MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba Serikali ya Tanzania imepitia Awamu Sita za uongozi; Awamu ya Kwanza ilijikita kwenye kujenga viwanda kwa ajili ya kuboresha ajira na uzalishaji, Awamu ya Tatu iliamua kubinafsisha viwanda hivi ili kuviboresha zaidi pamoja na kuongeza ajira, Awamu ya Tano ilikuja tena na Sera ya Ujenzi wa Viwanda ili kuongeza ajira pamoja na uzalishaji.
Swali langu; viwanda vilivyobinafsishwa kwenye Awamu ya Tatu vingi havifanyi kazi iliyokusudiwa, kwa mfano viwanda vya korosho Mkoa wa Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma. Nini msimamo wa Serikali wa Awamu ya Sita kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havifayi kazi iliyokusudiwa? Ahsante.
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba uchumi wa nchi yetu hutegemea nyanja nyingi ikiwemo na ujenzi wa viwanda ambavyo vina faida pana kwa Watanzania na mifano yote uliyoieleza kutoka Awamu ya Kwanza mpaka ya Tatu. Awamu ya Tatu ya Serikali yetu ililenga kutoa fursa kwa Sekta Binafsi kuhakikisha kwamba nazo zinaingia kwenye mchakato wa uchumi kwa kushika viwanda na kuviendeleza. Lakini nasikitika kwamba baadhi ya waliopewa viwanda hivyo hawakufanya vizuri sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, nini Serikali imefanya ni kuchukua viwanda vyote ambavyo havikufanya vizuri na tuliunda Tume iliyoongozwa na Msajili wa Hazina pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya mapitio viwanda vyote vile ambavyo vilibinafsishwa na havifanyi kazi ikiwemo na viwanda vya korosho. Na kwa bahati nzuri mimi ni mdau wa korosho na natambua viwanda vyetu kule vingi hata vilivyopo Mkoani Pwani na Tanga wameshindwa kuviendesha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali tulichofanya, tumechukua viwanda vyote na sasa vinafanyiwa uchambuzi na Serikali na timu iliyoongozwa na Msajili wa Hazina baadaye tupeleke kwenye Baraza la Mawaziri. Malengo yetu ni kutoa viwanda hivyo kwa watu ambao wana uwezo sasa kwa sababu Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anasisitiza pia kwamba Sekta Binafsi lazima iwe karibu na Serikali ili kuweza kupanua wigo wa uchumi kwenye nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baadaye tukipata wale ambao wana nia ya kuendesha tutawapa kwa masharti ambayo tutayaweka ili kuendeleza ule mkakati wetu wa uchumi wa viwanda hapa Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie tu mheshimiwa Mbunge kwamba viwanda hivi ambavyo havifanyi kazi tayari vimesharatibiwa na vitatolewa kwa watu ambao wenye uwezo. Kwa hiyo, niwakaribishe Watazania wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda kuwa tayari kupokea baada ya Baraza la Mawaziri kufanya maamuzi ili waweze kuviendesha viwanda hivyo kwa ufanisi mkubwa zaidi kuliko ilivyo hivi sasa, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru pia kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu.
Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imefanya juhudi kubwa sana kwa kipindi kirefu kuondoa tozo mbalimbali hasa zaidi kwenye mazao ya biashara kama vile pamba, kahawa, korosho pamoja na mazao mengine. Nia ya kuondoa tozo hizi ilikuwa ni kumletea nafuu mnunuzi ambaye naye anakwenda kumpelekea nafuu mkulima ili aweze kupata faida nzuri kwenye mazao yake ya kilimo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo siku za karibuni kumeonekana kama tozo zilikuwa zinajirudia na kusababisha kuanguka kwa bei ya mazao ya kilimo, ikiwemo ya Korosho. Ni nini, kauli ya Serikali kuhusu kufanya marejeo ya tozo mbalimbali ambazo zinaathiri bei ya Korosho? (Makofi)
WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba haya mazao yetu yote na hasa yale mazao yanayolimwa kwa ushirika kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameyataja, ni mazao ambayo miaka mingi huko nyuma kumekuwa na ongezeko la tozo mbalimbali na ikasababisha hata kuanguka kwa bei na pia kero kwa wakulima kwa kupata kipato kidogo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tulifanya mapitio kwenye mazao yote yenye bodi na yanayouzwa kwa mifumo ya ushirika na kugundua kwamba tuna makato mengi. Mazao mengine yana makato mpaka 30 au 20. Tulifanya hizo jitihada kupunguza makato hayo na kufikia kiwango cha mwisho makato sita na kuleta unafuu mkubwa kwa wanunuzi na pia kuwapa kipato cha kutosha wakulima. Hiyo inaendelea hata sasa, mazao aliyoyataja pamoja na kakao kule Kyela, sasa hivi bei imepanda juu sana baada ya kuwa tumesimamia kuondoa tozo mbalimbali.
Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali bado inaendelea na imeshatoa maagizo kwa bodi zote za mazao kufanya mapitio ya mara kwa mara ya tozo na pia mwenendo wa soko la mazao yenyewe. Lengo hapa, tunataka Serikali tuone kuwa mkulima anayelima zao hili, ambaye anatumia muda wake mwingi kulima zao hili, ananufaika kwa kupata bei nzuri. Sasa, bei nzuri ni pale ambapo tunapunguza gharama kwa wanunuzi ili gharama hiyo iweze kuhamia kwa wakulima wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato huu unaendelea na hasa usimamizi wa Vyama hivi vya Ushirika vya Msingi ambako ndiyo kunaanza kuwekwa kwa tozo, pia vyama vyake vikuu ambako nao ndio wanatoa vibali vya tozo kuhakikisha kwamba tozo hizi haziendelei. Tumeweka ukomo wa tozo muhimu kwenye zao husika kulingana na mazingira waliyonayo ili kuweza kuleta unafuu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nikuhakikishie kuwa Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wote ambao mnatoka kwenye maeneo yanayolima mazao yenye bodi na kuuzwa kwa ushirika kwamba, Serikali itaendelea kusimamia kwa ukaribu, kuhakikisha kwamba wakulima wananufaika na mazao haya kwa kuwatafutia masoko, lakini baada ya kuwa tumeuza tozo mbalimbali zisiingie bila kuwa na utaratibu. Bodi nazo tumesisitiza kufanya ufuatiliaji wa kuhakikisha kwamba hakuna tozo nyingi kwenye eneo hili ili makundi haya mawili; wanunuzi na wakulima waweze kunufaika, ahsante sana. (Makofi)