Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Primary Questions from Hon. Cecil David Mwambe (26 total)

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

(a) Je, Serikali imejipanga vipi kuhakikisha wanafunzi hawarudishwi shule kwa sababu ya michango ya mlinzi, madawati na chaki?

(b) Je, Serikali ina mpango wa kuanzisha Chuo cha Ufundi (VETA) kwenye Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza Sera ya Elimu bila malipo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imetoa Waraka wa Elimu Na. 6 wa mwaka 2015 unaofafanua majukumu ya kila mdau katika utekelezaji wa elimu msingi bila malipo.

Mheshimiwa Spika, Serikali imeanza utekelezaji wa utoaji wa elimu msingi bila malipo ambapo jumla ya shilingi bilioni 15.71 zimepelekwa katika Shule za Msingi na Sekondari za Umma kwa mwezi Disemba, 2015. Fedha hizi ni kwa ajili ya ruzuku ya uendeshaji shule, fidia ya ada kwa shule za sekondari za bweni na Kutwa na chakula kwa wanafunzi wa bweni.

Mheshimiwa Spika, Walimu Wakuu na Wakuu wa Shule wamepewa Mwongozo wa matumizi ya fedha hizo ambazo zitatumika kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, zikiwemo chaki, gharama za ulinzi, mitihani na chakula. Aidha, Serikali kupitia Halmashauri za Wilaya, Miji, Manispaa na Majiji itahakikisha inatenga fedha kila mwaka kwa ajili ya ununuzi wa madawati. Sambamba na hilo, wananchi na wadau wengine wa elimu wataendelea kusaidia kuchangia katika upatikanaji wa madawati kwa kadiri watakavyoona inafaa.

Mheshimiwa Spika, kwa maelezo hayo, napenda kulihakikishia Bunge lako Tukufu kwamba hakuna Mkuu wa Shule au Mwalimu Mkuu yeyote ambaye atamrudisha mwanafunzi nyumbani kwa kutolipa michango ya mlinzi, madawati na chaki kwa sababu, majukumu hayo ni ya Serikali. (Makofi)

Serikali ina dhamira ya kuendelea kuboresha utekelezaji wa mpango huu kadiri ya tafiti zitakavyoonesha, pamoja na maoni ya wadau mbalimbali yakiwemo ya ninyi Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, Serikali ina mpango wa kujenga Chuo cha Ufundi Stadi katika Wilaya zote zisizo na Vyuo vya Ufundi Stadi vya Serikali au visivyo vya Serikali. Wakati utafiti wa kubaini Wilaya zisizo na Chuo unafanyika, Wilaya ya Masasi ilikuwa na Vyuo viwili vya ufundi stadi kikiwemo Chuo cha Ufundi Stadi Ndanda, chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 180 na Lupaso chenye uwezo wa kudahili wanafunzi 38, vinavyomilikiwa na madhehebu ya dini. Kwa kuzingatia kigezo hicho, Jimbo la Ndanda ambalo lipo katika Wilaya ya Masasi, haipo katika mpango huu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo katika kutekeleza azma hii ya kila Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi, Serikali imeviwezesha Vyuo 25 vya Maendeleo ya Wananchi vilivyopo katika Wilaya mbalimbali ili kutoa mafunzo ya ufundi stadi kikiwemo Chuo cha Maendeleo cha Wananchi Masasi kwa kuwajengea uwezo Walimu, kuboresha miundombinu na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Utekelezaji wa utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika chuo hicho ulianza mwaka 2012/2013. Napenda kumshauri Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Jimbo la Ndanda kutumia Vyuo hivyo vilivyopo Wilayani Masasi ili kupata mafunzo ya ufundi stadi.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, Serikali ina mpango gani wa kujenga wodi ya wazazi (maternal ward) kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwa kuwa wazazi hujifungulia kwenye chumba kilichomo ndani ya jengo ambalo pia hutumika kulaza wagonjwa wa kiume na kike?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMESEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Kituo cha Afya Chiwale hakina wodi ya wazazi na hali hiyo niliishuhudia mwenyewe nilipofanya ziara kituoni hapo mnamo tarehe 9 Januari, 2016 ili kujionea hali ya utoaji wa huduma kituoni hapo. Katika bajeti ya mwaka 2015/2016, Halmashauri imetenga shilingi milioni 80 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa wodi ya wazazi katika Kituo cha Afya, Chiwale. Kati ya fedha hizo, shilingi milioni 20 zinatokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na shilingi milioni 60 ni ruzuku kutoka Serikali Kuu ambazo bado hazijapelekwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, ili kuharakisha utekelezaji wa mpango huo, Halmashauri imeshauriwa kutumia fursa ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) ili kupata mkopo utakaowezesha kujenga jengo kila maabara na wodi ya kisasa ya wazazi kutokana na ukosefu wa miundombinu hiyo muhimu katika kituo hicho.
MHE. DAVID E. SILINDE (K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE) aliuliza:-
Barabara ya Masasi – Nachingwea imekuwa na matatizo kwa muda mrefu ya kupitika kwa shida:-
Je, barabara hiyo itajengwa lini kwa kiwango cha
lami ili kufanya wananchi wa Jimbo la Ndanda waondoe imani kuwa wametengwa?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Nanganga yenye urefu wa kilometa 91 kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami. Katika mwaka wa fedha 2017/2018, mradi huu umeombewa fedha za jumla ya sh. 3,515,394,000/= kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu ya barabara ya Masasi – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 45 imekuwa ikifanyiwa matengenezo ya kawaida na matengenezo ya muda maalum kila mwaka na inapitika vizuri katika kipindi cha mwaka mzima. Serikali itaendelea kuifanyia matengenezo ya aina mbalimbali barabara hiyo ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka wakati barabara hii inaendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
MHE. CECIL DAVID MWAMBE aliuliza:-
Wananchi wa Jimbo la Ndanda hawako tayari kabisa kuona mfumo wa uuzaji korosho wa stakabadhi ghalani ukiendelea.
Je, Serikali chini ya kauli mbiu “Hapa Kazi Tu” ipo tayari kuondoa kabisa mfumo huo ambao ni kandamizi na hauendani na gharama za uzalishaji?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabla sijajibu lazima niseme kwamba kama Mheshimiwa Cecil Mwambe asingerekebisha swali ningeshangaa sana kama swali la aina hiyo lingetoka kwake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa Stakabadhi za Maghala ni utaratibu ulioanzishwa kisheria wa namna ya uuzaji wa mazao kwenye maghala kwa wakulima kukusanyia mazao yao kupitia chama chake cha misingi na mazao hayo kupelekwa katika ghala kuu ambapo ubora wa zao huhakikiwa kulingana na Sheria ya Maghala na mkulima kupewa stakabadhi ambayo hutumika kama dhamana ikiwa mkulima atahitaji mkopo wakati akisubiri mazao yake kuuzwa sokoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo huu una mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na wakulima kupata uhakika wa soko, kupanda kwa bei ya zao la korosho ambapo wakulima waliuza korosho zao kwa bei ya ushindani sokoni kwa wastani wa shilingi 2,500 kwa kilo na bei ya juu kufikia hadi shilingi 4,000 kwa kilo katika msimu huu wa 2016/2017. Aidha, mfumo huu pia umewezesha kuongezeka kwa uzalishaji wa zao la korosho ambapo uzalishaji uliongezeka kutoka tani 155,244.64 katika msimu wa 2015/2016 hadi kufikia tani 264,887.52 kwa msimu wa 2016/2017.
Mheshimiwa Mwenyekiti, faida nyingine ya mfumo huu ni kwamba wakulima wa korosho kwa sasa wanapata bei za juu kutokana na wakulima kupata bei sokoni kwa utaratibu wa kuvumbua (pride discovery).
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ajili hiyo, Serikali haiko tayari kwa sasa kuondoa mfumo wa Stakabadhi Ghalani katika uuzaji wa zao la korosho nchini kutokana na mafanikio hayo, badala yake Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha mfumo huu na kuwahamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho zenye ubora ili kujiongezea kipato chao na nchi kwa ujumla.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Bwawa la Lukuledi ambalo huhudumia Kata za Lukuledi, Mpanyani na Chikinja ni muhimu sana kwa wananchi.
Je, Serikali itafanya lini ukarabati wa bwawa hilo kwa sababu kiwango cha maji kinapungua kwa kujaa mchanga?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA) alijibu:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mwaka wa fedha 2017/2018 Serikali kupitia Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa (DDCA) inaendelea na kazi ya usanifu wa kina wa miundombinu ya Bwawa la Lukuledi lililojengwa mwaka 1954 ambalo ukarabati wake utakapokamilika litahudumia wananchi wapatao 11,544 kwenye vijiji vya Lukuledi A, Lukuledi B, Mraushi, Mkolopola, Ndomoni na Naipanya.
Mheshimiwa Naibu Spika, usanifu huo unahusisha mabwawa mengine mawili yenye uwezo wa kuhudumia wananchi 15,746. Mabwawa hayo ni Bwawa la Mihima litakalohudumia vijiji vya Mihima, Muungano na Mpanyani na Bwawa la Chingulungulu litakalohudumia vijiji vya Chingulungulu, Namatutwe na Namalembo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la usanifu huo ni kubaini gharama zitakazohitajika kukarabati mabwawa hayo matatu yenye uwezo wa kuzalisha na kusambaza huduma ya maji kwa wananchi wapatao 27,290.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, Serikali itapeleka lini gari la wagonjwa kwenye Kituo cha Afya Chiwale kwani ni zaidi ya miaka miwili sasa baada ya gari lililokuwepo kuungua moto?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya Chiwale ni moja kati ya vituo vya kutolea huduma za afya 33 vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Ni kweli gari la wagonjwa la Kituo cha Afya Chiwale lilichomwa moto na wananchi mwaka 2013, suala hili lilisababisha kituo hicho kukosa gari la wagonjwa kwa muda mrefu na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za rufaa.
Mheshimiwa Spika, hata hivyo, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imefanya jitihada za kuhakikisha huduma za dharura kwa wagonjwa wanaohitaji rufaa hazikwami kwa kutoa gari lililokuwa linatumiwa na timu ya Menejimenti ya Afya ya Halmashauri ya Wilaya ya Masasi (CHMT). Aidha, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imepewa maelekezo na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kutenga fedha kwenye bajeti kwa ajili ya kununua gari la wagonjwa ili kuwaondolea wananchi usumbufu.
MHE. TUNZA I. MALAPO (K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE) aliuliza:-
(a) Je, Serikali ina mikakati gani ya haraka kuhakikisha Vijiji vya Mumburu, Mkwera na Nanditi vinapata huduma za umeme kwani vipo karibu na nguzo kubwa za umeme?
(b) Je, Serikali itapeleka lini umeme kwenye Zahanati za Chikundi, Mbemba na Kituo cha Afya cha Chiwale?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, lenye kipengele (a) na (b), kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, nia ya Serikali ni kuvipatia umeme vijiji vyote Tanzania Bara visivyokuwa na miundombinu ya umeme ifikapo mwezi Juni, 2021. Ili kutimiza azma hiyo, Serikali imeanza kutekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza na jumla ya vijiji vitano vimeingizwa kwenye mradi huu unaotekelezwa na Mkandarasi aitwaye JV RADI Services, Njarita Contractors and Aguila Contractors. Vijiji hivyo ni Mwambao, Mji Mwema, Nanganga B, Tuungane na Nanditi. Wigo wa kazi katika eneo hilo ni ujenzi wa kilometa 7.16 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 33 na kilometa 14 za njia ya umeme wa msongo wa kilovoti 0.4/0.23, ufungaji wa transfoma saba na kuunganisha wateja wa awali 184. Gharama za kazi hizo ni shilingi milioni 683.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Vijiji vya Mumburu na Mkwera ni miongoni mwa vijiji 36 visivyokuwa na umeme kati ya vijiji 64 katika Jimbo la Ndanda vitakavyopatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, mzunguko wa pili utakaotekelezwa kuanzia mwezi Julai, 2019 hadi mwezi Juni, 2021.
(b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Zahanati ya Chikundi ina umeme tangu tarehe 25, Aprili, 2017. Aidha, Kituo cha Afya cha Chiwale kina umeme baada ya kuunganishwa wakati wa utekelezaji wa Mradi wa REA Awamu ya Pili. Vilevile Zahanati ya Mbemba itapatiwa umeme kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu mzunguko wa kwanza unaoendelea kutekelezwa. Ahsante.
MHE. PASCAL Y. HAONGA (K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE) aliuliza:-

Pembejeo za kilimo ni ghali sana, hivyo wakulima wengi hushindwa kununua na kusababisha kupata mavuno haba. Je, Serikali ipo tayari kupunguza au kuweka bei elekezi iliyo nafuu kwa mkulima ili aweze kupata pembejeo za dawa, mbolea na zana za kilimo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha pembejeo za kilimo yaani mbegu, mbolea, viwatilifu na zana za kilimo zinapatikana kwa wakati na kwa bei nafuu. Hatua hizo ni pamoja na uagizaji wa pamoja, utoaji wa ruzuku, kufuta au kupunguza tozo na kodi zinazochangia kuongezeka kwa bei ya pembejeo na kufanya tafiti katika mnyororo wa thamani wa mazao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina utaratibu wa kuweka bei elekezi ya mbolea kupitia mfumo wa ununuzi wa pamoja nchini kwa mbolea za kupandia aina ya DAP na kukuzia aina ya Urea. Utaratibu huu ulilenga kuhakikisha upatikanaji wa mbolea kwa wakati na kwa bei nafuu kwa wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika jitihada za kuongeza uzalishaji wa kipato cha mkulima, Serikali hununua na kusimamia udhibiti na usambazaji wa viuatilifu vya kupambana na milipuko ya visumbufu vya mazao na mimea kama vile kweleakwelea, viwavijeshi, viwavijeshi vamizi, panya, nzige wekundu na nzi wa matunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kumpunguzia mkulima harubu katika uzalishaji na uongezaji thamani ya mazao, Serikali imeendelea kutoa kutoa mikopo nafuu ya zana za kilimo kupitia Mfuko wa Taifa wa Pembejeo za kilimo, Benki ya Maendeleo ya Kilimo na Shirika la Maendeleo la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa mbegu na viuatilifu, Serikali inafanya utafiti wa kubaini gharama za uzalishaji wa mbegu kwa kulinganisha na bei za mbegu zilizopo sasa ambazo utaiwezesha Serikali kuamua endapo kuna ulazima wa kuweka bei elekezi katika viuatilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hatua hizo, Serikali inahamasisha ujenzi wa viwanda vya mbolea, viwatilifu, zana za kilimo na uwekezaji katika mashamba ya mbegu ili kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Mradi wa Maji wa Mto Mbwinji upo kwenye chanzo chenye maji ya kutosha, ambapo bomba la mradi linaloelekea Nachingwea limepita kwenye vijiji vyenye matatizo makubwa ya maji.

(a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha vijiji vyote vinavyopitiwa na bomba la maji vinapata huduma hiyo?

(b) Je, Serikali ipo tayari kuwahakikisha wananchi wa Ndanda kuwa zahanati na vituo vya afya vitaunganishwa na huduma hii muhimu ya upatikanaji wa maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda lenye sehemu (a) (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Mradi wa Maji Safi wa Masasi – Nachingwea licha ya kuhudumia miji ya Masasi na Nachingwea, pia unatoa huduma ya maji katika vijiji vilivyo kandokando ya mabomba makuu yatokayo kwenye chanzo cha Mbwinji kuelekea katika miji hiyo. Hadi sasa jumla ya vijiji 30 katika Wilaya ya Masasi, Nachingwea na Ruangwa vimeshaunganishwa na mradi huo. Serikali kupitia Mamlaka ya Maji Safi Nachingwea (MANAWASA) itaendelea kuunganisha vijiji vyote vilivyopo kandokando ya bomba kuu ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeshaanza kuunganisha zahanati mbalimbali na huduma za maji ambapo hadi sasa imeshaunganisha zahanati za Nangoo, Chisegu na Chikundi zilizopo Wilaya ya Masasi. Aidha, kwa zahanati za Naipanga na Mkotokuyana Wilaya ya Nachingwea, zahanati za Nandanga na Mbecha Wilaya ya Ruangwa zinapata huduma za maji katika vituo vya kuchotea maji vilivyojengwa karibu. Serikali itaendelea kuhakikisha zahanati zote pamoja na vituo vya afya vinaunganishwa na huduma ya maji.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Je, nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa mlipuko wa magonjwa ya nguruwe hayajitokezi mara kwa mara nchini?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mifugo na Uvuvi naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika,ni kweli hivi karibuni kulijitokeza mlipuko wa ugonjwa wa homa ya nguruwe katika mikoa kadhaa nchini na kusababisha hasara kwa wafugaji. Ugonjwa huu unaosababishwa na virusi, hauna chanjo wala tiba. Njia pekee za kudhibiti ugonjwa wa homa ya nguruwe ni kuzingatia kanuni bora za ufugaji wa nguruwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali na wadau wengine inafanya jitihada za kudhibiti ugonjwa huu, jitihada hizo ni pamoja na:-

(i) Kuhimiza wafugaji kuacha kufuga nguruwe kwa njia huria;

(ii) Kuzuia wageni kuingia kwenye mabanda ya nguruwe;

(iii) Kuhimiza wafugaji wapulizie dawa za kuua virusi na kupe kwenye mabanda na kuweka dawa ya kuchovya kwenye milango ya mabanda;

(iv) Kuweka katazo la kusafirisha nguruwe na mazao yake kutoka sehemu zenye ugonjwa;

(v) Kuhimiza wafugaji kutokuruhusu wachinjaji au wafanyabiashara kuingia katika mabanda na kuchagua nguruwe wa kununua;

(vi) Kuepuke kulisha nguruwe mabaki ya vyakula kutoka kwenye mahoteli na migahawa;

(vii) Kuacha kuchanganya nguruwe wageni na wenyeji kwenye banda moja; na

(viii) Wafugaji kutoa taarifa za ugonjwa au vifo vya nguruwe pindi inapojitokeza kwa mtaalamu wa mifugo aliye karibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wa Serikali kupitia Wizara ni kuendelea kutoa elimu ya udhibiti kwa wadau wote katika mnyororo wa thamani, wakiwemo wafanyabiashara na wasafirishaji wa nguruwe pamoja na watoa huduma za afya ya mifugo. Kazi hii tunaendelea kuifanya kwa kuzingatia uhalisia katika kila eneo kwa wafugaji wakubwa na wadogo.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali baada ya kukamilika kwa Mradi wa Utafiti wa Madini ya Graphite Kata ya Chiwata?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, nipende kulieleza Bunge lako tukufu kuwa, Mikoa ya kusini mwa Tanzania ikiwemo Lindi na Mtwara imebarikiwa kuwa na hazina kubwa ya madini ya kinywe ambayo kitaalam inaitwa graphite ambayo ni madini ya kimkakati yanayohitajika sana duniani kwa sasa kutokana na matumizi yake kama malighafi za viwandani.

Mheshimiwa Spika, kutokana na uwepo wa hazina ya madini hayo, yapo makampuni mengi yanayomiliki leseni za utafutaji na uchimbaji madini ya kinywe katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Lindi na Mtwara. Hadi sasa kwa nchi nzima kuna jumla ya leseni 68 za utafutaji, leseni 24 za uchimbaji wa kati na leseni moja ya uchimbaji mkubwa wa madini ya kinywe.

Mheshimiwa Spika, katika Kata ya Chiwata ambayo ipo Jimbo la Ndanda, Wilayani Masasi kuna leseni mbili za uchimbaji wa kati zilizotolewa kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited na leseni hizo zilitolewa mwaka 2018 baada ya kuwa kampuni hiyo imekamilisha shughuli za utafiti. Na kinachosubiriwa ni Kampuni hiyo kuanza uchimbaji na hatimaye uchakataji wa madini ya kinywe katika leseni hizo.

Mheshimiwa Spika, mpango wa Serikali ni kuona kuwa makampuni yanayomiliki leseni za utafutaji madini yanakamilisha shughuli za utafiti na kuomba leseni za uchimbaji mkubwa na wa kati. Kuwepo kwa leseni za uchimbaji wa madini katika maeneo hayo kutasababisha kuanzishwa kwa miradi ya uchimbaji ambayo italeta mapinduzi makubwa ya kiuchumi katika Sekta ya Madini.

Mheshimiwa Spika, aidha, uanzishwaji wa miradi hiyo utaiwezesha Serikali kukusanya mapato zaidi, kutoa fursa za ajira kwa Watanzania hasa wanaoishi katika maeneo yanayozunguka miradi, uhaulishaji wa teknolojia, fedha za kigeni, lakini pia na manufaa mengine kwa jamii kupitia local content pamoja na CSR.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Je, nini mpango wa Serikali baada ya kukamilika kwa Mradi wa Utafiti wa Madini ya Graphite Kata ya Chiwata?
NAIBU WAZIRI WA MADINI alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Madini, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, baada ya kukamilika kwa shughuli za utafiti wa madini ya kinywe katika Kata ya Chiwata ambayo ipo Jimbo la Ndanda, Wilayani Masasi, mpango wa Serikali ni kutoa leseni ambapo hadi sasa leseni mbili za uchimbaji wa kati zimekwishatolewa kwa Kampuni ya Volt Graphite Tanzania Limited.

Mheshimiwa Spika, mara baada ya kupewa leseni, ni wajibu wa kampuni iliyopewa leseni sasa kuendeleza mradi huo kwa kuanza uchimbaji.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasaidia na kufanikisha kutoa Namba kwa Vijiji vya Chipunda, Mkalinda na Sululu ya Leo vyenye wakazi zaidi ya elfu kumi katika Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji vya Chipunda na Sululu ni vijiji halali ambavyo vimeendelea pia kutambulika kupitia Matangazo ya Serikali Namba 536 Mamlaka za Miji na 537 Mamlaka za Wilaya ya tarehe 19/07/2019. Vijiji hivyo pia vilishiriki kikamilifu katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na changamoto ya uchakavu na upotevu wa Hati za Usajili za baadhi ya Vijiji, mwaka 2019/2020, Ofisi ya Rais – TAMISEMI ilihuisha taarifa za vijiji vyote nchini na kuandaa kanzidata ya Hati za Usajili wa Vijiji vyote nchini kwa kuzingatia matakwa ya kifungu cha 22 na 26 cha Sheria ya Serikali za Mitaa, Mamlaka za Wilaya, Sura ya 287. Hati hizo kwa sasa zipo katika hatua ya uchapishaji na zitatolewa kwa vijiji vyote nchini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na zoezi hilo, Kijiji cha Chipunda kilichopo Kata ya Mkululu, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi Namba yake ya Usajili ni MTR-091-0900989. Kijiji cha Sululu kilichopo Kata ya Sululu, Halmashauri ya Mji wa Masasi Namba yake ya Usajili ni MTR-092-09011574.Kijiji cha Mkalinda hakipo katika Orodha ya Vijiji vilivyopo nchini.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itasaidia na kufanikisha kutoa namba kwa Vijiji vya Chipunda Kata ya Namatutwe, Mkalinga Kata ya Chikunja na Sululu ya Leo Kata ya Namatutwe vyenye Wakazi zaidi ya elfu kumi katika Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, namba za usajili wa vijiji hutolewa kupitia Hati za Usajili wa Vijiji kwa kuzingatia matakwa ya Kifungu cha 22 na 26 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya), Sura ya 287. Aidha, Vijiji hivyo hupaswa kuwa vimetangazwa kupitia Gazeti la Serikali kama ilivyoainishwa katika Kifungu cha 30 cha Sheria ya Serikali za Mitaa (Mamlaka za Wilaya) Sura ya 287.

Mheshimiwa Naibu Spika, Chipunda na Mkalinga ni Vitongoji katika Kijiji cha Namatutwe na Napata na Sululu ya Leo ni eneo ndani ya Kitongoji cha Maleta katika Kijiji cha Namatutwe, Kata ya Namatutwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, hivyo maeneo hayo hayatambuliki kama Vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa wakazi wa maeneo hayo wameonesha uhitaji wa kuanzisha Vijiji ni vema wakaanzisha kusudio la kuyafanya maeneo hayo kuwa vijiji kwa kuzingatia sheria pamoja na Mwongozo wa Uanzishaji Maeneo ya Utawala wa Mwaka 2014 kupitia mikutano na vikao kwenye ngazi ya vijiji, Baraza la Madiwani, Kamati ya Ushauri ya Wilaya, Kamati ya Ushauri ya Mkoa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, Serikali imefikia hatua gani katika kutekeleza amri ya Mahakama ya kuwalipa fidia Wanakijiji wanaozunguka katika eneo la Gereza la Namajani?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Napenda Kujibu Swali La Mheshimiwa David Cecil Mwambe Mbunge wa Jimbo la Ndanda lenye vipengele (a) na (b) kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kulikuwepo na mgogoro wa ardhi baina ya Gereza la Namajani na wanakijiji wa Kijiji cha Ngalole. Mgogoro huo ulitatuliwa na Mahakama kwa kuamuru Jeshi la Magereza kulipa fidia ya shilingi bilioni 2.4 kwa eneo la ukubwa wa ekari 2,064 lililokuwa na mgogoro.

Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza amri ya Mahakama ya kulipa fidia kwa wanakijiji wanaozunguka eneo la Gereza Namajani, Serikali kwa nia thabiti tayari imefanya utambuzi wa Wanakijiji wanaostahili kulipwa fidia kama hatua za awali na hivi sasa inaendelea na mchakato wa upatikanaji wa fedha za kulipa fidia hiyo na pindi fedha itakapopatikana italipwa haraka kwa wananchi hao.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, nini mkakati wa Serikali kumaliza kero ya kukatikakatika kwa umeme Mikoa ya Kusini hasa Wilaya ya Masasi na Vijiji vyake?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, hali ya upatikanaji wa umeme katika Mkoa wa Mtwara imeendelea kuimarika na kuwa ya kuridhisha ukilinganishwa na kipindi cha nyuma. Serikali inao mkakati wa dhati wa kumaliza changamoto hii kwa mikoa ya Kusini na maeneo mengine ya Tanzania nzima.

Mheshimiwa Spika, ili kuondoa changamoto hii, Serikali imetenga jumla ya shilingi milioni 600 kwa ajili ya kurekebisha miundombinu katika line za Newala, Nyangao, Masasi na Mahuta. Aidha, jumla ya shilingi bilioni 2.2 zimetengwa kwa ajili ya kujenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Nanganga hadi Masasi. Pia, jumla ya shilingi bilioni mbili zimetengwa kuweka transfoma kubwa kati ya Tunduru na Namtumbo ili kupata umeme mkubwa kutoka Ruvuma bila kuathiri watumiaji wengine.

Mheshimiwa Spika, katika mpango wa kudumu wa kuimarisha Gridi ya Taifa, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 250 kujenga Gridi ya Taifa kutoka Songea – Tunduru – hadi Masasi. Kwa mwaka 2022/2023 Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 66.7 kuanza ujenzi wa njia hiyo.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itapeleka maji katika Kata za Namajani, Mpanyani, Mlingula, Msikisi na Chingulungulu (Kata ni Namalutwe) zilizopo katika Jimbo la Ndanda?
NAIBU WAZIRI WA MAJI alijibu: -

Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwa niaba ya Waziri wa Maji naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Kata ya Mlingula ina Vijiji vitano vyenye huduma ya maji ambavyo ni Mlingula, Chikoweti na Nambaya. Aidha, katika kuboresha huduma ya maji kwenye Kata hiyo vijiji vya Namichi na Masikunyingi vinapata huduma ya maji kupitia bomba kuu linalopeleka maji kwenye maeneo yanayohudumiwa na Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (NAWASA). Kazi ya usanifu wa miundombinu ya maji itakamilika mwezi Juni, 2022 na ujenzi utafanyika katika mwaka wa fedha 2022/2023.

Mheshimiwa Spika, Kata za Namajani zina vijiji vitano ambavyo vinapata huduma ya maji ni Namahinga, Ngalole, Namajani. Kata ya Mpanyani ina vijiji vitano ambapo Vijiji vya Muungano Nambawala A na Nambawala B vinapata huduma ya maji. Kata ya Nsikisi ina vijiji vitatu ambapo Kijiji cha Namalembo kinapata huduma ya maji. Vile vile katika Kata ya Namalutwe pale pameandikwa Chingulugulu, naomba isomeke Namalutwe kwa sababu Chingulugulu ni kijiji na Kijiji cha Chingulugulu kina huduma ya maji. Katika mwaka wa fedha 2021/2022 kazi ya utafiti wa maji chini ya ardhi imekamilika katika vijiji nane katika Kata hizo nne na uchimbaji wa visima unaendelea na miundombinu ya maji itafanyika katika mwaka wa fedha 2022/2023.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itafikisha umeme katika Kata mbili ambazo hazijawahi kupata umeme kabisa katika Jimbo la Ndanda?
WAZIRI WA NISHATI alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli katika Jimbo la Ndanda kuna Kata 16 ambapo Kata mbili (2) kati ya Kata hizo hazina umeme. Kata hizo ni Msikisi na Mpanyani. Aidha, Kata ya Msikisi inaundwa na vijiji vya Miwale, Namalembo na Msikisi yenyewe, wakati Kata ya Mpanyani inaundwa na vijiji vya Nambawala A, Nambawala B, Mhima, Muungano na Mpanyani yenyewe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Vijiji hivyo vyote vya Kata hizo vinapatiwa umeme kupitia mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili ulioanza kutekelezwa na Mkandarasi M/s Namis Corporate Engineers and Contractors mwezi Aprili, 2021 na unatarajia kukamilika Desemba, 2022.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Masasi – Nachingwea kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Waziri Ujenzi na Uchukuzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya Masasi – Nachingwea yenye urefu wa kilometa 45 ni sehemu ya barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale yenye urefu wa kilometa 175 ambayo ipo katika hatua ya Manunuzi kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kwa kutumia utaratibu wa EPC+F. Uchambuzi wa zabuni upande wa technical umekamilika na sasa unafuata uchambuzi wa financial ambao utafanywa na Wizara ya Fedha na Mipango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. (Makofi)
MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, lini Serikali itakarabati majengo ya shule za msingi chakavu Wilayani Masasi yaliyojengwa kati ya mwaka 1905 na 1960?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI) alijibu: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais -TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Daniel Cecil Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ina jumla ya shule za msingi 40 ambazo ni kongwe na chakavu. Kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023 Serikali imepeleka shilingi milioni 200 katika shule kongwe na chakavu za Liloya na Lusonje kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vitano vya madarasa na tayari yamekamilika. Aidha, shilingi milioni 180 zimepelekwa katika Shule Kongwe ya Luatala kwa ajili ya ujenzi wa vyumba tisa vya madarasa, na taratibu za ujenzi zimeanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shule nyingine kongwe za Mkalapa, Rivango, Chikoropola, Mwena na Lulindi Maalum zimetengewa fedha kupitia mradi wa BOOST na utekelezaji unatarajiwa kuanza hivi karibuni.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, ni lini Serikali italipa fidia eneo la Nanganga ambako ujenzi wa barabara iendayo Ruangwa unaendelea?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE) alijibu: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007 na Kanuni zake za Mwaka 2009 wananchi ambao mali zao zipo ndani ya mita 22.5 hawatastahili kulipwa fidia kwani wamo ndani ya eneo la hifadhi ya barabara. Kwa upande wa wananchi ambao wamo ndani ya nyongeza za mita 7.5 kwa nchi nzima Serikali inafanya kazi na kuandaa mapendekezo ambayo yatabainisha maeneo gani wananchi wataruhusiwa kuyaendeleza na yapi Serikali itayachukua na kuyalipa fidia. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Je, ni lini Serikali itaviunganishia umeme vijiji vya Jimbo la Ndanda vilivyopitiwa na nguzo za umeme wa msongo wa 33KV kuelekea Masasi?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Jimbo la Ndanda lina jumla ya kata 16 na vijiji 69, vijiji 33 vina umeme na 36 bado havijapata umeme vikiwemo vijiji vya Mkungu, Chipite, Mkang’u, Mumburu B, Muongozo, Mdenga na Mbemba vinavyopitiwa na njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33 kutoka kituo cha kupoza umeme cha Mahumbika kuelekea Masasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vijiji vyote 36 ambavyo havina umeme katika Jimbo la Ndanda vinapatiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa pili unaotekelezwa na Mkandarasi M/s Namis Corporate Engineers and Contractors. Mradi huu unatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Desemba, 2022.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza: -

Je, Serikali haioni haja ya kurejesha kwa wananchi eneo la Namajani - Masasi kwa vile Jeshi la Magereza limeshindwa kuwalipa fidia?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu,

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, baada ya kupokea malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi Serikali iliwaelekeza wataalam wa ardhi wa Jeshi la Magereza na wataalam wa ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kupima eneo lililovamiwa na kubaini kuwa na ukubwa wa ekari 2,054 na eneo ambalo halikuwa limevamiwa na wananchi lilikuwa na ekari 1,696.

Mheshimiwa Spika, Jeshi la Magereza kwa sasa linaendelea kumiliki eneo la ekari 1,696 ambazo hazikuwa na mgogoro. Kama hatua ya muafaka wa kumaliza mgogoro, Serikali ilikubali kuwaachia wananchi eneo lenye ukubwa wa ekari 2,054 lililokuwa tayari linatumiwa. Mwafaka huo ulifikiwa kwa kuwashirikisha wananchi wa Kijiji cha Ngalole, uongozi wa wilaya na Mkoa wa Mtwara, Wizara ya Ardhi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, nashukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Je, kweli kuna wazee wanaodai haki zao kutokana na ushiriki wao kwenye Vita vya Dunia au Jeshi la KAR?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA alijibu:-

Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba wapo wazee waliopigana Vita ya Pili ya Dunia (1939 - 1945) wakiwa askari wa Jeshi la KING’S AFRICAN RIFLES (KAR) lililokuwa chini ya Serikali ya Kikoloni ya Uingereza. Haki wanazodai zinahusiana na mali walizoachiwa na Serikali ya Uingereza mara baada ya utawala wao Tanganyika kukoma.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru.
Ujenzi wa Mahakama Kata ya Chikundi – Ndanda

MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-

Je, lini ahadi ya ujenzi wa Mahakama Kata ya Chikundi - Ndanda itatekelezwa?
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA alijibu:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania, imeendelea kuimarisha majengo ya Mahakama katika ngazi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kujenga majengo mapya na kukarabati yaliyo katika hali ya uchakavu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sasa mradi wa ujenzi wa Jengo la Mahakama ya Mwanzo Chikundi unatekelezwa kwa kutumia bajeti ya mwaka 2024/2025 na mkandarasi yupo eneo la site na ujenzi unaendelea, nashukuru. (Makofi)
MHE. AGNES E. HOKORORO K.n.y. MHE. CECIL D. MWAMBE aliuliza:-
Je, lini majengo ya Chuo cha VETA Chikundi – Ndanda yataanza kutumika?
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa elimu ya mafunzo ya ufundi stadi katika kuimarisha ustawi wa uchumi wa wananchi katika Wilaya ya Masasi. Katika kutambua hilo, Serikali imejenga Chuo cha Ufundi Stadi katika eneo la Chikundi, Ndanda, Chuo ambacho kina jumla ya majengo 17 ambayo ni jengo la utawala, karakana nne, jengo la madarasa, majengo matatu ya maliwato, stoo ya vifaa, bwalo la chakula na jiko, jengo la mlinzi, jengo la kupokelea umeme, bweni la wavulana, bwei la wasichana, nyumba ya Mkuu wa Chuo na nyumba pacha kwa ajili ya watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chuo hiki kwa sasa kimeshafunguliwa na majengo yote katika chuo hicho yanatumika. Aidha, katika mwaka 2023/2024 Chuo kimedahili wanafunzi na kuanza kutoa mafunzo, nakushukuru.