Answers to Primary Questions by Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA) (54 total)
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Katika mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa Mkoa wa Katavi uliofanywa na Halmashauri ya Mpanda mwaka 2004 kwa kushirikisha ngazi ya Mkoa na ngazi ya Wizara, zililipwa sehemu za Hifadhi za Misitu North East Mpanda (JB94) na Msanginia (JB215) na ramani mbalimbali kuidhinishwa ikiwemo 48870, 48893 na 40250.
Je, ni lini Serikali itabadili mipaka hiyo kwa mujibu wa Sheria ya Misitu ya 2002 (Namba 14) Kifungu cha 28?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni mara yangu ya kwanza kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu naomba nichukue nafasi hii kwanza kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa uhai na kuniwezesha kufika siku hii ya leo. Pili, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe Magufuli kwa kuniamini na kuniteua katika nafasi hii. Tatu, nimshukuru Mheshimiwa Spika pamoja na uongozi mzima wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Wenyeviti wa Kamati nilizokuwa Mjumbe kwa malezi yao ambayo wameyatoa kwangu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Misitu wa hifadhi wa Mpanda North East na Msangimya ni misitu ya Serikali inayosimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Msitu wa North East Mpanda umehifadhiwa kwa tangazo la Serikali Na. 296 la mwaka 1949. Aidha, Msitu wa Msangimya umehifadhiwa kwa Tangazo la Serikali Na. 447 la mwaka 1954 na inasimamiwa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 Sura ya 323.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Mpanda ilipima maeneo ya Hifadhi ya Msitu wa Mpanda North East na Msangimya kupitia ufadhili wa Shirika la Africare chini ya mradi wa Ugalla Ecosystem ili kuanzisha maeneo ya usimamizi wa Wanyamapori (Wildlife Management Area- WMA) na makazi pamoja na kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji. Baada ya upimaji huo ramani 48870, 48893 na 40250 zilichorwa na Halmashauri husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya nia njema iliyokuwepo ya kuwapatia wananchi makazi yaliyopimwa kwa mujibu wa sheria na uanzishwaji wa maeneo ya usimamizi wa wanyamapori (WMA) na kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji, utaratibu huu haukuzingatia Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 pamoja na Sheria ya Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009. Kwa mujibu wa kifungu cha 31(1) cha Sheria ya Wanyamapori, WMA zote zinaanzishwa kwenye misitu iliyoko kwenye ardhi ya kijiji au ardhi ya ujumla na siyo kwenye misitu ya Hifadhi ya Serikali Kuu. Aidha, mpango wa matumizi bora ya ardhi ya kijiji inafanyika kwenye ardhi ya kijiji husika na siyo kwenye misitu iliyohifadhiwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili ardhi ya msitu wa hifadhi uweze kutumika kwa matumizi mengine, Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 katika kifungu cha 29 inatoa utaratibu wa kisheria wa kufuta hadhi ya msitu wa hifadhi ambapo Waziri wa Maliasili na Utalii anaweza kufuta sehemu ya msitu au msitu wote wa hifadhi baada ya kujiridhisha kuna umuhimu ya kufanya hivyo. Mara baada ya mchakato huu kukamilika ndipo ardhi ya msitu itatumika kwa matumizi na shughuli zingine za kibinadamu mbali na uhifadhi. Aidha, Waziri wa Maliasili na Utalii atatoa maamuzi hayo baada ya kushauriana na Kamati ya Taifa ya Ushauri wa Misitu (National Forestry Advisory Committee) ambayo inatajwa katika Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002 katika Kifungu cha 10.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mchakato wa kupima sehemu ya misitu ya hifadhi niliyoeleza hapo juu umefanyika kinyume cha sheria na taratibu zilizopo, hadhi ya misitu hiyo ya hifadhi inaendelea kubaki kisheria kama ilivyoainishwa kwa mujibu wa matangazo ya Serikali niliyoyataja hapo juu. Aidha, Serikali itaangalia kama kunaweza kuwa na uwezekano wa maeneo hayo kutolewa kwa ajili ya matumizi mengine kwa mujibu wa sheria, lakini ikiweka kipaumbele kwanza kitatolewa kwa maslahi mapana ya Taifa na kwa kufuata ushauri utakaotolewa na Kamati ya Taifa ya Ushauri ya Misitu.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Katika Wilaya ya Mbogwe kuna Kitalu cha Kigosi North kilichopo katika Pori la Akiba la Kigosi.
(a) Je, ni lini Serikali itaanza kulipa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe asilimia 25 ya ada ya uwindaji?
(b) Je, ni lini Serikali italitengeneza greda lililoko Kifura Kibondo Makao Makuu ya Mapori ya Kigosi Moyowosi ili lisaidie matengenezo ya barabara ndani ya mapori haya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imekuwa na utaratibu wa kutoa fedha kiasi cha asilimia 25 kwenye Halmashauri za Wilaya zinatokana na malipo ya ada ya wanyamapori (game fees) wanazowinda kwenye maeneo yanayopakana na Wilaya husika kwa ajili ya kusaidia shughuli za maendeleo na uhifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kitalu cha Kigosi North kimekuwa kikitumika kwa ajili ya utafiti wa madini uliokuwa unafanywa na Kampuni ya TANZAM na siyo kwa shughuli za uwindaji wa kitalii. Hali hiyo inafanya Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe isipate fedha za asilimia 25 kwa ajili ya uwindaji wa kitalii katika kitalu hicho. Kitalu cha Kigosi East ndiyo kitalu kilichotengwa kwa shughuli za uwindaji wa kitalii kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2018. Hata hivyo, mwekezaji katika kitalu hicho amejaribu kuleta wageni mara mbili mwaka 2013 na 2014 kwa ajili ya kuwinda lakini hakuweza kuwinda kutokana na kuwepo kwa ng’ombe wengi badala ya wanyamapori katika kitalu hicho. Kwa sababu hiyo, hakuna wanyamapori waliowindwa kwa kipindi cha mwaka 2013 hadi 2016 kutokana na kuwepo kwa ng’ombe na hivyo kitalu husika kurudishwa Serikalini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na jitahada za Serikali za kuondoa mifugo katika maeneo yote ya hifadhi, ni wazi kuwa mazingira ya asili pamoja na wanyamapori watarejea na hivyo kuwezesha kitalu hicho kutumika kwa uwindaji wa kitalii kuanza kufanyika. Kufanyika kwa uwindaji wa kitalii katika kitalu hicho kutawezesha upatikanaji wa fedha ambazo zitaweza kuanza kuwasilishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe. Wizara yangu inatoa wito kwa Wilaya zote zenye uvamizi wa mifugo kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kuhakikisha mifugo inaondolewa ili kurejesha hadhi ya vitalu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kutengeneza greda, Wizara yangu tayari imeshatengeneza greda lililopo Kifura katika Pori la Akiba Moyowosi Kigosi na sasa linafanya kazi.
MHE.BALOZI ADADI M. RAJAB aliuliza:-
Vitalu vya miti ya tiki – Lunguza Muheza huuzwa kwa njia ya mnada hali inayosababisha viwanda vidogo vidogo vya Muheza kukosa miti.
(a) Je, ni lini Serikali itahakikisha wenye viwanda katika maeneo hayo wanapata vitalu ili kulinda ajira za wanavijiji?
(b) Je, kwa nini wanaopata vitalu wasichane magogo hayo hapo Wilayani ili kulinda viwanda vidogo vidogo vya Muheza?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Balozi Adadi Mohamed Rajab, Mbunge wa Muheza lenye sehemu na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye biashara ya miti ya misaji, njia mbili ambao ni mnada na makubaliano binafsi hutumika. Mbinu mbalimbali zimekuwa zikitumika katika kuuza miti ya misaji ili kuongeza bei ya miti kwa kutumia ushindani wa bei iliyopo sokoni. Hivyo, ili kupata bei ya soko, mbinu inayotumiwa ni pamoja na kuuza kiasi kidogo cha ujazo wa miti ya kuvuna kwa njia ya mnada. Hivyo, asilimia 30 ya malighafi inayotarajiwa kuvunwa katika shamba husika huuzwa kwa utaratibu huu. Njia hii inasaidia kubaini nguvu ya soko na kuongeza mapato ya Serikali. Njia ya makubaliano binafsi hutumika pia katika uuzaji wa miti mara baada ya bei ya soko kupatikana katika mnada. Hivyo asilimia 70 huuzwa kwa makubaliano binafsi ili kutoa fursa kwa wadau wengi zaidi kushiriki kwenye biashara hiyo. Utaratibu huu kwa kiasi kikubwa umewawezesha wenye viwanda wanaoshindwa kununua kupitia njia ya mnada kupata malighafi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza wigo wa soko la ndani, Wizara imeanzisha utaratibu utakaowawezesha wanunuzi wengi wa miti ya misaji walioko nchini kunufaika. Utaratibu huu unawalenga wale wote wenye viwanda vinavyotengeneza samani vilivyopo nchini. Hivyo, katika mwaka wa fedha 2017/2018 asilimia 10 kati ya asilimia 70 ya ujazo wa miti uliotengwa kwa ajili ya kuuzwa kwa njia ya makubaliano binafsi utauzwa kwa watengenezaji wa samani ndani ya nchi ili kuongeza thamani ya mazao yao na kuongeza ajira. Matangazo ya mauzo ya miti hufanyika kwa kubandika katika mbao za matangazo na kutolewa katika magazeti kwa muda wa siku 14 kabla ya mauzo. Wenye nia ya kuvuna na wenye kumiliki mashine za kupasua magogo ikiwemo wana vijiji wanaozunguka shamba letu la miti la Mtibwa na Longuza hupewa matangazo hayo kuhusu mnada huo ili nao waweze kujitokeza katika kununua.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kulinda viwanda vya ndani na kuongeza ajira kwa Watanzania, uchakataji wa magogo yanayovunwa katika mashamba ya miti hufanyika ndani ya nchi. Baada ya kuuziwa malighafi kutoka katika mashamba ya miti, uchakataji hufanywa na mteja mwenyewe kulingana na mahali alipoweka kiwanda chake. Sheria na mwongozo wa uvunaji wa mazao ya misitu haimlazimishi mwenye kiwanda kujenga kiwanda mahali malighafi inapopatikana.
Nashauri Waheshimiwa Wabunge, tuendelee kuhimiza Halmashauri zetu ziweke mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa katika maeneo yaliyo karibu na mashamba ya miti ili kuongeza ajira kwa wananchi wanaoishi karibu na mashamba hayo.
MHE. MWANNE I. MCHEMBA aliuliza:-
Mkoa wa Tabora umepata usafiri wa uhakika wa ndege ya ATCL na kwa kuwa Tabora ina historia mbalimbali na kumbukumbu za mambo ya kale.
Je, Serikali ipo tayari kuutangaza Mkoa wa Tabora kwa utalii?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwanne Ismail Mchemba, Mbunge wa viti maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora umo katika Kanda ya Kati inayounganisha Mikoa ya Dodoma, Singida na Kigoma. Ni kweli kabisa kuwa Mkoa wa Tabora kama sehemu ya Kanda ya Kati una historia mbalimbali na kumbukumbu za mambo ya kale ikiwa ni pamoja na Tembe lililokaliwa na missionary Dkt. Livingstone, ambaye ni mpinga biashara ya utumwa kutoka Uingereza mwaka 1871 akiwa njaini kuelekea Ujiji - Kigoma. Pia kuna kituo cha njia ya kati ya biashara ya utumwa na vipusa vilivypo Ulyankulu eneo la Mtemi Mirambo na Gofu lililokuwa hospitali ya kwanza ya Kijerumani katika Mkoa wa Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tembe la Dkt. Livinstone limekarabatiwa na kuna Watumishi ambao wanatoa maekelezo kwa wageni wanaotembelea kituo hicho. Katika mwaka wa fedha 2013 hadi 2017 kituo kilitembelewa na wageni 1,642 na jumla ya shilingi 2,292,000 zilikusanywa kutoka kwa watalii wa ndani na nje. Aidha, mipango ya usimamizi wa maeneo mengine niliyoyataja hapo juu imeandaliwa ili yaendelezwe kuwa vituo vya kumbukumbu na taarifa kwa matumizi mbalimbali yakiwemo ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ufanisi wa utangazaji, utalii wa Mkoa wa Tabora juhudi za utangazaji zinahusu vivutio vingine zaidi ya vivutio vya mambo ya kale vinavyopatikana katika eneo hilo. Juhudi hizo zinahusu utamaduni, wanyamapori, mazao ya nyuki na historia pana ya harakati mbalimbali za kijamii za nchi yetu zilizofanyika Mkoani Tabora.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa juhudi za kuendeleza na kuutangaza Mkoa wa Tabora kiutalii zimekuwa zikiendelea hata kabla ya kuwepo kwa usafiri wa ndege ya ATCL. Kwa kuwa sasa Mkoa umepata usafiri wa uhakika wa ndege ya ATCL, Serikali itaongeza juhudi za kuutangaza Mkoa wa Tabora nje na ndani ya nchi ili kuhakikisha wageni wengi wanatembelea Mkoa huo kwa lengo la kukuza utalii na kuongeza pato la Taifa.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Wanyama hasa Tembo wamekuwa wakiharibu sana mazao ya wananchi kwa fidia ndogo sana ya Sh. 20,000 kwa heka na hii hupunguza ushiriki wa wananchi katika kuzuia ujangili ndani ya Hifadhi:-
Je, Serikali imejipangaje kukaa vizuri na wananchi wa vijiji vinavyopakana na Hifadhi ili kuwa na ushirikiano katika kuzuia ujangili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kutambua umuhimu wa maisha ya binadamu, mazao na mifugo imeweka utaratibu wa kulipa kifuta jasho na machozi kwa uharibifu unaosababishwa na wanyamapori wakali na waharibifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, Serikali kupitia halmashauri zake za Wilaya na taasisi zilizo chini ya Wizara ya maliasili na utalii imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuelimisha jamii kuhusu uhifadhi na sheria zake ikwemo za kufukuza wanyamapori mara inapotokea wameingia katika makazi ya wananchi.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa uhifadhi kutoa elimu kwa wananchi juu ya kutumia pilipili na ufugaji wa nyuki kandokando ya mashamba ili kuzuia wanyama hususani tembo kuingia mashambani. Elimu hii ilianza kutolewa katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ili kufanya zoezi hili kuwa endelevu vikundi 23 vilisaidiwa kuanzisha Mfuko wa Kuweka na Kukopa na fedha wanayopata isaidie kununua baadhi ya vifaa vinavyotumika kuzuia wanyama kuingia mashambani pamoja na kuviwezesha vikundi kiuchumi ili visaidiwe katika kuzuia ujangili.
Mheshimiwa Naibu Spika, kati ya vikundi vilivyoanzishwa, kumi vimepata usajili toka halmashauri ya wilaya na vingine 13 bado vinaendelea kushughulikia usajili wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imetoa mizinga 180 kwa wananchi wa Kijiji cha Maharaka ikiwa ni kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wananchi katika kutekeleza maazimio ya kutumia pilipili na mizinga ya nyuki kuzuia tembo kuingia katika mashamba yao. Vilevile elimu inaendelea kutolewa katika Vijiji vya Mikumi, Mkata na Ihombwe ili nao kutumia mfumo wa pilipili katika mashamba yao.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuzishauri Halmashauri za Wilaya kuajiri Askari Wanyamapori na kuwapatia vitendea kazi ili waweze kusaidia wananchi pale kunapojitokeza tatizo la uharibifu wa mazao na mifugo kuvamiwa na wanyamapori.
MHE. PHILLIPO A. MULUGO aliuliza:-
Ziwa Rukwa lina wanyama wengi aina ya mamba waliofugwa humo ambao husababisha vifo kwa wananchi waishio pembezoni mwa ziwa hilo, wakiwemo wananchi wa Songwe na Serikali imekuwa ikitoa vibali vichache kuvuna mamba hao:-
(a) Je, kwa nini Serikali isiongeze idadi ya kuvuna mamba hao ili kuwapunguza?
(b) Kwa kuwa vifo vingi vya wakazi wa maeneo hayo vinatokana na kuliwa na mamba na Serikali haitoi mkono wa pole kwa wananchi walioathirika na vifo hivyo; je, Serikali haioni haja ya kuwafikiria wafiwa hao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimwa Philipo Augustino Mulugo, Mbunge wa Songwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, uwindaji wa mamba katika mbalimbali nchini hufanyika kwa kuzingatia takwimu kuhusu idadi ya mamba kwa mujibu wa sensa zinazofanywa katika maeneo husika. Lengo la uwindaji wa mamba ni pamoja na kupunguza madhara yanayosababishwa na wanyama hao kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu kupitia taasisi ya utafiti wa wanyama pori Tanzania TAWIRI, imepanga kufanya sensa ya mamba na viboko kwa nchi nzima kwa mwaka wa fedha 2017/2018. Sensa hii inalenga kubaini idadi ya wanyama hao ili kuwezesha upangaji wa mgao utakaovumwa. Maeneo yatakayohusika katika sensa hii, ni maeneo ya maziwa na mito yote ikiwemo Ziwa Rukwa ambako kwa sasa inaonekana kuwa na tatizo la mamba.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu hufanya malipo ya kifuta machozi na jasho kwa wahanga baada ya kupata taarifa zenye takwimu ya matukio ya wananchi kuuawa au kujeruhiwa na mamba kutoka kwenye maeneo husika. Malipo hayo hufanyika kwa mujibu wa Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009 na kanuni za kifuta jasho na machozi za mwaka 2011. Aidha, malipo hayo hayawahusu watu waliopoteza maisha au kujeruhiwa wakati wakifanya shughuli ambazo haziruhusiwi kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 71(3) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
Mheshimiwa Spika, Wizara yangu imeandaa mikakati ya muda mfupi na muda mrefu ya kukabiliana na wanyama pori wakali wakiwemo mamba katika Ziwa Rukwa…..
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa rai kwa Waheshimiwa Wabunge na Mamlaka za Wilaya husika ili ziwasilishe nyaraka zinazothibitisha wananchi kuathirika na wanyamapori wakali ili Serikali iweze kuchua hatua sitahiki.
MHE. VENANCE M. MWAMOTO aliuliza:-
Je, ni kiasi gani cha fedha kinatolewa kwa Wilaya ambazo zinapakana au zilizo na Hifadhi za Taifa ikiwamo Wilaya ya Kilolo katika Hifadhi ya Udzungwa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Venance Mwamoto, Mbunge wa Kilolo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Maliasili na Utalii, kupitia Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), inatekeleza Mpango wa Ujiarni Mwema (Support for Community Initiated Projects) ulioanzishwa mapema miaka ya 1990. Lengo la mpango huu ni kuishirikisha jamii katika kupunguza changamoto za uhifadhi na kuwanufaisha wananchi waishio jirani na hifadhi. Utekelezaji wa Mpango wa Ujirani Mwema unahusisha vijiji katika Wilaya zinazopakana na Hifadhi za Taifa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, vijiji vinaibua miradi ya maendeleo na kuchangia asilimia 30 ya gharama za miradi na shirika kuchangia asilimia 70 ya gharama hizo. Kupitia mpango huu kila mwaka TANAPA inatenga kati ya 5% hadi 7% ya bajeti yake kwa shughuli za miradi hiyo. Vilevile mpango huu unahusisha utoaji wa elimu ya uhifadhi na kuwashirikisha wananchi katika uhifadhi wa maliasili na mazingira kama vile upandaji wa miti na kadhalika.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2000/2001 hadi mwaka 2017/2018 Hifadhi ya Taifa ya Udzungwa imefanikiwa kutekeleza miradi ya ujirani mwema katika Wilaya ya Kilolo yenye thamani ya jumla ya shilingi 435,962,656. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa Wilaya ya Kilolo inahusu uwekaji wa umeme, ujenzi wa barabara, ununuzi wa samani na ununuzi wa vifaa vya maabara vya Sekondari ya Lukosi katika Kijiji cha Mtandika ambapo jumla ya shilingi 49,460,937 zimetumika.
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa nyumba wa awamu za walimu katika Kijiji cha Ikura umegharimu shilingi 60,000,000; ukarabati barabara ya Ilula – Udekwa, ujenzi na ununuzi wa samani Kituo cha Polisi, nyumba ya walimu, shule ya msingi katika Kijiji cha Udekwa umegharimu shilingi 227,501,719 na mpango wa matumizi bora ya ardhi na nyumba ya walimu shule ya msingi Msosa katika Kijiji cha Msosa shilingi 81,000,000 na ununuzi wa madawati kwa ajili ya Wilaya ya Kilolo umegharimu shilingi 18,000,000. Jumla ya fedha zote zilizotolewa na Shirika ni shilingi 435,962,656.
MHE. RAPHAEL J. MICHAEL aliuliza:-
Je, Serikali imejipanga vipi kumaliza madai ya msingi na ya muda mrefu kwa waongoza watalii, wapagazi na wapishi kutambuliwa kwa kima cha chini cha mishahara, mikataba ya kazi inayoendana na kazi zao, malipo ya posho kwa huduma wanazotoa kwa siku, sera shirikishi katika kutatua matatizo yao na utalii wa nchi kwa ujumla na malipo ya huduma za jamii kama vile afya na majanga?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII MAJIBU alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Raphael Japhary Michael, Mbunge wa Moshi Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, madai ya wapagazi, wapishi na waongoza watalii yameshughulikiwa na Wizara kwa kushirikiana na Vyama vya Tanzania Association of Tour Operators (TATO); Kilimanjaro Association of Tour Operation (KIATO); Tanzania Tour Guides Association (TTGA); Kilimanjaro Guides Association (KGA); Tanzania Porters Organization (TPO); Ofisi ya Waziri Mkuu, (Kazi Ajira, Vijana na Ulemavu) na Vyama vya Wapagazi na Wapishi.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkutano uliofanyika Arusha tarehe 12 Desemba, 2015 Wizara na wadau walikubaliana kuhusu viwango vya chini vya ujira kwa wapagazi wapishi na waongoza watalii. Viwango vinavyopendekezwa kwa siku ni shilingi sawa na dola za Marekani 10 kwa wapagazi 15; kwa wapishi na 20 kwa waongoza watalii kwa siku.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika makubaliano hayo, Serikali ilisisitiza juu ya umuhimu wa kuingia mikataba ya kazi baina ya waajiri na waajiriwa. Serikali ilitoa miongozo ya mikataba ili izingatiwe kwa mujibu wa matakwa ya kila kundi na ilianza kutumika katika Sekta ya Utalii. Waajiri na wajiriwa wanatakiwa kisheria kutekeleza wajibu wao wa kusaini mikataba na kuzingatia viwango vilivyokubaliwa. Endapo makubaliano yao hayatazingatiwa, ni wajibu wa waajiriwa kutoa taarifa kwenye mamlaka husika za Serikali.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kima cha chini cha mishahara na malipo ya posho kwa huduma za jamii kama vile afya na majanga, Serikali inaendelea kuhimiza kuwa waajiri wazingatie kima cha chini cha mishahara kilichotolewa na Serikali na michango inayopaswa kutolewa kwenye mifuko mbalimbali kama vile Shirika la Taifa la Hifadhi wa Jamii (NSSF), Bima ya Afya na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
MHE.DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Migogoro ya ardhi na mipaka ya vijiji na hifadhi bado imeendelea kuwa tatizo sugu licha ya kuwepo kwa ahadi na kauli mbalimbali na Serikali.
Je, mgogoro wa Pori la Akiba Kijereshi na Sayanka katika Wilaya ya Busega utatatuliwa lini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba la Kijereshi lenye ukubwa wa kilometa za mraba 65.7 ililtangazwa rasmi na tangazo la Serikali Na. 215 la mwaka 1994. Pori hilo lilikabidhiwa rasmi kwa Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori mwaka 2005 kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu. Pori la Akiba la Kijereshi limepakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kwa upande wa Kaskazini na Kijiji cha Lukungu upande wa Mashariki, Mwamalole, Mwakiroba, Kijilishi, Igwata na Muungano upande wa Kusini Mashariki mwa pori hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, uvamizi wa mapori haya ya akiba kwa kilimo, makazi na ufugaji umesababisha ongezeko la matukio ya wanyamapori kuharibu mazao na kudhuru wananchi. Aidha, hali hii imesababisha migogoro baina ya wananchi na mamlaka ya usimamizi wa wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua migogoro kati ya wakulima, wafugaji na maeneo ya hifadhi nchini Serikali imechukua hatua mbalimbali. Wizara kwa kushirikiana na wananchi imetambua na kuweka mipaka kwenye maeneo ya hifadhi ikiwemo Pori la Akiba la Kijereshi na Hifadhi ya Msitu wa Sayanka. Hadi mwisho wa Januari, 2018 jumla ya vigingi 74 vimesimikwa katika pori la Akiba Kijereshi, Aidha, katika Hifadhi ya Msitu wa Sayanka jumla ya vigingi 67 vimesimikwa, hatua hii imesaidia kupunguza migogoro ya mipaka kati ya wananchi na hifadhi.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, tatizo lililobaki kwa sasa ni baadhi ya wananchi kutaka kulima na kuanzisha makazi ndani ya Hifadhi ya Misitu ya Sayanka na wengine kutaka kulima ndani ya mita 500 kutoka mpaka wa Pori la Akiba la Kijereshi kinyume cha Sheria ya Misitu na Wanyamapori.
Wizara kwa kushirikiana na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Busega na Halmashauri ya Wilaya ya Busega inaendelea kutoa elimu na kufanya vikao na mikutano na wananchi wanaozunguka Pori la Akiba Kijereshi. Mikutano hiyo inalenga kuwakumbusha wananchi umuhimu wa uhifadhi na kuepusha kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 500 kutoka mpaka wa pori la Akiba. Katazo hilo ni kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009. Aidha, Serikali inatoa wito kwa wananchi kuacha kuvamia maeneo ya hifadhi ili kudumisha uwepo wa bioanuai kwa faida yetu ya sasa na vizazi vijavyo. (Makofi)
MHE. GOODLUCK A. MLINGA aliuliza:-
Sehemu kubwa ya Jimbo la Ulanga imezungukwa na Hifadhi ya Selous Game Reserve hivyo kufanya wananchi wa Kata za Mbuga, Ilonga, Kataketa na Lukunde kukosa maeneo ya kilimo.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia wananchi wa maeneo hayo maeneo ya kilimo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Goodluck Mlinga, Mbunge wa Ulanga, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba Selous lilianzishwa kati ya mwaka 1896 na 1912 na Serikali ya Kikoloni ya Wajerumani. Wajerumani waliligawa pori hilo katika maeneo manne ambayo ni Ulanga, Kusini, Muhoro na Matandu. Mnamo mwaka 1951 pori hili lilisajiliwa rasmi kwa GN Na. 17 chini ya Fauna Consveration Ordinance CAP. 302.
Mheshimiwa Naibu Spika, Pori la Akiba la Selous ni muhimu sana kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni siyo tu kwa Taifa letu bali pia Kimataifa. Pori linaliingizia Taifa fedha za Kitanzania na za kigeni kupitia utalii, lina misitu ya Ilindima inayosaidia upatikanaji wa maji, linachangia kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi na makazi na mazalia ya viumbe hai wakiwemo wanyamapori, samaki na viumbe wengine. Kutokana na umuhimu huo Umoja wa Mataifa umelitambua eneo hili kuwa urithi wa dunia. Sambamba na hilo Serikali ya Kikoloni ilianzisha pori tengefu la Kilombero mwaka 1952 ili kuunganisha mfumo wa kiikolojia katika maeneo hayo awili.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kutatua changamoto za matumizi ya ardhi katika maeneo yaliyotajwa, Serikali inatekeleza mpango wa Kilombero na Lower Rufiji Wetlands Ecosystem Management Project, mradi huu unahusisha kutatua matatizo ya mipaka ya vijiji na mapori ya hifadhi yaliyo katika Wilaya ya Ulanga, Malinyi na Kilombero pamoja na kuwawezesha wananchi kumiliki ardhi kupitia hati miliki za kimila.
Aidha, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia mradi wake wa Land Tenure Support Programme (LTSP) inaendelea kuhakiki mpaka wa pori tengefu la Kilombero ambalo ni sehemu ya Wilaya ya Ulanga na kupima ardhi ya vijiji kwa ajili ya urasimishaji wa ardhi kwa wananchi na hatimaye kupata hati za kumiliki. Serikali inaamini kuwa kupitia miradi hii miwili changamoto ya matumizi ya ardhi kwa shughuli za kilimo, ufugaji na makazi zitatatuliwa kikamilifu.
MHE. JOSEPH R. SELASINI (K.n.y. MHE. JAMES F. MBATIA) aliuliza:-
(a) Je, kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita Mlima Kilimanjaro umeliingizia Taifa mapato ya fedha kiasi gani kwa njia ya utalii?
(b) Je, ni asilimia ngapi ya mapato hayo yametumika kuweka miundombinu endelevu ya kuuhifadhi Mlima huo?
(c) Je, ni asilimia ngapi ya mapato hayo yametumika katika dhana nzima ya ujirani mwema katika kutoa huduma zinazokuza utu wa wananchi wanaozungukwa na Mlima huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Vunjo, lenye sehemu (a), (b) na (c) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Hifadhi Taifa Tanzania (TANAPA) ni Shirika la Umma ambalo limeanzishwa kwa Sheria Na. 482 ya mwaka 1959 na kufanyiwa marejeo na kuwa Sheria Na. 282 ya mwaka 2002. Shirika linatekeleza majukumu yake ya uhifadhi na kuendeleza utalii katika Hifadhi za Taifa 16.
Kati ya Hifadhi hizo ni hifadhi tano tu ndizo zinazokusanya mapato ya ziada yanayotumika kuendesha Hifadhi za Taifa nyingine 11. Hifadhi hizo ni Serengeti, Mlima Kilimanjaro, Tarangire, Ziwa Manyara na Arusha. Mapato yaliyotokana na Mlima Kilimanjaro na fedha zilizotumika kuweka maendeleo endelevu ya kuhifadhi mlima na kiasi kilichotumika katika dhana ya ujirani mwema kwa wananchi wanaozunguka mlima huo ni kama ifuatavyo:-
(a) Mapato ya Hifadhi ya Kilimanjaro katika kipindi cha miaka kumi, yaani kuanzia mwaka 2007/2008 hadi mwaka 2016/2017 ilikuwa ni shilingi bilioni 471.5.
(b) Fedha zilizotumika kutekeleza majukumu ya uhifadhi ikiwa ni pamoja na kuweka miundombinu ya kuendeleza mlima ni shillingi bilioni 67.5 ambazo kati ya hizo shilingi bilioni 20.89 zilitumika kwa maendeleo na shilingi bilioni
46.6 zilitumika katika uendeshaji wa hifadhi.
(c) Fedha zilizotumika katika kuendeleza miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo jirani na Hifadhi ya Kilimanjaro ni shilingi bilioni 2.28.
MHE. ORAN M. NJENZA aliuliza:-
Kuna mgogoro wa muda mrefu wa ardhi kati ya TANAPA na Wananchi wa Kata za Ilungu, Igoma, Uleuje na wananchi walikuwa tayari kuachia ardhi yao ili upanuzi wa Hifadhi ya TANAPA lakini Serikali imeshindwa kuwalipa wananchi hao fidia:-
(a) Je, ni lini Serikali itafanya tathmini mpya ya fidia kwa wananchi wa Ilungu, Igoma na Uleuje?
(b) Kama Serikali imeshindwa kulipa fidia; je, ni lini itarudisha eneo hilo kwa wananchi wa Kata hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge Oran Manase Njenza, Bunge wa Mbeya Vijijini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa Kitulo ilianzishwa mwaka 2005 ili kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya Bonde la Ziwa Nyasa, Bonde la Usangu na Mto Ruaha Mkuu ili kuhifadhi baioanuai ya aina za mimea adimu zikiwemo Chitanda. Hifadhi ya Taifa Kitulo imejumuisha maeneo yaliyokuwa yakimilikiwa na taasisi za Serikali. Maeneo hayo yanajumuisha Msitu wa Livingstone, Msitu wa Numbe na eneo lililokuwa shamba la mifugo (Diary Farming Company-DAFCO).
Mheshimiwa Mwenyekiti, tathmini iliyofanywa na Mkoa wa Mbeya kufuatia malalamiko ya wananchi wa Kijiji cha Kikondo, Kata ya Ilungu ilibaini kuwa kuna baadhi ya wananchi ambao taarifa ziinaonesha kuwa hawakulipwa fidia mwaka 1965 wakati shamba la DAFCO lilikuwa linaanzishwa. Serikali inakusudia kufanya uthamini kwa wananchi mwezi Februari mwaka 2018 ambao hawakulipwa fidia mwaka 1965. Aidha, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na uongozi wa Mkoa wa Mbeya itahakikisha kuwa fidia inalipwa katika mwaka wa fedha 2017/2018.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Kumekuwa na mgogoro wa mipaka katika Pori la Hifadhi ya North Ugala, Wilayani Urambo, Kata ya Nsenda, Kijiji cha Kangome, Kitongoji cha Lunyeta. Mgogoro huo umesababishwa na mipaka mipya iliyowekwa na hivyo kusababisha upungufu wa eneo la shughuli za kilimo na ufugaji.
(a) Je, Serikali inafahamu kuwepo wa mipaka ya zamani ambayo haikuzingatiwa wakati wa kuweka mipaka mipya?
(b) Je, ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mipaka ili wananchi wapate eneo la kutosha kwa ajili ya kilimo na ufugaji?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo lenye sehemu
(a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu wa Hifadhi ya North Ugala unapatikana katika Wilaya za Urambo na Kaliua. Msitu huu unaomilikiwa na Serikali Kuu chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na una ukubwa wa hekta 163,482.39 na ulianzishwa rasmi 1956 na kuchorewa ramani ya JB Namba 307 ya tarehe 22/10/1956.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu wa North Ugala umehifadhiwa kutokana na umuhimu wake hasa katika kuhifadhi vyanzo vya maji, mapito (shoroba) za wanyamapori hasa wanapohama kutoka katika Mapori ya Akiba ya Kigosi, Ugala na Rungwa kuelekea Pori la Akiba la Rukwa, Lukwati hadi Hifadhi ya Taifa ya Katavi iliyopo Mkoani Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, hifadhi hii inatumika katika uzalishaji na uvunaji wa mazao ya misitu ikiwemo asali, nta, mbao na mkaa. Serikali iliagiza kuweka vigingi kwenye mipaka yote ya Hifadhi za Taifa, misitu, mapori ya akiba na tengefu. Katika hifadhi ya msitu wa North Ugala, vigingi viliwekwa na baadae kuwaondoa wananchi wote waliokuwa wamevamia hifadhi hiyo. Baada ya kupitia na kuweka vigingi katika mpaka, ilionekana kwamba mpaka umenyooka kutoka kigingi namba 5 hadi 6 na kupitia katika mpaka wa vijiji vya Izengabatogilwe, Isongwa, Azimio, Mtakuja, Ifuta, Utenge, Tumaini, Kamalendi, Igombe, Zugimlole na Uyumbu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mpaka mpya uliowekwa bali vigingi viliwekwa kwa mujibu wa GN iliyounda hifadhi hiyo. Ili kumaliza migogoro kati ya hifadhi na wananchi wanaopakana na hifadhi ya misitu; Serikali itaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa misitu, ushirikishwaji wa wananchi katika uhifadhi, kuimarisha mipaka kwa kuweka vigingi na mabango ya tahadhari, kupanda miti mipakani, kushirikiana na sekta nyingine katika kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi na kuhamasisha ufugaji na kilimo cha kisasa. (Makofi)
MHE. MWANTUMU DAU HAJI aliuliza:-
Kumekuwa na sintofahamu ya matumizi ya ardhi pamoja na masharti maalum yanayotakiwa katika mapori yetu hususan kwa wawekezaji na wananchi wanaozunguka hifadhi na mapori tengefu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza tatizo hili?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mwantumu Dau Haji, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, maeneo ya hifadhi na mapori tengefu yametengwa kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.
Aidha, uwekezaji katika hifadhi, mapori ya akiba na tengefu, maeneo ya wazi yenye wanyamapori, maeneo ya Jumuiya ya Hifadhi na Wanyamapori (WMAs) husimamiwa na sheria hiyo. Sheria na Kanuni husika hutoa taratibu za usimamizi wa maeneo hayo muhimu kwa maslahi ya uhifadhi, maliasili na mazingira, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi kupitia matumizi endelevu. Mwekezaji anapaswa kupata kibali na leseni ya kumruhusu kuendesha shughuli za utalii kutoka mamlaka zinazohusika kabla ya kuanza biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali inapitia upya kanuni na taratibu za uwekezaji katika maeneo ya hifadhi na mapori tengefu, miongoni mwa kanuni zinazopitiwa ni pamoja na Kanuni ya Jumuiya za Hifadhi Wanyamapori (WMAs).
Aidha, Serikali iko katika hatua za mwisho katika maandalizi ya kanuni za maeneo ya mapito (shoroba) ya wanyama na mtawanyiko wa wanyamapori.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara itaendelea kutoa elimu kwa wawekezaji na wananchi wanaozunguka maeneo yaliyohifadhiwa. Aidha, natoa wito kwa wawekezaji kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo ili kuepukana na migogoro ya ardhi baina ya wanavijiji, wawekezaji na Mamlaka za Hifadhi.
MHE. RICHARD P. MBOGO aliuliza:-
Serikali imeendelea na juhudi mbalimbali za kulinda Nyara za Serikali:-
Je, vitalu vya uwindaji vinachangia kiasi gani katika upotevu wa Nyara za Serikali?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Richard Philip Mbogo, Mbunge wa Nsimbo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwindaji wa kitalii ni sehemu ya matumizi endelevu ya wanyamapori na unafanyika kwa mujibu wa Sera ya Wanyamapori ya Mwaka 2007, Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori, Sura 283 na Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za Mwaka 2015 zikisomwa kwa pamoja, pamoja na marekebisho yake ya mwaka 2017. Ili uwindaji uweze kufanyika, kampuni iliyopewa kitalu huomba na kupatiwa mgao wa wanyamapori (quota) watakaowindwa katika msimu husika. Mgao wa wanyamapori huandaliwa na Kamati ya Ushauri wa Mgao wa Wanyamapori (Quota Allocation Advisory Committee).
Mheshimiwa Mwenyekiti, vigezo vinavyotumika kutoa mgao ni pamoja na; moja, idadi ya wanyamapori (population status) kulingana na sensa; pili, taarifa kutoka kwa Maafisa Wanyamapori wa maeneo yanayohusika; tatu, mafanikio katika matumizi ya mgao wa wanyamapori (offtake levels); nne, ukubwa wa nyara zinazopatikana mwaka hadi mwaka (trend of trophy size) na tano, matakwa ya Mikataba ya Kimataifa kama vile CITEs.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imeweka udhibiti wa kutosha ili kuzuia uwezekano wa kupotea nyara wakati wa uwindaji. Udhibiti huo unaanzia kwenye kutoa vibali ambavyo ni vya kielektroniki, usimamizi porini wakati wa uwindaji ili kuhakikisha aina na idadi ya wanyamapori wanaowindwa waliotolewa kwenye kibali inazingatiwa, umilikishwaji wa nyara zilizowindwa na ukaguzi wa nyara kabla ya kusafirishwa kwenda nje ya nchi. Aidha, pale inapotokea ukiukwaji wa sheria na kanuni wahusika hufikishwa mbele ya sheria na adhabu stahiki hutolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imeendelea kuongeza udhibiti katika usimamizi wa uwindaji wa kitalii kwa kutumia sheria na kanuni ambazo wanyamapori huwindwa kwa kuzingatia jinsi, umri na ukubwa wa nyara. Udhibiti huo umesaidia kupunguza uwezekano wa wanyamapori kupungua kutokana na kuwindwa na pia kumesaidia kupatikana kwa mapato yatokanayo na uwindaji wa kitalii. Hivyo basi, vitalu vya uwindaji husaidia katika kulinda na kuhifadhi nyara na kutoa mchango katika uchumi wa nchi, hasa kwa kuchangia fedha za kigeni, kutoa ajira kwa wananchi na kuchangia maendeleo ya jamii.
MHE. HAWA M. CHAKOMA aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya urithi wa Dunia wa Kisiwa cha Kilwa Kisiwani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kisiwa cha Kilwa Kisiwani kinapatikana katika Wilaya ya Kilwa Mkoa wa Lindi. Kisiwa hiki kina utajiri wa magofu ya kale yaliyoorodheshwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia mwaka 1981 na Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni yaani UNESCO.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha urithi wa Dunia wa Kilwa Kisiwani unaendelea kuwepo, Serikali imetekeleza mipango ifuatayo:-
(a) Kukarabati majenzi yaliyoorodheshwa kwenye Urithi wa Dunia. Ukarabati unafanywa na vijana wa Kitanzania kutoka Kisiwa cha Kilwa Kisiwani ambao wamepata mafunzo kutoka kwa wataalam wa UNESCO. Aidha, katika mwaka wa fedha 2018/2019, Wizara itajenga Ofisi itakayotumiwa na watumishi wa Urithi wa Dunia wa Kituo cha Magofu ya Kilwa Ksiwani na Songo Mnara.
(b) Kutangaza magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara ndani na nje ya nchi ili kuvutia watalii. Serikali imeandaa jarida la karibu Kilwa (Kilwa District heritage resources) linaloonyesha picha na maelezo ya vivutio vya utalii vilivyopo Wilayani Kilwa yakiwemo magofu ya Kilwa Kisiwani. Jarida hili linatolewa kwa wageni wanaotembelea Kilwa pamoja na kutumika kutangaza utalii wa Kilwa katika maonyesho ya ndani ya Sabasaba na Nanenane.
Mheshimiwa Spika, aidha, Serikali sasa imeandaa mpango wa kuuza utalii wa malikale na wanyamapori kwa pamoja yaani one package. Kilwa Kisiwani itanufaika na mpango huu kwa kuunganishwa na package ya Pori la Akiba la Selou.
(c) Kushirikisha jamii ya Kilwa Kisiwani kuhifadhi na kujipatia kipato kupitia malikale zilizopo kwenye Urithi wa Dunia. Serikali itawapa fursa za ajira na mafunzo katika fani ya ukarabati wa majenzi, kuongoza wageni, huduma za chakula na fani nyingine za ujasiriamali. Elimu waliyoipata itawasaidia kuanzisha ofisi ya kuongoza wageni Kilwa Masoko na wengine wanafanya kazi za ukarabati wa magofu ya Urithi wa Dunia Kilwa Kisiwani.
MHE. MAGDALENA H. SAKAYA aliuliza:-
Serikali imeunda timu ya wataalam kutoka Wizara nne kupitia nchi nzima kuangalia hadhi za hifadhi zetu (Mapori ya Akiba na Hifadhi za Msitu) ili kuja na mpango utakaondoa kabisa migogoro ya ardhi inayotokea kati ya Hifadhi na Wafugaji, Wakulima na Hifadhi na watumiaji wengine.
(i) Je, ni lini kazi hiyo itakamilika?
(ii) Je, mpaka sasa Timu hiyo imetembelea maeneo mangapi na ni mikoa gani?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali iliunda timu ya Kitaifa kwa ajili ya kushughulikia migogoro ya ardhi hapa nchini. Timu hiyo ilijumuisha wataalam kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Maliasili na Utalii, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Tume ya Taifa ya Takwimu.
Mheshimiwa Spika, kazi ya timu hii ni pamoja na kutembelea mikoa yote yenye migogoro; Kupitia na kuchambua kwa kina taarifa na mapendekezo yaliyowahi kutolewa na Kamati, Tume au timu mbalimbali kuhusu utatuzi wa migogoro nchini; Kuainisha vyanzo vya migogoro iliyopo; Kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro ya muda mrefu pamoja na kukutana na wadau mbalimbali katika maeneo hayo; na Kutoa ushauri na mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Mheshimiwa Spika, mpaka sasa timu imefanikiwa kupitia taarifa mbalimbali za migogoro; kutembelea Wilaya 20, Halmashauri 24, Kata 40, Vijiji 74 na kufanya majadiliano na wadau 1,106 katika Mikoa ya Morogoro, Kagera, Geita, Tabora na Katavi. Taarifa ya Timu imekamilika na mapendekezo yamewasilishwa katika Wizara husika kwa utekelezaji.
Mheshimiwa Spika, jumla ya migogoro 1,750 ilifanyiwa uchambuzi. Kati ya hiyo 564 ilihusu uvamizi wa maeneo ya hifadhi; 218 mwingiliano wa mipaka ya kiutawala; 366 uanzishwaji wa vijiji ndani ya maeneo ya hifadhi; 204 migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji; migogoro 206 ilihusu wananchi na wawekezaji kwenye maeneo ya ranchi, mashamba na migodi; na migogoro 115 inatokana na madai ya fidia. Vilevile kulikuwa na migogoro 77 ambayo inatokana na mchanganyiko wa vyanzo mbalimbali.
Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara husika itaendelea kushirikiana na wadau wakiwemo wananchi kufanyia kazi mapendekezo ya timu ili kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi iliyopo na inayoendelea kujitokeza nchini. Ni matumaini yangu kwamba utatuzi wa migogoro kwa njia shirikishi utasaidia kuondoa migogoro iliyopo kati ya wananchi, maeneo yaliyohifadhiwa na wawekezaji.
MHE. OSCAR R. MUKASA aliuliza:-
Serikali inakusudia kuyaondolea hadhi ya uhifadhi baadhi ya maeneo ya hifadhi kwa kuwa yamepoteza sifa hiyo. Kwa mujibu wa kauli ya Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii alipokuwa akihutubia huko Benaco Wilayani Ngara, Mkoa wa Kagera mnamo tarehe 22 Desemba, 2015.
(a) Je, Serikali imeshaanza kuandaa mpango kupitia Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ili kuhakikisha kuwa kuna matumizi yenye tija na usawa baina ya wakulima na wafugaji pindi maeneo hayo yatakapokuwa huru ili kukuza uchumi na kuondoa hatari ya uvunjifu wa amani unaotokana na mgawanyo usio sawia kama ilivyo sasa?
(b) Je, kama Serikali imeshaanza kuandaa mpango huo, ipo tayari kuzishirikisha mapema Halmashauri za Wilaya zitakazoguswa na jambo hili ili nazo zianze kufanya maandalizi ya suala hili kwa ngazi yao?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya hifadhi yameanzishwa na kutangazwa kisheria kwa kuzingatia umuhimu wake kiikolojia, kiuchumi, kiusalama na kijamii kwa maslahi ya Taifa. Aidha, baadhi ya maeneo yanakabiliwa na uvamizi unaotokana na shughuli za kibinadamu kama kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hali hii imesababisha baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa kupoteza sifa ya kuendelea kuhifadhiwa. Kutokana na hali hiyo, Wizara yangu ilifanya tathmini ya maeneo hayo na kubaini jumla ya mapori tengefu 12 yalipoteza sifa na hivyo kuanzisha mchakato wa kuyarudisha kwa wananchi ili yatumike kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Wizara yangu imepanga kufanya tathmini ya maeneo yaliyopoteza sifa kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI). Maeneo yaliyohifadhiwa pamoja na vitalu vya uwindaji wa kitalii yatafanyiwa tathmini ili kubainisha yale yote yaliyopoteza sifa za kuendelea kuwa hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya tathmini kukamilika, Serikali itaandaa mpango ambao utahusisha Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Halmashauri za Wilaya ili kuhakikisha kuwa maeneo yatakayoondolewa hadhi ya uhifadhi yanatumika ipasavyo.
MHE. PROF. NORMAN S. KING aliuliza:-
Hifadhi ya Kitulo iliyoko Mkoa wa Njombe, Wilaya ya Makete ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu na ni hifadhi ya kipekee katika Afrika kwa sababu ina aina tofauti ya maua zaidi ya 120.
Je, ni lini TANAPA kwa kushirikiana na TANROADS itaona umuhimu wa kujenga kwa lami barabara ya kutoka Chimala – Matamba – Kitulo – Makete ili kurahisisha uingiaji wa watalii kwenye mbuga hiyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Profesa Norman Sigalla King, Mbunge wa Makete, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inakubaliana na hoja ya Mheshimiwa Mbunge kwamba, kujenga barabara ya Chimala – Matamba – Kitulo kwa kiwango cha lami ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yetu na hasa jamii zitakazotumia barabara hiyo ikiwa ni pamoja na hifadhi ya Kitulo. Napenda kuchukua fursa hii kumwarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa kwa hivi sasa Wizara yangu ina mchakato wa kuboresha miundombinu ya barabara, utalii na utawala kwenye hifadhi zetu, mojawapo ikiwa ni Hifadhi ya Kitulo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jukumu la ujenzi wa barabara zilizo nje ya hifadhi ni jukumu la Halmashauri za maeneo husika ikishirikiana na TANROADS. Kutokana na hali halisi ya mapato ya Shirika la Hifadhi ya Taifa, Hifadhi ya Taifa haina uwezo wa kuchangia ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kama alivyoomba Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na changamoto hiyo, Wizara yangu itaendelea kushirikiana na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili barabara hiyo iwekwe kwenye mpango wa ujenzi wa lami. (Makofi)
MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani juu ya wanyama waharibifu hususan tembo ambao wamesambaa hovyo katika Jimbo la Mtera na kufanya uharibifu mkubwa pamoja na kuua watu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Joseph Lusinde, Mbunge wa Jimbo la Mtera kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanyamapori wakali na waharibifu limekuwa likijitokeza kwenye Wilaya zaidi ya 80 hapa nchini. Wanyamapori wakali na waharibifu ambao kwa kiwango kikubwa wamekuwa wakileta madhara kwa maisha ya binadamu na uharibifu wa mazao yao kisheria ni tembo, mamba, nyati, kiboko, simba, fisi na faru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ongezeko la watu limesababisha kuzibwa kwa shoroba za wanyamapori pamoja na maeneo ya mazalia na mtawanyiko wao. Kuzibwa kwa shoroba hizo kumeongeza migogoro baina ya binadamu na wanyamapori. Hali hiyo kwa ujumla wake imeongeza ukubwa wa tatizo la mwingiliano kati ya binadamu na wanyamapori hususan tembo na hivyo kusababisha matukio mengi ya uharibifu wa mali na upotevu wa maisha ya binadamu katika maeneo mbalimbali likiwemo Jimbo la Mtera.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali itaendelea kufanya doria za kudhiti wanyamapori katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chamwino. Pia Wizara itaendelea kutoa elimu ya njia nyingine za kudhibiti tembo zikiwemo matumizi ya mizinga ya nyuki, uzio wa kamba uliopakwa mchanganyiko wa pilipili na oil chafu kuzunguka mashamba na kuchoma matofali ya kinyesi cha tembo kilichochanganywa na pilipili. Moshi unaotokana na uchomaji wa matofali ya kinyesi chenye pilipili ni mkali na hivyo hufukuza tembo mashambani kwa mafanikio makubwa. Njia hizi mbadala zimeonesha mafanikio makubwa pale zinapotumika vizuri na kwa wakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na mikakati hiyo, Serikali itaendelea kutoa fedha za kifuta jasho kwa uharibifu wa mali, yaani mazao na mifugo na kifuta machozi kwa wahanga waliouwawa au kujeruhiwa na wanyamapori hao. Kwa mfano, mwaka wa fedha 2017/2018 Wizara yangu imelipa jumla ya shilingi 7,520,000 kwa wananchi 27 wa Wilaya ya Chamwino walioathirika na wanyamapori.
MHE. AMINA S. MOLLEL aliuliza:-
Je, ni kwa kiwango gani Serikali imetekeleza agizo la Bunge la kukusanya kodi katika huduma za mahoteli kwenye Hifadhi za Taifa kwa njia ya Concession Fee Fixed Rate?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Amina Saleh Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ukusanyaji wa Tozo ya Concession Fees kwa utaratibu mpya wa Fixed Rate ulianza kutekelezwa tarehe 1 Julai, 2017 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na.234 la mwaka 2017. Kwa mujibu wa Tangazo hilo, kila mgeni anatozwa kati ya Dola za Kimarekani 25 na 50 kulingana na hadhi ya hifadhi husika. Kwa mfano, Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ni Dola za Kimarekani 25 na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ni Dola 50 za Kimarekani. Kwa hivi sasa wawekezaji wote wanalipa tozo hiyo kwa viwango vilivyoainishwa katika Tangazo hilo la Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kiasi cha Tozo ya Concession Fees kilichokusanywa katika kipindi cha Julai, 2017 hadi Machi, 2020 kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ni shilingi bilioni
18.8 ikilinganishwa na shilingi bilioni 6.9 iliyokusanywa katika kipindi hicho mwaka 2016/2017. Hili ni ongezeko la shilingi bilioni 11.9 ambazo ni sawa na 174%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyokusanywa kutoka katika makusanyo ya Tozo ya Concession Fees kwa kipindi hicho ni shilingi bilioni 3.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho cha mwaka wa fedha 2016/2017 ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.2 zilikusanywa na kupelekwa TRA.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Bagamoyo ni mji mkongwe wenye vivutio vya kitalii kama ilivyo miji mingine nchini kama vile Zanzibar, Kilwa na Mapango ya Amboni, Tanga.
Je, Serikali ina mkakati gani wa kuboresha vituo vya kitalii nchini ikiwemo Bagamoyo ili kupata wageni wengi zaidi na kukuza pato la Taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Bagamoyo ni moja ya miji mikongwe katika historia ya utamaduni na maendeleo ya Tanzania ukiwa kando kando ya Bahari ya Hindi. Bagamoyo ni moja ya vituo vya Malikale ambavyo ni mojawapo ya vivutio vya utalii hususani wa utamaduni hapa nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, vivutio hivyo havitumiki ipasavyo katika kukuza utalii kutokana na changamoto mbalimbali ambazo ni ufinyu wa bajeti, ukosefu wa huduma muhimu kwa watalii, kutofikika, kuchakaa kwa vioneshwa na kutotangazwa ipasavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia changamoto hizo, Wizara imeandaa mkakati wa kuvitambua na kuvitangaza vivutio vyote nchini ukiwemo Mji wa Bagamoyo. Mpango huu unalenga kushirikisha mashirika yaliyo chini ya Wizara, yaani Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, vivutio vya malikale vilivyo Bagamoyo ni miongoni mwa maeneo yatakayoendelezwa kwa ushirikano na mashirika hayo. Aidha, vivutio vyote vya utalii nchini vitaendelea kutangazwa kupitia taasisi zinazohusika ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania (TTB). Kazi zitakazotekelezwa na mashirika hayo ni pamoja na kuweka huduma muhimu kwa watalii, kuboresha miundombinu ya vituo hususani majengo na barabara ili kuwezesha kufikika kwa urahisi na kuwa na mwonekano unaovutia; kujenga vituo vya kumbukumbu na taarifa pale ambapo vinahitajika, kuboresha vioneshwa na kuvitangaza na kuhamasisha wawekezaji wa hoteli, michezo na vivutio vingine vya watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mkakati huu, Wizara itaendelea kusimamia majukumu yote ya uhifadhi, utafiti na kuandaa taarifa zitakazosaidia kuboresha na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini, kwa kutoa elimu kwa umma juu ya uhifadhi na matumizi endelevu ya malikale na maliasili za nchi yetu. (Makofi)
MHE. LEAH J. KOMANYA aliuliza:-
Serikali hupeleka katika Halmashauri zilizopo katika Hifadhi ya Wanyamapori asilimia 25 ya fedha zitokanazo na mapato ya uwindaji wa kitalii na upigaji picha pasipo Halmashauri husika kujua msingi wa tozo hizo.
• Je, ni lini Serikali itaanza kupeleka takwimu ya mapato yanayopatikana ili Halmashauri ziweze kujua stahiki zake?
• Je, ni kiasi gani cha mapato kimepatikana kutokana na Maswa Game Reserve na Hifadhi ya Makao na kiasi gani kilipelekwa katika Wilaya ya Meatu kila mwaka kuanzia mwaka 2015 hadi 2017?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Leah Jeremiah Komanya, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara imekuwa ikitoa mgao wa asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ada za wanyamapori wanaowindwa kwenye vitalu vilivyopo kwenye maeneo ya Wilaya husika. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017 Wilaya ya Meatu ilipata mgao wa shilingi 40,017,158 na shilingi 41,696,616.43 sawia ikiwa ni asilimia 25 ya mapato yatokanayo na wanyamapori waliowindwa katika vitalu vya Mbono na Kimali katika Pori la Akiba la Maswa na Makao WMA.
Mheshimiwa Mwenyekiti, takwimu za mapato yanayotokana na wanyamapori waliowindwa na upigaji picha katika vitalu vya uwindaji na utalii wa picha nchini huandaliwa na kutolewa taarifa mbalimbali. Aidha, Wizara ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mfumo wa kielektroniki ujulikanao kama MNRT Portal ambapo taarifa zinazohusu Wizara ikiwa ni pamoja na mapato ya uwindaji wa kitalii zitapatikana humo. Mfumo huo unatarajiwa kuzinduliwa rasmi tarehe 1 Julai, 2018. Aidha, nakala ngumu zitatumwa kwenda Wilaya husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe wito kwa Halmashauri nchini zinazopata mgao huu kutumia asilimia 40 ya fedha hizo kwa ajili ya shughuli za uhifadhi ikiwa ni pamoja na ulinzi wa maisha ya wananchi na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali kama ilivyokubalika.
MHE. DKT. RAPHAEL M.CHEGENI aliuliza:-
Kwa muda mrefu kumekuwepo na migogoro mingi kati ya Hifadhi za Taifa na wananchi ambao ni wakulima na wafugaji hali inayosababisha uvunjifu wa amani:-
(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa tatizo hili linapata ufumbuzi endelevu hasa maeneo ya Lamadi, Makiloba, Kijereshi na Nyamikoma katika Wilaya ya Busega?
(b) Baadhi ya wanyama kama tembo wamekuwa wakifanya uharibifu wa mali na mazao ya wananchi wanaoishi maeneo hayo. Je, Serikali inatoa tamko gani la kuzuia tatizo hilo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Masunga Chegeni, Mbunge wa Busega, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Lamadi, Mwakiloba, Nyamikoma na Kigereshi yanapakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Pori la Akiba la Kijereshi, hivyo kuna muingiliano kati ya wanyama pori na binadamu jambo linalosababisha migogoro. Aidha, maeneo yaliyohifadhiwa yanakabiliwa na changomoto nyingi ikiwemo uvamizi unaotokana na shughuli za kibinadamu kama kilimo na mifugo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumaliza tatizo la migogoro ya mipaka, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wananchi na wadau wengine, inayo nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba migogoro kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi inatatuliwa. Kazi hii inahusisha kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji vyote vinavyozunguka hifadhi, kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, kuimarisha miradi ya ujirani mwema na kupitia upya mipaka iliyopo katika maeneo yenye migogoro. Kazi ya kupitia mipaka na kuweka vigingi kwa sasa itaendelea kwa ushirikishwaji wa wadau wote muhimu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na madhara yanayosababishwa na wanyamapori hususan tembo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kunusuru maisha na mali za wananchi waishio kando ya Hifadhi ya Serengeti na Pori la Akiba la Kijereshi kama vile kuimarisha Timu ya Udhibiti wa Wanyamapori Hatari na Waharibifu ambao inajumuisha watumishi kutoka Kikosi dhidi ya Ujangili Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Kigereshi na Halmashauri ya Wilaya, pia kwa kutumia ndege zisizo kuwa na rubani kwa ajili ya kufukuza tembo. Lengo ni kuhakikisha kwamba tukio lolote la uvamizi wa tembo linashughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inaendelea kusizitiza kuhusu umuhimu wa kuepuka kufanya shughuli za kibinadamu kwenye shoroba za wanyamapori na maeneo ya mipaka ya hifadhi ya vijiji. Aidha, Wizara imeandaa kanuni za kutenga na kuhifadhi shoroba na maeneo ya mtawanyiko ili kuruhusu mwingiliano wa kiikolojia kati ya wanyamapori utakaoimarisha utofauti wa vinasaba pamoja na kuboresha ustawi endelevu wa bioanuai.
MHE. MARGARET S. SITTA aliuliza:-
Wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopakana na hifadhi za misitu katika Wilaya ya Urambo wamepitia migogoro mingi ya mipaka na hata kuchomewa nyumba na mali:-
Je, ni lini Serikali itamaliza migogoro ya mipaka katika Kata za Nsenda, Uyumbu na Ukondamayo ili wananchi waendelee na kilimo pamoja na shughuli nyingine za kuwaletea maendeleo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Margaret Simwanza Sitta, Mbunge wa Urambo, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Nsenda na Ukondamoyo ni mojawapo ya kata zinazopakana na Msitu wa Hifadhi wa North Ugalla. Msitu wa Hifadhi wa North Ugalla ulitengwa mwaka 1956 ukiwa na hekta 278,423.3 na kusajiliwa kwa ramani namba 307 chini ya Wilaya ya Tabora. Mwaka 2008 eneo la mpaka wa kaskazini mwa msitu ulipunguzwa kwa zaidi ya umbali wa kilomita tano, sawa na eneo la hekta 114,940.91 kwa ajili ya matumizi ya wananchi. Hivyo, mwaka 2008 eneo la msitu wa North Ugalla lililobaki ni hekta 163,482.39 kwa ramani 2,567 iliyosajiliwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msitu huu umehifadhiwa kwa madhumuni ya kutunza ardhi na udongo eneo la lindimaji (catchment area), kuhifadhi bioanuai, kurekebisha hali ya hewa, kuzalisha mazao ya timbao na yasiyo ya timbao kwa ajili ya kutumiwa kwa utaratibu maalum.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2014, wananchi waliovamia msitu huo waliondolewa kwa mujibu wa Sheria ya Misitu Namba 14 ya mwaka 2002. Hatua zilizochukuliwa za kuondoa migogoro ya mipaka kati ya Vijiji vya Kata za Nsenda na Ukondamoyo ilikuwa; kwanza kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi ya vijiji husika. Mpango huo uliandaliwa mwaka 2017 na Serikali za Vijiji kwa kushirikiana na Mradi wa Miombo chini ya usimamizi wa Tume ya Mipango ya Matumizi Bora ya Ardhi Tanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii ya kutayarisha mpango wa matumizi bora ya ardhi ilifanyika bila ya kuwa mgogoro wowote. Aidha, hati miliki za kimila zinaendelea kutolewa na elimu kuhusu usimamizi shirikishi wa misitu katika vijiji husika. Hatua hii ya utoaji wa elimu kwa wananchi juu ya kutambua, kubaini mipaka halali ya vijiji na mpaka wa hifadhi ya msitu wa North Ugalla zinafanyika kwa ushirikishaji wa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Kata ya Uyumbu kuna Jumuiya ya Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori ya UWIMA ambayo inaundwa na Vijiji vitatu vya Izimbili, Nsogoro na Izegabatogilwe. Vijiji hivyo vilisaidiwa kutengeneza Mpango wa matumizi bora ya ardhi mwaka 2004. Mwaka 2006 mpaka 2007, baadhi ya wananchi walivamia eneo la ukanda wa malisho linalotumika kama ushoroba. Mwaka 2007 wananchi hao waliondolewa kwenye eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Kijiji cha Tebhela ambao awali kilikuwa Kitongoji cha kijiji cha Nsogoro walivamia eneo hilo kwa kuweka makazi, kuendesha kilimo na malisho ya mifugo. Hivyo, tatizo lililopo ni uanzishwaji wa eneo jipya la utawala (Kijiji cha Tebhela) bila kuzingatia eneo lililopo. Hata hivyo UWIMA na Halmashauri ya Wilaya ya Urambo wamefanya mikutano kuwaelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuheshimu mipaka ya Hifadhi ya Jamii na matumizi bora ya ardhi.
MHE. SUSAN L. KIWANGA aliuliza:-
Serikali iliahidi kuweka mipaka ya kutenganisha Vijiji vya Jimbo la Mlimba na RAMSAR SITE kwa kuwashirikisha wanavijiji wa maeneo husika lakini kazi hiyo haikufanyika badala yake wakulima waliambiwa mwisho wao kwenye maeneo hayo ni mwezi Agosti na wafugaji mwisho wao kwenye maeneo yao ni Julai:-
• Je, kwa nini Serikali haikutekeleza jukumu lake la kuweka mipaka badala yake wakulima na wafugaji wamepewa barua ya kusitisha kutumia maeneo hayo na kusababisha taharuki kubwa kwa wananchi?
• Kwa kuwa wananchi hao walifungua kesi kupinga maonevu hayo mwaka 2015 kesi Na. 161 kuhusu mgogoro huo na bado kesi hiyo haijakwisha, kwa nini Serikali imewasitisha wananchi hao kuendelea kutumia maeneo hayo kabla ya kesi haijakamilika?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Susan Limbweni Kiwanga, Mbunge wa Mlimba, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekaji wa alama za mipaka kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria hufanyika kwa kuwashirikisha wananchi wa maeneo husika. Katika Pori Tengefu la Kilombero, zoezi la uwekaji wa alama za mipaka (vigingi) limefanyika kwa kuwashirikisha wananchi ambapo hadi kufikia Agosti, 2018, jumla ya vigingi 143 vimesimikwa kwa upande wa Wilaya za Malinyi na Ulanga.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika Wilaya ya Kilombero zoezi la uelimishaji wananchi limefanyika katika vijiji saba vya Miwangani, Namwawala, Idandu, Mofu, Ikwambi, Miomboni na Kalenga. Baada ya hatua hiyo, uwekaji wa alama ya mipaka utaendelea na utashirikisha wananchi wa maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba wananchi walifungua Kesi ya Ardhi Na.161 ya mwaka 2015 kupinga zoezi la Operesheni Okoa Bonde la Kilombero iliyofanyika mwaka 2012 kwa madai ya kuwa watu wanaofanya shughuli katika bonde hilo walipwe stahiki zao na kupewa muda muafaka wa kuondoka. Hoja ya wananchi hao ililenga kuiomba Mahakama izuie Serikali katika kuendesha operesheni tajwa kupitia Shauri Na.357 la Mwaka 2017 yaani Miscellaneous Land Application No.357 of 2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya Mahakama kusikiliza ombi la wananchi hao ilionekana kutokuwa na tija hivyo ikaamua kutokukubaliana na shauri hilo na badala yake ikaelekeza kesi ya msingi Na. 161 ya mwaka 2015 iendelee kusikilizwa, kesi hiyo itatajwa tena tarehe 19/9/2018. Hata hivyo, kesi iliyopo mahakamani kwa sasa haizuii Serikali kuendelea na operesheni itakayosaidia kuokoa Bonde la Kilombero ambalo ni muhimu sana katika kulinda ardhi oevu na ni chanzo kikubwa cha maji ya Mto Rufiji unaotegemewa kwa uzalishaji wa umeme kupitia mradi wa Rufiji.
MHE. SUZANA C. MGONUKULIMA aliuliza:-
Serikali inamhudumia Faru Fausta kwa gharama ya shilingi milioni 64 kwa mwezi na ambae hazalishi kutokana na kuwa ni mzee sana lakini Serikali hiyo haiwezi kumhudumia mwananchi aliyezeeka ambae hawezi kufanya shughuli zozote za kujikimu maisha na hana mtu wa kumsaidia.
Je, ni kipi kilicho muhimu zaidi kwa Serikali kati ya Faru Fausta au mwananchi mzee asiyeweza kufanya lolote na hana wa kumsaidia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Suzana Chogisasi Mgonukulima, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Faru Fausta amekuwepo eneo la Hifadhi ya Ngorongoro tangu mwaka 1965. Kwa sasa Faru huyu ndiyo mwenye umri mkubwa kuliko wote duniani. Kutokana na uadimu wa wanyama hao, uwepo wa Faru Fausta umekuwa kivutio kikubwa kwa watalii na watafiti wa ndani na nje ya nchi na hivyo kuchangia kwa kiwango kikubwa mapato ya hifadhi ya Ngorongoro na Serikali kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uzee, Faru Fausta alijeruhiwa na fisi tarehe 9 Septemba, 2016 hivyo kulazimisha atunzwe kwenye kizimba (cage) kwa ajili ya uangalizi maalum ambao unahusisha matibabu, chakula na ulinzi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama kubwa iliyokuwepo kipindi ikilichopita ilitokana na hali ya dharura iliyohitajika ikiwemo miundoimbinu, ulinzi, matibabu na malisho maalum ambapo matumizi kwa mwezi yalikuwa ni takribani shilingi 1,435,571. Kwa sasa afya ya Faru Fausta inazidi kuimarika kadri siku zinavyozidi kwenda hivyo gharama za uangalizi zimeshuka hadi kufikia shilingi 285,000 kwa mwezi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo Faru Fausta si kwamba ni muhimu kuliko binadamu wazee bali uamuzi wa kumtunza kwenye kizimba ulifanyika kwa lengo la kunusuru maisha yake ili hatimaye aendelee kuwa kivutio cha utalii na kuingiza fedha za kigeni nchini. Fedha zote hizo zinaingia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mgogoro wa ardhi kati ya Mbuga za Wanyama Selous – Kilwa na wananchi wanaoishi karibu na mbuga hiyo umezidi kuwa mkubwa kwa sababu mipaka halali haijulikani. Kwa mfano, mwaka 1974 mpaka halali ulikuwa Mto Matandu, mwaka 2010 mpaka huo ulisogezwa kufikia Bwawa la Kihurumila katika Kijiji cha Kikulyungu:-
a) Je, Serikali iko tayari kuhakiki eneo hilo ili kuondoa mgogoro mkubwa uliopo kati ya Wanakijiji wa Kihurumila na Mbuga?
b) Je, Serikali iko tayari kutatua mgogoro uliopo kati ya wananchi wa Kilwa na Mbuga.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohamed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Pori la Akiba Selous uliwekwa kwa kuzingatia Tangazo la Serikali Na. 275 kwa mujibu wa Sheria ya Uhifadhi wa Wanyamapori Na. 12 ya mwaka 1974. Tangu wakati huo hadi sasa mpaka huo haujafanyiwa marekebisho yoyote.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mgogoro wa mpaka kati ya Kijiji cha Kikulyungu na Pori la Akiba la Selous unatokana na kijiji hicho kutokukubaliana na uhakiki wa mpaka wa pori hilo uliofanyika mwaka 2010 kwenye eneo la Wilaya ya Liwale kwa kuwatumia wataalam kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kuwa, Wizara yangu ilitembelea Pori la Akiba la Selous – Kanda ya Kusini Liwale tarehe 3 na 4 Agosti, 2018 na kukutana na wananchi na viongozi wengine wa Serikali ikiwemo Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro huo. Kupitia ziara hiyo, wananchi sasa wameridhia kazi ya uhakiki ifanyike upya na kuhakikisha kuwa watatoa ushirikiano kwa wataalam.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu itashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi; wanakijiji; na Halmashauri ya Mji kuhakiki mpaka wa Pori la Akiba Selous katika eneo la Kijiji cha Kikulyungu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi kati ya wananchi, wawekezaji na maeneo yaliyohifadhiwa, Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wote katika uhakiki wa mipaka na uwekaji wa alama kwenye mapori yote nchini na kuandaa na kusimamia mipango ya matumizi bora ya ardhi.
MHE. ESTER M. MMASI (K.n.y. MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:-
Gharama za kupanda Mlima Kilimanjaro ni mara mbili ya gharama za kupanda Mlima Kenya; hali hii imesababisha kushuka kwa idadi ya watalii na kuinyima Serikali mapato. Je, ni lini Serikali itafanya marekebisho ya bei hizo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Mlima Kilimanjaro ni mlima mrefu kuliko yote Barani Afrika ukiwa na urefu wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari. Mlima huu una sifa nyingi za kipekee ikiwemo ya kuwa mlima mrefu duniani uliosimama peke yake (the only free standing mountain in the world), asilimia 85 ikiwa ni vertical, wenye barafu japo upo katika Ukanda wa Ikweta. Ni moja ya eneo la Urithi wa Dunia na umetunukiwa tuzo ya kuwa kivutio bora (One of the Africa Wonders).
Mheshimiwa Spika, aidha, Mlima Kilimanjaro una aina zaidi ya 200 ya ndege na zaidi ya aina species 140 za mamalia wakiwemo tembo, pofu, pongo, jamii ya swala, minde, twiga, simba, chui na wengineo, sifa ambazo Mlima Kenya hauna.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kununi za kupanda mlima, Mlima Kilimanjaro hupandwa kwa wastani wa siku sita. Safari ya kupanda mlima huu kwa mtalii kutoka nje ya nchi huipatia Serikali mapato ya dola za Kimarekani 684.4 pamoja na kodi ya VAT. Mtalii anayepanda Mlima Kenya kwa siku sita hulipa dola za Marekani 460. Tofauti ya gharama kati ya milima hii zinatokana na umuhimu wa kipekee pamoja na sifa ya Mlima Kilimanjaro ambazo haziwezi kulinganishwa na Mlima Kenya.
Mheshimiwa Spika, njia ya kupanda Mlima Kilimanjaro zimetengenezwa vizuri kiasi cha kuwezesha mtu wa kawaida asiye na utaalam kupanda mlima hadi kileleni wakati kwa Mlima Kenya upandaji unahitaji utalaam (technical climbing). Tofauti hizi husababisha gharama za utalii kati ya milima hii zisifanane.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2017/2018 Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ilipokea na kuhudumia watalii 51,825 ambao waliingizia Taifa mapato ya shilingi bilioni 76.16. Kwa sasa Serikali imepanga kukutana na wadau wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro ili kukubaliana masuala mbalimbali ikiwemo bei ya kupanda Mlima Kilimanjaro.
MHE. YAHAYA O. MASSARE aliuliza:-
Mjasiliamali au mtu yeyote anapokata mti anatakiwa achukue 70% ya kile anachokilipia:-
• Je, ni lini recovery rate ya 30% ya mbao ilifanyiwa utafiti?
• Je, ni taasisi gani ilifanya utafiti huo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Yahaya Omary Massare, Mbunge wa Manyoni Magharibi, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mauzo ya miti ya Serikali kwa ajili ya kuvuna hufanyika baada ya kufanya tathmini ya ujazo wa miti kwa kupima unene na urefu wa miti inayotarajiwa kuuzwa. Ujazo huu hauhusishi ujazo wa matawi, majani na mizizi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tafiti zilizowahi kufanywa na wataalam wetu wa misitu kati ya mwaka 1996 hadi 1999 wakati wa kutekeleza Mradi wa FRMP (Forest Resource Management Programme), zilibainisha kuwa mteja anaweza kupata mbao kati ya asilimia 60 – 70 ya ujazo wa mti uliopimwa kama atachakata magogo hayo kwa kutumia mashine zenye ufanisi wa kiwango cha juu ambazo ni frame saw au band saw. Mashine hizi hupatikana kwenye viwanda vikubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika viwanda vidogo vidogo na vya kati ambavyo hutumia mashine zenye ubora wa chini kiwango cha uzalishaji ni kati ya asilimia 20 - 43 ambapo wastani ni asilimia 30 ya ujazo wa mti. Utafiti huu ulifanywa kati ya mwaka 2005 na 2007 na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Chuo cha Viwanda vya Misitu cha Moshi (FITI). Teknolojia duni, uelewa mdogo na usimamizi hafifu ndiyo chanzo cha kuwa na ufanisi huo mdogo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia utafiti huo na ufanisi wa teknolojia iliyopo sasa ya msumeno wa mkono na msumeno wa duara (circular saw) hauwezi kuzalisha mbao zenye ujazo wa zaidi ya asilimia 30 ya ujazo wa mti uliopimwa. Kiwango cha asilimia 30 kitaalam tunakiita recovery rate.
MHE. MBARAKA K. DAU aliuliza:-
Papa aina ya potwe (whale shark) ni samaki ambaye duniani kote anapatikana Australia na Tanzania katika Kisiwa cha Mafia tu:-
Je, ni lini Serikali itakuja na mpango mkakati wa kumtangaza samaki huyo pamoja na vivutio vingine vya utalii kama vile scuba diving na sport fishing duniani ili kuvutia watalii nchini?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbaraka Kitwana Dau, Mbunge wa Mafia, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, papa aina ya potwe (whale shark) anapatikana katika maeneo mbalimbali duniani hususan nchi zilizoko katika maeneo ya tropiki kama Australia, Taiwan, Pakistan, India, Ufilipino, Indonesia, Afrika Kusini, Kenya, Msumbiji na kwa Tanzania anapatikana katika Visiwa vya Mafia (Kilindoni), Pemba na Zanzibar. Samaki huyu ni mmoja kati ya samaki wakubwa sana duniani na uzito wake unaweza kufikia mpaka tani zaidi ya 20 na urefu kufikia zaidi ya mita nane na hivyo kuwa kivutio kikubwa cha watalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Bodi ya Utalii Tanzania inaendelea kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi vikiwemo vivutio vya Wilaya ya Mafia ikijumuisha papa aina ya potwe kwa kutumia mikakati mbalimbali ya utangazaji kama vile vipeperushi; majarida mfano (Afrika Asilia, Selling Tanzania, Tan Travel, Tanzania Explore Magazine na Tanzania Map; tovuti yenye anuani www.tanzaniatourism.com; mitandao mbalimbali ya kijamii mfano youtube, instagram, twitter, facebook; Tanzania Tourism App inayopatikana kwenye Google Play Store kwenye simu za mkononi aina ya smart phone. Vilevile, utangazaji hufanyika kwa kutumia maonesho mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na mikoa na wilaya inaendelea kubaini maeneo ya fukwe katika mwambao wa bahari ya Hindi kwa ajili ya uendelezaji wa shughuli za utalii kama vile kuzamia (scuba diving), kuogelea (swimming), michezo ya kuvua samaki (sport fishing), kupiga mbizi (snorkeling) na sunbathing. Aidha, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi hususan wavuvi ili kuwatunza samaki aina ya papa potwe. Hivi karibuni, Serikali itazindua studio ya utalii, channel ya utalii itakayokuwa chini ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na utambulisho wa Tanzania (Destination Branding). Hatua hii itaongeza ufanisi katika kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini. (Makofi)
MHE. HADJI H. MPONDA aliuliza:-
Serikali kupitia aliyekuwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda alitoa agizo la kuweka utatuzi wa kudumu katika migogoro ya ardhi iliyopo baina ya wananchi na Serikali katika maeneo ya vijiji na mapori tengefu. Aidha, katika kampeni zake Wilayani Malinyi Mheshimiwa Rais aliahidi uhaulishwaji wa Buffer Zone ya pPori Tengefu la Kilombero kwa vijiji vinavyopakana ili wawe huru katika shughuli zao, lakini hadi leo hakuna utekelezaji wowote.
(a) Je, utekelezaji wa ahadi na agizo hili umefikia wapi?
(b) Je, Serikali ina mpango mbadala kwa wananchi wanaoishi kihalali katika maeneo hayo ya Buffer Zone ya Pori Tengefu la Kilombero?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Hadji Hussein Mponda Mbunge wa Malinyi lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ilianza kutekeleza agizo la Mheshimiwa Waziri Mkuu mstaafu mwezi Februari, 2016 wakati ilipozindua programu maalum ya upimaji wa vijiji na urasimishaji wa ardhi (Land Tenure Support Programme) vya Wilaya za Kilombero, Ulanga na Malinyi unaosimamiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Programu hiyo ya miaka mitatu inafadhiliwa na DFID, DANIDA na SIDA kwa jumla ya dola za Kimarekani milioni 15.2.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi mwezi Mei, 2018 jumla ya vijiji 12 kati ya vijiji 14 vinavyopakana na hifadhi katika Wilaya ya Malinyi vimepimwa. Hii ni sawa na asilimia 85.71 ya vijiji vinavyotarajiwa kupimwa. Aidha, katika Wilaya ya Ulanga jumla ya vijiji saba vimepimwa na kati ya hivyo vijiji vitano alama za mipaka zimeshawekwa. Katika Wilaya ya Kilombero jumla ya vijiji 22 vinavyopakana na hifadhi vinatarajiwa kupimwa. Elimu na uhamasishaji umefanyika katika vijiji saba vya Wilaya hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mpango huu, Serikali inaamini kwamba matumizi ya ardhi katika maeneo yanayozunguka Pori Tengefu la Kilimanjaro yakiwemo maeneo ya Wilaya ya Malinyi yatawekwa bayana na hivyo kupatikana kwa utatuzi wa kudumu wa migogoro ya ardhi iliyopo baina ya wananchi na Pori Tengefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo, Serikali imeunda Kamati Maalum kwa ajili ya kuongea na wadau mbalimbali kwa lengo la kupata picha halisi ya mgogoro ili kutoa ushauri na mapendekezo yatakayowezesha kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro wa matumizi ya ardhi katika Bonde la Kilombero. (Makofi)
MHE. RITTA E. KABATI aliuliza:-
Serikali inafanya mkakati gani ili kutangaza vivutio vilivyopo katika Mkoa wa Iringa katika sekta ya utalii? Je, Serikali inavitambua vivutio hivyo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Iringa ni miongoni mwa mikoa yenye vivutio vingi vya utalii kama vile Hifadhi za Taifa za Ruaha na Udzungwa, Makumbusho ya Mtwa Mkwawa ya Kalenga, Isimila, Eneo la Zana za Mwanzo za Mawe na Maumbile Asilia na Makumbusho ya Mkoa ambayo inaonesha utamaduni wa asili wa Iringa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza Sera ya Taifa ya Utalii ya mwaka 1999 na mpango kabambe wa uendelezaji utalii, Serikali imekuwa ikitangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ukiwemo Mkoa wa Iringa. Mpango kabambe wa kuendeleza utalii nchini ulioandaliwa mwaka 1996 na kufanyiwa mapitio mwaka 2002 umeainisha Mkoa wa Iringa kama kitovu cha maendeleo ya utalii (tourism hub) kwa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, zoezi la kuainisha vivutio katika Mkoa wa Iringa lilianza kufanyika mwaka 2007 ambapo mpaka sasa takribani maeneo 38 ambayo ni vivutio vya utalii yameainishwa katika Wilaya za Mufindi, Kilolo na Iringa. Kazi inayofuata sasa ni kuendeleza na kutangaza vivutio hivyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia taasisi zake ikiwemo Bodi ya Utalii Tanzania imeweka mikakati madhubuti ya kutangaza utalii. Mikakati hii ni pamoja na kujenga utambulisho wa Tanzania (Destination Tanzania Brand), kukuza maonesho ya utalii wa Kimataifa yanayofanyika ndani na nje ya nchi kama vile Karibu Kusini, kuanzisha channel ya utalii, kuanzisha Studio ya kutangaza utalii kwa njia ya TEHAMA, kuadhimisha Mwezi wa Urithi (Urithi Festival) na kuimarisha uhamasishaji kwa makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo wanafunzi. Vivutio vya utalii katika Mkoa wa Iringa vimejumuishwa katika mikakati hii ya kutangaza utalii nchini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada hizo hapo juu na ili utalii Mkoani Iringa, Serikali imeendesha mafunzo ya muda mfupi ya utalii na ukarimu kupitia mradi wa SPANEST kwa takribani watu 300, imefungua Ofisi ya Utalii ya Kanda ya Kusini iliyoko Iringa na imezindua mradi wa kukuza utalii Ukanda wa Kusini ujulikanao kama REGROW. Aidha, Iringa ni miongoni mwa mikoa iliyoajiri Maafisa Utalii kuanzia ngazi ya Mkoa hadi Halmashauri za Wilaya.
MHE. JOHN P. KADUTU (K.n.y. MHE. MAGDALENA H. SAKAYA) aliuliza:-
Serikali ilianzisha Wakala wa Misitu (TFS) kwa lengo la kuhifadhi misitu, kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya rasilimali ya misitu:-
Je, ni kwa kiasi gani Maafisa wa Misitu walioko Mikoani, Wilayani wameweza kuokoa misitu inayozidi kuteketea hapa nchini?
NAIBU WAZIRI MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya, Mbunge wa Kaliua, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS) inasimamia misitu ya hifadhi ya Serikali Kuu ipatayo 455 sawa na hekta15.48 milioni ambayo ni takriban asilimia 35 ya eneo lote la misitu nchini. Eneo hili hujumuisha misitu ya asili na ile ya kupandwa (Forest Plantations). Aidha, TAMISEMI wanasimamia hifadhi 161 sawa na hekta 3.36 milioni wakati serikali za vijiji zinasimamia hifadhi za misitu 1,200 sawa na hekta milioni 21.6. TFS ina kazi za kutafiti, kuhifadhi, kulinda na kusimamia matumizi endelevu ya misitu yote nchini. Kazi hizi zinatekelezwa na Maafisa Misitu wa TFS waliopo katika Kanda Saba na Wilaya 135 za Tanzania Bara wakishirikiana na Maafisa Misitu waliopo chini ya Halmashauri za Wilaya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Maafisa Misitu walioko Mikoani na Wilayani wameweza kusimamia hifadhi za misitu hii na kuwezesha kurejea kwa uoto wa asili katika misitu 271 nchini. Kazi zilizotekelezwa na Maafisa hao ni pamoja na soroveya (Survey and Resurvey) ya misitu husika; kuimarisha mipaka ya misitu kwa kuwezesha takriban kilomita 13,100 za mipaka hii kusafishwa; Kuweka vingingi (beacons) 14,200 vyenye kuonyesha mipaka na hifadhi; Kupanda miti katika mipaka ya misitu na kuweka mabango (sign boards) 4,553 kwa ajili ya kutoa taarifa za uwepo wa misitu ya hifadhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Maafisa Misitu wameendelea kuwaelimisha wananchi kuhusu hatari ya kuwasha moto katika misitu ya hifadhi, athari za kilimo cha kuhamahama, ufugaji ndani ya hifadhi, uchimbaji wa madini na utengenezaji wa mkaa usiozingatia weledi.
MHE. HASNA S. MWILIMA aliuliza:-
Wananchi wa Humule, Ubanda, Tandala na maeneo mengine ya Itebula wamekuwa wakisosa maeneo ya kulima kwa madai kuwa wanaingilia maeneo ya hifadhi:-
• Je, Serikali haioni sasa ni muhimu kusogeza mipaka kwa kushirikiana na TAMISEMI ili wananchi wapate maeneo ya kulima?
• Je, ni lini Serikali itamaliza usumbufu wanaoupata Wananchi wa Kijiji cha Kalilani kwa kudaiwa kuwa wamo ndani ya Hifadhi wakati Kijiji hiki kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hasna Sudi Katunda Mwilima, Mbunge wa Kigoma Kusini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
• Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo ya Humule, Ubande, Tandala na Itebula ni vitongoji ndani ya Kijiji kipya cha Lufubu kilichozaliwa ndani ya kijiji cha Kashagulu, Kata ya Kalya, Wilaya ya Uvinza ambacho kinatambulika kisheria. Eneo tajwa lilifanyiwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi mwaka 2006. Mchakato wa kuidhinisha mipaka ya ramani ya kijiji ulikamilika mwaka 2007 na ramani hiyo kusajiliwa kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji kama Kashagulu pia kilifanya mpango wa kurasimisha msitu wao wa kijiji wenye ukubwa wa hekta 38,313 kupitia mchakato shirikishi kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria ya Misitu Na.14 ya 2002. Eneo hili ni vyanzo vya maji na linatambuliwa kama mapito ya wanyamapori yaani (Ushoroba) hususani tembo, nyati, sokwe na wengine wahamao kutoka Hifadhi ya Taifa Mahale kwenda Hifadhi ya Taifa Katavi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kuongeza maeneo ya kilimo lazima lifanyike kisheria kwa kuwa Mpango wa Matumizi Bora ya Ardhi uliidhinishwa na mkutano mkuu wakati huo. Mpango huo uliangalia matumizi ya wakati huo na ya baadaye kwa miaka 10 mpaka 15 ijayo.
• Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Milima ya Mahale ilitangazwa rasmi katika GN Na. 262 ya tarehe 14 Juni, 1985. Maeneo ya Kalilani ni muhimu sana kwa uhifadhi wa sokwe, tembo, wanyama wengine pamoja na mazalia ya samaki. Aidha, wakati hifadhi hii inatangazwa, eneo hilo lilikuwa na wananchi jamii ya Watongwe waliopisha kutangazwa Hifadhi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kijiji cha Kalilani kilisajiliwa tarehe 5 Juni, 1995 ikiwa ni miaka takriban 10 baada ya Hifadhi ya Taifa kutangazwa. Wakati huo wavuvi wachache waliobakia eneo la Kaskazini Magharibi mwa hifadhi hii walianzisha kitongoji na baadaye kijiji kinachofahamika sasa kama Kalilani. Hii inadhihirisha kuwa eneo ambalo wanakijiji wanadai kuwa ni sehemu ya kijiji bado kisheria ni sehemu ya Hifadhi ya Mahale.
MHE. RHODA E. KUNCHELA aliuliza:-
a) Je, ni lini Serikali itatatua mgogoro wa ardhi kati ya Hifadhi na wananchi katika Kata ya Kapalamsenga, Isengule na Ikola?
b) Kwa kuwa migogoro hiyo imechukua muda mrefu bila suluhu hivyo kusababisha usumbufu na hasara kwa wananchi; Je, Serikali haioni kuwa migogoro hiyo imesababisha umaskini mkubwa kwa wananchi kushindwa kuendeleza shughuli za kiuchumi kwenye maeneno yao hivyo ifanye haraka kutafuta ufumbuzi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Rhoda Edward Kunchela, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Kapalamsenga, Isengule na Ikola zipo katika Wilaya ya Tanganyika na zinajumuisha maeneo ya ushoroba wa wanyamapori ujulikanayo kama Katavi – Mahale. Ushoroba huu ni njia kuu ya wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa Katavi kwenda Hifadhi ya Taifa Mahale. Kutokana na wanyamapori hususani tembo kupita katika maeneo hayo, wenyeji wanautambua ushoroba husika kama “Tembo na Mwana.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ushoroba huu kufahamika kwa baadhi ya wananchi kulikuwa na mkanganyiko kuhusu eneo sahihi la (mipaka), yaani mipaka ya mapito ya wanyamapori na hii inatokana na baadhi ya wananchi na hasa wahamiaji na wafugaji kutoka mikoa ya jirani, kuvamia na kuharibu maeneo ya mapito ya wanyamapori bila kufuata taratibu na kujichukulia ardhi kiholela.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutafuta ufumbuzi wa migongano hii iliyopo juu ya matumizi ya ardhi, Serikali kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika ilichukua hatua mbalimbali kama ifuatavyo:-
• Kuhakikisha kuwa mipaka ya ushoroba inajulikana kwa wananchi kwa kutenga na kuainisha maeneo kwa ajili ya uhifadhi wa wanyamapori kama vile Sokwe. Sokwe hao wanapatikana katika Kata za Kapalamsenga, Ikola, Isengule, Mwese na Kasekese hasa katika safu za milima ya Mwansisi na Mgengebe.
• Kuandaa mipango ya matumizi bora ya ardhi ya vijiji na kutunga sheria ndogo za usimamizi wake kwa mwaka wa fedha 2015/2016 na 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa vijiji vyote vilivyopo katika Kata ya Kapalamsenga, Ikola na Isengule vimeshafanyiwa mpango shirikishi wa matumizi bora ya ardhi. Pia, eneo la ushoroba wa wanyamapori limebainishwa na kutengwa hivyo kuondoa mkanganyiko uliokuwepo awali. Aidha, kwa kutumia Kanuni ya usimamizi wa shoroba na maeneo ya mtawanyiko zimeshaandaliwa (GN 123 ya mwaka 2018).
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina mpango wa kutafuta suluhu ya kudumu kwa wananchi katika vijiji vyote vinavyopitiwa na shoroba za wanyamapori, vinavyopakana na maeneo ya hifadhi na vyanzo vya maji ili kuondoa migongano inayohusiana na umiliki wa matumizi ya ardhi. Hivyo, tunawaomba wananchi wote kuheshimu mipaka ya matumizi bora ya ardhi pamoja na kanuni mpya za ushoroba.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Mgogoro wa ardhi katika Hifadhi ya Wanyamapori Selous-Kilwa umechukua nafasi kubwa kati ya Serikali na wananchi wanaoishi karibu na hifadhi hiyo. Mpaka halali haujulikani kwani mwaka 1974 mpaka halali ulikuwa Mto Matandu na mwaka 2010 mpaka huo ulisongezwa mpaka Bwawa la Kilurumila, Kijiji cha Kikulyungu.
Je, Serikali ipo tayari kuhakiki eneo hilo ili kutatua mgogoro uliopo kati yake na wananchi wa Kijiji cha Kihurumile?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Abdallah Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Kikulyungu ni moja ya vijiji tisa vinavyopakana na Pori la Akiba la Selous kwa Wilaya ya Liwale. Ndani ya pori hilo kuna bwawa lijulikanalo kama Kihurumila ambalo ni sehemu muhimu kwa mazalia ya samaki na wanyamapori kama vile mamba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika miaka1970 wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu walikuwa wakivua samaki katika bwawa hilo baada ya kupewa vibali maalum. Hata hivyo, mwaka 1982 Serikali ilizuia shughuli za uvuvi kutokana na baadhi ya wananchi kukiuka taratibu za kuvua samaki ikiwemo matumizi ya sumu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpaka wa Pori la Akiba Selous umewekwa kwa kuzingatia Tangazo la Serikali Na. 275 la mwaka 1974. Tangu wakati huo hadi sasa mpaka huo haujafanyiwa marekebisho yoyote. Hata hivyo, wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu hawakubaliani na tafsiri na uhakiki wa mpaka uliofanyika licha ya vijiji vinne kukubaliana na uhakiki huo. Aidha, wananchi wa Kijiji cha Kikulyungu wanadai kwamba Bwawa la Kihurumila ni sehemu ya eneo la kijiji hicho.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ilituma maafisa kuhakiki mipaka ya vijiji vitano kati ya vijiji tisa vinavyounda WMA ya Liwale vinavyopakana na Pori la Akiba la Selous. Vijiji hivyo ni Kimambi, Kikulyungu, Barikiwa, Chimbuko na Ndapata. Uhakiki huo ulishirikisha pia Maafisa kutoka Tume ya Matumizi Bora ya Ardhi Tanzania, Maafisa Ardhi Wilaya ya Liwale, Taasisi isiyo ya Kiserikali ijulikanayo kama World Wide Fund for Nature (WWF) na wananchi na Viongozi wa Kata na Vijiji vinavyounda Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori ya Liwale. Zoezi hili lililenga kutatua mgogoro wa mpaka na kutangaza WMA ya Liwale. Hata hivyo, wananchi wa Kikulyungu waliwafanyia vurugu watalaam wa Wizara ya Ardhi walipotembelea eneo la mgogoro kwa ajili ya kutafsiri Tangazo la Serikali na kusababisha watalaam kukimbia kuokoa maisha yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia hali hiyo, Wizara imepanga kukutana na viongozi wa Mkoa wa Lindi akiwemo Mheshimiwa Mbunge kwa lengo la kutatua mgogoro huo kwa manufaa ya uhifadhi na ustawi wa wananchi.
MHE. ALLY SALEH ALLY (K.n.y. MHE. YUSSUF SALIM HUSSEIN) aliuliza:-
Je, Chuo cha Utalii kimetoa wahitimu wangapi wa fani za hoteli za kitalii kwa mwaka 2016/2017?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa maliasili na utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Yussuf Salim Hussein, Mbunge wa Chambani, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Chuo cha Taifa cha Utalii ni Wakala uliopo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii wenye dhamana ya kutoa mafunzo ya ukarimu na utalii nchini. Aidha, chuo kinatoa ushauri wa kitaalam na kufanya utafiti katika fani ya ukarimu na utalii. Chuo cha Taifa cha Utalii kina ithibati kutoka Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ili kutoa mafunzo ya ukarimu, usafiri na utalii kwa ngazi za stashahada na astashahada.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa masomo 2016/2017 kupitia kampasi zake tatu za Bustani, Temeke Dar es Salaam na Sakina Arusha, kilitoa mafunzo ya ukarimu, usafiri na utalii kwa wahitimu 329 kama ifuatavyo:-
(a) Stashahada ya Usafiri na Utalii (Ordinary Diploma ni Travel and Tourism) wahitimu 43;
(b) Stashahada ya Ukarimu (Ordinary Diploma in Hospitality Operations) wahitimu 15;
(c) Astashahada ya Ukarimu (Technician Certificate in Hospitality Operations) wahitimu 78;
(d) Mafunzo ya Muda Mfupi (Short Courses in Food Production and Pastry and Bakery) wahitimu 78; na
(e) Mafunzo ya Uhitaji Maalum (Tailor Made Courses in Hospitality and Tourism) wahitimu 79.
Mheshimiwa Naibu Spika, mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa kutumia mitaala inayofuata Mfumo wa Kujenga Ujuzi na Maarifa (Competence Based Education and Training) inayosimamiwa na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
MHE. SHAABANI O. SHEKILINDI aliuliza:-
Wilaya ya Lushoto imezungukwa na misitu lakini misitu mingi imeungua kwa moto:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kurudisha uoto ule wa asili uliopotea kutokana na misitu kuungua?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Shaabani Omari Shekilindi, Mbunge wa Lushoto, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, misitu iliyoungua moto katika kipindi cha kuanzia Agosti, 2016 hadi Februari, 2017 ni mitano ambayo ina jumla ya hekta 357.05 kati ya misitu 11 ambayo ina jumla ya hekta 22,855. Misitu hiyo ni Msitu wa Hifadhi Asilia Magamba wenye jumla ya hekta 9,381, zilizoungua ni hekta 338; Msitu wa Mkussu wenye hekta 3,674, zilizoungua ni hekta 3.8; Msitu wa Shagayu wenye hekta 7,830, zilizoungua ni hekta 2.75; Msitu wa Baga I wenye hekta 3,572, zilizoungua ni hekta 12; na Msitu wa Ndelemai wenye hekta 1,421, zilizoungua ni hekta 10.5.
Mheshimiwa Naibu Spika, misitu ya asili iliyoungua au kuharibiwa inaweza kurejeshwa kwa namna mbili. Mosi, kupanda miti maeneo yaliyoungua; na pili, kuliacha eneo liote miti lenyewe kwa kutofanya shughuli zozote za kibinadamu. Njia ya kwanza hutumika zaidi kwenye misitu ya kupandwa. Kutokana na asili ya eneo la Lushoto, njia nzuri zaidi ya kurudishia miti eneo lililoungua ni kuacha kufanya shughuli zozote za kibinadamu ili uoto wa asili urejee wenyewe. Aidha, kupanda miti isiyo ya asili ndani ya misitu ya hifadhi unaharibu uasilia wa msitu na huenda ukaleta matokeo hasi katika uoto wa asili uliopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara kupitia Wakala wa huduma za Misitu Tanzania unaendelea kutoa Elimu kwa jamii ili wananchi wanaoishi jirani na misitu ya hifadhi wawe makini wanapotumia moto wakati wa kusafisha mashamba yao, kwani chanzo kikuu cha moto wote uliounguza misitu katika kipindi hiki umetokana na wananchi kutayarisha mashamba yao bila kuchukua hatua za tahadhari.
MHE. HAMIDA M. ABDALLAH aliuliza:-
Kilwa ni moja ya miji mikongwe katika Afrika Mashariki tangu Anno Domino (AD) 900 -1700 pamoja na miji mingine ya Lamu, Mombasa, Sofala na Zanzibar. Miji hiyo ilipewa heshima ya jina la Urithi wa Dunia (World Heritage Site). Kwa kawaida miji hiyo husaidiwa na Mataifa mbalimbali ikiwemo Marekani, Japan, Ujerumani, Uingereza na Shirika la UNESCO:-
Je, Serikali ya Tanzania imefaidika nini kutoka katika Mataifa hayo yanayosaidia nchi za urithi wa dunia?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Hamida Mohammed Abdallah, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara yaliorodheshwa kwenye orodha ya Urithi wa Dunia mwaka 1981. Mwaka 2004 eneo la hifadhi la visiwa hivi liliingizwa kwenye orodha ya maeneo yenye urithi ulio hatarini kutoweka (Endangered Site). Hatua hiyo ilisababishwa na hali yake ya uhifadhi kutokidhi kiwango cha Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (UNESCO).
Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2005, Wizara kwa kushirikiana na UNESCO na nchi za Ufaransa, Norway, Japan na Marekani iliandaa miradi ya kukarabati magofu ya Kilwa Kisiwani na Songo Mnara na mafunzo. Baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na mradi wa Euro 600,000 kutoka Serikali ya Ufaransa; Mradi wa Dola za Kimarekani 201,390 kutoka Norway; mradi wa Dola 119,000 kutoka Ufaransa na UNESCO; mradi wa Dola 66,000 kutoka ILO; mradi wa Dola 100,000 kutoka World Monuments Fund; mradi wa Dola 700,000 kutoka Ubalozi wa Marekani; na mradi wa Dola 43,900 kutoka UNESCO. Kukamilika kwa ukarabati kuliwezesha magofu hayo kuondolewa kwenye orodha ya urithi uliokuwa hatarini kutoweka mwaka 2015.
Mheshimiwa Naibu Spika, faida nyingine zilizopatikana ni pamoja na ushauri wa kitalaam na misaada ya vifaa mbalimbali; kuendelezwa kwa miundombinu katika maeneo husika na ongezeko la kipato kwa jamii husika kupitia biashara ya utalii.
MHE. QAMBALO W. QULWI aliuliza:-
Matukio ya Wanyamapori kutoka nje ya Hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo Wilayani Karatu na kuharibu mazao ya wananchi na kujeruhi watu yamekuwa yakijirudia mara kwa mara:-
• Je, ni nini mkakati wa Serikali kuwadhibiti wanyama hao ili wabaki katika maeneo waliyotengewa;
• Fidia/Kifuta jasho kinachotolewa pindi wanyama wanapofanya uharibifu ni kidogo sana na imepitwa na wakati. Je, ni lini Serikali italeta marekebisho ya kifuta jasho, ili kuendana na mazingira ya sasa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Qambalo Willy Qulwi, Mbunge wa Karatu, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uharibifu wa mali na maisha ya binadamu kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu unajitokeza katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na maeneo yanayozunguka Hifadhi ya Ngorongoro. Katika Eneo la Ngorongoro uharibifu unajitokeza zaidi katika maeneo ya mashamba na makazi ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa hifadhi hiyo.
Mheshimiwa Spika, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Karatu inakabiliana na changamoto ya uharibifu wa mali na maisha ya binadamu kwa kufanya doria za pamoja. Aidha, Mamlaka ya Ngorongoro ina vituo vitano katika maeneo ya Kilimatembo, Elewana, Nitini, Bonde la Faru na Masamburai kwa ajili ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, vilevile magari mawili yamenunuliwa kwa ajili ya madhumuni hayohayo.
Mheshimiwa Spika, juhudi nyingine zinazofanyika ni kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujihami na kudhibiti wanyamapori, hususan tembo. Elimu hiyo, inahusisha matumizi ya pilipili, mafuta machafu na mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba kama njia ya kufukuza tembo.
Mheshimiwa Spika, fedha za kifuta jasho na kifuta machozi hazitolewi kama fidia bali hutolewa kwa ajili ya kuwafariji wananchi walioathirika na wanyamapori wakali na waharibifu. Hivyo, fedha hizo kuwa ni kidogo na hazilingani na hali halisi ya uharibifu.
Mheshimiwa Spika, kulingana na wingi wa matukio pamoja na ufinyu wa bajeti Serikali imeamua kupitia Kanuni za Kifuta Machozi na Kifuta jasho ili kuondoa changamoto zilizopo kiutendaji.
MHE. BONIPHACE M. GETERE aliuliza:-
Kila mwaka wanyama waharibifu wamekuwa wanakula mazao ya wakulima katika Jimbo la Bunda na Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi katika kulipa fidia ya kifuta jasho na kifuta machozi kwa wakulima hao:-
Je, Serikali ina mikakati gani ya kuzuia wanyama hao wakiwemo Tembo?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Boniphace Mwita Getere, Mbunge wa Bunda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Wizara inatambua madhara yanayosababishwa na wanyamapori waharibifu na wakali, hususan tembo, kwa wananchi waishio kandokando ya maeneo ya hifadhi, ikiwemo Wilaya ya Bunda. Katika Wilaya ya Bunda Vijiji vinavyopata usumbufu wa mara kwa mara kutokana na wanyamapori waharibifu na wakali ni Kunzugu, Bukore, Nyatwali, Balili, Tamau, Serengeti, Nyamatoke, Kihumbu, Hunyari, Mariwanda, Mugeta, Guta, Kinyambwiga na Kinyangerere.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuwanusuru wananchi kutokana na madhara ya wanyamapori wakali na waharibifu katika maeneo yote yanayopakana na maeneo ya hifadhi. Utekelezaji wa mikakati hiyo unaendelea ambapo katika Wilaya ya Bunda yafuatayo yamefanyika:-
a) Umeanzishwa ushirikiano wa kudhibiti wanyamapori waharibifu kati ya watumishi kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili Bunda, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Pori la Akiba Ikorongo - Gurumeti, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti na Mwekezaji Gurumeti Reserve;
b) Kutafuta vitendea kazi kwa ajili ya doria za wanyamapori waharibifu;
c) Vikundi 83 vimeanzishwa kwenye vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi kwa ajili ya kuchukua hatua za awali za kudhibiti wanyamapori hao pindi kunapokuwa na matukio ya wanyamapori waharibifu, wakati wakisubiri msaada wa Askari Wanyamapori;
d) Wizara imetoa tochi 100 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda. Mwanga mkali husaidia kufukuza tembo usiku kwa vijiji vinavyounda vikundi hivyo vya kufukuza wanyamapori;
e) Mafunzo kwa wananchi juu ya mbinu za kukabiliana na wanyamapori waharibifu yametolewa kwa vijiji, sambamba na kuwashauri kuepuka kulima kwenye shoroba za wanyamapori;
f) Kuweka madungu (minara) ambayo Askari Wanyamapori wanaitumia kufuatilia mwenendo wa tembo;
g) Kutumia teknolojia ya mizinga ya nyuki ambayo imewekwa pembezoni mwa mashamba; na
h) Mpango wa kutumia ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kufukuza tembo unaendelea.
Mheshimiwa Spika, lengo la mikakati hii ni kuhakikisha kwamba, matukio ya uvamizi wa tembo yanashughulikiwa kwa haraka iwezekanavyo. Sambamba na mikakati hiyo Wizara imekuwa ikitoa fedha za kifuta jasho au kifuta machozi pale ambapo mazao yameharibiwa au wananchi wamejeruhiwa au kuuawa na wanyamapori wakali, akiwemo tembo.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha mwezi Machi hadi mwezi Oktoba, 2017, Wizara imelipa kifuta jasho na kifuta machozi cha jumla ya Sh.249,741,250 kwa wahanga 1,284 na vijiji 14 katika Wilaya ya Bunda.
Mheshimiwa Spika, sababu kubwa inayosababisha matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu kuendelea kuwepo ni kuzibwa kwa shoroba na mapito ya wanyamapori. Kutokana na hali hiyo Serikali ina mpango wa kufufua shoroba za wanyamapori katika maeneo mbalimbali nchini kwa mujibu wa Kanuni za Shoroba, GN. 123 ya tarehe 16 Machi, 2018. (Makofi)
MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA aliuliza:-
Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi sana vya utalii ambavyo vikitumika vizuri vinaweza kuchangia pato la Taifa na wananchi kwa ujumla; moja kati ya vivutio hivyo ni pamoja na Mbunga za Hifadhi ya Wanyama Mikumi ambayo inaongeza mapato mengi, lakini mbuga hizo hazina hoteli nzuri za kitalii zenye kukidhi viwango vya kimataifa, kutokana na kuungua kwa Hoteli ya Kitalii ya Mikumi.
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga hoteli kubwa za kitalii ndani ya Mbuga ya Mikumi ili kuvutia watalii wengi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Jasmine Tisekwa Bunga, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuwa Mkoa wa Morogoro una vivutio vingi vya utalii ikiwemo Hifadhi ya Mikumi. Baada ya kuungua kwa lodge ya Mikumi, Serikali kupitia TANAPA imeendelea na juhudi mbalimbali za kuhamasisha uwekezaji katika hifadhi hiyo, ambao fursa za uwekezaji hususan huduma za malazi zimekuwa zikitangazwa. Aidha, mwekezaji wa kuifufua lodge ya Mikumi alishapatikana na kazi ya ukarabati inaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, watalii wanaotembelea Hifadhi ya Mikumi kwa sasa wanatumia kambi tatu za mahema (tented camps) zilizoko ndani ya hifadhi, lodge na hoteli kumi zilizopo Mikumi Mjini. Wizara kupitia TANAPA imetenga maeneo saba kwa ajili ya uwekezaji wa hoteli na lodge ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi zenye hadhi na viwango vya kimataifa ili kuleta watalii wengi na kuongeza mapato.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuchochea maendeleo ya sekta ya utalii katika Ukanda wa Kusini kwa ujumla, Serikali ilizindua rasmi mradi wa kuendeleza utalii Ukanda wa Kusini wa Tanzania ujulikanao kama REGROW tarehe 12 Februari, 2018 Mjini Iringa. Lengo la mradi huu ni kuwezesha maendeleo ya utalii kwa kuboresha miundombinu, kuhifadhi maliasili na mazingira katika hifadhi ya Ukanda wa Kusini ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Mikumi.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maelezo hayo, napenda kutumia fursa hii kumwomba Mheshimiwa Mbunge, uongozi pamoja na wakazi wa Mikumi kwa ujumla kutenga maeneo ya uwekezaji wa huduma za malazi na utalii ili kunufaika na biashara ya utalii nje ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi. (Makofi)
MHE. INNOCENT L. BASHUNGWA (K.n.y. MHE. ESTER A. MAHAWE) aliuliza:-
Sekta ya utalii inachangia pato kubwa la fedha za kigeni katika nchi yetu.
Je, ni lini Serikali itatengeneza barabara ya Serengeti ambayo ni mbovu kiasi cha kufanya watalii kukataa kupita huko?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Alexander Mahawe, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Kilimanjaro na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro ndiyo zinachangia zaidi katika mapato ya fedha za kigeni zitokanazo na shunguli za utalii hapa nchini. Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ina ukubwa wa kilometa za mraba 14,763 na barabara zenye urefu wa kilometa 3,155. Barabara hizo ni pamoja na barabara kuu zinazounganisha Hifadhi na Mikoa ya Arusha, Mara na Simiyu. Barabara nyingine ni zile za mizunguko ya utalii na nyingine ni za utawala na doria. Barabara zote hizo ni za kiwango cha changarawe.
Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zenye matumizi makubwa ni zile kuanzia mpaka unaotenganisha Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro hadi Kituo cha Seronera yenye urefu wa kilometa 60 na kilometa 30 kutoka Seronera hadi lango na Ikoma. Barabara hizi wakati wa msimu wa watalii wengi zinatumiwa na magari zaidi ya 300 kwa siku. Kutokana na matumizi makubwa kiasi hicho, barabara hiyo yenye kiwango cha changarawe uchakavu wake huongezeka kwa kasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuanzia mwezi Agosti, 2016 hifadhi inaendelea kuelekeza nguvu za ziada kuhudumia barabara hizi wakati wote wa msimu wa watalii.
Mheshimiwa Naibu Spika, juhudi zinazoendelea zinahusisha kufanya matengenezo ya barabara hizo kwa kutumia nyenzo mbalimbali ikiwemo mitambo miwili ya barabara yaani motor graders pamoja na malori. Ili kupata ufumbuzi wa muda mrefu kukabiliana na changamoto hiyo ya ubovu wa barabara, Shirika la Hifadhi za Taifa linaendelea kutafuta teknolojia mbadala ili kuwa na barabara zitakazodumu bila kuathiri ikolojia ya wanyamapori.
MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:-
Kumekuwepo na tabia ya askari wa SENAPA kuwakamata wananchi ndani ya hifadhi na wakati mwingine wasipouawa huwapeleka mbali na Mahakama za Wilaya ya Serengeti.
(a) Je, ni lini vitendo vya mauaji ya watu wanaozunguka Hifadhi ya Serengeti vitakoma?
(b) Je, ni lini askari wa SENAPA wataacha kuwapeleka watuhumiwa waliokamatwa ndani ya hifadhi nje ya Mahakama za Wilaya?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Askari wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo mbalimbali iliyopo. Ni kweli kwamba baadhi ya wananchi wamekuwa wakikamatwa na kufanya shughuli au kuingia kwenye hifadhi bila ya kufuata taratibu zilizopo. Wengi wamekuwa wakijihusisha na ujangili ndani ya hifadhi. Kwa msingi huo, Askari wa Hifadhi huwakamata watuhumiwa wote na kuwafikisha katika Jeshi la Polisi na hatimaye Mahakamani kwa hatua zaidi. Jumla ya kesi 437 zimefunguliwa na zipo katika hatua mbalimbali za usikilizaji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imepakana na Wilaya nane tofauti. Mtuhumiwa anapokamatwa ndani ya hifadhi, anapelekwa katika Kituo cha Polisi kilicho jirani kwa hatua zaidi. Baadhi ya watuhumiwa wamekuwa na tabia ya kufanya uhalifu kwa kufuata mienendo ya wanyamapori wahamao. Kwa mfano, kati ya mwezi Mei na Juni ya kila mwaka, wanyama wengi wanahamia maeneo ya Kusini na Magharibi mwa Hifadhi ambapo kiutawala yako Wilaya ya Bariadi na Bunda.
Hivyo baadhi ya watuhumiwa kutoka Wilaya ya Serengeti huenda katika Wilaya nyingine kufanya ujangili wa wanyamapori ambapo kwa kipindi hicho hawapatikani kirahisi katika aneo la Wilaya zao. Kutokana na hali hiyo, watuhumiwa wamekuwa wakikamatwa na kushitakiwa katika Mahakama za eneo au Wilaya waliyokamatwa wakifanya uhalifu.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vyema wananchi wakazingatia taratibu zote za Hifadhi na niwaase wananchi hao kuachana na ujangili ili kuepuka adhabu hizo na kuwataka washirikiane na Serikali kulinda hifadhi za Taifa.
MHE. MARYAM SALUM MSABAHA aliuliza:-
Sekta ya Utalii imekuwa ikitoa ajira kwa vijana wetu wa Visiwani na Tanzania Bara; kutetereka kwa sekta hii kumesababisha kupungua kwa ajira kwa kiasi kikubwa na vijana kurudi mitaani;
Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha na kuboresha sekta hii ili ajira zipatikane kwa wingi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa Taifa ambapo sekta hii huchangia zaidi ya asilimia 17 ya Pato la Taifa (GDP) na asilimia 25 ya fedha za kigeni nchini. Sekta hii inatoa ajira nyingi za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja hapa nchini ambapo kwa sasa sekta ya utalii huchangia ajira takriban 1,500,000.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mchango mkubwa wa sekta ya utalii katika kuchangia ajira nchini, Wizara inaendelea na mikakati mbalimbali ya kuongeza fursa za ajira ikihusisha:-
(a) Kupanua wigo wa mazao ya utalii ili kuongeza fursa za ajira kama vile; utalii wa mikutano, utalii wa fukwe, utalii wa matamasha mfano urithi festival, utalii wa miamba (geo-tourism), utalii wa meli, utalii wa reli, mfano TAZARA na Tanga Line, utalii wa michezo, utalii wa matibabu na kadhalika.
(b) Kuhamasisha uwekezaji katika Sekta ya Utalii. Katika kutekeleza hili, Wizara imekamilisha zoezi la kubaini maeneo ya fukwe katika mwambao wa bahari ya Hindi kwa ajili ya uwekezaji wa shughuli za utalii.
(c) Wizara inaendelea kuhamasisha wananchi kuanzisha miradi ya utalii wa utamaduni (Cultural Tourism Programme) ambapo mpaka sasa miradi 66 imeshaanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini.
(d) Wizara kupitia Wakala wa Chuo cha Taifa cha Utalii hutoa mafunzo ya kozi za utalii na ukarimu katika ngazi ya astashshada na stashahada. Kozi hizo zimesaidia kupata wahitimu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira za sekta ya utalii.
(e) Kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga, nchi kavu na baharini, kuanzisha channel na studio mahsusi kwa ajili ya kutangaza utalii, kuhamasisha wawekezaji kwenye maeneo ya utalii na kuandaa na kutangaza utambulisho wa Taifa (destination branding).
(f) Aidha, Sheria ya Utalii ya mwaka 2008, kifungu cha 58(2), imetenga shughuli mahsusi za biashara ya utalii kwa ajili ya Watanzania. Vile vile, Wizara imepunguza ada ya leseni za biashara ya utalii kwa lengo la kuwawezesha Watanzania wengi kushiriki kufanya shughuli za utalii.
MHE. ALFREDINA A. KAHIGI aliuliza:-
Wananchi wa Bukoba Vijijini wanakabiliwa na tatizo kubwa la wanyama waharibifu kama vile ngedere na kadhalika na wanyama hao sasa wanavamia vijiji na kusababisha madhara kwa wananchi:-
Je, Serikali ina mkakati gani madhubuti wa kuwanusuru wananchi wa Bukoba Vijijini na balaa la wanyama hao waharibifu?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba nijibu swali la Mheshimiwa Alfredina Apolinary Kahigi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua uwepo wa tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu linalojitokeza katika wilaya zaidi ya 80 hapa nchini ikiwemo Wilaya ya Bukoba Vijijini. Wanyamapori wanaoleta usumbufu kwa wananchi katika wilaya hiyo ni tembo, mamba na ngedere. Tembo kutoka kwenye Ranchi za Kagoma na Mabale wamekuwa wakivamia maeneo ya mashamba na makazi ya wananchi jirani na ranchi hizo. Aidha, mamba wamekuwa wakijeruhi wananchi pembezoni mwa Ziwa Viktoria hususan maeneo ya Kemondo. Vilevile ngedere wanasumbua wananchi kutoka kwenye misitu ya asili ya Kizi, Bugando, Katangarara, Kereuyangereko, Kemondo na Rasina. Misitu hiyo ipo kwenye Kata za Katoma, Karabagaine, Bujogo na Kishongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imechukua hatua za kudhibiti tatizo hilo kwa kufanya doria ambapo Askari wa Wanyamapori kutoka Kikosi Dhidi ya Ujangili - Mwanza na Pori la Akiba Biharamulo - Burigi - Kimisi (BBK) wakishirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini ambapo waliua jumla ya ngedere 103 na kufukuza makundi kadhaa. Doria hizo zilifanyika katika Kata za kemondo, Katerero, Kanyengereko, Maruku, Katoma, Bujugo, Karabagaine, Nyakato, Kikomela, Ibwela, Nyakibimbili, Kaibanjara, Buterankunzi, Mikoni, Kyamlaile, Lubafu, Kagya, Lukoma, Ruhunga, Buhendangobo na Kishanje. Sambamba na doria hizo, elimu kuhusu mbinu za kujiepusha na kujihami na wanyamapori wakali na waharibifu imetolewa katika kata 21 ka kushirikiana na Maafisa Ugani. Wananchi wameelekezwa mbinu rafiki za kuwafukuza na kuwadhibiti wanyamapori hao wakiwemo ngedere.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua uhaba wa Askari wa Wanyamapori katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini hivyo itaendelea kushirikiana na halmashauri husika katika kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu ili wasilete madhara kwa maisha na mali za wananchi. Hata hivyo, naomba nitoe rai kwa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Vijijini kuajiri Askari wa Wanyamapori kwa ajili ya kuharakisha udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu.
MHE. JOSEPH L. HAULE aliuliza:-
Kumekuwa na migogoro ya mipaka kati ya hifadhi na wananchi kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi hizo kama vile Ruhembe, Kitete, Kikwalaza, Mji Mpya, Ihambwe, Mululu na sasa Kitongoji cha Lugawilo, Kata ya Uleling’ombe:-
Je, ni lini Serikali itaweka mipaka ili wananchi hao wasiendelee kunyang’anjywa ardhi yao kwa kisingizio cha kuwa wameingia kwenye Hifadhi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Leonard Haule, Mbunge wa Mikumi, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa hakuna mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa Mikumi na Vijiji vya Ruhembe na Ihambwe wala na Vitongoji vya Kikwalaza na Mji mpya ambavyo vimepakana na Hifadhi ya Taifa Mikumi. Mgogoro uliokuwepo ulishughulikiwa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kilosa, Viongozi wa Hifadhi, Viongozi wa Vijiji na wajumbe wane kutoka kila kijiji. Uhakiki wa mpaka wakati wa usuluhishi wa migogoro hiyo ulisimamiwa na viongozi wa Ardhi wa Mji Mdogo Mikumi, wataalam wa Ardhi Wilaya ya Kilosa, Mshauri wa Ardhi Mkoa wa Morogoro na wataalamu wa mipaka wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi. Kufuatia utatuzi huo, eneo la mpaka unaotenganisha vijiji na hifadhi, ulifwekwa na vigingi vya kudumu (beacons) kuwekwa pamoja na vibao vya kuonesha mpaka wa hifadhi katika baadhi ya maeneo. Vilevile hifadhi imeendelea kusafisha mpaka wake na vijiji vyote kila Mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Mikumi haina mgogoro wa mpaka na Kijiji cha Kitete Msindazi, kwani mpaka uliobainishwa na Tangazo la Serikali Na.121 la mwaka 1975 ulitafsiriwa ardhini kwa usahihi na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo uliridhiwa na pande zote husika zilishirikishwa katika uhakiki wa mpaka huo ambao ni viongozi wa vijiji na Hifadhi ya Mikumi chini ya usimamizi ya Kamati ya Ulinzi wa Usalama ya Wilaya ya Kilosa. Hata hivyo, lipo eneo la ardhi (general land) ambalo siyo sehemu ya hifadhi wala kijiji kati ya mpaka wa hifadhi na Kijiji cha Kitete Msindazi. Kisheria eneo hilo liko chini wa Kamishna wa Ardhi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mikumi na Kitongoji cha Lugawilo, Kata ya Uleling’ombe kwa kuwa hifadhi haipakani na kijiji chochote cha Kata ya Uleling’ombe. Aidha, naomba Mheshimiwa Mbunge atakapopata nafasi atembelee Hifadhi ya Taifa Mikumi kupata uhalisia wa kile kinachofanyika.
MHE. CECILIA D. PARESSO – (K.n.y. MHE. JULIUS K. LAIZER) aliuliza:-
Je, ni lini Serikali itatoa fidia stahiki kwa wananchi ambao mazao yao yaliharibiwa na wanyamapori tangu mwaka 2010 hadi 2017 katika maeneo ya Mswakini, Makuyuni, Naiti, Mbuyuni, Lokisale na maeneo mengine Wilayani Monduli?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer, Mbunge wa Monduli, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wanyamapori wakali na waharibifu ni kubwa na linajitokeza katika zaidi ya Wilaya 80 nchini. Uharibifu mkubwa wa mali na madhara kwa binadamu vikiwemo vifo husababishwa na tembo, mamba, nyati, kiboko, simba na fisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, uharibifu unaotokana na wanyamapori kwa sehemu kubwa unasababishwa na ongezeko la watu na shughuli zao ambazo mara nyingine zinafanyika katika maeneo yaliyo karibu na hifadhi au kwenye mapito ya wanyamapori. Aidha, mabadiliko ya tabianchi yamechangia pia katika kubadili mzunguko na mtawanyiko wa asili wa wanyamapori wakati wa kutafuta mahitaji muhimu, hususani chakula na maji. Hali hiyo kwa ujumla wake imeongeza ukubwa wa tatizo la muingiliano wa binadamu na wanyamapori na kusababisha uwepo wa matukio mengi ya uharibifu wa mali na madhara kwa binadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kuzingatia changamoto zilizopo, Wizara yangu kwa kushirikiana na halmashauri ya Wilaya ya Monduli, inaendelea kukabiliana na tatizo la wanyamapori wakali na waharibifu kwa kufanya doria za udhibiti wa wanyamapori hao katika maeneo mbalimbali ya Wilaya hiyo kulingana na taarifa za uharibifu zinazowasilishwa na wananchi husika. Aidha, Wizara itaendelea kutoa elimu ya njia mbadala ya udhibiti wa tembo na wanyamapori wengine katika Wilaya ya Monduli na maeneo mengine, mathalani matumizi ya uzio wa kamba zilizopakwa mchanganyiko wa pilipili na oili chafu, matumizi ya matofali ya kinyesi cha tembo kilichochanganywa na pilipili na mizinga ya nyuki kuzunguka mashamba ambayo tembo huogopa na kuondoka maeneo hayo. Sanjari na hayo, Wizara itaendelea kuelimisha wananchi kuhusu njia bora za kujikinga na wanyamapori wengine kwa kuhimiza ujenzi wa nyumba bora na imara.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Kanuni za Kifuta jasho na Machozi za Mwaka 2011, Serikali imekuwa ikitoa fedha kidogo za kuwafariji wananchi kwa kuwalipa kifuta jasho kwa uharibifu wa mali (mazao na mifugo) na kifuta machozi kwa madhara kwa binadamu (vifo na majeruhi). Katika kutekeleza mpango huo, jumla ya shilingi 48,015,000 zililipwa kwa wananchi 251 wa vijiji vya Wilaya ya Monduli waliokidhi vigezo vya kulipwa kuanzia mwaka 2010 hadi mwezi Aprili, 2018.
MHE. AUGUSTINO M. MASELE aliuliza:-
Pori la Akiba la Kigosi Moyowosi linakabiliwa na tatizo sugu la kutokuwa na barabara za uhakika kwa ajili ya shughuli za utalii na doria.
• Je, ni lini Serikali italifufua greda aina ya katapila lenye namba za usajili ST 892 lililosimama kufanya kazi tangu mwaka 2015 ili lisaidie kukarabati barabara?
• Kwa kuwa gari aina ya Grand Tiger linalotumika kwa shughuli za utawala limekufa, je, ni lini gari hilo litatengenezwa au kuleta gari lingine ili lisaidie shughuli za utawala katika Pori la Kigosi Moyowosi?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Augustino Manyanda Masele, Mbunge wa Mbogwe, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu inatambua umuhimu wa barabara na miundombinu mingine katika hifadhi zetu ili kuimarisha utalii na kufanya kazi za doria ipasavyo. Kwa kutambua umuhimu huo, Serikali iliamua kufufua mtambo, hususani greda lililokuwa limeharibika kwa muda mrefu katika Pori la Akiba la Moyowosi Kigosi ili liendelee kutumika kuimarisha barabara zilizopo ndani ya pori hilo. Greda hilo aina ya katapila lenye namba za usajili ST 892 limetengenezwa na linafanya kazi.
Aidha, Wizara ipo katika harakati za kufufua gari aina ya Grand Tiger ambalo hutumika kwa shughuli za utawala katika Pori la Akiba Moyowosi Kigosi ambapo mafundi wameshafanya tathmini ya ubovu wa gari hilo na Serikali imeshatenga fedha kwa ajili ya matengenezo hayo.
MHE. ANNA J. GIDARYA aliuliza:-
Mkoa wa Manyara ni moja kati ya maeneo yanayokubaliwa na changamoto ya migogoro ya ardhi katika wananchi wa Babati Vijijini hasa katika Vijiji vya Amayango, Gedamara na Hifadhi ya Tarangire kwa takribani miaka 11 sasa bila ufumbuzi wowote, migogoro hiyo imesababisha wananchi kukosa elimu, afya na uchumi kushuka ambapo majengo ya jamii yaliyopo ni madarasa manne, bweni moja, matundu 13 ya vyoo vya shule na jengo la zahanati na majengo haya yote yamejengwa kwa nguvu za wananchi.
• Je, Serikali ina mkakati gani wa kumaliza migogoro hiyo iliyodumu kwa muda mrefu na kurudisha maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa na hifadhi?
• Endapo itabainika mipaka kati ya vijiji na hifadhi iliyooneshwa kwenye ramani ni batili. Je, Serikali husika iko tayari kuwalipa fidia wananchi wote walioathirika na migogoro hiyo kwa muda wa miaka 11?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii naomba kujibu swali la Mheshimiwa Anna Joram Gidarya, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, uhakiki wa mpaka wa Hifadhi ya Taifa Tarangire na Vijiji vya Gedamar na Ayamango ulifanywa na wataalam wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mwaka 2004 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Namba 160 la mwaka 1970 lililoanzisha Hifadhi ya Taifa Tarangire. Baada ya uhakiki huo eneo hilo lilisimikwa vigingi (beacons) vya kuainisha mpaka wa hifadhi na vijiji husika ambao unafahamika kwa wananchi.
Mheshimiwa Spika, katika uhakiki huo ilibainika kuwa kaya 245 za vijiji vilivyotajwa hapo juu zilikuwa ndani ya eneo la Hifadhi ya Taifa Tarangire kimakosa. Ili kuwaondoa wananchi wa vijiji hivyo kutoka kwenye eneo la hifadhi, Serikali iliamua kuwalipa wananchi waliokuwa ndani ya eneo la hifadhi kifuta jasho kilichohusisha fidia ya mali, posho ya usumbufu, posho ya makazi na gharama za usafiri.
Mheshimiwa Spika, wananchi wa Vijiji vya Gedamar na Ayamango walilipwa jumla ya shilingi 137,845,592 tarehe 2 Februari, 2011 kupitia Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati. Baada ya malipo ya kifuta jasho wananchi wengi waliondoka isipokuwa kaya 42 ambazo ziliomba kupewa eneo mbadala la kuhamia. Halmashauri ya Wilaya ya Babati ilikubali kuwapatia wananchi hao eneo maeneo ya kuhamia kwenye shamba la Ufyomi lililopo Gallapo ambapo wananchi hao wameshapatiwa maeneo katika shamba hilo.
Mheshimiwa Spika, kwa sasa hakuna mgogoro wa mpaka uliopo kati ya Vijiji vya Gedamar na Ayamango na Hifadhi ya Tarangire na mpaka uliopo kati ya hifadhi na vijiji hivyo ni sahihi.
MHE. ESTER A. BULAYA aliuliza:-
Vijiji vya Tamau, Nyantwali, Serengeti, Mcharo, Kanzugu, Bukore na Mihale Wilaya ya Bunda vinapakana na Hifadhi ya Serengeti lakini havinufaiki na chochote kutoka katika hifadhi husika.
Je, ni utaratibu gani umeandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori ili kusaidia vijana wanaozunguka hifadhi kupatiwa ajira ili kunufaika na hifadhi husika kama njia mojawapo ya kudumisha ujirani mwema?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ester Amos Bulaya, Mbunge wa Bunda Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Taifa ya Serengeti inapakana na Wilaya nane ambazo ni Ngorongoro, Meatu, Itilima, Bariadi, Busega, Tarime, Bunda na Serengeti. Aidha, Wilaya ya Bunda ina vijiji sita vinavyopakana moja kwa moja na hifadhi ambavyo ni Serengeti, Nyatwali, Tamau, Balili, Kuzungu na Bukore. Aidha, vijiji vya Mihale na Bukore vinapakana na pori la Akiba la Ikorongo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha 2017/2018 hifadhi imetenga jumla ya shilingi 32,233,180 kuchangia ujenzi wa madarasa mawili katika shule ya msingi Bunyunyi, Kijiji cha Hunywari.
Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda inaendelea kukusanya tozo za huduma yaani hotel levy kwenye hoteli na lodges katika hifadhi zilizopo kwenye eneo la utawala la Wilaya hiyo. Mchango wa hifadhi katika Wilaya ya Bunda kutoka mwaka 2004/2005 hadi mwaka 2017/2018 ni shilingi 276,720,630 ambazo zimetumika kutekeleza jumla ya miradi tisa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na miradi ya ujirani mwema, Wizara imekuwa ikichangia katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda asilimia 25 ya mapato yanayotokana na ada ya shughuli za uwindaji wa kitalii zinazofanyika katika mapori ya Akiba ya Ikorongo na Gurumeti.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kipindi cha mwaka 2004/2005 hadi 2014/2015 Halmashauri wa Wilaya ya Bunda ilipokea jumla ya shilingi 156,200,125.87. Katika kipindi cha mwaka 2016/2017 na 2017/2018 yaani kuanzia juni mwaka 2017 hadi Januari 2018 Halmashauri ya Wilaya ya Bunda imepokea jumla ya shilingi 77,559,441.84.
MHE. ANATROPIA L. THEONEST aliuliza:-
(a) Je, ni kwa nini Serikali inawazuia wakulima wanaoshirikiana na sekta binafsi, kuuza mazao yao ya biashara hasa kahawa, mahindi na korosho nje ya nchi kwa lengo la kujipatia faida?
(b) Je, ni kwa nini Serikali isiongeze ruzuku ya NFRA ili inunue mazao hayo pindi bei zinaposhuka?
WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Anatropia Lweikila Theonest – Mbunge Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa na inaendelea kutoa vibali kwa wakulima na wafanyabiashara mbalimbali wanaosafirisha mazao ya kilimo hususan mahindi nje ya nchi au kuingiza ndani ya nchi. Vibali vitolewavyo na Wizara ya Kilimo ni vya kuingiza mazao ya kilimo nchini au kusafirisha mazao ya kilimo nje ya nchi (Import and Export Permits) pamoja na cheti cha Usafi wa Mazao yanayosafirishwa (Phytosanitary Certificate).
Mheshimiwa Spika, Serikali haina mpango wa aina yoyote wa kuwazuia wakulima kushirikiana na sekta binafsi kuuza mazao yao nje ya nchi na Serikali inaendelea kuhimiza wakulima waendelee kujiunga katika vikundi ili waweze kuwa na nguvu ya pamoja katika kuuza mazao yao na kuweza kuongezea thamani mazao yao ili waweze kujiongezea kipato zaidi.
(b) Mheshimiwa Spika, Majukumu ya Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) ni kununua na kuweka akiba ya chakula cha Taifa, kudhibiti mfumuko wa bei wa vyakula vya nafaka kwa kuingiza nafaka sokoni ya bei nafuu pamoja na kutoa chakula cha msaada kwa maelekezo ya Mfuko wa Maafa wa Taifa pindi Taifa linapopatwa na majanga ya maafa. Kwa kuzingatia majukumu hayo, Wakala umekuwa kimbilio la wakulima kwa kuwa umekuwa ukinunua nafaka kwa bei nzuri katika masoko inayozingatia gharama za uzalishaji za mkulima.
Mheshimiwa Spika, Serikali hutenga ruzuku kwa ajili ya ununuzi wa nafaka kila mwaka. Kwa kuzingatia majukumu ya Wakala, ununuzi huu hauhusishi mazao yasiyo ya nafaka. Aidha, Wakala hutumia vyanzo vingine vya mapato kununua nafaka zikiwemo mauzo ya nafaka na mikopo kutoka taasisi za fedha, mikopo ambayo hurejeshwa kwa kutumia fedha za mauzo ya nafaka.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI aliuliza:-
Zao la pamba linakabiliwa na kero nyingi kutokana na kukosekana uhakika wa bei yake.
Je, Serikali inawaambia nini wakulima wa pamba?
WAZIRI WA KILIMO aliuza:-
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. Raphael Chegeni Mbunge wa Jimbo la Busega kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua tatizo la kuyumba kwa bei ya pamba katika soko la Kimataifa. Aidha, kufuatia tatizo hilo, Serikali ili ingilia kati ununuzi wa pamba katika msimu wa ununuzi wa 2019/2020 ili kuhakikisha mkulima anapata bei yenye tija.
Mheshimiwa Naibu Spika, Suluhisho la kudumu kuhusu bei ya pamba ni kuongeza kiasi cha pamba inayochakatwa ndani ya nchi ili kuzalisha bidhaa zitakazotumika hapa nchini na hivyo kupunguza utegemezi wa soko la nje. Ili kutekeleza Mpango huo, Serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya kibiashara kwa ajili ya wawekezaji wa ndani na wa nje kujenga Viwanda vya kuongeza thamani ya zao la Pamba kwa kufuta tozo na kodi mbalimbali, kuzalisha umeme wa uhakika na bei nafuu, kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kuongeza tija na uzalishaji ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza bei na kipato kwa wakulima wa pamba, kuendelea kuongeza mitaji katika Taasisi za kifedha na maendeleo kama vile Benki ya Maendeleo ya kilimo na Benki ya Rasilimali ili ziweze kutoa mkopo ya muda mrefu na kati kwa Viwanda vya Pamba ili kuongeza soko na mahitaji ya soko la ndani la Pamba na kupandisha uhitaji na Bei ya Pamba kupanda.
Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara ya Kilimo imekipatia Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kazi ya kuandaa taarifa ya kina ya uwekezaji katika viwanda vya pamba ili kukuza soko la pamba. Taarifa hiyo itatoa dira ya namna ya kuanzisha viwanda vikiwemo vya kusindika pamba na inatarajiwa kukamilika kabla ya Julai, 2020.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kuimarisha huduma za ugani na upatikanaji wa pembejeo kwa wakulima ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kupunguza gharama za uzalishaji na kuongeza kipato kwa wakulima.