara ninayoitaja pia inapita Jimboni
kwako, nadhani shahidi tayari sasahivi imeshaanza kuvimba, nimeona tu nikuulizie bosi wangu.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pia mashahidi, ukarabati unaofanywa hata kwenye barabara
za hapa Dodoma, Area D, Area C pia uko chini ya kiwango, unaigharimu sana Serikali kuwa tunakarabati barabara mara kwa mara pindi Waheshimiwa Wabunge wanapokuja Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kingine, barabara ya kutoka Musoma – Bunda na yenyewe pia, ilishaharibika kabla hata
ya kukabidhiwa.
Swali langu, je, mna mkakati gani katika barabara mpya ya kutoka Kisorya - Bunda Mjini - Nyamswa, ambayo
bado haijajengwa, inajengwa kwa kiwango cha lami, ili barabara hiyo isiigharimu Serikali fedha za kutosha na iwe ya kiwango? Naomba jibu zuri na ujue unamjibu Waziri Kivuli na Mjumbe wa Kamati Kuu.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, nimechanganyikiwa kwa sababu swali ninalotakiwa nilijibu ni moja, sijui ni jibu lile la Mbande, niache lile la Kisorya au nijibu la Kisorya niache haya ya Mbande?
SPIKA: Nimekuachia kama Engineer nikajua tu utapata moja la kujibu hapo.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka
Morogoro hadi Dodoma na viunga vya Dodoma huwa zinajengwa kwa kufuata mikataba. Katika ile mikataba kuna
viwango ambavyo vinawekwa kwa mkataba na kutokana na kiwango cha fedha. Kwa hiyo, mimi nimhakikishie
Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba barabara hizi za kutoka Morogoro hadi Dodoma, pamoja na Dodoma Mjini,
tunahakikisha kwamba kile kiwango cha mkataba kinafikiwa. Nichukue nafasi hiyo kuwapongeza watu wa
TANROADS kwa kuhakikisha kwamba wanasimamia kwa kiwango kikubwa na pale inapotokea mkandarasi
aliyetengeneza hajafikia kiwango, hatua bhuwa zinachukuliwa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Napenda niulize swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri shemeji yangu. Hivi tunavyoongea mradi mkubwa wa maji katika Mji wa Bunda unakaribia miaka 10 bila wananchi wa Bunda kupata maji safi na salama, yaani kama mihula ya Mheshimiwa Rais ni mihula miwili. Tatizo kubwa…
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa ni mkandarasi, mkandarasi yule ni mwizi, ana madeni, kila pesa mnayoiweka Serikalini kwa ajili ya kukamilika mradi ule ili wananchi wa Bunda wapate maji safi na salama…
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 tumetenga bilioni 1.6 kwa ajili ya kumpata mkandarasi wa kutengeneza chanzo cha maji. Tumeendelea na shughuli ya kufanya ununuzi wa makandarasi, tukapata makandarasi wabaya, kwa hiyo tumetangaza tena. Hata hivyo, kuhusu hao wakandarasi hao wanaoendelea Mheshimiwa Bulaya nimuahidi kwamba nitaenda huko niende nikawaone. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la wanyama waharibifu ni kubwa sana katika Jimbo langu la Bunda Mjini na Jimbo la kaka yangu Boni. Sisi wananchi wa Mkoa wa Mara hatuhitaji kuomba chakula na mwaka jana Mheshimiwa Waziri wa Sera, Uratibu na Bunge, Mheshimiwa Jenista alikuja akaliona tatizo hilo na Mheshimiwa Waziri mwenyewe anajua, tatizo la tembo kuharibu mazao ya wananchi, kuua wananchi pamoja na mali zao. Sasa nataka kujua, ni lini Serikali mtahakikisha mnakuwa na mkakati wa kudumu wa kumaliza tatizo hili katika vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika Mkoa wa Mara na hasa Wilaya za Bunda, Serengeti, Tarime na Wilaya za maeneo yale kuna kadhia kubwa sana ya wanyama waharibifu wanaotoka hasa katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kuingia katika mashamba na wakati huu ambapo mavuno yanakaribia ndiyo kadhia hii inaongezeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hatua za muda mfupi, mwaka tutachukua hatua ya kuongeza askari na magari ya patrol ili kuhakikisha kwamba kama mwaka jana tunawaokoa wananchi na tatizo hili.
Pili, tunazungumza na washirika wetu wa maendeleo kuona ni namna gani tunaweza kuweka fensi ya kilometa 140 ili kuangalia kwa majaribio kama itakuwa ni suluhisho la tatizo hili.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na mimi napenda niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini na Halmashauri ya Mji ya Bunda Mjini wanataka Hospitali ya Manyamanyama iwe Hospitali ya Wilaya na tayari vikao vya Halmashauri vilishakaa. Tatizo hawana jengo la mortuary na tayari kupitia wadau wameshaanza ujenzi. Je, Serikali haioni kwamba inapaswa kuisaidia Halmashauri ya Mji wa Bunda na hasa ukizingatia Halmashauri ile ni changa kumaliza jengo lile ili sasa ile dhamira ya Hospitali ya Manyamanyama kuwa hospitali ya Wilaya ifanikiwe?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, nilipata manufaa na faida ya kwenda kutembelea Halmashauri ya Bunda nikiwa na ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na kwa bahati mbaya Mheshimiwa Mbunge hakuwepo, angekuwepo tungeenda Manyamanyama tukapata fursa ya kujua nini hasa ambacho kinatakiwa kifanywe ili tuweze kushirikiana. Naomba kwa wakati mwingine tuungane tuone namna nzuri ya kuweza kusaidia ili wananchi waweze kupata huduma.
MHE. ESTER A. BULAYA: Ahsante Mwenyekiti na Mtemi wa Wanyantuzu kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Kwa kuwa dhamira ya Serikali ya kuanzisha benki ya kilimo, ni kwa ajili ya kuinua sekta ya kilimo na kuwasaidia wakulima kwa ujumla ambao ndiyo sekta hiyo ndiyo inayochangia katika ajira pamoja na pato la Taifa. Tunajua, Benki ya Kilimo ….
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo naenda Benki ya Kilimo ina mtaji wa Bilioni 60, ili kufikia malengo ya kuwasaidia wakulima ilikuwa inapaswa kuwa na Bilioni 800, Serikali mkaji-commit kwa kila mwaka kwa miaka minane kupeleka bilioni 100, 100 lakini mpaka hivi tunavyoongea hamjapeleka.
Je, ni lini Serikali sasa mtapeleka fedha hizo kwenye Benki ya Kilimo, ili wakulima wanufaike na benki hiyo na kuhakikisha wanachanigia zaidi katika pato la Taifa na Sekta ya Kilimo kwa ujumla?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jana tu Mheshimiwa Waziri wa Fedha alisema vizuri sana kuhusu Benki ya Kilimo. Kwa hiyo, na Mheshimiwa Ester alikuwepo naamini anakumbuka na Bunge lako Tukufu linakumbuka kwamba dhamira ya Serikali yetu ni kuhakikisha kwanza tunaimarisha ufanisi wa utendaji kazi wa Benki ya Kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Waziri wa Fedha naomba nikope maneno yako uliyoyasema jana; “Kwamba tayari tuko mchakato unaelekea mwisho wa kuhakikisha menejimenti inakaa vizuri ili pesa ya Serikali inayoingizwa kwenye benki hiyo iweze kufanya kazi vizuri na waweze kuwafikia wakulima wetu.” (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nikumbushe Bunge lako Tukufu, nimekuwa nikisema benki hii sasa pamoja na ukakasi uliopo kwenye menejimenti lakini tayari walishaanza mchakato wa kufungua matawi kwenye kanda sita ndani ya Tanzania, hii ikiwa ni dhamira ile ya dhati ya Serikali yetu yakuhakikisha benki hii inawafikia wakulima kule walipo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, dhamira yetu ni ya dhati na ndiyo maana tumechukua pesa kutoka African Development Bank na kuzipeleka benki ya Kilimo. Kwa hiyo, hii bilioni moja, moja kwa miaka nane inayosemwa mbona hatuongelei hizi pesa za African Development Bank. Hizi ni pesa za Serikali pia na ndiyo maana tumepeleka ili kuiwezesha benki yetu iweze kuhudumia wananchi wetu. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Tunajua kuna Halmashauri nyingi mpya na kutangaza Halmashauri mpya ina maana kama Halmashauri ilikuwa moja kuna mgawanyo wa vyanzo vya mapato na kadhalika. Hizi Halmashauri mpya nyingi vyanzo vyake vya mapato ni vidogo ikiwepo Halmashauri ya Mji wa Bunda na huko ambako wewe pia una interest nako barabara nyingi hazipitiki.
Nataka kujua Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha wanapeleka fedha za kutosha kwenye Halmashauri hizi mpya kupitia TANROADS Mikoa ili waweze kuhakikisha barabara zinapitika ikiweko na barabara yangu kutoka Rwahabu – Kinyabwiga na barabara ya kutoka Tairo – Gushingwamara? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo nimeeleza huko nyuma kwamba TANROADS Mkoa siyo wa TANROARD Taifa na wale Wahandisi wa Halmashauri wote sasa nchi nzima, wakae na kuhakikisha zile barabara ambazo zimekatika sasa tunazirudishia, hii ni pamoja na Mfuko wa Barabara ambako fedha zinatoka. Tunajua hizi barabara zingine ni za Halmashauri, zingine za Mkoa na zingine za Kitaifa lakini hii ni dharura, kwa hiyo wote tunashirikiana kwa pamoja ili tuweze kufungua mawasiliano pale ambapo yamekatika.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Mwenyekiti wangu wa zamani wa vijana.
Mheshimiwa Spika, kama ilivyo kwenye majibu yake, anasema moja ya mikakati ni kuhakikisha wanafanya doria imara; ni jambo zuri kabisa. Sasa huwezi kufanya doria imara kama huna magari mazuri.
Mheshimiwa Spika, katika Wilaya ya Bunda kuna magari mawili na mabovu na ndiyo ambayo yanatakiwa yafanye doria kwenye Jimbo la Kangi na Jimbo la Boni. Sasa uhalifu unazidi kuongezeka.
Mheshimiwa Spika, maswali yangu, katika kuhakikisha
hiyo doria imara kama Mheshimiwa Waziri amejibu, je, Serikali iko tayari sasa kutupatia gari jipya ili kupunguza vitendo vya uhalifu kwa kufanya hiyo doria imara? (Makofi)
Swali la pili, ili kuweza kukabiliana na hizi changamoto, moja ya vituo ambavyo vipo hohehahe ni Kituo cha Polisi cha Bunda. Sasa wameanza mradi wa ujenzi wa jengo la upelelezi kupitia michango ya polisi, ya wadau, nami Mbunge wa Jimbo kupitia Mfuko wa Jimbo nimewachangia. Serikali mpo tayari kuungana na jitihada zetu kukamilisha jengo hilo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, kuhusiana na suala la magari, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba tumepokea changamoto yake ya magari. Wakati ambapo magari yatapatikana tutatoa kipaumbele kwa Jimbo lake ili tumpatie gari la ziada ili aweze kuongeza nguvu ya yale magari machache yaliyopo sasa hivi.
Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ni suala la ujenzi
wa kituo cha upelelezi. Kwanza nachukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kuamua kutoa fedha za Mfuko wake wa Jimbo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha polisi. Natambua kwamba Mfuko wa Jimbo una fedha kidogo na Majimbo yetu yanachangamoto nyingi. Kwa hiyo, kitendo cha Mheshimiwa Mbunge kuamua kwamba sehemu ya fedha hizo ziende kwenye ujenzi wa vituo vya polisi ambavyo vina changamoto kubwa ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Ester kwamba jitihada zake pamoja na za wananchi zimezaa matunda, kituo hicho kimekamilika, tunatarajia wakati wowote mwaka huu tutakizindua. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwanza ninachoweza kusema Mheshimiwa Waziri katika mgawanyo takwimu wamekuongopea, Halmashauri yangu imepata walimu ambao hawafiki hata 60; ni 58 tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ninalotaka kusema, hao wanane Bunda sisi hawatutoshi. Hisabati mahitaji ni 55 waliopo 20 peke yake, fizikia mahitaji 27 waliopo 10 peke yake, biology mahitaji 32 waliopo 15 chemistry kidogo
ndio mmejitahidi mahitaji 29 waliopo 21 bado wanane. Ukiangalia yaani hao tuliogawanywa na mahitaji kwa ujumla wake ni 68. Ni lini Serikali mtatupa Bunda walimu wa sayansi? Tumechoka Bunda kuwa miongoni mwa Wilaya zinazofanya vibaya katika masomo, swali la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, tunajia TEA ina- deal na masuala ya infrastructure. Hivi kwa nini Serikali msitenge fedha za kutosha, mkawapa TEA wakajenga pia na nyumba za walimu mbali na kwamba kuna changamoto kwenye shule za walimu ili pia walimu wawepo shuleni kuepuka usumbufu ambao unajitokeza na kusababisha watoto kufeli halafu hatimaye tunalaumiana mnaanza kuwafukuza wao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upungufu wa walimu uliopo katika shule za Jimbo lake; ni kweli kwamba kuna upungufu wa walimu wa sayansi nchi nzima na ndiyo maana katika jibu langu la msingi nimeeleza mikakati iliyopo ya kuhakikisha kwamba, tunaondokana na upungufu huo.
Kwa hiyo, naomba nimhakikishie tu kwamba tunafahamu kwamba kuna upungufu na si kwake tu. Kwa hiyo tutaendelea kuhakikisha kwamba, upungufu huo unafanyiwa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) kujiingiza zaidi katika kujenga shule za walimu, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kutegemeana na bajeti ambayo TEA wanatengewa ambayo kimsingi kwa miaka mitatu sasa mfululizo wanatengewa shilingi bilioni 10, itaendelea kujenga nyumba za walimu, lakini ikumbukwe kwamba jukumu hasa la TEA ni suala la kuongeza ubora, lakini vilevile kuhakikisha kwamba kuna upatikanaji wa elimu na suala la usawa yaani access, equity na quality.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, TEA haikuundwa ili ichukue majukumu yote ya miundombinu za shule katika Halmashauri zetu. Jukumu la kujenga miundombinu katika shule ambazo ziko chini ya Serikali za Mitaa litabakia kuwa jukumu la Serikali za Mitaa.
Kwa hiyo, nimuombe Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wote kwa sababu sisi wenyewe ni Madiwani tuendelee kuwahamasisha wananchi washirikiane na Serikali kujenga miundombinu kwa ajili ya shule za msingi na shule za sekondari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini TEA vilevile na hasa nyie Waheshimiwa Wabunge mkiwaongezea bajeti kwa sababu nyie ndiyo hasa mnaongeza bajeti itaendelea kufanya hayo kuhakikisha kwamba kunakuwa na usawa, ubora lakini yale maeneo ambayo yatakuwa na upungufu yaweze kupatiwa kipaumbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nieleze utaratibu kwamba ukiacha mbali la Halmashauri yenyewe kuomba TEA waweze kupatiwa fedha kwa ajili ya ujenzi lakini vilevile Wizara kwa kushirikia na Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunakusanya takwimu, kwa hiyo, tunajenga miundombinu kulingana na takwimu ambazo tumepata za nchi nzima. Nashukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Katika Mkutano wa World Heritage ambao ulifanyika nchini Qatar, Pori la Akiba la Selou na lenyewe lilitangazwa kama urithi wa dunia na nchi mbalimbali zilikubaliana kuisaidia Tanzania takribani dola milioni mbili kwa ajili ya kupambana na ujangili wa tembo. Nataka kujua status ya hali ya ujangili wa tembo katika Pori la Akiba la Selous?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa sasa hivi hali kidogo ni nzuri, hakuna tena ujangili kama ambavyo umekuwepo na ndiyo maana matukio mbalimbali yale ambayo tulikuwa tunapotelewa na tembo na maeneo mengine yamepungua kwa kiwango kikubwa sana katika hili eneo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kuniona.
Kati ya wakulima wanaopata taabu kwa kulaliwa bei na watu ambao hawana soko la uhakika ni wakulima wa pamba. Kwa sababu wanunuzi wengi wanalangua na wanapanga bei wanayoitaka wao na mwisho wa siku wakulima wanapata hasara.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu ni kwamba, ni lini Serikali itawatafutia wakulima wa pamba soko la uhakika ili na wenyewe waweze kunufaika na kilimo cha pamba? (Makofi)
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba tu nitofautiane kidogo sana na Mheshimiwa Bulaya kuhusu uhakika wa soko. Soko la pamba ni la uhakika na hatujawahi kuwa na tatizo la kuuza pamba nchini. Pamba ni bidhaa inayouzwa na nchi nyingi duniani.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, soko la Tanzania haliwezi kuwa tofauti na Soko la Dunia la Pamba. Majadiliano yanapofanyika kati ya wadau na wauzaji, ni zao pekee ambalo kwa msingi wadau wanajadiliana na wanunuzi, wanafikia muafaka wa bei. Hii inakuwa pegged kwenye bei ya pamba katika Soko la Dunia.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, bei inayopatikana siyo kwamba inawalalia wakulima, lakini pia inawapa faida wafanyabiashara na wakulima wanapata haki yao kutegemea na soko la dunia lilivyo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa Wabunge wenzangu watakubaliana na mimi kwamba hakuna mtu anayeunga mkono uvuvi haramu na sisi tunaotoka Kanda ya Ziwa tumekua kutokana na samaki. Kitu ambacho tunahoji ni namna gani hii operesheni watu wasiowatakia mema wananchi wetu wanavyoiendesha.
Mheshimiwa Spika, nilimwambia Waziri Jimboni kwa Mheshimiwa Kangi watu walienda kuvunja mafriji (fridges) ma-frizer (freezers) na kuwakamata wale watu na kuchukua pesa zao kinyume na utaratibu. Hivi navyoongea jimboni kwangu juzi Polisi wamewavamia akina mama na kuwapiga mabomu wakishirikiana na Mkuu wa Wilaya. Swali langu, hivi ni kweli operesheni yenu inalenga kunyanyasa watu na mnatoa tamko gani kwa watu ambao wanafanya vitu vya namna hii? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, kwanza natoa shukrani kubwa sana kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuwa Bunge zima limetuunga mkono juu ya suala linalohusu uvuvi haramu, kwa sababu uvuvi haramu ni uharibifu wa maliasili za nchi yetu.
Mheshimiwa Spika, swali lake linahusu ni kwa nini watu wanaotekeleza jukumu hili la operesheni dhidi ya uvuvi haramu wananyanyasa wananchi. Kwa heshima kubwa na taadhima nataka niseme kwamba tunachokifanya tunakiita kwa kifupi Operesheni Uvuvi Haramu, lakini sisi tunakwenda mbele zaidi na kupambana na biashara haramu ya mazao yanayotokana na uvuvi.
Mheshimiwa Spika, kesi anayoisema Mheshimiwa Ester Bulaya ni maalum, kwamba kuna tatizo la wananchi katika jimbo lake au jimbo la Mheshimiwa Kangi Lugola wamenyanyaswa katika mafriji yao. Naomba nimhakikishie kwamba Serikali ipo kuanzia katika ngazi za Wilaya, sisi tuko tayari kupokea malalamiko yote yanayohusu specific cases na kuyashughulikia.
Mheshimiwa Spika, nataka nimwambie tumewatuma kufanya kazi ya kudhibiti uvuvi haramu na biashara haramu ya mazao ya uvuvi na siyo kuwanyanyasa watu. Kwa hivyo, kama ipo kesi maalumu inayohusu mtendaji wetu amenyanyasa mtu, sisi tuko tayari kupokea kesi hiyo, kuichukulia hatua na hata kumchukulia hatua Mtendaji yeyote atakayethibitika kwamba amefanya vitendo vya uvunjifu wa maadili kwa kuwaonea Watanzania.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwanza niwapongeze vijana wote wa JKT wanaoendelea kujitolea. Kumekuwa na malalamiko ya kubaguliwa katika upande mzima wa suala la kupewa ajira kwa vijana wanaomaliza JKT hasa ajira ambazo zimetokea kwenye Jeshi la Polisi na hasa katika Operesheni ya Jakaya Kikwete.
Sasa swali langu, nini tamko la Serikali kuhusiana na tabia hii ya kibaguzi, na wapo vijana wa jimboni kwangu?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Ester Bulaya kwa kuamua kwa makusudi kujiunga na Mfunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa akiwa hapa Bungeni, pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la malalamiko ya ubaguzi wakati wa ajira, nataka nimfahamishe kwamba mara zote kuna kuwa kuna uhaba wa idadi ya vijana wanaoajiriwa ukilinganisha na wale walioko kwenye kambi. Kwa mfano katika kipindi kilichopita jeshi la Ulinzi liliajiri vijana 2,000 kati ya vijana 9,000 waliokuwepo kule; bila shaka wale 7,000 wataona kwamba wamepaguliwa, lakini ukweli ni kwamba nafasi zinakuwa chache wakati wao wako wengi. Ni kweli hivi karibuni Jeshi la Polisi lilitoa ajira, lakini vile vile idadi ya vijana walioajiriwa ni chache sana ukilinganisha na vijana waliokuwepo katika Kambi za JKT.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wakati mwingine vigezo vya ajira vinaweza vikafanana lakini kwa sababu ya idadi imekuwa ndogo basi kuna wengine bilashaka wataachwa ndiyo hayo yanasababisha malalamiko.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kuna mgogoro unataka kufukuta katika Jimbo langu kwenye Kata ya Nyatwali inayojumuisha wakazi zaidi ya 11,000. Lile sio Pori la Akiba ni maeneo yao ambayo wanaishi, inasemekana Serikali inataka kuwahamisha haijawashirikisha, hawajui wanaenda wapi na wanalipwa nini. Nini tamko la Serikali kuondoa hili tatizo kwa sababu mna migogoro mingi msitengeneze migogoro mingine na Bunda hatutakubali.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nampongeza kwa jinsi ambavyo anawateea wananchi wake. Niseme tu kwamba mpaka sasa hivi hatuna taarifa rasmi kwamba tunataka kuihamisha hiyo Kata ya Nyatwali. Kwa hiyo, kama kuna fununu za namna hiyo lazima zitazingatia taratibu na sheria zote zilizopo kuhakikisha kwamba wananchi wanashirikishwa kikamilifu na viongozi wote wanashirikishwa ndipo hapo wananchi wanaweza kuhamishwa. Kama wananchi watakuwa waliingia kinyume na taratibu hapo ndiyo lazima nguvu zitatumika lakini kama siyo hivyo nikuhakikishie tu kwamba wananchi watashirikishwa vizuri kabisa ili kuhakikisha kwamba sheria inazingatiwa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Waziri katika majibu yake wataalam wanajibu kana kwamba bado Halmashauri ni moja lakini tuna Halmashauri mbili; Halmashauri ya Wilaya ina majimbo mawili ya Mwibara kwa Mheshimiwa Kangi na Bunda kwa Mheshimiwa Boniphace; Halmashauri ya Mji ina Jimbo moja tu la Ester Bulaya, Bunda Mjini. Sasa haya majibu waliyompa ni ya enzi zile za babu, za Wasira, sio kipindi hiki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nauliza maswali yangu mawili ya nyongeza. (Kicheko)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipofanya ziara kwenye Jimbo langu la Bunda alitembelea Kikundi cha Igebesabo kilichopo Kata ya Nyatwali ambacho kina mradi mkubwa wa umwagiliaji uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 700. Pale wana changamoto ya mashine kubwa ya kusukuma maji ambayo yanatoka Ziwa Viktoria aliwaahidi atawasaidia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini ahadi hii itatekelezwa kwa sababu pia katika hicho kikundi kuna vijana kama wewe Mheshimiwa Waziri?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, Idara ya Umwagiliaji ina changamoto nyingi ikiwepo ya bajeti na vitu vingine, lakini kwa sasa hivi hawana gari la kuweza kufanya patrol katika miradi mbalimbali ya umwagiliaji katika Wilaya nzima ya Bunda. Ni lini sasa watawapatiwa gari ili sasa kilimo cha umwagiliaji Bunda kiweze kushamiri na vijana wengi graduates sasa hivi wamejiajiri wenyewe kwenye shughuli za umwagiliaji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze kwa maswali mazuri lakini kubwa ambalo nataka nimhakikishie, ahadi ni deni. Kwa kuwa hii ni ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo katika kuhakikisha tunaitimiza kwa wakati ili wananchi wake, kwa maana ya kile kikundi, waweze kupata mashine hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala zima la gari, ili mradi uwe bora na wenye tija kwa wananchi lazima kuwe na usimamizi na ufuatiliaji wa karibu. Kwa hiyo suala la gari ni jambo la muhimu sana. Niagize wataalam wetu wa Bunda kufuatilia kitendea kazi hiki na sisi kama Wizara ya Maji tutatoa ushirikiano wa dhati kabisa katika kuhakikisha kinapatikana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto katika utekelezaji wa mradi wa REA pia ni upatikanaji wa nguzo. Katika Jimbo la Bunda Mjini ni lini sasa nguzo zitafika katika maeneo ya Bunda Store, Nyamswa, ambapo katika Kitongoji cha Zanzibar pamoja na Nyabeu Sazila ili wananchi wahakikishiwe kupata umeme wa uhakika kwa sababu tatizo kubwa la maeneo hayo ni nguzo? Ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini, Mheshimiwa Esther Bulaya, juu ya masuala ya upatikanaji wa nguzo katika maeneo ambayo ameainisha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme Mkandarasi DEM yuko site anaendelea na kazi. Kama changamoto ilikuwa ufunguaji wa Letter of Credit kwa ajili ya kuagiza vifaa kwa wingi, tumeshawafungulia Wakandarasi wote; na kwa kuwa pia viwanda vya kuzalisha nguzo ambavyo viko ndani ya nchi, tumekutana navyo na nguzo zipo. Kwa mfano, hapo Kuwaya Iringa, Saw Mill Iringa na tumefanya uhakiki kwamba nguzo za kutosha zipo. Rai yangu kwa wakandarasi wote, waagize hivyo vifaa kwa wakati ili kusiwe na visingizio. Nakushukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.
Kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri mambo mengi wamekuongopea humu, siyo Wilaya wala Halmashauri ya Mji ambayo imewahi kunufaika na chochote kutokana na Mbuga ya Serengeti. The way walivyokujibu kama Bunda, kuna Halmashauri moja. Hivi vijiji vyote viko kwenye Halmashauri ya Mji na asubuhi nimetoka kuongea na Mkurugenzi na Mhasibu hatujawahi kupata hata shilingi moja. Ni lini sasa tutapata hii asilimia 25 ya tozo za uwindaji? Swali la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, wananchi wanaozunguka Mbuga ya Serengeti katika Jimbo langu wamekuwa wakipata tatizo kubwa sana la tembo kuharibu mali zao na Mheshimiwa Jenista ameshajionea uharibifu huu. Takribani wananchi 880…
...kati ya hao waliolipwa ni 330 tu, bado watu 550 hawajalipwa kifuta jacho japo kidogo. Ni lini sasa watalipwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba ni kweli kabisa Wilaya ya Bunda ina Halmashauri mbili na haya majibu sisi tunayoyatoa tunatoa katika Wilaya, siyo katika Halmashauri. Tunatoa katika Wilaya nzima, tunazungumzia Wilaya. Kama ingekuwa kwamba labda inatakiwa tuangalie kwenye Halmashauri, basi majibu hayo yengefanana. Hayo majibu niliyoyasema na hizo fedha ambazo nimezisema ni zile zilizoletwa katika Wilaya nzima ya Bunda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nijibu maswali yake kama ifuatavyo; kwa asilimia 25 na kwa kuwa Halmashauri yake ya Mji ina vijiji vinavyopakana na haya Mapori ya Akiba na hizi fedha nilizosema zimeshapelekwa, kama bahati mbaya Halmashauri yake haijapata mgao, basi tukitoka hapa nitafuatilia kuhakikisha ule mgawanyo unakwenda katika vijiji vyote vinavyohusika. Kwa hiyo, hilo nitalifanya. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, naomba nirekebishe kidogo takwimu, kwa takwimu sisi tulizonazo Mheshimiwa Mbunge, katika Wilaya ya Bunda, kifuta jasho kilicholipwa ni kwa wahanga 1,127 ambao jumla ya shilingi 186,333,350 zimelipwa kama kifuta jasho. Shilingi milioni moja zililipwa kama pole kwa mhanga mmoja ambaye alipoteza maisha.
Kwa hiyo, suala la kusema kwamba hazijatolewa, zimetolewa na katika list niliyonayo mpaka sasa hivi nimeangalia kama Bunda kuna wahanga ambao wanadai, bado sinayo. Kwa hiyo, kama wapo ambao bado wanadai, naomba hiyo list tuipate ili tuweze kuifanyia kazi kusudi waweze kulipwa mara moja. (Makofi)
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri na Mheshimiwa Spika wewe ni shahidi, huu mradi ni wa muda mrefu sana zaidi ya miaka 11. Miaka mitatu mizima tunazungumzia suala la chujio, si sawa kwa wananchi wa Bunda na Mkoa wa Mara. Naomba niulize maswali yangu mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, mbali na changamoto za wakandarasi kutokulipwa, mbali na changamoto za wakandarasi kuondoka site, Mamlaka ya Maji ya Mji wa Bunda kupitia vyanzo vyake vya ndani vimeanza kusambaza mitandao ya maji. Sasa nilitaka kujua Serikali mna mkakati gani wa kusaidia jitihada hizi za mamlaka ya maji Mji wa Bunda mbali na kwamba, haipati ruzuku Serikalini, kuendelea na zoezi la usambazaji wa miundombinu ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwepo Manyamanyama, Bunda Store, Gerezani, Olimpas, Sazila; Serikali lini mtahakikisha hii mitandao ya maji yanafika kwenye maeneo hayo ambayo hakuna kabisa?

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili; Mheshimiwa Naibu Waziri unajua Mamlaka ya Mji wa Bunda, Halmashauri yetu ya Mji wa Bunda ni Mpya. Tumekuta kuna madeni ya umeme ambayo mwisho wa siku takribani milioni 603 hayo tumerithi. Mamlaka yangu ya Mji wa Bunda inalipa bili current bili inalipwa, lakini haya madeni yamerithiwa kupitia halmashauri iliyopita tangu Mzee wangu Wassira. Wizara mna mkakati gani kuhakikisha hli deni linalipwa, ili umeme usikatwe wananchi waweze kupata huduma ya maji maana wao ndio wanaoathirika na bili inalipwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, cha kwanza nataka nikiri kwamba, moja ya changamoto kweli tuliyokuwanayo ilikuwa wakandarasi wababaishaji, lakini uanzishwaji wa RUWASA mmekwishatupa rungu sisi viongozi wa Wizara ya Maji, hatuna sababu hata moja ya kulalamika. Tutachukua hatua kwa mkandarasi yeyote ambaye atataka kutuchelewesha katika kukamilisha miradi yetu ya maji.

Mheshimiwa Spika, kikubwa kutokana na mradi ule Mheshimiwa Waziri amekwishatoa agizo kwamba, mradi ule sasa tutatekeleza kupitia wataalam wetu wa ndani katika kuhakikisha tunawapa uwezo Mamlaka ile ya Bunda kwamba, tutatoa milioni 375 na wataalam wetu wa ndani wataukamilisha mradi ule kwa haraka. Na kazi iliyobaki ni wataalam wetu wa mamlaka sasa kuwaunganishia wateja wao, ili waweze kupata huduma hii ya maji.

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala zima la ukatikaji wa umeme na madeni yaliyopo, hii ni Grade C mamlaka yao. Sisi kama Wizara yetu ya maji tumeona haja sasa ya wao kulipa kidogo na sisi tuweze kuwaongezea ili katika kuhakikisha tunakamilisha deni lile na wananchi wa Bunda waendelee kupata huduma ya maji. Pia natambua kwa Mheshimiwa Kangi Lugola kukamilika kwa mradi huu maeneo ya vijiji jirani kwa maana ya Buzingwe, Bulamba na Kabainja nao watapata huduma ya maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Esther Bulaya kukamilika kwa mradi huu utafanya maamuzi sahihi sasa ya kurudi nyumbani, ahsante sana.
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali dogo la nyongeza. Najua mradi wa Maji Bunda ni wa muda mrefu na nimeushughulikia sana, hilo halina ubishi. Najua tatizo sasa hivi siyo maji kutoka kwenye chanzo kule Nyabehu, tayari sasa hivi maji yanakuja. Tatizo kubwa ni mtandao wa kuhakikisha wananchi wengi wa Bunda Mjini wapate maji safi na salama. Sasa, ni lini Serikali watahakikisha wanasambaza mtandao mkubwa wa maji na kuunga mkono juhudi zangu kwa kutenga fedha za Mfuko wa Jimbo kuwasaidia kutandaza huo mtandao ili wananchi wa Bunda kwenye kata zote 14 wapate maji safi na salama, ni lini?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Bulaya kama ifuatavyo:

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda atambue kwamba Serikali imefanya jitihada kubwa sana katika Jimbo lake la Bunda, tuna utekelezaji wa mradi zaidi ya bilioni 10, huo unaendana sambamba kabisa na utandazaji wa mtandao wa maji. Kikubwa ambacho ninachotaka kumhakikishia, Serikali hii ya Awamu ya Tano tutahakikisha kazi ile inakamilika kwa wakati na wananchi wake waweze kupata huduma hii muhimu sana ya maji.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza, wnanchi wa Jimbo la Bunda Mjini na Wilaya ya Bunda kwa ujumla walikubaliana kwamba hospitali ya Manyamanyama iwe hospitali ya Wilaya. Lakini kuna baadhi ya mambo ambayo hospitali hiyo haina pamoja jokofu la kuhifazia maiti. Wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini wanapata tabu kupeleka maiti Nyamswa Jimbo la Bunda.

Sasa ningependa kujua ni lini Serikali itapeleka jokofu katika hospitali ya Manyamanyama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, ni kweli maneno yako yako ya utangulizi yanafaa sana ndiyo maana tufanye mabadiliko makubwa katika eneo hili ikiwa na Wabunge wanaopatikana wakatI wote Bungeni kusemea watu wao kama Mheshimiwa Ester Bulaya.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba kwanza Bunge imepata Kituo cha Afya ni suala la kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano ya Dkt. John Pombe Magufuli tumepata hospitali pale inajenga katika eneo hili lengo ni kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali hii. Mheshimiwa sema Mheshimiwa hoja yako imepokelewa tuangalie uwezo wa Serikali tupeleke jokofu katika eneo hili ili maiti ikipatikana pale basi iweze kuhifadhimiwa eneo la karibu na kupunguza gharama zausafirishaji wa ndugu wa marehemu, ahsante sana.
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba niulize swali dogo la nyongeza, najuwa kuna ujenzi wa barabara kutoka Mbezi Mwisho ile ya Kimara, Goba, mpaka Makongo mpaka kutokea Survey. Sasa kwa upande wa Goba tayari huu mradi umekamilika kwa upande wa Jimbo la Kawe kumejengwa kilometa moja na ninajua Mheshimiwa Naibu Waziri kuna bilioni nne za TARURA kwa ajili ya fidia sasa hivi ule mradi kwa upande wa Jimbo la Kawe umesismama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitaka kujuwa ni lini sasa kwa upande wa Kawe kuanzia kwenye mpaka wa Goba mpaka Survey utakamilika kwa sababu wananchi tayari wako tayari kutoa maeneo yao kwa sababu hii barabara kwa kweli haipitiki na inawasaidia sana wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kupunguza foleni? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge atakubaliana na mimi kwamba kazi kubwa sana kazi nzuri sana imefanyika kupunguza msongamano katika jiji la Dar es Salaam na ninafahamu pia kwamba Mheshimiwa Mbunge unafahamu kumekuwepo na changamoto baadhi ya watu kunapokuwa na harakati za kulipa fidia wanakuwa na mahitaji labda kuna mambo kadhaa wa kadha kwa sababu hiyo saa nyingine inatuchelewesha kwamba kukamilisha ili tuendelee.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu hiyo Serikali ilikuwa inafanya juhudi za kuhakikisha kwamba kwanza eneo la fidia linakaa vizuri kwamba watu wote wanaridhika watu wote wanakuwa wamelipwa ili mradi uweze kuendelea kwahiyo nikusihi Mheshimiwa Mbunge uvute subira lakini pia endelea kuamasisha wananchi hawa ambao saa nyingine wanaweka pingamizi kidogo kwenye maeneo yao wanatuchelewesha kwenye mradi. Kwa hiyo, tukimalizana na wananchi tutaenda kumalizia eneo hilo kufanya ujenzi wa lami uweze kukamilika maeneo yote ambayo tayari tumeshakuwa na mkataba. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu mazuri ya dada yangu; kwa sababu ameji-commit kwamba mnafanya utafiti ili kuona gharama halisi ambazo zitasababisha mfufue.

Mheshimiwa Spika, sasa nina maswali mawili ya nyongeza. Kwanza Bunda tulikuwa tuna Ginnery tano ambayo ni Kibara, Ushashi, Mara Rint, Bulamba na Olam na zinazofanya kazi ni mbili. Tatu ukiwepo na Ushashi hazifanyi kazi zinafanya kazi Olam na Bulamba lakini Mara Rinti ni nzima na ina kila kitu tatizo lake ni mwekezaji. Sasa ni lini Serikali mtatafuta mwekezaji ili hii Ginerry ya Mara Rinti ifanye kazi na ipo kwenye eneo very strategic na ikifanya kazi itapunguza changamoto ya ajira kwa akina mama na vijana wa Jimbo la Bunda Mjini na Wilaya nzima ya Bunda kwa ujumla.

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Mara tuna kiwanda cha nguo, kipo Musoma. Hata hivyo sasa hivi hiki kiwanda hakifanyi kazi kwa ufanisi na ukiuliza changamoto kubwa kwa nini kiwanda hiki hakifanyi kazi; na kuwepo kwa kiwanda hiki ni kutokana na malighafi ile ya pamba iliyopo kwenye Mkoa wetu wa Mara na maeneo jirani. Sasa nimeuliza changamoto ni mtaji, na kama hakifanyi kazi kwa ufanisi ina maana kunapunguza ajira kwa wafanyakazi.

Mheshimiwa Spika, sasa ningependa kujua, ni lini Serikali Mtaongeza mtaji ili akina mama, vijana na wazee wa Mkoa wa Mara wanufaike kwa ajira kutokana na kuwepo kwa kiwanda hiki katika Mkoa wa Mara?

Sasa ningependa kujua ni lini Serikali mtaongeza mtaji ili wamama, vijana na wazee wa Mkoa wa Mara wanufaike kwa ajira kuwepo na kiwanda hiki katika Mkoa wa Mara? Ahsante.
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo;

Mheshimiwa Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Naibu Waziri kwa kujibu vizuri swali la msingi. Serikali imeona umuhimu wa kufanya uchambuzi katika kutekeleza Sera ya zao la pamba ya cotton to cloth kwa hiyo, lipo zoezi la kuhakikisha tunachambua na kuangalia namna bora ya kufufua ginnery zote za pamba kwa sababu value chain ya cotton to cloth inaanzia kwenye ginnery kufanya kazi mpaka kwenye textile industries.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Bulaya kwamba hata kiwanda cha MUTEX kiko sehemu ya hili zoezi. Nimeshafika kwenye kiwanda hicho na ninakuhakikishia katika zoezi hili tutafia pia kwenye ginnery hizi ulizozitaja na tunashirikiana na Wizara ya Kilimo kuhakikisha zoezi hili linafanyika haraka sana iwezekanavyo. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ambayo kuna wavuvi ni pamoja na Jimbo la Bunda Mjini, wapo wavuvi ambao wanavua kupitia Ziwa Victoria. Hakika vijana wengi wa Jimbo la Bunda Mjini wamehamasika kujiajiri wenyewe kupitia Sekta ya Uvuvi lakini changamoto ni zana za uvuvi nyavu pamoja vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa Serikali inijibu ili kuwapa moyo vijana ambao wameamua kujiajiri wenyewe kutokana na uvuvi kupitia Ziwa Victoria, ni lini sasa watawawezesha mitaji ili waweze kuvua kisasa waache ugomvi na DC Bupilipili ambaye anawakamata kila siku?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inayo progamu kama nilivyojibu katika majibu ya msingi ya kuwawezesha wavuvi. Kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, moja ya jambo ambalo tuliligundua ni kwamba wavuvi na hata wafugaji wetu hawakopesheki. Ndiyo maana vijana wengi wanaojihusisha na shughuli hizi wamekosa fursa ya kuweza kupata mikopo na hatimaye kuweza kuboresha shughuli zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, sababu kubwa za kukosa mikopo zipo mbili; ya kwanza mabenki yanataka dhamana na pili ni bima kwa maana shughuli za mifugo na uvuvi hazina bima. Nataka niwahakikishie Wabunge wote wa Bunge hili Tukufu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzana, Wizara imefanya kazi nzuri na sasa mabenki yametukubalia.

Naomba nitoe shukrani zangu za dhati kwa Benki ya Posta Tanzania imefungua na kuanzisha Akaunti Maalum ya Wavuvi (Wavuvi Account) yenye lengo mahsusi la kuweza kuwasaidia kwa unafuu sana wavuvi wote. Kwa hiyo, nitawaelekeza Benki ya Posta waje pale Bunda Mjini waweze kuwapata vijana na waweze kushirikiana nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili la pili la dhamana, tumefanya kazi kubwa ya kuhakikisha tunalishawishi Shrika letu la Bima la Taifa na limekubali mwezi huu wa pili tutasaini nao mkataba maalum utakaowawezesha sasa kuwa na bima ya mifugo na uvuvi. Hii itakuwa ni hatua kubwa sana kuelekea katika kuhakikisha wavuvi na wafugaji wetu wote wanaweza kupata mikopo katika benki kama vile ambavyo wanaweza kupata Watanzania wengine baada ya kuwa na uhakika wa dhamana na bima.
MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi tunajua moja ya Serikali kuwa na mikakati ya mipango bora ya ardhi ni pamoja na kuzuia watu kujenga mabondeni na pamoja kwenye mikondo ya mito na Serikali ilianzisha operesheni ya kubomoa nyumba za watu ambao wamejenga kwenye mikondo ya mito na hili ni tangu Bunge lililopita Mheshimiwa Lukuvi nadhani analijua na amebomoa nyumba nyingi tu kule Kawe lakini kuna nyumba ya kigogo mmoja tu ameiacha na wamekuwa wakitoa ahadi humu ndani hiyo nyumba itabomolewa. Nataka kujua ni lini ile nyumba itabomolewa?
WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge wa Bunda Mjini kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali imekuwa inachukua hatua za mara kwa mara na nikisema Serikali maana yake kwa umoja wetu na wasimamizi wa sheria zote za mipangomiji ni mamlaka ya upangaji ambayo ni halmashauri yenyewe. Ukisikia operesheni ya vunja vunja au kuondoa watu waliojenga kinyume cha sheria katika halmashauri fulani, ujue inaendeshwa na halmashauri ambayo ndiyo yenye mamlaka na hata ile enviction order ya kwenda kuwavunjia haitolewi na Wizara yangu, hapana inatolewa na Afisa Ujenzi wa Wilaya. Kwa hiyo mazoezi haya yamekuwa yanafanyika katika wilaya mbalimbali ili kuwaondoa watu ambao wamevunja sheria naamini ni kweli katika wilaya mbalimbali ikiwepo Dar es Salaam Kinondoni operesheni kama hizo zimeendeshwa kwenye bonde la Msimbazi kwa watu ambao wamevunja sheria.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninachoomba tu ni kwamba wananchi wazingatie sheria. Wasijenge bila vibali, wahakikishe kwamba kila wanapojenga wanajenga maeneo ambayo siyo hatarishi, wanafuata sheria ili angalau hatua kama hizi zinazozungumzwa na Mheshimiwa Mbunge zisiwapate. Hilo ndilo ombi langu.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi tatizo la kusuasua kwa miradi ya barabara Mkoa wa Mara halijaanza kwenye Bunge hili tu, tangu Bunge lililopita na Wabunge wa Mkoa wa Mara kujali itikadi zetu katika vikao vyetu tumekuwa tukionesha uhitaji wa miradi hii kukamilika mapema. Issue ya mradi wa Natta - Mgumu - Serengeti ni wa muda mrefu na unafanana kabisa na mradi wa ujenzi wa barabara kutoka Kisolya - Bunda - Nyamuswa na wenyewe umekuwa ukisuasua mbali na tatizo la wakandarasi, lakini tatizo kubwa ni Serikali kutopeleka pesa ili miradi hii ikamilike haraka.

Sasa ni lini Serikali itapeleka pesa za kutosha barabara hizi za muda mrefu takribani miaka 10 ziweze kukamilika?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Spika, kwanza nimuombe Mheshimiwa dada yangu Ester Bulaya kwamba hata hiki kinachofanyika na kwa sasa na kwa kasi hii angalau aone shukrani, aweze kushukuru kwa sababu niseme kazi kubwa inafanyika barabara hii ya Bulamba - Kisolya ni muda mrefu imekuwepo na kumekuwa na changamoto nyingi. Zipo changamoto ambazo zimekuwa kwa upande wa mkandarasi na zipo changamoto ambazo zimekuwepo kwa upande wa Serikali.

Mheshimiwa Spika, lakini nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali sasa ipo kazini, Serikali sasa inafanya kazi nzuri na wiki iliyopita mkandarasi huyu kwa miradi ambayo anaendelea amelipwa zaidi ya bilioni tano. Nitumie nafasi hii niishukuru sana Wizara ya Fedha. Sasa kazi yetu kubwa ni kusimamia yale ambao yalikuwa saa nyingine tunaona kwamba tumekuwa na madeni mengi, lakini wakandarasi wote nchini wamelipwa sasa tupo current tunaenda vizuri.

Kwa hiyo, Mheshimiwa Ester nenda Bunda uone kazi inavyoendelea na tumepokea wiki mbili tu zilizopoita zaidi ya shilingi bilioni 184 kwa ajili ya kulipa wakandarasi nchi nzima. Kwa hiyo kwa upande wa Serikali tupo vizuri, Wizara ya Fedha inafanya vizuri na sisi kwenye usimamizi tuko vizuri.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kweli kwa sababu unaona tunaanza mradi wa kutoka Bulamba kuja Bunda kwenda Nyamuswa kilometa 56 na Bunge lako limetenga fedha kuhakikisha kwamba mradi huu nao unaenda.

Mheshimiwa Spika, niseme kama nilivyosema mwanzoni kwamba ipo mradi mingi, ipo mradi mzuri iko hatua katika Mkoa wa Mara, miradi mingi inaendelea kutekelezwa, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Pamoja na changamoto za maji na umeme katika shule zetu kumekuwa na tatizo kubwa sana katika shule nyingi nchini hasa Mkoa wa Mara pamoja na Jimbo la Bunda Mjini; tatizo la matundu ya vyoo. Athari kubwa ni kuleta magonjwa ya mlipuko kwa wanafunzi wetu pamoja na shule kufungwa. Sasa ningependa kuiuliza Serikali, ina mpango gani wa kushirikiana na taasisi mbalimbali katika kuhakikisha kwamba matundu ya vyoo yanajengwa shuleni ili kuwafanya wanafunzi wetu wasome wakiwa katika hali ya usalama zaidi wasipate magonjwa ya mlipuko?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya Mbunge wa Bunda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba tuna upungufu mkubwa sana wa matundu vyoo nchi nzima kwa shule za msingi na sekondari.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili linapaswa kuwa jambo shirikishi, haiwezi kuwa kazi ya Serikali peke yake. Serikali imetoa Waraka ambao umeanza kutumika, wa mwaka 2016 ambao unaonesha namna ambavyo wadau mbalimbali wakiwepo na wananchi wa kawaida wanaweza kushirikiana kuweza kupunguza changamoto za miundombinu ya elimu. Serikali imekuwa ikifanya kazi hii awamu kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha; na mwaka wa fedha ambao unaanza Julai mwaka 2019/ 2020 tumetenga fedha zaidi ya shilingi bilioni 184 kwa ajili ya kuondoa kero katika miundombinu ikiwepo matundu ya vyoo. Nimuombe Mheshimiwa Mbunge na wadau wengine tushirikiane; unapokuwa unaweza kuchangia tuchangie ili kuweza kupunguza adha hizi ambazo zipo katika shule zetu, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ucheleweshwaji wa ukamilishaji wa miradi ya barabara limekuwa tatizo sugu, ninapozungumza ujenzi wa barabara wa kutoka Kisolya, Bunda, Nyamswa, ahadi na uanzaji umechukua takribani miaka 15. Sasa nataka kujua ni lini barabara hiyo itakamilika kwasababu ikishakamilika kuanzia Kisolya inakuja Bunda Mjini kwenda Nyamswa inaunganika na barabara ya Serengeti na ni kilio cha muda mrefu cha Wilaya ya Bunda na wananchi wa Mkoa wa Mara, lini itakamilika baada ya ahadi na uanzaji takriban imechukua miaka 15? (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, bado nanukia nukia ujenzi. Napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Esther Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, tujifunze tu kushukuru kwa sababu najaribu kuangalia miradi ambayo inaendelea sasa hivi kwenye Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Ester dada yangu anacheka pale, kuna miradi kemkem.

Mheshimiwa Spika, labda nimkumbushe tu Mheshimiwa, kweli barabara ya Bulamba-Kisorya, ilichelewa lakini imekamilishwa. Kuna mradi wa kutoka Kisorya kwenda Nyamuswa tayari mkandarasi ameshapatika, barabara inajengwa. Iko barabara ya kutoka Makutano – Nata - Sanzate imejengwa na kuna mradi kutoka Sanzate kwenda kule Serengeti na harakati za kujenga barabara kwenda kule Arusha zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nafikiri Mheshimiwa Bulaya nimkaribishe tu Bungeni na anafahamu kwamba Serikali inafanya kazi kubwa sana katika Mkoa wa Mara. Kimsingi niseme Mheshimiwa Rais ameyapendelea sana maeneo hayo na kuyapa kipaumbele ili wananchi wa Mara waweze kupata barabara nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama ningeanza kutaja miradi iliyoko Mara nadhani Mheshimiwa Ester anafahamu, nafikiri niishie tu hapo. (Makofi/Kicheko)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Mheshimiwa Waziri anajua Mradi wa Maji wa Bunda umetumia zaidi ya miaka 13, tayari maji yameshatoka Ziwa Victoria, kata saba za mjini wameanza kueneza mtandao wa maji na takriban milioni 300 zilienda. Ninachotaka kujua kama Mbunge senior wa eneo lile na kipenzi cha Wanabunda, ni lini Kata 14 zitapata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kuhusiana na Bunda mradi uliokaa kwa miaka 13 kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maji lengo letu ni kuona kwamba tunaleta mapinduzi makubwa sana kuona maji sasa yanakwenda kupatikana. Miradi hii ambayo miundombinu imekamilika bado maji hayatoshelezi, wataalam wanaendelea na kazi na tutahakikisha maji yanaenda kupatikana. Napenda kusema kwamba Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo alishafika kwangu mara kadhaa na suala hili tunakwenda kulitekeleza haraka. Ziara yangu baada ya hapa ni kuelekea ukanda huo, basi Bunda napo pia nitafika na maji yatapatikana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Najikita katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri, amesema walisitisha mafunzo ya vijana kwa sababu kuna mambo wanataka kuyaweka sawa. Tunajua moja ya mafunzo wanayopewa vijana wa JKT ni pamoja na matumizi ya silaha na mbinu mbalimbali za kivita na ulinzi wa nchi yetu. Naamini Serikali inajua ni idadi gani ya jeshi la akiba wanaowahitaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuhakikisha wanajipanga vizuri kwa nini wasihakikishe mafunzo fulani fulani ya silaha wanapewa watu kadhaa ambao wanajua wataajiriwa katika vyombo vyetu vya ulinzi na usalama na wale wengine ambao hawaajiriwi wapewe mafunzo ya ujasiriamali ili waende kujiajiri wenyewe? Nasema hivyo kwa sababu siyo wote watakaopewa mafunzo ya kutumia silaha za kivita wakayatumia vizuri wanapokosa ajira. (Makofi)
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli tunatoa mafunzo kwa vijana na ziko sababu na uko utaratibu mzuri wa mafunzo hayo. Hatutoi mafunzo tu kiholela bali ni kulingana na mahitaji na matumizi ya nguvu kazi ya vijana tuliyokuwa nayo. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mafunzo haya tunayoyatoa yana dhamira ya kulifanya taifa letu likae katika hali nzuri. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Mji wa Bunda ni Halmashauri inayokua lakini pia ina route nyingi za usafiri ikiwepo kwenda Arusha, Mwanza na maeneo mengine, lakini stendi yake ni mbaya sana.

Ni lini sasa Serikali mtatusaidia hasa Halmashauri yetu changa kutujengea stendi ya kisasa na hasa ukizingatia Mji wa Bunda unakua? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wa Bunda ni Mji ambao unakua, una muingiliano mkubwa wa kibiashara, lakini pia una muingiliano wa magari yanayokwenda katika Mikoa mbalimbali, kwa hiyo, una kila sifa ya kupata stendi ya kisasa na mimi nichukue nafasi hii kwanza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba Serikali inalitambua hilo, lakini Serikali inalitambua hilo lakini Serikali ya Halmashauri kwa maana ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Halmashauri ya Bunda waanzishe utaratibu wa kufanya tathmini ya gharama ambazo zinahitajika kujenga stendi ile ili wawasilishe Serikalini na sisi tutafanya tathmini na kuona uwezekano wa kupata fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi wa stendi ya Bunda. Nakushukuru. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, moja ya kazi ya Serikali ya ujenzi wa vituo vya afya vilevile ni kupandisha hadhi vituo vya afya kuwa Hospitali za Wilaya. Hospitali ya Manyamanyama ni hitaji la Halmashauri ya Bunda kuwa Hospitali ya Wilaya. Hili swali nimeuliza huu ni mwaka wa 11; na liliamuliwa tangu enzi ya Mheshimiwa Mama Anna Abdallah, Mheshimiwa Mwakyusa, mpaka leo wameweka kibao cha Hospitali ya Wilaya, lakini vifaatiba na madawa mnatoa mgao wa kituo cha afya:-

Mheshimiwa Spika, ni lini sasa Serikali hii itaipa Hospitali ya Manyamanyama mgao wa vifaatiba na madawa kama Hospitali ya Wilaya na siyo tena kituo cha afya, maana kinatoa huduma mpaka katika Wilaya za jirani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, utaratibu wa kupandisha vituo vya afya kuwa hospitali una vigezo kadhaa ambavyo vimewekwa. Moja ni kuwa na Halmashauri ambayo haina Hospitali ya Wilaya ndipo kituo kimojawapo cha afya ambacho kinakidhi sifa, kinapandishwa hadhi kuwa Hospitali ya Halmashauri. Kwa mfumo, sera na miongozo ya sasa,

Mheshimiwa Spika, Hospitali ya Wilaya ipo moja tu katika Halmashauri. Kwa hiyo, kwa sababu Halmashauri ya Mji wa Bunda ina Hospitali ya Halmashauri; na hiki kituo cha afya kwa nature yake kinahudumia wananchi wengi, tutahakikisha tunaongeza mgao wa dawa na vifaatiba ili iweze kuendana na idadi ya wananchi wanaopata huduma pale wakati tunaendelea kuboresha Hospitali hii ya Wilaya iliyopo katika Halmashauri ya Bunda. Ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Wewe utakuwa shahidi hiki ni kipindi changu cha tatu katika Bunge lako Tukufu na siku zote tatizo kubwa kwenye Wizara ya Maji imekuwa ni vitu viwili, mosi; miradi kutokukamilika kwa wakati au ikikamilika haitoi maji. Hii WIzara tangu 2016 imekuwa ikitengewa pesa nyingi, lakini ufanisi na ubora na kile kinachokusudiwa, wananchi wapate maji safi na salama hakipo. Swali langu, je, Serikali ipo tayari kufanya ukaguzi maalum nini chanzo cha miradi kukamilika lakini maji hayatoki au ni nini kinachosababisha miradi ichukue muda mrefu? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, awali ya yote nikushukuru. Nikiri, moja ya changamoto kubwa sana ya miradi yetu ya maji ilikuwa moja, usimamizi lakini Bunge lako Tukufu limeona hili na ndiyo maana tukaanzisha Wakala wa Maji Vijijini kwa maana ya RUWASA, lakini kuhakikisha wahandisi wote wa maji waliokuwa chini ya halmashauri kuja chini ya Wizara yetu ya Maji. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tumeshaainisha miradi zaidi ya 177 na RUWASA imeshaanza kuitatua miradi hiyo zaidi ya 85. Kubwa ambalo nataka niwaelekeze Wahandisi wa Maji pamoja na Wakandarasi, vipo vya kuchezea. Ukishiba, chezea kidevu chako au kitambi, si miradi ya maji, tutashughulikiana ipasavyo! Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niulize swali dogo la nyongeza. Kama alivyosema kwenye swali lake alilokuwa akilijibu sasa hivi. Ni kweli ili tuweze kufanikiwa katika kilimo ni lazima tu-invest kwenye kilimo cha umwagiliaji. Mbali na miradi ya Serikali, wananchi katika maeneo mengi wamehamasika kwenye kilimo cha umwagiliaji wakiwepo wananchi wa Bunda, Kata ya Nyatwali ambayo ina maeneo matatu, Nyatwali, Serengeti na Tamau na Mheshimiwa Waziri Mkuu…

NAIBU SPIKA: Swali Mheshimiwa…

MHE. ESTER A. BULAYA: … alishaenda kuutembelea huo mradi mkubwa na akatoa ahadi pale. Kitu kikubwa ambacho…

NAIBU SPIKA: Uliza swali Mheshimiwa Ester.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika… ndiyo naenda kwenye swali. Kitu kikubwa wanachohitaji hawana mashine zenye uwezo mkubwa wa kutoa maji ziwani na kuleta kwenye mradi. Sasa, ni lini Serikali au ina mkakati gani wa kuhakikisha wananchi ambao wameamua ku-invest kwenye mradi wa umwagiliaji wanawezeshwa katika vifaa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwaomba Waheshimiwa Wabunge wote. Serikali, hasa Serikali za Mitaa, na tumewaandikia TAMISEMI kuwaomba wa-involve Serikali za Mitaa, maeneo ambayo mnadhani kuna quick wings ambazo tunaweza kuwa na gharama ndogo za uwekezaji na zinahitaji cost ndogo karibuni. Na Mheshimiwa Esther nakukaribisha wizarani njoo tuleteeni andiko kama mnadhani kwamba, kuna mahitaji rahisi ya kuweza kufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nitumie nafasi hii kuwaomba wakurugenzi wa halmashauri. Suala la umwagiliaji na suala la kilimo sio suala la Wizara ya Kilimo peke yake ni suala ambalo linatuhusu pamoja. Tuwaombe wakurugenzi kwa kuwa, moja ya chanzo cha mapato wanachokipata kinatokana na mazao. Ni lazima asilimia 20 ambayo imeelekezwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu inayotokana na sesi ya mazao wairudishe katika sekta ya kilimo, hasa umwagiliaji na ugani, ili tuweze kuwasaidia wananchi wetu kuweza kujikwamua katika umasikini. Na sisi Wabunge ni Wajumbe wa Baraza la Madiwani na Kamati za Fedha kwa hiyo, tunaomba tusaidiane katika hili.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, kama unavyojua changamoto ya barabara mikoani ni kubwa na kwa Mkoa wa Mara katika miaka zaidi ya mitatu, minne TANROADS Mkoa wa Mara imekuwa haipewi fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati wa barabara. Sasa tunauliza ni lini Serikali itapeleka fedha za kutosha TANROADS Mkoa wa Mara ili iweze kukarabati barabara zote za Majimbo 10 ya Mkoa wa Mara ikiwepo Bunda Mjini; barabara ya kutokea Sazira – Nyamswa; barabara ya kutoka Kinyambwiga kuja Rwagu kutokea Ng’ombe mpaka Manyamanyama? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika mgao wa fedha za TANROADS, fedha zinagawiwa sawa na hakuna upendeleo unaofanyika na Serikali kwenye barabara zake zote za Mikoa mbalimbali. Nataka tu nimjulishe Mheshimiwa Mbunge kwamba kuna miradi kadhaa kwa kiwango cha lami ambayo mpaka sasa hivi inatekelezwa katika Mkoa wa Mara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimhakikishie Mbunge kwamba tunatoa fedha kwa usawa na hasa kwa miradi ambayo inatekelezwa na yeye ni shahidi zipo barabara za Nyamuswa, Bunda zinajengwa. Kwa hiyo, hatuwezi tukakamilisha miradi yote kwa wakati mmoja, lakini ni mpango wa Serikali kwamba barabara zote ambazo zimeainishwa kwenye Ilani na zimeahidiwa na viongozi zitajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na double standard, mifugo inapoingia hifadhini sio tu wanatozwa fidia na wengine ni fidia kubwa na hata wale wafugaji wamekuwa wakipata mateso, lakini tembo wanapokwenda kuharibu mazao ya wananchi na nyumba za wananchi fidia yake ni kidogo, hususan wananchi wa Serengeti, Wananchi wa Tamau, wananchi wa Nyamatoke, Wananchi wa Kunzugu wote hao wapo kando kando ya Hifadhi ya Mbuga Serengeti. Je, ni lini sasa Serikali itarekebisha fidia ya tembo wanapoharibu mazao au mali za wananchi ili iendane na hali halisi kuliko ilivyo hivi sasa fidia ya Shilingi 100,000/=. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza nimshukuru sana Mbunge wa Viti Maalum Ester Bulaya kwa swali lake zuri.ni kweli kumekuwa na changamoto hii ya kwamba wafugaji wanatozwa fedha kubwa kwa maana ya kiwango ambacho kimewekwa kwenye sheria zetu hizi lakini inapokuja kwa mwananchi inaonekana kwamba Serikali haioni umuhimu.

Mheshimiwa Spika, lakini nimtoe wasi wasi Mheshimiwa Esther kwamba sisi tunachofanya ni kukemea uingizaji wa mifugo kwenye hifadhi na niwaombe wananchi ambao wanaishi kwenye maeneo ya pembezoni mwa hifadhi tembo hawa wanaangalia ni nini ulichopanda kwenye maeneo hayo na tunawahamasisha wananchi wapande pilipili lakini pia waweke mizinga ya nyuki.

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo hawa tembo na Wanyama wengine wana Serikali yao na Serikali yao hii na wenyewe wanajadili kama ambavyo tunajadili sisi hapa. Na ukumbuke maeneo mengi ambayo ni ushoroba wa wanyama sisi wananchi ndiyo tumeenda kuwafata kule hata wao wanatushangaa kwamba kwanini sisi maeneo yetu wananchi wameyasogelea. Ndivyo sasa sisi kama Serikali tunajitahidi angalau kuwa tunawaondoa wale tembo kuwarudisha kwenye maeneo ya hifadhi. Lakini tutambue kwamba wananchi ndiyo tunaowafuata hawa tembo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, lengo la kutoza hiki kiwango ni kuzuia hawa wafugaji sasa kutoingiza mifugo yao kwenye hifadhi, na niombe Waheshimiwa kwenye hili tushirikiane lisionekane kama ni la Wizara ya Maliasili ya Utalii sheria hizi tumezitunga sisi wenyewe na utekelezaji wake basi tutekeleze sisi wenyewe. Wafugaji wanaaswa kutoingiza mifugo yao kwenye maeneo ya hifadhi ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Wewe ni shahidi Mradi wa Maji Bunda sasa hivi unachukua takribani miaka kumi na tatu, najua kuna awamu ya tanki imekalimilika. Awamu nyingine ilikuwa ni kuhakikisha wanasambaza mabomba na kueneza mtandao wa maji katika kata zote 14. Hivi ninavyozungumza ni kata saba tu tayari ndiyo zimeanza kusambaza mradi wa maji na wana uhakika wa kupata maji angalau kwa asilimia 50. Je, ni lini sasa Wizara itahakikisha kata zote 14 za Bunda Mjini zinapata maji na ukizingatia humu ndani mimi ndiyo nawasemea hakuna anayewasemea. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nipende kupokea pongezi kwa kuona kwamba tanki limekamilika na angalau asilimia hamsini ya usambazaji umeshakuwa katika utekelezaji. Kwa sababu tuna kata 14 na kata saba tayari utekelezaji unaendelea hiyo ndiyo kazi ya Wizara ya Maji.

Vilevile kama ambavyo umemtaja Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo kazi hii imefanyika kwa usimamizi madhubuti. Mbunge wa Jimbo amekuwa akifuatilia mara nyingi na kwa sababu Mbunge wa Jimbo amekuwa akiwasiliana na Wizara mara kwa mara ndiyo maana maji kata saba, kati ya kata 14 yameweza kutolewa. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza. Mbali na mkakati wa Serikali katika jibu lake la msingi la kuchimba mabwawa na marambo. Jimbo la Bunda Mjini limekuwa na changamoto sana ya ukarabati wa marambo.

Sasa ni lini Serikali mtatukarabati Rambo la Nyabehu, Kinyambwiga na Gushigwamara ili sasa wananchi wa maeneo hayo wapate huduma ya maji vile vile mifugo iweze kupata huduma ya maji. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ukarabati wa mabwawa na marambo kwa ajili ya mifugo, sisi kama Wizara tunaendelea kukarabati awamu kwa awamu kadri fedha inavyopatikana. Hivyo, pia kwa suala hili la Bunda Mjini, Bwawa la Nyabehu, Kinyambwiga pamoja na hilo lingine yote yapo katika mkakati wa Serikali kuona kwamba yanarudi katika hali bora. Hivyo, nipende kukupongeza Mheshimiwa Esther kwa kufuatilia na uongeze ushirikiano na Mbunge wa Jimbo ili mambo yakae sawa zaidi. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa kuuliza swali la nyongeza. Ni dhahiri kwamba kwa Afrika nchi yetu inahifadhi nzuri inawanyama wengi ukienda Ruaha ukienda Serengeti, Ukienda Tarangire na maeneo mengine…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Bulaya ukipewa swali la nyongeza usianza na utaalam mwingi nenda straight to the question.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mikakati ya Serikali ni ile ile ya kushiriki matamasha ya Kimataifa, kutangaza kwenye TV lakini bado hayajatuletea manufaa chanya ya ongezeko la watalii kulingana na vivutio vyetu na hifadhi zetu.

Je, hamuoni kwamba ni wakati muafaka wa kuwa na mikakati Madhubuti ya kiushindani ili idadi ya watalii iendane na hifadhi zetu na vivutio vyetu? (Makofi)
WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante nimshukuru Mheshimiwa Ester Bulaya kwa swali lake hilo, takwimu zetu zimeonesha kwamba idadi ya watalii imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka. Ongezeko hilo limetokana na juhudi ya Serikali ambayo imeifanya katika kutangaza utalii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma Ilani ya Chama Cha Mapinduzi imeelekeza wazi kwamba tuje na mazao mapya na mikakati mipya katika kutangaza utalii, mikakati yote ipo mezani iko tayari kinachotukwamisha ni gonjwa hili la Covid, nimhakikishie Mheshimiwa Ester Bulaya pindi ugonjwa huu utakapokwisha ataona ongezeko kubwa la watalii hapa Tanzania, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa swali dogo la nyongeza; wewe ni shahidi mradi wa Bunda umechukua muda mrefu sana takribani miaka 13; lakini moja katika makubaliano kwenye mkataba wa mradi ule ni kujenga vitu kabla mradi haujafika Bunda Mjini kwenye eneo linalotoka kule Nyabeu.

Sasa nataka kuuliza maeneo yanayopita mradi kama Gushigwamara, Kinyambwiga, Tairo, Guta na Bunda Store kabla hayajafika centre; ni lini mtaweka vituo ili wale wananchi wa maeneo yale wasisikie tu mradi umetoka chanjo cha maji vijiji ambavyo vinapita havijapata maji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, sisi kama Wizara tayari tunaendelea na kuona kwamba maeneo ya miradi ambayo imekaa muda mrefu inakamilika, na sera ya maji inataka pale kwenye chanzo na kadri ambavyo mradi unakwenda tunaendelea kusambaza maji. Yule wa karibu ya chanzo ataendelea kupata maji kwa kwanza kulikoni aliyekuwepo kule mbali. Hivyo nikuhakikishie Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba maeneo yote ambayo umeyataja yatazingatiwa katika kuona kwamba miundombinu ya usambazaji maji inawafikia. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza. Najua Serikali mna mkakati wa kujenga Mahakama kila Wilaya. Wilaya ya Bunda haina jengo la Mahakama, imepanga kwenye nyumba ya Mzee Wasira muda mrefu, sasa hivi wamehamia kupanga eneo lingine. Ahadi mlitoa tangu enzi ya Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe akiwa Waziri wa Katiba na Sheria. Nataka kujua ni lini Mahakama ya Wilaya ya Bunda itajengwa ya kwao?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa kama mnavyofahamu nchi inapitia changamoto mbalimbali. Kwa sasa kama nilivyoahidi, kufikia 2025 sehemu zote ambazo hazina Mahakama za Wilaya na Makao Makuu ya Tarafa zote katika ngazi ya Kata zitakuwa na majengo mapya. Tuvumilie, tutaendelea kuazima majengo lakini mwisho wetu tumeuweka kwenye 2025 iwe ni mwisho wa habari hii. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kuendelea kuzungumzia mradi wa Mchuchuma na Linganga kwenye Bunge letu bila utekelezaji dhabiti ni aibu, ni wa muda mrefu tangu enzi ya akinamama Mary Nagu wakiwa Mawaziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu unasuasua kwa sababu mwekezaji hana mtaji wa kutosha, ndiyo maana ameshindwa kulipa fidia. Kwa nini Serikali inamkumbatia huyu mwekezaji, kwa nini isiachane naye kama mama Samia anataka mradi huu uendelee, ikamtafuta mwekezaji mwingine na Serikali ikawekeza vya kutosha?
WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nijibu swali nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli mradi umechukua muda mrefu lakini lazima tukubaliane kwamba mwekezaji huyu Situan alikuwa na mkataba na Serikali kupitia NDC. Kwa hiyo mkataba wake lazima uhitimishwe kisheria, tukienda papara tutapata matatizo. Hata hivyo, nimpe taarifa kwamba leo hii wanakaa na tunaamini ndani ya mwezi huu mazungumzo yatakamilika. Baada ya hapo tuatajua ama twende naye au tuachane kisheria twende kwa mwekezaji mwingine, lakini tumesema kabisa kwamba kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais mradi huu lazima uanze ndani ya mwaka ujao wa fedha.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua Sera ya Afya mbali ya ujenzi wa zahanati pamoja na vituo vya afya lakini pia kuna kupandisha hadhi vituo vya afya. Hospitali ya Manyamanyama imepandishwa hadhi na kuwa hospitali ya wilaya lakini bado inapata mgao kama kituo cha afya. Ni lini sasa itapatiwa mgao wa vifaatiba na dawa kama hospitali ya wilaya kwa sababu ipo barabarani na inatoa huduma si tu kwa Wilaya ya Bunda, hata kwenye mikoa Jirani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ya Serikali ni kwamba vituo vile vyote ambavyo vimepandishwa hadhi kutoka kituo cha afya kwenda kuwa hospitali kama ilivyo Hospitali ya Manyamanyama vinastahili kuwekewa bajeti kwa ngazi ya hospitali na vifaatiba lakini pia hata ikama ya watumishi. Kwa hiyo, nimhakikishie kwamba tutalifanyia kazi hilo kwa haraka iwezekanavyo ili liingie kwenye mgao wa hospitali. Ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; sera yetu ya utalii mbali ya kwamba inatuingizia mapato, pia wananchi wanaozunguka maeneo yenye hifadhi pia wananufaika. Halmashauri ya Mji wa Bunda imezungukwa na mbuga ya Serengeti.

Sasa swali langu, Mheshimiwa Waziri mbali ya kwamba wananchi wanalinda Hifadhi ya Serengeti lakini tembo wanapokuja kwa wananchi kuharibu mazao pamoja na nyumba zao wamekuwa hawalipwi fidia. Kwa mfano, Mcharo wananchi 350, Guta, 403, Bunda Store, 86, Kunzugu 65, Nyatwali 51 na Mheshimiwa Waziri nimeshaleta ofisini kwako watu hawa wanadai fidia kwa muda mrefu takriban watu 900. Lini watalipwa fidia yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimtoe wasiwasi Mbunge. Mbunge wa Jimbo alishawahi kunifuata akanipa orodha ya wanaodai, lakini pia hata yeye mwenyewe ameshanipa orodha ya wanaodai. Kwa hiyo, tulikubaliana kwamba nitaenda mimi mwenyewe kuongea na wananchi, lakini wale wote wanaodai nitahakikisha kwamba Serikali imewalipa, lakini pia tutaongea na wananchi waendelee kuwa wahifadhi, maana hao ndiyo wanaotusaidia sisi hata kuhifadhi maeneo yanayozunguka hifadhi, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili ya nyongeza. Mbali tu na tatizo la kemikali ya zebaki, lakini wachimbaji wadogo wamekuwa na tatizo kubwa sana la mitaji wakiwemo wachimbaji la Nyamongo Mkoa wa Mara. Ni lini sasa Serikali watawawezesha wachimbaji wadogo wa Nyamongo hasa vijana na akinamama ili waweze kuchimba vizuri dhahabu zao.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili kuhusiana na kemikali zinazodhuru wananchi, si tu kwa wachimbaji wadogo mbali na kwa wananchi wanaozunguka migodi. Sasa wananchi wa Nyamongo wameathirika sana na mara nyingi Serikali imesema italipa fidia, ni lini sasa itawafidia wananchi ambao wameathirika na kemikali zinazotoka migodini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kuhusu mitaji Serikali kupitia Wizara ya Madini imefanya lile linalowezekana kuhusisha benki zetu za ndani ambazo zimehiari kutoa mitaji kwa ajili ya wachimbaji wetu wadogo na kwa taarifa mwezi wa Sita Mheshimiwa Waziri wa Madini alizindua NMB Mining Club ambapo wateja wachimbaji wadogo wanaweza wakaenda pale na wakakopeshwa.

Mheshimiwa Spika, pia benki zetu zingine za ndani zimehiari tayari na tayari tumeona kwamba wanashiriki katika shughuli za kuwakopesha wachimbaji wadogo. Ambacho tumewaasa wachimbaji wadogo ni kwamba kabla ya kwenda benki awe na leseni halali, inayotambulika na Tume ya Madini, lakini pia awe basi na takwimu za kazi anazozifanya ionekane kwamba unaonekana ukizalisha, ukiuza unapata faida benki wamehiari kutoa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo limefanyiwa kazi kwa namna hiyo na wachimbaji wadogo wameanza kupata matunda. Pia kwa taarifa benki zetu za ndani zimekwenda mbali zaidi hadi kutoa fedha kwa ajili ya miradi mikubwa. Kwa hiyo tunadhani kwamba, hiyo ni hatua na suala la mitaji limeendelea kushughulikiwa halimradi wachimbaji wetu wadogo waweze kutoa ushirikiano kwa jinsi hiyo.

Mheshimiwa Spika, suala la mazingira yanayozunguka migodi. Ni kweli kwamba inapokuja kwenye mgodi ambao Mheshimiwa Mbunge ameutaja, Serikali imeendelea kufanya hatua, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba hakuna tena maji yanayotiririshwa katika maeneo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, limeendelea kushughulikiwa na timu yetu ya Wizara ya Madini pamoja na NEMC pamoja na watu wa Wizara ya Maji, wamekuwa wakishirikiana katika kufanya ukaguzi kuhakikisha kwamba hakuna uchafu tena unaoendelea kutiririshwa kutoka katika migodi.

Mheshimiwa Spika, suala la fidia pia limeendelea kufanyiwa kazi na yule Mthaminishaji Mkuu wa Serikali. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimemsikiliza Mheshimiwa Waziri wakati anajibu, amesema moja ya changamoto ya kuchelewa kulipwa kwa wastaafu ni pamoja na waajiri kuchelewa kupeleka michango. Wakati jana nimeomba mwongozo, nimepokea message 165, wengine hawajalipwa kuanzia mwaka 2012; lakini kwenye Bunge la Bajeti Mheshimiwa Waziri aliji-commit kwamba atafanya ziara kwenye vyombo vyote vya habari kuhakikisha wanapeleka michango ili Waandishi wa Habari na watu wengine binafsi walipwe kwa wakati. Sasa nataka niulize, ni lini ataanza hiyo ziara ili Waandishi wa Habari michango yao ipelekwe ili na wenyewe wawe na uhakika, baada ya kumaliza kazi zao wapate stahiki zao? Ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE, KAZI, AJIRA NA WATU WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Spika, masuala haya ya haki ya wafanyakazi ni masuala yanayotakiwa kuangaliwa kwa utaratibu mzuri sana. Masuala haya hayafanani tu labda na maamuzi ya mtu, kuamua kukaa hapa, ukae na nani na ufanye nini? Hapana, ni lazima kuyatengenezea utaratibu madhubuti.

Mheshimiwa Spika, naomba kumwambia Mheshimiwa Mbunge, tumeshaanza hiyo kazi. Kazi ya kwanza tuliyoifanya ni kupata ushirikiano kutoka kwa Waandishi wa Habari, kutambua vyombo ambavyo vimekithiri kwa kutokulipa mishahara na mafao ya Waandishi wa Habari. Kazi hiyo, tumeshaitekeleza na baada ya hapo sasa ndipo tutakwenda kuanza ziara ya kukutana na vyombo hivyo. Huwezi kuanza tu kukutana nao kabla hujapata taarifa.

Kwa hiyo, naomba nimwambie Mheshimiwa Mbunge Serikali inafanya kwa utaratibu, inatengeneza mikakati kusudi utaratibu huo ukianza kuchukuliwa hatua, hatua hizo ziwe zimezingatiwa kwa mujibu wa sheria na utaratibu. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, Serikali ilihamasisha wananchi mbali ya kujenga shule, lakini waweze kuanza kujenga zahanati na mwisho wa siku Serikali kutoa mchango wake. Sasa wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini walihamasika sana na kwa mfano maeneo ya Zahanati ya Changuge, Mchalo, Gushigwamara, Nyamatoke, maeneo hayo yote wananchi walihamasika na nilichangia kwa kuweka fedha ya Mfuko wa Jimbo.

Je, Serikali ni lini sasa mtamalizia ili wananchi wa Jimbo la Bunda Mjini kwa maeneo ambayo nimeyataja wawe na uhakika wa kupata huduma ya afya katika maeneo yao? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kujali afya za wananchi kwa kuwahamasisha kutoa nguvu zao kujenga zahanati na Serikali kuchangia nguvu za wananchi katika ukamilishaji wa maboma ya zahanati. Na katika jibu langu la msingi nimeeleza jumla ya maboma 758 yatakwenda kujengwa mwaka huu wa fedha.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, jitihada zake, lakini pia jitihada za Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini zimeendelea mara kwa mara kuikumbusha Serikali. Na nimhakikishie kwamba, tutaendelea kuhakikisha kwamba, tunatafuta fedha kwa ajili ya kukamilisha maboma hayo. ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Utakubaliana na mimi kwamba tatizo la ajira kwa vijana kwa nchi hii limekuwa kubwa na la muda mrefu na Serikali ilishaji-commit, wakati nikiwa Mbunge wa Vijana kipindi kile wakati tunapitisha hapa Sheria ya Baraza la Vijana. Kwamba, kila Halmashauri itatenga maeneo ya kilimo kwa ajili ya vijana hasa ambao ni graduate waweze kwenda kujiajiri wenyewe. Lakini ardhi yenye rutuba ya daraja la kwanza, daraja la pili wamekuwa wakipewa wawekezaji. Hii ardhi ambayo vijana wanaitumia unakuta wamepewa na Mjomba, Shangazi na Bibi.

Je, lini Serikali mtatimiza ahadi ambayo mmeweka kutenga ardhi kwa vijana na kuwawezesha ili asilimia kubwa ya vijana waweze kujiajiri wenyewe? (Makofi)

Swali la pili; Serikali tulishatunga Sheria ya Baraza la Vijana na Vijana wanakosa chombo chao cha kujadili Kitaifa bila kujali itikadi zetu na Rais alishasaini. Je, ni nini kigugumizi cha kushindwa kutenga bajeti ya uanzishaji wa Baraza la Vijana kuanzia Taifa mpaka Kata? Tunahitaji commitment ya Serikali hatutaki ahadi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA (MHE. PASCAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, tayari Serikali kwa agizo hilo la Serikali lililotolewa kupitia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, tayari imekwisha kutenga maeneo kwa ajili ya shughuli za vijana katika Halmashauri 84 zimekwisha tenga maeneo kwa ajili ya shughuli hiyo na eneo ambalo ni la mfano katika uzinduzi wa programu hii ya kutengewa maeneo kama agizo la kwenye Halmashauri nchini, lilifanyika hivi karibuni pale Kahama – Zongomela, kuna eneo kubwa ambalo vijana wanafanya shughuli mbalimbali pale zikiwemo pia za kilimo lakini pia biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili anauliza ni lini Serikali sasa itaenda katika kukamilisha mchakato wa kupata Baraza la Vijana ikiwa sheria tayari. Tayari eneo hili ni agizo la Mheshimiwa Rais ambaye alizungumza alipokutana na vijana pale Mwanza, alitoa maelekezo na maelekezo hayo yanafanyiwa kazi na kwa kipindi chote tayari tumekwishaanza na mabadiliko kwa sasa. Tumeshafanya mabadiliko ya sera ya vijana ya mwaka 2007 na hatua ya pili itakuwa kwenda katika kuangalia uhitaji wa sasa katika sheria kama italazimika kuweza kufanya mabadiliko.

Mheshimiwa Spika, hatua ya tatu itakuwa sasa kuangalia kulingana na mazingira yaliyopo kama kutakuwa na ulazima kwa wakati wa sasa kuendana na situation iliyopo katika mahitaji ya vyombo vingi pia vya Kimataifa kama tutaweza tukaandaa Baraza la Vijana kwa kipindi hiki, lakini tayari michakato hii tayari tumekwisha kuianza kwa upande wa Serikali. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Wakati Mheshimiwa Waziri anajibu maswali ya nyongeza, alisema wamefanikiwa kupeleka vifaa vya maabara kwenye maeneo mawili. Nchi yetu ukichanganya na Zanzibar ina mikoa 31, kwa Bara ni 26: Je, hamwoni kwamba hiki ni kikazi kiduchu kwa tatizo kubwa ambalo limetukumba la Covid? Ni lini mtahakikisha hizo maabara zinakuwepo nchi nzima na siyo hizi mbili ambazo zimetokana na pesa ya mkopo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo niliyoyasema ni mifano tu. Nataka nimweleweshe Mheshimiwa Mbunge kwamba toka Uhuru tumekuwa na CT- Scan mbili tu kwenye nchi hii, kwenye hospitali za mikoa mbili tu, lakini amekuja leo Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, tunakwenda kupata 29 ambazo zina gharama kubwa kuliko mashine za kupima Corona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ninachotaka tu kumhakikishia ni kwamba tuna uwezo huo, mpaka leo tunapoongea hivi Mount Meru Hospital wanapima, Mbeya wanapima, kila mahali tutafikiwa. Kwa hiyo, usiogope, kazi inapigwa. Sisi tuendelee kusherehekea, karibuni upande huu kumenoga. (Kicheko/Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, nami niulize swali dogo la nyongeza: -

Mheshimiwa Spika, wewe ni shahidi; hii sera ni ya muda mrefu na haitekelezeki. Wabunge mnajua kwenye majimbo yetu, akinamama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano hakuna matibabu bure. Sasa Mheshimiwa Waziri anasema atatoa miongozo, kama hakuna kitu cha kumbana mambo ni yaleyale.

Je, kwa nini kusiwe na sheria kwamba ni lazima akinamama wajawazito, watoto chini ya miaka mitano na wazee wapate matibabu bure ili wazee wasiweke tiba ya kisaikolojia tena, wakienda hospitali wapate matibabu bure? Sera imekuwepo haitekelezeki, leteni sheria kama mna dhamira njema.
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO (MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL): Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge na ndiyo maana umekuwa mkali sana kwenye suala zima la bima ya afya kwa wote. Nataka kukuhakikishia tukienda kutekeleza agizo lako la suala la bima ya afya kwa wote, haya mambo yatakuwa ni historia. Kwa wakati huu miongozo iliyopo tutaendelea kuifuatilia na kusisitiza, lakini Mheshimiwa Ester Bulaya aendelee kushirikiana na sisi ili tuweze kufanya hilo litekelezeke. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kwa moyo wa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Aweso, kwetu sisi amejitahidi kuutendea haki Mradi wa Bunda umepiga hatua. Sasa ningependa kuuliza swali la nyongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maji yametoka Nyabehu yamekuja Bunda Mjini. Katika mkataba wa ule mradi ilikuwa ni pamoja na kujengwa vituo. Hivi tunavyozungumza bado vituo havijajengwa Kata tu ya Gutagushigwamara hakuna kituo. Nyabeu yenyewe kiko kimoja, ukienda Kinyambwiga hakuna kituo, ukija Bunda Store huku hakuna kituo. Manyamanyama, Nyasura, Sazila hayo maeneo yote kama kungejengwa vituo tungeweza kupata maji katika Kata zote 14 kwa huo mradi uliochukua zaidi ya miaka 13. (Makofi)

Sasa kwa mujibu wa ule mkataba ni lini sasa hivyo vituo vitakamilika ili wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mjini wasahau biashara ya kupata shida ya maji safi na salama? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa na nzuri anayoifanya. Lakini nataka nimuhakikishie sisi kama Wizara ya Maji tumefanya mageuzi makubwa sana, kupitia Wizara yetu ya Maji na Rais wetu support kubwa ambayo anatupa ya kifedha. Tulikuwa na miradi kichefuchefu zaidi ya 177 asilimia nyingi tumekwisha ikamua. Sasa nataka nimpe mwaliko mahususi kabisa tarehe 7 Mheshimiwa Rais wetu mpenzi Mama Samia Suluhu Hassan atakuwepo Bunda. Naomba tujumuike ukaone kazi kubwa na nzuri ambayo imefanywa na Wizara yetu ya Maji katika Jimbo lako. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kiuhalisia Wizara ya Elimu ni miongoni mwa Wizara ambayo inaonekena inatengewa bajeti kubwa, lakini unakuta pesa nyingi katika Wizara hii ni pesa za mikopo ya elimu ya juu ambayo mara nyingi wanaziweka kama ni fedha za miradi ya maendeleo, lakini kimsingi pesa zile zilitakiwa ziwe kwenye matumizi ya kawaida kwa sababu, zinaenda kuwasaidia vijana wetu pesa za kujikimu. Hii imekuwa ni mapendekezo ya Kamati mbalimbali, ikiwepo Kamati ya Bajeti.

Je, ili kuitendea haki Wizara hii kwa nini hizi pesa za mikopo msiziweke kwenye matumizi ya kawaida ili sasa tujue, kama Bunge, tuna jukumu gani la kutenga pesa za kutosha kwenye miradi ya maendeleo iende kwenye utekelezaji? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile hili ni wazo la Mheshimiwa Mbunge na amesema kwamba, ni mapendekezo ambayo yalitolewa na Kamati mbalimbali, sisi kama Wizara tutaenda kukaa na Wizara ya Fedha kuweza kuona namna gani jambo hili linaweza kwenda kufanyiwa kazi, lakini kimsingi tunaomba tulibebe. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru.

Mheshimiwa Spika, tunajua Serikali ina mkakati wa kujenga barabara na kuunganisha Mikoa lakini barabara nyingi mnazojenga hamzingatii ile mifumo ya maji kwa hiyo unakuta barabara nyingi mvua inaponyesha magari hayapiti. Mfano ni barabara ya kutoka Dodoma kupitia Mtera kwenda Iringa ni barabara muhimu sana lakini hivi ninavyozungumza mvua ikinyesha barabara haipitiki. Najua kuna ukrabati unafanywa, Je, mna mkakati gani wa kuhakikisha barabara zinapitika wakati wote kwa kuweka mifumo ya maji. Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, katika ujenzi wa barabara zetu moja ya maeneo ambayo sasa tumeweka kipaumbele, kwanza ni kuhakikisha barabara zetu kwenye designing zinaweka kipengele cha kuweka mifereji ya ku-drain maji ili kuepusha maji kukatisha katika barabara zetu na kuziathiri lakini katika maeneo ambayo madaraja au culvat zinajengwa tumeweka utaratibu wa kuhakikisha kwamba madaraja yanakuwa juu ili kuepusha maji kukatisha katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikiri kwamba kuna baadhi ya maeneo kulikuwa na changamoto hizo na ndiyo maana sasa designing zetu zote zimeboreshwa kuhakikisha haturudi kwenye changamoto hizo na tutaendelea kutekeleza kwa utaratibu huo. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kama unavyojua Mji wa Bunda unakua kwa kasi na Serikali ya Awamu ya Nne iliji-commit kujenga kilomita 10 katika mitaa ya Mji wa Bunda na hasa ukizingatia sasa kuna barabara moja tu ya lami kutoka pale Mjini kwenda Bomani. Nataka nijue ni lini Serikali itakamilisha ahadi hii ya kilomita 10 ili Mji wa Bunda ufanane na Miji mingine kwa lami? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa
Mwenyekiti, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu awali kwamba ahadi zote viongozi zipo na tunachokifanya sasa hivi zote zimeshatengewa fedha yaani kwa maana thamani halisi. Kwa hiyo, tunavyopata fedha ndipo ambavyo tunatekeleza. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge nimwahidi najua Mji wa Bunda na bahati nzuri na mimi mwenyewe nimefika, kwa hiyo ninachokiahidi ni kwamba zile barabara zitajengwa kwa kadri ya upatikanaji wa fedha hizo. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wilaya ya Bunda ina majimbo matatu, Bunda Mjini, Bunda na Mwibara. Tuna kituo kimoja ambacho ni chakavu hakiendani na hadhi ya Kituo cha Wilaya. Mheshimiwa Naibu Waziri anakijua, anapita pale akienda jimboni kwaeo, nimeuliza zaidi ya mara tatu swali hili.

Lini Serikali itakifanyia ukarabati Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bunda kiendane na hadhi ya wilaya? Nilipokuwa Mbunge nilitengeneza Ofisi ya Upelelezi. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bunda nakifahamu na kama zilivyo wilaya nyingi na hasa wilaya mpya kinahitaji kuimarishwa.

Sasa hivi tunaendelea na ujenzi wa Vituo vya Polisi vya ngazi ya mikoa maana tunayo baadhi ya mikoa ambayo haina Makao Makuu ya RPC; na wilaya mpya ambazo zimeanzishwa tangu mwaka 2012. Naomba kumuahidi Mheshimiwa Bulaya katika mpango wetu wa ukarabati wa vituo hivyo Bunda pia itazingatiwa. Nashukuru. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, tunajua bandari yetu ni miongoni mwa chanzo cha mapato, na kumeibuka kuwepo kwa bandari bubu zaidi ya 58 katika Mikoa mbalimbali ambapo Serikali yetu inakosa mapato. Naibu Waziri ulikuwa Mwenyekiti wa Kamati na huu ni mfupa mzito ambapo mapato ya Serikali yanapotea.

Je, ni lini sasa mchakato wa kuangalia hizi bandari zote kama walivyokuwa wameahidi walipokuja kwenye kamati. Ni lini sasa mtazirasimisha rasmi ikiwemo na badari ya Mbweni ili Serikali iweze kukusanya mapato ya kutosha na kupeleka maendeleo kwa Watanzania? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, kwanza nitambue Mheshimiwa Ester Bulaya kama ulivyosema nilikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma changamoto hizi tuliziona na hivi sasa kati ya bandari zote nchini tuna bandari 693 nchi nzima ya Tanzania ambazo ni bandari bubu. Na tunazo bandari 66 tu ambazo ni rasmi. Bandari ya Mbweni ambayo ni miongoni mwa bandari 24 ambazo tutakwenda kuzirasimisha hivi sasa ninavyosema.

Mheshimiwa Spika, badari hizi zinaingiza fedha kwa mwaka shilingi milioni 200 kwa hiyo, kuna umuhimu mkubwa sana wa kurasimisha bandari bubu ambazo zinaingiza fedha Serikalini. Nitoe wito pia kwa kuwa siyo kila sehemu tutaajiri kama TPA kwa maana tutashirikiana na halmashauri husika katika maeneo hayo ili hizo bandari ziewe kurasimishwa. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Halmashauri ya Mji wa Bunda, imeanza ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri kwenye Kata ya Bunda Store, na Serikali ilitenga Shilingi milioni 500: Kuna mkakati gani wa kutenga fedha kila mwaka wa fedha ili ile hospitali iweze kukamilika haraka? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, dhamira ya Serikali ni kuendelea kutenga fedha kila mwaka wa fedha, ndiyo maana tulipeleka Shilingi milioni 500 na kila mwaka wa fedha tutatenga Shilingi milioni 500 au zaidi kuhakikisha Hospitali ya Mji wa Bunda pia inakamilika. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na ningependa kujua, Serikali ina bei maalum elekezi ya unit moja ya maji kwa sababu, kila halmashauri inajipangia bei na mwisho wa siku mzigo unabaki kwa mwananchi; kwa mfano Bunda, unit moja 1,800/= ukienda maeneo mengine ni 1,000/= mpaka chini ya 1,000/=. Je, hamwoni kuna haja ya kupanga bei maalum ili kuwaondolea mzigo wananchi?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari Wizara ilishatangaza kupitia Waziri mwenye dhamana, bei elekezi kwenye maeneo yote ilishatangazwa. Bei hazifanani kulingana na uwekezaji wa miradi. Mradi ambao unatumia source ya kusuma maji kama ni diesel, bei yake haiwezi kufanana na inayosukuma maji kwa kutumia umeme wa TANESCO, tofauti na bei ambapo maji kutoka katika chanzo chake yatakuwa yanasukumwa na umeme wa jua, lakini vilevile ukubwa wa mradi kulingana na jiografia ya eneo ulipo huo mradi. Hivyo, bei haziwezi kufanana, lakini bei elekezi tayari zimetolewa kulingana na mradi namna ambavyo ulitengenezwa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Halmashauri ya Mji ya Bunda ni mpya tayari imejenga jengo la ofisi ya Halmashauri, lakini kuna changamoto kubwa sana ya nyumba za watumishi wakiwemo Walimu, Madaktari na watumishi wa halmashauri. Ni lini sasa Serikali itajenga na hasa ukisema utegemee Halmashauri ya Bunda mapato yake ni madogo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Halmashauri ya Mji wa Bunda, imejengewa jengo la halmashauri kwa maana ya jengo la utawala, lakini changamoto ya nyumba za watumishi ipo na Serikali inatambua changamoto hiyo. Nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge na Wananchi wa Bunge Mjini kwamba wewe pamoja na Mheshimiwa Mbunge Maboto mnashirikiana vizuri kuhakikisha nyumba za watumishi zinajengwa pale na Serikali itaendelea kufanya utaratibu kuona uwezekano wa kujenga nyumba za watumishi pale.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru lengo la mfuko huu ni kusaidia kaya maskini lakini unakuta bado haileti tija kutokana na pesa ambazo wanatoa elfu 50, laki, mwisho tunawafanya wanakuwa tegemezi. Ni mkakati gani wa Serikali kuhakikisha unabadilisha huu mfumo na matokeo yake kwenda kuwapa mitaji ili wasiendelee tena kutegemea zile 50, 50 waweze kukidhi maisha yao moja kwa moja? Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI
WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, tunatoa elimu kwa wale waratibu wetu kule chini na wao waweze kutoa elimu kwa walengwa ya namna bora ya kuweza kuzitumia fedha hizi wanazozipokea. Tukiangalia kwamba kaya hizi nyingi zilikuwa hazina uhakika wa kula yao, hazina uhakika wa milo mitatu.

Kwa hiyo kwa kuingia kwenye mpango huu kwa kupata kiwango cha fedha ambacho Mheshimiwa Bulaya amekitaja na wengine hupata zaidi, imeshawapa boost ya kutosha ya kuweza kuanza kufuga kuku, mbuzi ili kuweza kuboresha maisha yao na kuwa na uhakika wa kula kila siku.

Mheshimiwa Spika, vile vile tunawasisitiza sana wenzetu wa Serikali za Mitaa kwa maana Wakurugenzi kule kuhakikisha wanawaweka hawa walengwa katika mpango wa ile 4, 4, 2. Kwa sababu kwenye kaya hizi maskini wapo akinamama, kwenye kaya hizi maskini wapo walemavu, kwenye kaya hizi maskini wapo vijana. Kwa hiyo tunasisitiza sana kwamba hawa walengwa waliokuwepo kwenye kaya hizi kuweza kuingia katika 4:4:2 ili waweze kupata mkopo wa vikundi kuweza kuongeza kipato na kuweza kufanyabiashara mbalimbali.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kituo cha Polisi cha Wilaya Bunda ni chakavu sana na Mheshimiwa Waziri anakijua, amefika pale na kinahudumia Majimbo matatu Mwibara, Bunda Mjini na Bunda. Je, ni lini Mheshimiwa Wizara atakikarabati kituo hicho ili kiendane na hadhi ya Wilaya?
WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Kituo cha Bunda kiko chakavu na binafsi nakumbuka niliwahi kutembelea kituo hiki na hata Mheshimiwa Mbunge wa Jimbo hili naye vilevile alinikumbushia juu ya ukubwa wa changamoto hii. Hivyo basi, nimhakikishie Mheshimiwa Ester Bulaya kwamba tunafahamu na pale ambapo hali ya kibajeti itakapokaa vizuri, basi tutakifanyia kazi kituo hiki.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, mbali ya watu kuharibu mazingira, I mean miti na kadhalika kwenye vyanzo vya maji, kumekuwa na wimbi kubwa la watu kwenda kujenga kwenye vyanzo vya maji kwenye mito na maeneo mengine hatimaye kusababisha maji kushindwa kupita kwenye mikondo yake na wengine ni vigogo tu.

Je, Wizara yako kushirikiana na NEMC mna mkakati gani madhubuti wa kuhakikisha watu hawaendi kujenga kwenye vyanzo vya maji?(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, awali ya yote nampongeza Mheshimiwa Ester kwa kuweza kufuatilia vyanzo vyetu vya maji. Maeneo haya namna yanavyojengwa tunayafanyia kazi siyo tu na NEMC, tuna Wizara ya Kisekta sasa hivi tunapita huko. Moja ya shughuli tunayofanya ni kukataza na kuondoa wale wote ambao wamejenga kandokando ya vyanzo vya maji. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, nchi yoyote ambayo inahitaji kukusanya mapato kwa wingi na kuwatengenezea mazingira mazuri wananchi wake wamekuwa wakiweka mazingira mazuri ya kodi yaani kodi zinakuwa rafiki si kubwa kulingana na biashara ya mtu anayoifanya. Lakini hapa katikati kodi zimekuwa kubwa kulingana na biashara ya Watanzania wanazozifanya na kumekuwa na malalamiko mengi.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Serikali inamkakati gani wa kuweka kodi rafiki ili mtanzania ajivunuie kulipa kodi ili kuchangia maendeleo katika Taifa lake?
NAIBU WAZIRI FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa mazingira rafiki ya ulipaji kodi isipokuwa baadhi ya wafanyabiashara wanakuwa ni wababaishaji katika biashara zao baadhi yao, lakini nalo niseme kwamba tunalichukua kwenda kulifanyia kazi.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Tatizo la majosho lipo maeneo mengi. Halmashauri ya Mji wa Bunda, nadhani mjomba unajua kuna wafugaji wengi, lakini kuna malambo ambayo hayako kwenye hali nzuri; Kinyambwiga, Gushigwamara, Kisangwa pamoja na Rwabu: Ni lini mtayakarabati hayo malambo ili wananchi wa Bunda waweze kupata huduma ya kulishia mifugo yao?

Mheshimiwa Spika, ahsante.
WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nilishafika Bunda, nilishayaona hayo malambo, tulishaenda na Mheshimiwa Getere tukazunguka tukaona maeneo ya malambo ambayo yameharibika. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwenye mwaka ujao 2023 tuna mpango wa kukarabati malambo mengi kidogo. Pia tuna mpango wa kujenga malambo mapya, yatakuwa mengi, zaidi ya manne ambayo mlitupa bajeti ya mwaka huu. Kwa hiyo, tutafikiria kuangalia wananchi na wafugaji wa Bunda ili tuone malambo yao ambayo yameharibika ni kwa namna gani tutaweza kuyakarabati.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Mji wa Bunda imepokea kwa mikono mikubwa uhamasishaji wa Serikali wa ujenzi wa hospitali ili kusogeza huduma ya afya kwa wananchi. Najua wametenga milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya ya halmashauri kwenye Kata ya Bunda Stoo. Je, Serikali kwa mwaka huu wa fedha mko tayari kuwatengea fedha ili wananchi wa Bunda waweze kukamilisha hospitali yao ya mji ambayo iko kwenye Kata ya Bunda Stoo?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba Serikali inaendelea kujenga hospitali za halmashauri ikiwemo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda. Kama Mheshimiwa Mbunge alivyosema, tayari Serikali imepeleka milioni 500. Mpango huu ni endelevu, nasi tutaendelea kupeleka fedha kwa awamu mpaka majengo yote yakamilike ili wananchi waendelee kupata huduma bora za afya. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali dogo la nyongeza. Serikali imekuwa ikitoa kiwango cha fedha kinachofanana katika umaliziaji wa maboma yote bila kuangalia hali halisi ya gharama za ujenzi.

Je, hamuoni kuna haja ya kufanya tathmini ili kutoa fedha kulingana na gharama ya ujenzi na maeneo husika ili maboma yaweze kukamilika kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba tumekuwa tukitoa fedha kwa kiwango kinachofanana kwa maeneo tofauti na hivi sasa Serikali inafanya tathmini ya kutoa bei au BOQ kulingana na maeneo kijiografia, umbali lakini pia na gharama kutokana na maeneo hayo.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Jimbo la Bunda Mjini, limetenga eneo la Kata ya Mgeta kwa ajili ya Ukanda wa Uwekezaji, mpaka sasa hivi hawajawekeza; na Bunda pia tunavua: Kwa nini sasa Wizara isione kwamba kuna haja ya kujenga kiwanda kwa ajili ya vifaa vya uvuvi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UWEKEZAJI, VIWANDA NA BIASHARA:
Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli, kama nilivyosema kwenye jibu la msingi moja juu ya changamoto tulizonaao: Kwanza, ni mazao yenyewe yanayotokana na uvuvi kupungua; pili, kukosekana kwa viwanda ambavyo vinazalisha vifaa vya uvuvi ambavyo ndiyo teknolojia mahususi ambayo itapelekea kuvua kwa ubora zaidi mazao ya samaki.

Mheshimiwa Spika, katika mikakati ambayo tunaendelea nayo ni kuvutia wawekezaji kujenga viwanda vya kuchakata, lakini pia naamini tukifanikiwa hilo, hatua inayofuata nadhani ni kuweka sasa viwanda ambavyo vinazalisha vipuri vitakavyoweza kuzalisha zana za kuvuali Samaki katika sekta hii ya uvuvi. Kwa hiyo, nachukua hili kama sehemu ya changamoto na juhudi zetu kama Serikali, kuvutia zaidi wawekezaji katika viwanda vya kuzalisha vifaa vya kuvulia samaki katika maeneo mbalimbali hapa nchini. Nakushukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Natambua Serikali imekuwa ikitenga fedha katika ujenzi wa hospitali wa halmashauri ya Mji wa Bunda. Sasa ningependa kusikia kwa mwaka huu wa fedha nini tamko la Serikali ili hospitali ile iweze kumalizika haraka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE):
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa hospitali za halmashauri ikiwemo hospitali ya Halmashauri ya Bunda unakwenda kwa awamu. Kuna awamu ya kwanza ambapo fedha zilipelekwa, awamu ya pili majengo yapo yaliyokamilika na yako ambayo hayajakamilika. Nimhakikishie kwamba Serikali imeweka mpango mkakati wa kuhakikisha inatafuta fedha kwa awamu zinazofuata ili hospitali hizi zote zikamilike na kuwa na miundombinu inayotakiwa kutoa huduma kwa wananchi na hospitali hii ya Bunda pia itapewa kipaumbele.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru, natambua kwamba ujenzi wa barabara ya Kisorya – Nyamswa – Bunda tayari umeshafika Nyamswa, lakini bado ujenzi unatakiwa uendelee na imekomea pale Makongoro Sekondari na inatakiwa ifike mpaka Isenye. Je, ni lini sasa ujenzi huo utaendelea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ukishafika Nyamswa unapita kwenye T, aidha uende Mjini Musoma ama uende upande wa Nata. Na upande wa Nata ndiyo Isenye ambapo tayari kuna mkandarasi ambaye ameshajenga kutoka Makutano – Sanzate na Sanzate kwenda Nata tayari mkandarasi yuko site, nadhani kuna eneo Isenye pale tayari wameshajenga. Na wiki kama tatu nimekuwepo pale wakiwa wanaomba baada ya kuinua tuta wanahitaji kurekebisha maji pale, tumeshawarekebishia. Kwa hiyo, hiyo barabara iko kwenye ujenzi na mkandarasi yuko site (kilometa 40).

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, katika Jimbo la Bunda Mjini, hasa kata saba za vijijini, kumekuwa na changamoto ya umeme kutofika kwenye nyumba za wananchi, unaishia senta: -

Je, ni lini sasa mtapeleka nguzo za kutosha ili ile dhana ya umeme vijijini iwe imekamilika?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama Ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hii miradi ambayo tunaitekeleza inalenga kumfikia kila mwananchi. Lakini kwa sababu ya bajeti tuliyokuwa nayo na fedha ambayo haitoshelezi kwa wakati huu kwa maeneo yote, advancement inakwenda taratibu.

Mheshimiwa Spika, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba katika mradi wetu wa ku-electrify vitongoji vyote ambapo tunatafuta trilioni sita na bilioni mia tano, tunaamini kwamba kila mtu atafikiwa na umeme na katika miaka mitatu, minne, mitano ijayo, hakutakuwa kuna mwananchi katika kitongoji au eneo lolote ambaye hana umeme kwa sababu hiyo ndiyo azma ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Hospitali ya Manyamanyama inatoa huduma kwa wananchi wa zaidi ya Mkoa wa Mara pale Bunda Mjini, lakini wana changamoto ya nyumba ya watumishi wa afya. Ni lini sasa mtatupatia nyumba mbili ya watumishi wa afya katika Hospitali ya Manyamanyama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimwambie Mbunge hongera kwa swali lake zuri, nawakumbuka watu wake huko Bunda. Nimwambie tu kwamba kwa nafasi zilizotolewa zaidi ya 21,000 tutashirikiana na wenzetu wa TAMISEMI tuone ni namna gani tunaweza tukatatua hilo tatizo mapema zaidi kwenye nafasi zilizotoka sasa.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na changamoto sana kwenye suala la masoko hasa katika kilimo cha zao la parachichi na wakulima wamekuwa wakihangaika wenyewe. Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha kuna soko la uhakika katika zao hili la parachichi ambalo litaleta Tanzania pesa nyingi za kigeni?
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester, Mbunge wa Viti Maalum na mkulima wa parachichi kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni ukweli kwamba parachichi ni moja zao ambalo linakuwa kwa kiwango kikubwa na hivi sasa kama Serikali tuko katika hatua za mwisho tukishirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kufungua Soko la China ambalo ni soko la uhakika. Vile vile, Waheshimiwa wataona kwamba Serikali imefanya kazi kubwa ya kufungua masoko mengi katika zao la parachichi. Mwaka huu 2023 zao la parachichi export imeongezeka kutoka katika tani 8,000 mpaka tani 29,000. Kwa hiyo, sisi kama Serikali tunaendelea kuchukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto kubwa ambayo inawakabili wakulima wa parachichi sio soko tu, ni miundombinu ya uhifadhi na miundombinu ya umwagiliaji katika maeneo hayo. Nataka tu niwahakikishie kwenye bajeti mwaka kesho 2024/2025, mtaona mwaka huu 2023/2024 tunaanza kujenga common use facility, lakini mwaka 2024/2025, katika bajeti ya Wizara ya Kilimo kutakuwa na program mpya ya kuwasaidia wakulima 10,000, kuwachimbia visima na kuwapa irrigation kit za Hekta moja kwa kila mtu ili aweze kuweka katika shamba lake. Kwa hiyo Serikali inaendelea kufanya kazi hizo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Nimuulize Naibu Waziri swali dogo; Halmashauri ya Mji wa Bunda wananchi wamehamasika na wameanza ujenzi wa Sekondari mpya katika kata ya Nyamakokoto. Ni lini sasa mtamalizia majengo manne ya shule ya sekondari Nyamakokoto ili watoto wetu wa Bunda nao wapate nafasi ya kusoma vizuri?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimtoe hofu pia Mheshimiwa Mbunge wa Viti Maalum Mheshimiwa Ester Amos Bulaya ambaye amewazungumzia wananchi wa Bunda, kwamba moja ya malengo makubwa ya serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kwamba shule zote ambazo zimeanza zinapata fedha na kumaliziwa. Kwa hiyo na hilo lipo katika mpango itapelekwa fedha kwa ajili ya kuhakikisha shule hiyo inakamilika.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Miongoni mwa Wilaya ambazo hatuna chuo kipya cha VETA ni pamoja na Wilaya ya Bunda;

Je, ni lini sasa Serikali mtatujengea Chuo cha VETA katika Wilaya ya Bunda ili vijana wetu waweze kupata ujuzi na kujiajiri wenyewe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Bulaya Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kama nilivyokwisha eleza kwenye majibu ya swali la msingi, katika mwaka wa fedha 2022/2023, yaani huu tunao endelea nao, tunawilaya 64 na mkoa mmoja ambao hauna chuo cha VETA Mkoa huo ni wa Songwe. Wilaya hizi 64 miongoni mwa Wilaya ya Bunda. Kwa hiyo nikuondoe wasiwasi, katika Mkoa wa Mara tuna wilaya nne ambazo ni Serengeti, Bunda, Tarime, ndizo wilaya ambazo hazina vyuo vya VETA. Katika mwaka huu tayari tumeshapeleka fedha zile za awali na sasa tuna peleka fedha awamu ya pili kwa ajili ya kuanza ujenzi rasmi ikiwemo na chuo hiki cha Wilaya ya Bunda. Kwa hiyo nenda kawaambie wananchi Serikali ya Mama Samia iko kazini inawatendea haki wana Bunda.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Halmashauri ya Mji wa Bunda inazungukwa na Ziwa Victoria na hatuna uhaba kabisa wa maeneo. Je, Mheshimiwa Waziri, ni lini mtatujengea skimu ya umwagiliaji ikiwa ni moja ya mkakati wa kuhamasisha vijana kujihusisha na kilimo?

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti yetu tumeeleza vizuri kabisa, maeneo yote ambayo yana vyanzo vya uhakika vya maji hasa ikiwemo mito na maziwa tutahakikisha tunawawezesha wakulima wa maeneo hayo kufanya kilimo kupitia umwagiliaji. Kwa hiyo, nimwondoe hofu Mheshimiwa Mbunge juu ya eneo lake la Bunda, pia tutafanya kazi hiyo kuhakikisha kwamba wakulima wa Bunda wanafanya kilimo cha umwagiliaji.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Mheshimiwa Naibu Waziri, kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya wazee katika maeneo mbalimbali wakiwemo wa Mkoa wa Mara, kwamba hawapati ile pensheni yao kwa wakati. Je, ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha wazee hawa ambao wamelitumikia Taifa wanapata pesa yao kwa wakati?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, niombe tu kwa sababu hilo ni suala mahususi kabisa la Mkoa wa Mara, niwasiliane na Mheshimiwa Mbunge niweze kupata taarifa za kwa nini ucheleweshwaji unafanyika kwa sababu ni jambo ambalo kwa sasa tunalipa kimtandao na taarifa zinapatikana kwa wakati na tumekuwa tukilipa kwa wakati kabisa katika kipindi hicho. Kwa hiyo jambo hili litakuwa mahususi, nimwombe Mheshimiwa Ester Bulaya anipatie taarifa hizo niweze kufanya ufuatiliaji mara tu baada ya Bunge hili, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Halmashauri ya Bunda inajenga hospitali yake kwenye Kata ya Bunda Stoo na tunatambua Serikali imeshatoa bilioni moja na zinahitajika zaidi ya bilioni tatu ili ile hospitali ikamilike. Je, Serikali ina mkakati gani wa kutoa hizo pesa haraka ili hospitali ikamilike na wananchi wa Bunda wapate mahitaji sahihi na kwa karibu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama Mheshimiwa Bulaya alivyokuwa ameshasema, Serikali imeanza kupeleka fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya kule Bunda na tutaangalia katika mwaka wa fedha unaokuja huu wa 2023/2024 ni shilingi ngapi imetengwa kwa ajili ya kuendelea na ujenzi huu wa Hospitali ya Wilaya na tutahakikisha kama Serikali tunapeleka fedha mara moja kuendelea na ujenzi huo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Katika jibu ambalo Mheshimiwa Waziri ametoa, amesema wanufaika kwa sasa hivi wameongezewa pesa kwenye yale mafao ya kila mwezi, lakini lalamiko lao kubwa ni mafao ya mkupuo ambayo mmetoa asilimia 50 mpaka 30. Leo mtu anayestaafu ambaye angepaswa kulipwa shilingi milioni 100, anapata milioni 50. Huo ndiyo msingi wa swali: Ni lini mtaleta sheria mbadilishe ili wastaafu wapate asilimia 50 waweze kujikimu ili sasa wakipata hicho cha mwezi, tayari msingi utakuwa una maana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, ahsante. Nazidi kusisitiza kwamba suala hili ni la uelewa tu na elimu ambayo tutaendelea kuitoa. Mafao katika hatua ya awali katika Mifuko hii ya GEPF, PSPF, LAPF pamoja na PPF na NSSF, kila mfuko ulikuwa na aina yake ya utoaji wa mafao kulingana mfuko. Pia kwa hatua ya sasa, ukiangalia kwenye hili suala analosema la malipo ya Mkupuo, yalikuwa asilimia 25 na kwa mapenzi ya dhati Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kupitia vikao, mashirikisho ya vyama vya wafanyakazi sasa

hivi imefikia asilimia 33 ya ulipaji wa mafao hayo, hayakufika kwenye hiyo asilimia 50 ambayo anaisema kwenye hatua ya awali.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jambo hili tutaendelea kutoa elimu bila kuchoka, na wanufaika ambao ni wanachama wenyewe hawajawa na tatizo kubwa hili. Kama wapo, nazidi kusisitiza kwamba Serikali tuko tayari kuwasikiliza na kuwahudumia ili kuweza kuhakikisha manufaa hayo wanayapata. Serikali hii inawapenda sana wastaafu na ndiyo maana maboresho yamefanyika kila wakati; kisera, kisheria, kimiundo, kimfumo na utoaji. Hata kwenye utoaji sasa tumeenda katika teknolojia ya tehama, ahsante. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mbali na fisi kusumbua wananchi na kuleta madhara kwa watu wenye hifadhi pia kumekuwa na tatizo kubwa la mamba katika Ukanda wa Ziwa Victoria hasa maeneo ya Tairo na Guta Pamoja na Wilaya ya Bunda upande wa Mwibala;

Je, nini tamko la Serikali katika kuhakikisha mnaenda kuvuna mamba hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwenye upande wa mamba tumeshaanza programu ya kutengeneza vizimba na kuwafundisha wananchi namna ya kujikinga nao. Kwa sababu tatizo linajitokeza ni pale ambapo wananchi walizoea kuogelea ziwani, wengine wana mazoea ya kwenda kucheza kandokando ya ziwa. Nakumbuka enzi za zamani hasa wale tulioishi Kanda ya Ziwa, tulikuwa tuna maeneo yetu ambayo huruhusiwi kwenda kucheza maeneo hayo kwa sababu kuna Wanyama wakali hususan mamba na viboko.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kadri tunavyozidi kuongezeka wananchi wanaendelea kuyasogelea yale maeneo. Kwa hiyo tunaendelea kuwaelimisha wananchi kama yale mazoea ya wananchi ya kila siku ya Kwenda kuogelea kama ilivyo zamani tuyaache, na matokeo yake tunatengeneza vizimba kama wanaenda kuchota maji basi waende kwenye maeneo yale.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kadri tunavyozidi kuongezeka wananchi wanaendelea kuyasogelea yale maeneo. Kwa hiyo, tunaendelea kuwaelimisha wananchi kwamba, yale mazoea ya kila siku ya kwenda kuogelea kama ilivyokuwa zamani tuyaache na matokeo yake tunatengeneza vizimba, kama wanaenda kuchota maji, basi waende kwenye maeneo yale tu ambayo yameainishwa, ili kuepuka hii athari inayojitokeza ya hasa watoto wanachukuliwa na mamba na inakuwa ni athari kwa wazazi pia na kwa jamii kwa ujumla. Kwa hiyo, tunawaelimisha wananchi pia waendelee kuyaheshimu haya maeneo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo la watu wanaostaafu kuchelewa kulipwa mizigo ni kubwa, hata kwenye Ripoti za CAG ipo na tatizo la uhamisho na lenyewe ni kubwa. Kwa Mkoa wa Mara, kuna watu ambao hawajalipwa huu ni mwaka wa tatu mpaka wa nne mfululizo ikiwemo na Wilaya ya Bunda.

Je, ni lini Serikali mtalipa madeni ya mizigo na uhamisho kwa waataafu wa Mkoa wa Mara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA K.n.y. WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Ninaomba niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba Serikali ina dhamira njema ya kuhakikisha wastaafu wanalipwa stahili zao kwa wakati, ikiwemo usafirishaji wa mizigo na mafao yao ya kustaafu. Kwa hiyo, moja ya maeneo ambayo tunaweka msisitizo ni kuhakikisha kila mwaka wa bajeti tunaweka bajeti ya kutosha ili kufidia madeni ya nyuma. Pili, kuhakikisha wale wanaostaafu katika mwaka husika wanalipwa kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba, Serikali itaendelea kuwalipa kwa wakati kadri ambavyo fedha zitapatikana katika bajeti ya kila mwaka. Nakushukuru sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, Mji wa Bunda ni mji unaokua. Serikali iliahidi kujenga barabara za mitaa kwa kiwango cha lami; je, ni lini sasa Serikali itahakikisha inajenga kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, barabara za lami katika Halmashauri ya Mji wa Bunda ni jambo la msingi na Serikali ilishaahidi na imeshaanza utekelezaji kwa awamu. Najua kuna barabara za lami pale zinaunganisha mitaa, lakini nafahamu kwamba kuna uhitaji mkubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha kwamba tunajenga barabara za lami kwa kadri ya mahitaji ya Mji wa Bunda, ahsante sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante, nami niulize swali dogo la nyongeza. Waziri unacheka kwa sababu unajua ninachouliza.

Mheshimiwa Spika, Kituo cha Polisi Bunda hakina hadhi ya Wilaya na kinahudumia majimbo matatu; ni lini sasa mtatuhakikishia mnatujengea kituo chenye hadhi ya Wilaya na hii ni zaidi ya mara kumi nakuuliza wewe hapo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, nashukuru, swali analoliuliza Mheshimiwa Bulaya najua kwamba Mbunge wa Jimbo ameshaniuliza mara kadhaa pia. Namuahidi tu kwamba pale Bunda eneo kilipo Kituo cha Polisi ni eneo dogo, limebanwa na barabara, kupitia jukwaa hili, nauomba uongozi wa Wilaya ya Bunda wapate eneo la kutosha kwa ajili ya kuweka mpango wa ujenzi wa Kituo cha Polisi cha hadhi ya Wilaya, nashukuru sana. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Wananchi wa Bunda Mjini katika Kata ya Manyamanyama walianza ujenzi wa nyumba mbili za watumishi kwa nguvu zao;

Je, ni lini Serikali sasa mtakamilisha maboma hayo ya nyumba za watumishi ambayo yamekaa kwa muda mrefu kwenye Hospitali ya Manyamanyama?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Bunda Mjini na wa Kata hii ya Manyamanyama kwa kuweza kujitoa na kuanza ujenzi wa majengo ya nyumba za watumishi. Serikali itafanya tathmini ya majengo hayo kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Bunda Mjini, na pale tathmini itakapokamilika tutaona ni namna gani tunatenga fedha katika mwaka wa fedha 2024/2025.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Natambua zaidi ya bilioni 10 zimetumika katika mradi wa maji Bunda kutoka Nyabeu kuleta Mjini. Bado kuna tatizo la usambazaji katika Kata zote 14, tunahitaji shilingi bilioni saba ili kata zote 14 zipate huduma ya maji safi na salama.

Ni lini sasa Serikali mtakamilisha usambazaji? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, maeneo haya aliyoyataja Kata Saba tayari kama Wizara tunayafanyia kazi na usanifu unaendelea, tutahakikisha usambazaji hautachukua muda utakamilika ndani ya wakati. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi niulize swali dogo la nyongeza.

Wananchi walihamasika sana katika ujenzi wa vituo vya afya pamoja na zahanati. Je, Serikali hamuoni kwamba kuna haja ya kumaliza yale maboma yote nchi nzima kabla hamjaanza ujenzi mpya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe Mheshimiwa Bulaya kwamba Serikali hii ya Awamu ya Sita ya Mama Samia Suluhu Hassan ilianza ujenzi wa vituo vya afya 234 nchi nzima ambavyo vimekamilika na ilitumika gharama ya bilioni 117. Sasa tunaangalia kutafuta fedha kwa ajili ya ku-support jitihada za wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, kwa ajili ya umaliziaji wa vituo vya afya na zahanati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie tu kwa kusema kuna shilingi milioni 50 ambazo zilipelekwa katika kila Halmashauri kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati za maeneo ambayo wananchi walianza ujenzi wenyewe. Hii inaonesha ni namna gani Serikali hii ya Daktari Samia Suluhu Hassan ipo committed katika ku-support jitihada za wananchi ambazo wameanza kujipelekea maendeleo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kujenga kilometa kumi za lami kwenye mitaa ya Mji wa Bunda?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, kwa kushirikiana na wenzetu wa TAMISEMI, ipo mipango ya kutimiza hiyo ahadi ya kujenga barabara ya kilometa kumi ambazo ziliahidiwa na viongozi wetu katika Mji wa Bunda kwa kiwango cha lami. Ahsante.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kupata fursa hii kuuliza swali la nyongeza. Katika Halmashauri ya Mji wa Bunda kuna walimu takribani 28 wamekuwa wakikwama kupandishwa madaraja na ili hali kuna wenzao wamekuwa wakipandishwa madaraja kila mwaka walioajiriwa kwa mwaka mmoja. Tumelifuatilia suala hili wanasema tatizo ni mfumo na mimi nimechukua hatua ya kumpigia Katibu Mkuu Utumishi. Ningependa kujua ni lini sasa tatizo hili litaisha kwa hawa walimu 28 wa Halmashauri ya Mji wa Bunda ili waweze kupata haki yao kama wengine?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maelekezo ya Serikali ni kwamba watumishi wote wanaostahili kupandishwa vyeo wapandishwe kwa mujibu wa taratibu kama nilivyoeleza kwenye swali la msingi. Na hapa nakusudia na nimaelekezo ya Serikali, kwamba kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bunda Mji na viongozi wote katika Halmashauri nyingine zote Tanzania, maelekezo ya Serikali yako wazi na wayafate na kutotii maelekezo hayo ni kutotii uelekezo halali ya Mheshimiwa Rais, ambayo ameelekeza katika, alipokuwa anatoa maelekezo tarehe 19 Aprili, kwamba anataka wafanyakazi wote wanaostahili kupandishwa vyeo wapandishwe vyeo, wanatakiwa kufanyiwa recategorization wafanyiwe recategorization, lakini pia wale ambao kwa muda mrefu sana wamekuwa wanasubiri kuajiliwa nao pia wenye sifa za kuajiriwa, waajiriwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo maelekezo haya yote nataka nikuhakikishie Bunge sisi kama Wizara au Ofisi ya Rais, TAMISEMI tunayasimamia hayo na ni maelekezo yetu kwamba tunataka halmashauri zote nazo zisimamie na kama kuna sehemu yeyote pamekwama basi wawasiliane na Ofisi ya Katibu Mkuu Utumishi ili kuweza kushughulikia changamoto zitakazokuwa zimejitokeza. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Nimemsikia Mheshimiwa Naibu Waziri anasema Serikali iko tayari kupitia mkataba tu ambao ameusema Mheshimiwa Jesca Kishoa. Lakini Wizara yenu ina changamoto nyingi tu ya mikataba mbalimbali ambayo inahusaina na umeme na inailetea hasara Taifa hili, ikiwepo ule wa Pangea na Mgodi wa Geita na maeneo mengine. Hamuoni kwamba kuna haja sasa kama Serikali kupitia mikataba yote ili kuona tumekosea wapi huko tunakoenda nchi yetu isipate hasara na iweze kurekebisha sasa hivi, ukiwepo na mkataba wa Bwawa la Mwalimu Nyerere? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mawazo na maoni yaliyotolewa kwa niaba ya Serikali niseme ninayachukua, tutaendelea kushirikiana Serikalini kwa ajili ya kushauriana namna bora ya kuweza kuwa tunafikia mikataba yenye tija kwa watu wote. Ile ambayo itakuwa imekwisha tutahakikisha tunafanya vizuri zaidi kwa nyakati zilizopo na ambayo inaendelea tutaona namna bora zaidi ya kuifanya iwe na tija kwa watu wote.
MHE. ESTER N. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Bunda unaotoka Nyabehu hivi sasa hivi una takribani miaka 15; na mimi Ester Bulaya huu ni mwaka wa 12 naulizia mradi huu. Ni lini mradi huu utakamilika ili wananchi wa Bunda Mjini wapate maji katika kata zote 14 na usifike mwaka wa 13 nikiwa nauliza hili swali?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Bunda tayari tupo kazini na kama miaka 15 kazi haikufanyika basi Mama Samia fupa lililomshinda fisi linakwenda kutafunwa, tumejionea miradi ambayo imekuwa sugu na sasa hivi inatoa maji, hivyo, Bunda pia wakae mkao wa kufungua bomba na kupata maji safi na salama na kata zote 14 tunahakikisha zinakwenda kupata maji safi na salama. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali ndiyo ilihamasisha ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo mbalimbali nchi nzima na kuwahamasisha wananchi washiriki lakini leo hazijakamilisha. Je, mliamua kuwahamasisha wananchi bila kuwa na fedha za kutosha ndiyo maana kila Mbunge leo anaulizia kituo cha afya. Kwa nini sasa msikamilishe wakati ninyi ndiyo mliwahamasisha wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tukubaliane kwamba kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa vituo vya afya ni dhamira njema na jambo jema kwa sababu wananchi wetu wamekuwa wanasafiri umbali mrefu sana kupata huduma za afya. Kwa hiyo, kwa kuanza tu jambo hilo lilikuwa ni jema na nia njema ya Serikali lakini tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma.

Mheshimiwa Spika, mwaka uliopita maboma 555 ya zahanati Bilioni 33.5 zilipelekwa, mwaka huu tumepeleka katika maboma zaidi ya 234 ya vituo vya afya na zahanati. Mwaka ujao tunayo maboma 300 ya zahanati ambayo yanakwenda kukamilishwa. Kwa hiyo, Serikali inafanya kazi ya kukamilisha maboma hayo kwa nia njema ya kusogeza huduma kwa wananchi, lakini safari ni hatua, tutakwenda kwa awamu mpaka kukamilisha majengo hayo yote. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipatia nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani Mheshimiwa Waziri anajua Bunda kuna wachimbaji Kamkenga na Kinyambwiga naye amefika. Sasa sisi kule wachimbaji wetu wanataka watengenezewe mazingira bora ya uchimbaji, kwa sababu hali iliyoko pale siyo nzuri, na siyo kuwahamisha: Ni lini sasa mtawapatia mikopo wachimbaji wa Kinyambwiga na Gwishigwamara ili waweze kununua mashine ya kisasa na waweze kuchimba kama wachimbaji wengine kwenye maeneo mengine?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikubali kwamba Kinyambwiga na maeneo mengine aliyoyataja ni maeneo ambayo kwenye Wilaya ya Bunda ndiyo yanatupatia mapato mengi sana. Wachimbaji wa kule wanafanya kazi nzuri ya kuchimba. Pamoja na kwamba kuna changamoto kidogo za ki-management, katika eneo lile wako watu ambao wana mashamba, wako watu wenye leseni, tunakamilisha ule mgogoro ili uchimbaji uendelee kufanyika kwa tija.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikopo, ni kama nilivyoeleza kwenye jibu langu la msingi, ni lazima tukubali Waheshimiwa Wabunge kwamba, kumpatia mtu fedha ni lazima kuwe na utaratibu ambao uta-guarantee fedha hiyo kuweza kurudi na kuwakopesha watu wengine. Tusingependa kutoa mikopo ambayo mwisho wa siku fedha hizi zitapotea na aliyepewa pesa haonekani na pesa hazionekani na tunashindwa kuwakopesha wengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tungeomba Waheshimiwa Wabunge watupe muda, study hii inaendelea na Mheshimiwa Rais mwenyewe analijua jambo hili na ametupa maelekezo mahususi ya kuangalia namna bora ya kulifanyia kazi ili wachimbaji wetu waweze kupata tija.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru; Mheshimiwa Waziri Engineer rafiki yangu nadhani wananchi wa Nyatwali nilikukutanisha nao kata yao wana mradi mkubwa umekamilika na wamekuambia huo mradi haujazinduliwa, kigugumizi cha kuzindua huo mradi ni kitu gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Ni kweli Mheshimiwa Ester tulikutana na wale madiwani na wananchi wa ile kata nilikubali nitakuja tusubiri Bunge liishe tutafika na litazinduliwa kwa sababu tunahitaji wananchi wapate maji.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Moja ya sababu za kujenga ofisi na kupeleka vifaa ni pamoja na kuhakikisha huduma ya TANESCO inakuwepo kwa wananchi; sasa pale Halmashauri ya mji wa Bunda tuna ofisi lakini bado hamjaweza kutoa huduma stahiki ya umeme, watu wameomba maombi ya umeme, wana control number, lakini mpaka leo hawajaunganishiwa umeme.

Ni lini mtahakikisha huduma bora inaenda kwa wananchi na sio tu ofisi peke yake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, katika bajeti tutakayoisoma hapa siku chache zijazo itaoneshwa ni kwa kiasi gani Serikali ya Awamu Sita imejipanga kuwahudumia wananchi kwa kuongeza fedha kiasi zaidi ya bilioni 500 kwa ajili ya kupeleka huduma kwa wananchi. Kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba baada ya siku mbili ataona neema iliyoshushwa na Mheshimiwa Rais kupitia Wizara ya Nishati. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Serikali ndiyo ilihamasisha ujenzi wa vituo vya afya katika maeneo mbalimbali nchi nzima na kuwahamasisha wananchi washiriki lakini leo hazijakamilisha. Je, mliamua kuwahamasisha wananchi bila kuwa na fedha za kutosha ndiyo maana kila Mbunge leo anaulizia kituo cha afya. Kwa nini sasa msikamilishe wakati ninyi ndiyo mliwahamasisha wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza tukubaliane kwamba kuhamasisha wananchi kuchangia nguvu zao katika ujenzi wa vituo vya afya ni dhamira njema na jambo jema kwa sababu wananchi wetu wamekuwa wanasafiri umbali mrefu sana kupata huduma za afya. Kwa hiyo, kwa kuanza tu jambo hilo lilikuwa ni jema na nia njema ya Serikali lakini tumeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma.

Mheshimiwa Spika, mwaka uliopita maboma 555 ya zahanati Bilioni 33.5 zilipelekwa, mwaka huu tumepeleka katika maboma zaidi ya 234 ya vituo vya afya na zahanati. Mwaka ujao tunayo maboma 300 ya zahanati ambayo yanakwenda kukamilishwa. Kwa hiyo, Serikali inafanya kazi ya kukamilisha maboma hayo kwa nia njema ya kusogeza huduma kwa wananchi, lakini safari ni hatua, tutakwenda kwa awamu mpaka kukamilisha majengo hayo yote. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kuna baadhi ya wizara kama Wizara ya Kilimo mbali ya kwamba kuna mikopo kwenye halmashauri na mifuko mingine wao wamekuwa wakitoa motisha kwa vijana ambao wana invest kwenye kilimo. Unapozungumzia tatizo la ajira kwa graduate ni kwenye Wizara yako.

Je, hamuoni kwamba kama wizara mnapaswa kuwa na fungu maalum kwa ajili ya kuwasaidia vijana graduate wanaoenda kujiajiri wenyewe kama Wizara kama ambavyo mnavyofanya kwenye Bodi ya Mikopo na maeneo mengine? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba kujibu swali dogo la Mheshimiwa Ester Bulaya kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu kwenye swali la Mheshimiwa Shangazi, sisi Wizara ya Elimu jukumu letu ni kuhakikisha kwamba tunaratibu utaratibu wa utoaji wa elimu nchini. Wanafunzi wakishahitimu linakuwa si jukumu la Wizara ya Elimu, lakini ni jukumu la Serikali.

Kwa hiyo, kwa vile umezungumza habari ya motisha kwa vijana wetu wanaokamilisha masomo yao na kuangalia namna gani tunaweza tukaratibu taratibu zao za kuweza kujiajiri au kupata ajira, tuchukue ushauri huo, lakini Mheshimiwa Ester nadhani baada tu ya kikao hiki kuna umuhimu wa kukaa. Kwa sababu sasa hivi tunafanya mapitio ya mitaala yetu huenda kuna kitu kinakosekana nadhani na wewe unaweza kuwa na input na Mungu akipenda tarehe 13 tutakuwa na kongamano kubwa sana pale Dar es Salaam la kuhakikisha kwamba mitaala yetu ile inakwenda kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge juu ya suala hili la ajira pamoja na suala la umahiri kwenye masomo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba tuubebe ushauri wako twende tukaufanyie kazi kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo tuweze kuangalia namna gani bora ya kuweza kulifanyia kazi jambo hili. Nakushukuru sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru; Mji wa Bunda uliahidiwa kujengwa kilometa 10 barabara za mjini kwa kiwango cha lami ni lini sasa zitajengwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kusaidiana na Wizara yangu pamoja na TAMISEMI tutahakikisha kwamba ahadi iliyoahidiwa inatimizwa na Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kujenga zile kilometa 10 katika Mji wa Bunda. Ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru; ukatili katika jamii kama ambavyo umeibuka ukatili wa wahalifu wa panya road, kumeibuka ukatili mkubwa sana kwa wanawake na watoto hasa kipindi hiki wanawake wanauliwa, watoto wanafanyiwa vitendo vya ajabu, lakini bado hatujaona jitihada za dhati za Serikali kupitia Jeshi la Polisi kukabiliana na uhalifu huu wa kuwadhuru wanawake na watoto ambao wanatakiwa walelewe vizuri, wawe watumishi bora huko baadae? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli yapo matukio mengi yanaripotiwa ya uhalifu yanayohusisha mauaji, lakini na mateso kwa watoto, kwa wanawake lakini wakati mwingine hata kwa wanaume. Mimi niseme kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, uhalifu ni zao la jamii. Ipo haja ya wazazi, walezi, watu wa dini, viongozi kama sisi kwa pamoja tushirikiane kukabiliana na uhalifu huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, Jeshi la Polisi kila inapotokea kupata taarifa ya uhalifu huu, huchukua hatua bila kumchelea mtu. Kwa hiyo, niahidi tu Mheshimiwa Bulaya tutaendelea kushirikiana na wadau wa amani kokote walipo ili kudhibiti matendo ya namna hii kwenye jamii zetu. Nakushukuru sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali dogo la nyongeza. Mradi wa Maji wa Bunda kutoka Nyabeu tayari Serikali imeshafikisha Bunda Mjini, lakini changamoto kubwa iliyokuwepo ni miundombinu ya usambazaji maji, ni ya zamani, ndiyo maana mpaka leo wananchi wameshindwa kupata maji safi na salama. Je, ni lini sasa Serikali watahakikisha wanaweka miundombinu mipya ili kata zote 14 za Bunda Mjini ziweze kupata maji safi na salama? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Bulaya, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kama alivyokiri maji yameshafika mjini; lengo la Wizara ni kuhakikisha maji yakishafika katika maeneo ya mwanzoni, basi sasa usambaji utafuata na miundombinu ya zamani yote tunakwenda kuendelea na ukarabati kuhakikisha tunaleta mabomba na miundombinu ambayo itaendana na idadi ya watu waliopo kwa sasa. Hivyo, nipende kukwambia tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mwaka ujao wa fedha tutaendelea na ukarabati wa mradi huu. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, tatizo la maboma ya zahanati nchi nzima imekuwa kero na ya muda mrefu tangu 2010, je, Serikali imefanya utafiti ni yapi yanaweza kutengenezeka?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Ni kweli, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba kumekuwa na maboma mengi katika vijiji vyetu kwa ajili ya zahanati lakini kwa kweli katika kipindi cha miaka hii mitatu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amekamilisha maboma zaidi ya 900. Kwa hiyo, kazi ya Serikali ni kuendelea kutambua maboma ambayo tayari yanakidhi vigezo vya kukamilishwa na fedha zinaendelea kutengwa. Mwaka huu wa fedha shilingi bilioni 90 zimetengwa kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma hayo.

Mheshimiwa Spika, tunafanya utafiti na tutaendelea kuyakamilisha kwa awamu, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Halmashauri ya Mji wa Bunda ina mahitaji ya watumishi wa afya wakiwepo Madaktari na Manesi 402. Waliopo ni 184, mahitaji ni 218: Je, katika hizo ajira mpya katika mgao wa nchi nzima, Halmashauri ya Mji wa Bunda ni sehemu mojawapo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA: Mheshimiwa Spika, naweza kumwambia ni sehemu mojawapo ambayo inafikiriwa kupangiwa, lakini wala asiogope kwa sababu inapokwenda kuwa Hospitali ya Nyerere, ile ya Kanda ambayo inajengwa Mara nayo ni sehemu mojawapo ambayo itakwenda kupunguza mahitaji ya watumishi kwenye eneo hilo la mkoa wao.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Kwenye jibu la msingi, Waziri anasema Mbunge, aombe, mimi naamini kunakuwa kuna timu ya kufanya utafiti kutokana na vigezo. Hiyo habari ya Wabunge kuomba unakuta maeneo mengine yanagawanywa kisiasa, linaitwa Jimbo la Mjini, lina kata saba vijijini mwisho wa siku linaleta athari kwenye Mipango Miji ya maendeleo kwenye maeneo husika.

Mheshimiwa Spika, ni vigezo gani vya msingi ambavyo mnavitumia ili kuhakikisha jimbo linagawanywa kwa ajili ya kuleta maendeleo ya wananchi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, BUNGE NA URATIBU (MHE. UMMY H. NDERIANANGA) Mheshimiwa Spika, ahsante, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nilipokuwa natoa maelezo yangu ya awali nilisema Mbunge aombe, maana yake ni baada ya Tume kuweka ule utaratibu sasa utafanya uweze kuomba, lakini vigezo naomba nivitaje kama ifuatavyo: -

(i) Ukubwa wa Jimbo husika, unaangaliwa;
(ii) Mipaka ya kiutawala;
(iii) Hali ya kiuchumi kama inaturuhusu;
(iv) Hali ya Kijiografia;
(v) Upatikanaji wa mawasiliano;
(vi) Jimbo lisiwe ndani ya Halmashauri au Wilaya mbili; na
(vii) Kata moja isiwe ndani ya Majimbo mawili.

Mheshimiwa Spika, lakini lipo sharti lingine la Ofisi yako ya Bunge, kutuambia kama tunayo nafasi humu ndani yakuendelea ku-accommodate idadi kubwa zaidi ya Wabunge. Kwa hiyo, nimetaja kwa uchache naomba niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, muda utakapofika Tume ikitangaza basi vigezo na masharti vitakavyowekwa vitatuongoza kuona kwamba Jimbo hili linafaa kugawa au halifai, ahsante. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Na mimi nichukue fursa hii kuishukuru Serikali kwa kutujengea Mahakama ya Wilaya ya Bunda; imekamilika na inafanya kazi. lakini katika Wilaya ya Bunda Mahakama za Mwanzo zina hali mbaya Nansimo, Jimbo la Mwibara wanatumia Ofisi ya Kata, haifanyi kazi, Mgeta, Jimbo la Bunda Vijijini, Kabasa Jimbo la Bunda Mjini, zote zina hali mbaya.

Je, ni lini mtatujengea Mahakama ya Mwanzo?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Nipende kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwanza tupokee shukrani zako kwa kukiri kwamba Serikali inafanya kazi. Suala la uchakavu wa Mahakama za Mwanzo kama nilivyojibu muda mfupi uliyopita, ni kwamba tunaendelea na mkakati wa ukarabati kwenye majengo yale yanayowezekana kukarabatiwa. Lakini tunakwenda kuanza ujenzi wa Mahakama katika kila Makao Makuu ya Tarafa hapa nchini na ifikapo 2025 kama nilivyooeleza hapo nyuma nchi nzima tutakuwa na Mahakama katika kila Makao Makuu ya Tarafa. Lakini mbali zaidi ni kwamba maeneo yote ambayo tutayabaini yako mbali na Makao Makuu ya Tarafa, vilevile yanaenda kupata upendeleo.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tunashukuru kwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda maana tulipanga kwenye nyumba ya mtu kwa muda mrefu, tumeshaondoka na hilo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uchakavu wa Mahakama za Mwanzo hasa ambazo zimechakaa sana Mahakama ya Mwanzo Kabasa na Mcharo. Ni lini sasa mtahakikisha mtatukarabatia au kutujengea Mahakama za Mwanzo katika hayo maeneo niliyoyataja kwenye Jimbo la Bunda Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa pongezi zilizotolewa na Mheshimiwa Bulaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa Mahakama ya Bunda ya Wilaya, nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa mahakama ni kujenga na kukarabati. Kwa maana ya juhudi zilifanyika sasa na hivi karibuni Mkoa wa Mara unafahamu Mheshimiwa Bulaya, ulijengewa Intergraded Justice Centre (Kituo Jumuishi cha Mahakama), zinajengwa Mahakama, zimejengwa Mahakama Butiama, imejengwa Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama za Mwanzo, mwaka huu tutajenga Kinesi, Mugumu na tutajenga Lugangabilili. Kwa hiyo, pale fedha zitakaporuhusu mahakama uliyoitaja ya Kabasa na Mcharo zitaweza kujengwa wa upya au kukarabatiwa kulingana na kiwango cha uchakavu uliofikiwa, nashukuru.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, pale Bunda tuna mradi wa maji kutoka Nyabihu umekamilika, lakini kuna changamoto ya miundombinu na ninyi Serikali moja ya changamoto ambayo mnakabiliana nayo ni upotevu wa maji. Kuna bomba kubwa kutoka Butakale, Kata ya Bunda Stoo, unaenda Kasakwa kule kwenye tenki, Mlima Balili, inahitajika shilingi bilioni 1.7 kujenga lile bomba ambalo ni chakavu kuokoa maji yasipotee ili wananchi wa Bunda Mjini wapate maji safi na salama. Lini sasa mtatoa hizo shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya ujenzi wa bomba kuu?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Ester Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Bulaya kama Serikali tukushukuru kwa kutupatia taarifa kama hiyo. Ni mkakati wa Serikali kuendelea kuboresha miundombinu chakavu yote ambayo inatusababishia kuwa na upotevu wa maji kwa sababu tunayazalisha kwa gharama na yanapokuwa yanapotea maana yake ni kwamba Serikali inaingia kwenye hasara kubwa.

Kwa hiyo, nakuhakikishia Mheshimiwa Mbunge nalipokea hilo na nitaenda kulifuatilia ili tuone tunafanya nini kuhakikisha kwamba bomba hilo linaenda kujengwa, ahsante sana.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikichukuwa fedha kwenye mifuko na kwenda ku-invest maeneo ambayo aidha ulipaji wake, return yake inachelewa au kwenye miradi isiyokuwa na tija kabisa kama Mradi wa Dege Beach na kuleta usumbufu kwa wastaafu wanapotaka kuchukuwa mafao yao. Ni lini Serikali itafanya tathmini ya kina kwenye miradi yote na kugundua hasara iliyojitokeza kutokana na ku-invest kwenye miradi isiyokuwa na tija?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU (MHE. PASCHAL P. KATAMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru Mheshimiwa Ester Bulaya kwa mwongozo au angalizo ambalo amelitoa. Ni kweli tayari Serikali imeshaandaa mwongozo maalum wa namna ya kueleza Mifuko ya Hifadhi za Jamii ikiwemo pia taasisi nyingine za Serikali namna ya kuweza kuwekeza kupitia Benki yetu ya Taifa (BOT) na tayari mwongozo huo ndiyo unaotoa kanuni hiyo na hata kabla ya uwekezaji, hufanyika tathmini ya kuangalia mradi, lakini pia maandiko ya mradi na baadaye kwenda kwenye hatua ya kuweza kupitishwa. Kwa hiyo, zile hatua za kwenda kupitisha miradi hii inahitaji pia idhini au ithibati ya BOT na tumeendelea kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, pia suala la return on investment, kuna maeneo ambayo yanalenga zaidi katika kutoa huduma na kuleta nafuu kwa wananchi. Kwa mfano, Daraja la Kigamboni ingekuwa kama tumelenga zaidi katika faida, tungejikuta kwamba wananchi wanapata changamoto na adha ya kuhudumiwa kuliko lile lengo la Serikali la kuhakikisha kuna social welfare katika jamii.

Mheshimiwa Spika, tunaendelea pia kuweka miradi ambayo inaleta tija na miradi yote ambayo tunaendelea nayo imefanyiwa tathmini ukiacha mabadiliko mbalimbali ya hali za kiuchumi na kifedha ambazo zinatokea duniani kote.

Mheshimiwa Spika, swali la pili kuhusu suala la tathmini, tayari tumeendelea kufanya tathmini na tunayo sheria ambayo inaongoza, tunafanya actuarial evaluation kila wakati, kila baada ya miaka mitatu. Kwa hiyo, suala la tathmini nalo pia linatupa mwongozo wa kujua changamoto zilizopo au changamoto ambazo zinaweza zikaja kutokea katika uwekezaji wa miradi hii.

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho ni kuhusiana na kwamba wanacheleweshewa malipo. Sheria ya NSSF inaeleza malipo ya mstaafu yatalipwa ndani ya siku 60 na tumeshaanza kulipa hata chini ya siku 10 kwa kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA. Kwa hiyo, NSSF tumeshaboresha mambo mengi na kwa sasa changamoto za ulipaji hazipo tena.

Mheshimiwa Spika, fedha hizi zinazowekezwa siyo sehemu ya fedha ambazo zinaenda kulipa wastaafu. Kwa hiyo, mstaafu wakati wowote atakapokuwa tayari amestaafu ndani ya siku 60, sheria inaelekeza tunakuwa tumeshamlipa mafao yake na tumeshafanya hivyo, ahsante.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali. Kwenye halmashauri nyingi ambazo sisi tunakutananazo Kamati ya LAAC kumekuwa na watumishi wanaokaimu muda mrefu kiasi kwamba wanashindwa kufanya maamuzi sahihi kutokana na kukaimu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mnajaza nafasi kwenye halmashauri zote nchini ili kuwe na ufanisi na utendaji kazi ambao unaridhisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, suala la kukaimu ni kweli limelalamikiwa na Serikali tumelichukua kwa uzito mkubwa. Hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tuna zoezi la kufanya assessment nchi nzima kuona wale watumishi wanaokaimu katika nafasi mbalimbali. Wale watakaokuwa wamekidhi vigezo, tayari Serikali imeandaa utaratibu wa kuwa-confirm na wale ambao watakua hawajakidhi vigezo basi utaratibu mwingine wa kujaza nafasi zile utafanyika. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kata ya Nyatwali yenye Vijiji vitatu, Tamau, Serengeti na Nyatwali, imekuwa katika mgogoro mrefu wa kusubiria malipo, lakini vilevile wamekuwa wakiilaumu Serikali kwamba, wanataka kulipa fidia ndogo, tathmini wamefanya zaidi ya mwaka na tunasikia kuanzia Tarehe 05 wana mpango wa kuwalipa. Wanataka kujua wanalipwa kwa fidia ipi? Ileile ya malalamiko, mbali ya kwamba, wamekiuka taratibu zaidi ya miezi sita na hawajawalipa? Nakushukuru.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali dogo la nyongeza la Mheshimiwa Bulaya, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, taratibu za fidia zinafahamika kwa mujibu wa Sheria. Uthaminishaji unapofanyika wananchi wanapaswa kulipwa kwa vigezo hivyo, lakini kama malipo yatakuwa yamechelewa zaidi ya miezi sita, upo utaratibu wa kuwalipa pamoja na riba, kwa ajili ya kufidia muda uliopotea. Ninamwomba Mheshimiwa Mbunge awe na imani kwamba, wananchi watapatiwa haki yao kama vile wanavyostahili. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, katika ajira mpya, tungependa kujua kwa Jimbo la Bunda Mjini tutapata mgao hasa katika walimu wa sayansi na hesabu?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Spika, naomba nichukue nafasi hii kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba, katika Jimbo la Bunda naye atapata mgao wa walimu wa shule za sekondari na shule za msingi. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali. Kwenye halmashauri nyingi ambazo sisi tunakutananazo Kamati ya LAAC kumekuwa na watumishi wanaokaimu muda mrefu kiasi kwamba wanashindwa kufanya maamuzi sahihi kutokana na kukaimu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuhakikisha mnajaza nafasi kwenye halmashauri zote nchini ili kuwe na ufanisi na utendaji kazi ambao unaridhisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Spika, suala la kukaimu ni kweli limelalamikiwa na Serikali tumelichukua kwa uzito mkubwa. Hivi sasa kupitia Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, tuna zoezi la kufanya assessment nchi nzima kuona wale watumishi wanaokaimu katika nafasi mbalimbali. Wale watakaokuwa wamekidhi vigezo, tayari Serikali imeandaa utaratibu wa kuwa-confirm na wale ambao watakua hawajakidhi vigezo basi utaratibu mwingine wa kujaza nafasi zile utafanyika. Nakushukuru sana. (Makofi)
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mara ni mkoa wenye historia katika nchi hii, kwani anatoka Muasisi wa Taifa letu Baba Julius Kambarage Nyerere. Tumeona mkiwa mnamuenzi kwa matembezi na kwa vitu mbalimbali. Sisi watu wa Mkoa wa Mara, moja ya kumuenzi Baba wa Taifa ni kuhakikisha mnakamilisha Uwanja wa Ndege wa Musoma kwa kiwango cha lami. Ni lini mtatenga fedha za kutosha kuhakikisha Uwanja wa Ndege wa Musoma unakamilika? Wabunge tumechoka kushukia Mwanza.
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Ester Bulaya kwa swali lake ambalo ameuliza kwa umakini mkubwa. Serikali hii ya Awamu ya Sita inatambua, inazingatia na inafahamu umuhimu wa Baba wa Taifa. Pia inatumbua umuhimu wa viwanja vya ndege nchi hii, ndiyo maana pamoja na viwanja vyote nilivyosema vinaendelea kujengwa na kukarabatiwa, Uwanja wa Ndege wa Musoma upo, umeshatengewa fedha na unajengwa. Hivi ninavyozungumza, upo 60%. Labda ninachoweza kumhakikishia, ni kuiagiza mamlaka inayosimamia iharakishe ujenzi huo ukamilike ili uweze kuanza kutumika.
MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi nami niulize swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tunashukuru kwa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Bunda maana tulipanga kwenye nyumba ya mtu kwa muda mrefu, tumeshaondoka na hilo tatizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna uchakavu wa Mahakama za Mwanzo hasa ambazo zimechakaa sana Mahakama ya Mwanzo Kabasa na Mcharo. Ni lini sasa mtahakikisha mtatukarabatia au kutujengea Mahakama za Mwanzo katika hayo maeneo niliyoyataja kwenye Jimbo la Bunda Mjini? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kwa pongezi zilizotolewa na Mheshimiwa Bulaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ujenzi wa Mahakama ya Bunda ya Wilaya, nimweleze tu Mheshimiwa Mbunge kwamba mpango wa mahakama ni kujenga na kukarabati. Kwa maana ya juhudi zilifanyika sasa na hivi karibuni Mkoa wa Mara unafahamu Mheshimiwa Bulaya, ulijengewa Intergraded Justice Centre (Kituo Jumuishi cha Mahakama), zinajengwa Mahakama, zimejengwa Mahakama Butiama, imejengwa Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mahakama za Mwanzo, mwaka huu tutajenga Kinesi, Mugumu na tutajenga Lugangabilili. Kwa hiyo, pale fedha zitakaporuhusu mahakama uliyoitaja ya Kabasa na Mcharo zitaweza kujengwa wa upya au kukarabatiwa kulingana na kiwango cha uchakavu uliofikiwa, nashukuru.