Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Supplementary Questions from Hon. Cecil David Mwambe (105 total)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini ningependa kuuliza swali la nyongeza lenye sehemu (a) na (b).

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa tufahamu wazi kwamba Serikali sasa hivi imeamua kutoa elimu ya bure, lakini hata hivyo haikujipanga nayo. Naweza nikatoa ushahidi katika hili kwa sababu katika Jimbo la Ndanda kuna shule inaitwa Liloya, wamepelekewa pale shilingi 86,000/=. Hii ni shule yenye idadi ya wanafunzi 600, na hiyo ni sawasawa na shilingi 146/= kwa kila mwanafunzi kwa mwezi mmoja. (Makofi)

Je, Serikali haikuona kwamba jambo hili ingeliacha kwanza mpaka pale itakapokaa Bunge la Bajeti na kupitisha bajeti ambayo itakidhi mahitaji ya wakati badala ya kukurupuka kufanya jambo ambalo haijajipanganalo? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili la msingi niliuliza kwamba lini Serikali itakuwa tayari kupeleka ruzuku katika Chuo cha Ufundi Ndanda ili kiweze kudahili wanafunzi wengi zaidi kwa sababu kile ni Chuo kilicho bora kuliko vyuo vyote vya Serikali vinavyotoa elimu ya ufundi vilivyopo katika Mkoa wa Mtwara na Lindi? Naomba kuwasilisha maswali yangu.
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, naomba nijibu maswali ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Serikali haijakurupuka. Haijakurupuka kwa sababu Serikali hii ndiyo inayoishi na wananchi na kufahamu matatizo yao. Ndiyo inayofahamu hali halisi ya mazingira tuliyonayo na ndiyo maana ikajiwekea mpango kupitia Ilani yake ya Uchaguzi wa CCM kwamba itatoa elimu bure kuanzia Chekechea mpaka kidato cha nne. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo basi, kama ambavyo tumejionea katika mipango mingine tuliyokuwa tumeianza, ikiwemo na Mipango ya MMEM, Mipango ya MMES na mipango katika sekta nyingine, kila wakati tumekuwa tukianza na tunaboresha kadiri tunavyoendelea. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, kwa hali hiyo, kama ambavyo nimesema, kimsingi tunafahamu hata baadhi ya shule, tulipowaambia walete idadi ya wanafunzi pamoja na mahitaji kulingana na uhalisia, kuna wengine walileta sawa, kuna wengine hawakuleta vizuri. Pamoja na hayo, tumeshadhamiria kuona ni namna gani tunaendelea kufanya uchambuzi na kuboresha kadiri itakavyowezekana.

Hivyo tunasema kwamba katika majukumu yale yanayoihusu Serikali kwa sababu elimu inaendeshwa kwa ubia baina ya Serikali na wananchi; wazazi kwa ujumla, kwa hali hiyo, katika yale majukumu yote ambayo tumejipangia, tutahakikisha Serikali inatimiza wajibu wake. Huo ndiyo msimamo wa Serikali yangu. Katika swali la pili…
NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI, TEKNOLOJIA NA UFUNDI: Najibu swali la nyongeza la pili. Katika swali la nyongeza la pili la Mheshimiwa Cecil, kimsingi swali la mwanzo ulikuwa unahitaji ujenzi wa Chuo na sasa hivi umezungumzia juu ya utoaji wa ruzuku.

Kwa sasa hivi bado hatujafikiria kutoa ruzuku katika Chuo hicho ambacho kipo Ndanda. Hata hivyo, ni suala la kuangalia, kama kuna uwezekano na itaonekana lina faida kufanya hivyo, basi tutazidi kushauriana na kuona suala hilo linaweza likafanyika.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza. Nataka kufahamu pia kuhusiana na mgogoro wa wafanyakazi uliopo katika Hospitali ya Ndanda. Serikali iliahidi itaajiri wafanyakazi 85 na wale Wamisionari sasa hivi wameamua kupunguza wafanyakazi 59 kwa sababu Serikali haijatekeleza ahadi yake toka mwaka 2012 hali inayotishia kuifanya Hospitali ya Ndanda isiwe tena Hospitali ya Rufaa katika eneo la Kusini. Je, ni lini Serikali itakuwa tayari kutekeleza ahadi yake ya kupeleka pesa kwa ajili ya wafanyakazi wa Ndanda Hospitali?
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu pia ni lini Serikali italipa pesa za fidia katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kwa vile katika vitu vilivyoharibika ni pamoja na gari la wagonjwa la hospitali ya Chiwale ili waweze kujinunulia wenyewe tena lile gari liweze kusaidia baada ya kujenga wodi ya akinamama katika eneo lile? Ahsante
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la changamoto ya watumishi ni kwamba Serikali tumelichukua. Sasa hivi tuna mchakato wa kuajiri watumishi mbalimbali katika Halmashauri zetu na Wizara ya Afya ina-finalize stage hiyo. Nina imani kwamba siyo muda mrefu ndani ya mwezi huu wa Mei na Juni tutaenda kupunguza hii gape ya watumishi, lakini changamoto ya Ndanda tutakwenda kuifanyia kazi. Naomba nimwahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba tutakwenda kulifanyia kazi kwa karibu zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala la ambulance zilizoungua, ni kweli na mimi mwenyewe nimefika pale. Pale kuna ambulance tatu zilichomwa moto na kwa njia moja au nyingine siyo kwamba Serikali ni ya kulaumiwa. Katika hili, naomba nitoe maelekezo kwa wananchi, inawezekana kwa jazba zetu tunaharibu vitu ambavyo vilikuwa kwa maslahi ya wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kipindi kile pale Mtwara watu walienda kuchoma ambulance ambazo zinabeba akinamama na watoto. Fikiria mtu anachukua kibiriti na petrol anakwenda kuchoma ambulance tatu mpya, unategemea nini katika mazingira hayo? Kwa kweli ni jambo lenye kuhuzunisha na ndiyo maana nilipofika pale Masasi nilienda kutembelea maeneo yake, kwa kweli ni jambo la kuhuzunisha, lakini Ofisi ya Rais, TAMISEMI tutaangalia jinsi gani tutafanya kwa sababu mwisho wa siku ni wananchi na akinamama ndiyo wanaopata shida zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunalichukua hili kwa upana wake lakini kwa kweli kama Ofisi ya Rais, TAMISEMI tumesikitika sana kwa sababu ile ni fursa ambapo wananchi walikuwa wanapata huduma kila siku. Naomba nitoe onyo kwa watu wote, tusichukue jazba zetu mbalimbali tukazielekeza katika vitu ambavyo vinawasaidia wana jamii kupata huduma bora katika maisha yao.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nina maswali mawili ya nyongeza kwa Wizara ya Nishati na Madini. Kwa vile Wilaya za Masasi, Nanyumbu na hasa Masasi Mjini, Kijiji cha Ndanda pamoja na Chikundi, kuna tatizo sana la umeme kukatika kila mara na umeme huu ndiyo ambao tunaambiwa sasa unapelekwa Liwale. Je, Mheshimiwa Waziri anawahakikishiaje wakazi wa Liwale kuwa na umeme wa uhakika, wasije wakapata matatizo ambayo wakazi wa Masasi wanayapata kila mara?
Swali la pili, tuliambiwa watakapoanza kutumia umeme wa gesi, basi hata gharama za kuunganisha, lakini pia na gharama za kuwafikia wale wakazi umeme toka siku ambazo wamelipia zitakuwa ni chache sana. Katika hali ya kushangaza kuna wakazi wa maeneo ya Nachingwea, pia Ndanda na hizo Wilaya nyingine nilizozitaja wanaweza kukaa hata miezi mitatu au minne bila kuunganishiwa umeme toka tarehe waliyolipa. Pia, kuna vijiji vingi ambavyo vinapitiwa na nguzo kuu za umeme zinazokwenda Liwale na Masasi Mjini; Unawaambiaje wakazi wa Masasi juu ya mambo haya mawili?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna changamoto za upatikanaji wa umeme hasa katika maeneo ya Masasi na Nanyumbu, siyo Masasi tu hata maeneo mengine ya Liwale pamoja na Nachingwea. Hata hivyo, juhudi zilizofanyika ni kubwa. Nimhakikishie Mheshimiwa Cecil Mwambe kwamba kazi inaendelea. Hata hivyo, kwenye Awamu ya Pili ya REA ni vijiji kwa Wilaya zote alizotaja 152 vimepatiwa umeme.
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kuna vijiji mia moja na kumi na moja (111) kwa Wilaya zote havijapata umeme. Mkakati uliopo kwa niaba ya wananchi wa maeneo ya Masasi, Nanyumbu, Nachingwea na maeneo ya karibu yatapelekewa umeme kwenye REA Awamu ya Tatu inayoanza mwezi Oktoba, Novemba hadi Disemba mwaka huu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na suala la uhakika wa umeme kwa wananchi wa Masasi nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na nakushukuru sana kwa sababu umekuwa ukifuatilia jambo hili. Suala la upatikanaji wa umeme kwa Wilaya za Masasi na maeneo ya jirani linafanyiwa kazi na kwa kweli litatatulika kwa muda mfupi sana kuanzia sasa.
Mheshimiwa Naibu Spika, gharama za umeme; kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwaeleza wananchi kwamba gharama za umeme kwa kweli zinashuka. Ni kweli kabisa baada ya kuanza kutumia gesi asilia gharama za umeme zimeshuka na kwa nchi nzima. Gharama za umeme kwa miradi ya REA ni sh. 27,000 na hiyo ni nchi nzima.
Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, gharama za kulipa umeme kwa wananchi wanaotumia gesi asilia, hasa kwa Mikoa ya Lindi na Mtwara na maeneo ya jirani, hata kwa kazi wanazounganishiwa na TANESCO ni za chini; badala ya sh. 177 kwa mikoa hiyo miwili ni sh. 99. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tutaendelea kutumia gharama hizo kwa Mikoa ya Lindi, Mtwara pamoja na Wilaya nyingine za Masasi na Nanyumbu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ujenzi. Nataka kufahamu kwa uhakika ni lini Serikali itasema waziwazi siku ambayo kazi ya ujenzi wa barabara ya Masasi, Nachingwea utaanza? Kwa sababu upembuzi yakinifu ulifanyika pale muda mrefu, wananchi wanakosa amani katika eneo lile kwa sababu nyumba zao nyingi zilichorwa „X‟ na hawajui lini zitavunjwa au waendelee na ujenzi katika eneo lile. Tuliona tija ya Serikali imetoa nguvu kubwa sana na sasa hivi wanakaribia kuanza ujenzi wa barabara inayokwenda Ruangwa kuanzia Nanganga. Tunataka tuone pia na upande wa Masasi Nachingwea na wenyewe ujenzi unaanza mara moja.
Kwa hiyo, tunaomba commitment ya Serikali watueleze, ni lini ujenzi wa hii barabara utaanza au kama siyo hivyo, basi wananchi wale waambiwe waendelee kuendeleza yale makazi yao kwa sababu wanaishi katika maisha duni, hawajui ni lini nyumba zao zitavunjwa kwa sababu ya uendelezaji wa barabara katika eneo hilo? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Mwambe awaelimishe wananchi waliopo katika barabara hiyo kwamba wasijenge, kwa sababu Serikali ina dhamira ya dhati ya kuijenga barabara hiyo kwa kiwango cha lami. Mheshimiwa Mbunge anafahamu kwamba katika mwaka huu wa fedha kuna fedha zimetengwa kwa ajili hiyo. Suala la lini, naogopa sana kusema kwa sababu kuna process ya kufikia hiyo hatua. Naomba tukamilishe hiyo process, itakapokamilika tutamjulisha lini tunaanza.
nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo Kyerwa linafanana moja kwa moja na tatizo lililopo katika Halmashauri ya Wilaya Masasi. Tatizo letu kubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ni masuala ya miundombinu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tuna maji ya kutosha. Serikali iliahidi kutenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuleta miundombinu itakayofikisha maji katika Vijiji vya Mbemba, Mbaju, Maparagwe pamoja na Chikunja. Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kupeleka pesa angalau kidogo kidogo katika hii miradi ili iweze kutekelezwa mara moja?
WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti ya mwaka 2016/2017, kila Halmashauri imetengewa fedha kwa ajili ya kuendeleza miradi ambayo ilishakuwa imeanza. Hii ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Masasi. Fedha hizo hatutapeleka moja kwa moja; tumeagiza kwamba walete certificate kwa sababu nyingi wameshakuwa na Wakandarasi. Walete certificate ili tuweze kuwalipa wale Wakandarasi waweze kuendelea na utekelezaji wa miradi hiyo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge kuna Mkandarasi na kuna certificate ambayo haijalipwa, niletee ili tuweze kulipa, fedha zipo. Hatuwezi kupeleka fedha zikakae tu, tunataka fedha ziende na zifanye kazi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi, kuna jambo moja nataka tuliweke kwenye rekodi lakini pia swali langu kwa Mheshimiwa Waziri; kwa sababu kwa muda mrefu Serikali ilikuwa ikitangaza kwamba gongo ni pombe haramu kama ambavyo umeona watu wengi swali hili wakiliuliza, lakini kuna pombe mbalimbali zinazotengenezwa kutokana na mazao.
Mheshimiwa Spika, kule kwetu kuna pombe inatengenezwa nipa ndiyo hiyo hiyo gongo inatokana na mabibo makavu lakini pia ni sehemu ya kuongezea wakulima kipato.
Je, Serikali haioni sasa kama hawataki wakulima wale wapike gongo kwa kutumia zile malighafi zao ambao ni sehemu ya korosho kwa nini sasa isinunue wakaenda kufanya hata chakula cha mifugo kwa nia ya kuwaongezea wakulima kipato?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kama nilivyozungumza kwenye suala la Mheshimiwa Selasini, suala linalotukwamisha, na ndiyo maana watu wengine kwa kutokujua wanaichukia TFDA, hoja ni kwamba kinywaji kile kinatengenezwa vipi? Kinakuwa packed vipi? Na kinapimwa kuthibitisha huo ubora, na nimeshaahidi, na niwaeleze wataalam wangu watakao kwenda Mikoa ya Lindi kafuatilie kinywaji hicho.
Mheshimiwa Spika, lakini nikutake wewe Mheshimiwa Mbunge rafiki yangu Bwana Mwambe na wewe ni rafiki yangu na unajua. Njoo unieleze wazo hilo tutumie wawekezaji wa ndani hata wa nje tuweze kutengeneza kinywaji kizuri hicho tuweze kuuza Tanzania na masoko ya nje.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante kwa kunipa swali kwenye Wizara ya Afya. Suala linalotokea Hospitali ya Mnazi Mmoja ni sawasawa kabisa na masuala yanayotokea katika Hospitali ya Rufaa ya Ndanda, Mkoa wa Mtwara. Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi alipotembelea alitoa ahadi ya wafanyakazi wasiopungua 85; hivi ninavyoongea sasa hivi hospitali ya Rufaa ya Ndanda inakaribia kukosa hadhi ya kuitwa Rufaa kwa sababu kuna Daktari Bingwa mmoja tu. Je, Wizara yake ina mpango gani wa kuwawezesha watu hawa ili waendelee kutoa huduma kwa sababu ni hospitali ambayo ina vifaa vingi lakini inakosa wataalam wa kuvitumia?
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwamba mpango tulionao ni kusubiri kibali kutoka kwa wenzetu wa utumishi kitoke, kitakapotoka tutaajiri Madaktari Bingwa kwa kiasi ambacho tutakuwa tumekasimiwa na kuwatawanya kwenye hospitali zote za Rufaa za Mikoa nchini ikiwemo Hospitali ya Ndanda.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nataka kufahamu kwamba kwa muda mrefu Serikali kupitia Mfuko wa Wakfu wa kuendeleza zao la korosho umekuwa ukiruhusu pesa kwa ajili ya kufanya tafiti mbalimbali kwenye kuongeza thamani ya mazao ya wakulima ikiwemo mabibo kwa ajili ya kupata juice ambayo inaonekana ina uwezo mara tano zaidi wa kupata vitamin c kuliko ilivyo kwenye machungwa. Pia mabaki ya korosho kavu ambayo ni kochoko na yenyewe kuna uwezekano mkubwa sana wa kuweza kupata gin. Baada ya tafiti hizi kukamilika ni muda mrefu sana umepita, je, Serikali iko tayari kuanzisha viwanda kwa ajili ya kutengeneza juice pamoja na gin ili kuweza kuongezea wakulima hawa kipato kwa sababu mabibo pamoja na kochoko sasa vitakuwa rasmi na vitaweza kununuliwa na Serikali?
WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi nilijibu swali la Mheshimiwa Conchesta na naomba nirudie kwa maslahi ya Wabunge wote na Watanzania. Serikali kazi yake ni kuweka mazingira bora ya wawekezaji. Mheshimiwa Mbunge, nakuomba uje tukae wote kusudi hizo taarifa ulizonazo za fursa ya uwekezaji tuweze kuziweka pamoja kwenye andiko zuri, tutangaze ili tuweze kupata wabia wa kuweza kuwekeza kwenye kiwanda hicho. Hata hivyo, mwekezaji mzuri ni Mtanzania, ni mwananchi wa Jimbo lako, ni wewe mwenyewe Mheshimiwa Mbunge. Kwa hiyo na sisi tutafute rasilimali tuweze kujenga viwanda sisi wenyewe.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kimsingi swali langu linafanana na swali namba 107 linakwenda Wizara ya Kilimo. Kimsingi ninataka kufahamu, tukiwa tunaelekea kwenye uuzaji wa korosho msimu uliopita tumeshuhudia Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Mtwara (MAMKU) viongozi wake, watendaji wakuu wakishikiliwa kwa ajili ya uchunguzi kutokana na ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini suala hili pia limejitokeza katika vyama vikuu vya TANECU, Lindi Mwambao, Ilulu pamoja na Chama Kikuu cha Mkoa wa Pwani. Tumeona Mheshimiwa Waziri Mkuu akichukua hatua kwa viongozi hawa wa Chama Kikuu cha MAMCU sasa tunataka kufahamu kutoka kwa Waziri amejipangaje na yeye kuwachukulia hatua viongozi wa vyama vikuu nilivyovitaja kwa sababu ya kudhulumu na matumizi mabaya ya pesa za wakulima za korosho katika Mikoa ya Mtwara, Lindi pamoja na Pwani? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kabisa kama alivyosema katika msimu uliopita wa korosho kumekuwepo na changamoto nyingi sana kuhusu malipo kwa wakulima wa korosho na ndiyo maana Waziri Mkuu alichukua hatua ya kuhakikisha kwamba sheria inachukua mkondo wake kwa watu wa MAMCU, lakini vilevile mtunza ghala wa Chama cha Msingi cha Ushirika ambapo kosrosho ziliweza kupungua bei na tunavyozungumza tayari wahusika wamefunguliwa kesi ya kuhujumu uchumi na kesi inaendelea mahakamani, lakini vilevile tunawahakikishia wakulima wale ambao wamepata changamoto hiyo ya fedha zao kutolipwa kwa kiwango ambacho kilitarajiwa kwamba Chama cha Ushirika ambacho kilisababisha korosho zile ziweze kuingia kwenye sales catalogue wao watalazimika kurudisha ile tofauti ili mkulima asije akapata tatizo lolote. Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile tunafahamu kwamba changamoto iliyotokea Mtwara lakini vilevile Nanyumbu tunafahamu vilevile imetokea Mkoa wa Pwani kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba tayari Serikali inachunguza changamoto hizo, Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kashafanya uchunguzi huo na tumepata repoti.Lakini vilevile Waziri Mkuu mwenyewe aliagiza ufanyike uchunguzi wa kina na repoti iko tayari Serikali inapitia taarifa zile ili wale wote ambao wamehusika wakiwemo viongozi na watumishi wa MAMCU, TANECU na vyma vingine vya ushirika kama KORECU ambao watakuwa wamehusika watachukuliwa hatua za kisheria. Cha maana zaidi, wakulima wale ambao hawakupata malipo stahiki kwa sababu ya vurugu au uzembe wa watumishi wa Vyama Vikuu au Vyama vya Msingi tunawahakikishia kwamba fedha zao zitalipwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda kuuliza maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kadri ya muuliza maswali, kipengele namba (c) kinasema je, Serikali ipo tayari kusimamia wananchi walipwe fidia kutoka kwa wawekezaji wanaoingiza vifaranga wasio na chanjo toka nchi za nje?
Kimsingi kwenye jibu lake haja-commit, hajasema kama Serikali sasa hivi iko tayari kuhakikisha wafugaji wale wanaopata hasara wanalipwa fidia yao, kwa hiyo tunaomba Serikali itoe neno kwenye hili. Pia itueleze kama hali ni hii basi izuie kabisa watu wasiingize vifaranga ambavyo havina chanjo.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kutokana na kuongezeka kwa gharama za uzalishaji hasa wa chakula kama alivyosema yeye mwenyewe na tumeona gharama kubwa sana kwenye chakula cha mifugo. Kwa kipindi hiki ambapo kuna tatizo kubwa la chakula na njaa, Serikali haioni sasa umefika wakati iondoe angalau kodi fulani ili kuweza ku-compensate wakulima katika kupata chakula chenye bei nafuu na wananchi waweze kununua kuku kwa bei nafuu?
Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu fidia, kimsingi suala la fidia halitokei kwa sababu kama nilivyosema kwenye jibu la msingi, kimsingi ni kinyume cha sheria na taratibu kuingiza kuku na mayai kutoka nje, kwa hiyo wale ambao
wanaingizwa kwa taratibu ambazo sio rasmi, wanaingizwa kwa utaratibu wa njia za panya. Kwa hiyo, kimsingi Serikali imeweka utaratibu kuhakikisha kwamba hairuhusu uingizwaji, hivyo kutokea na ndiyo maana tumesema tayari
katika kipindi cha miaka minne tumeteketeza vifaranga zaidi ya 67,000. Hata hivyo, tunachotaka kutoka kwa Mheshimiwa Mbunge ni kuonesha ushirikiano kama wanaweza wakatuonesha watu ambao wanaingiza vifaranga na mayai kinyume na taratibu.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na gharama ya vyakula vya mifugo, hasa kuku, kama nilivyosema vilevile ni kweli kwamba kuna gharama kubwa sana katika kutengeneza vyakula vya kuku kwa sababu kiinilishe kinachotumika ni maharage ya soya ambayo hatuzalishi hapa nchini. Kwa hiyo, hatua ambazo tunazichukua ni
pamoja na kuhamasisha wananchi walime zao la soya.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile kupitia hotuba ya bajeti ya Wizara yetu kwa ajili ya mwaka wa fedha unaokuja, Serikali imechukua hatua kadhaa kupunguza kodi na tozo za mazao na bidhaa mbalimbali ili basi vyakula vya kuku na mazao mengine viweze kupatikana kwa bei nafuu. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la kodi na tozo litashughulikiwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona na kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Swali la Mheshimiwa Masoud ambalo kwa masikitiko tu niseme Mheshimiwa Waziri hajalijibu kadri ya mahitaji ya watu wa Mtwara na Kusini kwa ujumla. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, swali letu sisi ni kwamba kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita Serikali ilikuwa haijatengeneza barabara inayounganisha Mtwara na Dar es Salaam. Baada ya utengenezaji wa barabara hii na mara Kiwanda cha Dangote kikafunguliwa ambacho kina magari zaidi ya 1,500 yanayosafirisha cement kutoka Mtwara na kuzileta Dar es Salaam.
Sasa tunataka kufahamu Serikali kwa nini isizuie usafirishaji wa cement kwa kutumia magari ambayo yanaleta uharibifu mkubwa sana kwenye barabara za Mtwara, Lindi kufika Dar es Salaam na badala yake wanawaaachia wasafirishaji wale wale wa magari. Kwa nini wasizuie na wakapa uwezo watu wa kuleta meli wakasafirisha cement hiyo mpaka Dar es Salaam kwa distributors?
WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO:
Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyozungumza na Mheshimiwa Naibu Waziri alivyosema kwenye jibu lake la msingi, kwanza barabara ile imekuwa designed kuchukua mzigo mkubwa, hilo la kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili mzigo wote wa Dangote wa cement hauendi Dar es Salaam, unaenda sehemu mbalimbali za Tanzania na tatu, Serikali tunaendelea kufanya utaratibu na kampuni mbalimbali za meli kuhakikisha kwamba mzigo huo unakwenda kupitia vilevile upande wa baharini.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nilitaka nimueleze Mheshimiwa Waziri kwamba Mkoa wa Mtwara ndiko inakozalishwa gesi inayozalisha umeme wa Dar es Salaam ambako haukatiki kila mara, kiasi tumeanza kuamini gesi yetu haitunufaishi ni bora tungerudishiwa yale majenereta yaliyokuwa yanazalisha umeme Mtwara wakati huo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la umeme la Mtwara linasababishwa na kuharibika kwa transfoma ya jenereta moja yake ambayo nafahamu mpaka sasa kuna mvutano mkubwa kati ya TANESCO pamoja na MANTRAC Tanzania Limited kwa ajili ya ku-supply ile transfoma kwa sababu ya madeni sugu ambayo TANESCO hawajalipa.
Mheshimiwa Waziri, naomba utueleze kinagaubaga ni lini matatizo ya TANESCO na MANTRAC yatakwisha ili kuwarejeshea wananchi wa Mtwara umeme wa uhakika? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mweyekiti, ni kweli kabisa liko tatizo la kuharibika kwa mashine moja Mtwara kiasi cha kushindwa kupeleka megawatt 18 kwa ujumla wake. Kwa sasa hivi ni kweli kabisa Mtwara wanapata megawatt chini ya 18, wanapata 16 na 15.6
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wa Mtwara na Lindi lakini hatua zilizochukuliwa ni kwamba hivi sasa ukarabati umeshaanza. Mgogoro uliokuwepo kati ya TANESCO na MANTRAC umekwisha na jenereta inatengenezwa, ni hatua ya kwanza. Hatua ya pili, Mtwara tunawaongezea mashine nyingine sita ambapo kila mashine itakuwa na megawatt mbili. Kwa hiyo, mtakuwa na megawatt nyingine za ziada 12 na jumla kuwa na megawatt 30. Kwa hiyo, sasa umeme wa Mtwara pamoja na Lindi maeneo ya jirani utakuwa ni wa uhakiki zaidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba suala hili linashughulikiwa na baada ya Bunge hili Mheshimiwa Mbunge tutakwenda wote kukagua mashine hii ikiwa imeshakamilika na umeme unapatikana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la Mheshimiwa Mhagama, matatizo yaliyoko Madaba yanafanana moja kwa moja na matatizo yaliyoko Jimbo la Ndanda. Kwenye bajeti ya mwaka jana Mheshimiwa Waziri utakumbuka zilitengwa fedha shilingi bilioni moja kwa ajili ya kupeleka MANAWASA ili kununua viunganishi pamoja na mabomba ambayo yangeweza kupeleka maji katika kata za Chikukwe, kijiji cha Maparagwe pamoja na kijiji cha Chikunja. Wananchi walikubali watajitolea nguvu zao, lakini mpaka sasa hivi mabomba yale hayajakwenda.
Je, unaweza kutueleza ni lini Serikali itapeleka pesa hiyo, wakati tumebakisha siku chache tu kumaliza mwaka wa bajeti? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ni kweli kabisa kwamba Serikali ilitenga shilingi bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza Mradi wa Mbwinji pale Masasi, kupitia Mamlaka ya MANAWASA. Juzi juzi hapa Mheshimiwa Mbunge tuliwasiliana, walileta andiko na andiko hilo tayari limesapitishwa ili MANAWASA waweze kusaini mkataba kwa ajili ya procurement ya hivyo vifaa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari kwa maana ya Wizara imeshaidhinisha kwa hiyo, ni kazi ya Mkurugenzi wako sasa kusaini mkataba na mkandarasi yule ambaye mmempa kazi. Ile kazi ni ya kununua vifaa; vifaa vile ni kitu cha wiki mbili vitakuwa vimeshanunuliwa na mkishamaliza, kwa utaratibu wetu, mnaleta certificate tunatoa hela, mkandarasi analipwa. Kwa hiyo, kama MANAWASA watafanya haraka, hela hiyo lazima mtaipata katika huu mwaka wa fedha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Swali lililoulizwa na Mheshimiwa Martin Mtonda kuhusu madai ya Mawakala wa Pembejeo Mbinga Vijijini linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilaya ya Masasi Mkoa wa Mtwara na hasa Jimbo la Ndanda; kwamba katika msimu wa kilimo wa mwaka 2016 wakulima wa korosho na hapa Mheshimiwa Naibu Waziri amekiri kwamba hasara nyingine huwa zinasababishwa na watumishi wa Serikali wasio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jambo hili pia limetokea Mtwara kwa wakulima wa korosho baada ya wamiliki wa maghala kwa kushirikiana na Watendaji wa Chama Kikuu cha Ushirika kuwaibia wakulima pesa zao na kesi zinaendelea kwenye Mahakama. Je, Serikali haioni sasa ni wakati wa kutoa pesa zilizopo kwenye Mfuko wa Wakfu na kufidia hasara hii waliyoipata wakulima wakati wao wanaendelea na wale watu waliopo Mahakamani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na uwezekano wa Serikali kulipa fedha ambazo kwa sasa zipo kwenye Mfuko wa Wakfu kwa ajili ya kufidia zile fidia, ingekuwa ni jambo jema, lakini kwa sababu suala lenyewe bado liko Mahakamani, ni vizuri tukasubiri tupate majibu, kwa sababu inawezekana kule Mahakamani, wale ambao tunafikiri wamesababisha hasara ikaja ikatokea uamuzi tofauti. Kimsingi tunataka kila mtu abebe mzigo wake ili kama wale watakuwa wamehusika kulingana na hukumu ya Mahakama, wenyewe watabeba jukumu la kurudisha fedha za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachofanya sisi kama Serikali ni kuhakikisha kwamba matatizo kama haya hayatokei tena. Ndiyo maana tunavyozungumza, tayari Bodi za Vyama vya Ushirika zaidi ya 200 Mtwara na Lindi zimevunjwa, ni kwa sababu tunajaribu kuwalinda wakulima wasiendelee kuibiwa na watu wachache ambao sio waaminifu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile hizo kesi ziko Mahakamani na Afisa yeyote wa Ushirika au wa Serikali ambaye atabainika kuhusika katika upotevu wa fedha za wakulima, naye vilevile atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria zetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kuboresha ubora, ni swali ambalo liliulizwa awali ambalo linahusiana na hili. Sasa hivi Serikali ina mpango wa kuagiza mbolea kwa mkupuo (bulk procurement) na hii itasaidia sana sisi tuweze kuchagua mbolea ambayo tunahakikisha kwamba inakuwa na ubora. Kampuni yetu inayohusika na ubora wa mbolea itahakikisha kwamba mbolea yote inayoingia ni bora lakini vilevile hata kwa mbegu…
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, lakini kuna suala moja hajatoa ufafanuzi wa kina.
Mheshimiwa Spika, mwekezaji analalamika kwamba 6% za uzalishaji na gesi inayochukuliwa haitamfanya aweze kurejesha gharama za uwekezaji kwa kipindi cha miaka 25 kadri walivyokubaliana na Serikali; na Mheshimiwa hapa anasema kwamba kadri siku zinavyokwenda basi gesi nyingine itahitajika.
Mheshimiwa Spika, nataka kufahamu, ni lini Serikali itamhakikishia mwekezaji kwamba bomba hili litatumika kwa asilimia 100 ili aweze kurejesha gharama zake ndani ya miaka 25, ikizingatiwa kwamba sasa hivi yupo kwenye mwaka wa 11? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa niseme mradi ule ni wa Serikali kwa asilimia 100, hilo ni la kwanza kabisa. Kwa hiyo, unamilikiwa na Serikali kwa asilimia 100. Hata hivyo, kama nilivyosema, mwaka gani tutaweza kupata gesi asilimia 100 inayozalishwa pale? Ni mradi ambao ni endelevu. Iko miradi mingine inajengwa Mtwara ambayo inaanza mwezi Machi mwakani ambayo tutaanza kuzalisha megawati 500 kwa Mheshimiwa Mbunge.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niseme tu kwamba bado kuna muda wa kutosha, ifikapo mwaka 2020/2022 tuna matarajio kwamba gesi inayozalishwa katika Madimba tutaweza kuitumia kwenye miradi yetu ya umeme.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwa sababu miradi ni mingi, ifikapo mwaka 2022 matarajio kati ya asilimia 80 hadi 100 tutaanza kutumia gesi yote asilia.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kuniona. Swali la Mheshimiwa Mdee linafanana kabisa na suala ambalo liko katika Jimbo la Ndanda hasa katika maeneo ya Lukuledi - Chikunja - Nachingwea. Barabara ile siku za karibuni itajengwa kwa kiwango cha lami lakini tunaomba kufahamu fidia ya watu wale itafanyika kwa njia gani na ni umbali gani toka katikati ya barabara mpaka mwisho wa hifadhi ya barabara? Watu wale wanahitaji kufahamu jambo hili, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumjibu Mheshimiwa Mbunge swali la nyongeza la kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, kama alivyosema hiyo barabara hatujaanza kuijenga na tumeiwekea bajeti mwaka huu unaokuja wa 2016/2017. Nadhani unafahamu kwamba tunafuata ile Sheria ya 1967 ya Road Reserve ambayo sasa hivi tunaongelea kila upande kutokea katikati ya barabara wale wote ambao wako ndani ya mita 60 na wale ambao wako nje ya mita 60 wana haki tofauti. Wale ambao wako nje ya road reserve wana haki ya kulipwa fidia na wale ambao waliifuata barabara, nadhani kama sheria inavyosema na kama tulivyopitisha humu Bungeni hawana haki ya kulipwa fidia. Kwa hiyo, huo ndiyo umbali ambao umwekwa kisheria na ni sisi wenyewe tulipitisha humu ndani. Sisi kazi yetu ni kuisimamia tu, hapa kazi tu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nitakuwa nina maswali mawili ya nyongeza kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba Serikali imejipanga kuhakikisha wanafikisha umeme pamoja na maji hasa zaidi kwenye shule pamoja na sehemu zingine za kutolea huduma za kijamii, lakini ningependa kwa uhakika kabisa aseme kwamba ni lini Serikali itatimiza suala hili kwa sababu ni muda mrefu wamekuwa wakiliongea kila mara bila kuwa na tarehe ya uhakika kwamba itakapofika wakati fulani tutakuwa kwa kweli tumetekeleza, bado shule nyingi pamoja na vituo vya afya vinakosa huduma ya umeme pamoja na maji?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, kuna vijiji vingi sana, kama anavyosema kwamba Serikali imeazimia kupeleka umeme kwenye vijiji vyote zaidi ya 7,000, lakini ukipita Jimbo la Ndanda kwa mfano Vijiji vya Nangoo, Liputu, Ndolo pamoja na Mdenga vinapitiwa na umeme wa msongo wa megawati 33. Sasa Waziri angetusaidia kutueleza ni lini kwa hakika Serikali sasa wako tayari kushusha umeme ule kwa ajili ya matumizi ya watu wale walioko chini ya hizi waya ambazo kwao ni hatari kwa maisha?Ahsante.
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa
Mwenyekiti, katika maswali yake mawili ya nyongeza aliyouliza Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda yeye mwenyewe ni shahidi anafahamu kwa sababu ameshiriki kupitisha bajeti hapa anajua mipango ya Serikali ilivyo. Sina shaka kwamba anatambua kwamba ahadi iliyoko kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano inaendelea kutekelezwa vizuri na tuna uhakika vijiji vyote nilivyovitaja kwenye jibu la msingi vitapata umeme pamoja na vitongoji vyake kama ambavyo Wizara ya Nishati imeahidi, na mikakati iko wazi na yeye mwenyewe Mheshimiwa Mbunge ni shahidi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la maji, Mheshimiwa Waziri wa Maji ametoa ahadi hapa Bungeni kuhusu kutekeleza awamu ya pili ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji, na hii itaongezeka kasi zaidi pale ambapo tutaanza kutekeleza miradi ya maji vijijini kupitia ile Wakala wa Maji Vijijini ambao utafanya kazi sawasawa na REA inavyofanya kazi. Kwa hiyo, ndugu yangu Mwambe ondoa shaka katika swali lako la kwanza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, huu umeme ambao umepita kwenye vijiji alivyovitaja na msongo anaujua ameutaja, mimi kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati namuahidi kwamba mikakati ya Serikali itatekelezwa na wanavijiji aliowataja hao watapata umeme.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi kwa kuuliza swali la nyongeza, linalohusiana na masuala ya madini kama ambavyo Mheshimiwa Hamida ameuliza hapo mwanzoni.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo lililopo Ruangwa linafanana kabisa na tatizo lililopo Jimbo la Ndanda katika kijiji cha Chiwata.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji cha Chiwata sasa hivi kuna uwekezaji unaendelea kwa ajili ya madini ya graphite, lakini uwekezaji huu umekuwa ukufanyika kwa siri kubwa sana kiasi kwamba wananchi wa Chiwata hawafahamu nini kinaendelea na hawako tayari kuendelea kukaa kimya, wamenituma nimuulize Waziri.
Je, Serikali ipo tayari sasa kuleta mkataba ambao utatumika kwa ajili ya uchimbaji wa madini katika kijiji cha Chiwata ili kuondoa sintofahamu ambayo inaweza ikajitokeza miaka ya baadaye ya kuhitaji kufanya review na ku-cancel mikataba ile? Ninaomba commitment ya Serikali ni lini iko tayari kuleta mkataba ule ujadiliwe na Bunge ili ukatumike kwa ajili ya manufaa ya wananchi wa Jimbo la Ndanda? Ahsante.(Makofi)
NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza Mheshimiwa Mwambe nampongeza sana, tumekuwa tukishirikiana naye sana kwenye masuala ya wachimbaji wadogo mbali na masuala yake ya masuala ya nishati kwenye eneo lake. Kuhusiana na eneo analolitaja yuko mwekezaji ambaye sasa anajiandaa na kukamilisha utafiti, atakapokamilisha utafiti ndio aanze shughuli za uchimbaji, kwa hiyo hata hatua ya kuingia mkataba bado.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo nikuombe sana Mheshimiwa tukae, tujue kitu gani kinahitajika na itakapofikia wakati wa kuingia mikataba tukushirikishe, sasa ni lini mkataba tutauleta nadhani bado sana kuzungumza jambo hilo akamilishe utafiti, akishaanza uchimbaji akaingia mikataba tutajadiliana, kama kutakuwa na haja ya kuuleta basi tutaona ni utaratibu gani utumike ili Mheshimiwa Mbunge kuweza kuuona mkataba huo.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza na nitakuwa nina maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya changamoto zilizojitokeza kwenye msimu wa korosho mwaka wa jana ni pamoja na wizi uliofanyika katika maghala ya YURAP yaliyoko Masasi kwa kushirikisha wamiliki wa ghala lakini pamoja na viongozi wa mkoa walibariki jambo hili; na sasa hivi kuna kesi zinaendelea mahakamani kwa ajili ya kuweza kupata haki ya wakulima wale. Sasa tunataka kufahamu Serikali haioni haja ya kuwalipa wakulima pesa zao, kwa sababu walikuwa wanatoa michango kwenye mfuko wa kuendeleza zao la korosho wakati ninyi mnahangaika na wale wezi wenu?
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, sasa hivi tunaelekea kwenye msimu wa kilimo na wananchi wanaendelea kutayarisha mashamba yao kwa ajili ya msimu wa korosho ujao. Hata hivyo kumekuwa na sintofahamu kubwa sana kuhusiana na pembejeo baada ya Serikali kutangaza kwamba itapeleka pembejeo za bure. Sasa tunataka kufahamu, ni lini pembejeo zitawafikia kwa asilimia 100 ili waweze kutayarisha mashamba yao, kwa sababu wanategemea zinatolewa na Serikali tena kwa bure? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA KILIMO, MIFUGO NA UVUVI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijajibu maswali yake ningependa kusema kwamba zao la korosho ni moja kati ya mazao ambayo yamefanikiwa sana katika miaka ya karibuni. Mwaka huu korosho ndiyo imeongoza kwa kuiingizia nchi yetu fedha za kigeni kati ya mazao yote, imeipiku tumbaku. Vilevile katika msimu huu Serikali imefanikiwa kuwapatia wananchi wa mikoa inayolima korosho shilingi bilioni 800. Kwa hiyo, tunapozungumza korosho tunazungumza mafanikio makubwa sana ya Serikali ya Awamu ya Tano.
Mheshimiwa Mwenyekiti, na kuhusu utaratibu wa Stakabadhi Ghalani tunaelekea sasa kwenye mazao mengine hususan Kahawa, lakini vilevile na mazao ya jamii ya mikunde.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maswali yake, ni kweli kwamba kuna mapungufu yametokea ikiwa ni pamoja na mapunjo ya fedha za wakulima. Kama mnavyofahamu, tayari kuna watumishi wa MAMCU wamepelekwa mahakamani na kufunguliwa mashtaka ya kuhujumu uchumi. Vilevile katika fedha ambazo zimepotea tayari Serikali imesha- recover shilingi bilioni 1.5 na hizo zitaenda kwa wakulima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu pembejeo naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tani 9,000 za sulfur tayari zimeishaingia nchini na sulfur hiyo inagaiwa bure na iko njiani kuelekea kwenye mikoa inayolima korosho ili wananchi waweze kugawiwa, nashukuru sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Matatizo yaliyopo Uyui kwenye miradi inayosimamiwa na TASAF na TAMISEMI yanafanana kabisa na matatizo yaliyopo katika Jimbo la Ndanda hasa kwenye Kata ya Mwena.
Mheshimiwa Mwenyekit, kwenye hii TAMISEMI phase III ambayo imekuwa ikishirikisha wananchi. Kuna miradi pale ya mabomba ambayo Mheshimiwa Diwani kwa kushirikiana na watendaji wamekuwa hawatekelezi wajibu wao; kwa maana ya thamani ya pesa haionekani kwenye miradi. Sasa Mheshimiwa Waziri tunaomba atuleze badala ya kusubiri mpaka haya mambo yaharibike kabisa ndipo Wizara yake ikachukue hatua, je, hawaoni kuna haja ya kufuatilia utoaji na matumizi ya pesa ya TASAF katika maeneo mbalimbali kadiri siku zinavyokwenda?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme wazi kwamba jambo la kusimamia fedha (value for money) katika maeneo yetu naomba tulipe kipaumbele sana. Mheshimiwa Cecil nakumbuka tumetembelea mpaka kwenye bwawa lake pale chini. Kama fedha lakini usimamizi si mzuri na kama fedha imekwenda wengine wanatengeneza caucus kule kwa ajili ya kula ile fedha, jambo hilo halikubaliki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niwaombe Waheshimiwa Wabunge kwa sababu wao ni Wajumbe wa Kamati ya Fedha, wasikubali kupitisha mradi wa aina yoyote katika site na Majimbo yao ambayo wanaona katika njia moja au nyingine, mradi huu baadhi ya watu wanahujumu kwa makusudi. Tukifanya hivi ndipo tutalinda fedha hizo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, sasa naomba nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Masasi, kwamba aangalie kwanza nini kilichotokea katika mradi huo ambao tunasema kwamba lengo ni kuweza kuwasaidia wananchi halafu tupate taarifa. Nitaenda kufanya follow up ya haraka ili fedha zinapokwenda kule site lazima fedha zile ziweze kuleta matunda makubwa sana kwa manufaa ya wananchi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza linalohusiana na masuala ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la maji lililopo Songea linafanana kabisa na tatizo lililopo Wilayani Masasi hasa katika Vijiji vya Lukuledi, Chikunja, Maparagwe, Liputu, Mlingura pamoja na Namajani. Maeneo haya yote yanahudumiwa na mradi wa maji wa MANAWASA kutokea mradi wa Mbwinji ambao unapeleka maji mpaka Nachingwea. Tunataka kufahamu sasa kwa sababu tatizo kubwa ni miundombinu ya kusambaza maji haya kwa watumiaji. Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka pesa kwa ajili ya kununua vitendanifu kwa ajili ya kuunganisha maji katika maeneo niliyoyataja? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wiki mbili zilizopita nilienda Masasi mpaka mradi wa Mbwinji, Mamlaka ya Maji MANAWASA Mkurugenzi wake ameomba milioni 500 na tunampatia ili akamilishe kuunganisha vijiji vilivyobaki ambavyo viko pembezoni mwa bomba linalotoa maji Mbwinji kupeleka Masasi Mjini, lakini pia kwenda Nachingwea pamoja na vijiji kadhaa vya Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, kwa hiyo kote tunapeleka maji.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Kwanza ningependa kutambua kazi inayofanyika kwenye Kata ya Mwena, Chikundi pamoja na Chigugu ya kusambaza miundombinu kwa ajili ya maji na Mheshimiwa Waziri wa Maji ametoa ushirikiano mkubwa pale.
Mheshimiwa Naibu Spika, bwawa hili la Lukuledi tunalolitaja hapa sasa hivi kwa mara ya kwanza kabisa lilichimbwa mwaka 1955 lakini mpaka sasa hivi limekauka zaidi ya mara tano kwa sababu linategemea tu maji ya mvua kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya kuiongezea nguvu Mamlaka ya Maji Safi Masasi (MANAWASA) kwa kazi nzuri inayofanywa na Engineer David ili waweze kufikisha maji Kata ya Lukuledi na vijiji vyake vyote maji safi na salama badala ya kuendelea na huo mradi wa bwawa?
Swali la pili, pamoja na nia njema kabisa ya Serikali kutaka kuweka mabwawa kwenye maeneo waliyoyataja hapo ya Chingulungulu, Mihima pamoja na Mpanyani lakini tu niseme wanachokisema hapa sasa hivi, mwaka huu wametenga kazi ya usanifu.
Je, nini nia ya Serikali kuhakikisha wanawaondolea wananchi hawa taabu ya kupata maji kwa siku zijazo kwa sababu bajeti ya mwaka huu inaonesha tu ni kazi ya usanifu peke yake? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya kwanza ya swali lake ni kweli kwamba bwawa hili limekuwa linapata matatizo makubwa ya kukauka kwa sababu mbalimbali, lakini miongoni mwa sababu hizo ni kujaa mchanga na matatizo mengine yanayosababishwa na kutotunza mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, wazo lake kwamba tuwaambie MANAWASA wapeleke maji katika maeneo hayo badala ya kutegemea bwawa lile, naomba sana nimshauri tusubiri usanifu wa kina ukamilike, usanifu huo utatushauri kama chanzo hicho kitatosheleza mahitaji ya maeneo hayo na kama usanifu huo utashauri kwamba chanzo hicho hakitatosheleza basi tutaona njia nyingine ya kupata chanzo kingine ikiwemo hiyo ya kuchukua maji kutoka kwenye chanzo kilecha Mbwinji ambacho ndiyo kinategemewa na MANAWASA, kwa sasa hivi naomba sana tusimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tutachukua maji kutoka Mbwinji.
Mheshimiwa Naibu Spika, wito wangu kwenye sehemu hii ya swali la kwanza, ninamuomba sana usanifu utakapokamilika, kama utakaposhauri kwamba wananchi watunze mazingira na wengine watapisha katika eneo la mita 500 kutoka kwenye chanzo kwa ajili ya utunzaji wa mazingira ya bwawa basi naomba sana ashiriki kuwaelimisha wananchi wakubali hatua hizo.
Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili ya swali ameonesha wasiwasi kwamba mwaka huu tuna bajeti ya kufanya usanifu peke yake, ndiyo tumetenga shilingi milioni 60 ili tufanye usanifu wa kina na ukamilike na DDCA wamepewa hiyo kazi wakamilishe usanifu mwaka huu wa 2017/2018. Watakapotupatia gharama sasa hapo ndiyo tutapanga lini utekelezaji utaanza kwa kushirikiana na Wizara ya Maji.
Mheshimiwa Naibu Spika, namuondolea wasiwasi kwamba suala hili kwa sababu sasa limeletwa katika utaratibu wa vipaumbele, asiwe na wasiwasi awahakikishie wananchi kwamba tutatekeleza mradi huu ndani ya mwaka mmoja.(Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Naibu Spika, mazingira yaliyopo Jimbo la Nyang’hwale yanafanana kabisa na mazingira yaliyopo kwenye Jimbo la Ndanda na hasa kwenye Kata ya Chiwata ambapo kuna Shule ya Sekondari ya Chidya. Wananchi wa Chidya waliamua wenyewe kutumia nguvu zao kujenga jengo pale kwa ajili ya kuweza kupata zahanati. Kwa bahati mbaya kabisa, maelekezo niliyokuwa nawaambia, watakapokuwa wamefanikiwa kukamilisha boma, wawe wameendelea juu wameweka mpaka bati, Serikali itakuja kumalizia kuwaletea vifaa pamoja na kufungua.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri ya kututaka tusubiri, lakini napenda watu wale wasikie, Chidya ni sehemu ya mkakati wa hiyo mikakati yenu ya Wizara kukamilisha maboma hayo na lini hiyo kazi itafanyika? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni azma ya Serikali na pia ni azma ya CCM; ukisoma katika Ilani ya CCM ukurasa wa 81 Ibara ya 50 tumetaja kabisa kwamba kila sehemu ambayo ipo kijiji tutahakikisha kwamba inajengwa zahanati, kila Kata itakuwepo na Kituo cha Afya na kila Wilaya itakuwa na Hospitali ya Wilaya. Kwa hiyo, ni azma thabiti na ndiyo maana imeandikwa. Naomba nimweleze Mheshimiwa Mbunge avute subira.
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mbunge amesema kwamba wananchi wake kama ilivyo Nyang’hwale wamejitolea, lakini sina uhakika kama naye Mheshimiwa Mbunge amefanya kazi nzuri kama Mbunge wa Nyang’hwale. Na yeye tumtake ashirikiane na Serikali, kwani wanaotibiwa ni wananchi wetu. Kwa hiyo, ni vizuri wote tukashiriki katika suala zima la kuhakikisha kwamba afya inakuwa bora. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na majibu yaliyotolewa na Mheshimiwa Waziri, tunafahamu kwamba swali hili limekaa muda mrefu kwa sababu hizi barabara zinafahamika kwamba zimekamilika kwa kiasi fulani kwa sasa hivi. Kuna barabara za muhimu ili kuweza kukamlisha matumizi na kupunguza foleni kwa wakazi wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Kibamba inayoanzia Mbezi Mwisho - Mbezi Sekondari inayokwenda kuunganisha Bunju pamoja na Kibaha. Barabara hii mnategemea kuikamilisha lini?
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hizo barabara nilizozitaja, kuna wananchi wa maeneo hayo walibomolewa nyumba zao, wengine wamewekewa ‘X’ nyekundu wanakaa pale bila kuwa na amani kwa sababu hawajui lini wataondolewa; je, ni lini Serikali imepanga kulipa fidia ili kuweza kupisha wananchi wale, waendelee na kazi nyingine za maisha? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKA): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kwanza napenda nimfahamishe tu Mheshimiwa Mbunge kwamba upande wa Serikali tumejipanga vizuri kupunguza au kupambana na suala la msongamano wa magari. Kwa ujumla wake, zipo barabara zenye urefu wa zaidi ya kilometa 124 ambazo tunaendelea kuzishughulikia ili kuhakikisha kwamba msongamano unapungua na hatimaye unaweza kwisha kabisa.
Mheshimiwa Naibu Spika, swali lake la nyongeza, anataka kujua, lini hii barabara ya Mbezi – Kibamba itakamilika? Kubwa alilotaka kujua ni kama kuna compensation. Niseme tu kwamba kwa wale ambao wanastahili kulipwa fidia watalipwa baada ya fedha kuwa zimepatikana. Kwa hiyo, utaratibu unaendelea kwa wale wanaostahili. Niseme tu kwamba kwa upande wa Kibamba zipo barabara nyingi ambazo tunaendelea kuhakikisha kwamba tunasaidia kupunguza msongamano.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, iko barabara ambayo inatoka Kibamba kwenda Kisopwa kilometa 12. Kilometa nne kutoka Kibamba kwenda Mloganzila imeshakamilika kwa kiwango cha lami. Kwa hiyo, nimhakikishie tu Mheshimiwa Mbunge pamoja na wananchi wa Kibamba, Serikali imejipanga vizuri kwa ajili ya kufanya marekebisho ya hizi barabara ili ziweze kupitika kiurahisi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama Mheshimiwa Mbunge atapenda kujua maelezo ya ziada, ipo mipango mingi na barabara zipo nyingi, naomba tu tuonane ili wakati mwingine aweze kupata kwa undani kwamba ni barabara kiasi gani ambacho kinakwenda kutengenezwa upande wa Kibamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, nimhakikishie kwamba kwa barabara hizi za kupunguza msongamano upande wa Kibamba tunazo barabara nyingi sana ukilinganisha na maeneo mengine kutokana na umuhimu wake.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali lanyongeza kutokana na swali namba 101 la Mheshimiwa bwana Jerome Bwanausi. Kwa muda mrefu pia Serikali imekuwa ikiwakopa wazabuni na kusababisha madeni makubwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo Chuo cha Wauguzi Masasi, Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Masasi, Ndanda High School pamoja na Chidia Sekondari yanayotisha wazabuni hawa kufilisika lakini pia…
…wanataka kusitisha kutoa huduma zao; sasa swali langu, ni lini Serikali kwa makusudi kabisa itaamua kuwalipa wazabuni wa ndani hasa wa vyakula katika hizi shule zetu za mabweni?
NAIBU WAZIRI ELIMU SAYANSI NA TEKNOLOJIA:
Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kwamba swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe halina uhusiano wowote na swali la msingi, lakini nipende tu kusema kwamba kwa sasa Serikali imejidhatiti vilevile kuhakikisha kwamba inalipa madeni yote ikiwa ni pamoja na madeni ya wazabuni. Hata hivyo, ifahamike kwamba madeni yote yatalipwa tu baada ya uhakiki kufanyika, kwa sababu huko nyuma kuna madeni mengi yamelipwa lakini hayakustahili kulipwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kutoka kwenye swali namba 273 la msingi ambalo liliulizwa na Mheshimiwa Lathifah Chande.
Mheshimiwa Spika, tunafahamu kabisa nia ya Serikali ya kutaka kuwa na viwanda kwenye maeneo mengi na kwamba mikoa ya Kusini Mtwara na Lindi kimkakati kabisa miaka ya 1970 tayari tulikuwa na viwanda vingi tu vya korosho Masasi ukienda Lindi, ukienda Nachingwea na maeneo mengi tu.
Sasa swali, mara nyingi tumekuwa tukiwasiliana na Waziri anatueleza kwamba kuna kesi mbalimbali mahakamani ambazo zinasababisha viwanda vile visiendelezwe, lakini wamiliki waliouziwa vile viwanda sasa hivi wanavitumia kama maghala. Wakati Serikali inasubiri hizi kesi ziishe Mahakamani wengine wanapata faida kwenye maeneo hayo hayo.
Sasa swali langu, kwa nini wasiwasimamishe watu wale kutumia viwanda hivi kama maghala kwa sababu wanajipatia pesa na Serikali haipati faida yoyote?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Spika, kimsingi nchi yetu inatekeleza shughuli zake kwa mujibu wa sheria lakini vilevile tusingependa kuona sheria zikatumike kama kichaka cha kuwanufaisha watu wachache. Tumeshafanya hivyo katika mashamba ya mpira Kihui ambapo mtu alikuwa na kesi, akasingizia kesi yeye akawa anaendelea kuvuna, tukafanya jitihada ameondoka. Kwa hiyo, hata hayo tutayafuatilia na ushauri wako tutauzingatia.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Serikali ya Awamu ya Tano imejinasibu kwamba ni Serikali ya viwanda na tunataka kuhakikisha tutakapofikia mwaka 2025 tuwe kwenye nchi ya kipato cha kati. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Waziri; tulipofanya vikao vya Kamati alikuwa anatueleza kwamba maghala ya korosho yaliyopo Masasi yamegeuzwa, tunafahamu, kufanywa maghala badala ya viwanda na kwamba kuna kesi zilizoko mahakamani kwa sababu ya kutanzua migogoro iliyoko pale.
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu ni kwamba, mpaka sasa hivi wamefikia hatua gani ya kesi hizi zilizoko mahakamani ili kuhakikisha viwanda vile vinafufuliwa badala ya kuendelea kutumika kama maghala na wale watu waliovinunua wakati huo? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA, BIASHARA NA UWEKEZAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwanza katika majibu yangu ya hapo awali niliahidi kutembelea eneo hilo, nasikitika kuliarifu Bunge kwamba sikuweza kutembelea. Hata hivyo, kama ambavyo nimekuwa nikizungumza siku zote, Wizara kwa kushirikiana pia na Kamati yetu ya Viwanda, Biashara na Mazingira tupo katika kuendelea kuhakikisha kuona kwamba wawekezaji wanatimiza wajibu wao, lakini pia kuhakikisha maeneo yote ambayo yanalima korosho basi korosho hiyo iweze kubanguliwa au kuongezwa thamani kabla ya kusafirishwa. Kwa hiyo tupo katika mchakato na mchakato wa kisheria kawaida huwa hatuuingilii.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kadri ya swali namba 65 linaelezea zaidi kuhusu kutelekeza watoto na familia zao, kwa maana ya matunzo na hili jambo linakwenda sambamba kabisa na masuala ya uzazi wa mpango. Jana tulishuhudia Mheshimiwa Rais kwenye mkutano wake akisema kwamba Watanzania ambao tumeshiba tunaweza tukazaa kadri tunavyotaka bila kuwa na mipaka.
Sasa swali langu ni kwamba je, Serikali imeamua kubadilisha sera yake ya uzazi wa mpango kutokana na kauli iliyotolewa jana na Mheshimiwa Rais? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Spika, Serikali ina Sera ya Uzazi wa Mpango na Sera yetu inasema kwamba hatujaweka kikomo cha idadi ya watoto ambayo familia inapaswa kuzaa. Sera yetu inasema mtu apate idadi ya watoto ambao anamudu kuwatunza na kuwapa nafasi kati ya mtoto mmoja mpaka mwingine. Huo ndio mwelekeo wetu wa sera na Mheshimiwa Rais hajatoka sana katika nje ya sera. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.
Mheshimiwa Spika, kwanza nianze tu kuweka taarifa sahihi kadri ya majibu ya Mheshimiwa Waziri hapa, kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ina Vituo vya Afya vinne tu ambapo viwili ni vya Serikali na viwili ni vya mission ya Wakatoliki vikiwemo Kituo cha Namombwe na Lukuledi na siyo vituo 33.
Mheshimiwa Spika, suala la gari la wagonjwa la Kituo cha Afya cha Chiwale ambalo liliungua moto mwaka 2010, wananchi waliunguza moto pale na walioliunguza moto gari hilo siyo wananchi wote wa Chiwale isipokuwa ni watu wachache ambao hawakuwa na nia njema wakati huo, lakini Serikali inaonekana kwamba imekuwa ikitumia jambo hili kama adhabu kwa ajili ya watu wa Chiwale.
Mheshimiwa Spika, sasa nataka kupata kauli ya Serikali na tunafahamu kabisa kwamba mapato ya Halmashauri sasa hivi yamechukuliwa na Serikali Kuu, kwa hiyo, isingekuwa rahisi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kuanza kutenga pesa ukizingatia pia ahadi ya Waziri Mkuu wakati tunafanya uzinduzi wa wodi ya akina mama kwenye Hospitali ya Chiwale…
Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, Serikali, pamoja na hili inalolieleza, vipi, inaweza kutekeleza ile ahadi ya Waziri Mkuu ya kuweza kuleta gari kwenye zahanati ya Chiwale?
Mheshimiwa Spika, swali la pili, kama utakumbuka mwaka 2017 kwenye bajeti iliyopita, Serikali ilitenga shilingi milioni 70 kutoka kwenye basket fund kwa ajili ya kudhamini ujenzi wa Kituo cha Afya cha Lukuledi ambapo mpaka sasa hivi naongea hapa, wananchi wako pale wakijitolea pamoja na nguvu ya Ofisi ya Mfuko wa Mbunge. Sasa swali langu ni je, ni lini ahadi ya shilingi milioni 70 ya basket fund itapelekwa Lukuledi kwa ajili ya kuwasaidia na kuwaunga mkono wananchi wale? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Spika, katika majibu yangu ya msingi nimesema kuna vituo vya kutolea huduma za afya vitatu, sijasema vituo vya afya. Kwa hiyo, nilikuwa niko sahihi katika jibu nililokuwa nimetoa.
Mheshimiwa Spika, katika maswali yake mawili, kwanza anasema Halmashauri yake haina uwezo wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua ambulance ambapo lengo la fedha hizo ni kwa ajili ya kusaidia wananchi wanaohitaji huduma ya afya.
Mheshimiwa Spika, ni jana tu nilikuwa naongea na Mkurugenzi wa Halmashauri; uwezo wa Halmashauri wanakusanya jumla ya shilingi bilioni 2.7. Nia ya dhati ikiwepo wakati inasubiriwa ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, kutenga pesa kwa ajili ya kununua gari kwa ajili ya wagonjwa kutoka kwenye shilingi bilioni 2.7 inawezekana kabisa.
Mheshimiwa Spika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu itatekelezwa kwa kadri pesa zitakavyopatikana, lakini siyo vibaya kama wakatenga kutoka kwenye bilioni 2.7 kwa ajili ya ambulance.
Mheshimiwa Spika, katika swali lake la pili, anasema kwamba walishaanza ujenzi na tayari kuna ahadi ya shilingi milioni 70 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa zahanati au kituo cha afya.
Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge; ni azma ya Serikali inayoongozwa na CCM kuhakikisha kwamba huduma za afya zinaboreshwa na kusogezwa kwa wananchi. Kwa hiyo, avute subira. Azma yetu ndani ya miaka mitano ambayo ndiyo ahadi yetu na sisi kwa wananchi, tutatekeleza.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo lililoko Kigoma Kusini linafanana kabisa na tatizo lililoko kwenye Jimbo la Ndanda hasa maeneo ya Namajani na Mahinga ambako mipaka kati ya Jeshi la Magereza pamoja na wananchi haieleweki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna tatizo kama hilo kwenye Kata ya Chingulungulu, Kijiji cha Misenjesi kati ya Hifadhi ya Taifa pamoja na wananchi. Sasa nataka kufahamu, ni lini Serikali itakwenda kutoa ufafanuzi mzuri na kuweka mipaka hii sahihi kati ya Mbuga ya Misenjesi na wanakijiji wa Kijiji cha Chingulungulu kwa sababu pametokea matatizo makubwa ya kutoelewana maeneo hayo? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba kama nilivyosema kwenye nchi nzima kuna maeneo ambayo yana matatizo ya mipaka na kama alivyosema mwenyewe kwenye Jimbo lake kuna maeneo hayo. Nataka nimhakikishie tu kwamba, tuko tayari sasa hivi, tunapitia mipaka yote nchi nzima na tutakwenda huko pia kuangalia huo mpaka ili tuone kwamba ni nani ameingia nani hajaingia kusudi tuweze kurekebisha matatizo hayo na migogoro yote iweze kumalizika, hiyo tutaifanya karibu nchi nzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Mbunge awe na uvumilivu kidogo, baadaye tatizo lake hilo litamalizika. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kutokana na swali namba 424.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri Mkuu alikuja Kijiji cha Chiwale na tulifanya pale uzinduzi wa jengo la mama na mtoto, lakini hata hivyo, Kituo cha Afya cha Chiwale tulipewa ahadi ya gari ambayo hatujajua itatekelezwa lini na sasa hivi kile kituo kimekuwa kikubwa na kinahudumia watu wengi sana wa kata zile kwa sababu Jimbo la Ndanda lina Kituo cha Afya kimoja tu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kufahamu kutoka kwa Mheshimiwa Waziri: Je, ni nini mpango wao wa kuweza kutusaidia pale kuweza kupata angalau mobile x- ray ili kuwasaidia watu wa jirani? Kwa sababu kwenye Kata zote 16 tuna kituo cha afya kimoja tu, kwa hiyo, ni safari ndefu sana kutoka Chiwale kwenda Masasi kwa ajili ya kwenda kupata huduma za afya kwenye Hospitali ya Wilaya ilipo sasa hivi na wenyewe x-ray yao ni mbovu. (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPH G. KAKUNDA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mwambe amezungumza mambo mawili ndani ya swali moja; amezungumzia ahadi ya gari la wagonjwa; nimwambie kwamba tuendelee na mawasiliano ya karibu ili kusudi hiyo ahadi iweze kutekelezwa, kwa sababu nia ya Serikali ni kutekeleza ahadi zake.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili hili la x-ray, na mimi nimwombe sana kwamba pamoja na kuweka kipaumbele cha Halmashauri kwenye bajeti zake kwa mwaka ujao wa fedha katika fedha za ruzuku ambazo mwaka ujao zitapatikana mapema zaidi, kama zisipotosha, basi naomba tuwe na mawasiliano ya karibu na ofisi yetu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Ndanda limegawanyika katika maeneo matatu ya mtandao wa maji. Kuna upande wa Mashariki ambao unaanzia Kata ya Nanganga mpaka Chikukwe kwenyewe kuna mradi mkubwa wa maji unafanyika pale. Kata ya Magharibi kwenye Vijiji vya Chingulungulu…
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, sasa hivi Serikali imeanzisha utaratibu wa kuchimba mabwawa kwa ajili ya maji na kuendeleza mabwawa ya zamani ikiwepo bwawa lililoko Kata ya Lukuledi. Nataka kufahamu kutoka kwa Waziri kwa sababu maji safi na salama yanayotokea bomba la Mbwinji yamefika mpaka Kata ya Chikunje ambapo ni kilomita 10 tu kufika kwenye Kata ya Lukuledi. Je, Serikali haioni haja ya kuendeleza mradi huu wa maji badala ya kwenda kuendeleza lile bwawa ambalo halina chanzo cha uhakika cha maji zaidi ya maji ya mvua?
NAIBU WAZIRI WA WIZARA YA MAJI NA UMWAGILIAJI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu lengo lake ni kuhakikisha wananchi wanapata maji. Kwa ushauri wa Mheshimiwa Mbunge kama kuna chanzo cha uhakika, tunaweza kuweka utaratibu kuhakikisha wananchi wako wanapata maji safi, salama na yenye kuwatosheleza.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kuniona.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda Mheshimiwa Naibu Waziri pia atueleze, kwa sababu wakati alipokuja Mtwara alipita pia kukagua barabara ya Umoja, hii inayoanzia Mtwara – Newala mpaka Masasi lakini pia inayokwenda mpaka Nachingwea. Wakati wa kampeni Mheshimiwa Rais aliahidi kwamba barabara ile itajengwa kwa mara moja na wataweka pale wakandarasi wanne ili kuweza kufanya barabara hiyo ijengwe kwa haraka zaidi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kufahamu, ni lini hasa barabara inayotokea Masasi - Nachingwea - Lukuledi - Chikunja - Ndomoni - Nachingwea, itaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama ambavyo iliahidiwa? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA):
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nimetembelea Mtwara na Lindi na nimeona harakati za ujenzi. Kwanza kwa ufupi tu ni kwamba maeneo yote yaliyokuwa na shida kubwa ujenzi unaendelea. Ukiangalia kwenye bajeti hii pia tuliyopitisha tumeweka fedha za kutosha kukamilisha daraja katika Mto Lukuledi kwa sababu eneo hili lilikuwa ni hatari, wananchi walikuwa wanapita kwenye maji na walikuwa na hatari ya kuliwa na mamba. Kwa hiyo, tumeweka fedha za ujenzi pale na tunaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kifupi kwa barabara hii ambayo ameitaja ili kuwa na Lot 4 kama alivyosema kuharakisha ujenzi ule, utaratibu unaendelea vizuri kwa sababu tunatafuta fedha. Wakati tunafanya juhudi za kupata fedha za kutosha ziko fedha ambazo zimetengwa wakati wowote tutaweza kutangaza ili kuweza kuanza ujenzi huu. Kwa hiyo, nimpongeze sana, tuendelee kuwasiliana, nami nitapita pia wakati mwingine nione harakati hizi zikiendelea. Nimeona barabara hii ni muhimu sana inawaacha watu wengi walioko kule Liwale kwani tukikamilisha eneo hili tunaweza kwenda tena kilometa 129 kutoka Nachingwea kwenda Liwale ambayo sasa tumeiweka kwenye hatua ya usanifu ili wananchi wa maeneo yale waweze kunufaika na barabara hii itakapokuwa imejengwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Ukizunguka Tanzania nzima kwenye vituo vya polisi vyote utakuta magari mengi sana mabovu ambayo ni ya polisi wenyewe kwa maana ya kwamba ni ya Serikali hayajatengenezwa na hayafai tena kutengenezwa yanavyoonekana mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo ukija Jimbo la Ndanda, Kituo cha Polisi cha Ndanda ambacho kinahudumia jimbo zima na tuna kituo kimoja tu cha polisi hivi karibuni tuliletewa gari ambalo nalo linaonekana ni bovu kwa sababu toka limefika halijawahi kutumika. Sasa nataka Waziri atuambie ni lini mahususi kabisa wataamua kutengeneza gari la Kituo cha Polisi cha Ndanda kwa ajili ya kuweza kutoa huduma maeneo ya Jimbo la Ndanda ambayo yanasaidia pia na Jimbo la Ruangwa.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI:
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nizungumze kwa ujumla kwamba, tunakiri juu ya uwepo wa baadhi ya magari chakavu katika maeneo mbalimbali nchini. Hata hivyo, nataka nimthibitishie Mheshimiwa Mbunge na Wabunge wengine wote waliopo humu ndani na wananchi kwa ujumla kwamba tuna jitihada mbalimbali zinafanyika. Nyingine zinafanyika katika mikoa lakini nyingine zinafanyika katika ngazi ya Kitaifa kuhakikisha kwamba magari haya yanakuwa katika hali nzuri. Magari mengi tu ambayo yapo katika maeneo mbalimbali nchini tumeanza kuyafufua yanatumika, yale ambayo yanawezekana kufufulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hili suala la gari hii ya Ndanda specifically kwanza nataka nilichukue hili suala kwa sababu ni jambo ambalo haliingii akilini kwamba gari inapelekwa katika kituo na wakati huo gari haijaanza kutumika inakuwa mbovu. Kwa hiyo, nijue kwanza gari hii ilitoka wapi na kwa nini iwe haitumiki? Halafu tuangalie sasa baada ya hapo nini kifanyike ili kuweza kurekebisha.
MHE. CECIL M. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kufahamu kutoka Serikalini kwamba barabara ya Masasi inayopitia Vijiji vya Nangaya – Chikunja – Lukuledi – Naipanga – Mkotokuyana mpaka Nanganga inaelekea kujengwa kwa lami hivi karibuni. Hata hivyo, uthamini wa mali na rasilimali za watu katika maeneo hayo yote niliyoyataja umefanyika zaidi ya miaka mitano iliyopita. Je, Serikali itakwenda kurudia kufanya uthamini au itawalipa watu wale fidia zao kutokana na uthamini uliofanyika miaka mitano iliyopita? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo:-
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimfahamishe tu Mheshimiwa Mwambe pamoja na wananchi kwamba uthamini uliofanyika kama hakuna matatizo makubwa ya kurudia, ndiyo utakaotumika kulipa wananchi hawa. Niwafahamishe tu wananchi kwa ujumla kwamba utaratibu uliopo kuna namna ya kuangalia thamani ya fedha kwa sasa, lakini base itakayotumika ni ule uthamini uliofanyika kipindi ambacho Mheshimiwa Mbunge amekitaja. Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge asiwe na wasiwasi, uko utaratibu mzuri wa kuhakikisha kwamba fedha zile zitalipwa kulingana na hali ya sasa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi kwa ajili ya kuuliza swali kwenye Wizara hii. Mheshimiwa Naibu Waziri atakumbuka wakati wa ziara ya Waziri Mkuu Jimbo la Ndanda kwa maana ya Mkoa wa Mtwara alitembelea Kituo cha Afya cha Chiwale ambacho alikizindua siku ile.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na yote, Kituo cha Afya cha Chiwale kina uhaba mkubwa sana wa watumishi na barua tulishaipeleka toka mwezi wa Tatu kwa Waziri wa Utumishi, Mheshimiwa Mkuchika, nafikiri kwa kushirikiana na idara yake na Mheshimiwa Waziri Mkuu alisema, pamoja na kufungua kituo kile cha afya mara moja atahakikisha watumishi wameletwa pale kwa ajili ya kupunguza tatizo lililoko pale. Je, ni lini sasa Wizara itapeleka hao watumishi Kituo cha Afya cha Chiwale?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kwamba kuna suala zima la upungufu wa watumishi kwa upande wa afya na hivi karibuni Ofisi ya Rais, TAMISEMI imetangaza nafasi kwa ajili ya kuajiri watumishi wa afya ili kujaribu kupunguza pengo hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge mchakato uko kwenye hatua za mwisho kabisa, haitapita mwezi kazi hii itakuwa imeshakamilika. Namwomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge katika maeneo ambayo kuna upungufu mkubwa tutazingatia kuhakikisha kwamba watumishi wanapalekwa ikiwa ni pamoja na kituo chake cha afya.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza ambalo linaelekezwa kwenye Wizara ya Madini.
Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Naibu Waziri mtakumbuka kwamba miaka ya karibuni pamefanyika ugunduzi wa madini ya aina ya graphite kwenye Wilaya ya Masasi, Kijiji cha Chiwata, Kata ya Chiwata, vile vile Wilaya ya Ruangwa na vijiji vyake; ikiwemo baadhi ya maeneo ya Jimbo la Mtama.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa swali langu, Kampuni ya Nachi Resources ndiyo ambao ilionesha nia ya kutaka kuwekeza, lakini mawasiliano ya mwisho tuliyoyafanya na wao yalionyesha kwamba hawawezi kuwekeza kwenye hayo maeneo kwa sababu pamekuwa na ucheleweshaji wa upatikanaji wa ripoti ya environmental assessment. Sasa Mheshimiwa Waziri, haoni haja ya kuwasaidia Nachi ili kuweza kukamilisha huu utaratibu ili waweze kuchimba hayo madini?
NAIBU WAZIRI WA MADINI (MHE. STANSLAUS H. NYONGO) Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli Nachi Resources ni kwamba wanasubiri kupata ripoti kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ambayo iko chini ya Mheshimiwa Makamu wa Rais. Sisi hatuna shida kwa upande wa Wizara ya Madini, ni kwamba wale tunaendelea kuwasaidia ili waweze kuwekeza, kwa sababu tunafahamu uchimbaji wa graphite sasa hivi duniani ndiyo unahitajika kwa sababu madini ya graphite sasa hivi ndiyo yanayohitajika zaidi duniani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi kama Wizara ya Madini tunashirikiana nao kuhakikisha kwamba baada ya muda waweze kuanza kuwekeza na kuanza kuchimba. Kwa hiyo, nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba tunashirikiana nao na tunaendelea kuwasiliana na Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) ili iwawezeshe kupata environment impact assessment report ili kusudi waweze kuwekeza na waweze kuendeleza shughuli zao za uchimbaji kama kawaida. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Swali la kwanza, ukiangalia majibu ya Mheshimiwa Waziri anasema kwamba baada ya kukamilika barabara ya Kinyerezi - Mbezi ndipo wanapotegemea kuanza ujenzi wa barabara hii inayoongelewa hapa na Mheshimiwa Kubenea.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimkumbushe Mheshimiwa Waziri kwamba hizi ni barabara mbili tofauti na mahitaji ya wananchi wale ni tofauti. Tunataka kufahamu ni lini Serikali specifically itaanza ujenzi wa barabara inayotajwa iliyoahidiwa miaka mitano iliyopita? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, suala lililopo Jimbo la Ubungo linafanana moja kwa moja na masuala yaliyopo katika Jimbo la Ndanda, Mkoa wa Mtwara kwamba Serikali iliahidi kujenga kwa kiwango cha lami barabara inayoanzia Mtwara Mjini – Nanyamba – Tandahimba – Newala - Masasi mpaka Nachingwea kuja kutokea Nanganga. Sasa tunataka kufahamu pamoja na mkandarasi kuwepo pale ambaye anasuasua kwenye kazi hii, ni lini Serikali specifically itaanza ujenzi wa barabara inayotokea Masasi kwenda Nachingwea kuja kutokea Nanganga?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO (MHE. ELIAS J. KWANDIKWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba katika barabara ambazo nimezitaja awali ndiyo zilikuwa na matatizo makubwa na ndiyo zilikuwa kipaumbele. Niseme tu kwamba nafahamu maeneo haya ambayo Mheshimiwa Mbunge anayazungumzia ni korofi na kama nilivyosema tutaendelea kuyashughulikia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, yako maeneo matatu ambayo tulikuwa tunaendelea nayo kuhakikisha kwamba barabara hii inatoa huduma iliyokusudiwa wakati sasa tukikamilisha hii barabara ni fursa tosha kuja kuijenga barabara hii. Yako maeneo pale Kwa Bichwa, Kwa Mahita na eneo la Makange Sekondari ndiyo zilikuwa sehemu korofi. Alikuwepo mkandarasi anaendelea kurekebisha maeneo yale lakini kutokana na mvua nyingi zilizonyesha amesimama kidogo ili hali ya hewa ikiwa nzuri hii barabara tuiimarishe halafu baadaye sasa wakati barabara hizi zinakamilika ni fursa tosha kuja kuijenga hii barabara kama ahadi ilivyokuwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Ndanda kuja Nachingwea kupitia Nanganga kama tulivyoizungumza katika bajeti tumetenga fedha kwa ajili ya kutengeneza kipande hiki kutoka Nachingwea - Nanganga na Nachingwea – Ruangwa – Nanganga. Mheshimiwa Mbunge anafahamu pia liko daraja katika Mto Lukuledi tunaendelea kulijenga na hii ni sehemu ya kukamilisha barabara hii anayoitaja ili sasa tuweze kuunganisha kwa kiwango cha lami.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimsihi tu Mheshimiwa Mbunge avute subira na wananchi wa Ndanda wategemee kwamba barabara hii tunaenda kuikamilisha ili waendelee kupata huduma kama wananchi wengine katika maeneo ya Tanzania.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Swali la kwanza wakati Mheshimiwa Rais anasema kwamba Serikali itanunua korosho yote kutoka kwa wakulima na aliwatangizia wakulima wote wa Watanzania kwamba korosho kilo moja itanunuliwa Sh.3,300 kwa maana ya kutaka kuwasaidia wakulima wanyonge. Pia hivi karibuni tumeshuhudia Serikali hiyo hiyo inawalipa wakulima chini ya bei ya Sh.3,300 maeneo mengine Sh.2,600 na maeneo mengine chini hapo ikiwemo Mikoa ya Pwani, Mtwara pamoja na Lindi. Sasa nataka kufahamu kauli ya Serikali, Mheshimiwa Waziri hapa atuambie, je, ni kwa nini wanakiuka maagizo yaliyotolewa na Mheshimiwa Rais kwa ajili ya kuwalipa wakulima hao korosho zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwenye majibu ya msingi ya swali (a) anaongelea suala la Bodi ya Mazao Mchanganyiko na kwamba ni ya wao kukusanya korosho ni pamoja na kuzuia biashara ya kangomba, lakini hapa kwenye majibu yake na tumeona karibuni kampuni ya INDO, kutoka Nairobi imepewa kazi ya kuuza korosho kwa niaba ya Serikali. Sasa nataka anitofautishie kangomba hii inayofanywa na Serikali kupitia INDO pamoja na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kwa sababu wamesema wanaziuza korosho zile kwa faida, kuna tofauti gani na wale kangomba wadogo wadogo waliokuwa wanakusanya korosho kwa wakulima na kuzipelekwa kwenye Vyama vya Msingi?
NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii, kwa niaba ya Waziri wa Kilimo ningependa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli, Serikali kupitia Mheshimiwa Rais aliutangazia umma wa Tanzania na ulimwengu kwamba korosho mwaka huu 2019 tutanunua kwa Sh.3,300 na ni kweli sasa tunanunua na tunalipa hivyo kwa korosho daraja la kwanza.

Mheshimiwa Spika, niendelee kuongeza jibu hilo Mheshimiwa Mwambe anafahamu, tunapozungumza korosho ina madaraja mawili makubwa; daraja la kwanza yaani standard grade na daraja la pili maana yake under grade, Mheshimiwa Rais alipokuwa anazungumza tunakwenda kununua korosho kwa Sh.3,300 maana yake ni kuhamasisha ubora katika nchi hii, kwamba hiyo ni bei ya daraja la kwanza. Kwa hiyo inafahamika kisheria na kikanuni mahali popote pale.

Mheshimiwa Spika, korosho daraja ya pili bei yake ni asimilia 80 ya bei ya daraja la kwanza. Ndiyo maana nilikwishawatangazia wakulima na wanafahamu wenyewe, daraja la pili litanunuliwa kwa asilimia 80 ya bei ya daraja la kwanza, maana yake inakwenda kununuliwa kwa Sh.2,640 na korosho hapo hapo ikizidi chini ya daraja la pili, haitanunuliwa, atarudishiwa mkulima akaichague ili ailete ama iwe daraja la pili au daraja la kwanza.

Mheshimiwa Spika, tulipomaanisha tunanunua korosho hatumaanishi tunanunua mpaka vigawe au mawe, mnafahamu mwaka jana 2019 nchi hii iliharibika duniani kwa kupata sifa potofu na mbovu, tumepeleka matofali badala ya korosho kwenye soko la kimataifa. Kama Serikali hatuwezi kurudia hilo na mtu yeyote hawezi kuchafua jina la nchi yetu na kuharibu ubora wa korosho yetu ikakosa soko katika soko la kimataifa.

Mheshimiwa Spika, swali la pili anataka kufahamu kati ya kampuni iliyonunua korosho kutoka Bodi ya Nafaka ya Mazao mchanganyiko na kangomba. Kwanza Mheshimiwa kuna mambo ya msingi tuyaweke kwenye mambo ya msingi kama nchi, siyo kila jambo linahitaji siasa, korosho ni uchumi, nilitarajia Waheshimiwa Wabunge tuwe pamoja katika hili kwa nia nzuri ya Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli alipoamua kununua korosho hizi kwa bei ya Sh.3,300 badala ya ile wakulima walikuwa wanakwenda kulipwa Sh.2,700 ambayo wameikataa wakulima wenyewe.

Mheshimiwa Spika, sisi kama Serikali tusingeweza kukaa kuona wakulima wanagoma, bei ni ndogo hailipi gharama zao, Serikali ndiyo imechukua jukumu hilo kuhakikisha kwamba tunanunua kwa Sh.3,300. Leo tunapopata wanunuzi ambao wananunua zaidi hilo, siyo kubeza, mlipaswa kupongeza la sivyo sasa hivi wakulima wote wangelipwa Sh.2,700.

Mheshimiwa Spika, anasema tofauti ni nini, katika biashara ya korosho kuna watu kwenye mnyororo wa thamani kuanzia mzalishaji, kuna mawakala, kuna madalali, kuna wafanyabiashara wadogo na kuna wanunuzi wakubwa, tofauti kati ya kangomba na yule, yule ni mnunuzi, hizi korosho tumezinunua au kuzikusanya kwa mkulima siyo kuzila ila kuziuza.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo yule ni mnunuzi kwenye soko la kimataifa, tofauti ya yule na kangomba, yule ananunua kwenye mfumo rasmi unaotambulika kisheria. Kangomba ni watu ambao wananunua korosho kinyume cha sharia. Kama tunavyofahamu korosho ni moja ya zao la kimkakati ambalo tumeliweka ununuzi wake kwenye mfumo rasmi tunanunua na tunakusanya kwenye mfumo wa stakabadhi ghalani na kwa maana hiyo haruhusiwi mtu yoyote kwenda kununua ila ni Vyama vya Msingi na Ushirika..

SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri ameelewa, yanatosha usiongeze, Mheshimiwa Naibu Waziri inatosha…

NAIBU WAZIRI KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba niongezee kidogo…

SPIKA: Inatosha kabisa.

NAIBU WAZIRI KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kwa niaba ya akina mama wote wa Tanzania, napenda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze waziwazi, nafahamu wazi kabisa huduma ya bure iliyokuwa inatolewa kwa mama na mtoto kupitia Huduma ya Tumaini la Mama imefutwa na kwamba hakuna mzazi yeyote anayeandikishwa sasa hivi kuanzia tarehe 31 Desemba.

MWENYEKITI: Swali.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu, ni nini tamko la Serikali kutokana na jambo hili kwa sababu hailijatangaza waziwazi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Cecil Mwambe kwa swali nzuri kwa niaba ya wanawake wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi kama Serikali tunakiri kwamba huu utaratibu wa Tumaini la Mama ulikuwa na mchango mkubwa sana katika afya ya uzazi katika Mikoa ya Kusini. Mkataba ule umekwisha na sisi ndani ya Serikali bado tunaendelea kuufanyia kazi pamoja na Wizara ya Fedha. Taratibu zitakapokamilika tutatoa taarifa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Msingi wa swali langu uko kwenye swali namba 170, kipengele (b) kuhusiana na suala la bei ya mazao kwamba imekuwa ni holela.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda sasa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara itueleze, kwa sababu watu wa Wizara ya Kilimo wanasema wao walishamaliza kazi ya kukusanya, je, korosho ghafi na korosho iliyobanguliwa mnaiuza kwa shilingi ngapi?
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi baada ya Serikali kufanya uamuzi wenye hekima kabisa wa kununua korosho kwa hawa wananchi ili kuwapunguzia maumivu ya kuuza kwa bei mbaya, korosho iliyopo sasa hivi tunaendelea kuiuza na hatujapanga bei maalum, inategemeana na mteja anavyokuja na pale itapofikia sisi kuwa imelipa gharama zetu zile ambazo tulitumia. Kwa misingi hiyo, nikuombe Mheshimiwa Mwambe ukiwa pia ni mdau na mwananchi mwingine yeyote anayenisikia hata watu wa nje korosho ghafi zipo na zilizobanguliwa zaidi ya tani 391 zipo na ziko katika hali nzuri basi yeyote anayetaka kununua karibu sana aweze kuuziwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Kilimo. Serikali kupitia Wizara ya Kilimo mwaka juzi walianzisha utaratibu wa kwamba zao la korosho lilimwe katika kila mkoa hapa Tanzania kwenye mikoa 17. Wakati wa uhamasishaji huo, wakawahamasisha pia akinamama wengi sana kwenye Wilaya ya Masasi, Wilaya ya Tandahimba ikiwemo pamoja na Newala, Lulindi pamoja na Ruangwa wakope pesa kwenye mabenki lakini pia walikopeshwa pesa pamoja na Halmashauri. Sasa bahati mbya sana mpaka sasa hivi Serikali haijalipa pesa hizo za hao akinamama na wameanza kutaifishwa, kufilisiwa na wanashindwa kufanya shughuli zao na hapa tunasema tunataka tuwawezeshe akinamama. Sasa nataka tusikie kauli ya Serikali, je, ni lini watawalipa akinamama hao waliozalisha miche iliyopelekwa mikoa mingine 17 pesa zao?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, nashukuru. Napenda kujibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kwanza ni kweli Serikali miaka yote tuna mradi wa kuongeza uzalishaji wa korosho hapa nchini kutoka tani 300,000 za sasa kwenda tani milioni moja ndani ya miaka mitano ijayo. Kwa hiyo miongoni mwa miradi hiyo lazima tulikuwa tuongeze eneo la uzalishaji na moja ya mikakati ilikuwa kwamba kuzalisha miche zaidi ya milioni 10 kwa kila mwaka kwa muda wa miaka hiyo mitatu. Pia ni kweli kwamba miche hii ilizalishwa kwa vikundi mbalimbali vya akinamama na vijana, lakini baada ya kupitia yale madeni, tumegundua kwamba kuna kasoro nyingi katika yale madeni.

Mheshimiwa Spika, kama ninavyosema siku zote kwamba hizi ni pesa za umma, kama Serikali tuliona ni busara kwamba tufanye uhakiki wa kina ili tujue, tubainishe na kutambua yapi madai halali na yapi madai yaliyopikwa ili wale halali waweze kulipwa. Niendelee kumsihi tu Mheshimiwa Mwambe na wengine wote waendelee kuvuta subira, jambo hili karibu linafika mwisho, timu ya uchunguzi iko katika hatua za mwisho kumaliza, tukimaliza hela zipo na tutawalipa wote waliozalisha miche hii.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, suala linaloulizwa na Mheshimwa Sannda na sisi pia watu wa halmashauri ya Masasi linatuletea shida. Halmashauri ya Wilaya ya Masasi ilipanga kulipa posho Madiwani na stahiki zao nyingine kutokana na makusanya yaliyokuwa yanakusanywa kutoka kwenye ushuru wa korosho ambao Mheshimiwa Rais amesema hatapeleka tena. Sasa swali langu, ni je, Serikali haioni umuhimu wa kuwalipa Madiwani hawa posho moja kwa moja kutoka kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali?
NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA, (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu yangu ya msingi kwamba suala la posho za Madiwani, kwanza kimsingi yanatokana na mapato ya ndani na suala lingine ni uwezo wa halmashauri yenyewe na Mheshimiwa Rais alishatoa maelekezo kwa Wilaya hizi ambazo zilikuwa zinakusanya mapato kupitia korosho wajipange kwa msimu mwingine wa korosho wafanye kazi vizuri ili waweze kupata mapato hayo. Sisi maelekezo yetu ni kwamba tutatoa maelekezo na halmashauri italipa Madiwani kulinga na uwezo wao wa ndani, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili niulize maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka wakati Mheshimiwa Rais, Dkt. John Joseph Pombe Magufuli analihutubia Bunge hili wakati wa ufunguzi wake alisema asingependa tena kusikia tena hili neno la upembuzi yakinifu likiendelea kutumika kwa sababu linaonesha ni ambalo limekuwa liki-roll on mambo yaani ni utaratibu tu wa kutaka kuchelewesha. Sasa tunafahamu Serikali ina mipango yake na hapa unasema specifically kwamba itafanyika kwenye Mwaka wa Fedha 2019/2020. Sasa je, Serikali iko tayari kutueleza ni lini specifically mradi huu utaanza kufanyika ili kuondoa kero ya watu wa Liwale? Swali langu la kwanza.

Mheshimiwa Spika, swali langu la pili, ni kwamba matatizo yaliyoko Liwale yanafanana kabisa na matatizo yaliyoko Jimbo la Ndanda hasa kwenye Kata ya Nanganga. Kata ya Nanganga kuna mradi ambao ulikusudiwa upeleke maji kwenye vijiji vya Chinyanyila, Nanganga A na B, Mkwera moja na Mbili pamoja na Mumburu 1 na 2 pamoja na vijiji vya Chipite. Mpaka sasa hivi tunaonge ahapa mradi ule ulitekelezwa chini ya kiwango na inasemekana kwamba mkandarasi amekimbia hajaukamilisha na hajaukabidhi kufanya commissioning kama ambavyo ilikusudiwa.

Sasa nimuulize Mheshimiwa Waziri, je, yuko tayari kupeleka wataalam wake kutoka Makao Makuu ya Wizara ya Maji wakauchunguze mradi huu na kutoa majibu stahiki kwa wananchi wale?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Spika, napenda kumjibu Mheshimiwa Mbunge, moja; Wizara yetu ya Maji jukumu lake ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji safi na salama lakini katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji katika Mji huu wa Liwale, kuna miradi ambayo inaendelea. Moja, mradi wa Kipure pamoja na Mangilikiti na Nanyungu yote ni katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji na hata katika bajeti hii yetu ya 2019/2020 tumetenga zaidi ya 699,000,000 katika kuhakikisha tunatatua tatizo la maji. Kubwa, Mhandisi wa Mkoa, wahandisi wa wilaya wahakikishe fedha hizi zinatumika kuweza kutatua tatizo la maji.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili kuhusu mradi ambao ameuelezea nataka nimhakikishuie, sisi kama Wizara ya Maji hatutakuwa kikwazo kutuma wataalam kwenda kuukagua mradi huo na mimi kama Naibu Waziri niko tayari kuongozana na wewe katika kuhakikisha tunaenda kuchukua hatua nzitio. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kuumuliza Mheshimiwa Waziri kwamba suala hili la nishati mbadala tuliaminishwa kwa ugunduzi ule wa gesi, basi wananchi wa vijiji wangefikishiwa ile gesi wakaachana kabisa na mambo ya kutumia mkaa ili kuweza sasa kutumia gesi ambayo inapatikana maeneo ya Mtwara. Hata hivyo, mpaka sasa hivi hata Mtwara kwenyewe matumizi ya gesi si makubwa kwa sababu ile miradi ni kama imekuwa abandoned, Serikali haiifanyii tena kazi. Sasa nataka kufahamu kutoka kwa Naibu Waziri, je, Serikali inatoa kauli gani kuhusiana na masuala ya gesi iliyopo Mtwara?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza napenda nimshuruku sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu ya maswali ya msingi ya Waheshimiwa Wabunge. Pia napenda niungane na Mbunge Mwambe kwa matumizi ya gesi kule Mtwara na nimpongeze kwa ufuatiliaji wake.

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi karibu mwezi uliopita tumeanza kutekeleza rasmi, mwaka jana tulizindua usambazaji wa gesi Mtwara na katika maeneo 12 ambayo tunaanza nayo vifaa tayari vimepatikana na tarehe 30 mwezi huu ujenzi wa usambazaji gesi Mtwara unaanza. Tunaanza na vituo cha Chuo cha Ufundi pamoja na maeneo yote yanayokwenda mpaka gerezani na maeneo ya Mtwara Mikindani. Nitake tu kuwapa taarifa na uhakika wananchi wa Mtwara kwamba yataanza sasa mwezi huu tarehe 30 na yatachukua takribani miezi 15 ili wananchi wa Mtwara waweze kupata gesi kama ambavyo tumepanga.
MHE. CECIL D. MWAMBE:Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, suala hili la chai, linafanana kabisa na suala ambalo liko kwenye mikoa inayolima korosho.

Mheshimiwa Spika, mlolongo huu wa kuongeza thamani ya mazao na mwaka kama utakumbuka Mheshimiwa Waziri alipokuja kwenye Kamati yetu ya viwanda na bishara walileta pale ndani wakasema wanafanya utafiti namna ya kuongeza thamani kwenye kochoko ambayo inazalisha nipa ili kuwaongezea mapato wakulima kwa maana ya gongo…

SPIKA: Kochoko ndiyo nini?

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, kochoko ni zile washi zinazotokana baada ya mavuno ya korosho, wakulima huwa wanazitupa lakini wengine huwa wanaziuza na wanatengeneza gongo na inafahamika na kwamba kongo si pombe haramu isipokuwa namna inavyotengenezwa.

Sasa nataka nimuulize Mheshimiwa utafiti huo ambao ulikuwa unafanywa na Chuo cha Kilimo cha Naliendele umefikia wapi mpaka sasa hivi ili wakulima waweze kujipatia kipato cha ziada kutokana na mazao yao ya shambani? Ahsante.
WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Naibu Waziri kwa majibu mazuri aliyoyatoa, pia nichukue nafasi hii kumpongeza ndugu yangu Mheshimiwa Mwambe kwa jinsi ambavyo ameendelea kufuatilia suala hili la korosho.

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa Chuo chetu kupitia tawi letu la Naliendele tumefanya utafiti wa kina na tumebaini kwamba kuna mazao mengi tunayoweza kuzalisha kutokana na korosho ikiwemo juice na ikiwemo mvinyo maalum ambao unatokana na haya mabibo ya korosho na tumetoa maagizo kwenye tawi letu sasa hivi kujenga kinu cha kuweza kuchakata hiyo ili tuweze kuzalisha mvinyo pamoja na juice ambayo tutaiuza hapa nchini na hivi itaongeza thamani na kuongeza mapato yanayotokana na zao la korosho.

Mheshimiwa Spika,kwa hiyo Mheshimiwa Mwambe awe na subira baada ya muda mfupi tu atakiona kile kiwanda kikiwa kimejengwa pale na kuweza kuchakata hiyo, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza. Swali la kwanza, Mheshimiwa Waziri ametaja mkandarasi anayesimamia ujenzi kwenye hivyo vijiji, lakini amekuwa akifanya kazi hii kwa taratibu sana na analalamika kwamba hapewi pesa yake ya kukamilisha kazi zake kwa wakati. Je, Mheshimiwa Waziri uko tayari kutueleza hivi viporo vya REA II vitakamilika lini specifically?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; matatizo yaliyopo Jimbo la Momba kwenye masuala haya ya umeme yanafanana moja kwa moja na shida pia zilizopo kwenye Jimbo la Ndanda, Wilaya ya Masasi, hasa zaidi kwenye Vijiji vya Mkwera, Mumburu, Chipite, Mdenga, Liputu, Ndoro pamoja na Mbaju pamoja na Kata za Msikisi na Mlingula. Vijiji hivyo nilivyovitaja vyote vinapitiwa na umeme mkubwa juu wa kilowati 33 lakini chini wanakokaa wananchi hakuna umeme. Je, ni lini Serikali kwa makusudi kabisa itatekeleza kazi hii ya kushusha umeme walau kwenye vile vijiji vinavyopitiwa na umeme mkubwa unaoelekea Masasi?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kumshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri katika swali la msingi, lakini nimpongeze sana Mheshimiwa Mwambe katika maswali yake mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, ni kweli yapo maeneo yaliyobaki katika utekelezaji wa REA II na maeneo yote yaliyobaki katika utekelezaji wa REA II yamechukuliwa na Mradi wa REA III unaoendelea sasa. Kwa maendeleo yote, hasa katika Jimbo la Mheshimiwa kama alivyotaja, eneo lote la kutoka Sumbawanga kwenda Tunduma kwenda mpaka Mpanda, yaliyobaki yote yamechukuliwa na Mradi wa REA III unaoendelea. Kwa hiyo nimpe tu taarifa Mheshimiwa Mbunge kwa niaba ya muuliza swali kwamba maeneo yote yaliyobaki yatachukuliwa na REA III inayoendelea kufanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na swali la pili, ni kweli kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mwambe; maeneo ya Ndanda, hasa eneo la Liputi pamoja na Mbemba pamoja na Kitongoji cha Ndoro, yako chini ya line inayopita KVA 33, lakini kama ambavyo nimeshatoa utaratibu na Mheshimiwa Mbunge anafahamu, hivi sasa TANESCO wanapeleka umeme katika vitongoji vyote hivyo. Bahati nzuri sana Kitongoji cha Ndoro kiko nyuma ya Sekondari ya Ndanda ambayo tayari ina umeme. Kwa hiyo, maeneo haya yatafanyiwa kazi na yatakamilishwa ifikapo mwisho wa mwezi Juni, mwaka huu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshmiwa Spika, pamoja na majibu marefu sana Mheshimiwa Waziri, lakini kinagaubaga kabisa hajasema wazi ni nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sukari pamoja na miwa ya wananchi inapata bei nzuri ukilinganisha na sukari inayoletwa toka nje?

Mheshimiwa Spika, sasa nataka kufahamu kwa Mheshimiwa Waziri, ili kuweza kulinda viwanda vya ndani, anasema nini kuhusu sukari inayoingizwa nchini kwa bei nafuu kuliko sukari inayozalishwa Tanzania?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, utakumbuka mwaka 2018 Serikali ilichukua maamuzi mazuri kabisa ya kuamua kukusanya korosho zote kwa wakulima na baadaye kutangaza bei nzuri na kusema watawalipa wakulima wote. Hivi sasa kumekuwa na sintofahamu kubwa sana kwenye mikoa yote inayolima korosho Tanzania kwa sababu mpaka sasa hivi Serikali haijakamilisha malipo kama ambavyo iliahidi. Utakumbuka maelekezo ya Mheshimiwa Rais na maneno yake alisema kwamba Serikali imeshatenga pesa na sasa hivi pesa hizo zinatakiwa kulipwa kwa wakulima kwa 100%.

Mheshimiwa Spika, sasa swali langu, nataka nipate commitment kutoka wa Serikali, ni lini hasa watakamilisha malipo ya pesa za wakulima wa korosho wa Tanzania kwa sababu walisema pesa hizo wanazo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO (MHE. OMARY T. MGUMBA): Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mwambe anasema katika majibu yetu hakuna mkakati. Angerudia kwenye swali lake la msingi, hilo halikuwa swali la msingi, sisi tumejibu majibu yetu kwa kuzingatia swali la msingi tuliloulizwa.

Mheshimiwa Spika, kwenye swali lake hili la nyongeza la kwanza anasema kwamba sukari inatoka nchi na ina bei ndogo kuliko sukari inayoazalishwa hapa nchi. Nini mkakati wa Serikali kulinda viwanda vya ndani? Kwanza ni kweli sukari yote inayotoka nje kuletwa hapa nchini ina bei ndogo kuliko sukari yetu. Ni kwa sababu wenzetu gharama za uzalishaji zipo chini kuliko gharama za hapa ndani kwa sababu wenzetu wanakwenda mpaka kwenye by product nyingine kwa hiyo wanashusha gharama za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, sisi ili kulinda viwanda vya ndani kama tulivyosema, hii Serikali ya Awamu ya Tano ni Serikali ya Viwanda na ndiyo maana mkakati wa kwanza tumewapa ile gap sugar, wenye viwanda vyenyewe ndio waagize sukari ile pungufu ili kuvilinda viwanda vya ndani viweze kuongeza uwezo wa kimtaji na kulinda masoko yako.

Mheshimiwa Spika, hili limetupa manufaa makubwa. Kwa mfano, kiwanda cha sukari cha mtibwa, kabla ya utaratibu huu, uwezo wake wa kuzalisha ni zaidi ya tani 60,000 lakini ulikuwa unazalisha tani 15,000 tu kwa mwaka. Baada ya utaratibu huu, mwaka 2018 kwa mara ya kwanza imefikia kuzalisha tani zaidi ya tani 32,000. Kwa hiyo, hayo ni mafanikio makubwa sana katika kulinda viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo swali lake la pili anataka kujua malipo ya watu wa korosho. Ni kweli tumesema Serikali fedha tunazo na kweli Serikali fedha tunazo. Ndiyo maana katika hili la utaratibu wa sukari, tulielekeza kampuni yetu au Taasisi ya Serikali ya Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote kutoka kwa wakulima. Taasisi hii ilienda kukopa kutoka Benki ya Maendeleo ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba ile limit ambayo walipangiwa kwamba wameshafikia ukomo ilikuwa lazima kwamba wauze korosho kwanza ili wapunguze lile gap waweze kuuza tena. Sasa tumeshauza korosho hizo, nikuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kabda ya msimu huu kuanza wakulima wote watakuwa wamelipwa fedha zao.(Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza:

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunatambua hivi karibuni TAMISEMI wamekuwa wakitoa rating kwenye Halmashauri zetu kwa maana ya kuwapa namba kutokana na makusanyo na utekelezaji wa makusanyo wanayoyafanya. Kwa bahati mbaya sanaHalmashauri nyingi ambazo walipanga mipango yao ikitegemea makusanyo ya mazao ya kilimo hawakuweza kufanikiwa kupata hizo pesa kwa wakati kwa sababu Serikali iliamua kuingilia mchakato fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kuuliza kwa Mheshimiwa Waziri, kwamba miradi mingi imesimama kwenye Halmashauri zetu, pesa za posho kwa ajili ya Madiwani hazilipwi kwa wakati na hasa miradi ya afya kwa sababu hivi karibuni – na niipongeze Serikali kwamba wametupatia pesa za 4PRkwa mfano Jimbo la Ndanda tumepata zaidi ya madarasa 13. Sasa ninataka kufahamu; ni lini Serikali mtapeleka pesa kwa ajili ya kukamilisha maboma yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwenye Kata za Ndanda, Lukuledi, Mihima na Mpanyani kwa ajili ya vituo vya afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MWITA M. WAITARA): Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Mheshimiwa Mwenyekiti, ameeleza maelezo mengi lakini kwa ufupi ni kwamba kama kuna mahitaji mahsusi unaandika TAMISEMI ili waweze kuyafanyia kazi. Lakini mpango wa Serikali ni kwamba hata Mwaka wa Fedha tunapoanza 2019/2020, fedha zimetengwa kwenda kumalizia maboma ambayo yapo ya msingi na sekondari katika Halmashauri zenu. Kwa hiyo tuvute subira lakini kama una jambo mahsusi tuandikie ili tuweze kuchukua hatua za haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme hii haisemwi amesema 4PR, hii EP4R ndiyo lugha sahihi, maana yake ni kwamba Education Payment For Results. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi niulize swali la nyongeza suala linalohusiana na Hospitali ya Mwananyamala juu ya CT–SCAN inafanana kabisa na suala ambalo liko Mkoa wa Mtwara hasa Hospitali ya Ndanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, itakumbukwa kwamba Serikali ilifanya Hospitali ya Ndanda kuwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda, na Wamisionari wale wamejitahidi sasa hivi wanatoa huduma ya dialysis na huduma nyingi tu na ndiyo sehemu kubwa hasa inayotumika kama Hospitali ya Wilaya kwa sababu Hospitali ya Mkomaindo haina facilities nyingi, sasa swali langu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu wanafanya kazi hii na Ubia wa Serikali, Je, Serikali haioni haja ili kupunguza msongamano wa watu kupelekwa Muhimbili na Rufaa hizo kuwapelekea Hospitali ya Ndanda CT-SCAN pamoja na MRI machine?
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana Mheshimiwa Cecil Mwambe Mbunge wa Ndanda kwa swali lake zuri, kwanza nataka kutambua umuhimu au kazi nzuri inayofanywa na Mashirika ya Dini katika kutoa huduma za Afya na sisi Sera yetu ya Afya ya mwaka 2007 inatambua na kuthamini mchango wa Mashirika ya Dini katika utoaji wa huduma za Afya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sasa, je tutapeleka CT-SCAN na MRI katika Hospitali ya Rufaa ya Ndanda ni kweli Hospitali hizi tumezipandisha hadhi mwaka 2010 kuwa Hospitali za Rufaa za Mikoa. Lakini Mheshimiwa Mwambe utakubaliana na mimi, tunayo Hospitali pia ya Serikali ya Rufaa ya Mkoa Ligula.

Kwa hiyo, sasa mtuambie wana Kusini, wananchi wa Mtwara kwamba tupeleke Ligula, au tupeleke Ndanda? Lakini ambaye nasimamia moja kwa moja, Hospitali zangu za Serikali kipaumbele unajenga kwako kabla hujajenga kwako kabla hujajenga kwa mwingine. Tutaendelea kuthamini na kuheshimu mchango wa Mashirika ya Dini na ndiyo maana zaidi ya asilimia 70 ya watumishi waliokuwepo katika Hospitali hizi za Mashirika ya Dini wanalipwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, zikiwepo nyingi tutapeleka Ndanda na Ligula, lakini ukiniambia nichague, nitaanza na Ligula kwa sababu ndiko pia wananchi wengi wanaenda kupata huduma za Afya katika ngazi ya Mkoa wa Mtwara. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza.

Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ningependa pia tuyafanye yafuatayo; kwanza kabisa, chanzo cha maji cha Mbwinji kilitengenzwa maalum kabisa kwa ajili ya kusaidia Wilaya za Masasi kama ambavyo umesema, lakini hivi sasa mimi na wewe tunaongea kwa mfano, Kijiji cha Liputu ambapo bomba linalokwenda Nachingwea likitokea Kijiji cha Nangoo kilometa tano tu mpaka sasa kijiji kile hakina maji na kwamba watu wa MANAWASA maka leo hawajaweza kuweka maji kuwaunganishia wananchi wa pale. Je, kauli yako ni nini kuhusianan na hiki kijiji?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kwenye mpango mkubwa wa bajeti ya Wizara yako iliyoletwa hapa kwetu umeongelea kuhusu mabwawa yatakayojengwa Mihima, Mpanyani pamoja na Chingulungulu, lakini mimi wakati nashauri Serikali nilijaribu kueleza kwamba ni bora tukafanya utafiti ili kuweza kutumia maji safi na salama yaliyopo kwenye hili bomba kubwa la Mbwinji ili kuweza kuyafikisha Lukuledi.

Sasa ningependa kujua kauli yako. Mko tayari kufanyia kazi wazo langu ili wananchi wa Kata ya Lukuledi wapate maji safi na salama badala ya kutegemea maji ya bwawa ambayo ni gharama kubwa?
NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Mbunge kwa maswali yake mazuri lakini kikubwa ambacho nataka kusemani, maji ni uhai na maji hayana mbadala na jukumu la kulinda uhai wa Watanzania wa mijini na vijijini tumepewa sisi Wizara ya Maji. Nataka nimhakikishie tumefanya mageuzi makubwa sana ndani ya Wizara yetu ya Maji.

Moja ni kuhakikisha kwamba eneo la kijiji ambacho kinapitiwa na bomba kuu, kilometa 12 upande wa kulia ama kushoto vinahakikishiwa vinapata huduma ya maji. Kwa kuwa vijiji hiki kiko katika kilometa tano tutamuagiza Mkurugenzi wa MANAWASA aangalie afanya tathmini ili tuwaangalie wananchi hawa wa Nangoo nao waweze kupata huduma hii muhimu sana ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu suala zima la kuhakikisha katika eneo hili la Lukuledi wanapata maji ukiachana na mabwawa, sisi jukumu letu ni kuhakikisha Watanzania wanapata maji na kama kuna njia mbadala ambayo itakuwa haitumii gharama kubwa sisi nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge tuko tayari na nipo tayari mimi mwenyewe kwenda kuona hali halisi ili mwisho wa siku tuweze kuchukua hatua. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Waziri, utakumbuka siku za karibuni umefanya ziara kwenye Mkoa wa Mtwara na hasa Wilaya ya Masasi ili kuweza kuona athari zilizopo hasa zaidi kwenye vijiji vile ambavyo vinapitiwa na umeme mkubwa ukielekea Wilayani Masasi.

Sasa swali, toka umeondoka takribani ni wiki mbili sasa, unaweza kutueleza ni hatua gani na ni kazi gani inatakiwa kufanyika katika maeneo hayo?
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nijibu swali moja la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kuwa ziko hatua tatu, la kwanza katika Jimbo la Mheshimiwa Mbunge, ingawaje nilifika jimboni uliniagiza tu haukuweza kuwepo, lakini tumekuwashia vijiji viwili.

Kwa hiyo, ni hatua ya kwanza imefanyika, lakini hatua ya pili tumeainisha maeneo yote ya Jimbo la Masasi ambapo umeme haukufika, wakandarasi wameshapewa maeneo hayo na mengine tumewapa TANESCO kwa sababu bei ni moja ili maeneo hayo yafanyiwe kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, hatua ya tatu mkandarasi ameshapeleka nguzo na vitendea kazi maeneo yote ili kazi iweze kwenda kwa haraka zaidi. Hizo ndizo hatua tumechukua. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Swali la kwanza Mheshimiwa Naibu Waziri je, yupo tayari kuwaeleza Watanzania ni namna gani wanatakiwa kuzitumia alama za barabarani ikiwemo pamoja na zebra cross kwa sababu sasa hivi hata kama hakuna mtu lakini kuna askari wanasimama maeneo hayo na kuwavizia watu ili wakipita wawakamate sehemu inayofuata? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili kumekuwa na tabia mbaya sana ya askari wetu wa usalama barabarani kwa vijana wetu wa bodaboda na hii nadhani ni Tanzania nzima, wanapotaka kuwakamata huwa wanakimbiza na kuwachapa viboko migongani na wengine kuwavuta na wale vijana wanadondoka chini wanaumia. Ni nini tamko la Serikali kuhusu suala hili kwa sababu nia ni kuzuia ajali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusiana na elimu juu ya matumizi ya alama barabarani nadhani alama za barabarani ziko nyingi, kwa hiyo, kuanza kuzungumzia elimu hapa itachukua muda mrefu, lakini yeye ametoa mfano wa hii zebra cross ni kwamba utaratibu wake unatakiwa unapofika kwenye zebra cross unaangalia kulia, unaangalia kushoto, unaangalia kulia tena halafu unakata kwa mwendo wa kawaida si kwa kukimbia wala mwendo wa taratibu na huo ndio utaratibu na gari ambapo inapopita inapokuja inatakiwa itakapoona mtu amegusa kwenye ile zebra cross isimame na kumsubiri na sio kuongeza speed ili yule mtu asivuke.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kuhusiana na swali lake la pili kwamba askari wanachapa viboko, askari wa Jeshi la Polisi hawachapi viboko, mimi hiyo sijawahi kuona pahala au kusikia kwamba kuna askari wa Jeshi la Polisi amechapa viboko badoboda. Kwa hiyo naomba nisizungumze hatua kwa sababu hakuna hilo tukio ambalo tumelipokea kuhusiana na tuhuma za askari polisi kuchapa viboko waendesha bodaboda. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza dogo, kwamba Jimbo la Ndanda lenye kata 16 lina Kituo cha Afya kimoja tu cha Chiwale. Hata hivyo wananchi wa Ndanda, Lukuledi, Panyani, Mihima pamoja na Chilolo walijitahidi kwa kutumia nguvu zao pamoja na nguvu ya Ofisi ya Mbunge kujenga maboma kwa ajili ya zahanati na mengine kituo cha afya. Nini kauli ya Serikali kuhusu kuwapokea wananchi mzigo huu wa kukamilisha maboma haya ili yaweze kutumika na kutoa huduma za afya?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nitumie nafasi hii kuwapongeza wananchi wa Jimbo la Ndanda kwa kujitolea nguvu zao na kuanza ujenzi wa zahanati na vituo vya afya na hiyo ni kauli ya Serikali ya kuhakikisha kwamba wananchi wanaibua miradi na Serikali inaunga nguvu miradi hiyo ya wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mwaka huu wa Fedha 2020/2021, Serikali imetenga fedha kiasi cha shilingi bilioni 27.75 ambazo zitakwenda kufanya kazi ya kuchangia nguvu za wananchi katika kukamilisha ujenzi wa maboma 555 nchini kote. Kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mwambe kwamba jimbo lake na vijiji na kata husika zipo katika mpango huu na Serikali itahakikisha inatoa mgao kwa ajili ya umaliziaji wa vituo hivyo ili viweze kutoa huduma kwa wananchi.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye suala hili la viwanda tutakumbuka pia kulikuwa na viwanda vingi vya korosho vilivyopo maeneo ya kusini, Mtwara, Lindi, Masasi, Nachingwea na maeneo mengi. Serikali imesema imeamua kubinafsisha na kuna vingine vilikuwa vinatumika kama maghala ya kuhifadhia mazao badala ya kuviendeleza kuwa viwanda vya korosho ili kuweza kutoa ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunataka tusikie commitment ya Serikali, ni lini zoezi hili wanalolifanya litakamilika ili kuweza kuvirejesha hivi viwanda, watu muda sahihi wa kukamilisha? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil David Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kama nilivyosema katika jibu la msingi ni kweli kuna viwanda vingi ambavyo vimekuwa havifanyi kazi baada ya wawekezaji wengi kuvitelekeza au kutokuviendeleza au kuendeleza kwa kusuasua au kubadilisha matumizi ya viwanda hivyo ikiwemo wengine waling’oa hata mitambo ya viwanda hivyo na kubadilisha kuwa ma-godown.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Waheshimiwa Wabunge watuelewe kwamba Serikali ina nia ya dhati ya kuona sasa tunapata wawekezaji mahiri. Kwa hiyo hata viwanda vya korosho ambavyo vilikuwa vimetelekezwa kama nilivyosema tunaenda kutangaza utaratibu maalum wa kuweza kuwapata wawekezaji kwa njia ya wazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, baada ya hapo naamini wengi ambao wana nia ya kuwekeza katika viwanda hivi watapatikana na hakika tunaamini viwanda hivi vitaenda kufanya kazi kwa tija kama ambavyo Serikali imekusudia. Nakushukuru sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo Mheshimiwa Kuchauka ameonesha masikitiko yake makubwa kabisa, naamini nasi umetupa nafasi kwa maana ya Wabunge wa Nachingwea, Ndanda, Masasi na maeneo mengine kwenye umuhimu wa hii barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nami nimuulize Mheshimiwa Waziri, Wizara imetenga shilingi bilioni 1.5 tu, kwa makisio ya sasa ni kama kilometa moja na nusu, wanapotaka kuanza kujenga barabara hii wataanzia kujenga upande gani? kwa sababu shida ipo Masasi, shida ipo pia Nachingwea. Watueleze wanataka kuanza kujenga upande gani kwa pesa kidogo namna hiyo waliyoitenga. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, Wizara tunachojenga ni kilometa hizo 45 kati ya Masasi na Nachingwea. Lakini hata ukianza Masasi, ukianza Nachingwea bado barabara ni ileile mtu atakapopita, atapita kokote. Nadhani nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Mbunge kwamba suala la kuanza wapi ama wapi nadhani isingekuwa ni hoja kubwa cha msingi tukamilishe hizo kilometa 45 kwa sababu hata kama itaanzia Masasi, itaanzia Nachingwea, lakini atakayepita, atapita tu kwenye hiyo barabara.

Mheshimiwa Spika, nadhani hilo aiachie Wizara na wataalam wataangalia pia wapi tunapofanya mobilization inaweza kuwa ni rahisi, jambo la msingi tukamilishe hizo kilometa 45. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Tatizo la maji lililopo Kilwa linafanana kabisa na matatizo ya maji yaliyoko Jimbo la Ndanda hasa zaidi upande wa Magharibi kwenye Kata za Mlingula, Namajani, Msikisi, Namatutwe pamoja na Mpanyani. Swali langu, je, ni nini hasa mpango wa Serikali wa muda mfupi wa kuhakikisha kata hizi nilizozitaja zinapata maji kabla hatujaingia kwenye kiangazi kikuu kinachoanza mwezi Julai na Agosti. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kutoka Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia Wizara ya Maji wakati wote tunajitahidi sana kuona tunatatua tatizo la maji kwa kutumia vyanzo mbalimbali kwa sababu tuna michakato ya muda mrefu pamoja na kutumia Mto Ruvuma kwa mwaka ujao wa fedha, lakini katika kuona kwamba wananchi tunakwenda kuwapunguzia makali ya matatizo ya maji kwa mwaka huu wa fedha, Mheshimiwa Mwambe kama ambavyo umekuwa ukifuatilia mara zote, tumeongea mara nyingi. Kwa hiyo, hili nalo tukutane tuone tuanze na kisima upande upi ili tuweze kupunguza haya matatizo. Maji Ndanda ni lazima yatoke, mabomba yamwage maji, tuokoe ndoa za akinamama, tutahakikisha hawaendi kukesha kwenye vyanzo vya maji. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri wa Mifugo, naomba nipate nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Swali la kwanza, sekta ya nguruwe sasa imekuwa ikikuwa kwa kasi kubwa sana na hapa nchini na kwamba ufugaji wa nguruwe ni rahisi kidogo kuliko mifugo mingine kwa sababu wanatunzwa ndani ukilinganishwa na ng’ombe, sasa kumekuwa na incentives mbalimbali zinazotolewa kwenye mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwenye bidhaa zinazosaidia kwenye ufugaji wa nyuki, samaki, kuku ng’ombe na mifugo mingine zina nafuu ya kodi. Je, kwa sababu sekta hii nayo inahitaji kuboreshwa na kuwa ya kisasa zaidi Serikali haioni kuna haja ya kutoa incentives kwenye vifaa vinavyotumika kwenye ufugaji wa nguruwe kwenye eneo la kodi?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na muingiliano mkubwa sana kwenye sekta ya nyama, huko utakutana na watu wa NEMC utakutana na watu wa TBS, ambao wanashughulika machinjio wengine usafirishaji, na wengine ubora wa nyama kitu ambacho kinasababisha mazao ya nyama kuwa na gharama kubwa sana ambayo Watanzania wengi hawawezi ku-afford kununua na kilo bei ya nyama ukiangalia katika mchanganuo wake gharama ya uununuzi inatokana mwingiliano huu wa mamlaka mbalimbali zinazosimamia suala la nyama sasa swali langu.

Sasa swali langu, Serikali haioni haja ya kuhamisha shughuli zote zinazofanywa na idara mbalimbali ili zikasimamiwe na Wizara na Mifugo ambayo yenyewe ndio yenye uwezo mkubwa sana wa kusimamia kutokana na utaalamu uliopo?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa
Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni juu ya incentives kwa ajili ya wafugaji wa nguruwe kama ambavyo wanapata wafugaji wengine. Naomba niichukue rai hii ya Mheshimiwa Mwambe ya kwamba Serikali tuitazame ufugaji wa nguruwe na kwa kuwa tuo kwenye kipindi cha bajeti jambo hili limekuja kwa wakati muafaka na Serikali tunalichukua, litatazamwa katika vikao vyetu kadri itakavyoonekana inafaa, wataalam pamoja nasi viongozi tutashauriana kwa ajili ya kuhakikisha kwamba ukuaji wa tasnia hii ya nguruwe inakwenda sambasamba na ukuaji wa mifugo mingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ameuliza juu ya suala zima la muingiliano mkubwa wa taasisi mbalimbali za Serikali unaopelekea kupandisha bei ya nyama na mazao yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika awamu iliyopita Serikali ilifanya kazi kubwa sana ya kuhakikisha kwamba tunaunganisha vyombo vyetu vinavyosimamia tasnia zetu hizi, kwa mfano baadhi ya mazao yatazamwe na moja tu katika taasisi, miaka michache iliyopita tuliamua kwa dhati kabisa kwamba TMDA itatazama vyakula na kwa upande wa mazao ya mifugo yatatazamwa na wataalam wenyewe wa mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie ya kwamba rai yako yakuondoa mgongano huu wa kitaasisi na la lenyewe tumelichukua kwa kusudio la kupunguza changamoto inayowapata wafanyabiashara wa mazao ya mifugo na wafugaji pia vilevile. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye hili suala la maji, ninashukuru sana kwamba matatizo haya yanayotokea kwenye Jimbo la Namtumbo yanafanana sawa kabisa na matatizo yaliyopo Jimbo la Ndanda hasa kwenye Kata za Mlingula, Msikisi, Namajani pamoja na vijiji vyake. Ninataka kufahamu sasa mpango mkakati wa Serikali wa kuhakikisha kabla ya kiangazi kikuu tunapata maji ya kutosha na uhakikisha kwenye maeneo haya. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, mpango mkakati wa Serikali ni kuhakikisha tatizo la maji linapungua. Na ndiyo maana Wizara ya Maji iliweza kuunda chombo hiki cha kushughulikia maji vijijini pamoja na usafi wa mazingira kwa maana ya RUASA. Hivyo maeneo yote ambayo kwa sasa hivi yamekuwa yakipitia changamoto ya maji tunaendelea kuyashughulikia kwa karibu kabisa kwa nia ya dhati kuona kwamba tatizo la maji tunakwenda kulipunguza kama si kulimaliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, basi na maeneo ya Ndanda kama tulivyoongea Mheshimiwa Mbunge nimekuahidi kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha tutakuja angalau tuanze na kisima kimoja, viwili. Lakini mpango wa muda mrefu ni utaanza mwaka ujao wa fedha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kufahamu kwa Mheshimiwa Waziri: Ni lini miradi mikubwa ya kutatua changamoto ya maji kwa hatua ya awali iliyopo Jimbo la Ndanda itatekelezwa, zaidi kwenye Kata za Namajani, Mpanyani, Msikisi pamoja na Chiwale? (Makofi)
WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Nampongeza Mheshimiwa Mbunge, kaka yangu Cecil Mwambe, kwa kweli amekuwa mfuatiliaji mkubwa hasa katika Jimbo lake la Ndanda. Ahadi ambayo nampa katika maeneo ya kipaumbele nitakayokwenda mimi mwenyewe baada ya Bajeti, ni katika eneo lake katika Jimbo la Ndanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa ni kwamba katika Bajeti hii pia tumezingatia ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. Ni imani yangu maeneo ambayo ameyataja yatakuwemo ili kuhakikisha tunakwenda kutatua tatizo la maji. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, Serikali haioni umuhimu sasa wa kupeleka majina ya waajiriwa moja kwa moja kwa Wakurugenzi ili Wakurugenzi wawapangie vituo vya kufanya kazi badala ya kupangwa moja kwa moja kutoka TAMISEMI?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; Wakurugenzi ndio wanaofahamu idadi ya upungufu wa walimu, ukiangalia Jimbo la Ndanda Wilaya ya Masasi kwa mfano, sasa je, Serikali haioni haja ya kuwapa nafasi Wakurugenzi kupendekeza nafasi za ajira kutokana na watu wanaostaafu au kufariki kwenye maeneo yao? (Makofi)
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naomba kujibu maswali madogo mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, ni kweli kabisa tumekuwa na taratibu tofauti hususani kwa walimu ambao wamekuwa wakiajiriwa kuwapeleka katika maeneo yao husika na moja utaratibu ni kwamba sisi tumekuwa tukiwatuma katika halmashauri husika katika vituo ambavyo wao wenyewe wamekuwa wakiomba. Kwa hiyo, wao wanaoomba zile ajira huwa wanaainisha maeneo gani wanataka kwenda kufanyia kazi na sisi tumekuwa tukitekeleza kufanya hivyo.

Mheshimiwa Spika, lakini la pili kuwapa mamlaka Wakurugenzi ni taratibu za kiutumishi na Serikali inafanya kazi baada ya kupata kibali kutoka Ofisi ya Rais (Utumishi) ambao wanatuletea namna, vigezo na sababu mbalimbali za mtu kuajiriwa. Kwa hiyo, kama kuna mapendekezo hayo ya kutaka kubadilisha ni Bunge lako Tukufu ndio lenye mamlaka hiyo, ahsante sana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kama ilivyo madeni kwa wakulima waliozalisha miche ambao hawajalipwa lakini Serikali inakiri kuwatambua. Pia kuna watu waliotoa huduma mbalimbali kwenye msimu ule wa korosho ambao Serikali ilinunua; watu walisambaza magunia, vifungashio na wengine sulphur. Tunataka pia Serikali itoe commitment kwa sababu watu hao walikopa kwenye mabenki, ni lini nao mtamalizana nao kwa kuwalipa pesa zao. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe. Ni kweli kwamba katika sekta ya korosho sio tu madeni yaliyotokana na msimu ambao Serikali ilinunua korosho a wakulima. Madeni yaliyotokana na Serikali/korosho zilizochukuliwa na wakulima, Serikali imelipa sehemu kubwa na imebaki kiwango kidogo kisichozidi shilingi bilioni 2.8 ambazo zimahusisha madeni ya wasambazaji wa watoa huduma lakini sekta nzima ya korosho kuanzia vyama vya msingi, Vyama Vikuu vya Ushirika, wakulima wenyewe wanadaiwa zaidi ya bilioni 66.

Mheshimiwa Spika, kama Serikali hatua tuliyoichukua ya kwanza ni kukaa na wadai wote ikiwemo mabenki na watoa huduma na tukaweka utaratibu ambao tumeanza ku-collect fedha ambazo tutaanza kulipa kwa wale wanaohakikiwa na mchakato huo umekwishaanza na utaratibu unaendelea na kwa kuwa tutakuwa na kikao tarehe 6 Lindi ambacho kitaongozwa na Waziri Mkuu, naamini kwamba yote haya tutayajadili na tutatoka na majibu na wadai wote tumewaalika katika mkutano huo.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu ya Serikali, nina maswali mawili ya nyongeza, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kutokana na kutokuanza kwa mradi huu imesababisha kukosekana kwa shughuli za CSR kama ambavyo nilisema wakati uliopita. Kwa hiyo, Mji wa Chiwata na Jimbo la Mtama kwa sababu kuna sehemu inagusa mradi huu, Jimbo la Ruangwa pamoja na Jimbo la Newala DC imesababisha kutokuwepo kwa ajira zaidi ya 1,500 za moja kwa moja na zingine za kwenye mgodi na kukosekana kwa mapato ya Serikali pamoja na Halmashauri hizo nilizozitaja kiwango cha dola milioni 62. Sasa swali langu…

SPIKA: Eehe swali!

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, Wizara hii ndiyo iliyosababisha tufike hapa, hawaoni kwamba wanafanya hujuma kwenye uchumi wa maeneo haya niliyoyataja?

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kutokana na Sheria ya Madini iliyobadilishwa mwaka 2018 ndiyo hasa chanzo cha mgogoro huu na kampuni zinazotaka kuwekeza, Serikali sasa haioni haja ya kufanya mabadiliko ya sheria hii ili wawekezaji hawa waweze kuja na mitaji yao badala ya kulazimishwa kukopa kwenye benki za ndani? Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama kuna maeneo ambayo yamefaidika na mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ni pamoja na CSR na local content. Yawezekana kweli katika maeneo ambayo miradi haijaanza Waheshimiwa Wabunge wanaweza kuwa hawajaona faida ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ila Wabunge walioko katika Mkoa wa Geita katika mikoa ambayo kuna migodi mikubwa tayari watakubaliana na Serikali kwamba ndipo mahali ambapo Serikali imeweza kubainisha sheria pamoja na kanuni za CSR na kuweza kufanya bora zaidi. Kwa hiyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba mara mradi utakapokuwa umeanza Serikali itasimamia sheria zake pamoja na kanuni za local content na CSR ili kuona kwamba wananchi wa maeneo husika wanaweza kupata faida.

Mheshimiwa Spika, swali la pili linahusu mabadiliko ya sheria. Mabadiliko haya yalipita katika Bunge lako Tukufu na kwa mahali ambapo sheria hizi zimetekelezwa vizuri tumeona kwamba kuna tija.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimuombe Mheshimiwa Mbunge aone kwamba wawekezaji wengine wameshindwa kupata mitaji na wawekezaji wake hawa ni watu wa Australia na Australia ni mahali ambapo kulikuwa kuna total lockdown ya COVID kwa hiyo kupata mitaji mahali hapo imekuwa ni shida. Hata hivyo, tunaona kwamba wengine wanaona kwamba Tanzania bado ni mahali pazuri pa kuwekeza na Serikali kwa kweli milango ya Wizara iko wazi kuendelea kujadiliana ili tuone kwamba wawekezaji wanakuja, wanachimba na kama ilivyo sera ya Serikali wao na sisi tuweze kupata. Ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa barabara hii inayotajwa pia upo kwenye kufungua Mkoa wa Lindi na kwa ajili ya uchumi wa Kusini. Lakini Serikali mara nyingi imekuwa ikiongea tu kuhusu eneo hili la kusahau junction inayoanzia maeneo ya Mbingu kule Ifakara inapita Liwale inakwenda kutokea Nachingwea mpaka Masasi na yenyewe ni muhimu kama ilivyo hivyo.

Sasa Serikali itueleza hapa kwa sababu tulikuwa tukiongea kuhusu barabara hii mara nyingi kwamba ni lini sasa pamoja na nia njema ya kutaka kutengeneza hii barabara inayokwenda Ruvuma mtamalizia na ile junction inayokuja kutokea Liwale kuja Nachingwea mpaka Lindi?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara aliyoitaja kuanzia Mbingu, Liwale hadi Nachingwea ni barabara ambayo kweli ipo imeahidiwa lakini ujenzi wa barabara hii utategemea na upatikanaji wa fedha. Kwa hiyo, kwanza itatakiwa ifanyiwe upembuzi na baadaye usanifu wa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumepitisha bajeti, kwa hiyo, itategemea na upatikanaji wa fedha ambayo kama itapatikana fedha basi miradi hii itaanza kutekelezwa sawasawa na miradi mingine. Lakini kikubwa ni ufinyu wa bajeti ambao unafanya barabara hizi zote haziwezi kutekelezwa kwa wakati mmoja. Lakini ni nia ya Serikali kuhakikisha kwamba barabara hii inajengwa ili kuweza kufungua maeneo haya na pia kupunguza umbali ambao wananchi wanasafiri kuzungukia barabara ambazo ni ndefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara ya Ujenzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi wakazi wa Mtwara, Lindi pamoja na Ruvuma tunalazimika kufika Dar es Salaam kabla ya kuja Dodoma ambako ndiko Makao Makuu ya nchi. Lakini kimsingi kuna barabara inayoanzia Songea barabara nyingine inaanzia Masasi, Nachingwea, Liwale, Lupilo inakuja kutokea Morogoro, Ifakara, Malinyi ili kuweza kufika Dodoma kirahisi badala ya kutulazimisha tufike kwanza Dar es Salaam ndipo tuje Dodoma.

Sasa swali langu kwa Serikali kutokana na umuhimu wa barabara hii kwa watu wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma ili tuweze kufika kirahisi Makao Makuu ya nchi ambako ni Dodoma, ni lini itatengenezwa kwa kiwango cha lami?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG.
GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli barabara anayoitaja ni barabara kuu; siyo barabara ya mkoa, ni barabara kuu, ambayo kama nimemuelewa ni hii barabara ambayo inaoanzia Lumecha, Londo, Kilosa kwa Mpepo, Malinyi, Ifakara hadi Mikumi ambayo nadhani inaunganisha mikoa ya Mtwara, Lindi na Songea kuja Makao Makuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii iko kwenye mpango, na kama ameangalia bajeti tayari, na baadhi ya maeneo kuanzia tumejenga Daraja lile la Magufuli pale Mto Kilombero lakini pia kuna kipande cha lami ambacho kinajengwa kati ya Kidatu kuja Ifakara, na sasa ipo kwenye mpango kwa ajili ya kuendelea na barabara kuanzia Lupilo kwenda huku Kilosa kwa Mpepo hadi kuunganisha huku Songea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachotakiwa tu ni fedha kupatikana halafu tukamilishe hiyo barabara kuu ambayo kwa kweli imekuwa ni hitaji kubwa sana kwa wananchi na Wabunge wa mikoa ya kusini ambayo ni ya Ruvuma, Mtwara, Lindi na Morogoro yenyewe. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, majibu ya Serikali ni mazuri hata hivyo majibu haya yanatofautiana na majibu ambayo Serikali hii ilijibu mwaka 2016. Wakati huo walisema kwamba wamesimamisha kutoa namba za maeneo ya utawala mpaka pale watakapokamilisha taratibu zote kwa maana ya kupata watendaji, ofisi na mahitaji muhimu ili kuweza kuwa na vijiji. Leo Serikali inasema kwamba endapo watakamilisha taratibu hizi ambazo zilishakamilika zaidi ya miaka kumi, sasa swali langu kwa je, endapo nitaleta hizo documents zote zinazotoka kwenye Halmashauri ya Wilaya Masasi, Serikali itachukua muda gani kuhakikisha namba za vijiji hivi zinatolewa? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, kumekuwa na migogoro mingi ya ardhi katika maeneo mbalimbali kwa sababu Serikali imekuwa inatoa namba lakini baadaye maeneo mengine yanatangazwa kuwa ni hifadhi, maeneo mengine ni mipaka kati majeshi pamoja na vijiji mfano Kijiji cha Chingulungulu ambapo kuna Hifadhi ya Misinjesi lakini Kijiji cha Ngalole ambapo wanapakana na Magereza ya Namajani, Wilaya ya Masasi. Vijiji hivi vyote vina namba na Serikali ipo pale inasema kwamba na yenyewe pia ni maeneo yao.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya taasisi hizi kujiridhisha kwanza kabla ya kuamua kutwaa maeneo haya ili waweze kuwalipa fidia ama yachukuliwe na Serikali? (Makofi)

Swali la pili; kulikuwa na migogoro mingi katika maeneo mbalimbali ya ardhi, kwa sababu Serikali imekuwa inatoa namba lakini baadaye maeneo mengine yanatangazwa kuwa ni hifadhi na mengine ni mipaka kati ya majeshi pamoja na vijiji, kwa mfano Kijiji cha Chingulungulu ambapo kuna Hifadhi ya Misinjesi na Kijiji cha Ngalole ambako wanapakana na Magereza ya Namajani Wilaya ya Masasi; vijiji hivi vyote vina namba na Serikali iko pale inasema kwamba na yenyewe pia ni maeneo yao.

Je, Serikali haioni sasa kuna haja ya taasisi hizi kujiridhisha kwanza kabla ya kutwaa maeneo haya ili waweze kuwalipa fidia kabla ama yachukuliwe na Serikali?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Ni kweli kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza, kwamba Serikali kwa kipindi kile cha mwaka 2016 kilikuwa kinafanya mapitio ya kukamilisha mfumo bora zaidi wa usajili wa maeneo mapya ya utawala. Kwa hiyo, tangazo na maelekezo yale ya Serikali yalikuwa sahihi na yalifanyika kwa wakati ule na ndiYo maana leo Serikali imetoa maelekezo kwamba sasa Halmashauri ya Ndanda pia tunaweza tukaanza utaratibu wa kusajili vijiji hivi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge kwamba akileta documents zinazohitajika, tutapitia taratibu husika na muda siyo mrefu sana, baada ya mamlaka kujiridhisha uhalali na vigezo vya vijiji vile, basi tutapata vijiji vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, mahusiano ya usajili wa vijiji; ili kiwe Kijiji ni lazima kipate Hati ambayo inatolewa na TAMISEMI. Hivi sasa vijiji vilivyosajiliwa kwa record yangu havipungui 12,319. Baada ya hapo kila Kijiji kinatakiwa kipate Cheti kutoka kwa Kamishna wa Ardhi ili kuonyesha mipaka ya Kijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kila Kijiji Tanzania lazima kiwe na vyeti viwili; Hati ya kusajiliwa, ni Mamlaka ya Utawala kwamba sasa mnaweza kuchaguana, ni Serikali kamili. Baada ya hapo inatakiwa Kijiji kipimwe ili kiweze kupata Hati, yaani Cheti kinachoonyesha sasa utawala wenu wa Serikali unamiliki ardhi kiasi gani. Kwa hiyo, hivi sasa kuna vijiji 1,557 ambavyo havijapata Hati au Vyeti vile vya Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nahisi namna ya kuondoa mgogoro huu wa Ndanda, kwanza ipatikane hiyo Hati ya kusajili Kijiji, halafu tukapime mipaka ya Kijiji kile. Siyo kweli kwamba Kijiji hakiwezi kuwa na msitu, kinaweza kuwa na msitu, lakini Cheti chenye heshima na kinachothaminiwa na kinachotakiwa kisheria ndani ya Kijiji ni Cheti cha umiliki wa ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, ningeomba Waheshimiwa Wabunge, tushirikiane kuhakiki kwenye vijiji vyetu kuhakikisha kila Kijiji kina vyeti viwili; kwanza, wana Hati ya kusajiliwa kama Serikali na pia vyeti vya kumiliki ardhi. Sasa ndani ya Kijiji kunaweza kuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi unaoonyesha misitu, makazi, kilimo na ufugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kuongeza hilo, sikuwa namjibia Waziri wa Maliasili, lakini nilikuwa natoa ufafanuzi kwamba kila kijiji kinatakiwa kipimwe kipewe Cheti cha Ardhi ya Kijiji. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sawa. Mheshimiwa Waziri, tunakushukuru kwa huo ufafanuzi. Nadhani hoja ya msingi ni kwamba Kijiji kinapopewa Hati lazima kuna vigezo ambavyo inatakiwa iwe navyo, ikiwa ni pamoja na ardhi na idadi ya watu. Kwa hiyo, Maliasili sasa wakienda pale, ile ardhi ambayo inajulikana ni ya Kijiji, halafu wao wakaweka hifadhi hapo, halafu na nyie mkaja mkakipunguza ukubwa kile Kijiji, nani anakuwa amekuja kwanza kabla ya hapo? Aliyemtangulia mwenzie ni nani? (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, Maliasili hawawezi kupora ardhi kwenye vijiji, hawawezi. Kwanza Maliasili hawatoi Cheti, wala hawatoi Hati. Wao wanatengeneza GN. Msitu wa Maliasili unaweza kuwa sehemu ya ardhi ya Kijiji. Kikubwa hapa ni Hati; Cheti kinachotawala ardhi ya Kijiji, lakini ndani mle kunaweza kuwa na shughuli mbalimbali hata za kibinadamu ndani ya Kijiji.

NAIBU SPIKA: Sawa, ahsante.

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Naibu Spika, mnaweza kuwa na ardhi ya Serikali au ya watu binafsi ndani ya Kijiji, lakini Cheti cha Kijiji kinaonyesha mipaka ya utawala ya Kijiji kizima pamoja na ardhi iliyopo.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Hivi karibuni na katika Jimbo lote la Ndanda kuna matatizo sana ya network na hasa eneo la Ndanda ambako ndio Makao Makuu ya Jimbo na mtandao tunaotumia pale sana ni Vodacom pamoja na Airtel na Airtel kuna hisa za Serikali. Hata hivyo, wataalam walipopewa taarifa mpaka leo hawajaenda kufanya marekebisho. Sasa kwa nini Mheshimiwa Waziri asiwakumbushe watu wa Airtel kwenda kuufanyia marekebisho mnara ule ili mawasiliano yawe bora?
NAIBU WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kimsingi ameomba Serikali tuongee na watu wa Airtel ili wakarekebishe changamoto iliyojitokeza. Tunaipokea changamoto hiyo na tutawasiliana na wenzetu wa Airtel ili kwenda kuifanyia kazi hiyo changamoto. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi kuuliza swali la nyongeza. Kuna wakati fulani sisi wakazi wa Mikoa ya Kusini hasa Mtwara huwa tunafikiri kama huwa hatuonekani na Wizara hii ya Ujenzi, na ninasema hivyo kwa sababu kuna barabara inayotoka Mtwara, Nivata, Newala, Masasi ikipitia Kata za Chikunja, Lukuledi kuelekea Ndomoni Nachingwea mpaka Liweke ilitengewa kipande hichi cha Masasi Nachingwea kilitengewa kiasi cha shilingi billioni 1.5 tu, na tulimuuliza Waziri kwamba anategemea kuanza wapi katika hili alijibu lakini hakuwa wazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninataka kufahamu kipindi cha mvua kinakaribia kuanza sasa hivi na baadhi ya maeneo mvua zimeanza kunyesha na barabara hii wakati wa mvua huwa ni usumbufu mkubwa huwezi kufika Newala kirahisi hauwezi kufika Nachingwea kirahisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa Serikali ilitenga shilingi billioni 1.5 sasa sisi tunataka kufahamu ni lini hasa na Serikali ituambie kinaga ubaga barabara hii inakwenda kutengenezwa na kukamilika sio maneno maneno yanayotokea sasa hivi. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niwahakikishie Wabunge wa Mtwara, Newala, Masasi na Ndanda kwamba barabara hii ya kilomita 210 ya kuanzia Mtwara Nivata, Ndanda, Newala hadi Masasi tumeshajenga kilomita 50 bado kilomita 160. Naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba tuko kwenye asilimia zaidi 85 na Benki ya Maendeleo ya Afrika iko tayari kuijenga hii barabara na tunauhakika kufikia mwishoni mwa mwezi wa 11 huu tutakuwa tumekamilisha mazungumzo na tunauhakika kwamba wako tayari kuijenga hii barabara. Na kipande hiki cha Masasi kwenda Nachingwea tayari tumeshatenga billion 1.5 kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge Serikali ya Awamu ya Sita haibabaishi ipo serious na kazi hii itafanyika ahsante. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, majibu haya yaliyoletwa haya reflect kabisa hali halisi iliyoko Jimboni Ndanda na Kwenye Kijiji cha Namajani hasa zaidi kwenye Vijiji wa Ngalole, Namajani, Kijiji cha Pangani na Matutwe pamoja na Mahinga.

Mheshimiwa Spika, utakumbuka swali hili nilileta kwa mara ya kwanza 2016 na majibu yaliyotolewa yanafanana na kesi hii wanakijiji hawa walishinda mahakamani mwaka 2012 na mara nyingi wizara wamekuwa wanajitetea kwa kusema kwamba wanafanya tathimini na wanatafuta pesa. Kwa mara ya mwisho wamefanya tathimini mwaka jana kabla hatujaingia kwenye bajeti kuu na hakuna pesa yoyote iliyotengwa na Serikali kwa nia ya kwenda kuwalipa kwa hiyo nina amini hawana nia njema sana ili kulimaliza jambo hili. Mgogoro uliopo sasa ni wa malipo.

Sasa swali langu kama Serikali au Magereza wameshindwa kulipa fedha hii hawaoni sasa kuna haja ya ku-vacate na kuondoka eneo hili wakawaachia wananchi wafanye shughuli zao?

Mheshimiwa Spika, swali la pili kwa sababu imekuwa ni muda mrefu sana endapo Mheshimiwa Waziri sasa atoe commitment kwamba kufikia lini jambo hili litakuwa limekwisha na wananchi wale watakwenda kupata stahiki zao. Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe Mbunge Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Mbunge anataka tu tuone namna ambavyo tunaweza tukaondoka hapa katika eneo hili, lakini nimwambie tu kwamba waliokuwepo hapa ni chombo cha Serikali ambacho kwa kusema tu tuondoke tu kirahisi rahisi nimwambie hili kwamba ni jema lakini inabidi sasa tukae tuone namna itakavyowezekana kwa sababu waliokuwepo hapa ni Jeshi na wanashughulikia wananchi na wanasaidia kutoa huduma kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, lakini Je, lini hili jambo litakwisha akisoma katika jibu langu la msingi ni kwamba Tayari tumeshaanza hatua kwanza za uhakiki kujua nani anastahili kulipwa na nani hastahili kulipwa zaidi ukizingatia kwamba mahakama amri hapa mahali sisi tuondoke. Kikubwa ni kwamba tunaenda kutafuta fedha kwa sababu hizi fedha siyo kidogo ili tuweze kuwa compensate hawa waliokuwepo basi tuone namna itakavyowezekana, nakushukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kwenye Jimbo la Ndanda tuna mradi mkubwa wa maji uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni tano uliokusudiwa kuhudumia Kata ya Mwena, Kata ya Chikundi pamoja na Kata ya Chikukwe. Hata hivyo mradi huu unafanya kazi kwa kiwango cha chini kabisa kwa sababu inaonekana ilikuwa ni poor designing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali langu kwa Mheshimiwa Waziri, je, haoni haja ya kuwaagiza wataalam wake wakakague mradi huu na kupeleka mapendekezo bora Serikalini, ili kuweza kuboresha ili wananchi wa Kata hizo wapate maji kwa kipindi chote cha mwaka?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi la kupeleka wataalam wakakague mradi huu na ni mradi ambao unakwenda kugharimu Serikali fedha nyingi zaidi ya Shilingi bilioni tano. Hii ni moja ya majukumu yetu Mheshimiwa Mbunge, tayari Mheshimiwa Waziri, amewasisitiza sana watendaji wanatakiwa kufuatilia hii miradi. Hivyo, nami napenda kusisitiza Managing Director na Regional Manager wa Mkoa wa Mtwara wahakikishe wanakwenda kusimamia huu mradi kuona unatekelezwa kadri ambavyo unapaswa kuwa. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama utakumbuka mwaka jana mwishoni, Mheshimiwa Spika aliunda Kamati Maalum kabisa ambayo ilikuwa ni Kamati ya Viwanda na Biashara pamoja na Kamati ya Bajeti na tulikaa kwa nia ya kutaka kupitia mambo mbalimbali kwa sababu tulipokea taarifa za malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara kuhusiana na bei kubwa za stamp za kielektroniki. Lakini nimesimama hapa nikwambie tu kwamba pamoja na mazungumzo yale Serikali au TRA waliendelea kusaini mkataba huo ambao umekuwa wa kinyonyaji kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nimuulize Waziri wetu wa Katiba kwamba je, yupo tayari sasa kuleta mkataba kati ya SICPA na Serikali unaohusisha masuala ya stamp za kielektroniki ili tuweze kuwasaidia wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili, pamoja na hiyo mikataba mingi uliyoisema na sisi kama Wabunge wengi tunatamani kujifunza na wengine siyo wahudhuriaji kwenye Kamati hizo ulizozitaja. Hauoni sasa ni wakati mikataba hiyo kwa mfano hiyo SGR, mkataba wa Bandari ya Bagamoyo, mkataba wa gesi wa kule Mtwara na mingine mingi kuwa wazi kwa Wabunge wote kuisoma na kupata uelewa wa kina kuweza kuishauri Serikali? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikianza na swali la nyongeza la kwanza la Mheshimiwa Mwambe hili linalohusu stamp, nadhani tutafanya mawasiliano na taasisi inayohusika ili tuweze sasa kujiweka sawa katika eneo hili ambalo limeonesha mashaka ya mkataba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili kuhusu suala la kuwasilisha mikataba katika Bunge lako tukufu kama nilivyoeleza mwanzo, mikataba hii huwa inapita kwenye Kamati kwa sababu ndiyo taratibu zilizowekwa. Kama Bunge lako tukufu litataka mkataba ufikishwe mbele ya Bunge lote basi maamuzi yanatoka kwenye Kamati baada ya kupitia zile taarifa zinazowasilishwa. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwenye Wizara hii. Kati ya wilaya kongwe zilizoko nchini Tanzania, ni pamoja na wilaya ya Masasi pamoja na wilaya ya Nachingwea. Hata hivyo wilaya ya Nachingwea na Masasi zinaungwanishwa kwa barabara yenye urefu wa kilometa 42, wilaya ile sasa ina miaka zaidi ya 50 kwa sababu ilikuwepo hata kabla ya uhuru na ilikuwa na jina lingine…

SPIKA: Uliza swali lako Mheshimiwa Mwambe.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Sasa swali langu, ili kukuza uchumi wa Nachingwea tunahitaji barabara hii ijengwe kwa lami…

SPIKA: Uliza swali.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Ni lini Serikali itahakikisha barabara ya Nachingwea Masasi yenye urefu wa kilometa 42 inaunganishwa kwa lami?
WAZIRI WA UJENZI NA UCHUKUZI: Mheshimiwa Spika, ninaomba kumjibu Mheshimiwa Mwambe kama ifuatavyo. Barabara Masasi Nachingwea yenye urefu wa kilometa 41 ni kweli ni barabara ya siku nyingi na sisi tunaitambua hivyo na tuko kwenye mpango wa kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha ili tuweze kujenga kwa kiwango cha lami.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, majibu ya Serikali ni mazuri kama tulivyosikia, lakini swali: Mpaka sasa kiasi kinacholipwa kutoka kwenye dhamana ni shilingi 1,500,000 tu hata kwa mteja aliyeweka pesa nyingi sana na wanasubiri kuuza mali za benki ndipo waweze kuwalipa; na benki nyingine hazina mali za kutosha.

Je, Serikali haioni kuna haja sasa ya kuleta sheria kwenye Bunge hili ili kuweza kuwasaidia wateja wa benki hizi? Benki ya Greenland, pamoja na benki ya FBME na zenyewe zimefilisika kwa muda mrefu na sasa tunaona Covenant Bank lakini hakuna muda mahususi wa kufanya minada na kuwalipa wateja: -

Je, Serikali na yenyewe haioni kuna haja ya kupanga specific time ili kuweza kuuza mali hizo na ikishindikana Serikali ichukue dhamana hiyo? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, kabla ya kujibu naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Cecil Mwambe kwa maswali yake haya mazuri, maana yake maswali yake yanaonekana ni mawazo ushauri. Mfano swali la mwanzo, Serikali inalichukua wazo hili na ushauri huu wa kuongeza idadi ya kulipa hiyo fidia ya shilingi milioni moja na nusu kwa wale ambao amana yao iko zaidi ya shilingi milioni moja na nusu.

Mheshimiwa Spika, la pili pia inaonekana ni ushauri kwetu. Kwa hiyo, Serikali itatenga muda mahususi au wakati mahususi wa kukusanya mali na madeni kwa zile Benki ambazo zimefilisiwa na Serikali kwa mujibu wa sheria. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza kwa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata za Nanganga, Nangoo, Ndanda, Mwenda, Chikundi, Chigugu, Chikukwe, Chikunja pamoja na Lukuledi ambazo zinapitiwa na barabara kuu inayokwenda Nachingwea kutokea Masasi au barabara kuu inayotoka Mingoyo kulekea Mbamba Bay na Songea. Kwa muda mrefu sasa zaidi ya miaka Kumi hadi Ishirini nyumba za watu pamoja na mali zao zimewekewa alama za X. Ziko alama za X za kijani lakini pia zipo alama za X nyekundu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi hawa wameshindwa kufanya shughuli zao zozote kwa sababu hawaelewi tafsiri ya alama hizi. Nataka kauli ya Serikali itueleweshe ni nini maana ya kuweka alama (X) nyekundu au alama (X) ya kijani kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, alama hizi zinaonesha kwamba wananchi wamejenga kwenye hifadhi ya barabara ama barabara itapita kwenye maeneo hayo. Wapo ambao barabara imewafuata kijani na wale ambao watatakiwa kufidiwa walikuwepo barabara wamewekewa alama ya (X) lakini ni kwamba hawa wote wataondolewa kwa utaratibu na kwa mujibu wa sheria. Ahsante. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri ya Serikali, lakini kumekuwa na uendelezaji mdogo sana wa miradi ya REA iliyopo kwenye Majimbo yote ya Mkoa wa Mtwara.

Swali la kwanza; pamoja na mikakati hii ya Serikali ya kutaka kuimarisha upatikanaji wa umeme kwenye wilaya zetu, ni lini sasa tutahakikisha Miradi ya REA iliyopo kwenye Majimbo yote ya Mkoa wa Mtwara inakamilika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; tunataka kufahamu kwa uhakika kwa sababu mpaka sasa kuna vijiji zaidi ya 300 havijapatiwa umeme, wanaleta umeme wa grid kutoka Mtwara na hii wanayosema kutoka Mombika ili kuimarisha upatikanaji wa umeme kwenye Wilaya ya Masasi, nayo tunaomba kufahamu miradi hii itaanza kutekelezwa lini?
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa David Cecil Mwambe kwa pamoja, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, mikataba mingi ya REA III, round two ilikuwa inatakiwa kuisha Desemba, lakini kwa changamoto ambazo zilijitokeza ambazo tayari tulishazisema, muda wake wa kukamilika utaongezeka kidogo kulingana tofauti tofauti ya maeneo. Hata hivyo, nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine wote kwamba Serikali kupitia Wizara ya Nishati inahakikisha kwamba mikataba hii inakamilika na wananchi wanapata umeme katika vijiji vyao, kwa sababu pesa ipo na usimamizi unaendelea kufanyika wa karibu. Kwa hiyo, tutaendelea kulisimamia hili ili umeme uweze kupatikana katika maeneo yetu.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Kimsingi ninachotaka kufahamu ni kwamba mradi huu utakamilika lini? Kwa sababu kumekuwa na tatizo kubwa sana la maji kwenye Wilaya ya Newala, Tandahimba pamoja na Nanyamba hasa zaidi wakati wa kiangazi ambacho ndiyo tunakwenda sasa hivi. Sasa nataka kufahamu ili kuwapa comfort wananchi, mradi huu utakamilika lini ili waweze kupata maji safi, salama na ya kutosha?
NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, katika jibu la msingi, nimeeleza kuwa awamu ya tatu na ya nne itakamilika mnamo mwezi Desemba, mwaka huu wa 2022.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza. Kwa namna ya pekee nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Naibu Waziri na Waziri na Wizara nzima ya Maji kwa utekelezaji wa miradi hii aliyoitaja swali lake na majibu ni mazuri sana. Hivi sasa Kata ya Nanganga, Mumburu unatekelezwa mradi wa maji wa shilingi milioni 500, Ndanda shilingi milioni 400, Chiwata mradi unaendelea shilingi milioni 500. Hata hivyo, napenda kufahamu toka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, wakati wa usanifu wa miradi ya Kata ya Mpanyani alipokuja Katibu Mkuu tulikubaliana kwamba Kijiji cha Mraushi patawekwa tenki. Je, ni lini kazi ya ujenzi wa tenki Kijiji cha Mraushi itaanza kufanyika?

Mheshimiwa Spika, swali la pili; kati ya Mwena na Liloya kuna mradi unaoendelea. Kwa bahati mbaya sana mradi huu unafanya kazi vizuri sana wakati wa mvua na wakati wa kiangazi haufanyi kazi vizuri, unahitaji tena kufanyiwa marekebisho. Je, ni lini Serikali itakwenda kuufanyia marekebisho Mradi wa Liloya-Mwena? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba nipokee pongezi, nafahamu anayeshukuru anaomba tena, tutarudi Ndanda tutaendelea kufanya kazi pamoja Mheshimiwa Mbunge na nampongeza Mbunge kwa uwajibikaji wake mzuri.

Mheshimiwa Spika, ujenzi wa tenki tunautarajia ndani ya mwaka wa fedha 2022/2023 uweze kukamilika. Vile vile katika ule mradi ambao tayari unatoa huduma japo maji kidogo yana chumvi na wakati wa kiangazi inaleta shida, Mheshimiwa Mbunge hili tumeshaliongea mara nyingi, amefika ofisini na sisi tayari tumeshalifanyia kazi, tumeshatoa maagizo pale Mtwara. Kwa hiyo, litaendelea kuangaliwa kwa jicho la kipekee kuhakikisha wananchi wanakwenda kupata maji safi, salama na ya kutosha. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Barabara ya Lupio – Malinyi- Kilosa kwa Mpepo- Londo mpaka Lumecha ina umuhimu sana sawasawa na ilivyo barabara ya Masasi -Nachingwea - Liwale- Lupilo - Malinyi mpaka Kilosa inaunganisha Mkoa wa Lindi na Mtwara. Nini mkakati wa Serikali kuunganisha kipande hiki cha barabara ili kuwasaidia wakazi wa Mkoa wa Mtwara na Lindi kufika Dodoma kirahisi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, barabara hii iko kwenye mpango wa Serikali kuijenga, kwa hiyo nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba kadri Serikali inavyopata fedha barabara hii itajengwa ili kurahisisha mawasiliano kati ya Wilaya hizo mbili. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri kabisa ya Waziri na tumekuwa tunafanya mjadala kwenye jambo hili.

Nimhakikishie kwamba Mkandarasi tayari yupo site, kwenye Kata ya Mpanyani hajaanza kazi imeanza Kata ya Msikisi, Je, ni lini Mkandarasi huyu ataanza kazi pia katika Kata ya Mpanyani ili kuweza kufanya kazi yake kwa wakati tuliokubaliana?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali langu la pili Kitongoji cha Ndolo kilichopo kwenye Kata ya Ndanda kiko mita 200 tu kutoka Shule ya Sekondari ya Ndanda lakini kitongoji hiki kimekosa umeme kwa muda mrefu sana.

Sasa niombe Mheshimiwa Waziri utoe maelekezo kumwelekeza Engineer wetu wa Mkoa Ndugu yetu Fadhili kwamba ni lini atapeleka umeme kwenye Kitongoji cha Ndolo kwa sababu kipo mjini kabisa lakini hakina umeme na kuna wakazi wengi ambao wameshafanya wiring? Ahsante.
WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu maswali mawili madogo ya Mheshimiwa Cecili David Mwambe Mbunge wa Ndanda kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, nakubaliana kwamba kuna haja ya kuharakisha ili Mkandarasi huyu afanye kazi kwa pamoja katika vijiji vyote kwa mpigo na nimepokea pia ushauri na maombi ya Mheshimiwa Mbunge kwamba Mkandarasi huyu pia apeleke umeme katika kitongoji hicho na jambo hilo linawezekana.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Kwanza kabisa majibu ya Serikali, swali langu lilisema ni lini? Sasa Serikali wanasema wapo kwenye hatua za kukamilisha utaratibu wa financial. Sasa nataka kufahamu, huu utaratibu wa financial utakamilika lini ili kuweza kutoa pesa kwa ajili ya kujenga hiyo barabara kwa kiwango cha lami kwa sababu Wilaya ya Nachingwea na Wilaya ya Masasi na Wilaya nyingine pale hazijaunganishwa kwa muda mrefu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kuna barabara ambayo pia inaendelea kujengwa kwenye eneo hilo hilo kati ya Nanganga – Ruangwa, inaunganisha hizo Wilaya mbili, lakini jengo la Chama cha Mapinduzi, Ofisi ya Kijiji, Msikiti pamoja na majengo ya wananchi mbalimbali yalivunjwa sawa sawa na hii barabara ninayoisema ya Nachingwea – Masasi: Ni lini Serikali italipa fidia kwa watu hawa waliopata athari za kuvunjiwa majengo yao kwa sababu ya ujenzi wa barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze na suala la kwanza ambalo pia umetaka nitoe maelezo kwa Waheshimiwa wote. Ni kweli tuna barabara nane ambazo zimeingizwa kwenye mpango wa EPC + F. Katika barabara nane, barabara itakwenda kwa Mpango wa PPP ambayo ni barabara ya Kibaha - Chalinze hadi Morogoro. Hiyo itaingia kwenye PPP na barabara zilizobaki hizo saba ambazo ni pamoja na hii niliyoisoma ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale zimeingizwa kwenye Mpango wa EPC + F.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu ni mfumo ambao ni mpya ambapo wakandarasi wanatafuta fedha, wanajenga, halafu Serikali inatafuta utaratibu wa namna ya kuja kuwalipa kwa makubaliano ambayo yatakuwepo. Sasa kuna sehemu mbili; kuna sehemu ya Engineering ambayo ni Wizara ya Ujenzi wanakwenda na wakandarasi wanaangalia, wana-bid, wanaagalia kwa upande wa ufundi na kuona kwamba wamekubaliana, halafu baada ya hapo sasa, wanapeleka hiyo mikataba Wizara ya Fedha ili kuona kama kwa kuingia nao mikataba hiyo Serikali itakuwa imefanya jambo sahihi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mfumo ambao ni mpya ambao ni lazima Serikali iende kwa umakini sana ili tusije tukaingia kwenye mkataba ambao hatukujipanga vizuri. Kwa hiyo, kuna umakini mkubwa sana ambao unafanyika ili tuweze kwenda na miradi hii mikubwa ambayo kama tutaijenga, basi tutakuwa tumepunguza kero nyingi sana za usafiri. Tumechukua barabara nyingi zile ambazo ni ndefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa idhini yako nitataja barabara chache. Ni Barabara ya kutoka Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo hadi Namtumbo. Tuna barabara ya Mafinga hadi Mgororo, tuna barabara ya Kongwa – Kibaya hadi Arusha, tuna barabara ya Karatu hadi Arusha, tuna barabara ya Karatu – Mbulu – Hydom hadi Sibiti. Pia tuna barabara ya Masasi – Nachingwea hadi Liwale; na tuna barabara ya Igawa – Songwe hadi Tunduma. Hizo ni baadhi ya barabara ambazo zimeingia kwenye mpango huu. Kwa hiyo, ukiangalia ni barabara kubwa ambazo tungetamani tuzijenge kwa wakati mmoja kwa utaratibu huu wa EPC +F, ahsante. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu mazuri kabisa ya Serikali, ninashukuru sana kwa uamuzi huu uliofikiwa sasa hivi, Mheshimiwa Waziri atakubaliana na mimi kwamba kuna mkanganyiko mkubwa hasa zaidi kwenye Sheria hizi mbili za Sheria ya Ndoa na Sheria ya Mtoto. Mtoto anatambulika chini ya miaka 18 lakini ndoa inaruhusiwa kufungwa akiwa na miaka 14. Kwa hiyo, ushauri wangu ni kwamba tunaiomba Serikali sasa ilete kwa haraka sasa sheria hii ili Wabunge tuweze kuipitia na kuifanyia marekebisho makubwa.

Mheshimiwa Spika, hoja yangu ya pili ni kwamba kumekuwa na usumbufu mkubwa sana kwa Wajane na Wagane hasa wanapofuatilia masuala ya mirathi na yenyewe hapa kwenye majibu ya Serikali wamasema watahakikisha wanaleta kwenye Bunge hili, tunataka tufahamu wakati mahususi kwa sababu sheria hii imepitwa na wakati ili iweze kujadiliwa na Wabunge na kupata matokeo mazuri. Ahsante. (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Spika,
nakushukuru, naomba nijibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Cecil Mwambe kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Spika, nakubliana nae kwamba Sheria hii ya Ndoa kuna baadhi ya vifungu ambavyo kwa kweli vimekuwa vikilalamikiwa hasa kile kifungu cha 13 na kifungu cha 17 ambazo zimetofautina katika umri wa mtoto wa kike kuolewa, lakini wakati mwingine Mahakama imekuwa ikitoa ruhusa hiyo pale wazazi wanapokuwa wameridhia, ndiyo maana Wizara tumeshakamilisha mchakato huu sasa tuwaleteeni katika Bunge hili tuweze kuamua na umri ambao utakuwa umependekezwa tutauona katika Muswada ambao tutauleta katika Bunge hili.

Mheshimiwa Spika, swali lake la pili ameeleza kuhusu Wagane na Wajane ambao wamekuwa wakisumbuliwa katika masuala ya mirathi. Nimeeleza katika Sheria hizi ambazo zinasimamia mirathi ya kidini lakini pia wale ambao wanatumia Sheria hii ya Indian Succession nimeeleza kwamba taratibu hizi zipo lakini bado kuna malalamiko ndiyo maana Tume yetu ya Kurekebisha Sheria tumeiagiza pia ifanye utafiti watuletee. Katika Bunge hili tunategemea kuleta marekebisho ya Sheria zaidi ya 27.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuweza kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni mwezi mmoja sasa tangu nisimame hapa nikiuliza kuhusu Barabara ya Masasi – Nachingwea, na Mheshimiwa Naibu Waziri utakumbuka ulinijibu kwamba iko kwenye hatua za financing. Na niliuliza lini mchakato huo utakamilika, hatukuweza kupata majibu wakati ule. Sasa ninauliza tena: -

Ujenzi wa Barabara ya Nachingwea – Masasi ambao ulikuwa kwenye hatua ya financing; hatua hiyo itakamilika lini?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii ya Masasi Nachingwea inakwenda mpaka Liwale. Kama nilivyosema, ni kati ya barabara saba ambazo ziko kwenye EPS+F; na taratibu za manunuzi kwa maana ya upande wa finance kwa wenzetu wa fedha bado zinaendelea zote kwa pamoja, kwa barabara zote saba. Kwa hiyo zitakapokuwa mchakato huu umekamilika tutamjulisha Mheshimiwa Mbunge.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niulize swali la nyongeza. Kata ya Ndanda wananchi walijitolea, lakini pia walishiriki na nguvu ya Ofisi ya Mbunge kwa maana ya Mfuko wa Jimbo, kukamilisha Kituo cha Afya baada ya kupata pesa Shilingi milioni 50 kutoka Serikali Kuu. Sasa hivi limebaki suala moja tu ili iweze kufunguliwa, ambalo ni choo. Mheshimiwa Waziri yuko tayari kutoa maelekezo kwa DED wa Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, DC, wakamilishe choo hicho ili zahanati ianze kutumika?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DEOGRATIUS J. NDEJEMBI): Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri mbele ya Bunge lako hili kwamba Mheshimiwa Mwambe alishakuja kulifuatilia jambo hili ofisini kwa karibu kabisa. Nitumie nafasi hii kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kumwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha anajenga choo hiki kupitia mapato yake ya ndani ili huduma ziweze kuanza kutolewa katika kituo hiki.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Ninapenda kufahamu kwenye Vijiji vya Mpanyani Shule ya Sekondari, Huria, Chiroro, Masiku pamoja na Namichi tayari pameshachimbwa visima virefu. Je, ni lini sasa Serikali iko tayari kuweka pampu kwenye maeneo haya ili wananchi waweze kupata maji?
NAIBU WAZIRI WA MAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil David Mwambe, Mbunge wa Jimbo la Ndanda, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji hivi alivyovitaja vyote tunatarajia viweze kuendelezwa visima vilivyochimbwa. Tumshukuru Mheshimiwa Rais tumeendelea kupata fedha za P4R, Mikoa yote itapelekwa fedha, kwa hiyo tunatarajia sasa distribution itakwenda kufanyika na wananchi wataanza kunufaika na visima vilivyochimbwa.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Spika, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo iliahidi kupeleka mbegu bora za soya kwenye vijiji vingi vilivyopo Jimbo la Ndanda ikiwemo Kijiji cha Mumburu kwa sababu soya ilikuwa inalimwa hapo zamani, ni mwaka wa tatu sasa mbegu hiyo haijaenda.

Je, ni lini Serikali itatimiza ahadi yake ya kupeleka mbegu kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, nimesikiliza hoja ya Mheshimiwa Mbunge, nimeichukua. Tutakwenda kuifanyia kazi ili wakulima wake waweze kupata mbegu za soya. (Makofi)

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ni miezi mitatu sasa Barabara ya Masasi – Nachingwea mkataba ulisainiwa;

Je, ni lini ujenzi wake utaanza? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, barabara kama nimemsikia Masasi – Nachingwea – Liwale ni barabara ambazo ziko kwenye EPC+F na taratibu za kuzijenga hizi barabara zote zinaendelea, ikiwa ni pamoja na kuangalia maeneo ya kujenga makambi, kuvigawa vipande ambavyo vitatumika kujenga hizo barabara lakini pia mkandarasi kupitia upya usanifu na kuangalia fidia ambazo zitalipwa kwa wananchi ambao wataathirika na ujenzi. Kwa hiyo taratibu zimeshaanza na zinaendelea. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza sikubaliani na majibu yaliyotolewa na Serikali na swali hili limerudi kwa mara ya pili baada ya maelekezo ya Mheshimiwa Spika wakati fulani hapo nyuma kwa sababu zifuatazo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili tunalolizungumzia barabara ilihama kwenye original plan na barabara hii imewafuata wananchi. Kwa sababu hiyo haina qualification ya mita 22 wala mita hizo zinazotajwa 22.5 wala nyongeza ya mita 7.5. Mheshimiwa Waziri Mbarawa alifika kwenye hiki kijiji tarehe 22 mwezi wa kwanza, mwaka 2022 eneo ambalo Misikiti, Kanisa pamoja na Nyumba za Serikali zilivunjwa. Swali langu la msingi ni lini Serikali itakwenda kulipa fidia kwa sababu wenyewe walifuatwa na barabara na si wao waliifuata barabara? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama nilivyosema kwenye jibu langu la msingi; kwamba kama barabara imemfuata mwananchi ama imehama na kwenda sehemu ambayo haikuwepo maana yake hawa watu wanastahili fidia; na kama suala alilolielezea Mheshimiwa Mbunge kwamba barabara imehama kabisa. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wananchi hawa watakuwa wanastahili fidia. Kwa hiyo, kwa sababu swali lake ni specific na eneo linalohusika, naomba baada ya hapa tuweze kukutana naye ili tuweze kuangalia. Kama barabara iliwafuata hawa wananchi kama alivyosema basi wananchi hao wana haki ya kulipwa fidia. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi ya kuuliza swali la nyongeza. Mheshimiwa Waziri, Chuo cha TARI Naliendele zaidi ya miaka 20 sasa wamekamilisha utafiti unaoonesha kwamba kutokana na nipa inayopatikana kwenye korosho ina uwezo wa kuzalisha ethanol methanol pamoja na alcohol kwa matumizi ya burudani pamoja na hospitali, lakini pia kuongezea kipato wakulima na kupunguzia Taifa hili hasara. Je nini mkakati wa Serikali kuhakikisha sasa nipa inakuwa rasmi kwa ajili ya kupunguzia hasara Taifa letu?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mbunge, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumesikia hoja ya Mbunge, tutaishirikisha TARI pamoja na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali ili ikibainika kwamba nipa hiyo inaweza ikatumika katika maeneo ambayo ameyataja, basi sisi kama Serikali kwa kushirikiana na TARI tutasaidia kuongeza mnyororo wa thamani wa zao la korosho.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Spika, mwezi Septemba ni mwezi ambao tunategemea kuanza kilimo katika maeneo yetu;

Je, Serikali haioni haja ya kuwataka Benki ya CRDB waanze kutoa mikopo kwa wakulima ili waweze kutayarisha mashamba yao? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, Kata za Msikisi, Kijiji cha Namalembo na Matutwe, Chiwalwe, Namajani pamoja na Mpanyani zipo mbali sana na makao makuu ya wilaya ambako ndiko zinatolewa huduma za kibenki kwenye Jimbo la Ndanda;

Je, Serikali haioni haja ya kuwasogezea wananchi huduma kwenye maeneo hayo?
NAIBU WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, naomba kujibu Maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimuhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba benki itatoa huduma zote mara tu baada ya kukamilika kule Liwale ikiwemo mikopo CSR na mengineyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu swali lake la pili, tutashauriana na benki ili wapeleke huduma hizo za kibenki katika zile kata ambazo hazijafikiwa na benki ili kuepusha utapeli ambao unafanyika katika shughuli za wanadamu kiuchumi za kila siku.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Barabara inayoanzia Nanganga kwenda Ruangwa inajengwa sasa kwa kiwango cha lami. Hata hivyo, wakazi wa Nanganga wanadai fidia. Ni lini Serikali italipa fidia kwa watu waliobomolewa nyumba zao eneo la Nanganga? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI (MHE. ENG. GODFREY K. MSONGWE): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge kama ifuatavyo:_

Mheshimiwa Spika, tumekuwa na utaratibu wa kulipa fidia tunapoanza ujenzi wa barabara zote. Namwomba Mheshimiwa Mbunge, kama kuna changamoto kwa hiyo barabara, tuweze kuonana ili tujue tatizo ni nini ambapo wananchi hao wanaodai mpaka sasa hivi wakati barabara inajengwa na tulitatue kwa kuwalipa fidia hao wananchi wa barabara ya Nanganga hadi Ruangwa, ahsante.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana na mimi kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza, kwamba kazi ya mshauri ilifanyika toka mwaka 2016 ikiwa ni pamoja na uthamini kwenye eneo ambalo reli hii itakwenda kupita.

Ni lini sasa Serikali itaanza kulipa fidia kwa wananchi waliopo kwenye eneo ambalo reli hii ambapo mradi unaenda kutekelezwa? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UCHUKUZI (MHE. ATUPELE F. MWAKIBETE): Mheshimiwa Spika, ahsante, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimekwisha kusema kwamba upembuzi yakinifu ulikwishafanyika tangu miaka hiyo ya 2016 na Serikali hatua iliyofikia sasa ni kumuajiri Transaction Advisor kwa maana ya Mshauri wa Kifedha ambaye ndiye atakayetupa miongozo yote hadi kulipa fidia, lakini pia kupitia mthamini mkuu kwa sababu hili jambo lilishafanyika miaka mingi kwa vyovyote vile kutakuwa na haja ya kurudia kupitia daftari ambalo lilikuwa limeandaliwa kipindi hicho, nashukuru.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kazi ya usambazaji umeme kwenye vijiji ambavyo Mheshimiwa Naibu Waziri amevitaja unaendelea, lakini hata hivyo kazi hii bado inafanyika kizamani, kwa maana ya kwamba inafanyika tu sehemu kubwa ya makao makuu ya kata. Lakini inasababisha sasa kwa mfano Kijiji cha Mumburu A na B kwenye vitongoji vya Chalinze na Mtakuja. Lakini pia Chipite, Mkang’u, Mwongozo na Nganga A Shule ya Msingi, Mbemba pamoja na Namali kazi ya kuweka umeme inafanyika kwenye maeneo madogo sana, kwa maana ya scope.

Mheshimiwa Naibu Spika, je, Wizara haioni kuna haja maeneo mapya wanapoweka umeme wakafanya kazi kubwa tofauti na ilivyokuwa zamani wanapeleka nguzo 20 tu?

Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili; kwenye Wilaya yetu ya Masasi kumekuwa na tatizo kubwa sana la kukatika katika kwa umeme na Serikali hii ilituahidi kwamba itatengeneza line ya pekee kutoka Maumbika mpaka Masasi kwa bajeti ya shilingi bilioni 10. Nataka nifahamu kutoka kwa Mheshimiwa Naibu Waziri, kazi hiyo inakusudiwa kuanza lini? Ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Cecil David Mwambe kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kwenye swali la kuongeza wigo wa upelekaji wa umeme kwenye vitongoji, nikiri kwamba kweli bado tunavyo vitongoji vingi ambavyo havijafikiwa na miundombinu ya umeme, lakini Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan imejitahidi kwa kuanzia na mradi wa REA III round two kwa kupeleka umeme kwenye vitongoji vya kuanzia katika vijiji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo tumeshasema hapa mara kadhaa, Serikali inatafuta pesa ya kutosha kabisa kuweza kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote nchini vilivyobakia takribani trilioni sita zinahitajika kwa ajili ya kukamilisha kazi hii na hatua za kuendelea kutafuta pesa hiyo zinaendelea na tunaamini chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan tutafanikiwa kwa jambo hilo katika muda mfupi unaokuja.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye swali la pili, ni kweli Serikali iliahidi kujenga njia ya msongo wa kilovoti 33 kutoka Maumbika kuja mpaka Masasi na tayari upembuzi umeshafanyika na pesa imeshapatikana na katika bajeti ambayo tunaisoma hapa kesho kipande hicho ni kimoja wapo katika ambavyo tunaviahidi kuvitekeleza katika mwaka wa fedha unaofuata. Nashukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Kumekuwa na utaratibu sasa hivi, wazee wanatufuata kule vijijini au watoto wao wakiamini kwamba wanadai fidia kutokana na ushiriki wao kwenye Jeshi lile la Mkoloni (KAR) au Vita ya Kagera. Nataka kufahamu kutoka Serikalini, hivi ni kweli kuna watu wanaodai fidia kutokana na maeneo hayo mawili niliyoyataja kwa maana Jeshi la KAR pamoja na Jeshi la waliokwenda kupigana kwenye Vita ya Kagera?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kwa sababu swali la msingi ni Vita ya Kagera, naomba suala la KAR liweze kuletwa kama swali la msingi ili tuweze kulifanyia utafiti na hatimaye tutoe majibu fasaha katika Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu uwepo wa Wazee wa Vita ya Kagera ambao pengine wanalalamika kutopata fidia, ndiyo maana nimesema, tunazo takwimu kwamba wapo 272, kama wapo wazee wa namna hiyo Mheshimiwa Mbunge, nimeeleza hapa katika moja ya jibu la msingi kwa Mbunge aliyetangulia, waripoti kwenye Makambi ya Jeshi yaliyoko karibu na maeneo yao ili taarifa zao zihakikiwe, hatimaye waweze kapata haki wanayostahili, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, Jimbo la Ndanda lenye kata 16 tunacho Kituo cha Polisi kimoja tu kilichopo Ndanda. Hata hivyo, majengo ya Kituo cha Polisi pamoja na nyumba ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Ndanda, kwa maana ya OCS, ni mali ya Wamisionari wa Benediktini wa Ndanda. Kutokana na umuhimu na ukubwa wa Jimbo la Ndanda, kuna haja ya kuwa na Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Chiwale. Nini msimamo wa Serikali wa kujenga Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Chiwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tunaongea kwa nyakati tofauti, ni dhamira ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba kata zote na tarafa za kimkakati zinajengewa vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyakati tofauti nimeongea na Mheshimiwa Mbunge wa Ndanda na ninamshukuru sana kwa namna anavyofuatilia suala la usalama wa raia wa jimbo lake; na kwa vile kuna mfuko wa jimbo kidogo ambao anapata, wajitahidi tu kuanzisha ujenzi na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi lita-support ujenzi wa hicho kituo hadi kitakapomalizika, nashukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi, nina swali kwa Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba, Jimbo la Ndanda lenye kata 16 tunacho Kituo cha Polisi kimoja tu kilichopo Ndanda. Hata hivyo, majengo ya Kituo cha Polisi pamoja na nyumba ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Ndanda, kwa maana ya OCS, ni mali ya Wamisionari wa Benediktini wa Ndanda. Kutokana na umuhimu na ukubwa wa Jimbo la Ndanda, kuna haja ya kuwa na Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Chiwale. Nini msimamo wa Serikali wa kujenga Kituo cha Polisi kwenye Kata ya Chiwale?
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo tunaongea kwa nyakati tofauti, ni dhamira ya Serikali ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kwamba kata zote na tarafa za kimkakati zinajengewa vituo vya Polisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nyakati tofauti nimeongea na Mheshimiwa Mbunge wa Ndanda na ninamshukuru sana kwa namna anavyofuatilia suala la usalama wa raia wa jimbo lake; na kwa vile kuna mfuko wa jimbo kidogo ambao anapata, wajitahidi tu kuanzisha ujenzi na Wizara ya Mambo ya Ndani kupitia Jeshi la Polisi lita-support ujenzi wa hicho kituo hadi kitakapomalizika, nashukuru.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Jimbo la Ndanda tuna skimu mbili za umwagiliaji ambazo ni Mkwera, Kata ya Nanganga pamoja na Skimu ya Ndanda, skimu hizi ziko kama zimekuwa abandoned, sasa nimuombe Mheshimiwa Waziri, kwa sababu ya uwekezaji mkubwa ambao ulifanyika pale, nini malengo ya Serikali na skimu hizi mbili ili ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa vizuri?
NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Cecil Mwambe, Mbunge wa Ndanda, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja kati ya kazi kubwa ambayo tumeipa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ni kuhakikisha inapitia miradi yote ya umwagiliaji nchini Tanzania kwa maana ya kufahamu status zake, tujue ipi inafanya kazi, ipi imekwama na ipi inahitaji namna gani iweze kutoka hapo ilipo iendelee kufanya kazi. Kwa hiyo, nimuahidi Mheshimiwa Mbunge kwamba siyo dhamira yetu kuiacha na kui-abandon miradi hiyo mikubwa ya umwagiliaji, tutaifanyia kazi kuhakikisha kwamba inafanya kazi ili tutimize lengo la kuwa na eneo kubwa la umwagiliaji hapa nchini.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, Vita ya Pili ya Dunia ilikwisha mwaka 1945 na wapiganaji Tanzania walikuwa 680 na sasa wamebakia 58 maana yake wanazidi kuisha na Serikali haijafanya uhakiki ili waweze kulipwa fidia ama kurejeshewa mali zao nataka nifahamu ni lini Serikali itamaliza zoezi la uhakiki ili hawa watu waweze kupata stahiki zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, swali la pili, kulikuwa na Vita ya Kagera pia hapa Tanzania waathirika wa Vita ya Kagera pamoja na Wanajeshi Wastaafu wako mtaani, kila mara wamekuwa wanakwenda kwenye Ofisi za Wilaya kujiandikisha wakiamini kwamba wanastahili kupata stahiki zao lakini pia pamoja na pensheni na matibabu. Ni lini Serikali itakamilisha taratibu hizi ili hawa watu wetu ambao ni wazalendo waweze kupata haki zao za msingi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI K.n.y. WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Spika, kuhusu lini tutamaliza zoezi hili naamini muda si mrefu kwa sababu awali tulikuwa tunawasiliana na Serikali ya Uingereza, baadaye tukabaini kwamba KAR hawa taarifa zao zilikuwa makao makuu ya wakati huo Nairobi, sasa hivi Wizara yetu ya Mambo ya Nje inawasiliana na wenzetu wa Kenya ili kupata taarifa hizo na kwa sababu kwa sasa waliopo ni wachache tunaamini baada ya miezi miwili tutakuwa tumepata taarifa hizi.

Mheshimiwa Spika, kuhusu hawa wa Vita ya Kagera tumeshajibu swali kama hili huko nyuma ni kwamba baada ya Vita ya Kagera askari waliokuwa na sifa ya kuendelea kubaki jeshini waliajiriwa na wale ambao walikosa sifa walilipwa malipo yao ya mkupuo na kutakiwa kurudi nyumbanI, lakini tumebaini kwamba majemedari wetu hawa baadhi yao wameendelea kuwa na changamoto za kiafya na hivyo Serikali ikakubali kuanza kuwahudumia kwenye Hospitali za Jeshi zilizo karibu na wao.

Mheshimiwa Spika, suala la pensheni lilishindikana kwa sababu kwa vigezo vya ajira hawakukidhi na hivyo ilikuwa ni vigumu kuwaingiza kwenye utaratibu wa pensheni, nashukuru (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri kwamba barabara ya Nachingwea – Masasi - Liwale alisema ujenzi wake utaanza kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha. Wakati wa ziara ya Mheshimiwa Waziri alisema wanatafuta mkandarasi wakati tayari mwaka jana mwezi Juni tulisaini mkataba kwa ajili ya mkandarasi. Nataka kusikia kauli ya Serikali, mkandarasi amepatikana au bado hajapatikana? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, Barabara ya Masasi – Nachingwea – Liwale, kilometa 175 mkandarasi amepatikana, ahsante. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mhesimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Ni kweli mkandarasi yuko site anaendelea na ujenzi Chikundi na kazi hiyo inaenda kwa kasi sana, naamini ndani ya muda mfupi itakamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo ni kwamba mahitaji ya majengo ya Mahakama ni makubwa. Tunatambua ni maeneo mengi. Hivi sasa Kata ya Lukuledi ambayo inasimamia kwenye Tarafa ya Lisekese wanatoa huduma za Mahakama kupitia Ofisi ya Kata ambayo inamlazimu Hakimu baada ya kutoa hukumu abebe ma-file yake pamoja na documents nyingine na kusafiri nazo zaidi ya kilometa 40 kwenda kuzihifadhi Masasi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naiomba Serikali ione uwezekano wa kujenga jengo la Mahakama kwenye Kata ya Lukuledi ambako tayari eneo lilishatengwa kwa ajili ya Tarafa ya Lisekese. Naipongeza sana Serikali kwa kutekeleza hayo.
NAIBU WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mhehimiwa Naibu Spika, kwanza nashukuru kwa shukrani hizi anazozitoa Mheshimiwa Mbunge na kwa kweli shukrani zimwendee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye kwa dhamira safi ameamua kuimarisha sekta ya utoaji haki na haki jinai katika nchi yetu, ikiwa ni pamoja na kuimarisha hii sekta ya Mahakama.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ombi lake juu ya Kata yake ya Lukuledi kule Masasi tutaona uwezekano wakati tunahuisha mpango wa awamu ya pili ya ujenzi na uimarishaji wa sekta ya Mahakama uwezekano wa kuiingiza Mahakama aliyoitaja katika mpango wa ujenzi, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka jana mwezi Juni tulisaini miktaba kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Nachingwea – Masasi mpaka Liwale na sasa hivi ni mwaka mzima, kazi hiyo haijafanyika. Nataka kufahamu, ni lini hasa ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, alichosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, lakini swali hili jana tulilijibu lilikuwa kama swali la msingi. Tulieleza kwamba barabara hii ilikuwa imesainiwa kwa kutumia utaratibu wa EPC+ F na tukasema Serikali inapitia upya utaratibu huo wa ujenzi kulingana na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa utaratibu huo. Tayari tunafanya mapitio na tutakuja kutoa taarifa kamili kuhusu utaratibu ambao tunaona utakuwa ni bora ili tuendane na kasi ya kuanza kujenga barabara hizo, ikiwezekana kwa utaratibu mpya. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, ni kweli kwamba vijiji vyote 785 vya Mkoa wa Mtwara tulipokea taarifa ya kutoka kwa Mkuu wa Mkoa kwamba vimeshapatiwa umeme. Isipokuwa, kazi hii sasa inaendelea kwenye vitongoji. Kijiji cha Mnyambe, Mitema pamoja na Kijiji cha Mapinduzi tayari wakandarasi wako huko. Tunaiomba Serikali itoe maelekezo ya kuhakikisha kazi hii inafanywa kwa spidi ili iweze kukamilika mapema.

Mheshimiwa Spika, kumekuwa na mwingiliano wa kazi, kama utakumbuka, kulikuwa na vitongoji 15 ambavyo sisi Waheshimiwa Wabunge tulipendekeza, lakini kuna kazi ya ujazilizi katika maeneo mbalimbali ikiwemo Chiwata, Mkalinga, Ngalole, Chikoweti, Maswela pamoja na Kitongoji cha Magomeni na Mjimwema…

SPIKA: Mheshimiwa Cecil Mwambe, swali la nyongeza.

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, tunaomba sasa Serikali iweze kufanya review ya ramani kwenye maeneo hayo, ahsante.
NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu maswali mawili ya Mheshimiwa Cecil, kama ifuatavyo: -
Mheshimiwa Spika, kwa yale maeneo ambayo miradi inaingiliana, huu wa vitongoji 15 na miradi ya ujazilizi ambayo pia imeanza, kwa niaba ya Mheshimiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, naomba nimwelekeze Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Nishati Vijijini, waweze kufanya mapitio pamoja na wakandarasi ili kuhakikisha miradi hii haiingiliani, ila yote inatekelezwe kwa kasi ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya umeme kwa haraka, ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Mwaka jana mwezi Juni tulisaini miktaba kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Nachingwea – Masasi mpaka Liwale na sasa hivi ni mwaka mzima, kazi hiyo haijafanyika. Nataka kufahamu, ni lini hasa ujenzi wa barabara hii utaanza?
NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Spika, alichosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli, lakini swali hili jana tulilijibu lilikuwa kama swali la msingi. Tulieleza kwamba barabara hii ilikuwa imesainiwa kwa kutumia utaratibu wa EPC+ F na tukasema Serikali inapitia upya utaratibu huo wa ujenzi kulingana na changamoto ya upatikanaji wa fedha kwa utaratibu huo. Tayari tunafanya mapitio na tutakuja kutoa taarifa kamili kuhusu utaratibu ambao tunaona utakuwa ni bora ili tuendane na kasi ya kuanza kujenga barabara hizo, ikiwezekana kwa utaratibu mpya. Ahsante.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi karibuni ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kwenye Kata ya Chiwale ulianza kwa kutumia fedha za Jimbo pamoja na fedha za tozo ambazo ziko ring-fenced. Hata hivyo, wakandarasi wengi wameji-mobilize wameondoka maeneo yao ya kazi kwa sababu hawajapewa fedha zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninataka kufahamu, ni kwa nini fedha hizi haziwafikii wakandarasi, nani anazishikilia?
NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ZAINAB A. KATIMBA): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza nianze kumpongeza Mheshimiwa Mbunge kwa kazi yake nzuri anayoifanya ya uwakilishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali hili mahsusi kabisa naomba baada ya kipindi hiki cha maswali na majibu mimi na yeye tuweze kukaa ili tuweze kufanya ufuatiliaji wa wakandarasi hawa ambao wame-raise certificate na bado hawajapata malipo yao, kwa sababu malengo ya kutaka wazawa waweze kushiriki katika zabuni kama hizi hasa za ujenzi wa miundombinu muhimu kama ya barabara, dhamira ni kuwawezesha wazawa. Kwa hiyo, hatuko tayari kuona kwamba wanaangamia. Nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, mimi na yeye tutafanya ufuatiliaji ili tuweze kupata muafaka wa wakandarasi hao.
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu mazuri sana ya Mheshimiwa Waziri, lakini atakumbuka barabara ya Kibiti – Lindi – Mtwara – Masasi ilifungwa mwaka 2023, wakati wa mvua za El-Nino. Ni kweli Serikali imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hizo, lakini sasa hivi mvua zinakaribia na hakuna mkandarasi yeyote aliyeko site pamoja na Serikali kusaini mkataba na wakandarasi hawa. Tunataka kufahamu, kabla ya mvua hizi za El-Nino, lakini pia atuhakikishie wananchi wa Mtwara kwamba barabara hiyo haitafungwa mwaka huu. Ni lini, mkandarasi anayetakiwa kujenga barabara ya Kibiti – Lindi – Mtwara – Masasi atakuwepo site? (Makofi)
WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Cecil Mwambe amekuwa akifuatilia barabara hii na ningependa kujibu swali lake kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tuko hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kujenga barabara ya Mtwara – Masasi – Mingoyo, na ni mkakati wa Serikali kujenga upya barabara hii kwa sababu imeharibiwa sana na mvua. Kwa hiyo, namhakikishia Mheshimiwa Mbunge, tumejipanga na ninawatoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania, kama ambavyo tulifanya mwaka 2023, tulipata mvua kubwa za El-Nino na Kimbunga Hidaya lakini Serikali inayoongozwa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mvua kubwa ambazo tulizipata tulihakikisha mawasiliano yanakuwepo. Hata msimu huu wa mvua ambao unakaribia kuanza tumejipanga. Kwa hiyo, nawaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na Watanzania. Kupitia TANROADS ikishirikiana na TARURA tumejipanga ipasavyo kuhakikisha mawasiliano yanakuwepo muda wote, ahsante sana. (Makofi)
MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya ya Masasi imeendelea kukua, lakini nyumba za polisi zilizopo zimechakaa na ni za muda mrefu. Je, Serikali haioni haja ya kujenga nyumba mpya kwa ajili ya askari polisi wa Wilaya ya Masasi? (Makofi)
NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante, ninajibu swali la Mheshimiwa Cecil Mwambe, kama ifuatavyo: -

Mheshimiwa Naibu Spika, timu yetu ya wataalamu inapita nchi nzima kupitia nyumba zetu za askari polisi na kuona jinsi ambavyo zimechakaa ili sasa tupange, tujenge awamu kwa awamu kwa sababu hatuwezi kujenga zote kwa mara moja. (Makofi)