Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Contributions by Hon. Kiswaga Boniventura Destery (32 total)

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema zake kwa kuniwezesha kufika ndani ya ukumbi huu na nawashukuru wananchi wa Jimbo langu la Magu kunipa Ubunge ili niweze kuwatumikia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naipongeza hotuba ya Mheshimiwa Rais, kwa kadri ambavyo imejikita kuonesha kwamba Watanzania wana mahitaji. Imegusa mahitaji ya kila Mtanzania lakini pia imeonesha huruma kwa Watanzania, naipongeza sana. (Makofi)
Sisi Watanzania tumepata kiongozi. Vitabu Vitakatifu vimeandika, ukisoma 2 Timotheo 2:20, unasema; “Nyumbani mwa Bwana kuna vyombo vingi, viko vyombo vya dhababu, vipo vyombo vya miti.” Mheshimiwa John Pombe Magufuli ndicho chombo cha dhahabu ambacho Mwenyezi Mungu Watanzania ametuandalia. Naomba tumuunge mkono wakati wote. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na maji. Jimbo langu la Magu lina matatizo makubwa sana ya maji kama zilivyo wilaya zingine. Sisi wenye nguvu ukirusha jiwe linakwenda moja kwa moja ndani ya maji lakini Wilaya ya Magu haina maji. Tumeahidiwa na viongozi waliopita, Rais wa Awamu ya Tatu, Rais wa Awamu ya Nne mpaka leo Magu haina maji. Bahati nzuri Mheshimiwa John Pombe Magufuli wakati wa kampeni naye ameahidi.
Mimi sina shaka kwa sababu hotuba hii amezungumzia sana suala la maji na sina shaka kwa sababu Waziri wa Fedha ni type ileile ya Mheshimiwa Profesa Muhongo kwamba hataki ubabaishaji kwenye makusanyo ya fedha, nampongeza sana. Ili miradi hii itekelezeke lazima fedha zikusanywe na nawaomba wakaze kamba wasilegeze hata siku moja kwa sababu nchi hii ilikuwa imefikia pabaya sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, unajua asali ni tamu sana lakini wako watu ambao hawanywi asali lakini kila mmoja anakunywa maji. Hebu tuangalie sasa suala hili, Serikali ifanye kila linalowezekana hata kukopa Benki ya Dunia ili kuweza kutekeleza miradi ya maji iliyoko kwenye nchi hii hasa Wilaya ya Magu. Wilaya yangu vijiji vingi havina maji na Wanamagu wana uvumilivu ukubwa sana na hili ndilo lililonileta Bungeni kwamba maji ndilo hitaji la wananchi wa Magu. Ili nirudi tena hapa Bungeni 2020 lazima maji yapatikane. Waziri wa Maji, Waziri wa Fedha, nisaidie hili ili Mheshimiwa Rais aliposema kwamba tumwachie jambo hili la maji Magu litekelezeke kweli kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, upo mradi ambao umeanza upembuzi yakinifu leo ni miaka miwili watu wanachakata, wanachakatia wapi? Mheshimiwa Rais alisema hawa watu wanaochakata watachakatia nje, Mtaalamu Mshauri anachukua miaka miwili anafanya upembuzi yanikinifu bila kukamilisha, hii ni kweli? Hii Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Pombe Magufuli ya „Hapa Kazi Tu‟ imwangalie huyu Mtaalamu Mshauri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la elimu bure Serikali imeanza vizuri. Mpango wa capitation ulikuwepo tangu mwaka 2002 lakini naomba niishauri Serikali kwamba wakati inatoa dola 10 kwa kila mtoto…
NAIBU SPIKA: Naomba umalizie Mheshimiwa.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Exchange rate ilikuwa ni Sh1,000 leo ni Sh.2,200. Kwa hiyo, waangalie hali ilivyo sasa ili kumudu uendeshaji wa shule hizi ili ziweze kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga hoja lakini nina mambo mengi ya kuzungumza, kumbe ningeanzia mchana, basi niishie hapo.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi. Dakika tano ni chache, nianze tu kwa kusema kwamba Wilaya za Magu pamoja na Wilaya ya Ilemela inavyo visiwa, vinahitaji vipate vivuko kwa sababu visiwa hivyo ni vijiji. Katika Kisiwa cha Besi, Wilaya ya Ilemela, pamoja na Kisiwa cha Ijinga, Wilaya ya Magu, tumeomba kwenye RCC lakini mpaka leo na ninaangalia kwenye bajeti sioni, naomba Mheshimiwa Waziri aliweke hili ili tuweze kusaidiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ambayo imeahidiwa na Rais wa Awamu ya Nne na Rais wa Awamu ya Tano, barabara ya Ngudu - Magu pamoja Nhungumalwa kwa kiwango cha lami. Upembuzi yakinifu umeshakamilika, lakini nimepitia hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijawahi kuona fedha za kutosheleza ujenzi huu wa mradi wa barabara ya lami. Naomba sasa aliweke ili ahadi ya Mheshimiwa Rais ikamilike. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Magu - Kabila - Mahaha; barabara hii ni muhimu sana kwa uchumi wa Wilaya ya Magu pamoja na Bariadi. Mheshimiwa Rais ameahidi lami, lakini sijaona hata kwenye utaratibu wa upembuzi yakinifu, bali kuna hela kidogo tu ambazo zimetengwa kwa ajili ya kuendeleza barabara hii. Naomba barabara hii nayo ya Magu - Kabila - Mahaha, iwekwe kwenye mpango mzima wa lami. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara inayofungua Mkoa wa Simiyu, kwa maana ya Bariadi - Salama - Sayaka - Bubinza na Kisamba. Barabara hii ni barabara ya karibu sana ikitengenezwa kwa kiwango cha lami ili kuepusha watu wa Bariadi kwenda mpaka Lamadi; ni barabara muhimu kiuchumi kama tunataka kujenga uchumi kwenye kanda hiyo. Tunaomba sana barabara hii iwekwe, lakini kipande hiki cha Sayaka - Bubinza - Kisamba, huwa tunaomba kwenye Road Board, kwa sababu ni kipande kidogo, kipande daraja kihudumiwe na TANROADS, lakini mpaka leo hakijaweza kuwekwa. Niombe Mheshimiwa Waziri akiweke kipande hiki, ili kiungane na wenzetu wa Simiyu na kiwekwe lami kipande hiki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, iko barabara ikijengwa tunaweza kuondoa msongamano wa Mwanza. Watu wa kutokea Mara wanapokwenda airport hawana sababu ya kuingia mjini…
MWENYEKITI: Ahsante! Ahsante,
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia nami hotuba ya Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wanatheolojia wanatufundisha kwamba ili Mungu akusikilize lazima uanze kumsifu kwanza. Kwa hiyo, ili Serikali iweze kunisikiliza ni vizuri nikasema mazuri ambayo inayafanya.

Kwanza napenda kumshukuru na kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anazozifanya likiwemo hili la ununuzi wa ndege. Unajua historia wanaweza watu wasiifahamu sana. Nchi yetu ilikuwa na ndege ambazo tuligawana kutoka East Africa na ndege mpya ikanunuliwa sasa ya Rais na Benjamin William Mkapa. Kwa hiyo, tangu hapo huyu ni Rais wa kwanza kununua ndege mpya za nchi ya Tanzania. Kwa hiyo ni jambo ambalo limeingia katika historia na atakumbukwa milele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukafahamu hilo, lakini tujue pia kwamba yale mambo yote yanayofanyika ya kitaifa ni kwa ajili ya kuhakikisha kwamba Watanzania wanafikishwa mahali ambapo wanahitaji, tunampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa uhamasishaji wake wa mazao matano ya kibiashara ikiwemo pamba. Ili uchumi ukue ni vizuri mazao ambayo yanaleta uchumi yahamasishwe na kusimamiwa na Serikali. Serikali ya Awamu ya Tano imefanya hivyo chini ya Waziri wa Kilimo pamoja na Waziri Mkuu. Tumepata madawa ya kutosha ya pamba na pamba tunaamini kwamba inaweza kuwa nyingi. Kinachotakiwa sasa ni kuhakikisha kwamba wanunuzi wanapata fedha za kutosha ili mkulima asiweze kukopwa, ni kazi kubwa sana ambayo Waziri Mkuu ameifanya ya kuhamasisha pamoja na kufanya mambo mengine ambayo anayasimamia katika Serikali yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya yote yanaweza kuwepo maneno, lakini nataka nikwambie kwamba katika zawadi ambazo Mwenyezi Mungu ametujalia Tanzania ni pamoja na kuwa na Kiongozi, Rais wa Jamhuri ya Muungano Ndugu John Pombe Magufuli, Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na Makamu wa Rais hizi ni zawadi ambazo Mwenyezi Mungu ametupa Watanzania, ni vizuri tukawaombea kwa sababu wanafanya kazi ile ambayo wananchi wanaihitaji, ile ambayo hata Mwenyezi Mungu anaihitaji, kwa hiyo lazima tuwapongeze.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu mwanzo Wafalme wakiendelea walikuwa wanalalamikiwa hivi hivi, Mfalme Daudi alilalamikiwa sana, lakini katika utenzi wake wa nyimbo zake Zaburi ya 34:19 alisema maneno mafupi tu kwamba; “Mateso ya mwenye haki ni mengi lakini Bwana humponya nayo.”

Kwa hiyo, tunaamini mateso, mahangaiko ambayo viongozi wetu mnahangaika nayo mnateseka nayo, Bwana Mungu atawaponya nayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nianze kuchangia yale ambayo wananchi wanayahitaji. Ofisi ya Waziri Mkuu ina mradi wa MIVARP ambao unaongeza thamani kwa mazao ya wakulima kwa kujenga barabara pamoja na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu ni muhimu sana umefanya mambo makubwa sana, yako maeneo ambayo wananchi walikuwa hawawezi kusafirisha mazao yao sasa wanasafirisha. Lakini mradi huu sasa ni vizuri ukaendelea. Kwa mfano, kule Magu tunalo eneo bovu sana sasa ambalo tunategemea wakulima wabebe pamba yao kwa tela za ng’ombe kutoka kilometa tano mpaka kilometa kumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri MIVARP kwa wakati huu sasa maeneo yale ambayo tunataka kusafirisha mazao ikapeleka nguvu za ziada ili ziweze kutengeneza barabara hizo na kuongeza thamani ya zao la mkulima, kwa sababu bila barabara hizo hatutasafirisha pamba yetu kuleta kwenye soko na barabara hiyo ni Ng’haya - Mwabulenga ni barabara muhimu sana kiuchumi na ndiko wananchi pia wanalima mpunga wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiziachia TARURA hizi barabara nina imani kulingana na uwezo mdogo wa kibajeti havitatosha. Pia niombe kwenye TARURA hapa; mfumo ambao tumeuweka kwenye TARURA nadhani si rafiki sana kwa sababu TARURA haina bodi sasa, haingii hata kwenye Baraza la Madiwani, kwenye Kamati ya Fedha, je, barabara hizo zinahojiwa na nani? Mpaka twende Road Board ndipo tukakutane na matatizo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri ukatengenezwa mfumo wa kiwilaya, ikawepo Bodi ya TARURA ya Wilaya ili Waheshimiwa Wabunge na Waheshimiwa Madiwani na viongozi wote wa Serikali waweze kwanza kudhibiti upungufu wa barabara zilizopo kwenye Halmashauri ndipo sasa twende kwenye Road Board. Kwa hiyo, naomba sana hilo liweze kuangaliwa kwa makini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kila Mheshimiwa Mbunge anahitaji maji hapa, kila tunaposimama tunahitaji maji; mimi nadhani ni wakati muafaka sasa wa kuangalia kama Taifa. Kama ambavyo hotuba ya Waziri Mkuu imesema kwamba tunao uwezo wa kukopesheka, hivi hatuwezi kukopa tukaweka miundombinu ya maji ili wananchi waweze kupata maji salama kwa ukaribu? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuishauri Serikali hii ambayo ipo tayari kuwatumikia Watanzania, tukope, tuweke miundombinu ya maji ili wananchi akina mama ambao wanateseka kwa muda mrefu kuchota maji, wanachelewa kwenda kuzalisha shughuli za kiuchumi tuweze kuwawekea mtandao wa maji unaostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nalalamika kila Bunge ninaposimama hapa, kila ninapochangia hotuba hizi za Waziri Mkuu, TAMISEMI na Maji yenyewe, Waziri wa Maji, Tarafa ya Ndagalu ni kilometa 58 kutoka Magu Mjini, ni kilometa 65 kutoka Ziwa Victoria lakini haina hata mto. Ni Tarafa kame inapakana na kwa Mheshimiwa Chenge kule naye ana shida ya maji, imepakana na Itilima na Maswa kule nako kuna shida ya maji. Ni vizuri tukaangalia namna ambavyo tunaweza kuisaidia Tarafa hii, ni Tarafa kubwa lakini wananchi wake wanateseka, haina mto wala mabwawa. Mheshimiwa Waziri nikuombe sana uangalie utakapokuja kwenye bajeti yako uweze kuona utaisaidiaje Tarafa hii ya Ndagalu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo suala la walemavu, bahati nzuri Serikali ya Awamu ya Tano inawajali kikamilifu walemavu na ndiyo maana hata Naibu Waziri ikamteua yule anayelingana na mazingira ya hawa ambao nataka kuwasemea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walemavu bado hatujawaangalia sawasawa hasa kwenye mikopo ya uzalishaji mali, tunawaunganisha tu kwenye mifuko ya vijana na wanawake, lakini hii mifuko tungeweka mfuko kwa sababu ya kuwawezesha walemavu ili waweze kujikomboa kwenye biashara ndogo ndogo, wawe na uchumi ambao unaweza kuwasaidia katika maisha yao na familia zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo malalamiko ya watumishi ambao wakati huo walikuwa wanachangia NPF na baadae wakahamishiwa NSSF kwamba zile fedha zao walizokuwa wamechangia NPF wanapokwenda kustaafu wanategemea NSSF itakuwa imeziingiza na zile, wanajikuta hizo fedha hazipo, wanahangaika kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Waziri wa Fedha kwenye jambo hili litazame kwa moyo wako wa huruma maana hawa watumishi wametumika kwa muda mrefu sana, wanapokosa mafao haya wanapata taabu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini Mfuko huu wa NSSF inaonekana mteja anapochangia kwa maana ya mtumishi, hakuna ongezeko lolote ambalo linaongezeka kwenye mchango wake. Anapokwenda kulipwa mafao yake analipa mafao yale yale, hilo ndilo lalamiko la watumishi wengi hasa waliopo kwenye Idara ya Afya. Niombe sana hili jambo Serikali iweze kuliangalia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niungane na wenzangu kuzungumzia suala la Watendaji wa Vijiji ambao waliajiriwa kwa darasa la saba, hawakuwa na kiwango cha elimu ya sekondari. Hawa wametumika kwa nchi hii na hawa si wengi sana waliobaki, ni vizuri tukawaangalia namna pekee ya kuwasaidia ni kuwarudisha kazini kwa sababu wamebakiza muda mchache. Mambo ambayo wanayafanya yanalingana kabisa na elimu yao, hawa ndio waliojenga shule za msingi, zahanati, sekondari na ndio walinzi wa amani kwenye vijiji hivyo, leo tukiwaacha hawa hiyo ndiyo adhabu yao? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana, Mheshimiwa Waziri wa Utumishi yupo hapa, Makatibu Wakuu wapo na Waziri Mkuu yupo, muone namna, hatuna sababu ya kuendelea kujadili Bungeni hapa, ni kutoa waraka tu hata kama ni kesho ili warudishwe kazini wale ili baadaye sasa tuangalie utaratibu wa wale wanaoendelea kuajiriwa wenye sifa zinazostahili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na mimi nataka niwaambie hawa wanafanya kazi…

(Hala kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Bajeti ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mabula amenipa hapa Biblia zote mbili ya Agano la Kale na Agano Jipya; yote nitayatumia kwa nafasi yake. Agano la Kale Wizara ya Kilimo ndio wazalishaji wa mazao yote. Nimetoka Iringa nimeona alizeti nyingi, nimekuwa hapa Dodoma nimeona alizeti nyingi, nimekuwa Singida nimeona alizeti nyingi, Kigoma alizeti nyingi; inaonekana mikoa zaidi ya 20 sasa inalima alizeti. Kwa hiyo kwa sababu uzalishaji upo upande wa Wizara ya Kilimo ambalo ni Agano la Kale, jipya ni Wizara ya Viwanda na Biashara. Hapa ndipo tunataka tuzungumze vizuri. Unapotaka kulinda viwanda lazima udhibiti mianya yote ya magendo na u-fix kodi ambayo itasababisha bidhaa yote ya nje isinunuliwe ili kulinda viwanda vyako.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa nataka kuzungumza nini. Mikoa ambayo inalima alizeti, wakulima wamekopa benki, TADB imewapa fedha. Wasipouza mbegu yao kwa bei nzuri, TADB inafilisika, NMB inafilisika, CRDB inafilisika na mwananchi anafilisika. Viwanda wamekopa kwenye mabenki, wasipozalisha; kwa sababu taarifa wa Mheshimiwa Waziri imesema asilimia 25 ndivyo viwanda hivi vinazalisha maana yake miezi minne kwa mwaka, viwanda hivi vinakwenda tena kufilisika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tukiwa kama nchi tunafilisi viwanda kwa sababu ya kuachia room ya watu kuingiza bidhaa zao kutoka nje, hatuwasaidii Watanzania. Kwa hiyo Agano Jipya linapaswa litimilize Agano la Kale, kwamba wanazalisha lakini Agano Jipya linahakikisha kwamba watu wanauza. Kwa hiyo mwaka jana tuliweka kodi equity duty kwa sababu ya kuogopa mfumuko wa bei; sasa tumekwenda kuwauwa wakulima wetu. Bahati nzuri Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara huko kwako ndiko wanakolima alizeti, kwa hiyo tunakwenda kuwafilisi wapigakura wako, lakini tunakwenda kuwafilisi wapigakura wa Mwigulu, hapo Singida.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeona Mkalama wanalima alizeti nyingi. Kwa hiyo niombe hivi, mwaka huu tusiruhusu tukaondoa kodi ya mafuta ya nje, tukiruhusu tunakwenda kufilisi viwanda vyetu na wakulima wetu. Leo mkulima wa alizeti anauza shilingi 600 kwa kilo ambayo alikuwa anauza shilingi 900 mpaka 1000, hiyo huwezi kumlinda mkulima. Lakini mwenye mafuta anakwenda kuuza dumu 60,000 badala ya 70,000, maana yake huwezi kulinda viwanda. Kwa hiyo hatuwezi kulinda viwanda kama tunaruhusu magendo, tunaruhusu kuondoa kodi kwenye kwenye mafuta ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana na huu ndio ugonjwa ambao umeua viwanda vingi duniani. Hatuwezi kuendelea kukubaliana na jambo hili, lazima sasa Serikali ione namna ya kuweka kodi kwenye mafuta yanayotoka nje, kwa sababu mikoa yote 20 hii inalima alizeti. Na kwa hali hiyo ukiangalia Iramba na Singida yote, ukiangalia Dodoma hii wananchi maisha yao wamebadilisha kulingana na alizeti ambayo wanakamua ndani wanauza barabarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo niombe sana, ili nchi iendelee lazima tuwe na wivu wa kuwaonea wivu wakulima wetu waendelee kuzalisha kuliko kuruhusu mataifa nje kuingiza mafuta. Niombe sana hili kwa mwaka huu Wabunge tusikubali kuondoa kodi kwenye mafuta ya nje, tutakuwa tunaua viwanda vyetu. Hili ni simu, ni kama vile Biblia inavyosema, kwamba asiyempenda wa nyumbani kwake ni mbaya kuliko asiyeamini. Kwa sababu sisi tunawapenda wa nje tunashindwa kuwapenda wa kwetu, tunaruhusu kuondoa kodi ili watu waingize mafuta wa kwetu wanabaki maskini, hapana. hii ni Hapana, lazima tukubaliane Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimemsikiliza vizuri Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, lakini nimemsikiliza vizuri mchangiaji King, na mimi nilikuwa najiuliza, mikoa 17 inayolima pamba leo pamba yote tunaiuza nje; ni umaskini mtupu. Haiwezekani tukazalisha, tukaendelea kuuza raw material badala ya kuuza production iliyokamilika. Na hili nakwenda kuandika historia kwamba Rais mwananke ameamua kuhakikisha kwamba maghala yanatengenezwa hapa; na hii ni lazima Serikali i-set fedha kama ambavyo imependekeza. Hatuwezi kukubali kila mwaka kurudi pale pale. Nchi hii tuna miaka 60 ya uhuru hatuwezi kuwa tunauza raw material tunashindwa ku-produce material yetu hapa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili linakwenda kuweka rekodi, Waziri wa Viwanda na Biashara mwanamke wewe, na hili linakwenda kuweka rekodi, Spika wa Bunge mwanamke, Tulia huyu hapa. Kwa hiyo haya mambo hayatokei hivi hivi. Kwa hiyo niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa uamuzi mzuri ambao sasa anakwenda kuuchukua kwa ajili ya pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, unajua tukizalisha majora hapa, kwanza tukijenga tu kiwanda hiki ni zaidi ya bilioni 500, mfanyabiashara wa kawaida hawezi kupata fedha hizi. Hata ukienda kwenye benki wanakuona kama umechanganyikiwa hivi kwa sababu mitaji ile ni midogo na wanaogopa risk kuwekeza kwa mtu mmoja. Kwa hiyo Serikali lazima i-set fedha kwa sababu kama tunajenga madaraja, tunashindwaje kujenga kiwanda? Kwa hiyo hili ni jambo zuri. Na tukiweza hiki kiwanda, kwamba bidhaa ya pamba ina vitu vingi ambavyo Mheshimiwa Lucy alikuwa anazungumza hapa; kama vile vifaa vya hospitali na vifaa tiba, vinatokana na mabaki ya pamba inayotoka kwenye majora. Kwa hiyo tunakwenda ku-save hela nyingi ya kuagiza pamba nje; dola ya kigeni itakuja badala ya kuipeleka nje (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini, kama watu watakuja hapa Afrika kununua, Afrika tukawa tunauza majora, hapa Tanzania, akija hapa Mkongo analala hoteli, anapanda taxi, anakunywa soda, anakunywa bia anapata na kamchepuko kidogo mambo yanaendelea. Kwa hiyo kuna vitu vingi ambavyo tutavifikia kuliko sasa. kwa hiyo mimi niombe Serikali iangalie wigo mpana, isiangalie tu kwamba tunakwenda kuzuia fedha za nje, tunazuia fedha kwenda nje, tunataka fedha za kigeni ziingie ndani ili zisaidie ukuaji wa kiuchumi hapa Tanzania. Na ndipo tutawafanya wakulima walime wakiwa na uhakika bei wa soko zuri la pamba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo soko la dunia hatuna uwezo nalo. Mwaka jana tumeuza pamba 1,560 mpaka 2,000 mwaka huu uki-google wewe unapata senti 0.71. Ukiondoa gharama zingine unapata senti 75. Kwa hiyo maana yake pamba inakwenda kununua kwa 1,060. Kwa hiyo tukiwekeza hiki kiwanda ndio mwarobaini na ndipo kukuza uchumi wa nchi hii. Halafu nikuombe; kwa sababu pamba inalimwa sana, mikoa 17, na tayari pale katikati Simiyu na Magu kuna eneo lipo basi muangalie namna ya kuleta maeneo hayo ili kuongeza uzalishaji wa zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kufanya research viwanda, vyetu hivi; kwa mfano viwanda vya miwa ambavyo vinatoa sukari, ni viwanda ambavyo wawekezaji wake wamejitahidi sana, na kwa kweli hata uzalishaji unaendelea. Nilipata kutembelea kiwanda cha Kagera sugar nikakuta wana mitambo matata ya kimarekani ambayo sijawahi kuona. Wanafyeka mapori kuongeza uzalishaji na bado wanahitaji. Sasa, yaandaliwe maeneo ambayo hayalimwi, yamebaki waongezewe kule Kagera Sugar ili waweze kulima na kuzalisha vizuri zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuendelee kuwashauri pia wafanye research nzuri. unajua kwenye miwa si tu unaweza kutoa sukari na molasses pekee, Hapana; kwenye miwa unaweza uka-produce mpaka diesel, ipo kwenye miwa, kama tuta-set vizuri viwanda. Kwa hiyo lazima Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ifanye research ya kwamba zao hili linaweza ku-produce vitu gani ndani; huko ndiko kukuza mnyororo wa thamani. Hata ukienda kwenye mkonge, mkonge sio umera pekee, lile zao la katikati ninyi watu wa Tanga lile likisindikwa linapandwa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tunataka mfanye research kwa sababu tatizo tuna akili nyingi lakini maarifa hatuna, sasa hilo ndilo tatizo. Sasa tutumie maarifa kufanya research ili kuhakikisha kwamba tunakwenda kwenye viwanda ambavyo ni vya kisasa zaidi na ambavyo vinaweza kutoa vitu vingi kwenye mmea mmoja. Hili ndilo itakuwa ni suluhisho, kwa sababu hata ukienda Brazil kiwanda cha sukari kikikamua sukari kinatoa bidhaa nyingi mpaka kwenye mafuta lakini sisi bado tunabaki kwenye sukari, molasses na makapi mengine, tuondoke huko. Serikali iwasaidie wawekezaji wa sukari kufikia hatua hiyo ya uwekezaji wa kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Kilimo
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kukupongeza kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia. Kwanza, nianze kumpongeza Waziri, Naibu wake, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu pamoja na Wakurugenzi wa Wizara. Hapa ndipo ninapoendelea kumpongeza Mheshimiwa Rais, kwamba ametuteulia watu wazuri, watu wenye mtizamo, siyo msimamo. Kwa kweli, niliposoma hotuba ya bajeti, mimi binafsi nataka nikueleze kwamba, naunga mkono hoja ili huko mwisho kama dakika zinapungua niwe nimemaliza kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilio chetu kikubwa ilikuwa ni kutatua tatizo la msingi. Tatizo la msingi ni ukame. Wakati wote wananchi wanalima, lakini hawana uhakika wa kuivisha. Kwa bajeti hii ambayo imelenga umwagiliaji kwa kiasi kikubwa, pamoja na kuchimba visima virefu kila Wilaya kwa ajili ya kumwagilia mashamba, huu ni mwarobaini kabisa. Kwa kweli unaweza ukaandaa mbegu, lakini mvua ya kuivisha isiwepo; unaweza ukaandaa mbolea, lakini mvua ya kuivisha isiwepo. Kwa hiyo, jambo hili la kwenda kuweka umwagiliaji mkubwa, tunakwenda kutatua tatizo la msingi. Hapa ndipo tunakwenda kukuza uchumi wa wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Kilimo inatenga fedha na iko vizuri sana, tatizo hapa ni kupewa fedha za utekelezaji wa miradi hii ambayo wameiweka. Ndipo tatizo kubwa lilipo. Naiomba sana Serikali, tufike mahali tuwe tunaamua mambo makubwa, haya mambo ya mapinduzi ya kilimo. Kwa sababu ukiangalia leo, mimi nataka nikwambie, kule Magu, Busega, Kwimba walilima vizuri sana, mvua ikaishia Christmas, kwa hiyo, mahindi yote yakakauka kwa jua lililopiga miezi mitatu. Hakuna mavuno ya mahindi kwenye maeneo hayo. Kwa maana hiyo, njaa ipo. Hapa namwomba Waziri sasa aandae mahindi ya bei nafuu yaje yauzwe kule Magu, Kwimba na Busega kwa sababu wana njaa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Fedha tunapotenga fedha, tunaomba zipelekwe kwa wakati. Leo ukisoma vizuri ripoti ya Waziri, kuna miradi ya umwagiliaji ndiyo inaanza sasa, wakati tuko mwezi wa tano. Kwa hiyo, hapa tunachelewa wapi? Tuangalie kipaumbele chetu kwa sababu bila kuwa na kilimo endelevu, uchumi wetu bado utakuwa chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napendekeza pia mfuko mwingine. Tuwe na mfuko wa umwagiliaji. Kama ambavyo tuna mfuko wa maji, kama ambavyo tuna mfuko wa barabara na hii tuweke tena Shilingi mia moja kwenye mafuta, tusiogope. Tatizo la Watanzania ni kuogopa. Tunaogopa wakati wananchi wetu wanakufa masikini! Hatuwasaidii. Naomba sana kwa sababu, kama tutaweka shilingi 100 tukapeleka kwenye mfuko wa umwagiliaji, maana yake ni kwamba tutatengeneza scheme za umwagiliaji za kutosha kila mahali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, inauma sana. Ukiwa kule Jimbo la Magu, bonde la Bugando Chabula, mkono mwingine ni maji ya Ziwa Victoria; ukiwa kwenye Bonde la Nkwiji Lugeye mkono mwingine ni maji ya Ziwa Victoria; ukiwa kwenye bonde la Ngashe Nkwizu Ngongwa, mkono mwingine kuna maji ya Ziwa Victoria; ukiwa kwenye bonde la Magu pale Kandawe, mkono mwingine kuna maji, mita 300 maji; ukiwa kwenye bonde la Mwambanga kuja Sawenge, mbele yake kuna maji ya Ziwa Victoria; ukiwa Mwabuyenga kuna mto Simiyu; ukiwa kule Chandulu, kuna bonde zuri sana linaloweza kutengenezewa bwawa la maji ya kukinga, Kabila, Igombe na Mahaha vile vile. Sasa inauma sana; na ili tutekeleze, lazima tuwe na mfuko. Tunaogopa nini? Kwa sababu Watanzania ni hawa hawa ambao wanahitaji wawe na uchumi endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ukienda kwenye maduka yoyote, biashara zozote, viwanda vyovyote, hawauzi, hawazalishi kama ilivyotarajiwa. Maana yake nini? Ni kwamba mkulima ndiye anayekwenda kununua kwenye bidhaa mbalimbali. Akinunua kwenye bidjhaa mbalimbali huko, mfano akinunua mabati, kuna kodi ya Serikali; akinunua godoro, kuna kodi ya Serikali; akininua cement, kuna kodi ya Serikali; akinunua nguo, kuna kodi ya Serikali, huko ndiko kujenga uchumi na kupanua wigo wa kodi kwa Serikali. Kwa hiyo, naomba sana, tuje na mpango wa kuongeza Shilingi 100/= kwenye mafuta, tupeleke kwenye umwagiliaji pekee, tutakuwa tumemeliza matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulinda wakulima. Katika Bajeti ya Wizara ya Viwanda nilichangia, nami nampongeza Mheshimwa Waziri. Nchi yoyote duniani lazima ilinde wakulima wake. Nawe kwa sababu ni Mwenyekiti wa Bajeti, angalia vizuri, import duty ambayo tuliiondoa mwaka 2022 kwenye mafuta ya nje, iwekwe mwaka huu 2023, ili kulinda wakulima wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili nakuomba sana kwa sababu wewe ndio unasimamia. Wakulima wote wa mazao yote hasa wanaochakata mafuta, wanapata bei ndogo kwa sababu sisi tulikubaliana hivyo. Tulikubaliana hivyo kwa sababu, hali ya mfumuko wa bei ilikuwa hivyo ili kuvusha kidogo mfumuko wa bei. Sasa hivi alizeti wamezalisha nyingi, pamba wamezalisha nyingi, yaani mbegu zote na mazao yote yanayotoa mafuta yamezalishwa kwa wingi sana. Ni lazima tuwe na wivu kuhakikisha kwamba tunalinda wakulima wetu ili kuhakikisha wanazalisha, na mabenki haya yanapata fedha nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikwambie tu kwamba, pamba haina ruzuku. Nimesema hapa, Waziri amesema atapeleka ruzuku kwenye mazao ya alizeti, (ngoja niangalie hapa) kwenye mazao ya alizeti, ngano na miche ya michikichi. Pamba haina ruzuku. Hatuna ruzuku ya mbegu, na hatuna ruzuku ya madawa. Pamba inajihudumia yenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atusaidie tu ruzuku ya madawa, kwa sababu ndiyo tatizo kubwa ili wakulima wetu waweze kuzalisha. Halafu kuna tatizo kubwa, inapofikia mahali ile pamba inataka kuzaa, majani yanabadilika, yanakuwa brown. Nadhani kuna wadudu ambao wananyonya. Naomba tufanye research ya kutosha kwa ajili ya dawa hiyo. Wakulima wanalalamika sana kwa sababu hawana namna ya kuweza ku-control ugonjwa huo. Mwaka huu tulitegemea zao liwe kubwa, lakini litashuka kwa sababu ya mnyauko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, nimesema sina shaka na Wizara yako, sina shaka na wewe Mheshimiwa Waziri, kwa hiyo, naomba…

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Cherehani.

TAARIFA

MHE. EMMANUEL P. CHEREHANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, wakulima wa pamba katika nchi yetu ni Mikoa 18, na mwaka huu malengo ni kuzalisha kilo milioni 350 na wametumia pembejeo bilioni 100. Kwa hiyo, hawana ruzuku wakulima wa pamba.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Boniventura, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa sababu kwa kweli anayesema kwanza ni mhanga, nami ni mhanga, na mikoa yote 18 ni wahanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hivi, Mheshimiwa Rais katika hotuba yake alisema tunazalisha tani milioni moja. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri, wewe ni m-NEC; Mheshimiwa Mwigulu, Waziri wa Fedha ni wa NEC, naomba tujibu Ilani ya Chama cha Mapinduzi kama ambavyo Mheshimiwa Rais wetu amekusudia kujibu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye ngano. Tunatumia fedha nyingi sana za kigeni kwenye ngano, lakini tuna maeneo potential ambayo yanaweza kulima ngano. Mkoa wa Njombe ni potential sana kwa kulima ngano, Katavi kuna eneo potential la kulima ngano, Arusha, na maeneo mengine. Lazima tuamue kama Taifa. Hivi tutagiza malighafi kutoka nje mpaka lini? Kwa nini tusiamue? Hivi tukisema, baada ya miaka mitatu, wale wanaoagiza sasa waanze kulima mashamba makubwa, wapewe mashamba, watapanua ajira, watafungua uchumi kwenye nchi hii ili baada ya hapo miaka mitatu au minne tusiagize ngano nje. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hili linauma sana. Kama hatutaweka mwisho, tukaruhusu tu kuagiza agiza, mfanyabiashara anapenda tu kununua na kuuza. Mfanyabiashara hapendi kuwekeza kwa muda mrefu, kwa sababu ni gharama kubwa. Anataka anunue leo, auze kesho. Naomba sana, kwa Waziri aliyepo, Katibu Mkuu Gerard aliyepo na Wakurugenzi wa Wizara waliopo, naomba sana kama nchi tuzuie ngano baada ya miaka kadhaa, tulime ya kwetu ili kuhakikisha kwamba tunapanua uchumi na kuwekeza sana kwenye viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naunga mkono hoja tena kwa mara ya pili. (Makofi)
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2022 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nishukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Spika, kwanza niweze kumpongeza Mheshimiwa Rais kwa kazi nzuri ambayo anaendela kuifanya kwa ajili ya Watanzania, lakini pia nimpongeze Waziri wa Fedha, Naibu wake, Katibu Mkuu na taasisi ya TRA ambayo inakusanya mapato kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bajeti hii kwa kweli imetoa mwelekeo kwa wananchi maskini, hasa kwenye vyuo ambavyo ni vyuo vya ufundi kuwa na ada bure. Hili tunakwenda kuongeza wataalam ambao walikuwa wanabaki, wanapochaguliwa na Serikali kwenda kwenye vyuo hivyo wanakosa ada. Kwa hiyo, hapo tumekwenda kumgausa mwananchi moja kwa moja.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kwenye vyuo vya kati vya sayansi afya na mambo mengine, kutoa mkopo ambao W abunge hawa mmeridhia miaka yote ili hawa wanafunzi waweze kupata mikopo na wao waweze kusoma kwa sababu wengi walikuwa wanabaki. Napongeza sana na ninakupongeza sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Rais kwa kukubaliana na jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, juzi nilimsikiliza vizuri Mheshimiwa Waziri wa Fedha, alisema tozo siyo za Rais, tozo siyo za Waziri Mwigulu na mimi nakubaliana na yeye, tozo ni za Watanzania kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Kama kuna tozo vikwazo ni nafasi yetu sisi Bunge kuziondoa tozo hizo vikwazo, kuliko kumuachia mzigo Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba kushauri hapa ili angalau tuone ni namna gani hawa wafanyabiashara wanaweza kukwepa kodi kwa sababu ya tozo vikwazo na naomba nianzie na service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, msingi wa service levy uliwekwa kwa ajili ya viwanda wanapozalisha wanatozwa service levy kwa ajili ya Halmashauri zetu. Lakini msingi wake ulitokana na kwamba ili hii service levy itozwe ni kwamba Halmashauri zetu baada ya kuangalia mauzo ambayo yanauzwa kwenye Wilaya zetu, yanapeleka moja kwa moja viwandani, viwanda vinalipa. Naomba nitoe mfano, pale Ilemela Kiwanda cha Bia service levy Halmashauri ya Ilemela inatoza moja kwa moja pale, lakini hata yule agent ambaye kiwanda kinamuuzia kwenda pale pale mita 100, na yeye akiuza Halmashauri inamtoza kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini bidhaa hizi zote ukiangalia kwa mfano tu nataka nitoe mfano, bundle moja ya bati mfanyabiashara ananunua shilingi 370,000 ukimtioza 0.3% sawa sawa na shilingi 1,100 lakini huyu anapata shilingi 1,400. Je, atakuwa tayari kutoa risiti? Ndio maana sasa unakuta wafanyabiashara hawatoi risiti kwa sababu wakitoa risiti, service levy inakwenda kuwa nyingi kuliko faida ambayo anapata mfanyabiashara. Kwa hiyo, hapa tunakwenda moja kwa moja kupunguza mapato ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, service levy mwanzo msingi wake ilikuwa ni income, lakini leo wanatoza kwa revenue. Income maana yake ni kwamba umeshatoa matumizi yote na gharama zote, kinachobaki ndicho kinachopaswa kutozwa, lakini wao sivyo, kwa hiyo, ndiyo maana sasa tunakwenda wafanyabiashara wanakwepa kutoa risiti kwa sababu ya vikwazo hivyo na hilo wanajifanya sasa wafanyabiashara kuandamana kwenye mambo haya. Sasa lawama zinamrudia Mheshimiwa Rais, zinamrudia Waziri wa Fedha lawama, kumbe vikwazo hivi inapaswa tukae chini tuangalie je, tutoze kwa revenue? Je, tutoze kwa income au tupunguze badala ya 0.3% tuwe na 0.03% hapo ndipo sasa risiti zote zitatolewa, nilitaka kushauri hili jambo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shilingi 100 ambayo imeongezwa kwenye mafuta kwanza niwatoe hofu Watanzania na niwatoe hofu Waheshimiwa Wabunge, nataka tu kutoa mfano, lori likipakia lita 1,000 kule Dar es Salaam kubeba mzigo kwenda Mwanza inayoongezeka ni shilingi 100,000 tu.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hiyo unaweza ukasema kwamba inaweza kupunguza gharama za uendeshaji au kuongeza gharama za uendeshaji. Kwa hiyo, mimi nataka kusema kwamba kwa sababu soko la dunia la mafuta hatuna uwezo nalo, kuna kushuka na kuna kupanda kodi hii inakwenda kutusaidia kwenye miradi ya kimkakati hasa kwenye kilimo ambapo kwa kweli Watanzania wengi wapo kwa sababu tunaweza kutengeneza hofu, lakini tukashindwa kutengeneza huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi naendelea kusema kule Magu mahindi yanakauka kwa sababu ya kukosa maji. Kwa hiyo, hii shilingi 100 pamoja na kwenda kwenye miradi ya kimkakati hasa reli ya Standard Gauge lakini pia lazima iende kwenye kilimo kwa ajili ya umwagiliaji ili wananchi wetu waweze kupata mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nasikitika kidogo na ninashangaa sana sijui wataalam hawa Waziri wa Fedha wanakushauri vizuri? Leo Serikali imetoa ruzuku ya mbolea, Serikali imetoa ruzuku ya mbegu, watu wamelima vya kutosha, alizeti Mwanza, Simiyu, Tabora, Singida, Mbeya na Iringa na maeneo mengine Babati imelimwa ya kutosha; pamba ipo ya kutosha, mikoa 17 inayolima pamba. Kwa hiyo, tuna uhakika wa kuwa na mafuta mengi ya kutosha kwenye nchi hii, kwa hiyo, unapokwenda kutoa kodi kwa mafuta yanayotoka nje unaweka 25% badala ya 35% unakwenda kuwafanya wakulima wa nchi hii kwa masikini, siyo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili siyo sawa, halafu unakwenda kuongeza 18% VAT kwenye mafuta yanayozalishwa nchini unatoa ya nje, kwa kweli hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha hawakukushauri vizuri. (Makofi)

Naomba nishauri Serikali, hatuwezi kuongeza ajira ya wakulima wetu, hatuwezi kuongeza ajira kujenga viwanda kama kodi za mafuta yanayotoka nje tunazipunguza. Napendekeza 35% ya mafuta yanayotoka nje iwekwe ili kuhakikisha kwamba wakulima wetu wa alizeti wanapata bei nzuri, wakulima wetu wa pamba wanapata bei nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, haiwezekani tukatajirisha nje, tukawaweka wananchi wetu kuwa maskini, hili haliwezekani. Nishauri sana, naunga mkono lakini kwenye hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha nitashika shilingi. Kama 35% haitawekwa, kama VAT haitaondolewa kwenye mafuta ya ndani, hili nitashika shilingi kwa sababu tunakwenda kuwatia umaskini wananchi na hivi viwanda vinamilikiwa 80% na Watanzania. Leo ukiruhusu hiyo 25% maana yake viwanda vyetu vinakwenda kufa. Hili siyo sawa, niombe sana kwa kweli Waziri wa Fedha unafanya kazi vizuri, lakini katika hili niombe kwa kweli lazima tulinde wakulima wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuja kwenye ngano; ngano tunalima, kule Njombe wanalima, kule Katavi wanalima, kule Arusha, Babati wanalima, lakini mapendekezo ya wataalam wako Mheshimiwa Waziri yanasema unaondoa 35% unaweka 10%. Sasa hawa Watanzania wanalima ngano ya nini? Kwa sababu ukipunguza tu kodi ya ngano nje maana yake kwamba unamfanya mkulima wa Tanzania asiendelee kulima. Sasa hapa tunakuza uchumi? Hapa tunakuza uchumi au tunakuza mapato? Haiwezekani, lazima tuwe tayari, tumetoa mbegu za ngano, tumetoa ruzuku kila mahali, kwa hiyo lazima tulinde wakulima wetu na tulinde biashara ya Tanzania na niombe sana hapa, kama tuna mazao ambayo ni ya kimkakati ambayo yanaweza kwenda kuinua uchumi na kupunguza fedha za kigeni kwenda nje lazima tuyalinde kwa wivu, tusiyaachie hivi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hili Bunge ndilo ambalo linaweza kutengeneza mwelekeo wa uchumi kwa nchi hii. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri mimi nataka uwe na uwezo wa kukusanya fedha ili heshima ya nchi iwepo ni mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo tunapokwenda kupunguza kodi, tunapunguza mapato. Ili heshima ya familia iwepo ni mapato kwenye familia. Familia ukikosa baba wa familia hela hauna heshima. Kwa hiyo, tunapokwenda kupunguza mapato kwa sababu ya vitu kutoka nje tunakwenda kupunguza heshima ya nchi. Lazima tujitegemee, tutaendelea kukulaumu, tutaendelea kumlaumu Mheshimiwa Rais, lakini lazima tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la mwisho...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Sekunde 30.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, naomba ni-declare interest mimi ni Mwenyekiti wa Wachambuaji wa Pamba Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mwaka 2019 Serikali ilisema wanunuzi wa pamba wanunue pamba kwa bei yoyote itafidia. Bunge lako limeshatoa azimio na hawa wafanyabiashara 100% ni Watanzania. Leo benki interest zinaendelea kuwa cruel. Niombe kwa sababu ni Azimio la Bunge na fedha tunaamini zipo, Mheshimiwa Waziri aone namna ya kuweza kulipa ili kuwawezesha hawa wafanyabiashara na kuwezesha viwanda viweze kuendelea. Hatuwezi kulipa madeni ya nje tushindwe kulipa madeni ya ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niunge mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 20 16/2017 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Utumishi na Utawala Bora
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba kumshukuru Mwenyezi Mungu anayeneemesha neema nyingi nami akanineemesha neema ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipongeze hotuba za Waheshimiwa Mawaziri wote wawili kwa kadri zilivyojielekeza kuhudumia na kutatua kero za wananchi. Nianze na eneo la elimu bure. Safari moja huanzisha nyingine, tumeanza, pamoja na changamoto, inapaswa sasa kama Serikali ione namna ambavyo itaongeza fedha hizi ili ziweze kukidhi mahitaji ya uendeshaji wa shule. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati suala hili la MEM linaanza 2002 capitation tulikuwa tunapeleka dola kumi kwa kila mwanafunzi. Wakati huo exchange rate ilikuwa ni shilingi1000 leo ni shilingi 2000. Maana yake kwamba ili zitosheleze lazima tupeleke mara mbili. Naishauri Serikali iweze kuliona hili ili iweze kuongeza kiwango hiki kinachotolewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu bure chekechea hadi kidato cha nne ni sahihi. Mimi najiuliza hivi mtoto wa maskini huyu anapofika kidato cha tano anatajirika?
Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iangalie kwa upana wake hata kama siyo bajeti hii, bajeti ijayo iweze kuwaangalia watoto hawa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye jambo la maji, maji ni hitaji la kila mmoja wetu tulioko mahali hapa. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri wa Maji alitembelea Wilaya yangu ya Magu kwa kweli alinitendea haki na Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa Serikali ijielekeze kuhakikisha kwamba wale ambao tunazungukwa na Ziwa Victoria tunapata maji ya kutosha na wengine ambao wanazungukwa na Ziwa Tanganyika nao wapate maji ya kutosha. Haiwezekani watu tunasimama tunaliangalia ziwa lakini maji hatuna, hamtutendei haki.
Naishauri Serikali hii iangalie kwa sababu uchumi wa nchi hii wachangiaji wakubwa ni akina mama lakini inapofika saa tisa za usiku akina mama wanaondoka kwenda kutafuta maji. Ninapotembelea vijiji vyangu wanalalamika wanasema hata watoto asubuhi hawawaoni hawa akina mama. Naomba sana Serikali iangalie hata kama ni kukopa kwenye mifuko ya fedha tuwekeze kwenye maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nishati. Namshukuru sana Naibu Waziri wa Nishati na Madini alitembelea Jimbo langu, tukatembea naye siku moja vijiji kumi, alinitendea haki Mungu ambariki sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ili uchumi ukue umeme unahitajika kila mahali. Tunapozungumzia viwanda vidogo wakati mahali ambapo vinahitajika viwanda hivi vijengwe umeme haupo. Niombe Serikali kwa jitihada ilizonazo kupitia REA Phase II na III tuweze kukamilisha vijiji vyote kwa kuvipatia umeme. (Makofi)
Naomba nizungumzie afya. Hotuba ya Waziri inasema vijiji 8,043 havina zahanati. Wewe ni shahidi kwenye vijiji vyako Jimbo la Bariadi ni vijiji vikubwa sana ukizingatia na Jimbo langu la Magu nalo lina vijiji vikubwa, kuondoka kijiji kimoja kufuata huduma ya afya kijiji kingine unachukua kilometa 15 na hakuna hata zahanati za private, hakuna hata maduka ya dawa. Niishauri Serikali kwa sababu wananchi wa Wilaya ya Magu wameanzisha maboma ya kutosha ya zahanati tupewe fedha za kukamilisha zahanati hizo ili wananchi waweze kupata huduma hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la viongozi wa kisiasa kwa maana ya Wenyeviti wa Vitongoji, Wenyeviti wa Vijiji na Waheshimiwa Madiwani. Katika uongozi mgumu duniani sijui dunia au Tanzania hii, hakuna uongozi mgumu kama Mwenyekiti wa Kitongoji, Mwenyekiti wa Kijiji na Mheshimiwa Diwani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa lazima tuelewane vizuri na naomba Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa sababu kuna kipengele kwenye viapo vyenu kinasema utamshauri Mheshimiwa Rais kwa hekima, hapa ndipo mnatakiwa mumshauri kwa hekima. Mwenyekiti wa Kitongoji yeye ndiye anayefanikisha ujenzi wa madarasa, ujenzi wa zahanati na vitu vyote vilivyoko kule. Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kitongoji leo mwananchi akikamatwa mahali popote yeye ndiye anayekwenda kuandika dhamana adhaminiwe, huyu ni mtu muhimu sana. Mimi leo nikitaka kufanya ziara yeye lazima aweko. Naomba Serikali tuelewane iweke siyo fedha nyingi, tuanze na za kuanzia ili hawa watu waweze kupata posho zao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Mheshimiwa Diwani mimi nimetokea huko niseme tu kwamba hawa watu ndiyo walionileta hapa kwamba tumpeleke mwenzetu anayetufahamu. Diwani aliyefanikiwa kuwa na gari halali usiku kucha gari yake ndiyo ambulance kupeleka wagonjwa hospitali. Leo maslahi yake tunayaona kama yanatosha hayatoshi. Niombe sana wasaidieni watu hawa na ndiyo wanaojenga siasa kwenye maeneo yetu, ni Wenyeviti wa Vitongoji, Vijiji na Madiwani. Naomba tuelewane vizuri hapa katika bajeti hii au bajeti ijayo. (Makofi)
Niendelee kusema kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ndiyo ambayo wananchi walikuwa wakiingoja, ni Serikali shupavu, Serikali ya kazi tu. Mwaka fulani Mheshimiwa Rais Nyerere alitangaza Kilimo cha Kufa na Kupona, Rais Magufuli ametangaza kazi ya kufa na kupona, huyo lazima tumpongeze. Wale wanaobeza ni mioyo ambayo haina shukurani. Maandiko Matakatifu yanasema mioyo ambayo haina shukurani hukausha mema mengi. Naiomba Serikali hii ya Awamu ya Tano, wale watu ambao hawashukuru ikaushe miradi ya maendeleo isipeleke kwao. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu aombaye hupewa, huwezi kuwa unasimama unatukana Serikali inayokujali halafu unapewa miradi. Naomba Serikali hii isiwape miradi watu hawa ambao hawana shukurani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, walikuwa wakisema Serikali hii haina meno, Serikali imeanza kutumbua majipu wao wanakuwa mawakala wa wale waliotumbuliwa.
Haiwezekani, tuipe heshima Serikali iweze kufanya kazi. Naomba tunapopanga miradi hii isimamiwe…
Na Wizara ili tuweze kutekeleza miradi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, kwanza nianze tu kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Nishati kadri ambavyo imejielekeza namna ya kutatua matatizo ya wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Profesa Muhongo anaondolewa kwenye Wizara hii wananchi wa Tanzania walisikitika sana na wakati amerudishwa wananchi wa Tanzania wameshukuru sana, kwa hiyo, endelea kuchapa kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba katika Wizara, Wizara hii ni ngumu sana, dunia yote hutafuta madini, hutafuta kupata utajiri kupitia madini, hii ni Wizara ngumu sana. Kwa hiyo lazima tukupongeze wewe pamoja na Naibu wako kwa kadri ambavyo mnachapa kazi Mungu awabariki sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina vijiji ambavyo vimepitiwa na REA Phase II, lakini vijiji hivyo ni Ng’haya, Bundlya, Kabila, Kigangama na Kisamba zimewekewa nguzo chache sana na sehemu zingine hata shule za msingi, makanisa na zahanati hazijapata umeme. Shahidi ni Naibu Waziri wa Nishati, tulitembelea maeneo hayo. Naomba mtakapokuja kujibu mseme pia kwamba mnaongeza vijiji hivyo ili vikamilike vionekane kwamba kweli REA Phase II, imevitendea haki.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninavyo vijiji viwili pia ambavyo havikuwekewa umeme, umeme huu umekwenda kwenye vijiji vingine, kwa mfano Nyashigwe, iko kwenye REA Phase II, lakini umeme wake umekwenda kitongoji cha Mawe ambacho ni kijiji cha Welamasonga. Kwa hiyo, kijiji hiki hakijawekewa umeme, mtakapokuja kutoa majibu mniambie je, mtakiingiza kwenye Phase III, aumtakipelekea umeme sasa?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kipo kijiji kingine cha Kitongo Ndagalu ambapo makao makuu ya kijiji ambayo ni center kubwa haijawekewa umeme, umeme umewekwa kitongoji cha Misungwi, napo mje mniambie ili wananchi hawa waweze kupata umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ha utainga sasa hivi REA Phase II, basi uingizwe REA Phase III. Lakini umeme ambako wamekamilisha kama Kabila, Ng’haya haujawaka, naomba Wizara kwa maana ya Waziri muhimize ili kama umekamilika umeme huu uweze kuwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, vijiji vya Magu havina umeme asilimia 70, ninaomba sasa kupitia REA Phase III, vijiji hivi viwekewe umeme, nimeongea na wewe Mheshimiwa Waziri, nimeongea na Naibu Waziri, nimeongea na Meneja wa Kanda, naomba sasa vijiji hivi kwa kweli viweze kupatiwa umeme wa kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni declare interest nilikua mchimbaji mdogo mwaka 1993 katika machimbo ya Ulyankulu na huko ndiko nimeanzia maisha. Wachimbaji hawa wanateseka sana kila siku, wanahama kila leo, lakini wachimbaji hawa ni ajira yao. Tunapozungumzia Tanzanite, wachimbaji wale sio wa Arusha tu, wa Magu wapo, wa Bariadi wapo, wa Sengerema wapo. Tunapozungumzia almasi, wachimbaji wa nchi nzima wako kule na wa Magu wapo, tunapozungumzia dhahabu, wachimbaji wa Magu wapo. Kama walivyolalamika Waheshimiwa Wabunge wenzangu, ninaomba hawa wachimbaji wadogo wadogo kama azma ya Serikali ni kuwatafutia maeneo iwatafutie maeneo ili waweze kupatiwa maeneo ya uchimbaji, hiyo ndio ajira yao ya kudumu.
Mhehimiwa Mwenyekiti, yako malalamiko kwamba mikataba ya madini tunapata fedha kidogo sana kama nchi. Ninaomba sasa haya nayo ni maeneo ambayo yanalalamikiwa na kila mmoja wetu ili yaweze kupitiwa na kuangaliwa ili Serikalil iweze kupata mapata ambayo kwa kweli yatanufaisha Taifa letu la Tanzania. Maana tunaweza kuwa na madini baadaye tukaachiwa mashimo na nchi isinufaike. Naishauri Serikali iangalie kwa uhakika ili kuhakikisha kwamba mikataba hii inawanufaisha watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambayo yamewekewa umeme wa REA wananchi wanashukuru sana, sasa niguse tu kwamba tutakapokamilisha maeneo ya vijiji, viko vitongoji ambavyo navyo ni kama vijiji, kwa hiyo, tusiishie REA Phase III, lazima tuende na REA Phase IV. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishie hapo na niunge mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizara ya Maji na Umwagiliaji
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Sanjo ina vijiji 24 na wananchi 120,000. Ina hali mbaya sana, haina hata bwawa wala mito, lakini imezungukwa na Ziwa Victoria. Maji yanatakiwa yatoke Lutale ambapo ndiyo chanzo, yaende Vijiji vya Kageye, Kayenze, Itandula, Langi, Makamba, Shilingwa, Kongolo, Chabula, Bugando, Nyashiwe, Ihayabuyaga, Welamasonga, Matale, Sese, Ihushi, Isangijo, Busekwa, Bujora, Kisesa, Kanyama, Wita, Welamasonga na Igekemaja.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Ndagalu ina vijiji 26 wakazi 86,000. Tarafa hii haina hata mto wala bwawa sasa wanafuata maji kilometa hadi 58. Tunaomba watu hawa muwaonee huruma, chanzo cha maji kitoke Nsola kwenda Misungwi, Kitongo, Lumeji, Nyang’hanga, Iseni, Mwamibanga, Buhumbi, Nyashoshi, Ng’haya, Mwabulenga, Nkungulu, Kayenze ‘B’, Chandulu, Bugatu, Salama, Kabila, Ng’wamagoli, Jinjimili, Nhobola, Kabale, Nyasato, Mahaha, Shishani, Isolo, Igombe, Ndagalu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa hii ya Ndagalu hata visima virefu havipo. Naomba tusaidiwe hata kwa dharura visima virefu kila kijiji pamoja na bwawa la Kabila likarabatiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, Naibu Katibu Mkuu, Engineer Kalobelo alifika akaona shida iliyopo akatuma wataalam kutoka MWAUWASA walifanya ziara wakaandika andiko la miradi hii miwili na Mkurugenzi alileta kwenye bajeti, Baraza likapitisha na tukapeleka hata Wizara ya Maji kwa Mkurugenzi wa Maji Bwana Mafuru, pamoja na kwa Naibu Katibu Mkuu Engineer Kalobelo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasikitika kutoona miradi hii kwenye bajeti. Jamani wanionee huruma hata waniwekee fedha za kuanzia ili kila mwaka waendelee kuniwekea, hususan naamini tutaongeza sh.50/= kwa kila lita ya mafuta.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukinisaidia hii, utakuwa umeokoa maisha ya Watanzania wengi sana wa Jimbo la Magu.

Mhshimiwa Naibu Spika, natanguliza shukurani.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ili niweze kuchangia hotuba ya Wizara ya Maji kama ambavyo Mheshimiwa Waziri ameiwasilisha. Kwa kweli imesheheni mambo mengi ambayo yakitekelezwa yatatatua kero za Watanzania na kidogo sana katika Jimbo la Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesoma hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri, Magu kwa ujumla ina shida ya maji, miaka yote tumekuwa na shida ya maji. Kilio kikubwa cha Wan-Magu ni maji, mpaka najiuliza kwamba Wilaya ya Magu imekosea nini, imeikosea nini hii nchi mpaka tupate matatizo makubwa ya maji kiasi hicho ambapo Wilaya ya Magu imezungukwa na maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu cha hotuba ya Waziri nimeona mradi mkubwa wa maji Magu Mjini, ambao utasaidia wananchi wa Magu wapatao 36,000, lakini wananchi 340,000 hawatakuwa na huduma ya maji, ninasikitika sana na ukizingatia kwamba hata Wilaya ambazo zinanizunguka majirani zangu kwa maana ya Wilaya Bariadi ambako wewe uko, nayo haina maji, Wilaya ya Busega nayo haina maji, Wilaya ya Kwimba nayo haina maji. Kwa hiyo, najikuta niko katikati pale hata majirani hawawezi kunisaidia, wewe unajua kabisa kwamba bhuzengano bhutikubhwaga makira. Lakini huo uzengano hauna chochote napata taabu sana, yaani kwamba ujirani huwa haunyimani mambo mazuri manono. Kwa hiyo, napata taabu kwa sababu majirani zangu hawana maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpango huu wa maji kwa kweli kama hotuba inavyosema kama kweli wakandarasi wameshapelekewa vitabu, kama kweli unaweza kuanza mwaka huu utarudisha imani kwa wananchi wa Magu kwamba sasa wanaanza kupata huduma ya maji. Lakini kama nilivyosema wananchi 340,000 bado wanakunywa maji ambayo wanachangia na ngo‟mbe, mbwa na fisi huko vijijini, wana shida kubwa ya maji. Ni vema katika Mji wa Kabila ambao wewe unaujua vizuri Mahaha, Ng‟haya, Nkhobola Serikali ikawa na mpango mzuri wa kuwafikishia maji wananchi hawa hata kama siyo bajeti hii kwa sababu naona bajeti hii imelenga kutekeleza miradi hii, bajeti ijayo nifikiriwe vizuri zaidi katika Wilaya ya Magu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna kijiji cha Nyang‟hanga ambacho kimetoa Wabunge wa Nne tangu Magu ianze kupata Wabunge, wote wanatoka kijiji hiki cha Nyang‟hanga hakina maji. Kijiji hiki Mheshimiwa Dkt. Festus Bulugu Limbu alifanikiwa kuchimba visima virefu vya maji, vina maji mengi ya kutosha kwa ajili ya kusambaza katika kijiji hiki cha Buhumbi pamoja na kijiji cha Nyang‟hanga, lakini kila mwaka nina- declare interest kuwa nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri tulikuwa tukiomba maombi maalum ya shilingi milioni 700 ili mradi huu uweze kusambaza maji hatukupatiwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninamuomba Mheshimiwa Waziri anihurumie Jimbo la Magu, atuhurumie kijiji hiki atafute fedha mahali popote ili aweze kutusaidia shilingi milioni 700 tuweze kusambaza maji katika kijiji cha Nyang‟hanga na Buhumbi.
Tunao mradi ambao unaendelea wa Sola Bubinza, huu ni mradi ambao umeanza tu lakini umekosa fedha, Wizara inajua, Katibu Mkuu anajua na Mheshimiwa Waziri anajua. Ninamuomba sasa kwa sababu ni mradi ambao ulikuwa unaendelea kuliko kupoteza fedha nyingi za walipa kodi wa nchi hii, tupewe fedha kwenye bajeti hii ili mradi huu uweze kukamilika na wananchi wapate huduma ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika sana, mradi huu unaopeleka maji Magu chanzo chake kinatoka Kata ya Kahangala, kijiji cha Bugabu. Lakini Makao Makuu ya Kata ambayo ni kilometa nane tu kutoka pale chanzo kilipo au bomba litakapopita hakimo kwenye mpango wa kuwekewa maji, hii ni haki kweli? Niombe Waziri atafute kila linalowezekana ili Makao Makuu haya ya Tarafa ya Kahangala ambako maji yanatoka yaweze kupata maji ni hela kidogo tu. Naomba sana Mheshimiwa Waziri asaidie jambo hili. Tunayo Kata ya Mwamanga ambayo nayo ilikuwa na Mradi wa Matokeo Makubwa sasa wa awamu iliyopita. Kuna miradi ambayo ilianza lakini fedha zake hazijapatikana, niombe kwenye bajeti hii ni vizuri tukamaliza viporo ambavyo vilikuwa vimeanzishwa ili wananchi waweze kupata huduma inayostahili. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi wa Lugeye Kigangama, Mheshimiwa Waziri alifika kwenye mradi huu na Mheshimiwa Lubeleje pia alifika kwenye mradi huu. Unadaiwa shilingi milioni 94 tu ukamilike, chonde chonde naiomba Serikali yangu ya kazi, Serikali ya Awamu ya Tano itupe hizo shilingi milioni 94 ili mradi huu uweze kukamilika. Tuna kiangazi kikubwa sana, kwa kweli katika Wilaya ya Magu la sivyo tutapata taabu haingii akilini, kwamba shilingi milioni 94 zinakosekana ili mradi huu uweze kukamilika maji yameshavutwa yameshaletwa kwenye tank ni kusambaza tu kuunganisha koki mbalimbali, naomba nisaidiwe na Serikali hii ya Awamu ya Tano. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tarafa ya Sanjo inazungukwa na maji lakini haina maji, na Tarafa ile inaongoza kwa kupata kipindupindu kwa sababu wanatumia maji ambayo hayajatibiwa, Tarafa ile ina Mji wa Kisesa, Mji wa Bujola bado una shida kubwa ya maji. Population ya pale inazidi hata Makao Makuu ya Wilaya ya Magu. Ninaomba angalau utafutwe mradi ambao unaweza kutokea Ilemela, Buswelu, Nyamongolo ulete maji katika Mji wa Kisesa, lakini hata Lutale, Kongolo pamoja na Chabula nao wanahitaji maji haya ya kutoka Ziwa Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sana, ninajua kwamba fedha zilizotengwa kwenye bajeti ya maji ni kidogo, lakini zitaleta impact sana kama miradi hii itatekelezwa. Tuombe mahala ambapo sisi hatujapata fedha tufikiriwe sana bajeti ijayo ili tuwemo kwenye utaratibu wa kusaidiwa miradi hii ya maji.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kanda ya Ziwa imebaki kuwa jina tu, Wilaya zake zote hazina maji tunahangaikia Sengerema…
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Ahsante sana.
Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia hotuba hii ya Waziri wa Fedha.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabla sijaanza kuchangia nianze kuweka rekodi sawa sawa. Hapa ndani kwa sababu kuna Wabunge wenzangu wakati mwingine wanasema kwamba Mawaziri waache siasa. Nataka niongee tu jambo hili; kwanza siasa ni taaluma; na sisi tuliopo wote hapa tumeingizwa kwenye siasa. Siasa ni ngumu sana, lakini ni nzuri sana, tatizo ni tunavyoitumia tu kama wenzetu wanavyoitumia vibaya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala la kupata Ubunge ni kazi kweli kweli na suala la kupata Urasi ni kazi kweli kweli! Sisi ambao tumepita kwenye mchakato huu tunajua joto lake. Kwa hiyo, hata wote tunapokuwa humu tumebeba mizigo; wa kuteuliwa, sijui wa kutoka group gani, inategemea mizigo hiyo ina uzito gani; lakini uzito wa Jimbo ni uzito kweli kweli. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba duniani kote hakuna mtu anayehitaji kulipa kodi. Hata vitabu vya dini vimezungumza sana suala la kulipa kodi na aliyekuwa akitoza kodi wakati wa Yesu alikuwa ni mtu ambaye anachukiwa na Umma wote. Kwa hiyo, Serikali kukusanya kodi isiogope, ni jambo la kawaida, ndiyo uhai wa Serikali. Naiomba sana Serikali hii isirudi nyuma, ihakikishe inakusanya kodi ili wananchi waweze kupata huduma. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na suala la maji. Suala la shilingi 50 kuongezwa kwenye dizeli na petroli ili iende kugharamia maji, ninasikitika sana, kwamba Serikali imeona kwamba ikiongeza shilingi 50 italeta mfumuko wa bei. Nataka kuuliza au mmeshatuuliza? Sisi Wabunge humu ndio watumiaji wa mafuta. Tumeshakataa kuongezwa hii shilingi 50? Sisi tumeshakubali tuongezwe shilingi 50 kwenye petroli pamoja na dizeli ili kugharamia Mfuko wa Maji Vijijini. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sera yetu inasema mita 400 wananchi waweze kupata maji. Kwa namna hii tunayokwenda, hatutaweza kuifikia hiyo sera na mwaka 2020 tutapata taabu kweli kweli kurudi humu Bungeni, kwa sababu wakina mama wanateseka kila asubuhi, kila saa kumi na moja wanakwenda kuteka maji. Tuwahurumie! Wanapoteseka akina mama na sisi akina baba tunateseka. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siku moja nimewahi kusema asali ni tamu sana lakini wako watu hawaitumii asali, lakini kila mmoja anaguswa na maji; awe mtumia gari, anaguswa na maji aoshee gari lake. Kwa hiyo, naishauri Serikali hii ya Awamu ya Tano, Serikali ya kazi; kwa sababu unaweza kuwa na Serikali sikivu, ikawa inasikia tu, isifanye kazi. Sasa hii ni Serikali ya kazi, ifanye kazi kuongeza shilingi 50 ili akina mama waweze kupata maji ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, ninaongea haya kwa sababu nimetoka Jimboni, hali ni mbaya, akina mama wanasumbuka na mimi nina hali mbaya! (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza ungenionea huruma ukanipatia chupa ya maji hapa ili niweze kuongea vizuri huku nakunywa maji. Naomba hili, wala halipaswi kujadiliwa, iongezwe shilingi 50 kwenye mafuta, wala tusijadili hili; kama haitaongezwa, kama kuna kushika shilingi, mimi nitashika shilingi kwa sababu ya maji. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimeangalia kwenye fedha za ujenzi wa zahanati. Ilani yetu inazungumza kwamba kila Kijiji kiwe na zahanati; kila Kata iwe na vituo vya afya. Humu tuliomo ndani humu na wengine tunachagua mahali pa kwenda kupata matibabu, lakini mwananchi wa kawaida, maskini, hana hata mahali pa kwenda kupata matibabu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, zahanati ni jambo la muhimu sana kujenga ili kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma hii. Sasa kama Ilani yetu inazungumza kwamba tuwe na zahanati kila kijiji, tuwe na kituo cha afya, wananchi wameshaandaa maboma ya kutosha, wanasubiri fedha za Serikali ili Serikali iwaunge mkono; tupelekeeni fedha hizo ili kupunguza matatizo ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Serikali imekuja na mpango wa kupunguza kodi kwenye mazao, lakini nimeangalia kwenye zao la pamba; kilichoondolewa kile siyo tija kwa wananchi. Umeondoa mwenge, umeondoa kikao ambacho ni fedha ambazo zinalipwa na jina, ni hela kidogo sana hizo. Tunazungumzia shilingi 400,000 kwa jina; hiyo inaongeza nini kwenye bei ya pamba?
Mheshimiwa Naibu Spika, zipo kodi mbalimbali cess za Halmashauri, kuna CDTF, mfuko wa kuendeleza zao la pamba; hizi zote inapashwa Serikali ifidie ili mkulima aweze kupata bei nzuri. Tusipofanya hivyo, zao la pemba linakwenda kufa. Sasa mnapozungumzia viwanda, kwa mazao yapi? Mnapozungumzia viwanda, kwa sababu viwanda vinavyoongeza ajira ni viwanda ambavyo malighafi yake ni pamba. Hili Mheshimiwa Waziri wa Fedha aliangalie ili tuweze kuona ni jinsi gani tunaweza kuwasaidia wakulima wa pamba.
Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kodi ambazo Mheshimiwa Rais alikuwa anasema ataziondoa; kodi zenye kero, lakini naona kama hatujaziondoa hivi.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wana shida, akina mama ntilie, sokoni wauza nyanya na michicha wana shida. Tungeangalia jambo hili kwa mapana yake, upo ushuru hauna tija, hata Halmashauri haiongezei kitu chochote. Naomba anakapokuja kumalizia hapa atuambie, hizi kodi ambazo Mheshimiwa Rais aliahidi, ushuru wenye kero, utaondolewa kwa namna gani? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie tu kuongeza usajili wa bodaboda. Hili ni kundi ambalo ni maskini sana, lakini ni kundi ambalo linarahisisha usafiri wa wananchi wetu vijijini ambako gari hazifiki. Yapo maeneo barabara haziko; wanaotusaidia ni hawa watu wa bodaboda.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunapoongeza usajili maana yake tunataka kuwapunguza hawa watu. Kama tungeacha kodi ilie ile, ingechochea kuingiza bodaboda nyingi zaidi, ikachochea hao bodaboda kununua mafuta mengi zaidi na kuongeza uchumi wa nchi hii. Naomba hili nalo liondolewe; halina sababu na halina tija sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wamezungumza suala la CAG, na mimi naendelea kusema nilikuwa Mwenyekiti wa Halmashauri, chombo hiki ni muhimu sana; chombo hiki ni cha kitaalam. Mheshimiwa Profesa Muhongo anasema haya ni mambo ya kitaalam.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama haya ni mambo ya kitaalam halafu tunayapunguzia fedha, itakuwa ni aibu. Halmashauri zitakuwa na hali mbaya na Wizara zitakuwa na hali mbaya. Naomba fedha ziongezwe ili tuweze kuhakikisha udhibiti wa fedha hizi tunazozipeleka, zinakuwa na uhakika zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo duniani huwa hayajadiliwi. Suala la mafao kwa Wabunge ni jambo ambalo duniani halijadiliwi. Ku-maintain Jimbo ni sawasawa na kujenga kiwanda cha kati. Wabunge hawa wabishe. Ku-maintain Jimbo ni sawa na kujenga kiwanda cha kati.
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba hili liondolewe mara moja, halina mjadala, halina nafasi ili kuhakikisha kwamba Wabunge hawa sio pensionable. Mbunge hapa akienda kupigwa dafrao, unaweza kumshangaa, ni hali ngumu. Naomba hili kwa kweli lisiingizwe, wala lisijadiliwe na liondolewe mara moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naendelea sasa kuipongeza Serikali, kazeni buti kukusanya kodi ili huduma za wananchi zipatikane. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru kwa kunipatia nafasi ya kuweza kuchangia.

Kwanza nianze na barabara yangu ya kutoka Magu - Kabila - Mahaha. Barabara hii ina kilometa 58, lakini mwaka huu haijatengewa fedha, matengenezo maalum au matengenezo ya mara kwa mara haina fedha. Nashukuru kwamba imetengewa fedha kwa ajili ya daraja ambalo Serikali inagharamika kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya daraja hili. Ninajua kwamba tayari upembuzi yakinifu umeshakamilika na mkandarasi ameshapatikana, tatizo ni fedha za kuendelea. Niiombe Serikali nikiamini kwamba bajeti ambayo tunayo tulitenga fedha kwa ajili ya kulijenga lile daraja angalau zitoke fedha za kuanzia lile daraja Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninamuomba tu Waziri kwa sababu sihitaji kulalamika, aiandike barabara hii ili aiwekee fedha angalau ipate fedha za matengenezo kwa mwaka huu wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara hii pia ni ahadi ya Rais kuwekewa lami alipokuwa kwenye kampeni Mheshimiwa Rais alipotembea aliona ametembea umbali mkubwa zaidi sana. Alipofika kule Kabila akasahau kwamba yuko Magu akasema yuko Kwimba, baada ya pale akasema basi barabara hii tutaijenga kwa kiwango cha lami, naomba ahadi hii nayo iheshimiwe.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna barabara hii ya Isandula - Ngudu ni barabara muhimu iko kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi tangu 2005, hebu tupeni fedha ili iweze kutengenezwa kwa kiwango cha lami.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunazo barabara ambazo tuliziomba Road Board zipande kutoka Wilaya kwenda Mkoa, bahati nzuri Wizara yako Mheshimiwa Waziri ilileta wataalam wa kuzipitia, zikaonekana hizi zina qualify, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri sasa uzipandishe hizi barabara kwa sababu uwezo pekee wa Halmashauri hatuwezi kuzigharamia. Hizi ni barabara ya Kisamba - Sayaka - Salama na Simiyu kule Bariadi ni barabara muhimu sana ya kufungua uchumi. Tunayo barabara ya Ilungu kuelekea Kwimba mpaka Maswa ni barabara muhimu sana kiuchumi, tunayo barabara ya Kisesa - Kayenze - Ilemela inaweza kupunguza pia msongamano wa kuingia Jiji la Mwanza, tonayo barabara ya Nyanguge - Kwimba hizi barabara zote zime-qualify, ningetegemea kwamba bajeti hii zingeweza kupatiwa fedha, naomba zipatiwe fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara muhimu inayotoka Airport - Ilemela ambayo ikitengenezwa kwa kiwango cha lami mpaka Nyanguge inapunguza msongamano kabisa wa wananchi wote kutoka Musoma kuelekea Mwanza hawatapita Mwanza Mjini watakwenda airport itapunguza msongamano. Hebu muiweke vizuri kwa sababu tumeomba kila siku.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ipo barabara ya kilometa
1.2 ya Kisesa – Bujora, barabara hii inapitiwa na viongozi wote wa kitaifa kila mwaka kwa ajili ya kwenda kwenye makumbusho, tumeiomba kama Road Board kila mwaka kiongozi wa kitaifa lazima apite, naomba na hii iingie ni kilometa 1.2.

Mheshimwa Naibu Spika, ahadi ya Rais ya kilometa tano za lami Magu Mjini, bahati nzuri Mheshimiwa Waziri ulikuja Magu nikakutembeza kwenye barabara zile ukaziona zilivyo, hebu tusaidie kwenye bajeti hii angalau ahadi hii ya kilometa tano za lami ianze ili wananchi waweze kupata huduma inayokubalika.

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo mengi nataka nijikite kwenye taasisi hii ya marine. Taasisi hii ya Marine Services ina uhakika wa kuingiza kipato kwenye nchi hii, nina uhakika mkiijali inaweza kuchangia uchumi kwenye nchi hii pia shirika hili linaweza kujiendesha. Mheshimiwa Waziri hili shirika ni kama limetelekezwa, tunazo meli 15 katika maziwa yetu haya matatu, sekta binafsi wako ambao wana meli kule Ziwa Victoria wanafanya vizuri wana meli na kila mwaka wanaongeza meli, kwa nini Marine isihudumiwe? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti iliyopita tulitenga fedha, lakini mpaka leo fedha hizi Marine hawajapewa taasisi hii. Ni kama dhahabu ambayo iko ndani hatujaipeleka sokoni, hebu tuisaidie Marine ili iweze kuchangia uchumi na iweze kujiendesha.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati mbaya kabisa wapiga kura wetu kule ni wafanyakazi wa taasisi hii mishahara hawalipwi, bima ya afya wamefungiwa, kuna mambo kede wa kede. Ushauri wangu ni kwamba kwa sababu hii ni taasisi ambayo iki-link na bandari; ika-link na reli naamini mizigo yote ambayo inakwenda Uganda inaweza ku-support sana kupata fedha nyingi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunacho kivuko ambacho alikiongelea hapa Mheshimiwa Mabula, Ilemala pale tumeomba kivuko cha Kayanze, Bezi na Ijinga. Wananchi walioko visiwa vile ni zaidi ya wananchi huku wako 600,000 Bezi lakini na Ijinga wapo zaidi ya 400,000. Kwa hiyo, wakipata kivuko hiki kinatasaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo mambo ambayo Serikali imefanya, makubwa sana kwa muda mfupi na wala hayawezi kuelezeka. Na mimi nilikuwa najiuliza sana, Mheshimiwa mmoja alikuwa anasema kwamba kipindi hiki tumepata Rais wa ajabu, nilishindwa kumuelewa, lakini sasa nimeanza kumuelewa kwamba kweli tumepata Rais wa ajabu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna kitu kinaitwa Bombardier ndege mbili zimekuja, nne bado zinakuja jumla ndege sita, kwa muda mfupi, huyu ni Rais wa ajabu haijawahi kutokea! Kuna kitu kinaitwa standard gauge tukitafakari kidogo Waheshimiwa Wabunge hili ni jambo kubwa la kihistoria, nasema huyu ni Rais wa ajabu. Kupambana na ufisadi haijawahi kutokea, kupambana na dawa za kulevya haijawahi kutokea, kupambana na rushwa haijawahi kutokea, huyu ni Rais wa ajabu lazima, tumpe hongera zake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yote haya yanayofanywa na Serikali kwa miradi yote ya kiuchumi na huduma za kijamii hili ni tendo la huruma, na sisi viongozi tunapaswa kuwa na huruma. Mithali ya pili maandiko matakatifu ambayo siyo ya kwako wewe sura ya 19:17 unasema, amhurumiaye maskini anamkopesha Mungu naYe atamlipa kwa tendo lake jema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa huruma hii ya Mheshimiwa Rais na Serikali yake na Waheshimiwa Mawaziri na watendaji wake wakuu wa Serikali, wanafanya kazi ya huruma wanamkopesha Mungu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niunge mkono hoja. Ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018 - Wizari ya Maji na Umwagiliaji
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwakunipa nafasi hii ya kuchangia. Nianze kwanza kwa kutoa shukrani kwa Wizara hii ya Maji kwa maana ya Mawaziri wote na Watendaji Wakuu wa Wizara kwa namna ambavyo wanafanya kazi. Wako watu asubuhi walisema Mawaziri hawa ni wazee, lakini nataka niseme aliyewateua bahati nzuri amefanya nao kazi, hawa ni Mawaziri makini kwelikweli na ni wachapakazi kweli. Ukienda ofisini kwao, ukiwaita jimboni wanakuja haraka kuja kuona shida ulizonazo. Kwa hiyo, kwa kweli nawapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee nimpongeze Mheshimiwa Rais. Wakati anaomba kura alifika Magu akasema hapa shida moja ni maji na mimi wakati naomba kura niliwaeleza wanachi kama maji hayatapatikana sirudi 2020. Bahati nzuri wakati anazunguka hivi karibuni kwenda Simiyu alipita Magu akasema nakwenda kumuagiza Waziri wa Maji ili aweze kuja kusaini mkataba haraka na wakandarasi wawe site. Hivi ninavyozungumza mkataba ule tuliusaini hadharani kule Nyasaka ambapo utahudumu kata nne kule mjini Jimbo la Ilemela pamoja na kata tatu Jimbo la Nyamagana lakini mradi huu unaunganisha pia na Lamadi na Misungwi. Magu wakandarasi wako site.Nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa ahadi yake ya kweli na Wanamagu watapata maji, Magu ilikuwa imesahaulika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yapo maeneo mengi, mradi huu wa Magu Mjini utahudumia wananchi 46,000 lakini Tarafa ya Ndagalu ambayo haina bwawa, haina mto, vijiji 21 wakazi 86,000 wana hali mbaya kutokana na kukosa huduma ya maji. Kwa hiyo, pamoja na kwamba bajeti hii inasemwa haitoshi na mimi nikisema hii inatosha maana yake tarafa hii haitaingizwa. Hata hivyo, niendelee kusema tunapokuwa na shilingi bilioni 600 zikaenda zote shilingi bilioni 600 mwaka huo tunahama hapo, tukiongeza ifike shilingi bilioni 900 halafu hatuna uwezo wa kuwa nazo haitusaidii. Mimi niombe shilingi bilioni 600 hizi ziende zote, wale ambao mmepangiwa miradi tutahama kwenda maeneo mengine. Pamoja na hayo,


tuuongeze huu mfuko wa shilingi 50 kwa kila lita ya mafuta ifike shilingi 100 ili usaidie kuharakisha kutekeleza miradi hii. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, Tarafa ya Ndagalu na Tarafa ya Sanjo wana hali mbaya kama nilivyosema. Hawana mito, hawana mabwawa na bahati mbaya kabisa wanakwenda kuchota maji kilometa 58 wengine, wanaamka saa tisa za usiku. Nazungumza haya kwa sababu Mheshimiwa InjiniaLwenge ameshawahi kufanya kazi kule Mwanza na Magu anaijua vizuri, Ndugu Kalobelo anaijua vizuri Magu. Wanaamka saa tisa na unajua Wasukuma muda ule wa mapema baba mwenye mji anakaa kwenye kimunya anachunga ng’ombe kwa hiyo kuingia kulala ni saa saba, naye amechoka, anafika kwenye kitanda puu, akiamka saa tisa amuangalie mwenzake ili atafute mtoto hayupo yuko kwenye maji. (Kicheko/Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana tuwahurumie hawa wananchi, ni tatizo kubwa. Kwa hiyo, muone kwamba wazalishaji wakubwa wa uchumi ni akinamama, muda mwingi wanaumalizia kuchota maji kuliko kuzalisha. Niombe, kama tutaongeza Mfuko wa Maji, Tarafa za Ndagalu na Sanjo ziangaliwe kwa umakini wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna watu hapa bado wanabeza Serikali hii ya Awamu ya Tano na bado wanasema 2020 haitarudi. Nataka niwahakikishie kwamba Serikali hii inarudi kwa kishindo kifua mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya maneno yanathibitishwa na Biblia Takatifu. Wakorintho 10:23, inasema, vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vifaavyo. Ikaongeza, vitu vyote ni halali bali si vitu vyote vijengavyo. Vyama vyote ni halali lakini chama kinachoweza kujenga ni Serikali ya Chama cha Mapinduzi. Vyama vyote ni halali lakini chama ambacho kinaweza kuwa kizuri ni Chama cha Mapinduzi. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, mnazungumza kwamba mmemezwa demokrasia kwenda kuwaeleza watu mtaenda mkaeleze nini? Kama ni demokrasia, juzi MArehemu Mheshimiwa Dkt. Macha amefariki tukatarajia mtaleta mtu yuleyule (mlemavu), hamkuleta mlemavu, ninyi mna demokrasia gani?

Mlituletea hapa wagombea wawili tukasema waongezeni, mkaleta sita mkawanyima kura hata ninyi, hata Makamu Mwenyekiti mmemnyima kura, hao wote wangejiuzulu wakarudi CCM. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, msiseme kwamba hakuna demokrasia.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba watuvumilie kidogo, tuwe na uvumilivu wa kisiasa ili tuelewane kidogo, ninyi mmezungumza asubuhi hapa.

TAARIFA...

HE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza taarifa siikubali kwa sababu chama kina mamlaka ya kubadilisha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii Rais Dkt. Magufuli, kama ni upele umepata mkunaji sasa. Unajua ili uwe jemedari lazima upigane vita, huwezi kuwa jemedari bila kupigana vita. Rais Dkt. Magufuli amepigana vita ya ufisadi, rushwa, vyeti hewa na mambo mengi, kwa hiyo, amefanya kazi ambayo alikusudia.

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais Dkt. Magufuli wakati ....Yeye atafanya kazi, hatajali chama…

Wale ambao wanatoka vyama vya upinzani tutapata wapi Rais wa namna hii? Kwa hiyo, naomba niwaambie Wabunge wenzangu wajue kwamba dereva mliyenaye atawafikisha salama na CCM itashinda mwaka 2020. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga, muda wako umekwisha, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja lakini tuvumiliane kisiasa, tuwe na ngozi nene.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali kwa kazi nzuri inayofanya kuhakikisha kwamba inatatua kero za wananchi wake japo kwa muda ambao imejiwekea. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri wake na Makatibu Wakuu kwa namna ya pekee ambavyo wanajituma kwenda kuwaangalia wananchi huko vijijini wanavyotaabika na huduma hii ya maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wabunge wote hapa kila linapoulizwa swali la maji wanasimama nusu ya Bunge. Maana yake ni kwamba hakuna hitaji muhimu tofauti na maji kwa wananchi. Wananchi hawa wanapata taabu sana hasa wakati wa kiangazi. Mimi nimekwisha kusema hapa kwamba sisi tunayo maeneo ambayo wananchi wanapata shida lakini maji yako karibu. Kwa mfano, kijiji changu cha mwisho kule Mahaha, Tarafa ya Ndagalu ni kilometa 58 kutoka Ziwa Victoria, lakini mpaka leo tunazungumza hapa hakijaweza kupatiwa maji. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu nimeshampelekea andiko mara nyingi, nimeshazungumza naye lakini bado sijaona njia sahihi ya kuweza kutatua kero ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma sana kwenye kitabu hiki nimeona Tarafa ya Ndagalu yenye wakazi takribani 80,000 imetengewa shilingi milioni 100. Shilingi milioni 100 ni visima vitano tu vya maji ambavyo ni vijiji vitano. Hii tarafa ina vijiji 21, ni kubwa kama ilivyo Wilaya na Jimbo la Mheshimiwa Waziri. Ni tofauti sana, tunapozungumza hapa kuna majimbo na vijimbo, sisi tunayo majimbo na wengine mna vijimbo, mtuelewe tunapozungumza jambo hili. Tarafa moja tu inameza jimbo lako, lakini haina maji, lazima mtuelewe vizuri Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mimi niombe sana tusiwe tunalalamika hapa tusaidieni kutatua kero za maji. Tukitatua kero za maji ndipo tutakapokuza uchumi wa Watanzania, uchumi wa wananchi wetu kwa sababu akina mama ndiyo wazalishaji wakuu, lakini wanapoteza muda mwingi sana kuchota maji na wala hawaendi tena kuchangia shughuli za kiuchumi. Kwa hiyo, niombe sana tatizo hili lishughulikiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewahi kusema hapa kwamba asali ni tamu sana na kila mmoja anatamani kuinywa, lakini wako humu watu hawanywi asali lakini kila mmoja anakunywa maji.

Kwa hiyo, mimi niombe sasa pamoja na kwamba inaonekana katika makusanyo yetu hatuwezi kutosheleza miradi ya maji tuje na mpango. Kama tumekuwa na mpango wa kununua ndege, tumekuwa na mpango wa kujenga standard gauge, kwa nini tusije na mpango wa kumaliza tatizo la maji? Kama ni kukopa shilingi trilioni tatu tukaondokana na tatizo la maji kwa nini tusikope? Tuamue kama Taifa, tuamue kama nchi kwamba hivi tukimaliza tatizo la maji, tukasogeza huduma kwa wananchi tutakuwa tumepunguza mambo mengi sana. Magonjwa yote yanayowasumbua Watanzania wetu yanatokana na maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe sana Serikali hata kama siyo leo ndani ya miaka mitatu au mitano tuje na mpango wa kukopa tumalize tatizo la maji ili Wabunge waendelee kusemea mambo mengine ambayo yanaweza kusaidia. Jambo hili likifanikiwa kama ambavyo tumefanikiwa kununua ndege, kama ambavyo tumefanikiwa kujenga standard gauge, litaleta matumaini mapya kwa Watanzania. Kwa hiyo, nikuombe hili liendelee kusisitizwa na Serikali na iweze kuweka mpango muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapozungumza maji tunazungumzia uhai. Mji wa Kisesa wangu wa Kisesa, Jimbo la Magu ni mji mkubwa sana na nimesoma kwenye kitabu hiki nilitarajia kwamba nitaona mpango ndani ya miji ambayo inatekelezewa miradi ya maji lakini sijaona Mji huu wa Kisesa ukiwekewa maji. Kwa hiyo, niombe kama ambavyo tumeshaendelea kuzungumza na Waziri, kama ambavyo tumeshaendelea kuzungumza na Katibu Mkuu muone mipango ya miaka ijayo hasa mwaka kesho kuja na mpango madhubuti kuhakikisha kwamba maji katika Mji wa Kisesa yanapatiwa majibu. Kwa hiyo, niombe tu kwamba vijiji vyote hivi ni vizuri tukahakikisha kwamba tunaweka maji ya kutosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu skimu za umwagiliaji, ripoti inaonyesha tunazo skimu nyingi sana za umwagiliaji lakini ni skimu ambazo zinategemea hasa wakati huu wa masika ambazo zinakinga maji yale yanayotiririka kutokana na mvua nyingi, mvua zikikatika skimu hizi zinakauka. Ni vizuri tukaandaa skimu ambazo zitatumia mito isiyokauka, mabwawa yasiyokauka na ziwa ambalo haliwezi kukauka ili hizi skimu ziweze kuleta impact. Skimu zilizopo sasa hivi hazileti impact kwa sababu wananchi hawamwagilii wakati ambapo mvua haipo, zinasaidia tu wakati wa mvua.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niombe na hili Serikali iwe na mipango madhubuti ya kuweza kusaidia ili tuweze kukuza uchumi hasa uchumi wa kilimo ambao kila mmoja wetu unamgusa na mwananchi wa kawaida unamgusa. Badala ya kupumzika muda mwingi aweze kuendelea kulima mazao ambayo atatumia skimu hizi za umwagiliaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako maeneo hata tukizungumza leo tupeleke maji ya Ziwa Victoria hayatafika, yanahitaji mabwawa. Mabwawa haya yakichimbwa maeneo hayo ambayo ni kame zaidi yanaweza kusaidia sana katika umwagiliaji, unyweshaji wa mifugo lakini pia katika matumizi ya binadamu. Kwa hiyo, tunapozungumza mabwawa mtuelewe vizuri wale ambao tuko maeneo ambayo yana shida na maji. Kwa mfano, Bariadi, Kwimba na Maswa yote haya yana shida na ukame mkubwa sana ni vizuri tunapojenga hoja mtuelewe kwamba hawa watu wanahitaji kupata maji yanayostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nasikitika sana, kuna msemaji mmoja hapa amesema Serikali imefeli, juzi tu tarehe 1, yeye mwenyewe amempongeza Mheshimiwa Rais na Serikali yake kwamba Serikali ya Chama cha Mapinduzi haina ubaguzi wa chama chochote inapeleka maendeleo kwa kila jimbo. Leo amejifanya tena kuwa mnafiki, hawa watu ni vuguvugu. Hayuko baridi, hayuko vuguvugu, huyu anapaswa kutapikwa. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwakawa Fedha 2018/2018 – Wizara ya Kilimo
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na kesi ya miti, miti inalalamika inakatwa, tunamalizwa, tunamalizwa, mwisho wake ikakaa kikao ikabaini kwamba nani anatumaliza ni shoka. Baadae wakasema shoka hili nani analileta ni mpini. Mpini si ni sisi humu tuliomo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kuna tatizo Wabunge wanalalamika, wananchi wanalalamika pamba kuuzwa kwenye ushirika. Kwa hiyo, wananchi wamegundua wanaopeleka hili jambo kwenye ushirika ni akina nani, ni viongozi tuliowatuma kwa maana ya sisi Wabunge pamoja na Serikali. Maana yake ni nini? Badala ya kufika mahali tukaona kwamba tunapaswa kuwatetea wananchi lakini hatuwatetei. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushirika Wabunge wamelalamika wasikilizeni, viongozi wa ushirika waliochaguliwa si wale tuliokuwa tunawatarajia. Wahasibu waliochaguliwa ni wale waliotumia rushwa kupita. Maana yake ni nini? Maana yake wanakwenda kuwaibia wakulima pamoja na wanunuzi wa pamba, hili jambo halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikataba iliyoko kule ni ya kukopa wakulima kwamba washirika wakusanye pamba halafu ipelekwe kiwandani, baada ya kupimwa kiwandani ndipo mkulima alipwe, siku ngapi hizo? Kwa nini tuliweka soko huria? Tuliweka soko huria kwa sababu wananchi wetu waliteseka, hili jambo haliwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri tukaliangalia upya, wananchi wanalalamika sana na sisi ndiyo viongozi na sisi ndiyo watu wa kuwasemea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi niishauri sana Serikali kwamba tumechelewa kwa sababu washirika waliokwenda kuchaguliwa wamechaguliwa na bodi ya watu wachache, watu saba/kumi wale washirika wangeweza kuchaguliwa na mkutano wa hadhara tungepata watu wanaostahili. (Makofi)

Kwa hiyo, hili jambo tungelifanya mwakani halafu sasa tukaruhusu mfumo wa soko huria ukafanya kazi. Mtawapa shida ma-DC, mtawapa shida Wakuu wa Mikoa, hakuna kazi watakayokuwa wanaifanya bali kulinda tu wezi wa ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu katika mkokotoo wa soko ni kweli bei iko hivyo, lakini makato yameongezwa. Tunapokwenda kuulipa ushirika shilingi 45 halafu shilingi 33 inabaki kwenye AMCOS, shilingi 12 inakwenda ushirika (union), hivi tunawasaidia wakulima? Kwa nini hata hiyo shilingi 12 tusiiache kwenye kijiji? Kama kijiji kimeuza kilo 800,000 sawa na shilingi 9,600,000 hizo zitanunua madawati, zitajenga zahanati ili watu waone impact kweli hata ya kurudisha ushirika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nashauri, jambo hili tunalipeleka kwa kweli wananchi hawako tayari, wananchi hawa hatujawashirikisha, jambo hili limetoka juu halijashirikisha wananchi. Naomba tushauri tubaki na soko huria kama ilivyokuwa mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuzungumzia uwezo wa ushirika, kama kituo kitanunua kilo 40,000 kwa siku tunazungumza shilingi ngapi? Tunazungumza shilingi 44,000,000 kwenye kituo kimoja; je, fedha hizo zina ulinzi na ni vituo vingapi, tuna polisi wangapi wa kulinda fedha hizo? Tunapeleka maafa kwa wakulima na benki, hili jambo linapaswa litazamwe upya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini tuliingia kwenye soko huria? Tuliingia kwenye soko huria baada ya Vyama vya Ushirika kushindwa. Hivi vyama kama nilivyotangulia kusema mwanzo vimejigeuza kuwa vyama ambavyo hata Waziri Mkuu hukuhitaji hivyo, Waziri Mkuu ulihitaji AMCOS ziundwe kutokana na wakulima wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa washirika tunaokueleza Mheshimiwa Waziri Mkuu wengine, hawana hata shamba wala pamba, sasa mtu anakwenda kumnunulia mwingine ambaye hata zao hilo? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo msipoangalia Mheshimiwa Waziri na Serikali, wapo viongozi/watendaji wanashauri vibaya, wanataka ku-sabotage Serikali na hili litakuja litugharimu sisi kama wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia kwenye mkokotoo; kwenye mkokotoo ni sahihi lakini ile shilingi 100 ingepungua. Mwaka jana tulikuwa na shilingi 30 ya kuendeleza zao la pamba, inakuwaje tunaweka mara nne/tuna-double mara nne kwa nini tusiende kwenye shilingi 60? Hii shilingi 60 tumeijaribu tukaona haiwezi kulipa madeni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Serikali iliangalie hili, ione ili angalau tukokotoe vizuri tumuongeze mkulima ili angalu mkulima mwaka kesho aweze kulima vizuri kama ambavyo wameitikia mwaka huu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wanalalamika mahindi hapa, mahindi haya bila kuweka utaratibu mwaka huu yataoza. Ni vizuri Serikali ikafungua mipaka ikaachana na suala la vibali ili watu waweze kusafirisha nje ya nchi waweze kuuza haya mahindi na mahindi haya yakiuzwa ndio uchumi wenyewe unaozunguka… (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 - Wizara ya Mifugo na Uvuvi
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Kwanza naomba niliambie Bunge na Watanzania kwa ujumla kwamba kwa mujibu wa maandiko matakatifu, samaki hazijaweza kutosha Ziwa Victoria wala baharini. Kwa sababu Yesu alipokuwa akitembea kule Galilaya, aliwakuta akina Petro na ndugu zake wametupa jarife, wamechoka, wamekosa samaki, akawauliza, kwa nini mmechoka? Wakasema, tumekesha tunavuta, lakini hatujapata samaki. Akafanya miujiza yeye mwenyewe, ndipo wakavuta wakapata samaki. Kwa hiyo, kwa mujibu wa Biblia, samaki baharini, samaki ziwani hawajawahi kutosha. Hilo lazima Bunge lijue na Taifa kwa ujumla lijue. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi nzuri iliyokuwa imeanzishwa na Mheshimiwa Waziri ilikuwa ni nzuri sana kwa sababu uchafu ulikuwa umeshakithiri katika maziwa yetu. Tatizo ni moja tu kwamba badala ya kudhibiti uvuvi haramu, watu wanaonewa.

Mheshimiwa Naibu Spika, haiwezekani leo tunazungumza uvuvi haramu, mtu unamkuta ana sangara mmoja wa sentimita 52 au wa sentimita 86 ambaye amempata tu kwa sababu nyavu hizi zinanasa samaki yeyote bila kubagua wakati mwingine. Huyu samaki wa sentimita 86, ukimkuta naye mmoja, unamkamata, unamwambia uhujumu uchumi, faini yake shilingi milioni 10, faini yake ni shilingi milioni 20, unategemea kwamba tunawasaidia wavuvi? Hatuwasaidii hata siku moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, inaonekana Wizara hii haijapewa fedha za maendeleo miaka mingi, ndiyo maana sasa inatafuta fedha za faini ziwe fedha za maendeleo. Haiwezekani jambo hili brother, haiwezekani. Ni vizuri Serikali tukaiwezesha Wizara hii ikapata fedha za kutosha kuendesha Wizara yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea kusema kwamba ni Serikali hii ndiyo itakayomaliza uvuvi haramu, lakini siyo kwa staili hii. Kwanza wamefanya kazi kubwa. Wavuvi wale wakubwa sasa hivi hakuna anayevua haramu, yaliyobaki ni makokoro ambayo wameshindwa kuyadhibiti kwisha. Hata hivyo, najiuliza sana kwamba tukienda kwa style hii tutamaliza uvuvi haramu?

Mheshimiwa Naibu Spika, niungane na Mheshimiwa Dau kwamba ni muda muafaka wa kutoa elimu sasa kwa wavuvi ili tuwe na uvuvi endelevu. La sivyo, tutamaliza gharama bure. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi task force ambazo ziko kule zinaendesha operesheni, ofisi zao ni Guest House. Hivi hakuna Ofisi za Serikali? Majengo ya Wakuu wa Wilaya yana nini? Wao ofisi zao zimegeuka kuwa Guest House, ni sawa sawa? Watueleze! Kwa sababu hata Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama wa Wilaya hatambuliki na operesheni hizi, ni sawasawa?

Mheshimiwa Naibu Spika, halafu hata faini hizi wanakataa kuingiziwa benki, wanataka uwapelekee cash, wakati mwingine unalipa kwa M-Pesa, ni sahihi? Ushahidi tunao. Yawezekana Mheshimiwa Waziri na Katibu Mkuu hamjui, lakini Watendaji wenu wanaofanya operesheni kule wana-sabotage Serikali. Haiwezekani hii brother! Lazima tukubaliane kwamba operesheni hii siyo msaada sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti umefanyika TAFIRI na wavuvi, ripoti ipo ya madhara ya macho 26 na madhara ya macho 78. Kuna madhara gani? Mapendeklezo ambayo tunajua sisi ni kwamba macho 78 hayana madhara yoyote kwa uvuvi wa Ziwa Victoria. Tunawasitisha wavuvi wetu wa nchi hii, Kenya inavua macho 78, Uganda inavua macho 78, hivi tunawasaidia Watanzania? Yawezekana Mheshimiwa Waziri hajui vizuri, kazi yake inaweza kuharibiwa na watu wachache. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hizi nchi jirani tunaamini kwamba kuna sheria ambazo zinashabihiana: Je, tumeshindwa kuwa na sheria moja ambayo inaweza kuwezesha uvuvi endelevu kwa nchi zote hizi tatu ambazo tunatumia ziwa letu na bahari nyingine? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kiwanda cha Nyavu cha Arusha. Kiwanda hiki kilikuwa kinatengeza vyandarua, lakini kiwanda hiki kimegeuzwa kuwa kinatengeza nyavu. Wavuvi hawa wanasema, material yale ya vyandarua hayadumu kwenye maji kwa muda mrefu. Kwa hiyo, wanachukua miezi sita nyavu hizo zote zinaisha, tunawatia umaskini. Naomba wataalam wawashauri vizuri Mawaziri, ni material yapi yanayofaa kutengenezwa nyavu za kuvua katika Ziwa Victoria? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la mifugo. Mifugo inakamatwa kwenye hifadhi. Inapokamatwa inapelekwa Mahakamani, wafugaji wakishinda kesi, hawarudishiwi mifugo yao. Tunawasaidia? Kama Mahakama imesema mifugo hii irudishwe kwa wenyewe, hairudishwi tunawasaidia? Itafutwe njia ya kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, wengine mtu alikuwa amekamatiwa ng’ombe zake 260, anarudishiwa 76, wengine wamekufa. Ni sahihi? Tunataka wanapokamatwa ng’ombe wa wafugaji wetu, watunzwe, walishwe mpaka ambapo kesi itafikia muda wake wa mwisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala hili la ufugaji, kuna na viwanda. Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga ni kiwanda ambacho kiko eneo zuri na kubwa, lina uwezo kabisa la kufugwa ng’ombe na kuchakata ng’ombe, lakini kiwanda hiki kimesimama. Namwomba Mheshimiwa Waziri na Serikali kwa ujumla, ifanye mkakati wa haraka kuweza kufufua kiwanda hiki pamoja na kiwanda cha maziwa kilichopo Utegi na kiwanda cha ngozi kilichopo Mwanza ili kusaidia mazao haya ya mifugo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuniruhusu dakika moja, kuna mifugo inakamatwa inapotoka Minadani, wanataka ipakiliwe kwenye malori; ng’ombe watatu au wanne, hata mahali pa kupakia huko kwenye Minada ya Serikali hatujatengeneza. Tunawapiga faini bure hawa wafugaji. Hata wanapopeleka maeneo ya kwenda kupakilia, wamekaribia na gari wanaliona, ile task force. Wanawakamata wanawatoza faini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli hili namwomba sana Mheshimiwa Waziri hata kama alikuwa halijui, alifuatilie watamharibia sifa na heshima ambayo alikuwa ameanza nayo vizuri. (Makofi

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali Pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi na kwanza naomba niunge hoja mkono mapendekezo ya mpango ulioletwa kwetu pamoja na mapendekezo na ushauri wa Kamati ya Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili mpango tufanikiwe kiuchumi, tunahitaji mali ghafi inayozalishwa nchini. Kwenye kilimo ni vizuri tukatoa kipaumbele kwenye kilimo cha umwagiliaji, tunayo mabonde mengi wengine wapo kandokando na maziwa ni muhimu tukawekeza kipaumbele ili watu walime wakati wote, tunayo mifano ya wale ambao wanatumia irrigation scheme kwa mfano kule Magu tunaye Ngongoseke analima green house, ni green house nzuri ambayo imeajiri watu wengi, lakini ana uhakika na soko la biashara ya kwake. Lakini tunaye mwingine anitwa Vick Fish amewekeza vizuri, tunaye Mtemi Chenge hapa amewekeza vizuri kilimo cha umwagiliaji cha mpunga cha mfano. Kwa hiyo niombe sana Serikali tutoe kipaumbele kwenye uwekezaji wa kilimo cha umwagiliaji ili tuweze kuzalisha malighafi ambayo kimsingi itatumika viwandani ili kuhakikisha viwanda tulivyonavyo material yake yapo hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhitaji viwanda lakini wawekezaji wetu bado wanakumbwa na changamoto nyingi kwamfano exemption ya viwanda kwa maana ya mitambo pamoja na godowns wanapata shida sana hebu tuangalie tuweze kutoa exemption ili wananchi wetu waweze kujenga viwanda baadae kodi tu watalipa. Kwa mfano wawekezaji wa wazawa ndani hatuwapi tax holiday, tukiwapa tax holiday wanapata namna ya kujenga uwezo ili baadae waweze kuimarika na kuweza kutoa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niishauri sana Serikali yetu ambayo inahitaji kwa kweli uchumi wa viwanda, lakini ili tufikie kwenye uchumi mzuri na kuboresha mpango huu suala la Stiegler’s Gorge ni jambo muhimu sana kupewa fedha za kutosha ili tuweze kupata umeme tuweze kuendesha hii hivi viwanda pamoja na mambo mengine ambayo wananchi wanahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu ya barabara kwa sababu tunapozungumza uwekezaji wa viwanda lazima tusafirishe malighafi, lazima tusafirishe bidhaa, ni vizuri ikawekwa kipaumbele kama ambavyo kwenye hotuba yako umesema umeliwekea kipaumbele, cha muhimu ni fedha zipatikane ili utekelezaji uwepo haraka zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo miradi ambayo wananchi wameianzisha, miradi ya afya, miradi ya elimu.

Kuna maboma mengi Ilani ya Chama cha Mapinduzi inasema zahanati kila kijiji sisi tumejitahidi kuhamasisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wamejenga maboma ya kutosha. Kwenye mpango huu tuone namna ya kuweza kukamilisha tunapokuja kwenye bajeti tuweke fedha za kukamisha maboma haya ili wananchi waweze kupata huduma wanayoihitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe wataalam, wachumi wabobezi watueleza sisi Wabunge na watueleze wananchi hivi umaskini mnaupima kwa namna gani? Kwa sababu hapa asubuhi kila mmoja anazungumza uchumi, wabobevu wa uchumi mtueleze uchumi mnaupima kwa namna gani, kwa sababu unaweza leo wewe watu wasema wananchi hawana fedha mfukoni, unaweza ukawana na fedha mfukoni lakini huwezi kusafiri kwa sababu miundombinu haipo, huo ni uchumi; unaweza ukawa na fedha mfukoni lakini huduma ya afya ukakosa huo ni uchumi? Unaweza ukawa na fedha mfukoni ukakosa elimu nzuri huo ni uchumi? Leo vyuo vipo umaskini wa elimu watu hawana, mtueleze kwamba uchumi manaupima kwa namna gani kwa sababu nchi hii imepiga hatua sasa kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaona wananchi wake leo kule vijiji wanashindana kujenga nyumba nzuri huo sio uchumi? Wanashinda kusomesha huo sio uchumi? Wanashindana kuishi maisha bora huo sio uchumi? Tunaupima uchumi kwa namna gani, uchumi wa kukosa hela mfukoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wachumi wabobevu mueleze jambo hili mnaupimaje, kwa sababu tumeweza kuwa tunapata taabu, halafu mimi nashangaa sana ndio maana Mwenyenzi Mungu wakati anataka kuumba nchi, mbingu na dunia hakuumba kwanza mwanadamu, aliona akiumba mwanadamu atampa taabu kuumba mambo yote ambayo aliyafikiria kuyaumba. (Makofi)

Sasa mimi niwaombe na wale wote manao hangaikia Katiba, Katiba yetu haiwezi kuwa inajadiliwa na watu 600 na kama mtaamua Serikali kuleta Katiba wakae watu wachache wabobevu, wachache waweke mpango mzuri wa namna Katiba yetu sio watu 600 ndio maana nasema hivi Mungu alipotuumba wanadamu hapa Tanzania kwa awamu hii ni kama aliumba mapacha wanne. Akamuumba John Magufuli, akamuumba Samia, akamuumba Majaliwa, akamuumba na Dkt. Mpango. Yale mnayoyafanya ninyi watu wanne fanyeni hivyo hivyo, kwa sababu tukitaka watu wote tutoe mawazo yetu tutapotosha Taifa. Kwa hiyo niwaombe sana, tunapoleta mapendekezo ya mpango kazi yetu sisi Wabunge ni kushauri ili tuweze kuboresha mpango wenyewe. (Makofi)

Kwa hiyo, Serikali imefanya kazi kubwa na naendelea kuipongeza Serikali. Leo ukienda Dar es Salaam barabara zinajengwa kila mahali, ukienda Arusha barabara zinajengwa kila mahali, ukienda Mwanza barabara zinajengwa kila mahali, ukienda Mbeya barabara zinajengwa kila mahali, tunataka uchumi wa namna gani? Tunataka viongozi wa namna gani fanyeni kazi wala msikatishwe tamaa wananchi wapo bega kwa bega na ninyi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji nchi iliyotulia, tunahitaji vyombo vya ulinzi na usalama vilinde raia wake, unajua watu tunasema watu wanakufa, duniani kote watu wanakufa na hili jambo la kawaida, unajua tusifanye iwe hoja, kutekwa kwa ma-billionaires tusifanye iwe hoja, duniani kote watu watekwa. Ndio maana vyombo vyetu vya ulinzi wa Kangi Lugola linda raia wako. Hakuna mahali popote nchi hailindi raia wake, ndio maana hata Mwenyezi Mungu kule mbinguni analindwa na jeshi kubwa la malaika, kwa hiyo, lazima watu wote walindwe, tuimalishe lakini tuwape angalau namna ya majeshi yetu kadri ambavyo wanaulinda tuwaongezee uwezo wa kuweza kukabiliana na matatizo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.
Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2018 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kuhusu Usimamizi wa Matumizi ya Fedha za Umma katika Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2017
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, naomba niipongeze Kamati hii ya PAC ikiongozwa na Mama Kaboyoka kwa kadri ambavyo ilijikita kuchambua Taarifa Maalum za Ukaguzi. Maana kitabu hiki chote kina Taarifa Maalum za Ukaguzi. Kwa hiyo, naipongeza sana Kamati hii kwa sababu imefanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niweke wazi jambo hili kwamba watu wengi walihitaji kuingia kwenye Bunge, zaidi ya watu 5,000 tuliokuwa tunagombea nao kwenye Majimbo, lakini Mwenyezi Mungu aliweka kibali cha Waheshimiwa Wabunge 393 tu kuingia ndani ya Bunge hili. Kwa hiyo, sisi ni wateule yale ambayo tunapaswa kuyafanya kwa niaba ya wananchi lazima tuzingatie haki na ukweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nianzie hapo hapo ambapo wengi wanataka kujua na wananchi wanataka kujua kwamba kwa nini trilioni 1.5 ilileta kizaa zaa kwa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali. Wengi hapa wanapotosha ukweli na umma unapotoshwa lakini kwa sababu sisi Kamati ya PAC ni Kamati makini na ina maadili ilisubiri ripoti halisi ambayo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ameipitia akaileta kwetu. Kamati hii siyo ya twitter au instagram kwa hiyo tunataka tueleze kwa umma yale yaliyoonekana kwa CAG. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uhakiki wa CAG na bahati nzuri wanaopotosha tulikuwa nao ndani wakati Mheshimiwa Maida anauliza kwa CAG kwamba hebu tupe ufafanuzi wa shilingi trilioni 1.5 wapotoshaji tulikuwa nao ndani. Kwa mujibu wa Hansard Mkaguzi alisema hakuna hata shilingi iliyoliwa baada ya kufanya uhakiki, kwa hiyo, haya mambo ni ya upotoshaji. Ni vizuri tukajikita kueleza umma dosari na yale ambayo tunaweza kuishauri Serikali ili iweze kuyafanyia kazi. Kwa hiyo, uhakika ni kwamba shilingi trilioni moja haijaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa najiuliza sana, hivi nyakati hizi kwa Mheshimiwa Magufuli unaweza ukala shilingi trilioni moja kweli? Nilikuwa nashangaa, hivi hawamjui vizuri Mheshimiwa John, inaweza ikawa hawamjui Mheshimiwa John, lakini nataka kuwahakikishia kwamba sasa mali za Watanzania, miradi ya Watanzania inadhibitiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, misingi ya haki ilikuwa imeharibika na maandiko Matakatifu yanasema, misingi ya haki ikiharibika mwenye haki afanyeje? Kwa hiyo, yaweza kuwa wapotoshaji zamani walikuwa wenye haki lakini misingi ilipoharibika na wao waliharibika. Nataka kukuhakikishia kwamba misingi ya haki sasa inapangwa vizuri, inajegwa vizuri na Mheshimiwa Rais wetu mpendwa John Pombe Magufuli kwa hiyo mambo yatakwenda vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naenda kwenye kifungu cha 3.1 ambacho kinahusu NSSF. Tumethibitishiwa na Ukaguzi Maalum, Kamati imepitia kwa kina tumeuona ubadhirifu mkubwa ulikuwa ukifanywa na NSSF kwa kununua viwanja ambavyo havina tija vingine hata tu kuhamisha umiliki kutoka kwa yule aliyenunuliwa haijafanyika na viwanja vingine vimevamiwa. Kamati yetu imependekeza vizuri sana na mimi nataka kuongezea uzito tu na haya yote yalifanywa na wanaopotosha wengine walikuwa viongozi kwenye Kamati hizo leo wanakuja wanageuka. Naomba sasa nipendekeze mambo ili Serikali ya Awamu ya Tano iweze kuchukua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, NSSF kama Serikali haitaunda Kamati Maalum ya kuchunguza na kuchukua hatua stahiki tutatia hasara mashirika haya ambayo tumeyaunganisha kwa sasa. Kwa hiyo, tuombe Serikali…

T A A R I F A

MHE. GOODLUCK A. MLINGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga taarifa.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naipokea taarifa hii. (Makofi)

MHE. ESTER A. BULAYA: Taarifa.

TAARIFA

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, sipokei taarifa hiyo….

WABUNGE FULANI: Aaaaaa. (Kicheko)

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Kwa sababau aliyekuwa anaongea alikuwa mwingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba uovu na uozo uliofanywa na taasisi hii siyo wa kuvumiliwa. Kwa sababu inaonesha wazi kwamba kilikuwa ni kama kichaka cha upigaji...

MBUNGE FULANI: Kweli.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, ni lazima iundwe Kamati itakayoweza kushughulikia watu hawa. Hawa watu wakipatikana wakusanywe wote wapelekwe huko kizuizini ili kuleta heshima ya nchi. Watanzania wanategemea Mifuko hii ya Hifadhi ya Jamii inapoendesha shughuli zake ilete faida ili impact ile iweze kuwasaidia wanachama wake lakini ilionekana kwamba ni kama kikundi ambacho kinaunda, miradi yote haijafanyiwa upembuzi yakinifu, miradi yote imebuniwa na watu wachache sana. Kwa hiyo, niombe sana jambo hili kwa kweli Serikali isilifumbie macho kwa sababu CAG ametuletea na sisi Kamati tumetoa mapendekezo yetu hapa. Tunaomba iundwe Kamati kwa haraka sana ili kuipa nguvu Kamati kwa yale ambayo imeyapendekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunalo Shirika letu la Maendeleo (NDC) liliingia uwekezaji na Kampuni ya IETL na kuunda kampuni ya TANCOAL. Ukaguzi huu Maalum umebaini mapungufu mengi sana hasa ya kimkataba. Mikataba ambayo iliingiwa ni mibovu na haiwezi kuisaidia Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, unaingia mkataba ardhi na madini uliyonayo hayakuingizwa kwenye mtaji. Kwa hiyo, ardhi na madini hayo yamekwenda bure, share yetu ni fedha taslimu bila kuanzia kwanza ardhi tuliyonayo, hii ni mikataba mibovu sana. Kama ambavyo tumeeleza kwenye taarifa yetu ya Kamati lazima tuhakikishe kwamba ndani ya miezi sita tuna review ili mkataba mmoja baada ya mkataba mwingine irekebishwe ili kuleta faida kwa Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imekiukwa mikataba mingi sana. Kwa mfano, Kamati tumebaini kuna fedha nyingi zilikuwa zikilipwa bila kufuata mkataba jambo ambalo kwa kweli limeisababishia hasara Serikali. Kampuni hii haijawahi hata siku kuipa faida Serikali kwa kulipa gawio, kwa hiyo, kila siku inapata hasara.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini NDC kama wabia tumegundua kwenye Menejimenti kuna udhaifu mkubwa sana, kwa hiyo, Menejimenti ni ya upande ule mwingine na Bodi ya Wakurugenzi ipo inaangalia bila kuyaangalia haya makandokando ambayo yanaitia hasara Serikali. Kwa hiyo, pamoja na mambo hayo tuangalie kama kuna mapungufu kwenye Shirika letu la Maendeleo kwa maana ya Menejimenti ibadilishwe na wachukuliwe hatua za kutosha. Kwa sababu huwezi kuwa na Shirika la Maendeleo ambalo haliangalii mbele. Tunaingia uwekezaji ambao hauleti faida kwa nchi, haiwezekani. Kwa kweli hatuwezi kukubaliana na kuendelea na jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe sana yale ambayo Kamati imeyabaini, yale ambayo tumeyapendekeza kwa Serikali, Serikali ichukue hatua mara moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi, nilikuwa mbali sana nikiamini kwamba nitachangia mchana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa namna inavyoendesha nchi na kuwahudumia wananchi wake. Pia naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri Mkuu pamoja na Mawaziri na Makatibu Wakuu na wote ambao wanaomsaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi kubwa imefanyika kwa nchi hii ambayo wengi hawakuitarajia lakini ndani ya miaka minne tumeshuhudia mengi na nchi imepiga hatua hasa katika huduma za kijamii. Sina sababu ya kuzitaja kwa sababu kila mmoja wetu anafahamu jambo hili. Naomba niishukuru Serikali hapa karibuni imetoa fedha za kuezeka madarasa na kukamilisha madarasa yetu ya shule za sekondari lakini bado tunauhitaji wa maboma yale ya zahanati zetu pamoja na shule za msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nataka nizungumzie sehemu ndogo sana lakini ni kubwa kwa nchi hii hasa kwenye suala la wastaafu. Watumishi wetu wa Serikali wa kada mbalimbali; walimu, madaktari, wataalam wa ugani na kadhalika, wanaitumikia nchi hii kwa uadilifu mkubwa sana. Hakuna hata mmoja wetu hapa ambaye hajapita kwa mwalimu, daktari na manesi, hata kama hujatibiwa lakini mama yako alipita labour, hata kama hakwenda labour alihudhuria kliniki, kwa hiyo, watumishi hawa wanafanya kazi kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, tunasema kwamba walimu ni wito lakini hawa walimu wanaifanya kazi ya Yesu mwenyewe ya kufundisha wanadamu ili waweze kuelewa mambo yote hapa duniani. Huyu daktari na nesi tunasema hiyo kazi ni ya wito lakini hawa nao wanafanya kazi ya Mungu mwenyewe ya kurudisha uhai wa mwanadamu, kazi hizi ni nzito sana. Inapofika sasa wakati wa kustaafu, mafao yao hayaandaliwi kwa wakati. Wako watumishi wamestaafu wamemaliza zaidi ya miezi sita bila kulipwa mafao. Pia wakati huo wakiwa wanasubiri mafao hawalipwi nusu mshahara wao kwa miezi hiyo, tunawatesa sana watumishi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niiombe na kuishauri Wizara kwa sababu taarifa za mtumishi huwa zinafika Wizarani kabla ya miezi sita kustaafu, kwa nini mtumishi huyu asiandaliwe mafao yake kwa uharaka? Tunamfanya mtumishi huyu akiwa anasubiri mafao kwenda kukopa mikopo ambapo anaingia mikopo ya riba kubwa ya asilimia 100, anapokuja kupata mafao yake yanaishia kwenye riba, hatumtendei haki mtumishi huyu. Naishauri Wizara hii iweze kuandaa mapema iwezekanavyo mafao ya watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mtumishi huyu anapotumika miaka 35 anafikisha miaka 60 ya kustaafu kimsingi amechoka anahitaji kupata mafao yake kwa uharaka zaidi. Wakati akisubiri mafao yake, wakati mwingine anapokuja kulipwa yale malimbikizo yake ya nusu mshahara hayapati kwa wakati pia. Niiombe Serikali ya Awamu ya Tano kama ambavyo Mheshimiwa Rais alipoangalia Kikokotoo na kuwahurumia watumishi maskini wa nchi hii akarudisha asilimia zote zilizokuwepo na mafao yao yaendane na muda. Tunaimani mifuko hii wanakochangia watumishi orodha ipo tayari ni uvivu tu wa Wizara kupeleka majina yao ili waweze kupata mafao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii watumishi tunawategemea na watumishi hawa anapokwenda kupumzika anayo mengi ya kufanya. Kama hatutamtendea haki mtumishi mstaafu hatutakuwa tumewatendea haki Watanzania. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Hukubaliani na suala la wastaafu?

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni taarifa nampa Mheshimiwa Kiswaga.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Mwakajoka.

MHE. FRANK G. MWAKAJOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa Mheshimiwa Kiswaga na ikiwezekana arekebishe kauli tu yake kuhusiana na Kikokotoo, siyo Mheshimiwa Rais aliyewaonea huruma ni Mheshimiwa Ester Bulaya ndiye aliyepiga kelele sana kama Waziri Kivuli wa Kambi Rasmi ya Upinzani. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, sipokei taarifa hiyo kwa sababu haina kichwa wala miguu. Nataka niseme kwamba mwenye maamuzi na jambo lolote kwenye nchi hii ni Mheshimiwa Rais, ndiye aliyefanya uamuzi. Unaweza ukapiga kelele na kelele yako isisikilizwe kama hatuna kiongozi mwenye huruma. Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni kiongozi mwenye huruma anayehurumia wananchi wake. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, yako mambo mengi ambayo yanafanywa na Serikali. Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kumuweka Waziri anayeshughulikia Uwekezaji kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu. Hata hivyo, yako manung’uniko mengi ya wawekezaji hasa mtu anapotaka kuwekeza kiwanda, iko mifumo mbalimbali ambayo sisi Wabunge ama nchi tumeiweka mwekezaji apitie hatua hizo ili akafikie uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikuombe Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana ya Uwekezaji ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu angalia mifumo yote ambayo haileti tija, inamkwamisha mwekezaji ulete mapendekezo hapa tuweze kuweka utaratibu mzuri ambao utawasababisha wawekezaji wawekeze kwa urahisi zaidi la sivyo tutakuwa tunasema kwamba wawekezaji wanakwenda kuwekeza nchi nyingine. Tunayo mifano mingi hatuna sababu ya kutaja majina yao lakini watu wamekuja kutafuta uwekezaji hapa nchini lakini kwa bureaucracy za taasisi hizo wamekwenda kuwekeza nchi nyingine, Watanzania tunakosa ajira, fedha na kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba sana tuiangalie NEMC kwani haina watumishi wa kutosha kufika kila eneo ambalo mwekezaji anaomba kuwekeza kiwanda chake…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Asante sana Mheshimiwa Kiswaga.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, nilistahili nipate dakika 15 nilikuwa na mengi ya kuchangia lakini basi. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba hii. Moyo usio na shukrani hukausha mema mengi. Napenda kuwapongeza Mawaziri; Mheshimiwa Jafo, Mheshimiwa Mkuchika na Naibu Mawaziri, Makatibu Wakuu pamoja na Wakuu wa Taasisi wanazoziongoza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa jambo hili kwanza napongeza kwa sababu nimepata vituo viwili vya afya; na cha kwanza kiko hapa cha Kahangara kwenye mfano wa hotuba hii. Bado nina vituo vya afya vitatu; Kituo cha Afya cha Kabila pamoja na Kituo cha Afya cha Kisesa na Nyanguge. Vituo hivi ni muhimu sana, Serikali ione namna ya kuweza kunisaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati Mheshimiwa Mbatia anachangia hapa, ndiyo maana nimeanza na moyo usio na shukrani; Mheshimiwa Mbatia ameishukuru Serikali hii. Kama wapinzani wa nchi hii wangekuwa kama Mheshimiwa Mbatia, upinzani ungeweza kusaidia nchi. Kwa sababu michango aliyoitoa ni kwa maslahi ya Taifa hili. Mungu akubariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii inaendelea kuboresha huduma. Kwenye hospitali, ninajua mnaendelea kujenga hospitali mpya, lakini hata hospitali yangu ya Magu, Mheshimiwa Jafo ni shahidi amefika mara mbili, inahitaji ukarabati. Kwa sababu tumezungumza naye ninaamini jambo hili atalichukua kwa uzito wa pekee kwa sababu yeye ni shahidi amefika OPD, inaweza kuanguka wakati wowote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye barabara. Magu tuna kilometa za barabara 1,600. Kwenye bajeti hii tumepangiwa shilingi milioni 900, hazitoshi hata kidogo. Naiomba Serikali, kwa sababu TARURA inapokea asilimia 30 na TANROADS inapokea asilimia 70, wangalie namna ya kubadilisha sheria ili mradi TARURA ipate asilimia 50 na TANROADS ipate asilimia 50 ili barabara zetu za wilayani kule ziweze kutengenezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naendelea kumpongeza sana Chief wa TARURA ni msikivu. Ukimpigia simu wakati wowote anapokea, naye anazunguka kwenye barabara zote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna daraja pale Mahaha, Itubukiro kwako kule, tunaunganishwa na daraja, halipo. Ili kuunganisha mawasiliano ya kiuchumi ni vizuri waangalie TARURA namna yoyote ambayo wanaweza kutusaidia madaraja ili tuweze kuunganisha hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tuna barabara ya Magu – Isolo, kuanzia Kabila – Isolo na Isawida kule kutokea Itilima, pale tunatenganishwa na daraja. Magu tumelima mpaka kwenye mpaka wa Itilima na Itilima imelima mpaka kwenye mpaka wa Magu; TARURA ninakuomba utupatie daraja na tulikuja ofisini kwako na Mheshimiwa Njalu kuomba pale utupe daraja ili tuweze kuunganisha mawasiliano ya wilaya hizo mbili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Magu tumejenga maboma vijiji 21 ambayo yako tayari, zinahitajika fedha za kuweza kukamilisha na hili ni la ki-Ilani. Tulisema Ilani ya Chama cha Mapinduzi kila kijiji kiwe na zahanati, wananchi wameitikia, wamejenga, wanahitaji kusaidiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara hii kama ambavyo inafanya kazi, iangalie namna ya kutoa fedha kwa ajili ya maboma ya nchi hii ikiwemo Wilaya ya Magu ili tuweze kuwapa nguvu wananchi kwa kazi ambazo wamezifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mkanganyiko wa waraka. Waraka uliokuja unasisitiza nyaraka zilizopita, lakini Wakurugenzi wameshindwa kutafsiri waraka huu. Wamefuta per diem wamekwenda kusisitiza kwenye sitting pekee. Madiwani hawa ni viongozi, ndio wanaofanya kazi, ndio Wenyeviti wa Kamati za Maendeleo za Kata, ni vizuri tukawaona. Kwa sababu hawa huwa tunachagua nao siku moja, ni vizuri tukawapa maslahi yao ya kweli. Kuna Diwani anatoka kilometa 40, kuna Diwani anatoka kilometa 20; wao wameangalia tu pale mwisho kwamba kama kuna uwezekano wa kutolala wasilipwe per diem. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wewe ni Mbunge. Mbunge na Diwani kila kunapokucha asubuhi watu wanajaa ukiwa Jimboni au kwenye Kata yako. Ndiyo maana ikawekwa per diem ili Diwani atoke kwenye familia yake aende akalale Makao Makuu ili concentrate vikao vya Halmashauri. Kwa hiyo, perdiem hii wanapaswa walipwe Waheshimiwa Madiwani hawa. Madiwani hawa hakuna sherehe inayompita, hakuna kilio kinachompita na hakuna mgonjwa anayempita. Mimi nilikuwa Diwani na sasa ni Diwani kwa mujibu wa sheria kwa sababu ya Ubunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana TAMISEMI, Mheshimiwa Kandege uko hapo. Kandege andika hili, Kandege andika hili, mtafasiri waraka huu, ili Madiwani waweze kulipwa per diem yao. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga naona umepandisha? Mwite tu Mheshimiwa Kandege.

MHE. MUNGE FULANI: Aongezwe dakika huyu.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, niongeze kwa mamlaka uliyokuwanayo.

MWENYEKITI: Tumia basi lugha ya Kibunge, mwite Waziri Mheshimiwa Kandege.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Kandege. Mheshimiwa Kandege. (Makofi)

MBUNGE FULANI: Tena, rudia!

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Kandege, sikiliza hili na aandika ili mtafsiri waraka huu Madiwani waweze kulipwa perdiem. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sauti yangu ni ya msisitizo, nasisitiza tu, siyo kwamba, labda nafoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakwenda kwenye Service Levy. Hii Service Levy wakati inatungwa Sheria ya Serikali za Mitaa ilikuwa inalenga viwanda. Kwa mfano, kama kiwanda cha Tanga Cement kimezalisha simenti na inauzwa hapa Dodoma, Halmashauri ya Dodoma ina-claim madai yake ya Service Levy Tanga. Leo Tanga Cement kama hapa Dodoma ina tawi, inatozwa hapa, akinunua Dodoma hapa kupeleka Mvumi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Kiswaga.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa…

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, basi naunga mkono hoja. Kumbe dakika 15 ni muhimu sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia hotuba hii ya miundombinu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, naomba niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano kwa namna ambavyo inatekeleza miradi yake ya kimkakati. Nchi zote duniani zilizofanikiwa kiuchumi ni pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya reli, baharini kwa maana ya meli pamoja na anga. Hizo nchi zimefanikiwa sana kiuchumi duniani. Jambo hili limefanywa na Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Awamu ya Tano Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na barabara ya Magu – Bukwimba – Ngudu na Hungumalwa. Barabara hii imeelezwa asubuhi na kaka yangu, Mheshimiwa Ndassa hapa, ni barabara ambayo iko kwenye ilani, lakini inafungua uchumi kwa sababu inaunganisha barabara kuu mbili; barabara ya kutoka Mwanza – Shinyanga na barabara kutoka Mwanza – Musoma – Nairobi, kwa hiyo, barabara hii ni muhimu sana kiuchumi. Ni vizuri Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, Waziri, tunajua ni mchapakazi pamoja na Manaibu pamoja na mzee wa TANROADS, Engineer Mfugale. Mfugale kwetu maana yake huwezi kufa haraka, kwa hiyo, ndiyo maana Eng. Mfugale upo hapo, Rais alikuteua, tuone barabara hii unaiweka kwa sababu huwezi kufa haraka kwa maana ya Kisukuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo barabara ya Magu – Mahaha – Itubukilo – Bariadi, inaunganisha Mkoa wa Mwanza na Mkoa wa Simiyu. Pale katikati Itubukilo na Mahaha tunahitaji daraja. Ni vizuri sasa Mheshimiwa Waziri uone, hili nimekuwa nikiomba kila ninapochangia kila mwaka. Naomba sasa kwenye bajeti hii sasa tusaidie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye Daraja la Sukuma, daraja mmeshatangaza na mkandarasi ameshapatikana, tatizo kibali tu Daraja la Sukuma lianze kutengenezwa. Hii nadhani ni ile Sheia ya Msamaha wa VAT, inachelewesha sana kwa sababu documents za nchi nzima zinakwenda Wizarani kurundikana, inachukua muda mrefu sana kibali kwa ajili ya ujenzi kupatikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria hizi ambazo tunaziweka Waheshimiwa Wabunge, mimi nishauri tu zile ambazo zinakwamisha kufanya miradi yetu kwenda haraka ni vizuri zikaletwa tukazirekebisha. Kwa sababu hizi sheria zinataka mpaka miradi hii itangazwe kwenye GN na inachukua muda mrefu sana kutangazwa kwa sababu ni miradi ya nchi nzima. Hata linapotokea dharura mhusika hawezi kutangaza kazi iweze kutekelezwa, anachukua muda mrefu kwa sababu ya sheria ambazo tumeziweka, ni vizuri tukazirekebisha sheria hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna barabara ya Mwanangwa – Misasi – Kahama, usanifu tayari umeshafanyika, ni vizuri sasa zikatengwa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu. Pia tunayo barabara muhimu sana ya Nyakato – Igombe TX na barabara ya lami ambayo inatokea airport kuja Nyanguge - Kayenze, hizi ni za ring roads ambazo zinafungua Mji wa Mwanza kuondokana na misongamano ambao upo. Mheshimiwa Eng. Kamwelwe nakuangalia hapo huandiki, andika ili niweze kuona kweli uko serious na jambo hili. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa kweli unaendelea kubaki nyuma. Nimeona mmetenga fedha, ni vizuri sasa utekelezaji wake ukaanza, hasa jengo la abiria ili kuweza kuchukua abiria wengi kama ilivyotarajiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwenye hilihili, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe na mnaohusika na ndege, hebu wekeni ndege ya kutoka Dodoma - Mwanza, Mwanza – Dodoma, kuna Mikoa mitano ya Shinyanga, Geita, Mara, Simiyu, Mwanza yenyewe, watumishi tu wa Serikali wanaokuja Dodoma kila siku ni wengi sana, wanatumia magari, ni risky. Nawahakikishia mkiweka route hii mtapata abiria wengi sana, hata mara mbili tu kwa wiki. Tusaidie Mheshimiwa Eng. Kamwelwe, hili tumeshakwambia na tumeshalizungumza mara nyingi na Mheshimiwa Ndassa amezungumza hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe barabara tatu ambazo zipo kwenye Wilaya yetu ya Magu; barabara ya Kisamba – Sayaka – Salama – Bariadi inaunganisha Mkoa wa Simiyu, Wizara ichukue barabara hizi. Mheshimiwa Eng. Kamwelwe ulipoanza kazi kwenye Wizara hii nilikuomba tutembelee pale, nikuombe tena, kama utamaliza bajeti yako wakati wowote twende tuione barabara ya Kisamba – Sayaka – Salama – Bariadi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunayo barabara ya Kabila – Isawida ambayo inatoka kwa Mheshimiwa Ndassa, Maligisu na Kabila tuna junction sasa ya kwenda Isawida ambako ni Wilaya ya Itilima, Mkoa wa Simiyu. Hizi ni barabara muhimu sana za kutufungua kiuchumi katika mikoa hii miwili. Niombe Wizara izitilie maanani barabara hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye suala la mawasiliano, Naibu Waziri nimekueleza na nimekuandikia maeneo ambayo Wilaya ya Magu inapata taabu kwa mawasiliano katika Vijiji vya Mwamabanza, Salong’we, Sayaka, Ndagalu, Nobola, Mahaha, Kigangama pamoja na Bundiria. Hebu tusaidie minara hii angalau wananchi waweze kupata mawasiliano na kuingia kwenye uchumi kirahisi zaidi kwa sababu mawasiliano ya simu yanarahisisha ukuaji wa uchumi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo barabara ya kutoka Nyanguge kwenda border kwa maana ya Musoma, kule Musoma imetengenezwa mpaka Lamadi lakini kipande hiki cha kilometa 80 kutoka Nyanguge mpaka Lamadi ni barabara kama uko kwenye bumps, unaijua vizuri. Mheshimiwa Engineer Kamwelwe, hebu fanyeni utaratibu wa kuijenga upya barabara hii ili iweze kukamilishwa kama ambavyo Musoma mmeshakamilisha. Nikuombe sana jambo hili ni muhimu, pamoja na Daraja lenyewe la Simiyu, naamini upembuzi yakinifu umeshakamilika. Tunapata adha sana hasa wakati wa masika hakuna mahali popote pa kuweza kupita Mto Simiyu ukiwa umefurika. Hebu daraja hili lijengwe ili angalau watu wa Musoma na Mwanza wasipate adha yoyote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja na nakushukuru sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara
MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hoja iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa naomba niipongeze Serikali kwa namna ambavyo inaendelea na jitihada zake za kuhakikisha kwamba wawekezaji kwenye nchi hii wanapatikana. Japo zipo kasoro ndogondogo ambazo tunapaswa sisi Wabunge tushauri na tusikilizwe na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamwona Mheshimiwa Rais anapokuwa na mahangaiko makubwa sana moyoni mwake, kadri ambavyo anachukizwa na mwenendo ambao unazuia uwekezaji wa haraka kwenye nchi hii kwenye viwanda vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na viwanda vingi ambavyo tulivibinafsisha, ningeshauri Serikali iweze kuvipitia upya tuone kama vinafanya vizuri kazi iliyokusudiwa. Kwa sababu inaonekana kuna viwanda vingi havifanyi vizuri na viwanda hivi kama vikifanya vizuri tutaondoa kabisa tatizo kubwa la ajira lililoko nchini mwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, viwanda ambavyo vilikuwa vikileta uchumi kwa nchi hii, bado havijatazamwa vizuri. Tulikuwa na Kiwanda cha Zana za Kilimo kule Mbeya, tulikuwa na viwanda vya nguo mpaka leo havifanyi vizuri, tulikuwa na viwanda vya kapeti, vimeshakufa, tulikuwa na viwanda vya kutengeneza vifaa vya umeme nchini, vimeshakufa. Namshauri sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, aweze kuvipitia upya viwanda hivi ili tuweze kuona kama vinaweza kuendelea kuzalisha kama vilivyokuwa vinazalisha zamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapowekeza kwenye viwanda, tunaongeza ajira kubwa, tukiongeza ajira, watumishi wale wanalipa kodi, kwa maana ya PAYE, SDL pamoja na WCF. Kwa hiyo, huo ni mkusanyiko mkubwa ambao unaweza kuchochoe uchumi kwenye nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ziko kasoro nyingi ambazo wawekezaji wanazipata kupitia taasisi zetu nyingi ambazo wengine jana walichangia, ziko taasisi kwenye viwanda na uwekezaji wa jumla karibu 27 na kuendelea. Tungeshauri, taasisi hizi za Serikali ziunganishwe ziwe mlango mmoja, zipunguze bureaucracy ili wawekezaji waweze kuwekeza kwa haraka zaidi. Bila hivyo, tutakuwa tunaimba wimbo uleule bila mabadiliko kwenye nchi hii. Niishauri sana Serikali isikilize ushauri wa Wabunge wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende pia kwenye service levy. Wakati sheria hii ya service levy inatungwa ilikuwa imejielekeza kwenye viwanda, wala haikujielekeza kwenye maduka ya jumla ya rejareja lakini leo biashara hizi zinakufa kwa sababu ya kutoangalia upana wa sheria hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati wanatunga sheria hii, kwa mfano, Breweries, ikiwa pale Mwanza Ilemela, distributer wa Shinyanga, Geita, Singida na Tabora, akiuza bia yake watu wa Tabora, Singida, Shinyanga wana-claim madai yake Breweries Ilemela. Leo distributer wa Ilemela na Shinyanga, ukichukua bia pale kwa distributer wa Ilemela, ukapeleka Misungwi, unadaiwa service levy, hata yule mwenye bar ya kawaida naye anadaiwa service levy. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, mwenye biashara kwa mfano mfuko wa sukari, gharama yake ni shilingi 108,000, faida yake ni Sh.500, akitozwa service levy ni shilingi 324. Kwa hiyo, anabakiza kama shilingi 170. Service levy inatozwa kwa mauzo, mfanyabishara hawezi ku-declare kodi yote kwa sababu inachukua gharama kubwa kuliko ingetozwa kwa faida. Kwa nini tusibadilishe sharia ya service levy tukatoza kwa faida, tukiwa tumeondoa gharama za uendeshaji kama ambavyo tunatozo corporate tax. Tukifanya hivyo, tutawaondolea adha wafanyabiashara hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Waziri wa Viwanda na Biashara, naomba ukae na wafanyabiashara, kama ambavyo Waziri Mkuu alikaa na wafanyabiashara kule Kariakoo, alibaini mambo mengi. Niombe pia Mawaziri mnaohusika, Rais alipokaa na wafanyabiashara na wachimbaji wa madini akaleta mapendekezo ya sheria hapa, leo tunaona ambavyo madini yetu yanalipa zaidi ya kile kilichokuwa kinalipwa, wakwepaji kodi wanaondoka.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapokaa na wafanyabiashara, wana manung’uniko mengi ambayo kwa kweli tukiwasikiliza na kuleta hapa marekebisho ya sheria, tunaweza kusaidia biashara nchini. La sivyo, hatutakuwa tumesaidia biashara nchini, tukiendelea kuwa na kodi nyingi ambazo hazina faida. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama inashindikana service levy kutozwa kwa faida, basi ipungue iwe 0.1% badala ya 0.3%. Kwa sababu hata benki wamepewa waraka na Katibu Mkuu, Wizara ya TAMISEMI, wawe wanachajiwa 0.1%, kwa nini wafanyabishara wengine nao wasipate huo mwanya wa kuweza kutozwa kwa asilimia hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, OSHA ina msaada gani kwa biashara? Tulikuwa tunajua OSHA inasimamia usalama wa watumishi kazini lakini leo wamekuwa watozaji wa kodi, watu wenye viwanda, petrol station na hoteli, wanalalamika, kwa sababu badala ya tozo zile zingine za kawaida (WCF) ambapo ni mchango ambao unasaidia wakati mtumishi anapata tatizo, labda la ajali kama fidia wanatoza kwa mwaka, kati ya milioni moja mpaka milioni tano, wafanyabiashara hawa wanalalamika sana. Tuangalie tozo ambazo haziwezi kusaidia kwenda mbele…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, muda wako umekwisha, ahsante sana.

MHE. KISWAGA B. DESTERY: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa kwa Miaka Mitano (2021/2022 – 2025/2026) na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2021/2022 pamoja na Mapendekezo ya Muongozo wa Maandalizi ya Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/2022
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili nami niweze kuchangia Mpango wa Mwaka Mmoja na Mpango wa Miaka Mitano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Fedha kwa namna ambavyo amewasilisha mafanikio ambayo yamefikiwa kwa miaka mitano iliyopita na matarajio ya miaka mitano ijayo. Inatupa faraja kwamba nchi hii tutasonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu Nyerere huko nyuma alitangaza Kilimo cha Kufa na Kupona, wengine sasa wamekuja na slogan nyingi. Kusema ukweli wananchi wengi walioko vijijini wanahusika na kilimo, lakini kilimo chetu hiki ni cha kutegemea mvua wakati Mungu ametupa ardhi yenye maji chini. Ni vizuri Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo zikaja na mpango wa kila eneo kuliko na shamba tuchimbe visima virefu, tusafishe maji, tusukume, tutengeneze miundombinu ya umwagiliaji ili wakulima wetu waweze kulima kwa awamu karibu tatu kwa mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vizuri sana wakulima kulima miezi minne wanapumzika miezi nane, kibiashara haikubaliki. Mfanyabiashara halisi hupenda kufanya biashara kila siku bila kupumzika. Tumpeleke mkulima wetu afanye biashara, kwa sababu kilimo ni biashara, ndipo tutafikia kipato cha juu kwa kila mwananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hayo ni mawazo ambayo yanapaswa yaanze sasa. Kwa sababu tumezungumza sana miaka mingi, Bunge hili litaisha, Bunge lijalo litaisha na mengine. Ni vizuri mipango hii ikaanza kutekelezwa kwenye uongozi wako, tukaacha legacy kwenye kilimo cha wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani kote ili Mpango wa Maendeleo ufanikiwe, ni lazima wananchi na viongozi wake wawe tayari. Kwa nchi yetu ya Tanzania viongozi wako tayari na wananchi wako tayari kwa sababu wakati wote wanawajibika kikamilifu, kwa hiyo, ni mambo tu ambayo tunatakiwa tufanye. Tulipokuwa tunaandaa mazao matano ya kimkakati, ni vizuri tukaandaa na viwanda vya kimkakati ili kuhakikisha kwamba tunakuza uchumi wa kilimo na kukuza ajira kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie suala la pamba. Kulikuwa na Mpango wa C2C (Cotton to Clothes). Mpango huu hauwezi kufanikiwa kama Serikali haitaamua yenyewe kuwezesha sekta binafsi kama dunia ilivyoweza kuwezesha sekta binafsi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, unapotaka kutengeneza kiwanda cha majora, yaani vitambaa vya aina mbalimbali kama kitambaa cha suti, kitenge, kanga, jeans, t-shirt au shati, unahitaji uwekezaji usiopungua Dola milioni 100, kwa sekta binafsi haiwezekani. Dola milioni 100 tunazungumzia shilingi bilioni 230, benki zinaweza ku-collapse.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zilizoendelea ziliwezesha sekta binafsi. Ukienda Bangladesh, pamba yetu ya Tanzania inaliwa na kiwanda kimoja tu. Kweli tunavyo viwanda vidogo vidogo hivyo vya nyuzi, vitambaa, haviwezi kumaliza raw material tuliyonayo hapa. Kwa hiyo, ili tukuze uchumi ni lazima Serikali iweke guarantee kwa sekta binafsi ziweze kukopesheka duniani ili tuweze kuwekeza na tutoe majora ya aina mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukitoa majora, kwanza tutakuwa na uhakika wa bei halisi ya pamba. Kwa sababu mnyonyoro wa thamani tutaujenga vizuri ili kuhakikisha kwamba mkulima huyu ananufaika. Ndipo tutakapokwenda sasa kwenye viwanda vya nguo ambavyo vilikuwa vinazungumzwa hapa na wenzangu, kwamba mtu mwenye cherehani tano au nne, hivyo ni viwanda. Ukienda Vietnam, kila familia ina kiwanda nyumbani kwake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lazima tubadilishe mawazo yetu, NEMC ije na mawazo chanya. Kwa sababu hapa kwetu ukitaka kuweka kiwanda kwenye nyumba yako unaambiwa unaharibu mazingira. Ukienda China unakuta familia moja, chumba kimoja inatengeneza mabegi; familia moja chumba kimoja inatengeneza simu; ndipo sasa utaweza kwenda kwenye viwanda vikubwa. Huwezi kuanzia juu ukaja chini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali yetu iweke guarantee kwa wale walio tayari, kama sivyo, Serikali tu- sacrifice, shilingi bilioni 230 ni nini, tuipe Jeshi lijenge kiwanda kikubwa, wafungwa waendeshe kiwanda, watoto wa JKT waendeshe kiwanda, tutafikia uchumi ambao tunautarajia. Kama hatutafanya hivyo, tutakuwa tunazungumza pamba ambayo haitusaidii sana, tunaagiza nguo kutoka nje na pamba tunayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali, lazima iamue, tunajenga madaraja na barabara…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga nilitaka kukukumbusha tu kwamba sasa huo ndiyo uchangiaji wa Mpango. Ile habari ya barabara ya kutoka mahali fulani kwenda kwenye kijiji changu, hiyo subirini wakati wa bajeti. Sasa hivi tueleze Mpango, ili mpango huu ukatuletee hela Serikalini, Serikali iwe na fedha halafu sasa ndiyo tutaongea habari ya barabara yako ya kata moja hadi nyingine. Kama unavyotueleza kwamba tukiwekeza kwenye pamba tunaweza tukatoka. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Kiswaga, endelea. (Makofi)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunajenga barabara, madaraja, stendi na masoko kadhaa, kwa nini Serikali isiamue kutoa shilingi bilioni 230 ikakabidhi hata Jeshi kama sekta binafsi haiaminiki, hapo sisi tutakuwa soko la Afrika kwa vitambaa na tutamaliza matatizo mengi. Wale wakija kununua vitambaa, watalala hoteli, kuna kodi ya Serikali; watakunywa bia, kuna kodi ya Serikali; watatumia taxi, watatumia mafuta, kuna kodi ya Serikali; wenye taxi watanunua tairi, kuna kodi ya Serikali. Kwa hiyo, tusiangalie tu jambo moja tukashindwa kuangalia kwa upana wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wowote wa Maendeleo duniani huhitaji kuongeza ajira, kukusanya kodi na kuweka mifumo mizuri ya kuhakikisha mpango ule unatekelezeka. Kuna wakati taasisi zetu wakati mwingine zinaweka mipango ambayo haitekelezeki na kandamizi. Mfano, wenye mabasi; kuna kitu kinaitwa LATRA, wameingizwa kukata tiketi kwa mfumo, ambapo kimsingi wanalazimishwa kuweka fedha kwenye mashine. Kama una magari 40 lazima asubuhi uweke milioni 60.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao wafanyabiashara wetu wa mabasi wana uwezo, kwanza basi wanakopeshwa, halafu unapoweka huo utaratibu, maana yake kuna 2% wanakatwa hawa wafanyabiashara. Hiyo pia, hakuna mkataba wowote ambao unawafanya wafanyabiashara hawa wawe na imani kwamba fedha hizi zikikatwa kwa mtandao zitarudi au zitaenda Benki?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Mheshimiwa ni kengele ya pili.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti…

MWENYEKITI: Ni hoja muhimu lakini muda wako umekwisha.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wapewe EFD machine wafanye kama ambavyo wafanyabiashara wengine wanafanya bila kupitia utaratibu huo. Hapa tutaongeza ajira, Mama Ntilie watapika chakula, wapiga debe nao watafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na naunga mkono hoja. Tutachangia kwenye Mipango mingine. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga, huja-declare interest, una mabasi mangapi? (Kicheko)

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sina basi ila kwenye pamba.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia. Kwanza naomba nimpongeze Waziri wa TAMISEMI na Manaibu wake, pia Katibu Mkuu na Manaibu wake wa Afya na Elimu. Sisi Wabunge wote humu tunalia na TARURA. Tusikilize ushauri wa Waheshimiwa Wabunge, kwa sababu ili uchumi wa viwanda uendelee tunahitaji barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunazo barabara nyingi ambazo ni muhimu kwa kusafirisha mazao ya wakulima na tunapoangalia uchumi, tunawaangalia hasa wakulima ambao wanaweza kusafirisha mazao yao. Kwa hiyo, naomba sana TARURA iongezewe fedha na michango ya Wabunge inayozungumzwa kuongeza tozo kwenye simu, hilo lisikilizwe. Hatuna ubabaishaji kwa sababu hatuhitaji kukaa miaka 40 bila kujenga barabara zetu. Tunahitaji kukaa miaka mitano tumalize barabara zote za wananchi ili uchumi uweze kukua.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tuongeze tozo kwa sababu wanaosafiri ni hao hao wananchi, wanaotaka maendeleo ni hao hao wananchi. Kwa hiyo, tuongeze tozo kwenye mafuta pamoja na mitandao ili kuhakikisha kwamba barabara zetu zinajengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninayo barabara muhimu sana ya Isolo, Kabila Isawida ambayo inahudumia Wilaya ya Itilima pamoja na Magu. Ninayo barabara ya Kisamba - Sayaka ambayo inahudumia barabara ya Wilaya ya Busega pamoja na Magu. Ninayo barabara ya Mwamanga kisasa ‘B’ ambayo nayo kwa kweli ni barabara muhimu sana katika uchumi wa Wilaya ya Magu.

Mheshimiwa Spika, kulikuwa na ahadi ya Mheshimiwa Rais Hayati Dkt. Magufuli ya kuboresha barabara ya Bujora - Kisesa kwenye makumbusho ya Wasukuma, imejengwa kilometa 400 bado kilometa 1.3. Naomba iingizwe kwenye barabara ambazo zitawekewa lami katika miji hii midogo midogo. Pia tunapoboresha miji na majiji tukumbuke pia kwenye Halmashauri zetu, nasi tunahitaji kuwekewa barabara za lami kwenye Wilaya zetu ili angalau wananchi waweze kupata huduma za kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye Afya tumefanya kazi kubwa sana, lakini wenye umri wa kwangu miaka 47, ni muhimu sasa nikapatiwa fedha ili tuweze kuikarabati hospitali hiyo na yenye ionekane kwamba ni hospitali ya kisasa. Pia kuna ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kugawa Wilaya ya Magu pamoja na Wilaya ya Misungwi na Nyamagana kidogo kuwa Wilaya mpya ya Kisesa. Hii Wilaya nayo inategemewa ianze ili kusogeza huduma kwa wananchi wetu. Tumejenga vituo vya afya, kinachohitajika sasa ni vifaa; X-Ray pamoja na cold room katika Kituo cha Afya cha Tangala pamoja na Kabila na Lugeye ili kuhakikisha kwamba vinatoa huduma iliyo nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi wa P4R wa kujenga madarasa umeleta matumaini makubwa sana kwa Watanzania, umepunguza uhaba wa madarasa katika shule zetu. Ushauri wangu ni kwamba, fedha hizi kama itawezekana, kwa sababu kuna maboma ya wananchi, kwa sababu fedha hizi zinapokuja, kwanza zinakwenda kujenga maboma mapya. Kwa sababu tuna maboma ya wananchi ambayo yameshajengwa tayari, fedha hizi ziwe zinamalizia. Sikija shilingi milioni 20 zimalizie maboma mawili, tunakuwa na madarasa mawili badala ya kujenga darasa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninalo jengo la Halmashauri. Mwaka huu wa fedha tuliomalizia lilitengewa shilingi milioni 750, tumeletewa shilingi milioni 136, ni vizuri fedha ambazo zimebaki ziletwe ili tuweze kuendeleza ujenzi ule. Bajeti ya mwaka huu umetutengea shilingi bilioni moja.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga, muda washilaga.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Ahaa!

SPIKA: Mmh!

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mhesimiwa Spika, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja nikiamini kwamba Wizara hii Waziri na Makatibu Wakuu na Watendaji wadogo wadogo kama akina Ntuli na akina Cheyo wanafanya kazi. Ni Wizara barabara, itakwenda bam bam.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maji
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Wizara hii muhimu ya maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, naomba kwa namna ya pekee nimpongeze na kumshukuru Waziri wa Maji, ndugu yangu Mheshimiwa Awesso ambavyo anajitahidi sana kuhangaikia kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maji katika nchi hii pamoja na Naibu wake na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, ndugu yangu Sanga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ambavyo wenzangu wamesema hapa, kwa kweli maji ni uhai na hakuna kitu kingine ambacho kila mwanadamu anakitumia kama siyo maji. Kuna vitu vingi vizuri, vitamu duniani lakini wanadamu hawavitumii, lakini kila mmoja anatumia maji. Kwa hiyo, tutakapokwenda kuhakikisha kwamba tunatoa huduma za maji kwenye vijiji vyetu, tutahakikisha kwamba wananchi sasa tunawajengea uchumi ambao wanastahili kuwa nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moyo usiokuwa na shukrani hukausha mema mengi. Kwa hiyo, napenda kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kutuletea mradi wa maji mkubwa katika mji wetu mkubwa wa Magu. Kwa hiyo, Mji wa Magu umepata maji, lakini maji yale ni mengi mno ambayo yanastahili kuhudumia vijiji 32 vyenye takribani wakazi 180,000. Maombi haya tumeshayaleta ili angalau haya maji yaweze kuwafikia wananchi wa Jimbo la Magu. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, katika vijiji hivyo 32, kuna Kijiji cha Mahaha ambacho kina wakazi wengi sana; Shishan, Isolo, Kabale pamoja na vijiji vingine; Kungulu, Ndagalu, Salama, Mobulenga, Nyashoshi, Kuhumbi, Misungwi, Sagani, Mwalina, Mwamabanza, Watelesha, Mwamibanga, Iseni, Bugabu, Chandulu, Vijinjibili pamoja na Nyahanga. Ni vijiji 32 vyenye wakazi 182,000. Vijiji hivi vikipata maji tutakuwa tumewakomboa sana wananchi wa vijiji hivyo na hasa akina mama ambao wanaamka usiku wa manane kwenda kuchota maji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unajua wazalishaji wengi wa uchumi kule vijijini ni akina mama, lakini muda wote wanaumaliza kutafuta maji. Anaamka saa nane anakwenda kwenye maji, anarudi saa tano, hana muda hata wa kwenda kwenye mashamba kwa ajili ya kuzalisha kwenye kilimo. Kwa hiyo, naiomba sana Wizara ya Maji, kwa sababu Mheshimiwa Awesso ameshafika Magu pamoja na Sanga, waone namna ambavyo wanaweza kutusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mradi huu kulikuwa na upungufu wa kilometa 24 katika Mji wa Magu pale na ninaamini Rais wetu mpendwa, hivi karibuni atakuja kuufungua huu mradi wa maji. Sasa hizo kilometa 24 zilikuwa zinahitaji shilingi milioni 260. Wakati huo Awesso akiwa Naibu Waziri na Sanga akiwa Naibu Katibu Mkuu, wote wamepandishwa kuwa Waziri na Katibu Mkuu, hebu mwelekeze shilingi milioni 260 ili kilometa 24 katika Mji wa Magu wananchi waweze kupatiwa maji. Kwa sababu, akija kufungua Rais, halafu wananchi wakanyoosha mabango, sasa sijui atafukuzwa Mkurugenzi au DC au atafukuzwa Waziri au Katibu Mkuu? Nami nataka Waziri na Katibu Mkuu mwendelee kuwepo kwenye Wizara hii. Hebu angalieni namna ambavyo mnaweza kusaidia ili wananchi wasiinue mabango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna Mji wa Kisesa pale ambao chanzo chake ni Butimba. Chanzo hiki ni cha muda mrefu na tayari mkandarasi ameshapitishwa. Tatizo kubwa ni exemption ili aweze kutoa vifaa vyake bandarini. Hebu tuliangalie suala hili la exemption kwa sababu ni suala ambalo linakwamisha sana kuendeleza miradi ambayo iko tayari na fedha ziko tayari. Mradi huu utahudumia katika Mji wote wa Rwanyima, Nyamagana kwa ujumla, Buswelu pamoja na Kisesa, Usagara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba sana kwa sababu mradi huu ndiyo utakaokwenda kutatua changamoto nyingi katika Mji wa Kisesa ukiwa na Kata ya Bujola, ukiwa na Kata ya Bukandwe, ukiwa na Kata ya Bujashi. Kwa hiyo, haya ni maeneo muhimu sana ya kiuchumi na tunaamini kwamba maji yakifika na kwa sababu Mheshimiwa Hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitaja Kisesa kwamba iwe Makao Makuu ya Wilaya mpya ya Kisesa, kwa hiyo, maji haya ni muhimu sana, yanasubiriwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, haya ni maeneo muhimu sana ya kiuchumi. Tunaamini kwamba maji yakifika, kwa sababu hayati Rais Dkt. John Pombe Magufuli alitaja Kisesa kwamba iwe Makao Makuu ya Wilaya Mpya ya Kisesa. Kwa hiyo, maji haya ni muhimu sana, yanasubiriwa na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulikuwa na miradi inayozunguka Ziwa Viktoria vijiji 16. Wataalam wa Wizara ya Maji walifika na tayari upembuzi yakinifu umekwishafanyika. Tulikuwa na matarajio kwamba mradi huu ungekuwa umeanza bajeti hii ya fedha tunayoendelea nayo, lakini mradi huu haujaanza. Vijiji hivi viko kabisa kwenye maeneo ambayo Ziwa Victoria linapita pale. Vijiji hivi ni Shinembo, Bundilya, Nyamhanga, Inolelo, Mwamanga, Kigangama, Lutale, Kayenze, Kageye, Itandula, Rangi, Matale, Ihushi, Sese na Busekwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati Mheshimiwa Waziri anakuja ku-wind up hapa atueleze kwa sababu ni ahadi ya wananchi kwamba tutakwenda kutatua kero za maji na kumaliza kabisa ili wananchi waweze kupata huduma ya maji safi ili angalau wananchi wawe na matumaini ya kutosha kwa Serikali yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, niunge mkono hoja kwa sababu namwamini Waziri pamoja na Naibu na Katibu Mkuu Wizara ya Maji. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hotuba ya bajeti ya miundombinu. Kuna lugha pale mbele nilitoa, nilikosea kidogo ni ulimi tu nadhani itafutwa kwenye Hansard siwezi kuchongea wizara hii kubwa na muhimu kwa Taifa letu. Najua sisi Kiswahili tulikijua shuleni hatukukijua kabisa nyumbani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nimpongeze Waziri na Naibu Waziri wa Uchukuzi kwa sababu tunajua kwamba kabla ya kuwa Waziri alikuwa alikuwa Katibu Mkuu kwenye Wizara hii, miradi yote ambayo ameisimamia ni miradi ya kielekezo. Kwa hiyo, tunaamini kwamba kwenye bajeti yake kadri alivyojipanga atafanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia tumpongeze Katibu Mkuu na yeye tunajua kwamba yuko vizuri katika wizara hii na atafanya kazi vizuri sana. Pamoja na wasaidizi wao anayesimamia reli Bwana Kadogosa, anayesimamia bandari Bwana Erick, anayesimamia TEMESA Bwana Masele, anayesimamia ndege Bwana Majingi na anayesimamia Ndugu yangu Mfugale naye yupo vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, uchumi wowote duniani ili ukue unategemea miundombinu, miundombinu ya reli, miundombinu ya barabara, miundombinu ya ndege na meli. Kwa hiyo, ujenzi wa reli ya Standard Gauge ulivyoanza Dar es Salaam na Morogoro – Makutupora na sasa Mwanza – Isaka kuna ulazima wa haraka sana kuanza ujenzi wa reli kutoka Makutupora – Tabora na Tabora - Isaka ili kuhakikisha kwamba vipande hivi vinakuwa na maana ya kuleta uchumi kwenye taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu tutakapokamilisha kutoka Dar es Salaam mpaka Makutupora, tukikamilisha Mwanza – Isaka, tukawa na gape hapa katikati hatutakuwa tumejenga uchumi unaostahili katika Taifa letu. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais wakati anahubia Bunge alisema vipange vyote hivi vianze. Sasa niombe waziri mshaurini Mheshimiwa Rais hata kama ni mapato ya ndani, hata kama ni kukopa kwa sababu deni letu ni himilivu tukope ili tuweze kuunganisha vipade hivi ili tuweze kuleta uchumi kwa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunahitaji ndege ya mizigo, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliahidi kwamba atanunua ndege za mizigo. Wanalalamika sana watu wa Kusini wanaolima matunda, tunalalamika sana sisi wa Kanda ya Ziwa tunaosafirisha Samaki na matunda pamoja na mbogamboga tunahitaji ndege ya mizigo ili kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika kutoa mazao yetu hapa na kwenda Nchi za Nje. Kwa hiyo, naamini kwamba msimamizi wa Shirika la Ndege ajiweke vizuri, aishauri vizuri Serikali ili tuhakikishe kwamba tunanunua ndege hiyo mpya ya mizigo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwamba tunayo mahitaji makubwa sana ya barabara zetu kama ambavyo wenzangu wamesema. Nina barabara ya Magu, Bukwimba, Ngudu ambayo ipo kwenye Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi ukurasa wa 74 na hii barabara inahitaji kujengwa tu kwa sasa. Lakini nimeona kwenye hotuba ni kwamba Serikali inatafuta fedha hata mwaka jana Serikali ilikuwa inatafuta fedha. Ina maana utafutaji wa fedha huu haukamiliki? Barabara hii ikaweza kujengwa? Mwaka jana mmetafuta fedha na mwaka huu mnatafuta fedha, maana na mwaka kesho mtatafuta fedha, tunakamilisha lini hii barabara! Kwa sababu tunaamini kwamba baada ya standard gauge kukamilika hii barabara ndiyo itakayosafirisha shehena za mizigo kupeleka Nairobi.

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nimweleza msemaji, ni kwamba barabara hii ya Magu, Ngudu – Kwimba hadi Hungumalwa imeahidiwa na Marais wanne haijawahi kutokea katika nchi hii. Ameahidi marehemu Mkapa ameahidi, ameahidi Mheshimiwa Kikwete, ameahidi Mheshimiwa Marehemu Magufuli na ikaahidikiwa na Mheshimiwa Samia, haijawahi kutokea sasa nafiriki labda tu ifutwe. Mheshimiwa Kiswaga. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Sasa Mheshimiwa Tabasam tunaifutaje barabara. Mheshimiwa Kiswaga endelea.

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, siungi mkono kufuta, lakini naunga mkono kwamba imeahidiwa na Marais wanne. (Makofi)


Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sasa tupate hizo fedha, Lakini kuna barabara ya Magu mpaka Mahaha, barabara hii inafungua uchumi kutoka Simiyu mpaka Magu Mwanza iliahidiwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli mwaka 2015. Waziri ninakuomba barabara hii uione kwa macho mawili ili uweze kuitengea fedha itekelezwe kwa lami kwa sababu ni barabara muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunashukuru kwamba design sasa inaendelea barabara ya daraja pale Sukuma itatusaidia pia kuendeleza barabara hii. Tuna barabara ya Kisamba – Sayata, Simiyu hii ni barabara ambayo ina sifa za kuingizwa kwenye TANROADS, lakini haijaingizwa kwenye TANROADS miaka yote tunaomba pamoja na ya Kabila Isolo, Isawida kule Itilima hizi niombe tu waziri kama itakupendeza uzikasimu zihudumiwe na TANROADS kwa sababu uwezo wa TARURA ni mdogo sana kusimamia hizo barabara. Nikuombe sana hizi barabara ni barabara muhimu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina barabara kutoka Nyanguge Airport, barabara hii inapunguza msongamano kwa sababu ni barabara ambayo inatokea Musoma inapita Nyanguge kwenda Kayenze mpaka Airport inapunguza msongamano wa Jiji la Mwanza. Nalo hili liko kwenye upembuzi yakinifu na ninaamini kwamba imeshakamilika kwa ajili ya kuwekewa lami. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Ilani ya CCM ukurasa 83, tumeahidi kwamba tutatengeneza kivuko cha Ijinga – Kahangala. Ninashukuru kwenye hotuba ninaona kuna maandalizi kivuko hiki ni muhimu sana kwa wananchi wangu wa Ijinga na Kahangala pamoja na visiwa vyote vya Ukerewe ambavyo vina vua samaki pamoja na mazao mengine itasadia sana kusaidia wananchi hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna daraja la Simiyu, daraja la Simiyu lile linaunganisha Simiyu na Mwanza katika barabara kuu ya kutoka Nairobi, Mwanza mpaka Rwanda, kwa hiyo, hili ni daraja muhimu sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimeona hapa maelezo hayajaniingia vizuri kichwani labda uangalie Mheshimiwa Waziri uone namna ya kulijenga daraja hili la Simiyu ili kuondoa adha ambayo wakati wote wananchi wanaosafiri watanzania wanapata shida sana. Ni pamoja na kukijenga kipande cha kutoka Nyanguge kwenda Ramadi kimeharibika kabisa na wewe unakijua hebu tuona namna ambavyo tunaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana na niunge mkono hoja. Nawapongeza wote katika Wizara ya Ujenzi. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii ambayo nilipaswa kuchangia asubuhi lakini nikaamini kwamba umeniweka akiba.

Mheshimiwa Spika, naomba kumpongeza sana Waziri wa Nishati na Naibu wake, Katibu Mkuu na Mkurugenzi wa REA Vijijini bwana Maganga kwa kazi kubwa ambayo wameifanya kwenye nchi hii katika kuhakikisha kwamba umeme unapatikana wa uhakika pamoja na matatizo madogo madogo, lakini angalau wananchi wanaendelea kupata huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye miradi hii ya REA imesaidia sana kufungua maendeleo kwenye vijiji vyetu kila mahali ambapo umeme umewekwa wa REA kuna viwanda vidogo vidogo vimefunguliwa na wananchi kwa hiyo, vimeongeza ajira kubwa sana katika maeneo yetu, lakini pia na kuchangamsha center na ujenzi mpya kabisa wa nyumba za kisasa vijijini sasa unaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumewahi kutembelea Kamati yetu PAC kule Iringa pamoja na Manyara na Singida tumekuta kule vijijini wananchi wako happy kabisa kwa sababu ya kuona umeme vijijini umekwenda na ninawapongeza na Waziri kwa kweli Mungu amempa kipaji cha kukariri vijiji vyote vilivyoko hapa Tanzania. Kwa hiyo, nakupongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa kweli umeme walipofanya evaluation uliongeza tija kwa sababu scope zilizokuwa zimeandaliwa mwanzo zilikuwa chache sana na hii imeifanya CCM kupata kura nyingi baada ya umeme huu wa REA kufika vijijini. Kwa hiyo, kwa sina kipingamizi cha kupitisha bajeti ili wakatekeleze hasa kwenye vijiji vyangu 42 ambavyo vimebaki kule jimbo la Magu, Kalemani anavijua na Maganga anavijuwa kwa sababu wamekwenda kule karibu mara nne kwenye maeneo yetu, vijiji vya Isolo, Shishani, Ingombe, vyote wanavifahamu, vijiji vya Chandulu, Mwabulenga, Kisamba vyote wanavifahamu, kwa hiyo, nahitaji hivi vijiji 40 viweze kufikiwa umeme wa uhakika ili wananchi waweze kuwekeza viwanda vya kuchakata mazao mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la pili ni suala la KVA wamiliki wa viwanda wanalalamika wanamatatizo, kwamba unapofanya kazi kwenye viwanda, ni mdau wa kiwanda naomba ni declare interest unapochambua pamba miezi miliwi, ukikata umeme unachajiwa KVA miezi mitatu bure unalipa hewa. Kwa hiyo, kama mazao yapo umekusanya kidogo ukachambua kwa muda mfupi unaingia hasara tena za kuilipa TANESCO bure, miezi mitatu hii inakatisha tamaa wawekezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano kama mwezi wa kwanza ulilipa bill ya milioni 60 na mwezi wa pili ukalipa bill ya milioni 60 maana yake miezi mitatu utalipa milioni 60 mara tatu milioni 180, ndiyo maana wawekezaji wanashindwa hata kule kwako Kongwa, mwekezaji mkubwa wa kiwanda cha Oil Meal Kahama, alikula kwa miezi michache tu mbegu zikaisha. Kwa hiyo, akashindwa kwa sababu faida yote aliyoipata akalipa KVA, pamoja na hasara zingine kwa hili linaleta shida na sheria hii ilitungwa wakati tunatumia umeme wa mafuta IPTL. Kwa hiyo, sasa tunatumia umeme wa kwetu tuondoe hii sheria ili tuweze kuwasaidia wafanyabiashara wa viwanda waweze kuchakata hatuwezi kuvutia wawekezaji kama tunafanya jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na hili waziri haliitaji wadau kwa sababu tunataka kuongeza wazalishaji na wasindikaji wa mazao yetu ili alizeti Kongwa Singida, Dodoma Mwanza ilimwe watu wakitegemea viwanda vyao vitafanya kazi kwa murefu bila kulipa KVA. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilizungumze kidogo hili la vinasaba na niweke vizuri kumbukumbu kwamba SIPA ndiye aliyekuwa mwenye Kampuni ya kuuza vinasaba na kuweka vinasaba kwenye nchi mbalimbali, lakini Msumbiji walimfukuza, Uganda walimfukuza, Kenya walimfukuza, Brazil walimfukuza, akaja hapa kwa namna fulani fulani akaanzisha kampuni ya GFI, GFI ndiyo inayonunua vinasaba kwake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kwa hiyo, uwamuzi wa Serikali hii sikivu wa kuipa TBS wa kushughulika na hili jambo ni uhamuzi sahihi kabisa. Kama kuna watu labda wametumwa kuja kumpigania mnyonyaji washindwe na walege. Kwa sababu, tunajua kwamba TBS ndiyo tumeipa kazi sasa na yenyewe TBS inanunua hivi vinasaba kwa SIPA. Kwa hiyo, tunaamini kwamba TBS itakavyo endelea itatengeneza teknolojia ya kwakwe kuhakikisha kwamba vinasaba hivi hivi vinapatikana hapa hapa au duniani sehemu nyingine. Lakini fedha zile ambazo TBS italipwa hizi shilingi 14 zitabaki kwa Serikali yetu hata kama kuna shida ya reli, kuna shida ya umeme hizi fedha zitasaidia kuliko kuipa kampuni nyonyaji hatuwezi kurudi huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge ni mdau wa mafuta pia, siwezi kutetea kampuni nyonyaji, lazima tuitetee nchi na nchi ifanye kazi TBS inauwezo mkubwa wa kuweza kusimamia hili jambo bila matatizo yoyote. Kwa hiyo, niseme tu kwamba nchi imeamua sahihi na tuhakikishe kwamba tunapokuwa wazalendo, lazima tuangalie vitu vyenye tija siyo vitu ambavyo vinaipunguzia Serikali fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hizi fedha halipi mfanyabiashara, hizi fedha EWURA wanapotengeneza mkokoto wa mafuta, kwamba Mwanza petrol itauzwa 2,400/= kama ilivyo leo maana yake kwamba anayelipa ni mtumiaji wa mwisho. Kwa hiyo, tunaamini kwamba baada ya TBS kukaa vizuri wanaweza kuwa wanataja hata shilingi saba kama ambavyo mwezangu Boniface hapa amesema maana yake shilingi saba inaweza kupelekwa kwenye TARURA, inaweza kupelekwa kwenye maji tukaongeza mifuko hii ya kutekeleza miradi yetu tukaweza kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niunge mkono kwa sababu Wizara hii Waziri mwenyewe na Naibu wake anaiweza, unajua hapa duniani kuna watu ambao wanauwezo wa kubeba mizigo mizito na hatuna sababu ya kuwapunguzi hiyo mizigo kwa sababu Nishati, Waziri wanatosha, Wakurugenzi wake, wa REA TANESCO TPDC nao wanatosha wafanye kazi karibu ili kumsaidia Waziri tusipunguze hapo na hayo maneno, tunaweza tukampa mtu akashindwa sasa sisi tuombe sana kwamba tusigawanye wizara huyu anauwezo wa kuibeba Wizara, ameibeba muda wote. Kwa hiyo, niombe sana mpeni kazi aweze kufanya ahsante sana. (Makofi/ Vigelegele)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Ofisi ya Waziri Mkuu
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii, ili niweze kuchangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuipongeza Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Mawaziri wake, lakini pia ninapojikita Ofisi ya Waziri Mkuu naomba nizungumzie uchumi kwa wananchi mmoja-mmoja wetu kwa sababu ndiyo tunaowategemea zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nchi hii ardhi hatujaitumia kwa kilimo. Pamoja na jitihada mbalimbali ambazo zinafanywa na Wizara hii kubwa, tunapaswa tufikiri upya. Ardhi tuliyonayo yote inategemea mvua, lakini Mwenyezi Mungu ametupa mito, ametupa maziwa, ametupa maji ya chini pia, lakini wananchi wetu wanakuwa na likizo ya miezi sita bila sababu, wakati Mtumishi wa Serikali anakuwa na likizo ya mwezi mmoja kwa mwaka. Ili kuinua uchumi wananchi hawa wanastahili kufanya kazi ikiwezekana miezi kumi ili wapumzike miezi miwili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo tuna upungufu wa mafuta, lakini mazao ambayo yanasababisha tupate mafuta yote tunategemea mvua, mfano michikichi, alizeti, pamba, yote inategemea mvua. Kwa hiyo, naomba ushauri wangu ni kwamba akili zetu zitumike, akili za watendaji zitumike na akili za viongozi zitumike.

Mheshimiwa Naibu Spika, mahali ambapo tuna mito, maji yatumike kwa ajili ya umwagiliaji ndiyo itakuwa mkombozi. Mahali ambapo hatuna mito tuna ziwa, milima itumike kutengeneza mabwawa juu ya mlima. Kama tunatengeneza matenki ya maji, tunashindwaje ku-pump maji kwenda mlimani na kushuka kwenye mashamba ambayo yako kwenye mwinuko hayo ya pamba, alizeti pamoja na michikichi, ili mwananchi aweze kuvuna mazao wakati wote? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo inapokosekana mvua mwananchi anapata hasara, Serikali inapata hasara, viwanda vinapata hasara kwa sababu vinakosa malighafi ya kuzalisha. Ajira inakufa, kodi inakosekana kwa hiyo, tufikiri upya kuona namna ya umwagiliaji tunaweza kuutumiaje? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mahali ambapo hakuna ziwa maji ya chini yatumike. Tunakwenda nchi za wenzetu zilizoendelea, mashamba yote kuna maji ya chini, maji yameelekezwa kwenye mashamba wananchi wanavuna masaa yote. Tubadilishe kilimo hiki kiwe kilimo ambacho wananchi kweli kinawasaidia, kwa sababu leo tunaweza kuwa tunalalamika mfumuko wa bei ni kwa sababu wananchi wetu hawana fedha, hawana kipato cha kukidhi kununua hayo mahitaji, kwa hiyo, tubadilike. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hapa ije na mpango wa miaka mitano au miaka kumi kwa sababu jambo hili linahitaji fedha nyingi, lakini kama tutaendelea kutegemea mvua nataka nikuhakikishie hatutabadili kilimo chetu, tutapeleka pembejeo, tutapeleka mbolea, tutapeleka viuadudu, lakini kama hawana mvua ya kuivisha, hawana maji ya kuweza kuivisha, hawana maji ya kuweza kuivisha mazao, tunapiga kelele bure. Hatutakuwa tunasaidia wananchi. Multisectoral wenzangu sasa wafikiri hapa kwenye jambo hili ili waweze kuona nje ya box kuhakikisha wakulima hawa tunawasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili. Serikali imewekeza kwenye vituo vya afya, lakini vifaa muhimu ambavyo vinahitajika bado hafijafika. Liangaliwe jambo hili kwenye bajeti hii ili tuweze kupeleka vifaa kuvipunguzia hospitali za Wilaya majukumu yake kwa sababu, kuna vitu ambavyo vinapaswa viishie tu kwenye vituo vya afya, kama Kituo changu cha Kisesa ambacho kwa kweli kinahudumia watu wengi ni kama hospitali ya Wilaya, Mheshimiwa Ummy ananua jambo hili, lakini kituo changu cha Rugeye, Mheshimiwa Ummy anajua jambo hili, kituo cha Kabila, Mheshimiwa Ummy anajua jambo hili, Shishani kinachomalizika, Mheshimiwa Ummy anajua jambo hili. Kwa hiyo, Serikali ione namna ya kuweza kusaidia jambo hili liweze kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara zetu zitengenezwe. TARURA tuiongezee fedha kama ambavyo wengine wamependekeza. Huko huduma wanayohitaji wananchi ni kusafirisha mazao yao, kusafiri wakati wote. Uchumi tunaposema umekua siyo fedha mfukoni bali miundombinu ambayo inawawezesha kusafirisha bidhaa zao ndiyo inayohitajika kwa hiyo, kwa kazi ambayo mwaka jana tumeifanya na mwaka huu wa bajeti unaoendelea, tuongeze fedha kwenye TARURA ili tuweze kufungua barabara nyingi zaidi na wananchi wetu waweze kusafirisha mizigo yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapohitaji kuendeleza nchi lazima sisi sote tuamue. Hili jambo si la Rais peke yake, hili jambo ni la Watanzania wote. Kila mmoja mahali pake alipo tuamue kubadilisha mawazo yetu ili kuwahakikishia wananchi tunawasaidia kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Maji
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwenye Wizara hii ya maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli Wizara ya Maji imetekeleza miradi mingi ya Kitaifa ambayo kwa kweli ukifika unajivunia. Kwa hiyo, tunapo mpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Katibu wake maana yake ni kwamba wanafanya kazi ambayo inaonekana sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la maji kama ambavyo ndugu yangu Ng’enda pale amemaliza halina mbadala. Kwetu Magu tulikuwa na shida kubwa sana, ninakuomba sasa ndugu yangu Mheshimiwa Aweso kama itakupendeza mradi ule wa Magu Mjini umekamilika mwaka 2019 ni vizuri sasa ukazinduliwa ili uweze kuonekana kwamba ni mradi ambao kwa kweli unafanya kazi vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapokupongeza wewe tunampongeza Ndugu Sanga tunawapongeza na Watalaam ambao mmetuletea. Engineer Msenyele kwa upande wa MWAUWASA kwa kweli anasimamia vizuri sana. Ule mradi wakati unakamilika ulikuwa una mapungufu mengi, Ndugu Sanga unajua lakini kwa kweli mpaka sasa hivi Watalaam ambao tunao pale wanafanya kazi vizuri mapungufu yamepungua sana. Tunaomba muwape ushirikiano kwa sababu wanawasaidia sana miradi hiyo kuhakikisha kwamba inafanyakazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni Mjumbe wa Kamati ya PAC tumepita Arusha kuna mradi mkubwa sana. Kule Arusha ule mradi kwa kweli vyanzo vyake ulivyojengwa unaweza ukalisha Mikoa hata mitatu. Arusha yenyewe, Kilimanjaro na Manyara, ni mradi mkubwa mno nanimradi wa kielelezo kwa kweli tunawapongeza mno. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dar es Salaam tulipita Ndugu Luhemeja kwa kweli unafanyakazi kubwa sana, miradi yako haina query ni miradi inayoonekana na kwa kweli inawasaidia wananchi wa Dar es Salaam, endelea kumsaidia Waziri wa Maji pamoja na Katibu Mkuu mnafanyakazi vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nina matatizo bado makubwa ya maji kule Magu. Ukiwa pale Mji wa Kisesa Kata ya Bujola, Kata ya Bukandwe, Kata ya Bujashi ile Miji ndipo sasa Jiji linapanukia kuja kuongeza Mji ule. Jiji la Mwanza na Ilemela wote wanahamia kwenye Kata hizo, bado kuna tatizo kubwa la maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri unafahamu sana Ndugu Sanga tatizo hilo, kwa sababu hatua sasa hivi ule mradi wa Butimba ndiyo tunaoutarajia na kwa sababu tayari tenki pale limekamilika na nimeambiwa na Ndugu Msenyele kwamba tayari Mtalaam Mshauri ameshapatikana wa kusanifu ule mradi na mwezi ujao unaanza, ninaomba msaidieni Waziri ili uweze kwenda kwa kasi na Kata hizo Nne ziweze kupata maji ambayo yatatosheleza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Kisesa, Bujora, Bukandwe na Bujashi ndiyo Mji wa kisasa sasa hivi, tusipowapatia maji hatuwatendei haki Watanzania hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe tunawapongeza kwa sababu mnatusikiliza nyinyi, tunapokuja ofisini kwenu mnatusikiliza na kwa kweli tunaomba muendelee kuwa na moyo huo. Kwa sababu leo umeomba bilioni 700 lakini tunaona kumbe bilioni 700 hazitoshi ni vizuri sisi Wabunge hapa na Serikali tuone njia mbadala ya kuongeza bajeti tupate hata trilioni moja ili miradi hii iweze kukamilika kwa sababu kumbe tatizo siyo nyie watu wa Wizara tatizo ni fedha kidogo. Kwa hiyo, ni kazi yetu sasa sisi Wabunge kuhakikisha kwamba tunasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Ndagalu, Tarafa ya Ndagalu...

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa subiri taarifa, Mheshimiwa Amar.

T A A R I F A

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpe taarifa mchangiaji Mbunge Kiswaga, Mbunge wa Magu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majuzi nilikuwa kwenye msiba pale Magu kwa kweli wananchi wa Magu wanakupongeza na wanaipongeza sana Serikali kwa kukamilika ule Mradi wa Magu wanampongeza sana.

MWENYEKITI: Mheshimiwa, taarifa hiyo umeipokea?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea kwa mikono miwili kwa sababu Magu ilikuwa ni janga la Kitaifa kukosa maji na hicho ndicho kilichonirudisha humu na nitaendelea kurudi Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ule Mradi wa Magu ni Mradi mkubwa Tarafa ya Ndagalu ina Vijiji 16 tayari tumeshafanya design tumeshaleta Wizarani hebu ione hata kama si bajeti hii, bajeti zijazo tuweze kuwapelekea maji watu wale kwa sababu ni mteremko kule anaenda kwa gravity hatutakuwa na gharama kubwa san Mheshimiwa Waziri. Mlione hili kwa sababu tunaamini kwamba Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuwahudumia wananchi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli lazima nimpongeze Mkurugenzi wa RUWASA, Mkurugenzi Clement kwa kweli ni msikivu sana nilikuwa na matatizo makubwa sana kwenye Jimbo langu. Mradi wa Solar Bubinza ulikuwa umekwama kabisa leo maji yanapatika kwa usimamizi wake mkubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunapowapongeza tunamaanisha, Serikali hii tunapoipongeza tunamaanisha kwamba inawatendea haki watanzania. Mradi wa Lugehe tunataka kuoboresha, Mradi huu utahudumia kata tatu, Kata ya Kitongosima, Kata ya Bwamanga na Kata ya Kahangara. Na kwa kweli mradi huu upo ukiboreshwa utasaidia sana wananchi hasa wale ambao akina mama wanapata tabu ya kuchota maji umbali mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunao mradi pia pale Nyambuge sasa pamekuwa ni Mji Mradi ule ni mdogo unapaswa uongezwe kwenda kule Matera na tayari tumeshaleta maombi haya Wizarani nazani Sanga unajua, tunaomba sana hili nalo uliangalia. Kule Sanjo maji yako kuanzia nukta moja ambapo wananchi wanakaa na tumeshaleta design katika Kata ya Rutare, Kata ya Kongoro, Kata ya Chabula ili waweze kupata maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningeomba sana jambo hili Waziri wa Maji aweze kuliona ili tuweze kuwasaidia watu ambao wako karibu sana na maji lakini hawapati majisafi na salama. Maji wanayo lakini siyo safi wala salama. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niombe sana, tunajua nchi hii ni kubwa mahitaji ya wananchi ni mengi na hata tunajionea hapa swali likiulizwa la maji, nusu ya Wabunge wewe ni shahidi wanasimama wote kuuliza maswali ya nyongeza kwa ajili ya maji. Kwa kweli tuombe Serikali bajeti zijazo tuone mbadala tungeweza kusema tuongeze tozo mahala fulani lakini kwa ajili ya mfumuko wa bei tunakaa kimya ili tuweze kuangalia namna ambayo inaweza kusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwenyezi Mungu hatujamkosea tutapata fedha nyingi kwenye mapato yetu ya ndani yakisimamiwa na wafadhili mbalimbali ambao wanaonyesha kutusaidia katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana kazi hii ni ya kwenu, kazi ya usimamizi ni ya kwenu na sisi tutawasaidia kwenye Majimbo yetu, wale wataalam ambao mmetuletea tunashirikiana nao vizuri tunaamini kwamba tutaendelea kushirikiana nao vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niunge mkono hoja, ahsante sana.
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 – Wizara ya Kilimo
MHE. BONIVENTURE D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi hii. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu kwa namna ya pekee ambavyo wamelichukulia suala la Wizara ya Kilimo kwa mtazamo si msimamo. Nchi zote duniani viongozi ili tupate mabadiliko lazima tuwe na mitazamo kuliko kuwa na misimamo. Kwa hiyo, hili Mheshimiwa Waziri ameliweza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo mazao matano ya kimkakati ambayo Waziri Mkuu aliyasimamia ili kuondokana na adha mbalimbali ambazo wananchi wetu wanazipata. Leo ukienda kule mitaani mfumuko wa bei wanalalamikia mafuta ya kula, mfumuko wa bei wanalalamikia sabuni. Sasa sisi tunayo mazao ambayo yanaweza kumaliza tatizo hili. Zao la kwanza; zao la michikikichi hili linatoa mafuta pamoja na sabuni. Kama tutalisimamia na kuliimarisha tutaondokana na tatizo hili kubwa ambalo wananchi wetu wanaendelea kuwa nalo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pamba pamoja na zao la alizeti, hizi zote ni mbegu ambazo zinatoa mafuta ambayo wakulima wetu na wananchi wanaweza kupata mahitaji muhimu zaidi. Zao hili la pamba na alizeti ni mazao ambayo yanalimwa kila mwaka, ni mazao ambayo yanahitaji mvua ya kutosha. Nipo kule Magu nimeona mazao ya pamba pamoja na alizeti ambavyo yanakabiliwa na ukame wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimewahi kutoa hapa mchango kwamba tunayo mabonde, tunayo maziwa, tunayo mito, tutumie kwa ajili ya umwagiliaji, hapa ndipo ambapo wawekezaji ambao wanatafutwa na Wizara mbalimbali kuja kuwekeza hapa Tanzania, waje wawekeze miundombinu ya umwagaliaji ili wananchi wetu waweze kulima, waweze hata kuchangia kulipa hiyo miundombinu. Tukifanya hivyo, tutaondokana na adha na tutazalisha mazao ya kutosha kuhakikisha kwamba tunapata mafuta na sabuni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba hivi sayansi imegota kutengeneza mbegu ya zao la pamba ambayo inaweza kuwa ni mti? Ukilimwa leo unapaliliwa miaka mitano ili wananchi wasiwe wanalima kila mwaka ili tuwe na uhakika wa kuvuna miaka yote. Kwa sababu wananchi wetu wanahangaika sana kila mwaka kulima zao hili. Hivi sayansi imegota ndugu zangu? Tuone utafiti ambao unaoweza kusaidia ili tuweze kuwasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa ninampongeza sana Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba na Wataalam wake kwa kusimamia zao hili muhimu. Ninaomba, wananachi wamenituma mbegu za pamba ziwe zinakwenda mwezi wa Septemba. Maana wanapolima mwezi wa Oktoba na wa Novemba haya ni mazao ambayo sasa yanaonekana hata wadudu hawapati shida kwenye kupulizia. Kwa hiyo, ninaomba sana mbegu za pamba ziweze kwenda mwezi wa Septemba. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Taarifa Mheshimiwa Tabasam.

T A A R I F A

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumpa taarifa mchangiaji kwamba suala la kugawa mbegu za pamba liendane na dawa za pamba na mbolea wakati huo huo.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kiswaga unapokea taarifa?

MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napokea naunga mkono. Kwa sababu ardhi yetu kule Kanda ya Ziwa imechoka. Nampongeza Waziri hapa amesema hatafanya kazi nyingine bora mbolea iende kwa wakulima. Tatizo kubwa tulilonalo sisi kule, mvua yetu ni ya wastani na wananchi wetu wanapata taabu kutumia mbolea hii. Wanataka mbolea ya samadi au mbolea ambayo inaweza kuendana na hali ya hewa kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hapa ndipo utafiti sasa unatakiwa utumike kwa hali ya juu sana. Hili nakwenda na kwenye mbegu, nimesikia hapa Mheshimiwa Waziri amesema kwamba mbegu za asili, mbegu za mahindi, mbegu za alizeti, mbegu za pamba za asili zitaanza kutumika. Nchi ikikosa mbegu za asili ni hatari. Kwa hiyo, nakupongeza sana kwa sababu vituo vyetu vya utafiti vimeanza kuizalisha mbegu hii na kuwa nyingi. Mbegu hii ndiyo ambayo inavumilia magonjwa mbalimbali ambayo yanakuja kutuathiri Watanzania na kutuondolea kabisa tija ya mazao. Kwa sababu tatizo tunalohangaika nalo hapa ni tija. Mazao tunazalisha kidogo kwa sababu ya wadudu kuwa wengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la mwisho tusijifungie, dunia imekwisha kubadilika. Kule duniani nchi za wenzetu zilizoendelea wana kilimo cha aina mbalimbali ambacho kinasaidia. Kwa mfano, kuna mbegu za mahindi ambazo zinaweza kutoa mafuta ya kula na mafuta mengine. Hebu tutafiti, tuone namna ambavyo tunaweza kulifanya Taifa likawa na mazao mbadala mchanganyiko ambayo yanaweza kusaidia. Hata maua pia, kuna maua yanatoa mafuta halafu hayo hayo majani yanakwenda kulisha mifugo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Mheshimiwa Waziri umeleta mfumo mpya, watu wako leo wanavaa sare za kilimo, tuone sasa kwamba wanamfikia mkulima na kwa sababu umeamua jambo hili na sisi tunakuunga mkono. Wewe bado ni kijana, wewe bado una nia njema, wewe bado una mtazamo, tunauhakika kilimo chetu kinakwenda kubadilika. Tuombe wataalam wako wakusaidie, kama hawatakusaidia walete mbele ya Bunge tuweze kukusaidia hao ambao hawawezi kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nikushukuru kwa kunipa nafasi ili nami niweze kuchangia Wizara muhimu sana ya TAMISEMI ambayo inawagusa wananchi. Niipongeze Serikali kwa namna ya pekee Serikali ya Awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa namna ya pekee inavyoleta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kihuduma kwenye halmashauri zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze moja kwa moja kwa TARURA. TARURA kila mmoja hapa anahitaji iongezwe fedha, ni kwa sababu kwamba ili maendeleo ya kiuchumi yaweze kuwepo barabara zinahitajika. Mtu ambaye alikuwa anasafiri masaa manane aweze kusafiri masaa mawili. Mtu ambaye alikuwa anakwenda kupata huduma ya kiafya asafiri kwa haraka ili aweze kufika kwenye huduma za kiafya. Kwa hiyo TARURA ni muhimu sana kwa kweli tukaona namna ambavyo tunaweza kuiongeza fedha ili iweze kuhudumia barabara zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazo barabara ambazo kwa kweli zinahitaji madaraja tu kuunganishika, hakuna mawasiliano ambayo yanapatikana bila kuwepo na daraja. Nyuma kule tulikuwa na Mradi wa Bottleneck ambao ulisaidia sana barabara ambazo zilikuwa haziunganiki, kata kwa kata, kijiji kwa kijiji, wilaya kwa wilaya. Kwa hiyo niombe tena, kwa mfano kule kwangu Barabara ya Kahangala, Mwamanga kwenda Kisesa B pale huwezi kwenda mahala popote kama mvua imenyesha; na kuna vijiji vitatu ni kama viko visiwani. Kwa hiyo niombe sana, kwa mfano Inolelo, juzi nilikuwa na mikutano ya hadhara kule, nimemaliza Kijiji cha Kisesa B ikabidi nizunguke Kata ya Nyanguge, Kata ya Kitongo Sima, Kata ya Kahangala ndipo nifike tena kwenye Kijiji cha Inolelo. Kwa kweli ni mateso makubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara hii tumekwishaiomba siku nyingi TAMISEMI, na tulikaa na Mheshimiwa Waziri Angellah Kairuki nikaiomba hiii Barabara ya Kahangala, Mwamanga, Kisesa B; mwaka huu nipeni fedha ili iweze kutengenezwa na wananchi tuweze kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, siishii hapo, kuna Barabara ya Kisamba Sayata Mkurugenzi wa TARURA, Ndugu Seth, nimeshakuomba mara nyingi kwamba huwezi kufika salama kuelekea Bariadi bila kuwa na daraja pale Kinsalama kuja Sayaka; ninaomba sana mwaka huu. Mheshimiwa Waziri umeanza utaratibu mzuri wa kukaa na Wabunge. Hata tulipokaa na wewe nilikutajia hii barabara. Kwa kweli nakupongeza sana Waziri endelea kuwa na upole huo, sisi tunatoa matatizo yetu ndani tukiwa tuna uhakika kwamba haya yote yatafanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo Barabara ya Isolo kwenda Isawida kule Itirima. Barabara hii ni ya muhimu sana, inahitaji tu bottleneck kuweza kukamilika ili wananchi wa Itirima, Isolo, Kabila kuja Wilaya ya Magu waweze kusafiri kwa haraka sana. Niombe sana hili jambo liweze kufanyiwa kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli miji yetu inakuwa, Mji wa Magu unakuwa ni wa siku nyingi tangu mwaka 1974 ni wa umri wangu. Lakini Miji ya Kisesa na Bujora nayo unakuwa, nimekuomba Waziri wa TAMISEMI, tulipokaa pale Msekwa, kwamba angalau nipate kilometa sita za lami zitengeneze Magu Mjini, zitengeneze Bujora na Kisesa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni miji inayokua; ili miji iweze kuendelea tusaidieni. Wenzetu wanapata TaCTIC sisi hatupati; tusaidie Mheshimiwa Waziri hili litakuwa ni mkombozi kwa wananchi wetu. Tumetengeneza barabara za mitaro ni vizuri zikawekewa lami ili kuhakikisha kwamba tunawasaidia wananchi. Niombe sana jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, afya, tunayo majengo maboma 20 tumeezeka kwenye Wilaya ya Magu. Kule Jijimiri ni mbali sana na huduma, kule Isolo ni mbali sana na huduma, kule Ndagalu ni mbali sana na huduma, kule Bwamanga ni mbali sana na huduma, kule Kisamba ni mbali sana na huduma, kule Lutale ni mbali sana na huduma. Ninaomba Mheshimiwa Waziri tupatieni; hizi milioni 50 mnazotupatia kwa zahanati tatu tunashukuru lakini bado hazitoshi kwa sababu mahitaji ni mengi. Ukienda pale Walina wana jengo kubwa sana lakini hatuna fedha za kuweza kulimaliza. Kwa hiyo Mheshimiwa Waziri tukuombe basi zile zahanati tumeziezeka tupatie tu fedha ni milioni 50, ni bilioni moja kwa zahanati 20, tunakamilisha maboma haya Magu na wananchi wanaanza kutindua. Niombe sana jambo hili tuweze kupewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna vituo vya afya vya kimkakati. Kule Ng’haya tumeishukuru Serikali milituletea fedha za ukarabati wa zahanati, lakini tukajiongeza Halmashauri ya Wilaya ya Magu tukaleta ombi mkatubalia kuanza kujenga kituo cha afya, tupeni fedha za kumalizia pale Ng’haya ili kituo hicho kikamilike. Sambamba na Kata ya Mwamanga ambayo imezungukwa na mito mingi tusaidie sana Mwamanga nayo tuweze kupata kituo cha afya, pamoja na Lutale tuweze kupata kituo cha afya. Tuangalie pia kukikarabati kituo cha afya cha Nyanguge ili kiweze kukamilika. Ninaomba sana hili kwa Serikali sikivu ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan iweze kutupatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira hizi zilizotoka, ajira za afya na ajira za walimu. Kuna intake ya walimu kuanzia 2016 hawajachaguliwa. Huu mfumo unawasoma akina nani? mfumo ambao hauwasomi watu waliotangulia? wa 2016 hawajachaguliwa, wamechagua 2019, hawa watoto wa maskini ambao wamebaki wanasaidiwa na nani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe na niweze kushauri, kwa kweli kama inawezekana ajira hizi zilenge wilaya, kila wilaya ipewe watu wake ili tuangalie waliotangulia kumaliza na wanaoendelea. Kwa kweli tunawakatisha tamaa wazazi hata kusomesha. Niombe sana kwa kweli, hili linaumiza sana. Sasa hivi kwenye begi langu nimejaza CV za vijana, sina hata pa kuzipeleka. Kwa hiyo ushauri wangu, tutafute namna ya kuwezesha kila wilaya ni nafasi kiasi gani ipelekewe iajiri watu wake ili watoto hawa tuweze kuwasaidia. Niombe sana jambo hili Waheshimiwa Wabunge mliunge mkono, pigeni makofi ili Serikali ijue kwamba leo mmeniunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi nyingi zinaendelea kufanyika, lakini niombe; kuna mapunjo na madai ya watumishi wetu kwenye halmashauri, wanalalamika hawajaweza kupewa mapunjo hayo. Niombe Serikali ione ili kumpa moyo mtumishi huyu anayemsaidia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alipwe haki zake, alipwe madeni yake na mapunjo ambayo wanaendelea kushughulika nayo wakati wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo niunge mkono hoja na nikupongeze sana pia kwa kuendesha Bunge kwa standard kama hii, ahsante sana. (Makofi)
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 – Wizara ya Maji
MHE. BONIVENTURA D. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi hii na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Maji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa namna ya pekee ambavyo anaisimamia Serikali, kwa namna ambavyo Bunge linapitisha bajeti na yeye anaendelea kuleta fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninampongeza Waziri wa Maji na Naibu wake. Sina shaka na vijana hawa kwa sababu ya kazi wanazozifanya ni kielelezo kwa Umma; kwa kweli mnafanya kazi nzuri. Nimpongeze Katibu na Naibu Katibu wake kwa namna ya pekee ambavyo kwa kweli tunashirikana nao vizuri, unapohitaji ufafanuzi mara moja wanakusikiliza. Nimpongeze sana Mkurugenzi wa RUWASA, Engineer Clement Kivegalo, kwa kweli huyu amekuwa ni mtu wa mfano, wakati wote ukimpigia simu Engineer Clement anakupokea, wakati wowote ukitaka kwenda ofisini anakuruhusu kwenda. Kwa kweli nakupongeza sana kwa kazi nzuri unayoifanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na Miji ya Kisesa, Bujora, Bukandwe pamoja na Bujashi. Kwa kweli hii ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. Nikushukuru sana Waziri wa Maji, alipokuja Makamu wa Rais kwa kweli ulisimama kidete kusema kwamba sasa kazi zinaanza. Naomba nikutaarifu kwamba tenki ambalo ulisema linaanza mwezi huu wa tano bado halijaanza. Ninayo matumaini kwamba labda litaanza baadaye kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, hili nikuombe tu kama mradi huu hautakwenda haraka mwaka kesho kitaumana humu ndani ya Bunge. Lazima kuhakikisha kwamba miradi hii inakamilika. Hili nasema kwa sababu nina uhakika kwamba wananchi wale wameteseka siku nyingi na idadi ya watu tayari ni 100,000 kwenye miji hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri nikuombe, nimeona miradi hii kwenye Kata ya Lutale, huu mradi umesanifiwa na unaweza kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 19. Huu mradi ukikamilika unakwenda kutatua changamoto ya vijiji vinane katika kata tatu. Kwa hiyo, niombe sana kwa kweli kama ambavyo umesanifiwa uweze kutekelezwa ili yasiwepo mabadiliko ya usanifu kwa sababu tunapochelewesha miradi hii baadaye kunakuwa na mabadiliko ya usanifu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Lugeye, Kigangama ambao umeanza kutekelezwa, kwa kweli huu unakwenda kutatua changamoto kubwa ya Kata za Kitongosima, Nyanguge, Mwamanga pamoja na sehemu ya Kata ya Kahangala. Kwa hiyo niombe sana mkandarasi ameanza, asimamiwe vizuri ili aweze kukamilisha miradi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, tunao mradi ambao umekamilika Magu Mjini, lakini hamjaufungua. Nikuombe umlete Rais ili aweze kuufungua huu mradi. Umekamilika vizuri, una mapungufu machache. Mwaka jana mamlaka ya maji iliomba shilingi bilioni moja mkapitisha hapa Bungeni na ipo kwenye bajeti. Tunaomba sasa hiyo shilingi bilioni moja ipelekwe Magu ili vifaa na namna ya kutekeleza vifaa ambayo imebaki iweze kutekelezwa. Kwa sababu akija Mheshimiwa Rais kufungua siyo vizuri wananchi ambao hawajapata maji wakasimama na mabango. Niombe sana jambo hili liweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimuombe Waziri, tunayo Tarafa ya Ndagalu yenye Kata tano, vijiji 18 ambayo ina ukame kila mwaka wananchi wanapata shida. Mto Simiyu unapokamilika wananchi wanapata shida kubwa sana ya kuchota maji. Niombe mwaka huu sasa, Engineer Clement kwa sababu nakuamini, bahati nzuri Mkurugenzi huyu Engineer Clement, hataki miradi midogomidogo, ukienda kwake anakushauri mradi mkubwa ambao unaweza kutatua changamoto ya wananchi wengi, sasa Tarafa hii ya Ndagalu yenye vijiji 18 nikuombe sana Waziri umruhusu Mkurugenzi ili aweze kufanya usanifu na vijiji hivi viweze kupata maji ndipo tutakapo kuwa tumewasaidia wananchi watanzania, ndipo tutakapokuwa tumepunguza magonjwa kwa wananchi wetu lakini pia tutampa heshima Mheshimiwa Rais kwa sababu kazi kubwa anayofanya ni kuhakikisha kwamba na wakina mama anawatua ndoo kichwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna miradi inayoendelea katika Kata ya Mwamabanza, Kata ya Sukuma na Kata ya Uhumbi, miradi hii imebakiza fedha kidogo sana na kwa kweli miradi hii ikikamilika, Tarafa yote ya Itumbili itakuwa na maji ya bomba kwenye kila Kijiji. Kwa hiyo, naomba fedha ambazo zimebaki Wizarani, na wakandarasi wapo asilimia 80, ziweze kuja ili waweze kuikamilisha miradi hii, ikiwezekana kabla ya kuanza mwaka mpya wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja hii. Kwa kweli nawapongeza sana Wizara hii. (Makofi)