Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu (18 total)

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU aliuliza:-
Walimu wamekuwa wakiidai Serikali stahiki zao mbalimbali na tatizo hili la kutowalipa kwa muda muafaka limekuwa likijirudia rudia:-
(a) Je, walimu wanadai stahiki zipi na kwa kiasi gani?
(b) Je, Serikali imejipangaje kutatua tatizo hilo na kulimaliza kabisa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, madai ya walimu yasiyo ya mishahara ni shilingi bilioni 26 hadi kufikia Desemba, 2016. Deni hili limeshahakikiwa na kuwasilishwa hazina kwa taratibu za mwisho ili liweze kulipwa.
Aidha, madeni yanayotokana na mishahara ni shilingi bilioni 18.1. Uhakiki wa deni la shilingi bilioni 10 umekamilika na linasubiri kulipwa kupitia akaunti ya mtumishi anayedai. Deni linalobaki la shilingi bilioni 8.06 linaendelea kuhakikiwa ili liweze kulipwa.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kudhibiti uzalishaji wa madeni, mamlaka za Serikali za Mitaa zimetakiwa kutohamisha walimu endapo hakuna bajeti iliyotengwa. Vilevile Serikali imeondoa kipengele kinachohitaji mwalimu akubali cheo chake kwanza ili aweze kulipwa mshahara wake mpya baada ya kupandishwa daraja jambo ambalo lilisababisha malimbikizo makubwa ya mishahara. Aidha, Serikali imeweka utaratibu wa kukusanya madeni katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili yaweze kupatikana, kuhakikiwa na kulipwa kwa walimu wanaoidai kwa wakati.
MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE (K.n.y. MHE. BERNADETA K. MUSHASHU) aliuliza:-
Wazabuni wanaotoa huduma shuleni wanaidai Serikali fedha nyingi kwa huduma walizotoa miaka iliyopita.
(a) Je, Serikali inadaiwa fedha kiasi gani na kwa miaka ipi na wazabuni hao?
(b) Je, ni lini madai hayo yatalipwa?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (TAMISEMI), naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kuwa wapo wazabuni mbalimbali ambao wanaidai Serikali baada ya kutoa huduma Serikalini. Wapo wazabuni waliotoa huduma za vyakula katika shule zenye wanafunzi wenye mahitaji maalum za msingi na shule za bweni za sekondari na wazabuni waliochapisha na kusambaza vitabu shuleni. Kiasi cha shilingi bilioni 54.86 zinadaiwa na wazabuni waliotoa huduma ya chakula, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 9.907 ni za wazabuni waliotoa huduma ya uchapishaji na usambazaji wa vitabu vya shule za msingi. Hivyo jumla ya deni ni shilingi bilioni 64.767.
(b) Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kuwa madeni haya ni yale yaliyojitokeza kabla ya Serikali kuanza kutekeleza elimu msingi bila malipo. Kwa kutambua umuhimu wa kuwalipa wazabuni hawa Serikali kupitia Wizara ya Fedha imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 13.239 hadi kufikia Mei, 2016. Wazabuni wengi ambao madeni yao hayajalipwa hadi sasa wataendelea kulipwa kwa awamu kwa kadri ya uwezo wa Serikali na upatikanaji wa fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaomba wazabuni hawa wawe na uvumilivu kama ambavyo wamekuwa wakifanya wakati Serikali ikiendelea kulipa madeni haya ikiwa ni pamoja na madeni mengine ya ndani.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU aliuliza:-

Kahawa ni zao la biashara na la kimkakati ingawa kwa miaka kadhaa bei ya zao hilo imeendelea kuwa chini:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuinua zao hilo Mkoani Kagera ikiwemo kupandisha bei ili kumnufaisha mkulima?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benardetha Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, zao la kahawa ni miongoni mwa mazao ya kimkakati ambalo Serikali imeamua kuboresha mazingira ya uzalishaji pamoja na masoko ili kumnufaisha mkulima. Ili kufikia lengo hilo, Serikali imeimarisha usimamizi katika uzalishaji na kuboresha mifumo ya masoko. Bei ya mazao ya kilimo ikiwemo kahawa inategemea nguvu ya soko kwa kuzingatia mahitaji na ugavi wa uzalishaji duniani. Aidha, Serikali kupitia Bodi ya Kahawa imeruhusu na kuratibu uuzwaji wa kahawa moja kwa moja yaani direct export kwenye masoko ya Kimataifa yenye bei nzuri kuliko mnadani kwa kufuata Sheria na Kanuni zilizopo kwa kahawa maalum yaani Kahawa ya Haki yaani fair and organic coffee na kahawa zingine zenye mahitaji na masoko maalum.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika kuboresha mazingira ya biashara ya zao la kahawa, Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwa ni pomoja na kuamua kuanzisha minada ya kahawa kwenye maeneo ya uzalishaji kuanzia msimu wa mwaka 2019/2020. Lengo la utaratibu huo ni kuharakisha malipo na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa minada na kuwashirikisha wakulima wengi zaidi katika mikoa inayozalisha zao la kahawa ukiwemo Mkoa wa Kagera.

Mheshimiwa naibu Spika, Serikali pia imedhibiti makato yasiyo na tija kwa wakulima na yanayokatwa kwenye Vyama Vikuu vya Ushirika na Vyama vya Msingi ili kubaki na makato yanayolenga kuendeleza zao la kahawa. Aidha, kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB), Serikali imewezesha Vyama vya Ushirika vya Kahawa vikiwemo Vyama vya Mkoa wa Kagera kupata mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya kufanikisha shughuli za ukusanyaji na uuzaji wa kahawa ya wakulima, hivyo kumpunguzia mkulima mzigo wa riba uliokuwa unatozwa na mabenki ya kibiashara kwani TADB inatoza riba ya kiwango cha asilimia nane ukilinganisha na benki za kibiashara zilizokuwa zinatoza na zinazotoza riba ya asilimia 18 hadi 22.

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na mikakati hiyo, Serikali imefuta tozo na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinatozwa kwa wakulima ikiwemo pamoja na kupunguza tozo zinazotozwa katika biashara ya kahawa pamoja na kupunguza viwango vya makato mbalimbali vilivyokuwa vinakusanywa kwa mkulima. Aidha, Serikali pia imepunguza kiwango cha ushguru wa mazao unaotozwa na mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka asilimia tano hadi asilimia tatu ya bei ya kahawa ya shambani. Kwa kufanya hivyo, wakulima wa kahawa Mkoani Kagera na mikoa mingine watapata bei nzuri na hivyo kuongeza mapato yao na kuinua uchumi wa Taifa letu.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU aliuliza:-

Miundombinu ya Shule ya Sekondari Rugambwa ilijengwa mwaka 1964 na Sekondari ya Bukoba imejengwa mwaka 1939, hivyo imechakaa sana:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuzifanyia ukarabati shule hizo?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuongeza fursa na kuhakikisha kuwa elimu inayotolewa ni bora, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule na vyuo nchini. Hii ni pamoja na utekelezaji wa mpango wa ukarabati wa shule zote kongwe 88 na sekondari nchini ambapo hadi sasa shule 48 zipo katika hatua mbalimbali za ukarabati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule ya Sekondari ya Bukoba ni moja kati ya shule zinazoendelea na ukarabati ambapo tayari kiasi cha Sh.1,481,701,194 kimetolewa. Aidha, Shule ya Sekondari Rugambwa ipo katika mpango wa ukarabati awamu ya pili ambao utafanyika katika mwaka huu unaoisha 2018/2019. Tathmini ya kupata gharama halisi za ukarabati (conditional survey) ilishafanyika chini ya usimamizi wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, hivyo ukarabati unatarajiwa kuanza tarehe 15 Aprili, 2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya kufundisha na kujifunzia katika shule na vyuo nchini kadiri uwezo wa kifedha utakavyoruhusu.
MHE. HALIMA A. BULEMBO (K.n.y. MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU) aliuliza:-

Mkoa wa Kagera una vijiji 134 ambavyo havijafikiwa na umeme wa REA; Biharamulo Vijiji 29, Bukoba Vijiji 9, Karagwe Vijiiji 8, Kyerwa Vijiji 31, Misenyi Vijiji 5, Muleba Vijiji 25 na Ngara Vijiji 27:-

(a) Je, ni lini Serikali itapeleka umeme wa REA katika Vijiji hivyo?

(b) Umeme wa REA ulifika kwenye vijiji vingi lakini haukusambazwa: Je, mradi wa ujazilizi utaanza lini Mkoani Kagera ili wananchi waliorukwa wapatiwe umeme?
WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu lililoulizwa na Mheshimiwa Halima Bulembo, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi kabambe wa kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini kufikia mwezi Desemba, 2021. Kwa sasa Mkandarasi Nakuroi anaendelea na kazi ambapo kufikia mwezi Oktoba, 2019 vijiji 82 vimewashwa umeme katika Mkoa wa Kagera na kazi ya uunganishaji wa wateja inaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote vitakavyosalia katika Mkoa wa Kagera vitapatiwa umeme kupitia mradi wa REA awamu ya pili, unaozunguka kuanza sasa ambao utakamilika mwezi Januari, 2020. Pia kukamilika kwa mradi huu mwezi Desemba, 2021 kutapeleka umeme katika maeneo yote katika Mkoa wa Kagera pamoja na Vitongoji vyake.

(b) Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa ujazilizi awamu ya pili (Densification IIA) utatekelezwa katika Mikoa tisa na utaanza kutekelezwa kuanzia mwezi Novemba, 2019 hadi mwezi Juni, 2020. Mradi wa ujazilizi katika Mkoa wa Kagera utaanza kutekelezwa kupitia mradi wa ujazilizi awamu ya IIB (Densification IIB) utakaoanza kutekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2020 na kukamilika mwezi Machi, 2021. (Makofi)
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU aliuliza:-

Mafuriko yanayotokea katika Mji wa Bukoba husababisha uharibifu mkubwa wa chakula, mali, barabara na hata kusababisha vifo kwa watu na mifugo; mafuriko hayo husababishwa na Mto Kanoni kujaa mchanga na takataka:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwaondolea kero ya mafuriko kila mwaka ikiwemo kusafisha na kuongeza kina cha Mto Kanoni?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, chanzo cha uchafuzi wa Mto Kanoni unaosababisha mto huo kujaa mchanga na taka ngumu zinazopelekea wakati wa masika maji kujaa na kuleta athari za mafuriko kwenye makazi ya watu, ni kuwepo kwa shughuli za kibinadamu pembezoni na ndani ya mto zikiwemo; ujenzi wa nyumba, ujenzi wa karo za maji taka, kilimo (mashamba), ujenzi na utumiaji wa mazizi na vyoo, ufuaji, uogaji na uoshaji wa magari na kadhalika.

Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Manispaa ya Mji wa Bukoba imeanza kuchukua hatua za muda mfupi kwa kupiga marufuku na kuondoa shughuli zote za kibinadamu zinazofanyika ndani ya mto kama zilivyobainishwa hapo juu, pamoja na kuhakikisha eneo la hifadhi ya mto kisheria, linasafishwa.

Aidha, hatua nyingine ambazo Halmashauri inaendelea kuchukua ni pamoja na kuondoa miti yote isiyokuwa rafiki wa mazingira iliyokuwa imepandwa ndani ya Mto Kanoni na kupanda miti rafiki wa mazingira, kufuatilia ubora wa maji ya mto na kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira kupitia redio, mikutano ya hadhara, semina na makongamano. Halmashauri ya Manispaa ya Mji wa Bukoba inaendelea kuwahamasisha wananchi kujitolea kupanda miti ili kuhifadhi kingo za mto na uondoaji wa mchanga unaosababisha kupungua kwa kina cha mto kunakosababisha mafuriko wakati wa masika.
MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU Aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga Chuo Kikuu katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA Alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benardetha Kasabago Mushashu Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kutokana na gharama kubwa za uwekezaji unaohitajika katika kuanzisha Vyuo Vikuu, ni vigumu kwa Serikali kuanzisha Chuo Kikuu katika kila Mkoa. Vyuo Vikuu vya Serikali na Binafsi vilivyopo nchini vinapokea wanafunzi kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani na vilevile kutoka nje ya nchi ambapo ndiyo utamaduni wa Vyuo Vikuu Duniani.

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wa Kagera kuna tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kilichopo katika Makao Makuu ya Mkoa ambacho ni cha Serikali. Kwa sasa Serikali inaendelea na mpango wa kuboresha Vyuo Vikuu na Taasisi za Elimu ya Juu zilizopo kwa kukarabati na kujenga miundombinu mipya pamoja na kuongeza vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza nafasi ya udahili na kuongeza ubora wa elimu ya juu itolewayo ili kukidhi mahitaji ya nchi. Ahsante.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, ni lini wananchi waliokuwa wameweka fedha zao katika Benki ya Wakulima wa Kagera ya KFCB iliyofungwa na Benki Kuu Mwaka 2018 watarejeshewa fedha zao?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnamo tarehe 4 Januari, 2018, Benki Kuu ya Tanzania iliifutia leseni ya kufanya biashara, Benki ya Wakulima wa Mkoa wa Kagera (Kagera Farmers’ Cooperative Bank Limited) kwa mujibu wa Sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka, 2006.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuifutia leseni benki hiyo, Benki Kuu ya Tanzania iliiteua Bodi ya Bima ya Amana (Deposit Insurance Board – DIB) kuwa mfilisi wa Benki hiyo kwa mujibu wa sheria. Ambapo kuanzia mwezi Machi, 2018 ilianza zoezi la kulipa fidia ya Bima ya Amana ya kiasi cha hadi shilingi 1,500,000 (Pay-out of insured deposits), kwa wateja waliostahili kulipwa Bima ya Amana. Zoezi hilo bado linaendelea kwa wateja ambao hawajajitokeza kuchukua fidia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sanjari na zoezi hilo la kulipa fidia kwa wateja ambao hawajajitokeza, Bodi ya Bima ya Amana inaendelea na zoezi la ufilisi wa Benki hiyo kwa kukusanya mali na madeni ya Benki hiyo ili kupata fedha za kuwalipa wateja waliokuwa na amana zao katika benki hiyo, isiyozidi shilingi 1,500,000/=, ambapo kwa mujibu wa sheria na taratibu za ufilisi kiasi kitakacholipwa kitategemea, fedha zilizopatikana kutokana na kuuza mali za benki hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba, 2021 jumla ya Sh.737,137,082.44 zimeshalipwa kwa wateja 1,389 waliokuwa na amana kwenye Benki ya Wakulima wa Mkoa wa Kagera - KFCB kati ya wateja 7,096 wanaostahiki kulipwa fidia hiyo. Malipo hayo ni sawa na asilimia 90.25 ya kiasi cha Sh.816,801,700.15 zilizotengwa kwa ajili ya kulipa fidia. Ahsante.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, Serikali ina mkakati gani wa kukomesha ukatili wa kijinsia nchini?
NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WANAWAKE NA MAKUNDI MAALUM alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago Mushashu, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatekeleza Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia unaozingatia kuimarisha uchumi wa kaya, kutokomeza mila na desturi zinachochea ukatili, kuimarisha malezi na makuzi na kusimamia sheria na kuwezesha huduma kwa waathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kamati za Ulinzi wa Wanawake na Watoto zimeundwa kuanzia ngazi ya Taifa hadi Kijiji. Zinafanya kazi zake katika Halmashauri kuhusu kutokomeza ukatili. Vituo vya Jeshi la Polisi, Magereza na Madawati ya Jinsia, Vyuo na Sehemu za Umma wanaunda madawati ya jinsia, Shule za Msingi na Sekondari zinaunda Madawati ya Ulinzi wa Watoto. Vilevile, Kampeni za kupinga ukatili zinaendelea sambamba na hatua za kuboresha sheria mbalimbali, ahsante.
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, ni vijiji vingapi havijapatiwa umeme wa REA na nini mpango wa Serikali kusambaza umeme kwenye vijiji vyote vya Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera una vijiji 662, ambapo kati ya hivyo, vijiji 139 havijafikiwa na miundombinu ya umeme. Vijiji vyote 139 vilivyobaki vitapatiwa umeme kupitia utekelezaji wa Mradi wa Umeme Vijijini Awamu ya Tatu – Mzunguko wa Pili unaoendelea. Mkandarasi ambaye ni Joint Venture wa kampuni za M/S JV Pomy Engineering Company Limited na Qwihaya General Enterprises Company Limited ndiyo wanaotekeleza mradi huo kwa Mkoa wa Kagera. Gharama ya mradi ni Shilingi Bilioni 34.078.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi za mradi zinahusisha ujenzi wa kilomita 812 za njia za umeme msongo wa kilovoti 33, ufungaji wa mashine umba 176, ujenzi wa kilomita 139 ya miundombinu ya usambazaji ya msongo wa voti 400 na uunganishaji wa wateja wa awali wapatao 3,058. Utekelezaji wa mradi umeshaanza kwa mkandarasi kukamilisha upimaji na usanifu wa kina na kuanza uagizaji wa vifaa vya utekelezaji. Mradi unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba, 2022.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itatafuta soko la uhakika la zao la vanilla?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi inatekeleza mikakati mbalimbali ili kuhakikisha wakulima, wakiwemo wa zao la vanilla, wanapata soko la uhakika. Mikakati hiyo ni pamoja na kuhamasisha kilimo cha kibiashara kinachozingatia mahitaji ya soko, kushiriki makongamano na maonesho ya kibiashara na uwekezaji, ujenzi wa miundombinu ya masoko na kuimarisha mifumo ya kielektroniki ambayo itasaidia upatikanaji wa taarifa za masoko.

Mheshimiwa Spika, Serikali inahamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uongezaji thamani wa zao la vanilla ili kupanua wigo wa soko la zao hilo. Aidha, wakulima wa vanilla wanahimizwa kuvuna vanila zilizokomaa ili kukidhi mahitaji ya soko hususani vanillin isiyopungua asilimia 1.8 na unyevu wa wastani wa asilimia 25 hadi 30.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, lini Serikali itajenga hospitali kubwa katika Mkoa wa Kagera?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kagera una Hospitali kubwa ya Mkoa ambapo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali imekamilisha jengo la huduma za dharura (EMD) ambalo limegharimu shilingi 560,000,000, jengo la uangalizi (ICU) lililogharimu shilingi 650,000,000, jengo la huduma za mionzi (Radiology) lililogharimu shilingi 237,000,000, nyumba ya mtumishi iliyogharimu shilingi 90,000,000 pamoja na ununuzi na ufungaji wa mashine ya CT-Scan ambayo imegharimu kiasi cha shilingi 1,810,000,000 na huduma zimeanza kutolewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kupeleka fedha zaidi kwa ajili ya kuboresha miundombinu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera ikizingatia pia kuboresha eneo la majanga na magonjwa ya mlipuko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka wa Fedha 2022/2023, Serikali imetenga shilingi milioni 725 kwa ajili ya kutekeleza Mpango Mkakati wa Tatu wa Kitaifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza (2021 – 2026) ambapo umeainisha mikakati mahususi ya udhibiti wa visababishi vya magonjwa yasiyoambukiza ambayo ni kuimarisha uratibu na ushirikishwaji wa sekta mtambuka; Kuimarisha miundombinu ya utoaji wa huduma; Kuwajengea uwezo watumishi katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza; Kuimarisha na kusimamia shughuli za utafiti; pamoja na kuhamasisha wananchi kuhusu njia za kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza. Njia hizi ni kufanya mazoezi, pamoja na kuzingatia kanuni bora za lishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, Serikali ina mpango gani wa kutokomeza kabisa ugonjwa wa Malaria nchini?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Afya, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadeta Kasabago, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali inatekeleza afua kuu zifuatazo katika kutokomeza ugonjwa wa Malaria: -

(i) Udhibiti wa mbu waenezao Malaria kupitia njia kuu zifuatazo:-

(a) Kusambaza vyandarua vyenye dawa kwa jamii kupitia kampeni za kugawa vyandarua kwa kila kaya; kliniki za mama wajawazito, watoto na vituo vya kutolea huduma kwa makundi maalum kama wazee.

(b) Upuliziaji wa dawa ukoko kwenye kuta ndani ya nyumba katika maeneo yenye kiwango kikubwa cha maambukizi ya malaria.

(c) Unyunyiziaji wa viuadudu vya kibaiolojia kwenye mazalia ili kuuwa viluilui wa mbu.

(ii) Kuhakikisha vipimo na dawa za malaria zinapatikana wakati wote katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini. Vipimo na dawa za Malaria zinapatikana bila malipo kwenye vituo vyote vya kutolea huduma vya Serikali.

(iii) Kuhamasisha jamii kutumia njia mbalimbali za kujikinga na ugonjwa wa malaria.

Mheshimiwa Spika, ili kuharakisha kufikiwa kwa azma ya kutokomeza ugonjwa wa malaria hapa nchini, Serikali imeanzisha Baraza la Kutokomeza Malaria (End Malaria Council) lililozinduliwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu tarehe 25 Aprili, 2023. Ahsante.
MHE. BERNADETHA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itahakikisha kuwa Mto Kanoni uliopo katika Manispaa ya Bukoba unasafishwa, kina kinaongezwa na kingo za mto zinajengwa?
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MUUNGANO NA MAZINGIRA alijibu: -

Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Bernadetha Kasabago Mushashu kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Serikali tayari imeshachukua hatua muhimu za kudumu za kuondoa changamoto za Mto Kanoni uliopo katika Manispaa ya Bukoba. Kupitia Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba tayari imeibua mradi wa utunzaji wa Mto Kanoni kupitia mradi wa TACTIC unaotarajia kuanza Januari, 2023 wenye thamani ya shilingi milioni 500. Lengo la mradi ni kuondoa kero kubwa ya mafuriko ambayo hutokea kila mwaka nyakati za mvua ya masika na kuathiri zaidi ya kaya 331. Mradi huu utahusisha ujenzi wa maeneo makuu mawili ambayo ni kuongeza kina na upana wa mto; na ujenzi wa kingo za mto.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kwa sasa Serikali imeendelea kuchukua jitihada za muda mfupi ambapo Manispaa ya Bukoba kila mwaka hutenga kiasi cha shilingi milioni sita kwa ajili ya shughuli za kusafisha, kupanua na kuongeza kina cha mto kwa kuondoa tope, uchafu na miti.
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, lini Serikali itapeleka Walimu wa kutosha katika Shule za Msingi na Sekondari Mkoani Kagera?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO K.n.y. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Benardeta Kasabago Mushashu, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2022 Serikali iliajiri Walimu 9,800 na Mkoa wa Kagera ulipangiwa walimu ajira mpya 640. Kati ya hao, walimu 351 wa shule za msingi na 289 kwa shule za Sekondari. Kwa mwaka 2023 Serikali iliajiri Walimu 13,130 na Mkoa wa Kagera ulipangiwa walimu 590, kati yao, walimu 312 ni kwa shule za msingi na 278 ni kwa shule za Sekondari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua mahitaji ya Walimu katika Mkoa wa Kagera na maeneo mengine nchini. Hata hivyo serikali kila mwaka inaendelea kupunguza mahitaji ya walimu katika sekta ya elimu; na hivi karibuni Serikali itatangaza ajira za walimu baada ya taratibu za kibali kutoka Ofisi ya Rais – Utumishi kukamilika na kadiri ya upatikanaji wa fedha.
MHE. BERNADETA K. MUSHASHU aliuliza:-

Je, lini Serikali italipa madeni ya Wazabuni wanaotoa huduma za vyakula kwenye shule mbalimbali tangu Mwaka 2023 hadi 2024? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. ZAINAB A. KATIMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Spika, Serikali imekuwa ikipokea madeni mbalimbali ya wazabuni wa chakula kwa shule za msingi na sekondari za Serikali kutoka katika halmashauri zote. Madeni hayo yamekuwa yakilipwa baada ya uhakiki na kadri ya upatikanaji wa fedha. Mwaka wa Fedha 2020/2021 – 2022/2023, Serikali imelipa wazabuni wa chakula shuleni kiasi cha shilingi bilioni 26.3.

Mheshimiwa Spika, Mwaka wa Fedha 2023/2024, Ofisi ya Rais, TAMISEMI imekusanya madeni ya wazabuni wa chakula katika shule za msingi na sekondari yenye jumla ya shilingi bilioni 21.7 (shule za msingi shilingi milioni 761.8 na shule za sekondari shilingi bilioni 20.9). Madeni haya yamewasilishwa Hazina, kwa ajili ya taratibu za uhakiki na malipo. (Makofi)
MHE. BENARDETA K. MUSHASHU aliuliza: -

Je, lini Serikali itakamilisha ujenzi wa jengo la kuwatenga walioathirika na magonjwa ya mlipuko Kagera?
NAIBU WAZIRI WA AFYA alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imekamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa jengo la kuwahifadhi wahisiwa wa magonjwa ya kuambukiza lililopo katika mpaka wa Mutukula, Wilaya ya Missenyi, Mkoa wa Kagera ambalo limegharimu kiasi cha shilingi milioni 140. Kwa sasa jengo hilo limekamilika na limewekewa huduma za maji, umeme, kuwekewa vitanda na tayari limeanza kutumika kuwahifadhi wanaohisiwa kuwa na magonjwa ya kuambukiza.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2024/2025 kiasi cha shilingi milioni 80 kimetengwa kwa ajili ya maboresho ya sehemu ya nje ya jengo hilo ikiwamo kuweka sehemu yenye kivuli (lounge) kwa ajili ya wasafiri, pamoja na uwekaji wa viyoyozi na samani nyingine kwa ajili ya utoaji wa huduma.