Primary Questions from Hon. Abdulaziz Mohamed Abood (6 total)
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ina tatizo kubwa la msongamano katika wodi ya akina mama ambao wamekuwa wakilala zaidi ya wawili kwenye kitanda kimoja;
(a) Je, ni lini Serikali itaongeza wodi ya wazazi katika hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Morogoro?
(b) Je, kwa nini Serikali isiboreshe baadhi ya zahanati kama Mafiga Sabasaba ili kuwa na uwezo wa kupokea kina mama wajawazito kujifungua na kupunguza msongamano katika hospitali ya rufaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Azizi Abood Mbunge wa Morogoro Mjini lenye sehemu a na b kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, msongamano wa wagonjwa katika wodi ya wazazi ya hospitali ya Mkoa unatokana na kukosekana kwa hospitali ya Wilaya ya Morogoro. Ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali imepanga kuanza ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Morogoro katika bajeti ya mwaka 2016/2017. Fedha zilizotengwa ni shilingi bilioni 2.5 ili kuanza ujenzi wa jengo la utawala na jengo la wagonjwa wa nje (OPD).
Mheshimiwa Naibu Spika, mpango wa Serikali ni kuimarisha kituo cha afya cha Mafiga ambacho tayari kimeanza kutoa huduma za mama wajawazito. Katika mwaka wa fedha 2015/2016 Halmashauri imepanga kutumia shilingi milioni 100 kwa ajili ya kujenga jengo la upasuaji na wodi. Vilevile, zimetengwa shilingi milioni 71 katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017 kwa ajili ya upanuzi wa wodi ya wazazi katika zahanati ya kihonda. Hivyo, mpango wa Serikali ni kuimarisha huduma za wazazi katika zahanati na vituo vya afya ili kupunguza msongamano katika hospitali ya rufaa ya Morogoro.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Morogoro Mjini bado ina kero ya maji katika maeneo mbalimbali ya Manispaa kama vile Kata ya Tungi, Mkundi, Kiegea A na B, Kihonda, Kisanga na Ngerengere:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kuondoa kero hii ya maji katika Manispaa ya Morogoro?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Azizi Abood Mbunge wa Morogoro Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) inaendelea kutatua kero ya maji iliyoko katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro. Katika mpango wa muda mfupi wa kuboresha huduma ya maji, kazi zilizopangwa ni upanuzi wa mtandao wa bomba katika maeneo yasiyo na mtandao, ufungaji wa mita za maji, ubadilishaji wa bomba chakavu na uzibaji wa mivujo ya maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imepanga kufunga pampu eneo la mizani na bomba kuu la kupandisha maji kwenye tanki lililopo Kilima cha Kilimanjaro ambalo litahudumia eneo la Kiegea A na B na Kata ya Mkundi. Aidha, eneo la Kasanga, Kata ya Mindu kuna mradi mpya unaojengwa na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro ambao ukikamilika utaondoa kero ya maji kwa wakazi wa Kasanga.
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mpango wa muda mrefu, Serikali imeanza kutekeleza awamu ya pili ya mradi wa maji, ambapo hatua za kumpata mtaalam mshauri atakayepitia usanifu wa vitabu vya zabuni inaendelea. Ujenzi utaanza mara baada ya kukamilika kwa mapitio hayo. Kukamilika kwa ujenzi wa mradi kutamaliza kero ya maji kwa kiasi kikubwa na kukidhi mahitaji hadi itakapofika mwaka 2025.
Mheshimiwa Naibu Spika, fedha za kutekeleza mradi zitachangiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na Serikali ya Ufaransa kupitia Benki ya Maendeleo ya Ufaransa EFD ambao wameahidi kuchangia Euro milioni 40. Utekelezaji wa mradi huu unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Maeneo mengi katika Jimbo la Morogoro Mjini bado hawajapata nishati ya umeme kama vile Kata za Mindu, Lugala, Mkundi, Kiegea A na B, Kihonda, Mafisa, Tungi, Kingolwira na Kauzeni A.
Je, ni lini Serikali itamaliza tatizo hili la muda mrefu?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati na Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Aziz Abood, Mbunge wa Morogoro Mjini, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Shirika la Umeme (TANESCO) inatekeleza miradi ya kufikisha miundombinu ya umeme maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Morogoro Mjini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi unaoendelea katika Kata za Mindu, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 8.973, ujenzi wa njia ya umeme msongo wa kilovoti nne yenye urefu wa kilometa 35.4, lakini ufungaji wa transfoma saba pamoja na kuwaunganishia umeme wateja 834.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu utafikisha umeme kwenye maeneo ya Mindu, Kasanga na Madanganya ambapo ni transfoma nne zimefungwa tayari na baadhi ya wananchi pia wameshaunganishiwa umeme. Gharama za mradi ni shilingi bilioni 1.113. Unajumuisha Mindu -Lugala ambao unajumuisha ujenzi wa msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilometa 8.9, ujenzi wa njia ya umeme wa msongo wa voti 400 yenye urefu wa kilometa 10.7 na ufungaji wa transfoma tatu. Hali kadhalika utaunganishwa umeme kwa wateja 206. Gharama za mradi huu ni milioni 106.784. Utekelezaji wa miradi hii utakamilika mwezi Juni mwaka huu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yaliyobaki katika Mji wa Morogoro yataendelea kupatiwa umeme kupitia bajeti ya TANESCO zinazopangwa mwaka hadi mwaka.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Serikali imeahidi mradi wa maji ambao utamaliza kero ya maji katika Jimbo la Morogoro Mjini hasa maeneo ya Kihonda, Tungi, Lukobe, Mkundi katika Kata ya Mindu.
(a) Je, ni lini mradi huo wa maji utaanza ili kuondoa kero za maji katika Jimbo la Morogoro Mjini?
(b) Je, mradi huo utagharimu fedha kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul- Aziz Mohamed Abood, Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imeandaa mipango madhubuti katika kuhakikisha inaboresha huduma ya maji kwa wakazi wanaoishi katika Manispaa ya Morogoro. Katika kufikia lengo hilo, Wizara inatekeleza mipango ya muda mfupi na muda mrefu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa muda mfupi, katika mwaka wa fedha 2017/2018, Serikali ilitenga jumla ya shilingi bilioni 2.5 kwa ajili ya mradi wa kuboresha huduma ya maji kwa maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Morogoro. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na ujenzi wa mtandao wa usambazaji maji wenye urefu wa kilometa 41.9 na kituo cha kusukuma maji eneo la Mizani. Kukamilika kwa mradi huo kutawanufaisha wakazi wapatao 17,000 wanaoishi maeneo ya Kihonda, Kilimanjaro, Mkundi, Yespa, Kiyegea na Kihonda Kaskazini. Mradi huo unatarajiwa kukamilika mwezi Juni, 2018.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa kupitia Shirika lake la Maendeleo la AFD itatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya majisafi katika Manispaa ya Morogoro. Kazi zinazotekelezwa katika mradi huo ni pamoja na kuongeza kina cha bwawa la Mindu, ujenzi wa mtambo wa kusafisha maji, ujenzi wa bomba kuu la maji kutoka Tumbaku hadi Kingolwira, upanuzi wa mtandao wa kusambaza maji, ukarabati wa miundombinu ya majisafi na ukarabati wa mabwawa ya majitaka. Gharama ya utekelezaji wa mradi huo ni Euro milioni 70. Aidha, kwa sasa Serikali inaendelea na taratibu za kusaini mkataba wa kifedha.
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD aliuliza:-
Kuna mgogoro wa ardhi kati ya Jeshi la Wananchi kwenye mipaka katika Kata ya Kauzeni na Luhongo ambapo wananchi wanashindwa kufanya shughuli zao za maendeleo hasa kilimo, Jeshi linaweka mipaka na kuingiza ndani ya mashamba ya wananchi wakati miaka yote maeneo hayo yalikuwa nje ya mipaka ya Jeshi:-
• Je, ni lini Serikali itawarudishia wananchi maeneo yao ya kilimo?
• Je, kwa nini Serikali isichukue hatua kwa kuruhusu wananchi wamiliki maeneo hayo ambayo ni ya asili na Jeshi limewakuta wananchi katika eneo hilo?
WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Aziz Mohamed Abood, Mbunge wa Morogoro Mjini, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ufumbuzi wa mgogoro wa mipaka ulishafanyika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro. Hivyo, kimsingi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania halina mgogoro na wananchi kwenye mipaka ya Kata za Kauzeni na Luhongo hasa baada ya upimaji mpya wa mwaka 2002 ambapo uliacha nje maeneo ya vijiji. Manung’uniko yaliyopo yanatokana na uamuzi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kusitisha utaratibu wa kuwaruhusu kwa muda baadhi ya wananchi kulima mashamba ndani ya mipaka yake kwa sababu za kiulinzi na kiusalama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo yanayomilikiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania yapo kwa ajili ya ulinzi wa nchi na sehemu hizo zipo kimkakati kwa ajili ya usalama wa nchi. Serikali imetumia rasilimali nyingi za wananchi wa Tanzania kujenga miundombinu iliyopo kwenye eneo hilo. Hivyo, haitokuwa vema kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kuondoka katika maeneo yaliyochaguliwa kistratejia kwa ajili ya ulinzi. Ni vema wananchi waelimishwe juu ya jambo hili na nimwombe Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na wadau mbalimbali katika Halmashauri ya Mkoa kutoa elimu kwa wananchi. (Makofi)
MHE. ABDUL-AZIZ M. ABOOD Aliuliza:- Serikali iliahidi kuleta mradi wa maji katika Jimbo la Morogoro Mjini ambao utamaliza kero ya maji katika maeneo mbalimbali ikiwemo Kihonda, Tungi, Lukombe na Mkundi katika Kata ya Mindu.
(a) Je, ni lini mradi huo utaanza?
(b) Je, mradi huo unategemewa kugharimu kiasi gani?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI Alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul-Aziz Mohamed Abood, Mbunge wa Morogoro Mjini lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Serikali iliahidi kutekeleza miradi mbalimbali kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji katika Jimbo la Morogoro Mijini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza ahadi hiyo, Serikali kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Morogoro (MORUWASA) imeandaa mipango ya muda mfupi na mrefu. Katika mipango ya muda mfupi katika mwaka wa fedha 2018/2019, Serikali imetekeleza mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji katika Kata za Kihonda na Mkundi. Mradi huo umegharimu kiasi cha shilinigi bilioni 1.9 na umewanufaisha wakazi wapatao 17,000 wanaoishi maeneo ya Kihonda, Kilimanjaro, Kiyegea na Kihonda Kaskazini.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mpango wa muda mrefu, Serikali kwa kushirikiana na Serikali ya Ufaransa kupita Shirika lake la Maendeleo la AFD itatekeleza mradi wa kuboresha huduma ya maji safi katika Manispaa ya Morogoro. Kazi zitakazotekelezwa ni kuongeza kina cha Bwawa la Mindu, ujenzi wa mtambo wenye uwezo wa kusafisha na kutibu maji, upanuzi wa matandao wa kusambazi maji, ukarabati wa mabwawa ya majitaka. Gharama ya mradi huo ni Euro milioni 70. Taratibu zakusaini mkataba wa kifedha zinaendelea na zitakapokamika utekelezaji wa mradi utaanza.