Primary Questions from Hon. Japhet Ngailonga Hasunga (CPA) (25 total)
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Tatizo la ajira nchini kwa wahitimu wa vyuo vya kati na juu ni kubwa sana:-
(a) Je, ni wahitimu wangapi hawana kazi hadi sasa kutoka Vyuo vya Elimu ya Juu nchini?
(b) Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa ajira kwa wahitimu au kuwawezesha kujiajiri hasa vijana?
NAIBU WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU – SERA, BUNGE, KAZI, VIJANA, AJIRA NA WALEMAVU - (MHE. ANTONY P. MAVUNDE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali namba mbili la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, kwa mwaka 2014 vijana wahitimu wa elimu ya juu wasio na ajira wanakadiriwa kuwa 27,614 ambapo kati yao 14,271 ni wanawake na 13,343 ni wanaume. Hata hivyo, Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kukabiliana na tatizo la ajira kwa vijana wahitimu wa Elimu ya Juu kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuajiriwa au kujiari.
(b) Mheshimiwa Spika, jukumu kubwa la Serikali ni kusimamia Sera na Sheria mbalimbali ambazo zinaweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira ikiwemo kilimo na biashara), pia kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili viweze kuajiri sehemu kubwa ya nguvu kazi nchini na wengine kujiajiri wenyewe.
Mheshimiwa Spika, ili kukabiliana na tatizo la ajira kwa wahitimu wa elimu ya juu, Serikali inatekeleza mipango ifuatayo:-
Kwanza, kuimarisha Wakala wa Huduma za Ajira Tanzania (TaESA) ambao una jukumu la kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri wa ndani na nje ya nchi.
Pili, kuandaa Mkakati wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao utaanza kutekelezwa mwaka ujao wa fedha wa 2016/2017, Mkakati huu umejikita zaidi katika kuwezesha mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi ili wawe na ujuzi unaohitajika katika maeneo ya kazi.
Tatu, kuendelea kusimamia utekelezaji wa Program ya Taifa ya Kukuza Ajira kwa Vijana, ambayo imelenga kuwajengea uwezo vijana kwa njia ya mafunzo ya stadi za ujasiriamali, stadi za maisha na stadi za kazi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kwa muda mrefu uchumi wa Nchi yetu umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa mwaka:-
Je, mapato ya Serikali yamekuwa yakiongezeka kwa asilimia ngapi kwa mwaka?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:
Mheshimiwa Spika, uchumi wa nchi yetu kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita 2010-2015 umekua kwa wastani wa asilimia 6.74. Ukuaji halisi wa asilimia katika kipindi hicho ulikuwa asilimia 6.4 mwaka 2010, asilimia 7.9 mwaka 2011, asilimia 5.1 mwaka 2012, asilimia 7.3 mwaka 2013 na asilimia saba mwaka 2014.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho mapato ya Serikali ambayo yanajumuisha mapato ya kodi na mapato yasiyokuwa ya kodi ya Serikali Kuu pamoja na mapato ya Halmashauri yamekuwa yakiongezeka kwa wastani wa asilimia 17.8 kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mwaka 2010/2011 mapato yalifkia shilingi trilioni tano nukta saba tatu na kuongezeka hadi Shilingi trilioni saba nukta mbili mbili mwaka mwaka 2011/2012 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.9, mwaka 2012 mapato yakafikia shilingi trilioni nane nukta tano moja, ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.9. Mwaka 2013/2014 mapato yalifikia shilingi trilioni kumi nukta moja mbili ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.6 na mwaka 2014/2015 mapato yakafikia shilingi trilioni kumi nukta tisa tano, sawa na ongezeko la asilimia 7.6.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Mwaka 2002 Serikali ilipitisha Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na Marekebisho yake ya mwaka 2008 yaliweka Mfumo wa Wazi wa Upimaji na Ujazaji wa Mkataba wa Utendaji Kazi (OPRAS):-
(a) Je, ni kwa kiasi gani mfumo huu umetekelezwa nchini?
(b) Ni lini mfumo wa kupima taasisi (institutional performance) utaanzishwa na kuanza kutangazwa hadharani?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAMISEMI, UTUMISHI NA UTAWALA BORA (MHE. ANGELLAH J. KAIRUKI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, mfumo wa kupima utendaji kazi kwa uwazi ulianzishwa mwezi Julai, 2004 ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kutekeleza Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1998 kama ilivyohuishwa mwaka 2008 pamoja na Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura 298.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2012/2013, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Tume ya Utumishi wa Umma ilifanya Tathmini ya Uzingatiaji na Utekelezaji wa Mfumo wa OPRAS katika taasisi za umma. Tathmini hiyo ilihusisha taasisi za umma 110 katika kipindi cha awamu tatu. Katika tathmini hiyo, lengo lilikuwa ni kufuatilia taasisi zilizokuwa na utekelezaji wa kiwango cha juu. Napenda tu kuliarifu Bunge lako kwamba matokeo ya tathmini hiyo yalionesha kwamba utekelezaji uko katika asilimia 51.
Mheshimiwa Spika, hatua zilizochukuliwa ili kuhakikisha kwamba mfumo huu unatekelezwa na watumishi wote, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora iliagiza waajiri kuhakikisha kwamba mtumishi atapandishwa cheo tu kwa kuzingatia matokeo ya OPRAS. Hatua hii imesaidia sana kuongeza kiwango cha utekelezaji kwani sasa kila mtumishi anatekeleza mfumo huu kama sharti la kupandishwa cheo.
Mheshimiwa Spika, kuhusu lini Serikali itaanzisha na kutangaza mfumo wa kupima taasisi (institutional performance) hadharani, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba Serikali inatarajia kuanza utekelezaji wa Mikataba ya Utendaji kazi katika mwaka wa fedha 2016/2017. Mikataba hii itatekelezwa na taasisi zote za umma ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika ya Umma na Taasisi nyingine za umma. Mfumo huu utaiwezesha Serikali kupima utendaji kazi kwa kila taasisi ya umma kwa kila mwaka.
MHE. DKT. RAPHAEL M. CHEGENI (K.n.y. MHE. JAPHET N. HASUNGA) aliuliza:-
Sheria ya Mahusiano Kazini ya mwaka 2004 inawataka wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi vya kisekta; walimu na wafanyakazi wengine wamekuwa wakiingizwa kwenye vyama hivyo bila ya wao wenyewe kukubali.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaruhusu wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanavyotaka kwa hiari badala ya kuwalazimisha?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Namba 6 ya mwaka 2004 imeeleza bayana kuwa wafanyakazi wanayo haki ya kuanzisha au kujiunga na vyama vya wafanyakazi wanavyovipenda wenyewe pasipo kumlazimisha mtu yeyote. Hivyo ni makosa kwa mtu yeyote, awe ni mwajiri au chama cha wafanyakazi, kumlazimisha mwanachama kujiunga na chama pasipo ridhaa yake. Taratibu ni kwamba mfanyakazi anatakiwa kujaza fomu namba TFN 6 ili kutoa idhini yake kujiunga na chama anachokipenda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nirudie tena kutoa wito kwa waajiri wa vyama vya wafanyakazi kuzingatia matakwa ya sheria kwa kutowalazimisha wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi pasipo ridhaa yao. Hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya waajiri na vyama vya wafanyakazi vitakavyokiuka matakwa ya sheria hii ili kuruhusu wafanyakazi kuunda vyama vya wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi. Hata hivyo Serikali inatoa onyo kwa waajiri wanaokiuka sheria za kazi kwa kuwalazimisha wafanyakazi kujiunga na vyama vya wafanyakazi wasivyovitaka. Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa waajiri wanaokiuka sheria za kazi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Katika eneo la Ndolezi Wilaya ya Mbozi kuna kimondo ambacho ni cha aina yake katika nchi hii na dunia kwa ujumla:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhamasisha watalii wa ndani na nje ya nchi kuja kukiangalia Kimondo hicho ili kuchangia pato la taifa?
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubalina na Mheshimiwa Mbunge kuwa Kimondo hiki kilichopo Kusini Magharibi mwa Kilima cha Marengi, Kijiji cha Ndolezi Wilaya ya Mbozi, Mkoani Mbeya ni cha kipekee hapa nchini, na kwakweli na duniani kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kulingana na taarifa za kitaalamu kimondo hiki kinaaminika kuwa kati ya vimondo nane vikubwa zaidi duniani kikikadiriwa kuwa na uzito wa tani 12, urefu wa mita 3.3, upana wa mita 1.63 na kimo cha mita 1.22. Sehemu yake kubwa ni chuma ambayo asilimia 90.45 na sehemu iliyobaki inajumuisha nikeli asilimia 8.69, shaba asilmia 0.66, sulphur asilimia 0.01, fosfori asilimia 0.11. Kwa kuzingatia upekee na umuhimu wake, mwaka 1967 kilitangazwa kuwa Urithi wa Taifa kwa tangazo la Serikali Na. 90 la tarehe 1967. Taarifa kuhusinaa na tarehe na mwaka wa kuanguka kwa kimondo hiki bado haijulikani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu imeendelea kutangaza Kimondo cha Mbozi kama moja ya vivutio muhimu na adimu nchini na duniani. Uhamasishaji umefanyika kwa kutumia njia mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na vipindi vya runinga vya zamadamu (Televisheni ya Taifa TBC1) na utalii wa ndani kupitia Kituo cha Channel Ten. Pia machapisho ya Tanzania; The Land of Great Heritage Sites na Tanzania Cultural Heritage Resources ambayo nakala zake pia husambazwa katika maonesho mbalimbali na balozi zetu nje ya nchi. Machapisho mengine ambayo hutolewa kwa Kiswahili ni pamoja na Jarida la Ifahamu Idara ya Mambo ya Kale na Jarida la Maliasili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maelezo na picha za kimondo hiki pia vimewekwa katikatovuti na mitandao mbalimbali duniani. Juhudi hizi pamoja na nyingine zimeendelea kuonesha matunda kwani takwimu zinaonesha kuongezeka kwa idadi ya watalii na mapato. Kwa mfano kati ya mwaka 2012/13 na 2014/2015 watalii waliongezeka kutoka jumla ya 990 hadi 1,681 na mapato kuongezeka kutoka Shilingi 811,000 hadi 2,426,000.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kuwepo kwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya nchini kumekuwa kukileta migongano katika utekelezaji wa sera na shughuli mbalimbali za maendeleo nchini:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuupitia upya mfumo wa ugatuaji wa madaraka (D by D) ili kuweza kuuboresha na kupunguza migongano mbalimbali ya kiutendaji?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Wakuu wa Mikoa wapo kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika Ibara ya 61(1) mpaka (5) na majukumu yake yamefafanuliwa vizuri katika Ibara ya 61(4) kwamba atakuwa na wajibu wa kusimamia utekelezaji wa kazi na shughuli zote za Serikali katika eneo lake.
Mheshimiwa Naibu Spika, dhana ya Ugatuaji wa Madaraka kwa Umma (Decentralization by Devolution) pia inatokana na Ibara ya 145 na 146. Madhumuni yake ni kupeleka madaraka kwa wananchi yakiwemo madaraka ya kisiasa, kifedha, kiutawala ili kusogeza huduma karibu na wananchi. Mkuu wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya ni wasimamizi wa sera, sheria, kanuni na miongozo katika Mikoa na Wilaya wanayoongoza.
Mheshimiwa Naibu Spika, Viongozi hao kisheria hawaruhusiwi kuingilia (interference) maamuzi na utendaji wa Serikali za Mitaa endapo hakuna sheria au taratibu zilizokiukwa kimaamuzi. Hata hivyo, wamepewa mamlaka na sheria kuingilia kati (interventions) endapo maamuzi yatakayofanywa na Serikali za Mitaa yatakiuka sera, sheria na miongozo iliyopo.
Mheshimiwa Naibu Spika, mahusiano kati ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa yamebadilika kutoka kwenye dhana ya utoaji amri na upokeaji amri au mdhibiti na mdhibitiwa, kuwa ya mashauriano, majadiliano na maelewano. Vilevile, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imeendelea kufanya vikao vya pamoja na Wizara za Kisekta ili kuwa na uelewa wa pamoja wa dhana ya ugatuaji na mantiki yake katika kusogeza karibu huduma kwa wananchi.
MHE. JAPHET N HASUNGA aliuliza:-
Kwa kuwa watumishi na viongozi wengi wamekuwa wanaingia kwenye madaraka mbalimbali ya nchi bila kupewa mafunzo ya kuwaandaa kama ilivyo katika nchi nyingi duniani na kama ilivyo kwenye vyombo vya majeshi yetu.
Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha kuwa viongozi wote wanapewa mafunzo ya awali kabla ya uteuzi wa madaraka yoyote katika utumishi wa umma?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa kuwapatia mafunzo ya awali watumishi na viongozi wa umma kabla ya uteuzi wa madaraka yoyote katika utumishi wa umma ili waweze kuuelewa utumishi wa umma na kufahamu misingi yake, sheria, kanuni na taratibu za utendaji kazi na kuwapatia stadi za uongozi zinazowezesha kutekeleza majukumu yao kwa weledi na ufanisi. Katika kutekeleza azma hii Serikali imechukua hatua zifuatazo:-
(a) Imeandaa na kuendesha mafunzo elekezi kwa watumishi wanaoteuliwa kushika nafasi za uongozi ili waweze kumudu madaraka mapya.
(b) Imeendelea kutoa mafunzo ya uongozi (Leadership Development Programmes), kwa watumishi waandamizi kwa lengo la kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, lakini pia kuwaandaa kwa ajili ya kushika nafasi za uongozi pindi watakapoteuliwa kushika nafasi hizo. Mafunzo hayo yamekuwa yakiendeshwa na taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo Taasisi ya Uongozi, Wakala wa Mafunzo kwa njia ya Mtandao (TaGLA), Chuo Kikuu cha Mzumbe pamoja na ESAMI. Katika kipindi cha mwaka 2015/2016 watumishi waandamizi 1,397 waliweza kupatiwa mafunzo ya uongozi.
(c) Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Serikali imeanzisha Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College of Tanzania) kinachotoa mafunzo ya uongozi kwa Maafisa Waandamizi wa Kijeshi na Kiraia (Inter Service Training) kwa kuhusisha Maafisa wa Jeshi na wa Kiraia (Defence-Civil Staff Training) ikiwa ni pamoja na kuwapatia uelewa wa masuala ya usalama na hivyo kuwajengea uwezo wa kutambua athari za kiusalama wanapotunga na kutekeleza sera, sheria na maamuzi mbalimbali ya kiutendaji.
(d) Mheshimiwa Mweenyekiti, lakini pia, Serikali kupitia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kimetoa mafunzo kwa viongozi waandamizi 86 na kiko katika maandalizi ya kuandaa utaratibu wa kuwa na mafunzo ya lazima kwa Maafisa Waandamizi katika utumishi wa umma (Mandatory Course for Senior Officers in the Public Service). Mafunzo haya ya lazima yanalenga kuwawezesha Maafisa Waandamizi kujua majukumu ya msingi ya uongozi na usimamizi katika taasisi za umma, hivyo kuwaandaa na kuwajengea uwezo wa kutekeleza majukumu hayo pindi watakapoteuliwa kushika nafasi za uongozi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kujua kusoma na kuandika ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya demokrasia na kudumisha umoja na amani nchini.
Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua elimu ya watu wazima kwa vijana wote walio chini ya miaka 40?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kujua kusoma na kuandika ni nguzo muhimu sana katika maendeleo ya demokrasia na kudumisha umoja na amani nchini. Takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 kwa Tanzania Bara zinaonyesha kuwa watu wenye umri wenye umri wa miaka 15 na kuendelea ambao hawajui kusoma na kuandika ni asilimia 22.4.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu wa kujua kusoma na kuandika Serikali imekuwa ikitenga fedha kwa ajili ya kutekeleza programu mbalimbali za kuwapatia vijana na watu wazima stadi za kujua kusoma, kuandika na kuhesabu.
Programu hizo ni pamoja na mpango wa uwiano kati ya elimu ya watu wazima na jamii (MUKEJA)unaojumuisha programu ya ndiyo ninaweza inayoendeshwa kama tarajali katika Wilaya tisa za majaribio ambazo ni Halmashauri za Wilaya za Bagamoyo, Mwanga na Mkurunga, pamoja na Manispaa za Ilemela, Dodoma, Songea, Kinondoni, Temeke na Ilala.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha elimu ya watu wazima na kuiwezesha jamii kuwa na stadi za KKK, Wizara yangu imeandaa miongozo ya wawezeshaji na vitabu ambavyo vimekwisha sambazwa katika Halmashauri zote nchini. Aidha, kila Mamlaka ya Serikali ya Mitaa imeelekezwa kutenga fedha katika bajeti zake kwa ajili ya kununua vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kutoa mafunzo kwa wawezeshaji, kulipa honoraria kwa wawezeshaji, kufanya ufuatilia na kuhamasisha jamii ili watu wazima na vijana wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu wajiunge kwenye madarasa ya kisomo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania kumetokana na kuruhusu kutoza bidhaa mbalimbali na huduma kwa dola na kuathiri thamani ya fedha yetu.
Je, Serikali inachukua hatua gani za kuimarisha shilingi yetu na kupiga marufuku matumizi ya fedha za kigeni nchini?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi hakutokani na kuruhusu bidhaa mbalimbali na huduma kutozwa kwa dola, bali hutokana na misingi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi (Micro Economic Fundamentals) na hali halisi ya uchumi wa nchi tunazofanyanazo biashara.
Mheshimiwa Naibu Spika, kushuka au kupanda kwa thamani ya shilingi kunaweza kusababishwa na mambo makuu yafuatayo:-
(i) Nakisi ya urari wa biashara; nakisi ya urari wa biashara ya nje ya nchi (balance of payments) husababisha sarafu kushuka thamani kama mauzo ya bidhaa nje ya nchi ni madogo ikilinganishwa na ununuzi wa bidhaa kutoka nje. hali hiyo, hufanya thamani ya shilingi kushuka kwa sababu mahitaji yetu ya fedha za kigeni ni makubwa kuliko mapato ya mauzo yetu nje ya nchi.
(ii) Mfumuko wa bei; pamoja na mambo mengine mfumuko wa bei husababishwa na ongezeko kubwa la ujazo wa fedha kuliko uzalishaji wa bidhaa na huduma mbalimbali katika nchi. Aidha, thamani ya fedha hupungua iwapo mfumuko wa bei wa ndani ni mkubwa kuliko mfumuko wa bei katika nchi tunazofanyanazo biashara ni za nje ya nchi.
(iii) Tofauti ya misimu (seasonal factors); upatikanaji wa fedha za kigeni kutokana na biashara za msimu husababisha kusesereka au kutoserereka kwa shilingi ya Tanzania. Kwa mfano, mapato mengi ya fedha za kigeni kutikana na biashara ya nje huongezeka wakati wa nusu ya pili ya kila mwaka yaani kati ya Julai na Disemba, ikiwa ni kipindi cha mavuno na kilele cha utalii hivyo, thamani ya shilingi huimarika au kuwa na utulivu zaidi katika kipindi kati ya Julai na Disemba.
Mheshimiwa Naibu Spika, takwimu zinaonesha kuwa pamoja na kuwepo kwa sheria ya kutotumia kabisa fedha za kigeni nchini Afrika ya Kusini, lakini sarafu ya nchi hiyo imapatwa na misukosuko mikubwa zaidi ya shilingi ya Tanzania. Hata thamani ya sarafu nyingine kubwa duniani kama vile Yen ya Japan, Renminbi ya China na Euro zimekuwa zikiyumba kwa kasi zaidi ya shilingi ya Tanzania.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuimarisha thamani ya shilingi Benki Kuu inaendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ili usitofautiane sana na wabia wetu wa biashara. Pia Benki Kuu imedhibiti biashara ya maoteo (speculation) katika soko la fedha za kigeni, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa miamala ya fedha za kigeni inayofanywa na benki kwa ajili ya shughuli za kiuchumi tu na sio biashara ya maoteo. Hali hii itasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni katika soko la rejareja na hivyo kupunguza shinikizo la kuporomoka kwa thamani ya shilingi.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni vema ikaeleweka kuwa pamoja na hatua zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na Benki Kuu, ufumbuzi wa kudumu wa kutengemaa kwa thamani ya shilingi hutegemea zaidi kupungua kwa nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamisho wa mali nchi za nje. Hii itawezekana tu endapo tutaongeza uzalishaji na kuwa na ziada ya kuongeza mauzo yetu nje ya nchi na pia kupunguza uagizaji wa bidhaa na huduma zisizo za msingi kutoka nje.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya Serikali na Taasisi zake.
Je, Serikali inategemea kuchukua hatua gani ili kutekeleza azma hiyo ya kudhibiti matumizi ya fedha za umma katika taasisi zake?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina imechukua hatua kadhaa katika kuboresha usimamizi wa mashirika na taasisi za umma hususan katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima. Hatua zilizochukuliwa zimegawanyika katika makundi makuu mawili. Kundi la kwanza ni kutungwa kwa sheria mbalimbali na Bunge lako Tukufu na kundi la pili ni miongozo mbalimbali iliyotolewa na Msajili wa Hazina katika utekelezaji wa majukumu yake ya kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria zilizopitishwa na Bunge lako Tukufu ni pamoja na Sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015, ambayo imebainisha hatua mbalimbali za kibajeti zenye lengo la kuongeza usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma katika mashirika na taasisi za umma. Pamoja na masuala mengine, sheria hiyo imebainisha utolewaji wa Mwongozo wa Mpango na Bajeti (Plan and Budget Guidelines) wa Serikali unaojumuisha mashirika na taasisi zote za Serikali ambao unatoa miongozo mbali mbali ya kuzingatiwa katika matumizi ya Umma kwa mwaka husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia sheria hiyo, Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa mamlaka ya kupitia bajeti za mashirika na taasisi zilizo chini yake kwa kuzingatia miongozo na mipango ya Serikali inayotarakiwa kutekelezwa. Pia Ofisi ya Msajili wa Hazina imepewa jukumu la kupitia na kuridhia kanuni za fedha (financial regulations) za mashirika na taasisi zote za umma ili kuimarisha usimamizi na udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Sheria nyingine iliyopitishwa na Bunge lako Tukufu ni marekebisho ya Sheria ya Fedha ya mwaka 2015 ambayo iliweka ukomo wa taasisi na mashirika ya umma kutumia asilimia 60 tu ya mapato yake kwa matumizi ya kawaida yasiyojumuisha mishahara. Aidha, kati ya asilimia 40 inayobaki, asilimia 70 ya fedha hizo inarejeshwa kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Msajili wa Hazina katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria ametoa miongozo mbalimbali yenye lengo la kudhibiti matumizi ya mashirika na taasisi za umma kama ifuatavyo:-
• Barua iliyotolewa na Msajili wa Hazina tarehe 10 Novemba, 2015 ya kudhibiti safari zisizo za lazima nje ya nchi kwa watumishi wa mashirika na taasisi za umma ambazo awali zilionekana kutumia sehemu kubwa ya fedha za umma.
• Waraka wa Msajili wa Hazina Namba 12 wa mwaka 2015 kuhusu Posho za Vikao vya Bodi ya Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma. Waraka huo umefuta posho za Vikao vya Bodi na kuondoa utaratibu wa Bodi kuwa na vikao zaidi ya vinne kwa mwaka mmoja.
• Waraka wa Msajili wa Hazina Namba 1 wa mwaka 2016 kuhusu posho za kujikimu kwa Wajumbe wa Bodi za Wakurugenzi wa Mashirika na Taasisi za Umma. Waraka huo uliweka ukomo wa posho hizo kwa Wajumbe wa Bodi kwa safari za ndani na nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kusimamia na kufuatilia miongozo yote inayotolewa na Serikali ili kuhakikisha kuwa lengo la kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima kwenye mashirika na taasisi za umma linafanikiwa.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mkakati gani wa kufufua zao la Kahawa nchini ambalo ni moja ya mazao ya kimkakati?
(b) Je, ni lini Makampuni binafsi yataruhusiwa kununua Kahawa kwa Wakulima moja kwa moja bila kupitia Vyama vya Ushirika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inaendelea kutekeleza Mkakati wa Miaka Kumi wa Maendeleo ya Zao la Kahawa wenye lengo la kuongeza tija na ubora wa kahawa nchini. Utekelezaji wa mkakati huo umewezesha kuongeza uzalishaji wa kahawa kutoka tani 43,872 za kahawa za msimu wa mwaka 2017/2018 hadi tani 67,000 msimu wa 2020/2021. Aidha, wastani wa bei kwa wakulima wa kahawa kavu aina ya Arabika umeongezeka kutoka shilingi 3,500 kwa mwaka 2019/2020 hadi shilingi 4,000 kwa mwaka 2020/2021 na bei ya kahawa ya maganda ya Robusta imeongezeka kutoka wastani wa shilingi 1,100 kwa mwaka 2019 hadi shilingi 1,200 mwaka 2020/2021.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, mkakati wa Wizara ni kuhakikisha kwamba tunaongeza tija; uwekezaji mkubwa katika Taasisi yetu ya Utafiti ya TaCRI; mfumo wa masoko; kuboresha mfumo wa ushirika, uzalishaji na ugawaji wa miche. Mpaka sasa Wizara imeshaanza mradi wa uzalishaji wa miche milioni 5.5 kwa ajili ya kuendelea kugawa bure kwa wakulima wa kahawa nchini. Vilevile Serikali imeipatia Taasisi ya TaCRI jumla ya shilingi milioni 300 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya utafiti.
Mheshimiwa Naibu Spika, aidha, kuhusu mfumo wa wanunuzi wa kahawa kupitia Vyama vya Ushirika umelenga kuongeza ushindani katika soko la awali kulingana na ubora wa kahawa na pia kuwawezesha wakulima kuwa na nguvu ya pamoja ya kushauriana ili kupata bei nzuri na kunufaika na kilimo, hivyo kuondokana na walanguzi ambao wamekuwa wakiwalaghai baadhi ya wakulima. Hivyo, kampuni binafsi na wenye viwanda vya kahawa wanaruhusiwa kununua kahawa kutoka kwa wakulima kupitia Vyama vya Ushirika vya Msingi na Vyama Vikuu.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Je, lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe itakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe?
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa kujenga majengo mawili ikiwa ni Jengo la Huduma za Uchunguzi wa Maabara ambalo limefikia asilimia 98 na Jengo la Huduma za Wagonjwa wa Nje (OPD) ambalo ujenzi umefikia asilimia 96. Majengo haya mawili yanatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Julai, 2021.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Jengo la Huduma za Afya ya Uzazi pale pale ambao utakamilika mwezi Februari, 2022 na kiasi cha shilingi bilioni tano kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Je, lini Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe itakamilika na kuanza kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe?
WAZIRI WA AFYA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe kwa kujenga majengo mawili ikiwa ni Jengo la Huduma za Uchunguzi wa Maabara ambalo limefikia asilimia 98 na Jengo la Huduma za Wagonjwa wa Nje (OPD) ambalo ujenzi umefikia asilimia 96. Majengo haya mawili yanatarajiwa kuanza kutoa huduma ifikapo mwezi Julai, 2021.
Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza ujenzi wa Jengo la Huduma za Afya ya Uzazi pale pale ambao utakamilika mwezi Februari, 2022 na kiasi cha shilingi bilioni tano kimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi huo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo la maji katika Mji wa Vwawa?
WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, mahitaji ya maji ya Mji Vwawa ni zaidi ya lita milioni 10 kwa siku ambapo kwa sasa hali ya upatikanaji wa huduma ya maji ni asilimia 43.2.
Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza mipango ya muda mfupi na muda mrefu ili kuboresha huduma ya maji safi na salama katika Mji wa Vwawa ambapo katika mpango wa muda mfupi mwaka 2020/2021, Wizara imechimba visima virefu vitatu vyenye uwezo wa kuzalisha maji lita 600,000 kwa siku. Ujenzi wa miundombinu ya usambazaji maji ya visima hivyo utafanyika ndani ya mwaka wa fedha 2021/2022 na kuongeza huduma ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa Mji wa Vwawa kufikia asilimia 70.
Mheshimiwa Spika, katika mpango wa muda mrefu wa kuboresha huduma maji safi, salama na yenye kutosheleza kwa wakati wa mji huo Serikali imepanga kujenga mradi kupitia chanzo cha maji cha Mto Bupigu uliopo Wilaya ya Ileje wenye uwezo wa kuzalisha maji kiasi cha lita milioni 73 kwa siku. Mtaalam Mshauri kwa ajili ya kufanya Usanifu wa Kina yaani detailed design wa mradi huu anatarajiwa kupatikana katika robo ya kwanza ya mwaka 2021/2022 mradi huu utanufaisha Miji ya Vwawa, Mlowo na Tunduma katika Mkoa wa Songwe.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha za kuendeleza Mradi wa Maji wa Lukululu ili kumaliza tatizo la maji katika vijiji 14 vya Jimbo la Vwawa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -
Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, Mradi wa Maji wa Lukululu unatekelezwa kwa awamu ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 Serikali imetenga shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya kujenga miradi ya maji katika vijiji vitano kati ya 15 vya Mradi wa Maji Lukululu ambavyo ni Myovizi, Mbewe, Mahenje, Mlangali na Ndolezi. Kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa matanki manne ambapo kwa pamoja yatahifadhi maji lita 450,000 na mtandao wa mabomba wa urefu wa kilomita 58.3. Kazi hii itaanza kutekelezwa mwezi Desemba, 2021.
Mheshimiwa Spika, awamu ya pili itahusisha Vijiji 10 ambavyo ni Mbulu, Ivugula, Igunda, Ichesa, Shaji, Shomola, Shidunda, Ilea, Mbwewe na Lukululu. Kazi ya usanifu imepangwa kukamilika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2021/2022 na matarajio ni kupatikana Mkandarasi na utekelezaji utaanza Julai, 2022.
Mheshimiwa Spika, jitihada hizi za Serikali zinalenga kuboresha huduma ya upatikanaji majisafi na salama Wilayani Mbozi.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mahenje - Ndolezi - Hasamba hadi Vwawa ambayo ni muhimu kwa utalii wa Kimondo cha Mbozi na usafirishaji wa mazao?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ninapenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Songwe inajenga kwa kiwango cha lami barabara hii kwa awamu. Hadi mwishoni mwa Machi, 2022 Kilometa 4.5 zimekamilika kujengwa kuanzia Mji wa Vwawa hadi Kijiji cha Mtambwe katika hospitali ya Mkoa wa Songwe. Aidha, ujenzi unaendelea kwa sehemu ya mita 800 na inatarajiwa ifikapo mwishoni mwa Mwezi Juni, 2022 ujenzi utakuwa umekamilika.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya barabara hii iliyobaki kilomita 26.56 kwa sasa inafanyiwa upembuzi yakinifu na usanifu wa kina na kampuni ya Mhandisi Mshauri M/S Inter Consult Ltd ya Dar es Salaam. Kazi hii inatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2022. Baada ya kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina kukamilika na gharama za ujenzi kujulikana, Serikali itatafuta fedha kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami. Ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itaanza kujenga soko la mazao la Kimataifa katika eneo la Mbimba TACRI Vwawa ili Wananchi wapate soko la uhakika?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa kilimo na ninaomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi imetenga ekari 25 kwa ajili ya ujenzi wa soko ambapo eneo hilo limeshafanyiwa upembuzi yakinifu kwa kushirikiana na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Aidha, gharama za ujenzi wa soko hilo ni takribani shilingi 14,117,640,924.91. Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini barabara ya kutoka njia panda ya Iyula – Idiwili - Nyimbili hadi Ileje itajengwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) imeanza kujenga barabara ya Njiapanda ya Iyula – Idiwili – Nyimbili hadi Ileje (kilometa 79) kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Mkandarasi amepatikana kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami kilometa 2.1 kwa sehemu ya barabara ya kuanzia Njiapanda ya Iyula kuelekea Idiwili. Aidha, Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuendelea na ujenzi kwa kiwango cha lami kwa sehemu iliyobaki.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, ni lini Serikali itatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Iyula – Ipyana hadi Idunda – Vwawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, Serikali ilitenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kufanya matengenezo ya barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 10 kwa kiwango cha changarawe. Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, Serikali imechonga kipande cha barabara hiyo chenye urefu wa kilometa 3.5 kilichobakia kutoka Idunda kwenda Kitongoji cha Itete kilichopo mpakani mwa Wilaya ya Songwe na Mbeya kwa shilingi milioni 10.5.
Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuweka mipango ya matengenezo ya barabara hii kulingana na upatikanaji wa fedha.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatenga fedha na kuanza ujenzi wa Mahakama ya Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria naomba sasa nijibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ujenzi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Songwe ulianza katika mwaka wa fedha 2021/2022, na jengo hilo lilijengwa eneo la Vwawa Wilayani Mbozi na lilikamilika Julai, 2022. Aidha, Jengo lilianza kutumika Agosti, 2022 na kuzinduliwa rasmi na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwezi Novemba, 2022 ambapo alizindua kwa pamoja na majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi katika Mikoa ya Lindi na Katavi, ahsante.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA katika Makao Makuu ya Mkoa wa Songwe?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu: -
Mheshimwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda sasa kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ipo mbioni kuanza utekelezaji wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma cha Mkoa wa Songwe ambapo tayari eneo lenye ukubwa wa ekari 50 limetengwa. Chuo hicho kinatarajiwa kujengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 2.99 kupitia mapato ya ndani ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA). Ujenzi huo unatarajiwa kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2022/2023. Nakushukuru sana.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Je, lini Serikali itatoa fedha kumalizia ujenzi wa maboma ya shule za msingi na sekondari yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi Mbozi?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Jimbo la Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Serikali ina utaratibu wa kukusanya takwimu za maboma yaliyojengwa na wananchi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuweka mkakati na mpango wa ukamilishaji.
Mheshimiwa Spika, ni kweli Halmashauri ya Mbozi ina maboma mengi ya madarasa yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi. Mwaka 2020/2021 kulikuwa na maboma 1,529 yakiwepo madarasa ya shule za msingi 1,513 na sekondari 86. Yaliyopo kwa sasa baada ya Serikali kwa kushirikiana na Wadau na wananchi kuyakamilisha ni ya shule za msingi 1,386 na sekondari 76 ambayo kati ya hayo 64 yamepauliwa. Aidha, maboma yaliyotengewa bajeti kwa kipindi cha 2023/2024 ni 18. Serikali kwa kushirikiana na wadau imeendelea kuyapunguza kadri inavyopata fedha.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Chuo cha Afya Vwawa utaanza mwezi Oktoba, 2024 na Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 2.9 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia fedha za Mradi wa Mama na Mtoto, kwa ajili ya kujenga jengo la mafunzo mseto (academic complex). Aidha, tayari utaratibu wa kupata eneo umefanyika na kiasi cha shilingi milioni 151 kimetumika kwa ajili ya kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi waliopisha eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza:-
Je, Serikali ina mkakati gani wa kupeleka walimu wa kutosha katika shule mpya kumi za msingi na sekondari zilizojengwa Vwawa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari, 2024 Serikali imepeleka jumla ya walimu 33 wa shule za msingi na walimu 32 wa shule za sekondari katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi kwa ajili ya shule mpya. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuajiri na kuwapangia vituo walimu mara baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais, Utumishi kukamilika ili kuboresha ikama katika shule za msingi na sekondari.
MHE. JAPHET N. HASUNGA aliuliza: -
Je, lini Serikali itajenga Chuo cha Afya Vwawa?
WAZIRI WA AFYA alijibu: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga, Mbunge wa Vwawa, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Chuo cha Afya Vwawa utaanza mwezi Oktoba, 2024 na Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 2.9 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kupitia fedha za Mradi wa Mama na Mtoto, kwa ajili ya kujenga jengo la mafunzo mseto (academic complex). Aidha, tayari utaratibu wa kupata eneo umefanyika na kiasi cha shilingi milioni 151 kimetumika kwa ajili ya kulipa fidia ya ardhi kwa wananchi waliopisha eneo hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.